SIMULIZI The Lost Boys – Ep 1
NEW AUDIO

Ep 1: The Lost Boys

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 1
SIMULIZI The Lost Boys – Ep 1

IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI

*********************************************************************************

Simulizi : The Lost Boys

Sehemu Ya Kwanza (1)

ALFRED MUSITA.

ANAPENDA kujiita Fred. Jina ambalo kazoeleka kuitwa na rafiki zake pamoja na ndugu zake pia. Ni kijana mwenye asili ya Kiarabu na Kiafrika, yaani Chotara kwa lugha yetu pendwa ya Kiswahili.

Ni kijana mwenye kila sifa ya kuitwa mtanashati na mtu yeyote duniani. Akiwa kavaa kofia au mzula, waweza sema huyu ni muafrika wa kawaida tu!, ila akivua ndiyo utamtambua kuwa ni mchanganyiko hasa kutokana na nywele zake nyingi na zilizojiviringa vizuri kabisa. Kwa kifupi jamaa ni mzuri na mtanashati.

Baba yake ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee Musita, ni Mtanzania halisi kabisa kutoka Mbeya. Na mama yake ni mtu wa Iran.

Alfred au Fred, yeye aliamua kuchukua dini ya baba yake ya kikristo kwa sababu muda mwingi aliishi na baba kuliko mama.

Baada ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya wavulana, Bwiru, Fred alichaguliwa kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano na sita Morogoro Sekondari, na alichukua masomo ya biashara kwa sababu ya hamasa aliyokuwa akipewa na baba yake Mzee Musita, ambaye alikuwa ni maarufu sana hapa Tanzania kutokana na biashara mbalimbali alizokuwa anazimiliki.

Alipomaliza kidato cha sita, matokeo yake yalikuja vizuri, hivyo alichaguliwa kuendelea na masomo hayo katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam au UDSM kama wengi hapa Tanzania walivyokiita. Na kama alivyokuwa anaota kila siku, aliweza kutimiza ndoto yake kwa kwenda kuchukua masomo ya Uhasibu.

Kwenye maisha yake tofauti na ya shule, Fred alikuwa ni mpole na mtulivu sana. Hakupenda kufuatilia wanawake japo wanawake wengi walimtaka kimapenzi na wengine kuomba japo wawe naye tu!. Naweza kusema ni dini ambayo alikuwa ameiweka kichwani mwake, ndiyo hasa ilimfanya ajiweke mbali na jinsia ya kike.

Aliishi kwa njia ya maneno ya MUNGU. Hata kwa wale wanawake waliokuwa wanamtakia wazi kuwa wanampenda na kumuhitaji, alikuwa anawakatisha tamaa kwa kutumia maneno hayo kutoka kwenye vitabu vitakatifu.

Kuhusu wazazi wake hasa baba yake, alikuwa si tajiri sana wala masikini kupindukia. Biashara alizokuwa anazifanya, zilikuwa zinampa chakula pamoja na makazi mazuri kabisa ya kulala yeye na mwanae yule wa pekee. Kila alichokitaka Fred, alikipata kwa wakati muafaka kama alivyoahidiwa.

Mama yake Fred alisha-talikiana na Mzee Musita hivyo hakuwa mtu wa mara kwa mara kuonana na Fred, na hata wakionana basi ni kwa muda mchache. Hiyo ni kutokana na mme wake mpya kuwa anambana sana pamoja na wivu.

Na sababu kubwa ya Mzee Musita kutalikiana na Mama Fred, ilikuwa ni rangi ya watu hawa wawili, mmoja Mwarabu na mwingine Mnyakyusa halisi, yule mweusi kabisa. Hapo wazazi wa Mama Alfred, waliingilia na kumtaka mtoto wao aolewe na Mwarabu mwenzake, na hicho ndicho kilichotokea.

Ukitoa Mama Fred kuonana na mwanae uso kwa uso ambapo ilikuwa nadra sana. Walikuwa pia wanawasiliana katika mitandao ya kijamii na MMS.

Neno la dini, ndilo lililokuwa kipaji chake huyu bwana mkubwa.

Hiyo ni kwa kifupi kuhusu Alfred Musita.

HASSAN JENGE.

Huyu alipenda kujiita Hans J, lakini wenzake walishambadilisha jina hilo toka akiwa kidato cha pili kwa kumuita Crazy Hans au kwa Kiswahili Kichaa Hans. Hiyo ni kutokana na mambo pamoja na tabia aliyokuwa nayo.

Hans J, yeye alikuwa ni mrefu kiasi, huku mwili wake ukijengwa kwa rangi ya maji ya kunde.

Baba yake, Mzee Jenge, alikuwa ni Mngoni na mama yake alikuwa ni Mchaga. Mchanganyiko huo, ulimfanya Hassan aonekane ni mtanashati kupindukia.Ndiyo maana yake, jamaa alikuwa ni Handsome haswaa.

Kuhusu tabia huyu jamaa, unaweza kusema ni mhuni sana kama ukimuangalia kwa nje tu!. Kila muda nywele zake zilikuwa tim-tim. Na alipenda sana kuvaa suruali za jinzi na kuzipiga mlege mkubwa tu.

Fulana zake mara nyingi zilikuwa ni mitumba tu. Hakuwahi kuingia dukani na kununua shati au nguo yoyote humo.

Licha ya hayo yote, yaani kuvaa kihuni, kutimua nywele, na kuvaa vitu vya mtumba, huyu Hans alikuwa anajipenda sana. Muda wote alionekana msafi wa kila kitu.Hizo nywele japo zilikuwa tim-tim, lakini zilikuwa ni safi na za kung’aa kutokana na mafuta aliyokuwa anayapaka.

Mwili wake uliyojaa kiasi, na mavazi aliyokuwa anayavaa, ndicho hasa kilimfanya huyu jamaa azidi kuteka wanawake wengi pale alipokuwa anasoma na kuishi.

Kidato cha nne, yeye alimalizia Makongo na baadae aliamua kuendelea na kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Merriwa iliyopo Dodoma. Alipomaliza masomo hayo, alipata alama za juu pia, na kuchaguliwa kwenda kuendelea na masomo yake katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Alikuwa ni mtu wa Sayansi, na aliweza sana kuyamudu masomo yake hayo. Mara nyingi alikuwa anafanya mambo ya hatari sana na ya kushtua kwa kutumia hiyo Sayansi yake, na ndio sababu kubwa ya wanafunzi wenzake kumuita Crazy Hans.

Akiwa kidato cha pili katika shule ya Muheza Muslim iliyopo Tanga. Huyu Hans aliwahi kuchukua kemikali na kuzichanganya kwenye chombo kimoja, na baadae alichukua mchanganyiko huo na kuufungia kwenye chupa ya soda. Aliporidhika, akatoka nje na kuitupa chupa ile kwenye eneo lililokuwa halina watu.

Chupa ilipodondoka, eneo lile la shule lilikuwa kama limevamiwa na magaidi kutokana na mlipuko uliotokea pale. Ilikuwa ni mshike-mshike wa kufa mtu pale shuleni, kuanzia waalimu hadi wanafunzi. Na hata Hans alipoitwa kujibu mashitaka, wala hakuwa na wasiwasi.

Pale alipofukuzwa shule kwa kitendo kile, yeye aliona hamna shida. Uwezo waliokuwa nao familia yake, ulimfanya apelekwe Makongo, ambapo kama ukichaa, ndiyo ulimpanda vya kutosha.

Nje ya maisha hayo, Hans J alikuwa ana wadogo zake wawili wa kike ambao wakati yeye anaingia UDSM, wao walikuwa kidato cha nne. Wakati huo, baba yake alikuwa ni daktari bingwa hapa Tanzania na mama yake alikuwa ni Mbunge wa viti maalumu.

Hivyo suala la umasikini kwao, wala halikuwepo kabisa. Walikuwa wanajiweza sana, na hawakupata kichwa, eti kwa kuwa mama na baba matajiri, basi tusisome. Hiyo ilikuwa hamna kwa watoto wa familia ile, walikuwa wanasoma kupita maelezo.

Uso wake mpana na wenye usiriazi kila mara, pamoja na kutokuwa na chunusi wala vidoa, huku ukipendezeshwa na rangi ya maji ya kunde, ndiyo nyenzo kubwa iliyofanya wasichana wengi washindwe kulala bali kumuwaza Hans J.

Jamaa alikuwa anatakwa na wanawake wengi sana, kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Lakini hakuwahi kuwa na yeyote kati yao.Alikuwa ni mgumu kupitiliza, yaani alikuwa haelewi ni nini maana ya mapenzi na wala alikuwa hana mpango wa kujua maana yake.

Ukiwatoa mama na wadogo zake, Hans hakuwahi kuwafikiria wanawake wengine wa nje hata mara moja katika kalia yake ya maisha.

Jina lake la Crazy Hans, halikuja hivi-hivi. Licha ya vituko vingi vya kisayansi alivyokuwa anavifanya, lakini pia alikuwa ni bingwa wa kuwaumbua wanawake hadharani hasa wale waliokuwa wanamtaka. Hilo pia,lilichangia jina la ukichaa kuendelea kukua siku hadi siku.

Mabinti wengi walikuwa wanawatumia wadogo wa Hans kumletea ujumbe za mapenzi. Lakini mara nyingi kwa Hans, mjumbe alikuwa anauawa tu!. Hao madogo walikuwa wanachezea sana makwenzi na mateke kama wakithubutu kuleta ujumbe hizo.

Sasa kafaulu kuingia UDSM. Huko msimamo wake utakuwaje? Endelea kusoma tu!

JUNIOR KING NICKSON.

Au King Jr kama alivyojiita kisanii. Huyu yeye alimaliza kidato cha nne katika shule iitwayo Bunazi iliyopo Mwanza. Na baada ya kumaliza na yeye akafanikiwa kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano na cha sita katika shule ya Sekondari ya Mwanza, iliyopo huko-huko Mwanza. Yeye alikuwa ni mpenzi wa masomo ya sanaa au arts kwa kiingereza, na aliyafaulu vizuri sana, hivyo naye akachaguliwa kuendelea katika chuo hicho-hicho cha Dar Es Salaam au UDSM.

King alikuwa ni msanii halisi kabisa. Uwezo wake wa kuongea na ucheshi uliopindukia kutoka mdomoni mwake,ndiyo unanifanya niseme haya yote na ndiyo chanzo cha King kuwa maarufu sana katika kila shule aliyokuwa anasoma na kwa kila mtaa aliokuwa anaukanyaga.

Ukitoa hayo ya ucheshi na wingi wa maneno,King alikuwa anaweza kupiga gitaa na kuimba vizuri sana kama R.Kelly au Ne-Yo. Sauti yake maridadi na ya kuvutia,ndiyo ilifanya watu wengi kuja karibu yake na kupata radha maridhawa ya muziki wa Junior.

Nje ya hayo,King yeye alikuwa ana pacha wake wa kike ambaye walikuwa hawaendani hata kidogo,kuanzia tabia hadi sura. Wakati King Jr akiwa bingwa wa sanaa,dada yake alikuwa ni mkali wa mambo ya Sayansi,hivyo ukiwakuta pamoja,basi ujue kuna kitu kinaendelea,labda wameagizwa au wanakula. Kwa kifupi walikuwa hawaendani.

Familia yao ilikuwa ni ya kawaida sana. Baba alikuwa ni Mkufunzi wa chuo cha Mtakatifu Aguastino na mama yeye alikuwa ni Afisa kilimo na mifugo pale Mwanza mjini.

Junior alikuwa si mrefu wala mfupi.Pia alikuwa ni mweusi kiasi huku uso wake mwembamba na wa kuvutia ukimfanya azidi kuwa mtanashati. Macho yake ambayo kiasi fulani yalikuwa ni ya kurembua,ndiyo yalikuwa kivutio cha wanawake wengi pale alipokuwa anasoma na kulipokuwa na makazi yao.

Ukiachilia mbali umbo lake la kisukuma lililobeba kifua kipana kama cha wacheza mpira wa kikapu,Junior pia alikuwa ni bingwa wa kuyapangilia mavazi yake. Kila mara alikuwa ni msafi kama macho ya samaki aliye-baharini.

Kama kawaida ya wasanii. Junior alikuwa ni mjanja na mwepesi sana katika kuongea kama nilivyosema hapo mwanzo,lakini tatizo lake yeye alikuwa ni muoga sana wa wanawake pamoja na mapenzi kwa ujumla.

Kila muda alijiweka mbali sana na mapenzi,hiyo ni kutokana na kusikia habari kutoka kwa watu wa karibu yake,ya kuwa mapenzi yanawaumiza. Mapenzi hayo-hayo,ndiyo yalimfanya dada yake aamue kwenda Sayansi. Sasa Junior,akawa hataki hata kuyasikia bali alipenda kuyaandika na kuyaimba.

Kama ilivyokuwa kwa Hans na Fred,naye Junior au King,wanawake walikuwa wanajigonga kwake kama kawaida,ila ujanja wake sijui niseme wa kijinga,aliweza kuwakimbia.

Mara kwa mara pacha wake alikuwa anakuja na rafiki zake mbalimbali nyumbani kwao,na kwa makusudi kabisa,Junior anaachiwa uwanja wa kuongea na rafiki mmoja-wapo. Basi yeye huongea hadithi nyingine tofauti,na wala alikuwa amuangalii huyo msichana ishara zake,bali akiona msichana huyo anaweka mikao ya ajabu-ajabu,yeye huchukua gitaa lake na kutoka nje na kuanza kulipiga.

Sasa kabahatika kufaulu vizuri kidato cha sita na kafanikiwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam katika mchepuo wa Sanaa au Arts. Na moja kwa moja baada ya kufika chuo,anapangwa chumba kimoja na Alfred,Hassan na Suarez Emmanuel ambaye historia yake sikuipata,kwani katika mkasa huu hakucheza sana kama walivyocheza hawa watatu wengine. Ila Suarez yeye alikuwa ni mtu wa mpira wa miguu sana na pale chuoni alikuwa anachukua masomo ya uandishi wa habari.Utamuona naye mambo yake.

CHUONI DAR ES SALAAM.

Kila mmoja alikuwa katika harakati zake za kuchukua funguo za Hostel za chuo kile kikuu,ili aende kukiandaa na kumpumzika kwa ajili ya kuianza siku mpya pale chuoni.

Wa kwanza kuingia katika chumba namba sita G (6G),alikuwa ni Hassan Jenge,ambaye baada ya kuingia,alitoa makorokoro fulani yakiwa mengi sana. Akayaweka kwenye kitanda cha pembeni. Kisha akatoa nguo zake kwenye begi na kuziweka kwenye kabati moja la upande wa kushoto. Nguo hizo ni kama alizirundika tu! Kwani alikuwa hajazikunja wala kuzinyoosha.

Baada ya kuridhika na uvundikaji huo wa nguo zake,Hans J alitoa shuka zake mbili na kutandika kwenye kitanda kimoja cha chini kabisa kati ya viwili vilivyofuatana upande ule wa kulia.

Baada ya kuweka mazingira ya kitanda chake katika hali nzuri,akaenda kwenye kile kitanda kingine kilichokuwa upande wa kushoto ambapo ndipo alipoweka makorokoro yake. Akachukua baadhi ya makorokoro yale na kuyaunga vizuri na kupata umbo moja la pembe nne.

Baada ya kupata umbo lile,alichukua kichupa kimoja chenye maji,na kuweka kidogo kwenye lile umbo. Akafunga vizuri kile kichupa,kisha akatoa mfuko mmoja mdogo na kuingiza mkono wake kwenye mfuko ule. Alipoutoa mkono,alitoka na unga-unga fulani wa rangi nyekundu. Akauweka mle kwenye lile umbo,na hapo-hapo yale maji yalibadilika na kuwa kama masizi.

Hapo Hans J alitabasamu na kwa uangalifu mkubwa,alifunika umbo lile kwa kifuniko kimoja kilichokuwa pale pembeni.

Alitikisa kwa nguvu lile umbo na kwa haraka akafungua kabati lake na kutupia yale makorokoro mengine,halafu kwa taratibu sana,akaanza kama kutega lile umbo kwenye kabati lake hasa ile sehemu yenye kitasa. Baada ya kuridhika na kutega kwake,taratibu akaanza kulifunga kabati lake,na alipofanikiwa alirudi kitandani kwake na kujilaza.


Baada ya dakika kama saba,akaingia Alfred Musita au Fred. Yeye alikuwa kabeba begi lake vizuri kabisa huku masikioni akiwa kaweka earphone. Alipofika,akamsalimia Hans J na baadae akaweka begi lake kwenye kitanda cha chini cha upande wa kushoto,kitanda kile-kile ambacho Hans J aliweka makorokoro yake.

Fred alifungua begi lake,akatoa shuka mbili na kutandika kitanda cha juu kwenye ule upande wa kushoto. Baada ya kutandika akatoa biblia na rozali,akaviweka pembeni ya mto wake na kisha akaanza kutoa nguo zake.

“Dogo yaonekana unapenda sana kusali”.Hans alianza kumuongelesha Fred wakati akimuona anapanga nguo zake pale kitandani.

“Sana kaka,si wajua MUNGU ndiye kila kitu?Hata yeye alisema,mimi ndimi nuru ya ………”.Hakumaliza kauli yake Fred akakatishwa na Hans.

“Aaagh,embu nitolee mambo ya upako hapa. Sitaki uanze kunihubiria”.Alimwambia Hans.

“Ha ha haaa. Usijali kaka,ipo siku utaniamini”.Fred akamjibu huku akiendelea kutoa nguo zake kwenye begi,na kuziweka pale kitandani kwa kuzipanga vizuri kabisa.

“Unaonekana upo smart sana dogo,kama shori bwana. Unapanga-panga minguo mwenyewe kama unasafiri kwenda mbinguni”.Hans akaendelea kumchokoza Fred huku akiwa amelala pale kitandani kwake.

“Hamna kaka. Si wajua tena,mende wengi chuoni”.Alijibu Fred kwa upole kabisa.

“Haya bwana. Unapenda sana vitanda vya juu eeh. Shida yako uwe unatuchora vizuri wa chini. Sasa ukizingua tu! Sijui unajidai unapumua pumua,tunakuchoma na bikari”.Hans aliendelea kumzingua Fred.

“Hamna noma kaka,siwezi kufanya hivyo”.Fred alionesha upole wake na heshima kwa Hans.

“Safi sana dogo. Hiyo ndiyo heshima nayoitaka. Kama mkiwa wote hivi humu gheto. Nitafurahi sana”.Hans akamsifu Fred na wakati huo Fred alikuwa kamaliza kutoa na kupanga nguo zake pale kitandani,kisha akaanza kuelekea kule kwenye makabati.

“Dogo angalia hilo kabati la kushoto,usithubutu kuligusa kwani utakuwa na sura mbaya kwa masaa kumi mbili”.Hans akatoa onyo ambalo Fred alilielewa na kutoligusa lile kabati ambalo Hans aliweka vitu vyake.

Yeye Fred akaweka nguo na baadhi ya vitu vyake kwenye kabati mojawapo la katikati.

Pale chumbani kulikuwa na makabati manne.Moja upande wa kushoto ambalo Hans aliweka mazaga yake.Mawili yalikuwa katikati ambapo mojawapo,Fred aliweka vitu vyake. Na lingine lilikuwa upande wa kulia.

FRED akapanga nguo zake kwenye lile kabati na baadae akalifunga vizuri. Pale nje ya kabati alibandika stika yenye ujumbe wa MUNGU,uliosema MIMI NI MZABIBU WA KWELI,NANYI NI MATAWI YANGU.

“Ha ha haa,kwa hiyo dogo wewe ni zabibu au matawi?”.Hans akaanza tena uchokozi kwa Fred.

“Mimi ni matawi kaka. Na Yesu Kristo ndiye mzabibu wa kweli ambaye anajua shida ya matawi aliyoyabeba,na ajuaye jinsi gani ya kuyaokoa”.Fred nae alijibu vilevile kwa heshima na kujiamini.

“Safi sana dogo,nimetokea kukupenda kwa sababu una heshima. Vipi una demu?”Hans akaanza kumchimba tena Fred.

“Demu ndiyo nini kaka”.Akauliza Fred huku akionekana dhahiri kuwa hajui maana ya demu.

“Kha! Haya majanga sasa. Yaani jitu zima kama wewe hujui maana ya demu. Kudadeki,kuna kazi ya kukufundisha ili uwe born-town”.

“Bado sijakuelewa kaka”.

“Demu ni mwanamke. Nimekuuliza una girlfriend?”.

“Ahaaa,ujue na nyie lugha zenu ngumu sana. Demu kwa kikwetu ni kitambaa cha kichwani. Ila jibu lako,mimi sina mwanamke. Nipo mimi kama mimi”.Fred akajibu.

“Hiyo good sana,tena sana. Mademu hawana mpango. Sijui hayo mengine yatakayokuja yana mademu au nayo ni kaaaa…..”.Hans hakumaliza kauli yake akawa ameingia King Junior huku mkono wa kulia kabeba begi na kushoto kabeba chupa ya maji, mgongoni akamaliza kwa kubeba gitaa lake.

“Dogo umeamishia nyumba yote huku?”.Hans alianza kumchokoza King baada ya kumuona.

“Kwanza mimi si dogo,halafu jibu lako ni hayakuhusu,jali biashara yako. Minywele kama mchicha”.Hapo Hans akawa kakutana kisiki cha maneno kutoka kwa msanii Junior au King Junior.

Fred alipoona hivyo,akatoka pale kabatini alipoenda kuweka vitu vyake, na moja kwa moja akapanda juu ya kitanda chake.

“Dogo inaonekana unajidai mtata sana. Hata sijakaa sawa umeshanitupia dongo si ndio eeh”.Hans aliendeleza tabia ya ubabe wake,lakini kwa Junior,ni kama alikuwa anamchampa kwa chelewa aliyevaa jinzi.

“Ndiyo maana yake,na tena kula ngumu kabla sijakushushia hili gitaa kwenye utosi wako”.Mapigo yakajibiwa na Junior.

“Mabishololo kama nyie dawa yenu ni kuwapiga mabomu tu! Sasa ngoja. Mimi naitwa Crazy Hans,na kama nilivyo,ndivyo nilivyo hata kitabia”.Hans aliongea huku bado akiwa pale kitandani.

“Hainihusu mimi. Uwe Crazy au mtambo,mimi nakula kwa hela yangu na wewe yako. Kama vipi funga loud spika hilo”.Junior aliongea huku akitua vitu vyake kwa kuviweka kitanda kilicho chini ya kile cha Fred aliyekuwa kimya akiendelea kujiangalizia filamu ya wababe wale.

Junior baada ya kuweka vitu vyake pale kitandani,akafungua gitaa lake na kisha akalijaribu kulipiga na baadae akakaza nyuzi na kuzidi kuendelea kulipiga.

“Oyaa,makelele bwana. Unadhani tupo THT hapa. Tunataka kupumzika,wengine tumetoka mbali”.Hans alikuja juu na kwa kuwa Junior alitambua kweli kafanya kosa,aliacha na kisha akaanza kupangua nguo zake kwa ajili ya kuzipanga kama walivyofanya wengine.

“Oya Mzee wa Upako jina lako halisi wewe ni nani?”.Hans alimuuliza Fred ambaye wakati huo alikuwa anasoma biblia huku Junior akiwa anaweka nguo zake kwenye kabati la mwisho kabisa ambalo lilikuwa bado halijawekwa kitu.

“Mimi naitwa Alfred Musita kaka. Wewe jina lako pia ni nani?.Fred alijibu na kuuliza.

“Mimi naitwa Hassan Jenge au Hans J The Crazy Hans. Unachukua nini hapa?”.Hassan akaendelea kudadisi.

“Hapa nataka kusomea masomo ya Uhasibu kaka”.

“Okey. Naona una mchongo heavy sana ndio maana unataka kusomea mambo ya njururu”.

“Sijakuelewa kaka”. Fred alimwambia Hans.

“Nasema inawezekana una sehemu umewekeza kazi nzuri ndio maana umekuja kusomea mambo ya fedha”.Hans alimjibu.

“Ha ha haaa. Ina maana jamaa hakuelewa ulichokizungumza mwanzo?”.Junior aliuliza huku akicheka.

“Jamaa wa upako sana huyu,si unacheki hata kwenye kabati lake? Mtu wa GOD huyu,mtaa kapita nao mbali,ila kwa kuwa yupo karibu na waridi ni lazima atanukia”.Hans akawa kama anamjibu Junior.

“Kwani wewe mwanangu unachukua nini?”Junior akamtupia Hans swali.

“Mimi nachukua masayansi bwana. Nataka siku moja nitengeneze bunduki na mabomu yangu.

Ha ha haa. Ndoto yaweza kuwa kweli,wewe kaza tu!”.Junior alimpa moyo Hans huku akitabasam.

“Na wewe unachukua nini na jina lako ni nani?”.Hans akageuza swali na kumuelekezea Junior.

“Aaa,mimi nachukua mambo ya Arts na jina langu naitwa Junior King Nickson,au King JR kisanii zaidi”. Junior akajibu.

“Basi fresh,naona kuna wa biashara,sanaa na mwanasayansi. Sijui huyo anayekuja atakuwa mpishi au?”.Hans akaendeleza maneno yake.

“Ha ha haaa,yawezekana atakuwa msafisha vyoo,maana UDSM inatoa hadi hiyo course sasa hivi”.Junior naye akamuunga mkono Hans.

“Ha ha haaa. Inaonekana kijana wewe ni wa komedi sana. Vipi una demu?”.

“Aaagh. Hayo tuwaachie bongo muvi. Mademu sitaki hata kusikia habari zao”.

“Huo ndio mpango mzima,siyo unakuwa na kidemu kinachuna hela kichizi. Halafu baadae kinakutosa. Sifanyi ujinga huo”.Hans aliongea lakini alikuwa kamuachambali sana Fred kwa lugha aliyokuwa anaitumia.

“Kwa hiyo na wewe huna ye bebee?”.Junior akadondosha swali kwa Hans.

“Si mimi tu! Hata Mzee wa Upako hapo juu”. Hans alijibu huku akimuoneshea kidole Fred.

“Basi good. Hili gheto litakuwa la mabachela,atakae kuja kama anakindimu chake,tunamkurupua”.Junior aliongea huku akifunga kabati lake baada ya kuweka nguo zake vema.

“Eee,kama kawa kama dawa. Nduki kali anatolewa mpaka anachachawa”.Hans alimjibu Junior wakati huo Junior alikuwa anatandika kitanda chake.

Kimya kikatanda kidogo. Na mara mlango ukafunguliwa akaingia jamaa mmoja mrefu na mweupe. Alikuwa kabeba mabegi mawili makubwa na mgongoni alikuwa ana-begi lingine dogo.

“Niaje wazee”.Jamaa yule aliwasalimia wakina Junior kwa kuwapa tano.Lakini kwa Fred ikawa tofauti kidogo,yeye alitaka kushikwa mkono kama wa-baba.

“Mwanangu vipi?Mbona unataka kujidai Kawawa hapa. Embu kunja ngumi na kugonga hapa”.Yule jamaa alimwambia Fred,naye Fred akatii.

Jamaa yule alionekana ni mhuni kupita hata wakina Junior na Hans. Hata mambo yake,alionekana kama anavuta bangi hivi au ni mtu wa mtaani sana.

“Naitwa Ban Diho. Nachukua Education. Wewe mwenzangu unaitwa nani?”.Ban alianza kujitambulisha na kisha akataka kuanza kuwajua wakina Junior huku akianza na Fred.

Hapo kila mmoja akajitambulisha kwa mwenzake,na baada ya Ban kuridhika na utambulisho ule,alianza kupanga vitu vyake.

“Oya toka sehemu hiyo ya chini,ni yangu toka nyumbani mimi nilishaiwahi”.Ban alimwambia Hans baada ya kutoridhika na ile nafasi ya juu ya kitanda.

“We boya nini. Unaanza kuleta tabia toka nyumbani unadhani kwenu huku?Nenda zako huko,kama umelewa mibangi hapa watu tumelewa vinyesi. Hatoki mtu hapa”.Hans J alijibu mapigo ya Ban na kumfanya Ban apandishe hasira.

“We kuku unasemaje?”.Ban alikuwa moto kiukweli. Alimfata Hans pale alipo na kurusha kofi ambalo Junior aliliwahi na kulidaka ili lisimkute Hans na kusababisha ngumi.

“Oya,wewe si umekuta watu wameshawahi?Mbona unataka kuleta za Wajerumani na wakati zilishapitwa hizo?”.Junior alikuwa anaongea huku anamsukumia Ban kwa pembeni.

“Kwa hiyo mnanichangia au?”.Ban aliendelea kuja juu na kitendo cha Junior kuamlia kilionekana kama anachangiwa.

“Hamna,mimi naamulia ili msipigane hapa”.Junior aliongea huku akiendelea kumsukumia pembeni Ban ambaye tayari alikuwa mwekundu kwa hasira.

Muda wote Hans alikuwa tayari kwa ugomvi kwani alishasimama na hasira zilikuwa zimemkaba hadi anashindwa kuongea. Fred yeye alikuwa anacheki filamu ya kipekee kabisa pale chini.

“Nakuuliza mnanichangia?”.Ban aliendeleza lile swali lake.

“Hamna bwana mimi nakusihi uache mamb………”.Junior hakumaliza kauli yake,akasukumwa pembeni na Ban,kisha jamaa kwa mahasira yake,akaanza kuvuruga hali ya mle ndani.

Akaanza na kitanda cha Junuior,akatupa tupa mashuka chini na godoro huko. Hakuchoka Ban,akaenda kwenye kitanda cha Hans na kuanza kufanya kama alivyofanya kwa Junior.

“Si mnajidai wajanja,ngoja leo niwaoneshe”.Ban aliendelea kuwa mtawala mle ndani,safari hii alielekea kwenye makabati ya nguo.

“Shika yote,ila hilo la mwisho usijaribu hata kidogo”.Hans alitoa onyo wakati Ban anaenda kwenye yale makabati.

BAN akaanza na kule alipoweka Junior mazaga yake. Akafungua na kuanza kutupa-tupa nguo za Junior hovyohovyo. Hakuridhika,akaenda la katikati alipoweka Fred,napo akavuruga vuruga kama kwa Junior.

“Sasa ni zamu ya huku sasa”.Ban aliongea kwa sauti huku maneno yale alikuwa akimwelekezea Hans.

Muda wote wakina Junior na Alfred walikuwa hawajui Hans kaweka nini mle kabatini,naye Hans wala hakuwa na muda wa kwenda kumzuia Ban aifungue lile kabati.

Ban kwa papara,akalivamia lile kabati la Hans na kulifungua kwa papara ileile. Eee bwana eee,kuna mlipuko mmoja ulitoka pale wa ajabu balaa. Haukuwa wa sauti kubwa bali ni kama wa kukung’uta nguo hivi. Na baada ya mlipuko ule,harufu ya chumba ikabadilika,ikawa kama chooni tena kile choo cha watu waliokula dengu,mbaazi au maharage.

Ban alibaki kasimama pale kabatini kama kapigwa na shoti au kagandishwa na rimoti. Aliporejewa na fahamu aligeuka na kuwaangalia wakina Junior.

Duuh! Jamaa na weupe wake usoni,lakini alikuwa ni mweusi kama jembe jipya au buti la mwanajeshi yule mpya.

Chumba kizima kiliangua kicheko baada ya kuona sura ile. Hata Fred naye hakusita kucheka hadi ilifika kipindi akataka kudondoka pale alipokuwa kalala. Hans ndiyo kabisaa,jamaa alikuwa anacheka hadi analala.

“Hii ni nini?”Ban aliuliza baada ya kujaribu kufuta sana ule weusi. Weusi ule ulikuwa hautoki hata Ban alipojaribu kujifuta na nguo. Yaani ulikuwa umenatia haswa,hata akifuta kwa nguo,nguo inatoka bila hata alama ya yale masizi.

“Utajua mwenyewe,wewe si unajidai mjanja,endelea sasa. Na hayatoki hayo,na hiyo harufu kama umekunya,mzee utajiju. Dawa ninayo mimi tu!”.Hans alimjibu Ban huku bado akiendelea kucheka.

“Nakwambia nipe dawa”. Ban alimjia juu Hans,na kwa kuwa Hans tayari alikuwa kishachokozwa,akamtuliza kwa ngumi kama mbili za haraka,na hata Ban alipojaribu kuzirudisha,aliambulia makofi na kipigo zaidi.

Alipoona kazidiwa,alitoka nje ya chumba kile na sijui alienda wapi. Lakini akili ya Hans ilicheza haraka sana kuliko wote,si mnajua watu wa Sayansi walivyo na akili za hivyo?. Mara moja alikimbilia kwenye kabati lake na kuficha yale makorokoro mengine,kisha akaanza kutupa-tupa hovyo na nguo zake huku wakina Junior wakiwa wanamshangaa wasijue jamaa anafanya nini.

Baada ya kuridhika na ile chaghala baghala aliyoifanya,alimwambia Junior na Fred wajifanye wanaokota vitu vyao,ila kwa taratibu huku wakisubiri ujio wa Ban.

Basi wakina Junior wakaanza kufanya hivyo kama walivyopata maelekezo kutoka kwa Hans. Hazikupita hata dakika mbili.Mlango wa chumba chao ulifunguliwa na Ban aliingia na mzee mmoja wa makamo aliyejitambulisha kama ni Dean wa wanafunzi wa chuo kile. Hans na wakina Junior,wakampa heshima yake,kisha wakaendelea kukusanya vitu vyao.

“Nini kimetokea humu?”.Dean yule aliwauliza wakina Junior.

“Huyu hapa Sir,kaja humu na kuanza kutupiga makofi,tulipojitetea akaanza kuvuruga vitu vyetu”.Junior kwa usanii wake akawa anaongea huku kama analia.

“Wewe ni kweli?”.Yule Dean alimuuliza Ban ambaye alikuwa kafura kwa hasira na ule weusi aliomwagiwa,utaweza kusema jamaa katoka kuchimbwa kwenye mkaa.

“Ticha sijapiga mtu”.Ban akajibu kwa hasira huku akikana lile kosa.

“Na hizo nguo wewe ndiyo umevuruga”.Dean akamuuliza tena.

“Wamenihudhi hawa ticha,wanaleta zao hapa chuoni sio nyumbani”.Ban akawa anaendelea kujibu vilevile kwa hasira.

“Sasa kumbe wewe ndiyo una makosa,ona ulivyovuruga vitu vya wenzako. Haya na huo weusi umetoa wapi”.Dean akaendelea kumuuliza maswali Ban lakini lile swali likawa kama kicheko kwa Hans.

“Si huyo jamaa kwenye kabati lake sijui katega nini,nimefungua kikaniripukia”.Ban akajibu huku kama anajifuta yale madude yaliyomrukia usoni.

“Eti wewe,hiyo ni nini?”.Dean akamuuliza Hans.

“Ticha mimi sifahamu kabisa hiyo ni nini. Alikuja humu ndani hivyohivyo. Sisi tukadhani kachanganyikiwa.Mara kaanza kutupiga,akaona hajatosheka,akaanza kuvuruga chumba chetu. Tulipomgusa kwa kumkanya aache,tukashangaa anatoka na aliporudi,kaja na wewe”.Hans hakuwa nyuma kudanganya.

“Tena katupiga kwelikweli Ticha,sisi huyu hatumtaki hiki chumba,atatuua. Yaani kampiga kofi huyu kaka hapa eti kisa anasoma biblia pale juu”.Junior akazidi kuchombeza maneno huku akimnyooshea kidole Fred kuwa naye ni muathirika wavurugu za Ban.

“Eti wewe. Unaonekana mtu wa MUNGU sana. Huyu kakupiga?”.Dean akamuuliza Fred ambaye alikuwa kapoa sana kuliko wote.

Hans na Junior wakawa wanasubiri jibu la Fred kwani ndilo lingewatoa kwenye ule msala. Na kwa kuwa walijua Fred ni mtu wa dini sana,basi hatoweza kudanganya.

Lakini Fred alijua akitetea kwa kusema hajapigwa,basi yule jamaa angeendelea kuwa kwenye kile chumba.

“Sir. Huyu kaka mimi hadi sasa hivi sijamuelewa ni kwa nini kanivuta toka kule juu hadi chini kisha akaanza kunipiga na kunitukana. Imeniuma sana”.Fred alijibu kisha akaacha kuokota zile nguo na kupanda juu ya kitanda chake,na kilichofata hapo ni kwikwi za kilio kutoka kwake.

Huo ndio ukawa msumali wa mwisho kwa Ban kwani hata kujitetea alishindwa kabisa.

“Wewe ni mjinga,sasa utalipa ujinga wako. Okota hizo nguo moja baada ya nyingine,na kisha zikunje vizuri kabisa na hawa watakuwa wanasema hiyo ni yangu,wewe utakuwa unaweka kwenye kabati husika,sawa?”.Dean alimpa adhabu Ban,adhabu ambayo Hans hakuwahi kuifikiria kama yaweza kutokea.Kwa mara ya kwanza nguo zake zingepangwa vizuri kabatini.

“Lakini Ticha mimi sija….”.

“Muda unaenda,na sibadili mawazo. Wewe bora umalize adhabu yako ili tupange jambo lingine”.Dean alimkatisha Ban na kumwambia aanze ile kazi mara moja,huku yeye dean akienda kwenye kitanda cha Junior na kukaa ili aangalie utekelezwaji wa ile adhabu.

Ban akaanza kupanga zile nguo huku akiuliza ya nani,na baada ya kupewa jibu,aliweka kabati husika.

Ni jambo la nusu saa,tayari likawa limekamilika huku chumba kikirudi katika hali yake ya mwanzo.

“Sasa wewe beba begi lako na nifuate napoenda”.Dean alimwambia Ban na Ban akafanya alivyoambiwa. Wakatoka kwenye kile chumba na kuwaacha Junior,Fred na Hans wakicheka na kufurahi sana.

“Mzee Wa Upako,wewe ni noma. Nilidhani utatusaliti. Dah! Big up sana mzee,nimekubali hii dunia kwa sasa haina mtakatifu”.Hans aliongea akimsifu Fred kwa kitendo alichofanya.

“Aaah,kaka. Dini inakaa pembeni kama unataka kujiokoa hasa katika majanga. Ilinipasa nidanganye ili kujiokoa maana nisingefanya hivyo,tusingesoma humu. Kwa hiyo nilidanganya kwa faida, na sio kwa kumkandamiza mtu japo ni kweli nilimkandamiza”.Fred akajibu huku ametabasamu.

“Basi Fresh Mzee Wa Upako. Nadhani sasa amani itatawala. Ngoja tumsubiri huyo mpya”.Hans aliongea na kumaliza ile hadithi.


Kule kwingine. Ban akapelekwa chumba kumi na mbili A (12A)kikiwa ghorofa ya chini kabisa za Hostel ile.

Alipoingia alifarijika sana,kwani karibu wanachuo wote waliokuwapo mle alikuwa anawafahamu kasoro mmoja tu!,ambaye ndiye aliyechukuliwa na Dean na kupelekwa chumba cha akina Hans.

“Kamanda Ban.Vipi mkubwa?Mbona mweusi usoni tu?”.Jamaa mmoja alimuuliza Ban baada ya Dean kuondoka na yule mwanachuo mwingine.

“Acha tu! Mkubwa Mose. Yaani huko nilipotoka,nimefanyiwa kitu mbaya kichizi”.Ban alimjibu yule jamaa ambaye alikuwa anaitwa Moses Frank.

“Haaa,wajinga gani hao wamefanya hivyo tuwafate sasa hivi”.Jamaa mwingine ambaye pia anafahamiana na Ban aliuliza.

“Achana nao kwanza kaka mkubwa Sunday. Hawa watalipa tu! Wamejiingiza kwa makamanda,watakiona”.Ban alimjibu yule jamaa mwingine ambaye anaitwa Sunday Magembe.

“Ndio maana yake kaka. Waache kwanza,halafu wakishasahau,sisi ndiyo tunaamka. Na watakoma. Wapo chumba namba ngapi?”.Jamaa mwingine aliuliza.

“Wapo kule 6G halafu maboya tu!mwanangu Moi.Sijui hata ilikuwaje”.Ban alijibu pia swali la yule jamaa aliyeitwa Moi Shabala.

“Kwani ilikuwaje man?”.Moses alimuuliza swali Ban,naye Ban alianza kuwasimulia mkasa mzima hadi alipofika pale.

“Pumbavu zao,na watalipa. Hawajui sisi ndiyo wazee wa kazi eeh. Yale ya Bunda,tunaleta huku,watasanda tu!”.Hapo Sunday Magembe aliongea kwa kujiamini

Chumba kile kilijaa marafiki ambao walisoma pamoja katika chuo cha ualimu kilichopo Bunda,na sasa waliamua kwenda kujiendeleza kwa kuchukua shahada ya katika mchepuo uleule wa ualimu. Baada ya kusikia mwenzao kafanyia sivyo na wakina Hans,basi tayari wakawa wameweka bifu.

“Tulia tulia kamanda. Yatatoka tu hayo,mbona unaanza kurudi hali yako?”.Moi alimpa moyo Ban na kweli jamaa akatulia huku kisununu cha kulipa kisasi kikiwa moyoni mwake.


NB:Dean ni yule mtu au mkufunzi anayehusika na tabia za wanafunzi chuoni.

Baada ya Dean kuondoka na kumuacha Ban kule kwenye makao yake mapya,alienda moja kwa moja hadi katika chumba walichopangwa wakina Junior. Akaingia na kuwapa mgeni wao mpya ambaye angekuwa nao mle ndani. Naye Dean akaacha maagizo katika chumba kile hasa akisisitiza nidhamu kutawala. Akapotea eneo lile.

“Oyo. Niaje kaka”.Hans kama kawaida yake. Mzee wa kupokea wageni.

“Fresh Jombaa,ni vipi”.Alijibu jamaa yule huku akiweka begi lake mahala pa kuweza kupekulia vitu vyake vizuri.

“Humu gado tu!We wapi hiyo”.Hans akamuuliza tena.

“Aah,mimi wa Singida kaka. Nimekuja kucheki degree hapa”.Jamaa akajibu huku akifungua begi lake na kuanza kutoa baadhi ya vitu vyake kama mashuka na kuweka katika kile kitanda cha juu ya Hans.

“Jina lako kaka mkubwa”.Junior alienda moja kwa moja kwenye kuuliza jina.

“Mimi naitwa Suarez Emmanuel, man”.Suarez alijibu.

“Ahaa,okey. Mimi naitwa Junior,nachukua mambo ya sanaa. Na hawa wengine watajitambulisha wenyewe”.Junior alijitambulisha na kuwapa nafasi nao wengine wajitambulishe.

Baada ya utambulisho huo,Suarez alimaliza naye kwa kusema yeye anachukua masomo ya uandishi wa habari.

“Okey. Sasa kama wewe mwandishi wa habari,basi fanya kama unanihoji mimi kilichotokea humu”.Hans alianza mbwembwe zake. Akampa Suarez mswaki ndio afanye ni kipaza sauti,halafu akakimbilia kwenye kabati lake na kuchukua koti la suti na kulivaa.

Suarez alikuwa ni mtu wa utani sana,na kwa kuwa alikutana na watu wa aina hiyo,ikambidi naye kuendana nao ili waishi kwa furaha.

“Eheee. Ndugu mheshimiwa. Nimekutana na mtu mwenye uso mweusi sana na wakati sehemu nyingine ni chungwa,alikuwa hapo mlangoni akitokea humu. Waweza kuniambia ni nini kilimtokea?”Suarez alikuwa amemwekea ule mswaki mdomoni Hans ili asikie atakachojibu. Wakati huo yeye Junior alikuwa kaweka gitaa lake begeni na kulifanya kama kamera. Fred yeye alikuwa mtu wa kucheka tu!,maana vile vituko,hakuendana navyo hata kidogo.

“Aaah,jamaa kalipukiwa na bomu la mavi. Ha ha haaa”.Hans alijibu huku anacheka.

“Bomu la mavi ndio bomu gani hilo aisee”.Suarez nae akiwa yupo siriaz na kazi yake,akauliza.

“Ni bomu ambalo nimetengeneza mimi mwenyewe kwa kutumia kemikali zinazotumika kukaushia kidonda hospitali na kemikali ya kutengeneza harufu mbalimbali. Nilifanikiwa kutengeneza harufu ya kinyesi baada ya kuweka mchanganyiko ule pamoja. Na kwa kuwa ile sehemu niliyoiweka ilikuwa ina joto na ni plastiki,basi mchanganyiko ule ukawa masizi”.Hans alimjibu huku akiwa anatengeneza koti lake la suti hasa ile sehemu ya tai.

“Kwa hiyo mheshimiwa umejipanga vipi na mapambano na huyu mtu uliyempiga bomu?”.Suarez aliuliza swali ambalo lilimfanya Hans acheke kabla hajajibu.

“Ndugu mtangazaji acha kunichekesha bwana. Yule nimempiga kama mtoto mdogo humu. Muulize Mzee wa upako”.Hans alijibu.

“Kumbe uliongeza tena kwa kumpiga?”.Suarez aliuliza na kama akaishiwa nguvu,huku ile hali ya utani ikawa inaondoka.

Suarez alikuwa anawajua wale jamaa waliokuwa katika kile chumba. Wote walikuwa wana urafiki na Ban,na wote wanatabia kama za Ban.

“Ndiyo maana yake,nimepiga kama toto dogo hapa”.Hans yeye alijibu kiutani kama kawaida.

“Hivi wajua kuwa kile chumba nilichotoka wale waliopo ni rafiki zake yule jamaa?Yaani namaanisha kwa ulichokifanya ni lazima waje kulipa kisasi”.Hapo Hans alikaa kimya kidogo na kuyachanganua yale maneno kwa kina. Wakati huo hata Junior naye alishusha kamera yake aina ya gitaa na kukaa kitandani. Fred naye macho yakawa kodo kwani naye alihusika sana kumkandamiza Ban.

“Isitoshe wale jamaa wote wana tabia zinazofanana. Yaani ni kama wasela fulani hivi. Na wana tabia za kibabe”.Suarez aliendelea kukandamiza uoga mioyoni mwa Hans na wakina Junior.

“Aaagh!Isiwe kesi bwana. Kwa kuwa ishajulikana,basi tutakuwa makini nao. Cha msingi ni kuwa na ushirikiano. Tunasaidiana kwa kila kitu. Si mkiona napigwa,nyie mnakaa pembeni. Hapa kazikazi,ngumi kwa ngumi,wali kwa wali,wakimwaga ugali sisi tunakomba mboga”.Hans aliongea kwa kujiamini na kuwapa moyo wengine.

“Hapo umenena Crazy. Hapa mkono mkonoe tu!Hamna kuleta maujinga. Wakitupa mabangi yao gheto kwetu,sisi tunaenda kutupa mabomu,uongo wa Baba Paroko”.Junior naye alitoa wazo la kusisitiza kauli ya Hans.

“Mmh! Mimi nitafanyaje jamani?Mbona matatizo haya”.Fred alionesha wazi alikuwa anaogopa.

“Mzee waUpako usijali man. Tutakupa maujanja. Hapa aogopwi mtu. Cha msingi tuwe pamoja kila mara,labda tukiwa tumeenda darasani ndio tuachane,ila kama tupo nje ya darasa,tukae pamoja”.Hans alimtoa shaka Fred.

“Dah! Ila mimi siwezi kupigana wala kupambana nao kimaneno”.Fred alizidi kuonesha udhaifu wake.

“Usijali mzee. Mimi mwenyewe nipo upande wenu. Hawataweza kufanya chochote”.Suarez naye aliamua kuwa upande wa akina Hans.

“Sasa kuna nini tena. Hapa watakaa tu!Labda sio sisi. Hadi waombe msamaha kama wakituchokoza”.Hans alifurahi sana ujio wa Suarez katika kundi lao.

“Basi tuwe na amani na tujipange kwa mashambulizi tu!. Wakitaka vita baridi,mimi nipo hapa,naweza kuongea asubuhi hadi asubuhi tena kwa makelele. Wakitaka vita ya silaha,yupo mzee wa mabomu hapa. Wakitaka kidini dini,tunakuachia Baba Paroko. Wakitaka kutangazwa ujinga wao,tuna kamanda hapa”.Junior aliongea huku akikabidhi majukumu mbalimbali kwa met wake.

“Ndio maana yake. Hamna kudevela”.Hans alimaliza.

Kimya kikatanda na kila mtu alikuwa katika pilika zake binafsi,huyu akipiga gitaa,yule anasoma biblia,mwingine anapanga nguo zake na mwingine yeye kulala tu!.

Maisha ya chuo kwa watu hawa,yakaanza kihivyo. Yameanza kwa kuweka bifu na kundi lingine palepale chuoni.


“Mzee Ban. Naona madude yameisha sasa. Umerudi katika hali yako”.Moses aliongea baada ya Ban kutoka bafuni alikwenda kuoga.

“Kama kawa kaka mkubwa Mose. Sasa najipanga kwa kujibu mapigo ya wale wajinga”.Ban alimjibu huku akifuta maji yaliyokuwa usoni pake.

“Hapa tuwaache kama wiki ili wasahau. Wakiingia,tunawateka wote,halafu ndiyo watatutambua”.Moses aliongea kwa kujiamini.

“Kama kawa. Wewe si ndo mzee wa mipango. Mimi nakusikiliza wewe. Watajuta kuingia anga hizi”.Ban alimjibu Mose ambaye alikuwa analala kitanda cha juu ya Ban.

“Halafu na yule boya aliyesepa humu na yeye kajiunga nao. Leo nimemuona wanaenda wote kupata msosi”Hapo Sunday aliongea.

“Wote watakuwa mulemule. Si anajidai kamanda,tutamwonesha kuwa sisi ndo wenyewe”.Ban aliongea huku akiwa anasura ya kumaanisha anachokiongea.

“Na atakoma kuingia kwenye kile kikundi,mbwa yule. Tutamfanya kitu mbaya mpaka aseme nisameheni”.Moses naye aliongea kwa kujiamini huku akiwa anahasira ambayo imesababishwa na tabia ya ubabe aliyokuwa nayo.

“Ndiyo maana yake. Samaki mmoja akioza wote wameoza hao. Habari ya Bunda tunaidrop pande za UDSM”.Moi alimaliza maongezi yale na mkwara wake bila kutambua hata hao anaowaongelea tayari wamejipanga kwa lolote.


Wiki ikafika tangu chuo kile kifunguliwe huku wale majamaa waliokuwa na bifu wakiwa wamejipanga sana kwaajili ya kulipa kisasi na wengine kwaajili ya kupambana nao.

Hakuna siku ambayo utawakuta kundi la wakina Hans wakiwa peke yao,na hakuna siku ambayo utakuta kundi la akina Ban limetengana. Kwa kifupi walikuwa wanatembea katika makundi makundi kama wahuni au majambazi,hasa ukiwaangalia mavazi yao.

Wale wakina Ban walipenda sana kuvaa mavazi makubwa na kusababisha chuo wawaite WAGUMU. Wale wakina Hans wao walikuwa wazee wa vimodo kasoro Fred ambaye nae ilibidi aendane na mazingira ya chuo. Mambo ya nguo za kushonesha kila siku,yalikuwa yana kazi sana. Heri kununua majinzi ambayo hata bila kunyoosha,wewe unavaa tu!.

Hawa bado walikuwa hawana jina. Ila baadae huko mbele,waliitwa THE LOST BOYS. Hadi leo jina hilo wanalo na wamelikubali japo mwanzoni walipinga sana. Lakini mwisho wa siku walikubaliana nali na kusema kweli sisi ni THE LOST BOYS,yaani wale walioshindwa katika jambo fulani au wale washindwaji. Utawaona huko mbele.

Lile kundi la akina Ban au WAGUMU walishindwa wafanyaje ili walipe kisasi kwa wakina Hans,hiyo ni kutokana na uwepo wa sura zao kila mahali uwaonapo. Yaani ukimuona Fred,basi utamuona Junior,Hans na Suarez.

“Sasa Ban tunafanyaje mkubwa”.Moi alimuuliza Ban siku moja baada ya kuona siku zinaenda bila ya kutimiza lengo lao.

“Hapa cha msingi ni kuvamia gheto lao na kuwavurugia haswa. Kuna jambo moja tu!, ni kutafuta funguo ya chumba chao ambayo ipo nyingine kule tunapochukuliaga risiti. Mimi nitaenda kuinyofoa,wakati huo wewe Sunday utakuwa unamzingua yule Madam wakati mimi nafanya maepe”.Ban aliongea wazo ambalo lilikubalika na wote.

Walikubali hilo kwa sababu walimuamini sana Ban kwa tabia hizo. Alikuwa ni mzoefu wa hayo mambo ya kuchukua kitu bila kugundulika.

Bila kuchelewa,mpango ukafanyiwa kazi kwa Ban na Sunday kwenda ofisi za utawala,na mmoja akabaki mapokezi akiongea na dada wa pale na mwingine ambaye ni Ban akasingizia kuna makabrasha anatakiwa ayawasilishe ofisi ya mkuu wa chuo,hivyo akapewa nafasi ya kuingia mle ofisini na kupekua makabrasha hayo.

Funguo za vyumba za Hostel zile za chuo,zilikuwa zimetundikwa kwenye ubao mmojawapo mle ofisini na kila funguo ziliandikwa namba ya chumba zinapofungua.Hivyo haikuwa ngumu kwa Ban kuangaika kutafuta funguo zilipo.

Dakika tatu,walikuwa wametoka ofisini na makaratasi machache huku kwa chini yake walikuwa wameweka funguo ya kufungulia chumba cha akina Fred. Safari ya kuelekea huko,ikashika nafasi yake.

Baada ya kufika eneo la tukio. Ban Diho alitoa ule ufunguo kisha akafungua mlango ule wa chumba cha wakina Hans. Baada ya kuufungua,wakaingia ndani bila wasiwasi wowote.Wote wanne walikuwepo.

Walichofanya ni kufungua makabati ya chumba kile na kuanza kutoa nguo za waenyeji. Walizizagaza chumba kizima,wakati huo wanachuo wengi walikuwa darasani.

Baada ya kuzizagaza,Mose na Sunday wakatoka nje,kisha wakarudi na ndoo moja iliyokuwa na maji na nyingine ilikuwa na michanga au udongo ili unielewe.

“Sasa hawa si walijidai wajanja na masharobaro,ngoja leo tuwaoneshe”.Ban aliongea kwa jazba na kuchukua ndoo moja yenye udongo na kuanza kumwagia zile nguo za walizozagaza pale chini.

“Kalete mwingine”.Ban alimpa ndoo Sunday akalete udongo mwingine.

Alipoondoa Sunday,Ban akachukua ndoo ya maji na kuanza kumwaga maji juu ya udongo ule uliokuwa juu ya nguo za kina Hans. Hakuridhika na hali ile,akaanza kuukanyaga kanyaga kama anaushindilia chini.

“Kaongeze maji”.Alimpa ndoo Mose na Mose naye akatoka haraka kwenda kuleta maji. Dakika mbili,tayari wote walikuwa chumba kile kwa ajili ya kufanya akili yao inachowatuma.

“Hapa watajuta,wameingia choo cha kike halafu wamemkuta mama mkwe kachutama anajisaidia. Pumbavu zao,hapa ndio Bunda Boys”.Ban kwa hasira alikuwa anaongea huku akichukua tena ndoo ya udongo na kumwagia kwenye vitanda vya wakina Junior.Nao wale watatu wengine hawakuwa nyuma kumsaidia kwa kuendelea kukanyaga zile nguo ambazo tayari zilikuwa kwenye majanga.

Baada ya kumwaga udongo,maji yakafata juu ya vitanda ambavyo ndivyo vinawapa usingizi Junior,Hans,Fred na Suarez.

“Sasa hapo nimeridhika. Twen’zetuni”.Ban aliongea na kuwaoneshea ishara washirika wake waondoke pale.

Haikujulikana wanafanya vile ili iweje,na pia ni upotofu tu uliochanganyika na akili za kijinga ambazo zimetengenezwa na hali isiyokuwa na huruma ndani ya mioyo yao.

Waliondoka mle ndani huku wakiwa vifua mbele kana kwamba kile walichofanya ni sahihi. Lakini kwa kuwa ilipangwa katika maisha yao ije itokee vile,basi ni sahihi kwa walichokifanya,hiyo ni kiimani zaidi.

Nukta ya safari yao iliishia bafuni ambapo walijiweka safi na baadae kwenda vyumbani mwao na kuvaa mavazi nadhifu katika miili yao.

Baada ya unadhifu huo,safari nyingine iliwadia,nayo ilikuwa ni kuurudisha ule ufunguo wa chumba cha wakina Junior.

“Oya sasa hivi zamu yenu Mose na Moi. Njia ni zilezile tulizochukulia huo ufunguo. Ni zilezile za Bunda,hamna kilichoongezeka”.Sauti ya kibabe kutoka kwa Ban iliamrisha kwenda kwa Mose na Moi. Nao kwa kuwa walimwogopa Ban,wakafanya walichoambiwa.

Walitoka mle chumbani huku wakiwa na zile karatasi zao,kwa chini walifunika ile funguo.

Baada ya dakika tatu.Mose na Moi walikuwa ofisi ya utawala huku Mose akiwa mchangamfu sana kwa yule dada wa mapokezi ya ofisi ile. Wakati huo Moi alikuwa kaomba kutafuta karatasi zake ambazo alidai zinahitajika kwenye usajiri.

Kulikuwa hakuna kipingamizi kwa wanachuo kuomba kutafuta karatasi zao hasa pale wahusika wa ofisi ile wanapokuwa katika harakati zao nyingine.

Huku akiwa makini asionekane kwa watu,Moi aliuweka ule ufunguo katika sehemu iliyoandikwa namba ya funguo ile. Na alipofanikiwa,alimwambia yule dada hajaona karatasi zake,hivyo anaenda kuangalia ofisi nyingine. Bila hiyana na kutojua kilichonyuma ya pazia,dada wa watu alikubali na kumruhusu Moi kuondoka.

“Oya umefanikiwa kurudisha funguo ile bila kuonekana?”.Sauti nzito ya Ban iliuliza baada ya Moi na Mose kurudi chumbani.

ITAENDELEA

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 2

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment