Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Nne
KIJASUSI

Ep 04: Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden

SIMULIZI Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden
Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi: Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden 

Sehemu ya Nne (4)

Baada ya kufanikiwa kumshawishi Dk. Shakil matangazo yakawekwa kuhusu mpango wa kutoa chanjo katika eneo hilo kwa mwezi February na Mwezi April 2011. Ili kuwapiga chenga serikali ya mji wa Abbattobbad wasihusike kwenye zoezi hilo Dk. Shakil alieleza kuwa amepata ruzuku kutoka mashirika ya kimataifa ili atoe chanjo hiyo bure na chanjo hiyo ni ya kuwakinga watoto dhidi ya Hepatitis B.

Hivyo basi alifanya zoezi lake kwa Uhuru pasipo kuingiliwa na watu wa serekali za mitaa na manesi ambao walijumuika nae kutoa chanjo hiyo walipata posho iliyoshiba.

Ili kuepuka watu kuanza kuuliza maswali na kuwa na wasiwasi, alianza kutoa chanjo hiyo katika mitaa wanayoishi masikini kama vile mitaa ya Nawa Sher. Alifanya hivyo kwa mwezi February na aliporejea tena alitoa chanjo hiyo katika mtaa wanaoishi watu matajiri katika mji wa Abbattobad yaani mtaa wa Tabil ambapo ndipo kulikuwa na hilo jumba linalotiliwa mashaka.

Ilipofika zamu ya kutoa chanjo kwa watoto waliopo ndani ya hilo jumba walikaribishwa kwa ukarimu na Dk. Shakil mwenyewe akabaki nje getini na akamruhusu nesi aliyeitwa Bakhto aingie ndani ya kasri atoe ‘chanjo’ kwa watoto.

‘Chanjo’ ikatolewa, zoezi likaisha Dk. Shakil na manesi wake wakarejea Khyber na kukabidhi sampuli walizozipata kwa CIA.

Sampuli zikasafirishwa mpaka marekani, zikafanyiwa uchambuzi wa DNA kisha ikalinganishwa na DNA ya dada yake Osama Bin Laden aliyefariki dunia mwaka 2010 jijini Boston nchini Marekani kwa uvimbe kichwani.

Baada ya sampuli hizo za DNA kupimwa na kulinganishwa, majibu yakapelekwa mezani kwa Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena. Baada ya Pattena kuyaona majibu hayo akatabasamu mpaka ufizi wa mwisho, akainua simu ya mezani na kupiga ikulu ya Marekani na kuomba kuongea na Rais Obama.

Mara baada ya kuunganishwa na Rais Obama, Pattena akampa taarifa Rais, taarifa iliyosubiriwa muda mrefu na kwa shauku kubwa, kwa kifupi akamueleza Rais kwa furaha “we got him.!” (“Tumempata.!”)

OPARESHENI NEPTUNE SPEAR

Baada ya kupatikana uhakika kuwa Osama Bin Laden anaishi ndani jumba hilo lililopo Abbottabad, CIA wakafanya kikao maalum na Jemedali Msaidizi (Vice Admiral) William H. McRaven ambaye ni kamanda wa kitengo maalum kinachosimamia oparesheni maalum zinazofanywa na majeshi yote ya marekani ( Joint Special Operations Command – JSOC) ambapo katika kikao hicho CIA walimpa taarifa wa kila wanachokifahamu kuhusu makazi hayo waliyoyagundua.

Baada ya kupewa taarifa hiyo, Admiral McRaven akapendekeza kuwa wanaweza wakatuma kikosi cha makomando kufanya uvamizi kwenye jumba hilo lakini akawa na wasiwasi inaweza kuleta mushkeli na jeshi la Pakistan ambalo lipo kilomita moja na nusu tu kutoka makazi ya siri ya Bin Laden.

Baada ya majadiliano ya kina Admiral McRaven akawaagiza maafisa kadhaa kutoka Jeshi la Wanamaji (U.S. NAVY) kitengo cha Maandalizi ya ya Mapigano/vita Maalum ( Special Warfare Development Group – DEVGRU) kwamba waweke ofisi ya muda makao makuu ya CIA Langley na washirikiano kuandaa mpango maalumu utaoenda kupendekezwa kwa Rais juu ya kushugjulikia makazi yaliyoaminika kumficha Osama Bin Laden.

Baada ya miezi miwili ambayo DEVGRU waliitumia kuaandaa mpango kwa kushirikiana na CIA hatimaye wakawasilisha mapendekezo yao kwa Mkurugenzi wa CIA Bw. Pattena na kwa waziri wa ulinzi Bw. Robert Gates.

Kisha Rais Obama akaitisha kikao maalum cha Baraza/kamati ya usalama ya Taifa ili kujadili suala hilo.

Baada ya majadiliano marefu kwenye kikao hicho ilionekana kuwa Rais Obama alipendelea zaidi pendekezo la kulipua makazi hayo kwa bomu kutoka angani. Lakini maswali yakaibuka je ni vipi kama kuna handaki kwenye jumba hilo na Osama labda huwa anakaa chini ya hilo handaki. Katika upelelezi wao wote CIA hawakuweza kung’amua kama kulikuwa na handaki katika jumba hilo ama la.

Kwa kuzingatia hivyo basi (uwepo wa handaki) kama wataamua kulipua makazi hayo kwa bomu basi itawabidi watumie bomu lenye uzito usiopungua Kg. 910 ili liweze kusambaratisha kabisa makazi hayo pamoja na handaki kama lipo.

Lakini pendekezo hili nalo likawa na changamoto zake kwani kama litatumika bomu lenye nguvu kubwa hivyo, kulikuwa na nyumba kadhaa za majirani ambazo zitakuwa ndani ya kipenyo cha mlipuko (blast radius). Pia kama makazi hayo yangelipuliwa kwa bomu kusingekuwa na ushahidi wowote wa kujiridhisha kuwa Osama ameuawa kwenye shambulio hilo.

Baada ya kubainishwa kwa changamoto hizi katika kikao kilichofuata cha kamati ya Usalama wa Taifa, Obama akasitisha mpango huo wa kulipua makazi kwa bomu usitekelezwe.

Chaguo la pili lilikuwa kwa makomando wa kikosi cha Wanamaji (Navy) SEALs, wavamie makazi hayo kwa kutumia helikopta maalum zinazoruka bila kutoa kelele na sio rahisi kuonekana na Rada ya adui. Chaguo hili lilikuwa ni zuri lakini lilikuwa na changamoto moja kubwa. Kumbuka makazi haya yapo karibu kabisa na kituo cha Kijeshi cha Pakistani, itakuwaje kama wakishtukiwa kabla hawajamaliza kutekeleza oparesheni?

Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye kikao akiwemo waziri wa ulinzi Bwa. Robert Gates akapendekeza kuwa labda wawashirikishe watu wa kitengo maalumu cha ushushushu cha Pakistan (ISI). Wazo hili likapingwa vikali na Rais Obama kuwa hawaamini hata chembe Wapakistani na endapo wakiwaeleza kuhusu oparesheni hiyo basi siku hiyo hiyo Osama ataamishiwa sehemu nyingine.

Obama akapendekeza kuwa kama ikitokea makomando wao wamekamatwa kabla hawajamaliza oparesheni yao basi Admiral McRaven atatakiwa ajiandae kumpigia simu Mkuu wa Majeshi Pakistani Ashfaq Parvez Kayani kumshawishi kuwaachia makomando hao wa Marekani.

Lakini pia Obama akamuagiza Admiral McRaven awaandae makomando wake kwa mapambano ya kijeshi kama ikitokea wamepewa upinzani na wanajeshi wa Pakistan na hawataki kuwaruhusu waondoke.

Watu wote waliohudhuria kiako hicho cha kamati ya usalama wakakubaliana na mpango huo wa kuvamia makazi ya Bin Laden kwa kutumia helikopta isipokuwa Makamu wa Rais Joe Biden pekee aliupinga mpanga huo kwa asilimia zote.

Licha ya Makamu wa Rais kuupinga mpango huo, siku ya tarehe 19 April kamati ya Usalama wa Taifa ilipokutana tena Rais Obama akatoa idhini ya awali kukubali oparesheni hiyo itekelezwe. Na ikapewa jina Oparesheni Neptune Spear.

Kesho yake McRaven pamoja na kikosi chake cha SEALs wakaondoka marekani kuelekea Afghanistan ambapo walitumia takribani wiki mbili kufanya mazoezi kuhusu oparesheni waliyoenda kuifanya.

Kikosi hiki kilifikia katika kambi ya Bagram nchini Afghanistan na hapo palitengenezwa mfano wa nyumba kama ile inayosadikiwa kumuhifadhi bin laden na kikosi cha SEALs wakafanya wazoezi ya kutosha jinsi watakavyotekeleza zoezi hilo.

Ilipowadia siku ya tarehe 29, Rais Obama alimpigia simu Kamanda McRaven kumuuliza juu ya maendeleo ya maandalizi. Pia akamuuliza kama alikuwa na angalau ya chembe ya shaka kuhusu kufanikiwa kwa oparesheni hiyo na kama alikuwa na shaka yoyote basi oparesheni hiyo itahairishwa. McRaven akamjibu kuwa vijana wake wako tayari kwa kutekeleza Oparesheni.

Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Tano

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment