Roman Abramovich – Utajili wa Damu, Risasi na Umafia Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA : THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi : Roman Abramovich: Utajiri Wa Damu, Risasi Na Umafia
Sehemu Ya Kwanza (1)
HOW TO BECOME A BILLIONARE.?
i)Invent โ kama una uwezo mzuri wa kiakili buni kitu kipya ambacho kitakuwa na uhitaji mkubwa kwenye jamii.
ii)Innovate โ tafuta kitu fulani, bidhaa au huduma na kisha boresha ufanisi wake au ufanyikaji wake na kisha ifanye kibiashara huduma hiyo au bidhaa.
iii)invest โ tafuta biashara au kampuni ambayoโฆโฆโฆ
Wrong..!!
Haya ndiyo majibu ambayo bila shaka yanatujia vichwani endapo tukipatwa na ndoto za labda siku moja kutengeneza utajiri wa kuzidi dola bilioni moja za kimarekani. Tunafikiria kufanya bunifu, kuboresha huduma, kuwekeza au kuwa wajasiriamali. Mbaya zaidi tunaamini kwamba yeyote yule ambaye amefanikiwa kuupata utajiri wa kiwango hicho cha โkufuruโ basi twamuhusudu kwamba ni mfanyabiashara au mjasiriamali nguli na hodari au labda ni mbunifu au mgunduzi mwenye akili iliyopitiliza. Nimekuwa nikiamini hivi pia kwa miaka mingi sana huko nyuma, nakumbuka nikiwa mwanafunzi wa sekondari niliwahi kutawaliwa sana na โwehuโ wa kutamani sana siku moja kuwa billionaire. Kuna jamaa mmoja muhindi alikuwa na duka maeneo ya upanga UN road la kuuza vitu kwa rejareja. Nilikuwa na rafiki yangu anaitwa Castro, basi tulikuwa tukitoka shuleni tunapita mara nyingi sana dukani kwake kwa ajili ya kuchukua jarida la Forbes. Dukani kwa huyu jamaa ndio mahalapekee ambapo kipindi hicho nilikuwa nafahamu naweza kulipata jarida la Forbes. Nakumbuka namna ambavyo ungeniona kipindi kile macho yakijawa na tabasamu pindi nikishika tolea jipya la Forbesโฆ namna ambavyo nilikuwa makini kufuatilia orodha ya matajiri wakubwa zaidi dunianiโฆ kipindi kile ningeweza kukutajia mabilionea wakubwa wa dunia kutoka kichwani kuanzianamba moja mpaka namba thelathini, majina yao, kiwango chao cha utajiri na majina ya kampuni zaoโฆ unguli wa Carlos Slim, Buffet na Gatesโฆ historia za kusisimua za kina Lakshmi Mitalโฆ kuibuka kwa kina Aliko Dangote na Mike Adenuga ambao walikuwa ni โnewbiesโ kipindi kile kwenye orodha ya Forbes. I loved itโฆ breathed it, nilisoma Forbes kama msahafu na ikanipa ndoto za ajabuโฆ kutamani kwamba niumize kichwa na kufanya gunduzi moja matata sana ya kunifinya siku moja kuwa na ukwasi huo kufikia dola bilioni moja za kimarekani.
Lakini kadiri ambavyo miaka iliongezeka na kuanza kufunguka macho kuelewa mfumo na mwenendo wa dunia nikaelewa kwamba kuwa bilionea ni kitu ambacho kinahitaji zaidi ya talata ya biashara, zaidi ya ujasiriamali na zaidi ya kufanya gunduzi au bunifu murua. Unaweza kuwa tajiri, unaweza kuwa milionea kwa kufanya gunduzi au bunifu makini au kuwa mfanyabiashara au mjasiriamali makini. Lakini kufikia ukwasi wa ubilioneaโฆ sio ubilionea kama ule wa Arusha wa kununua Nissan Patrol na kuwa na nyumba Njiro kesho kila mtu mtaani anakuita bilioneaโฆ hapana, naongea kuhusu ubilionea halisi wa ukwasi wa kuzidi dola bilioni mojaโฆ zaidi ya shilingi trilioni mbili za kitanzaniaโฆ utajiri ambao Watanzania wawili tu wamefanikiwa kuufikia, โmtoto wa mjiniโ Rostam Aziz na mhafidhina wa kibiashara Mo Dewji. Ukwasi wa ngazi hiyo unahitaji zaidi ya talanta ya ujasiriamali na biashara na zaidi ya upekee wa gunduzi na bunifu.
Niliwahi kuandika kwenye mada moja, โkatika kila kila utajiri kuna ukafiri nyuma yake.!โ Kuna ngazi ya utajiri ili kuifikia inahitaji purukushani, โkash kashโ na kufanya mambo ambayo yawezekana wengine hatuna kifua kuyafanya.
Nitatoa mfanoโฆ mfano wa moja wa billionare ambaye anahusudiwa sana ulimwnguni na moja ya mabilionea wa kupigiwa mfano sana ni Billionare Roman Arkadyevich Abramovich au kama ambavyo anajulikana kwenye inner circle pale Kremlin, โOligarch Abramivichโ au โMr Aโ.
Huyu muheshimiwa akiwa na umri wa miaka 34 tu Roman tayari alikuwa na tittle ya โOligarchโ, title ambayo jamii ya Urusi imewapachika watu wenye ushawishi mkubwa nchini humo na ambao wako kwenye โinner circleโ ya utawala wa nchi ya Russia. Katika miaka hiyo 34 tayari alikuwa anamiliki kampuni kubwa ya uzalishaji mafuta ya Sibneft na pia alikuwa moja ya wanahisa wakuu wa kampuni ya RUSAL (Russia Aluminum) ambayo kwa kipindi kile ndio ilikuwa kampuni inayoongoza kwa uzalishaji mkubwa zaidi wa Aluminum wakichangia zaidi ya 9% ya Aluminium inayotumika duniani kote. Katika umri huu wa miaka 34 ni ngumu kusema kwa hakika hasa utajiri wa Oligarch Abramovich ulikuwa unafikia kiasi gani kutokana na usiri kuhusu mapato yake, lakini hakuna shaka kabisa kwamba utajiri wake ulikuwa unazidi dola bilioni 6 za kimarekani.
Unaweza kujiuliza ni kwa namna gani katika umri mdogo kiasi hicho mtu anaweza kuwa na utajiri wa kupindukia kiasi hicho na hata kuwa moja ya wamiliki wakuu wa kampuni ya kuzalisha zaidi ya 9% ya aluminium inayotumika duniani.
Nataka tutazame mfano wa Abramovich kupata picha ni kwa namna gani unapaswa kuwa na โngozi ngumuโ kupitiliza ili kuukwaa ubilionea.
Tuanze mwanzo kabisaโฆ.
Roman Arkadyevich Abramovich ni yatima aliyelelewa katikika umasikini wa kupitiliza na baadae kufanikiwa kuwa moja ya matajiri wakubwa zaidi kuwahi kutokea duniani. Historia yake ni mwanana kabisa kumtia mtu moyo namna ambavyo unaweza โkuinuka kutoka mavumbini na siku moja kuketi na wafalme.โ Wazazi wake walifariki angali bado akiwa mdogo kabisa kabisa na hivyo kupelekea yeye kulelewa na nduguze waliokuwa wanaishi kaskazini mwa Urusi kwenye eneo la Komi.
Japokuwa wazazi wake na yeye mwenyewe wameishi maisha yao karibia yote nchini Russia lakini asili yao hasa ni Israel. Babu yake mzaa baba, mzee Nahim Abramovich alikuwa ni mfanyabiashara ambaye aliishi pamoja na mkewe (bibi mzaa baba) Tauba Berkover waliishi wote huko jamuhuri ya Lithuania kwenye jimbo la Taurage. Baba yake Abramovich, Arkady Abramovich alikuwa ni afisa wa serikali katika jamuhuri ya Lithuania. Mama yake Abramovich aliyeitwa Irina Michaleno wazazi wake (babu mzaa mama) Vassili Michalenko na mama yake (bibi mzaa mama) Faina Grutman nao wote waliishi jamuhuri ya Lithuania. Wazazi wake (Arkady na Irina) walifariki akiwa mdogo kabisaโฆ mama yake Abramovich, Irina alifariki Roman akiwa bado mchanga kabisa na baba yake Arkady alifariki kwa ajali ya gari miaka michache baadae. Na ndio hii ilisababisha Abramovich kwa mara ya kwanza kabisa kwenda kuishi Komi kwa nduguze, kaskazini mwa Urusi na baadae Uktah eneo lenye baridi kweli kweli na umasikini uliokithiri.
Katika ujana wake Abramovich aliwahi kujiunga na jeshi kwa muda mfupi sana kabla ya kuacha na kuanza kufukuzia ndoto zake. Kama ilivyo ndoto ya vijana wengi Tanzania miaka ya nyuma โkwenda Dar es salaam kutafuta maishaโ ndicho hicho pia kinawakumba vijana wengi duniani kote kutaka kwenda kwenye miji mikubwa ya nchi zao husika, ndicho hiki pia alikifanya Romanโฆ aliondoka Uktah na kwenda Moscow โkutafuta maishaโ. Akiwa Moscow alifanya akili ya kujiunga na kozi ya masuala ya mafuta na gesi katika taasisi ya Gubkin Institute of Oil and Gas ambako alikuwa anasoma huku akiuza matairi chakavu ya gari ili kuweza kujikimu kimaisha. Akiwa bado anapambana kutafuta nafuu ya maisha hapa Moscow ndipo pia alikutana na mkewe wa kwanza, Olga na kumuoa.
Maisha hayakuwa mepesi sana kwa Abramovichโฆ kipindi hiki ni kipindi ambacho Urusi ilikuwa inapitia kipindi cha mpito mgumu sana wa kiuchumi na kifalsafa. Ni kipindi ambacho ujamaa ulikuwa unadondoka na ubepari kushamiri nchini Urusi. Ni kipindi ambacho Urusi ilikuwa moja ya sehemu hatari zaidi kuishi kutokana na uhuni na ubabe ambao ulikuwa unatokea Urusi na nchi nyingi za Ulaya ya Mashariki. Ni kipindi hiki ambacho nchi za ulaya mashariki zilibatizwa jina la โWild Eastโ. Abramovich alifanya kila aina ya kazi ya hali ya chini, kuanzia kuuza bidhaa ndogo ndogo mitaani mpaka kuwa makenika kwenye viwanda na hata kuwa โbodyguardโ.
Waswahili tunasema kwamba โanayejua, anajua tuโ, kwamba kuna watu unaweza kuwapa ndimu ukidhani unawakomoa lakini atakushangaza kwa kuikamua na kutengeneza โjuisi ya lemonadeโ na kuinywa kwa raha mustarehe. Ndicho ambacho Roman alikifanya, kuanguka kwa ujamaa na kuibuka kwa ubepari, tena ubepari wa kihuni na ubabe aliona yaweza kuwa fursa adhimu kabisa kwakeโฆ akaanza kufanya biashara ya kila namna. Roman akaanzisha biashara ya kuuza midoliโฆ ile biashara ya kuuza tairi chakavu akaikuza zaidi na kuifanya kwa upana na mpaka kuwa wakala rasmi wa tairi mpya kutoka viwandani.
Lakini moja ya biashara ambayo ilimsaidia kumpa โconnectionsโ ilikuwa ni pale alipofungua biashara ya kutoa ulinzi binafsi (bodyguards). Pale juu nilieleza kwamba kipindi anaanza maisha Moscow Roman aliwahi kufanya kazi ya u-bodyguard, lakini safari hii sio yeye alikuwa bodyguard bali alikusanya vijana wake kadhaa na kufungua kama kampuni ya kutoa ulinzi kwa wadosi.
Nimesema kwamba hiki ni kipindi ambahi Urusi ilikuwa ni โWild Westโ, kipindi ambacho uhuni na ubabe ulikuwa ndio namna ya maisha. Kipindi ambacho ujamaa unandoka, serikali ikibinafsisha nyenzo zake za kiuchumi kwa watu wachache. Hapa kwetu Tanzania tumepita pia kwenye kipindi kama hiki hiki na wazee wetu wanajua shurba waliyopitiaโฆ anguko la ujamaa na kuibuka kwa ubepari. Kipindi ambacho tulibinafsisha kila kitu na kuacha wake zetu tu. Tofauti ni kwamba hapa kwetu wajanja ambao walibinafsishiwa mali za nchi walikuwa wanashindana ni yupi ambaye atatoa rushwa kubwa zaidiโฆ lakini kule โWild Eastโ haikuwa rushwa tu pekeeโฆ naam, ilikuwa lazima utoe rushwa kubwa kumzidi mwenzako lakini aliyekuwa mtemi na muhuni zaidi ndiye ambaye angeweza kujihakikishia umiliki wa kiwanda au rasilimali husika. ilikuwa ni kula au uliwe. Jifunze kula โnyma ya mtuโ au subiri ufanywe kitoweo.
Katika biashara za makampuni makubwa kuna kitu kinaitwa โhostile take-overโ. Yaani kwa mfano bwana Mo Dewji na kampuni zake za MeTL waanze kuuza hisa za kampuni zake za MeTL Group kwa ummaโฆ anakuja mtu ambaye kwa muda mrefu alikuwa anatamani aiweke MeTL mikononi mwakeโฆ tumuite mtu huyu Paul (mfano tu). Ananunua hisa nyingi zaidi kumuwezesha kupata ujumbe wa bodi ya wakurugenzi wa MeTL. Kisha anaanza kukaa kwa siri na wanabodi mmoja mmoja na kuwashawishi kumuondoa Dewji kama MD na Mwenyekiti wa bodi โฆ kikao kinaitwa, kura zinapigwaโฆ bodi inamuondoa Dewji kuwa MD na mwenyekiti wa bodi na kumfanya Paul kuwa MD na mwenyekiti mpya wa bodi. Dewji anabakia kuwa mwanahisa tu wa kawaida kama wengine bila uwezo wowote wa kimaamuzi juu ya kampuni yake ambayo aliinzisha. Hii inaitwa โhostile take-overโ. Lakini kipindi hicho huko โWild Eastโ, Urusi ya miaka hiyo walikuwa na namna ya tofauti ya โHostile Take-overโ. Tajiri mwenzako anakuvizia, anakutekaโฆ anakutesa mpaka unasaini makaratasi. Kisha anakutandika risasi na kesho yake inatangzwa kuwa kampuni/kiwanda chako ni chake na mliuziana kwa maandishi na nyaraka anazo. Wiki moja baadae mwili wako unaokotwa jalalani and nobody cares, maisha yanaendeleaโฆ Wild wild East.!!
Katika mazingira kama haya ambapo miili ya matajiri, waandishi wa habari na hata viongozi wa kisiasa ilikuwa inaokotwa kila siku imetupwa mitaani unaweza kupata picha ni kwa namna gani ambavyo biashara ya u-bodyguard iliweza kushamiri. Matajiri walikuwa na hofa na maisha yao muda wote, kwa hiyo walihitaji ulinzi muda wote. Biashara ya Roman ikashamiri.
โDiliโ hizi za kulinda matajiri na bishara zake za hapa na pale zilimpa โconnectionโ na kusaidia kujuana na watu muhimu ndani ya Moscow. Moja ya watu hawa muhimu ambaye baadae alikuja kuwa kama โmentorโ wake alikuwa ni Boris Berezovsky Mwanamahesabu nguli na mhadhiri wa chuo kikuu ambaye alikacha kufundisha chuo na kugeukia biashara ili asipitwe na upepo wa utajiri uliokuwa unavuma Urusi kipindi hicho.
Berezovsky alikuwa ni moja ya ma-Olygarch wa kwanza kabisa ndani ya Urusi. Nimeeleza pale mwanzoni Oligarchy ni watu wa namna gani. Borozevsky alikuwa ni moja ya matajiri wakubwa zaidi Urusi kipindi hicho ambaye alinufaika sana na ubinafsishaji wa mali za umma. Oligarch Boris Berezovsky hakuwa tu Oligarch bali alikuwa ni sehemu ya ma-Oligarch wachache ndani ya Urusi ambao waliojulikana kama โThe Familyโ.
The Family ilikuwa ni โinner circleโ ya watu wachache sana ambao walikuwa karibu na Rais wa Urusi kipindi hicho Boris Yeltsin. Watu hawa walikuwa ni wanafamilia wa Yeltsin pamoja na matajiri wachache sana akiwemo Berezovsky. Kikundi hiki cha matajiri wachache pamoja na familia ya Rais ndio kiuhalisia ndio walikuwa wanaendesha nchi.
Kwa hiyo kitendo cha Abramovich kujiweka karibu na Berezovsky ilimaanisha kwamba alikuwa amefanikiwa kujenga urafiki na moja ya watu muhimu zaidi ndani ya Urusi na mwenye ushawishi ndani ya inner cirle ya Rais.
Watu wenye asili ya uyahudi twaweza kuwachukia na kuwasema tutakavyo kwa uonevu ambao labda wanaufanyaโฆ lakini jambo moja ambalo hatuwezi kubisha ni uwezo wao wa asili kiakili na kimkakati. Japokuwa Abramovich kwa kipindi hicho alikuwa ni mrusi tu lakini kuna damu ya kiyahudi ilikuwa ndani yake na ni wakati huu ambao alidhihirisha umahiri wake kimkakati.
Baada ya urafiki wao Abramovich na Berezovsky kukomaa na kushibana, Abaramovich alimuomba Berezovsky amsaidie kumtambulisha kwa watu muhimu Kremlin. Moja kwa moja Berezovsky akahisi labda Abramovich anataka kutambulishwa kwa Rais au mawaziri na akamjibu bado hajafikia ngazi ya kutambulishwa kwa watu haoโฆ lakini Abramovich akamwambia hapana haitaji kutambulishwa kwa Rais au mawaziriโฆ anahitaji kutambulishwa kwa mtu anaitwa Valetin Yumachev ambaye kipindi hicho alikuwa ni afisa wa kawaida tu wa Ikulu kitengo cha habari na maelezo na hukuwa na ushawishi kwa Rais Yeltsin. Berezovsky alishangaa maana Yumachev hakuwa na ushawishi wowote ule pale Kremlin.
Ndio hapa ambapo nasema kuna watu ni โborn tacticiansโโฆ akili yao inawaza kimkakati kwa kila hatua na moja wapo ni huyu Abramovich. Abramovich alielewa wazi kabisa hawezi kutambulishwa kwa Rais na japo alikuwa na tuhela tudogo twa kubadili gari na nyumba lakini ukilinganisha na ma-Oligarch kipindi hicho yeye alikuwa ni kidagaa tu, โhohe haheโ ambaye hawezi hata kukaa meza moja na rais. Lakini anaitaka hiyo connecvtion kuliko kitu chochote kile ili afike pale anapopataka kimafanikio. Ndipo hapa ambako aliona kitu ambacho wengine hawakukionaโฆ Valentin Yumachev, afisa habari mdogo wa Ikulu. Abramovich aligundua kwamba Yumachev alikuwa na mahusiano ya siri ya kimapenzi na binti wa Yeltsin aliyeitwa Tatyana. Binti huyu wa Rais pia alikuwa anapendwa mno na baba yake na alikuwa moja ya watu anaowasikiliza sana na kuwaamini.
Abaramovich akapiga hesabu zakeโฆ kama akiweza kujenga urafiki wa kushibana na Yumachev, na kisha kufanya uhusisano wa Yumachev na Tatyana ukue na hatimaye labda kuoana. Maana yake ni kwamba atakuwa ni rafiki wa mkwe wa Rais wa Urusi. Na kutokea hapo kujiweka karibu na Rais kupitia mgongo wa โbest friendโ wake itakuwa ni rahisi kama kusaga maini.
Berezovsky akamtambulisha Abramovich kwa Yumachev. Hata Yumachev mwenyewe akashangaaโฆ โmtoto wa mjiniโ Abramovich ambaye ni rafiki wa ma-Oligarch kutambulishwa kwake. Kwa hiyo hata urafiki ukakua kwa haraka sana Yumachev kuona ni heshima kubwa kwake kwa mtoto wa mjini kama Abramovich kumthamini na kumuona ana umuhimu.
Lakini Abramovich alikuwa anaiona โpotentialโ ndani ya Yumachev ambayo hata mwenyewe alikuwa haioniโฆ Abramovich alikuwa anaona miaka mitano mbele ambayo wengine walikuwa hawaioniโฆ
Nimeona niwekee sehemu hii ya pili usiku usiku ili tukalale na tafakuri nzito kuhusu ulimwengu wetu na nama ambavyo unakwenda
Sasa,
Kipindi hiki ambacho nimeeleza kwamba Abramovich aliomba kutambulishwa kwa Yumachev, Abramovich alikuwa ni kijana mdogo tu wa umri wa miaka 28. Kutokana na urafiki wao wa kushibana na Berezovsky, Berezovsky alimtambulisha Abramovich kwa Yumachev bila kusita. Nimeeleza kwamba kipindi hicho Yumachev alikuwa ni afisa habari tu wa Ikulu lakini hakuwa na ushawishi wowote kwa Rais Boris Yeltsin.
Lakini baada ya urafiki wa Yumachev na Abramovich kukoleaโฆ Abramovich akaanza โkumuazima akiliโ Yumachev. Kumuonyesha ni kwa namna gani uhusiano wake wa kimapenzi na mtoto wa Rais wa nchi kama akichanga karata zake vyema uhusiano huo unaweza kumuinua kutoka mavumbini kwenye uafisa habari wa ikulu na pengine kumfanya kuwa moja ya watu muhimu zaidi kwenye โinner circleโ ya Rais Yeltsin.
Yule binti wa Rais ambaye Yumachev ana uhusiano naye wa kimapenzi hakuwa binti tu legelege wa kula mkate kwa siagi mezaniโฆ binti huyu alikuwa ni moja ya washauri wakuu wa Rais Yeltsin. Alikuwa ni moja ya watu wenye kuaminiwa zaidi na Rais. Sasa ambacho Abramovich alikuwa anakifanya ni kumpa mikakati ya Yumachev na kisha Yumachev anakwenda kushauriana na Tatyana na kisha wanaenda kumshauri Rais. Kadiri muda ulivyokuwa unakwenda Yumachev akaanza kuonekana kwamba naye ni mtu mwenye bongo makini na mwenye kujua mikakati. Si miezi mingi, Yeltsin akamapandisha cheo Yumachev akamfanya kuwa โHead of Adminstrationโ wa Ikulu, cheo ambacho kwa kipindi hicho nchini Urusi kilikuwa adhimu mno. Si hapo tu kwa ushauri wa Abramovich Yumachev akamuoa kabisa Tatyana. Hapo ndipo hasa pale ambapo Abramovich alikuwa anapataka.
Kwa pamoja Abramovich, Yumachev na safari hii pamoja na Tatyana urafiki wao ukaota mizizi haswa. Kutokana na ukaribu huu wa Abramovich na Afisa mkuu wa masuala ya utumishi Ikulu na nchi pamoja na ukaribu na binti wa rais ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais moja kwa moja Abramovich akatambulishwa na โmarafikiโ zake hao wawili kwa Rais Yeltsin na kutokana na uwezo wake wa hali ya juu wa kimikakati na kufikiri, Abramovich hakuchukua muda sana akawa sehemu ya โThe Familyโ.
Nilieleza pale mwanzoni kuhusu โThe Familyโ, ile inner circle ya Rais Yeltsin ambayo ilikuwa inaundwa na wanafamilia ya Rais pamoja na ma-Oligarch wa Urusi. Hii โThe Familyโ ndio hasa ilikuwa inaendesha nchi ya Urusi kipindi kile. Sasa baada ya Abramovich kuwa sehemu ya โThe Familyโ kukaibuka inner circle ndani ya Inner circle. Yaani kwamba kwenye wale watu wachache ambao walikuwa wanaaminiwa mno na Rais Yeltsin (The Family) kukaibuka kikundi cha watu wachache zaidi kati yao The Family ambao walikuwa wanaaminiwa zaidi na Rais uzidi wengine wote, ndio hapa nasema inner circle ndani ya inner circle. Watu hawa walibatizwa jina la โUtatu Mtakatifuโ na utatu huu mtakatifu walikuwa Abramovich, Yumachev na Tatyana.
Kijana yule yatima, aliyekimbia umasikini kutoka kwenye maisha ya kulelewa na ndugu zake jimboni Komi, ati leo hii akiwa na miaka ishirini na nane tu anaketi meza moja na moja ya binadamu mwenye ushawishi na nguvu zaidi duniani, Rais wa Urusi na tena anaketi akiwa moja ya watu ambao Rais anawaamini sana na kuwasikiliza sana.
Ndani ya hii โThe Familyโ Abramovich alipachikwa jina la โFamily Walletโ. Hii ni kutokana na kutumiwa sana na Rais Yeltsin na familia yake kwenye usimamizi wa masuala yao ya fedha na utajiri wao.
Nimeeleza, wakati huu ndipo ambapo Ujamaa ulikuwa umedondoka na Ubepari kuanza kushamiriโฆ kwa hiyo kwa wanasiasa na wazee ambao wamekuwa kwenye maisha ya kijamaa hawakuwa na uelewa mpana sana wa namna ambavyo mizania ya kibepari inavyofanyakazi. Lakini Abramovich alikuwa ni mfanyabiashara japo hata kama alikuwa akiuza midoli na matairi, amekulia mtaani akijua ni namna gani kanuni za โnatural selectionโ zinafanyakaziโฆ vyenye nguvu vinakula dhaifuโฆ na zaidi ya yote Roman alikuwa na uwezo wa kuzaliwa wa kiakili, mikakati na โkujiongezaโ. Kwa hiyo akatumia ujuzi wake huu kushauri familia ya Rais namna bora zaidi ambavyo wanaweza kutunza utajiri waoโฆ akaanza kuwafundisha na kuwezesha familia ya Rais Yeltsin kufungua offshore accounts, uwekezaji kwenye masoko ya hisa, kufungua offshore companies ambazo wamiliki wanafichwa kwenye mifumo โcomplexโ kujua nani hasa ni mmiliki na mambo mengine mengi ya kibepari. Kwa maneno mengine Abramovich alikuwa anawafungua macho namna ya โkuibaโ na kuficha fedha za umma kisasa katika namna ambayo ni ngumu kujulikana na namna za uhakika zaidi kwa fedha hizo kuwa salama.
Urusi ilikuwa inabadilika haraka mnoโฆ kutoka kuwa mpigia chapuo mkuu wa Ujamaa duniani na kuwa nchi ya kibepari tena ubepari wa kihuni kabisa. Japo suala la ubinafsishaji wa makampuni ya umma kwenda kwenye umiliki wa watu binafsi lilipongezwa sana na nchi za magharibi wakiona kama hatua nzuri ya nchi hiyo kuhama kutoka kwenye uchumi unaoshikiliwa na dola na kuanza kwa โsoko huruโ la kiuchumi ndani ya Urusi lakini wananchi wa Urusi hawakuona kile ambacho wadosi hawa wa magharibi walikuwa wanakiona. Wananchi walikuwa na hasira wakihisi kwamba nchi yao na uchumi unaganywa kwa kikundi cha watu wachache huku wao wakiendelea kuteseka na hali duni za kimaisha.
Kipindi cha ubinafsishaji wa makampuni ya umma kuna jambo mojaambalo mwanzoni lilikuwa jema lilikuwa limefanyika kabla ya kugeuka shubiri mbeleni.
Kila mwananchi alipewa โvoucherโ yenye thamani ya fedha ya Urusi rouble 10,000. Lengo la vocha hii ilikuwa ni kuwapa nafasi kila mwananchi wa urusi kumiliki hisa kwenye kampuni za serikali ambazo zilikuwa zinabinafsishwa. Kivipi? Yaani kwamba kampuni ya serikali ikiwa inauzwa na ikatangazwa kwamba kampuni hiyo ina thamani ya kiasi fulani cha fedhaโฆ ni kweli watajitokeza matajiri ambao watanunua hisa nyingi zaidi lakini bado mwananchi wa kawaida alikuwa anaweza kupeleka vocha ile ya rouble elfu kumi na akanunua hisa zenye thamani ya vocha hiyo.
Lakini kwenye miti hapana wajenzi na mtu aishiye mwituni ambaye hajui thamani ya almasi siku akiishika hawezi kuona tofauti yake na kokoto, aweza kuipiga kwenye manati kama jiwe ili aue ndege chiriku akafanye kitoweo. Ndicho ambacho kilitokea Urusi. Nchi ilikuwa ndio kwanza ilikuwa imetoka kwenye ujamaaโฆ wananchi hawakuwa wanajua namna gani hasa ubepari unafanyakazi. Nini kilichotokea? Wajanja wachache wakawa wanatuma mawakala wao vijijini na mijini kwa wananchiโฆ wanawashawishi wananchi wawape vocha na wao wanawapa fedha tasilimu. Karibia kila mwananchi alikuwa anakubali. Anatoa vocha yenye thamani ya rouble 10,000 alafu yule ajenti anampa labda rouble 200 cash. Unaweza kujiuliza wananchi hawa walikuwa vichaa au?? Hapanaโฆ maarifaโฆ maarifaโฆ fikiri mwananchi huyu amezaliwa na kukulia kwenye ujamaa. Leo hii ati unampa kipande cha karatasi unamwambia kina thamani ya pesa (wakati yeye anaona ni karatasi tu) alafu unamwambia atumie karatasi hiyo kwenda kununua hisa za kampuni (hajui hata hisa ina maana gani zaidi ya kusikia tu kwenye rediio inatajwa tajwa)โฆ alafu unamueleza akiwa na hisa kwenye kampuni fulani siku moja inawezekana labda (hakuna uhakika) kama kampuni hiyo husika ikianza kutengeneza faida atalipwa โdividendsโ (dividends ndio โmduduโ gani). Unaweza kuona mnyumbuliko wa mawazo ya mtu huyu aliyekulia kwenye ujamaa? Yawezekana hata sisi tungekuwa kwenye nafasi zao tungeuza vocha ya thamani ya rouble elfu kumi kwa rouble 200 cash tukale wali na nyama tushibe, tulale, tuamke tuanze kuhangaika tena kesho.
Na hii imetokea hata hapa kwetu nchini tena juzi juzi tu hapaโฆ unakumbuka kipindi cha ruzuku ya pembejeo za kilimo za serikali katika utawala wa Mzee Kikwete? Watu walikuwa wanauza vocha kwa shilingi elfu kumi tu alafu wale mawakala wanapeleka NMB wanalipwa laki na sitini kwa kila vocha au zaidi.!! Yale yae, almasi kuiona kokoteโฆ
Sasa pale Urusi wajanja wachache sana walinunua hizi vocha na na kuzitumia kununua hisa za makampuni yaliyokuwa yanabinafsishwaโฆ makampuni ya mafuta, gesi asilia na kadhalika. Ndipo hapa kukaibuka matajiri wale ambao nilisema wakabatizwa jina ma-Oligarch. Mbaya zaidi Yeltsin akawaweka karibu mno ma-Oligarch akishirikiana nao kuendesha nchi.
Wananchi walikuwa na hasira kweli kweli na Yeltsin.
Umaarufu wa kisiasa wa Rais Yeltsin ulikuwa umeshuka mno kupitiliza. Ukichangiwa pia kwa sehemu nyingine kutokana na matatizo ya moyo mara kwa mara akipatwa na mshituko na kufanyiwa upasuaji na kumfanya asionekane sana kwa umma.
Ukafika mwaka 1996โฆ mwaka wa uchaguzi mkuu wa Urais. Kila mtu alikuwa anasubiri kusikia Yeltsin atamtangaza nani kama mgombea kwenye chama chake maana hakuna ambaye alikuwa anadhani kwamba Yeltsin atagombea tena maana umaarufu ulikuwa umeporomoka mno, wananchi wanamchukia na afya yake ilikuwa mgogoro.
Ajabu ni kwamba mwezi February mwaka huo 1996 Yeltsin akatangaza kwamba atawania muhula mwingine wa uonngozi. Vyama vya upinzani vilishangilia maana walijua kwamba ushindi wa kishindo uko barazani kwao.
Kabla ya kupiga kura mwezi Desemba, katikati ya mwezi July yalitolewa matokea ya kura za maoni na mgombea wa chama cha Upinzania cha Kikomunisti Bw. Gennady Zyuganov alikuwa anaongoza kwa asilimia nyingi akimuacha mbali kabisa Rais Boris Yeltsin.
Kambi ya Rais presha ikawapandaโฆ paniki ikiwatawala. Kila mti unateleza. Hakuna mwenye kujua wafanyejeโฆ waliona kabisa wanaelekea kuupoteza โmnofuโ wao. Nani awaokoe?
Pale mwanzoni niliandika kwambaโฆ a born tactician, haijalishi ni mazingira gani utamuwekea lazima apate namna ya โku-surviveโ, lazima aone upenyo mwembamba wa shaba kwenye giza totoro. Mpe limao ukidhani unamkomoa, ukirudi baadae utakuta amelikamua na kutengeneza juisi ya โlemonadeโ akinywa kwa starehe kabisa. Hivi ndivyo ambavyo Roman Abramovich akili yake inanyumbulikaโฆ wakati ambapo timu nzima ya Rais Yeltsin imepaniki hawajui nini cha kufanya yeye aliona hiyo ndio fursa kwake kumdhihirishia Boris Yeltsin kwamba kichwa chake kimebeba mbongo ambayo sio ya mchezo mchezoโฆ
Uchaguzi ulikuwa unakaribia, wananchi walionekana dhahiri wanaegemea upande wa mkomunisti Zyuganov. Taarifa hii si kwamba ilikuwa mbaya kwa Rais Boris Yeltsin pekee bali pia na genge lake lote la โThe Familyโ kwa sababu ilikuwa dhahiri kwamba kama ikitokea mkomunisti Zyaganov akichukua nchi kitu cha kwanza ambacho angekifanya ni kurejesha serikalini viwanda na makampuni yote ambayo yalikuwa yamebinafsishwa na Rais Yeltsin kwa watu binafsi.Hakuna ambaye alikuwa na jawabu kichwani wa nini hasa wakifanye kunusuru kile ambacho kilikuwa kinaelekea kutokeaโฆ baadhi ya watu kwenye inner circle wakamshauri Rais Yeltsin afute uchaguzi na atawale nchi kidikteta. Lakini hili lilikuwa ni wazo la kipuuzi kabisa labda kutokana na maji kuwafika shingoni maana mfumo huu ulikuwepo Russia huko mwanzoni miongo kadhaa nyuma na ukafeli na kudondoka.
Wakati ambapo kila mtu akiwa amechanganyikiwa na kutoa mawazo yasiyo na mbele wala nyuma kuleta auheni yoyote ndipo ambapo Abramovich akaingilia kati. Akakaa mstari wa mbele na kushika usukani wa mikakati ya uchaguzi kambi ya Rais Yeltsin. Russia ilikuwa imetoka kwenye ujamaa na ubaya ni kwamba ile akili ya kijamaa bado ilikuwa haijawaisha. Kama wasemavyo, unaweza kumtoa kijana kutoka โnanjilinjiโ kuja mjini lakini kamwe huwezi kuitoa โnanjilinjiโ akilini mwa huyo kijana. Nchi ilikuwa imeingia kwenye ubepari lakini wazee bado walikuwa wanawaza na kufanya mambo yao kama wajamaa. Abramovich akataka kuwaonyesha namna ambavyo chaguzi zinafanyika kwenye nchi za kibepari.
Kwanza akamshawishi Rais Yeltsin amfute kazi meneja kampeni wake. Kisha nafasi hiyo akashauri apewe mtoto wa Rais Tatyana. Kwa nini? Kwanza kwasababu Tatyana atakuwa na uchungu zaidi na kampeni hiyo kwa kuwa โana kitu cha kupotezaโ kama wasiposhinda. Lakini pia kama ambavyo nilieleza kuwa Tatyana hakuwa binti legelege wa kula mkate kwa siagi tu, bali alikuwa ni mpambanaji haswa. Lakini tatu Abramovich alitaka Tatyana ashike wadhifa wa meneja kampeni kwa kuwa alikuwa rafiki yake na walau alikuwa kwa mbali Tatyana alikuwa ameanza kuwaza nama ambavyo yeye Abramovich anawaza. Wanasema ukikaa karibu na waridi lazima unukie.
Kisha Abramivich akafanya kitu ambacho kwa kipindi kile nchini Rusia hakikuwa kimezoeleka sana japo kwa nyakati zetu hizi twaweza kuona ni cha kawaida. Abramovich akatengeneza mkakati wa namna ya โkuchezaโ na media.
Jambo moja ambalo tunapaswa kulifahamu ni kwamba katika kipindi hiki kutokana na udhaifu mkubwa wa mbinu za uongozi za Yeltsin, uchumi wa Russia ulikuwa umeyumba sana kiasi kwamba mpaka serikali ilikuwa imechacha kweli kweli. Serikali kwa kipindi hicho ilikuwa inajiendesha kwa kutumia fedha za mkopo dola bilioni kumi ambazo serikali ilikuwa imekopeshwa kutoka IMF.
Sasa basi, vituo vya televisheni vyote ambavyo awali vilimilikiwa na serikali vilikuwa navyo vimebinafsishwa. Kwa hiyo hata serikali ikitaka kurusha matangazo walikuwa wanapaswa kulipia. Lakini serikali ilikuwa imechacha.
Abramovich akaitisha kikao maalumu na watu ambao walikuwa wamebinafsishiwa vituo vya habari nchini Russia na hata wale ambao wamejitutumua kuanzisha vya kwao wenyewe. Abramovich alikuwa na ombi moja tu kwaoโฆ waache kurusha habari yoyote kumuhusu Zyuganov, mpinzani mkuu wa Yeltsin ambaye alikuwa anaongoza kwenye kura za maoni na badala yake vyombo vyote vya habari virushe habari kuhusu kampeni za Rais Yeltsn.
Abramovich akawaeleza kwamba atafanya kila namna mpaka Rais Yeltsin ashinde kiti cha Urais na akishashinda โatawakumbukaโ wamiliki hao wa vyombo vya habari kwa hicho walichokifanya.
Hakuna mmliki yeyote wa chombo cha habari ambaye alikataa โofaโ hiyo. Hakuna ambaye hakutaka โkukumbukwaโ pindi ambapo Yeltsin akishika muhula mwingine.
Katika kundi hili la wamiliki wa vyombo vya habari ambao Abramovich alikuwa anamlenga hasa alikuwa ni swahiba wake wa zamani Berezovsky. Yule Oligarch ambaye alimtambulishaga kwa Yumachev. Berezovsky alikuwa anamiliki โmedia houseโ ambayo ndiyo ilikuwa ina ushawishi kuliko vyombo vingine vyote. Sio tu kwamba alikuwa amemlenga kwa kuwa alikuwa na media house yenye nguvu zaidi, Abramovich alikuwa na wazo lingine la siri zaidi, wazo mwanana kabisa ambalo kama likitimia basi laweza kumfanya ghafla kuwa moja ya watu matajiri zaidi nchini Russia na duniani. Nitaeleza baadaeโฆ
Kampeni ikaendeleaโฆ kufumba na kufumbua, kila televisheni, kila redio, kila gazeti kila siku kukicha kulikuwa na habari moja tu, Boris Yeltsin, Boris Yeltsin, Boris Yeltsin. Tofauti na ambavyo Yeltsin alikuwa amezoeleka kwamba sio โmtu wa watuโ lakini ghafla Yeltsin alionekana akiwa na haiba nyingine mpya kabisa. Kila siku yuko mahala fulaniโฆ leo ametembelea shule fulani ya upili Moscow, kesho yuko sokoni akisikiliza shida za wachuuzi, kesho kutwa yuko kiwanda fulani akila chakula cha mchana na wafanyakazi. Warusi walishuhudia Yeltsin mpya ambaye hawakuwahi kumuona. Yeltsin akaongeza ruzuku kwa wanafunzi, akatoa fedha nyingi kutoka serikalini mabilioni kwa ajili ya kuwalipa pensheni wazee. Na kila hatua, kila kitu haijalishi ni kikubwa au kidogo ndogo kiasi gani kiliripotiwa na kila chombo cha habari nchini Russia.
Vyombo vya habari vilimpamba kwa kila namna ambayo waliweza huku wakiwaeleza wananchi kwamba wakimchagua Zyuganov kutokana na sera zake zinaweza kuifanya Urusi kuingia kwenye vita.
Mara moja mikutano ya kampeni ya Yeltsin ikaanza kujaa watu kwa mafuriko. Yeltsin akageuka kuwa โsweetheartโ wa Warusi wote. Katika mikutano Yeltsin aliongea kama mtu muungwana tofauti na kawaida yake ya kufokafoka kama jendaheka. Aliongea kwa ustaarabu na kumwaga ahadi kedekede.
Siku ya uchaguzi ikawadia, December 5, 1996. Kura zikapigwa. Siku moja mbele matokeo yakatangazwaโฆ Boris Yeltsin alikuwa ameshinda kti cha Urais kwa kupata 52% ya kura zote zilizopigwa. Yaani kama mtu alikuwa amelala usingizi miezi mine nyuma na kuamka siku hiyo umwambie Yeltsin alikuwa amemshinda Zyuganov angeweza kukuona ni mwendawazimu.
Yaani ndani ya miezi mine tu, โadacadabraโ za mikakati ya Abramovich zilikuwa zimebadili mioyo ya warusi kumchukia Yeltsin na sasa kuwa โsweetheartโ. Ilikuwa nikitu ambacho hata Yeltsin mwenyewe hakutegemea.
Baada ya Yeltsin kuapishwa kushika muhula mwingine wa uongozi watu wa kwanza kuhakikisha wanapata โmnofuโ mnono zaidi walikuwa ni ule Utatu Mtakatifu. Tatyana, Yumachev na Abramovich. Tatyana akateuliwa na baba yake kuwa rasmi mshauri wake mkuu. Yumachev akateuliwa kuwa katibu Mku Kiongoziโฆ na Abramovichโฆ naam Abramovich akateuliwa kuwa nani? Waziri Mkuu? Hapanaโฆ Waziri wa Mambo ya Nje? Hapanaโฆ Waziri wa Ulinzi? Hapanaโฆ aliteuliwa kuwa nani?
Abramovich alikataa kupewa nafasi yoyote ile ndani ya serikali. Uwendawazimu? Noโฆ Abramovich, a born tacticianโฆ anaona kile ambacho wengine hawakioni.
Alimweleza tu Yeltsin kwamba ameshiriki namna ile katika uchaguzi na kuhakikisha anashinda kwa kuwa anampenda Yeltsin kama baba yake kabisa na anadhani ndiye mtu sahihi zaidi kuingoza Russia.
Moyo wa Yeltsin ukamomonyoka na kububujikwa kabisaโฆ hakika huu ni upendo wa kuzidi kipimo, mtu anakupigania kwa jasho na damu ushinde kiti cha Urais alafu hataki umlipe kwa kumpa cheo chochote? Yeltisn akajihisi kama amepata mtoto wa kiume ukubwaniโฆ tena mtoto mtiifu na mwenye kumpenda baba yake.
Japokuwa kipindi hiki Abramovich hakuwa tajiri kabisa hata kidogo kama tumjuavyo sasa, lakini Abramovich alikuwa anajua ni nini anakitakaโฆ hakutaka papara ya kurukia vyeo vya serikaliโฆ alijua lengo lake hasa liko wapi. Kila kitu sasa kilikuwa kiko sawa, mkakati wake umeenda vile ambavyo alikuwa amepanga. Kitu pekee alichohitaji sasa ilikuwa ni subiraโฆ naam, subiraโฆ subira ni โnecessary ingredient of geniusโ.
Akasubiri serikali iundwe. Wagawane vyeo. Walioukwaa uwaziri na ukuu wa maidara washerehekee na kupongezana, kisha aingie โkaziniโ.
Miezi kadhaa ikapitaโฆ serikali mpya ikiwa imeshaundwa na imetengemaa na inafanyakazi zake kama kawaida. Huu sasa ulikuwa ni wakati muafaka aliokuwa anausubiri.
Siku hiyo miezi ya mwanzoni kabisa mwa mwaka 1997 akampigia simu yule swahiba wake wa zamani, Bw. Berezovsky. Yule jamaa mwenye media house yenye nguvu zaidi kipindi kile nchini Urusi, ambaye pamoja na wamiliki wengine wa vyombo vya habari kipindi kile cha kampeni Abramovich aliwaomba wamsaidie Yeltsin kushinda kiti cha Urais na kuwaahidi Yeltsin atawakumbuka kwenye utawala wake.
Alipompigia simu na Berezovsky kumuuliza wanakutana kwa lengo ganiโฆ. Akamjibu jibu moja tu kwamba, โmuda wa Rais kuwakumbuka umewadia.!โ
Boris hakujua na hakuna ambaye angeweza kujua zaidi ya Abramovich mwenyewe kwamba, ndani ya wiki chache baada ya simu hiyo Abramovich alikuwa anaelekea kuwa moja ya binadamu mwenye utajiri mkubwa zaidi juu ya uso wa dunia.
Baada ya kikao hicho muhimu kati ya Berezovsky na Abramovich kufanyika na mambo ya siri kukubalianaโฆ hatimaye ukasubiriwa utekelezaji.
ITAENDELEA
Roman Abramovich – Utajili wa Damu, Risasi na Umafia Sehemu ya Pili
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;
