Bondia Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA : HUSSEIN ISSA TUWA
Simulizi: Bondia
Sehemu ya Kwanza (1)
Lango kuu la gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam lilifunguliwa na mtu mmoja mrefu alitoka nje ya lango lile kwa hatua za kujiamini na kusimama kiasi cha hatua zipatazo tano nje gereza lile. Nyuma yake, lile lango lilifungwa, na hivyo kufungia historia ya miaka miwili ya taabu, mateso, kazi ngumu na uchungu mwingi ambayo mtu huyu alipitia alipokuwa upande wa pili wa lango lile. Ilikuwa ni saa tatu na robo asubuhi siku ya jumatano.
Jamaa aliangaza kulia na kushoto pale nje huku akivuta pumzi ndefu zilizoingiza hewa nyingi mapafuni mwake, kisha akashusha pumzi zile zikiambatana na mguno wa faraja, iliyotokana na kuvuta hewa ile ya ulimwengu huru, akiwa mtu huru. Hili ni jambo alilokuwa akilisubiri kwa hamu katika muda wote ule aliokuwa akitumikia kile kifungo chake cha miaka miwili.
Pamoja na kimo chake kirefu, mtu huyu alikuwa na mwili ulioshiba pamoja na kuwa alikuwa kifungoni. Hii ni kutokana na mazoezi mazito aliyokuwa akijilazimisha kufanya akiwa kule gerezani kwa lengo maalum. Misuli yake ya mikono iliyojaa vizuri ilijidhihirisha wazi kwa kututumka na kufanya mikono ya fulana yake ya mikono mifupi ionekane kumbana. Vivyo hivyo, misuli yake ya mapaja ilionekana kututumka na kuifanya ile suruali yake ya jeans nayo ionekane kuwa inambana.
Bila kugeuka nyuma, jamaa alianza kutembea kwa hatua moja moja zilizokuwa zikivutwa bila ya haraka yoyote kuelekea barabara kuu iliyokuwa mbele yake, akiliacha lile jengo la gereza nyuma yake akiwa na azma ya kutorejea tena ndani ya kuta za jengo lile maishani mwake.Bora kufa, kuliko kurudi tena gerezani.
Alishaazimia hivyo muda mrefu, na bado alibaki na azma hiyo.
Kwake yeye mji aliuona ukiwa umebadilika sana ndani ya miaka ile miwili, lakini hilo halikuwa na maana yoyote kwake, kwani alijua kitambo kuwa pindi atakapotoka gerezani angekuta mabadiliko mengi sana jijini. Alikuwa akitembea huku akijaribu kutazama mambo yote yaliyokuwa mbele yake kwa jicho la kudadisi. Aliona kuwa magari ya usafirishaji wa abiria yalikuwa yamechorwa mistari ya rangi, tofauti na hali aliyoiacha wakati anaingia gerezani. Kidogo hili lilimpa taabu, kwani alianza kujiuliza ni jinsi gani ataweza kujua ni rangi ipi ndio ilikuwa ikiwakilisha basi la kuelekea sehemu ambayo alikuwa ameazimia kwenda baada ya kutoka gerezani.
Aliweka sawa mkoba wake mdogo alioupitisha begani kwake na kuuacha ukining’inia mgongoni na kuzidi kuikurubia ile barabara ambayo juu yake, magari yalikuwa yakipita kwa kasi sana kiasi cha kumkosesha amani.
Jamaa alikuwa na sura ya kuvutia ambayo baada ya miaka miwili gerezani, ilikuwa imeingia ukomavu fulani ambao haukuwepo hapo kabla, na ambao kwa namna yake uliongezea mvuto kwenye sura ile.
Lakini wakati akitembea taratibu kwa mwendo wake wa hatua moja moja kukiendea kituo cha mabasi yaelekeayo katikati ya jiji kilichokuwa upande wa pili wa barabara, uso wake ule wenye mvuto ulionekana wazi kuwa ulikuwa una dhamira thabiti juu ya nini alikuwa anataka kufanya baada ya kutoka gerezani, kwani baada ya miaka miwili ya kupanga na kupangua akiwa kule gerezani, hakika alikuwa anajua ni nini haswa alichotakiwa kukifanya.
Kwenye kituo cha mabasi yaliyokuwa yakielekea maeneo ya Kariakoo na katikati ya jiji kilichokuwa upande wa pili wa ile barabara kuu, mmoja wa watu waliokuwa wakisubiri mabasi pale kituoni alikuwa akifuatilia kila hatua ya yule mtu mrefu aliyetoka kule gerezani, ambaye sasa alikuwa akisubiri nafasi muafaka ya kuvuka barabara ili naye aende pale kituoni.
Alikuwa ni mwanamke aliyejitanda khanga mwili mzima hadi kichwani, kama jinsi wanawake wengi wa pwani wapendavyo kujitanda, na usoni alikuwa amevaa miwani myeusi iliyoficha kabisa sura yake. Ingawa alionekana kuwa ni msafiri miongoni mwa wale wasafiri wengi waliokuwa wakisubiri daladala pale kituoni, ukweli ni kwamba mwanadada yule aliyejitanda khanga, alikuwa akimsubiri yule mtu mrefu aliyetoka gerezani asubuhi ile!
Jamaa alivuka barabara na alikuwa akikiendea kile kituo cha mabasi, wakati mlango wa mbele wa gari dogo aina ya Hyundai nyeupe yenye namba za serikali ulipofunguka na msichana mmoja mwenye kimo cha kawaida alipoteremka na kusimama nje ya lile gari huku mkono mmoja bado ukiwa umeshikilia mlango wa gari lake.
Huyu naye alikuwa amevaa miwani ya jua, ingawa yeye alikuwa amevaa gauni refu la kitambaa laini chenye maua madogo madogo lililokuwa na mpasuo mpana upande mmoja. Kichwani alikuwa amebana nywele zake ndefu zilizotiwa dawa za kulainisha na kupendezesha nywele katika ile staili ya Pony Tail , ambapo kile kimkia cha nywele kilichokuwa kikining’inia kisogoni mwake kilikuwa kimechomoza kutokea kwenye sehemu ya nyuma ya kofia aina ya kapelo aliyokuwa ameivaa. Aliweka mkono wale wa pili juu ya paa la gari na kumtazama yule jamaa akipita upande wa pili wa lile gari akielekea kule kituoni.
“Roman!” Aliita.
Jamaa alisimama katikati ya hatua na kugeuka taratibu ule upande ilipotokea sauti iliyoita jina lake. Alimtazama yule dada mwenye kapelo na miwani ya jua huku akikunja uso kujaribu kumtambua. Yule dada aliendelea kumtazama bila ya kusema neno zaidi, akimpa muda yule mtu aliyemwita kwa jina la Roman amtambue.
Kule kituoni yule mwanamke aliyejitanda khanga naye alianza kupata waiswasi baada ya kuona yule jamaa aliyekuwa akimvizia akisimama na kumgeukia yule dada aliyetoka kwenye lile gari lenye namba za serikali.
Ni nini tena pale?
Jamaa alimtazama kwa makini zaidi yule dada na alihisi kuwa alishapata kuiona ile sura wakati fulani huko nyuma, ingawa bado hakuweza kuioanisha sura ile na kumbukumbu zake za miaka miwili iliyopita.
“Miaka miwili ni mingi kiasi cha kukufanya unisahau Roman?” Hatimaye yule dada alimuuliza yule jamaa huku akitoa miwani usoni kwake, na hapo jamaa akaachia mdomo kwa mshangao.”Afande Fatma…?” Yule dada alirudisha tena miwani yake usoni. “Sasa nimekuwa Inspekta…Inspekta Fatma.”
Jamaa alikunja uso, safari hii ikiwa ni kwa kukereka, na kubetua midomo kwa namna ambayo ilionesha kuwa hakufurahishwa na hali ile.”Unataka nini Inspekta?” Roman aliuliza, huku akitilia mkazo wa kebehi lile neno “Inspekta.”
“We need to talk Roman…you and me! (Tunahitaji kuzungumza Roman…mimi na wewe!)” Inspekta Fatma alimwambia yule jamaa bila ya kujali kebehi na kukereka kwake kwa wazi. Roman alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Yaani siku yangu ya kwanza nikiwa mtu huru! Halafu mtu wa kwanza kukutana na kuongea naye ni askari! What’s this (Nini maana yake hii)?” Roman alisema kwa hasira.”We need to talk Roman, and we need to talk now!(Tunahitaji kuzungumza Roman, na tunahitaji kuzunguza wakati huu!)”
“About what (Kuhusu nini)? Nimetumikia kifungo changu, nimemaliza. Sasa mimi ni raia huru…”
“Ingia kwenye gari Roman!” Inspekta Fatma alimkatisha. Na sauti yake ilikuwa imebeba mamlaka yote aliyokabidhiwa na jamhuri kama afisa wa jeshi la polisi mwenye jukumu juu ya usalama wa raia wote wa Tanzania.
Kule kituoni yule mwanamke aliyejitanda khanga alizidi kujichanganya katikati ya kundi la watu waliokuwepo pale kituoni huku akizidi kufuatilia kwa makini kila kilichokuwa kikiendelea kule kwenye lile gari dogo lenye namba za serikali. Na kwa kadiri ilivyokuwa, ni wazi kuwa kile kitendo cha yule mtu aliyeitwa Roman kusimama na kuongea na yule dada aliyetoka kwenye lile gari lenye namba za serikali kilimchanganya sana.
Ni nini kinaendelea pale? Roman alibetua mabega na kuuliza kwa kukereka kwa hali ya juu. “Ili iweje afande? Ni lazima niingie kwenye hilo g-” “Sio lazima. Lakini ni muhimu tuongee. Nataka kukupa lifti…”
Mtu aliyeitwa Roman alimtazama yule askari wa kike kwa muda, na yule askari aliendelea kumtazama bila ya kutetereka. Kisha, bila ya kusema neno zaidi, Roman alipiga hatua moja kubwa na kufungua mlango wa upande wa abiria wa lile gari na kuingia. Inspekta Fatma aliingia nyuma ya usukani na kuliondoa lile gari kutoka eneo lile kwa ustadi mkubwa.
Huku kituoni, mwanamke aliyejitanda khanga alichanganyikiwa vibaya sana. Alilitazama lile gari likiondoka kutoka eneo lile kwa fadhaa iliyochanganyika na hasira.
“Unaelekea wapi?” Inspekta Fatma aliuliza huku akiwa amekaza macho yake barabarani. Roman alikuwa amegeuzia uso wake nje ya dirisha akiangalia mandhari ya jiji alilolikosa kwa muda wa miaka miwili. Hakufanya juhudi yoyote kuficha jinsi alivyokereka na hali ya kuwa na yule askari ndani ya lile gari.
“Umesema unataka kuongea. Ongea nami nakusikiliza.
Unaweza kuzunguka jiji lote hili wakati tunaongea…sio lazima ujue niendako!” Alimjibu kwa hasira huku bado akitazama nje ya dirisha. “Nimesema tunahitaji kuongea…mimi na wewe. Hivyo natarajia na wewe uwe unaongea. Na ndio maana nimekuuliza swali ambalo naomba unijibu. Unaelekea wapi Roman?””Hiyo inakuhusu nini? Wewe si ndugu yangu, si jamaa yangu, na wala si mke wangu! Sasa sioni swala la mimi ninaelekea wapi linaingiaje kwako.
Mimi ni mtu huru bwana!” Roman alimjibu kwa jazba. Inspekta Fatma alimtupia jicho la pembeni halafu akabaki kimya kwa muda, akijishughulisha na kuendesha gari, ingawa uso wake ulionesha kuwa na mawazo mazito. Roman alifumbata mikono yake kifuani na kuendelea kutazama nje ya dirisha la lile gari.
Safari iliendelea katika hali ile kwa muda mrefu, na katika muda ule walikuwa wameanza kuingia katikati ya jiji.
Walipita uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam, na mwendo mfupi baadaye, Inspekta Fatma alipunguza mwendo wa gari na kuingia kulia ambapo aliliegesha kwa ufundi mkubwa nje ya mgahawa maarufu wa Best Bite katika lile tawi lake lililopo barabara ya Nyerere, zamani Pugu Road.
“Okay, Roman, nadhani hapa tunaweza kuongea kwa kituo zaidi.”
Inspekta Fatma alimwambia yule mtu mrefu mwenye mwili ulioshiba huku akiteremka kutoka kwenye gari. Bila ya kuongea neno, lakini akionesha wazi kuwa alikuwa amechukia, Roman aliteremka na mkoba wake kutoka kwenye lile gari na kumfuata yule afisa wa polisi mrembo ndani ya ule mgahawa mzuri.
Baada ya kuagiza soda aina ya Coca Cola kwa ajili yake na bilauri ya juisi ya nanasi kwa ajili ya Roman kwa mujibu wa utashi wake, Inspekta Fatma alianzisha tena maongezi. “Roman, najua kuwa utakuwa unanichukia sana hivi sasa kwa kufanya haya niyafanyayo, lakini naomba uelewe kuwa hii ni kwa faida yako na si vinginevyo…”
Roman alimtazama yule binti bila ya kusema neno, na Fatma aliendelea.”…najua kuwa baada ya kumaliza kifungo chako utakuwa tayari una mipango uliyojipangia katika maisha yako mapya. Basi na iwe ya kheri Roman, vinginevyo itakuwa mbaya sana kwako.”
Roman alizidi kumtazama tu yule dada bila ya kusema neno. “Mimi nimeamua kuja kukusubiri pale Ukonga leo hii kwa sababu najali maisha yako, na kwa jinsi ninavyohisi, naona una hatari ya kurudi tena gerezani kama hutaamua kusahau yaliyopita na kutazama mbele.”
Inspekta Fatma alizidi kumueleza kwa upole na msisitizo wa hali ya juu. Bado Roman alikuwa akimtazama kwa macho makavu bila ya kusema neno lolote wala kupitisha hisia yoyote usoni mwake ambayo ingeweza kusomwa na macho makini ya yule askari wa kike. Lakini Inspekta Fatma alikuwa anajua ni nini alichokuwa anataka Roman aelewe, hivyo hali ile haikumkatisha tamaa hata kidogo.
“Sahau yaliyopita Roman, na uanze maisha mapya sasa. Kama utahitaji msaada mimi niko tayari kukusaidia kwa kadiri nitakavyoweza, lakini achana kabisa na mawazo uliyonayo Roman, hayatakusaidia kitu…”
Hapo Roman hakuweza kuendelea kubaki kimya.
“Mnhu! Yaani we’ unataka kuniambia kuwa unajua mi’ n’na mawazo gani? Achana na mimi kabisa afande!”
“Sahau yaliyopita Roman, na uanze maisha mapya sasa. Kama utahitaji msaada mimi niko tayari kukusaidia kwa kadiri nitakavyoweza, lakini achana kabisa na mawazo uliyonayo Roman, hayatakusaidia kitu…”
Hapo Roman hakuweza kuendelea kubaki kimya.
“Mnhu! Yaani we’ unataka kuniambia kuwa unajua mi’ n’na mawazo gani? Achana na mimi kabisa afande!”
Inspekta Fatma alitikisa kichwa taratibu.
“Huwezi kunidanganya Roman. Nimekuwa nikikutazama tangu unasubiri kuvuka ile barabara pale nje ya gereza hadi ulipokuwa ukipita mbele ya gari langu pale jirani na kituo cha basi. Katika sura yako kulikuwa kuna kusudio la wazi kabisa ambalo lilithibitisha hofu yangu juu ya mambo utakayotaka kuyafanya muda huu ukiwa umemaliza kifungo chako. Achana na mawazo hayo kabisa Roman…”
“Hujui usemalo Fatma…na kama huna la zaidi naomba niende zangu!” Roman alimjibu kwa hasira. Lakini Inspekta Fatma alikuwa na msimamo.
“Mimi najua, Roman. Na usidhani utanilaghai na huo ukimya wako au utanipoteza lengo kwa hayo maneno yako ya hasira. Najua! Na ndio maana nimekuja kukuasa mapema Roman. Acha yaliyopita yawe yamepita. Angalia mbele…!”
Roman alitikisa kichwa kwa kustaajabia upotofu wa mawazo ya yule askari. Lakini Fatma hakuwa mjinga.
“I am telling you Roman, let it go!(Nakuambia Roman, achana nayo kabisa!)”
“Let what go, Fatma?(Niachane na nini, Fatma?)” Roman alimuuliza kwa kukereka huku akimkunjia uso.
Fatma alitomasa hewa mbele ya uso wa Roman kwa kidole chake cha shahada kutilia msisitizo maneno yake.
“You know what!(Unajua!). Mi’ najua miaka miwili uliyokaa gerezani ulikuwa ukisubiri tu siku hii ya leo ifike…na sasa imefika, unataka kutimiza yote yale uliyodhamiria wakati ukiwa kifungoni. Niamini mimi Roman, asilimia tisini ya mambo watu wanayodhamiria kufanya baada ya kutoka huko ulikotoka wewe leo hii huwa ni juu ya uovu, udhalimu zaidi na visasi! You can’t be any different! (Wewe huwezi kuwa tofauti na hao)”
Roman aliguna na kutikisa kichwa.
“Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa jela haisaidii kurekebisha tabia? Sasa kwa nini basi huwa mnatupeleka huko?” Alimuuliza kwa kejeli ya wazi. Sasa ilikuwa zamu ya Inspekta Fatma kutikisa kichwa.
“You are a good guy Roman…(U-mtu mzuri Roman…)”
“Good guys do not get sent to prison, do they? (Watu wazuri huwa hawapelekwi gerezani, au sivyo?)” Roman alidakia kwa jazba na huku akipiga meza waliyokuwa wamekalia kwa kiganja cha mkono wake. Baadhi ya watu waliokuwamo mle ndani waliwageukia na kuwakodolea macho na mhudumu mmoja alisogea na kuuliza iwapo kulikuwa kuna tatizo lolote. Ilibidi Inspekta Fatma afanye kazi ya ziada kumhakikishia kuwa hakukuwa na tatizo lolote wakati Roman akibaki akiwa amekunja uso kwa ghadhabu. Inspekta Fatma alimtazama kwa upole uliochanganyika na simanzi yule jamaa.
“You used to be a good guy Roman!(Kabla ya kupelekwa gerezani ulikuwa mtu mzuri Roman!). Nataka uendelee kuwa hivyo sasa baada ya kutoka gerezani. Usiiache hii hali…haya mambo yaliyotokea, yakuharibu. Let it go!(Achana nayo!)” Inspekta Fatma alimjibu kwa hisia kali. Kidogo macho yalimtembea Roman na alitazama pembeni. Hakutaka kabisa kumtazama yule dada usoni.
“Lakini bado hiyo haikutosha kunifanya nisipelekwe gerezani Inspekta!” Roman alisema kwa uchungu.
“Ndio, lakini…You don’t belong there Roman! (gerezani si mahala pako Roman!) Ndio maana sitaki ufanye kosa litakalosababisha urudi tena gerezani, kwani ikitokea hivyo Roman, ujue huko ndiko kutakuwa makazi yako for good (milele)! Yaani hukutakiwa kabisa kwenda huko…”
Roman alitikisa kichwa taratibu na kumuuliza.
“Una maana sheria ilikosea iliponipeleka gerezani?”
“No! Lakini mazingira yaliiwezesha sheria ikupeleke gerezani. Ndio maana nakuasa usifanye jambo litakalokufanya uje ujute maisha yako yote Roman!”
“Aanhaa! Kwa hiyo na wewe unakubali kuwa hii tunayoiita sheria ina upungufu? Kwamba inaweza ikatengenezewa mazingira fulani, kisha ikatumika kuwaadhibu wasio na kosa na kuweka huru waliokosa?”
Inspekta Fatma alipepesa macho kidogo. Ilikuwa ni hoja ngumu kwake kuiafiki.
“Aa…sometimes, but…(mara nyingine, lakini…)
“Kwa hiyo unakubaliana na mimi?”
Inspekta Fatma alimtazama Roman kwa macho makali.
“This does not apply to your case Roman, and you know it!(Hali hiyo haipo kwenye swala lako Roman, nawe walijua hilo!)”
Roman alibetua mabega.
“Sawa. So what do you want from me now?(Kwa hiyo sasa unataka nini kutoka kwangu?).
Inspekta Fatma alijibu moja kwa moja bila kusita. “Achana na yote yaliyopita Roman. Just Forget it! (Yaani sahau tu!)”
Roman hakumjibu na badala yake alitazama pembeni. Inspekta Fatma alimtazama kwa makini, na kwa muda mrefu.
“Hunipi ushirikiano mzuri Roman.” Hatimaye alimwambia.
“Kwa sababu sitaki kushirikiana nawe afande!” Alimjibu huku akiendelea kutazama pembeni, kisha akaongezea; “…na nisingependa kuendelea kukuona maishani mwangu, if you don’t mind (kama hutajali)”
Jibu hili lilionekana wazi kuwa lilimuumiza sana Inspekta Fatma.
“Naamini kama utafuata ushauri wangu hutaniona tena maishani mwako Roman. Lakini ukipuuzia na kufuata mambo ambayo nadhani ndio unataka kuyafanya…” Afande Fatma alimjibu kwa upole, huku akiiachia ile sentesi yake ielee hewani bila kuimalizia. Roman alisoma kitisho kilichokuwa ndani ya kauli ile, na alimkazia macho ghafla.
“Nikipuuzia…then what?(kisha nini?) Alimuuliza kwa jazba huku akimtolea macho ya ghadhabu ambayo yangeweza kumtisha mtu mwingine yeyote, lakini sio Inspekta Fatma.
Inspekta Fatma hakufanya haraka kumjibu, badala yake alimtazama kwa muda, kisha huku bado akimtazama moja kwa moja machoni, alimjibu kwa sauti ya upole lakini iliyojaa yale mamlaka yake yote iliyokabidhiwa na jamhuri.
“Basi nasikitika kuwa itakubidi uwe unaendelea kuniona tu kwa muda wote utakaohitajika ili kukutupa tena jela rafiki yangu!”
Jibu hili lilikuwa nje kabisa ya matarajio ya Roman na alifinya macho yake kumtazama vizuri yule askari wa kike mwenye msimamo. Walitazamana kwa muda na katika muda ule hakuna mmoja kati yao aliyekubali kushusha chini macho yake.
“Unanitishia afande?” Hatimaye Roman alimuuliza kwa sauti kavu huku akiendelea kumtazama kwa makini yule askari. Badala ya kumjibu, Inspekta Fatma alimuita mhudumu kwa ishara ya vidole vyake, na kulipia vile vinywaji walivyoagiza. Alibandika miwani yake ya jua usoni na kuinuka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia.
“Good Luck in your new life Roman!(Kila la kheri katika maisha yako mapya Roman!)”
Aligeuka na kuondoka eneo lile kwa mwendo wa madaha ya kike lakini ukionesha kuwa alikuwa akijiamini na asiyetishika na lolote hapa duniani.
Kwa muda mrefu Roman alibaki akiwa amekaa pale kwenye ule mgahawa nadhifu huku uso wake ukionekana kuwa na mawazo mazito. Hatimaye aliinuka na kutoka nje ya mgahawa ule kuendelea na safari yake aliyokuwa ameidhamiria wakati alipotoka kule gerezani, akiiacha ile bilauri ya juisi aliyonunuliwa na Inspekta Fatma pale juu ya meza ikiwa haijaguswa hata kidogo.
Kate aliingia ndani ya sebule ghali na kuubamiza mlango nyuma yake kwa ghadhabu. Alirusha funguo za gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado Metallic, Short Chasis, juu ya meza ndogo na nzuri sana iliyokuwa ndani ya ile sebule iliyojitosheleza kwa kila kitu. Alirusha miguu yake mbele mmoja baada ya mwingine huku akisonya na kuviacha viatu vyake vizuri vya kuchomeka vikiruka kila kimoja upande wake na kubaki vikigaa gaa juu ya zulia zito lililotandikwa pale sebuleni.
Alisonya tena na kutupa pembeni zile khanga aliyokuwa amejitanda kichwani na sehemu ya juu ya kiwiliwili chake, na hivyo kuachia nywele zake nzuri zilizokuwa zimewekwa katika ule mtindo wa ‘utajiju’, na kudhihirisha fulana nyeupe kubwa iliyoonesha mwinuko mdogo wa matiti yake mazuri ambayo yalionekana wazi kuwa hayakuwa yamebanwa na sidiria na wala hayakuonesha kuwa yalikuwa yanahitaji kubanwa na sidiria yoyote.
Alitoa na ile khanga nyingine aliyokuwa amejitanda kiunoni na kuitupia juu ya sofa jingine lililokuwa karibu yake na kudhihirisha suruali ya jeans iliyoukamata mwili wake kwa namna ya kutamanisha haswa, ikionyesha jinsi makalio yake yalivyochongwa kwa mvuto wa kipekee.
Aliinua uso wake na kutoa ile miwani yake ya jua aliyokuwa ameivaa na kuiweka taratibu juu ya meza ya Runinga kubwa aina ya Sony Plasma. Aliliendea jokofu lililokuwa kwenye kona moja ya sebule ile na kulifungua huku akiinama na kuchungulia ndani ya jokofu lile ambalo nalo lilikuwa la bei mbaya na ambalo daima lilikuwa halikauki mahitaji muhimu ndani yake.
Kwenye sofa lililokuwa kwenye kona moja ya sebule ile, mtu mmoja wa makamu aliyepata umri wa miaka ipatayo arobaini na minane hivi ambaye muda wote huo alikuwa akitazama nyendo zote za yule binti kwa utulivu mkubwa tangu aingie mle ndani, aliitazama ile sehemu ya nyuma ya yule binti mrembo akiwa ameinama namna ile kwa macho yaliyoonesha kuwa yalikuwa yanavutiwa na yalichokuwa yakikiona.
Kate aliinuka akiwa na juisi ya boksi aina ya Ceres mkononi na kugeuka huku akiinua lile boksi ambalo lilikuwa limeshafunguliwa na kulipeleka kinywani. Wakati huo huo yule mwanaume aliyekuwa akimtazama kwa utulivu tangu aingie mle ndani alionesha umakini na kumtupia swali.
“Kwani imekuwaje huko…?”
Alikuwa ni mtu aliyevaa mavazi ghali na shingoni alikuwa amening’iniza cheni moja ya dhahabu kinyume na jinsi ambavyo wengi wangetarajia kutoka kwa mtu wa umri wake. Alionekana wazi kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa pesa na yule binti angeweza kabisa kuwa mwanawe wa kumzaa.
Kate alibugia ile juisi kwa mfululizo huku akiwa ameinua juu kichwa chake ili ile juisi ishuke vizuri kooni mwake huku akimtupia jicho la pembeni yule mwanaume mtu mzima mwenye mwili mnene wa wastani na mvi chache kila upande wa kichwa chake. Alishusha lile boksi la juisi kutoka kinywani mwake.
“Sikuweza kuongea naye chochote bwana!” (Akasonya). Kisha aliinua tena lile boksi la juisi na kupiga funda jingine dogo la kile kinywaji alichokipenda sana huku akiliendea sofa lililokuwa karibu yake kwa mwendo wa pozi.
“Lakini umemuona? Ni yeye hasa? Ametoka leo?” Yule mzee aliuliza kwa bashasha. Kate aliafiki kwa kichwa kabla ya kumthibitishia kwa maneno.
“Yep! Ndiye haswa!”
Jibu hili lilionesha kumfurahisha yule bwana, lakini alitaka kujua vije amuone mtu aliyemkusudia halafu asiongee naye.
“Ah!(Aliguna) Kwa taarifa yako sio mimi peke yangu niliyekuwa nikimsubiri Roman pale nje ya gereza leo hii…” Kate alimjibu kwa kushutumu huku akiwa amembetulia midomo na yule bwana alionekana kushitushwa na habari ile huku akijisogeza mbele kwenye lile kochi alilokuwa amekalia kwa kiherehere.
“Eti Whaat?” Aliuliza kwa kutoamini.
“Kabisaaa!” Kate alimjibu na kuendelea kumuelezea mambo yote jinsi yalivyotokea hadi pale yule mtu aliyeitwa Roman alipoondoka na lile gari lenye namba za serikali. Yule bwana alibaki mdomo wazi huku akiwa amekunja uso wake katika jitihada ya kujaribu kuelewa undani wa maelezo ya Kate.
“Yaani yule mwanamke ameniboa! Laiti angejua kuwa kuna wanawake wanaoendesha gari za bei mbaya kuliko kile kimkebe chake cha serikali wala asingejitia kumchukua yule jamaa pale. Yaani nimepoteza muda wangu bure…!” Kate aliponda kwa hasira huku akiwa amekunja uso. Lakini yule mwenzake alikuwa na wasiwasi na mambo mengine kabisa kutoka katika yale maelezo yake
“Umesema Roman amechukuliwa na gari yenye namba za serikali…?” Yule mzee aliuliza tena, na kwa mara nyingine Kate alimthibitishia kuwa hivyo ndivyo. Jamaa aliguna na kutikisa kichwa.
“Sasa hii itakuwa nini…?” Aliuliza kwa sauti ya chini, ni kama alikuwa anajisemea mwenyewe tu.
“Sa’ mi’ n’tajuaje, Master D? Labda yule ni demu wake….” Kate alimjibu huku akijilaza kwenye lile sofa alilokuwa amekalia. Yule mtu alimtupia jicho la pembeni kisha akaendelea kutazama ukutani alipokuwa akitazama hapo awali.
“Hapana, Kate. Demu wake aje na gari la serikali? Sivyo. Hii ni issue kubwa kuliko unavyodhani…”
“Aaah, kwani si kuna mademu wengi tu humu mjini wanaofanya kazi serikalini na kupewa magari ya kutembelea? Kwa nini asiwe demu wake? Jamaa anaonekana handsome kwa kiasi chake, ingawa nilimuona kwa mbali…” Kate alimbishia.
Yule bwana aliinuka na kwenda kusimama nyuma ya dirisha na kutazama nje ya sebule ile. “Hapana. Nadhani hao ni askari…itabidi kuwa makini sana katika hili jambo.”
Kate aliinua macho na kumtazama yule bwana mtu mzima kwa muda, lakini hakusema kitu zaidi. Aliamua kuziweka safi kucha zake kwa kuzichokoa-chokoa kwa kijiti cha kuchokolea meno alichokiokota sehemu fulani ndani ya sebule ile.
Muda mrefu ulipita bila yeyote kati yao kusema lolote, yule mtu mzima akiwa kwenye dimbwi la mawazo, wakati yule mrembo mwenye deko aliyeitwa Kate akiendelea kucheza na kucha zake.
“Sasa tutampataje tena huyu mtu…” Yule jamaa wa makamu aliyeitwa Dan alijisemea mwenyewe. Dan Dihenga ndilo jina lake halisi, ingawa marafiki zake wa karibu walizoea kumkatisha na kumuita Master D. Kate alimtazama yule bwana kwa muda, kisha akamjibu huku akiendelea kucheza na kucha zake.
“Mi’ kazi yangu nilishaifanya ila nd’o hivyo imeingiliwa na huyo mwanamke. We’ ndiye unayejua…toa maelekezo, mi’ n’tafuata.”
Sasa ilikuwa zamu ya Master D kumtazama yule binti mrembo aliyekuwa akiendelea kuchezea kucha zake, ila sasa alikuwa ameziingilia za miguuni. Muda mrefu ulipita bila yeyote kati yao kusema neno, hatimaye Master D alirudi kwenye sofa alilokuwa amekalia hapo mwanzo na kukunja nne.
“Nadhani sasa kuna sehemu moja tu ambayo tunaweza kubahatisha kumpata. Na nadhani itatubidi tuelekee huko haraka.”
Sasa ilikuwa zamu ya Master D kumtazama yule binti mrembo aliyekuwa akiendelea kuchezea kucha zake, ila sasa alikuwa ameziingilia za miguuni. Muda mrefu ulipita bila yeyote kati yao kusema neno, hatimaye Master D alirudi kwenye sofa alilokuwa amekalia hapo mwanzo na kukunja nne.
“Nadhani sasa kuna sehemu moja tu ambayo tunaweza kubahatisha kumpata. Na nadhani itatubidi tuelekee huko haraka.”
Roman aliusogelea ule mwinuko mdogo wa udongo kwa hatua za pole pole mno, na kadiri alivyozidi kuusogelea ndivyo miguu ilivyozidi kumuwia mizito, na moyo ulivyozidi kumuuma. Ingawa alijua fika tangu alipotoka gerezani asubuhi ile kuwa mahala pale ndipo alipokuwa amedhamiria kuja kabla ya kwenda mahala pengine popote, lakini baada ya kufika alitamani kuwa asingekuja kabisa.
Lakini isingewezekana kuwa vinginevyo. Kwa vyovyote ilimbidi afike mahala pale. Na kama si yule askari wa kike kuingilia utaratibu wake, muda huu angekuwa ameshahudhuria eneo hili na kuwa mahala pengine kabisa.
Alisimama mbele ya ule mwinuko na kumbukumbu ya mara ya mwisho aliposimama mbele ya sehemu hii kabla haijawa na mwinuko kama ilivyo sasa ilimrudia na hapo alitoa sauti ya uchungu na macho yakamchonyota kwa machozi huku donge kubwa likamkaba kooni.
Wakati aliposimama mbele ya sehemu hii kwa mara ya mwisho palikuwa na shimo badala ya mwinuko…
Roman alipiga goti moja mbele ya ule mwinuko uliokuwa mithili ya tuta na kuinamisha uso wake kwa uchungu, paji la uso wake likiwa limelalia juu ya mkono wake uliolazwa juu ya goti lake. Machozi yalimbubujika na uchungu mwingi uliutawala moyo wake. Alijaribu kumuomba Mungu lakini hakuna neno takatifu hata moja lililomjia akilini mwake wakati ule. Kichwa kilimrindima kwa ghadhabu na moyo ulimtetema kwa uchungu.
Aliinua uso wake na kuuangalia msalaba uliochomekwa mbele ya lile kaburi, na moyo wake uliingia mlipuko mpya wa simanzi iliyochanganyika na uchungu pale aliposoma jina lililoandikwa kwenye ule msalaba.
Rachel Koga.
Ilimuwia vigumu kuamini kuwa alikuwa akilisoma jina lile kwenye msalaba…hakika hakuwa ametegemea kabisa kitu kama hicho maishani mwake.
Chini ya jina lile la marehemu aliyelala chini ya ule mwinuko wa udongo kulikuwa kuna tarehe yake ya kuzaliwa na ile aliyoaga dunia, tarehe ya kuaga kwake dunia ikiwa ni miaka miwili iliyopita.
Kwa mujibu wa zile tarehe zilizoandikwa kwenye msalaba ule, ilionesha kuwa yule marehemu aliyekuwa akiitwa Rachel, aliiaga dunia hii akiwa na umri wa miaka kumi na tisa.
Miaka kumi na tisa tu!
Roman alilia!
Alilia akiwa amepiga goti pale mbele ya lile kaburi bila ya kujizuia. Alilia kwa uchungu na hasira na majonzi. Hatimaye alipata maneno ya kuongea na Mungu wake akiwa pale mbele ya lile kaburi, hivyo huku machozi yakimbubujika kwa wingi, Roman aliinua uso wake na kutazama mbinguni na maneno yakamtoka kinywani mwake huku bado kilio kikiwa kimemkabili.
“Mungu wangu! Natumai utanisamehe kwa nitakalolifanya. Ni wewe pekee ndiye mwenye uwezo wa kusamehe hata wale waliokukosea kwa namna kubwa kabisa…lakini mimi ni mwanadamu tu Mungu wangu, na ni kiumbe dhaifu sana. Sina uwezo wa kusamehe kama ulio nao wewe…na sina namna ya kutofanya makosa kwani hiyo ni ada yangu kama mja wako. Sina ninalotumainia isipokuwa msamaha wako, kwa hiyo naomba msamaha kabisa mola wangu kwa sababu jambo nililodhamiria kulifanya kwa hakika linahitaji msamaha wako…”
Hakuweza kuendelea.
Aliinamisha kichwa kwa simanzi huku machozi yakimtiririka kwa wingi na sauti ndogo za uchungu zikimtoka ilhali mabega yakimpanda na kumshuka kwa kila kwikwi ya kilio iliyomtoka.
Kwa hakika alikuwa ni mtu mwenye uchungu wa hali ya juu.
Alilia mpaka akaishiwa machozi, ndipo alipoinuka kutoka pale alipokuwa amepiga goti na kuanza kujishughulisha na kuling’olea majani lile kaburi na kuuweka sawa ule msalaba ambao kidogo ulilalia upande mmoja kutokana na kumong’onyoka kwa udongo upande mmoja wa lile kaburi.
Alijazia udongo sehemu zilizokuwa zimemong’onyoka kwa mikono yake bila kujali kujichafua. Alipomaliza alijipangusia mikono yake kwenye suruali yake ya jeans na kurudi nyuma hatua chache na kutazama kazi yake.
Ilimridhisha.
Alilitazama lile kaburi kwa muda mrefu, kisha aligeuka na kuondoka eneo lile la makaburi kwa unyonge mkubwa.
Bila ya yeye kujua, watu wawilli waliokuwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa hatua kadhaa kutoka kwenye yale makaburi ambayo hayakuwa yamejengewa uzio, walikuwa wakishuhudia mambo yote aliyokuwa akiyafanya pale kaburini kwa utulivu mkubwa. Alipotoka na kuanza kuelekea kituo cha basi kilichokuwa karibu kabisa na makaburi yale, alipita karibu na lile gari bila hata ya kuliangalia. Muda huo Kate alianza kufungua mlango ili amfuate, lakini Master D alimzuia huku akiendelea kumtazama yule mtu mwenye majonzi akijikongoja kutoka eneo lile.
Kate alimgeukia Master D kwa mshangao huku akitoa sauti ya kukereka na kumuuliza kulikoni anamzuia asimwendee yule mtu ambaye walikuwa wanamhitaji sana na hawajui kuwa wakimkosa wakati ule wangempata wapi tena.
“Huu sio muda muafaka Kate…” Dan alimjibu kwa sauti ya upole huku uso wake ukionesha mawazo mazito wakati akimtazama yule mtu aliyetoka gerezani asubuhi ile.
“Sasa tutampata vipi tena Master D?” Kate aliuliza wakati akimshuhudia Roman akipanda daladala mbele yao.
Bila ya kujibu, Dan aliingiza ile Prado Short Chasis barabarani na kuanza kulifuata lile daladala aina ya kipanya.
“Kazi yako ni kuangalia Roman anateremka kituo gani baby…mengine niachie mimi!” Alimwambia yule binti. Badala ya kumjibu Kate alijiegemeza vizuri kwenye kiti chake na kuikazia macho ile daladala iliyokuwa mbele yao.
Safari ya Roman iliishia maeneo ya Kawe ambako alienda moja kwa moja hadi kwenye eneo kubwa kidogo la biashara ambalo lilikuwa limezungukwa na milango mingi ya maduka ya biashara mbali mbali, zikiwamo saluni za kike na za kiume, maduka ya bidhaa mbalimbali za rejareja, maduka ya mavazi, simu za mikononi, huduma za kupigisha simu na mauzo ya vocha za simu mbalimbali na vitu kama hivyo. Nje ya eneo lile alimuulizia mtu aliyekuwa akimtaka na alielekezwa kwenye mlango mdogo wa chuma ambao alipoingia ndani yake alitokezea nyuma ya maduka yale ambako kulikuwa kuna baa iliyojificha. Kwa muda ule ile baa haikuwa na wateja isipokuwa walevi wachache sana waliobobea. Pale aliulizia tena na kijana aliyekuwa akifanya usafi pale baa alimuelekeza kwa kidole upande mmoja wa ile baa ambako kulikuwa kuna ukuta uliokuwa na mlango mpana wa chuma.
Roman aliusukuma ule mlango na kuingia ndani. Alitokea kwenye eneo pana lililozungukwa na mabenchi na viti vya namna mbali mbali katika kila kona ya eneo lile, ilhali eneo la katikati ya ukumbi ule kukiwa kuna ulingo wa ndondi uliokamilika.
Roman alitembeza macho mle ndani na kushuhudia vijana wengi wakiwa katika harakati za mazoezi mbali mbali ya viungo na kujenga miili yao kama mabondia wanavyotakiwa kufanya, na ile taswira ilimrejeshea kumbukumbu za siku nyingi za nyuma na akahisi mwili ukimsisimka na moyo ukimlipuka kwa matarajio na kuanza kumuenda mbio. Alibaki akiwa amesimama pembeni ndani ya ukumbi ule kwa muda akitazama zile harakati zilizokuwa zikiendelea mle ndani kwa namna ya kuvutiwa sana. Kwenye ukuta uliokuwa mbele yake upande wa pilli wa ukumbi ule kulikuwa kuna maadishi makubwa yaliyosomeka KAWE BOXING CLUB.
Hapo alijua kuwa hakuwa amepotea, kwani ndipo haswa mahala alipokuwa amekusudia kufika baada ya kutoka kule makaburini.
Wale vijana waliendelea na harakati zao bila ya kumtilia maanani, naye alilisogelea benchi moja lililokuwa kwenye kona moja ya ukumbi ule na kuketi akitazama zile harakati huku akijaribu kuangaza huku na huko mle ndani akimtafuta mtu aliyekuwa amemkusudia, lakini ilikuwa wazi kuwa hakuwepo.
Hilo halikumtia wasiwasi wowote.
Alijua kuwa angetokea tu, naye aliamua kusubiri huku akiwatazama wale vijana wakitokwa jasho kwa harakati zao za kujiweka sawa kimazoezi.
Muda mfupi baadaye mtu mmoja mfupi mwenye upara na aliyeonekana kuwa na umri wa kati miaka arobaini na saba na hamsini aliingia mle ndani kwa mwendo wa haraka akitokea kwenye mlango mwingine mdogo uliokuwa upande wa pili wa eneo lile, kando ya yale maandishi yaliyosomeka “Kawe Boxing Club”.
“Alright! Alrght! Alright….! Hey!” Yule mtu alisema kwa sauti ya juu huku akipiga makofi na wale vijana waliacha mazoezi yao na kujipanga pamoja kumsikiliza.
Roman aliachia tabasamu kubwa baada ya kumuona yule mtu ambaye haikuwa na shaka kabisa kuwa ndiye mkufunzi au kocha wa wale vijana. Alikuwa amevaa suti ya mazoezi (Track Suit) iliyomkaa vizuri sana, na viatu vya raba aina ya Reebok. Alipendeza sana, na Roman alikumbuka nyakati za siku za nyuma alipokuwa pamoja na mtu yule mzee mwenye roho ya kipekee.
Yeye na mwenzake mwingine…
Alijitikisa kichwa kwa namna ya kuyafuta mawazo yale kichwani mwake na kurejesha akili yake kule kwa bwana mwenye upara na vijana wake.
“Okay! Tuna mechi ya kugombea ubingwa wa wilaya kesho kutwa na wote tunawajua wapinzani wetu tulionao hapa wilayani ni akina nani. Lengo letu ni kuchukua ubingwa wa taifa, lakini hatuwezi kufanya hivyo kama hatujashinda ngazi ya wilaya na mkoa. Mko tayari?”
“Ndiyoooo!” Wale vijana walijibu kwa sauti ya juu huku wengine wakipiga mbinja na kurukaruka huku na huko, wakitupa mgumi hewani kiufundi kwa jazba na kujijaza hamasa. Roman alizidi kuachia tabasamu kufurahishwa na hali ile.
“Okay! Dulla!”
Bondia aliyeitwa Dulla alichomoka mbele kwa mbwembwe kali za kibondia, akitupa ngumi nyingi za mfululizo hewani kwa nguvu na kasi ya kuvutia, huku akibonyea mara kwa mara kama anayekwepa masumbwi ya mpinzani na kujiinua tena na kutupa ngumi nyingine kwa mitindo ya hook na upper cut, kisha akatulia mbele ya kocha wake akiwa ameinua ngumi zake usoni mwake kama jinsi mabondia wanavyosimama wakiwa wanasubiri amri ya mwamuzi kabla ya kuanza kwa pambano.
Yule kocha alimtazama mpiganaji wake kwa namna ya kuridhishwa na makeke yake, kisha akamueleza.
“Utapanda ulingoni na Chumbi wa timu ya Wandava Boxing katika uzito wa Bantam! Chumbi ni moto wa kuotea mbali na sina haja ya kukumbusha juu ya hilo, tatizo lako kubwa ni kujiamini kuliko kawaida Dulla, na usipoangalia, hilo ndilo litakuwa kaburi lako katika ndondi…” Hapo macho ya yule mtu mwenye upara yalimuona Roman akiwa ameketi kwenye benchi kando kabisa ya ukumbi ule na hapo hapo alikatisha maelezo yake. Badala yake uso wake ulijaa mshangao huku akifinya macho kumtazama vizuri yule mtu aliyetoka gerezani asubuhi ile. Wale vijana wote nao wakafuata macho ya kocha wao na kumgeukia Roman.
“Roman…!?” Yule mzee alisema kwa sauti ya chini iliyojaa mshangao na maswali ya kutoamini.
Taratibu yule bwana aliyejengeka kimazoezi aliwasogeza pembeni wale vijana waliokuwa mbele yake na kumuendea Roman kwa mwendo wa taratibu. Roman aliinuka kutoka kwenye lile benchi alilokuwa amekalia na kuanza kumsogelea yule mzee. Walitazamana kwa muda huku wakisogeleana, na hatimaye yule mzee alijihakikishia kuwa ni kweli macho yake yalichokuwa yakimuonesha, kwamba kwa hakika yule aliyekuwa akimuona alikuwa ni mtu aliyemtambua kwa jina la Roman.
“Roman! Roman…! Umetoka…?”
Walikimbiliana na kukumbatiana kwa nguvu na upendo wa hali ya juu kwa muda mrefu. Hatimaye yule mzee alimsukuma nyuma kidogo Roman na kumtazama usoni huku akiwa amemshika mabega.
“Ah! Roman! Umetoka lini? Mbona sikuwa na taarifa…? Unaonekana uko fiti sana!” Aliuliza.
“Leo, Kocha! Nimetoka leo…asubuhi hii hii…” Roman alimjibu yule mzee ambaye kufikia pale hakuweza kuyazuia machozi yasimtiririke.
“Ah, Roman my boy! Miaka miwili sio mingi kumbe afterall eenh?” Alisema huku akiachia machozi yamtiririke bila ya kufanya bidii yoyote ya kuyafuta.
“Yeah, Coach…sio mingi kama ilivyoonekana hapo mwanzo.” Roman alimjibu huku akimpangusa machozi yule mzee aliyemwita ‘Coach’ kwa kiganja cha mkono wake. Wale vijana waliokuwa wakifanya mazoezi pale ukumbini walikuwa wakitazama tukio lile kwa udadisi wa hali ya juu. Yule bwana mwenye upara alimshika mkono Roman na kumuongoza kuelekea kule kwenye mlango aliotokea hapo awali na kuwakuta wale vijana wake wakifanya mazoezi pale ukumbini.
“Come on! Twende tukaongee ofisini kwangu!’ Alimwambia bila kujali mshangao ulioonekana wazi kwenye nyuso za wale wanafunzi wake. Waliingia ndani ya ile ofisi na yule bwana alifunga mlango na kumuelekeza Roman aketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake mle ofisini naye akaketi juu ya meza, akikiacha kiti chake kilichokuwa nyuma ya ile meza.
Walitazamana kwa muda, kisha Roman aliongea kwa upole. “I am out now Mark (Nimetoka sasa Mark). Umeniwekea vitu vyote nilivyokuagiza?”
Makongoro “Mark Tonto” Tondolo, kocha wa ndondi wa muda mrefu, na bingwa wa zamani wa taifa wa ngumi za ridhaa katika uzito wa juu (Heavy Weight) alimtazama Roman kwa muda bila ya kusema neno. Kisha aliinuka na kuzunguka nyuma ya ile meza aliyokuwa ameikalia na kutoa faili jembamba kutoka kwenye droo ya meza ile na kumkabidhi.
“Kila kitu kimo humo ndani Roman, kama jinsi ulivyoagiza!” Alimwambia.
ITAENDELEA
Bondia Sehemu ya Pili
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;