Bondia Sehemu ya Nne
KIJASUSI

Ep 04: Bondia

SIMULIZI Bondia
Bondia Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA : HUSSEIN ISSA TUWA


Simulizi: Bondia

Sehemu ya Nne (4)


Siku mbili baadaye alikuwa amekaa kwenye mgahawa maarufu wa Brake Point akijisomea kitabu cha historia ya bondia Mohammad Ali huku akimsubiri Kate ambaye alikuwa na miadi naye. Mara alishtukia gazeti likitupwa mbele yake pale mezani, na alipoinua uso wake alimuona Inspekta Fatma, ndani ya sare zake za kiaskari, akiwa amesimama mbele yake. Alishusha macho yake na kulitazama lile gazeti. Ukurasa wa michezo wa lile gazeti ulikuwa umebeba kichwa cha habari kilichomnadi: “Roman: Bondia aliyekuja kuchukua nafasi yake katika ndondi”. Chini ya habari ile kulikuwa kuna picha yake akiwa ameinua ngumi juu ilhali bondia msauzi aliyemsambaratisha kule afrika kusini akiwa amechutama kando yake ulingoni. Roman aliachia tabasamu pana na kumtazama tena yule askari wa kike ambaye sasa alikuwa ameshaketi kwenye kiti kilichokuwa mbele yake.

“Vipi afande, ina maana sasa unanifuatilia kila niendapo?”

“What’s this Roman, eenh?” Fatma alimuuliza kwa jazba huku akiioneshea kidole ile habari iliyokuwa pale gazetini, akilipuuzia lile swali la Roman.

“What’s what Fatma? Mi’ sikuelewi! Unataka kuniambia kuwa we’ hujui kuwa hilo ni gazeti?” Roman alimuuliza kwa kebehi. Fatma alifunua kinywa lakini hakusema kitu, akabaki akimtazama kwa huzuni yenye ghadhabu ndani yake. Kisha akashusha pumzi ndefu na kujitahidi kudhibiti jazba zake, kabla ya kumuuliza kwa upole.

“Kwa nini unafanya hivi Roman?”

“Kwa nini nafanya nini Fatma? Mbona sikuelewi?”

Inspekta Fatma alimtazama kwa muda, kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko, kabla ya kufafanua zaidi swali lake.

“Kwa nini unajiingiza kwenye hii michezo ya ndondi namna hii, eenh? Na kwa nini sasa hivi…una lengo gani wewe?”

“Kwa sababu ni nchi huru Inspekta, na kwa sababu kila mtu yuko huru kucheza mchezo autakao na auwezao…infact, hata wewe unaweza kucheza kama unaweza, ila nadhani kwako “marede” ndio ungekuwa mchezo muafaka!”

“Roman!” Inspekta Fatma alimaka kwa mshangao kwa jibu lile.

“Nini?”

“Ndio majibu unayonijibu hayo? Unanikosea adabu mimi wewe?”

Roman hakumjibu, badala yake alirudisha macho yake kwenye kitabu chake. Inspekta Fatma alimtazama kwa muda, kisha akamwambia kwa upole.

“Roman, hili ndilo nililokuwa nikikuasa siku kwanza kabisa ulipotoka gerezani…”

“Sikumbuki kabisa kukusikia ukiniambia kuwa nisicheze ndondi afande!” Roman alimjibu huku akifunua-funua kurasa za kitabu chake.

“Sina maana hiyo Roman, nawe unajua! We unataka kupambana na Deus!”

“Sasa hilo kwako ni tatizo?” Roman alimuuliza huku bado akiendelea kufunua-funua kurasa za kitabu chake. Inspekta Fatma alikikwapua kile kitabu kutoka mikononi mwake, na Roman aliinua uso wake huku akitoa sauti ya kukereka.

“Nitazame ninapoongea nawe Roman!” Fatma alimkemea, na kubaki akimkodolea macho huku akitweta kwa ghadhabu. Roman alibaki akimtazama kwa hasira. Hali ya hewa pale mezani ilikuwa ikinuka ghadhabu tupu.

“Sikiliza Roman…wewe na mimi tunajua kuwa we’ umezuiwa kushiriki mchezo huu Roman…”

“Sijazuiwa…nilizuiwa… ni wakati uliopita huo afande…past tense!”

“…na sote tunajua ni kwa nini umezuiwa kushiriki mchezo huu Roman…!” Inspekta Fatma alimwambia kama kwamba Roman hakuingilia kati ile kauli yake ya hapo mwanzo.

“Hiyo ilikuwa zamani sana afande, na ilikuwa amri ya kijeshi! Amri ambayo niliitii kwa miaka yote niliyokuwa nje ya ulingo. Na niliitii kwa kuwa ilikuwa ni amri halali ya kijeshi nami nilikuwa mwanajeshi ninayewajibika kutii amri zote za kijeshi! Lakini sasa mimi si mwanajeshi tena! Sasa mimi ni raia tu kama raia wengine hapa nchini na hivyo hiyo amri uisemayo hainihusu tena!” Roman alimjibu kwa hamasa.

Inspekta Fatma alibaki mdomo wazi akimkodolea macho kwa mshangao,hatimaye alipata jibu.

“Sawa Roman, inawezekana kuwa hiyo amri isiwe na nguvu tena kwako hivi sasa…”

“Sio inawezekana…ndivyo ilivyo! Hiyo amri haina nguvu kabisa kwangu hivi sasa!”

“…lakini sababu na mazingira ya amri ile kutolewa bado hayajabadilika Roman, kwa hivyo acha kujifanya mjinga…achana na hili swala Roman, tafuta jambo jingine ufanye…uishi kwa amani!”

“Kwa hiyo unataka kuniajiri niwe karani wako sasa Inspekta?” Roman alimuuliza kwa kebehi, kisha akaendelea kwa hisia kali, “Mimi ni raia niliyemaliza kutumikia kifungo changu Inspekta. Sina namna yoyote ya kupata kazi popote pale, kwani hakuna mtu anayetaka kuajiri mtu aliyetoka gerezani, sina ujuzi wowote wa kujiajiri na sina mtaji wowote kusema labda nianzishe biashara hata ya karanga! Sasa nimeamua kuendesha maisha yangu kwa kutumia michezo ili nami nijipatie rizki halali kama wengine. Si kosa langu kuwa mchezo pekee niuwezao ni ndondi Fatma, sijui ni kipi kigumu kwako kuelewa hapo, eenh? Acha kunifuata fuata bwana!” Roman alimjia juu. Inspekta Fatma alifunua mdomo kutaka kumjibu lakini hapo hapo alikatishwa na sauti kutoka nyuma yake.

“Hey, vipi…nimechelewa sana nini?” Kate alisema huku akimtazama Roman akiwa amesimama kando ya ile meza waliyokuwako, macho yake yakahamia kwa Inspekta Fatma, yakarudi kwa Roman na kuyarudisha tena kwa Inspekta Fatma, na mara moja akamtambua.

Wale wanamama walitazamana kwa muda, kisha Kate akamtupia Fatma salamu. Lakini inaelekea Fatma hakuwa na muda wa kusalimiana, na badala yake alimgeukia tena Roman kwa ghadhabu. Lakini kabla hajasema alichotaka kusema, Roman akamgeukia Kate.

“Ah, Kate! Wala hujachelewa. Tena ndio umefika katika muda muafaka haswa, kwani Inspekta Fatma hapa nd’o alikuwa anaaga.” Roman alisema, kisha hapo hapo akamgeukia Inspekta Fatma, “Kwa heri Inspekta, na…usikose kuhudhuria mapambano yangu yajayo, okay?”

Kate akavuta kiti kingine kilichokuwa pale mezani na kuketi. Inspekta Fatma alimtupia Roman jicho la ghadhabu, kisha akainuka huku bado akiwa amemkazia macho Roman.

“Huu mjadala haujaisha Roman!” Alisema kwa hasira, kisha akapachika kofia yake ya kiaskari kichwani, akageuka na kuondoka kikakamavu. Kwa muda Kate na Roman walibaki wakiukodolea macho mgongo wa yule askari wakati akiondoka eneo lile, kisha Kate akamgeukia Roman.

“Inahusu nini hii Roman?”

Roman alibaki akitabasamu huku akiendelea kumtazama Inspekta Fatma akiondoka eneo lile.

“Inahusu askari aliyeshindwa kupata akitakacho kutoka kwangu!” Roman alimjibu huku bado akitabasamu.


Siku zilizofuatia mkabala ule baina yaje na Inspekta Fatma zilikuwa za mishughuliko sana kwa Roman na bondia Deus “deadly” Macha. Baada ya waandishi wa habari kuzidi kuandika habari za Roman magazetini, wengi wao wakipewa motisha wa kufanya hivyo na Dan Dihenga, promota wa bingwa wa dunia Deusdelity Macha alimuandalia pambano jingine dhidi ya bondia kutoka Kenya, ambaye alipigwa kwa Knock-out mnamo raundi ya sita. Magazeti yakaandika sana kuhusu ushindi ule wa Deus na kidogo akarudi tena kwenye vyombo vya habari.

Dihenga naye akamuandalia Roman pambano jingine la kimataifa, safari hii akipata mpinzani kutoka Zimbabwe. Ilipofika raundi ya nne kwenda ya tano Mzimbabwe akagoma kurudi ulingoni, kipigo alichokuwa akipokea kutoka kwa Roman kilikuwa kizito sana, na refa akasitisha pambano, Roman akatoka mshindi!

Ushindi wa Roman nao ukaandikwa kwa sana na vyombo vya habari, ukielezewa kuwa ni ushindi wa aina yake katika historia ya ndondi, kwani haijawahi kutokea bondia kugoma kurudi ulingoni akihofia kipigo kutoka kwa mpinzani wake.

Sasa ikawa Deus anapambana, anashinda. Roman naye anapamana, anashinda. Ilikuwa kama kwamba kila mmoja anamtumia ujumbe mwenzake kwa kumpiga mpinzani anayepambana naye. Ikiwa ni pambano la Roman, Deus naye hakosi kwenda ukumbini kushuhudia. Na Roman naye ikawa hivyo hivyo, siku Deus akipambana naye hakosi ukumbini. Hali hii iliendelea hata kwa mapambano yaliyokuwa yakifanyika nje ya nchi, ambapo Roman na Dan walisafiri hadi nje ya nchi kushuhudia mapambano ya Deus.

Kutokana na umahiri wake ulingoni, Roman akapachikwa jina la bondia asiye na mpinzani. Jambo hili lilimkera sana Promota wa Deus kiasi cha kuita mkutano na waandishi wa habari, akisema kuwa anashangaa kuwa mabondia wasio na ubingwa wowote wasemekane kuwa hawana wapinzani wakati mabingwa wapo. Deus pia alikuwapo kwenye mkutano ule wa waandishi wa habari, na alipoulizwa juu ya hilo, alisema kwa dharau na kujiamini.

“Dunia nzima inajua kuwa mimi ndiye bingwa wa dunia…hakuna mwingine katika uzito wangu. Sasa kama kuna mabondia wasio na wapinzani, basi ni wazi hao hawana hadhi ya kuwa mabondia, watafute michezo mingine tu wacheze…kuna netiboli, marede…kuruka kamba, kombolela au mdako…yaani michezo ni mingi tu sio lazima ndondi.”

Sasa ikawa ni uhasama wa wazi baina ya mabondia Deus na Roman. Waandishi wa habari hawakufanya ajizi, walimfuata Roman mazoezini kwake na kumuuliza ana kauli gani juu ya yale maneno ya Deus.

“Mimi huwa sipigani kwa maneno…napigana ngumi ulingoni. Sasa kama kuna mtu anayetaka kujua iwapo mimi nina hadhi ya kuwa bondia au vinginevyo, apande nami ulingoni tu. Hapo ndipo kila kitu kitakuwa wazi, au unaonaje mwandishi?”

Loh, jibu la Roman likaleta mjadala mzito miongoni mwa wapenzi wa michezo, hususan ndondi. Swala kubwa sasa likiwa ni nani mbabe kati ya Deus na Roman.

“Naona sasa mambo yanaenda kama tulivyokuwa tukiyatarajia Roman…wananchi wanataka mpambano baina yako na Deus sasa!” Mark Tonto alimwambia Roman.

“Yeah…na ndicho nilichokuwa nikikitaka…mambo yanaelekea kule tulipotaka yaelekee Mark…muda si mrefu azma itatimia…muda si mrefu!” Roman alijibu huku uso wake ukionesha azma ya wazi.

Mwezi mmoja baadaye Roman akaandaliwa pambano jingine la kirafiki na bondia wa hapa hapa nchini. Pambano lilifanyika ndani ya ukumbi wa hoteli marufu ya Ubungo Plaza, ambapo ulingo wa kisasa uliwekwa maalum kwa pambano lile. Kutokana na ushabiki wa mchezo ule, ukumbi ulifurika kweli kweli siku ya pambano, na kama kawaida yake, Deus na promota wake walifika ukumbini.

Pambano lilikuwa kali sana, na bondia mpinzani alitoa upinzani wa hali ya juu kwa Roman, huku mashabiki wake wakimshagilia kwa nguvu. Mpaka raundi ya sita wote walikuwa nguvu sawa. Kutokea kule ulingoni Roman alimuona Deus akiwa na tabasamu la kejeli, akiona kuwa Roman alikuwa amewekwa katika wakati mgumu na yule bondia asiye na jina hata kidogo. Ghadhabu zilimpanda. Raundi ya saba Roman aliingia kwa nguvu na akitumia mtindo tofauti kabisa wa upiganaji na ule alioanza nao. Yule bondia ambaye tayari alishajiona kuwa ameusoma mchezo wa Roman alichanganyikiwa vibaya sana, na ndipo Roman alipomporomoshea masumbwi mazito na ya mfululizo ambayo hakuweza kuyahimili. Akawa anatupa ngumi ovyo, ngumi ambazo Roman alizipisha kirahisi sana huku akizidi kumtandika ipasavyo. Ndani ya ile raundi ya saba, Roman aliyumba kushoto na kumgusa mpinzani wake kwa ngumi nyepesi ya kulia, jamaa akayumba kushoto kuikwepa, na hapo ndipo Roman aliyejawa ghadhabu sio kwa mpinzani wake bali kwa Deus aliyekuwa akijichekesha kwa dharau nje ya ulingo, alipomvutia ngumi ya kushoto aliyokuwa inaenda kuua.

Nje ya ulingo Mark Tonto aliona kile ambacho Roman alikuwa anataka kukifanya, na aliinuka huku akimpigia bondia wake ukelele, “Roman Noooo!”

Ngumi ya kushoto ya Roman ilikuwa ikimshukia yule mpinzani wake aliyeleweshwa masumbwi, na katika sekunde ya mwisho kabisa, Roman aliirudisha nyuma ngumi ya kushoto, na hapo hapo alimchimbua yule mpinzani kwa upper cut ya mkono wa kulia.

Jamaa alienda chini kama mzigo na kutulia huko huko. Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi na shangwe. Nje ya ukumbi Mark Tonto alishusha pumzi za faraja na kuketi kitini akishuhudia jinsi watu walivyokuwa wakishangilia ushindi mwingine wa Roman. Kule ulingoni Roman wala hakuwa akizisikia zile shangwe, mishipa ilikuwa imemtutumka kwa ghadhabu wakati akienda kutulia kenye kona muafaka, wakati refa akimtangaza mshindi kwa knock-out.

Hoi hoi na vifijo vilirindima huku na huko. Roman alienda hadi ule upande ambao Deus na promota wake walikuwa wameketi na kumnyooshea ngumi Deus, kisha akajiashiria alama ya mkanda wa ubingwa kiunoni mwake na kujipiga-piga kifuani kibabe.

E bwana we!

Deusdelity Macha alichachamaa na kusimama kutoka pale alipokuwa ameketi.

“Nini wewe! Unataka mkanda wangu? Unadhani unaweza kuchukua mkanda wangu wewe?” Alipiga kelele huku akijaribu kuparamia ulingoni, wapambe wake wakimzuia na kumrudisha pale alipokuwa amekaa. Roman alibaki akimtazama huku akimcheka kwa dharau.

“Wewe huna ubavu wa kuchagama na mimi wewe!” Deus alibwata kwa hasira akiwa nje ya ulingo. “Mimi ndio bingwa wa dunia na hakuna anayeweza kunivua ubingwa huu!” Deus alizidi kujigamba kwa jazba. Roman alimcheka sana, kisha akamnyooshea kidole na kumfanyia ishara ya kuonesha kuwa alikuwa akiongea sana.

Ukumbi ulilipuka kwa shangwe na hoi hoi mpya, jina la Roman likirindima kila kona.

Wakati Deus aliondolewa ukumbini kwa kubururwa na wapambe wake, mwenyewe akitaka kupanda ulingoni kukabiliana na Roman, mwenzake aliondoka akiwa amebebwa juu juu na wapambe wake.

Kutokea kwenye kona moja ya ukumbi ule, Inspekta Fatma alikuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikitokea pale ukumbini kwa umakini wa hali ya juu, uso wake ukionesha kusikitishwa na kile alichokuwa akikiona.

“Sasa kwa nini pale ulipiga kelele kumwambia Roman No? Yaani hukutaka ashinde… au…? Sikuelewa kabisa pale!” Kate alimuuliza Mark Tonto baadaye usiku ule wakiwa kwenye kambi yao baada ya pambano. Mark alimtupia jicho la wizi Roman, ambaye aligeuza uso wake pembeni.

“Yeah…hata mimi sikukuelewa pale coach…nini ilihusu ile?” Dan Dihenga alisaili. Mark Tonto aliguna kidogo na kukaa kimya kwa muda.

“Unajua pale niliona kabisa kuwa Roman alikuwa akipigana kwa hasira zaidi kuliko busara…ni hatari sana namna ile…na mabondia wengi hupoteza mapambano kwa kuruhusu hasira ziwatawale ulingoni…lakini nashukuru nilipompigia kelele alinielewa na akajirekebisha, na tukashinda pambano!” Hatimaye Mark alifafanua, muda wote alipokuwa akitoa maelezo yale, macho yake yalikuwa yamefungana na yale ya Roman. “Sasa unaona Roman? Jazba itakuja kutuaibisha bwana!” Dan Dihenga alidakia. Roman alimtazama kidogo, kisha bila ya kujibu kitu, alirudisha macho yake kwa Mark na kubaki wakitazamana kwa muda. Baina yao, walijua kuwa ile sio sababu iliyomfanya Mark apige ule ukelele wakati Roman alipokuwa akipigana pale ulingoni usiku ule.


Siku mbili baadaye, Dan Dihenga aliitisha mkutano wa waandishi wa habari, na katika mkutano huo, alitangaza rasmi nia ya bondia wake asiye na mpinzani, Roman, kuwania mkanda wa ubingwa wa dunia katika uzito wa Super Middle. Mkanda ambao ulikuwa ukishikiliwa na bondia Deusdelity “deadly” Macha.

Kilichofuatia hapo ni malumbano makali kupitia vyombo vya habari baina ya Deus na Roman, Deus akijitamba kuwa Roman hana uwezo wa kupambana naye hata kidogo, Roman akiendelea kusisitizia kauli yake kuwa yeye ni bondia anayepigana kwa ngumi ulingoni na si kwa maneno redioni na magazetini. Na katika malumbano haya, kila mmoja alijikusanyia mashabiki lukuki, wale waliokuwa wakimshabikia Deus hapo awali, sasa walipata wapinzani waliokuwa wakimshabikia Roman. Sasa na malumbano yakahamia kwa mashabiki, na homa ya mpambano baina ya Roman na Deus ikazidi kupanda. Swala kubwa likiwa ni je itatokea siku wawili hawa wakapambana uso kwa uso ulingoni? Hii ilitokana na ukweli kwamba si Roman pekee aliyekuwa akiuwania ule mkanda wa Deus. Kulikuwa kuna mabondia wengine waliokuwa wakiutaka ule mkanda wa Deus duniani. Ndipo hatimaye, shirikisho la mchezo wa ngumi duniani, lilipopitisha uamuzi wa kumpambanisha Roman na bondia Sergoyev “the hulk” Sucuchev kutoka Serbia, ambaye naye pia alikuwa akiuwania mkanda ule. Mpambano ulipangwa kufanyika katika ukumbi wa hoteli kubwa na maarufu ya The Conrad, kandokando ya mto Nile, ndani ya jiji la Kairo, nchini Misri. Pambano lilipangwa kufanyika miezi miwili baada ya Roman kutangazwa kuwania mkanda wa Deus.

Mshindi katika pambano hili angeondoka na kiasi cha dola za kimarekani zipatazo elfu kumi na saba, na ndiye ambaye angepambana na bingwa wa dunia Deus “deadly” Macha kutoka Tanzania.


Sergoyev Sucuchev, kama jinsi ambavyo jina lake la kimichezo “the hulk” lilivyomnadi, alikuwa ni bondia mwenye mwili mkubwa, akimzidi urefu Roman kwa inchi tatu, na alikuwa amejichora tojo, au tatoo, nyingi mwilini. Alikuwa na historia ya mapambano kumi na saba ya kimataifa, kumi kati ya hayo akiwa ameshinda kwa knock-out, manne kwa pointi, mawili suluhu na kupoteza moja.

Siku ya pambano, The Conrad ilifurika mashuhuda kutoka kila pembe ya dunia, na kutoka Tanzania, Dan aliweza kutumia uwezo wake kama promota kupata ufadhili wa makampuni maarufu na makubwa nchini ambayo yalidhamini safari ya watanzania wapatao hamsini kwenda Kairo kushuhudia pambano lile, wakiwemo waandishi wa habari.

Na kwa upande wake, promota mpinzani wa Dan Dihenga,alitumia wadhamini wake kugharamia safari yake na bondia wake Deus kwenda Kairo kushuhudia jinsi ndoto ya Roman ya kumvua ubingwa Deus ikisambaratishwa na bondia yule hatari sana kutoka Serbia.

Kwa Roman lile lilikuwa ni pambano kali kabisa miongoni mwa mapambano aliyowahi kushiriki tangu aingie kwenye ndondi za kulipwa. Sergoyev “the hulk” Sucuchev alikuwa na ngumi kali na nzito, na kwa mara ya kwanza Roman alijikuta akipokea masumbwi yaliyomletea kizunguzungu ulingoni. Tangu raundi ya kwanza ya pambano,mabondia wale hawakuwapa nafasi ya kutulia vitini watazamaji wa pambano lile. Ilikuwa ni piga nikupige, na kufikia raundi ya tano mabondia wote wawili walikuwa wakivujwa damu, lakini si kwa kiasi cha kumlazimisha mwamuzi kusimamaisha pambano.

“Roman vipi…naona sasa ubadili mtindo wa upiganaji…huyu jamaa ni mzuri kweli kweli!” Mark Tonto alimwambia bondia wake wakati wa mapumziko kabla ya raundi ya sita. Roman aliafiki kwa kichwa huku akitweta. Kengele ikagonga, na mabondia wakaingia tena ulingoni kuanza raundi ya sita, lakini Roman hakubadili mtindo wa upiganaji ingawa pambano lilikuwa kali zaidi, mabondia wote wawili wakitupiana makonde mazito. Kengele ilipogonga kumaliza raundi, ilikuwa wazi kuwa raundi ya sita ilikuwa nguvu sawa baina ya mabondia wale wawili.

“What’s the matter with you Roman? Nimekwambia ubadili mtindo wa upiganaji! Una nini leo? Huyu Mserbia mjinga sana! Unataka atuadhiri hapa? Sisi tumekuja huku ili…”

“Relax Mark! Hana ubavu wa kuniadhiri yule!”

“Usipobadili huo mtindo wako atatuadhiri…”

“Sibadili mtindo Mark!”

“Why, for God’s sakes Roman, why?” Mark alipandwa wahka. Kengele ya kurudi ulingoni kwa raundi ya saba iligonga.

“Kwa sababu sitaki Deus aone mtindo wangu mwingine wa upiganaji Mark!” Roman alimjibu, kisha akainuka na kurudi ulingoni.

Raudi ya saba ilikuwa na msisimko wa aina yake, na ukumbi wa hoteli ile maarufu jijini Kairo ulirindima kwa hoi hoi na vifijo kutoka kwa watazamaji. Sergoyev “the hulk” sasa alikuwa amepandwa jazba, kwani naye alimuona Roman kuwa ni mpinzani tata kwake. Alikuwa akimuendea kwa ngumi kali na za mfululizo, wakati Roman aliendelea kumkwepa na kumtandika ngumi za hapa na pale. Ndipo ilipotokea nafasi ambayo Sergoyev “the hulk” asingeweza kuipoteza hata kidogo, pale alipotupa konde zito lililomsukuma Roman mpaka kwenye kamba, kisha akasukumwa tena ulingoni na zile kamba akionekana kabisa kuwa alikuwa amepoteza uelekeo, mkono wake wa kulia ukiwa chini na ule wa kushoto ukiwa umeinuliwa juu. Na hapo, uso wa Roman ukibaki bila kinga yoyote.

Ni nafasi ambayo bondia yoyote duniani huwa akiiombea, na Sergoyev hakufanya ajizi.

Alikwenda mzima mzima, akimtupia Roman konde la kulia lililokuwa limebeba nguvu zake zote nyuma yake. Ukumbi uliachia mguno wa fadhaa ilhali watazamaji wengine, akiwemo Deusdeadly Macha, wakiinuka vitini kwa midadi huku wakiwa vinywa wazi. Kila mtu alijua kuwa sasa Sergoyev alikuwa anamaliza mchezo.

Roman aliliona konde la m-serbia likimjia wazi wazi usoni, na katika nukta ya mwisho kabisa alijipindua haraka kutokea sehemu ya kiuno kwenda juu akilalia kulia kwake, na kwa namna isiyotegemewa, ngumi nzito ya m-serbia ilimkosa kwa kupita kiasi cha milimeta chache sana mbele ya uso wake.

Sergoyev Sucuchev aliachia mguno wa mshangao na wakati huo huo akageuza uso wake kumtazama Roman bila ya kuamini kuwa ngumi yake ilikuwa imemkosa mtanzania yule, na wakati huo huo akipoteza muelekeo na kupepesuka kama mlevi. Sasa Roman alikuwa akiutazama uso wa m-serbia ukiwa hauna kinga yoyote, na hii ndiyo nafasi ambayo yeye alikuwa akiitarajia.

Mkono wake wa kushoto uliokuwa juu muda wote ulishuka na pigo moja lililotukuka, na kushuka kama nyundo usoni kwa m-serbia. Sergoyev Sucuchev alienda chini kama gogo lililooza.

E Bwana we!

Hakika ile ilikuwa ni sucker punch ya hali ya juu na m-serbia hakuiona kabisa ilipotokea.

Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi.

Haraka sana yule m-serbia, ambaye hakuamini kama kweli alipokea pigo kwa mtindo wa ajabu namna ile, aliinuka tena, lakini miguu ikamkatalia na akaenda tena chini kwa kishindo.

Ukumbi ukaachia ukulele mwingine mkubwa.

Sergoyev bado alijitahidi kuinuka tena huku akishikilia kamba za ulingo na kupiga hatua moja…

Refa akamkibilia huku akiumuashiria kuwa atulie.

M-serbia akapiga hatua ya pili…

Sasa ukumbi ulikuwa kimya kabisa, ukifuatilia kile kilichokuwa kikitokea pale ukumbini.

M-serbia akanyanyua mguu kupiga hatua ya tatu…kisha macho yake yakapinduka na kubaki weupe tu, na akapiga mweleka mwingine mzito sana, akisambaratika chali kwenye sakafu ya ulingo.

Kwisha kazi!

Ukumbi ulirindima kwa mayowe yenye mchanganyiko wa hisia wakati refa alipomtazama Sergoyev na hapo hapo kuamua kuwa hawezi tena kuendelea na pambano. Roman akainuliwa mkono juu na kutangazwa mshindi kwa Knock-Out!

Si mchezo!

Hoi hoi, nderemo na vifijio vilitawala pale ukumbini kutoka kwa watanzania na wananchi wa nchi nyingine waliokuja kushuhudia mpambanao ule wa kukata na shoka. Hoi hoi pia zilikuwa zikirindima sehemu mbali mbali nchini Tanzania kutoka kwa watanzania waliokuwa wakiufuatilia mpambano ule wa kimataifa kupitia kwenye chaneli za Supersport na ESPN kupitia kwente runinga zao. Sergoyev Sucuchev aliyepoteza fahamu alitolewa ulingoni akiwa kwenye machela, wakati Roman alibebwa juu juu huku akiwa ameinua ngumi yake hewani, macho yake yakimtafuta Deusdelity Macha pale ukumbini bila mafanikio.

Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali vya kimataifa walimzonga Roman kwa maswali kem kem juu ya ushindi wake ule. Aliongea kwa kifupi tu kuwa kwake lile ndilo lilikuwa pambano la kugombea mkanda wa ubingwa wa dunia katika uzito wa Super Middle, na kwa ushindi ule ni kwamba tayari yeye alikuwa ndiye bingwa wa dunia.

“Lakini tunavyofahamu sisi ni kwamba mpaka sasa bingwa wa dunia bado ni mtanzania mwenzako Deusdelity Macha, Roman, sasa una maana gani kwa kauli yako hiyo?” Mwandishi wa shirika la habari la Reuters ya uingereza alimuuliza kwa kimombo.

“Ndio Roman… una maana gani? Kwani tujuavyo ni kwamba sasa unatakiwa upambane na bingwa aliyepo, Deusdeadly Macha, na mshindi wa hapo ndiye atakayekuwa bingwa!” Mwandishi mwingine alidakia.

“Kwangu mimi pambano langu na Deus si la kugombea ubingwa!” Roman alijibu kwa kimombo fasaha, kisha akafafanua; “…Kwangu lile ni pambano la sherehe tu ya kunikabidhi mkanda wangu niliojinyakulia leo hii!”

“Hatujakuelewa Roman…” Mwandishi wa chanel ya televisheni ya Al-Jazeera aliuliza. Roman alitulia kwa muda akiwaangalia waandishi wale, kisha akajibu.

“Namaanisha kwamba Sergoyev Sucuchev…the hulk…ni bondia mzuri mara tano zaidi ya huyo Deus…na nyote mmeona jinsi nilivyomfanya hapa!” Kisha akageuka na kuwaacha waandishi wakitupa maswali zaidi ambayo hakujishughulisha kuyajibu.

Sasa azma yake ilikuwa inaelekea kutimia.


Siku mbili tu baada ya pambano la kule Kairo, Deus “deadly” Macha alitupa gazeti kwa hasira huku akiachia tusi zito la nguoni, na kusimama kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia na kubaki akitweta huku amejishika kiuno. Promota wake aliyekuwa naye mle ndani alimtupia jicho la mshangao na kuyarudisha macho yake kwenye lile gazeti lililotupwa kwa ghadhabu na yule bondia wake.

“Nini sasa Deus?”

“Ujinga mtupu! Mimi nimuogope Roman mimi?” Deus alimaka kubisha kile kilichokuwa kimeandikwa gazetini.

“Ah, hayo si magazeti tu? Sioni sababu ya kujijaza upepo kwa habari kama hiyo, hao wanataka kuuza magazeti tu!” Promota alimwambia. Walikuwa sebuleni nyumbani kwa Deus. Deus alibaki akiwa amekunja uso bila ya kujibu kitu. Lile gazeti lilikuwa limeandika kuhusu kauli ya Roman aliyoitoa siku ile aliyomuangusha m-serbia Sergoyev Sucuchev kuwa pambano lake na Deus lilikuwa ni la sherehe za kumkabidhi Roman mkanda wa ubingwa ule. Tangu kauli ile itolewe, Deus hakujibu kitu, na ndio maana gazeti liliandika namna ile.

“Sasa kwani ni kweli kuwa we’ unamuogopa Roman Deus…?” Promota alimuuliza kwa mashaka. Deus alimgeukia yule promota na kumtazama kwa hasira, kisha akarudi na kuketi kitini.

“Mi’ siwezi kumuogopa Roman hata siku moja…haniwezi!”

“Sasa ya nini kujijaza jazba?”

“Kwa sababu we’ hutaki nimjibu kashfa zake gazetini bwana! Mi sipendi namna hii…!”

“Kama nilivyokwambia Deus…sasa maneno basi. Tutapambana naye ulingoni tu, kwisha!” Promota alisisitiza.

Dakika kumi baadaye promota alitoka na kumuacha Deus peke yake pale nyumbani kwake. Alikaa kimya kwa muda akiwa amejawa na mawazo mazito, akilini kwake akikumbuka siku alipopambana na Roman miaka kadhaa iliyopita… wakati huo wote wawili wakiwa wanajeshi katika jeshi la wananchi wa Tanzania, wote wakiwa mabondia wa ridhaa katika michezo ya majeshi…. Mwili ulimsisimka.

Alikaa vile kwa muda mrefu, kisha akachukua simu yake ya mkononi na kupiga namba ambayo alikuwa akiijua kwa kichwa.

“Ni mimi…” Alijitambulisha kwa yule mtu aliyepokea ile simu, kisha akaendelea, “…sasa nataka nikupe tena ile kazi uliyoshindwa kuitekeleza wakati ule…” Alisikiliza kwa muda, kisha akaongea tena, “…si tatizo pesa yako utapata, ila nataka safari hii kusiwe na makosa bwana…Roman apatwe na ajali mbaya…!” Alisikiliza kwa muda kisha akasema neno moja tu kabla ya kukata simu.

“Okay!”

Wiki moja baadaye shirikisho la ndondi duniani lilitangaza kuwa pambano kati ya Roman na Deus lingefanyika miezi mitatu baadaye, jijini Dar es Salaam.


Maisha ya Roman yalibadilika sana baada ya yale mapambano yake mawili ya kulipwa. Aliweza kununua gari zuri la kutembelea na kiwanja ambacho alipanga kuanza kukijenga taratibu. Dan Dihenga naye kama promota wake na Mark Tonto kama mwalimu na rafiki yake nao walinufaika na mamilioni yale aliyoyakumba baada ya kumuangusha m-serbia kule Kairo. Lakini vyote hivi, bado havikuwa lengo la Roman kuingia kwenye ndondi za kulipwa. Lengo lake kuu bado lilikuwa halijatimia, ingawa sasa lilikuwa limekaribia sana.

Baada ya kurejea kutoka Kairo, Roman alipokelewa kwa shangwe sana uwanja wa ndege na mashabiki wa ndondi.

Ushabiki baina ya kambi ya Roman na Deus ukapamba moto maradufu, mashabiki wakiisubiri kwa hamu siku ambayo mabondia wale wawili wenye upinzani mkali nchini wangekutana ana kwa ana ulingoni.

Bondia Deusdelity Macha alikuwa na mkataba wa udhamini na kampuni moja kubwa ya simu za viganjani nchini, ambayo ilisimamia mapambano yake yote, na kumdhamini kwa namna mbalimbali katika vifaa vya mazoezi, mavazi na hata safari zake za kimataifa. Deus kwa upande wake naye alitokea kwenye matangazo mengi ya biashara ya kampuni ile. Sasa ilijitokeza kampuni nyingine ya simu za viganjani ambayo nayo ilikuwa ikigombea soko la watanzania katika uteja wa huduma zake za simu. Matokeo yake makampuni haya mawili yakawa kwenye ushindani mkali wa kibiashara. Dan Dihenga aliona nafasi ya kuwanufaisha yeye na bondia wake katika hili, na hivyo aliweza kuishawishi ile kampuni ya simu pinzani kumdhamini Roman kama sehemu ya upinzani wake na ile kampuni iliyokuwa ikimdhamini Deus. Hoja yake ilipita bila kupingwa.

Na ndipo bila ya yeye mwenyewe kujua, alipofanikiwa kuyaokoa maisha ya Roman kutokana na ajali ya kupangwa ya kugongwa na gari akiwa mazoezini, pale alipoishawishi ile kampuni kudhamini maandalizi ya Roman kwa pambano lake na Deus kwa kumuweka kambini nje ya nchi, kwenye visiwa vya ushelisheli, kwa siku zote mpaka siku ya pambano lake na Deus.

Siku ilipotangazwa kuwa Roman hatokuwapo nchini kwa muda wote hadi siku ya pambano lake na Deus, bingwa wa dunia Deus “deadly” Macha alipokea simu kutoka kwa mtu wake.

“Sorry boss, naona zoezi halitawezekana tena…Roman anaondoka nchini ndani ya siku mbili, nami sina uhakika wa kumpata akiwa mazoezini barabarani ndani ya siku mbili hizi!” Alimueleza. Deus alifura kwa hasira.

“Si bado yuko nchini ndani ya siku mbili? Mtafute, mfuatilie mpaka umpate! Hakikisha jambo linamtokea kabla hajaondoka bloody fool!” Deus alifoka, kisha akakata simu. Alibaki akiwa amefura kwa hasira.


Mark Tonto alingia sebuleni kwa Roman pale kwenye nyumba aliyopangiwa na Dan Dihenga kule bagamoyo, na kushusha pumzi ndefu.

“Wheew! Si joto hilo! Nijaalieni maji ya kunywa tafadhali jamani.” Alisema. Roman, aliyekuwa amejilaza kwenye kochi aliachia tabasamu pana wakati, Kate aliyekuwa kwenye kochi lile lile alilokuwa amelalia Roman, alijiinua na kwenda kumletea maji Mark.

“Pole sana mzee…vipi za Dar?” Roman alimuuliza.

“Huko shwari tu…” Mark alijibu huku akipokea gilasi ya maji baridi kutoka kwa Kate. Muda huo ulisikika muungurumo wa gari lililokuwa likiegeshwa nje ya nyumba na muda si muda hodi ikabishwa pale mlangoni. Roman na Mark walitazamana.

“Vipi, unatarajia mgeni nini?” Mark aliuliza. Roman alitikisa kichwa.

“Hapana. Dan hatokuja leo, na zaidi yake na sisi tuliomo humu ndani, hakuna mtu mwingine apajuaye hapa!”

Kate alienda kufungua mlango, na mara alipoufungua tu, Roman na Mark walimsikia akiachia mguno wa mshangao. Walitazamana, kisha wote wakakurupuka kuelekea kule mlangoni…


“Vipi Kate…hujawahi kuona askari akibisha hodi mlangoni?” Inspekta Fatma, akiwa ndani ya sare zake za kiaskari, alimuuliza huku akiachia tabasamu la upande mmoja. Kate alibaki akimkodolea macho ya kutoamini. Aliishia kujiona sura yake kwenye miwani myeusi ya jua iliyokuwa usoni kwa yule askari.

Roman na Mark walifika pale mlangoni, nao wakabaki wakishangaa.

“Mark…unaendesha gari kwa kasi sana wewe. Hujui kuwa ni hatari kwa usalama wa barabarani?” Fatma alimwambia Mark, kisha akamgeukia Roman, “…siku nyingine ukimuachia kocha wako hili gari lako jipya hakikisha umelifunga kidhibiti mwendo Roman, ama si hivyo utalikuta mtaroni siku moja!”

Roman alimtazama kwa kutoamini yule dada. Mark alikunja uso.

“Khah! Ina maana…” alianza kusema, lakini Fatma alimkatisha. “Ndio hivyo Mark…nimekufuata kwa gari tangu Dar mpaka hapa…vinginevyo ningepajuaje huku?”

“Na kwa nini umepata taabu yote hiyo afande, kama naruhusiwa kuuliza?” Roman alimuuliza kwa hasira. Fatma alimtazama kwa muda.

“Kwa hiyo sikaribishwi ndani?” Akamuuliza.

Roman alimtazama kwa muda kisha akageuka na kurudi ndani kwake, wengine wote wakimfuata ndani. Roman alisimama katikati ya sebule na kumuuliza.

“Okay Fatma, unataka nini tena kwangu?”

“Nahitaji kuongea nawe Roman.”

“Ongea nakusikiliza…!”

“Naomba tuongee peke yetu…mimi na wewe.”

“Hilo halitawezekana…” Roman alianza kujibu, lakini hapo hapo Mark Tonto akaingilia.

“Eh, mi’ na Kate tutakuwa nje kwa muda…”

Roman na Fatma walibaki peke yao pale sebuleni.

“Hongera kwa ushindi wa Kairo Roman…” Fatma alianza.

“Fatma usinipotezee muda. Hukuja mpaka huku eti kunipongeza. Sema lililo kuleta uende zako!”

Fatma alimtazama kwa huzuni, kisha akatikisha kichwa kwa masikitiko.

“Roman, nadhani bado nina wajibu wa kukuasa juu ya pambano lako na Deus…najua utaondoka ndani ya siku mbili kwenda ushelisheli kwa maandalizi, lakini…bado mi’ nilikuwa nadhani kuwa hutakiwi kufanya hivyo Roman…bado una nafasi ya kubadili mawazo!”

“Kwa hiyo unachoniambia ni kwamba niite waandishi wa habari halafu niwaambie kuwa nimeamua kujitoa kwenye pambano langu na Deus? You must be crazy Fatma. Mi’ sirudi nyuma!”

“Kuna namna nyingi za kulimaliza hili Roman, sio lazima iwe hivyo…unaweza kujitoa kutokana na sababu za kiafya…achana na…”

“No! Sina tatizo la kiafya Fatma…” Roman alimjia juu, kisha akamwambia, “Lakini Fatma, kwa nini unanifuata fuata mimi tu? Kwa nini usiupeleke ushauri huu kwa mtu ambaye atanufaika nao zaidi?”

“Mtu gani sasa?”

“Deus!” Roman alimjibu mara moja, na kuendelea, “Deus ndiye haswa ambaye ungepaswa umpe ushauri huu Fatma, sio mimi. In fact, sasa naomba nikutume rasmi kwa Deus…kamwambie kuwa mimi niko tayari kusahau yote yaliyopita iwapo atatangaza kujitoa kwenye pambano na kuusalimisha mkanda wake kwangu. Akiweza kufanya hivyo, kila kitu kitakuwa sawa!”

Fatma alibaki akimtazama kwa muda mrefu kabla hajaongea.

“Naona umeamua kutimiza ahadi uliyoitoa miaka miwili iliyopita Roman.”

“Khah! Mbona sikuelewi…mi’ nimekupa ufumbuzi wa hili tatizo halafu…”

“Unajua kabisa kuwa Deus hawezi kukubali hiyo hoja Roman…”

“Ila kwa kuwa mimi bwege, tena bwege mtozeni, ndiye ninayetakiwa nikubaliane na huo upuuzi wako? Toka nyumbani kwangu Fatma. Peleka ujumbe niliokutuma kwa Deus, ama si hivyo sitaki nikuone tena mbele ya uso wangu!” Roman alimjia juu. Fatma alimtazama kwa muda mrefu, kisha aliinuka taratibu na kuelekea mlangoni. Alifungua mlango, lakini kabla ya kutoka, alimgeukia tena.

“Okay, Roman. Mi’ nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu kuokoa ubinaadamu wako Roman…”

“Nashukuru kwa hilo. Sasa naomba uende!”

“…ila tu nataka uelewe kuwa ni ile kauli yako ya mwisho wakati unapelekwa gerezani, na azma niliyoiona wazi machoni mwako wakati ukitoa kauli ile, ndivyo vilivyonifanya nipate taabu yote hii kwa ajili yako…kwa sababu mi’ bado naamini kuwa ndani kabisa ya huo moyo wako uliozongwa na chuki, kuna binadamu mwema na mstaarabu. Nahofia kuwa binaadamu huyo yuko mbioni kupotezwa kabisa na ile kauli yako Roman…usiruhusu hilo litokee!” Fatma alimweleza kwa kirefu. Na baada ya maelezo yale, alibaki akimtazama Roman usoni kwa macho makavu. Roman alifunua kinywa kutaka kumjibu, lakini hakupata neno muafaka la kumwambia. Walibaki wakitazamana tu, kisha Fatma akatoka nje, akiufunga mlango taratibu nyuma yake.

Mark na Kate walirudi mle ndani na kumkuta Roman akiwa ameketi ilhali uso wake ukiwa na mawazo mazito.

“Haya, leo amekuja na lipi tena yule askari?” Kate alimuuliza.

“Yale yale tu ndugu zangu…Inspekta Fatma anadhani nitakuwa binaadamu na mstaarabu zaidi kama nikijitoa kwenye kugombea mkanda wa Deus…”

“Ana wazimu…!” Kate alimaka kwa hasira.

“Tena sana…” Roman aliafikiana na Kate, bado uso wake ukiwa na mawazo mazito. Mark alimtazama kwa mashaka, lakini hakusema kitu.

…ni ile kauli yako ya mwisho wakati unapelekwa gerezani, na azma niliyoiona wazi machoni mwako wakati ukitoa kauli ile, ndivyo vilivyonifanya nipate taabu yote hii kwa ajili yako…

“Sasa mmemalizana vipi?” Kate alihoji zaidi.

“Nimemtuma kwa Deus…akamwambie ajitoe kwenye mpambano na asalimishe mkanda wake kwangu…”

“Wacha bwana!” Mark alimaka.

“Ndiyo…! Na akishindwa kufanya hivyo, basi asirudi tena kwangu na ule upuuzi wake!” Roman alimalizia, lakini bado alionekana kuwa kuna kitu kilikuwa kikimsumbua akilini mwake.

Nahofia kuwa binaadamu huyo yuko mbioni kupotezwa kabisa na ile kauli yako Roman…

“Roman, uko sawa lakini…? Mbona nakuona kama kwamba una kitu kinakusumbua?” Kate alimuuliza kwa wasiwasi. Roman alimtazama kwa muda, kisha akamgeukia Mark, halafu akatazama ukutani kwa muda.

…usiruhusu hilo litokee…

“Aam…nadhani nahitaji kuwa peke yangu kwa muda jamani…samahani…” Hatimaye aliwaambia wenzake, na bila kusubiri kauli yao, aliinuka na kuelekea chumbani kwake. Mark na Kate walibaki wakitazamana.

“Usijali…mpe muda atulie kwanza…bila shaka Inspekta Fatma amemkumbusha mambo mengi mazito, lakini atakuwa sawa tu.” Mark alimwambia Kate. Kate aliafiki kwa kichwa bila ya kusema kitu.

Chumbani kwake Roman alivuta droo na kutoa picha ya msichana aliyekuwa amesimama kwenye bustani huku akiwa ameachia tabasamu mororo, furaha iliyokuwa moyoni mwake ilikuwa wazi machoni mwake, na ikanaswa sawasawa na kamera. Alikuwa ni binti mrembo aliyepata umri wa miaka kama kumi na minane hivi wakati picha ile inapigwa.

Aliketi kitandani taratibu huku akiitazama ile picha ilhali uso wake ukiwa na simanzi kali, na hapo kwikwi ya kilio ilimtoka bila kutarajia, tone la chozi likiangukia kwenye ile picha.

“Oh, Rachel mdogo wangu! Nisamehe malkia wangu…nilikuacha mikononi mwa shetani mdogo wangu, na sasa haupo tena duniani…” Alibwabwaja huku akilia kwa uchungu. Alilia kwa muda mrefu, kisha alijitahidi kujifuta machozi, na kuitazama tena ile picha, sasa uso wake ukiwa na ghadhabu zaidi kuliko huzuni.

“…lakini nakuahidi mdogo wangu…nakuahidi, kama jinsi nilivyokuahidi hapo awali Rachel…nitahakikisha kuwa nalipiza kifo chako, nitalipiza kisasi…na muda si mrefu azma hiyo itatimia Rachel…!” Aliiambia ile picha huku akibubujikwa na machozi.

…kwa sababu mi’ bado naamini kuwa ndani kabisa ya huo moyo wako uliozongwa na chuki, kuna binadamu mwema na mstaarabu…

“Inspekta Fatma anadai kuwa nikilipiza kisasi nitapoteza moyo wangu wa ubinaadamu na ustaarabu…” Roman alizidi kuongea na picha ya hayati mdogo wake, akaachia mguno wa dharau, kisha akaendelea, “…kitu ambacho haelewi ni kwamba huo moyo wa ustaarabu na ubinadamu ndio uliosabaisha nikuache mikononi mwa shetani, nikiamini kuwa naye ni binadamu na mstaarabu kama mimi Rachel…shetani aliyekuja kukuangamiza mdogo wangu. Hapana Rachel, ni bora nipoteze ubinaadamu na ustaarabu, kuliko kuacha kifo chako kipite bila kulipizwa! Nitalipiza…nitalipiza…na nitalipiza kwa namna ambayo ninaiweza! Hiyo ni azma yangu!” Roman Kogga aliongea kwa uchungu na ile picha ya hayati mdogo wake, Rachel Kogga. Na ndani ya muda huo, matukio ya miaka kadhaa iliyopita yalimrudia kichwani mwake kama kwamba yalikuwa yametokea jana tu…


MIAKA KADHAA ILIYOPITA…..

Roman Kogga alikuwa ni miongoni mwa vijana waliojiunga na jeshi la wananchi wa Tanzania baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha sita. Baba yake, ambaye naye alikuwa ni afisa katika jeshi la wananchi wa Tanzania, ndiye aliyekuwa kishawishi kikubwa cha yeye kujiunga na jeshi. Akiwa jeshini, alijiunga na chuo cha usimamizi wa fedha, akisomea shahada ya uhasibu, chini ya udhamini wa jeshi la wananchi. Na wakati akiwa anakamilisha masomo yake, wazazi wake wote wawili walipata ajali mbaya ya gari na kufariki dunia. Ndipo Roman alipojikuta akikabiliwa na jukumu la kumlea Rachel, mdogo wake wa pekee ambaye muda huo alikuwa kidato cha pili. Lakini kwa kuwa tayari yeye alikuwa ana kazi ya uhasibu katika jeshi la wananchi, na wazazi wao waliwaachia nyumba na mali kadhaa, hawakutetereka kimaisha. Roman alimchukua mdogo wake na kuishi naye kwenye nyumba aliyopewa na jeshi, na ile nyumba waliyoachiwa na wazazi wao wakaipangisha. Hivyo maisha hayakuwa na tatizo.

Tangu akiwa shuleni, Roman alikuwa akipenda sana mchezo wa ngumi, na alikuwa akihudhuria mazoezi ya vikundi mbali mbali vya ngumi. Lakini alipata nafasi ya kujiingiza zaidi kwenye ndondi wakati alipojiunga na jeshi. Na huko ndipo alipokutana na Sajini Meja Makongoro “Mark Tonto” Tondolo, ambaye alikuwa ni mwalimu wa ndondi katika jeshi la wananchi wa Tanzania. Roman aliondokea kuwa bondia mzuri sana katika timu ya jeshi, na katika maandalizi ya michezo ya majeshi, Sajini Meja Mark Tonto alimchagua kwenye timu ya kikosi chake. Na hapa ndipo Roman alipokutana na bondia mwingine aliyekuwa akija juu sana katika mchezo ule jeshini, Desudelity Macha.

Baada ya uteuzi wa timu, Sajini Meja Makongoro TAondolo aliinoa timu yake kwa mazoezi makali, na hapa akajionea uwezo mkubwa wa mabondia Roman Kogga na Deusdelity Macha. Moja kwa moja Mark akajua kuwa wawili wale ndio ambao wangekuwa vinara wa timu yake.

Kwa upande wao, Roman na Deus walijenga urafiki haraka sana. Wote walikuwa wakiupenda mchezo ule, na walikuwa wakikutana kila siku kwenye mazoezi. Na katika siku ambazo hakukuwa na mazoezi ya timu yao, wao wenyewe walikuwa wakikutana na kupeana mazoezi mbali mbali. Lakini nyota ya Roman katika ndondi za ridhaa ilianza kuzimika pale ambapo siku moja, wakiwa katika mazoezi ya maandalizi, alipopanda ulingoni na bondia mwenzake katika timu ya kikosi chao, na katikati ya pambano, Roman alichomoa sumbwi la mkono wa kushoto kwa mtindo wa upper-cut, sumbwi lililotua sawia kidevuni kwa mpinzani wake na kumpeleka chini kama puto lililotobolewa.

Jamaa aliaga dunia pale pale!

Heh!

Lilikuwa ni tukio la kushtua sana, ingawa mwisho wa yote lilionekana kuwa ni ajali tu ya kimichezo. Lakini kuanzia wakati ule kocha Mark Tonto alianza kumtazama Roman kwa makini sana. Siku zilipita, mashindano ya michezo ya majeshi yalikaribia, lile tukio likasahaulika, na Roman akapambanishwa na Deusdelity Macha katika mazoezi. Mark Tonto alikuwa makini sana na pambano lile, kwani wapiganaji wale ndio walikuwa vinara wa timu yake, na pambano lao lilikuwa kali sana. Deusdelity alikuwa mpiganaji mzuri sana aliyetoa upinzani mkali kwa Roman. Pambano lilikuwa linaelekea kuwa nguvu sawa, lakini ilipokuwa imebaki raundi moja pambano liishe, Deus alitupa konde kali sana lililokuwa linaelekea usoni kwa Roman. Roman aliyumba, konde likamkosa, na hapo hapo mkono wake wa kushoto ulichomoka na hook iliyotua kwenye taya la Deus, na hapo hapo aliona macho ya mpinzani wake yakitumbukia ndani huku akienda chini kama mzigo!

E bwana we!

Roman alibaki akimshangaa Deus akiwa chini wakati kocha Mark Tonto na wauguzi wakiwahi ulingoni. Dakika chache baadaye Deus alitolewa ulingoni akiwa kwenye machela akiwa hana fahamu.

Si mchezo!

Deus alipona, lakini hakuweza tena kushiriki mashindano ya majeshi ya mwaka ule, kwani alikaa hospitali wiki mbili akitibiwa taya lililovunjika, na baada ya hapo alitakiwa awe nje ya ulingo kwa miezi sita.

“Roman, nadhani unabidi uwe makini sana na hiyo ngumi yako ya kushoto…ningeshauri utumie zaidi ngumi ya kulia, na utumie mkono wa kushoto kujikingia na kutupa ngumi ndogo ndogo tu…inaonekana ni ngumi hatari sana!” Kocha Mark Tonto alimwambia Roman baada ya tukio lile.

“Ah, coach…sasa ndio n’takuwa bondia gani wa kutumia mkono mmoja tu bwana? Mi’ naona hili shoto ndio turufu yangu ulingoni bwana…”

“Hapana Roman, hiyo ngumi ni hatari sana…inaua!”

“Aaw, come on coach…ile ilikuwa bahati mbaya tu bwana…”

“No Roman, hii si maskhara. Ona jinsi ulivyomfanya Deus…bahati ile ngumi imemshukia kwenye taya, ingempata juu kidogo tu kichwa, juu ya sikio, nakuhakikishia naye tungemzika!” Kocha Mark Tonto alimwambia kwa hamasa. Roman alibaki akishangaa.

“Kwa hiyo basi unaniambia kuwa niache ndondi kocha!”

“Hapana…ila nataka nikuulize swali moja Roman…je unajua iwapo utotoni mwako ulipata kuchanjiwa mkono wako wa kushoto?”

Roman alimshangaa zaidi yule mkufunzi wake.

“Kuchanjiwa?”

“Ndio Roman…kuchanjiwa! Nasikia kuna makabila ambayo huwa yanachanjia vitu kama hivi…mtu anakuwa na ngumi nzito yenye uwezo wa kuua…je nawe ulifanyiwa kitu hicho Roman?” Mark alimuuliza. Roman alidhani kuwa mwalimu wake alikuwa akimtania, lakini alipomtazama aliona kuwa hakuwa akitania hata kidogo.

“Hapana coach…sina habari ya kitu kama hicho…kama kipo basi wazazi wangu hawakuniambia…” Roman alimjibu kocha wake. “Basi zingatia ushauri wangu.” Mark alimwambia na mjadala ukaishia pale. Roman hakuyatilia maanani kabisa yale mazungumzo, kwani kwake kitu cha mtu kuchanjiwa kuwa na ngumi ya kuua hakikumuingia akilini hata kidogo.

Kwa hiyo timu ya kikosi cha Mark Tonto iliendelea na mashindano yale bila ya Deus. Na katika mashindano yale, ambayo ndio yalikuwa ya kwanza kabisa makubwa kwake kushiriki, Roman aliua mtu mwingine ulingoni kwa sumbwi la mkono wa kushoto!



Waraka aliopokea kutoka makao makuu ya jeshi ulikuwa unajitosheleza. Kufuatia matukio mawili ya kuua wapinzani wake ulingoni, na moja la kumjeruhi vibaya mpinzani mwingine katika mchezo wa ndondi, Kapteni Roman Kogga, kuanzia tarehe ya waraka ule, alikuwa amezuiliwa kushiriki katika mchezo wa ndondi popote pale ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Ni amri.

Imezuiliwa.

Ndoto za Roman kuwa bondia bora wa ngumi za ridhaa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilikatikia hapo.


Roman Kogga aliachana kabisa na ndondi, na kuendelea na utumishi wake ndani ya jeshi kama mhasibu. Lakini muda wote huo urafiki wake na Deus haukutetereka. Alikuwa akienda kumtembelea hospitali na hata alipotoka na kulazimika kukaa nje ya ulingo kwa miezi sita, Roman na Deus walikuwa wakiendelea na urafiki wao. Baada ya kupona Deus alirudi tena ulingoni na kuwa bondia mzuri sana ndani ya jeshi. Walikuwa wakitembeleana na siku za mwisho wa wiki, walikuwa wakienda kwenye kumbi za starehe na kujifurahisha kwa starehe mbali mbali.

Miezi sita baada ya Deus kupona na kurejea ulingoni ndani ya jeshi,Kepteni Roman Kogga alipata udhamini wa jeshi la wananchi kwenda kusomea shahada ya pili ya uhasibu nchini Uingereza. Ilikuwa ni habari ya furaha sana kwake, lakini pia ilikuwa na wingi wa huzuni, kwani ilimaanisha yeye kuwa mbali na mdogo wa pekee wa kike, Rachel, kwa miaka miwili!

Roman aliongea na rafiki yake mpenzi, Deus juu ya hatima ya Rachel wakati yeye akiwa nje ya nchi. Akamuomba amuangalie mdogo wake wakati yeye yuko nje ya nchi. “Usijali partner…Rachel ni mdogo wetu sote bwana, kwa hiyo hatokuwa peke yake. Mimi nitachukua jukumu la kumuangalia katika muda wote ambao hutakuwepo…nenda ukasome salama rafiki yangu, na mungu akujaalie!” Deus alimwambia.

“Loh, ahsante sana partner…ahsante sana. Nilijua kuwa ninaweza kukutumainia rafiki yangu.” Roman alimjibu kwa shukurani.

Kufikia wakati huu Rachel alikuwa ameshamaliza kidato cha nne na alikuwa amefaulu kuendelea na kidato cha tano. Kabla hajaondoka, Roman alihakikisha kuwa dada yake ameshapata nafasi kwenye bweni la shule aliyoteuliwa kujiunga nayo jijini Dar, na hivyo Rachel hakulazimika kuishi peke yake nyumbani kwa Roman. Pia alimfungulia akaunti na kuweka maelekezo maalum ya kukatwa sehemu ya mshahara wake kila mwezi na kuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Rachel. Siku ya safari ilipowadia, kaka na dada waliagana kwa huzuni.

“Usiwe na wasiwasi Rachel, tutakuwa tukiwasisliana kwa mtandao mara kwa mara…na kama kuna tatizo lolote litakalokuwa nje ya uwezo wako, muone kaka yako Deusdelity…atakusaidia”. Roman alimwambia mdogo wake wakiwa uwanja wa ndege.

“Sawa kaka…uende salama…” Rachel alijibu huku akibubujikwa machozi.

“Come on Rachel…sio kwamba Roman anaenda kuuawa huko bwana…anaenda kuongeza elimu kwa faida yenu nyote. Usilie namna hiyo…tumuombee mungu tu huko aendako arudi salama, au sio?” Deusdelity Macha, aliyekuwa pamoja nao pale uwanja wa ndege alimfariji Rachel.

“Najua kaka Deus…lakini…” Rachel alijitahidi kujibu lakini hakuweza kumalizia, alizidi kulia. Roman alimkumbatia mdogo wake kwa muda mrefu, kabla ya kumtazama usoni kwa muda, machozi yakimlenga-lenga, na kumbusu kwenye paji la uso. Aligeuka na kuingia ndani ya uwanja ule bila kugeuka nyuma. Akiwa ndani ya uwanja, ambapo alijua hawataweza kuona jinsi alivyokuwa akitiririkwa na machozi, aligeuka na kuwapungia mkono. Deus na Rachel walimpungia, naye akapotelea ndani ya eneo la kusubiria ndani ya uwanja ule.

Ndio ilikuwa mara yake ya mwisho kumuona mdogo wake akiwa hai…


Ndani ya mwaka wake wa kwanza alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na Rachel na Deus, na mara moja moja sana alikuwa akiwasiliana na Sajini Meja Makongoro Tondolo. Na katika moja ya mawasiliano yao adimu na kocha wake wa zamani wa ndondi, Mark alimfahamisha Roman kuwa alikuwa ameamua kustaafu jeshi ili aweze kusimamia miradi yake binafsi na apate muda zaidi wa kuinua mchezo wa ndondi. Roman alimtakia kila la kheri, naye akaendelea na masomo yake. Siku moja, akiwa ameanza mwaka wake wa pili wa masomo yake kule uingereza, Roman alipokea simu usiku wa manane kutoka Tanzania.

“Eh…hallo…”

“Roman…this is Mark…Mark Tondolo!”

“Mark…? Coach…? vipi za huko, kwema?”

“Huku si kwema Roman…ni Rachel…”

“Rachel…?”

“Amekunjwa sumu…ana hali mbaya sana…”

“Whaaaat? Ame…Deus yuko wapi…?” Roman alihamanika, usingizi wote ukimkauka ghafla, moyo ukimuenda mbio.

“Sijui Roman…Deus hapatikani…mi’ nimepigiwa simu na wanafunzi wenzake waliomfikisha hapa hospitali…walipewa namba na Rachel mwenyewe kabla hajaingizwa ICU…!” Mark alijibu.

Saa tano baadaye, Roman alikuwa kwenye ndege akirejea Tanzania. Akili ilikuwa ikimzunguka muda wote alipokuwa angani, machozi yakimbubujika, donge kubwa likiwa limemkaba kooni.


Mark Tonto alikuwa akimsubiri uwanja wa ndege. Alipomuona tu alijua kuwa kuna kitu hakikuwa sawa. Alitupa chini begi lake na kumkimbilia pale alipokuwa amesimama.

“Mark! Coach…vipi Rachel…yuko hospitali gani….? Deus je…?” Roman alimvurumishia maswali ya wahka, lakini Mark alikuwa amesimama kimya akimtazama kwa huzuni, midomo ikimtetemeka. Roman alimshika mabega na kumtazama kwa woga mkubwa. Macho ya Mark yalimthibitishia kile alichokuwa akikihofia tangu anapanda ndege kurudi nyumbani.

“No, Mark…No!” Alisema kwa maombolezo. “…usiniambie kuwa Rachel ame…ame…”

“She is dead Roman…Rachel is dead!” Mark alimjibu kwa huzuni huku akimkumbatia. Maneno yale yaliuchoma moyo wake kama kwamba yalikuwa ni msumari wa moto.

“Ah! Coach…imekuwaje? Kwa nini lakini…?” Roman aliuliza huku akilia kama mtoto.

“Twende nyumbani Roman…ni hadithi ndefu kidogo…”

“No! Nipeleke nikamuone mdogo wangu bwana! Na Deus yuko wapi lakini?” Roman alibwabwaja wakati Mark akimuongoza kwenye teksi.

“Tutamtafuta Deus baadae Roman, sasa tushughulikie msiba uliopo mbele yetu…” Mark alimjibu.

Alipouona mwili wa mdogo wake Roman alipoteza fahamu pale pale hospitali. Alipozinduka, alikuwa amelazwa kitandani pale hospitali. Mark Tonto alikuwa ameketi kwenye kiti kando yake.

“Oh, Mark…Rachel ametutoka Mark…” Roman alibwabwaja huku akiinuka na kuketi pale kitandani. Mark aliinuka na kuketi pamoja naye pale kitandani. “Ni amri ya mungu Roman…kuwa jasiri ndugu yangu…”

“Si amri ya Mungu hii Mark…ndugu yangu amekunywa sumu. Ina maana aidha amejiua, au ameuawa…sijui kipi ni kipi, lakini lolote litakalokuwa kati ya hayo mawili, jibu linabaki kuwa hii si amri ya Mungu!” Roman alisema kwa uchungu. Mark alimkumbatia rafikiye kwa kumfariji.

“Usikufuru Roman…hakuna litokealo bila mapenzi ya Mungu bwana. Wewe ni mpiganaji, pigana na hili kijasiri Roman…”

Roman alianza kulia upya.

Muda mfupi baadaye tabibu aliyempokea Rachel pale hospitali alifika kuonana na Roman.

“Pole sana Kepten Kogga…pole sana.” Yule tabibu alimwambia, na Roman alimtazama na kuitika kwa kichwa.

“Okay, sasa…nadhani unahitaji kujua mazingira ya kifo cha mdogo wako Kepten…” Tabibu alimwambia.

“Najua…amekunywa sumu…” Roman alisema taratibu.

“Yeah…ilikuwani sumu kali na nyingi, kiasi kwamba pamoja na jitihada zetu zote, hatukuweza kuokoa maisha yake wala ya kiumbe kilichokuwa tumboni kwake…”

“Whaaat?” Roman alimaka na kumtazama kwa makini yule tabibu. “…ki…kiumbe? kiumbe gani tumbon…oh, My God, yaani Rachel alikuwa mjazito?”

“Oh, hukuwa na habari…? Ndiyo, Rachel alikuwa na ujauzito wa miezi minne…”

Roman aliona kuwa dunia yote ilikuwa imeamua kumsaliti na kumzonga. Alimtazama yule tabibu kwa uchungu, kisha akamgeukia Mark.

“Ni nini hiki kinachotokea kwangu jamani, enh? Ni nini lakini…?” Aliuliza kwa uchungu huku akilia. Mark alibaki akitikisa kichwa tu.

“Sasa…sasa…huyu mwenye ujauzito huo…aliyembebesha ujauzito mdogo wangu…anafahamika? Mark, we unamfahamu?” Alimuuliza Mark kwa hamaniko kubwa kabisa. Mark aliuma midomo yake kwa uchungu. “Hata mimi hii habari imenijia kwa mshituko mkubwa Roman…”

“Oooh, Mark….!” Roman alisema kwa masikitiko, machozi yakimbubujika.


Mark aliandaa taratibu zote za mazishi. Msiba uliwekwa nyumbani kwake, na maziko yalifanyika siku iliyofuata, bila ya Deusdelity Macha kuhudhuria. Baada ya maziko, watu wachache walioshiriki kwenye msiba ule walibaki pale nyumbani kwa Mark, wakiwemo wananfunzi na walimu wa shule aliyokuwa akisoma marehemu.

Roman alimfuta Mark na kumwambia, “Mark, sasa nimekubali kuwa Rachel amekwenda na hatorudi tena. Ila bado nina mambo matatu yanayosumbua kichwa changu Mark, na haya sitatulia mpaka niyapatie majibu…”

Mark Tonto alimtazama tu rafiki yake bila ya kusema kitu, na Roman aliendelea, “Kwanza, ilikuwaje hata Rachel akanywa sumu…” alitulia kidogo, na kuendelea, “…pili, ni kwa nini Deus, ambaye ndiye niliyemkabidhi jukumu la kumuangalia Rachel wakati mimi sipo, hajaonekana kabisa katika msiba huu…” kisha akamalizia, “na tatu, ni nani huyu aliyempa ujauzito mdogo wangu…?”

Mark alitikisa kichwa kuafiki umuhimu wa mambo yale huku uso wake ukiwa umefanya tafakuri zito. Alikaa kimya kwa muda mrefu, kisha taratibu aliinua uso wake na kumtazama Roman.

“Majibu ya maswali hayo yapo Roman, ila ni machungu sana rafiki yangu…”

“Hayawezi kuwa machungu kuliko uchungu wa kifo cha mdogo wangu Makongoro…”

Kimya kilitawala kwa muda baina yao, kisha Mark akasema. “Basi itabidi nikukutanishe na binti aitwaye Sada, Roman, yeye ana majibu ya maswali yote hayo…”

Roman alishikwa wahka mkubwa.

“Ni nani huyu Sada, na…yuko wapi?”

“Huyu ni rafiki mkubwa wa marehemu…na yupo hapa hapa msibani.”

Maelezo ya Sada yalibadili kabisa muelekeo wa maisha ya Roman…


Sada alikuwa rika moja na Rachel, na alipoonana uso kwa uso na Roman hakuweza kujizuia kuangua kilio upya. Mark na Roman walijitahidi kumtuliza, na baada ya muda, alijifuta machozi kwa upande wa khanga yake, akapenga kamasi laini kwa khanga ile ile na kuwaangalia wale watu wawili waliokuwa mbele yake.

“Sa…samahani sana…”

“Usijali, ni msiba mkubwa kwetu sote Sada.” Mark alisema kwa upole, kisha akaendelea, “Sasa naomba umueleze Kapten Roman hapa, yale uliyonieleza mimi juu ya Rachel, na mazingira ya kifo chake.” Mark alimwambia.

“Okay…kaka zangu…” Sada alisema na kupenga tena kamasi.

“Na…naweza kusema kuwa mimi ndiye nilikuwa rafiki wa karibu sana wa mar…wa Rachel. Alikuwa akikuongelea sana kaka Roman. Kwake wewe ulikuwa ni shujaa asiyeshindwa na lolote…” Roman aliuma midomo kwa uchungu, lakini alijitahidi kujizuia, alitaka kujua ukweli wa kifo cha ndugu yake. “…pia alinieleza kuhusu Deus, ya kwamba ni rafiki yako mkubwa na kwamba ndiye angekuwa anamsaidia iwapo atakutwa na tatizo lolote kubwa. Kiujumla tuliishi bila matatizo pale shuleni, na kaka Deus alikuwa akija kumtembelea Rachel mara kwa mara na mara nyingine, siku za mwisho wa wiki alikuwa akija kutuchukua na kutupeleka kula Ice Cream au sinema na kuturudisha shuleni…”

Roman alizidi kusikiliza kwa makini.

“Sa’ siku moja, tukiwa kwenye likizo ya katikati ya muhula, Rachel alienda mjini na Deus, na aliporudi aliniambia kuwa …kuwa…kaka Deus alim…alimtaka kimapenzi!”

“Whaat??” Roman alimaka kwa kutoamini, macho yakimtoka pima. “Deus???”

“Ndio kaka Roman…nilishituka sana. Rachel alilia sana siku ile, hakuamini kuwa kaka Deus angeweza kumtamkia jambo kama lile…”

“Mwanaharamu…! Yani Deus anaweza kunifanyia hivi?” Roman alisema kwa uchungu.

“Hujasikia habari yote Roman…muache binti aendelee, kisha tutajadili kwa undani swala hili.” Mark alimwambia.

“Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa ni Deus ndiye aliyembebesha mimba Rachel?” Roman aliuliza kwa jazba, mishipa ya shingo ikiwa imemtutumka. Sada alitikisa kichwa kwa masikitiko.

“Mnhu! Dunia ina mambo kaka zangu…hali ilienda mpaka Rachel akajikuta akikubaliana na hoja za Deus…nadhani Deus alikuwa na nguvu ya kubwa ya ushawishi. Wakawa wapenzi…” Sada alisema na kuanza kulia.

“Ah!” Roman aliguna, na kubaki akitikisa kichwa, macho yake yakitoa mng’aro wa ghadhabu isiyo kifani. Sada aliendelea kueleza kuwa Rachel alimwambia kwamba Deus alimuahidi kumuoa “…alimwambia kuwa…kuwa hata wewe, kaka Roman, ungefurahia kuwa shemeji yake…”

“Ah, sasa mbona sikuambiwa juu ya uchumba huo? Uongo mtupu!” Roman alimaka.

“Walikubaliana kuwa wakusubiri mpaka urudi…Deus ndio angeongea nawe kwanza…ilionekana ni utaratibu mzuri tu kwa wakati ule…”

“Mzuri? Ni utaratibu mzuri huo? Mtu namkabidhi mdogo wangu yeye anaenda kumtongoza?”

“Namaanisha huo utaratibu wa kukusubiri urudi na Deus aongee nawe…lakini mambo yaliharibika pale Rachel aliposhika ujauzito…”

“Deus akamkana…!” Roman alidakia kwa jazba, sasa machozi yakimtiririka waziwazi. Sada alitikisa kichwa kwa simanzi. “Hapana. Akamtaka atoe ile mimba…!”

“Ama!?” Roman alimaka kwa mshangao, “Yaani…kwa nini?”

“Kuna sheria kali sana dhidi ya wanaume wanaowatia mimba wanafunzi kaka Roman. Deus alikuwa akiogopa hilo, lakini Rachel hakutaka kutoa mimba. Alimwambia akupigie simu huko uliko akueleze kila kitu…Deus hakuwa tayari, alisisitiza msimamo wake kuwa Rachel atoe mimba. Ikawa mizozo na majibizano. Rachel akaanza kukosa kuhudhuria masomo, kutwa barabarani akimtafuta Deus. Hali ilipozidi kuwa mbaya, Rachel akamtishia kumshitaki kwa wakuu zake wa kazi. Deus alikuja juu, na hapo ndipo alipomtakia kuwa haujui ule ujauzito…”

“Hah!”

“Ndiyo kaka…Rachel alichanganyikiwa!”

Kufikia hapa Roman alikuwa akilia waziwazi. Uchungu aliokuwa nao haukuwa na mfano. “Kwa…kwa…kwa hiyo nd’o mdogo wangu akanywa sumu kwa hilo…? Why Rachel…? Why…?” Roman alisema huku akizongwa na kwikwi za kilio. Sasa na Sada naye alikuwa akilia pamoja naye. Mark alitikisa kichwa huku naye akitiririkwa na machozi. Ilikuwa ni hali ya kutia uchungu sana. Lakini uchungu bado ulikuwa haujatimia.

“Hapana kaka Roman…hilo silo lililosababisha Rachel achukue uamuzi aliochukua…” Hatimaye Sada alimjibu. Roman alimtazama kwa mshangao.

“Sio hilo…?” Aliuliza kwa kutoamini, akitembeza macho baina ya Mark na Sada. “Sasa kuna ubaya gani tena zaidi ya huu ambao mdogo wangu amefanyiwa jamani? Hebu niambie Sada…ni nini tena Deus alichomfanya mdogo wangu…?”

“Ah, kaka Roman…we’ acha tu…” Sada alisema na kuangua kilio upya.

“No! Nieleze tafadhali…niambie tu mdogo wangu…ni nini kilichosababisha Rachel ajiue?”

Sada alilia kwa muda, kisha akajilazimisha kumueleza.

“Siku hiyo…kiasi cha wiki moja baada ya Deus kuukana ujauzito wake, Rachel aliniomba nimsindikeze nyumbani kwa Deus ili ajaribu kuzungumza naye…” Sada alitulia kidogo, akipenga kamasi na kujifuta machozi, “…huko tulimkuta Deus akiwa na mwanamke mwingine!” Sada alimalizia kauli yake na kuangua kilio kizito.

Duh!

Mark na Roman walitazamana, uchungu aliokuwa nao Roman ukijiweka wazi machoni mwake.

“Ilikuwa ni vurugu kubwa…Rachel akilia na kumshutumu Deus kwa kumlaghai, yule mwanamke mwingine naye akimshutumu Deus kwa kumlaghai, Deus naye akimkana Rachel na kumuita malaya….”

“Ah, jamani…hivi ni Deus huyu huyu nimjuaye ndiye aliyefanya mambo hayo?” Roman alisema kwa mshangao na uchungu.

“Ndiye kaka…ndiye.” Sada alimjibu huku akishindana na kwikwi za kilio, kisha akaendelea, “…na kitendo alichomfanyia Rachel pale nyumbani kwake siku ile ndicho kilichogongelea msumari wa mwisho…pamoja na kuwa nilikuwa naye muda wote siku ile baada ya kutoka kule kwa Deus…Rachel aliamka usiku wakati wote tumelala, na kunywa sumu…nilikuja kuamshwa na sauti zake akikoroma na kugumia…nilipogundua alichofanya, niliwaarifu waalimu na tukamkimbiza hospitali…” Sada alimalizia na kuangua kilio. Hakuweza tena kuendelea. Alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa.

“Mimi nilipigiwa simu na mmoja wa waalimu wao…Rachel aliandika namba yangu na ya Deus pale shuleni kwa ajili ya dharura yoyote itakayotokea…walisema namba ya Deus ilikuwa haipatikani. Nilipofika hospitali na kukuta hali ilivyo, ndipo nilipokupigia simu. Baada ya hapo nimekuwa nikijaribu kumafuta Deus kwenye simu bila mafanikio. Jamaa hakuwa hewani kabisa…nadhani aliamua kubadilisha namba kabisa.” Mark aliingilia kati na kufahamisha zaidi.

“Lakini mi’ nilimpata…wakati Rachel anahangaika usiku ule, kabla hata sijawaita waalimu nilimpigia na nikampata…nikamwambia kuwa amesababisha Rachel anywe sumu…na kwamba nitahakikisha namfikisha mbele ya sheria…nadhani baada ya hapo ndio akaamua kufunga kabisa simu yake!” Sada alisema huku akilia.

Roman alilia! Alilia sana.Alilia kwa uchungu, majuto na hasira pia.Alilia kweli kweli.

“Kwa hiyo…Rachel hakuacha ujumbe wowote kueleza sababu za uamuzi wake ule?” Hatimaye Roman aliuliza.

“Hapana…hakuacha chochote…” Sada alisema.

Roman alibaki akitikisa kichwa kwa masikitiko.

“Na ndio maana tunashindwa kumchukulia Deus hatua yoyote sasa Roman…mimi nilishindwa kwenda polisi…nigekuwa na ushahidi gani? Ni ushuhuda wa Sada tu, ambao unakanika kirahisi sana…” Mark alisema kwa uchungu.

“Dah! Ni kweli Mark…hakuna ushahidi wa kushikika na kuukabidhi kwa polisi…lakini ushahidi wa kuwa Rachel…mdogo wangu, amekufa upo…she is dead Mark!Dead! Bado binti mbichi kabisa!” Roman alisema kwa uchungu, “…na Deus ndiye anayehusika…lazima alipe! Hii haina mjadala kabisa, lakini kwanza nataka nisikie kutoka kwake mwenyewe…anasemaje kuhusu kifo cha mdogo wangu niliyemkabidhi kwake?” Hatimaye alisema.

“Mimi nilikwenda kumuona Deus jana kabla sijaenda uwanja wa ndege kukupokea Roman…” Mark alisema, na kuendelea, “… hakukana kabisa kuwa alikuwa na uhusiano na Rachel…alisema ni jambo la bahati mbaya naye hakulitegemea…hakutegemea kuwa Rachel angechukua uamuzi ule…na hakika alikuwa na majuto makubwa…”

“Sasa mbona hakuja hata kwenye maziko Mark…?”

“Alisema hataweza kuja…hataweza kukutazama tena usoni baada ya yote yaliyotokea…”

Roman alilia sana. Alilia kwa muda mrefu.

“Basi ana bahati mbaya sana… kwa sababu mimi nataka nimtazame yeye usoni…” Hatimaye Roman alisema huku akijifuta machozi.

ITAENDELEA

Bondia Sehemu ya Tano

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment