SIMULIZI

Ep 01: Geza Anasakwa Auwawe

SIMULIZI Geza Anasakwa Auwawe - Ep 01
SIMULIZI Geza Anasakwa Auwawe – Ep 01

Mwandisi: George Iron Mosenya
RIWAYA: GEZA (anasakwa auwawe):
Imeandikwa Mwaka: 2015
DODOMA, Tanzania
SEHEMU YA KWANZA

Joto la uchaguzi mkuu lilikuwa limepamba moto, vyama vya siasa vikiwa katika hekaheka za kusimamisha wagombea makini katika ngazi tofautitofauti ili waweze kupambana baadaye katika uchaguzi mkuu na kuwatoa kimasomaso katika ngazi za udiwani, ubunge na ngazi ya juu kabisa ya uraisi.

Wapinzani wakisema hivi, watawala wanajibu vile… wananchi nao wanatafsiri kivyao, huku wakipima uzito wa hoja za wagombea lakini mikono yao haikuacha kupokea rushwa kutoka kila upande!Nani asiyetaka vitamu vya bure!

Wakati haya yanaendelea, palikuwa na habari ambazo zilikuwa hazijapewa uzito kabisa, kwa sababu tu hazikutokea katika jiji la Dar es salaam, Mwanza ama mji mkuu Dodoma.

Ilikuwa ni habari kutoka katika vijiji vya Nyarukongo wilayani Mugumu Serengeti.
Nani atajali!
Mwisho wa dunia huko!
Hakuna aliyejali, kila mmoja kwa nafasi yake alikuwa ametingwa na joto la uchaguzi, mashuka mengi yalishirikiana na vitanda katika upweke wa kukosa kulaliwa.
Nani alale?
Ukilala wewe wenzako wanakula rushwa.
Mjini Dodoma, shangwe zilikuwa kubwa sana siku hii. Mgombea udiwani kutoka chama tawala alikuwa anatarajiwa kufanya mkutano wa kampeni jirani kabisa na uwanja ambao mpinzani wake pia atakuwa na mkutano.
Hivyo ilikuwa ni kama mechi baina ya Yanga na Simba katika mpira wa miguu, wananchi walivaa sare za vyama huku wakipigana vijembe vya hapa na pale.
Jambo jema ni kwamba hakuna aliyerusha ngumi wala kuvunja amani japokuwa vile vijembe vingine vilikuwa vinakera sana. Ukikosa tunu ya uvumilivu waweza kutupa konde.
Hatimaye ikatimu saa kumi alasiri, kimya kila upande. Si upinzani uliojinadi kuwa utajaza watu wengi wala wale wa chama tawala waliojihakikishia kuwa inyeshe mvua liwake jua. Ushindi ni jadi yao.
Mshehereshaji akiwa anarejea maneno yake mara kwa mara kuwa mgombea anafika muda wowote ule na hapohapo mkutano utaanza rasmi.
Haikuwa!
Vikundi vilivyopangwa kutumbuiza, vilikuwa vimemalizika na sasa vilikuwa vinajirudia.
Wananchi wakaanza kunong’ona kuwa yawezekana kuna masuala ya ushirikina kila mgombea amepewa masharti na mtaalamu wake kuwa asifike mkutanoni kabla mpinzani wake hajafika.
Hayo yapo, usibishe!
Yanaonekana katika viwanja vya mpira kila mara. Mganga nd’o huyohuyo mmoja, masharti hayatofautiani.
Ikafika saa kumi na moja na nusu, msema chochote naye akaishiwa na kusema akabaki katika pumbazo la aina yake asijue ni kitu gani kinaendelea.
Wakati mkutano wa chama tawala ukiwa umejawa na pumbazo mara ule upande wa upinzani vilianza kusikika vilio na watu kutaharuki.
Chama ni chama na utu ni utu.
Baadhi ya wahudhuriaji wa mkutano wa chama tawala ambao hawakuwa wamevaa sare za chama walijisogeza huko ili kupata lolote la kuwafanya waendelee kuwa hapo.
Msiba!
Mtu aliyekuwa ameandaliwa jukwaa lile na tayari mshereheshaji alikuwa amemnadi kwa kila aina ya kilemba, alikuwa yu mfu.
Taarifa hii ikawafikia wale waliokuwa wamevaa sare zao za chama tawala, hakuna aliyejali tena kuhusu mavazi. Utu ukatangulizwa wakauacha mkutano wao na kukimbilia kule ilipotolewa taarifa.
Wakawa kitu kimoja.
“Mwili wake umekutwa mtaroni!” mtoa taarifa alizungumza kwa uchungu. Ikapokelewa kwa aina tofautitofauti ya hisia.
Wengi wakiamini kuwa ameuwawa kutokana na nguvu yake kubwa ya ushawishi huku akiwa tishio kwa mpinzani wake aliyekuwa anawania kiti kilekile kwa kofia ya chama tawala.
Nani amemuua zaidi ya mgombea wa chama tawala?
Hawakuyasema bali walijisemea!
Hapakuwa na mkutano tena, wakaanza kujiondokea. Njiani walioamua kutawala mazungumzo wakailaani siasa na moja kwa moja wakamlaani mgombea wa chama tawala.
Kwa mbali wanaliona kundi la vijana wakiwa wamevaa fulana za chama tawala wakijongea mbiombio.
Wauaji wakubwa! Mama mmoja alitamka kwa ghadhabu.
Kundi lile la vijana sita lilipowafikia wawili wakapunguza mwendo, jasho linawatoka wanahema kwa fujo.
“Ombeni ameuwawa jamani!” alizungumza kwa sauti ya juu. Wote wakamsikia.
Vijana wale wakaendelea kukimbia, robo tatu ya kundi lile ikaungana nao katika mbio zile kurejea kule walipotoka.
Yule waliyemsadiki kuhusika na mauaji ya mgombea wa upinzani, naye alikuwa ameuwawa.
Ajabu!
Habari hii ikawagawanya tena, wa chama tawala wakajadili juu ya mtu wao na wapinzani wakijadili yao.
Miili ya wawili hawa ilifikishwa katika hospitali ya mkoa wa Dodoma, na uchunguzi ulipofanyika ilibainika kuwa muuaji wa Ombeni ni huyohuyo alimuua Tusajigwa! Kwa aina ileile ya uuaji. Hakuna alama aliyoacha.
Ni mauaji haya ya wanasiasa wawili wa vyama tofauti yaliwakumbusha watu juu ya kijiji cha Nyarukongo, Mugumu Serengeti.
Sasa kila mmoja alitaka kujua nini kinatokea kule.
Waandishi wa habari nao wakaona huu ulikuwa wakati muafaka wa kuoanisha matukio yale yaliyofumbiwa macho ya kule Nyarukongo na haya yaliyotokea Dodoma katika kampeni.
Siku iliyofuata bila utafiti wa kina, waandishi wakaandika maneno waliyojua kuhusu tukio hilo.


Tukio hili la mauaji yasiyokuwa na sababu ya wazi mjini Dodoma lilitokea huku mkuu wa majeshi akiwa tayari katika mji huo, alikuwa ameenda kwa ajili ya kikao na wakuu wa polisi mikoa na wilaya za mikoa kadhaa teule ambayo ilisifika kwa kuanzisha fujo na migomo yenye madhara.

Kutokea kwa mauaji haya katika mji wa Dodoma ambao naye alikuwa hapo lilikuwa jambo la kushtua sana, katika kile kikao cha dharula alihimiza wasaidizi wake waingie kazini na kuhakikisha kuwa wahusika wanapatikana ilimradi tu kuleta amani kwa wananchi ambao walikuwa katika hofu kubwa wao na familia zao wakihofia kujihusisha na shughuli za uchaguzi, hasahasa kampeni.

Wanasiasa wasivyokuwa na dogo, lile tukio la watu kupoteza maisha wao wakaligeuza kuwa hoja zao katika majukwaa ya siasa.

Mkuu wa jeshi la polisi alichachamaa sana na kuwaelekeza vijana wake kuwa yule muuaji asipopatikana ndani ya siku saba basi hatasikiliza maelezo yao.
Jeshi la polisi likaingia kazini!!

Siku saba zikapita muuaji hakuwa amepatikana wala sura yake kufahamika, lakini kama ilivyokawaida… vijana wasiokuwa na hatia walitupwa rumande kusaidia upelelezi.

Kwa kauli ya mkuu wa polisi, walitolewa na kuachiwa huru bila dhamana ya aina yoyote.

Alijua kuwa wameangushiwa tu jumba bovu ili kusafisha utendaji kazi wa polisi.
Wale wanasiasa wakazikwa na kampeni zikaendelea!
Wengine waliyasahau mauaji yale lakini mkuu wa jeshi la polisi hakutaka kuamini kuwa kile kimya cha siku kumi ati ni kwamba muuaji ameogopa ule msako na kukimbia.

Alitambua sana mbinu za wauaji, hutulia nanyi mkitulia anasimama.
Akawahamasisha vijana wake kuendelea na msako.
Wakaendelea na msako katika baadhi ya sehemu, walipopasahau muuaji naye akapitia hapo.

Isikupite Hii: Mikononi Mwa Nunda – EP01


ILIKUWA ni siku ya jumamosi, mkutano mkubwa wa kampeni ulikuwa umemalizika katika viwanja vya furahisha jijini Mwanza, wageni walirejea katika nyumba za kulala wageni walizopanga hapo ni baada ya kupata chakula na marafiki pamoja na burudani kadhaa.

Msongamano wa watu ulikuwa mkubwa sana, magari yalikuwa yanatembea hatua chache sana kabla ya kusimama kupisha umati wa watu upite. Kila mara taa nyekundu zilimweka kuashirikia kuwa gari inasimama.

