SIMULIZI

Ep 04: Mtuhumiwa

SIMULIZI Mtuhumiwa Episode 01
SIMULIZI Mtuhumiwa Episode 04

IMEANDIKWA NA : HUSSEIN TUWA

*********************************************************************************

Simulizi : Mtuhumiwa
Sehemu Ya Nne (4)

“Kwa nini unasema hivyo Dokta…kuna kitu hujaniambia?”
Mgunda alishusha pumzi ndefu kabla ya kumuuliza.
“Unadhani alipata hayo majeraha wakati akilazimishwa kumeza hivyo vidonge?”
Vata aliafiki kwa kichwa. Mgunda aliendelea kumtazama kwa muda. Vata akashindwa kuendelea kucheza mchezo ule wa paka na panya.
“Una kitu cha kuniambia Dokta niambie, sio tena unanifanyia ana-ana-anado hapa! We’ unadhani kama hakukuwa na mtu mwingine hayo majeraha angeyapataje? Talk to me bwana, ni nini ambacho bado hujaniambia Dokta juu ya swala hili?”
Sasa Mgunda aliangua kicheko. Kwa hakika alikuwa akiifurahia sana sehemu hii ya kuwachezea askari kila wanapokuja kupata taarifa muhimu za kitaalamu kutoka kwake.
“Vata, Vata, Vata…Relax bwana, okay?” Mgunda alimwambia kwa mzaha huku akionekana wazi kuwa amefurahia sana hali ile, kisha kabla Vata hajajibu, akaendelea akiwa amemakinika, mzaha wote akiwa ameuweka pembeni, “ Uchunguzi umeonesha kuwa marehemu alikuwa ameingiliwa kimwili…au ameshiriki tendo la ndoa, muda mchache kabla ya kufariki…hivyo unaweza ukaanza kufikiria kuwa huenda hayo majeraha yalitokana na mtu kumlazimisha marehemu kufanya naye tendo la ndoa…”
“Alibakwa?”
“Manii yameonekana katika sehemu ya uke wake…manii ya kiume yaliyoganda. Huenda ikawa alibakwa, huenda ikawa alifanya tu mwenyewe kwa ridhaa yake, hiyo sasa ni juu yako kung’amua.”

“Ndio. Majeraha mwilini, manii ya kiume…inawezekana. Hivyo akaamua kujiua baada ya kubakwa…” Vata alijiwazia kwa sauti huku akimtazama Dokta Mgunda kama vile ndio kwanza anamuona.
Mgunda aliguna.
“Kwa hawa mabinti wetu wa sasa bwana you never can tell my friend. Anaweza akafanya kwa hiyari yake mwenyewe, halafu baadaye akajifanya kamkumbuka mola wake, akajiliza na kuona bora afe tu kuliko kuishi duniani na dhambi hiyo…headache tupu!”
“Majeraha dokta…majeraha ndio jibu…hakukuwa na ridhaa kabisa hapo. Lete data zaidi dokta, kuna dalili zozote katika mwili wa marehemu zinazoonesha kuwa marehemu alikuwa ametumia kilevi chochote kabla ya kifo chake?”
“Hilo ndilo jambo la ajabu katika swala hili Sajenti.” Mgunda alijibu huku akichomoa picha kutoka kwenye lile faili, akainuka kutoka pale kwenye kiti alichokuwa amekalia na kwenda kusimama kando ya kiti cha John Vata huku akiitupia ile picha juu ya meza mbele ya yule askari. Vata aliinua ile picha na kuitazama kwa karibu zaidi. Ilikuwa ni picha ya Rose akiwa marehemu, ikionesha sura ya msichana yule na kuishia kifuani.
Kwa hakika alikufa kifo cha uchungu sana binti huyu. Vata alijikuta akiwaza baada ya kuona sura ya binti yule katika umauti.
Ilimuonesha Rose akiwa ametumbua macho katika ile dakika ya mwisho ya uhai wake hapa duniani. Mchirizi mdogo na mwembamba wa damu ulionekana kutoka kwenye moja ya tundu za pua yake, na michirizi mingine ya damu ilitoka katika kila kona ya mdomo wake. Sehemu yote ya mbele ya kifua chake ilikuwa imetapakaa damu iliyokuwa imetoka kinywani mwake alipokuwa akitapika kabla ya kukata roho.
Baada ya kuitazama ile picha Vata alimgeukia Mgunda kwa macho ya kuuliza .
“Hakukuwa na mabaki yoyote ya pombe au kilevi chochote kwenye damu ya marehemu nilipoipima mara baada ya kufika hapa…” Mgunda alimwambia, na kuendelea baada ya kutulia kidogo, “…ila damu iliyotoka hapa ilikuwa na kiasi kidogo sana cha aina ya kilevi, baada ya kupimwa, ambayo inathibitisha juu ya uwezekano wa marehemu kuwa katika hali ya ulevi baina ya muda aliobakwa na muda alipomeza vidonge vilivyosababisha kifo chake.” Dokta Mgunda alisema huku akielekeza ncha ya kalamu yake kwenye mchirizi wa damu ulioonekana ukitokea kwenye moja ya tundu za pua ya marehemu kwenye picha ile.
John Vata alimuinulia nyusi na kumtazama Dokta Felix Mgunda kwa muda kabla ya kumuuliza huku moyo ukimwenda mbio.
“Ni kilevi cha aina gani kilichoonekana kwenye damu hii, Dokta?”
Dokta Felix Mgunda alimtazama kwa muda kabla ya kumjibu.
“Cocaine.”

___________________

Kifo cha Rose kilileta mabadiliko makubwa sana kwa Moze. Alikuwa mnyonge sana na muda mwingi alipenda kukaa peke yake akikumbuka mambo mengi waliyokuwa wakiyafanya pamoja. Hakuweza kuendelea kuishi katika kile chumba alichofarikia rafiki yake, hivyo akahama kabisa pale chuoni na kuamua kuishi nyumbani kwao, ingawa aliendelea na masomo yake pale chuoni kama kawaida. Katika muda anapokuwa pale chuoni, hutumia muda wake kati ya vipindi akiwa chumbani kwa mpenzi wake Jaka.
Kwa upande wa Jaka kifo kile kilimletea mawazo na maswali mengi sana. Alijiuliza iwapo kifo kile kilikuwa kina uhusiano wowote na uhasama uliokuwapo baina yake na kundi la Tony. Wazo hili lilimtia uchungu sana, kwani lilimaanisha kuwa Rose atakuwa amekufa kwa ajili yake na Moze. Vilevile, lilimletea mawazo kuwa pengine mambo yaliyomtokea Rose yalipaswa yamkute Moze…kama si yeye kumshawishi kuhama pale chuoni kwa muda.
Lakini kwa nini Rose ajiue?
Kwa vyovyote sababu ya kifo chake ingejulikana iwapo angewahi kumalizia kuandika ile barua…
Lakini bado Tony na wenzake walimjia sana akilini…
Kwa namna fulani alikuwa na uhakika kabisa kuwa Tony na wenzake walihusika na kifo kile…lakini kivipi? Na kwa ushahidi gani? Jaka alijikuta akiazimia kumfuatilia rasmi Tony na wenzake hadi ajue ni nini hasa alichokuwa akikifanya pale chuoni zaidi ya kutafuta digrii.
Ni uamuzi ambao ulimbadilishia kabisa muelekeo wa maisha yake.

___________________

Raymond Mloo alimtazama rafiki yake kwa muda bila ya kusema neno. Hakujua aseme nini, ila aliloliona mbele yake lilikuwa ni tatizo. Tena tatizo kubwa…
“Kwa nini unataka ujiingize kwenye balaa la kufuatilia sababu ya kifo cha Rose Jaka? Mimi nilidhani hiyo ni kazi ya polisi!” Hatimaye aliamua kumuuliza rafiki yake.
“Kwa sababu Moze anadhani mimi nilijua kuwa jambo lile lingetokea, ndio maana nikamwambia yeye ahame pale chumbani kwao na kumwacha Rose apambane na mkasa uliopelekea kifo chake.” Alijibu kwa uchovu.
“Aaakh! Rose si ame-commit suicide bwana? Ina maana wewe ulijua kuwa Rose angejiua?” Raymond aliuliza kwa mshangao.
“Inaweza ikawa hivyo au ikawa hivyo ndivyo wote tulivyotakiwa tuelewe Ray. Polisi wanaamini kuwa Rose aliuawa…kuwa hata hivyo vidonge alivyomeza inawezekana ikawa amelazimishwa kuvimeza ili wote tuamini kuwa amejiua….” Jaka alijibu.
“Aaa-aa? Jaka unajua kuwa hivyo sivyo ilivyokuwa! Na hata kama ndivyo, si jukumu lako tena kuingilia kati kazi za polisi! Au unataka hao polisi waje wakuchukulie digrii hapa kwa niaba yako?
“Ninachotaka ni kujua iwapo ni kweli Rose aliuawa ili aliyefanya ukatili huo atiwe katika mikono ya sheria …”
“Na Moze anadhani kuwa wewe ulijua kuwa Rose angeuawa ndio maana ukamwambia yeye aondoke ili asiwepo wakati Rose anauawa?” Raymond aliuliza kwa mshangao.
“Sio kwa namna ambayo wewe unaiweka Ray, lakini ni kitu kama hicho.”
“Akh! Moze hana haki ya kuwa na mawazo kama hayo Jaka…usimuendekeze kwa kujiingiza kwenye majanga yanayoepukika! Itakuletea matatizo bure…hapana, itatuletea matatizo bure!”
Raymond alimjia juu. Jaka alipiga kimya kwa muda.
“Uko sahihi…lakini moyo wangu hautatulia nisipolifuatilia hili swala na kuweka kila kitu bayana…kwangu binafsi na kwa Moze pia. Kifo cha Rose hakipaswi kupita tu hivi hivi!”
Raymond alibaki mdomo wazi huku akimtazama.
“Basi kama hivyo ndivyo, kwa hakika tumo kwenye trouble rafiki yangu…” Hatimaye alisema kwa sauti ya chini, akimaanisha kuwa wamo kwenye matatizo. Jaka alimtazama rafiki yake huku mdomo wake ukifanya tabasamu dogo.
“Mko kwenye trouble na nani Ray? Hili ni swala langu sasa, wewe kaa chonjo!”
“Sasa hapo ndipo utakuwa kwenye matatizo zaidi, kwa sababu kwa kadiri nijuavyo mimi, hili swala sio lako wewe wala sio langu mimi, bali ni la polisi…kwa hiyo kama ni kulifuatilia basi tunalifuatilia pamoja, vinginevyo sote tunakaa chonjo na kuwaachia polisi wafanye kazi yao na sisi tujikite kwenye kutengeneza digrii hapa…upo?” Raymond alimjibu kwa msisitizo wa hali ya juu ulioonesha kuwa hakuwa na nia ya kuyumbishwa kwenye msimamo wake ule. Jaka alitaka kusema neno akabadili mawazo baada ya Raymond kumuinulia mkono kumnyamazisha.
“Usijitie ushujaa hapa, Jaka.” Raymond alimwambia huku mdomo wake ukifanya tabasamu hafifu. Jaka naye alitabasamu huku akitikisa kichwa chake kwa kukata tamaa. Dakika kumi baadaye walikuwa wakilijadili swala la kifo cha Rose huku wakinywa chai ya jioni mle chumbani mwao.
“Kwa hiyo wewe unadhani tutaanzia wapi katika huu uchunguzi wetu usio rasmi?” Jaka alimuuliza Raymond. Ray alimeza funda la chai kabla ya kuongea.
“Kwanza, kwani ni lazima tufuatilie swala hili Jaka ?” Ray alimtupia swali.
“Ohoo, Ray tulishaufunga mjadala huo bwana. Kwangu ni lazima kufuatilia swala hili ili niweze kujua sababu ya Rose kujiua, na kama ameuawa, basi nimjue muuaji ni nani. Hii itaniwezesha kufuta mawazo ya ajabu yanayopita kichwani kwa Moze juu ya swala hili na hatimaye kutupatia sote utulivu wa moyo…”
Ray alimtazama kwa muda rafiki yake kama kwamba alikuwa akimpima iwapo ni kweli alikuwa na uamuzi usioyumba juu ya swala hili.
“Oke, unaonekana unajiamini kiasi cha kutosha…mi’ nadhani tungeanzia kwa kuwauliza rafiki na majirani wa Rose pale bwenini iwapo waliweza kuona tabia yoyote isiyo ya kawaida kutoka kwa Rose katika siku chache kabla ya tukio …” Hatimaye Ray alitoa wazo.
“Au iwapo Rose alipata mgeni yeyote jioni au usiku wa kuamkia asubuhi ya tukio…” Jaka aliongezea.
Kwa hiyo walikubaliana kwenda kuwahoji baadhi ya wasichana waliokuwa wakiishi jirani na chumba cha Rose usiku ule. Lakini hawakuwahi kufanya hivyo kwani John Vata alifika pale chumbani kwao usiku ule kabla hawajatoka kwenda kuanza uchunguzi wao.
Baada ya kukaribishwa John Vata aliingia ndani ya chumba kile akiwa katika mavazi yake ya kiraia na kumtupia macho Raymond Mloo aliyekuwa amekaa kitandani, akamtazama Jaka na kuyarudisha tena macho yake kwa Raymond.
“Jaka Brown Madega…anaishi humu ndani?”
Jaka na Raymond walitazamana.
“Ndio. Mimi ndio Jaka…na huyu mwenzangu anaitwa Raymond…” Jaka alimjibu.
“Sijui mwenzetu ni nani…” Raymond alidakia.
“…na una shida gani na mimi” Jaka alimalizia. Halafu wote wawili wakabaki wakimkodolea macho kusubiri majibu. John Vata alijikuta akitabasamu kwa jinsi wale vijana walivyomtupia maswali yale kwa staili ya aina yake.
Ama kweli hapa nipo Chuo Kikuu!
Alijiwazia kabla ya kujitambulisha kwa wale vijana.
“Mimi ni Sajenti John Vata kutoka kituo cha Polisi cha OysterBay. Nina maswali machache ambayo ningependa kukuuliza kuhusiana na kifo cha msichana aliyeitwa Rose….na wewe pia bwana Raymond kama utakuwa na msaada katika hilo pia ningeuhitaji.”
Jaka na Raymond walitazamana na kuendelea kumkodolea macho yule jamaa aliyejiita Sajenti John Vata. Vata aliwatazama na kushindwa kuelewa iwapo maelezo yake hayakusikika na wale vijana au hayakueleweka.
“Vipi…sijaeleweka…au…?”
“Tumekuelewa, ila hatukuamini…kuna uthibitisho gani kama wewe kweli ni askari?” Jaka aliuliza. John Vata akatabasamu kwa mara ya pili tangu aingie katika chumba kile.
Kwa hakika hapa nipo Chuo Kikuu.
Alitoa kitambulisho chake na kumkabidhi Jaka ambaye alikiangalia kwa makini, na bila ya kusema neno akamkabidhi Raymond Mloo. Raymond naye alikitazama kwa umakini kama ule alioonesha Jaka, kisha akamrudishia Jaka bila ya kusema neno. Jaka alikipokea na kumrudishia Vata kitambulisho chake kisha akamgeukia Raymond na wakatazamana tena bila ya kusema neno. Vata aliwaangalia kwa makini vijana wale. Hatimaye Jaka alimgeukia yule Sajenti na kumwambia huku akitoa tabasamu kubwa kama kwamba ndio kwanza wanaonana.
“Karibu sana Sajenti John Vata. Sijui ni nini hasa ulikuwa unahitaji kutoka kwetu?”
Vata alikaa vyema kwenye kiti alichokaribishwa na kukunja nne na kuielekeza kauli yake moja kwa moja kwa Jaka.
“Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, ninataka kukuuliza maswali kadhaa juu ya kifo cha msichana aliyekuwa akisoma hapa Chuoni aliyeitwa Rose…”
“Kwa nini mimi, Sajenti?”
“Kwa sababu kama sikosei wewe una uhusiano wa kimapenzi na msichana aitwaye Moze, ambaye ndiye alikuwa rafiki mpenzi wa marehemu, sio?”
“Ndiyo…”
“Na pamoja na kuwa rafiki mpenzi wa marehemu, Moze pia aliishi chumba kimoja na marehemu, sawa?”
“Sawa…”
“Je, hakuna hata siku moja ambayo Moze aliwahi kukuongelea juu ya tabia isiyo ya kawaida kutoka kwa Rose?”
Jaka alikaa kimya kidogo, kisha akashusha pumzi ndefu kabla ya kumjibu.
“Kwa kweli ni nadra sana mimi na Moze kuongea kuhusu Rose, na katika mara chache hizo, hakuna hata siku moja ambapo Moze aliwahi kuniongelea jambo baya juu ya Rose…na hiyo ni kwa sababu Rose hakuwa na tabia yoyote isiyo ya kawaida.”
John Vata alikuwa akimtazama kwa makini wakati akijibu swali lile. Na aliendelea kumtazama hivyo kwa sekunde kadhaa baada ya Jaka kumaliza kuongea, kisha akamtupia swali jingine.
“ Tabia ya Rose kujiua ni ya kawaida kwako?”
Swali lile liliwababaisha kidogo wale vijana. Raymond alitaka kusema neno akanyamaza. Jaka alifumbua mdomo, akaufumba, kisha akajibu akiwa makini zaidi.
“Si tabia ya kawaida…ila hakukuwa na kitu chochote ambacho kingewezesha kujua ni nini Rose alikuwa amepanga kufanya…”
“Kwa hiyo unaamini kuwa Rose amekufa kwa kuwa mwenyewe alipanga kujiua siku ile?”
“ Kama unataka kujua ninavyoamini Sajenti, basi mimi sijui ni nini cha kuamini…kwa sababu mpaka sasa sioni sababu ya Rose kujiua.” Jaka alijibu huku akimkazia macho yule Sajenti. Vata alimtazama kwa muda na kuandika kidogo kwenye kijitabu chake kidogo alichokitoa kwenye mfuko wake wa shati.
“Katika muda wote uliojuana na Rose, haijapata kukutokea kuwa Rose angeweza kuwa anatumia madawa ya kulevya?”
Swali lile liliwashitua tena Raymond na Jaka.
“Hapana aisee…Rose hakuwa akitumia madawa ya kulevya na wala hakukuwa na sababu yoyote ya kunifanya nimhisi kuwa alikuwa akitumia madawa ya kulevya…kwani vipi Sajenti?” Jaka alimjibu na kumtupia na swali. Vata alimtazama kwa muda na kuandika tena kidogo katika kijitabu chake kabla ya kuongea.
“Katika chumba alichokuwa akiishi marehemu, kumekutwa kiasi fulani cha unga wa kulevya. Unaweza kusema nini juu ya hilo?”
Jaka alibaki akimkodolea macho yule askari kama kwamba sasa alikuwa anagundua rasmi kuwa yule askari alikuwa mwehu.
“Una mawazo gani kuhusu swala hilo?” Vata aliuliza tena.
“Aah…mtu yeyote anaweza kuja na kumuwekea huo unga chumbani mwake…sidhani kama Rose alikuwa anatumia madawa ya kulevya afande…bia ya kawaida tu alikuwa haigusi, sembuse unga wa kulevya! Hapana…itabidi utafute maelezo mengine afande…”
“Ukizingatia kuwa alikuwa akiishi na Moze mle ndani, maelezo pekee yanayokuja ni kwamba huenda Moze akawa ndiye huyo aliyeupeleka ule unga mle ndani …unalionaje hilo?”

