SIMULIZI Shilingi Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA
********************************************************************************
Simulizi : Shilingi (Mwanzo Kati Na Mwisho)
Sehemu Ya Pili (2)
Nyuma hairudi mbele haiendi, dereva anakita manjonjo yake anakata kushoto, anarudi nyuma kidogo anakata kulia.
Wapi!! Hakuna kitu.
Ikazima, katikati ya lile bwawa dogo.
Wanamuonea aibu daktari, wanavifunga vinywa vyao lakini mioyo inashusha matusi mazitomazito.
Mwenyeji anatoa ushauri kuwa hapo inabidi watumie baiskeli kuimalizia safari ile.
“Upuuzi, nani apande baiskeli? Ni heri tusiende kabisa!” Anafoka mkuu wa wilaya ghafla.
Yupo hivyo, hafikirii kabla ya kuzungumza, sahau kuhusu kutenda.
“Sawa, dereva endesha gari tuondoke kurejea mjini” Daktari anamdhihaki mkuu wa wilaya.
“Kwani hakuna hata pikipiki za ofisi ya kijiji?” mkuu wa wilaya anaulizia. Wanatazamana, hakuna mwenye jeuri ya kumjibu, ni daktari tu nd’o anaweza kusema lolote.
“Mliwagawia?” anamuuliza kwa utulivu.
“Ilikuwa sera ya chama chetu katika uchaguzi, kila kijiji lazima kiwe na pikipiki walau moja kwa masuala ya dharula kama mama mjamzito, wagonjwa na ugeni kama huu wa mkuu wa wilaya. Hata katika ilani ya chama imeandikwa hivyo.” Akajieleza.
“Hiyo sera ilifanyiwa utekelezaji?”
Mkuu wa wilaya kimya!
“Hizo baiskeli tunazipata wapi? Lazima tufike Ulongoni leo hii..” Daktari akauliza.
“Tuzisubiri, huu nd’o muda wa bwana Ali kutoka kuangua embe shambani kwake, hawapishani sana na mzee Yusto, mida hii huwa anatoka kulangua bidhaa huko sokoni” Mwenyeji akajibu.
“Unavyosema mida hii, mida hii saa ngapi sasa na hata hauna saa.” Mkuu wa wilaya akauliza kwa dharau.
“Hatuhitaji saa katika kijiji chetu, wanaojua kuisoma ni wachache sana, jua linatutosha kutambua nyakati kiusahihi.” Mwenyeji akajibu.
“Mfano kwa hiyo teknolojia yenu, sasa hivi ni saa ngapi?” Daktari akamtupia swali yule mwenyeji, katika namna ileile ya dhihaka huku analazimisha cheko.
“Saa kumi na nusu!” akajibu upesi.
Daktari, mkuu wa wilaya na wengine waliokuwa na saa wakaziinamia saa zao. Kisha kwa pamoja wakamtazama yule mwenyeji.
Ilikuwa saa kumi na dakika ishirini na tano!
“Unaitwa nani aisee!” Daktari akauliza kwa utulivu.
“Naitwa Dingo!” akajibu asijali kuhusu mshangao wao. Njia nzima hakutaka kujua jina lake, sasa anajikuta anamuuliza.
Kwanza hakujua walichokuwa wanastaajabu.
Ikaanza kupita baiskeli ya mzee Yusto.
Mwenyeji yule akamsimamisha na kumweleza shida yao, hakutaja cheo cha mtu yeyote. Alielezea tu kama shida iliyowasibu. Wanatakiwa kufika Ulongoni
Wakati anazungumza haya, mzee Yusto macho yake yanalishangaa gari lile lililotwama katika maji yale. Akili yote ipo kule, gari lile lilikuwa zuri sana kiasi kwamba angeweza kulitazama tena na tena.
“Umeelewa mzee Yusto!” Dingo akamuuliza, baada ya kumaliza kujieleza.
“Nimeelewa eeeh! Nimeelewa bwana.” akajibu ghafla, asijue alichokuwa anasimuliwa.
“Utampatia aendeshe ama utamuendesha wewe?” Dingo akamuuliza.
“Kumpatia nani nini? Na kumuendesha nani?” Timamu zimemkaa anauliza sasa kwa wahka.
“Mwambie mimi ni mkuu wa wilaya.” Bwana mkubwa akabwata kwa sauti yenye mamlaka.
“Huyu ni mkuu wa wilaya anahitaji kufika Ulongoni kwa bwana Kindo. Gari kama unavyoona limepata shida, anahitaji huduma ya baiskeli yako.” Dingo akamueleza Mzee Yusto.
“Mkuu wa wilaya gani?” Mzee Yusto akahoji, bado ameikamata vilivyo basikeli yake kana kwamba kuna watu wanamlangua ili wamwibie. Na sasa amewashtukia janja yao.
Dingo akajishika kiuno, hajui afanye nini. Walinzi wa mkuu wa wilaya wakaona jinsi zoezi linavyokuwa gumu. Wakamsogelea kwa pamoja mzee Yusto.
Mzee akaziona dalili za kuibiwa mali yake. Akaikanyaga pedeli aweze kuwachomoka.
Akafanikiwa, lakini hakufika mbali.
“Mamaweee mgongo wanguu!” akapiga kelele, akaiachia baiskeli akaanguka kando.
Walinzi wale wakaifikia na kuiokota baiskeli.
“Mheshimiwa utaendesha ama…!” wakamuuliza mkuu wa wilaya.
“Kusema kweli sijui kuendesha baiskeli!” Mkuu wa wilaya akawahi kujibu. Tahayuri ikimtwaa.
Mlinzi mmoja akajipendekeza kumuendesha.
Bwana Ali naye akafika baada ya dakika zipatazo kumi na tano tangu Mzee Yusto ajeruhiwe kwa kirungu kilichorushwa kitaalamu na mmoja wa walinzi wa mkuu wa wilaya.
Mzee Yusto akapewa jukumu la kumwelewesha bwana Ali nini kinahitajika.
Ni ndani ya dakika moja tu tayari bwana Ali alikuwa ameiacha baiskeli yake huku anatetemeka.
Haijulikani mzee Yusto alimweleza kitu gani.
Mlinzi wa pili wa mkuu wa wilaya akaitwaa, daktari pasi na kuelezwa lolote akajiongeza. Akakwea katika baiskeli.
Wanajiandaa kuondoka!
“Nani atawafikisha nyumbani kwa Kindo?” Dingo akawauliza alivyoona wameridhika na wapo tayari kwa safari.
Walinzi wakapigwa butwaa, hawakuamini kuwa walikuwa tayari kuzinyonga pedeli kuelekea mahali wasipopajua.
“Itabidi wewe uje uniendeshe mimi!” Mkuu wa wilaya akamuamuru Dingo aliyekuwa mwenyeji wao.
“Sijawahi kuendesha baiskeli huku nikiwa nimepakia mtu.” Dingo akajitetea.
“Mtu wa ajabu kabisa wewe, kwanini sasa ujihesabie kuwa unaweza kuendesha baiskeli?” mkuu wa wilaya ile akafoka, akijisahau kuwa yeye hawezi kabisa kuendesha baiskeli.
Dingo akatabasamu.
“Unanicheka sio?” Mkuu wa wilaya akauliza huku akiwa katika taharuki.
“Nani? Mimi?” akauliza huku akiangaza huku na kule. Mkuu wa wilaya akamtazama kwa macho makali, anatamani kusema lolote lakini anahisi haitafaa kitu.
“Wewe mzee unapajua nyumbani kwa huyo Kindo?” swali likatupwa kwa mzee Yusto.
“Siwezi kuendesha baiskeli, mgongo umejeruhiwa!” Akajibu asiloulizwa, lakini bado uelekeo ni ulikuwa uleule.
Bwana Ali akaangushiwa mzigo wa kunyonga baiskeli aliyopanda mkuu wa wilaya. Mlinzi akashuka na hapa akatakiwa kuuongoza mchakamchaka wa wengine wote kuwafuata kwa nyuma.
Mzee Yusto kwa kuwa anaipenda baiskeli yake naye akalazimika kukimbia mchakamchaka.
Wanaimbishwa nyimbo mpya za ajabu. Wamechoka sana lakini wanatakiwa waendelee kuimba.
Wakati jua linamalizia mkia wake katika kuikimbia dunia, wakawasili nyumbani kwa Kindo.
Wote wamechoka!
Kindo na mkewe walikuwa wameuzunguka moto kwa ajili ya joto. Mtoto akiwa ndani amelala. Majirani hawakuwa tayari kulala. Hakuna aliyehitaji kusimuliwa, eti Kindo aliondoka na sasa ni tajiri mkubwa huko mjini.
Kila mmoja alihitaji kushuhudia, hivyo na wao wakajikokea viginga vya moto na kuvizunguka.
Ili watu wakusikilize unapaswa kuzungumza juu ya tukio la Kindo mwenye bahati.
Ulitakiwa kusema lolote juu ya shilingi ya ajabu!
Kinyume na hapo, baki katika ukimya. Wasikilize wenye jambo la kusema.
Wanatamani walau kuijua mikakati ya Kindo, lakini mara zote Kindo ni mkimya, anazungumza na mkewe na kucheza na mtoto wake. Ni kama hakuna kilichotokea.
“Ningekuwa mimi nisingeweza hata kukaa katika kiti.” Mwanakijiji akazungumza huku wakiibia kumtazama Kindo.
Maongezi yakanoga kisha yakapooza, hapakuwa na mpango wowote ulioendelea tangu mtumishi amtembelee Kindo.
“Mbona watu kutoka mjini hawafiki kuishangaa shingi ya ajabu?” Mmoja akauliza.
“Nani hasa amewaambia kuwa imepatikana? Kindo anapaswa kusimama na kwenda mjini awaeleze na watainunua.” Akajibiwa na mzee wa makamo.
Wakiwa bado katika vikundivikundi, unafika ugeni. Baskeli mbili zinafuatana kulifikia eneo alilokuwa anaishi.
Bwana Ali! Wanakijiji wakamtambua.
Kabla hawajaa sawa sana wanazisikia nyimbo kwa mbali, waliochutama wakasimama, waliosimama wakazinyanyua shingo zao juu.
Sauti zinazidi kujongea, wale wageni katika baiskeli wametulia pembeni ya zile baiskeli. Sauti za wanaoimba zinazidi kusogea.
“Aliselema hadija, aliselema hadija
Mchakamchaka chinjaaa, mchakamchaka chinjaaa!”
Wakawasili.
Mzee Yusto! Wakamtambua.
Dingo! Naye akatambulika.
Hawa wengine ni akina nani?
Jasho linawatoka, nyuso zinautangaza uchovu. Ni kama mateka waliokuwa wanakimbia kwa amri ya mtutu.
Ni akina nani hawa! Kindo alijiuliza.
Sura zilikuwa ngeni kabisa, licha ya kwamba mavazi yao yalikuwa yametingwa na vumbi zito la Ulongoni, bado walionekana nadhifu kulikoni wanakijiji wengine wa pale.
Ugeni ule ulipotimia, mkuu wa wilaya akamsogelea bwana Ali, kisha akamuita na mzee Yusto.
“Nawashukuru sana kwa moyo wenu wa ukarimu. Mmetufaa sana kwa usafiri huu hadi kutufikisha hapa.” Akaangaza huku na kule, akanyanyua mkono wake kuomba kitu. Ukaletwa mfuko wa plastiki.
Akapekua na kutoka na noti kadhaa.
“Hizi shilingi elfu sita, mtagawana. Zitawafaa katika matengenezo ya baiskeli zenu na chakula kwa familia zenu!” akazungumza huku akimkabidhi bwana Ali zile pesa.
Mzee Yusto akachangamka, uchovu ukatoweka. Bega kwa bega na bwana Ali. Hawaamini wanachokiona.
Wananchi wa Ulongoni hawaamini walichokisikia, shilingi elfu sita kwa ajili ya asante?
Haijawahi kutokea!
Huyu ni nani? Likawa swali.
Wengi wakajiwekea matazamio kuwa ule ujio wa wanunuzi wa shilingi ya ajabu ulikuwa umeanza kuwasili.
Kindo akiwa mwenyeji wa eneo lile, akasogea karibu kuwakirimu wageni wake.
“Naitwa Matayo Masindeke! Naamini umewahi kulisikia jina hili ndugu yangu.” Akajitambulisha. Kindo akajaribu kuvuta kumbukumbu ni wapi amewahi kulisikia jina lile.
“Hapana! Huenda nimesahau.” Akajibu kwa utulivu, pembeni yake amesimama Nyangeta mkewe. Hamuachi mbali mumewe.
“Mimi ni mkuu wa wilaya nzima ya Hekaya, kata, tarafa, mitaa na vijiji kikiwemo hiki cha Ulongoni unachoishi wewe. Vyote vipo chini yangu.” Akatamba Matayo.
“Shkamoo!” Nyangeta akasalimia kwa hofu, hakujua ni heshima gani zaidi anaweza kuitoa kwa kiongozi yule zaidi ya salamu ile.
“Ujio wangu katika kijiji hiki ni baada ya bwana huyu… (anamgusa daktari bingwa wa mkoa) huyu ni daktari wa mkoa mzima. Yeye amezipokea taarifa za ugonjwa wa mama yako kutokea mbali kabisa. Akanisisitiza, na kwa upendo nilionao kwa wananchi wangu nikasema sibaki nyuma, naongozana na daktari nijionee” Matayo akaendelea kuzungumza kwa sauti ya juu ambayo iliwafikia watu wengi. Ni kama aliyekuwa anahutubia.
“Safari hii imesababisha niyajue mengi, kijiji hiki kinahitaji umeme, barabara za kisasa na hospitali kubwa kabisa.” Anaendelea kutawala maongezi.
Tofauti na ziara zake mjini ambapo kila akiongea watu hupiga makofi, huku ilikuwa tofauti.
Wanamtazama, hawaelewi wafanye nini, hawajui umuhimu wa barabara nzuri, hawajawahi kuziona, daktari wa kijiji mwenye maringo aliwatosha hivyohivyo, umeme ulikuwa msamiati mpya kabisa.
Wafanye nini zaidi ya kumshangaa bwana yule na kisha kumuonea wivu kwa nguo alizovaa. Huku wakiendelee kuzionea donge shilingi elfu sita walizopokea wanakijiji wenzao.
Nguo zilikuwa zimekunywa vumbi lakini bado alikuwa nadhifu kuliko wale wanakijiji.
Walinzi kwa mara ya kwanza walijikuta hawana kazi kubwa ya kufanya, katika ziara nyingine mkuu wa mkoa huzongwa ongwa na watu hata ashindwe kufanya lililomleta kwa uzuri.
Ulongoni alikuwa anaogopwa! Hakuna anayetaka kumkaribia. Watu wanasukumana kurudi nyuma ili wasimkaribie bwana yule.
Baada ya kuzungumza kwa kina, akamruhusu daktari akamtazame mama yake Kindo aliyekuwa amelala ndani.
Wakatumia mwanga wa kurunzi kubwa kumulikia.
Daktari akaingia na wasaidizi wake. Muda huo mkuu wa wilaya akautumia kupata faragha kati yake na Kindo pamoja na mkewe.
Matayo Masindeke akiwa na kurunzi ndogo imebanwa katika pachipachi ya kwapa lake alichukua mkoba wake, akatoa kitabu kidogo.
“Kindo umewahi kumsikia Carl Peters ama John Speke? Ama umesikia jambo lolote kuhusu Dokta Livingstone?” akaanzisha jambo.
“Huyu aliyeingia humu ndani nd’o dokta lisitoni?” Akauliza kwa utulivu Kindo.
Matayo akatokwa na cheko jepesi.
“Hapana hawa ni watu wa zamani sana. Nilihitaji uwafahamu niweze kukusimulia jambo”
“Siwafahamu! Yawezekana nilikutana nao hapo kabla bila kujua..” Kindo mtulivu, akajibu. Mkuu wa wilaya akajikaza asitokwe na cheko kubwa.
“Unamfahamu mtu gani wa zamani? Kwa majina”
“Nyerere, Karume na Mkwawa,” akajibu, mkewe akajazilizia, “Kuna mwingine Kinjekitile Ngwale na Sokoine”
Matayo Masindeke akatabasamu.
“Enzi za watu hao palikuwa na watu wengine ambao walikuwa wanawalaghai mababu zetu katika masuala ya mikataba, waliwasainisha mikataba mibovu kama boers treaty ambao nd’o ulifanywa na huyo bwana niliyekutajia kwa majina ya Carl Peters.” Akaweka pumziko kidogo, anawatazama mmoja baada ya mwingine.
Wanasikia lakini hawaelewi!
Akakifunika kitabu chake.
“Sikia Kindo, habari ya sarafu yako imepepea kila mahali. Imewafikia hadi akina Carl Peters wa kizazi hiki. Mimi nilipoelezwa awali niliipuuzia kwa sababu sikujua anayemiliki sarafu ya ajabu kama ni mwananchi wa wilaya yangu. Niliposikia kuwa ni mkazi wa Ulongoni, nilishtuka. Maana mama yangu mzazi aaah! Bibi yangu kizaa mama yangu aliishi sana hapa Ulongoni, alifanya kilimo hapa na hata mauti yalimkutia hapahapa. Nikaacha shughuli zangu nikasema acha nikaonane na mwananchi wangu tuzungumze,” akaweka pumziko tena.
“Hiyo sarafu ni ya aina gani, maana mimi niliisoma tu katika vitabu shuleni.”
Kindo akaitoa ile sarafu na kumpatia mkuu wa wilaya.
Mikono inamtetemeka Matayo. Anaitazama mara mbilimbili.
“Ni nzito sana!” nd’o anachoweza kusema kwa wakati huo.
“Sasa watakufuata watu na kukutajia mambo mazuri mazuri ili waipate sarafu hii. Nikiwa kama mkuu wa wilaya nakushauri usiwasikilize, ama wasikilize lakini usidiriki hata kuwaonyesha wapi sarafu ilipo. Sio kila mtu ni mwema, kuna baadhi wakiiona hawatakubali kuondoka hivihivi, watakurubuni uongozane nao wakudhulumu njiani na hata kukudhuru wewe mwenyewe. Sio kila mtu ni mwema, mimi nazungumza haya kwa kofia mbili, kwanza kama mkuu wa wilaya hii na pia kama kijana mwenzako. Kuwa makini…..” akaweka kituo.
Akabaki kungoja Kindo ayaboreshe maongezi.
“Asante sana mkuu, tumeelewa na tutazingatia.” Nyangeta kajibu.
Mkuu wa wilaya akaona kama karata yake haijazaa matunda, kusikilizwa na kueleweka pekee haikuwa lengo lake. Alihitaji wacheze ngoma atakayoamua kuipiga yeye.
Hawakucheza!
£MKUU WA WILAYA kwa mara ya kwanza kabisa katika kijiji cha Ulongoni….. sababu kuu ukiwa mvumo wa shilingi ya ajabu. Je? Nini kitajiri, ugeni huu utakuwa wa manufaa kwa nani? Kindo na mkewe ama Daktari na mkuu wa wilaya.
Mkuu wa wilaya hakuwa na jingine la kufanya. Alimuacha Kindo na Nyangeta waende kumtazama mama ambaye tayari alikuwa amepatiwa tiba ya awali na daktari bingwa wa mkoa.
Maajabu!
Mama alikuwa anaweza kutabasamu vyema kabisa, na mirija ilikuwa ikidondosha vimiminika kuelekea katika sindano iliyojikita katika mkono wake.
“Mama ni mzima kwa sasa na ataishi miaka mingi!” Daktari yule mfupi mwenye mwili unaopambana usizae kitambi alizungumza.
Kindo akaitazama nuru iliyokuwa inang’ara katika wajihi wa mama yake.
“Asante sana daktari!” Nyangeta akamshukuru huku anajisogeza na kumgusa mama yake Kindo.
Mama mkwe!
Wakiwa wanamtazama mama, daktari alijisogeza hatua kadhaa akachungulia huku na kule.
Kiza!
“Mmemuacha wapi Matayo!?” Aliuliza kwa sauti ya chini.
“Matayo ni nani?” Kindo akahoji kwa mshangao.
“Mkuu wa wilaya!… yule niliyeongozana naye.” Daktari akajibu.
“Amebaki chini ya mkuyu!” Nyangeta akajibu. Daktari anavitua baadhi ya vifaa vyake, kisha anaanza kuzngumza.
“Sikia Kindo, nakuomba uniamini. Na uniamini kweli….” Daktari akaanza kuzungumza, anaidhibiti sauti yake isipae mbali. Anajikohoza kidogo.
Kindo anamtazama huku akiwa ameweka umakini, anaamini daktari anahitaji kuzungumza juu ya afya ya mama yake.
“Tunaweza kuzungumza tukiwa wawili?” Daktari akauliza huku akiwa anaifinyafinya mikono yake.
“Mke wangu anajua kila kitu kuhusu huyu mama, sema lolote mbele yake bila tatizo. Yaani huenda anamjua kuliko mimi”
“Sio kuhusu mama.”
“Nyangeta nenda ukamtazame mtoto, kuna mbu huko kamwangalie.” Kindo akamtoa mke wake nje.
Bila kupoteza muda daktari akamkaribia Kindo baada ya Nyangeta kuwaachia nafasi.
“Sikiliza mdogo wangu, katika maisha yako yote. Kama mtu hajawahi kukueleza bayana basi sasa nisikilize mimi nakusihi, usije ukakaa kuwasikiliza na kuwaamini wanasiasa.” Akaweka kituo, akamshika bega kisha akaendelea, “Matayo kama hajaongea na wewe…”
“Tayari tumezungumza…” Kindo akadakia
“Usijeukaamini hayo anayokueleza, huyo ni mwanasiasa, wamekuwa waongo kiasi kwamba uongo umekuwa mojawapo ya maisha yao. Kati ya masuala aliyokueleza basi asilimia tisini ni uongo, hayatekelezeki.” Akatulia, akamsogelea karibu zaidi, sasa akawa anamtisha Kindo kwa jinsi alivyokuwa anahema juu juu. Daktari alikuwa katika mchanganyiko mkubwa wa hofu na haraka.
“Unaweza kujiuliza ni kwanini unatakiwa kuniamini. Sawa, ipo hivi, mimi ninaachiwa wagonjwa mahututi katika chumba ambacho ni mimi ninayekuwa na maamuzi ya mgonjwa aishi ama uwe mwisho wa maisha yake. Tazama nimeachwa na mama yako katika hiki chumba nikiwa peke yangu, sindano moja tu ingetosha kuleta msiba katika kaya yako, na hata hiyo sarafu yako ya ajabu isingekuwa na maana tena si ndio?” Akamuuliza.
Kindo akakubali kwa kutikisa kichwa.
“Sisi tumefunzwa tukafunzika, daktari ni mtu muaminifu, akisema moja anamaanisha moja, achana na wanasiasa, akisema moja atasema alimaanisha mbili na atajitetea huku akicheka. Huo uzushi wao wanauita propaganda.” Akatulia, anajaribu kupambana na hofu yake, lakini ule mwili hauwezi kuficha namna yake ya kupumua.
“Unamaanisha nini kwa haya yote daktari.”
“Sarafu yako ni yako, una haki ya kuifanyia jambo lolote hata ukiamua kuitosa baharini hakuna atakayekulaumu ilimradi ulifanya hayo bila shinikizo lolote. Lakini akitokea mtu akakulaghai na mwisho ukampatia ile sarafu akatoweka, hakika itakuumiza kwa kipindi kirefu mno cha maisha yako. Mimi nimeamua kusimama na wewe, sikujui vyema nawe haunijui lakini kuniacha niirejeshe afya ya mama yako naomba iwe namna ya kujuana kwetu. Kwa namna yoyote ile usimruhusu mkuu wa wilaya akaondoka na sarafu yako. Mimi nitarejea hapa kijijini baada ya siku kadhaa nitakuelekeza nini cha kufanya…. ondoka humu sasa na usimweleze mtu yeyote juu ya mazungumzo haya.”
Kindo akatoweka na kuelekea alipokuwa mke wake. Akamkuta yu pamoja na mdogo wake wa kike, hajui amekuja wakati gani.
“Sh’kamoo shemeji!” Binti yule akamsalimia Kindo.
Ajabu! Hii inakuwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu kupokea salamu ya uzito ule kutoka kwa binti yule. Binti kisilani asiyekuwa na nidhamu, asiyeisha kumlaumu dada yake kila kukicha kuwa amejichanganya kukubali kuwa mke wa Kindo.
Si ndoto, huyu hapa anapiga goti na kusema ‘sh’kamoo’
Kindo hana hiyana wala haifadhi makandokando katika moyo wake. Anampokea
“Mar.. marhaba… mbona usiku? Kuna tatizo nyumbani” akamtunuku swali la ghafla. Swali ambalo asingeweza kuliuliza katika siku za nyuma, maana mtoto yule ambaye nd’o kwanza ana mwaka mmoja tangu aanze vita ya kukabiliana na damu za ajabu zinazofanya ugeni kila mwezi mwilini mwake, asingechelewa kumuuliza ‘Kama lipo tatizo unaweza kulitatua aua unauliza tu kupanua ukubwa wa mdomo’.
Leo ni mpole kupindukia.
“Nimekwishaongea na dada. Atakueleza kila kitu….. sasa dada mimi narejea nyumbani ishakuwa usiku sana.” Akaaga huku anawapa mgongo.
Akatoweka.
“Kwema?” Kindo akahoji huku anaketi vyema.
“Kwema, sijui huko ulipokuwa wewe?” Nyangeta akamuuliza.
“Ni kwema pia, Dokta ana jambo!” Kindo akalipuuza suala la daktari kumsihi asimueleze mtu yeyote kuhusu mazungumzo yale.
Nyangeta hakuwa ‘mtu yeyote’ kwake. Alikuwa zaidi ya mtu, zaidi ya ndugu wa damu.
Akamsimulia kwa hatua kila ambacho alikikumbuka kuambiwa na daktari.
“Walikuwa wapi kututembelea katika kijiji chetu na kutoa semina hizo, mara ya mwisho sijui mwaka gani ule walipotuletea vyandarua, wakatufundisha kwa kutukaripia. Leo hii wema wao upo wapi Kindo.” Nyangeta akajenga hoja juu ya madaktari.
“Kwa hiyo tufanye nini, maana kwa namna yoyote lazima hii shilingi iuzwe na hapo ndipo maisha yetu yatabadilika. Tukiendelea kuishi nayo humu ndani itaanza kuwa mzigo unaohatarisha maisha yetu.”
“Mama anakuita nyumbani!” Nyangeta akamweleza Kindo, mada kuhusu daktari ikaishia hapo.
“Usiku huu?” akatahamaki.
“Nami niliuliza mara mbili hadi tatu, ndio anahitaji uende usiku huu.” Nyangeta akajibu.
“Sawa, sikiliza mke wangu sitatembea na hii sarafu, naomba uibane katika pindo la nguo yako. Sitamweleza mtu nawe asilani usimweleze mtu.” Mwisho wa maelezo yale, tayari shilingi ya ajabu ilikuwa katika himaya ya Nyangeta.
Kindo hana nguo za maana, aliyoivaa siku tatu mfululizo ni bora kuishinda ile ambayo ana mwezi mzima hajaitia mwilini. Nguo imejikunjakunja mfanowe ilitafunwa na ng’ombe alipogundua haina ladha akaitapika.
Nd’o mararumararu yanayomstiri Kindo.
“Nikiiuza shilingi hiyo lazima niwe na nguo maalumu za kuendea ukweni,” Akajisemea wakati akiyatia malapa yake miguuni. “nguo ambazo ukiingia ukweni wazazi hawajutii uelekeo aliouchagua binti yao”
Akaondoka!
Wanakijiji waliogoma kulala wakampokea Kindo kwa macho ya hofu. Walikuwa wanamtetemekea tayari. Kindo alipopiga hatua kadhaa akaitwa.
“Wapi tena usiku huu bwana?” lilikuwa swali kutoka kwa mlinzi wa mkuu wa wilaya.
“Wewe ni nani haswa!?” akahoji. Haikuwa kawaida kabisa mtu kuweza kumuuliza mwanakijiji anaelekea wapi bila kujalisha muda.
“Nimepewa agizo na mkuu wa wilaya, nitazame usalama wako utokapo nje ya himaya yako.” Yule bwana akajieleza kwa utulivu na heshima kubwa.
“Amekuagiza unizuie nisitoke nyumbani kwangu?” Akaboresha maelezo ili aweze kueleweshwa.
“Hapana!”
“Ila”
“Nikutazame tu”
“Umenitazama tayari, ninaenda ninapoenda.” Akajibu kwa jazba. Kisha akaanza kuondoka.
Mlinzi yule akabaki kumtazama jinsi anavyoondoka upesiupesi.
Wanakijiji waliyoyasikia mazungumzo yale, wakatambua kuwa sauti ya Kindo imeanza kubadilika. Tayari alikuwa anaanza kuzungumza sauti yenye mamlaka.
Kindo anawafokea watu kutoka mjini!
__________
Maisha yalikuwa yaleyale, uzio wa miti iliyopandwa miaka mingi iliyopita nd’o iliileta tofauti. Lakini ndani palinuka shida za kila aina.
Watoto wadogo walitembea huku vidali na matako yakiwa wazi, walikuwa wamepauka. Hawakuzimudu gharama za kufanya tohara hivyo watoto wa kiume umri wa miaka sita hadi nane bado walikuwa wakiishi pasi na kuutambua msamiati wa tohara.
Kubwa linalokera, hadi umri huo bado hawakutambua thamani na ustaarabu wa kuzificha tupu zao.
Mlango mkuu wa kuingilia ulikuwa wa kubandua na kubandika, bawaba zililala popote zilipolala zamani hizo.
Mlango ukanyanyuliwa akakaribishwa.
“Ohooo! Muhesimiwa, karibu sana.” Kindo anajionea maajabu, ameyaona meno ya juu na ya chini ya baba mkwe. Mzee yule alikuwa amezungumza kwa furaha kubwa sana.
“Shkamoo baba…” Kindo akamjulia hali.
“Marahaba, hii meza ilikuwa inakungoja weye, hapa tulikuwa tunachungulia kila mara, Debora akatuhakikishia kuwa utakuja. Maana huyu shemeji yako naye ana mambo kwelikweli.” Uchangamfu wa baba mkwe haupimiki.
Kindo akajisogezea kiti akatulia mezani.
Mabakuli chakavu yaliyotengenezwa kwa kutumia mfupa wa bondo yakafunuliwa.
Mate yakaruka katika kinywa cha Kindo.
Kuku mwenye afya alikuwa amesitishiwa maisha yake, na sasa anang’ara katika bakuli kubwa la bondo. harushi mateke wala hadonoi, amejilaza tuli katika dimbwi linalovutia.
Hakuna nyanya, hakuna kitunguu, hakuna mafuta.
Mafuta ya nini wakati kuku alisitishiwa mkataba wa kuishi akiwa na mafuta yake.
Chukuchuku!
ITAENDELEA
SIMULIZi Shilingi Sehemu ya Tatu
Other related tracks from Simulizi;