Kama ilivyo ada ya vyama vya siasa kujinyenyekeza kwa wafuasi wao, kuwalipia gharama ili waende katika kampeni zao kukidhi haja za wapiga picha kuweza kuziita picha zao ‘mafuriko’, picha ambazo zitawatisha wapinzani wao.
Basi ilikuwa hivi, magari mbalimbali yalikuwa yamesheheni watu wa kutosha wakirejeshwa huko walipochukuliwa kwa hisani ya mgombea.
Gari moja aina ya Fuso lilikuwa limejaa shangwe tele, nyimbo za chama ziliimbwa kwa fujo huku nyingine zikiwa ni vijembe kwa wapinzani wao.
Wanawake walipiga vigelegele huku wanaume wakiunguruma mithiri ya Simba.
Sijui walilipwa shilingi ngapi kuunguruma hivi?
Kwa watu hawa foleni haikuwa tatizo kwao, ni kama walikuwa wakifurahia umoja ule waliokuwanao wakati ule.
Umoja wa kumuimba na kumsifu mgombea pamoja na chama chake!
Kijana mmoja aliyevalia vyema fulana ya chama alikuwa haishi kupiga miluzi kwa ustadi wa hali ya juu ili kuwachagiza wenzake waendelee kuimba kwa juhudi.
Hatimaye ikawa giza!
Waimbaji wale wakawa kama waliouona usiku, kisha wakakiona kitanda kizuri sana kikiwa kinawangoja wafanye maamuzi ya aidha kulala ama la!
Waimbaji walianza kusinzia, huyu anamlalamikia mwenzake kuwa amepatwa na usingizi wa ghafla, huyu anadai kichwa kinamuuma, mwenye tarumbeta akajikuta akiliona zito na kuliachia likaanguka chini.
Dereva alikuwa wa kwanza kushangaa, maana alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa wanakereka na nyimbo zile, alitamani afike na kuwashusha upesi awe huru na nafsi yake. Zile kelele zilikuwa zinamkera kwa namna mbili, lakini sababu kuu ni kwamba hakuwa upande wao.
Kiongozi waliyemshangilia yeye hakumuunga mkono. Laiti kama lile gari lingekuwa ni mali yake, asingewabeba watu wale.
Sasa wamenyamaza hata kabla hawajaifikia nusu ya safari!
Mara akajihisi ukiwa na kugundua kuwa licha ya kuziona sauti zile kama kelele, lakini pia ilikuwa ni burudani ya aina yake.
Akatoa shingo nje na kuwasihi waendelee kuimba, hivyohivyo hata kama wanamkera.
Kimya!
Akasihi tena kwa kuita jina mojawapo.
Kimya!
Alipoita mara ya tatu akamuona mwimbaji mmoja akiruka kupitia upande uleule aliokuwa dereva. Hapo foleni ilikuwa bado imewakaba koo.
Yule mtu aliyeshuka akiwa na fulana ya chama aligeuka kwa sekunde moja na kupunga mkono kwa dereva, kisha sekunde iliyofuata akaipungia mkono pikipiki, ikasimama akairukia na kutoweka kwa kasi.
“Wameshakula pesa hao!” alijisemea huku akimpuuzia.
Akarejea tena kuwahamasisha watu waimbe… alipokosa jibu safari hii akaona mambo hayapo sawa, haiwezekani kila mara wasimjibu wakati mara zote walikuwa wanazungumza naye wakimsihi aendeshe kwa kasi ya ajabu.
“Suka… oya suka eeh!” akamuita msaidizi wake aliyekuwa ameuchapa usingizi mzito akiwa hajafunga hata mkanda wake.
Suka akakurupuka na kuita jina la mpenzi wake.
Bila shaka alikuwa ndotoni.
“Hebu wacheki hao jamaa nyuma, sijui wameshuka wote?” dereva alizungumza huku akiwa anatazama mbele urefu wa ile foleni.
“Kwani hapa tupo wapi sasa hivi?” Suka akahoji. Dereva akambwatukia kuwa afanye alivyomwagiza.
Suka akaruka na kutua chini.
“Kamanda eeh! Sijui wamekunywa pombe gani hawa jamaa, wamelala wote…” alipaza sauti huku akiwa amening’inia akiwatazama.
“Wamelala? Kivipi?” Dereva akauliza.
“Wamelala usingizi!” Suka akajibu kulingana na swali, dereva akakereka na kumtukana kimyakimya, akataka kushuka. Foleni ikawa imesogea, akatembeza gari.
Suka alipoona gari linatembea, akaacha kuning’inia akaruka zaidi na kuingia ndani ya gari upande wa nyuma.
Akaweka tahadhari asimkanyage mtu lakini hakuweza, alijikuta akimkanyaga mzee mmoja.
“Samahani..” akawahi kuomba radhi.
Hakujibiwa!
Machale yakamcheza, akajaribu kuwatikisa mmoja baada ya mwingine hakuna aliyeonyesha dalili ya kuamka.
Suka akapaza mayowe kumsihi dereva asimamishe gari, dereva akashtushwa na kelele zile akayumba huku na kule na kujikuta akifunga breki mahali ambapo si sahihi, gari za nyuma nazo zikafunga breki lakini ile iliyokuwa ikimfuata kwa karibu haikuweza kusimama ghafla ipasavyo.
Akamvaa kwa nyuma.
Ajali!
Dereva wa ile gari ndogo alishuka upesi ili amkabili dereva wa Fuso kwa kusimamisha gari ghafla lakini alipishana naye akitoka mkuku kuelekea nyuma ya gari lake.
Kwa sababu dereva wa Fuso alikuwa kipande cha mtu, yule wa gari dogo akanywea.
Dereva akaruka juu kwenda kutazama nini kinajiri, sasa kila dereva alikuwa nje ya gari lake kwa sababu Fuso ilikuwa imeziba njia.
Maiti!
Dereva alibaini punde baada tu ya kuugusa mwili wa mtu mmoja, akastaajabu imewezekana vipi msaidizi wake hajagundua mda wote ule kuwa kuna maiti ndani ya lile gari?
Hapo sasa akapagawa na kupiga mayowe.
Mashuhuda wakaongezeka.
Kwa usasa wa teknolojia kila shuhuda akataka awe wa kwanza kupiga picha.
Hivyo tu!


PICHA za miili ile thelathini na mbili zilimfikia mkuu wa jeshi la polisi bwana Saidi Saidi Tangibovu, nusu saa baada ya jambo hili kugundulika.
Akaelezwa kuwa mahojiano ya juu juu yanadai kuwa kabla ya uhalifu huu kufanyika kuna bwana mmoja akiwa amevaa fulana ya chama alishuka na kumpungia mkono dereva kisha akapotea machoni pake kwa kutumia usafiri wa pikipiki.
IGP akaichukua simu yake aweze kuwasiliana na mtu aliyemuhitaji, lakini hakuwahi kupiga kabla hajapigiwa na mkuu wa polisi mkoani Morogoro.
Kuna mauaji ya kutisha yalikuwa yamefanyika, na anayesadikiwa kuwa muuaji alionekana akiwa amevalia fulana ya chama cha siasa.
IGP akakunja sura yake kisha akamshukuru mpigaji, akakata simu.
“Nachezewa sharubu!” akajisemea huku akichukua kitambaa na kujifuta jasho jembamba lilikuwa linamtiririka baada ya kupokea taarifa hizi mbili.


Sumu kali sana inayoua baada ya muda mfupi. Yalikuwa majibu ya daktari juu ya vifo vilivyotokea jijini Dar es salaam.
Zaidi ya maelezo ya dereva kumuona anayesadikika kuwa ni muuaji hapakuwa na ushahidi mwingine wa kuliweka jeshi la polisi karibu na muuaji ili wamkamate, kwa sababu waliovaa tisheti za chama siku ile katika mkutano walikuwa mamia kwa maelfu.
Utamkamata nani umwache nani?
Pagumu!.
Alikiri IGP Said Said Tangibovu.
Wakati anapokea taarifa hizi, simu yake iliita akaitazama na kuona jina la Sungura Sungura, akaipokea…. Bwana Sungura akampa pole.
Huyu alikuwa ni mkuu wa jeshi la polisi aliyemwachia kiti kile baada ya muda wake wa kustaafu kufika.

Mjini Morogoro mambo yalikuwa tofauti kidogo, mambo ya Morogoro yalilifanya jeshi la polisi kuhamia huko kwa muda.
Dimoso! Huyu ndiye aliyelivuta jeshi la polisi zaidi.SEHEMU YA PILI
Taarifa ya awali kutoka mkoani Morogoro ilitaarifu kuwa jumla ya watu wawili walikuwa wameuwawa katikia tukio linaloendana na lile la Dodoma pamoja na Nyarukongo, Mugumu Serengeti.
Jeshi la polisi lilibaki katika ugumu wa kumgundua muuaji kwa majina na sura na kipi ni nia yake.
Katika dimwit hili la ugumu, anatokea manusura wa hekaheka hizi.
Anafikishwa usiku katika kituo cha polisi, waliomfikisha walipachikwa jina la ‘wasamaria wema’. Akajitambulisha kwa majina mawili, Dimosso Kichuya.
Fulana yake iliyotawaliwa na madoa ya damu haikuficha picha ya mgombea uraisi kupitia chama tawala.
“Unasema alikuwa anagawa pesa. Pesa kwa ajiri ya matumizi gani?” Askari alimtundika swali lile.
“Ilikuwa ni nauli ili tufike katika mkutano.” Dimosso alijibu huku akiinamisha uso wake chini kukwepa soni.
Taarifa ya kupatikana kwa manusura huyu kutoka katika mikono ya wauaji iliyafikia masikio ya IGP. Pasi na kupoteza muda amri ikatolewa, ulinzi uongezwe maradufu wakati bwana yule akisafirishwa kwenda jijini Dar es salaam.
Dimosso alielezea muuaji anavyoonekana, akaelezea yote ambayo yangewezesha muuaji kukamatwa.
Kitu ambacho hakukumbuka ni jinsi yule mtu alivyojitambulisha….. lakini alisihi kwamba akituliza akili zaidi anaweza kumkumbuka ubini wake.
Ulinzi ukaimarishwa, Dimosso akafikishwa jijini Dar es salaam, akatibiwa katika hospitali ya jeshi pasi na taarifa hizi kusambazwa katika vyombo vya habari.


MACHO na masikio ya watanzania wengi yalikuwa makini kabisa siku hii yakisubiri kusikia juu ya upepelezi ulipofikia katika sakata la mauaji yaliyokuwa yanafanyika kwa mfululizo wa kutisha kiasi cha kusababisha watu kuacha kuaminiana na kuishi kwa hofu kubwa.
Hatimaye baada ya muuaji kuua kimyakimya kabisa, akafanya kosa na mateka mmoja akatoroka na kujikabidhi polisi ambapo alitoa ushahidi wake.
Zilisikika tetesi kuwa picha ya muuaji imepatikana, wengine walisema kuwa jina la muuaji limepatikana tayari na kuna waliofika mbali na kuzusha kuwa muuaji amekamatwa na atawekwa hadharani waandishi wampige picha wakauze magazeti yao.

Masaa yakasogea mbele ikafika saa saba mchana, waandishi walikuwa wamejaa ukumbini wakitaka kumsikia mkuu wa jeshi la polisi atazungumza nini juu ya sakata lile la kutisha na la kwanza kabisa kutokea nchini Tanzania.
Saa saba ikapita, ikawa saa kumi, na hii nayo ikapita hatimaye zikaanza tena kusikika tetesi, wajuaji wakazusha kuwa mtuhumiwa ametoroka, wengine wakasema kuwa kuna bomu limetegwa katika ukumbi ule wa mikutano hivyo IGP hataweza kufika.
Tetesi hii ikawapunguza watu makali, wengine wakajiweka mbali.
Majira ya saa kumi na moja na nusu hatimaye IGP alikuwa anazungumza na waandishi wa habari. Alielezea mafanikio yao juu ya upelelezi uliokuwa unaendelea, akathibitisha kuwa ni kweli muuaji yupo na mateka aliyetoroka ameelezea kwa kina juu ya muonekano wake.
Kisha akawaomba radhi waandishi kwa kuchelewa sana kufika, akadai kuwa zilikuwa zinafanyika jitihada za upesi za kuweza kuipata picha ya mtuhumiwa.
Na mchoraji alikuwa amefanikisha hilo.
“Kwa wale wanaotusikiliza kwa njia ya redio tutaelezea muonekano wa muuaji ili kila mmoja awe makini kwa nafsi yake na kwa mwenzake pindi atakapomuona muuaji, na kwa wale wanaotutazama katika runinga zao tutaionyesha picha ya muuaji.” Aliweka kituo IGP, kisha akafungua bahasha na kutoka na picha kubwa.


MSONGOLA, kijiji kilicho pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam kata ya Mbande, kundi la watu wanne walikuwa wakisikiliza redioni taarifa hii ya moja kwa moja kutoka kwa mkuu wa jeshi la polisi. Alianza kwa kutoa pole kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao, akalisifu jeshi la polisi kwa hatua stahiki walizochukua kumsaka muuaji ama wauaji hao.
Na hatimaye akalifikia lile lililokuwa linangojewa na wengi.
Muuaji ni nani?
Akaanza kuelezea jinsi muuaji anavyoonekana, na akawasihi watu wawe makini kwa sababu muuaji anaua usiku na hashirikiani na mtu bali yupo peke yake.
“Muwe makini, yawezekana mnacheka naye mchana kisha usiku anawageuka na kuua ndugu zenu!” akaendelea kutoa maelezo juu ya muonekano wa muuaji.
Maelezo yale yalianza kumtisha msikilizaji mmoja wa redio, ni kama alikuwa anaelezewa juu ya mtu aliyekuwa akimfahamu fika kabisa.
Alitulia tuli hadi mkuu wa jeshi la polisi alipomaliza kulielezea taifa juu ya muonekano wa muuaji huyo ambaye tayari alifanya mauaji katika mikoa kumi tofauti katika siku tofauti lakini za kufuatana.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa yanaenda kasi sana, na koo lilimkauka ghafla.
Aliondoka kimyakimya bila kuwaaga wenzake ambapo hawakumakinika katika kuisikiliza taarifa ile.
Alitembea huku ameinama akiwa na hofu kubwa sana, alikuwa anajiuliza maswali bila majibu.
Akafika nyumbani kwake, katika kile chumba kimoja alichokuwa amepanga.
Alifika na kuivua kofia yake, akajitazama katika kioo huku akivuta fikra kulingana na maelezo ya IGP aliyeitwa Saidi Saidi Tangibovu.
Yule aliyekuwa katika uoande wa pili wa kioo alikuwa na sifa zilezile anazoziona siku zote.
Mweusi!
Mrefu!
Mwili uliokakamaa!
Hana ndevu!
Hayakuishia hapo, huyu mtu anavyo pia visivyoonekana katika kioo kile.
Ana lafudhi ya kisukuma!
Ana masihara sana kana kwamba si muuaji!
Ana mikwara si haba!
Sifa zote hizi zilitajwa na IGP na aliyekuwa mmiliki wa sifa zote hizi kwa pamoja ni yeye.
“Mimi Kasunzu nimefanana na muuaji kiasi hiki? Yaani hadi lafudhi?!” alijiuliza huyu bwana aliyeitwa Kasunzu Lema mkazi wa Msongola.
Akichoma mkaa katika mapori ya Kidole kwa Jongo na kuuza kwa bei ya jumla katika banda lake lililokuwa maeneo ya Mbande.
Swali hili lilimtoka kinyonge sana na akiwa ametawaliwa na hofu kuu ya kuingia katika matatizo na jeshi la polisi pale ambapo mtu mmoja aliyesikia pia taarifa hizo atakapotoa taarifa kuwa amemuona muuaji.
Kasunzu hakuwa amejipanga kukabiliana na sakata kama hili.
Alijitazama tena katika kile kioo, sasa akagundua kuwa anatetemeka mikono yake. Na macho yalikuwa mekundu sana.
“Kwamba ninataka kulia au? Hebu niache ujinga…” alijisemesha huku akiyapikicha macho yake. Anajaribu kutabasamu, inashindikana.
“Sasa naogopa nini wakati sijaua! Unakuwaje wewe eeh! Umeanza kuwa na moyo wa kike tangu lini?” alizungumza peke yake Kasunzu akijishtaki.
Lakini tofauti na siku zote bado hakuingiwa na ujasiri aliojaribu kujitengenezea.
Alikosa ujasiri kwa sababu kuu moja, mara zote alikuwa akiingia matatani ni baina yake na kundi la watu fulani ambalo anaweza kukabiliana nalo kimyakimya bila jamii inayomzunguka kumsumbua. Biashara yake ya kuchoma mkaa aliifanya kwa kibali maalumu, ni kwa nadra sana aliingia matatani na askari wa maliasili. Na mara zote alibaki kuwa sahihi.
Lakini hii ya sasa ni taarifa kwa kila mtanzania, taarifa iliyomaanisha kuwa kila mtanzania anatakiwa kumchukia mtu aliyetajwa kama muuaji kimuonekano lakini jina likiwa halijatajwa hadharani.
Yaani hata wachoma mkaa wenzake watamwofia!
Hivyo atalazimika kuikwepa jamii yote, na pia kuwakwepa polisi waliopewa motisha ili wamkamate huyo muuaji na kumfikisha mbele ya sheria na kama hiyo haitoshi atakuwa akikabiliana na wauandaji wa mpango huo mahususi ambao aliupa jina la ghafla ‘TUMKOMESHE KASUNZU’
“Kweli wamenikomesha!!” alikiri kisha akatabasamu akiwa ameinama chini, hakutaka kuliona tabasamu lile katika kioo.
Kichwani akawafikiria watanzania wasivyokuwa na subira wanapomkamata muarifu, sheria mkononi ndo kanuni yao, akajiona jinsi atakavyosulubiwa kisha kufungwa katika tairi na kutiwa kiberiti baada ya kumiminiwa petrol lita tano.
Mawazo haya yakaendana na kumbukumbu ya jinsi anavyoyazika magogo ya miti katika mchanga na kuyatia moto ili baadaye yageuka kuwa mkaa.
Watanifanya hivyo!
Mwili wa Kasunzu ukasisismka na kutoa vipele vya ubaridi, akajiona tena jinsi atakavyokuwa anapiga kelele kujitetea kuwa sio yeye aliyekuwa amefanya mauaji hayo.
“Au sijajitazama vizuri katika kioo, labda sio mimi?!!” alijiuliza kwa sauti ya chini, swali lile alilojiuliza likamfanya acheke huku akijitukana tusi jepesi.
Akakiendea kitanda na kujilaza ili aweze kufanya uchanganuzi kiasi juu ya kile anachokiwaza, lakini hakuchukua muda mrefu akasikia hodi na kabla hajajibu mlango ukasukumwa.
Kasunzu akabaki bila utetezi wowote akiamini kuwa ni polisi wamemfikia.
Hawakuwa!
Alikuwa ni jirani yake, alipoingia alikuwa na simu, akamwonyesha picha aliyoipiga wakati inaonyeshwa katika runinga. Picha iliyochorwa kwa mujibu wa manusura, Dimosso Kichuya wa Morogoro.
“K mnafanana sana na huyu muuaji, yaani mnafanana sana.. wahi kituoni kaka katoe taarifa, utasumbuliwa na wananchi kaka. Najua wewe sio muuaji lakini hii picha kaka itakupeleka pabaya…” alizungumza yule bwana huku akimtazama Kasunzu na kumfananisha na ile picha katika simu yake.
“Yaani pale baa ilivyoponyeshwa hii picha watu wengi wanaokufahamu wameshtuka kweli. Yaani kwa kifupi, huyu aliyechorwa kama sio wewe basi ni pacha wako.”
Geza akamtazama kwa jicho lililotatiza hakujulikana ameelewa ama hajaelewa.
“Hiyo mimba ya mapacha miliitia nyie katika tumbo la mama yangu?” akamtupia swali bila kumtazama.
Bwana yule akashusha pumzi kwa nguvu.
Hajui aseme nini.
“Sikia, Kuna mafala wamenichoma!!” alizungumza kisha akasimama na kupiga ngumi kali hewani.
“Wanadhani nimezeeka, nina miaka thelathini na nne kama sikosei, bado kijana sana tu…” aliendelea kufoka. Yule mtu mbele yake hakuelewa lolote.
“Kuna uwezekano watu hawa wananifanyia mzaha?” Kasunzu akazungumza, yupo wima anatazama darini.
“Mzaha gani huu K!”
“Wanatamani tucheze, hawajui hata kama nimetingwa na ishu za mkaa. Ngoja nikawaambie sitaki mzaha wao.” Alizungumza kisha akapekua chini ya kitanda chake akatoka na furushi dogo, akatoka na kumwacha yule bwana katika chumba chake akiwa amepigwa na bumbuwazi.
Akatokomea!
Asubuhi sana, magazeti takribani yote yalikuwa na habari picha juu ya mtuhumiwa wa mauaji.
Gazeti linaloaminika kabisa likaandika kwa wino mweusi.
“GEZA ANASAKWA AUWAWE”
Chini ikaambatanishwa ile picha ya kuchora ya muuaji!!
Habari hizi Geza alizipata akiwa anaelekea Arusha kwa kupitia njia ya Bagamoyo! Na hapo walikuwa katika kijiji cha Msata.
“Wajinga washanasa na jina langu! Wamenikamata pabaya sana…na wananijua vyema” alijisemea huku akilisoma lile gazeti kijuujuu.
Kusoma lile gazeti, kukalizima jina la Kasunzu Lema alilojipachika baada ya kuimaliza oparesheni hekaheka yake katika mkasa wa ‘PUMBAZO’.
Jina Geza Ulole likafufuka.
£Geza anadai amefanyiwa mzaha, anawasaka waliomfanyia mzaha ili awaambie maneno machache tu, hataki mzaha wao.
Kipi kitajiri!!

SEHEMU YA TATU.
MACHO na masikio ya watanzania wengi yalikuwa makini kabisa siku hii yakisubiri kusikia juu ya upepelezi ulipofikia katika sakata la mauaji yaliyokuwa yanafanyika kwa mfululizo wa kutisha kiasi cha kusababisha watu kuacha kuaminiana na kuishi kwa hofu kubwa.
Mauaji ambayo chanzo chake hakikujulikana, muuaji aliua watoto aliuwa wazee aliua wanaume na nguvu zao aliua kila rika.
Lakini hakusema kwanini anaua!!
Hatimaye baada ya muuaji kuua kimyakimya kabisa, akafanya kosa na mateka mmoja akatoroka na kujikabidhi polisi ambapo alitoa ushahidi wake.
Zilisikika tetesi kuwa picha ya muuaji imepatikana, wengine walisema kuwa jina la muuaji limepatikana tayari na kuna waliofika mbali na kuzusha kuwa muuaji amekamatwa na atawekwa hadharani waandishi wampige picha wakauze magazeti yao.
Masaa yakasogea mbele ikafika saa saba mchana, waandishi walikuwa wamejaa ukumbini wakitaka kumsikia mkuu wa jeshi la polisi atazungumza nini juu ya sakati lile la kutisha na la kwanza kabisa kutokea nchini Tanzania.
Saa saba ikapita, ikawa saa kumi, nah ii nayo ikapita hatimaye zikaanza tena kusikika tetesi, wajuaji wakazusha kuwa mtuhumiwa ametoroka, wengine wakasema kuwa kuna bomu limetegwa katika ukumbi ule wa mikutano hivyo IGP hataweza kufika.
Tetesi hii ikawapunguza watu makali, wengine wakajiweka mbali.
Majira ya saa kumi na moja na nusu hatimaye IGP alikuwa anazungumza na waandishi wa habari. Alielezea mafanikio yao juu ya upelelezi uliokuwa unaendelea, akathibitisha kuwa ni kweli muuaji yupo na mateka aliyetoroka ameelezea kwa kina juu ya muonekano wake.
Kisha akawaomba radhi waandishi kwa kuchelewa sana kufika, akadai kuwa zilikuwa zinafanyika jitihada za upesi za kuweza kuipata picha ya mtuhumiwa.
Na mchoraji alikuwa amefanikisha hilo.
“Kwa wale wanaotusikiliza kwa njia ya redio tutaelezea muonekano wa muuaji ili kila mmoja awe makini kwa nafsi yake na kwa mwenzake pindi atakapomuona muuaji, na kwa wale wanaotutazama katika runinga zao tutaionyesha picha ya muuaji.” Aliweka kituo IGP, kisha akafungua bahasha na kutoka na picha kubwa.


MSONGOLA, kijiji kilicho pembezoni mwa jiji la Dar, kundi la watu wanne walikuwa wakisikiliza redioni taarifa hii ya moja kwa moja kutoka kwa mkuu wa jeshi la polisi.
Akaanza kuelezea jinsi muuaji anavyoonekana, na akawasihi watu wawe makini kwa sababu muuaji anaua usiku na hashirikiani na mtu bali yupo peke yake.
“Muwe makini, yawezekana mnacheka naye mchana kisha usiku anawageuka na kuua ndugu zenu!” akaendelea kutoa maelezo juu ya muonekano wa muuaji.
Maelezo yale yalianza kumtisha msikilizaji mmoja wa redio, ni kama alikuwa anaelezewa juu ya mtu aliyekuwa akimfahamu fika kabisa.
Alitulia tuli hadi mkuu wa jeshi la polisi alipomaliza kulielezea taifa juu ya muonekano wa muuaji huyo ambaye tayari alifanya mauaji katika mikoa kumi tofauti katika siku tofauti lakini za kufuatana.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa yanaenda kasi sana, na koo lilimkauka ghafla.
Aliondoka kimyakimya bila kuwaaga wenzake ambapo hawakumakinika katika kuisikiliza taarifa ile.
Alitembea huku ameinama akiwa na hofu kubwa sana, alikuwa anajiuliza maswali bila majibu.
Akafika nyumbani kwake, katika kile chumba kimoja alichokuwa amepanga.
Alifika na kuivua kofia yake, akajitazama katika kioo huku akivuta fikra kulingana na maelezo ya IGP aliyeitwa Saidi Saidi Tangibovu.
Kila kilichotajwa juu ya muonekano wa muuaji kilikuwa katika mwili wake pia.
Mweusi!
Mrefu!
Mwili uliokakamaa!
Hana ndevu!
Ana lafudhi ya kisukuma!
Ana masihara sana kana kwamba si muuaji!
Ana mikwara asilani!
Zote hizi alijiona kama anazo yeye pia.
“Mimi Geza nimefanana na muuaji kiasi hiki? Yaani hadi lafudhi?!” alijiuliza huyu bwana aliyeitwa Geza Ulole mkazi wa Msongola.
Swali hili lilimtoka kinyonge sana na akiwa ametawaliwa na hofu kuu ya kuingia katika matatizo na jeshi la polisi pale ambapo mtu mmoja aliyesikia pia taarifa hizo atakapotoa taarifa kuwa amemuona muuaji.
Geza alijitazama tena katika kile kioo, sasa akagundua kuwa anatetemeka mikono yake.
“Sasa naogopa nini wakati sijaua! Unakuwaje wewe Geza eeh! Umeanza kuwa na moyo wa kike tangu lini?” alizungumza peke yake Geza akijishtaki.
Lakini tofauti na siku zote bado hakuingiwa na ujasiri.
Alikosa ujasiri kwa sababu kuu moja, mara zote alikuwa akiingia matatani ni baina yake na kundi la watu fulani ambalo anaweza kukabiliana nalo kimyakimya bila jamii inayomzunguka kumsumbua.
Lakini hii ya sasa ni taarifa kwa kila mtanzania, taarifa iliyomaanisha kuwa kila mtanzania anatakiwa kumchukia mtu aliyetajwa kama muuaji kimuonekano lakini jina likiwa halijatajwa hadharani.
Hivyo atalazimika kuikwepa jamii yote, na pia kuwakwepa polisi waliopewa motisha ili wamkamate huyo muuaji na kumfikisha mbele ya sheria na kama hiyo haitoshi atakuwa akikabiliana na wauandaji wa mpango huo mahususi ambao aliupa jina la ‘TUMKOMESHE GEZA’
“Kweli wamenikomesha!!” alikiri kisha akatabasamu akiwa ameinama chini, hakutaka kuliona tabasamu lile katika kioo.
Kichwani akawafikirioa watanzania wasivyokuwa na subira wanapomkamata muarifu, sharia mkononi ndo kanuni yao, akajiona jinsi atakavyosulubiwa kisha kufungwa katika tairi na kutiwa kiberiti baada ya kumiminiwa petrol lita tano.
Mwili wa Geza ukasisismka na kutoa vipele vya ubaridi, akajiona tena jinsi atakavyokuwa anapiga kelele kujitetea kuwa sio yeye aliyekuwa amefanya mauaji hayo.
“Au mimi sio Geza!!” alijiuliza kwa sauti ya chini, swali lile alilojiuliza likamfanya acheke huku akijitukana tusi jepesi.
Akakiendea kitanda na kujilaza ili aweze kufanya uchanganuzi kiasi juu ya kile anachokiwaza, lakini hakuchukua muda mrefu akasikia hodi na kabla hajajibu mlango ukasukumwa.
Geza akabaki bila utetezi wowote akiamini kuwa ni polisi.
Hawakuwa!
Alikuwa ni jirani yake, alipoingia alikuwa na simu, akamwonyesha picha aliyoipiga wakati inaonyeshwa katika runinga.
“Geza mnafanana sana na huyu muuaji, yaani mnafanana sana.. wahi kituoni kaka katoe taarifa, utasumbuliwa na wananchi kaka. Najua wewe sio muuaji lakini hii picha kaka itakupeleka pabaya…” alizungumza yule bwana huku akimtazama Geza na kumfananisha na ile picha katika simu yake.
“Yaani pale baa ilivyoponyeshwa hii picha watu wengi wanaokufahamu wameshtuka kweli”
Geza akamtazama kwa jicho lililotatiza hakujulikana ameelewa ama hajaelewa.
Geza alikuwa matatani!
“Kuna mafala wamenichoma!!” alizungumza kisha akasimama na kupiga ngumi kali hewani.
“Wanadhani nimezeeka, nina miaka thelathini na mbili nadhani, bado kijana sana tu…” aliendelea kufoka. Yule mtu mbele yake hakuelewa lolote.
“Naitwa Geza Ulole….. sijabadilika jina na wala sitaibadili sura yangu.” Alimalizia kisha akapekua chini ya kitanda chake akatoka na furushi dogo, akatoka na kumwacha yule bwana katika chumba chake akiwa amepigwa na bumbuwazi.
Geza akatokomea!
Asubuhi sana, magazeti yote yalikuwa na habari picha juu ya mtuhumiwa wa mauaji.
Gazeti linaloaminika kabisa likaandika kwa wino mweusi.
“GEZA ANASAKWA AUWAWE”
Chini ikaambatanishwa ile picha ya kuchora ya muuaji!!
Habari hizi Geza alizipata akiwa anaelekea Arusha kwa kupitia njia ya Bagamoyo!
“Wajinga washanasa na jina langu! Wamenikamata pabaya sana…” alijisemea huku akilisoma lile gazeti kijuujuu.

Isikupite Hii: Ep 02: Geza Anasakwa Auwawe

Leave a Comment