SIMULIZI Pumbazo – Ep 3
SIMULIZI

Ep 4: Pumbazo

SIMULIZI Pumbazo – Ep 3
SIMULIZI Pumbazo – Ep 4

Simulizi : Pumbazo
Sehemu Ya Nne (4)

UCHANGANUZI wa Geza Ulole katika lile karatasi walilolitenga pale mezani ulikuwa uchanganuzi yakinifu haswa uliokuwa na viulizo vingi sana ndani yake.
Geza alielezea mashaka yake juu ya waziri wa mambo ya nje ama kiongozi yeyote yule wa ngazi za juu katika idara ya uhamiaji.
Geza akaenda mbali zaidi na kusema kuwa kama hawapo katika hisa za kampuni hiyo isiyojulikana basi wanapokea rushwa kubwa ili kurahisisha safari hizi batili.
Hapa alikuwa anazungumza huku akiitazama picha ya hayati Hajrati ambayo ilikuwa na zile jumbe za ajabu ajabu nyuma yake zikiwa katika lugha ya kiarabu.
“Nautazama urembo wa huyu binti, kisha nasimama mimi kama mwanaume kamili kabisa… hivi msichana mrembo kama huyu akiniletea jeuri unadhani adhabu yake nini?” aliuliza akamtazama Pilipili. Kisha akamalizia kwa kutoa jibu mwenyewe.
“Nambaka huyu…. Na nikishambaka mara moja si nitanogewa basi namgeuza kifaa changu cha starehe… hauhisi kuwa yawezekana huyu binti yalimkuta hayo….” Akasita akaitazama tena picha ya Hajrati. Kisha akamtupia swali Sajenti Pilipili.
“Umesema alikuwa na pacha wake… na aliondoka kwenda kufanya kazi nje ya nchi akiwa bado binti kigoli….” Hakusubiri jibu akaendelea.
“Hapa nafumba macho na kumtazama huyu binti alipokuwa kigoli alikuwa anavutia kiasi gani, mwanaume kikawaida anataka vinavyovutia.”
Akaendelea kuzungumza mengi kisha akamuuliza sajenti kuna kesi ngapi kama hizo za mabinti kupotea baada ya kuondoka kwenda kufanya kazi.
Sajenti akafungua bahasha yake na kumkabidhi Geza.
“Anna miaka kumi na sita, Dorika miaka tisa, Anastazia miaka ishirini, Lulu miaka kumi na nane….” Akaishia hapo na kisha akaanza kukuna kichwa, na hapo swali likamtoka. Swali zito kabisa lililokuwa na maana kubwa kabisa.

“ Kwa nini wasichana pekee katika hii orodha?” aliuliza swali hili kisha akasimama, halafu akamuuliza Sajenti ni kazi zipi wanawake wa umri huo wanaweza kufanya ili kujiingizia kipato.
“Kazi za ndani, kuuza dukani, kuuza baa…. Mi nadhani hizo ndo kuu.” Alijibu Pilipili.
“Hilo la kuuza baa liondoe kwanza, maana si umeniandikia kuwa Oman pana sharia kali sana. Sidani kama nchi hiyo ipo tayari kuona watoto wadogo wanateseka hadharani….! Alizungumza Geza.
Jibu lile likamkosha Sajenti, hapa akazidi kukiri kimyakimya huku akimwomba msamaha katika nafsi yake kwa kumfikiria Geza kama kichaa ama mwendawazimu.
“Yote uliyoyataja ni kweli yanawezekana, lakini naomba tufikirie juu ya mambo mawili tu, waarabu sio wajinga waache kuajiri waarabu wenzao kwenye maduka wakaajiri mswahili….. kwani hapa Tanzania huwaoni? Wana umoja wa hali ya juu wa kubebana wao kwa wao. Basi tushikilie mawili… ni kazi za ndani pamoja na jingine kubwa kabisa ambalo litatuongoza… kuna namna fulani ya kutumika kingono.” Geza akasita na kuyaacha maneno yake yamwingie Sajenti.
Chumba cha Geza kilikuwa na mbu sana, walisikika wakiunguruma na waling’ata haswa lakini sasa Sajenti alikuwa amewasahau kutokana na maneno ya Geza.
“Sasa Geza kwanini unataka tujihakikishie kuwa mabinti hawa wanateseka katika utumwa wa ngono?” aliuliza Sajenti kwa umakini kabisa.
“Unadhani ingekuwa ni kazi za ndani mtu amegoma kufanya ndo wangemuua kama walivyomuua huyu dada sijui Hajrati sijui nani majina ya kiarabu haya mi sijui…” alijibu Geza.
Jibu lile likawapa uelekeo, kwa pamoja wakakubaliana kuwa kuna msaada wanahitaji kutoka kwa IGP.
Walihitaji ruhusa maalumu ya kwenda uhamiaji na pia kuonanana na wawakilishi wa waziri wa mambo ya nje.
Wakati wawili hawa wakianza rasmi harakati, huko Oman Rama naye aliendelea kuitafuta kweli itakayowatesa walioificha.
_____
RAMA ANASIMULIA.
ILIKUWA ni siku nyingine tena katika chimbo lile la umauti, wenzangu walikuwa wanazidi kupukutika huku wengine wapya wakiingia, watu walikuwa wamekata tama sana na maisha na wengi hawakunijibu kwa lolote nililotaka kuzungumza nao.
Wangeongea nini angali walikuwa wanajitabiria vifo vyao?
Ndugu msikilizaji kifo kina dalili mbaya sana na usiombe aliyepo pembeni yako anakufa kisha unalazimishwa umbebe, umvue nguo zake na kisha ukamtupe kama mzoga!
Hapa ndipo hofu ya kifo hutanda kwa kila mja!
Nilipokuwa mafunzoni JKT kambi ya Mafinga kuna mwenzetu mmoja alipoteza maisha, watu tulidumu katika hofu kwa majuma kadhaa kila mtu akijiona kesho ni zamu yake kufa.
Sasa katika chimbo hili la mauti kila siku mtu mmoja alikufa tena anakufa mnamuona anavyopambana kuizuia roho isimsaliti na kuuacha mwili.
Nilikuwa nimeanza kuziona njia moja ama mbili za kuweza kutoka katika chimbo lile, nilijua kabisa nikiwa jasirinaweza kufika tena katika ile Oman halisi Oman yenye sharia kali niwashtaki wachache hawa wanaochafua jina la nchi, wachache wasiojua umuhimu wa maisha ya wenzao bali utajiri na ufahari wao.
Lakini kitu kilichonifanya nisichukue hatua ni kitendo cha kuwaacha wenzangu nyuma huku nikijua wazi kuwa watakufa tu!
Kibaya zaidi nilipotaka kuzungumza nao juu ya mpango kabambe hawakuwa tayari kunisikiliza. Kwa mmoja ama wawili waliozungumza walinisihi tu niachane na maisha yao kwa sababu wao ni wa kufa tu!!
Majibu yao yalinikatisha tama, na hapa nikaamua kupiga hatua mbele. Nikapiga goti kisha nikainama na kusujudu nikamkabidhi Mungu kila kitakachotokea mbele yangu.
Na hapa akili yangu yote nikaipeleka katika bomba la maji ambalo hufunguliwa asubuhi kwa ajili ya kukinga ili kusafishia vyuma vyao, kisha jioni kufungwa.
Kwa sababu nilikuwa nimeamua kujitoa muhanga sikutaka kumshirikisha yeyote asiyetaka kuzungumza.
Usiku ulinikuta nikiwa macho, mahali tulipokuwa tunalala tulichanganywa waume kwa wake. Nilimwona bwana mmoja mweusi ambaye pia alikuwa msimamizi katika chimbo hilo akimng’ang’aniza binti mmoja kwa nguvu sana hatimaye akambaka.
Nilishuhudia kwa macho yangu kitendo kile, binti alijaribu kupiga kelele lakini yule bwana hakujali akaendelea na alichokuwa amekusudia.
Nilimtazama na kisha kuikariri sura yake mbaya iliyojaa chuki!
Haikuwa mara ya kwanza kuona wakimbaka mfanyakazi mwenzangu, lakini hii ya siku hii kwa sababu tayari nilikuwa nimeamua kufanya kitu nikamsubiri akolee!
Nikawa namsoma sura yake hadi akakolea na kujisahau kama alikuwa anabaka akajiona yupo katika penzi halali na hapo nikajirejea mafunzo tuliyopewa jeshini ya kutembelea tumbo, nikatambaa hadi nikamkuta akiwa amefumba macho akifurahia anachokifanya.
Nikamvuta nilipokuwa, na kabla hajaweza kusema lolote nikamtandika ngumi kali katikati ya shingo.
Akabaki kukodoa macho asiweze kusema neno lolote, nikamnyoonya akawa amelala kama wengine walivyolala. Nikamdhibiti hadi nikahakikisha kuwa amepoteza maisha, nikamvua nguo zake taratibu kabisa akabaki uchi wa mnyama.
Ili nisiwaletee wenzangu balaa siku itakayofuata nikafanya kama tulivyoagizwa.
Nikasimama na kuita jina la ALWATANI… wasimamizi wote walipenda kuitwa hivyo.
Sijui kwa ulwatani gani waliokuwanao…
Alipoitika kiusingizisingizi nikamweleza kuna mwenzangu amefariki.
Kama ilivyo kawaida yao akaniambia nikamzike.
Hilo ni kosa kubwa sana walilofanya.
Nikalibeba lile jinamizi na kutoweka nalo.
Nilipofika kule chumba cha maziko nikamtupa. Kisha nikavaa nguo zake na moja kwa moja nikaelekea katika bomba pana la maji…..
Kiunoni mwangu nikiwa na silaha ninayojua kuitumia.
Bunduki!

Hofu ilikuwa jirani yangu wakati wote, na nilikuwa sawa kabisa kuwa na hofu kwani sikuchukua muda mrefu katika bomba lile kabla sijaanza kukutana na hekaheka!
Dunia ina mambo jama lakini haya mambo ninayokusimulia omba yasikukute wewe!!

Nilipotoka nje nikatazama mazingira halisi ya pale nje ikiwa nitatoa kile kifuniko, basi kwa namna yoyote ile maji yatatoka kwa kasi na kuzua balaa wale wasimamizi wakigundua jambo hilo na huo utakuwa nd’o mwisho wangu katika harakati za kutoroka na badala yake nitaishia katika mikono yao watanitesa sana na kuniua huku dunia ikiwa haijui lolote lile.
Sikutaka usiku huu wa matumaini upite hivihivi.
“Mwanajeshi kamwe harudi nyuma!!” niliikumbuka kauli tuliyokuwa tunapewa mafunzoni.
Nami sikutaka kurudi nyuma, nikarejea tena hadi kule walipokuwa wamelala wenzangu. Nikajikohoza kidogo kisha nikamuita tena Alwatan na kumweleza kuwa tumbo lilikuwa linaniuma sana.
Akaanza kunitusi sana, sikuchoka kumtia kero ili atoke kule alipokuwa aje katika ukumbi wetu wa kulala.
Mara nimwambie tumbo, mara nimwambie nimechoka kuishi!
Kweli akaghadhabika akashuka huku akitokwa na matusi mazito kiingereza na kiarabu.
Alipofika ukumbini akiwa hajajiandaa kabisa kwa shambulizi nililolipanga alijikuta akisalimiana na sakafu kisha nikatua juu yake, nikamkung’uta ngumi tatu kali shingoni akakakamaa!
Ukitaka ushangae maisha tuliyokuwa tunaishi kule, hakuna aliyejali kilichokuwa kinatokea wote walikuwa wamejikatia tamaa ya kuishi!
Sasa niliuona uhuru zaidi, nikamvua na yeye nguo na kumtupa kule ambapo walipatenga kwa ajili yetu pindi tunapopoteza maisha!
Baada ya hapo nikaingia tena katika lile bomba, hapa nikiwa na bunduki mbili katika himaya yangu. Zote zikiwa na risasi!
Nilikifikia kile kifuniko na kukifungua kisha nikajiachia maji yakanisukuma kwa kasi kubwa sana na kunitupa nje, nilishtuka kiuno lakini kama nilivyosema nilikuwa napigana ili ukweli huu uwafikie ninyi wasikilizaji na wasomaji.
Maji yalimwagika kwa kasi kubwa sana hadi yalipokoma pale ndani palikuwa kama bwawa. Maji haya yaliwashtua baadhi ya mateka wenzangu, lakini hawakuonyesha kujali, ni kama akili zao zilikuwa zimepumbazika kupita kawaida hasahasa walipokuwa wanautambua kuwa mwisho wao ni kifo.
Nikapenya tena na kuingia katila lile bomba nikaingia katika chanzo cha maji yale!
Lilikuwa na tanki kubwa kiasi la maji, nikaingia na kujikuta nikiwa napambana na giza nene sana, ombi langu kwa muumba likiwa moja tu….
Aniepushe na wadudu hatari ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuwa katika ile hifadhi.
Naam! Niliteseka narudia tena niliteseka sana lakini kamwe sikuwahi kukata tama, lilikuwa ni giza nene sioni mbele na wala sitaki kurudi nyuma tena.
Ndugu msikilizaji ukiamua kupigania jambo, kwanza mtangulize Mungu kisha jiamini kuwa unaweza kulifanya jambo uliloamua licha ya vikwazo utakavyokutana navyo…. Na mwisho piga hatua mbele na kamwe usikubali kurudi nyma.
Mimi Rama cha moto nilikiona, kila hatua niliyokuwa namaliza ni afadhali kuliko ile niliyokuwa naingia!!!
Mbu wale sijawahi kukutana nao maishani ndugu msikilizaji, na vile nilikuwa nimelowana walinipiga haswa, na ni kama walikuwa wanaalikana!
,bu hawa wakanikumbusha siku ile nilipokuwa nahojiwa na sajenti Pilipili kwa kesi isiyokuwa yangu kabisa.
Wakati namuwaza sajenti Pilipili na mateso aliyonipa kabla ya kunitupa katika janga hili mara nikasikia mchakacho fulani pale ndani, zilikuwa ni kama hatua za kiumbe hai!
Mapigo ya moyo yakaanza kupiga kwa kasi sana, giza lilikuwa nene mno na sikuwa naweza walau kubashiri ni kiitu gani kile ndani ya lile tanki.
Je, ni mnyama mkali anajiandaa kunishambulia, ama ni kiumbe hatarishi kinachonisaka?, ama ni wale walinzi wamegundua hila ambayo nataka kuwafanyia na sasa wanataka kunikwapua waniue kwa mateso makali?
Hofu ikachukua nafasi, nikajipapasa na kuitoa bunduki moja….. lakini nitaielekeza wapi?
Hili lilikuwa swali gumu sana!
Nikatulia tuli huku nikingoja kile kiumbe kama kitajaribu kushambulia basi na mimi nitashambulia hapohapo, ila nilikuwa najiuliza kuhusu ile bunduki je tayari imeandaliwa kutoa risasi? Maana nilikuwa gizani na nilikuwa katika hofu kuu.
Kimoyomoyo nikamuomba Mungu ile bunduki iwe tayari kwa ajili ya kufyatua ili adui yangu asiweze kuniwahi!
Nikiwa namwombea mabaya adui yangu mara nikasikia tena hatua nyingine.
Adui yangu ananiona!! Nilijisemea.
Nikapiga hatua nyuma kwa kunyata.
Mungu wangu! Nikakutana na utelezi ukanivuta nikapiga mweleka chini, bunduki ikanitoka na hapo nikamsikia adui yangu akinikimbilia.
Nilitetemeka vibaya mno.
_______
NCHINI TANZANIA
SAJENTI Pilipili na Geza walikuwa wamepata Baraka zote kutoka kwa IGP juu ya uhalali wao kutembelea ofisi ya waziri wa mambo ya nje na pia ubalozini, pia waliruhusiwi kufahamu mambo kadha wa kadha juu ya mambo yanayotokea ubalozini na uhamiaji!
Katika mpango huu Geza Ulole alisimama kama mwandishi wa habari wa kujitegemea.
Hawakuwa wawili katika safari hii, bali walikuwa watatu.
Sajenti alikuwa hajaafikiana sana na mpango aliousuka Geza ili kuupata mwanga wa tukio wanalofuatilia lakini Geza alisimamia kile alichokiamini na kisha akamsihi sajenti awe mtazamaji tu aone nini kinatokea.
Walifika ofisi ya waziri wa mambo ya nje na Geza akiwa kama mwandishi alihoji mambo kadha wa kadha kisha akaingia pia yule binti waliyeongozana naye, lakini hapakuwa na mabadiliko yule binti alimsalimia waziri na hayakuonekana mabadiliko yoyote katika sura ya waziri.
Kwa hapa wakawa wamegonga mwamba!
Safari yao ikaendelea, hatimaye wakafika uhamiaji.
Kwa sababu walikuwa na vitambulisho vya kuwaruhusu kuingia bila kujalisha dharula yoyote eneo lile basi ilikuwa rahisi sana kuingia.
Wakaingia wawili yule bintiakafuata nje.
Mazungumzo yao hayakupita hata dakika tano mara yule binti akaingia mle ndani akiwa anatembea upesiupesi.
Akafika na kumnong’oneza kitu Geza.
Geza naye akamnong’oneza sajenti, kisha wakaaga na kuondoka wakidai kuna dharula.
“Alivyoniona amekodoa macho sana na akaangusha bahasha yake…” alizungumza yule binti aliyejulikana kwa jina la Nasra pacha wa marehemu Hajrati.
Geza akatabasamu kisha akamtazama Sajenti.
“Tumekaribia nusu ya safari yetu!”
Binti akaelekeza mahali alipoingia mtu yule.
“Nenda ukamdhibiti maana nikienda mimi mtaonota maiti badala ya muhusika.” Geza alimweleza Sajenti.
Sajenti alimtazama kwa mshangao mkubwa sana Geza. Lakini hakusema neno akaondoka na Nasra hadi katika ile ofisi.
Wakaingia bila hodi.

La! Haula! Wakakuta watu watatu.
Mmoja kati yao akiwasimulia juu ya kukutana na Nasra ambaye wote walimtambua kama Hajrati.
Kitendo cha wawili wale kuingia ghafla kikazua tafrani.
Sajenti pilipili akalikumbuka swali aliloulizwa na Geza wakati wa mpango huu.
“Hivi utachukua hatua gani ukikutana ana kwa ana na mtu ambaye unaamini fika kuwa amefariki, na huenda maiti yake uliyaona?”
Sasa majibu yalikuwa yanajionyesha wazi, wale watu wote walikuwa wanamwogopa Nasra!
Wote wakijua ni Hajrati pacha wa Nasra yule aliyepoteza maisha.
Sajenti akatoa kitambulisho chake na kisha akawaweka chini ya ulinzi watu wale watatu.
Kwa sababu walijua walichokuwa wakikifanya walijaribu kufanya kukuru kakara za hapa na pale waweze kuchomoka katika mikono ya sajenti, na mmoja wao alifanikiwa kupenyeza mlango kiasi cha sajenti kuhisi kuwa amemponyoka.
Lakini alirejea mzima mzima ghafla akitua sakafuni.
Mara akaingia Geza!
“Nimemkosakosa teke aisee?” alisema Geza huku akitabasamu.
Sajenti akabaki kuduwaa, lakini alianza kumzoea Geza!
Unamkosaje mtu teke kisha anatua kama mzigo ndani?
Mpango wa Geza ukawa umenasa, watatu wale wakaulizwa ikiwa wanamfahamu yule binti, wawili wakakiri kumfahamu kwa jina la Hajrati mmoja akaweka ugumu na kusema hajui lolote.
Huyu ndiye aliyeshughulikiwa ipasavyo hadi akasema kila kitu alichokuwa anakijua.
Na jina lake aliitwa ERIC MLEWA!!

