Konstebo Nguzu Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Konstebo Nguzu

SIMULIZI Konstebo Nguzu
Konstebo Nguzu Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi: Konstebo Nguzu

Sehemu ya Pili (2)

“ANZIA hapo ulipo, TUMIA hicho ulichonacho, FANYA kile unachoweza….”

KILIANZA kitanda kumsaliti, kila mtindo aliojaribu kukilalia ukagoma kumburudisha. Akastaajabu kitanda chake mwenyewe lakini amtii. Akasimama wima na kukitazama kwa sekunde kadhaa jinsi kilivyokosa nidhamu.

Akaondoka bila kukiaga na kuelekea sebuleni,huko akajibwaga katika kochi kubwa lililokuwa sebuleni, hili likampokea vyema na ule mbonyeo ukamfurahisha.

Heri yako bado unanitii! akajisemea, huku akiukunja mguu wake na kujaribu kuvuta taswira ya kitu kilichomfanya ashtuke usiku wa manane na kuanza kubabaika.

Moshi mnene! hiki nd’o kitu kilichokuwa kikitishia afya ya akili yake kwa wakati ule.

Akainyanyua simu yake na kujaribu kupiga katika nambari alizokuwa amepiga awali na hazikuwa zikipatikana.

“Ni kweli Sule anavuta bangi tena sana tu, lakini sidhani kama bangi yake inaweza kumfanya akafanya upuuzi mkubwa namna hii…” Akajisemea huku akiketi.

Alipoketi na kuwa kimya kwa muda kidogo akakumbwa na kitu ambacho kilimfanya ashindwe kuketi bali kusimama wima kabisa.

Kuna vitu viwili vilikivamia kichwa chake, ulikuwa ni mfano wa picha ambazo zilikuwa gizani na sasa akabaini kuwa aliziona lakini pasi na uhakika.

Picha ya kwanza ilikuwa ni mtu chini ya mti.

Ni nani yule? akajiuliza huku akijilazimisha kuing’arisha picha ile katika kumbukumbu zake.

Haikung’aa!

Picha ya pili ni ya mwanaume akizungumza, na haikuwa ngeni sauti ile katika masikio yake. Haikuwa sauti aliyokuwa akiishikia mara kwa mara kama ilivyo sauti ya mkewe ambaye ni daktari. Hii ilikuwa sauti ambayo aliwahi kuisikia asijue mwaka wala tarehe, hakukaribia kukumbuka hata mahali alipowahi kuisikia.

Ila aliwahi kuisikia.

Baada ya miaka mingi ya mapambano na kisha kuamua kutulia tuli baada ya kuvunjika mguu wake, akabaki katika mapambano ya kalamu na karatasi huku akiwa yu katika chumba tulivu chenye urafiki wa dhati na kiyoyozi.

Kwa jicho lake pevu kabisa Inspekta Kobo akajiona anaungiza mguu wake mbovu katika mapambano mapya.

Licha ya mkewe kuwa daktari inspekta alipendasana kumshirikisha masuala yake pindi yanapomwendea kombo.

Na hili lilikuwa limemnyima usingizi, akabofya simu yake na kumpigia mwenza wake, simu ikaita lakini haikupokelewa.

“Yupo chumba cha upasuaji huyu…” alijisea na hakujaribu tena kupiga.

Akafikiria kumpigia mpenzi wake wa siri, koplo Zubeda, akajiuliza mara mbilimbili kisha akaikumbuka ile kauli mbiu ya ‘ukivuka mipaka basi siri mweleze mkeo unayempenda kwa dhati lakini kamwe usitapike siri zako mbele ya hawara. HAWARA hana dhamana…

Inspekta akakiri kuwa anampenda sana Zubeda lakini tahadhari lilikuwa jambo la muhimu sana.

Akarejea katika kochi akaketi.

“Nguzu atakuwa amekufa ama? na kama hajafa itakuwaje upande wangu…” alijiuliza Inspekta asipate wa kumjibu.

Watoto wake walikuwa wanaelea katika dimbwi la usingizi mzito.

Mawazo juu ya mawazo hatimaye usingizi ukamwonea imani, ukamsomba na kumuunganisha katika dimbwi walilokuwqa wakisafiri watoto wake kwa wakati ule.

Dimbwi la usingizi…..

Asubuhi akaamka akijisikia ahueni na akijaribu kujisahaulisha kuhusu kiza kilichojiri usiku uliopita.

Akiwa anafanya jitihada za kuyafuta haya akaipokea taarifa juu ya kuchomwa kwa nyumba aliyokuwa akiishi konstebo Nguzu, kilichosalimika ni nguo zake zilizokuwa zimeanikwa katika kamba iliyokuwa mbali kidogo na nyumba.

Si kichwa wala fuvu lake kilichosalia katika moto ule wa kutisha.

Inspekta akazishusha pumzi zake, akaanza kutembea huku na kule katika himaya ya nyumba yake. Akaunda mfano wa mzazi mdogo katika kichwa chake, akahisi uhai wa Nguzu ungeweza kuwa hatari sana kwake.

Hatari kwa sababu alikuwa na ubaya naye nafsi ya Kobo ikakiri kuwa ilikuwa imechefukwa haswa kutokana na uwepo wa Nguzu.

Kwa hatua hii ya kuzimika moja kwa moja akahisi kuwa itakuwa ni nafuu kubwa kama mtu aliyeingiliwa na mchanga jichoni akifanikiwa kuutoa na kisha jicho lake kubaki huru.

Lakini uhai huohuoungeweza kumweka matatani kwa sababu Nguzu angehojiwa juu ya nani amehusika katika moto ule, angwataja watu ambao ana ubaya nao, kwa nini asilitaje jina la inspekta Kobo kama jina la muhimu zaidi!!

Ni heri amezimika. Alihitimisha Inspekta Kobo.

Akahamia upande wa pili wa mzani, Nguzu amekufa vipi?

Je? ninahusika? akajiuliza, kisha akachukua simu na kupiga tena nambari aliyokuwa akihangaika nayo usiku uliopita.

Haikuwa inapatikana…

Hapo akarukia sehemu ya pili, ni nani alikuwa chini ya mti, na ni sauti ya nani aliisikia upande mwingine…

Haya yalikuwa maswali magumu zaidi. Maswali yaliyosababisha aamue kuwa upande wa yeyote yule ambaye amefurahia kifo cha Konstebo Nguzu.

Akaufunga ukurasa wa mawazo mazito juu ya ni nini atafanya ili Zubeda atulie na kuachana na Nguzu. Sasa aliwaza ni kitu gani amfanyie asije akazama kwa mwanaume mwingine kama ilivyokuwa kwa Nguzu.

Akaamua kumfanyia ugeni wa ghafla utakaotawaliwa na upya mkubwa sana kutoka kwake…

Akiwa mwenye kubwa tabasamu aliingia maliwatoni kujisafi mwili wake.

Kisha akalivamia jokofu na kutoa maji ya matunda. Akaigida kwa fujo glasi ya kwanza mpaka ikamalizika. Kisha glasi ya pili akainywa taratibu huku akiwa anaipanga ratiba yake kwa siku hiyo.

Simu yake ya mkononi ikatoa mlio kumaanisha kuwa kuna ujumbe mpya umeingia.

Akaifungua upesi kwa sababu simu ilikuwa kiganjani kwake.

“Bosi, shemeji kapata ajali yuko Temeke hospitali. Amekula mzinga na Suzuki yake”

Ujumbe ule wa maandishi ukawa kama ulioambatana na umeme mkali kuzidi kipimo, ukautekenya mkono wa inspekta glasi ikamtoka mkononi, kisha akaanguka chini kama mzigo baada ya miguu kuelemewa.

Mpasuko wa glasi na kishindo cha mwili mzito wa inspekta vikawashtua watoto waliokuwa wameamka tayari.

Balaa jingine likaibuka.

Walipiga mayowe huku wakiiitana kwa kusisitiza kuwa baba yao angali katika tatizo kubwa.

Inspekta Kobo alijaribu kusimama ili alete amani kwa watoto wake lakini akabaini kuwa hawezi kusimama, ule mguu wake ulioungwa kwa vyuma ulikuwa umeyumba.

Tusi pekee katika lugha ya kiitaliano alilolifahamu likamponyoka huku akiipigapiga sakafu.

Kelele zilivyozidi akatoa onyo, akawafokea watoto wake huku akijinadi zaidi ya mara mbili kuwa yeye ni mwanajeshi kamili wasihamanike.

Maneno ya shujaa huyu yakatuliza munkari, akafikishwa hospitali katika hali ya utulivu kabisa bila papara za kuwafanya majirani watambue kuwa inspekta Kobo amekumbwa na balaa.


MAJIRA YA saa nne usiku kiwiliwili cha kiume kikiwa katika koti kubwa lililoungana na kofia yake kilikuwa kikikatiza katika wodi ya wanawake kwa mwendo wa haraka huku kichwa chake kila mara kikinyanyuka juu kutazama uelekeo wa mbele na kisha kuinama tena.

Safari ile iliyojaa umakini iliishia katika chumba kilichojitenga mbali na wodi za wanawake.

Watu wawili walimpokea kimyakimya na kumwingiza chumbani, akamwona mgonjwa wake.

“Nakupenda sana Zubeda.” Lilikuwa neno la kwanza kumnong’oneza yule mgonjwa kisha akainama na kumbusu.

Zubeda akajaribu kutabasamu kidogo.

Inspekta Kobo alizungumza machache na Zubeda kisha akamweleza kuwa siku inayofuata atakuwa na muda mrefu zaidi wa kuzungumza mengi.

Akaaga na kuondoka!

Alitumia usafiri wa pikipiki, upesi akarejea nyumbani kwani kwa ratiba ya mkewe ilivyokuwa siku hiyo alipaswa kuwa nyumbani majira ya saa tano usiku.

Inspekta aliwasili baada ya dakika chache tangu saa tano ilipotimia. Hofu ilimtawala kidogo kwa sababu ya maswali ambayo angepokea kutoka kwa mkewe lakini pia angelaumiwa sana kwa kuanza mizunguko mapema kiasi hicho badala ya kupumzika.

Hakumkuta mkewe nyumbani, akaanza kujilaumu sana kwa kuhofia ujio wa mkewe, huenda angeweza kuendelea kuzungumza na Zubeda kwa muda mrefu zaidi.

Wakati akiwaza haya, Daktari Kobo ambaye ni mkewe alikuwa katika chumba cha mgonjwa akijaribu kuzungumza naye kwa lugha ya upole kabisa, ni kawaida ya madaktari kuitumia lugha inayoleta tumaini kwa mgonjwa.

Tofauti na ulivyokuwa utaratibu wa siku zote aliouzoea mgonjwa yule alistaajabu kuona mlango wa chumba kile alicholazwa unafungwa kwa ndani na yule daktari mwanamke.

Kisha mwanamama yule akakisogelea kitanda na kumjulia hali.

Mapigo ya moyo ya yule mgonjwa yakaanza kwenda mbio kupita kawaida.

“Bila shaka sina haja ya kujitambulisha…. na hakika sijaja kwa ubaya humu ndani. Unaitwa Zubeda na unajihusisha kimapenzi na mume wangu wa ndoa Inspekta Kobo.” Akaweka kituo kisha akamwinamia mgonjwa yule.

“Nimekusudia kuzungumza na wewe kwanza kwa sababu wewe ni mwanamke mwenzangu, unafahamu nini kuhusu kifo cha Konstebo Nguzu?” Swali lile lilikuwa kama upinde wenye moto mkali mbele yake. Likamchoma haswa Zubeda.

“Sijui lolote.” alijibu kwa ufupi mno.

“Zubeda, narudia tena, sipo hapa kwa sababu ya wivu wa kimapenzi, nina umri wa miaka thelathini na tisa sasa, nimeishi na inspekta kwa zaidi ya miaka kumi na nane. Nilikuwa ninao wivu zamani sio sasa…. ninawapenda sana watoto wangu sitaki wakose huduma zababa yao na huenda katika hili ni msaada pia kwako.Kuna taarifa ambayo haijazagaa kuwa wewe na inspekta mmeshirikiana kuichoma nyumba ya Nguzu huku yeye akiwa ndani na kusababisha mauti yake. Hili nd’o lililonileta hapa….. ungekuwa ni wivu wa mapenzi ningeagiza wakuchome sindano moja tu na siku inayofuata ungehamishiwa mochwari tayari kwa maziko, na mwili wako unmgeoza licha ya kupigwa na ubaridi wa mochwari. Sina nia mbaya… naomba unipe ushirikiano. Wewe na inspekta mpo matatani. Kumbuka kuwa IGP hapatani na inspekta Kobo sana, atawanyoosha katika hili. Niambie kama mmehusika ili tuweke kando masuala ya mapenzi kisha tuketi pamoja na kuitafuta suluhu kabla vithibitisho havijatapakaa.”

Maneno ya dokta Kobo yalikuwa mazito mno, Zubeda hakuamini kile alichokisikia, hakuwahi kuzungumza na inspekta Kobo hata siku moja juu ya mpango huu wa kinyama kiasi hicho.

“Ukiachana na hiyo njama, sijawahi hata siku moja kuzungumza na inspekta juu ya konstebo Nguzu.”

“Sema hayati…” Dokta alimrekebisha.

Marekebisho haya yakamuumiza Zubeda katika moyo wake, alikuwa amemzoea mno Martin Nguzu. Sasa anaambiwa amepoteza maisha.

“Inspekta Kobo nd’o mtu wa mwisho kuingia nyumbani kwa marehemu kabla moto haujaimeza nyumba ile. Hivi unadhani wakuijumlisha na tatizo la wewe kuwa na wapenzi wawili kwa waikati mmoja kuna mtu atahitaji ushahidi wa ziada. Zubeda utapotea vibaya mno, mimi sijui sana sheria lakini kama nikichaguliwa kutoa hukumu katika hili basi nikiwapeleka gerezani miaka michache kabisa ni thelathini thelathini. Wauaji wakubwa nyinyi..” Jazba ikataka kuchukua nafasi akatulia kwa muda kujizuia na hali ile.

“Shangazi, sijui lolote kuhusu huu mpango unaousema, sijawahi kuzungumza na Inspekta juu ya lolote kuhusu Nguzu. Hii ni kweli ya moyo wangu…”

“Sawa kama haujui. Mimi naondoka…” alizungumza doktahuku akiyanyanyua mabega yake juu. Akauendea mlango na kutoweka…..


LILIANZA kuwa saa moja, kisha likafuata la pili yalipofika matatu subira ikafikia kikomo. Inspekta Kobo akachukua simu yake na kujaribu kumpigia mkewe amuulize nini kinajiri hadi hajafika nyumbani hadi muda huo.

Simu iliita kidogo kisha ikakatwa. Alipojaribu tena haikuwa ikipatikana. Akajaribu kupiga ofisini wakaelezea kuwa Dokta Kobo alitoka kazini tangu saa mbili usiku, wakastaajabu kupokea simu usiku wote huo wa kuuliziwa kwake.

Inspekta Kobo ambaye tayari alijiona ni mtu ambaye ameandamwa na majanga ya ghafla akaingiwa mchecheto, haikuwa kawaida kwa mkewe hata kidogo kuchelewa nyumbani.

Akafikiria kuwapigia rafiki zake wachache aliowafahamu lakini mshale wa saa ulimfanya aone haya.

Saa nane usiku kumuulizia mke!

Hapana…. Akaendelea kungoja huku pepo la wivu likianza kumchokonoa, akajiuliza ikiwa yeye ameweza kuwa na mwanamke nje inashindikana vipi kwa mkewe?

Swali hili likamghadhabisha na kujiona hatendewi haki hata kidogo ikiwa ni kweli mkewe amediriki kufanya hayo.

Usingizi ulimsomba majira ya saa kumi na moja kasoro dakika chache.

Akagutuka saa moja na nusu asubuhi na bado mkewe alikuwa hajarejea nyumbani wala simu yake ya mkononi haikuwa ikipatikana.

Hofu ikatanda maradufu…..

LILIANZA kuwa saa moja, kisha likafuata la pili yalipofika matatu subira ikafikia kikomo. Inspekta Kobo akachukua simu yake na kujaribu kumpigia mkewe amuulize nini kinajiri hadi hajafika nyumbani hadi muda huo.

Simu iliita kidogo kisha ikakatwa. Alipojaribu tena haikuwa ikipatikana. Akajaribu kupiga ofisini wakaelezea kuwa Dokta Kobo alitoka kazini tangu saa mbili usiku, wakastaajabu kupokea simu usiku wote huo wa kuuliziwa kwake.

Inspekta Kobo ambaye tayari alijiona ni mtu ambaye ameandamwa na majanga ya ghafla akaingiwa mchecheto, haikuwa kawaida kwa mkewe hata kidogo kuchelewa nyumbani.

Akafikiria kuwapigia rafiki zake wachache aliowafahamu lakini mshale wa saa ulimfanya aone haya.

Saa nane usiku kumuulizia mke!

Hapana…. Akaendelea kungoja huku pepo la wivu likianza kumchokonoa, akajiuliza ikiwa yeye ameweza kuwa na mwanamke nje inashindikana vipi kwa mkewe?

Swali hili likamghadhabisha na kujiona hatendewi haki hata kidogo ikiwa ni kweli mkewe amediriki kufanya hayo.

Usingizi ulimsomba majira ya saa kumi na moja kasoro dakika chache.

Akagutuka saa moja na nusu asubuhi na bado mkewe alikuwa hajarejea nyumbani wala simu yake ya mkononi haikuwa ikipatikana.

Hofu ikatanda maradufu…..

Asubuhi akapokea ujumbe mfupi kutoka kwa mkewe.

“Nipo salama mume wangu, nipo kwa mama mdogo. Kuna jambo limenichanganya naomba uniache kidogo natafuta suluhisho. Watazame watoto…”

Inspekta akaufuta ujumbe ule. Alimjua vyema mkewe, haikuwa mara ya kwanza kuwa katika hali hiyo na kuamua kuwa mbali na mumewe.

“Nimemkwaza nini huyu?” alijiuliza lakini akipata ahueni kuwa mkewe yupo salama.


Mwanaume mweusi sana mwingi wa misuli katika mikono yake alikuwa amejitwika mfano wa gunia katika bega lake, mwili wake ulitokwa jasho lililoufanya ung’are kana kwamba ametoka kuogelea katika dimbwi la mafuta ya kula.

Alijitutumua na gunia lile huku akitweta.

Lilionekana kumzidia, lakini hakuwa tayari kukubaliana na hali ile moja kwa moja.

Macho yake makali mithiri ya nyoka yalikuwa makini kutazama huku na kule ikiwa kuna kitu kibaya aweze kujihadhari.

Zaidi alililinda lile gunia kuliko alivyowaza kujilinda yeye mwenyewe.

Alipoufikia mlima aliliweka chini lile gunia akapumzika kidogo kisha akajitwika tena na kuendelea na safari ile ambayo mwisho wake haukuwa bayana ikiwa ni wa matumaini ama la.

Kilima kikamalizika akaanza kupita katika vichaka vya hapa na pale, mwisho akaufikia mto na kuanza kuogelea. Gunia likiwa juu kabisa, japo lililowana lakini haikuwa kwa kiasi kikubwa sana.

Mkondo wa maji ulikuwa una nguvu sana lakini bwana yule mwenye misuli mingi alifanikiwa kuwa imara zaidi akapenya na kutokea upande wa pili.

Huko akapokelewa gunia lile huku akipongezwa na wenzake wawili waliosaidiana lile gunia.

Hawa nao walikuwa imara sana mmoja akiwa mfupi na mwingine mrefu. Wote weusi miili yao, wakaendelea na safari ya gunia lile kuelekea pahali lilipohitajika kufikishwa.

“Hivi mali itakuwa salama kweli?” Mmoja akahoji wakati wa pumziko fupi la kubeba gunia lile.

Swali lile likazua ukimya wa muda, wakalitazama gunia kwa pamoja. Kisha wakaangaliana kana kwamba waliambiana sekunde za kulitazama na sekunde za kutazamana.

Ukafuata mguno kwa pamoja tena.

“Unahisi jamaa atakuwa amefanya madhara yoyote?” aliyeulizwa swali naye akauliza swali kabla hajajibu alichoulizwa.

“Au tufungue kidogo?” Swali tena kutoka kwa muulizwa.

Swali hili likawafanya tena walitazame lile gunia kwa muda, halafu bila kukubaliana wala kupingana wakalibeba lile gunia safari ikaendelea.

Hawakulifungua!

Ilikuwa safari ya masaa kadhaa hadi walipolitua gunia mahali lilipostahili. Wakatulia wakilitazama kwa takribani dakika moja kisha wakainama na kulifungua gunia lile.

Waliacha wazi kisha wakatoweka.

Zikapita dakika kadhaa akaingia bwana aliyebeba bakora mkononi mwake, akalifikia lile gunia bila kusema neno lolote akaanza kuishusha bakora yake mara kadhaa guniani.

Gunia lilikuwa limetulia tuli bado.

Akazidisha juhudi kuliadhibu gunia lile na chochote kilichokuwa ndani yake huku akizungumza maneno mengi ya kulifokea na mengine ya kusihi. Jasho lilikuwa limemlowesha mwili mzima na alikuwa anatetemeka sana.

Baada ya bakora ya kwanza kuonekana haitoi adhabu ipasavyo akabadilisha bakora, akachukua ndefu zaidi.

Akaizungusha kwa ghadhabu zote akaitua katika gunia.

Gunia likatikisika!

Mchapaji akatulia tuli asiamini kile alichokuwa anakiona, akaanza kupiga mayowe akiwaita wenzake kutokea katika giza.

Kelele zile zikawa tishio kwa mali iliyokuwa katika gunia lile.

Kilianza kidole kutikisika na kisha macho yakaanza kulazimisha kuiona nuru.

Akajaribu kugeuka lakini akahisi maumivu makali yanamwandama na kuna kitu kizito kilikuwa kimeuegemea mwili wake.

Akajaribu kuongea akahisi koo limekauka sana huku kiu kikuu kikimwandama.

“Nini hiki?” alijiuliza baada ya kugundua kuwa ile si ndoto bali ni kweli tupu.

Akatuliza akili na kujaribu kufikiri tena na tena lakini hakuna jibu alilopata.

Akatumia nguvu ili aweze kujigeuza tena ikashindikana. Alipovuta pumzi zake akagundua kuwa hapumui vizuri sana. Kuna kitu kingine kilikuwa kimebana katika kifua chake.

“Hakikisheni amekufa aisee! Ishu sio nyumba ishu ni yeye…” Masikio yake yakazisikia sauti zikihimizana.

“Kina nani hawa Mungu wangu!” alihamaki akiwa palepale katika wakati mgumu.

Akajikuta anaijiwa na fikra mbili za ajabu zilizooana, akajihisi kuwa muda si mrefu alisikia shangwe na maneno ya kuhimizana huku akiwa amefunikwa katika kitu asichokijua na sasa anasikia maneno mengine akiwa mahali tofauti kabisa.

Ni nani hawa watu? alijiuliza.

Na nipo wapi hapa sasa eeh!

Milango ya fahamu yote ilikuwa imefanya kazi yake kwa ukamilifu, macho yaliishia kuona giza, masikio yakisikia sauti za ajabu, ngozi ilikuwa imebanwa na kitu asichokijua, ulimi ulibaini kiu kikali kutokanana ukavuu wa mdomo na koo, pua yenyewe ilikuwa imelala huku ikisahau wajibu wake.

Ikakurupuka na upesi baada ya kugundua kuwa bosi wake ameamka.

Ikanusa na kumweleza bosi wake kuwa kuna harufu ya petroli na moshi.

Moto! Akili ikaungana na pua kutoa majibu.

Mungu wee! nilichomewa ndani mimi! akajisemea na ili kuhakikisha kama haoti akajaribu kujipapasa.

Alikuwa uchi wa mnyama.

Ndio, mara ya mwisho alivua nguo zake harakaharaka baada ya kugundua kuwa hawezi kuukwepa moto ule upesi lakini angeendelea kubaki na nguo moto ungemvamia upesi kulikoni alivyokuwa mtupu.

Inspekta amenichoma moto! alijaribu kutoa sauti.

Akaishia kunong’ona, zile sauti alizozisikia nje zikawa zimetoweka kwa wakati huo.

“Mzee Majenga ni nani kwani?” alijiuliza swali lile, ilikuwa mara ya kwanza kabisa jina lile kuja katika fikra zake lakini alihisi amelisikia sehemu wakati akihangaika katika moto ule.

“Zile shangwe ndani ya lile gunia ina maana ilikuwa ndoto?” alijiuliza huku sasa akiutumia uimara wake wa jeshini kukinyanyua kile kifusi kilichokuwa kimemgandamiza.

Akafanikiwa.

Hamadi! Nyumba yote ilikuwa imeteketea. Kuta zilizoanguka ndizo zilisalia pamoja na bati.

“Nimeponaje mimi” alijiuliza huku akijaribu kusimama wima.

Mguu wake ulikuwa una maumivu makali sana. Kutokana na lile giza hakuweza kuona kilichojiri katika ule mguu.

Akatembea uchi vilevile, akitafuta muafaka wowote usiku ule.

Akaelekea hadi lilipokuwa bomba la maji, akafungua na kunywa maji ya kutosha.

Karibu na bomba palikuwa na kamba ya kuanika nguo. Akachukua nguo ambayo haikuwa yake, kumbukumbu za kuanika nguo zilikuwepo lakini angeutoa wapi muda wa kuitafuta?

Nguo ile ikamvaa lakini hakujali.

Akatoweka eneo lile huku jina Majenga likigoma kukimbia katika kumbukumbu zake.


“KONSTEBO ALIYECHOMEWA NDANI YA NYUMBA, Mengi yamejificha!”

“MAPENZI CHANZO CHA KONSTEBO KUUWAWA”

“KONSTEBO NGUZU. SI KIFO CHA KAWAIDA”

Vichwa vya habari vya magazeti matatu vilisomeka katika namna ya kutatanisha, ni nani ajihusihe na kifo cha konstebo iwe amekufa kifo cha kawaida ama ameuwawa?

Wachache sana, hata makonstebo wenzake wasingejihusisha.

Lakini vichwa hivi vya habari viliwashtua watu watatu kutoka pande tofauti lakini wawili kati yao walizungumza lugha moja huku muhusika wa tatu akiwa katika sintofahamu..

wawili wale walizungumza lugha ya biashara…

Wa kwanza kupagawa alikuwa ni Juma Kimbelembele muhariri wa gazeti la SIRI KALI, alichanganyikiwa kabisa kwa sababu ni yeye pekee aliyejiona ana umiliki wa habari kuhusu kifo cha Konstebo Nguzu kwa kuchomewa ndani huku akikihusisha na masuala ya mapenzi.

Penzi kati ya Konstebo na Inspekta Kobo.

Ajabu sasa anatazama gazeti linaizungumzia habari kwa kuhusisha yaleyale aliyoyaita siri.

Mbaya zaidi siri hii alikuwa ameiuza tayari na pesa ilikuwa ikitembea katika miradi yake mingine.

Upande wa pili, Dokta. Kobo mke wa Inspekta alikuwa anaelekea kurukwa na akili, kwa ajiri ya mume wake na familia kwa ujumla alikuwa ametokwa na pesa nyingi sana kwa ajili ya kumziba mdomo Juma ili asiandike habari zozote juu ya mume wake hasahasa skendo la kuwa kimapenzi na Koplo Zubeda.

Hata siku tatu hazijapita anaziona habari zile.

“Nimetapeliwa au?” alijiuliza akiwa katika chumba cha hoteli aliyojihifadhi mpaka pale ghadhabu zake juu ya mumewe zitakapomalizika. Alihofia kulala kitanda kimoja na mume wake ambaye amemsaliti, aliogopa sana shetani mpenda kifo asije kumwingia kichwani na kumsababisha amdunge mume wake sindano ya sumu.

Aliijua hasira yake hasahasa ambapo mumewe angejaribu kumwongopea zaidi.

Licha ya kujifaragua wakati yupo hospitali kwa Zubeda kuwa hana mapenzi ya dhati sana kwa mumewe, aliongopa na moyo wake ulilijua fika hilo.

Daktari huyu hakuwa na mahali pengine pa kuzilaza hisia zake zaidi ya kifuani kwa Inspekta Kobo.

Sasa angali anapambana mumewe asijafuliwe jina lake, tayari mambo yamekuwa kinyume.

Akanyanyua simu yake na kumpigia yule muhariri Juma aliyemfuata na kumshirikisha juu ya habari ile na kumtaka wafanye biashara.

Simu haikupokelewa.

Akatuma ujumbe mfupi ulioambatana na kitisho kikubwa.

Mmoja asiyekuwa na moja wala mbili alikuwa ni Inspekta Kobo.

Habari hii ilimfanya akayatafuta magazeti yale mara moja, akaziendea kurasa zilizoelezea kwa kina juu ya habari ile.

Akashusha pumzi kidogo baada ya kukuta jina lake halijawekwa wazi lakini mwandishi wa makala ile alionyesha kujua kila kitu ni vile hakuamua kutajha katika makala hii ili aje kuuza magazeti mengine wakati mwingine atakapoamua kulianika jina la muhusika waziwazi.

Inspekta akakumbuka kile kiwiliwili chini ya mti. Akaamini kuwa ni kiwiliwili kile kilimuona wakati anaingia na kutoka.

Yule mwandishi alijuaje nitaenda kwa Nguzu eeh! alijiuliza Inspekta huku ikimjia pia ile sauti aliyoisikia usiku ule.

Sauti ambayo si ngeni lakini alikuwa ameisahau tayari.

“Lakini sijamuua Nguzu mimi. Mungu wewe ni shahidi. Niliitafuta amani tu….. nilipanga kumuua lakini nilighairi wanishushudia mwenyezi Mungu.” Alizungumza peke yake Inspekta huku moyo wake ukiona haya kwa sababu ni mwaka mzima na miezi ilipita bila kuingia katika nyumba za ibada.

Akarejea katika magazeti yale na kusoma majina ya waandishi wa habari zile.

Akabaini kuwa zile habari zilifichwa jina la mwandishi wakaishia kufanya mazoea yao ya kuandika kuwa imeandikwa na MWANDISHI WETU.

“Attaccati a sto cazzo” Akabwatuka lile tusi pekee la kiitaliano analolifahamu huku akiyatupa yale magazeti mezani.

“Who the hell is mwandishi wetu?! eeh! kwani sisi hatujui aliyeandika habari hiyo ni mwandishi wenu you bastard!” Alilalama peke yake huku sasa akiwa wima.

Akajaribu kuwafikiria wafanyakazi wa magazetini ambao ni wasumbufu. Ambao siku hazipiti hawajapiga simu jeshi la polisi kuuliza maswali kadha wa kadha.

Akainyanyua simu yake na kupiga katika kitengo cha mawasiliano jeshi la polisi.

“Komredi, umekuwepo kwenye shifti tangu jana?” akaulizia.

“Nimekaa siku ya tano leo, mwenzangu anaumwa. Vipi afande…”

“Naulizia kama kuna simu yoyote kutoka gazeti la SIRIKALI…”

“Lile gazeti la Juma Kihwele..” akauliza kimasihara. wakacheka kidogo kwa sababu walimjua vyema.

“Yule bwabna sijui atakuwa anaumwa. Leo siku ya sita au saba hakuna simu kutoka kwake.”

Inspekta akashukuru na kukata simu.

“Huyu mjinga kuna kitu anajua, hawezi kukaa kimya siku zote hizi.” alijisemea huku akichukua kalamu yake na karatasi kisha akaainisha mambo kadhaa.

MOJA, Juma Kihwele anaijua hii habari lakini ameogopa kuiandika kwa jina lake…..

PILI, haijui hii habari lakini alivyo na kimbelembele anaifuatilia kwa kina akiandika awalipue wahusika.

Yote mawili yalimaanisha kuwa Juma ni mtu muhimu sana katika hili jambo.

Inspekta akaingia chumbani kwake, akaitoa bastola yake mafichoni na kuitazama kwa muda kisha akasema nayo.

“Let’s go to work boy! (Twend’zetu kazini)”

Simu yake ya mkononi ikaita wakati akiipachika bastola yake pahali alipozoea kuipachika.

Ilikuwa ni simu kutoka kwa mkewe…..

Mapigo ya moyo yakaenda mbio sana.

Inspekta akashukuru na kukata simu.

“Huyu mjinga kuna kitu anajua, hawezi kukaa kimya siku zote hizi.” alijisemea huku akichukua kalamu yake na karatasi kisha akaainisha mambo kadhaa.

MOJA, Juma Kihwele anaijua hii habari lakini ameogopa kuiandika kwa jina lake…..

PILI, haijui hii habari lakini alivyo na kimbelembele anaifuatilia kwa kina akiandika awalipue wahusika.

Yote mawili yalimaanisha kuwa Juma ni mtu muhimu sana katika hili jambo.

Inspekta akaingia chumbani kwake, akaitoa bastola yake mafichoni na kuitazama kwa muda kisha akasema nayo.

“Let’s go to work boy! (Twend’zetu kazini)”

Simu yake ya mkononi ikaita wakati akiipachika bastola yake pahali alipozoea kuipachika.

Ilikuwa ni simu kutoka kwa mkewe…..

Mapigo ya moyo yakaenda mbio sana.

Akaipokea ile simu huku akiwa anatetemeka mikono yake katika namna iliyomtishia amani.

Alipoiweka simu sikioni kimya kikatanda kutoka upande wa pili.

“Mama! Mama! Mke wangu… ongea basi mama.” alizungumza kwa upole wa hali ya juu.

Badala ya kujibiwa akaanza kusikia pumzi zikipishana kwa kasi sana na hapo akaanza kukisikia kilio.

Dokta Kobo alikuwa analia.

Suala la mkewe kuangua kilio ikawa kama msumari wenye ncha kali unasukumwa katika paja lake angali ana fahamu zote.

Maumivu!

“Mama Melinda! una nini mke wangu nieleze… au niambie basi upo wapi nije sasa hivi.” Alisihi Inspekta Kobo lakini simu ikakatwa bila kusikia neno lolote.

Akapagawa.


SHAMALIWA, Mwanza.

Umati wa watu haukuwa mkubwa sana. Walikuwa ni wanafamilia walioridhia ile taarifa ya kifo cha ndugu yao.

Mama mzazi wa Nguzu hakuisha kulia na kulalamika kuwa alimkanya mwanaye asijiunge na jeshi lakini hapohapo akikiri kuwa ugumu wa maisha ulikuwa chanzo cha yote hayo.

Waliojaribu kumbembeleza walikuwa wamefikia kikomo na sasa walimwacha alie kuzimia na kisha kuzinduka peke yake.

Kuzika majivu! Mama yake alikataa kata kata, alidai kuwa hakuyaaga majivu katika kituo cha basi bali alimuaga mwanaye tena kwa kumkumbatia, leo hii akubali kuyazika majivu asiyoyajua?

Hapana… akasimama kidete na wanafamilia wakamuunga mkono, hawakufanya maziko hayo.

Ambaye aliamini Martin Nguzu amefariki sawa, ambaye hakuamini sawa.

Mama Martin hakuwa katika upande wa walioamini.

Na kila alipojaribu kuamini, lilikuja wazo jingine kuwa yawezekana mwanaye amefanyiwa ubaya tu. Sio kifo cha kawaida.

Ndivyo walivyo akinamama.

Ule uchungu wa mwana unasababisha haya.

Siku ya tano ikiwa inayoyoma na jambo hililikiwa limepunguza makali mioyoni mwa wengine kasoro mama mtu.

Majira ya usiku ule uliingia ugeni ambao hakuna aliyeutilia maanani, maana kwa kipindi hicho watu walikuwa wanakaa nje, ndugu na jamaa wanacheza mchezo wa karata mpaka usiku wa manane na wengine kulala nje kabisa.

Huyu bwana alikuwa mkimya kabisa na koti lake kubwa la kuzuia baridi, alijitikisa kwa sababu za msingi tu na hakugeuka huku wala kule, alikuwa amejiinamia.

Kadri muda ulivyozidi kwenda na watu walizidi kupungua, wengi walienda kulala.

Huu nd’o muda ambao yule bwana alijitikisa tena kwa kiasi kikubwa.

Alisimama!

Akapiga hatua kadhaa bila mtu yeyote kumtilia mashaka, akasogea pembezoni akaichomoa pakti ya sigara na kutoa moja, akaiwasha na kuuvuta moshi wake ndani ya kifua chake na kwa umaridadi kabisa akaupuliza angani kisha akautazama unavyotokomea angani.

Akafanya vile takribani mara tatu, kisha akaizima. Akapiga hatua nyingine tena akaufikia mti kisha akaanza kuyatazama mazingira ya pale kwa uchache akahisi ni wakati muafaka wa kufanya kusudio lake na hakuona jambo lolote la kumzuia.

Akapiga hatua huku mkono wake ukiwa katika mifuko yake, akajipitisha jirani kabisa na kundi la akina mama wawili waliokuwa wamejilaza.

Akamwona muhusika wake.

“Ndiye!” akajisemea.

Kisha kwa kitendo cha upesi sana akainama, akamziba mdomo na kisha akaichomoa silaha yake na kwa lugha ya vitendo akazungumza naye.

“Ukileta vurugu nitakuchinja.”

Huku akiwa amemdhibiti vyema kabisa akamnyanyua wakaondoka kutoka katika eneo lile.

Alipomfikisha pembeni kiasi akampiga teke kali miguuni, kisha akatua naye chini.

“Mzee Majenga anaishi wapi?” lilikuwa swali kavu kabisa kutoka katika sura ngumu.

Mama akabaki kuhangaika asijue ni nini hiki kinatokea angali ana kovu la msiba wa mwanaye wanatokea watu kumuuliza juu ya mzee Majenga.

“Alihamia Shinyanga.” alijibu kwa ufupi.

“Nitakuua sina masihara. Alihamia lini na awali alikuwa ana anishi wapi? nani ndugu zake?” Alijaza maswali mazito.

“Kama mwanangu mmemchoma moto, ukinichinja hautakuwa umefanya dhambi mpya. Nipeleke kwa mwanangu, sina jibu jingine….” Alijibu kikaidi. Huku nafsi yake ikiwa radhi kabisa yule bwana amuue ili aondokane na huu uchungu wa kuishi bila mwanaye.

Mkono wenye nguvu ukashusha ngumi katika bega la yule mama kisha kiganja kikawahi kuziba mdomo.

Maumivu yakanyimwa kilio.

Yule mama akabaki kuhema juu juu huku akiwa ameyakodoa macho yake.

“Sasa utanijibu vizuri kabisa sivyo. Mzee Ma…” hakuweza kumalizia akahisi kuna mguso fulani kwa mbali katika bega lake.

Akageuka bila hofu yoyote, akakutana na giza likiwa ndani ya giza.

Lakini hili halikuwa giza ambalo linaweza kutembea.

Ngumi kali ikatokea katika lile giza la maajabu, ngumi moja ikatua katika koo la yule bwana.

Akajaribu kukohoa akawa ameikohoa roho yake. Umauti ukamfika.

“Mama!” giza lile likaita.

Mama aliyekuwa anahema juu juu huku akiwa anafanya dua maalumu kwa ajili ya kuiaga dunia akarejea katika fahamu zake.

Haikujalisha giza lile lilikuwa totoro kiasi gani, mama alitambua ubini wake ipasavyo.

“Martin!” akaita.

“Nipo hai mama.” akajibiwa.

Mama akaamka akaketi kitako asiamini kuwa alikuwa anapokea miujiza katika uzee wake.

Ubaya wa wanawake siku zote ni pale akili zao zikitulia.

Mwanzo alikuwa ametulia tuli akizungumza na lile giza, lakini baada ya akili kukaa sawa akaanza kupiga mayowe.

Mkono ukawahi kumziba mdomo.

“Mama, huyu alikuwa anataka nini kwako.”

“Simjui.”

“Mama, sijauliza kama unamjua. Alikuwa anataka nini?”

“Muulize labda wewe atakueleza vizuri.”

“Hakuna mzoga uliowahi kuzungumza katika dunai hii mama. Nieleze..”

“Amemuulizia mzee Majenga…. yule mzee alikuwa rafiki sana na babu yako. Wewe humjui…” alitoa maelezo yale.

Majenga!

Jina lile likapiga katika kichwa chake kwa kujirudiarudia, ni jina hili lilimjia punde tu baada ya kurejewa na fahamu asijue nani aliliingiza katika kichwa chake.

“Uliponaje mwanangu, nyumba iliteketea yote ile. Tuliona kwenye Televisheni..” mama alimuuliza.

“Mama usimwambie mtu yeyote kama umeonana na mimi, mimi nipo hai na ninaamini nina kazi kubwa ya kufanya kabla sijasimama hadharani na kuutangazia uma kuwa ninaishi.” Alisihi Nguzu. Kisha akamkumbatia mama yake na kumbusu shavuni.

Upesi mama akaipapasa shingo ya nguzu katika giza lilelile.

Na hapo akatokwa na tabasamu pana lililosindikizwa na machozi ya furaha.

Aliyekuwa mbvele yake alikuwa yuleyule mtoto aliyetoka katika tumbo lake.

Martin Nguzu!

Ameponaje? hilo halikuwa swali lililomuhangaisha……

Bora uzima.

Walizungumza kwa dakika kadhaa kuhusu Majenga kisha wakaagana.

Akiwa anafanana na giza kwa jinsi alivyovaa alitembea kwa tahadhari kubwa huku akiamini wapo wengine wanaweza kuvaa kama yeye na kufanana na giza, akapiga hatua na kutoweka eneo lile.

Begani akiwa na mzoga wake…


LILIANZA tumbo la kuhara, kila akiingia chooni linapoa anarejea chumbani. Linaanza tena anakimbilia chooni, linapoa.

Alikuwa amechanganyikiwa mno.

Hali hii ikamkumbusha kuwa angali akiwa mwanafunzi alikuwa anaugua haswa akisikia kuwa kuna bakora kwa ajiri ya wachelewaji ama ambao hawajafanya vyema kazi waliyoachiwa. Hivyo alikuwa mstari wa mbele kabisa kufanya kazi zote ipasavyo, kuheshimu sheria na kanuni za shule.

Na hata ilipotokea migomo hakutaka kushiriki, wenzake wakambeza na kumweka katika kundi la wanafunzi waitwao ‘MBWA WAOGA’ shuleni.

Alikuwa tayari kuitwa majina yale lakini alitambua kuwa anaitii sheria vyema.

Akaishi hivyo na akakua hivyo.

Akiwa katika utu uzima wake ana familia na yupo kazini, anajaribu kuisahau asili yake anaitaka pesa nyingi kwa njia zisizokuwa halali. Jaribio lake la kwanza linakuwa kuuza habari aliyoinasa mahali.

Kabla mchezo haujanoga anajikuta matatani.

Akatamani nyakati zirudi nyuma kidogo tu asijihusishe na hili jambo asilani. Lakini ni saa pekee inaweza kurudi nyuma na si wakati.

Juma Kihwele alikuwa amekamatika.

Akafikiria mtu wa karibu yake wa kuweza kumshirikisha hilo jambo, hasahasa ujumbe kutoka kwa Dokta. Kobo uliomfanya kupata tumbo la kuhara ghafla.

Mkewe, hapa asingethubutu kugusa hata kidogo kwa sababu tayari alikuwa amemwonya kuachana na masuala ya kufuatilia habari zisizomuhusu.

Akafikilia kukimbilia msikitini walau amweleze kiongozi wake wa dini. Huku napo akaona pagumu kuingilika, maana huku ni mambo kunyooshwa tu hakuna kona kona.

Kila sehemu aliyoiwaza akaona haiingiiliki.

Mwisho akajiwekea maamuzi ambayo aliyapa jina la ‘NANI ATAMFUNGA PAKA KENGELE’

Katika maamuzi haya yeye alikuwa panya.

Akawavika vyeo vya U-paka Inspekta na mkewe.

Kisha akamchagua inspekta Kobo kwa kujipa imani kuwa yule ni mwanaume mwenzake hivyo watazungumza na yatamalizika tu.

Akaingia bafuni akausafisha mwili wake, akavalia nadhifu kisha akaamua kujihukumu. Akachukua simu yake na kuipekua nambari za Inspekta Kobo. Akajihisi kutetemeka wakati anapiga simu ile.

Kitetemeshi kikaisha alipogundua kuwa simu ile haipatikani. Akachukua maamuzi ya kumpigia Koplo Mtani yule aliyemsababisha akajiingiza katika mchezo huu asioujua. Lakini maamuzi yake yakayeyuka baada ya kujiona kuwa atakuwa anawaingiza watu wengi katika hili jambo aliloliita kuwa ni maongezi ya kiume dhidi ya Inspekta Kobo.

Kwa sababu alipajua ofisini kwake akaamua kwenda kimyakimya wakayamalize.

Akatoka na kuingia katika gari yake, akaitazama tasbihi iliyokuwa inaning’inia katika kioo cha ndani cha gari lake.

Kisha akawasha gari na kuondoka zake.

Baada ya dakika moja, gari jingine dogo likatoweka na kumfungia tela.

Hakujua kuwa wakati anawaza kumfunga paka kengele na wengine waliwaza hivyohivyo juu yake.

Kwa wakati mmoja Juma ‘kimbelembele’ alikuwa panya na hapohapo paka.

Kiumbe wa ajabu kupindukia!

Aliiendesha gari yake kwa utulivu huku kila mara akijilaumu nafsi yake kwa tamaa za ajabu ajabu.

“Tazama nimejenga nyumba nzuri kabisa, hata kama sijahamia bado lakini nina uhakika wa kuhamia siku yoyote, nina gari na nimekaribia kumnunulia mkewangu la kwake, nina amani ya nafsi, mtoto wangu anaishi vizuri kabisa, anasoma shule nzuri. Hiki nini kiliniingilia kichwani nikapatwa na tamaa mimi lakini, eeh! Ninaheshimika ofisini, bosi ananipandishia mshahara kila leo. Ni kipi nilitaka tena Juma mimi. Yaani shuleni waliponiita kimbelembele nilichukia na kuwaona hawanipendi, sasa najionea mwenyewe. Ona sasa naanza kuhangaika na kimbelembele changu, mtu mwenyewe Inspekta unakuta ana hasira zake huko anipige mabuti, mi kupigana sijui, jeshi lenyewe sijapitia….. Hivi Juma nilikuwaje mimi eeh!” alilalamika kwa sauti ya chini, malalamiko yaliyopelekea machozi kuanza kumbubujika.

Akashindwa kuona mbele vizuri, akaamua kuegesha gari lake kando.

Akajifuta machozi. Akaitazama simu yake na kugundua kuwa ilikuwa inaita pasi na kutoa mlio.

Akakumbuka aliiweka simu yake iwe katika hali ile. Akaishika kwa utulivu na kutazama. Ni mkewe alikuwa amempigia.

Akampigia kuuliza kulikoni.

“Mume wangu naomba urudi nyumbani muda huu, sasa hivi mume wangu… atawaua watoto huyu. Njoo mume wangu…” Alizungumza huku amepagawa mno mke wa Juma.

Simu ikakatwa bila kusubiri majibu kutoka upande wa pili.

Lile tumbo la kuhara lililosumbua kuanzia akiwa nyumbani likayasikia mazungumzo haya, kwa kirehere cha hali ya juu likatamani kusikia zaidi.

Likatoa wawakilishi palepale akiwa ameketi katika kiti chake cha gari….

Hali ya hewa ikachafuka…

“YAKIMBIZE maisha ama la acha maisha YAKUKIMBIZE. Uchaguzi ni wako siku zote…”

ALIBAKI katika mzubao kama mwanaume aliyemwona mwanadada mwenye mvuto akijongea kwenda upande wake akajilaghai katika kichwa chake kuwa amekutana na bahati ya mtende akajiandaa kumpokea, kisha mrembo yule anatokwa na neno la ghafla.

“Kaka umesahau kufunga zipu yako..”

Mzubao huo ulimkumba Juma Kihwele, alipotoka katika mzubao akahamia katika mlowano katika suruali yake.

Chozi likamtoka alipotambua kuwa haikuwa ndoto bali alikuwa kama anavyojiona.

Mbele na nyuma palikuwa pameshirikiana kumfedhehesha.

Ubahili akauweka kando, kabla harufu ile haijawafikia wasiohusika Juma Kihwele akapandisha vioo vya gari lake kisha akawasha kiyoyozi.

Alitambua wazi kuwa kiyoyozi hakitakuwa na msaada mkubwa lakini walau linatimia lile neno la ‘Mchuma janga hula na wa kwao’ kwanini yeye ale na wasiomuhusu?

Acha ale na kiyoyozi….

Akaigeuza gari kwa kasi akiwa ametaharuki.

Akawa amebadilisha uelekeo na kuelekea alipokuwa ametoka.

Jambo lile likawa na maana nyingine kwa waliomtazama…


KITENDO kile cha kubadilisha uelekeo kikawashtua wale waliokuwa katika gari iliyokuwa ikimfuatilia toka alivyoliacha geti la nyumbani kwake.

Dereva akabweka na kuwashtua wenzake, wote hawakuamini walipoiona gari ile ikiondoka kwa mwendo mkali. Kila mmoja akabaki kumlaumu mwenzake kwa kuukosa umakini.

Lawama zisingekuwa na msaada wowote dereva akapambana naye kutafuta njia ya kugeuza gari ili afukuzane na lindo lao walilolivizia kuanzia linatoka nyumbani

Sasa lindo limewatoroka ghafla. Wakabaki kujiuliza ni wapi ambapo waliteleza hadi yule bwana akawaona….

Swali hili likawafanya waanze kuamini kuwa bwana Juma ana watu wengi nyuma yake ambao wanamsaidia katika suala la ulinzi.

Hapa wakaongeza umakini na ile hali ya kumchukulia Juma kama mwandishi asiyekuwa na tahadhari katika maisha yake ikatoweka.

Hawakujua kuwa Juma Kihwele alikuwa amevurugwa vibaya mno, na hata ule mwendo kasi wa ghafla ulikuja ghafla kama ulivyoonekana na hakujua kama alikuwa anafuatiliwa.

JUMA aliwasili nyumbani, bila kujali kuwa alikuwa amechafua nguo yake alishuka upesi na kuingia ndani ya nyumba yake huku akiwa amenyoosha mikono yake juu kama namna ya kujisalimisha ili wavamizi wakijitokeza kwa nia ya kushambulia basi awe amejitetea tayari kuwa hana madhara yoyote kwao.

Huenda wataingiwa na huruma juu yake.

Hicho nd’o kitu pekee alichoweza kufanya kwa wakati ule.

Alilivuka geti lake huku akijilaumu kwa ubahili wake uliokithiri wa kushindwa kumlipa mlinzi ili awe analinda masaa ishirini na nne badala yake akaona usiku nd’o wakati pekee wenye hatari akaamua kulipia masaa kumi na mawili.

“Mlinzi mwenyewe analinda na rungu?” Alitoa kauli ya kupuuzia majuto yake.

Alitembea hatua kwa hatua hadi akaufikia mlango wa kuingilia ndani ya nyumba yake akabaini kuwa ulikuwa umefungwa kwa nje.

Bila shaka mvamizi yupo nje.

Huku akiwa anatetemeka akaufungua ule mlango, akaikuta familia yake yote ikiwa inatazama ukutani. Mama mwana pamoja na shemeji yake aliyekuwa pale kwa ajili ya likizo.

“Jamani…. kuna nini mke wangu?” Akamuuliza, mkewe akageuka huku akiwa anatetemeka na asiamini kuwa aliyesema naye alikuwa ni mumewe.

Akaanza kuangua kilio huku yote anayoyasema yasisikike vyema kiasi cha Juma kuanza kumkaripia kuwa anapaswa kuzungumza kwa utulivu ili wajue ni kitu gani kinaendelea.

“Ni nani alivamia hapa na kukueleza upige simu.”

“Simjui, sijawahi kumwona hata siku moja.”

“Anafananaje? na ni kitu gani anataka kwangu…”

Mkewe akamsogelea Juma na kumkumbatia, hakuwa na sababu nyingine ya kumkumbatia bali kumsihi waende chumbani.

“Hapana… tuzungumze hili jambo kwanza tuelewe muafaka!” alipinga vikali.

Mke akamsogelea tena na safari hii akamueleza ukweli kuwa alikuwa ananuka, anapaswa kwenda kusafisha mwili wake kwanza.

Akili ya Juma ikaingiwa na mchecheto, akatembea kinyonge kabisa kuelekea chumbani.


NJE ya nyumba ya Juma wale waliokuwa wakimfungia tela walikuwa wamewasili tayari na waliegesha gari lao mbali na nyumba yake. Walikuwa watatu na walitembea kama wasiofahamiana katika suala hili. Kila mmoja alijiweka katika shughuli zake, ilimradi iwe ngumu kujulikana kuwa kuna jambo wanafuatilia.

Umakini wa sasa ulikuwa umezidi wa awali ambapo walimchukulia Juma kirahisi sana. Sasa walikuwa makini kana kwamba wanapambana na adui mwenye hatari sana zaidi yao.

Silaha zao ziliwekwa tayari tayari.

Jicho moja pevu lilikuwa katika kona ngumu kufikika, lilikuwa limewapokea kuanzia walipowasili awali, wakamfungia tela Juma akiwashuhudia. Kisha akatengeneza vamizi la kumrejesha Juma nyumbani bila maafa yoyote, ili aendelee kuwasoma watu wanaomfuatilia Juma.

Akaivamia nyumba na kutoa kitisho kikali.

Zoezi likafanikiwa Juma amerejea na wao wamerejea.

Ni akina nani hawa? na wanataka nini kwa Juma? haya yalikuwa maswali ambayo yalihitaji kupatiwa majibu upesi sana kabla naye hajajua ni kitu gani anaweza kufanya katika mchakato huu.

Aliitoa taarifa hii ya mashaka yake juu ya watu anaowaona eneo hilo, taarifa ikapokelewa huku akisisitizwa kuwa makini zaidi.

Masaa yalizidi kwenda bila kuona juhudi za watu wale kuingia ndani ya nyumba ya Juma, walibaki kurandaranda huku na kule bila kujua kuwa wanafuatiliwa.

Kwa kuwatazama jinsi walivyokuwa wanatembea na kufanya mawasiliano alihisi yawezekana ni askari waliopo kazini, ama waliopoteza kazi zao, na kama si maaskari basi yawezekana waliwahi kupata mafunzo ya kijeshi kwa sababu maalumu.

Akajinyoosha kidogo mwili wake na kujipima ikiwa anaweza kukabiliana na vijana wale.

Wakati anajinyoosha akabaki kujicheka kuwa anauhangaisha mwili wake wa nini wakati ana kijana wake wa kazi ambaye kamwe hazeeki.

bastola kiunoni!

Majira ya saa tatu usiku akapiga hatua na kujichanganya barabarani, na hapohapo akageuka muigizaji, akazuga kuwa amelewa na anayumbayumba.

Lengo lake likiwa kumfikia mmoja kati ya wale vijana.

Akafanikiwa kupita jirani na kijana mmoja, akajikuta akicheka ndani ya moyo wake alipotambua kuwa hata kijana yule naye alikuwa katika fani ya maigizo na alikuwa yu katika kitengo cha kuigiza kuwa ni kijana anayetumia madawa ya kulevya na sasa ametulia tuli baada ya kujidunga.

Safi! akajisemea kisha akamchokoza.

Akamsema maneno yanayoudhi huku akiendelea kujiweka katika hali ileile ya ulevi.

Yule bwana hakujibu kitu badala yake aliendelea kuwa mtulivu.

Wakati wote huu alipokuwa anamfanyia bughudha katika sikio lake alikuwa na kifaa kidogo kilichokuwa kinatumika kwa ajiri ya mawasiliano.

Yule bwana aliyekuwa amejiweka kama mtumiaji wa madawa ya kulevya hatimaye alinyanyua kichwa chake na kumtazama huyu mlevi kwa chati jinsi alivyokuwa anahangaika kumchokoza.

“Naomba uondoke hapa.” alizungumza maneno machache kisha akainama.

Mlevi akaanza kucheka huku akidiriki kumzongazonga yule bwana, alifanya vile kwa sababu alijiamini kuwa yule bwana hana ubavu walau wa kuingiza hata ngumi moja katika mwili wake iwapo watakusudia kutupiana makonde na hata akifanikiwa kutupa konde halitamletea athari.

“Naomba uniache uondoke hapa wewe mlevi.” alisisitiza. Lakini yule mlevi bado aliendelea kuwa pale. Mara atukane hivi mara aimbe vile.

Bwana aliyeketi akazidiwa na kero zile, akasimama wima na kumrushia ngumi kali yule mlevi, mlevi akaikwepa bila kujibu pigo.

Kukwepwa kule kukamfanya awe makini zaidi na yule mlevi. Macho yakamkagua haraharaka huku wakitazamana kama majogoo.

Akajaribu kurusha teke, mlevi akakwepa.

Wakati yule mlevi anakwepa teke lile, yule bwana aliyekuwa akikabiliana naye akaona kitu kilichomtisha.

Aliiona bastola.

Na hapohapo akazungumza maneno yaliyomchanganya yule bwana mlevi wa kuigiza.

“Angusha mbuyu kuna nyoka.”

Maneno yale yakasafiri upesi katika akili ya yule mlevi wa kuigiza, akajaribu kuyafanyia kazi upesi lakini hakuweza kupata maamuzi sahihi.

Jicho likamtazama mlevi yule kutokea mbali kabisa katika kifaa maalumu, mlango wa chuma ukafunguliwa kisha mwanga ukatoka bila mlio wowote, mwanga ukasafiri kwa kasi kubwa na kisha ukaweka makazi ya muda katika kifua cha yule mlevi wa kuigiza.

Akatokwa na yowe kidogo kisha akaanza kujitupa huku na kule. Maneno aliyoongea hayakuwa nyoofu akaamua kunyamaza huku damu ikimtiririka.

Yule bwana aliyekuwa ameweka kambi chini ya mti ule akampekua na kutoa bunduki katika kiuno chake.

“Zahoro! huyu mjinga alikuwa na bunduki, huyu hakuwa mlevi aisee. Katumwa huyu hakutakiwa kuuwawa…… dah!” alizungumza kwa kutumia kifaa kilichokuwa sikioni.

Maneno yale aliyozungumza yakapita moja kwa moja kwenda mahali ambapo hawakutaka yafike. Na hawakujua kama yanavuka mipaka hiyo.

Yule bwana marehemu alikuwa akiwasiliana na mtu mwingine kabla hajauwawa. Hivyo alisikia yote hadi mwisho.


INSPEKTA KOBO akachanganyikiwa upya, hii ni baada ya kuyasikia maneno yaliyozungumzwa katika kifaa kilichokuwa sikioni mwa kijana wake aliyemtuma kufuatilia mienendo ya Juma Kihwele.

Alisikia sauti yake wakati akitapatapa na mwisho akaisikia ile sauti ya mtu aliyekuwanaye.

“Ni akina nani hawa?” alijiuliza huku aking’ata vidole vyake baada ya kukiri kuwa kuna watu hatari katika sakata hili ambalo kwa namna yoyote ile linaelekea kumwangukia na kumzika kabisa.

Kijana wake alikuwa ameuwawa!

“Angusha mbuyu kuna nyoka…” Hii sauti ikawa inajirudia katika kichwa chake. Ni kama aliwahi kusikia mahali…

“Yeees!” akarusha ngumi hewani, alikuwa amekumbuka kuwa sauti ile aliisikia usiku ule alipokwenda kwa Nguzu kwa ajili ya kumsihi aachane na Zubeda wake na alipoondoka nyumba ile ikachomwa moto na kuaminika kuwa imeondoka na uhai wa Nguzu.

“Huyu ni nani lakini? na kwanini wamchomee kijana wa watu ndani eeh!” akawaza na kuwazua kisha akaamua kutoka nje.

Akaingia katika gari yake na kunyoosha moja kwa moja hadi hospitali aliyokuwa amelazwa Zubeda. Akaingia moja kwa moja katika kile chumba kile ambacho alikuwa amekiwekea walinzi wa siri hasahasa baada ya mkewe kuingia mle ndani na kumuhoji Zubeda mambo mazito.

“Zubeda kila kitu kimeharibika na mambo yanazidi kuharibika, huu sio wakati wa kuzungumzia kilichotokea hapo katikati, huenda hicho kina unafuu. Naomba usikilize hii sauti kwa umakini na unieleze kama umewahi kuisikia… naomba usinifiche hata kama umeisikia katika mazingira ambayo haupendi mimi niyafahamu.”

Akamwinamia na kumwekea kifaa sikioni kisha akakiwasha kile kifaa, Zubeda akaisikia sauti ya yule mwanaume ikizungumza yote iliyozungumza.

Koplo Zubeda akatikisa kichwa kuwa hakuna anachokielewa. Inspekta Kobo akashusha pumzi zake kwa juhudi zote, mambo yalikuwa yanazidi kuwa magumu.

“Vipi kuhusu Zahoro? unalifahamu hili jina?”

“Nawafahamu Zahoro kadhaa, ila sina ukaribu nao.”

“Kuna mjinga anaitwa Zahooro nahisi amemuua kijana wangu.” alizungumza kwa uchungu Inspekta huku akitazama juu.

Na alipoushusha uso wake alizungumza na Zubeda.

“Hautaendelea kulalia hiki kitanda, kuna watu wanaisaka roho yako wakati huu. Hakuna ninayemuamini kukulinda, nataka nikulinde mimi mwenyewe.” Inspekta akanong’ona kwa hisia kali huku akiwa anamtazama Zubeda moja kwa moja machoni. Kabla Zubeda hajasema lolote Inspekta akaendelea, “Mke wangu ana hasira sana najua, lakini si sababu ya mimi kukuacha wewe katika hali isiyokuwa salama. Yameniumiza mengi katika hii dunia ya mapambano, nitajitonesha upya nikishuhudia maiti yako”

“Mlinde zaidi mkeo…” Zubeda akaingilia kati katika hilo.

“Yupo katika ulinzi wa hali ya juu.” Alijibu Inspekta na hakutaka maongezi yaendelee, akatoweka kwa ajili ya kufanya hatua zote za kumwondoa Zubeda katika hospitali ile.

Zoezi likafanikiwa.


KUKUTWA ametupwa mtaroni?

Tena akiwa hana jeraha bali alama moja tu katika shingo lake…

Pigo la aina gani hii?

Nani alitoa pigo hilo barabara!

Haya yalikuwa maswali mfululizo yaliyopita katika kichwa cha kiongozi wa oparesheni isiyokuwa na jina rasmi. Hii ni baada ya kupokea taarifa kutoka jijini Mwanza kuwa kijana wake anayemuamini kupindukia alikuwa ameuwawa kwa kupigwa pigo moja kali kabisa shingoni.

Tabasamu hafifu lilimdondoka wakati anajaribu kufikiria upya juu ya jambo hili.

Akanyanyua mkonga wa simu yake, akataka kupiga mahali akaghairi na kubaki akielea katika mzani wa maamuzi.

Akaushusha ule mkonga na kunyanyua simu yake ya mkononi. Akabofya nambari zilizokuwa zimetoka kumpatia taarifa kutoka jijini Mwanza.

“Kwa hiyo umesema hakuna sehemu nyingine aliyojeruhiwa? Je ujumbe wowote kwa ajili yetu?” akatulia na kusikilizia upande wa pili ukijibu. Baada ya majibu akazungumza kwa ukali kidogo.

“Ongea na Cheyo, aamrishe askari wake wazunguke kila kona hapo Shamaliwa wakamate vibaka wote wanaorandaranda kijinga jinga mitaani. Wawabane watasema kama waliona hilo tukio. Mwambie asiache mtu hata mmoja.”

Waliendelea kuzungumza kwa sekunde kadhaa kisha simu ikakatwa.

Jijini Mwanza baada ya masaa mawili eneo la Shamaliwa nje kidogo ya jiji hapakuwa mahali salama hata kidogo, ukizurura unakamatwa, ukikaa unakamatwa ukicheka unakamatwa ukilia unakamatwa.

Hadi waliokutwa wanakata majani ya ng’ombe nao walikamatwa.

Kamata kamata ile ikazua jambo juu ya jambo


KONSTEBO MARTIN NGUZU alikuwa anajaribu kuutafuta usingizi katika kitanda ambacho kilitawaliwa na kunguni waliokuwa na maksudi mabaya, taa ikiwashwa wanatoweka na ikizimwa wanaingia uwanjani kuinyonya damu ya Nguzu.

Mchezo huu wa kunguni wale ukawa kikwazo kikubwa kabisa kwake. Lakini hakuwa na yeyote wa kumlaumu kwa sababu alikusudia kujihifadhi katika nyumba ile ambayo lingetokea lolote lile angeweza kupiga ngumi moja pamoja na teke kisha dirisha likahama pahali pake na kuacha njia.

Bughudha hii ikamnyanyua mpaka nje, akazurura huku na kule pasi na uelekeo maalumu.

Katika kuzurura huku akaona haitakuwa jambo la heri kuzurura huku kichwa chake kingali wazi.

Akafanya tathmini ya muda mfupi huku akijishangaa namna ambavyo yu hai, lakini zaidi zilikuwa ni hisia mpya zinazokisumbua kichwa chake.

Majina mapya na mtazamo mpya katika fikra zake, jina Majenga lilikuwa la kwanza kabisa kujenga naye urafiki.

Sanjari na jina hili kuna ndoto ambazo zimekuwa zikimfuata bila kukoma, mara amuote mama yake mzazi na alipoifuata ndoto ile na kurejea jijini Mwanza anamkuta mama yake akiwa mikononi mwa mtu mbaya.

Anatokwa na pigo moja, pigo lililomwangusha yule bwana moja kwa moja.

Kuhusu lile pigo akajiuliza upya, ni lini amekuwa na uwezo wa kuangusha mtu kwa ngumi moja pekee?

Jibu lilikuwa rahisi sana kuwa hakuwahi kuwa na uwezo huo hapo kabla.

Utata mwingine uliomsumbua ni kuhusu magazeti yaliyoandika kuhusu kifo chake.

Kifo gani? Alijiuliza, lakini swali hili halikumshtua hata kidogo.

Kufa si jambo dogo ujue? alijisemea huku akiendelea kuzurura.

Hata tukio la kukuta pesa katika nguo aliyoianua katika kamba usiku ule baada ya kujinasua katika kifusi katika nyumba iliyokuwa imeanguka bado kilimtatanisha.

“Nani wa kusahau pesa katika nguo ndani ya jiji la Dar es salaam!!” alijisemea na kujikuta akitokwa na tabasamu kubwa sana kulikumbuka jiji lile na vituko vyake.

“Mzee Majenga kuna kitu anapaswa kunieleza, sidhani kama nipo kawaida.” aliweka hitimisho lile.

Wakati anarejea katika chumba chake akaanza kumuwaza tena mama yake mzazi.

Nini kinatokea? alijiuliza huku hofu ikianza kumwingia.

Hakutaka kupuuzia hii hisia iliyomjia ghafla, akajiahidi kuwa siku inayofuata atalazimika kurejea jijini Mwanza.

Akarejea katika kile chumba chenye kunguni wapenda sifa. Akajilaza na kusinzia.

Alfajiri ilimkuta barabarani, akadandia gari na kurejea jijini Mwanza.

Ilikuwa kama hisia zake zilivyomuelekeza, alipoingia jijini Mwanza hata kabla hajajikita katika upelelezi wa chinichini akatambua juu ya kamakakamata ya wakazi wa Shamaliwa nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Akajipeleka Shamaliwa kuhakikisha tu!

Mama yake alikuwa mojawapo kati ya watu waliokuwa mikononi mwa polisi.

Cheko la hasira likamponyoka, akatembea hadi katika kituo cha mabasi akajiweka katika basi ndogo iliyokuwa inafanya safari zake kuelekea Nyegezi. Akatulia katika nafasi iliyokuwa wazi. Mkononi akiwa na pesa kamili kwa malipo ya nauli ya kutoka Shamaliwa hadi Mabatini.

Alishuka mbali kidogo na kutembea kwa miguu taratibu hadi zilizopokuwa nyumba za polisi. Nyumba zilezile alizoishi pale miaka kadhaa nyuma.

Nyumba zile zikaikamata akili yake, akaukumbuka ule ugomvi kati ya Janeth ambaye baadaye alibadili jina na kuitwa Zubeda jinsi alivyokwidana na mke wa inspekta na mwisho kujikuta akitupwa rumande kwa siku kadhaa.

Kumbukumbu zaidi za kumwandalia binti yule kifungua kinywa zikamfanya ayakumbuke mapenzi yao motomoto baada ya kukutana jijini Dar es salaam huku Zubeda akiwa ni Koplo na yeye akisalia katika nafasi yake ya ukonstebo.

Tabasamu liliunda kibanda katika uso wa Martin, akatembea upesiupesi hadi katika nyumba mojawapo akaitazama kwa sekunde kadhaa, kisha akapita kwa kasi akaelekea nyumba nyingine, hii nayo akaitazama upesi upesi.

Akafanya vivyo hivyo katika nyumba nane. Baada ya kuridhika kuwa alikuwa makini kabisa kwa kila hatua aliyopita katika makazi yale pasi na mtu kumshtukia akaamua kuzua balaa alilopanga kulizua.

Lilikuwa balaa haswa!

MARTIN Nguzu hakuwa mgeni eneo lile la kota za polisi Mabatini, hivyo hata sasa hakutembea eneo lile kama mgeni.

Udhaifu wa ulinzi aliufahamu vyema na uwepo wa kiwanja cha mpira katika maeneo yale ya kota yalisababisha iwe ngumu sana kwa mtu kupatwa na hisia zozote za kutisha juu ya ugeni wa hapo kota.

Nguzu alilifikia upesi eneo alilohitaji kufikia kisha akatazama kama kuna mabadiliko.

Hapakuwa na mabadiliko ya aina yoyote ile, akatabasamu na kujiwekea alama za ushindi waziwazi.

Majira ya usiku wa saa mbili akarejea eneo lile kwa ajili ya kutekeleza agano lake la kuhakikisha kuwa mama yake anakuwa huru kwa namna yoyote ile.

Wakati huo alikuwa ameanza kupata majibu kuwa mtihani uliopo mbele yake haukuwa mdogo hata nukta.

Mfumo wa umeme eneo la kota ya polisi Mabatini ulikuwa mbovu kupindukia, nyaya za umeme zilipita chini kwa chini katika namna iliyotia kero kutazama.

Wazazi wenye watoto nd’o walijitahidi kupigia kelele hili suala lakini majibu yalikuwa yaleayale ya siku zote.

“Kilio chenu kimesikilizwa!”

Hiki kilio kikaenda miaka nenda rudi huku kikigeuka kuwa kichekesho na si kilio tena.

Hakuna jema lililoboreshwa.

Kama nyumba zenyewe zinatia kichefuchefu vipi kuhusu huo umeme??

Nguzu aliikuta hii hali katika safari yake ya kutoka kuzimu na kurejea tena duniani na sasa yupo katika ile ardhi aliyozaliwa miaka mingi iliyopita.

Zile kota za polisi alizoziona angali akiwa anasoma, sasa hazitamaniki zinazidi kukera kuzitazama.

Anarejea katika anga zile kwa sababu maalumu.

Anatazama pande zote na kuzichimua kwa umakini zile waya. Akautazama uelekeo na kuchagua dakika ya kufanya balaa alilopanga kulifanya.

Akazihesabu dakika akachuchumaa kisha akaziachanisha nyaya kadhaa.

Giza likaingia katika eneo lile ghafla.

Sauti za manung’uniko zikasikika huku na kule.

Manung’uniko yale hayakudumu kabla Nguzu hajazua taharuki kubwa.

Akazigusanisha zile waya na hapo mlipuko mkubwa ukasikika eneo la chooni.

Akatimua mbio na kwenda upande mwingine na huko akagusanisha nyaya ukatokea mlipuko wa kushtukiza eneo ambalo zamani lilikuwa likitumika kama bwalo la chakula.

Sasa hali ikawa mbaya, wapo waliotoka nusu uchi ndani ya nyumba zao, wengine wakabeba vigoda badala ya watoto.

Hali ilikuwa tete!

Nguzu naye akachanganyikana katika ile taharuki na kujifanyaamepotea njia, akaingia katika nyumba mojawapo ambayo watu walikuwa wametoka kwa hofu.Akaikwapua simu na kuondoka nayo, upesiupesi akaitumia simu ile ya upepo kutoa taarifa ya kutisha kwa maneno machache mno.

“NINGEWEZA KULIPUA HIZI KOTA NA KUUA KILA KIUMBE HUMU NDANI. SIJASHINDWA ILA NI SALAMU TU. WAACHWE HURU WOTE WALIOKAMATWA BILA MAKOSA. OVA!”

Hakujitambulisha jina akaiacha simu ile ikizungumza peke yake huku akiuliza yeye ni nani.

Kama salamu za kivita hii ilikuwa imetangazwa katika namna ya kutisha kutoka kwa adui.

Ule upande uliofanya ukatili huu wa kuwakamata watu wasiokuwa na hatia ukaanza kutetemeka huku kila mmoja akijutia maamuzi haya ya ajabu.

Na hapo likaongezeka swali jipya juu ya adui mpya aliyejiamini kiasi kile cha kupitiliza akavamia kota za polisi na kuchafua hali ya hewa.

Wakati wanaukosa usingizi, Martin Nguzu alikuwa amelala katika nyumba ya kulipia yenye hadhi ya kawaida.

Uzuri wale ndugu zake wa Shinyanga hawakumtembelea usiku huu.

Hapakuwa na Kunguni!


GARI iliingia kwa mwendo wa kawaida na kulikaribia geti la nyumba aliyokuwa akiishia Juma Kihwele. Namna gari ilivyoingia haikutisha hata kidogo, lakini namna alivyoshuka aliyekuwa ndani ya gari ndiyo iliyovuta umakini wa watu waliopendezwa na kujua yasiyowahusu.

Ni wachache tu yaliwahusu.

Alishuka mwanamama na kuubamiza mlango, kisha kwa mwendo wa harakaharaka alitembea kulielekea geti kuu la kuingilia ndani.

Mlangoni akamkuta mlinzi, kwa mbali wakaonekana kuzozana. Mlinzi anamzuia asiingie naye analazimisha kuingia.

Mlinzi akazidiwa nguvu, yule mama akaingia mbiombio ndani ya ile nyumba.

Akaufikia mlango na hapo akakutana na mwenye nyumba.

Ujio ule wa ghafla ukampagawisha Juma Kihwele. Lakini hakupata nafasi ya kujiandaa kabla yule mama hajamvamia na kumkwida shati lake.

“Nipatie pesa zangu Kihwele, muda huu nazihitaji.” Alikoroma yule mama aliyekuwa na misuli imara.

Juma Kihwele huku akitweta akajaribu kumtuliza yule mama, lakini ilikuwa kazi bure kabisa. Mama alizidi kufoka kwa sauti ya juu sana. Hatimaye mke wa Juma akatoka akiwa amembeba mtoto wake. Kulikuta sakata lile akamtua mtoto wake na kuingia katika tukio lile moja kwa moja.

Wivu wa mapenzi!

Hicho ndo cha kwanza kilichovamia kichwa cha mke wa Juma!

Mke mwenza…

Hili nalo likamvamia na kumsulubu, ni kitu ambacho hakutaka kitokee japokuwa dini ilikuwa inaruhusu kabisa. Lakini ingekuwa kwa amri yake angezuia hili jambo kwa mume wake pekee, kwa wengine angeliacha kama lilivyo.

“Huyu ni nani Juma?” Aliuliza kwa shari kiasi.

Juma akashindwa kujibu.

“Wewe ni nani mama, na nini kinatokea hapa?” Akamgeukia yule mwanamke mpenda shari.

“Naitwa Dokta Kobo, ninamdai mumeo. Naomba anipatie pesa zangu nijiondokee hapa.” Alijibu kwa kirefu.

Juma Kihwele akafanya kosa kubwa kupinga kuwa hadaiwi kitu chochote na yule mwanamke.

Dokta Kobo hasira zikamjaa, akamkwida vyema zaidi Juma. Na hapa sasa ukazuka ugomvi, mlinzi akasogea eneo la tukio kwa ajili ya kumsaidia bosi wake.

Kuona kuwa wanaompinga wamekuwa wengi, Dokta Kobo akaingiza mkono katika pochi yake kubwa kiasi. Akarudi nyuma na hapo akatoa bunduki.

Wacha wee!

Wivu ukasahaulika, ubabe wa mlinzi nao ukaenda likizo huku rungu lake likimtoka mkononi, Juma akakaza mwendo wakamfuatia wenzake wakitimua mbio. Huyu akiita mama yule anaita Mungu wangu na mwingine haongei.

Mbio!

Dokta Kobo akamtazama vyema Juma Kimbelembele anavyokimbia kwa uoga huku akipiga mayowe, ndani ya sekunde chache akayahesabu maovu yote kutoka kwa bwana huyu na hapo akaufikia uamuzi wa kumuhukumu.

Akaielekeza silaha yake kule alipokuwa Juma Kimbelembele, kisha akaanguka chini na kutua kwa kutumia goti moja, akamweka Juma katika shabaha. Vilevile kama alivyowahi kufundishwa na mume wake ambaye ni ana cheo cha inspekta katika jeshi la polisi.

“Kafie mbele mwanaharamu mkubwa wewe…” Likamtoka neno lile na kisha akakifikia kitufe cha kufyatulia.

Mlio mkubwa ukasikika!


GIZA lilikuwa limetanda wakati fahamu zikirejea kinyonge katika mwili wa dokta Kobo. Alijihisi maumivu kwa mbali lakini alipojipapasa hakuwa na jeraha.

Akatulia kwa muda kisha akakumbuka kwa juhudi zote ni wapi alitoka hadi kulifikia giza lile.

Kama kawaida yake hakuwa mwenye papara, hili ni moja kati ya jambo lililopelekea inspekta Kobo kumtolea mahari upesi na kumuoa moja kwa moja.

Akazikusanya fikra zote na tabasamu hafifu likamtoka.

“Nimetekwa!” alijisemea huku akijiandaa kukabiliana na huo ukweli.

Akaukumbuka mlio mkali wa risasi uliopelekea ashindwe kukivuta kitufe cha kufyatulia na kumwondoa duniani Juma Kihwele.

Kwa maksudi akaanza kukohoa ili wenyeji wake waweze kujisogeza karibu yake.

Kimya! akabaki kuusikia mwangwi wa kikohozi chake mwenyewe.

Akakohoa tena, bado hali ilikuwa ileile.

Akasitisha zoezi lile akasimama na kuanza kupapasa gizani akijaribu kutafuta mwanga wa kutoka katika eneo lile ikiwa ni kweli hajatekwa.

Aliendelea kupapasa bila kukutana na kitu chochote kile.

Akajipapasa na kukuta amepungukiwa bunduki pamoja na mkoba wake. Akatambua wazi kuwa alikuwa amepekuliwa. Hakuwa na hofu kubwa.

Hiyo ilikuwa ni asili yake. Katika kazi yake ya udaktari alishuhudia wagonjwa wengi wakipoteza maisha, wengine mikononi mwake wengine katika mikono ya madaktari wengine.

Hivyo hakuwa akikihofia sana kifo. Alijua ipo siku atakufa…

Na sasa alijiona katika mdomo wa kifo. Aliendelea kutembea zaidi akipapasa huku na kule.

“Ni akina nani hawa? na wanataka nini?” Alijiuliza huku akiendeleza bidii katika kupapasa.

“Mamaaaaaa!” kelele kubwa zilisikika ghafla mbele yake na hapo akasikia vishindo vikiambaa kwa kasi.

Mungu wee! nini hiki? alijiuliza huku kwa mara ya kwanza akianza kupatwa na wasiwasi moyoni.

Akatulia tuli katika giza lile akisubiri kitakachojiri.

Hakuna aliyesogea, akasikia gari likiwashwa na kisha akauona mwanga kwa mara ya kwanza.

Mwanga ulipenya katika mboni ya macho yake katika namna ya kumsumbua.

“Tulia hapohapo mwanga mkubwa wewe!” sauti ikamuamrisha. Akatulia tuli huku akikumbuka nidhamu ya kunyoosha mikono yake juu.

Hatua zilizizidi kusogea hadi alipokuwa.

“Toa hicho kitambaa” Akaamrishwa.

Akaanza kujitazama.

“Toa kitambaa usoni!!” sauti ikaamrisha tena.

Ni hapa ambapo akili ya daktari Kobo ilifanya kazi.

Wakati wote aliokuwa akipapasa katika kiza kinene alikuwa na kitambaa usoni.

Ajabu!

Akajipapasa na kukifungua kile kitambaa. Ndio palikuwa na giza lakini sio kiza totoro kama alichokuwa akitembea kwa kupapasa.

Taa za gari zilikuwa zinammulika, akaendelea kunyanyua mikono yake juu hadi alipofika mwanaume mmoja akiwa na mkuki na rungu.

“Wewe ni nani usiku huu hapa na umefika vipi hapa. Tiketi yako ipo wapi? na kwanini haujatoka ndani hadi wakati huu…” Maswali debe yalitiririka.

“Sijui kitu chochote jamani.” alijibu kwa shida, koo lake lilikuwa limekauka.

“Unajua hapa ni wapi?”

“Sijui lolote, sijui hata nilipotoka mpaka kufika hapa.” aliendelea kusisitiza.

Taa zikazimwa! sasa aliweza kuwaona watu wawili zaidi, wote wanawake na kwa mbali akauona ufukwe.

Alikuwa jirani kabisa na bahari.

Kuhusu ni kitu gani kimetokea hakujua pa kuanzia lakini bado alihisi kuwa hajapaa hadi kufika katika ufukwe ule asioufahamu.

“Nipo wapi hapa jamani?” aliuliza ili apate mwanga.

Kabla jibu halijatoka, vikasikika vishindo na miale ikaanza kuonekana kuanzia mbali. Wote wakageuka nyuma kutazama kinachojiri.

“Kuna hatari hapa ndugu zangu. Ikiwa vyema tuondoke hapa” Yule bwana aliyefanania na mlinzi alitoa shauri.

Na hapo wale wanawake wawili wakaingia garini, kisha akafuata mlinzi na katukatu wakagoma kumbeba Dokta Kobo hata alipowasihi zaidi kuwa huenda alikuwa ametekwa.

Gari ikaanza kuondoka taratibu ikipambana na ule mchanga mwingi wa ufukoni mwa bahari.

Tulivu haikudumu, risasi zikaanza kufyatuliwa kuelekea lilipokuwa gari.

Dokta Kobo, akakimbia kwa kasi sana kuelkea yalipokuwa maji.

Shukrani za dhati zilikuwa kwa tabia yake ya kupenda kufanya mazoezi ya viungo kila siku.

Aliyafikia maji na kujirusha upesi ndani yake. Risasi ziliendelea kurindima huku gari lile ambalo sasa tairi moja lilikuwa limepasuliwa tayari likipambana kujinasua kutoka katika eneo lile.

Akiwa ndani ya maji dokta Kobo aliliona balaa jingine likimnyemelea, aliiona mbwa yenye afya ikijongea kule alipokuwa yeye huku ikibweka sana.

Mbwa ilizama majini, sasa haikuwa ikibwrka tena lakini ilikuwa na usongo wa hali ya juu.

“Come on lazy dog!!” alijisemea huku akijaribu kufanya hichoalichopanga kufanya.

Akaendelea kuyakata maji huku kila mara akikumbuka kuiita ile mbwa.

Alijua hawezi kuendelea kuogelea tu bila kupambana. Na alichokipanga wakati wake ukafika.

Mbwa ikamrukia na kumrarua na makucha yake.

Dokta Kobo akaukumbuka utoto wake akaujumlisha na ujana wake jinsi alivyokuwa fundi katika kukata maji. Wakati akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi alikuwa akiwazidi hadi wanafunzi wa kiume katika kukata maji.

Sasa yu katika maji kwa sababu maalumu sio mashindano ya kawaida ya mshindi kutunukiwa cheti, katika hili mshindi angetunukiwa uhai.

Dokta Kobo anayeyajua maji akavuta pumzi na kutoa nje mara kadhaa kisha akajigeuza na kumweka mbwa chini yake kisha wote wakazama.

Kilichofuata yalikuwa mashindano ya nani awezaye kuzitunza pumzi zake kwa muda mrefu awapo ndani ya maji.

Ni mbwa ama ni dokta Kobo.

Mbwa alisahau kuwa alikuja pale kwa lengo la kushambulia, sasa alikuwa anahaha huku akinywa maji mfululizo bila mpangilio.

Dokta Kobo alikuwa makini katika kuzitunza pumzi zake na wakati huo alimdhibiti yule mbwa asiweze kupanda juu kuvuta hewa.

Sekunde zake za uvumilivu zilipofikia ukomo. Akaiunganisha mikono yake miwili katika shingo ya yule mbwa kisha akairuhusu ile mbwa ifurukute.

Ikafurukuta na kumleta juu, akavuta pumzi za kutosha. Mbwa asiye na akili kama za Dokta Kobo akabaki kuhema hovyo.

Dokta Kobo akazama tena ndani ya maji, na hii ikawa safari ya mwisho.

Alipoibuka alikuwa hai peke yake, mbwa iligeuka mzoga wa ajabu unaoelea ndani ya maji kwa mara ya mwisho.

Dokta Kobo katika kichwa chake mpambano wa uhai ulikuwa haujamalizika nd’o kwanza ulikuwa unaanza.

Aliwaza na kuwazua akaukumbuka ule usemi wa wanamtaa usemao mume/mke si ndugu yako.

Akajaribu kuuhalalisha usemi ule katika hili linaloendelea.

“Ina maana Kobo mume wangu amemuua Nguzu na sasa anataka kuniua mimi kwa sababu nimejua ama?” alijiuliza huku akiendelea kuyakata maji kwa makini kabisa kujiweka mbali na hatari.

Akayakumbuka mema yote waliyoyapitia katika ujana wao, na sasa katika utu uzima huu yasahaulike?? Alijiuliza na kuingiwa na ukakasi mkubwa sana katika kuupata usahihi.

Zubeda!

Jina hili likamshambulia ghafla, akahisi wawili hawa lao ni moja. Wamekolezana kimahaba wamemuua Nguzu na sasa hawataki usumbufu wowote ule wanataka uhuru wameamua kumtokomeza.

“Koboko mume wangu? Hapana…. hawezi kunifanyia hivi mimi.” Alijiuliza na kujipatia jibu japokuwa hakutaka jibu lile limuathiri na kuwa jibu la uhakika.

Baada ya kukatab maji kwa juhudi zote na kuamini kuwa yu mbali na ile shari. Alienda hadi ufukweni akajinyoosha na kuvuta pumzi za kutosha.

Hakujua ilikuwa ni saa ngapi na mbaya zaidi hakujua maadui wake walikuwa upande gani kwa wakati ule.

Subira! ndo kitu pekee kilichohitajika kwa wakati ule pale alipokuwa.

Akaendelea kutulia mtaalamu yule wa magonjwa ya moyo.

Dakika takribani arobaini zilitimu bila purukushani yoyote, lakini hapakuwa tulivu zaidi.

Miale ikaanza kuonekana, akiwa ametuliapalepale akajigeuza upande wake wa kushoto na kuona kundi la watu wakirandaranda huku wakimulika maeneo mbalimbali.

Daktari Kobo akajipima nguvu katika mwili wake, asingeweza kukimbia walau mita mia mbili bila kuanguka.

Maji yalikuwa yamemdhaifisha sana.

Mapigo yake ya moyo yakaongeza kasi na kujiona kuwa ule ulikuwa mwisho wa ujanja wake katika hili tukio.

Akayafumba macho yake na kutazama angani. Akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana.

Hofu ya kifo ilikuwa jirani yake.

ITAENDELEA

Konstebo Nguzu Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment