Konstebo Nguzu Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
*********************************************************************************
Simulizi: Konstebo Nguzu
Sehemu ya Nne (4)
ILIKUWA safari iliyojaa katika kichwa chake ghafla baada ya vita ile ya usiku iliyoondoka na uhai wa watu watatu ambapo mmoja kati yao alikuwa ni kiongozi wao kwa mujibu wa maelezo yao.
Martin Nguzu ambaye sasa hakuwa akiushangaa uwezo wake wa kukabiliana na maadui alikuwa amewaangusha wengine watatu huku akifanikiwa kuwapokonya bunduki tatu pamoja na risasi za kutosha kabisa.
Hakutaka kulala baada ya kuhakikisha ameitelekeza ile miili mbali na ngome ya mzee Majenga. Alimwamsha mzee Majenga na kumweleza kwa ufupi juu ya kilichotokea.
Tofauti na matarajio yake kuwa taarifa ile itamtisha sana Majenga, hii ilikuwa kinyume. Mzee Majenga akatokwa na kicheko kidogo kisha akampigapiga kifuani Martin Nguzu na kumwita kwa jina la babu yake.
“Ngengekuzenza Nguzu umezaliwa upya…” Kauli ile ilimtoka na kumwacha Martin Nguzu katika pumbazo asielewe ni kitu gani bwana yule alimaanisha.
“Mimi nimezeeka kijana wangu, niliisubiri sana hii vita kwa muda mrefu lakini imekuja nikiwa mzee tayari. Nenda ukapambane hii ni vita yako na inakuhusu. Nakuachia haya maandishi niliyoyaandika bila kuongeza wala kupunguza neno kutoka katika kinywa cha hayati babu yako anayeishi sasa katika nafsi yako. Hakikisha unayamaliza yote kabla haujaivaa hiyo vita…… mimi nitakuwa salama kabisa na tutakutana nikiwa hai, na hata nikifariki ni kwa sababu ya uzee tu…” Aliongea kwa ujasiri mkuu. Kisha akachechemea hadi ndani na kuchukua makaratasi yaliyoandikwa kwa kalamu akamkabidhi Martin.
“Nilikuwa napenda sana kuandika na babu yako alikuwa anapenda sana kunisimulia, nadhani ni maneno hayo kwa ufupi yatakupa jawabu nilikutana vipi na babu yako.” Majenga alitoa kauli ile na Martin akaipokea lakini alikuwa na swali la ziada.
“Niliokoka vipi katika ule moto jijini Dar es salaam?”
“Mzee wako asingeweza kukuacha uangamie. Wazee wa zamani hawakuwa wa kawaida, akinuia jambo linakuwa kama lilivyo, nadhani ni kutokana na kutenda dhambi chache nd’o maana Mungu alikuwa akiwasikiliza.” Alifafanua na kuzidi kumvuruga Martin.
Akagundua mvurugano ule, akaongezea “Kasome haya yote kabla hujaamua wapi pa kuanzia”
Maongezi yakaishia hapo.
MAANDISHI YA NGENGEKUZENZA.
Ubaya ni kwamba wakati wa ukoloni, sisi watu wa rangi nyeusi hatukuishia tu kunyanyaswa na ngozi nyeupe katika uhai wetu, hata ulipokuja ustaarabu wa kuhifadhi maiti zetu sisi tuliwekwa katika kundi la mbwa koko aliyefia jaani baada ya kukabwa na mfupa aliodhani ni mnofu.
Ukipata bahati sana unafukiwa, ila ni waafrika wachache waliokuwa na bahati, wengi tulitunukiwa nuksi.
Ukiwa na nuksi unaachwa hapohapo ulipofia ama unasogezwa kidogo porini, ukawe chakula kwa wanyama wenye tabia ya uvivu katika suala la kuwinda na ndege wanaoona sifa kudonoa donoa.
Hata babu yangu alikuwa na nuksi vilevile baada ya kufariki alitupwa, akaipata bahati akiwa maiti tayari waafrika kadhaa wakamfukia.
Baada ya kuupata uhuru wetu nikawa naitembelea ile sehemu niliyoaminishwa kuwa babu yangu alifukiwa pale, pakawekwa alama nami nikawa naenda kumsalimia na kuzungumza naye bila kujali ananisikia ama la!
Sasa yule mwanahizaya baada ya kuona haitoshi kumchukua kiharamia mke wangu na kuniacha katika jitimai, akaona hata! hii haitoshi huyu bwege bado anapata raha. Akaanza kuniandama kivingine, najua aliwatuma mashushu wake waliokiamini na kukiabudu chama chao kuliko Mungu wa mbinguni na miungu ya porini.
Hawa wakamfikishia habari kuwa ninayo furaha nyingine, furaha ya kuzungumza na babu yangu makaburini.
Ikapita ajenda katika siku nisiyoijua na baadaye ikawa ni amri bila kutahadhalishwa.
Eneo lile lilipaswa kupandwa miti, mara lilitakiwa kupita barabara.
Sikuelewa hata kidogo, na hakuna aliyesubiri nielewe.
Kwani Ngengekuzenza nani mpaka aelewe?
Lile nililoamini kuwa ni kaburi likavunjwa na huyu mkoloni mshenzi mwenye rangi kama yangu huku akiiga miondoko ya wazungu na afro yake kichwani akiipaka kalikiti na kuwa laini kama nywele za mkoloni.
Lugha yake pia ilifanana na yao.
Poor Joseph Kazeze!
Kama ni kunipiga, hapa alinipiga na mjeledi wa chuma nikaangukia pua huku mikono yangu ikishika makaa ya moto.
Huyu mjinga aliniweza hakika!
Uchungu wangu ule nikamshirikisha mwanangu Salama nikamweleza kuwa Jose anataka kuvuka mipaka ambayo ameivuka tayari, yaani sielewi anachotaka.
Salama alinisihi niachane naye, nikaona hajui uchungu ninaoupitia kwa kupokonywa mke na kisha hapohapo nikapokonywa furaha yangu.
Babu yangu!
“Salama, nikiachana naye akagundua nina furaha kuwa na wewe atakuchukua na wewe pia….” nilimwambia Salama. Wazo hili likamkuna na kuiona hatari ya waziwazi.
“Sasa utamfanya nini?”
“Yule ni mjinga tu kwangu, nataka nimfanyie yale mambo ambayo wajanja huwafanyia wajinga wanaodhani pesa nd’o ujanja.” nilimweleza huku nikiona wazi kuwa hanielewi.
“Unataka upigane naye?” aliniuliza.
“Nikipigana naye wote tutakuwa levo ileile ya ujinga, nataka nimpige ili tuunde daraja kati ya nani mjinga na nani mjanja.”
“Lakini baba, huyu ana pesa na cheo atakusumbua sana. Yaani nina uhakika hautafikia hata nusu ya azma yako.”
“Kwanini unasema una uhakika.” nilimuuliza salama.
“Si kila kitu kipo wazi, ana pesa na vyeo na zaidi ana kundi kubwa la watu linalomzunguka.”
“Nd’o maana unasema ni hakika?”
“Ndio baba”
“Sikiliza mwanangu Salama na uliweke hili milele katika maisha yako, hapa duniani kuna kitu kimoja tu nd’o cha uhakika vingine vyote si vya uhakika. KIFO pekee ndo jambo la uhakika, kila mtu atakufa hii haina mjadala. Ujiue, unyweshwe sumu, ugongwe na gari ama hata ukilala usiamke. Vyote vina maana moja tu ya uhakika…. asije akakudanganya mtu kuwa jambo hili ni uhakika… anakulaghai na wewe unayemsikiliza na kumkubalia unakuwa upande wa mjinga. Sipendi uwe mjinga siku moja….” Nilimsomea mambo yale. Yakamuingia na kumpa ujasiri naye akanibariki katika uamuzi wangu na hiyo ilikuwa ni mnamo mwaka elfu tisa mia themanini na tatu ama nne kama sijasahau.
Sijui itakuwaje miaka ya huko mbele lakini enzi zetu hizi hapakuwa na ulinzi wa kutosha kwa viongozi, ulinzi huo tuliusikia tu na kuuona walipokuja viongozi kutoa nje, Mwalimu Julius Nyerere alihamasisha sera za kuishi kijamaa, nasi tukaamua kuishi kama ndugu.
Hapakuwa na wa kumpinga kirahisi mwalimu. Ukitaka kumpinga sisi tunakwambia nenda ukapambane kuileta Tanganyika huru ndipo ujilinganishe na mtaalamu huyu.
Hivyo tuliishi kijamaa sana, halikuwa jambo la ajabu kukutana na mwalimu Nyerere barabarani na kusalimiana naye kwa kushikana mikono. Sasa vipi kuhusu mjinga huyu anayeitwa Joseph Kazeze?
Sidhani kama kwa miaka yenu huko mbeleni itakuwa hivi. Nahisi hata balozi naye atatafuta ulinzi…
Nilikueleza awali kuwa tangu nilipokuwa mtoto nilikuwa nina uwezo mkubwa sana darasani, hata akili yangu haikuwa ndogo katika kufikiri.
Nikaamua kuitumia akili yangu kumwonyesha yule bwana nini maana ya mwanaume kutoa machozi.
Kwakweli nilimkosesha amani!
Kwanza nilifurahia kile kitendo cha mwalimu Nyerere kutowafukuza wazungu baada ya kutupatia uhuru, hivyo upatikanaji wa silaha hadi miaka ya themanini bado ulikuwa ni mwepesi sana, unaweza kuipata bunduki hata kwa kubadilishana na gunia la mahindi pekee.
Zilikuwa zimezagaa.
Nami nikajipatia bunduki yangu, uzuri nilipitia jeshini hivyo sikuhitaji kufundishwa lolote.
Nikamuaga mwanangu kuwa naanzisha mapambano rasmi.
Sikuwahi kuua ila nilijeruhi sana.
Nilianza na baba yake mzazi, akiwa katika mizunguko yake. Nikamteka na kumpiga kipigo cha mbwa mwizi, akavunjika mkono.
Sikumtumia salamu Jose Kazeze kama ni mimi ili aendelee kuhadaika.
Akafuata mdogo wake, huyu nilimfungia safari hadi Morogoro, nikamkamata na kumfunza adabu asiweze hata kuiona sura yangu.
Jose Kazeze kitu alichosahau ni kwamba sisi tulikuwa marafiki na nilimfahamu vyema yeye na familia yake.
Niliendelea kumpa presha bwana yule kwa kufikia hatua ya kuvamia kwake nikarusha risasi zikavunja vioo vya nyumba aliyokuwa akiishi lakini sikumdhuru mtu na sikutaka kumdhuru.
Uwezo wangu katika kupanga matukio ulianza kunishangaza hata mimi, kila nikilala na kuamka nawaza pigo jingine.
Jose akaanza kukonda!
Mara akaachana na yule mwanamke aliyenipokonya.
Nami sikurudiana naye mjinga yule aliyekosa hata nukta ya akili.
Nilikuwa nina hasira kali.
Baadaye baba yake alifariki, kwa magonjwa mengine sijui kama na kile kipigo kilichangia.
Sikujali!
Siku mbili baada ya kuzikwa nikaenda makaburini, huku nikaweka bomu nililolipata kwa bei nzuri tu.
Likafanya mlipuko uliotikisa nchi.
Hakuna kilichobaki zaidi ya jeneza kusambaratika huku na kule.
Hili lilikuwa pigo kubwa zaidi, wanandugu wakalundikana nyumbani kwa Jose Kazeze kujadiliana nini kinaendelea.
Nikavamia na huko na kurusha bomu jingine katika choo kilichokuwa mbali kidogo na nyumba na hii ni baada ya kuhakikisha hapakuwa na mtu ndani yake.
Mparangano uliojitokeza nilijikuta nacheka mwenyewe.
Amakweli mtenda akitendwa….
Jose akazidi kuzorota kiafya.
Ni hapa ndipo nikaamua kumweleza bayana ili kama ni kufa kwa mshtuko afe tu, who cares?
Hakufa!
Ila alipagawa vibaya mno, na hapo ndipo ikaanzishwa oparesheni ya Ngengekuzenza Nguzu anasakwa auwawe.
Kisa ni jambazi, yakaundwa matukio ya kushangaza kunihusu mimi na hapo nikaanza kusakwa rasmi.
Nilijua kuwa hali ni mbaya, nikaraejea kwa mwanangu… usiku wa mwisho kumwona mwanangu.
Akanieleza kuwa yu mjamzito, nikamweleza kuhusu kinachoandikwa na magazeti ya serikali huku nikimweleza kuwa moyo wangu u radhi kuwa nimemuweza yule bwana.
Zaidi ya hayo nikamsihi kuwa iwapo atazaa mtoto wa kiume basi amwite Nguzu!
Tulikumbatiana huku sote tukishindwa kuyazuia machozi.
Nikaondoka na kuja kwako Majenga unihifadhi nikusimulie ya kuandika kama ulivyohitaji wewe kijana wangu.
Na nimejitahidi sana kukusimulia.
Maandishi yale yaliacha nafasi kubwa kisha ikafuata aya ambayo mwandishi wake alikuwa ni Majenga.
Mnamo mwaka 1988 mwezi wa kumi na moja mzee Ngengekuzenza mwenye msongo wa mawazo kwa kuishi maisha ya mashaka kila kukicha aliniaga kuwa anakwenda msalani, ilikuwa majira ya usiku. Hakurejea mapema nikalazimika kutoka pamoja na mbwa kwenda kumtafuta.
Nilimtafuta sana hadi pambazuko likanikuta nikiwa namtafuta, mbwa asiyechoka ndiye alinihimiza kumsaka mzee wangu nimpendaye.
Hatimaye nikaufikia mti ambao alikuwa amejitia kitanzi.
Nasikitika kuwa sikuwahi kukiri kuwa ninamfahamu mzee yule kwa sababu za kiusalama, alikuwa anasakwa sana na jeshi la polisi kama jambazi sugu.
Niliporejea ndani nikakutana na karatasi katika kitanda alichokuwa akilalia. Haikuwa na maneno mengi sana aliniandikia kama nilivyokuwa nimefanya tayari.
“Umenihifadhi kwa moyo wote wa upendo, wewe ni kijana wangu nikupendaye. Ninaomba uendelee kunitunzia maneno yangu….. utawapatia wajukuu zangu ili wajifunze kuwa babu yao hakuwahi kuwa mtu dhaifu hata kama nilionewa, babu yao sikuwahi kuwa jambazi hata kama watayaona maandishi hayo, pia kwa imani yangu kuu naamini kuwa sijafa kirahisi rahisi. Mizimu ya mababu zangu waliouwawa kifedhuli utumwani imeniambia kuwa najipumzisha ila ipo siku nitazaliwa na nitazaliwa katika damu yangu mwenyewe. Ninapumzika Majenga ila nikizaliwa tena usishangae. Naamini mizimu hii kulikoni dini walizotuletea wakoloni, dini zilizotuongopea kuwa Mungu ni mzungu, zikaenda mbali na kusema kuwa Mungu anaishi katika majengo yao waliyoyajenga.
Dini za kishenzi zilizonipatia jina la kishenzi, Frolian na kunipokonya jina la kishujaa kutoka kwa babu yangu.
Dini zilizotulaghai kuwa kila asemacho yule mzee mweupe anayesimama mbele yetu basi ni sawa, anatuona tunateseka na anasema tumwachie Mungu, nasi tukijaribu kupambana anasema tena sisi ni watu wabaya sana na hatufai kuwekwa kundi la wanadamu.
Dini zao hazijaniambia kuwa siku moja nitarejea, lakini wazee wangu ambao tuliwalilia njaa wakatusikia katika miti, tuliwaomba kila kitu na walikuwa wakweli.
Wazee hawahawa wamesema nami, acha nipumzike ila ipo siku nitarejea na sitakuwa wa kujificha tena.
Kwaheri mjukuu wangu!”
Kisha akwakeka hitimisho Majenga kwa wino mzito.
“MNAMO MWAKA 1988 BABU YETU Ngengekuzenza aliaga dunia na ni mwaka huohuo mwanaye Salama alipata kujifungua… yule mtoto akaitwa NGUZU”
NGUZU alibaini kuwa alikuwa anatetemeka baada ya kuimaliza sentensi ile ya mwisho.
Akaituliza akili yake na kutaka kumaizi ni kitu gani kimempa majibu katika maandishi yake.
Kwanza, aliamini katika mizimu na kimyakimya akakiri kuwa mzimu wa babu yake ungali ndani yake.
Pili, Jose kazeze yawezekana aliweka kisasi cha kudumu, baada ya familia yake kunyanyaswa akaisambaza ile chuki kwa wajukuu na vitukuu kama wapo.
Hivyo yawezekana mmoja kati ya kitukuu ama mjukuu alikuwa akilishambulia jina la Nguzu popote atakapokutana nalo hivyo naye alikuwa ameshambuliwa.
Mambo haya mawili yakamwacha katika sintyofahamu nyingine mpya.
Akajaribu kulitaja jina la Inspekta Kobo…… akatazama kisa chake hadi kuja kumchomea ndani ya nyumba yake.
Hili akaliweka katika mabano, yawezekana kuna watu wengine walihusika katika hili jambo.
Akayakumbuka maneno ya yule kiongozi wa waliotumwa kumkamata Majenga.
Akakumbuka kuwa yule bwana ndiye aliyemueleza juu ya Inspekta Kobo kuwa yungali rumande akituhumiwa kwa kesi mbaya kabisa inayoweza kumtokomeza uraiani, lakini alimtajia jina la kiongozi wao mkuu ambaye hata wao hawakuwahi kumwona hapo kabla.
Zumbe!
Nguzu akafuatilia katika mitandao mbalimbali kutazama huyu mtu ni nani katika serikali ili ajue je? ana uhusiano na ukoo wa Kazeze? na kama hana uhusiano ni kitu gani anataka?
Kichwa kikamuuma alipojikuta anayo orodha kubwa sana katika kichwa chake.
Na kadri basi lilivyoikaribia ardhi ya jijini Dar es salaam,mara moyo wa Nguzu ukapiga kwa nguvu sana.
Kuna kitu alikuwa amekisahau kwa muda mrefu.
Koplo Zubeda!
Mungu wangu! Akahamanika kutokana na hali ile ambayo ilimtokea naye asijue ni kwanini imekuwa hivyo ghafla wakati analikaribia jiji na si wakati yupo mbali?
MAJIRA YA saa saba usiku Martin Nguzu alikuwa akirandaranda katika kona mbalimbali za jiji la Dar es salaam kusaka hoteli ambayo angeweza kulala kama si kupumzika mpaka patakapokucha na kuutaza uelekeo ambao anapaswa kuanza nao.
Hakuwa na mashaka yoyote ya kuufichaficha uso wake, habari zake zilikuwa zimesambaa lakini si picha yake.
Wasambaze picha yake kwa cheo chake cha u-konstebo kwani hawana mambo mengine ya kuandika.
Alifanikiwa kupata hoteli ya bei ya wastani, akafanya malipo na kujiandikisha kwa jina batili.
Akakabidhiwa chumba.
Alipoingia na kuufunga mlango akaiwasha taa, akakiona kioo kikubwa jirani na mlango.
Akajitazama jinsi alivyokuwa, kimaumbile alijiona yungali vilevile lakini ndani ya mwili wake alijihisi yupo ngangali sana tofauti na awali.
Bila kutarajia akajikuta akimuwaza tena Zubeda.
Akiwa palepale mkabala na kioo alifikiria ule ukaribu wao jinsi ulivyokuwa ukimpa raha ya kipekee, raha iliyomfanya ajikute akimwonea wivu inspekta ambaye alisemekana kummiliki Zubeda, kuna kipindi alikuwa akitamani hata kumdhuru yule inspekta ambaye ndiye kikwazo pekee kilichokuwa kati yake na penzi la uhuru baina yake na Zubeda.
Nguzu alikuwa akitamani kumtambulisha Zubeda kwa marafiki zake kama shemeji yao, ukiachana na kuufurahisha moyo wake na pia kuuweka wazi udhibiti wake dhidi ya Zubeda, Sifa pia kilikuwa ni kigezo cha kutamani uhuru ule.
Nani ambaye angeacha kumsifia kuwa anamiliki ‘mtoto mkali’
Zubeda alikuwa mzuri, urembo wake haukufichika hata alipojitundika katika gwanda zake za kazini.
Askari wengi walikiri kuwa binti huyu alikuwa wa aina yake, na hii ni sifa waliyoitoa huku akiwa katika gwanda zake.
Nguzu alikuwa amepata fursa ya kuziondoa zile gwanda kisha akamvesha kanga moja nyepesi mwanadada huyu na kisha kuambatana naye maliwatoni.
Macho yake mawili yenye nguvu yakifanikiwa kutazamana ana kwa ana na mzigo wa matiti ambayo yalikuwa yamevuka kidogo ule muda maarufu wa ‘saa sita’ lakini hayakuwa mbali sana kufananishwa na muda huo hasahasa yakipewa msaada mdogo wa sidiria.
Macho ya Zubeda yangeuamuru mwili wa mwanaume yeyote atakayemtilia maanani kujikuta ukisisimka na donge la hamu kumshika.
Macho yake makali angali akiwa kazini yalikuwa yanatepeta wakiwa wawili na Nguzu na kumfanya Nguzu ashangazwe na hali hii.
“Huyu mtu aliupata vipi ukoplo wa polisi? Kwa macho haya tepevu?” Haya ni baadhi ya maswali aliyojiuliza kabla hajachoshwa na mikono laini ya Zubeda. Mikono ambayo hakuamini hata kama inao uwezo wa kuzishika pingu na kumlazimisha mtuhumiwa azivae.
Ajabu Zubeda alisifika kwa kuwahenyesha watuhumiwa.
Kuhenyesha watuhumiwa??
Ilishangaza!
Lakini Nguzu naye akajikuta anahenya kupambana na msisimko uliokuwa ukimkumba kila mara mikono ile ilipomgusa.
Na hapo akakiri kuwa hata yeye ni mtuhumiwa pia na alikuwa anahenyeshwa wawapo chumbani wawili.
Kweli Zubeda ni kiboko!
Kumbukumbu hizi zikajirejesha nyuma kwa kasi ya ajabu, Nguzu akakumbuka jinsi alivyokutana na Zubeda jijini Mwanza.
Akaukumbuka utambulisho wake wa kijivuni dhidi ya Zubeda ambaye hakuwa na cheo chochote wakati ule na hata jeshini alikuwa hapajui.
“Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu!”
Tabasamu likamponyoka na kujikuta akipiga saluti ya kihuni.
Akakiendea kitanda na kujirusha hapo kwa fujo zote.
Kitanda kikahimili kishindo!
Na hapo kikaanza kuufyonza ule uchovu wote na kuugeuza kuwa raha ya kipekee.
Usingizi ukampitia…..
MAHAKAMA kuu ya Tanzania ilikuwa imesheheni haswa, maaskari walikuwa wanafanya kazi ya ziada kuwazuia watu waliozidi kumiminika pale mahakamani.
Punde ikasikika amri ya kumaanisha kuwa jaji na baraza zima la wazee lilikuwa linaingia pale mahakamani.
Kimya kikuu kikatanda ikiwa ni ishara ya kuheshimu mahakama.
Akiwa na pingu miguuni na mikononi kisha pingu hizo za miguu na mikono zikaunganishwa na mnyororo mgumu aliongozwa hadi katika kizimba.
Alipofikishwa kizimbani akafunguliwa zile pingu, akaingia akiwa huru kizimba kikafungwa.
Macho yake yaliyozama ndani na kuzidi kuonekana kuwa ni makubwa yaligeuka huku na kule, safari hii hakuwa na uoga tena alikuwa ameikubali hali halisi.
Macho yake yakatua katika kiti alichokuwa ameketi mama yake aliyepooza upande mmoja.
Licha ya kwamba alikuwa amelia sana hadi machozi kumkauka aliweza kuhisi machozi ya moyoni yakimlowanisha.
Wakagonganisha macho yao, akamwona mama yake akizungumza maneno yasiyoweza kusikika hata kidogo huku machozi yakimtoka kwa wingi.
Aliamini kuwa mama yake alikuwa akimwombea kwa Mungu ili kesi ile ipate muujiza wa yeye kushinda.
Uchungu uliomshika alitamani angepewa walau nafasi moja tu ya upendeleo naweze kuzungumza na mama yake, amkumbatie na kumfariji.
Jicho lile likaendelea kubarizi pale ndani ili aweze kuwaona watu wengine ambao huenda anawajua.
“Marafiki hawana maana!” Alijisemea baada ya kuhakikisha kuwa hakuna rafiki yake hata mmoja aliyefika mahakamani hapo.
“Kwa hiyo wameogopa kuwa nitawachoma ama?” alijiuliza.
Hakupata muda wa kujiuliza zaidi wakati jicho lake likitua katika kiti kingine upande wa kushoto.
Macho yakagongana tena na huyu mkaaji wa kiti hicho.
Zubeda!
Walitazamana kwa sekunde kadhaa kabla Martin Nguzu hajakwepesha macho yake.
Hakutaka kumwangalia binti huyu aliyekonda sana na kuonekana wazi alikuwa akitawaliwa na uchungu mkubwa.
Alipomaliza kuzungusha macho yake akamwona jaji akitoa ruhusa ya mwendesha mashtaka kumuuliza maswali mshtakiwa.
Maswali yalikuwa magumu sana, akayajibu kadri alivyoweza. Mengi alikuwa ameyasahau kabisa.
Miaka sita mahabusu bila kesi kusikilizwa, angekumbuka nini sasa.
Wakati wote huu alikuwa akishangaa kumwona wakili kwa ajili ya kumtetea.
“Lakini nilimkataza mama kuhangaika kuweka wakili.” Martin Nguzu alijiuliza huku akitikisa kichwa chake kama namna ya kusikitika.
Akakiri kuwa katika ulimwengu huu mzazi ni mzazi lakini mama ni bora zaidi kuliko baba. Mama anaumia sana akimwona mwanaye katika wakati mgumu wakati baba huhesabu ugumu ule kama changamoto na kusema ‘kijana wangu amekua na atatatua changamoto hizo’ mama huinama chini na kusema ‘mtoto wangu anateseka’
Ni hii tofauti aliikiri katika kesi yake hii. Mama mzazi aliyepooza mwili alikuwa mahakamani kushuhudia kile kiumbe alichokileta duniani baada ya suluba ya miezi tisa, kisha kuhangaika katika malezi.
Hakujali kupooza kwake, hakujali kuwa yawezekana mwanaye akahukumiwa kifungo cha maisha gerezani ama kunyongwa kabisa kwa jinsi kesi ilivyokuwa.
Alichokifuata pale ni kumwona mwanaye kwa jicho lake mwenyewe. Kama alivyomuona wakati amemzaa, alihitaji kumwona tena katika ugumu huu, ugumu wa kukondeana kwa sababu ya mateso na lishe duni, ugumu wa kuwaza kufia jela.
Mama alibaki kuwa shuhuda wa mwisho!
Ni nani kama mama kwani?
Wakili alisimama na kutema vifungu vya sheria ili kumnusuru Martin Nguzu kutoka katika janga lile.
Alionekana kuijua vyema sheria lakini upande wa mashtaka ulionekana kuwa imara zaidi, sura nyingi zilitawaliwa na hasira kali. Hasira hii iliboreshwa zaidi na mavazi yao, walifanania na kundi la mafia ambalo limemshukia mwenzao baada ya kuwasaliti na sasa wanataka kumpa adhabu ya kumzika huku akiwa hai akaupiganie uhai wake akiwa chini ya ardhi.
Nguzu akamgeukia jaji ambaye alionekana mwingi wa chuki kuliko haki.
Jaji alipounyanyua uso wake Nguzu akajikuta anagundua kitu kipya kabisa. Ile sura ya jaji haikuwa njgeni machoni mwake hata kidogo.
Hofu ikamjaa ya kutotendewa haki juu ya kesi ile ambayo alitambua wazi kuwa ni vile tu amekosa mashahidi lakini haikuwa ikimuhusu kabisa na alitakiwa kuwa mtu huru.
Jaji yule akaanza kusoma vipengele kimoja baada ya kingine kwa utulivu sana.
Ni kama aliyeelekea kutoa hukumu, hii ilimshangaza sana Martin.
Hukumu inatoka vipi kirejereja hivi bila kesi ile kupewa muda wa baraza la wazee kuipitia na kutoa mitazamo yao.
Jaji alisoma taratibu huku kila mahali akijaribu kumbana Nguzu.
Na hatimaye kauli ikamtoka.
“UTANYONGWA MPAKA UFE”
Mungu wangu! Nguzu akamwona mama yake mzazi akitua chini kama mzigo, watu wakakimbilia alipokuwa ili kumwokoa.
Palepale akawaona askari wanne wenye ghadhabu wakisogea katika kile kizimba na pingu kwa ajiri ya kumchukua na kumpeleka katika mahabusu ya mahakama kabla hawajampeleka gereza la Ukonga.
Gereza pekee ambalo washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa mpaka wafe huhifadhiwa huko mpaka siku ya hukumu yao.
Kuwaona watu wale kukamchanganya Nguzu, na jaji alikuwa amefunga mjadala tayari.
Nguzu akaona haiwezekani, akawahi kujirusha akaidaka silaha ya askari mmoja na mara moja akaielekeza alipokuwa yule jaji.
Jaji akakodoa macho yake alipojikuta anatazama ana kwa ana na bunduki iliyoshikwa na mtu asiyekuwa na masihara hata chembe.
Akafyatua risasi kiufundi lakini yule jaji akawahi kujificha chini ya meza.
Na hapohapo Nguzu akaisikia sauti ya kike ikimpigia kelele kumtahadhalisha.
Ilikuwa sauti ya Zubeda!
Akageuka na kukuta amechelewa tayari, bunduki nyingine ilikuwa inaelekea kufyatuliwa ili yeye adhurike.
Ilielekezwa kifuani pake.
Akajikuta anapiga mayowe ya hofu huku akikiziba kifua chake kwa mikono yake.
Bunduki ikacheua.
“Mamaaaa nakufaaa!” alipiga kelele kubwa sana na hapo akajikuta akibiringita kama chaguo lake la mwisho.
Akashangaa kujikuta anaelea hewani. Akaanza kutapatapa akirusha miguu huku na kule.
Hatimaye akasimama wima tena.
Hakuwa mahakamani! alikuwa amesimama katika kitanda huku akiwa amejifumbata mikono yake katika kifua chake.
Ndoto!
Jasho lilikuwa linamwagika vibaya mno, bado moyo ulikuwa unapiga kama unaotaka kutoka nje ya kifua chake.
Alikuja kutulia baada ya dakika kumi na hapo ndipo akakiri kuwa ile ilikuwa ni ndoto lakini ndoto ya ajabu sana.
“Yule jaji yule! Yule jaji ni nani!? Jaji, jaji….” Nguzu alibaki kusema kama ambaye anajaribu kulazimisha kung’amua vitu kutoka katika ile ndoto ya ajabu ambayo hakutaka kuamini eti ilikuwa ndoto ya kawaida.
Alihisi yule ni babu yake anasema naye. Hofu ikatanda alipokumbuka kuwa alihukumiwa kunyongwa katika ndoto yake.
Hofu ya kifo ikamjaa, akaanza kuhofia uwepo wake katika jiji la Dar es salaam.
Jiji ambalo ipo ile mahakama ya ndotoni na pia lile gereza wanalohifadhiwa wafungwa wa adhabu ya kunyongwa mpaka kufa.
Hiki nini? alijiuliza.
Bado hofu iliishi naye, akamkumbuka mama yake alivyokuwa akimlilia na hata alivyoanguka baada ya hukumu ile kutolewa.
Hofu ya kifo ikiwa haijaisha ikapanda hofu nyingine.
Hofu ya kumpoteza mama yake mzazi pindi atakaposhuhudia matatizo yakimpata.
Nguzu akakiri kuwa huu mpambano ulikuwa maji ya shingo kwake naye alikuwa hajui kuogelea vyema. Akaamini kuwa alikuwa anahitaji watu watakaosimama pamoja naye.
Kwa mara nyingine tena jina Zubeda likakiandama kichwa chake.
“Kwanini Zubeda?” alijikuta katika swali hili.
Hisia mbili zikaanza kupambana, mojawapo ilikuwa hisia za mapenzi. Nguzu akakiri kuwa alikuwa akihangaishwa na jina Zubeda kwa sababu tu aliwahi kumpa burudani ambayo ilikatishwa ghafla bila kufika ukingoni.
Pili alihisi kuwa anahitaji kupata msaidizi na msaidizi wa kweli katika vita hii ni koplo Zubeda.
Kujua hisia ipi ni ya kweli nd’o ukawa mtihani mzito.
“Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” Usingizi ulimkuta Nguzu akiwa katika uchambuzi hafifu wa kitabu hiki maarufu , alianza kwa kumpa kongole mwandishi Edwin Semzaba kwa kuandika kitabu hiki, kisha akahamia kwa Ngoswe na Mazoea na hadi anasinzia alikuwa amefikia mahali ambapo Mazoea ameanza kuzoeana na Ngoswe! Hii ni baada ya Ngoswe kumuhadaa kuwa atamtorosha waende wote mjini……
Alisinzia akiwa anatabasamu, bila shaka ni vile visa vya Ngoswe vilimpa tabasamu.
ASUBUHI ilimkuta konstebo Martin Nguzu katika ofisi ya gazeti mojawapo kati ya yale yaliyoandika habari ya kifo chake na kisha kusemekana aliyeandika ni ‘mwandishi wetu.
Kama ilivyomkera inspekta Kobo na kujikuta akiponyokwa na matusi ya kiitaliano, kwa Nguzu ilikuwa vilevile lakini hakuwahi hata siku moja kuota ndoto za kiitaliano.
Yeye aliponyokwa na matusi mfululizo ya kisukuma.
Lakini hakuishia kutukana tu, aliamua kupiga hatua na aliamini hatua hii inaweza kuwa ya muhimu zaidi kumfikisha katika hatua nyingine.
Akalisoma gazeti lile na kuyapata mawasiliano ya muhariri mkuu wa gazeti hilo.
“Huyu jamaa lazima anawajua waandishi wake wote, wenye majina na wasiokuwa na majina wanaojiita ‘mwandishi wetu’. Atawataja ama atakula maumivu yao…” Alizungumza konstebo wakati akizungusha macho yake huku na kule kabla hajazama ndani ya ile ofisi.
Awali alipanga kwanza kumjua sura huyu bwana na kisha ajiweke katika lindo zuri aweze kuijua gari yake.
Baada ya kujua hayo angeachana naye na kisha kumpangia siku ya shambulizi.
Alijua kuwa amezisahau taarifa zile tayari, na hata hao akina’mwandishi wetu’ walikuwa wanaendelea na maisha yao mengine.
Mambo yakaenda tofauti, Nguzu akiwa amejivesha miwani ya jua katika uso wake huku akiziachia nywele zake wazi kwa maksudi kabisa.
Hazikufanania na nywele za askari, hasahasa wa cheo cha konstebo.
Nguzu alikuwa katika hali ya utofauti.
Alianzia mapokezi na kuulizia ni wapi atampa muhariri, katibu muhtasi akauliza ikiwa ana shida binafsi ama ya kiofisi.
Maswali yao yaleyale kila siku! Nguzu alijisemea kabla hajajibu, “Shida ya kiofisi dada.”
“Ok! nyoosha moja kwa moja hadi katika ile korido kisha pinda kushoto utaiona ofisi, keti katika foleni subiri huduma.”
Nguzu akainama chini kidogo huku akijishika kifua chake kama ishara ya kushukuru.
Akatoweka!
Alimkuta bwana mmoja mwenye mvi akiwa anangoja kuingia, akaketi pembeni yake.
Bwana mwenye mvi akaanzisha soga kuhusu siasa mara ahamie katika mpira wa miguu, huku ndipo alizidi kumpoteza Nguzu.
Ushirikiano wake pekee ukawa ‘ndio’ ama kujichekesha.
Hatimaye mzee akaingia na kutoka baada ya muda mfupi.
Bila shaka muhariri hakuwa tayari kusikiliza soga nyingi kutoka kwa yule bwana.
Ikawa zamu ya Nguzu.
Hofu ikamwingia hakutambua kama yupo sahihi katika hatua ile ama ameitupa karata yake vibaya.
Akaufungua mlango na kuingia ndani huku akitambua kuwa yeyote yule anaweza kustaajabu kuhusu ile miwani lakini alifurahi kwa sababu ni watanzania wachache sana anaweza kukuona haupo sawa katika jambo fulani naye akawa kimya asikwambie badala yake anamweleza rafiki yake kisha wanacheka!
Hee! Watanzania?! Tusaidiane kujishangaa.
Kweli! hakuna aliyemuuliza.
“Karibu!” Sauti nyembamba lakini ya kiume ilimkaribisha huku mikono ikimwonyesha mahali pa kuketi.
Martin akaketi.
“Naitwa Sebastian! natokea Temeke Dar es salaam.” Alianza kujitambulisha.
Muhariri hakuonyesha kujali juu ya lile jina, Nguzu akaendelea.
Sasa akayafungua magazeti kadhaa aliyokuwa ameyashika mkononi akayatua mezani.
“Nakusikiliza bro..” Sauti ile iliyotawaliwa na kiburi cha kuwa muhariri ilizungumza.
“Nilikuwa nataka kuuliza…”
“Ulikuwa unataka ama nd’o unataka kuuliza mkuu?!” Muhariri akamuwahi Nguzu.
Nguzu akafadhaika na kuamua kutuliza akili yake, tayari alishagundua kuwa alikuwa anakosa kujiamini.
Akajipa sekunde kadhaa akaingia tena kushambulia.
“Nauliza, hizi habari ambazo anaandika mwandishi wetu, ni nani anaziandika na kwa nini asijitambulishe kwa majina yake.” Akaweka kituo.
“Samahani umeuliza ama umetoa lalamiko!” Muhariri mwenye nyodo akazungumza, sasa aliachana na kazi alizokuwa anafanya akamtazama Nguzu huku akiyabetua mabega yake.
“Nimeuliza.”
“Ni utaratibu wa kiofisi. Ukihitaji ubadilishwe utapaswa kuandika barua na kuiweka kuleee kwenye sanduku la maoni. Sijui kuna la ziada lililokutoa Temeke bwana…. bwana…” Akalisahau jina lake na kulipuuzia.
Konstebo Martin Nguzu akanywea na kujiona anazidiwa karata hivihivi mchana kweupe.
Akapaniki!
Akasimama wima, akawa anayetafuta neno la kuzungumza linakikataa kinywa linarudi kichwani.
Akaona haifai kuendelea kusimama hivyohivyo.
“Huyu aliyeandika hii habari ni nani?” Akafoka. Bado alikuwa wima.
Muhariri hakuligusa lile gazeti badala yake akainyoosha shingo yake na kuona nini anaonyeshwa.
Akakutanisha macho yake na habari juu ya kifo cha Nguzu na kuhusishwa sababu za kimapenzi na mengineyo.
Akajikuta anarudi nyuma kwa kasi, uso wake ukiitangaza wasiwasi yake.
Akaishika simu na kutaka kubofya nambari kadhaa, palepale Nguzu akauwahi ule mkono na kuugandamiza.
Kisha ili kuimarisha usalama akachomoa kisu kikubwa kutoka katika ficho lake.
“Huwa ninaua bila taarifa maalumu, sipendelei ufe hivyo. Jibu swali langu.” Hakuonekana kuonyesha mzaha.
Muhariri akalitambua hilo.
“Sijaandika mimi.”
“Mwandishi wetu ni nani?”
“Mwandishi wetu… sim… simj..”
Ngumi kali ikatua katika shingo ya muhariri.
Ilikuwa ngumi maalumu kwa ajili ya kumzuia yule mwanadamu anayependa kuongea kwa sauti ya juu, kumpunguza uwezo wa kupiga kelele na kujikuta akinong’ona.
Nguzu alimwacha akihangaika pale akauendea mlango na kuufunga!
“Simu yako ya mkononi…” Alisema kisha akautega mkono wake. Muhariri akaikabidhi huku akilia kwa sauti yake ile nyembamba ambayo ngumi kali ilizidisha ule wembamba na kujikuta akigumia kama mtoto wa kike.
Nguzu aliipekua ile simu upesi upesi katika sehemu za jumbe mbalimbali, hakupata ujumbe wa kumvutia.
“Unapendelea kufia ofisini ama nyumbani kwako?”
“Si… aahm! nisamehe si… nitasema lolote utakalo.”
“Unanijua mimi?”
“Sikujui.”
“Ni nani huyu mwandishi wetu na anapatikana wapi?”
“Niliandika mimi… lakini hata mimi nilipewa.”
“Nisikilize we fala…. ndoto yangu moja ambayo nahitaji kuitimiza ni siku moja nimuue mtu akiwa ofisini nimkatekate nimtie kwenye mfuko wa rambo, kisha nitoke na ule mfuko niingie nao katika daladala niutelekeze huko. Vyombo vya habari vishindwe kuelewa vitaandika nini kuhusu kifo hicho…… Nina hasira ya kutimiza ndoto zangu. Nakupa nafasi ya mwisho kujieleza ukitetereka natimiza ndoto yangu. Nakuhakikishia kuwa sitaacha walau tone la damu humu ndani kwa ajili ya wapelelezi.” Nguzu alizungumza huku akiwa amemkazia macho muhariri.
Kijasho kikamwagika…
Akatapika kila alichokuwa anakijua katika ile habari iliyoandikwa na ‘mwandishi wetu’.
_____
JAMBO la kwanza lililokituliza kichwa cha Martin Nguzu ni juu ya inspekta Kobo.
Nguzu alistaajabu asimini hata kidogo kuwa aliachoelezwa kipo kama kilivyo. Licha ya kukiri kuwa yule muhariri alikuwa ‘chamtoto’ sana na asingeweza kuficha lolote kwa kitisho alichompatia lakini bado hakutaka kumpatiliza na kumwamini kwa asilimia zote.
Nguzu alitoka pale moja kwa moja akisimamia wazo lake kuwa kwa namna yoyote ile ni lazima afike nyumbani kwa Koplo Zubeda, aliamini kuwa ni huku ambapo angeweza kuupata mwanga zaidi katika hatua zake.
Alikiri kuwa kuonekana kwake mbele ya Zubeda kutazua kizaazaa cha aina yake ambacho kinaweza kusababisha majirani wakajazana kutaka kujua nini kinatokea.
Nguzu akajipa tahadhari kubwa sana kuwa ni lazima umakini utangulie mbele kuliko kiherehere cha kutaka kukutana na Zubeda ambaye kichwani anaamini Nguzu ameuwawa.
Ili kuondoa macho mengi kumfuatilia juu ya alichokuwa anahitaji kufanya Nguzu akaamua kufanya uvamizi wake mchana kweupe. Alilipenda giza lakini alijua linavutia wengi sana….
Akauchagua mchana kwenda nyumbani kwa Zubeda.
Akajiapiza kuwa Zubeda akionyesha dalili zozote za kuwa upande usiokuwa wake basi hatasita kumshukia kama mwewe anavyomshukia kifaranga na kumwacha mamaye akipiga kelele asiweze kutoa msaada.
Majira ya saa nane mchana alikuwa analitazama geti la kuingilia nyumbani kwa Zubeda.
Hali ya ukimya ilitawala sana, akategea mpaka alipowaona wanaume wawili wakipita kuelekea njia ile naye akaunga tela ili asionekane kama anajihusisha kwa lolote na nyumba ile.
Akapita na kuangaza huku akiulazimisha ule ukimya umwingie akilini na kumpatia jawabu la ni kitu gani kinaendelea.
Kimya kilimtatanisha!
Si kwamba hapajawahi kuwa kimya ama huwa ni sehemu yenye kelele za kutisha, ila ni mwili uligoma kuupokea ukimya ule katika namna ya kawaida.
Alilipita geti lile kwa mara ya kwanza huku akifanikiwa kujifunza kuhusu mazingira yale upesiupesi, mara ya pili aliporudi alilifikia geti na kubisha hodi.
Mlinzi akajitokeza na kufungua.
Hakusema kitu akabaki kumsikiliza Nguzu mwenye miwani nyeusi.
“Ni mgeni wa Zubeda! Koplo Zubeda..” Nguzu akajitambulisha huku akigundua kuwa huyu mlinzi ni mpya sio yule wa awali.
Akasaili eneo lililomzunguka yule mlinzi na kugundua kuwa hata silaha imebadilika.
Sub Machine gun!
Akaduwaa, kunani mpaka Zubeda aamue kuajiri mlinzi ambaye ana utaalamu wa kutumia silaha hii tena mchana kweupe.
“Sub machine gun!” akajikuta anajisemea kichwani kwake, kana kwamba ni mashairi ya wimbo anaotaka kuukariri.
“Wewe ni nani?” Mlinzi akauliza.
Polisi! Machale yakamcheza Nguzu kwa jinsi mtu yule alivyouliza lile swali, hakuwa mlinzi wa kawaida huyu alikuwa polisi.
“Naitwa Sebastian Madeko. Ni jirani…” alijitambulisha.
“Nisubiri hapa!” mlinzi alimwamrisha kisha akapiga hatua kwenda katika mlango wa nyumba ya Zubeda.
Nguzu akamwacha hadi alipoufikia mlango akawa makini kumtazama atazungumza na nani…..
Alishatambua kuwa hali haikuwa shwari, ni aidha Zubeda alikuwa matatani ama la alikuwa analeta matata.
Mlinzi akarejea baada ya dakika mbili.
“Twende!” akamwambia huku akimkazia macho.
Nguzu hakutaka kuionyesha hofu yake badala yake alijiandaa kwa mapambano.
Mlinzi akalifunga geti vyema kabisa kabla ya kumwongoza Nguzu kuelekea katika mlango wa kuingilia nyumba ya Zubeda.
Wakaufikia mlango, Nguzu hakuendelea kuwa kondoo.
Katika mlango ule wa kioo, aliweza kumsoma yule mlinzi, kuna shambulizi alijiandaa kumkumba nalo kabla hawajaingia ndani ama kuishia palepale.
Nguzu akawa sekunde moja mbele, akatokwa na teke maarufu kwa jina la ‘Shukrani ya punda’.
Lilikuwa teke la nyuma!
Mlinzi ambaye hakutarajia pigo lile akapepesuka mpaka chini, alimanusura bunduki yake imuue yeye mwenyewe kwa kumchoma kooni.
Macho yakamtoka pima!
Nguzu akawahi kukitoa kisu chake na kujitoa mpaka pale chini kisha akadidimiza katika mkono wa mlinzi.
Akatokwa na yowe kubwa kwa muda mfupi, Nguzu akachomoa ile ngumi yake ya kupunguza sauti.
Ikamwingia yule bwana na palepale akaiondoa miwani yake.
“Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu. Sikijui kifo bado, ukifanya mfano wa kunidanganya utakijua kifo kabla yangu.” Alifoka Nguzu huku midomo yake ikitetemeka.
Mlinzi hakuamini alichokuwa anakiona, alijiona akiwa anatazamana na mzimu wa Nguzu ambaye anasadikika kuwa ni mfu.
“Ni nani amekuagiza kulinda eneo hili na ni nani yupo ndani ya nyumba hii zaidi yako?”
Mlinzi akajifanya hajasikia.
Nguzu akatokwa na ngumi kali hii ikatua katika sikio la kuume la mlinzi.
Hakuweza kutokwa na yowe kubwa, damu ikaanza kumtoka.
Nguzu akatokwa na tabasamu wakati akimuuliza kuwa ni kipi chepesi kusikia swali ama ngumi?
Mlinzi yule ngangari akaanza kutokwa na kamasi.
Bwege alikuwa amepatikana!
“Nipo mwenyewe…. nipo mwenyewe usiniue.”
“Amekuagiza nani?”
“Inspekta…. Inspekta Kobo.” Alijibu kwa utulivu.
Nguzu akaishiwa hamu! hakutarajia jibu lile.
Huu ukawa ni mkanganyiko mpya kutoka katika majibu ya muhariri na huyu bwana mlinzi.
Akamtazama kwa jicho lililotangaza chuki ya waziwazi kabla hajamtundika swali jingine katika namna ya kisharishari.
“Muonekano wake upoje huyo bwana wa kuitwa Kobo.
Huku akikumbuka kuwa akijifanya hajasikia swali lile basi kifuatacho ni kubamizwa ngumi na kuulizwa swali la kukera safari hii aliwahi kujibu.
Akauelezea wajihi wa inspekta Kobo.
Nywele ndefu nyeupe zinazojaribu kuuficha uwalaza wake, ndevu fupi zenye uwiano sawia na nywele zake katika rangi.
Umri wake ukichezea miaka sitini hadi sitini na nane.
Konstebo Nguzu akachoka upya!
Huyu hakuwa inspekta Kobo aliyekuwa akimfahamu yeye.
Lakini kilichomjaza nguvu upya ni ule utambulisho ulikaribiana na ule ambao alielezwa na muhariri wa gazeti baada ya kumbana vizuri.
Konstebo akiwa anajiandaa kumuuliza tena yule bwana swali jingine, akafanya kosa kuitazama anga kama anayefikiria aulize kwa namna gani nyingine ili apate mwanga mkali anaouhitaji katika giza lile nene.
Yule muhanga alitokwa na teke kali likatua vyema katikati ya mapaja ya Nguzu, teke lile likamfanya Nguzu ainame.
Naam! adui alihitaji hivyo.
Uso ukawa jirani naye, akatokwa na teke kali sana lililoongezewa uzito na kiatu kigumu alichokuwa amevaa.
Uzito huu ukatua barabara katika uso wa Nguzu.
Ilikuwa mchana ghafla ukawa usiku kwa Nguzu pekee. Pigo lile lilimsukuma mpaka mlangoni.
Akaingia na ule mlango, kiuno kikapokea maumivu stahiki.
Konstebo Nguzu akajaribu kurejea katika mapambano lakini giza lilikuwa linamuharibia, hakumwona adui yake. Sanjari na hilo alikuwa akipambana kuilamba damu iliyokuwa inamtoka puani.
Adui alikuwa amechachamaa.
Alijaribu kutapatapa lakini adui hakumwachia nafasi, ni kama alimaanisha kutaka kuondoka na roho ya Nguzu na hakuhitaji kumuuliza swali lolote lile.
Nguzu alibaki kuikumbatia sakafu wakati mateke yasiyokuja kimpangilio yakimwandama.
Pumzi zikaanza kumsaliti, na hapa akajaribu kwa mara ya mwisho kuusaka uhai wake ambao yule bwana alitaka kumpokonya angali hajamaliza shughuli yake.
Akaituliza akili katika maumivu. Kitu ambacho wanadamu wachache sana wanaweza.
Kasumba ya mwanadamu akisikia mlio wa risasi anaanza kukimbia asijue kama anaikimbia ama anaikimbilia risasi.
Nguzu akautafuta uelekeo wa yale mateke makali yaliyomaanisha kuua. Akaupata uelekeo wa mpigaji, na jinsia livyokuwa anapiga hovyo akatambua bayana kuwa anatumia zaidi hasira na hapohapo anapoteza muhimili wa umakini.
Teke lilipomwingia akajitutumua na kusimama wima, na kujirusha kulekule katika uelekeo wa adui yake.
Karata sahihi!
Akamsomba yule bwana na kutua naye chini.
Majogoo mawili yaliyochoka haswa yalikuwa yamelaliana.
Na heri tele ziwe kwa kwa jogoo lililomlalia mwenzake.
Martin Nguzu alikuwa juu.
Hakuweza kurusha ngumi, kuchimba mikwara wala lolote lililoonyesha umwamba. Wote walikuwa wanahema juu juu.
Martin akapambana na kufanikiwa kuyafumbua macho yake.
Likafumbuka jicho moja kwa shida sana.
Akamwona adui yake akiwa mdomo wazi, anahema juu juu!
Akaiona shingo ikiwa wazi.
Akajitutumua akaifikia na kuikaba, anayekabwa akaanza kurusha mikono kuzuia kitendo kile.
Hakika walikuwa wamechoka!
Vishindo vilisikika kwa mbali, Nguzu akahisi hatari kubwa inakuja mbele yake…..
Uwezo wa kupambana kwa wakati ule hakuwanao, kama huyu aliyechoka anashindwa hata kummalizia vipi hao wanaokuja huku wakiwa na nguvu mpya.
Akajigeuza na kutua chini kisha ukaanza mpambano mpya wa kila mmoja kujaribu kusimama.
Nguzu akajaribu akaanguka, mwenzake naye yakamkuta yaleyale.
Nguzu akakerwa na hali hii ya kujikuta mnyonge angali oparesheni ikiwa mwanzo kabisa.
Hali ikazidi kuwa mbaya alipomwona yule mlinzi akifanikiwa kusimama wima, akayafuatilia macho yake yakiwa yanaangaza huku na kule hatimaye kwa pamoja wakajikuta wakiitazama bastola iliyokuwa imetulia sakafuni ikisubiri yeyote ajuaye kuitumia na aitumie.
Nguzu alitamani nguvu zimjae na akimbilie kule kuiwahi lakini hakuwa na nguvu za kutosha na alikuwa katika maumivu bado.
Kifo kikanukia katika namna ya kukera. Yule mlinzi akaanza kujivuta kwa kasi kuifuata bastola ile, Nguzu akaanza kujiona yu mjinga kukisubiri kifo chake bila dalili zozote za kupambana.
Akapitiwa na fikra za harakaharaka juu ya hayati babu yake, aliyemrithisha jina hilo lenye maana kubwa.
Nguzu ‘chikichia’ hapa hapafai tena! alijionya huku akiangaza lilipo kimbilio.
Hakuliona kimbilio kabla hajamwona yule mlinzi akigeuka huku akiwa na bastola mkononi.
Akafyatua hovyo kwa mara ya kwanza, bastola isiyokuwa katika kiwambo cha kuzuia sauti ikatoa mlio mkubwa.
Mlio huu ukamuhamasisha Nguzu kujitutumua na kukimbia.
Alikimbia ndani ya ile nyumba huku akiamini kuwa ataukuta wazi ule mlango aliokuwa anaufahamu ili aweze kutokea upande mwingine.
Hofu ya kifo ilizidi kujenganaye urafiki, alijitutumua akaufikia mlango.
Mungu wangu!! ulikuwa umefungwa kwa kutumia mnyororo.
Hakuwahi kuiona hali kama hii hapo kabla. Huku nyuma akawa anamsikia yule mlinzi akitoa matusi yote huku kila mara akimaanisha kuwa iwe isiwe lazima amuue.
Nakufa! Hatimaye Nguzu akakiri, lakini hakubaki kibwegebwege afe bila kupambana.
Akausukuma mlango wa chumba cha Zubeda ambacho enzi zile alikuwa akiingia huku amebebwa mgongoni na koplo yule mwenye asili ya Tanga lakini akiishi zaidi Mwanza.
Sasa aliingia katika chumba hiki huku akiwa anasota, jicho moja likiwa linaona kwa tabu huku lile jingine likiwa limefumba kabisa.
Hamadi! mlango ulikuwa umezuiwa na kitu kwa ndani.
Hofu ya kichwa chake kusambaratishwa na risasi ikamfanya Nguzu ajitupe mzima mzima na kufanikiwa kukisogeza kizingiti.
Akajikuta ndani ya chumba.
Sauti ya yule mlinzi nayo ikazidi kutapatapa ikitishia kuua.
Chumba kilimkaribisha Nguzu katika hali ya utulivu, utulivu ule ulimtisha zaidi, akajaribu kufikiri ni wapi atajificha ili kumkwepa mshika bunduki.
Uvunguni! hili lilikuwa wazo la kizembe lakini walau naye aliwaza.
Akaanza kujitutumua aingie uvunguni, akaanza kujivuta kwa kutumia tumbo.
Hakuzama sana kabla hajabamizwa ghafla na kitu kigumu katika paji la uso wake.
Ile anajaribu kujiweka sawa akatandikwa teke kali usoni, akajikuta yungali nje ya ule uvungu huku akiwa nusu hai nusu mfu.
Alikuwa amepiga magoti damu zikimvuja.
Hazikupita sekunde nyingi kiumbe akauona mdomo wa bunduki ukitangulia kutoka katika ule uvungu.
Nipokee baba nakufa mimi Nguzu! alijifanyia dua upesiupesi.
Na hapo mlango ukasukumwa akamsikia yule mlinzi akiendelea kuropoka.
Nguzu akatambua kuwa nyuma yake palikuwa na mtutu na pia mbele yake alijionea waziwazi.
Swali likabaki juu ya nani atakayekuwa wa kwanza kufyatua ili auondoe uhai wake.
Yule wa uvunguni akawa wa kwanza kufyatua.
Risasi ikapenya jirani kabisa na sikio la Nguzu, ikafanya mlio kama wa nyuki mwenye hasira.
Kisha kishindo kikafuatia, Nguzu akatua chini akiangukia tumbo.
Kichwa chake kikawa jirani kabisa na ule mdomo wa bunduki iliyotokea uvunguni.
Na hapo akaviringika na kutoa uvunguni mshambuliaji yule aliyemkosa Nguzu maksudi na kumlipua aliyekuwa nyuma yake.
“Nilijua kuwa umekufa duniani, lakini si katika moyo wangu. Nikaamini tutakutana mbele ya haki, sijui kama ni mahali sahihi tulipokutana Martin, konstebo Martin Nguzu.” Sauti imara ya kike ilizungumza.
Nguzu hakuhitaji macho yake katika hili, masikio pekee yalitosha kutambua kila kitu. Hatimaye kinywa kizito kikajitutumua na kuzungumza.
“Koplo Zuu!”
“Nihakikishie kuwa sitakiwi kukulipua kwa sababu u mmoja kati yao…”
“Si..sijui kitu hapa. Usilipue koplo.” Alisihi Nguzu.
Zubeda akamdaka na kumsimamisha. Nguzu akakosa muhimili akataka kuanguka, Zubeda akatega mgongo wake kama alivyokuwa akiutega zama zao za furaha.
Nguzu akatua juu yake.
Zubeda akaanza kupiga hatua kutafuta uelekeo, Nguzu akiwa anakoroma.
Hali yake ilikuwa mbaya sana. Zubeda naye alikuwa anajitutumua, mguu wake mmoja ulikuwa haujaimarika..
Zubeda akiwa ndiye anayetegemewa alijaribu kufikiria juu ya uwepo wao pale ndani. Hapo kabla alikuwa amefanikiwa kuua na kisha kumpokonya bunduki mtu aliyewekwa kwa ajiri ya kumlinda asiweze kuleta bughudha yoyote.
Walimpatiliza kwa sababu ya miguu yake kuwa na mushkeli.
Dharau zao zikawafanya wapunguze ulinzi na kumwacha mbabe mmoja.
Yakamtokea puani!
Wakati Zubeda akiendelea kufikiria ni nini kilitokea hadi akabadilishiwa ulinzi ghafla, kutokea ule ulinzi aliowekewa na inspekta Kobo hadi ulinzi huu wa ajabuajabu. Akalishuhudia geti likifunguliwa na gari ikaingia huku askari watano waliovalia sare wakitangulia mbele.
Balaa!
Akajaribu kumshirikisha Nguzu aliyekuwa bado hoi. Nguzu hakuwa na la kuchangia.
Askari yule imara ndani kwa ndani na legelege kwa umbo la nje alitoweka mpaka chooni. Huku aliweza kuona kila kitu kilivyokuwa kinaendelea nje.
Alimtua Nguzu na kumsihi anywe maji yanayotoka katika bomba ili aweze walau kupata nguvu kiasi. Wakati huo akiendelea kuilazimisha akili yake ifanye kazi kwa kasi zaidi kuhusu tukio linalokuja mbele yao, alifahamu fika kuwa hakuna namna ya kuwa salama angali mle ndani kuna maiti mbili.
Kwa namna yoyote yeye na Nguzu watayamalizia maisha yao gerezani.
Maji yalikuwa msaada mkubwa sana kwa Martin Nguzu. Hayakumfanya kuwa imara sana lakini walau macho yake yaliweza kuona na aliweza kupumua vyema kwa sababu aliweza kuyaondoa mabonge ya damu yaliyounda uzio mbele ya pua zake na kumsababisha apumue kwa mdomo badala ya kutumia pua.
“Martin, Martin!” Zubeda aliita kwa kunong’ona.
Konstebo Martin akaupokea wito ule kwa kutulia akimsikiliza.
“Askari wote wanatuzingira.” alimweleza kana kwamba Nguzu alikuwa anafahamu tayari juu ya uwepo wa ugeni ule..
“Akina nani? wako wapi?”
Zubeda hakumjibu badala yake alimsaidia kunyanyuka na kisha akamwelekeza kila alichokuwa akikiona kwa nje.
Walichoka!
BAADA ya kukataa kata kata kubadili maelezo yake, amri ilitolewa ya kwenda kupekua nyumba ya inspekta Kobo ili iweze kubainika kama anayo mawasiliano yoyote aliyowahi kufanya na kikosi cha majambazi kilichoinyanyasa Shinyanga kwa wakati ule huku askari kadhaa wakiangushwa na kupoteza maisha.
Msako wa kwanza haukuzaa matunda yoyote waliyoyatarajia.
Walikata tamaa huku wakianza kuamini yawezekana kuwa inspekta Kobo aidha hajuani na lile kundi ama la ni mafia aliyefuzu mafunzo yote stahiki.
Yaani hata umkate mguu akisema sijui ni sijui. Anameza maneno yake na kuingia nayo kaburini…
Wakiwa wanakaribia kuondoka, askari mmoja akafika na kitu kipya.
Akamtupia swali Kobo.
“Hii nyumba unayoishi ni mali ya nani?”
“Binafsi.” Alijibu kwa sauti iliyokata tamaa.
“Umeijenga mwaka gani na umeanza kuishi humu lini?”
“Huu ni mwaka wa kumi sasa naishi humu.”
Jibu lile likamfanya askari yule afanye tabasamu hafifu kabla hajamtundika pagumu bila yeye kujua.
“Umejenga nyumba nyingine tofauti na hii?”
“Hapana!”
“Mtu akifika hapa kukutafuta na asikupate je? ni wapi zaidi anaweza kukupata?”
“Kazini kwangu.”
Jibu la sasa likayafanya meno ya yule askari yaonekane kwa sababu ya kicheko kidogo.
Na hapo akayabwaga makaratasi kadhaa mbele ya maaskari wenzake na Kobo akayashuhudia.
Alikuwa ni mnyonge lakini haya yalimtia unyonge zaidi.
Mikataba!
Mikataba baina yake na mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi hawara yake.
Koplo Zubeda!
Alitamani ardhi ifunguke atumbukie humo, alijiona waziwazi kuwa alikuwa anaelekea pabaya.
Kwanza alidanganya kuwa hana makazi mengine zaidi ya hayo, pili mikataba yote aliiandikisha kwa majina yake na si ya Zubeda.
Mkataba wa mwisho aliuandikisha miezi miwili tu iliyopita.
Anakwepa vipi rungu la sheria?
Watamuhesabu kama mnyang’anyi ambaye analo eneo la siri kwa ajiri ya kufanyia shughuli zake haramu.
Inspekta Kobo akaumia zaidi kwa sababu alikuwa anakwenda kumweka Koplo Zubeda na maaskari aliowaweka kumlinda matatani.
Wote hawa watahesabika kuwa ni chama kimoja cha kimafia na wataminywa kama alivyominywa yeye hadi kufikia hapo alipo.
Akaunganisha meno yake kwa uchungu mkubwa.
“Tunaenda moja kwa moja hadi katika nyumba hii. Ukithubutu kutudanganya utajutia uongo wako” Akachimbwa mkwara, akamtazama yule bwana kwa jicho kali, akajilaumu sana kwa sababu alikuwa na pingu, vinginevyo angefanya shambulizi kwake.
Hakupendelea masuala ya kuchimbwa mkwara!
Inspekta Kobo akawaelekeza nyumba ile inapopatikana, na hata asingewaelekeza bado kuna namba ya nyumba iliorodheshwa katika ile mikataba.
Bila kusahau kiherehere cha mmiliki wa nyumba ile kuweka nambari yake sahihi kabisa ya simu ya mkononi na ile ya ofisi.
Wakatoweka kuelekea nyumbani kwa Zubeda!
ITAENDELEA
Konstebo Nguzu Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;