WALA hakuwa amedanganya jina lake, ni kweli aliitwa Eric Mlewa, akaelezea kuwa kazi yake ya awali ilikuwa ni udalali jijini Mwanza, kazi ambayo haikuwa ikimlipa vizuri lakini katu hakuwahi kulala njaa.
Siku moja alikutana na bahati ya mtende pale alipopata mteja anayetaka nyumba nzima, na mkononi Eric tayari alikuwa na nyumba hiyo. Akamtajia bei kisha akampeleka nkatika nyumba hiyo!!
Kama ilivyo kawaida ya madalali sio wakimya, huzungumza sana mithiri ya dereva taksi.
Eric alizungumza mengi na yule mteja ambaye alikuwa amempakia katika gari lake wakielekea huko nyumba ilipokuwa inapatikana, Eric alizungumza mengi sana na kuonyesha ni kiasi gani anaujua ule mji mzima.
Maongezi yale yakamvutia yule mteja,hata baada ya kumfanikishia kupata nyumba yule bwana akamtafuta Eric kwa mara nyingine na hapa akamtangazia kazi iliyokuwa na manufaa makubwa, ilikuwa kama udalali lakini huu ni udalali wa kutafuta watu.
Wasichana wenye umri usiozidi miaka kumi na tano wasiokuwa na kile chochote na ikiwa vyema wawe na ule mvuto wa kike.
Eric aliona kazi hiyo ni ndogo sana kwake, akapewa maelekezo na kuanza mara moja.
Ni katika kazi hiyo maisha yake yalibadilika na hakuwahi kujiuliza kuna nini kimejificha nyuma ya pazia.
Aliishia kuambiwa kuwa hao wasichana wanakwenda kufanya kazi nzuri kabisa nchini Oman na huko Dubai. Alipowauliza wao wananufaika nini, akajibiwa kuwa asilimia ishirini ya mshahara wa hao mabinti ndo posho yao.
Neema zikamuangukia Eric Mlewa, kwa juma moja alipata hadi wasichana wawili, anawakabidhi kwa huyo mkuu wake wa kadhi na analipwa chake.
Baadaye kwa sababu ya uchapakazi wake akapandishwa cheo na kuongezewa kazi na posho, alitakiwa kutafuta msichana kisha yeye ndiye anamshughulikia masuala ya pasi ya kusafiria.
Eric akajenga nyumba kubwa jijini Mwanza, pembezoni kidogo maeneo ya Shamaliwa.
Maisha yakabadilika!
Baadaye akahamishiwa ofisi za Dar Es salaam.
Alipofika huku alikuta mzozo uliojitokeza juu ya mfanyakazi aliyetoroka nchini Oman na kurejea Tanzania huku akiwa na siri nzito.
Siri ambayo kamwe Eric hakuwahi kuifahamu.
“Kwa kweli nilianza kuhisi kuwa kuna mchezo mchafu unaendelea huko Oman dhidi ya hawa mabinti lakini sikuwa na namna ya kufanya, tayari nilikuwa katika huu mtandao….. siku kadhaa baadaye nikamwona huyo binti. Nilimuona katika picha, na hapo nikawaona vijana watatu waliopewa juikumu la kumrejesha kazini.
Siku kadhaa baadaye katika gazeti nikaona taarifa ya huyo binti kukutwa ameuwawa…. Niliona gazetini.” Alisita Eric kusimulia kisha akaendelea na hapo mbele yake walikuwepo watu watatu, IGP, Sajini Pilipili na Geza asiyekuwa na cheo.
“Nilifadhaika sana na kuhisi kuwa wale akina dada wote niliowashawishi kwa maneno matamu ya kidalali kisha wakaenda Oman wapo katika mateso, nakiri kuwa sikuwahi kushtaki popote hadi leo hii nipo mikononi mwenu wakuu. Ila sijui lolote kuhusu mtandao huu…. Nimejikuta tu ndani yake.” Alimaliza kusimulia Eric Mlewa.
Geza alikuwa hamtazami machoni, alipomtazama kwa mara ya kwanza alikuwa na swali kwake.
“Kwanini ulitaka kukimbia mpaka nikatumia teke kukurudisha ndani ikiwa hujui lolote…”
Eric hakutarajia swali lile, akaomba msamaha!
Hakujua anayemuomba msamaha ni mtu wa ainja gani.
Geza aliwageukia Sajenti na IGP kisha kwa upole kabisa akawaambia.
“Mmemsikia wenyewe ananitukania mama yangu…. Mmemsikia kwa hiyo msije kusema mimi mkorofi” na mara ghafla akajirusha na kumfikia Eric akamtandika ngumi moja kali sana katika sikio lake na hapohapo akamuuliza.
”Unasikia kitu gani sikioni kwako?”
Eric alikuwa hasikii chochote bali miluzi mikali kabisa.
Geza alijua kuwa hasikii, akamwacha kwa sekunde kadhaa.
“Geza muache usije kumuua bwana… tunahitaji kumsikia.” IGP alimuonya Geza.
Geza akasusa, akasimama atoke nje!
IGP kamfuata nyuma.
“Mkuu unamuoneaje huruma huyu mpumbavu? Hebu nenda ukamuulize kama wakuu wake walijiuliza wakati wanaikunja shingo ya Hajrati hadi akapoteza maisha, huyo ni mmoja ambaye tunamfahamu, unadhani wameua wangapi?? Je? Kuna hata mmoja wao amewahi kusimama akasema, ‘mwache huyo binti utamuua?…….. Geza alihoji bila kugeuka nyuma.
IGP akakiri kimya kimya kuwa Geza anajua anachokifanya na wala hakurupuki!
Kimoyomoyo akatamani kama siku moja Geza angejiunga na jeshi la polisi avikwe vyeo afanye kazi kihalali kabisa.
Lakini hiyo haikuwahi kuwa ndoto ya Geza Ulole.
“Nenda ukazungumze naye Geza… we nawe kidogo tu unataka utukimbie… au umeshawakumbuka wale mademu zako.” IGP kamtania Geza.
Na kwa mara ya kwanza katika maisha yake akayaona meno ya Geza akiwa anacheka!
Mkuu wa jeshi la polisi akajifunza kitu!
Geza akamwendea Eric Mlewa ambaye sasa alikuwa anaweza kusikia tena vizuri.
“We dogo! Niliwahi kuwa mpumbavu kama wewe, wakuu wangu wa kazi wanafanya ujinga kisha wananijaza ujinga eti siku nikikamatwa nisiseme lolote…. Usiwe mjinga kama nilivyokuwa mimi dogo. Nitakuua vibaya mno….na nikiamua kukuua siui kwa dakika moja, nitatumia masaa mawili na nusu hivi ili ukasimulie huko motoni inauma kiasi gani kutolewa roho na Geza.”

Maneno haya yakamwingia Eric, akaanza kuimba mengine anayoyajua kuhusu ule mkakati.
Akataja kuwa mkakati ule unahusisha mtu mzito nchini ambaye hajawahi kulijua jina lake lakini kuna siku alisikia wakimtaja kama kamanda, akaelezea kuwa ni mradi endelevu wa kurithishana na ni mradi ulioanzia Zanzibar koloni la zamani la waarabu wa Oman.
Mradi wa kupeleka wasichana Oman kufanya kazi huku wakilipwa kiduchu, lakini kuhusu kuwanyanyasa wasichana alikata kata kata hajawahi kusikia juu ya hilo.
Geza akamtazama na wala hakumpiga tena, akawavuta IGP na Sajenti Pilipili kando kisha akawaeleza kwa ufupi.
“Huyu kijana ametapika hadi nyongo”
Wote wakaduwaa, IGP akalalamika, “ndo maana nilikwambia usimpige utaua!!”
Geza akatabasamu akatambua walikuwa hawajaelewa maana yake, “Amesema kila kitu anachokijua….” Geza akafafanua kwa utulivu.
“Umemuaminije?”
“Nimemuuliza vizuri sana kwakweli.” Aliwajibu na kisha akamwachia Sajenti Pilipili jukumu la kuwahoji wale wawili waliobakia.
“Sasa unaenda wapi Geza?” Sajenti alimuuliza.
“Kule uliponitoa siku ile, wale mademu wamenitumia meseji wanalalamika eti sikulipa bili siku ile wamekamatiwa simu zao pale baa…. Naenda kusafisha jina mara moja!!” alijibu Geza huku akiondoka zake.
IGP na Sajenti walibaki na mzigo wa matabasamu bandia katika nyuso zao!
Geza alitoweka!!
Ni kama kuondoka kwa Geza kulizua balaa ama labda kuondoka kwa Geza alilikwepa balaa jipya!
______
NCHINI OMAN
Rama anasimulia!
Nilikiona kifo kikiwa kinaunda urafiki na mimi waziwazi kabisa, na sikuwa tena na silaha.
“Brother… help me… take me out with you” niliisikia sauti ikinisihi, ilikuwa ni sauti ya kike. Hapo hofu ikapungua ya kudhani ninakabiliwa na maadui ama kiumbe hatarishi.
Nikamuuliza kiingereza yeye ni nani akanijibu kuwa tulikuwa wote kule chimboni. Nikamuuliza maswali mawili matatu yaliyonijengea imani, kwa kupapasa nikaipata silaha yangu na hapo nikamsihi asogee nilipokuwa, akafanikiwa kunifikia, nikamgusa na kumwambia atulie palepale alipokuwa nitafute namna ya kutoka katika lile tanki ola maji.
Nilipapasa huku na kule hadi nikafanikiwa kuipata ngazi, nikaijaribu uimara wake kisha nikapanda hadi juu. Nikachungulia.
Hapakuwa na mtu yeyote yule!
Nikashuka hadi chini na kumweleza yule binti anifuate, tukapanda ngazi hadi kutoka nje kwa uangalifu mkubwa sana.
Eneo lote lilikuwa kimya kabisa, tukapita hadi tukafikia sehemu ambayo tulikutawatu wamelala, walikuwa wawwili.
Nikamzuia yule binti asiendelee kwenda mbele bali mimi mwenye silaha.
Nikajirusha upesi na kutua karibu na watu wale wawili.
Bunduki yangu mkononi, nikatarajia watainuka na kufikia mikononi mwangu.
La! Hawakuinuka, nikajaribu kumtikisa mmoja, lakini alikuwa wa baridi sana.
Maiti! Nikajisemea na nilipomgusa yule wa pili hali ilikuwa ileile.
Nikiwa bado palepale kwa mbali kabisa nikasikia sauti zikizungumza kwa luha ya kiingereza, kwa sababu ya mwangwi kuwa mkubwa sikuweza kusikia jambo lolote lakini mara nikawa nasikia neno Tanzania likirudiwa mara kwa mara, nikatega sikio nisikie walau nini kinajiri Tanzania lakini mwangwi uliniathiri na ninakiri kuwa si mwangwi pekee uliokuwa kikwazo hata lugha ya kiingereza kwangu haikuwa nyepesi hasaha mtu akizungumza upesiupesi.
Hapa nikabaki katika mkanganyiko wa aina yake!
Mara baada ya mazunguzo yale kengele ikagongwa kwa nguvu sana, na hapo nikaona taa zikianza kuwashwa.
Nikakimbia upesi sana na kumfikia yule dada niliyemuacha nyuma.
Nikamshika na kumlaza chini, jirani kabisa na zile maiti!!
“Usikubali kutikisika… usitikisike hata kidogo watatuua….” Nilimsihi huku nikikiri mbele yake kuwa tuna asilimia tano tu za kutoka hai ndani ya chimbo lile na tuna asilimia 95 za kupoteza maisha.
Kengele ikapigwa tena!! Sasa kila sehemu mwanga ulitanda……
Yule binti akajikojolea, nikamwonea huruma kuliko nilivyokuwa najionea mimi.
Kuja kushtuka nami mkono ulikuwa umepenya, kitu ambacho sina uhakika ni nani alikuwa wa kwanza kujikojolea kati yangu na yule binti!

Ile hali ya kila mmoja kujikojolea kwa wakati wake ilimaanisha kuwa hakuna aliyekuwa amekizoea kifo.
Ni kweli kifo kipo lakini hofu huja pale unapokiona kikija upande wako.
“Vua nguo upesi!” nilimwambia kwa kunong’ona yule binti naye harakaharaka kwa ustadi akalirarua gauni lake lililochakaa, wakati anamaliza na mimi nilikuwa uchi wa mnyama nguo nikiwa nimezitupa kando.
Ama! Asikusimulie mtu ambaye hajawahi kukutwa na balaa la namna hii, nisikilize mimi ambaye lilinikuta moja kwa moja.
Hakuna aliyemwonea aibu mwenzake, sasa tulitulia tukawa sawa kabisa na wale maiti. Mimi nilifumba macho yangu na kusubiri hatma ya jaribio lile la kujiokoa.
Sauti ile iliyokuwa inazungumza kwenye simu sasa ilisikika ikitoa amri bila shaka kwa walinzi ndani ya lile chimbo.
Amri ile iliendelea kunichanganya na vile nilisema awali kuwa sikuwa vizuri katika kusikia kiingereza hasahasa mtu akizungumza upesiupesi, lakini bado nilisikia neno Tanzania na mara moja walitaja jiji la Dar es salaam.
Aliendelea kuzungumza, mara nikamsikia yule binti akiniita.
Alizungumza akiwa ametulia vilevile na mimi nikiwa nimetulia pia.
Alinieleza kwa kiingereza chenye lafudhi ya kiafrika magharibi zaidi nami nilielewa, alisema kuwa maiti wote wanatakiwa kuzikwa upesi sana!
Aliposema hivyo nikajikuta nafumbua macho!
Hofu!
Ndugu msikilizaji kwangu mimi niliona ni afadhali kufa kwa mateso lakini sio kuzikwa nikiwa hai.
Nikiwa bado sijajua cha kufanya nikasikia hatua zikisogea kule tulipokuwa kwa kasi ya ajabu.
Sasa sikuwa na silaha yoyote bali uchi wa mnyama, nikamsihi yule dada aitetemeke hata akiguswa pia asikakamae bali ajilegeze.
Ikawa hivyo wale watu walivyofika pale hawakukagua hata kama kuna viumbe bado vinapumua badala yake walitusomba na kutupakia katika kitu mfano wa toroli kubwa.
Ulikuwa ni mchanganyiko wa maiti nyingi, waafrika kwa wahindi, baada tu ya kurushwa mle ndani nikageuka na kumsisitiza tena yule binti asikubali kuzamishwa chini ya maiti wengine, hivyo kila iliyorushwa maiti ikawa ni kazi kuinyanyua yenyewe iende chini nasi tuendelee kubaki juu.
Dada alijituma haswa na machoni alionekana kuwa hakika anaupigania uhai na uhuru wake.
Yule binti akanikumbusha kitabu cha nguli wa riwaya za taharuki nchini Tanzania, Hussein Issa Tuwa katika riwaya ya Mkimbizi alivyomuumba Tigga Mumba, kama msichana mpambanaji anayeipigania haki na uhai kwa jasho, machozi na damu. Huku akifanikiwa kuwashinda watu waliokuwa na mtandao mpana kabisa wa kinyang’anyi nchini Tanzania.

Na kufikia pale nikambatiza jina la Tigga Mumba bandia japokuwa sikuwahi kumueleza maana ya jina lile na chimbuko lake.
Toroli lile lilianza kuvutwa kuelekea mahali ambapo tulitambua kuwa shughuli za uzikaji zinafanyika.
“Tigga, ukiona wanataka kukuzika piga kelele tusikubali kuzikwa hai.” Nilimsihi naye akatikisa kichwa kukubali. Hakujali kuhusu jina, bila shaka hata ningemuita jina la kiume bado angeitika ‘rabeka’
Toroli lilienda kwa muda zaidi na kila mara lilikuwa linasimama na maiti zinaongezwa.
Ilikuwa hali ya kutisha sana kuishi na maiti nyingi angali ukiwa hai.
Kuna baadhi ya maiti zilikuwa zinatisha kuzitazama, na sitasimulia zilivyokuwa kimuonekano.
Eeh! Mwenyezi Mungu wasamehe walioyatenda haya.
Hatimaye tolori lilisimama kwa muda mrefu kiasi kisha ikasikika amri.
Amri ya kutuzika!!
Toroli likabinuliwa na mara tukajikuta hewani! Tukimwagika kwenda chini kama tipa linalomwaga mchanga.
Tulidumu kwa sekunde takribani thelathini kabla ya kujikuta ndani ya maji, yalikuwa maji baridi japo si sana.
Kumbe wanatutupa kama mizoga ndo namna yao ya kuzika!!
Nilijisemea huku nikipambana nisizame na hapo namsaka yule binti.
Uzuri ni kwamba nilikuwa vyema katika suala la kuogelea.
Nilifanikiwa kumuona akiwa anatapatapa majini.
Alikuwa anazama na kuibuka, nikatambua kuwa hakuwa akijua kuogelea, nikapiga mbizi na kumfikia. Nikafanya jitihada za kumuokoa.
Tatizo lilikuwa moja, kila nikijaribu kumwokoa ananishika kwa nguvu sana mimindo nazama.
Hiyo ni kawaida sana linapokuja suala la majini, yule anayeokolewa humzamisha muokoaji.
Nilipambana sikukubali kumwachia azame angali tumetoka mbali sana. Huyu angenifaa sana katika kusimulia mengi yanayojiri katika chimbo la umauti.
Nikafanikiwa tukalifikia bomba lililokuwa linapita juu ya yale maji, maji tusiyojua chanzo chake.
Nilimsihi ashikilie bomba, mimi nikapanda juu ya bomba kisha nikamvuta naye akawa juu ya bomba.
“Kaka, sitakuwa na muda mrefu wa kuishi…. Nakutakia kila la heri katika safari yako, ukifika hai duniani tafadhali waambie Nigeria kuwa mimi nimefia kuzimu, nimekufa nikiteseka.” Alinieleza kwa kiingereza kinachosikika vyema.
Nilimsihi sana awe jasiri, lakini badala ya kunijibu akatabasamu. Sote tulikuwa uchi tukipigwa na baridi kali lililovumishwa na upepo.
“Ningeweza kuwa jasiri lakini hadi kufikia hapa nina hitilafu nyingi sana kaka yangu…” alianza kunisimulia mkasa wake.
Akanieleza kuwa aliletwa Oman kufanya kazi za ndani, akajituma na kuwafurahisha waajiri wake haswa lakini shida ilianza baada ya bosi wake wa kiume na watoto wake kwa pamoja kuanza kumuhangaisha wakimtaka kimapenzi, hakuwa na pa kushtaki na alitishiwa kuwa akijaribu kushtaki atauwawa vibaya sana. Akaanza baba kuwa anamuingilia, baadaye watoto zamu kwa zamu…. Alimudu kuitunza siri lakini hofu yake ilikuwa siku ambayo mke wa bosi ambaye alimtambua kwa cheo cha ‘Madam’ wake akigundua itakuwaje.
Siku zikaenda hatimaye akaunasa ujauzito, hakujua ni ujauzito wa nani, je? Ni wa baba mwenye nyumba ama mtoto mmoja wao? Maana wote waliwahi kumuingilia tena bila kutumia kinga. Alimweleza mwenye nyumba kuwa ule ni ujauzito wake lakini aliambulia jibu lililotisha sana, alielezwa kuwa akithubutu kusema popote pale kuwa ule ujauzito ameupata ndani ya nyumba ile basi yeye na huo ujauzito wake watasambaratishwa…. Binti akajaribu sana kujikaza lakini utaanza vipi kuificha mimba?
Haikuwezekana, hatimaye mama mwenye mji ‘Madam’ akagundua.
Hapo ndipo alipohenyeshwa akamwagiwa maji ya moto na kujikuta akisema muhusika wa ile mimba.
Wahusika wakamruka maili mia.
Hapo ndipo alipoelezwa kuwa kamwe hatatoka katika kasri ile akiwa na ushahidi ule wa kujazwa mimba na bosi wake akishirikiana na watoto.
Akiwa hana hili wala lile, ghafla usiku alivamiwa chumbani kwake akakamatwa na klufungwa kamba na mwisho akatupiwa katika shimo hilo la umauti ambapo aliendelea kubakwa hadi ile siku mimba yake ilipotoka akiwa humohumo.
“Natamani sana kuendelea kukusimulia kaka yangu mjasiri, lakini ni roho inataka ila mwili umekataa, baridi ni kali sana linanitafuna na litaniua hili baridi… tafadhali ukifika duniani salama nakusihi sana usijipeleke ubalozini, nenda kiumakini sana na usimwamini mtu maana wana watu wao ubalozini, ndo maana kesi zinazopelekwa hapo ubalozini, huwa hazizai matunda…..”
Baada ya kuniambia vile huku akiwa anatetemeka sana meno yakigongana mdomoni binti alinisihi tena na tena kuwa nipambane hadi mwisho maana ni mimi niliyeikaribia dunia na nimeushikilia ukweli.
Nilimsogelea na kumsihi sana asikubali kufa kirahisi, lakini haikuwezekana.
Tigga Mumba bandia, akanifia mikononi mwangu!
Niliumia sana na kujikuta nikitokwa machozi.
Baada ya muda nikalazimika kumuachia, akazama na kupotelea katika maji yale ambayo wenzangu walikuwa wamezikwa tayari ndani yake.
Yaani baada ya safari ndefu vile, amekufa!!! Iliumiza.
Sasa swali likabaki kwangu nitatoka vipi katika eneo lile hadi nifanikiwe kuingia duniani kama alivyopaita yule binti.
Na baridi lilianza kuuzidi mwili wangu uliokuwa uchi wa mnyama….
______
NCHINI TANZANIA
GARI ya polisi ilikuwa imeegeshwa njea ya jengo maalumu lililotumiwa na sajenti Pilipili kwa ajili ya kuwahoji waharifu.
Gari hili halikukaa muda mrefu sana kabla kazi yake haijaonekana.
Sajenti Pilipili akiwa na mahabusu watatu waliounganishwa pingu walikuwa wakiongozwa kuelekea katika hiyo gari.
Tayari walikuwa wamehojiwa kwa kiwango cha awali ambacho sajenti alikuwa ameridhika nachona alikuwa amepanga kuendelea kuwahoji baadaye. Hivyo walitakiwa kurejeshwa katika vyumba vyao vya mahabusu.
Baada ya sekunde kadhaa tu za kutoka pale ndani Pilipili akajikuta akishuhudia jambo ambalo mara nyingi hulishuhudia katika filamu za mapambano. Sasa lilikuwa linatokea mbele yake.
Ilikuwa ni ndani ya sekunde kadhaa tu. Ni kama jambo hili lilifanywa na watu watatu lakini kwa wakati mmoja kabisa.
Utaalamu wa hali ya juu!
Haikusikika milio ya tendo hili lakini baada ya sekunde kadhaa, miili ya Eric Mlewa na wenzake wawili ilianguka chini kama mizigo, ikiwa imeendelea kuungana vilevile na pingu!
Damu ikiwa inachuruzika vibaya mno, wote walikuwa wamepigwa risasi katika mioyo yao.
Sajenti Pilipili alizama katika kuduwaa hakuamini kuwa risasi zilizopigwa zilipita nukta chache kutoka pale alipokuwa.
Na kama zilipita hii ilikuwa ni salamu tosha kabisa kuwa hawakumkosa maksudi ila lile ni onyo kali sana kwake.
Akaanza kuhaha huku na kule akiiacha ile miili mitatu pale chini ikitiririka damu. Akatimua mbio kuelekea ndani alipomuacha IGP.
IGP alijikuta tumbo linaanza kumkata.

Mashahidi muhimu walikuwa wameuwawa kwa maksudi kabisa na kwa utaalamu wa hali ya juu mno.
Nani yupo nyuma ya mambo haya?
Hili lilikuwa swali gumu sana.
Geza Ulole alivyopigiwa simu hakupokea iliita mara ya kwanza kimya.
Mara ya pili kimya.
Mara ya tatu haikuwa ikipatikana.
IGP akishirikiana na Sajenti Pilipili wakazama katika pumbazo wasijue ni hatua gani wanapaswa kuchukua kwa wakati ule.

IGP alijikuta tumbo linaanza kumkata.
Mashahidi muhimu walikuwa wameuwawa kwa maksudi kabisa na kwa utaalamu wa hali ya juu mno.
Nani yupo nyuma ya mambo haya?
Hili lilikuwa swali gumu sana.
Geza Ulole alivyopigiwa simu hakupoke iliita mara ya kwanza kimya.
Mara ya pili kimya.
Mara ya tatu haikuwa ikipatikana.
IGP akishirikiana na Sajenti Pilipili wakazama katika pumbazo wasijue ni hatua gani wanapaswa kuchukua kwa wakati ule.
Kuona vile IGP akampa ishara Sajenti Pilipili, wakatokea mlango wa dharula huku wakiwasiliana na timu kubwa ya jeshi la polisi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi eneo lile na ikiwezekana kuwatia mikononi waliorusha risasi zile kiustadi zikaondoka na uhai wa watu watatu muhimu kabisa.
_____
KATIKA chumba kimoja kipana sana chenye mwanga hafifu kisichokuwa na samani nyingi, mwanaume mmoja alikuwa ameketi katika kiti kilichokuwa na thamani kubwa sana. Alikuwa ametulia tuli akiwa anawaza na kuwazua hata asipate jawabu juu ya kipi ambacho anaweza kufanya ili kujitoa katika shida iliyokuwa inamkabili.
Hakuwa peke yake pale chumbani kulikuwa na watu wengine wawili, hawa hakuweza kuwashirikisha yaliyokuwa yanapita kwa kasi kichwani mwake.
Alibaki katika utulivu uleule kwa takribani nusu saa kabla watu wale wawili hawajafika mbele yake na kutaka awashirikishe alichokuwa anawaza.
Akawakata jicho kali kisha akainama tena!
Wakanung’unika na kuondoka tena!
Wakarejea walipokuwa wamekaa awali.
Akawarushia tusi kwa sauti ya chini kiasi lakini likawafikia, wakazidi kunung’unika.
_____
SIMU kutoka uhamiaji juu ya balaa lililozuka la vijana watatu kukamatwa ilipokelewa na kijakazi na kisha kumfikishia mkuu wake wa kazi, punde baada ya kuzungumza na kujua kilichotokea akanyanyua simu yake na kupiga mahali alipoamini panafaa kupiga simu kwa wakati ule.
Akazungumza maneno machache sana huku akilitaja jina la Pilipili.
“Hakuwa peke yake alikuwa na jamaa mwingine ila hakuna aliyeikamata sura yake na wengi wamekiri aliyemuona anadai ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuiona sura ile…” alijieleza na kisha akakata simu.
Akashusha pumzi kwa nguvu sana, kabla simu yake haijaita akaipokea na kuzungumza maneno machache sana.
“hakikisha ndani ya masaa kumi na mbili wamenyamazishwa kabisa…. Zingatia kunyamazisha wanaohusika pekee.” Akakata simu.
KUKATWA kwa simu ile kukamaanisha kuwa kuna vita ya kimyakimya imetangazwa, Pilipi akafuatiliwa nyendo zake zote hadi ile siku waliyowachukua Eric na wenzake kwa ajili ya mahojiano, timu iliyoagizwa kuwanyamazisha wahusika ikajipanga vyema kabisa kitaalamu na kusubiri wakati ufike.
Alianza kutoka Geza Ulole mle ndani, kisha baada ya muda wakatoka waliotakikana, viwambo vya kuruhusu risasi zitoke vikaruhusiwa na roho tatu zikatokomea!
Wakatoweka wakiwa wameimaliza kazi!
Kwa umakini waliokuwanao hawakuweza kumuacha Geza awe ametoka kirahisi vile mle ndani, Geza hakutembea muda mrefu kabla hajadhibitiwa.
Wakamchukua na kumwingiza katika jumba lao maalumu, akaingizwa katika chumba kikubwa cha wazi.
Sasa yupo katika kiti chenye thamani kubwa. Mikono yake ikiwa imefungwa na ndani ya chumba kile kuna wanaume wawili wanaosononeka kwa sababu Geza hatoi ushirikiano.
Kila walipokuwa wanavutana kando huyu alisema Geza ana matatizo ya akili mara huyu akapinga, na mara nyingine yule anayepinga akienda kuzungumza na Geza naye anakiri kuwa Geza ni mwendawazimu.
Laiti kama Eric Mlewa angekuwa hai awasimulie alivyobabatizwa na teke kali la Geza Ulole akabiringita chini kama mzigo hata wasingejaribu kumjadili jinsi walivyomjadili.
Kuna muda Geza alianza kulia kama mtoto mdogo, kuna muda alikuwa anakoroma kama mzee, kuna wakati alikuwa anachekacheka bila sababu na mara nyingine alinuna.
Mara zote hizi aliambulia vibao vikali katika shavu lake.
Alihimiri yote haya, shavu lake kamwe halikuwahi kusahau vibao vikali kutoka kwa askari magereza wakati alipokuwa gerezani, na hata hakuwahi kusahau ile suluba aliyoipata mara kwa mara alipokwa anahojiwa kwa makosa mbalimbali aliyowahi kuyafanya.
Lakini sasa alikuwa Geza mpya kwa ndani lakini mwili ulikuwa uleule.
Aliisikia mikono ya watu wale ilivyokuwa laini, akawasikitikia sana.
Akaendelea kuvumilia huku akiwangoja wafanye kosa moja tu na kisha ajitambulishe kwa majina yake kuwa anaitwa Geza Ulole.
Ilikuwa yapata saa nane kwa mujibu wa saa iliyokuwa pale ukutani, saa nane usiku.
Geza kichaa akaanza kulia njaa, alilia kiasi cha kuwakera wale wanaume wawili waliokuwa na jukumu la kuhakikisha usalama upo tele ndani ya chumba kile.
Kelele za Geza zikawafanya wafanye maamuzi ya kumpatia chakula.
Nani amlishe kichaa?
Lilikuwa swali lisilokuwa na jibu la papo kwa hapo.
Kung’atwa!!
Kila mmoja akawaza kwa wakati wake huku akimuhofia sana Geza kuwa anaweza kumng’ata.
Wakakubaliana kumfungua kisha watamlinda kwa bunduki.
“Bunduki ya nini sasa Solo…. Huyu akizingua unapiga vitasa akifa shauri zake wanatupa sisi kichaa kumlinda..” mmoja alibeza maneno yakamwingia mwenzake, wakamfungua GEza na kumpatia chakula.
Ilikuwa zaidi ya kichaa, mara achukue nyama mara aache, mara ubwabwa anakula anajipaka usoni.
Akawa anaambulia matusi mazitomazito na wakati mwingine vibao katika mngongo wake.
Hatimaye chakula kikamalizika alikuwa ameshiba kwa kiasi chake, angeweza kula sana lakini kwanini ajaze tumbo wakati kuna shughuli ilikuwa inamkabili mbele yake.
Ukafika wakati wa kufungwa kamba, kwa maksudi akauleta ule wazimu akajifanya anasumbua kufungwa kamba. Wakaja wote wawili ili wasaidiane, akamuona anavyoiacha silaha yake kizembe.
Alipofika na kumkamata Geza huku akimuinamia Geza akarudi nyuma kisha akafyatuka kwa kutumia kichwa akalenga kwa staili ileile ya wao walivyotumia kuwaua wale watu watatu wenye siri.
Kichwa kikatua katika mwamba wa pua, yule bwana akatua kama mzigo bila kupiga kelele yoyote, akawa anarusha miguu huku na kule na damu ikiruka vibaya mno.
Yule mwingine akashtushwa na tukio lile,lakini akilini akiamini kuwa Geza ni kichaa na tukio lile akili yake imemtuma.

Akapoteza sekunde mbili kumtazama mwenzake, aliporejea akapokelewa na ngumi ya kijelejele katika kifua chake, akatua chini kama gunia.
Geza akiwa anajua analolifanya akasimama akaendea sahani yake ya chakula akachukua lile paja la kuku aliloliacha akalitia mdomoni akalishughulia ipasavyo wakati anamalizia akaanza kumuhoji yule bwana aliyekuwa amejishika kifua akisota pale chini.
“Nakuona dogounaitamani bunduki, ila ipo mbali…. Nina spidi moja ya hatari sana mimi…. Nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa nashinda kila siku riadha, vipi unataka tushindane?” Geza akamuhoji huku akijilambalamba.
“Yaani kifua kipana hako kangumi hadi sasa hivi unagalagala…. Kwani mnalipwa shilingi ngapi kunenepa hivyo?” alauliza kwa sauti yake ileile iliyojaa masihara, sasa alikuwa anajifuta mikono.
Yule bwana akadhani Geza hamaanishi anachokisema, akakurupuka ghafla kuikimbilia bunduki, Geza akapiga tambo tatu kubwa akamfikia jamaa akamchota miguu yote miwili jama akatua chini kwa kutumia uso wake.
“Yametoka meno mangapi hapo maana nia yangu yatoke mawili tu ya mbele ili ukitoka humu mademu wakucheke…” Geza aliunguruma na wala hakujishughulisha kuishika bunduki waliyokuwa wanaikimbilia.
“Oya! Sasa tuache utani, ehee nyie ni akina nani na kwanini mmenikamata….. nijibu fasta maana kuna mahali nilikuwa naenda kuonana na watu najua watalalamika sana sijaenda na simu yangu mmechukua mkaizima.” Alizungumza kisha akamsogelea yule bwana. Akainama chini na kumweleza bila masihara.
“Dogo ninajua kuua sana, kila kiungo changu kinaua…. Mwenzako yule tayari nimeua na sina haja ya kuhakikisha, sasa wewe sitaki kukuua kwa sababu huna meno tayari, nieleze kwa ufupi sana nyie ni akina nani na kwanini mlinikamata.”
Hofu ilikuwa jirani kabisa na yule bwana akaanza kuongea kwa shida sana, akaelezea juu ya mradi wao kwa kadri alivyoweza.
Mwishowe akamtaja aliyewapa kazi ya kuua na kumkamata yeye.
Geza akapigwa na butwaa kusikia kuwa wale mashahidi wameuwawa wakati yeye anakamatwa.
Hapo akazidi kumchimba hadi akaelezea juu ya biashara zao za Oman na hapo akakiri kuwa aliwahi kwenda Oman pia mara mbili.
“Ulienda kufanya nini, ya kwanza nay a pili. Sitauliza maswali zaidi we jibu lolote ambalo unahisi nitauliza…” Geza alichimba mkwara.
Yule bwana ambaye Geza hakutaka walau kujua jina lake alielezea safari yake ya kwanza, nay a pili, akaelezea na mengine mengi aliyoyajua, Geza akachukua ya msingi hasahasa majina ya wahusika wakubwa katika mpango huu wa aina yake uliosukwa miaka kumi iliyopita.
Yale majina yalimtisha sana Geza.
“Swali la mwisho….. hiyo rost ya kuku mliyoniletea nani ameifanyia makeke.. maana dah!” alisema Geza huku akijisukutua na ulimi wake.
Yule bwana hakujibu kitu kabla Geza hajamtandika ngumi kali ya mgongo.
“Mamaaaa Nakufaaa!!” akapiga mayowe.
Geza akamziba mdomo kisha akamwambia, “Doh! Uliwahi kuwa mtabiri? Maana unakufa kweli sio masihara”
Alipomaliza kauli ile akasimama imara kisha akaunyanyua mguiu wake na kuutuliza katika shingo ya yule bwana kwa nguvu zote.
Hakugeuka kumuangalia akatembea hapa na pale akalifikia sahani lilokuwa limesheheni nyama za kuku.
Geza akazifakamia huku akisifia utaalamu wa aliyezitengeneza.
“Ndo maana haya majinga yanakuwa na vimikono laini laini….” Akageuka tena akazimwaga zile nyama huku akijilazimisha kutapika huku akijutia kuzila nyama zile na masimango ya hapa na pale.
Hakuweza kutapika.
Akili ya Geza aliijua ye mwenyewe.
Akatoka pale na kutaka kuondoka, akasikia kuna kitu kama kishindo kinasikika kwa mbali, akawa makini akasikiliza zaidi. Ghafla kikatoweka kile kishindo, Geza akaiendea bunduki na kuitwaa, lakini haikudumu katika mkono wake kwa muda mrefu. Ikapigwa teke kali.
Ile Geza anakaa sawa akapokea mapigo matatu makali mbavuni kwake akayumbayumba.
Akajaribu kumshambulia mpinzania wake lakinihali ilikuwa tete akapokea tena mapigo matatu kutoka katika mguu wa yule mtu aliyeibuka ghafla katikati ya chumba kikubwa.
Geza akaacha kudharau sasa akayapanga mapigo yake yale yaliyomfanya aitwe kaka mkubwa au steringi gerezani.
Akamruhusu mpinzani wake amsogelee karibu huku akiyavumilia mapigo yake makali, baada ya lengo kutimia akafyatuka kwa kutumia kichwa chake akakutana na mguu wa mpigaji.
Pasi na mashaka alimtegua.
Mpigaji akapiga mayowe huku akitua chini.
Geza mwenye hasira kali akamvamia pale chini yule mpigaji aliyekuwa anasota pale chini akishindwa kusimama imara baada ya mguu wake ulio peku kukutana na ujanja wa Geza wa kutega kichwa.
Geza alimfululizia ngumi kama nne za nguvu.
Akataka kupiga pigo la mwisho la kuua, mara akajikuta akitazamana na kifua kilichochomoza kuja juu huku kilichochomoza kikiwa hakijapachikwa.
Yalikuwa ni matiti madogo!!
Mwanamke!! Akashtuka Geza na kujitoa katika mwili wake.
Geza alishtuka kutokana na mambo mawili, kwanza alikuwa amehenyeshwwa na mwanamke katika mapambano ya ana kwa ana na pili alikuwa anataka kutoa shambulizi kali kana kwamba anataka kuua mwanaume.
“Wewe ni nani mwananmke. Na unahusika vipi katika mradi huu…” alihoji Geza.
Yule mwanamke alijitutumua na kuzungumza.

“Niache niondoke zangu kaka nakusihi, mmenitesa inatosha.. naomba mniache sitasema lolote….” Alijibu kwa kusuasua.
“Naitwa Geza Ulole…. Si mkazi wa humu, wewe ni nani humu.”
“Naitwa Zainabu… inspekta Zainabu” alijitambulisha.
“Mungu wangu!” Geza alijikuta akilitaja jina hili tukufu kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu sana kupita.
Akamsogelea yule binti akaitazama sura yake hakuweza kubaini chochote kwa sababu alikuwa ameichakaza tayari kwa ngumi kalikali.
“Unamfahamu Pilipili na Sungura naye unamfahamu…. Sungura ni nani?” alimuuliza kwa kumjaribu.
“IGP Sungura, Sajenti Pilipili..” alijibu kwa uhakika.
Hapo sasa Geza akatambua kuwa ameipata dhahabu bila kutarajia.
Zainabu anayedhaniwa kufa sasa yu hai mikononi mwa Geza.

ITAENDELEA

SIMULIZI Pumbazo – Ep 5

Leave a Comment