Jaka alimaka kwa sauti huku akimtumbulia macho ya kutoamini yule askari, na hapo Ray akaingilia kati.
“Hapana afande, sasa huko unakoelekea siko! Moze hawezi kufanya kitu kama hicho…”
“Na kwa nini afanye kitu kama hicho wakati Rose alikuwa rafiki yake?” Jaka naye alidakia, akaendelea, “…Kama kumekutwa unga wa kulevya mle ndani, basi ni dhahiri kuwa kuna mtu mwingine aliyeingia na kuuweka unga huo, mtu wa tatu, lakini si Moze wala si Rose, Sajenti. Na nadhani huyo ndiye unayemtafuta.”
John Vata aliwatazama wale vijana na kuyatafakari maelezo yao. Aliamua kutupa kombora jingine.
“Na utasema nini iwapo nikikueleza kuwa vipimo vilivyofanywa kwenye damu ya marehemu vimeonesha kuwa damu yake ilikuwa na kiasi fulani cha madawa hayo?”
Hapo Jaka na Raymond walitoa miguno ya mshangao kwa pamoja. Kwao hiyo ilikuwa ni taarifa mpya kabisa.
“Haiwezekani!” Jaka aliropoka.
“ No way!” Raymond alibwata.
Vata aliwatazama wale vijana mmoja baada ya mwingine. Mishangao aliyoiona kwenye nyuso zao ilikuwa ni ya kweli kabisa. Jaka alitaka kusema neno, akajikuta hajui aseme nini. Akabaki akimkodolea macho tu yule sajenti.
“Je, Rose alikuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote hapa chuoni au nje ya chuo?”
“Hapana.” Wote wawili walijibu kwa pamoja. Vata alitikisa kichwa kuafiki jibu lile, kwani ndilo alilolipata kutoka kwa Moze. Aliwatupia kombora jingine tena.
“Uchunguzi wa mwili wa marehemu umeonesha kuwa Rose alikuwa amefanya tendo la ndoa masaa kadhaa kabla ya kifo chake…”
“Whaaat?” Raymond alimaka kwa sauti, huku Jaka naye akitoa mguno mkubwa wa mshituko. Vata aliona ile mishangao iliyokuwa kwenye nyuso zao ikibadilika na kuwa mishituko. “…na pia mwili wake ulikuwa na alama za kutobolewa na kitu chenye ncha kali kama kisu, alama za kupigwa makofi usoni na kukabwa shingoni.” Alimalizia John Vata huku akiwatazama usoni wale vijana mmoja baada ya mwingine.
“Mungu wangu!” Jaka alisema kwa sauti ya chini huku hasira ikiongezeka katika ule mchanganyiko wa mshituko na fadhaa. John Vata alitulia kimya akiwaangalia jinsi wale vijana walivyozipokea taarifa zile.
Jaka aliinuka na kuelekea dirishani huku uso wake ukiwa na mchanganyiko wa mshituko na fadhaa kubwa.
“Kwa hiyo Rose atakuwa ameuawa…yaani siyo suicide tena bali ni murder…mauaji…Oh Shit! This is too bloody much sasa!” Raymond Mloo alilalamika kwa mshangao na kuchanganyikiwa.
“Au kuna mtu aliyemfanyia mambo mabaya binti yule…mambo ambayo yamemfanya Rose aone kuwa hakuwa na haja tena ya kuendelea kuishi hapa duniani, hivyo akajiua…bila shaka ndiyo huyo aliyekuwa akijaribu kumuelezea kwenye ile barua aliyoiacha…” Jaka aliongea kwa sauti ya chini sana, kama kwamba alikuwa akijiwazia peke yake.
“Na huyo mtu ndiye ninayedhamiria kumpata, kwa sababu ndiye atakayetoa maelezo kuhusu ule unga wa kulevya uliokutwa ndani ya chumba kile.” John Vata alimalizia.
Kisha kama aliyezinduka Jaka alimtaza yule Sajenti kwa muda kisha akamuuliza: “Kwa nini unatueleza mambo yote haya Sajenti?”
“Ili mpate kuona umuhimu wa msaada wenu kwangu katika kumtia mbaroni huyo mtu wa tatu, ambaye tunaamini kuwa ndiye aliyemfanyia Rose unyama wa hali ya juu kiasi hicho.”
Jaka alirudi na kukaa kwenye kiti akiwa amejiinamia huku amejishika kichwa kwa mikono yake miwili. Hasira zilizidi kumpanda kadiri alivyokuwa akitafakari unyama aliotendewa Rose. Alikumbuka jinsi Rose na Moze walivyomhangaikia siku Muddy na Alphonce Ng’ase walipompa kipigo kizito kule Club Billicanas. Wazo la Rose kubakwa ndilo lililomtia uchungu zaidi.
Masikini Rose…hakuwa na shari na mtu yeyote, alikuwa msichana muungwana na mtaratibu… alikuwa sawa na dada yangu kwa kweli, sasa leo anatokea mtu na kumfanyia unyama kiasi hiki!
Machozi yalimtoka kwa hasira na uchungu na alihisi fundo kubwa la mate likimkaa kooni. Tony alimjia akilini mwake…
“Moze alikuwa na Rose katika dakika zake za mwisho kabla ya kufariki…” John Vata alikuwa akisema. “…na maneno ya mwisho ya Rose kabla hajaaga dunia ni Moze pekee ndiye aliyepata bahati ya kuyasikia…” Vata aliendelea. Jaka alikuwa akimsikia kwa mbali sana, akili yake ilikuwa imegawanyika katika mafungu mengi na sehemu ndogo tu ya akili yake ndiyo iliyokuwa ikimsikia yule Sajenti.
“Fikiri kwa makini Jaka, kisha uniambie ni maneno gani hasa Rose alimwambia Moze, kutokana na jinsi wewe ulivyoongea na mpenzi wako? Iwapo bado hujaongea naye juu ya swala hili, basi fanya hivyo halafu tuwasiliane.” Vata alimwambia huku akimkabidhi kadi ndogo iliyokuwa na namba zake za simu. Jaka aliinua uso wake kumtazama yule askari huku akiipokea ile kadi. Macho yake yalibadilika rangi na kuwa mithili ya vidonge viwili vya moto vinavyoelea kwenye maji kutokana na machozi yaliyomjaa machoni. Alijipangusa machozi kwa viganja vya mikono yake.
“Eem, nilishawahi kuongea na Moze juu ya swala hilo.” Alisema, na Vata aliendelea kumsikiliza akiwa kimya, na Jaka akaendelea, “Kwa mujibu wa maelezo ya Moze, ni kwamba Rose alionekana kusisitiza sana kumwambia jambo fulani lakini alikuwa katika maumivu makali kiasi kwamba alishindwa kueleza ni jambo gani hasa…akabaki akirudia maneno ‘unajua ninachosema’, tena na tena.”
John Vata aliendelea kumtazama tu bila ya kusema neno, jambo lililomfanya Jaka amuulize.
“Nadhani na wewe pia amekueleza hivyo hivyo…?”
John Vata alimtazama Jaka kwa muda kabla ya kumjibu.
“Mimi najua Moze amenieleza nini, ninachotaka kujua sasa ni nini alichokueleza wewe.”
Jaka na Raymond walitazamana.
“Alichonieleza mimi ndio hicho afande…kwamba maneno ya mwisho ya Rose yalikuwa unajua ninachosema…” Jaka alimjibu, na alipoona bado John Vata anaendelea kumtazama bila ya kusema neno huku akionesha wazi kuwa alikuwa hamuelewi, aliongezea: “…Moze aliniambia kwamba, kwanza Rose aliyatamka maneno hayo kama swali, lakini mara ya pili na ya tatu aliyatamka sio kama swali, bali kama taarifa kamili…kwamba Moze anajua ni nini Rose alikuwa anasema…”
“Na Moze alijua ni nini Rose alikuwa anasema, au anamaanisha kwa kauli hiyo?” Aliuliza John Vata.
“Moze hakuelewa, na mpaka wakati naongea naye jambo hili bado alikuwa anashindwa kuelewa ni nini Rose alichokuwa anakiongelea, na kwa nini alikuwa akisema maneno yale…yeye anadhani labda ilikuwa ni katika kutapatapa tu kabla ya kukata roho.” Jaka alimjibu kwa kirefu. John Vata alimtazama kwa muda bila ya kusema neno. Kisha akaamua kuangalia ncha ya kiatu chake kizuri kwa muda ambao Jaka na Ray waliuona kuwa ni mrefu sana. Kimya kulitanda mle ndani. Hatimaye John Vata alishusha pumzi na kuangalia saa yake na kumwambia, “Fikiri kwa makini Jaka. Nataka maneno halisi ambayo Moze alielezwa na Rose siku ile, sio ufafanuzi wa maneno aliyoelezwa.”
“Kkha! Huyu jamaa vipi?” Raymond Mloo alishindwa kujizuia na kuuliza kwa mshangao huku akimtazama Jaka. Lile swali pia lilimkera Jaka ambaye alimtazama yule askari kwa hasira. John Vata alimtazama Raymond kwa utulivu mkubwa, kisha akamgeukia Jaka. Wakatazamana kwa muda, Jaka akiwa amefura kwa hasira, Vata akiwa na utulivu wa hali ya juu. Hatimaye Jaka aliongea.
“Sikiliza Sajenti, Rose alikuwa kama dada kwangu, na jambo lolote nitakaloweza kulifanya ili kuwezesha kukamatwa kwa mtu aliyesababisha kifo chake, nitalifanya. Sasa nisingependa wewe unifanye mimi kama mpumbavu tu ninayesema mambo nisiyoyaelewa, sawa bwana?”
“Bado hujajibu swali langu Jaka.” Vata alimwambia kwa utulivu, bila kuonekana kujali jinsi yule kijana alivyomkasikia. Raymond Mloo alitupa mikono yake hewani huku akizungusha mboni za macho yake kwa kuonyesha kuchoshwa na kukatishwa tamaa na tabia ya yule askari. John Vata alikiona kitendo kile lakini hakujali, aliendelea kumtazama Jaka, akisubiri jibu. Jaka alitaka kusema neno lakini alijizuia. Badala yake alianza kuhesabu kimya kimya moja mpaka kumi ili kujipa muda wa kupunguza ghadhabu zilizokuwa zikielekea kumshinda nguvu ya kuzizuia. Kisha alimwambia yule askari kwa utaratibu wa hali ya juu:
“Moze aliambiwa na Rose maneno yafuatayo kabla ya Rose kuaga dunia…” Hapo alitulia kidogo na kuendelea kumtazama yule askari, kisha akaendelea: “ U-na-ju-a ni-na-cho-se-ma.” Alimtamkia neno moja baada ya jingine ili kuhakikisha kuwa yule askari anamuelewa.
“Umeelewa sasa?” Raymond Mloo alidakia baada ya Jaka kumaliza kumtamkia maneno yale. Huku macho yake yakiwa bado yamemuelekea Jaka, John Vata alijibu.
“Nimekuelewa…pia naelewa kuwa na mimi Moze aliniambia kuwa Rose alimwambia maneno kama hayo…” Alimkazia macho Jaka na kutulia kwa muda kabla ya kumalizia kauli yake, “…kwa lugha ya kiingereza.”
Ilichukua kama dakika tatu nzima kwa maneno yale kuleta maana kichwani kwa Jaka. Na yalipoleta maana, Jaka hakutaka kuamini kuwa ni kweli ile ndio maana yake.
Lakini sasa ndio inaleta maana kabisa!
Alibaki kimya akiendelea kuyatafakari maneno yale, na kadiri alivyoendelea kuyatafakari ndivyo yalivyozidi kuleta maana na kumhakikishia kuwa alichokigundua kutokana na ufafanuzi ule wa John Vata ni sahihi kabisa.
Rose alijiua, na kuna mtu, mtu wa tatu, aliyesababisha Rose achukue uamuzi wa kuung’oa uhai wake yeye mwenyewe. Ni Rose pekee ndiye aliyewahi kumuona huyo mtu, na kwa kujua kuwa akifa hakuna atakayeweza kumjua mtu huyo anafanya bidii ya kumueleza Moze juu ya mtu huyo. Kutokana na kutapatapa na maumivu ya kukata roho, Rose anakumbuka maneno ambayo anajua Moze akiyasikia ataelewa ni mtu gani anayehusika na kifo chake. Anamueleza “unajua ninachosema”, kwa lugha ya kiingereza… unajua ninachosema…you know what I am saying…you know what I’m sayin’…
Tony…!
Ni Tony ndiye aliyependa sana kutumia maneno yale…you know what I’m sayin’…!
Kumbe Tony ndiye huyu mtu wa tatu tuliyekuwa tukijaribu kumtafuta! Ni Tony ndiye aliyemfanyia Rose unyama kiasi kile hata akaamua kujiua!
Muda wote huo John Vata alikuwa akimtazama Jaka kwa makini akitafakari juu ya maneno yale. Na wakati akimtazama aliweza kuona jinsi uso wa Jaka ulivyokuwa ukibadilika katika kila sekunde ambapo vipande vingi vya uerevu vilijiunga kichwani mwake na kuleta picha kamili ya kifo cha Rose.
Wazo la kuwa Tony ndiye aliyemtenda Rose mpaka akaamua kujiua lilimzonga sana moyoni kiasi alijihisi akishindwa kupumua vizuro kwa ghadhabu.
Yaani Tony! Tony! To…
“Aaaaaaaaarrrrgh!” Jaka alipiga ukelele wa ghadhabu, na kuishia kutupa tusi zito la nguoni huku akipiga ngumi nzito ndani ya kiganja cha mkono wake. Akasonya na kunyanyuka kwenda kusimama nyuma ya dirisha, akabaki akiangalia nje huku akitiririkwa na machozi. Vata aliinuka na kumsogelea Jaka pale dirishani.
“Ni nini Jaka? Umegundua nini?” Alimuuliza kwa utulivu, ingawa mapigo ya moyo wake yaliongeza kasi maradufu. Raymond Mloo naye alikuwa na hamu ya kuelewa ni nini kilichojengeka kichwani mwa Jaka kutokana na taarifa ile ya John Vata, kwani kwake yeye bado ilikuwa haijaleta maana.
“Ddah! Kumbe ni kweli hisia zangu zilikuwa sahihi…” Jaka aliongea kwa sauti ya chini huku akiendelea kuangalia nje ya dirisha. “…jambo lilikuwa wazi kabisa! Rose alikuwa akijaribu kumtajia Moze mtu aliyemfanyia unyama uliomfanya achukue hatua ya kujiua…na muda wote huu Moze…sisi…hatukuweza kuelewa ni nini maana ya maneno yale…”
“Ina maana sasa tunaweza kumtambua mtu aliyekuwa chumbani kwa Rose kabla ya kifo chake?” John Vata aliuliza kwa matumaini. Jaka alimgeukia yule askari.
“Ndiyo. Huyo mtu mimi nimeshamjua. Ni mtu mbaya sana. Lakini sidhani kama utaweza kufanya lolote hata kama nikikutajia.” Alimjibu kwa upole na masikitiko, na bila kusita John Vata alimajibu.
“Sheria haichagui bwana Jaka. Hakuna mtu yeyote, popote pale anayeweza kujiweka juu ya sheria. Sisi sote tuko chini ya sheria…nitajie mtu huyo bwana Jaka, halafu ushuhudie jinsi sheria itakavyofanya kazi yake.”
Jaka alimtazama kwa muda bila ya kumjibu. Alionekana kuwa mwenye kujiamini kiasi cha kutosha na lile jibu lake lilimtia imani kubwa sana. Alimtazama Raymond ambaye naye alikuwa akimtazama kwa matumaini makubwa. Alishusha pumzi ndefu kabla ya kumfumbulia Sajenti John Vata fumbo lililokuwa likiisumbua akili yake.
“Mtu unayemtafuta sajenti anaitwa Tony, Anthony Athanas Wanzaggi. Yeye pia ni mwanafunzi wa hapa hapa chuoni na ni mtoto mbaya sana…huyo ndiye aliyemfanyia Rose unyama uliopelekea kwenye kifo chake.”
“Jaka una hakika…?” Raymond Mloo alimuuliza kwa mashaka.
John Vata aliendelea kumtazama yule kijana bila ya kusema neno huku akiyatafakari maneno aliyoambiwa.
“Siku zote nilikuwa naelewa kuwa Tony ni mtoto mbaya, lakini sikutegemea kuwa ubaya wake ungefikia kiwango kama hicho…” Raymond alisema kwa mshangao uliochanganyika na simanzi ya hali ya juu. John Vata aliendelea kumtazama Jaka kwa makini, na aliona kuwa yule kijana aliamini kabisa maneno aliyokuwa anayasema.
“Nadhani sasa utahitaji kutoa maelezo zaidi juu ya huyu Tony, bwana Jaka…na kwa nini unadhani kuwa yeye ndiye mtu ninayemtafuta.”
“Not a problem, Sajenti.”
“Wacha niongeze chai, inaelekea kikao kitakuwa kirefu.” Raymond alisema huku akichukua birika la umeme wanalotumia kuchemshia chai.
Nusu saa baadaye, akiwa ameshasikia kila kitu kuhusu Tony na kundi lake, na historia mbaya baina yao na Jaka, Sajenti John Vata aliinuka na kupeana mikono na wale vijana. Aliwashukuru kwa msaada wao na kukumbusha kuwa iwapo kutatokea tatizo au taarifa nyingine yoyote mpya, wawasiliane naye.
Waliagana.

___________________

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Poisent Ndimbalema, mkuu wa kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya katika wilaya ya Kinondoni, aliisoma kwa mara ya pili ripoti iliyowasilishwa mezani kwake na Sajenti John Vata, na kwa mara nyingine tena alijikuta hajui la kufanya.
Ilikuwa ni ripoti nzuri na kwa kanuni na misingi ya kazi, jambo alilotaka kulifanya Sajenti Vata lilikuwa ni sawa kabisa. Lakini Mrakibu Mwandamizi Poisent Ndimbalema, akiwa na umri wa miaka arobaini na minane alielewa zaidi jinsi mambo yalivyokuwa yakiendeshwa kuliko Sajenti John Vata ambaye bado alikuwa mgeni katika jeshi la polisi.
Mzee Athanas Wanzaggi alikuwa ni mtu mkubwa sana sio tu jijini Dar es Salaam, bali pia nchini kote. Ingawa hakuwa Waziri wala kiongozi yoyote serikalini, utajiri wake ulifahamika na kila mtu nchini, mawaziri na viongozi wakubwa serikalini wakiwemo. Yeye pamoja na viongozi wake wa kazi walimtambua mzee Wanzaggi ni nani na ana uwezo gani katika nchi hii. Ndimbalema alijua kuwa kutokana na ripoti ile, John Vata alitakiwa amuweke chini ya ulinzi kwa mahojiano mtoto wa mzee Wanzaggi. Pia alitakiwa aende nyumbani kwa mzee Wanzaggi na afanye upekuzi katika chumba cha mtoto yule ambaye bado alikuwa chini ya himaya ya baba yake.
Alijaribu kufikiria jinsi magazeti yatakavyoiandika habari ile na mwili ulimsisimka. Waandishi wa habari wana namna ya kunusa mambo kama haya…sijui wananusaje…na wakishanusa huwa hawana simile…
Aliiweka pembeni ile ripoti ya kurasa ishirini na kuzitupia macho karatasi mbili zilizokuwa mezani kwake ambazo ziliidhinisha kufanyika kwa matendo ambayo Sajent Vata alipendekeza yafanyike katika ripoti ile yake.
Karatasi moja ilikuwa ni “Search Warrant” iliyomuidhinisha Sajenti John Vata kwenda kupekua vyumba vya Anthony Wanzaggi, kile cha nyumbani kwa baba yake na kile anachotumia pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Karatasi ya pili ilikuwa ni “Arrest Warrant”, ambayo ilimpa Sajenti John Vata idhini ya kumkamata na kumuweka chini ya ulinzi Anthony Wanzaggi kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha Rose na kwa mahojiano kuhusu kiasi cha unga wa dawa za kulevya kilichokutwa chumbani kwa Rose.
John Vata asingeweza kuzitumia idhini zile bila ya yeye, Mrakibu Mwandamizi Poisent Ndimbalema, kusaini katika sehemu zinazostahili kwenye karatasi zile. Ni saini zake ndizo zilizokuwa zinasubiriwa ili kumfanya John Vata aweze kutekeleza kazi yake ambayo kwa hakika alikuwa ana ari nayo sana.
Mrakibu Mwandamizi Poisent Ndimbalema alikunja uso na kufikiri kwa muda mrefu, kisha alishusha pumzi ndefu na kuchukua simu yake ya kiganjani, akaanza kumpigia mkubwa wake wa kazi, mkuu wa Idara ya kudhibiti madawa ya kulevya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) wa Polisi, Albert Bangusillo.

_____________________

“Kwa sasa hivi usifanye jambo lolote, Poisent. Umefanya vizuri sana kunitaarifu juu ya habari hii kabla ya kuchukua hatua yoyote…” Albert Bangusillo alitoa maelekezo kupitia kwenye simu baada ya kusikiliza maelezo ya Mrakibu Mwandamizi Poisent Ndimbalema, kisha akaendelea, “… nitakupigia simu baada ya muda mfupi kukupa maelekezo zaidi juu ya nini cha kufanya, na asijue mtu mwingine yeyote kuhusu hiyo ripoti ya Vata na swala zima hilo mpaka hapo utakapoelekezwa vinginevyo, sawa?” Akakata simu.
“Sawa mzee…” Albert alijibu, lakini simu ilikuwa imeshakatwa.
Upande wa pili wa simu ile, ACP Albert Bangusillo alifikiria kwa muda mfupi kisha akaitumia tena simu yake kupiga namba fulani. Upande wa pili simu ile ilipokelewa na Bangusillo aliisikia sauti aliyoitarajia, sauti iliyotulia, iliyotoka kama kwamba mwenye sauti ile alikuwa amepaliwa na moshi.
“ Hallo… Raul hapa…”
Dakika kumi baadaye simu ya Mrakibu Mwandamizi Poisent Ndimbalema iliita. Poisent alipoiinua simu ile, alipokea maelekezo kutoka kwa ACP Albert Bangusillo kuhusiana na Sajenti John Vata.

__________________

Upande mwingine, mapenzi baina ya Jaka na Moze yaliendelea kama kawaida, ingawa kwa siku za mwanzo baada ya kifo cha Rose yalilegalega kutokana na Moze kutokuwa katika hali yake ya kawaida na kujilaumu sana kwa kutokuwa pamoja na rafiki yake siku ile aliyokumbwa na maafa yale ambayo wao wangeweza kukisia tu yalikuwa ni makubwa kiasi gani, kwani ni Rose pekee ndiye aliyejua ukubwa wa maafa yale. Lakini kadiri siku zilivyopita, ndivyo hali ilivyozidi kurudi kama hapo awali.
Kufikia wakati huu hakukuwa na shaka tena baina yao juu ya nani aliyemfanyia Rose unyama ulioishia kwenye kifo chake kwani fumbo lililokuwa kwenye maneno ya mwisho ya Rose lilishafumbuliwa na wote waliamini kuwa baada ya muda mfupi, mkono mrefu wa sheria ungemtia Tony mbaroni kama jinsi Sajenti Vata alivyoahidi na alivyoonesha kudhamiria.
Waliamua kuwasahau Tony na wenzake na kuyaacha nyuma yaliyomtokea rafiki yao Rose, na kuangalia mbele.

____________________

Wiki mbili baadaye Raymond Mloo aliyeonekana mwenye wasiwasi na asiyekuwa na raha aliingia chumbani kwao pale chuoni na kumkuta Jaka akijisomea. Jaka alimuuliza kulikoni.
“Inakuwaje mpaka leo Tony bado anatemebea huru tu, Jaka?” Ray aliuliza kwa hasira, kisha akendelea, “Yaani…nilitegemea tangu siku ile yule sajenti alipokuja kutuuliza maswali yake hapa agalau angekuwa ameshakamatwa na kuhojiwa kikamilifu, sio…?”
“Sasa Ray, una hakika gani kuwa bado hajahojiwa na polisi mpaka sasa?”
Raymond alitupa mikono yake hewani na kwa kukata tamaa.
“Aakh! Kila kitu kiko wazi…ile sio tu kesi ya madawa ya kulevya, bali ni ya mauaji pia…usitake kuniambia kuwa ameweza kutoa maelezo ya kutosha kuwafanya polisi wamwachie kwa tuhuma zote mbili Jaka…yule wameamua kumuachia tu bwana!” Alimaka.
“Hizo ni tuhuma nzito sana Ray, sio rahisi kuachiwa hivi hivi tu bila ya kuchukuliwa hatua….”
“Eee..enhe-e? Then welcome to the world my friend…hivi ndivyo dunia ilivyo siku zote! Kinyume na utaratibu, kinyume na matarajio!” Alitoka tena nje kwa hasira na kubamiza mlango. Kwa muda mrefu Jaka alibaki akiwa anaukodolea macho ule mlango akiyatafakari yale maneno ya Raymond Mloo…
Wiki moja baadaye Jaka alimuona Tony.
Ilikuwa ni kiasi cha saa tatu za usiku hivi wakati alipokuwa akitoka maktaba kujisomea. Ingawa ilikuwa usiku, aliweza kumtambua mara moja kutokana na mwendo wake. Tony alipita kama hatua kumi mbele yake bila ya kumjua akielekea sehemu ya kuegesha magari iliyoko kando ya duka la vitabu la pale Chuoni. Huku moyo ukimwenda mbio, Jaka aliongeza hatua na kuanza kumfuata kwa nyuma, ingawa hakujua angemfanya au angemwambia nini pindi akimfikia–akilini mwake alikuwa akiyakumbuka maneno ya Raymond Mloo kuhusiana na swala zima la Tony kutochukuliwa hatua yoyote na polisi. Tony alipita ubavuni mwa jengo la ofisi ya posta lililokuwa jirani na duka la vitabu pale chuoni, na Jaka alipita upande wa pili wa lile jengo ambako ndio kulikuwa na njia ya wapitao kwa miguu, kwani ni wenye magari yaliyoegeshwa kwenye ule uwanja wa kuegeshea magari tu ndio waliopita upande ule aliopitia Tony. Kutokea pale alipokuwa aliweza kumuona Tony akiwa katika harakati za kufungua mlango wa gari lake lililokuwa limeegeshwa katika uwanja ule.
Kulikuwa kuna gari jingine moja lililoegeshwa kando ya lile la Tony, na mbele zaidi kulikuwa kuna Baa ya wanafunzi ambako muziki ulisikika ukitokea upande huo. Mara, kama aliyekumbuka kitu, Tony aligeuka kuangalia upande ule ulipokuwa ukitokea ule muziki, halafu aliondoka kuelekea kule Baa huku akiacha mlango wa gari lake ukiwa wazi. Haraka sana Jaka aliuruka uzio wa mabomba uliouzunguka uwanja ule na kukimbia upesi hadi ubavuni mwa gari la Tony. Kwa jinsi lile gari lilivyoegeshwa, ule mlango wa dereva ulikuwa upande ilipokuwa ile Baa.
Taratibu aliweka vitabu vyake chini na kukiweka kwenye mfuko wake wa shati kijitabu chake kidogo cha anuani, kisha alijiinua taratibu na kuanza kuchungulia ndani ya lile gari kwa kupitia dirishani. Kwenye kiti cha abiria kando ya kile cha dereva kulikuwa kuna mkoba mdogo wa kiofisi, au Briefcase, ambao hakuweza kung’amua mara moja ulikuwa wa rangi gani kutokana na mwanga hafifu katika eneo lile. Alitupa jicho kule alipoelekea Tony na kumuona akiongea na jamaa wengine wawili nje ya ile Baa hali wanafunzi wengine wachache wakiwa wamezagaa nje ya Baa ile, wengi wao wakiwa wanasubiri chipsi na mishikaki vilivyokuwa vikiuzwa pale nje.
Alirudisha macho yake kwenye kiti cha nyuma ndani ya lile gari na mara moja alibonyea tena ubavuni mwa gari lile baada ya kusikia sauti za watu zikielekea pale alipokuwa kutokea nyuma yake. Lilikuwa ni kundi la wanafunzi waliokuwa wanatoka kwenye mijadala ya kujisomea kwa makundi, na wengine, kama yeye walikuwa wanatoka maktaba. Lile kundi la wanafunzi lilipita kwa vicheko na maongezi ya sauti za juu. Jasho lilianza kumtiririka mgongoni na usoni huku moyo ukimwenda mbio kwa wasiwasi. Wale jamaa walisimama mbele ya duka la vitabu kwa kama dakika mbili hivi wakati mmoja kati yao akisimulia kituko fulani kabla ya wote kuangua kicheko kingine kikubwa sana na kuendelea na safari yao huku wakicheka na wengine wakikimbia. Na hapo sauti ya Tony ilimfikia wazi wazi kutokea kule kwenye baa, akicheka kwa sauti na baadhi ya watu wengine kule, kisha akawapazia sauti wale watu aliokuwa akicheka nao.
“Okay, see you tomorrow guys…mi’ naenda down town mara moja, you know what I’m sayin’!”
Jaka alimakinika pale alipojibanza.
Town saa hizi…?
Bila ya kufikiri zaidi, Jaka alipeleka mkono wake na kuvuta sehemu iliyofungua buti la lile gari na kule nyuma buti likafunguka. Alitambaa chini chini hadi nyuma ya lile gari na kuingiza mkono wake ndani ya buti kulizuia lisijifunge na kujibana, kisha akabaki akimchungulia Tony kupitia kwenye dirisha la nyuma la lile gari. Alimuona Tony akiwa amekaa kwenye kiti cha dereva huku akiwa anaongea na simu ya kiganjani. Kisha Tony aliweka simu yake pembeni na kuanza kutia gari moto. Jaka aliliinua lile buti na kujitumbukiza ndani na kabla hajajifungia kabisa ndani ya lile buti, alipachika tambara alilolikuta mle ndani kwenye loki ya buti ili lisijibane wakati yuko mle ndani akashindwa kutoka. Gari lilirudi nyuma na kugeuza kabla ya kuondoka kwa kasi kutoka eneo lile, yeye akiwa ni abiria asiyetakiwa ndani yake.
Safari haikuwa nzuri kwake, kwani alilazimika kujikunja mle ndani ya buti la gari huku akiwa amelalia ubavu, na akiwa ameukamatia kwa ndani ule mlango wa buti ili usiwe unajibamiza-bamiza naye akitupwatupwa kila gari lilipokuwa likizidi kukata mitaa kuelekea kusipojulikana. Kiasi cha kama dakika ishirini na tano baadaye Jaka aliinua taratibu mlango wa lile buti na kuchungulia. Walikuwa kwenye daraja la Salenda. Alishusha mlango ule taratibu na kujilaza tena ndani ya buti lile. Hakujua ni kitu gani kilichomfanya aamue kumfuatilia Tony kiasi cha kujikuta katika hali ile, lakini alijua kuwa kwa pale alipofikia, hakuweza kurudi nyuma tena.
Mwendo mfupi na kona kadhaa baadaye, alihisi lile gari likisimama na akasikia honi. Akajua wamefika walipokuwa wakielekea. Alisubiri kidogo kisha akainua mlango wa buti na kuchungulia. Hakuweza kuelewa pale walikuwa wapi. Aliona magari yakipita kwa mbali na alihisi kusikia harufu ya bahari, lakini hakuwa na uhakika. Gari lilianza kwenda tena kwa mwendo mdogo na Jaka alijifungia tena ndani ya buti. Mwendo mfupi baadaye gari lilisimama tena. Kwa mbali Jaka aliweza kusikia sauti za watu wakiongea, ikiwemo ya Tony, kisha gari likaondoka tena kwa mwendo wa kasi kidogo na baada ya mwendo mwingine mfupi na kona moja lilisimama na kuzimwa. Alisikia mlango wa gari lile ukifunguliwa na kufungwa. Aliendelea kutulia kwa kama dakika tano zaidi, kisha taratibu alilifungua lile buti na kuchungulia nje.
Mbele ya macho yake, kiasi cha kama mita hamsini hivi, aliona ukuta mrefu uliozungushiwa nyaya za misumari kwa juu. Eneo lote kutoka pale alipokuwa hadi pale kwenye ukuta, kulikuwa kuna majani yaliyokatwa vizuri na vichaka vidogo vya maua vilivyotapakaa hapa na pale katika eneo lile.
Alizungusha macho kulia kwake, ambako ndiko geti la kuingilia ndani ya eneo lile lilikuwapo na aliona njia safi ya lami iliyopinda na kupotelea kulia zaidi, hivyo kumfanya mtu aliyeko kule getini asiweze kuona yaliyokuwa yakitokea pale alipokuwapo.
Aligeuza macho yake kushoto. Kiasi cha hatua tano hivi kutoka pale lilipoegeshwa lile gari kulikuwa kuna gari jingine aina ya Land Rover Discovery. Mbele zaidi ndipo alipoliona lile jengo. Kwa pale alipokuwa, aliweza kuona sehemu ya juu tu ya lile jengo, ambayo ilimjulisha kuwa lilikuwa ni jengo la ghorofa moja. Kwa mbele zaidi kushoto mwisho wa ukuta ule, kulikuwa kuna taa kubwa iliyotoa mwanga mkali kutoka juu ya kona ya ukuta ule kuangaza jengo lile. Kulikuwa kuna taa nyingine kama ile kwenye kona nyingine ya ukuta ule iliyopo kulia kwake.
Kwa nini Tony aje kwenye jengo hili saa kama hizi?
Kwanza hili ni jengo gani…Ofisi…? Ofisi gani hii ya kutembelewa usiku?

Kiu ya kupata majibu ya maswali haya na kujua zaidi ilimfanya atoke kwa uficho wa hali ya juu nje ya buti lile na kubaki akiwa amepiga goti moja pale chini nyuma ya lile gari, akiwa makini kuushikilia ule mlango wa buti ili usijifunge wakati akiwa pale nje. Alitazama kulia kwake, kulikuwa shwari. Akageuka upande mwingine, ambako ndiko lilipokuwa lile jengo, na ndiko alipokuwa na uhakika kuwa Tony ameelekea. Kulionekena kimya.
Muda wote hu moyo wake ulikuwa ukimuenda mbio kuliko ilivyowahi kutokea. Aliliweka lile tambara baina ya makutano ya loki ya juu na ya chini ya buti lile ili kuendelea kulizuia lisijibane, kisha akajiviringisha chini kuelekea pale ilipokuwa ile Land Rover Discovery na kuchutama nyuma ya gari lile. Akiwa nyuma ya ile Discovery ambayo haikuwa mbali sana na kona ya jengo lile, alichungulia na kuweza kuona sehemu ya mbele ya jengo lile. Taa kubwa ilikuwa ikiwaka kutokea mbele ya jengo lile na aliweza kuona ngazi pana za saruji zilizoelekea kwenye lango kuu la jengo lile. Hakukuwa na mtu yeyote mbele ya jengo lile.
Alitupa macho yake ubavuni mwa lile jengo. Kulikuwa kuna kiza hafifu. Alikuwa anataka kugeuza tena uso wake ili aangalie tena mbele ya jengo lile ndipo ghafla alipoona, kupitia kwenye dirisha la moja ya vyumba vilivyokuwa katika sehemu ya chini ya jengo lile, taa ikiwashwa na mwanga wake kuonekana nje. Mbele kidogo kutoka pale alipokuwa, kulikuwa kuna kichaka kidogo cha maua. Alitaka akifikie kile kichaka ili kimkinge kabla ya kuiendea kona ya lile jengo.
Alitupa macho mbele ya jengo lile. Bado kulikuwa hakuna mtu, ingawa mbele zaidi kulikuwa kuna kiza kidogo hivyo hakuweza kujihakikishia iwapo hakukuwa na mtu katika kiza kile. Alikaa vile kwa muda huku akiwa ameyakaza macho yake kule kwenye kiza. Bado kulikuwa kimya. Moyo ulikuwa ukimpiga kwa kasi sana sasa, lakini alijitahidi kutoujali. Alipotaka kuchomoka tu kutoka nyuma ya ile Discovery kukiendea kile kichaka, alisita. Kitu kama kaa la moto kilielea hewani kwa muda halafu kikapotea. Moyo uliongeza kasi ya mapigo. Alikaza macho kuangalia kule kwenye kiza.
Hamna kitu.
Mawazo yake tu, au…?
Mara akauona tena ule moto. Safari hii ukitokea chini kuelekea juu, na ulipofika mahala fulani, ulisimama hewani kwa sekunde kadhaa na kutoa mng’ao zaidi, na ndipo alipoelewa. Ilikuwa ni sigara! Kulikuwa kuna mlinzi pale kizani aliyekuwa akivuta sigara! Jaka alishusha pumzi ndefu taratibu huku jasho likimvuja mwili mzima na miguu ikimtetemeka. Kwa kuelewa kuwa tayari maji alikuwa ameshayavulia nguo na kwamba ni sharti ayaoge, alilala kifudifudi kwenye majani mafupi na kwa upole mno alianza kutambaa kwa tumbo kukiendea kile kichaka kidogo cha maua huku macho yake akiwa ameyaelekeza katika eneo ambalo aliamini kuwa ndipo aliposimama yule mlinzi. Alikifikia kile kichaka bila ya kuonwa na yule mlinzi ambaye alionekana kufaidi sana sigara yake.
Akiwa nyuma ya kile kichaka, alitupa jicho kule alipokuwapo yule mlinzi, lakini hakumuona. Kona ya jengo lile sasa haikuwa mbali na pale alipochutama, hivyo kwa mwendo ule ule wa kutambalia tumbo aliiendea ile kona na alipoifikia alijibanza na kuchungulia mbele ya jengo lile, na moyo ukamlipuka.
Yule mlinzi alikuwa kiasi cha kama hatua kumi hivi kutoka kwenye kona ya jengo lile akitembea taratibu kuelekea pale alipokuwa amejibanza. Na muda huo yule mlinzi aliitupa chini na kuikanyaga ile sigara aliyokuwa akiivuta na kuishika vizuri bunduki aliyokuwa ameining’iniza begani. Jaka alijua kuwa sasa mchezo ulikuwa umekwisha. Alijilaza kimya pale chini akisubiri hatima yake. Yule askari alikuja na kusimama hatua chache kutoka pale alipokuwa amejilaza kifudifudi. Alijikuta akikodolea macho viatu vigumu vya yule askari mithili ya vile alivyokuwa akivaa wakati akilitumikia jeshi la kujenga taifa kwa mujibu wa sheria miaka michache nyuma. Alibaki akivikodolea macho vile viatu huku akitarajia teke zito la uso muda wowote ule. Hakuthubutu kuinua uso wake kumtazama yule mlinzi aliyesimama mbele yake. Alitulia tuli hali akiwa amebana pumzi na moyo wake ukipiga katika mipigo ambayo hajawahi kuisikia hata siku moja maishani mwake. Baada ya muda ambao kwake ulikuwa ni sawa na masaa mengi sana, miguu iliyovaa vile viatu ilianza kugeuka taratibu na hatimaye Jaka akajikuta akikodolea macho sehemu ya visigino ya viatu vile.
Yule mlinzi alikuwa hajamuona, na sasa alikuwa amemgeuzia mgongo!
Akiwa ameendelea kulala kifudifudi pale chini, wazo la kutisha lilimpitia: Je kama yule mlinzi angekuwa na mbwa? Wazo hilo lilimsisimua mwili na kuzidi kumkosesha amani. Mara yule mlinzi alianza kuondoka kutoka kwenye ile kona na kuelekea mbele ya jengo lile. Jaka aliinua kichwa chake na kuchungulia kule alipoelekea, na kumuona akiwa katika harakati za kuwasha sigara nyingine.
Chain Smoker.
Alishusha pumzi ndefu na taratibu alianza kutambaa kwa tumbo sambamba na ukuta wa jengo lile kuliendea lile dirisha lililotoa mwanga muda mchache uliopita huku akikumbuka somo la Camouflage, kujificha dhidi ya adui, walilofunzwa katika kipindi cha Mbinu za Medani (M.M.) wakati akilitumikia Jeshi la Kujenga Taifa. Sasa aliona matunda yake.
Alipolifikia lile dirisha alijiinua na kusimama kando ya dirisha lile huku akitazama kule alipotokea. Kulionekana kuwa shwari. Kwa uangalifu wa hali ya juu alichungulia ndani ya chumba kile kupitia kwenye lile dirisha la kioo ambapo aliweza kuona yote yaliyokuwa ndani ya chumba kile. Kilikuwa ni chumba kikubwa kilichoenezwa makochi makubwa ya thamani na meza moja ya kioo iliyokuwa katikati ya chumba kile. Ukuta uliokuwa moja kwa moja mbele ya macho yake ulikuwa una mlango wa kuingilia ndani ya chumba kile. Kwenye moja ya makochi yale ya thamani, Jaka alimuona Tony akiwa amekaa kimya hali amekunja nne. Kulikuwa kuna watu wengine wawili pamoja naye mle ndani, na Jaka aliwatazama kwa makini wale watu.
Mmoja, aliyekuwa amekaa kwenye kochi lililokuwa kulia ya lile alilokalia Tony, alikuwa mnene na mfupi. Uso wake wa duara ulikuwa umepambwa na tabasamu pana ingawa si Tony wala yule mtu mwingine mle ndani aliyeonekana kutilia maanani kuwepo kwa tabasamu lile usoni kwake. Jaka alijiuliza iwapo yule bwana alikuwa na kawaida ya kutasamu peke yake kila wakati huku akiendelea kumtazama kwa makini. Alikuwa ana nywele fupi mno kiasi kwamba alionekana kama aliyenyoa kipara. Alimkisia umri wake kuwa kati ya miaka arobaini na miwili au na mitano hivi. Hakuwa na ndevu hata kidogo kidevuni na hata juu ya mdomo wake hakukuwa na ndevu. Kitu pekee kilichoonesha kuwa alikuwa na umri mkubwa kidogo ni macho yake; Jaka alijikuta akiyaangalia yale macho kwa muda kidogo na mwili ulimsisimka. Nyama zilizokuwa chini ya macho yale zilikuwa zimelegea na hivyo kumfanya aonekane kama mwenye usingizi wakati wote. Lakini hicho sio kilichomsisimua mwili bali ni ukweli uliomjia kuwa alikuwa akiangalia macho ya mtu katili sana. Yule mtu alikuwa amevaa shati zuri na ghali lenye michirizi ya weupe na wekundu na shingoni alikuwa amefunga tai kubwa iliyorembwa kwa maua iliyomfanya apendeze sana.
Jaka alihamishia macho yake kwa yule mtu mwingine aliyekuwa mle ndani.
Huyu alikuwa tofauti sana na yule mtu wa kwanza. Yeye alikuwa mrefu na mwembamba. Uso wake mwembamba ulikuwa umejaa alama nyingi za ndui, na ingawa na yeye hakuwa na ndevu za kidevuni, alikuwa na ndevu nyembamba zilizotambaa chini ya pua yake, yaani mustachi. Macho ya Jaka yaliganda kwenye midomo ya yule jamaa kwa muda. Ilikuwa ni midomo myembamba sana, ambayo ilimkumbusha jambazi fulani alilopata kuliona kwenye filamu moja ya kizungu ya zamani sana, lililokuwa likiitwa Klaus Kinski. Kama jinsi ambavyo yule jamaa wa kwanza alivyokuwa na macho makatili, huyu wa pili alikuwa na midomo mikatili sana, kama kulikuwa kuna kitu kama hicho duniani.
Jaka alijikuta akimeza funda la mate huku akizidi kumchungulia yule jamaa aliyemletea taswira ya Klaus Kinski kichwani mwake.
Jamaa alikuwa amevaa kofia ya kepu na badala ya kukaa kwenye kochi kama wenzake, yeye alikuwa amesimama akiwa ameegemea ukuta huku akivuta sigara akitazama juu ya dari kama kwamba hakuwa na habari kabisa na wale wenzake waliokuwamo mle ndani. Jaka alimkisia kuwa na umri usiozidi miaka thelathini na saba.
Wote watatu waliokuwamo mle ndani walikuwa kimya kabisa. Jaka akarudisha tena macho yake kwa yule mtu mnene mwenye tabasamu pana. Bado uso wake ulikuwa ukitabasamu vile vile ila sasa alikuwa akichezea-chezea bastola kwa mikono yake.
Duh!
Macho yalimtoka Jaka. Dakika chache zilizopita yule jamaa alikuwa mikono mitupu, halafu ghafla bastola imetokea mikononi mwake. Hapo Jaka alijua kuwa pale hapakuwa pahala salama kuendelea kuwepo. Alimtupia macho Tony, na kushangaa kuona kuwa hakuonekana kujali wala kutishika kabisa na ile bastola iliyokuwa mikononi mwa yule…smiling face…mtu mnene mwenye tabasamu pana.
Inakuwaje Tony anakuwa na mahusiano na watu kama hawa?
Hapo alipata hamu ya kutaka kujua zaidi ni nini kilichokuwa kinaendelea ndani ya jengo lile. Huku moyo ukimdunda kwa nguvu, aligeuka na kutazama usalama wake katika eneo lile. Bado kulionekana kuwa shwari. Alichungulia tena dirishani ili kuendelea kuona yaliyokuwa yanajiri ndani ya chumba kile. Safari hii aliongezeka mtu mwingine ambaye hapo mwanzo hakuwemo mle ndani. Alikuwa amekaa kwenye kochi lililokuwa kushoto kwa lile alilokalia Tony na alikuwa akiwaelekeza mambo fulani Tony na wale watu wengine wawili ambao walikuwa wakimsikiliza kwa makini sana. Jambo moja la tofauti alilolibaini kwa yule mtu aliyeongezeka mle ndani ni nguo zake. Jamaa alikuwa amevaa pajama za kulalia na juu ya mapajama yale alikuwa amevaa jojo maalum la jioni la kitambaa cha Hariri kilichoonekana kuwa ni ghali sana.
Ah! Sasa ina maana huyu jamaa anaishi humu humu ndani ya jengo hili? Ina maana hili jengo sio tu ni kiwanda au ofisi, bali pia ni makazi ya huyu mtu?
Yule mtu mrefu mwenye sura ya ndui alikuwa amesimama nyuma ya kochi alilokalia yule muongeaji ambaye Jaka alipata hisia kuwa ndiye aliyekuwa na mamlaka kwenye jengo lile.
Ni nani huyu?
Alimtazama kwa makini zaidi yule mtu aliyevaa mapajama. Alikuwa ni mtu mwenye asili ambayo Jaka alihisi kuwa ni ya kihindi, nywele zake ndefu na nyeusi alizilaza nyuma na kuzifunga kwa kisogoni kama jinsi wafungavyo wasichana. Hakuweza kuiona vizuri sura ya yule mtu kwani alikuwa amegeuka kidogo kumtazama Tony, hivyo Jaka aliambulia kuona sehemu tu ya upande wa sura yake.
Aliendelea kuchungulia.
Baada ya maongezi yale ambayo Jaka hakuweza kuyasikia kutokea pale alipokuwa, yule mtu ambaye alionekana kuwa ndio bosi wao, aliinuka kutoka pale alipokuwa amekaa huku Tony na yule mtu mfupi mwenye tabasamu pana nao wakiinuka. Tony na yule mtu mrefu mwenye asili ya kihindi walipeana mikono. Hapo Jaka aliweza kuiona vizuri sura ya yule mtu, kwani aligeukia upande ule lilipokuwa dirisha ingawa macho yake yalikuwa yamemuelekea Tony.
Kitu cha kwanza kilichomgonga akilini ni macho ya yule mtu. Mboni za macho yale zilikuwa na rangi ambayo aliihisi kuwa ni ya buluu. Rangi ya macho yale ilifanya tofauti kubwa sana na rangi ya nywele nyeusi za yule mtu. Alikuwa mrefu na mwembamba na alikuwa amevaa suti ya buluu iliyomkaa vizuri sana mwilini mwake. Na alipokuwa akimtazama yule mtu, Jaka alipata wazo kuwa yule mtu hakuwa mhindi, ila hakuweza kujua kwa hakika alikuwa ni mtu wa asili gani. Na hata pale alipokuwa akimtazama yule jamaa, Jaka alijikuta akimkumbuka jambazi mwingine aliyepata kumuona kwenye filamu kadhaa za miaka ya karibuni aliyeenda kwa jina la Billy Drago. Wakati huo huo yule mtu mwenye macho ya buluu…Billy Drago…alitoa maelekezo fulani kwa yule jamaa mwenye sura ya ndui, ambaye alitoka nje ya chumba kile na kurudi muda mfupi baadaye akiwa ameshika mkoba uliofanana sana na ule aliokuja nao Tony, ambao muda wote ulikuwa umewekwa juu ya ile meza ya kioo iliyokuwa katikati ya chumba kile.
Mnh! Smiling Face…Klaus Kinski…Billy Drago…Tony unajihusisha na watu wabaya sana wewe…kwa nini?
Na hata pale wazo hilo lilipokuwa linapita kichwani mwake, Jaka alimuona yule mtu mwenye macho ya buluu ambaye yeye alishampachika jina la “Billy Drago” kisirisiri, akitoa ishara ya kichwa na yule mtu mfupi mwenye tabasamu pana aliufungua ule mkoba aliokuja nao Tony uliokuwa pale juu ya meza, na kumsogezea. Macho ya buluu aliangalia ndani ya mkoba ule kwa muda, na kumuashiria mzee wa kutabasamu aufunge, naye akatekeleza. Kisha akamuashiria yule mwenye sura ya ndui afungue ule mkoba mwingine aliokuja nao naye akafanya hivyo na Tony akasogea na kutazama ndani yake, kisha akaufunga. Tony na macho ya buluu walitazamana kisha Tony alitikisa kichwa kwa kuafiki.
Walipeana tena mikono kisha wakabadilishana ile mikoba iliyofanana, Tony akiuchukua ule ulioletwa na sura ya ndui wakati macho ya buluu akichukua ule aliokuja nao Tony huku wakitoka nje ya chumba kile wakiwaacha sura ya ndui na tabasamu pana peke yao ndani ya chumba kile.
Jaka alishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kimefanyika mle ndani, ila alijua kuwa lililofanyika halikuwa jema hata kidogo…au ndipo Tony anapofanyia biashara ya madawa ya kulevya…?
Taratibu aliinama chini ya dirisha lile tayari kuanza mwendo wake wa kutambaa kwa tumbo kurudi kule alipotoka, kwani alijua kuwa sasa Tony alikuwa anaondoka na hivyo ilibidi awahi kwenye buti la gari ili asiachwe, vinginevyo angebaki kwenye hekaheka kubwa.
Na hapo ndipo kwa mara ya kwanza alipoitilia maanani ile sauti.

Muda wote alikuwa kisikia sauti ya muungurumo hafifu ikitokea kwa chini ya pale alipokuwa amesimama akichungulia mle ndani, lakini akili yake ilitilia maanani zaidi yale yaliyokuwa yakitokea mle ndani kuliko muungurumo ule. Kutoka pale alipokuwa amepiga goti chini ya lile dirisha, aliweza kuisikia vizuri zaidi ile sauti. Ilikuwa ni sawa na mvumo wa kipoza hewa, lakini kwa nini utokee chini? Aliinama chini zaidi na kutazama kule alipohisi kuwa ule mvumo ulikuwa ukitokea. Kiasi cha kama hatua nne hivi kutoka pale alipokuwa, kulikuwa kuna mashine ya kupozea hewa iliyojengewa chini kabisa ya ukuta wa jengo lile na kufichwa na kichaka cha maua.
Kwa nini?
Aliitambalia ile mashine na kulalia tumbo kando yake ili apate kuichunguza vizuri huku moyo ukimwenda aksi akijua kuwa kila alivyozidi kuchelewa, ndivyo alivyojizidishia uwezekano wa kuachwa na Tony ndani ya uzio wa jengo lile.
Aliigusa mashine ile kwa mkono wake na kugundua kuwa ilikuwa ikifanya kazi na hivyo kujihakikishia kuwa ndiyo iliyokuwa ikito mvumo ule. Na hapo hapo, kando ya mashine ile aligundua kidirisha kidogo kilichokuwa chini kabisa ya ukuta wa jengo lile. Alizidi kushangaa ni vipi inakuwa namna ile. Akiwa amelalia tumbo pale chini, alijaribu kuchungulia kwenye kile kidirisha, na hapo ndipo alipoelewa.
Ingawa lile jengo lilionekana kuwa ni la ghorofa moja, lakini hasa lilikuwa ni la ghorofa mbili; kwani chini ya ile ghorofa ya chini, kulikuwa kuna nyumba vingine ambavyo bila shaka vilikuwa vya siri…vyumba vya chini ya ardhi.
Kutoka pale alipokuwa akichungulia, aliweza kuona chumba kingine kikubwa kuliko kile alichokuwa akikichungulia hapo awali, ambacho kilikuwa chini ya kile walichokuwamo akina Tony dakika chache zilizopita.
Macho yalimtoka kwa yale aliyoyaona ndani ya kile chumba cha chini.
Watu wapatao kumi walikuwa wamesimama nyuma ya meza mbili kubwa na ndefu zilizokuwamo mle ndani, moja kila upande wa chumba kile. Mbele ya watu wale, watano nyuma ya kila moja ya meza zile, kulikuwa kuna vikopo vingi vya ukubwa wa wastani. Wale watu walikuwa wanafanya kazi haraka haraka, na Jaka alikaza macho ili aone ni nini walichokuwa wanafanya. Kwa pale alipokuwa, alikuwa akiwaona kutokea juu kwa umbali wa kama futi kumi na tatu hivi.
Kutoka pale alipokuwapo, aliweza kumuona mtu wa kwanza katika meza iliyokuwa moja kwa moja usawa wa macho yake akiwa amepanga vikopo vingi kando yake na vifurushi vingi vya nailoni vilivyokuwa na unga mweupe ndani yake. Vile vifurushi vilikuwa virefu na vyembamba. Na hata pale alipokuwa akimtazama yule mtu wa kwanza kwenye ile meza, alimuona akichukua kifurushi kimoja na kukitumbukiza ndani ya moja kati ya vile vikopo na kumsukumia mtu aliyesimama kando yake nyuma ya meza ile. Kando ya yule mtu wa pili kulikuwa kuna rundo la vitu kama vifuniko hivi, ambavyo Jaka hakuweza kujua kama vilikuwa cha plastiki au vya bati. Alikipokea kile kikopo kisha akaokota moja kati ya vile vifuniko vingi vilivyokuwa kando yake na kukitumbukiza ndani kile kikopo kilichotumbukizwa kifurushi cha unga mweupe. Badala ya kufunika, kile kifuniko kilitumbukia ndani ya kile kikopo na kulala juu ya kile kifurushi cha unga mweupe.
Baada ya kufanya hivyo, yule mtu wa pili alikisukuma kile kikopo kwa mtu wa tatu aliyekuwa kulia kwake, ambaye kando yake kulikuwa kuna beseni safi sana la chuma. Kwa kutumia kitu kama kijiko kikubwa, mtu wa tatu alichota vitu fulani vilvyofanana na nyama ya kusaga kutoka kwenye lile beseni na kuvitumbukiza kwa uangalifu sana ndani ya kile kikopo, juu ya ule mfuniko uliozamishwa na mtu wa pili.
Baada ya kufanya hivyo, yule mtu naye alikisukuma kile kikopo kwa mtu wa nne aliyekuwa kulia kwake na wakati huo huo akipokea kikopo kingine kutoka kwa yule mtu wa pili.
Jaka likifuatilia kile kikopo kwa macho hadi kwa yule mtu wa nne. Huyu alikuwa na kitu kama mashine fulani ambayo baada ya kupokea kile kikopo, alikiweka sehemu fulani katika mashine ile na baada ya kubonyeza kitu fulani, kikopo kilivutwa ndani na kubonyezwa na kitu kama nyundo maalum kutoka sehemu ya juu ya mashine ile, na kilipotolewa upande wa pili wa mashine ile, kile kikopo kilikuwa tayari kimeshafungwa kiasi kwamba kufunguliwa kwake ilibidi ile sehemu ya juu ikatwe kwa kifaa maalum cha kufungulia makopo. Kama jinsi ambavyo inavyokuwa unapotaka kufungua nyanya ya kopo.
Haya mapya!
Mtu wa tano, baada ya kupokea kile kikopo kutoka upande wa pili wa ile mashine ya mtu wa nne, alibandika kitu kama alama, au lebo, fulani ya karatasi kwenye kile kikopo na kukitupia kwenye boksi kubwa lililokuwa pembeni yake chini ya meza ile.
Ilichukua chini ya dakika mbili kwa kile kikopo kimoja kukamilisha mzunguko ule, na Jaka aliyashuhudia mambo haya kwa mshangao mkubwa kabisa.
Kitu kingine kilichomshangaza ni kwamba watu wote wale waliokuwa wakifanya shughuli ile hawakuwa waswahili. Kwa jinsi alivyowaona, walikuwa ni watu wenye asili fulani ya mchanganyiko wa kihindi na kizungu, sawa na yule mtu mwenye macho ya buluu aliyekuwa na Tony katika chumba cha juu.
Pia ndani ya chumba kile, kulikuwa kuna watu wengine wa asili ile ile wapatao sita hivi ambao walikuwa wamesimama kimya kwenye kuta za chumba kile wakiangalia jinsi wale wenzao walivyokuwa wakifanya ile kazi. Mikononi mwao walikuwa wameshika bunduki ambazo mara moja Jaka alizijua kuwa zilikuwa ni silaha hatari sana zilizotengenezwa Israel ziitwazo Uzzi. Polepole Jaka alijivuta nyuma na kuanza kutambaa kwa woga wa hali ya juu kuelekea kule lilipoegeshwa gari la Tony huku akihofia kuwa huenda Tony akawa ameshaondoka na kumuacha mle ndani. Alichungulia kwenye kona ya jengo lile na moyo wake ulifarijika alipomuona Tony akiwa amesimama mbele ya jengo lile akiongea na sura ya ndui hali akiwa ameushikilia ule mkoba aliobadilishana na macho ya buluu muda mchache uliopita.
Taratibu mno, huku moyo ukimwenda mbio kwa hofu ya kuonwa na maadui wale, Jaka alitambaa kwa tumbo hadi nyuma ya ile Land Rover Discovery. Hapo alipiga goti na kuchungulia tena kule walipokuwa akina Tony.
Hawakuwepo.
Alichungulia kutokea upande wa pili nyuma ya ile Discovery.
Tony alikuwa ameshaingia kwenye gari lake!
Upesi sana alijiviringisha ardhini kutoka nyuma ya ile Discovery kuelekea nyuma ya gari la Tony. Akiwa nyuma ya ile Toyota Chaser ya Tony alijiinua na kuanza kupapasa mlango wa buti la lile gari.
Wakati huo huo Tony akapiga stati.
Jaka aliuinua taratibu mlango wa lile buti na kutanguliza mkono na mguu mmoja ndani yake.
Gari Lilianza kurudi nyuma taratibu.
Jaka akatumbukia kabisa ndani ya buti la gari.
Gari likageuza.
Jaka akaushusha na kuufunga taratibu mlango wa lile buti, akihakikisha lile tambara linaiziba ile sehemu ya loki ya lile buti.
Gari likaondoka kwa kasi kuelekea getini.
Jaka akajilaza kimya ndani ya buti, akilishikilia kwa ndani ili lisijibamize wakati gari likitembea. Walisimama kidogo getini kusubiri geti lifunguliwe kabla ya kutoka nje ya uzio wa jengo lile na kuanza safari nyingine. Mara hiyo hiyo Jaka alilifungua kidogo buti la gari na kuchungulia kule walipokuwa wakitokea, na ndipo alipoweza kusoma maandishi makubwa yaliyoandikwa kwenye uso wa lile geti kutokana na mwanga uliotoka kwenye mataa makubwa yaliyokuwa yakiangaza eneo lile.
ST. STANZA CANNED FISH (E.A.) CO. LTD
Butwaa lilimtawala huku akiyashuhudia yale maandishi yakizidi kuwa madogo kutokana na gari kuzidi kuongeza umbali baina yake na geti lile. Hatimaye aliushusha taratibu mlango wa lile buti na kujilaza kimya mle ndani, akihisi kuwa akili imemfa ganzi.

___________________

Ilikuwa ni kiasi cha saa tano na nusu za usiku wakati alipofungua mlango wa chumba chao pale chuoni. Wasiwasi wa Raymod Mloo uliotokana na kuchelewa kwake kurudi kutoka maktaba ulizidi maradufu pale alipoiona hali aliyokuja nayo rafiki yake. Nguo zake zilikuwa zimechafuka kwa vumbi, michanga na udongo. Nywele zake zilikuwa zimetapakaa majani na uso wake ulikuwa umechafuka kutokana na udongo uliochanganyika na jasho na grisi kutoka kule kwenye buti la gari .
“E bwana ee! Jaka! Vipi tena…? Umekuwaje?” Ray aliuliza kwa wahka huku akiinuka kutoka kitandani na kwenda kumsimamia mbele yake huku akimtazama kwa mshangao na woga. Jaka aliweka vitabu vyake mezani na kuanza kuvua nguo zake taratibu. Raymond alibaki akimtazma kwa mshangao mkubwa.
“Hamna kitu…usiwe na wasiwasi…” Alimjibu rafiki yake huku akiketi sakafuni akiwa na nguo yake ya ndani tu. Raymond alimtazama kama vile Jaka alikuwa amerukwa na akili.
“Hamna kitu?” Aliuliza huku akizikodolea macho nguo za Jaka zilizorundikwa sakafuni, na kumtazama jinsi yeye mwenyewe alivyochafuka. Jaka alimtazama bila ya kufanya bidii yoyote ya kuielezea hali ile.
Baada ya kufika pale chuoni, Tony aliegesha gari lake pale pale alipokuwa ameliegesha hapo awali, akafunga milango na kuondoka na ule mkoba aliotoka nao kule St. Stanza. Jaka aliendelea kujilaza mle ndani ya buti kwa muda, kisha akatoka taratibu na kulibana itakiwavyo lile buti. Alivikuta vitabu vyake pale pale alipovificha kabla ya kudandia lile, hivyo alivichukua na kurudi chumbani kwake huku akiwa na mawazo tele kuhusu yale mambo aliyoyashuhudia usiku ule.
Haikuwa mpaka alipomaliza kuoga ndipo alipomuelezea Raymond juu ya mambo yote yaliyotokea hata akarudi pale chumbani kwao akiwa katika ile hali aliyorudi nayo. Macho yalimtoka pima Raymond na mdomo ukabaki umemuanguka kutokana na habari ile, na kwa muda mrefu alibaki akiwa ameduwaa asijue la kusema.
“Rafiki yangu jambo ulilogundua ni kubwa na la hatari sana…” Hatimaye alisema, na Jaka alibaki kimya huku uso wake ukiwa ameukunjamana kwa mawazo.
“…hili ni swal la usalama wa taifa Jaka, na polisi lazima wajulishwe…” Raymond aliendelea kwa wasiwasi. Kimya kirefu kilitanda mle ndani, kila mmoja akiwa na mawazo yake kuhusiana na swala lile.
“Itabidi tuwasiliane na Sajenti Vata…” Hatimaye Jaka alisema, na Raymond alionekana kusita kidogo.
“Aah, inawezekana polisi wenyewe wakawa wajua juu ya swala hilo ila wanamezea tu…si unajua bwana?” Hatimaye alimwambia kwa kukata tamaa, na Jaka alibaki akimtazama bila ya kusema kitu. Alijua ni jinsi gani Raymond alivyokatishwa tamaa na kitendo cha Sajenti Vata kutomtia mbaroni Tony kama alivyoahidi pamoja na kuelezwa kila kitu kuhusu uovu wa kijana yule, lakini hakuona njia nyingine.
“Inawezekana Ray, lakini ni uwezekano ni mdogo sana…vinginevyo unadhani tutafanyaje juu ya hili?”
“Aaah…tuachane nao tu Jaka. Madhali hawajatudhuru sisi, basi tukae kimya tu. At least tutaendelea kuishi…tunaweza kujifanya wazalendo hapa halafu tukaishia kaburini na uzalendo wetu…”
“Unataka kuniambia kuwa tusiliripoti polisi swala hili Ray?” Jaka alimuuliza taratibu. Alikuwa amechoka sana.
“Haswa! Unaweza kusema kwa nia nzuri tu ya kizalendo, lakini ukajikuta unapatwa na zahma kubwa kabisa Jaka…sasa hivi nchi hii haieleweki. Huwezi kujua mzuri ni yupi, mbaya ni yupi…hata hao polisi…no, hususan hao polisi! Hebu ona jinsi walivyolichukulia swala la Tony! Kuna mtu amepoteza uhai Jaka…Rose sasa ni marehemu na Tony ndio huyo anapita akibadilishana mikoba na watu wenye macho ya buluu…! Sasa ni kipi cha busara zaidi ya kukaa kimya na kufuatilia mambo yako tu?” Ray alimjibu Jaka huku akiwa amemtolea macho kuonesha msisitizo.
“Kwa wewe ni sawa kusema hivyo Ray, lakini kwa mimi niliyeona jinsi yale madawa ya kulevya…kwani ni wazi kuwa yale ni madawa ya kulevya…yalivyokuwa yakipakiwa kwenye vile vikopo, siwezi kukubali kunyamaza tu, hasa ukizingatia kuwa kunyamaza kwangu kutamfanya mtu mbaya kama Tony aendelee kutembea akiwa huru baada ya yote aliyomfanyia Rose…” Jaka alimjibu rafiki yake, na kuunganisha na mwayo mrefu wa uchovu.
“Kwa hilo la pili hata mimi nakubaliana na wewe Jaka, lakini pia lazima tufikirie na usalama wa maisha yetu bwana…unajuaje kuwa askari utakayemueleza habari hiyo atakuwa kweli katika upande wa sheria na hanufaiki na biashara hiyo?”
Jaka alikaa kimya kwa muda akiyatafakari maneno yale ambayo kwa kweli yalileta maana sana kwake.
“ Basi angalau tujaribu kuwasiliana na Sajenti Vata ili tujue amefikia wapi juu ya swala la Tony na kifo cha Rose…labda hapo tutapata picha iwapo tutaweza kumwamini na habari hii…au la.” Hatimaye alisema.
“Hakuna bwana! Hata huyo Sajenti Vata ndio wale wale tu! Mi’ simuamini asilani! Bado naona tunahitaji kunyamaza kimya kwanza…”
“Mpaka lini, Ray?”

“Mpaka hapo tutakapoona inafaa kusema…au kutosema kabisa!”
Jaka alimtaza mwenzake kwa muda, kisha akamuuliza, “Ulishawahi kusikia kitu kiitwacho accessory to crime?”
Raymond alibakli akimtazama tu, na Jaka aliendelea, “Accessory to crime maana yake ni kwamba unashitakiwa kwa kusaidia, au kutumika katika kutendeka kosa lolote la jinai. Yaani hata kama ulijua juu ya kosa hilo halafu wewe ukaamua kukaa kimya kama ambavyo wewe unataka tufanye hivi sasa, unahesabika kuwa umesaidia kwa kosa hilo kutendeka, na adhabu yake huwa ni sawa na ile ya yule aliyetenda hilo kosa…”
“Aaa sasa hiyo sheria ya wapi? We’ si umeona tu? Kwanza nani atajua kuw
sasa wewe na mimi tukikaa kimya juu ya jambo hili moja kwa moja tunakuwa ni accessories to a crime…yaani kwa kugha nyepesi, tunahesabika ni washiriki katika kosa lile… tunatakiwa tuadhibiwe sawa na wale waliotenda kosa lenyewe!”
“Sasa hiyo ndio sheria ya wapi jamani! We’ si umeona tu na hujatenda? Na watu watajuaje kuwa umeona usiposema? Hapo ni kupiga kimya tu!” Ray alihoji na kutia hoja.
Jaka alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Sio mimi tena Ray…na wewe pia! Mimi hapa nilipo tayari ni mshirika wa kile kilichotokea usiku huu kule St. Stanza…mpaka pale nitakapokiripoti. Na kwa mimi kukusimulia wewe juu ya yale niliyoyaona, na wewe tayari umekuwa mshirika Raymond, samahani sana!”
“Duh!”
“Oooh yes, Duh kweli kweli tena!”
Kimya kilichukua nafasi wakati wale marafiki wawili wakitazamana, uzito wa swala lililokuwa mikononi mwao ukijizatiti akilini mwa kila mmoja wao.
“Sawa Jaka…tuwasiliane na Sajenti Vata…!” Hatimaye Raymond alikubali.
Jaka aliinuka na kuchukua lile shati alilokuja nalo likiwa limechafuka kutoka kule alipodandia gari la Tony. Alitia mkono wake kwenye mfuko wa shati lile ambamo aliweka kijitabu chake kidogo cha anuani kabla ya kutumbukia kwenye lile buti la gari la Tony. Ndani ya kijitabu kile alikuwa ameiweka ile kadi ndogo ya Sajenti Vata iliyokuwa ina namba zake za simu.
Kile kijitabu hakikuwemo.
Mwili ulimfa ganzi.
Alikung’uta nguo zote alizokuwa amezivaa usiku ule akijaribu kukitafuta kile kijitabu, bila mafanikio. Alipigwa na butwaa. Raymond aliona jinsi alivyopigwa butwaa, na akamuuliza kulikoni na Jaka akamueleza. Walitazamana kwa muda, kisha Raymond alimuuliza, “Kuna kitu chochote kinachoweza kukuhusisha wewe na kitabu kile?”
“Kuna jina langu, picha yangu na anuani za watu wengi ninaojuana nao…”
“Oh-hoooo!” Raymond alilaani huku akikunja uso.
Jaka alijua kuwa kile kijitabu kitakuwa aidha kimeanguka ndani ya ule uwanja wa lile jengo la St. Stanza wakati akitambaa kwa tumbo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, au kitakuwa kimeanguka ndani ya buti la gari la Tony. Vyovyote iwavyo, watakaokiokota kile kijitabu lazima watamtafuta.
Na wakimpata itakuwa balaa.
Walitoka usiku ule ule kwenda pale lilipoegeshwa gari la Tony ili waangalie iwapo atakuwa amekidondosha kile kijitabu ndani ya buti la lile gari, wakiazimia kufanya kila liwezekanalo ili kulifungua tena lile buti.
Lile gari halikuwepo.

____________________

Usiku ule Jaka hakulala kabisa. Alijiuliza sana ni wapi atakuwa amekiangushia kile kijitabu chake cha anuani. Hofu kubwa ilimpata alipofikiria ni kipi kitafuata iwapo atakuwa amekiangusha ndani ya ule wigo wa ile kampuni hatari, na wahusika wakakiokota. Si lazima watamtafuta? Na wakimpata je? Mawazo yake yakahamia kwenye yale mambo aliyoyaona kule St. Stanza usiku ule. Kwa kuyaona yale mambo, tayari alikuwa ameshajiingiza kwenye balaa kubwa, na ingawa hapo awali aliamini kuwa akijua siri ya nyenendo za Tony na wenzake angeweza kuzitumia siri hizo kuwabana na kujihakikishia usalama wake na wa mpenzi wake Moze, sasa aliona kuwa lile swala lilikuwa linaelekea pabaya zaidi. Wale watu aliowaona wakiwa na Tony usiku ule walikuwa ni watu hatari sana. Mtu yeyote anayejishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa namna ile lazima atakuwa ni mtu hatari sana. Sasa halikuwa swala la yeye na Tony na wale wenzake wa pale chuoni tu, bali liliwajumuisha pia na wale akina “Klaus Kinski”, watu ambao hakuwa na shaka kabisa kuwa wasingesita kumuua iwapo wangebaini kwamba alikuwa amegundua juu ya biashara yao ile haramu.
Sasa ilimjia wazi kuwa kwa kujifanya kushughulika na biashara ya kusambaza na kusafirisha samaki wa kusaga, ndani na nje ya nchi, ile kampuni kubwa kabisa ya St. Stanza Canned Food ilikuwa ikiingiza na kusambaza kiasi kikubwa cha madawa ya kulevya ndani ya vile vikopo ambavyo mtu yeyote angejua ni samaki tu wa kwenye makopo waliokuwa wakisafirishwa nchini na nchi nyingine mbali mbali za Afrika na hata nje ya Afrika, kutokea Tanzania…na lile jengo aliloenda Tony usiku ule ndio kitovu cha biashara hiyo.
Hili swala lilikuwa ni kubwa sana kiasi ilimuwia vigumu sana Jaka kuamini kuwa wale watu waliweza kuendesha shughuli ile bila ya polisi kujua…na alijikuta akikubaliana na mwazo ya Raymond kwa kaisi kikubwa sana.
Halafu wale watu waliokuwa wakifanya ile kazi ya kupakia yale madawa kwenye vile vikopo vya samaki wa kusaga…wote hawakuwa watanzania…kwa nini?
Alimfikiria Tony. Hakuweza kuamini kuwa Tony alikuwa anajishughulisha na biashara kama ile, lakini ndio amemuona kwa macho yake.
Kwa shida gani, Tony?
Sasa alielewa ni kwa nini Tony na wenzake hawakutaka kabisa azijue nyendo zao kiasi cha kukurupuka na kumtishia juu ya hilo kabla hata hajazijua nyendo hizo. Sasa alikuwa amezijua rasmi hizo “nyendo” zao, na pamopja na matarajio yake ya awali, bado hakujisikia salama kabisa kuzijua…kwani sasa alijua kwa yakini kabisa kwamba wakijua tu kuwa amewabaini, watamuua.

____________________

Asubuhi ya siku iliyofuata Tony aliamka akiwa na wazo la kwenda mjini kupeleka “mzigo” aliochukua kwa Raul kwa mteja mwingine maalum kama jinsi alivyoelekezwa usiku uliopita. Alikuwa ana kipindi saa tatu asubuhi ile, hivyo alijua angeweza kupeleka mzigo ule na kuwahi kurudi kabla kipindi hakijaanza.
Gari lake lilikuwa limejaa umande wa asubuhi, hivyo alifyatua kifungulio cha buti na kuzunguka nyuma ya gari lile na kuchukua tambara la kufutia gari ambalo huliweka kule kwenye buti. Alipoliinua tambara lile, alishangaa kuona kijitabu kidogo kilichokuwa kimejiviringa kwenye lile tambara kikidondoka mle ndani ya buti.
Alikiokota kile kijitabu na kukitazama kwa karibu zaidi huku kengele za hatari zikianza kugonga kichwani mwake. Yeye hakuwa na kijitabu cha aina ile na alishangaa kilifikaje ndani ya buti la gari yake. Alikitazama kwa makini huku akifunua kurasa za kitabu kile.
Kwanza alianza kuona picha, halafu jina la mmiliki wa kijitabu kile.
Sura yake ilijifinyanga kwa ghadhabu…

____________________

Bahati nzuri kwa Jaka, Raymond alizinakili zile namba za simu walizoachiwa na Sajenti Vata kwenye simu yake. Walikubaliana kuwa Jaka ampigie Sajenti Vata na kupanga sehemu ya kuonana naye ili waweze kumuuliza juu ya hatima ya swala la Tony kuhusika na kifo cha Rose, halafu waone iwapo wanaweza kumuamini na ile taarifa waliyoipata usiku uliopita kuhusiana na ile kampuni ya St. Stanza.
Hivyo, wakati Tony anashangaa jinsi kitabu cha Jaka kilivyofika ndani ya buti la gari lake, Jaka alikuwa akiisikiliza simu ya Sajenti Vata ikiita huku moyo ukimuenda mbio. Baada ya muda ambao yeye aliuona ni mrefu sana, ile simu ilipokelewa.
“Polisi Oysterbay…kitengo cha madawa ya kulevya, tukusaidie?” Sauti nzito ilimjibu. Haikuwa sauti ya Sajenti Vata.
“Eenh…naomba kuongea na Sajenti John Vata, tafadhali. Nilidhani hii namba yake? Au nimekosea nam…” Aliongea kuiambia ile sauti iliyopokea simu.
“Hii ni simu ya ofisi, iliyokabidhiwa kwa Sajenti Vata kwa ajili ya matumizi ya kikazi…sasa ninayo mimi…!” Ile sauti ilimkatisha, na Jaka akahamanika, Raymond akawa anamtupia macho ya kuuliza, uso wake ukiwa umejaa mashaka.
“Oh, sasa…naweza kumpataje?” Jaka aliuliza kwa wasiwasi huku akimuashiria Raymond atulie. Kimya kifupi kilitawala kutoka upande wa pili wa simu ile na Jaka alikuwa anataka kurudia tena ombi lake wakati ile sauti ilipomuuliza, “Ni nani unayeongea…na unaongea kutoka wapi?”
Jaka alikunja uso.
“Nahitaji kuongea na Sajenti Vata tafadhali…ni muhimu sana…!”
Kimya kilitanda tena kutoka upande wa pili wa simu ile. Jaka akazidi kupata wasiwasi, kisha yule mtu wa upande wa pili akampa jibu ambalo hakulitarajia.
“Sajenti Vata hayupo tena katika idara hii. Amehamishiwa kwenye kitengo kingine, hivyo kama kuna habari yoyote muhimu ya kikazi, unaweza kunieleza mimi….”
Jaka akakata simu, akaizima.
“Imekuwaje?” Raymond alimuuliza kwa wahka mkubwa.
Jaka akamueleza.
“Heeeeeh!” Raymond aligwaya.
Wote wawili walikubaliana kuwa kuhamishwa kwa John Vata kutoka kwenye kile kitengo, kama ni kweli alikuwa amehamishwa, kutakuwa kuna uhusiano mkubwa sana na uchunguzi aliokuwa akiuendesha dhidi ya Tony kuhusiana na kifo cha Rose na ule unga wa kulevya uliokutwa chumbani kwa Rose.
“Rafiki yangu sasa tuache ushujaa. Hii ngoma imeshakuwa nzito. Kuna watu wanahusika na swala hili ambao inaonekana wazi kuwa wako tayari kufanya lolote ili wasigundulike…tukae chonjo kabisa sasa mshikaji wangu, kwani hii hali sasa imeshakuwa ya hatari, tena ya hatari kubwa!” Raymond alimwambia Jaka kwa msisitizo.
Jaka alimtazama Raymond kwa muda bila ya kusema neno huku akijishughulisha kuichomoa kadi ya simu kutoka kwenye ile simu yake aliyoitumia kumpigia Vata na kuishia kuongea na mtumwingine. Raymond aliona labda rafiki yake hajamuelewa.
“Umenisikia Jaka?” Aliuliza.
“Ni kweli unayosema rafiki yangu…” Hatimaye Jaka alimjibu kwa upole, kisha akaendelea; “…lakini kwa bahati mbaya tumeshachelewa…”
Hakukosea.
Alitoka na kwenda kuitumbukisa chooni ile laini ya simu aliyoichomoa kutoka kwenye simu yake, kisha akarudi pale chumbani. Alikubaliana na Raymond kuwa wasimwambie mtu yeyote juu ya yale mambo waliyoyagundua kuhusu ile kampuni ya St. Stanza Canned Fish.
Jioni ile alikutana na Moze, na waliongea mambo mengi tofauti na yale kwani Jaka hakutaka kabisa Moze ajue juu ya St. Stanza kwa kutotaka kumtia wasiwasi. Aidha, alijua kuwa kadiri Moze asipojua lolote kuhusu St. Stanza, ndivyo alivyokuwa salama zaidi.
Jaka alifanikiwa kumshawishi Moze watoke na kwenda kujiliwaza mjini jioni ile, hivyo walitoka na kwenda kula Ice Cream wakimuacha Raymond pale chumbani. Baada ya kula Ice Cream au ramba-ramba kama ilivyozoeleka, waliamua kufanya matembezi zaidi mjini, wakifurahia kuwa pamoja. Hatimaye walifika sehemu maarufu kwa kuku wa kuchoma ambayo Moze aliipendasana. Waliagiza “kuku-choma” kwa vinywaji na kuanza kula kwa utulivu huku wakichombezana kwa maneno ya huba haya na yale. Moze alionekana kufurahia sana hali ile na Jaka aliona amefanya jambo la maana kutomueleza juu ya mambo aliyoyaona kule St. Stanza usiku uliopita.
Alimtazama mpenziwe kwa huba isiyo kificho jinsi alivyokuwa akifurahia kutafuna kuku huku akijirusha-rusha kufuatisha muziki wa kizazi kipya uliokuwa ukirindima kutoka kwenye maspika yaliyotawanywa eneo lile, na moyo wake ukayeyuka kwa faraja. Akajikuta akisahau kabisa matatizo aliyokuwa nayo kwa muda ule.
“Unawaza nini?” Moze alimuuliza huku akitabasamu.
Jaka aliendelea kumtazama kwa muda, kisha akamjibu kuwa alikuwa anastaajabia urembo wake na jinsi gani anavyojiona mwenye bahati kwa kuwa mpenzi wake.
Moze alifurahishwa sana na jibu lile. Akacheka kwa sauti na kumtupia busu la mbali mbali. Ikawa zamu ya Jaka kucheka kwa sauti, akifurahia hali ile.
Wapenzi walikuwa wanafurahia mapenzi yao.
“Kesho ni Birthday yangu Brown, unakumbuka?”Moze alimwambia na kumuuliza ghafla, akimaanisha kuwa siku iliyofuata ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa.
Jaka alisahau kabisa juu ya hilo, bila shaka kutokana na matukio yaliyomzonga ndani ya siku za pale karibuni.
“Ha! Ee bwana eee! Unajua nilishasahau kabisa mpenzi? Dah! Ahsante sana kwa kunikumbusha al-habiibi…!” Alimaka kwa hamaniko huku midomo yake ikifanya tabasamu dogo. Moze alimuigiza huku akibana pua kwa vidole vyake, kisha akaachia pua yake na kumwambia kwa utani huku akiwa amefanya sura ya kununa.
“Yaani kweli unaweza kusahau siku ya kuzaliwa ya al-habiibi wako? Ama kweli sasa nimechokwa Moze miye…!”
Wote waliangua kicheko kikubwa. Ulikuwani usiku wa furaha. Jaka alimtazama kwa muda mpenzi wake baada ya kumaliza kicheko.
“Toa utetezi wako hapa, sio unajichekesha-chekesha hapa ukadhani ndio imetoka hiyo…haijatoka! Bado una kesi ya kujibu!” Moze alimwambia huku akitabasamu, na Jaka akatabasamu.
“Ah, basi usikonde my sweetie…nitakutayarishia zawadi ambayo hutaisahau katika uhai wako wote hapa duniani, mpenzi.” Hatimaye alimwambia. Moze alimtazama mpenziwe huku akitabasamu.
“Mmnnh…zawadi gani hiyo dear nitakayoikumbuka maisha yote?”
“Kwa sasa ni siri yangu…lakini ikifika hiyo kesho haitakuwa siri tena, kwani zawadi itakuwa ni yako for the rest of your long, loving life!” Jaka alimjibu kwa majivuno makubwa na wote walicheka.
“Lakini siwezi nikaijua japo kidogo tu kabla sijaiona?” Moze alizidi kuchombeza.
“Kesho my dear…kesho. Kesho ikifika utaijua ni zawadi gani niliyokuandalia….au utaisikia ni zawadi gani, kwa sasa tutafune kuku tu hapa.” Jaka alimjibu huku akiinua kipaja cha kuku na kumpelekea kinywani mpenziwe kwa mbwembwe. Moze alimtazama kwa uso wa kuuliza huku akigoma kumega kile kipaja cha kuku alichokuwa anapewa, na Jaka alitikisa kichwa kusisitiza msimamo wake huku akitabasamu. Moze akakubali kushindwa. Akamega kidofu kutoka kwenye kile kipaja alicholishwa mpenziwe huku akitabasamu.
“Okay surprise boy…kesho sio mbali, au vipi?” Alisema huku akitafuna kuku na akipeleka bilauri ya juisi kinywani

“Smart girl!” Jaka alimjibu huku akiachia tabasamu pana.
Ilikuwa ni saa nne za usiku wakati Jaka alipoingia chumbani kwake pale chuoni na kumkuta Raymond akiwa na uso uliojaa wasiwasi, akionekana kuzongwa na mawazo tele.
Akamuuliza kulikoni.
“Rafiki zetu walikuja…” Raymond alimjibu huku akimtazama moja kwa moja usoni. Jaka hakumuelewa, hivyo aliendelea kumtazama kwa macho ya kuuliza.
“Tony na wenzake…walikuja.” Raymond akafafanua, na Jaka akaendelea kumtazama huku akili ikimzunguka.
“Walitaka kujua jana ulikuwa wapi kati ya saa tatu na saa sita za usiku…nikawaambia kuwa mimi sijui ulikuwa wapi kwa sababu mimi mwenyewe sikuwepo chuoni tangu jana saa kumi jioni hadi leo asubuhi ambapo nilikukuta umelala humu ndani…” Raymond alizidi kumpasha habari. Jaka alitabasamu kwa jibu alilowapa.
“Hawakukuamini…” Alisema, ikiwa ni nusu swali, nusu taarifa.
“Of course hawakuniamini! Wakanitishia kunipiga…wakatoa visu, na nini…”
“Visu?” Jaka akamanikika.
“Oh, yeah…visu ndugu yangu! Lakini walipoona bado jibu langu lilibaki kuwa lile lile waliamua kutaka kujua leo ulikuwa wapi…yaani muda ule waliokuja humu ndani na kukukosa leo hii, ulikuwa wapi…” Raymond alimjibu.
“Na…?” Jaka alimuuliza kutaka kujua aliwajibu nini.
“Na nikawaambia sijui…wakaamua kuniachia ujumbe na kuondoka.” Raymond alimalizia maelezo yake.
Jaka akashangaa.
“Ujumbe? Ujumbe gani?” Alimuuliza.
Raymond alimtazama kwa muda, kisha kutoka kwenye mfuko wa pajama alilokuwa amevaa, akamtolea kile kijitabu chake kidogo alichokipoteza usiku uliopita na kumkabidhi. Jaka alihisi ubaridi ukimtambaa mwilini wakati akikipokea kile kijitabu.
“Tony amesema kuwa ukikiona hicho kitabu utaelewa ni nini maana yake…” Raymond aliendelea kumpa ujumbe wa mdomo.
Jaka alishusha pumzi ndefu na kukitupia kitandani kile kijitabu na kujishika kichwa kwa mikono yake miwili.
“Yeah…ninajua sana inamaanisha nini rafiki yangu!” Alinong’ona.
Raymond alimtazama.
“Kitazame vizuri hicho kitabu, Jaka…kifungue…” Alimwambia.
Jaka alimtazama kwa jicho la umakini huku akikiokota tena kile kijitabu kutoka pale kitandani na kukitazama kwa makini. Kilikuwa vilevile alivyotarajia kukiona. Alikigeuza geuza na hatimaye alikifungua ndani. Alizipekua haraka haraka kurasa za kile kijitabu. Halafu akarudia tena kwa utulivu zaidi. Ndipo alipoona. Na hapo alielewa kwa yakini zaidi kwa nini Tony alisema kuwa akikipata tu kile kitabu, ataelewa ni nini maana yake.
Na kweli alielewa.
Katika ukurasa wa kwanza wa kile kitabu kulikuwa kuna picha ndogo ya ukubwa wa stempu iliyoonesha sura yake hali chini ya picha ile kulikuwa kumeandikwa jina, anuani na namba ya simu. Ni yeye mwenyewe ndiye aliyeibandika ile picha na kuandika anuani zile. Ni mwandiko wake mwenyewe. Lakini sasa hivi ile sura yake pale kitabuni ilikuwa imeongezewa kitu kingine. Juu ya sura yake pale kitabuni palikuwa pamechorwa alama kubwa ya “X” kwa kalamu nyekundu. Aliitazama ile picha kwa muda kisha akainua uso wake na kumtazama Raymond.
“Watakuua Jaka.”
Jaka hakumjibu. Alikitupa kile kijitabu mezani na kuketi kitandani, ghafla akijihisi mchovu sana.
“Watakuua Jaka.” Raymond alirudia tena.
Jaka alipiga mwayo wa uchovu na aligundua kuwa alikuwa ana usingizi.
“Potelea mbali…” Alijibu kwa sauti ya chini huku akiinuka na kwenda kufunga mlango kwa loki, akaegemeza mgongo wa kiti chini ya kitasa cha mlango ule halafu akarudi pale kitandani. “Kuniua ndio litakuwa jambo la busara zaidi kwao kwa sasa.” Alimjibu rafikiye bila kumtazama huku akijibwaga kitandani akiwa na suruali yake. Raymond alibaki akimkodolea macho kwa kutoamini jibu alilopewa, na dakika chache baadaye, alisikia Jaka akikoroma taratibu. Alibaki akimtazama rafiki yake kwa huruma, kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko. Akazima taa naye akapanda kitandani kwake kutafuta usingizi.

___________________

Tony aligeuka kwa hasira na kupiga meza kwa ubavu wa ngumi yake, kisha akasonya kwa ghadhabu.
“Mtu kama Jaka hawezi kuyaweka maisha yangu kwenye mashaka namna hii, mimi!” Alimaka kwa hasira. Alphoce Ng’ase na Muddy walimtazama tu bila ya kusema neno. Kimya kilitawala kwa muda mle chumbani kwao pale chuoni.
“Sasa ndio ameshakuwa tishio, Tony…kwa sababu ushahidi unaonesha kuwa Jaka alidandia buti la gari lako wakati we’ ukienda kwa Raul usiku ule…na kama aliweza kutoka kwenye buti lile na kwa namna moja au nyingine akawa ameona mambo yaliyokuwa yakifanyika ndani ya jengo lile, kwa nini basi asiwe Jaka ni tishio? Tena sio kwetu tu, bali pia kwa Raul na biashara yote.” Hatimaye Muddy alisema, akimthibitishia Tony kiini cha mashaka yake.
“Na hilo ndilo jambo ambalo siwezi kulipokea…kwa nini yeye mtu mmoja, tena fala tu, awe tishio? Polisi wenyewe sio tishio…!” Tony aliendelea kusema kwa hasira.
“Sasa tunafanyaje?” Alphonce Ng’ase aliuliza, kisha akaendelea, “…kwa sababu kitabu cha Jaka ni kweli kimekutwa kwenye buti la gari lako…na pia kadi ya anuani za Sajenti wa polisi ilikuwa ndani ya kitabu kile, hiyo inamaanisha kuwa…”
“Hiyo inamaanisha kuwa Jaka ameamua kufuatilia rasmi nyendo zetu ili akizitambua atuchomee utambi kwenye vyombo vya dola.” Tony alidakia kwa hasira.
“Na kuna uwezekano kuwa tayari ameshafanikiwa katika hilo…kwani inaonekana wazi kuwa huyu jamaa ameamua kupambana nasi, na inaelekea tayari ameshajipatia silaha nzuri ya kutupigia…yeye kujua kuwa tunaendesha biashara ya madawa ya kulevya ni silaha kubwa sana kwake!” Muddy alitoa hoja yake.
Tony hakupendezewa na hoja ile, ingawa alijua kuwa ilikuwa ina ukweli. Alikunja uso na kutafakari kwa muda. Alphonce Ng’ase alitoa kisu kirefu chenye ncha kali na kuanza kukichezea chezea.
“Bwana, Jaka angejua mambo yaliyofanyika kule ulipoenda jana, kwa vyovyote mpaka kufikia muda huu hii tayari ungekuwa umeshatiwa mbaroni Tony. Huyu hajagundua kitu, ila tayari ameshaonesha kuwa anaweza kuyafanya maisha yetu yawe magumu sana kama hatutachukua hatua muafaka, tena haraka sana!”
Mara hiyo hiyo Tony aliinua uso wake na kuwatazama wale wahalifu wenzake.
“Jaka lazima auawe, you know what I’m sayin’…he has to die! Na ni lazima afe mara…” Alisema kwa ghadhabu, lakini hakuwahi kumalizia kauli yake kwani mara ile ile walisikia sauti kutokea nje ya mlango wa chumba chao.
Ilikuwa ni sauti kama ya mtu akivuta pumzi ndani kwa ghafla, ikifuatiwa na sauti ya msuguano wa soli ya kiatu na sakafu.
Walitazamana bila ya kusema neno kwa kama sekunde tatu hivi, kisha kwa pamoja waliruka kuelekea pale mlangoni…

____________________

Sekunde kadhaa kabla mikakati ya akina Tony haijakatishwa na ile sauti iliyosikika kutokea nje ya mlango wa chumba chao, swahiba wao Joakim Mwaga alikuwa akipanda ngazi kuelekea pale chumbani kwao huku akipiga mbinja kuigizia wimbo wa mwanamuziki maarufu wa marekani, Lionel Richie. Mkononi alikuwa ameshika CD za muziki zipatazo tano ambazo alikuwa ameziazima kutoka kwa Tony kiasi cha wiki moja hivi iliyopita, akiwa na lengo la kuzirudisha ili ikiwezekana aazime nyingine.
Ingawa ukaribu wa urafiki wao ulipungua tangu Joakim alipoamua kupitisha suluhu na Jaka, bado walitembeleana mara moja moja na waliendelea kuazimana CD za miziki na filamu kama marafiki. Alipofika mlangoni kwa Tony aliinua mkono wake kutaka kubisha hodi, na ndipo aliposikia sehemu ya maongezi yao kutokea pale mlangoni, kwa nje.
“…hiyo inamaanisha kuwa Jaka ameamua kufuatilia nyendo zetu…”
Joakim alishusha mkono wake taratibu aliposikia jina la Jaka likitajwa, na alisimama kimya pale nje mbele ya mlango na kuanza kusikiliza maongezi yaliyokuwa yakiendelea ndani ya chumba kile, na aliyoyasikia yalimshitua sana. Moyo ulianza kumwenda mbio na kijasho kilianza kumtoka. Kadiri alivyokuwa akisikiliza kutokea pale nje ya mlango, ndivyo ilivyomdhihirikia wazi wazi kuwa wale “rafiki zake” walikuwa ni watu wa aina gani. Mshangao alioupata ulikuwa hauna kifani.
Kumbe siku zote nilikuwa natembea na kujihusisha na watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya!
Alijiwazia kwa kutoamini. Hapo alielewa kuwa kwa namna fulani Jaka aligundua kuhusu jambo hilo…
Kwa hiyo machoni kwa Jaka na mimi pia nahusika na biashara ya madawa…ndio maana siku zote amekuwa akikwepa kuwa karibu nami, hata baada ya kusuluhishana.
Mawazo hayo yalipita haraka kichwani mwake huku akijitahidi kuendelea kusikiliza yaliyokuwa yakiongewa kule ndani kutokea pale nje. Akiwa bado hajaamua iwapo aondoke kimya kimya eneo lile au abishe hodi na ajifanye kuwa hajasikia maongezi yale, alishtushwa na sauti ya Tony.
“Jaka lazima auawe, you know what I’m sayin’…he has to die!
Kauli ile ilimshitua vibaya sana, na kwa jinsi alivyoisikia sauti ya Tony ikiyatamka maneno yale, alijua wazi kuwa alikuwa hatanii. Mshituko alioupata ulimfanya pumzi impalie ghafla na hapo aligeuka na kuanza kuondoka kwa mwendo wa haraka huku akikanyagia ncha za vidole vyake ili asitoe sauti. Lakini alipogeuka, alizungusha miguu yake kiasi kwamba soli yake ilisuguana na sakafu yenye michanga, na kutoa sauti iliyosikika na wale wenzake kule ndani…

___________________

Muddy ndiye alikuwa wa kwanza kutoka nje ya chumba kile na kumuona Joakim akianza kuteremka ngazi.
“Joakim!” Alimwita, na mwili ulimfa ganzi Joakim, akajua kuwa alikuwa amebainika. Taratibu Aligeuka taratibu na kuwatazama wale wenzake ambao sasa walikuwa wamesimama kwenye ile korido ile fupi wakimuangalia kwa macho ya kusaili, kila mmoja kwa namna yake.
“Vipi Joakim, mbona unakuja hadi mlangoni halafu unatimua mbio…?” Tony alimuuliza kwa utulivu wa kutisha huku akimsogelea. Joakim hakuwa na jibu la haraka. Macho yake yakaagukia kwenye kisu chembamba na kirefu kilichokuwa mkononi mwa Alphonce. Alimeza funda kubwa la mate na kumtazama Tony kwa macho makavu.
“No problem, man…nilikuwa nakuletea CD zako lakini nilipofika hapa nikakumbuka kuwa kuna moja nimeisahau chumbani kwangu…” Alikokotoa jawabu.
“Kwa hiyo ukaamua kuifuata hiyo CD nyingine kwanza.” Tony alidakia kwa kebehi kumuonesha kuwa alijua kwamba anadanganya.
“Au ulisikia mambo fulani kutokea humu ndani ukiwa umesimama hapa mlangoni yaliyokufanya utake kuwa mbali na chumba hiki haraka iwezekanavyo…?” Alphonce Ng’ase alidakia huku naye akimsogelea.
Eh!
Joakim alimtazama Ng’ase kwa mashaka, akamgeukia Tony, halafu akamtazama tena Ng’ase.
“Sielewi unaongelea vitu gani, Ng’ase…” Alimjibu kwa mshangao. Wale jamaa walimtazama Joakim kwa macho yaliyomwambia kuwa ilibidi afanye bidii zaidi ya ile ili wamuamini.
“Au ulikuwa unawahi kituo cha polisi baada ya kusikia mambo yaliyokuwa yakiongelewa nyuma ya mlango huu?” Muddy alimuuliza kwa sauti ya chini huku akizidi kumsogelea.
Ohoo!
Joakim alianza kurudi nyuma.
“Oya! Msinizingue jamani, au vipi bwana? Mbona mi’ siwaelewi leo?” Alijitutumua.
Tony alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Usitake kuujaribu werevu wetu Joakim…nakumbuka nilikuazima CD tano. Naomba unipatie hizo ulizo nazo hapa kwanza, halafu utaniletea hiyo moja baadaye, unaonaje?” Alimwambia, na Joakim akajua amenaswa.
Alimpa Tony zile CD, ambaye alizipokea na kuanza kuzihesabu moja baada ya nyingine kwa sauti.
Zilikuwa tano.
“Hujasahau hata CD moja chumbani kwako Joakim…” Tony alimwambia kwa utulivu wa kutisha, kisha akamtishia amani zaidi kwa kumwambia, “…inaelekea sasa wewe na Jaka lenu moja.”
Joakim alitikisa kichwa chake kutoka upande mmoja kwenda mwingine huku macho yakimtembea kwa hofu.
“Mbona sielewi unachoongea Tony?” Alijifanya kutoelewa.
Tony alimtaza kwa muda bila ya kusema neno, kisha alishusha pumzi ndefu na kumwambia, “Usijali kaka. Hamna tatizo.”
Kisha akageuka na kurudi chumbani kwake. Alphonce Ng’ase na Muddy walibaki wakiendelea kumtazama Joakim kwa hasira kisha Ng’ase akatema mate sakafuni karibu kabisa na viatu vya Joakim, halafu naye akageuka kurudi chumbani. Muddy alibaki akimtazama kwa muda zaidi, hali akiwa amembetulia mdomo wake kwa dharau. Alimtazama kuanzia usoni hadi miguuni na kumpandisha tena hadi usoni, Joakim akiwa kimya. Muddy alimtolea msonyo mkali na mrefu sana, kisha naye akageuka na kuingia chumbani kwa Tony, akimuacha akiwa ameganda kama sanamu pale nje.
Joakim alibaki akiwa amesimama peke yake pale kwenye ngazi akitafakari nini cha kufanya, kwani hakuwa na shaka kabisa kuwa iwapo Jaka alikuwa ni tishio kwa akina Tony kwa kujua habari za biashara yao haramu, yeye alikuwa ni tishio zaidi kwao, kwani sio tu sasa alijua juu ya wao kujihusisha na biashara ile, bali na pia alijua kuwa walikuwa wamepanga njama ya kumuua Jaka.
Jaka lazima auawe, you know what I’m sayin’…
Inawezekana wakamuua Jaka kweli?
Aliuliza.
Na mimi je?
Alijiuliza zaidi.
…inaelekea sasa wewe na Jaka lenu moja.
Alipata majibu ya maswali yake yote mawili.
Aliteremka ngazi haraka haraka, akiwa ameshapitisha uamuzi. Ni lazima aonane na Jaka haraka iwezekanavyo na amtahadharishe juu ya hatari inayowakabili. Aliangalia saa yake huku akitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea bweni namba tano ambamo Jaka alikuwa akiishia. Ilikuwa ni saa saba na nusu za mchana.
Bila shaka Jaka atakuwa chumbani mwake saa hizi.
Hatua kadhaa nyuma yake, Tony alikuwa akimfuata, hali Muddy na Alphonce Ng’ase nao wakiwa wanaelekea kwenye bweni namba tano kwa njia nyingine. Joakim hakuwa na wazo la kugeuka nyuma wala kutazama pembeni kuona kama alikuwa anafuatwa. Akili yake ilikuwa inawaza kuonana na Jaka haraka iwezekanavyo.

Akiwa mbele ya mlango wa lifti ya kupandia kwenye ghorofa za juu za jengo lile alipata wazo jipya. Inawezekana Tony na wenzake nao wakaamua kumfuata Jaka chumbani kwake. Alitembeza macho huku na kule miongoni mwa wanafunzi wachache waliokuwa wakiisubiri ile lifti pamoja naye. Alimuona mtoto mdogo wa kiasi cha miaka kumi na mbili hivi aliyekuwa akiuza karanga mbele ya jengo lile. Alitoa kalamu na kuandika ujumbe mfupi kwenye kijitabu chake cha anuani na kuchana ule ukurasa alioandikia ujumbe ule. Alimsogelea yule mtoto na kumpa shilingi mia tano na ile karatasi yenye ujumbe ambayo aliiandika jina na namba ya chumba cha Jaka. Akamuomba yule mtoto aufikishe ujumbe ule. Yule mtoto alitoka mbio na kuanza kupanda ngazi kuelekea ghorofa ya pili ambako chumba cha Jaka kilikuwepo. Dakika mbili baadaye lifti ilifika pale chini na Joakim alijipenyeza upesi ndani yake. Milango ilifunga na lifti ikaondoka kupanda juu.
Tony alimuona Joakim akimkabidhi yule mtoto ile karatasi na kuingia ndani ya lifti. Kwa mwendo wa haraka alimuwahi yule mtoto kabla hajafika ghorofa ya pili na kumsimamisha. Alimuomba ile karatasi iliyopewa na Joakim, na yule mtoto bila kuelewa alimpa. Tony alisoma ujumbe ulioandikwa kwenye karatasi ile kisha akamrudishia yule mtoto huku uso wake ukifanya tabasamu dogo la ushindi.
“Okay dogo…ipeleke tu hiyo barua mahala ulipoagizwa.” Alimwambia, na yule mtoto bila ya kuelewa, alitimua mbio kupeleka ujumbe ule muhimu. Tony alirudi pale kwenye lifti, na muda mfupi baadaye ile lifti ilirudi tena naye akaingia pamoja na wanafunzi wengine wachache waliokuwa pale chini, wakiwemo Alphonce Ng’ase na Mohammed “Muddy” Shomari.
Ilikuwa ni saa nane kasoro dakika ishirini za mchana.

___________________

Jaka alitazama saa yake na kugundua kuwa ilikuwa ni saa saba na dakika thelathini na tano za mchana. Alikumbuka kuwa ile ilikuwa ndiyo siku ya kuzaliwa kwa mpenzi wake naye aliahidi kumpatia zawadi nzuri atakayoikumbuka daima. Alikuwa amemtungia shairi zuri ambalo aliamua kujirekodi kwenye simu yake ya kisasa akiliimba ikiwa ndio zawadi aliyomuandalia. Lilikuwa ni shairi la mapenzi aliloliandika kwa lugha ya kiingereza waliyozea kutumia pale chuoni na alikuwa na hakika kuwa Moze angelipenda sana.
Aliinuka kutoka kitandani alipokuwa amejilaza chali akilikariri lile shairi akiwa na simu yake pamoja na lile shairi mkononi. Akaketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake ya kusomea, akaiweka mezani ile simu kisha akalisoma kwa mara ya mwisho lile shairi kabla ya kuanza kujirekodi.

The day I saw you, my love began.
My heart went with you, when my love began.
But the day you said “Yes”, is when my life really began.

Sometimes I wonder, what’s in your love.
That’s such a wonder, in your kind of love.
‘Cause my heart can wander, not ever again.

You make me feel, my world is real.
I know no anger, not anymore.
I know no tears, yet I know.
When your love is gone, my tears will flow.

But until then, my life has just begun,
With our love…
Happy Birthday my love.

Lilikuwa ni sahiri lililoeleza ukweli wa mapenzi yake kwa Moze. Ya kwamba penzi lake lilianza pale tu alipomtia machoni, na siku Moze alipokubali kuwa wake wa maisha ndipo maisha yake yalipoanza.
Ni shairi lililoeleza ni jinsi gani Jaka alivyoliona penzi la Moze kuwa ni la ajabu kiasi kwamba hata moyo wake hautamani msichana mwingine yeyote maishani mwake. Jaka alimalizia shairi lile kwa kumueleza mpenzi wake kuwa penzi lake (Moze) limemfanya asijue kuchukia tena maishani mwake zaidi ya kupenda tu, na kwamba limemfanya asijue tena kutokwa na machozi, lakini pia anakiri kuwa anajua machozi mengi yatamtoka siku Moze takapoamua kuliua penzi lile…lakini mpaka siku hiyo itakapofika, maisha yake ndio kwanza yalikuwa yameanza…kwa penzi lililopo baina yao.
Jaka alitabasamu baada ya kulisoma tena lile shairi, akiwa na hakika kabisa kuwa maneno ya shairi lile yalikuwa ni ukweli uliotoka ndani kabisa ya moyo wake. Aliamini kuwa Moze akiupata ujumbe atakaomtumia kutokea kwenye simu yake ukiwa na sauti yake ikimchombeza kwa vina vya shairi lile, atafurahi sana na ataiona ile kuwa ni zawadi ambayo hataisahau maishani mwake.
Alivuta pumzi nyingi mapafun mwake, na kuzitoa taratibu, kisha huku akitabasamu, alibofya sehemu iliyoiwezesha ile simu kurekodi kile atakachokuwa anakisema, kisha kwa sauti ya kuchombeza alianza kusoma ubeti wa kwanza wa shairi lile.
“The day I saw you, my love began.
My heart went with you, when my love began.
But the day you said Ye…”
Alikatishwa na kishindo cha mlango wake ukigongwa kwa nguvu kutokea nje. Alikunja uso na kugeukia kule mlangoni na wakati huo huo mlango ukagongwa tena kwa nguvu.
“Oi! Nani…? Ingia!” Aliita kwa sauti, lakini mgongaji akazidi kugonga, sauti hafifu ikimfikia pale ndani. Kwa kuwa ile meza ilikuwa kando ya mlango ule, Jaka alijigeuza, akanyoosha mkono wake na kuufungua ule mlango bila ya kuinuka kutoka pale kitini. Alishangaa kumuona mtoto mwenye sinia lenye vipaketi vya karanga akiingia mle ndani na kusimama hatua kama mbili ndani ya kizingiti cha mlango ule.
“Shikamoo.” Yule mtoto alimuamkia.
“Aaam…Marahaba…unasemaje?”
“Jaka yupo?”
“Jaka ndio mimi, unasemaje?”
Yule mtoto alimpa kile kijikaratasi. Jaka alikipokea na yule mtoto akaanza kuondoka.
“Oi! Ngoja kwanza mtoto…nani kakupa hii karatasi…?”
“Simjui!” Yule mtoto alimjibu huku akitoka nje ya chumba kile bila kusubiri maswali zaidi.
Jaka alibaki amepigwa na butwaa.
Aliifungua ile karatasi na kuisoma. Maudhui ya waraka ule yalimfanya ashushe pumzi ndefu na kusajili sura ya kutoelewa. Alisukuma mlango wake kuufunga na kuiweka ile karatasi aliyopewa na yule mtoto juu ya simu yake pale mezani hali uso wake ukiwa kwenye hali ya kukosa uamuzi. Aliichukua tena ile karatasi na kuusoma tena ule ujumbe aliyoandikiwa:

Jaka, tafadhali sana sana fanya hima tuonane sasa hivi juu ya jengo hili.
Naomba uniamini kwani ni jambo la kufa na kupona kaka… kwako na kwangu. Ni mimi,
Joakim Mwaga.

Saa 7:28 Mchana.

Aliangalia saa yake. Ilikuwa ni saa nane kasoro dakika kumi mchana. Kwa hiyo ni dakika zipatazo ishirini na mbili zilikuwa zimepita tangu ujumbe ule uandikwe.
Jambo la kufa na kupona? Ni jambo gani hilo? Na kwa nini tuonane juu ya jengo hili na sio sehemu nyingine yoyote?
Kengele ya hatari ikagonga akilini mwake. Alihisi kuwa ule ulikuwa ni mtego wa akina Tony kutaka kumkamata kwa kumtumia Joakim, kwani kwa Joakim kutaka kuonana naye siku moja tu baada ya yeye kugundua kuwa Tony anajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ilikuwa ni ushahidi tosha juu ya hilo.
Lakini pia iliwezekana kuwa si Joakim aliyeandika ujumbe ule.
Sasa angejuaje?
Kuna njia moja tu ya kujua…kwenda kujionea mwenyewe!
Bila ya kufikiri zaidi, aliitia mfukoni ile karatasi yenye ujumbe, akachukua fulana iliyokuwa pale kitandani na kuivaa haraka haraka huku akitoka nje ya chumba kile akiacha mlango ukijibamiza nyuma yake. Alibonyeza kitufe cha kuiita lifti kisha akabaki akisubiri kwa wahka huku akitazama saa yake.
Saa nane kasoro dakika sita.
Taa nyekundu juu ya mlango wa lifti ile ilikuwa inawaka kwenye namba kumi. Akagundua kuwa tangu amefika pale, taa ile ilikuwa inawaka kwenye namba ile ile. Akaelewa kuwa kuna mtu ameizuia lifti ile kwenye ghorofa ya kumi. Aliendelea kusubiri.
Saa nane na dakika tatu.
Alianza kupata wasiwasi kuwa labda ile lifti ilikuwa mbovu. Wazo la kupanda kwa miguu mpaka juu ya jengo lile lilimfanya asonye kwa hasira. Akaangalia tena saa yake.
Saa nane na dakika saba.
Taa ikazimika kwenye namba kumi. Akajua kuwa sasa lifti ile ilikuwa inakuja. Alitamani sana awaone hao jamaa waliokuwa wameizuia ile lifti kule juu muda wote ule. Taa iliwaka kwenye namba nne kwa muda mfupi na kuzimika tena. Ilikuwa inakuja. Mlango wa lifti ulipofunguka pale chini hakukuwa na mtu yeyote ndani ya lifti ile. Aliingia na kubonyeza namba kumi na lifti ilianza kupanda kuelekea ghorofa namba kumi.
Jengo la bweni namba tano lilikuwa na ngazi tatu za kupanda kwa miguu. Ngazi ndogo kila upande wa jengo lile pana, ambazo mara nyingi zilikuwa zikitumika na wanafunzi walioishi katika vyumba vya pembeni na vile vya kwenye korido fupi za pembeni. Katikati ya jengo lile kulikuwa kuna ngazi kubwa kando ya lifti ambazo mara nyingi zilitumika na wanafunzi waliokuwa wakiishi kwenye vyumba vya kwenye korido fupi za kati na wale wa kwenye vyumba vilivyokuwa kwenye korido ndefu.
Sekunde chache baada ya lifti kuondoka ikiwa na Jaka ndani yake, watu watatu walitoka nje ya jengo lile kwa kutumia ngazi zile.
Tony alitoka kwa kutumia ngazi ndogo zilizokuwa kulia kabisa na kuzunguka nyuma ya jengo lile na kutoweka bila ya kuonekana na mtu.
Alphonce Ng’ase aliokea kwenye ngazi kubwa za katikati na kuambaa taratibu kutoka kwenye jengo lile, wakati Muddy Shomari alitoka kwa kutumia ngazi ndogo zilizokuwa kushoto mwa jengo lile na kutoweka.

_____________________

Lifti ilikuwa inaishia ghorofa ya kumi. Jaka aliteremka na kupanda ngazi zilizoelekea juu ya jengo la lile la ghorofa kumi na mbili. Hatua chache mbele yake kulikuwa kuna mlango uliotokezea kwenye ukumbi mwembamba na mrefu uliofanya paa la zege la jengo lile refu. Kabla ya kuufikia mlango ule, kulia na kushoto mwa ngazi zile alizokuwa akizikwea, kulikuwa kuna mlango mwingine mmoja kila upande. Mlango wa kulia kwake ulikuwa ni wa kuingia kwenye chumba kilichokuwa kina mitambo ya umeme uliotumika kuendeshea lifti ya jengo lile. Mlango wa kushoto kwake ulikuwa ni wa chumba kilichokuwa kina tanki kubwa la kuhifadhia maji kwa ajili ya wakaazi wa jengo lile.
Alichungulia kwenye vyumba vile huku akiita jina la Joakim kwa sauti ya chini huku akiwa makini sana. Hakupata jibu lolote. Alipita kwenye ule mlango uliokuwa mbele yake na kutokea kwenye paa la jengo lile. Alitazama kulia na kushoto. Hakukuwa na mtu.
“Joakim!” Aliita kwa sauti, na kupokewa na kimya tu. Alitembea taratibu kuelekea kushoto kwake. Mbele yake kulikuwa kuna vyumba viwili. Kimoja, kilichokuwa moja kwa moja mbele yake kilikuwa ni cha umeme kwani kilikuwa na nyaya nyingi za umeme zilizotoka kwenye mashine mbili kubwa zilizokuwa ndani ya chumba kile na kutambaa kuelekea ndani ya jengo lile.
Kilikuwa kitupu.
Chumba kingine kilikuwa pembeni ya kile cha kwanza kushoto kwake kiasi kwamba vyumba vile vilifanya herufu “L”. Alifungua mlango wa kile chumba kingine ambacho kilikuwa kina mabaki ya tanki la kuhifadhia maji lililoharibika.
Na chenyewe kilikuwa kitupu.
Wasiwasi ulianza kumtawala, na akaamua kuondoka. Aligeuka na kuanza kuondoka, lakini alipoufikia mlango wa kumrudisha ndani ya lengo lile kutokea kule juu, aliangalia kulia kwake. Kulikuwa kuna chumba kingine kimoja. Alichungulia ndani yake huku akiita jina la Joakim.
Kimya.
Kilikuwa ni chumba cha tanki la kuhifadhia maji sawa na lile aliloliona wakati akipanda ngazi kuelekea juu ya jengo lile.
Alishindwa kuelewa.
Iweje Joakim…au yeyote yule aliyeandika ujumbe ule…amtumie ujumbe wakutane kule juu halafu asitokee? Aliegemea ukuta mfupi uliozunguka eneo lile kuwazuia watu wasianguke kutoka kule juu na kuangalia chini huku akili yake ikijaribu kuelewa hali ile.
Jiji la Dar lilionekana likiwa limejitawanya kwa mapana na marefu kutokea pale juu, lakini akili yake muda ule ilikuwa kwenye ule ujumbe alioletewa pale chumbani kwake na yule mtoto muuza karanga.
Nini maana yake hii? Kama ule ujumbe ulikuwa ni mtego wa akina Tony, mbona hata wao hawapo huku juu?
Ilikuwa haileti maana.
Alisonya huku akigeuka kutoka pale kwenye ule ukuta aliokuwa ameuegemea kwa mbele na kuuegemea kwa mgongo. Alikuwa katika hatua ya kujisukuma kutoka pale ukutani kwa mgongo wake ili aondoke ndipo alipomuona.

Naam, alikuwa ni Joakim hasa.
Lakini hakuwa katika hali ambayo Jaka aliitarajia.
Kwenye kona baina ya ukuta wa kile chumba alichotoka kuchungulia punde tu, na ule ukuta uliozunguka ule ukumbi juu ya jengo lile, Joakim Mwaga alikuwa amejikunyata sakafuni, mgongo wake ukiwa umeegemea kwenye kona ile iliyofanya nyuzi tisini. Macho yake yalikuwa yamekodoka kwa mshangao wa kudumu, mdomo wake ulikuwa wazi hali ulimi wake ukining’inia nje. Eneo lote la kifua chake lilikuwa limetapakaa damu kutoka kwenye jeraha lililokuwa shingoni kwake.
Jaka alipiga yowe la mshituko huku miguu ikimwisha nguvu.
Joakima alikuwa ameegemeza kichwa chake kwenye bega lake la kushoto na sehemu ya kichwa kile ilikuwa imeegemea ukuta. Mpini wa kisu ulichomoza kutoka kwenye jeraha lililokuwa upande wa kulia wa shingo ile.
Jaka alipiga hatua tatu za haraka kumsogelea huku akimuita kwa wahka na woga mkubwa.
“Joakim! Joakim! Joakim…” Alizidi kumuita huku akiwa amechutama mbele yake, akimtikisa. Na hapo ndipo alipogundua kuwa ingawa macho yake yalikuwa yakitazama mbele kwa mshangao, Joakim alikuwa haoni, na alikuwa haoni kwa sababu sasa alikuwa marehemu. Joakim hakuwa hai tena. Alikuwa amekufa.
Ameuawa.
Ukelele wa woga ulimtoka Jaka na hapo hapo aliangukia mgongo alipojaribu kurudi nyuma ili awe mbali na ule mwili usio na uhai. Huku akipiga kelele Jaka alijaribu kuinuka huku akirudi nyuma, akadondoka tena. Akajaribu tena lakini kwa mara nyingine tena akadondokea matako. Akabaki akisotea makalio kurudi nyuma huku macho yamemtoka pima akimtazama Joakim kwa woga huku akipiga mayowe.
Hatimaye alifanikiwa kusimama na kujiegemeza kwenye ule ukuta na kubaki akitweta kutafuta pumzi ambazo zilimkaba kooni.
Ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kuona mtu aliyekufa, wachilia mbali aliyeuawa, hasa ikiwa mtu huyo ni ambaye alikuwa akimfahamu. Wazo la kwanza lililomjia kichwani mwake lilikuwa ni kwenda kutoa ripoti polisi juu ya tukio lile.
Alikurupuka mbio kutoka pale ukutani kuziendea ngazi za kuteremka kutoka eneo lile. Picha ya Joakim Mwaga, akiwa amejikunyata pale chini, mguu wake mmoja akiwa ameukunja kwa uchungu kiasi kwamba goti lake lilikuwa karibu sana kugusana na bega lake, wakati mguu wake mwingine akiwa ameunyoosha mbele pale sakafuni, mikono yake yote miwili ikiwa imeshikilia kwa nguvu sehemu chini kidogo ya shingo yake, karibu na pale mpini wa kisu ulipochomoza, bado ilikuwa kichwani mwake.
Mambo yote yaliyofuatia kuanzia muda ule yalitokea haraka sana.
Kabla hajaufikia ule mlango, alisikia vishindo vya viatu vikipanda zile ngazi kuelekea kule alipo kuwa. Havikuwa vishindo vya mtu mmoja. Ni watu wengi. Alitaka kugeuka arudi kule alipotokea, akagundua kuwa njia pekee ya kutokea eneo lile ni kupitia kwenye ule ule mlango, kuelekea kule kule vilipokuwa vikitokea vile vishindo. Kabla hajatanabahi, alipatwa na kihoro aliposhuhudia askari wa jeshi la polisi wanne wakiingia pale ju kupitia kwenye ule mlango, wakimlazimisha arudi nyuma bila kupenda, macho yakimtembea, mdomo ukimuanguka.
“Tulia kama ulivyo!” Mmoja wao alimfokea akiwa amemuelekezea bastola.
Jaka alibaki amepigwa na butwaa. Hakutaka kuyaamini macho yake alipoona wale askari wakimzingira huku wakimnyooshea mitutu ya bunduki aina ya SMG. Aliihisi akili ikimsinyaa na miguu ikimwisha nguvu.
“Sio mimi…I mean…sikufanya kitu…amekufa…nimemkuta ameuawa!” Aliropoka kwa hamaniko huku akipiga hatua kuwasogelea wale askari. Mara ile ile wale askari walikoki zile bunduki zao na yule aliyemuamuru atulie hapo mwanzo akamfokea.
“Tulia hapo hapo ulipo wewe! Hatua nyingine moja tu utakuwa kilema sasa hivi!”
Heh!
Jaka alikatisha hatua zake na kusimama huku akinyoosha juu mikono yakeiliyokuwa akimtetemeka vibaya sana.
“Kaa kimya!” Yule askari alimwamuru.
Jaka alijikuta akika chini, miguu ikishindwa kabisa kuendelea kumhimili. Macho makali ya yule askari yalimfuata pale pale chini na bila ya kutoa macho yake usoni kwa Jaka aliiita, “Koplo!”
“Afande!”
“Chunguza eneo hili haraka!”
Mmoja wa wale askari waliomzingira Jaka alichomoka na kuelekea kule alipotokea Jaka, mwisho wa ukumbi ule. Jaka alijua ni nini atakachokikuta kule alipoelekea, ila hakujua ni nini kingemkuta yeye baada ya hapo. Sauti ya mshituko ilisikika kutokea kule alipoelekea yule Koplo, na Jaka alifumba macho kama kwamba kufanya hivyo kungemsaidia asisikie maneno ambayo yangefuata.
“Kuna maiti hapa afande…kauawa…kama tulivyotaarifiwa!” Yule koplo alijibu kwa sauti.
“Mlivyotaarifiwa? Nan…na nani?” Jala alijikuta akiropoka, na hapo hapo alizabwa kofi kali sana la uso, yowe kubwa likamtoka bila kupenda, maumivu makali yakimtawala usoni.
“Kimya wewe! Unaua mtu halafu unajitia kushangaa?” Yule askari alimkemea, kisha alienda kule alipoelekea yule Koplo, wale askari wengine walibaki vilevile wakiwa wamemuelekezea Jaka mitutu ya bunduki zao. Jaka alianza kulia kwa majuto na uchungu, akijua kuwa tayayi alikuwa amebebeshwa kesi ya mauaji. Baada ya muda yule askari kiongozi alirudi na kumuuliza jina lake. Jaka akamtajia.
“Jaka Brown Madega…uko chini ya ulinzi kwa tuhuma ya kuhusika na mauaji!” Yule askari kiongozi alimwambia kwa ghadhabu.
“Sio mimi afande…! Sio mimi…”
Mikono yenye nguvu ilimkamata na kumfunga pingu mikono yake kwa mbele.
“Maelezo yote utatoa kituoni!” Alikemewa.
Mambo yote yaliyofuata baada ya hapo yalikuwa kama ndoto tu kwa Jaka. Wale askari waliwasiliana na askari wengine ambao bila shaka walikuwa chini ya jengo lile kwa redio maalum za mawasiliano na dakika chache baadaye walikuja askari wengine wakiwa na machela ya kubebea maiti. Mwili wa Joakim Mwaga ulipigwa picha ukiwa umejikunyata pale chini kabla ya kubebwa kwenye machela na kuondolewa kutoka eneo lile.
Jaka aliteremshwa haraka haraka kutoka kule juu hali akiwa amefungwa pingu. Ilikuwa ni heka heka baada ya wanafunzi wenzake kumuona akiteremshwa ngazi na askari namna ile. Walikusanyika vikundi vikundi na kuanza kuulizana juu ya mkasa ule ambao wote hawakuuelewa.
Askari walimuamuru Jaka awapeleke chumbani kwake, naye alitii bila ubishi huku kichwa kikimzunguka. Alijitahidi kufikiri lakini hakuna fikra yoyote njema iliyomjia. Mlango wa chumba chake ulikuwa wazi na yule askari alimuuliza iwapo aliuacha wazi kabla ya kutoka nje ya chumba kile.
“Nakumbuka niliubamiza lakini sikuufunga kwa ufunguo…” Jaka alijibu.
“Okay, tuingie ndani humo…!” Askari aliamuru, nao wakaingia na kuacha askari mmoja nje ya mlango wa chumba kile kuwadhibiti wanafunzi waliojaa kwenye korido pale nje ya chumba chake wakitaka kujua kilikuwa kinaendelea.
“Tunapekua chumba chako kutafuta ushahidi wowote tutakaoweza kuutumia katika kuchunguza swala hili, sawa?” Yule askari mwenye bastola, ambayo sasa ilikuwa imehifadhiwa kwenye mkoba maalum ulioning’inia kiunoni mwake alimwambia. Kabla Jaka hajajibu wale askari walianza kupekua chumba kile kwa vurugu. Makabati yalifunguliwa na nguo zilitupwa huku na kule, vitabu vilichakuriwa na kutupwa hovyo sakafuni, kapeti liliinuliwa na kuvutwa bila mpangilio.
Jaka aliangalia mambo yake huku akili ikimzunguka.
“Afande!” Katikati ya upekuzi ule wa fujo, mmoja wa wale askari aliita, naye akapeleka macho yake kule ilipotokea ile sauti. Yule askari mwenye bastola alisogea pale kando ya kitanda cha Jaka alipokuwa amesimama yule askari aliyeita huku akiwa ameinua upande wa godoro la kitanda kile. Jaka naye alisogea taratibu huku akihisi moyo wake ukitaka kumchomoka kutoka kifuani kwake.
Chini ya godoro lile, juu ya chaga za mbao za kitanda chake, kulikuwa kuna glovu mbili za mpira mithili ya zile zinazotumiwa na madaktari wanapofanya upasuaji.
Zile glovu zilikuwa zimetapakaa damu mbichi!
E bwana we!
Jaka alitoa ukelele wa ghadhabu na kutoamini huku akizikodolea macho zile glovu, ukweli kuwa alikuwa ametegwa na amenasa ukimshukia dhahiri fahamuni. Alijirusha juu kwa nguvu akijaribu kugeuka ili atoke nje ya chumba kile.
“Haiwezekani…! Haiwezekani hii! Hii ni njama tu hii1 Nimepakaziwa…! Nimesingiziwa mimi…Hii ni njama kabbisa!” Alibwata kwa hasira. Mikono yenye nguvu ilimshika na kumbana, lakini alizidi kufurukuta.
“Niacheni, niacheni nasema, vibaraka wakubwa nyie!”
Alitwangwa ngumi nzito ya tumboni, na pumzi zikamkatika ghafla, maumivu makali yakimtawala. Alipiga yowe la maumivu huku akienda chini akiwa amejishika tumbo. Aliinua uso kwa ghadhabu kumtazama aliyempiga, akajikuta akiutumbulia macho mtutu wa bastola iliyoelekezwa katikati ya macho yake.
“Tulia kama ulivyo fisi wee! Uko chini ya ulinzi kwa tuhuma za amuaji na sitakukumbusha tena juu ya hilo…fanya tena upuuzi wako uone jinsi nitakavyotawanya bichwa lako kwa risasi, fala we! Unaleta vurugu wakati uko chini ya ulinzi, ebbo!” Yule askari kiongozi alimfokea kwa hasira.
“Lakini mimi sijaua, afande…huoni kama hii ni njama tu?” Jaka alisema kwa kuombeleza huku akiwa amepiga magoti pale chini, machozi yakimbubujika.
“Hakuna aliyekuambia kuwa umeua kijana…kuanzia sasa na kuendelea wewe ni mtuhumiwa tu wa mauaji haya…mpaka hapo mahakama itakapoamua kuwa uwe mshitakiwa namba moja au uachiwe huru, sawa bwana? Kwa sasa nataka ushirikiano wako wa kila hali.” Yule askari alimwambia na kukaa kimya kwa muda kabla ya kuanza kumtupia maswali huku askari mwingine akinukuu kwa maandishi mahojiano yale.
“Hizi glovu ni zako?”
“Hapana…”
“Umeshawahi kuziona kabla ya hapa?”
“Hapana…sijawahi.”
“Unaweza kujua zimefikaje hapa chini ya godoro ?”
“Sijui…”
Yule askari alimtazama kwa muda, na Jaka akajua kuwa alikuwa hamuamini.
“Sawa…” Hatimaye alisema yule askari na kutoa maelekezo kwa wale askari wengine waliokuwamo mle ndani. Zile glovu ziliwekwa ndani ya mfuko maalum wa nailoni na kuchukuliwa kama ushahidi. Jaka alitolewa mkiki-mkiki nje ya chumba kile kuelekea kwenye Land Rover ya polisi iliyokuwa imeegeshwa nje ya jengo lile. Wanafunzi wenzake walikuwa wamejaa pale nje kushuhudia tukio lile huku baadhi wa wanafunzi wa kike wakilia baada ya kuuona mwili wa Joakim Mwaga ulipotolewa hapo awali. Jaka alipitishwa akiwa amefungwa pingu kuelekea kwenye gari ile. Aliangaza huku na kule kwa uso uliohamanika akitarajia kumuona Raymond au Moze katika kundi lile la wanafunzi.
Wote hawakuwepo.
Huku akibubujikwa na machozi, Jaka aliingizwa ndani ya lile gari la polisi, ambalo liliondoka kwa kasi kutoka eneo lile.

12

Raymond Mloo alizipokea habari za kukamatwa kwa Jaka akihusishwa na kifo cha Joakim kwa mshangao na mshituko mkubwa sana. Kama angesikia kuwa Jaka amekutwa akiwa ameuawa, bila shaka asingeshangaa kama jinsi alivyoshangazwa na habari ile. Lakini pamoja na kushangazwa kwake, jambo ambalo alikuwa na uhakika nalo kabisa kichwani mwake ni kwamba zile zilikuwa ni hila za Tony na wenzake za kutaka kumkomoa Jaka na kuhakikisha kuwa anafungwa miaka mingi, au maisha…au kunyongwa kabisa, na hivyo kuwapa wao nafasi ya kuendelea na biashara zao haramu.
Lakini kwa nini Joakim?
Na kwa nini Jaka akutwe eneo la tukio?
Ni maswali ambayo hakuweza kuyapatia majibu mara moja mpaka alipoonana tena na rafiki yake siku mbili baada ya tukio. Na hapo aliweza kupata jibu la swali moja tu kati ya yale mawili: ilikuwaje hata Jaka akakutwa katika eneo la tukio.
Kesi ya mauji!
Ama kweli Tony ni mtoto mbaya…tena mtoto mbaya sana.
Masikini Jaka…nani atamuamini atakaposema kuwa hakumuua Joakim Mwaga? Wanafunzi wengi pale chuoni walijua juu ya uhasama uliojengeka baina yake na Joakim Mwaga. Kuna wanafunzi pale chuoni walioshuhudia kwa macho yao siku Jaka na Joakim walipoamua kurekebisha tofauti zao kwa kutupiana makonde. Na tangu siku ile ilijulikana wazi kuwa hawakuwa na uhusiano mzuri kabisa, jambo lililopelekea Jaka kupewa kipigo kikali kule Club Billicanas na kulamizika kulazwa hospitali kwa siku kadhaa.
Na tangu hapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wanasubiri kuona Jaka atajibu vipi mapigo yale…
Na sasa Joakim ameuawa na Jaka amekutwa eneo la tukio.
Masikini Jaka…

___________________

Moze alikuwa akimsikiliza mhadhiri nusu nusu, kwani sehemu ya akili yake ilikuwa ikifikiria juu ya zawadi aliyoahidiwa na mpenzi wake siku ile. Aliangalia saa yake na kugundua kuwa ilikuwa ni saa tisa kasoro robo za alasiri. Ilikuwa imesalia robo saa tu kipindi kiishe, naye alikuwa ana ahadi ya kukutana na mpenzi wake baada ya kipindi kile na aliona kuwa yule mhadhiri alikuwa anamchelewesha tu.
Aliona askari wa jeshi la polisi akiingia mle darasani na kunong’ona na mhadhiri kwa muda. Kimya kilitanda darasani, kila kila mwanafunzi akiwa amemakinika na ujio wa yule askari mle darasani, na muda mfupi baadaye Moze alishangaa kusikia mhadhiri akiita jina lake na kumuomba aende kule mbele. Huku moyo ukimdunda kwa wasiwasi, Moze alienda kule alipokuwa amesimama mhadhiri na yule askari.
“Moze, huyu ni afisa wa polisi…alikuwa anahitaji kukuuliza maswali machache…” Mhadhiri alimwambia kwa upole. Moze alimtazama yule askari kwa mashaka halafu akamtazama mhadhiri, kisha akamtazama tena yule askari.
“Naomba tuongazane kituoni tafadhali.” Yule askari alimwambia. Moze alitaka kubisha, lakini akabadili mawazo. Akiwa haelewi ni nini kinachoendelea, alimfuata yule afisa wa polisi kuelekea kituo cha polisi cha Mlimani. Huko aliingizwa kwenye chumba kidogo na kuombwa asubiri. Alisubiri kwa muda wa nusu saa nzima huku akizidi kuchanganyikiwa juu ya sababu ya kuletwa pale kabla hajatokea mtu yeyote. Ndani ya muda huo mawazo mengi ya mashaka yalimuandama, yote yakiwa ni juu mpenzi wake kufanyiwa madhara na akina Tony.
Wamemfanya nini sasa Jaka wangu hawa watu yarabbi?
Wamemuua kama walivyomuua Rose? Oh Mungu wangu…isiwe hivyo jamani!
Alihamanika vilivyo.

Hatimaye askari mwingine aliingia mle ndani alimokuwa amesubirishwa.
“Wewe ndiye Moze Mlekwa?” Aliuliza yule askari huku akikaa kwenye kiti kilichokuwa mbele yake.
“Ye..I mean…ndio. Kwa…kwa nini niko hapa? Kuna nini?” Moze alimjibu na kumtupia maswali huku moyo ukimwenda mbio.
“Jina Jaka Brown Madega…linamaanisha lolote kwako?” Jamaa alimuuliza bila kujisumbua kumjibu yale maswali yale, na Moze alihisi ubaridi ukimtambaa kwa swali lile.
Ni kweli! Kuna jambo limemkuta Jaka!
“Kwa nini unaniuliza hivyo…kwani ni nini kimetokea…?”
“Umekuja hapa kujibu maswali, na sio kuuliza…sasa mimi nitauliza maswali na wewe utatoa majibu, sawa?”
“Kha! Mimi sielewi kwa nini nimeletwa hapa halafu unaniambia nisiulize maswali?”
“Wewe huna haja ya kuelewa…kazi yako hapa ni kujibu maswali yangu halafu uende zako…unafahamu nini kuhusu mtu aitwaye Jaka Brown Madega?”
Moze alimtazama yule askari kwa hasira. Akaamua kuwa hiyo haitamsaidia kitu.
“Jaka…ni mpenzi wangu…amekutwa na nini?”
Yule askari alilidharau swali la Moze na badala yake akamtupia swali jingine.
“Unamfahamu mtu aitwaye Joakim Mwaga?”
“Ndiyo..kwa nini?”
“Uliwahi kuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi au vinginevyo na huyu mtu aitwaye Joakim Mwaga?”
Eh! Maswali gani haya?
“Hapana…!” Moze alimjibu kwa mshangao, hakutarajia swali kama lile, “…kwa nini..?” Aliongezea jibu lake kwa swali. Kwa mara nyingine tena yule askari hakujisumbua kumjibu.
“ Kulikuwa kuna uhusiano gani baina ya huyo mpenzi wako Jaka na Joakim Mwaga?”
“Afande naomba unieleze ni nini hasa unachotaka kutoka kwangu…maana sioni sababu ya kunitoa darasani, kunileta huku na kuniuliza maswali kama haya!”
“Ninachotaka kutoka kwako ni jibu la swali ninalokuuliza…” Jamaa lilimjibu kwa utulivu, kisha akaendelea, “…kulikuwa kuna uhusiano gani baina ya Jaka na Joakim…walikuwa marafiki ?”
“Aam, kwa marafiki hawakuwa…”
“Hawakuwa marafiki?”
“Ndiyo!”
“Unaweza kujua ni kwa nini?”
“Walikuwa na tabia tofauti…wasingeweza kuelewana.”
“Sio kwa sababu yako wewe?”
Moze alitikisa kichwa kutokana na hoja ile.
“Sidhani kama hiyo inaweza kuwa ni sababu…ni kweli kuwa Joakim alitaka kuingilia kati uhusiano wetu, lakini hakufanikiwa…”
“Kwa hiyo ni kweli kuwa kulikuwa kuna uhasama baina yao juu yako?”
“Ndiyo…lakini ulikwisha…”
“Hebu nielezee juu ya uhasama huo na jinsi ulivyokwisha.”
Moze alisita kidogo. Bado alikuwa hajaelewa yale maswali yalikuwa yanaelekea wapi. Lakini alijua kuwa polisi wakitaka kujua yaliyotokea baina ya Jaka na Joakim watayajua tu, kwani wanafunzi wengi pale chuoni walikuwa wanaujua uhasama uliopo baina yao. Likini sio kama jinsi yeye anavyouelewa. Hivyo akaamua kumuelezea yule askari juu ya uhasama uliojengeka baina ya Jaka na Joakim. Alimuelezea tangu mwanzo jinsi Jaka na Joakim walivyopambana hadi Jaka alipopigwa vibaya na marafiki wa Joakim kule Club Billicanas na kulazwa hospitalini.
“Tangu hapo uhusiano haukuwa wa kirafiki…ingawa Joakim aliacha kabisa kunifuata fuata na Jaka hakutaka kabisa kuendelea na ugomvi wowote na Joakim wala marafiki zake.” Moze alimalizia.
Yule askari alimtazama kwa muda.
“Baada ya kutoka hospitali Jaka hakuongelea kabisa kuhusu kulipiza kisasi juu ya kipigo alichopewa na marafiki wa Joakim?”
“Hapana.”
“Una hakika?”
“Nina hakika afande…kwa sababu pamoja na mimi kumtaka asifanye hivyo, mama yake pia alimuasa kuhusu jambo hilo.”
Muda wote huu yule askari alikuwa akiandika kwenye daftari alilokuwa nalo pale mezani.
“Hivi ndivyo ulivyojibu maswali niliyokuuliza?” Alimuuliza huku akimsukumia lile daftari.
Moze alilichukua na kuanza kusoma. Aligundua kuwa maswali yote aliyoulizwa yalikuwa yametayarishwa mapema na chini ya kila swali yule askari aliandika jinsi yeye alivyojibu. Alisoma kwa makini, swali kwa jibu, mstari kwa mstari, neno kwa neno.
“Ndiyo. Ndivyo nilivyojibu…sasa naomba nielezwe ni kwa nini nimelazimika kupitia mambo yote haya hapa kituoni?” Moze alimjibu na kumuuliza.
“ Naomba usaini hapo chini.”
Moze alisita kidogo.
Kwa nini asaini?
Yule askari aliuona wasiwasi wake, akamwambia, “Hiyo ni kwa ajili ya kuthibitisha kuwa ni kweli wewe mwenyewe ndiye uliyetoa majibu hayo na kwamba hakiongezewi kitu chochote zaidi ya hapo.”
Moze alisaini kwenye ile karatasi kisha akamtazama yule askari.
“Kwa hiyo sielezwi ni kwa nini nimetolewa darasani na kuja kuulizwa maswali haya hapa kituoni? Jaka amekutwa na nini?” Alimuuliza huku akiwa amemkazia macho makavu.
“Sasa unaweza kwenda Bi. Moze…lakini iwapo ungependa kujua, ni kwamba mtu uliyemjua kama Joakim Mwaga amekutwa akiwa ameuawa muda mfupi uliopita juu ya jengo la bweni namba tano…”
Yale maneno yalimshukia kama pigo la nyundo nzito kichwani.
“Joakim ameuawa!?” Alimaka kwa mshituko huku akimkodolea macho yule askari, akili ikimzunguka.
“Oh, Yes…jamaa marehemu tayari.” Askari alimjbu kama kwamba lilikuwa ni jambo la kawaida tu. Moze alibaki kinywa wazi.
Masikini Joakim.
Alikumbuka siku ile alipomfuata chumbani kwake na kumkemea juu ya tabia yake mbaya wakati Jaka alipokuwa amelazwa hospitali. Alikumbuka jinsi Joakim alivyoumia wakati alipomtamkia kuwa yeye alikuwa hampendi hata akimuua Jaka…na jinsi alimuomba msamaha kwa yote aliyoyafanya na kuahidi kutowabughudhi tena yeye na mpenzi wake…na kweli masikini, hakuwabughudhi tena.
Sasa ni nani tena atakayetaka kumuua Joakim, na kwa nini?
Mawazo hayo yalipita kwa kasi sana kichwani mwake. Na hapo wazo jingine lilimjia.
Kwa nini polisi waje wamuulize yeye kuhusu Joakim…na Jaka…?
Aliinua uso wake na kumtazama yule askari kwa macho makali huku uso wake akiwa ameukunja, utambuzi mbaya ukimshukia kichwani mwake.
“Sasa…sasa…kwani Jaka anahusika vipi na swala hilo?”
“Yeye ndiye anayetuhumiwa kwa mauaji hayo.” Yule askari alimjibu taratibu.
“What? Jaka…?” Moze alimaka, kisha akafoka kwa sauti ya juu zaidi, “Haiwezekani! Haiwez…”
“Unaweza kwenda Bi. Moze..maelezo yako yote kuhusiana na swala hili yako kwenye maandishi haya, kwa hiyo lolote utakalosema sasa halina uzito wowote…”
“Ah, sasa…Jaka yuko wapi? Nataka kumuona…haiwezekani awe amefanya hivyo…anasingiziwa tu!”
“Mnh! Anasingiziwa wakati amekutwa eneo la tukio, akijaribu kukimbia kutoka mahala ambapo amrehemu amekutwa?”
“Hah!”
“Ndiyo hivyo bibie, kama ulikuwa unagonganisha magari basi sasa matokeo ndio hayo…kijana kamuua mwenzake huko!”
“No! Haiwezekani bwana…! Alikutwaje eneo la tukio wewe? Muongo mkubwa!” Moze alimjia juu yule askari.
“Shika adabu yako bibie! Usitake nikutose ndani na wewe hapa saa hizi! Ondoka hapa, na usicheze mbali maana huenda ukahitajika tena kwa ushahidi mahakamani!” Askari naye alimjia juu.
“Yu-wapi Jaka sasa, eeenh? Yu-wapi? Nataka kumuona kabla sijaondoka…niongee naye! Anihakikishie mwenyewe kuwa…”
“Yuko chini ya ulinzi kwa sasa, na wewe nimekwambia unaweza kwenda zako. Ukitaka kumuona fika hapo kaunta uombe kuonana naye!” Jamaa alimjibu huku akiondoka na lile daftari lake,akapotelea ndani zaidi ya kile kituo cha polisi.
Moze alichanganyikiwa.
Alitoka nje ya kile kituo cha polisi bila ya kujielewa na kuelekea kituo cha basi huku akitokwa na machozi. Mawazo yaliyomkabili kichwani mwake yalikuwa ni mazito sana.
Jaka ameua!
Amemuua Joakim!
Inawezekana kweli?
Na hilo la kukutwa eneo la tukio linakuwaje?
Yaani kumbe aliponiambia kuwa atanipatia zawadi ya siku yangu ya kuzaliwa ambayo sitaisahau maisha…alikuwa anamaanisha zawadi ya kumuua Joakim? Zawadi ya kuniulia mtu? Inawezekana kweli? Nani aliyemwambia kuwa mimi nataka Joakim afe? Yaani kweli Jaka atakuwa ameona kuwa hiyo ndiyo zawadi inayonistahili? Leo hii, siku yangu ya kuzaliwa ndio ameamua kumuua mwenzake?
Aaah, hii haiwezekani kabisa!
Jaka hawezi kufanya ujinga kama huu…ni kweli kuwa alikuwa hampendi Joakim, lakini sio kwa kiasi cha kufikia kutaka kumuua…
Oh! Mungu wangu! Kama ni kweli Jaka atakuwa amemuua Joakim, Mungu wangu, ni jinsi gani nitakavyomchukia! Siwezi kuwa na mapenzi naye tena maishani mwangu…!
Ghafla alisimama. Aligeuja na kuanza kurudi kule kituoni. Alienda moja kwa moja hadi kaunta na kuomba kuonana na Jaka.
“Kwa leo huwezi kumuona dada..labda kesho.” Yule askari wa akaunta alimjibu. Moze alishangaa na kuchanganyikiwa.
“Kwa nini?”
“Hii ni kesi ya mauaji bibie unajua hiyo? Huyo mtu unayetaka kumuona kaua mtu, na hilo sio jambo dogo. Kwa leo hii atakuwa na kazi kubwa ya kujibu maswali huko ndani, sio rahisi kwa mtu yeyote kumuona…we’ bora uje kesho tu.”
Moze aliondoka huku akibubujikwa na machozi kama mtoto mdogo.

__________________

ITAENDELEA

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment