Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Nne
KIJASUSI

Ep 04: Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili

SIMULIZI Mifereji Ya Dhahabu Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili
Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi : Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili 

Sehemu ya Nne (4)

Walitumia boti ndogo kusafiri katika mto Rivera mpaka mahali ambapo kiwango kidogo cha maji ya mto yanachepuka na kuingia katika mtaro mkubwa wa maji taka unaokusanya maji na kupita karibu na benki waliyotaka kuiba. Walipofika hapa walitumia maboya kuelea juu ya maji machafu ya mtaro yaliyojaa kinyesi cha binadamu na uchafu mwingine, walielea kuelekea mbele kwa takribani dakika ishirini wakiwa na ramani zao mikononi mpaka walipofika sehemu waliyoihitaji.

Baada ya kufika hapo Spaggiari akawapa maelekezo kuwa wanatakiwa wachimbe moja kwa moja bila kupindisha hata kidogo kwenda mita 8 ndani na kama watakuwa sahihi baada ya kufikisha mita 8 hizo alarm aliyoiweka kwenye vault ikilia basi wataisikia juu ya vichwa vyao, ikimaanisha kwamba wako chini ya sakafu ya vault.

Pia Spaggiari akawagawanya wenzake kwenye shift za kufanya kazi. Akawaambia kuwa kutakuwa na makundi mawili, kila kundi litafanya kazi kwa masaa kumi wakati huo wengine watakuwa wamelala na akawasisitiza kuwa ni lazima walale kwa masaa kumi. Kwahiyo shifti zilikuwa mbili, masaa kumi kazini na masaa kumi kulala. Pia akawakataza wasiguse kabisa pombe au kahawa kwa muda wote ambao watakuwa wanafanya hiyo kazi.

Siku iliyofuata kazi ilianza. Kazi ilifanyika bila papara, taratibu na kwa umakini mkubwa. Kazi ikaendelea kwa siku kadhaa, wiki kadhaa na baada ya miezi miwili hatimae walifikisha tanuru (tunnel) la urefu wa mita 8. Baada ya kufikisha umbali huo Spaggiari akawaambia wasubiri usiku wa manane kusikiliza saa ya muito ili wajue kama wako sahihi au la. Ilipofika usiku wa manane alarm ya saa iliyowekwa kwenye vault na Spaggiari iliita, na waliisikia juu ya vichwa vyao kabisa. Wakapongezana kwani sasa walikuwa na uhakika asilimia mia moja kuwa wako sahihi, walikuwa wako chini ya sakafu ya vault na kilichobakia ilikuwa ni kutoboa hiyo sakafu na kuchukua ‘mwali wao’.

Spaggiari akawaambia wenzake kuwa inabidi wapumzike kwa siku mbili kuisubiria Bestille Day ndipo watoboe sakafu na kuchukua mwali wao.

Bastille Day (siku ya Uhuru wa Ufaransa) ambayo husheherekewa kila mwaka tarehe 14 July na kwa mwaka huu 1976 ilikuwa inaangukia siku ya alhamisi, hivyo hii ilifanya kuwe na siku nne za mapumziko (alhamisi na ijumaa (sherehe za Bastille Day) Jumamosi na jumapili (mapumziko ya mwisho wa juma)). Kwahiyo Spaggiari alitaka wapate muda wa kutosha kwa siku nne ili wachukue fedha na vitu vingi kadiri wawezavyo.

Hatimaye alhamisi ikawadia na Spaggiari na genge lake wakamalizia kutoboa sakafu ya vault na kuingia ndani. Jambo la kwanza walilolifanya baada kufanikiwa kuingia ndani ya vault ni kuchomelea mlango wa vault kwa ndani ili mtu aliyepo nje asiweze kuufungua.

Kazi ikaanza na Spaggiari kwa kutumia uzoefu aliokuwa nao wa kufanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza ‘safes’ akawaongoza wenzake katika zoezi la kufungua visanduku. Kazi ilifanyika mchana na usiku kwa siku ya kwanza ya alhamisi na kesho yake siku ya Ijumaa Spaggiari akawaambia wenzake wapumzike kwa masaa machache ili nao washerehekee sikukuu ya Bastille kama wenzao walioko huko mitaani. Hivyo basi Spaggiari akatoka kwenye vault na kurudi mtaani kununua mvinyo pamoja na vyakula vya anasa na kurudi navyo kwenye vault kwa ajili ya kusheherekea. Baada ya kumaliza kula na kunywa kazi iliendelea usiku na mchana siku hiyo ya ijumaa, jumamosi na ilipofika jumapili mchana walikuwa wamefanikiwa kufungua yapata visanduku 400 vilivyokuwa na fedha taslimu, vito vya thamani, hati fungani na vitu vinginevyo vya thamani kubwa. Inakadiriwa kuwa thamani ya ‘mzigo’ wote ambao Spaggiari na genge lake walipata unafikia Faranga Milioni 60 za ufaransa (60 million French Frans).

Ilipofika muda wa mchana siku ya Jumapili mvua ilianza kunyesha na Spaggiari akahisi mitaro waliyotumia kuingilia inaweza kujaa maji na hivyo kufanya zoezi la kutoka kuwa gumu hivyo basi akawaamuru wenzake waondoke kabla mvua haijawa kubwa. Lakini kabla hawaondoka aliwaambia wenzake kuwa anahitaji kufanya jambo moja la muhimu la mwisho. Huku akionekana akiwa na hisia na msisimko wa hali ya juu, spaggiari alichukua kopo la rangi alilokuwa amekuja nalo pamoja na brashi ndogo ya kapakia rangi, kisha akausogelea ukuta mmoja ndani ya vault na kuandika maandishi makubwa yaliyo someka; “SANS ARMES, NI HAINE, NI VIOLENCE” (“Without weapons, nor hatred, nor violence” (“Pasipo silaha, wala chuki, wala ukatili”)).

Hiyo ndio ‘falsafa’ aliyotaka kuifikisha kwa ulimwengu mzima kujitambulisha yeye ni ‘mwizi daraja la kwanza’ wa dizaini gani.

Baada ya hapo wakafungasha mizigo yao, wakatokomea.

‘Maisha’ Baada ya Tukio..

Siku ya jumatatu benki ya Société Générale ilifunguliwa na shughuli ziliendelea kama kawaida pasipo yeyote kung’amua kuwa kuna jambo lilitokea ndani ya vault. Na kama ilivyo ada ilipofika majira saa Tatu na nusu asubuhi wafanyakazi wawili walielekea kwenye chumba cha Vault kukifungua ili kuruhusu wateja kuhifadhi vitu na wengine kuchukua vitu walivyohifadhi. Walipofika mlangoni wakaingiza namba maalumu na kisha kama ilivyo utaratibu wakaingiza funguo mbili katika matundu mawili juu ya mlango na kuzungusha funguo lakini jambo la ajabu mlango haukufunguka. Walihangaika kuzungusha funguo karibia nusu saa lakini mlango haukufunguka.

Baada ya juhudi zote hizo bila mafanikio wakaamua watoe taarifa kwa meneja msaidizi wa benki aliyeitwa Pierre Bigou. Bw. Pierre baada na yeye kuhakikisha kuwa mlango ulikuwa haufunguki ikabidi aagize aitwe muhunzi ili aje kuwasaidia. Dakika chache baadae muhunzi alifika na akaanza kuukagua mlango, na ndani ya dakika kumi na tano akawa ameng’amua kuwa mlango umechomelewa kwa ndani na hakuna namna ambayo wanaweza kuufungua wakiwa nje.

Sehemu ya mapokezi baadhi ya wateja walikuja kwa ajili ya kutumia visanduku vyao vya kwenye vault walianza kupaniki na ilimbidi meneja mwenyewe wa benki ahusike kuwatuliza na kuwaondoa wasiwasi. Meneja alitumia maarifa yake yote ya huduma kwa wateja kuwaondoa hofu wateja wake na kuwataka wawe watulivu, ” Nothing to worry about monsieur. A minor technical problem madame. Your valuables are quite safe but there may be a slight delay” (“ondoa hofu muheshimiwa. Ni tatizo dogo tu la kiufundi. Vitu vyenu viko salama ila itachukua muda kidogo kurekebisha.”) Meneja wa benki Bw. Jacques Guenet alisikika akiwatuliza wateja wake.

Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Tano

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment