Konstebo Nguzu Sehemu ya Tatu
KIJASUSI

Ep 03: Konstebo Nguzu

SIMULIZI Konstebo Nguzu
Konstebo Nguzu Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi: Konstebo Nguzu

Sehemu ya Tatu (3)

Miale ikaanza kuonekana, akiwa ametuliapalepale akajigeuza upande wake wa kushoto na kuona kundi la watu wakirandaranda huku wakimulika maeneo mbalimbali.

Daktari Kobo akajipima nguvu katika mwili wake, asingeweza kukimbia walau mita mia mbili bila kuanguka.

Maji yalikuwa yamemdhaifisha sana.

Mapigo yake ya moyo yakaongeza kasi na kujiona kuwa ule ulikuwa mwisho wa ujanja wake katika hili tukio.

Akayafumba macho yake na kutazama angani. Akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana.

Hofu ya kifo ilikuwa jirani yake.


UMATI mkubwa wa watu ulikuwa unasukumana kutazama tukio lile la kustaajabisha.

Huyu alisema hivi yule naye akapinga na kusema vile.

Baadaye majira ya saa nne asubuhi umati ulitawanyishwa baada ya askari kufika eneo lile na kuwasihi wasogee mbali.

Wakiwa wametangulizana na wataalamu wa afya, polisi waliwaacha wataalamu wale wawapatie majibu ikiwa mwili uliolala pale chini ulikuwa hai ama tayari kwa kuzikwa.

Ule ubishani uliokuwa kwa raia juu ya mwili ule ukahamia kwa maaskari watatu, na wao wakaanza kubishana chini chini juu ya mwili ule.

Askari mmoja alisimamia upande mmoja na wawili wakiunganisha nguvu kutetea hoja yao.

“Yupo hai lakini moyo wake unapiga kwa tabu sana.” Mtaalamu wa afya alitoa majibu, askari wakafuata taratibu zote na kuuingiza mwili katika gari ya wagonjwa huku wakikumbuka kupiga picha eneo lote ambalo waliukuta mwili ule.

Waliondoka pale na kuucha ubishani ukiendelea, na wale askari nao waliendelea kubishana lakini hii ya sasa ilikuwa katika namna ya utani tu.

Gari likaingia barabarani huku likipiga ving’ora.

Kutoka Kariakoo sokoni hadi Muhimbili sio kitambo kirefu sana hasahasa kwa gari hili ambalo linapishwa njia na magari mengine.

Hivyo hata msafara huu haukuchukua kitambo kirefu kuifikia hospitali.

Mwili ukashushwa huku ukipokelewa na wauguzi. Askari wakiwa bado na wawakilishi wao katika hili.

Hapa sasa hapakuwa na kufananisha tena, ulikuwa ni mwili ulioibeba sura iliyokuwa ikifahamika vyema katika hospitali ile ya taifa.

Sura ya dokta Kobo!

Jina ambalo umaarufu wake sasa ulikuwa umezidi tangu apotee kazini pasi na taarifa yoyote ile, kupotea huku kukakifanya kitengo kinachohusika na masuala ya moyo kupwaya sana.

Dokta Kobo alikuwa mtaalamu sana, lakini ucheshi wake na moyo wa upendo vilimfanya kuacha pengo alipokosekana.

Sasa anarejea akiwa katika machela, hana fahamu na hajulikani kama atapona.

Wauguzi na madaktari walilia huku wakimwombea dua aweze kupona.

Kutokea hospitali ya Muhimbili, simu ikapigwa kwa mume wa dokta Kobo yaani Inspekta Kobo.

SIMU hii ilifika katika wakati mbaya sana. Inspekta Kobo alikuwa amechanganyikiwa mno. Walinzi wa siri aliowaweka kumwangalia mkewe na nyendo zake walikuwa wamemueleza kuwa dokta alikuwa ameshindia siku nzima ndani ya chumba cha hoteli aliyofikia, walipojaribu kupeleleza chumba kile wanatanabai kuwa dokta Kobo alipitia mlango wa dharula kutoweka ndani ya chumba kile hivyo hawakujua ni wapi ameelekea.

Jitihada za kumsaka zikagonga mwamba.

Asubuhi akiwa bado hajajua nini hatma ya mke wake kipenzi anapokea ujumbe wa kitisho.

“MKEO AMETAPIKA KILA KITU.” Ujumbe huu ulimaanisha kuwa mkewe amesema kila kitu.

Kuhusu hili hakushtuka sana kwa sababu alikuwa akimuamini sana mkewe jinsi alivyokuwa jasiri pengine kuwazidi wanaume wengi tu.

Hofu yake ilikuwa usalama wa mkewe ambaye kufikia hapo alijua kuwa alikuwa ametekwa tayari.

Mawazo yake yalizunguka huku na kule na kumlazimisha kuwa watu hao wamemuua mke wake.

“Kama mmemuua mke wangu, mtaijua gharama halisi ya mguu wangu uliopotea kwa sababu ya kupambana…” Akamalizia na tusi lake la kiitaliano. Lakini kwa mara ya kwanza akajikuta akilitoa tusi hilo kinyonge sana.

Inspekta Kobo akagundua kuwa alikuwa yu na uoga wa ajabu mno, uoga ambao hajawahi kuwa nao hapo kabla.

Ni hapa alipokiri kuwa yumkini damu nzito kuliko maji lakini penzi ni zito kuliko vyote, maji na damu ukivichanganya pamoja.

Inspekta akakiri kuwa katika mapambano ya zamani hakuwa muoga kwa sababu aliingia katika mapigano huku katikati ya uwanja wa mapambano pakiwa hakuna ndugu yake wala mtu anayempenda, hivyo hata akifa mtu kwake haikuwa tatizo.

Sasa anawatukana watu walioshika hatamu ya maisha ya mkewe kipenzi.

Inspekta akatubu kimyakimya.

Wakati anakiri kuwa anawaogopa watekaji, simu yake ikaita.

Nambari ilikuwa ngeni, akajua wazi kuwa huyo atakuwa ni mtekaji na sasa anataka kutoa masharti ili mkewe apatikane huku akiwa hai ama akaidi na kupokea kichwa cha mkewe kikiwa kimelowa damu mbichi na ujumbe wa kukera ‘tengeneza supu unywe kama kweli ulikuwa unampenda’

Inspekta akaipokea simu ile kwa upole kabisa.

“Inspekta Kobo!” sauti kutoka upande wa pili ikamuita. Akaitikia ‘rabeka’

“Samahani kwa usumbufu mkuu, lakini mimi ni daktari hapa Muhimbili. Sijui kama una taarifa zozote kuhusu mke wako. Daktari Anna Kobo.”

Sijakuelewa taarifa kuhusu nini?” aliuliza kwa upole vilevile huku akiketi chini.

“Yupo hospitali hapa, naona amepatwa na hitilafu kidogo ila kila kitu kipo sawa. Itafaa ukifika huku.” Taarifa iliishia pale.

Inspekta alitamani kuuliza maswali mengi lakini hakuna hata moja lililotoka hadi simu inakatika.

Jasho lilikuwa limeulowanisha mgongo, uso, kwapa na kifua.

Inspekta alikuwa ameoga jasho huku amekaa tu bila kukimbia.

Jasho lile likamfadhaisha mno, aakaanza kujipepea na gazeti lililokuwa mbele yake.

Bado halin hii ilimbughudhi, akajikaza kikakamavu na kusimama akaukaza mwili wake kisha akajikumbusha kanuni za kijasiri za jeshini.

Alipomaliza akabiga saluti, kisha akajiwekea kiapo kuwa hatatumia tena muda mwingi kutetemeka, kutokwa jasho na kunung’unika badala yake atautumia muda mwingi kutafuta majibu ya maswali yanayokielemea kichwa chake.

Akaipapasa bastola yake na kisha akasemanayo. Kana kwamba inamsikia.

“Unaonaje kama nikizitoa hizi risasi kwenye chemba kisha ziwe eneo husika tayari tayari kwa kupasua kichwa cha mtu atakayethubutu kunishambulia. Maana si unajua hawa wapinzani wangu wananijua nami siwajui….. sema nawe unazingua ungekuwa na macho tungesaidiana. MI naangalia kulia we kushoto….” Alizungumza huku akiziweka risasi katika njia yake. Watoto waliozoea kutazama picha za mapigano wanasema ‘akaukoji mjegeja wake’.

Safari ya kuelekea hospitali kupokea taarifa mbaya kabisa kuwa mkewe alikuwa hai lakini alikuwa amezikosa fahamu zake. Kwa lugha ya kigeni ‘alikuwa katika coma’.

Ni heri angekuwa amepoteza fahamu, dokta Kobo hakuwa kabisa na fahamu zake.

Na haikujulikana zitarejea lini.

Inspekta alichoka!

Alijikaza chozi lisimtoke, hakuweza.

Yalibubujika kama mtoto mdogo.

Akatoweka hospitali na kwenda kumalizia kilio chake katika kitanda alicholala Zubeda kule kwenye eneo la siri aliloamua kumuhifadhi.

Kwa wakati huo hakujali jambo jingine zaidi ya watu wake wa karibu wanaoingia matatani kwa sababu yake.

Hasira zake akazihamishia kwa Juma Kihwele.

Kumbukumbu za jina lile zikasababisha sharubu zake kusisimka. Akaendelea kuhisi kuwa huyu bwana ndiye aliyeandika zile habari, na kama aliziandika basi kuna mawili. Anasakwa na waliompa tenda hiyo chafu ili wammalize asije kutoa siri, ama la yupo mikononi mwa watu wabaya tayari kwa kuuwawa.

“Zuu, hivi bi mkubwa hakukueleza ni nani aliyempa maneno yale mazito?” Inspekta alimuuliza koplo Zubeda kwa upole kabisa.

“Hapana hakutaja jina lolote wala hakuelekea kufanya hivyo. Alikuwa anajua anachokifanya wakati anazungumza na mimi.” Alijibu kwa kirefu huku akiwa ameketi.

Hali yake kiafya ilikuwa inaridhisha.

“Vipi kuna kitu kipya unahisi?” Zubeda akajazia swali.

Kimya kikatanda kabla inspekta hajaelezea hisia zake juu ya mwandishi wa habari aitwaye Juma Kihwele. Ili kuusadikisha ukweli akazimwaga hadharani sifa za kimbelembele alizonazo muhariri huyo.

Sifa zile zikamfanya Zubeda amuunge mkono inspekta katika hisia zake zile.

“Nilimsikia daktari akizungumzia juu ya risasi kushambulia nyumba ya Kihwele, usiku uliopita nadhani.”

“Risasi? nani na nani walikuwa wanarusha?” Swali la kipuuzi likamponyoka. Akawa mnyonge alipogundua kuwa ameuliza kipuuzi.

Hakurekebisha!

Akatwaa simu yake na kupiga kwa rafiki yake wa kitengo cha mawasiliano.

Akamuuliza nini kimejiri.

Taarifa zikatoka kuwa inasadikika kuwa familia ya Juma Kihwele yaani mke na mtoto pamoja na ndugu mmoja ilikuwa imepotea.

Nguo zilizotapakaa damu zimeonekana na hazijulikani kama ni majeraha ama zinamaanisha vibaya kwa wahanga.

Hadi wakati huo hakuna anayehusishwa na tukio hilo moja kwa moja.

Taarifa ile iliyakaanga maini ya inspekta Kobo, uzuri sauti ilikuwa yasikika vyema hivyo hata Zubeda alisikia kila kitu.

“Zuu mpenzi wangu, huu mkasa utanizeesha upya. Nilijidanganya mkasa huu utanichangamsha na kuwa kijana….. ajabu nazeeka tena kwa kasi mno. Sijui kuwaza vizuri, sijui kujikaza, yaani nimekuwa kama fala hivi aliyevuta sigara bwege halafu hana uhakika wa chakula cha mchana wala usiku.

Badala ya kulia kiume nalia kama mwanamke.

Looh! mkasa huu unanibadili hadi jinsia mimi inspekta Kobo.” Alilalama kwa uchungu mno huku akijitahidi chozi lisimdondoke.

Zubeda akafanya kosa kumbembeleza, Inspekta akaanza kulia kama mtoto.

“Wameanza na wewe wamekusababishia ajali, wamemzimisha mke wangu huko, na bado wanaendelea kuniumiza kichwa…..aah! Si wanikamate na waseme nini wanataka eeh! Kwani mimi ni mwanadamu wa kwanza kumsaliti mke wangu eeh! Mimi ni wa kwanza nauliza, mbona wameniandama hivi mimi lakini.”

Kwa kilio hiki Zubeda alikiri kuwa inspekta alikuwa amekamatwa pabaya.

Wakati kilio hiki kikiendelea simu yake ya mkononi ikatoa mwanga.

“Angalia ni nani anapiga, kama ni namba mpya naomba usipokee. Sitaki kufia humu ndani, waniache nikafie ndani ya nyumba yangu.” Alizungumza kwa hisia za malalamiko.

“Anapiga Komredi Kitengo.” Zubeda akamtajia jina linaloonekana pale.

Inspekta akaipokea simu huku akiilazimisha sauti yake iwe ya kawaida tena.

“Halafu komredi, si uliniambia kuwa unapenda sana samaki aina ya Sato na Sangara wa Mwanza?” Mpigaji aliuliza lile swali.

Inspekta mdomo ukamfunguka asiamini aliyepiga simu ile alikusudia kumsumbua kwa swali la kizembe namna ile.

Zubeda yeye alijikuta anatabasamu.

“Mbona kimya komredi ama pweza wa jiji washakuvuruga hutaki tena sato.” aliendelea.

“Komredi… najisikia usingizi mkuu. Niache nilale…” alijitahidi sana kulinda heshima iliyopo kati yao.

“Hivi Sato hata Shinyanga wapo au ni Mwanza tu?” Mpiga simu hakujali zile busara.

Inspekta akatamani kulitoa lile tusi lake la akiba lililo katika lugha ya kiitaliano lakini huyu mpiga simu licha ya kuwa na utani waliheshimiana sana.

Akabaki kujichekesha tu..

“Haya jiandae kwenda kula sato, hakikisha unaniletea walau mapande matatu yaliyokaushwa na mimi nijue utamu wa sato wa Mwanza.”

“Una maana gani komredi?” Akauliza inspekta.

“Ndani ya siku mbili hadi tatu mtapelekwa Shinyanga nyie mnaojifanya mnajua sana kutumia bunduki na kulenga shabaha. Kuna kazi inawaita huko, nimekuibia siri tu ili usije ukasema sikukuagiza mapema sato.” Alizungumza kwa utulivu kwa kuamini taarifa ile itakuwa njema kwa inspekta Kobo ambaye alikuwa mpenzi wa mapambano enzi zake.

“Komredi lakini mimi nimezeeka tayari na nimevunjika mguu mnajua… mbona..” Akataka kuendelea kulaumu akasita kwa kugundua kuwa analalamika sehemu isiyokuwa sahihi hata chembe.

“Sio wewe pekee kuna wenzako pia wamestaafu lakini umaridadi wao katika mapambano unawarudisha kazini.”

Mazungumzo yalimalizika na kumwacha inspekta akiwa katika mtihani mwingine mzito.

Mkewe yu katika ‘coma’ hawara yake anajiuguza bado na sasa anatakiwa kwenda Shinyanga kwa oparesheni maalumu.

Oparesheni asiyoijua. Na alimtambua vyema mkuu wake akisema amesema. Ukimjibu kuwa una mgonjwa anakuomba vyeti vyako ulivyofuzu mafunzo ya udaktari hadi ubaki kumtibu mgonjwa, ukisema unaumwa anakuambatanishia daktari katika msafara wa kwenda katika tukio.

Kwa kifupi hapakuwa na sababu ya kukwepa majukumu akiyatoa.

Na kingine kibaya ni uhasama uliokuwepo baina yake na kiongozi wake wa juu.

IGP!

Uhasama usiokuwa na historia maalumu. Ila uliendelea kuwepo.

Njia pekee ya kukwepa majukumu kiutoka kwa IGP ilikuwa ni kujiua.

Alikuwa hakwepeki!

Inspekta Kobo alichoka sana. Ndani ya masaa machache akausikia waziwazi udhaifu uliouchota mwili wake.

Alipoupeleka mguu wake ofisini akakumbana na barua aliyoitarajia.

Wito!

GIZA lilikuwa ndani ya giza kwa mara nyingine, Konstebo Martin Nguzu alikuwa amempokea mama yake ambaye alikuwa mmoja kati ya wahanga wa ile kamatakamata iliyofanywa kwa masilahi ya watu wachache waliokuwa wamekerwa baada ya mwenzao mmoja kuuwawa kifedhuli.

Ghafla bin vuu mambo yakabadilika, kota zikatishiwa kuchomwa. Wakagwaya na kuwaachia huru wale waliokuwa wamekamatwa katika namna ya uonevu.

Ni giza hilihili sasa lipo ndani ya giza tena, ana kwa ana na mama yake mzazi.

Martin Nguzu alimpa pole mama yake huku akiwa na haraka sana ya kujua ni wapi hasa anapoweza kumpata Majenga waweze kuzungumza na kutambua ama kujitambua upya yeye ni nani na kwa nini haya yote yanatokea.

Hasira zake bado zilikuwa dhidi ya inspekta Kobo aliyeamini kuwa alimchomea ndani ya nyumba kisa mapenzi.

Alipona vipi na nini kinaendelea katika maisha yake haya nd’o makuu aliyojiuliza.

Kuhusu kutafutwa kwa Majenga na watu asiowajua kukapunguza ile hisi yake kuwa chanzo cha kiila kitu ni mapenzi.

Akabaini kuwa lipo la nyongeza.

Mama Martin ambaye hakuwa ameimarika sana kiafya safari hii alionyesha ushirikiano wa hali ya juu, usiku uleule alimpeleka Martin hadi nyumba aliyowahi kuishi mzee Majenga ambapo baadaye alipangisha na kuondoka zake kuelekea Shinyanga.

“Ila Shinyanga sijamuona kabisa…” Nguzu alizungumza wakati wanaelekea katika nyumba ile.

“Bado haujabadilika mwanangu, yaani Shinyanga kubwa vile wewe umtafute mtu usiyemjua na ukampata kabisa. Labda muujiza ama maigizo.” Mama alimkata juu kwa juu Nguzu, haikuwa mara ya kwanza hali ile. Tangu utoto wake.

Mtoto hakui kwa mama!

Walipewa ushirikiano mkubwa sana walipowasili eneo lile, uzuri mtoto wa mzee Majenga alikuwa anaishi katika chumba kimojawapo, na alikuwa pale kama msimamizi wa nyumba ile.

“Kumpata kwa leo itakuwa ngumu sana, maana leo watu wametoa kodi. Na yule akipata kodi anamalizia katika ulevi wake.” Mtu aliyekuwa anawapa maelekezo alisema kwa masikitiko.

“Unaweza kujua baa ambazo hupenda kuzitembelea?” Nguzu aliuliza kwa udadisi.

“Bora angekuwa anaenda baa, huyu anaingia vilabuni, ana usemi wake unaosema kwamba mia mbili ya baa ni elfu kumi ya kilabuni”

Martin akajikuta anatokwa na tabasamu hafifu kwa kusikia haya.

Ghafla wakamwona yule mwenyeji akiwafanyia ishara ya kusikiliza kwa makini zaidi, wakasikia sauti ya mtu akiimba.

“Ni yeye… looh! leo amewahi kurudi hivi?” alishangaa na kuwashawishi Nguzu na mama yake washangae pia.

“Halafu….. halafu….. mama huyu kamfanana…. aahm! eeeh!” akaanza kujiuma uma. Alikuwa amemtazama Nguzu vizuri.

“Ninafanana naye sana alikuwa binamu yangu….” Nguzu akaiwahi hii kesi na kuisawazisha.

Mtarajiwa akawasili akiwa anaendelea kuimba nyimbo zake, nyimbo zilizomburudisha yeye pekee.

Hakuwa peke yake…..

Alikuwa na chupa kadhaa za pombe.

“Mnataka kuhama…. mnahama hama na hamjalipa kodi yangu.” Alizungumza huku akiwa hana hata uwezo wa kuona mbele vizuri, sembuse kung’amua kuwa kuna mtu anataka kuhama.

Akasogea kwa kunesanesa bila kuvunja chupa hata moja akawafikia.

“Shkamoo mama….. eeeh! mama nawe umehadimika kweli.” Alisalimia baada ya kumtambua mama Martin.

Salamu ilijibiwa, yule mwenyeji akajitoa katika mkutano huu akawaacha watatu hawa wakizungumza.

Walijitahidi hivyohivyo kuelewana japokuwa ilikuwa ngumu kwani yule mlevi kila mara alikuwa anasahau alichozungumza dakika kumi nyuma.

Mlevi huyu hakujua ni kiasi gani alikuwa faida kwa Martin Nguzu.

______

ASKARI aliyetegemewa na kuaminiwa zaidi alikuwa makini na silaha yake, alikuwa amejinyoosha chini na kunyanyuka kidogo sana usawa wa kifua na kuendelea. Bunduki yake kubwa ilikuwa imelazwa vyema katika muinuko huku akiona kila kitu kilichokuwa kikikatiza mbele yake.

Alitulia katika lindo lile kwa dakika nyingi akingoja walilotarajia litokee waimalize vyema siku yao.

Kilikuwa ni kikosi cha watu saba tu cha siri kilichokuwa kikitambua nini kinaendelea katika giza hili.

Majira ya saa nane usiku mchakacho ulisikika kutoka katika kichaka kimojawapo, mlengaji akatulia tuli bila kufanya shambulizi.

Alihitaji kupata uhakika wa kile alichokuwa anakwenda kukishambulia.

Barua kutoka kwa IGP ilielezea kuwa jambazi aliyekuwa anasakwa miaka mingi alikuwa mjini Shinyanga na huko alitarajia kuanzisha kampeni ya kuvamia na kuiba katika taasisi mbalimbali za kifedha.

Huu ukawa wakati wa askari kujitafutia nyongeza ya nyota kwa kumtia mikononi jangili huyo aliyekuwa anasifika kwa hatari yake na roho mbaya.

Simu ya upepo ilikuwa imeshikiliwa na askari mwingine, kazi yake ilikuwa moja tu kumweleza mlengaji nini cha kufanya ikiwa patakuwa na mabadiliko. Mlengaji hakupaswa kutikisika ama kujihusisha na mawasiliano mengine kwa sababu angeweza kuipoteza shabaha yake.

Mchakacho ule ukaongezeka tena, mlengaji akaendelea kutulia.

Na hapo redio ya upepo ikakoroma ikitoa taarifa kutoka upande wa pili.

“ANGUSHA MBUYU KUNA NYOKA! ANGUSHA HUO MBUYU…”

Sauti ile ikamfikia mlengaji, akaanza kutetemeka mikono nyake. Ile sauti haikuwa ngeni na lile neno hakuwa akilisikia kwa mara ya kwanza. Ni siku kadhaa nyuma alilisikia katika simu ya upepo kutoka kwa kijana wake wa kazi aliyeuwawa kwa kupigwa risasi.

Mikono ikazidi kutetemeka, sauti ile nayo ikazidi kusisitiza neno lilelile.

‘angusha mbuyu’

Mapigo ya moyo yakaongezeka kasi yake.

Adui akajitokeza kutoka katika kichaka, mlengaji akatakiwa kufyatua na kumwangusha adui.

“Afande Kobo, fyatua!!” mshika simu alimwamrisha Kobo aliyekuwa aanatetemeka na silaha yake.

Inspekta Kobo akaachia risasi ya kwanza, ikaenda malikiti.

Haikumkaribia adui badala yake ilimpa taarifa kuwa kuna hatari inawazunguka.

Kobo akamuona adui akirudi mbio kichakani, na baada ya sekunde chache hakutoka peke yake, lilikuwa jopo la maana lenye silaha za maangamizi.

Mpambano ukaanza.

Kobo akajaribu kutupa risasi nyingine, akakosa!

Ile kauli ya angusha mbuyu ilikuwa ikimsumbua kichwa chake.

Anayeitoa sauti ile ni nani? na kwanini alimuua kijana wake? na ni kipi kinamfanya amfuatilie Juma Kihwele kama yeye alivyokuwa anamfuatilia.

Mlolongo huu wa maswali ukazidi kumpoteza, kwa mara ya kwanza katika maisha yake anafyatua risasi tatu na hakuna hata moja iliyomlenga muhusika.

Kitimtimu kikaanza.

Askari saba ambao umri umewatupa mkono dhidi ya jopo la vijana majangili kumi na watano.

Risasi ziliruka hewani kwa fujo, huyu anarusha yule anajibu.

Inspekta Kobo alikuwa kama mpira wa kona, anakimbia huku na kule angali silaha anayo, badala ya kumkabili adui yeye anajiuliza ni nani mwenye ile sauti inayosema ‘angusha mbuyu’

Wasiwasi mara mbili, kwanza dhidi ya hao vijana majangili na pili juu ya adui ambaye wapo naye katika mpango huu kamambe.

Nguzu akatamani kumuuliza askari mwenzake ambaye alikuwa anashikilia simu, amuulize yule ni naji alitoa ile amri.

Lakini, licha ya kuamini kuwa ule wakati haukuwa wa kuuliza maswali bali kila mmoja kuutetea uhai wake. Hata nafasi hiyo pia hakuipata kabla ya kukiona kichwa cha yule askari kikisambaratishwa vibaya mno na risasi iliyotoka inapotokea.

Madonge mazito ya damu yakamrukia wakati akijirusha pembeni zaidi asijekukumbwa na balaa la kusambaratishwa.

Inspekta Kobo alikuwa anahema juu juu huku akiomba dua Mungu amtunze asife usikun huo.

Taswira ya mkewe ambaye yu katika kuzimia ilimvamia. Akahisi kuwa kifo chake kitasababisha mkewe akirejewa na fahamu zake naye apoteze maisha kwa mshtuko wa kupoteza mume.

Sasa hofu ya kifo ilimtawala waziwazi……

Akaiweka sawa silaha yake na kujipa maneno ya ujasiri kupindukia ambayo yangeweza kumrejeshea ari yake ya upambanaji.

Aliiweka vyema silaha mkononi, ikawa inateleza.

Kwa mara ya kwanza bunduki yake ikawa inamsaliti. Akairudisha katika bega lake na kujipapasa kiunoni, akaichukua ile bastola yake anayoiamini kupindukia akaiweka sawa mkononi, hii yenyewe ilimuheshimu ikakaa sawa.

“Serenaserena afande Kobo…. Kobo…” Sauti ikamuita kutokea gizani. Ilianza na utambulisho wao wa siri waliokuwa wamepeana.

Inspekta Kobo akabonyea chini kisha akatoka ‘mkuku’ hadi alipoisikia sauti ile.

Alimkuta mwenzake akiwa katika dimbwi la damu akiogelea bila kupenda.

Hali yake ilikuwa mbaya sana, na alionekana muda si mrefu ataikimbia dunia kuelekea popote anapoamini kwa imani yake.

“Kimbia, hatari…. viumbe hawa hatari. Tunateketea wote….” Alizungumza kwa sauti ya chini sana. Akaweka kituo na kuhema kwa nguvu zote.

“Hakikisha unaishi ili kuwa shuhuda…. viumbe hatari sana wana siri zote. Usimuamini mtu jiamini wewe mwenyewe kuanzia sasa….. kuna wasaliti kati yetu.” alizidi kusihi.

“Na… naku.. nakuf… nakufa afande.” Alizungumza huku akizidi kukauka koo lake na sauti kufifia.

Ikawa kama alivyojitabiria!

Inspekta akazidisha umakini, akabaki na maswali lukuki, ni kwanini bwana yule anamweleza kuhusu wasaliti ndani yao, kwanini amemchagua yeye na amemuamini vipi kuwa yeye sio msaliti?

Mwenzao huyu!! alijisemea huku akiondoka kutoka eneo lile.

Sasa kila upande ulikuwa umetulia, ilikuwa ni vita ya kuviziana baina ya pande hizi mbili. Inspekta hakutaka kumuamini mtu yeyote zaidi.

Alitilia maanani uhai wake pekee.

Akakimbia hadi alipolifikia shimo asilojua matumizi yake, akatumbukia na kutulia ndani yake.

Alikuwa macho kabisa kisije kumdhuru chochote kitu.

Aliendeleakutulia hadi palipokucha akauona mwanga.

Lakini mwanga huu ulikuwa ukingojewa na watu wengi.

Ile Inspekta anatoa kichwa chake nje akakutana na sauti kali zikimkaripia asithubutu kufanya jambo lolote lile atue silaha zake chini na kisha kunyanyua mikono yake juu.

Alijitahidi kujitambulisha lakini hakuna ambaye alimsikiliza.

Akatii, kwa umakini wa hali ya juu askari wenye sare wakamkaribia na kumtia pingu mikononi na miguuni.

Ajabu!

Alistaajabu ni kipi kimejiri hadi kujikuta katika balaa kubwa kiasi kile tena ghafla.

Alionywa asithubutu kusema jambo lolote lile. Akaingizwa katika gari lenye ulinzi mkali kupindukia.

Hawakutaka kulala tena Shinyanga.

Amri ikatolewa kuwa iwe isiwe lazima inspekta Kobo afikishwe jijini Dar es salaam, na hiyo ilikuwa ni amri na sio ombi.

Inspekta Kobo hakuamini, vijana walio chini yake ki-cheo walikuwa wanamlinda huku wakimkaripia mara kwa mara.

Alifedheheka ila hakuwa na la kufanya.

Huu ukawa mwanzo wa safari mbaya na ya kutisha.

Wakati anaiacha ardhi ya Shinyanga, katika ardhi hiyohiyo harakati mpya ilianza kusukwa.

FLORIAN NGENGEKUZENZA NGUZU.

USHINDANI wa nani kwao matajiri nilishindwa mapema sana, kila walichokuwanacho sisi tuliishia kukiona tu. Hatukuwanacho wala hatukukaribia kukipata.

Miaka ya elfu tisa mia na arobaini (1940), ni wale watoto ambao baba zao walikuwa wakijipendeza kwa wakoloni pekee ndo wangeweza kuwa na maisha yenye unafuu.

Katika hapa sikuwa mshindani wake.

Tulipata nafasi mara chache sana kucheza michezo ya kitoto, hatukuwa tukishindana sana.

Miaka ikazidi kwenda hatimaye ikafika wakati wa kwenda shule, huku napo hapakuwa na ule ushindani wowote. Alisoma katika shule ambazo walivaa viatu na sare nzuri angali sisi miguu yetu iliunda urafiki wa kinafiki na miba pamoja na matope.

Kitu pekee tulichopata katika maisha yetu duni ni aibu za wazazi wetu pindi waliponyanyaswa na mkoloni. Kisha baada ya hapo wanatusimulia simulizi za mashujaa wao ambao na wao walikuwa wakikiri kuwaogopa hawa watu wenye ngozi nyeupe.

Simulizi hizo zilinijenga barabara, katika akili yangu. Nikajikuta ni kijana ambaye uzalendo ulikuwa katika moyo wangu.

Baba yangu mzazi ambaye alipigana vita ya Majimaji huko Songea alikuwa akiniongezea ujasiri, ni kweli alikuwa akinyanyaswa na wazungu na aliwaogopa kweli lakini alikuwa akinieleza kuwa katika vita ile kwa mkono wake wa kuume akiwa na rungu kubwa aliwauawa wazungu watano.

Kwake ulikuwa ni ushindi mkubwa sana kumtandika mkoloni na bunduki yake mkononi.

Ni kweli watanganyika wengi walipoteza maisha lakini hii ilikuwa alama kubwa sana kuwa waliutaka uhuru kwa namna yoyote.

Baba alinieleza kuwa baba yake ambaye ni babu yangu alipoteza maisha kwa kunyongwa, na ni yeye ndiye alikuwa mmiliki wa jina la Nguzu ambalo maana yake ni NGUVU.

Jina Florian nilipewa na hawa ngozi nyeupe waliojifanya miungu katika ardhi yetu, silipendi jina hilo.

Naitwa Ngengekuzenza Nguzu. Yaani ‘Aliyerithi Nguvu’.

Baba yangu alinipatia jina lile kwa sababu aliniamini sana, nami nikajikuta najiamini mno.

Maisha magumu hayakuiathiri akili yangu, sijui mnaitaje kwa kizazi chenu hiki cha Tanzania, lakini wakati wa Tanganyika tulisema akili zinachaji, akili zangu zilikuwa zinachaji mno.

Nilifanikiwa kulimaliza darasa la nne la mkoloni.

Wakoloni bwana licha ya unyanyasaji wao lakini walikuwa makini sana, wakiona mtu ana akili sana wanamuwahi ili baadaye aje kuwa upande wao na aseme mazuri tu juu yao. Mkoloni akupatie elimu utaanzaje kumsema kwa mabaya angali tayari unaweza kusema’yes no’ kwa sababu yake!!

Hata mimi waliniwahi na hapa ndipo nilikutana na Joseph Kazeze.

Na upinzani ukaanza rasmi.

Wakatupeleka shule ya upili ambayo kwa sasa mnaiita Tabora boys lakini wakati ule iliitwa Tabora Central school. Ilikuwa shule ya vipaji maalumu haswa. Wanafunzi wengi walikuwa ni watoto wa machifu, ni baadaye sana walianza kuchukua wanafunzi wa kawaida.

Kwa wakati ule nadhani ni mimi na wengine wachache sana tuliokuwa tunasoma pale lakini si watoto wa machifu.

Mitihani ya hapa ilikuwa ni kutoka vyuo vya uingereza. Hawakutufundisha kuhusu yetu bali walitaka tuyajue yao.

Hata hayo yao bado nilipata alama za juu.

Urafiki kati yangu na Joseph Kazeze ukaanza kuyeyuka, hakutaka kupitwa alama na mtoto wa kimasikini kama mimi.

Tulipoenda jeshini mwisho wa kidato cha tatu kama ilivyokuwa ada nilikuwa bora zaidi yake katika kila kitu.

Hakupenda kabisa, ila mimi sikujua kama ni kwa kiasi kikubwa vile.

Tukarejea tena kumalizia kidato.

Katika uchaguzi nikateuliwa kuwania uongozi, Joseph naye akawania.

NIkamwangusha na kuwa kiongozi wake!

Wakati ananipa mkono wa hongera ndipo niliiona chuki katika macho yake.

Nikapuuzia.

Nikasema ikiwa wote tunatoka Mwanza, ya nini kuchukiana sasa. Nikadhani yale yataisha…

Kutingwa na uongozi nikasahau kabisa kuketi na Joseph tuzungumze.

Chuki ikakomaa!

Baadaye yakaibuka mapenzi, nadhani hapa ndipo chuki ilibalehe na kuota mapembe!

Joseph alimpenda binti ambaye alikuwa akinipenda mimi. Kuzidiwa huku kete Joseph akaleta ubabe na kunivimbishia kifua.

Mara ya kwanza nilimwacha, ya pili akanifuata tena akinitaka ugomvi, nikamweleza bayana kuwa sisi ni ndugu wa mji mmoja asiwe vile.

Akanipuuzia na siku hii akanisukuma nikaanguka.

Nilipoinuka nilimfundisha kuhesabu moja mpaka kumi kwa lugha ya kirusi.

Somo lilikuwa gumu na kila mara alianguka chini, kila akijaribu kunyanyuka namtandika ngumi ya uso. Akapasuka juu ya jicho lake, nami nikawa napiga palepale.

Siku hii nikatambua kuwa majina yana maana yake.

Ngengekuzenza Nguzu (Aliyerithi Nguvu)

Nilikuwa nimerithi haswa.

Ugomvi huu ulitikisa shule.

Ajabu yake ilikuja katika maamuzi, tulipigana na mgomvi alikuwa Jose lakini katika adhabu nikachukuliwa mimi.

Tabora Central School ilikuwa shule ya kijeshi wakati wetu, hata sare zetu zilikuwa za kijeshijeshi, tulivalia kombati za kaki kama wanazovaa wanamgambo, kila kitu kiliendeshwa kikakamavu, hapakuwa na adhabu za viboko.

Nilivyoadhibiwa nikikusimulia unaweza ukahisi huyu bwana kachanganyikiwa na sasa ananidanganya.

Niliingizwa katika chumba chenye giza nene na hapo nikaanza kulazimishwa kwenda mbele, kadri ninavyokwenda mbele ninazidi kuinama chini kutokana na muundo wa kile chumba, hatimaye paji la uso likayakaribia magoti.

Chumba kikabanwa nikawa siwezi kusogea mbele wala kurudi nyuma.

Niliumia mno, nikaamini kuwa sasa ninakufa.

Waliniacha kwa masaa mengi sikumbuki hata.

Waliponitoa nilikuwa nyang’anyang’a.

Wakanipelekaq msituni, huko sasa niliadhibiwa na wazungu. Walimwachia mbwa wao anikimbize na nilipewa ruhusa ya kukimbia kumzidi.

Nilivyochoka vile ningeweza vipi, si waliutaka uhai wangu tu wapuuzi wale.

Basi kama ni mchezo basi mbwa alipata wa kucheza naye, nakimbia hatua kadhaa naanguka mbwa anafika na kuning’ata wanamfukuza.

Wananiambia nisimame tena ninakimbia wanamwamuru mbwa anikimbize, ananifikia na kuniangusha ananing’ata.

Niliteseka mno!

Baada ya hapo nikapokea viboko kumi na viwili vya mkoloni.

Nilinyooka.

Joseph hakuadhibiwa nilipotoka kule kwenye adhabu nyinginyingi za kutisha nikaelezwa kuwa nimefukuzwa shule na wakati huohuo aliyechukua nafasi yangu katika uongozi ni Joseph Kazeze.

Nililia! Nililia sana.

Nikapakiwa katika gari moshi, elimu yangu ikaishia pale nikarejea kuwa mtumwa.

Nilipambana hivyohivyo hadi siku ile mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyokabidhiwa nchi huru.

Walau hali ikaanza kuwa ya heri, sikutamani kusoma tena.

Tayari nilikuwa nina familia ya mtoto mmoja niliyempa nikiwa Mwanza baada ya kufukuzwa shuleni.

Sikupata mtoto huyu na yule mwanamke aliyetuletea uhasama baina yangu na Jose. Nilizaa na maskini mwenzangu tukalea kimaskini hivyohivyo.

Niliamua kuanzisha familia kwa sababu sikuwa na familia tena, baba yangu alifariki na mama vilevile.

Halikuwa jambo la ajabu kwa wakati ile kupoteza familia yako.

Nikamsahau Joseph Kazeze katika kichwa changu. Niliamini yote yaliyotokea Tabora Central School ni mambo ya ujana tu.

Nilikuja kulisikia jina hili katika siasa.

Eti Joseph Kazeze ni mjumbe sijui wa kamati gani katika chama tawala. Hii ilikuwa mnamo mwaka 1977. Niliamua nisijihusishe na habari zozote kuhusu Jose kwa sababu kwa kufanya hivyo nilikuwa nakumbuka chanzo cha mimi kuishia kati katika masomo yangu na sasa sina thamani yoyote katika jamii.

Miaka mitatu baadaye yule mwanaharamu akaanza kunizongazonga tena.

Alinibomolea nyumba yangu. Japokuwa hakuja yeye moja kwa moja lakini nilijua kupitia waliokuja, akanibambikiza kesi kadhaa bahati nzuri ilikuwa upande wangu nikawa natoka salama.

Huwezi kuamini, akavuka mipaka baada ya kuona kila analofanya si kitu kwangu.

Hivi unaweza ukaamini Jose Kazeze akaamua kumposa upya mke wangu!

Andika kila ninachokueleza usiache walau neno moja, yote yana maana sana.

Nd’o hivyo bwana Joseph akamlaghai mke wangu ajuavyo yeye, alikuwa na gari lake aina ya Land Rover ya chama tawala basi aliitumia hii kuishika akili ya mke wangu.

Yule mwanamke naye alikuwa mjinga kweli, ujue nilishamweleza kinagaubaga kuhusu uhuni wa Jose lakini akashawishika akaniacha eti.

Hivi kama sio kuumizana nafsi ni nini hiki, kweli Joseph ambaye alikuwa ana pesa tayari anaamua kuniingilia anga zangu, tena bora ingekuwa kwa mwanamke ambaye ni kigoli, mwanamke huyu alikuwa amecharazwa bakora za mkoloni haswa hatamaniki, alikuwa amechanjwa mwili mzima chanjo za kinga ambazo ziliaminiwa na makabila mbalimbali. Haya yote akajifanya hayaoni…. akaamua kuniadhibu.

Alifanikiwa!

Nilimwambia mwanangu juu ya alichonifanyia mama yake. Nilimweleza huku ninalia.

Akatangaza kumchukia milele!

Basi rafiki yangu akabaki kuwa huyo mwanangu wa pekee, niliyemuita jina Salama.

Mama Salama akahamia katika maisha ya Joseph Kazeze.Iliniuma mno, huyu bwana katumia cheo chake kulipiza kisasi angali mimi sikufanya lolote enzi zile Tabora kwa kumkomesha.

Sasa mwanamke nikamuachia, sifa zote nikamuachia lakini yule bwana kumbe hajaridhika.

Hapo sasa zile jazba za enzi za shule zikarejea nikajisema kuwa nchi hii ni huru kabisa, tena sio uhuru wa bendera. Hakuna utumwa tena labda ukusudie mwenyewe. Ajabu anajitokeza mjinga mmoja mwenye ngozi kama yangu ananirudisha utumwani.

Siku ya tukio sikumuaga Salama!

“Naomba kwa leo tuishie hapo mzee wangu Majenga….. sitaki kusikia kilichotokea. Nakuomba sana alfajiri tutaendelea na mkasa huu. Nimefurahi sana kukukuta ukiwa hai mzee. Na badi nashangaa uliweza vipi kutunza karatasi hizi kila ulipoenda na kutarajia siko moja utamsomea mtu” Martin Nguzu lizungumza kwa hisia kali, sauti yake ilikuwa baridi mno. Alikuwa ameguswa mno na maandishi yale.

“Niliwahi kumsomea mama yako, sijui hata kama alinisikiliza kwa makini maana alikuwa analia kila akisikia lolote kuhusu hayati Ngengekuzenza Nguzu ambaye ni baba yake mzazi.” Alijibu Majenga kwa utulivu.

Na hapo akaitoa miwani yake usoni.

Akajifuta machozi.

“Babu yako alikuwa mtu wa aina yake sana. Namuona hai ndani ya macho yako…” Akaongezea huku akimshika begani Martin Nguzu.

Nguzu akamsaidia kuinuka, akamkokota mpaka ndani akamsaidia kukiandaa kitanda chake akamwacha akilala. Naye akaenda katika chumba kingine akalala.

Wakati Martin Nguzu na mzee Majenga wanakubaliana kulala ili siku inayofuata waendelee kusoma maandishi yale ambayo Nguzu aliamini kuwa si haba yatampa mwanga kidogo juu ya matukio yote yanayotokea. Upande mwingine palikuwa panapambazuka.

Inspekta Kobo akiwa na pingu miguuni na mikononi mwake alikuwa katika mahojiano mazito sana.

Mdomo wake ulikuwa umeanguka na na kubaki wazi kutokana na kipigo kikali alichopokea, midomo hii iliyokosa ushirikiano ilisababisha udenda ulioambatana na damu umwagike katika namna ya kusikitisha sana.

Mguu wake uliokuwa umeunganishwa kwa vyuma ulikuwa umepigwa na sasa baadhi ya vyuma vilikuwa vinachungulia nje.

Damu nzito iliyoganda katika chuma kile ilisaidia kuficha ukweli wa mambo.

Inspekta hakuwa na uwezo wa kutembea na hakulazimishwa kutembea badala yake aliburuzwa hadi akafika mahali alipohitajika.

Macho yake mekundu yalikuwa makubwa sana, na yalikuwa yakiviringika huku na kule katika namna ya kuomba huruma ya yeyote yule mwenye mamlaka ya juu yake.

Hakutokea japo mmoja wa kumtetea.

Maelezo aliyokuwa ameyatoa waliosikiliza hayakuwakuna kabisa na hivyo wakaona suluhu ni kumbana vyema kwa kumuumiza ili aweze kutapika siri zote alizomeza.

“Inspekta Kobo, hili ni agizo la mwisho kabisa la kukubembeleza wewe kusema ukweli wote ili ubaki kuwa salama ama la tutatumia nguvu. Na hatushindwi!” Sauti ya kusihi iliyojaa madaraka iliunguruma.

Inspekta akastaajabu, hawa mabwana tayari walikuwa wameitengua taya yake, wakaupoteza njia mguu wake na sasa yungali mahututi katika bahari ya maumivu, sasa anaelezwa kuwa asiposema ukweli watatumia nguvu.

Nguvu! alistaajabu…

Nguvu gani zaidi ama watamkaliza katika kiti chenye shoti ya umeme, au watampiga risasi?

Hizi nd’o nguvu ambazo walikuwa hawajatumia.

“Mkuu nilichokiandika katika maelezo yangu ni hicho hicho sijaongopa hata nikishtuliwa usiku wa manane siwezi kupindisha ukweli huo.” Alijibu kwa shida sana.

“Kama uliweza kupindisha shabaha yako maksudi na kumwacha hai jambazi mkorofi ambaye tumehangaika miaka nenda miaka rudi kumsaka unashindwa vipi kuupindisha ukweli?” Alihoji kisha akasimama wima na kuendelea kuzungumza.

“Kobo, katika maisha yako ya kulenga shabaha umeangusha mibuyu mingapi iliyoleta ukorofi?”

“Mingi sana afande.” alijibu kwa sauti ya chini.

“Umetunukiwa shani ngapi kutokana na kulenga kwako shabaha?”

“Tano afande.”

“Unaikumbuka shabaha yako ngumu kupita zote?”

“Ahh! mmh! ndio afande, ni ile ya kutoka ghorofa moja kwenda nyingine.” aliendelea kujibu upesiupesi. Bila kujua nini hatma ya maswali yale.

“Unaukumbuka umbali kimakadirio?”

“Mita mia tano….” alijibu kwa utulivu. Na safari hii sauti ilikuwa chini zaidi kwa sababu aliijua nia ya maswali yale.

“Yaani nusu kilometa sivyo? Na haukuwa katika utulivu wowote, na uliweza kuipata ile shabaha bila kukosa. Na ilikuwa ni usiku….. halafu leo hii unapiga risasi tatu maksudi unamkosa adui anayetikisa taifa. Kobo! Kwa kitendo chako hicho cha kumuacha adui wa taifa unadhani watanzania wapo radhi kukusamehe? Mimi kama mtanzania siwezi kukusamehe… nastaajabu wanakuchelewesha nini kukutia kitanzi bazazi wewe…. uliyechagua kumlinda mwanaharamu mwenzako!” Sasa alikuwa amewaka yule bwana aliyekuwa anamuhoji Inspekta Kobo. Na alikuwa anatetemeka mno.

Inspekta alikuwa amekamatwa pabaya.

“Ok! unalipwa shilingi ngapi kila anapofanya uhalifu wake…. tuzungumze kama wanaume na haya mambo yaishe. Maana Tanzania mambo ya kitanzi tulishayafuta, na hata ukifungwa maisha huyo mwanaharamu atakuja kukutoa tu utakuwa huru. Haya nieleze tu, unapewa kiasi gani kulisaliti jeshi la polisi katika oparesheni kabambe namna ile.” Swali likatupwa.

Inspekta Kobo akafadhaika mno, kwa sababu hakuwa kama walivyodhania.

Alipojaribu kupinga, hasira za yule bwana zikamuangukia.

Akapokea teke kali katika shingo yake, akarushwa na kutua pembeni akabaki kukoroma huku damu ikimtoka puani.

Akatamani kuelezea ukweli wa kila jambo lakini hakuona kama ataeleweka maana katika maandishi yake hakuandika kuhusu mashaka yake juu ya ile sauti inayotamka ‘ANGUSHA MBUYU’. Hakuandika kuhusiana na kifo cha utata cha Martin Nguzu na hakugusia hata kidogo juu ya mahusiano baina yake na koplo Zubeda.

Angeanza kuelezea hayo angeonekana ni muongo mara mia zaidi ya alivyochukuliwa awali.

Inspekta akaamua kubaki kimya.

“Inspekta Kobo hivi unajua kuwa hii kesi yako inaweza kuhesabiwa kama kesi ya uhaini na itakuweka pabaya wewe na familia yako, ama unajitazama wewe na masilahi yako pekee hauitazamani familia yako. Haumtazami mkeo ambaye hadi sasa hajui kinachoendelea ulimwenguni, hujali kuhusu watoto wako unajitazama wewe pekee. Sasa mimi nimekusihi sana imetosha naandika ripoti tusilaumiane katika hili.” Alizungumza kwa sauti tulivu kabisa huku akiwa anamtazama Inspekta Kobo.

Maneno yale juu ya familia yake yalimvuruga Kobo aliyejitambua wazi kuwa hana kosa lolote lile, lakini la kufanya nd’o hakuwa nalo.

Akarejeshwa katika chumba alichokuwa anafungiwa mle akiwa peke yake.

Tofauti na siku nyingine ambapo chumba hiki kilikuwa kinazimwa mwanga wa taa na kubaki katika giza siku hii kilikuwa kina mwanga na zaidi kiliongezeka kiti.

Nanyongwa!!

Hisia zikakipiga kichwa cha inspekta Kobo, tumbo likaanza kuunguruma kwa hofu ya kuupoteza uhai wake.

Akaingizwa pale chumbani.

Kimya kikatanda kwa dakika zisizopungua tatu. Kisha zikasikika hatua zikijongea katika kile chumba.

Mlango ukafunguliwa na askari wawili, kisha kwa mwendo wa taratibu akaingia Inspekta jenerali wa polisi (IGP).

Mwili wa inspekta Kobo ukaingiwa na ubaridi mkali sana, akaunyanyua uso wake na kumtazama bwana yule nadhifu kabisa aliyekuwa katika mavazi yake ya kazi.

“Funga mlango!” akawaamuru wale askari.

Wakatii! kisha wakaondoka na kuliacha eneo lile likiwa na watu wawili pekee.

Mwili wa Kobo ulikuwa umesulubika sana, lakini kwa kumtazama bwana huyu mwili ukajiona kuwa inayokuja nd’o suluba taslimu.

Kobo alitambua kuwa IGP aliisubiri hii nafasi kwa hamu sana ili aweze kumnyoosha na sasa alikuwa ameipata. Iwe isiwe atamwadabisha.

“K” IGP akaita kwa upole.

Inspekta akamtazama kisha akaitika kwa shida sana.

“Pole sana rafiki yangu. Pole!” IGP aliketi vyema.

Unafiki! Kobo akajisemea.

“Kabla sijazungumza mengi na wewe ninapenda kukueleza kuwa ninakupenda sana rafiki yangu, huwezi kuamini haya lakini elewa kuwa nimejaribu zaidi ya mara tano kuonana na wewe lakini nimeshindwa kwa sababu sikuwa tayari kukuona katika hali hii. Umeteseka sana K” alizungumza kwa hisia IGP.

Hali hii ilimtisha Kobo, akajiuliza anachokisikia ni sahihi ama kuna namna ya ulaghai.

Yaani huyu bwana ajisikie vibaya kwa yeye kuwa katika wakati ule mgumu.

Haiwezekani.

Inspekta Kobo akakumbuka vitisho vyote alivyowahi kupewa na IGP wakati huo akiwa hajapewa dhamana hii ya juu katika jeshi la polisi.

“K, yale yote yalikwisha kwa upande wangu. Nimetafiti sana na nikagundua kuwa wewe haukuwa chanzo cha mke wangu kuwa mlemavu. Niliumia sana awali na kujikuta nikikuchukia lakini nimeikubali hiyo hali na nipo hapa kwa ajili ya kukusaidia tu! Tafadhali sema nami”

“Niliyoyasema ni hayohayo.” Akajibu kwa ukaidi Kobo, bado alikuwa na hisia za chuki dhidi ya IGP bado hakuamini kuwa wao ni marafiki tena.

“K, sikiliza ndugu yangu. Ukaidi hautasaidia kitu chochote kwa wakati huu. Laiti kama ningekuwa juu ya sheria ningeamuru uachiwe huru na ubaki kujuta na nafsi yako ikiwa ni kweli umefanya yote hayo ama la. Lakini kwa hili mimi sina ninalazimika kuiheshimu sheria ya nchi, sio kuivunja kisa ninakuonea huruma. K, tafadhali nieleze ni nini kilitokea….” IGP alizungumza kiukarimu kabisa.

Inspekta Kobo akaamua kurusha karata yake ya kwanza. Akaelezea kwa ufupi sakata la Nguzu, hakulitaja jina la mwanamke ambaye alikuwa anahusika.

Akaitaja ile sauti ambayo aliisikia usiku wa tukio la Nguzu kuchomewa ndani na kisha akaitaja tena sauti ileile ilisikika siku ambayo alikuwa ameishika bunduki yake tayari kwa kufanya shambulizi.

“Nikapagawa sana kugundua kuwa licha ya kwamba nimelenga shabaha kwa ajili ya kummaliza adui ila ndani yetu pia kuna adui. Tena adui asiyekuwa na huruma aliyeiteketeza kwa moto nyumba ya askari mwenzetu pasi na huruma kabisa. Nilitetemeka sana, hata lile agizo alilonipa la kuushusha mbuyu lilinikwaza badala ya kunihamasisha. Hakika nilikuwa natetemeka…”Alimalizia.

Palepale IGP akamsogelea na kumnong’oneza jambo kwa kusihi.

“Usiyaseme maneno haya popote pale. Umeniamini mimi imetosha sana na ninakuahidi italeta manufaa. Nimeupata mwanga.”

IGP akatulia kidogo kisha akarusha suala jipya kabisa ambalo lilikuwa jipya kwa inspekta Kobo.

“Umesema juu ya Nguzu kuchomewa ndani ya nyumba yake, unadai ulienda kuzungumza naye usiku ule. Sawa kabisa…. na je Majenga unamfahamu vipi?”

“Ma nani?”

“Majenga” Aklajibu IGP huku akimtazama kwa ukaribu kabisa inspekta Kobo.

“Sijawahi kulisikia jina hili katika maisha yangu.”

“K, mbona hutaki kuamini kuwa ningali upande wako? nieleze nijue ni wapi nakusaidia rafiki yangu. Ujue kuna watu watatu wameuwawa huko Shinyanga na huu mlolongo wote unakuangukia wewe. Ndugu zao wamechachamaa si kidogo, huyo Majenga ni nani Kobo! Tell me…” alianza kupandwa na ghadhabu IGP.

“Simjui na sijawahi kulisikia jina hilo Gervas, mbona unanilazimisha kutema maneno ambayo akili yangu haijawahi kuyameza. Simjui huyo Majenga for God’s sake!!” Aling’aka inspekta Kobo huku akimtaja IGP kwa jina lake.

IGP akaanza kufura kwa hasira, akajitahidi kujiweka katika hali ya kawaida. Akauliza tena na tena bila majibu kubadilika.

Inspekta Kobo akasimamia analoliamini!

IGP akamtazama kwa sekunde kadhaa, akatoa kitambaa chake mfukoni na kujipangusa matone ya jasho na mwisho akamtupia Kobo neno la mwisho.

“Pambazuko hili litakuwa baya sana kwako na sitakuwa na namna ya kukusaidia. Nimejaribu sana Kobo nawe umeona. Umekataa kumtaja Majenga na unamjua waziwazi….”

Akasubiri kidogo, Kobo akamtazama kisha akalazimisha tabasamu na kisha akazungumza.

“Nimekuwa na mapambazuko mabaya sana tangu mke wangu apate janga lile, nimekuwa na mapambazuko mengine mabaya tangu vijana wako, vijana niliowafundisha ukakamavu jeshini walipougawana mwili wangu na kufanya kwa vitendo yale niliyowafundisha, mapambazuko mabaya hayataanza leo ama kesho yalianza tangu uliponituhumu kuwa nimeshiriki kumfanya mkeo awe mlemavu wa miguu angali nilijaribu kadri ya uwezo kuokoa maisha yake, niliokoa maisha yako pia Gervas kwa kukusukuma ili usipigwe risasi, nikawa na mapambazuko mabaya ulipozisahau fadhila zangu, ni pambazuko gani baya zaidi unaloniahidi sasa… eeh! pambazuko gani unalolisema, pambazuko la kupoteza uhai? Kuteswa? Kufungwa gerezani maisha yangu yote? Hakuna pambazuko la ajabu hata moja kati ya hayo, ni wewe utayaishi mapambazuko ya ajabu siku utakapoujua ukweli angali nimenyamaza katika kile kimya cha milele, Attaccati a sto cazzo.”

akaweka kituo huku akimalizia kwa kutokwa na lile tusi lake murua katika lugha ya kiitaliano.

IGP akabaki kuganda, midomo ikimchezacheza asijue ni maamuzi gani ayachukue.

Akatoweka pale na kwenda nyuma ya mlango. Akajibanza pale na machozi yakaijua njia yake, yakayalowanisha mashavu, kamasi nyepesi zikatoka kuchungulia nini kinaendelea katika uso wa IGP.

IGP alikuwa analia kiume!


Majira ya saa sita usiku aligutuka kutoka usingizi huku jasho likimtoka sana.

Majenga! jina hili likakivamia kichwa chake, akaketi kitako na kuanza kukumbuka juu ya maneno yale aliyokuwa akiyasoma yule mzee. Akatamani asubuhi ifike upesi aweze kuendelea kusikiliza ni kipi ambacho kitakuwa na faida kubwa sana kwake.

Akamaizi kuwa licha ya kushtuka vile na kuandamwa na jina hilo lakini pia alikuwa pia amebanwa na haja ndogo.

Na choo kilikuwa mita nyingi kutoka chumba alichokuwa amelala.

Akapatwa na uvivu sana huku akijilaumu kwa kukataa kunywa maji mengi baada ya chakula cha ili asije kupata shida kama hizi usiku na sasa amezipata shida zilezile.

Akajivuta taratibu kuelekea choo kilipokuwa. Nje palikuwa kimya sana, walisikika wale viumbe wanaopenda kulala mchana kisha usiku wanazurura kusumbua viumbe wengine.

Popo!

Umbali wa choo ulimtatiza sana, akajiona mpuuzi sana giza lote lile kuna vichaka vya hapa na pale ni kwanini ahangaike na choo.

Akakiendea kichaka kidogo alichokiona karibu yake.

Akakidhi haja yake lakini hakuweza kugeuka kabla ya kusikia sauti ikimuamuru asimame.

Akasimama tuli!

“Kwanini unakojoa vichakani we tahira?” sauti ikakaripia.

Martin Nguzu akastaajabu, tangu afike pale Shinyanga sauti karibia zote zilikuwa zinaambatana vyema kabisa na lafudhi ya kisukuma, iweje hii sauti inakuwa na miporomoko ya pwani ama Zanzibar?

Hakujibu kitu!

“Nakuuliza weye mwanaharamu…”

“Nisamehe tafadhali…” Hatimaye akazungumza.

“Mzee Majenga analala chumba kipi hapa? na ni nani ako….” Swali likatupwa.

“Analala nyumba kubwa!”

“Geuka utupeleke upesi..”

Nguzu akageuka na kukutana na mambo aliyoyazoea.

Mitutu ya bunduki.

Walioibebwa waliishika kizembe sana. Ni vile hawakujua kuwa ile hatari inayodhaniwa kuzikwa katika tanuru la moto, iliishia kung’arishwa na kuwa dhahabu yenye thamani kali huku ikiwa na makali ya kisu kipya.

Walisimama wanaume wawili, mmoja akiwa na bastola mkononi mwake. Huyu aliielekeza kwa Nguzu.

Nguzu akajitia kutetemeka huku akiwasihi wasimuue. Kutetemeka kule kukawazidishia uzembe.

Mmoja aliyebaki akasikika akizungumza kwenye simu kuwataarifu wenzake kuwa wamefika eneo la tukio na muda si mrefu watauchukua mzigo wao.

Walitembea hatua kumi kuelekea ilipokuwa nyumba ya mzee Majenga na familia yake.

Nguzu alizihesabu zile hatua vyema huku macho yake yakiwa makini sana kutazama kitu.

Hatimaye akakifikia, kilikuwa ni kigogo kilichokuwa njiani. Akakikanyaga na kujikwaa maksudi.

Akaanguka chini huku akitokwa na yowe la hofu.

“Inuka hanithi wewe…”

Kauli hii aliisubiri Nguzu kwa hamu, mkono wake ulikuwa tayari na jiwe, akatumia sekunde chache kubaini kuwa mshika bastola yule hakuwa anakaribia kufyatua, kidole chake kilikuwa mbali kabisa na kifyatulio.

Safi sana! akajisemea na hapo akajitutumua ainuke.

Alipoinuka akaliachia lile jiwe likampata bwana mwenye lafudhi ya kipemba usoni, kapiga yowe huku bunduki ikimtoka.

Yule mwenzake akajiweka sawa kufanya shambulizi kwa kutumia bunduki.

Nguzu akajirusha huku goti lake likitangulia mbele hadi katika kifuani kwa adui.

Akambwaga chini.

Nguzu akaitwaa ile bunduki.

“Acha ujinga dogo, vita sio kama kunywa urojo unakunywa hata kama ni kibogoyo. Vita inahitaji watu majasiri.” Alimwonya alipomuona akitafuta bastola.

Yule bwana akatulia asiamini kuwa kibao kimewageukia wao.

Mwenzake alikuwa amekodoa macho.

“Mwambie jamaa aje moja kwa moja eneo la tukio, ukiongeza neno nakuua muda huu, na usipoongeza nitakuua baadaye.” Nguzu akaamrisha.

Simu ikapigwa jamaa akazungumza aliyopaswa kuzungumza. Kisha simu ikakatwa.

“Nilikueleza ukiongeza neno nakufanyaje?”

“Unaniua!”

“Na usipoongeza?”

“Utaniua baadaye. Nisamehe tafadhali sisi tunatumwa tu” alijibu huku akitetemeka.

Nguzu akamgeukia yule mpemba.

“Shehe! mwenzako kaongeza neno tayari, anasema nimsamehe na sikusema hivyo.” Hakusubiri jibu, akaigeuza bunduki, hakutaka kupoteza risasi akaizamisha bunduki katika kifua cha yule bwana singe ikaingia nzima nzima.

Akagalagala kuusaka uhai wake.

Mpemba akakurupuka akairukia bastola. Lakini hakuweza kufyatua kabla Nguzu naye hajamrukia na kumkanyaga mkono.

“Swahiba, nakukumbusha tena huu sio urojo kila mtu anakunywa.” akamtia ngumi kali katika paji la uso wake.

Ilikuwa ni vita ya kistarabu sana, mtu akianguka chini waliolala wanajua ni maembe yanaanguka, wanajigeuza upande wa pili na kuendelea kuota ndoto zao.

Hawakujua kuwa roho zilikuwa zinatoka na uwanja ule ulikuwa umegeuka kuwa wa kivita.

Nguzu akambana maswali yule mpemba, akajibu kuwa huyo anayekuja ndiye kiongozi wao, wenyewe hawajui kiundani juu ya tukio lile.

“Kwa maana hiyo unamaanisha wewe hauna umuhimu wowote kwangu sivyo.”

“Walah! naapa mie wanionea bure tu sina nijualo.” Jibu lile likawa la mwisho.

Kama hauna maana unabaki na Nguzu kufanya nini.

Akaunganishwa katika safari ya mwenzake aliyekuwa ametulia tayari.

Nguzu akaweka windo lake kumngojea huyo aliyeitwa mjua mengi.

Windo hili likazua safari mpya ya Konstebo Martin Nguzu kurejea jijini Dar es salaam.

Jiji ambalo linaamini kuwa yu kwa muumba akijibu tuhuma zinazomkabili. Huku wengine wakiamini bado anahangaika na adhabu ya kaburi.

ITAENDELEA

Konstebo Nguzu Sehemu ya Nne

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment