SIMULIZI

Ep 04: The Escrow Mission

SIMULIZI The Escrow Mission Episode 01
SIMULIZI The Escrow Mission Episode 04

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Simulizi: The Escrow Mission
Sehemu Ya Nne (4)

Taarifa za upotevu wa nyaraka hizo ulilitikisa Bunge, kila aliyesikia habari hiyo hakuamini ama kile anachoambiwa au anachozikia. Maswali yasiyo na majibu ndiyo hasa yaliyotawala vichwa vya walio wengi. Jeshi la polisi nalo lilikuwa likajaribu kadiri ya uwezo wao kuona labda hiki au kile lakini yote ya yote hakuna aliyejua kabrasha hizo zimepoteapotea vipi.
Upande mwingine vijana wa Usalama wa taifa ambao daima huendesha shughuli zao katika eneo hilo nao walikuwa wamekutana kwa siri kujadiliana juu ya upotevu wa kabrasha hizo nyeti.

“Hii ni njama, lazima ifanywe na wenyewe,” mmoja alisema.

“Unataka kutuaminisha kuwa wameiba wenyewe?” mwingine akadakia.

“Ndiyo, sasa funguo unatunza wewe, ofisi ni yako, polisi wanasema hakuna mtu yeyote asiyehusika aliyeingia ndani ya wigo huu usiku wa jana. Sasa hii maana yake ni nini? Inabidi tumchunguze Yule katibu si ajabu kala njama,” mwingine akagongelea msumari ambao karibu jopo zime liliunga mkono.

“Itabidi tufanye hilo ijapokuwa vikao vinaisha leo na watakutana hapa miezi miwili ijayo…”

“Sasa huu ndo muda wa kufuatilia kila kona ili wakirudi bungeni kwenye kikao cha arobaini na nane tuwe na jibu na pia tuwe tumewashughulikia wanaohusika,” alidakia Yule aliyeonekana kama ndiyo mkubwa wa kile kikao. Baada ya majadiliano yaliyochukua muda mrefu muafaka ulifikiwa na kila mmoja alipewa jukumu lake katika kipindi hicho.
Mchana wa siku hiyo kikao kingine kiliendelea katika ofisi Fulani huko walikutana watu wasiozidi wanne; Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Dodoma, kiongozi wa askari wa Bunge na Spika. Mjadala uliochukua nafasi ulikuwa ni huo wa kupotea kwa hizo nyaraka nyeti.

Vichwa vilifanya kazi ya kuchambua hiki na kile, lakini jibu la uwazi halikupatikana, polisi walisema kuwa wana uhakika hakuna mtu aliyeingia ndani ya wigo huo kutokana na ulinzi mkali waliokuwa wameuweka kama ilivyo kawaida yao, hata walipohakikisha kwenye kamera za usalama bado hakuna mtu aliyeonekana kuingia ndani ya wigo huo. Baada ya kuchanganua njia zote ambazo kwazo zinaweza kuzaniwa zimetumiwa kuiba nyaraka hizo, bado jibu liligonga kuwa lazima Katibu wa Bunge anahusika kwani nduye ambaye anajua kila kitu jinsi kilivyo na kinavopangwa.

§§§§

Katika kikao cha siku hiyo cha Bunge, Mheshimiwa Kibanio hakuonekana kwenye siti yake, haikuwa kawaida. Kila mmoja alikuwa akimsubiri mtu huyo ambaye alipendwa kwa jinsi anavyojua kujenga hoja ndani ya vikao vya bunge. Mara kwa mara Waheshimiwa walikuwa wakiangalia saa zao lakini hawakumwona kutokea.
Hali hiyo pia ilikuwa kwa Spika wa Bunge, akiwa katika kiti chake alikuwa akitupa jicho mara kwa mara katika kile kiti lakini hakumwona Msesema, huyu leo vipi? Alijiuliza. Kwa siri akaagiza wahudumu wahusika ili kujua kwa nini mtu huyo hajafika bila taarifa na siku hiyo alikuwa na mswada wa kuwasilisha juu ya sakata la Escrow, ilikuwa ni siku aliyoahidi kuwataja wote waliomo kwenye hiyo ‘Orodha ya aibu’.

§§§§

Saa ya ukutani ilipiga muziki wa kuahiria saa kamili imefika, Mheshimiwa Kibanio aliinua uso na kuangalia saa ile, ilikuwa saa tano asubuhi inakimbilia kwenye saa sita huko, akakurupuka lakini alijikuta mwili mzito na kichwa kinamuuma sana. Nini hiki? Alijiuliza pasi na jibu. Akajilazimisha kuamka na harakaharaka akaingia maliwato ili kujiswafi, tayari alikuwa amechelewa kikaoni na ilibaki dakika chache sana kabla hajasimama kulieleza Bunge juu ya wale wote wanaohusika na lile sakata nyeti. Mara akaona simu yake ikiita, alipoinyanyua na kuitazama alimjua anyepiga simu hiyo ni nani.

“Mheshimiwa vipi, tunakungoja kwa hamu!” ile sauti ikamwambia.

“Aaaah! Yaani nashindwa kujielewa asee, ndiyo naamka sijui nini kimetokea,” Mh. Kibanio akajibu huku akivaa shati lake.

“Ok, pole sana, labda jana zilikuwa nyingi sana …”

“Aaaa hapana, jana sijaonja kabisa ila nashangaa nini kimenipata, hata sasa naona kichwa kizito sana na si kawaida,” akaeleza. Alipokwisha kuvaa kila kitu tayari, aliuvuta mkoba wake tayari kuondoka lakini alipounyanyua ukafunguka na kabrasha zote kumwagika, alitupa jicho pale sakafuni zile karatasi zilipozagaa. Hakuamini anachokiona, nani alifungua huu mkoba? Akajiuliza huku akiinama na kuokota yale makabrasha. Badala ya kuyaweka mkobani, akaanza kuyachakura chakura akitazama hili na lile.

“Shiiiit!” akang’aka kwa sauti, akaanza tena kuyachambua yale makabrasha.

“Sasa liko wapi?” akauliza kwa sauti kana kwamba kuna mtu anayeongea naye ndani ya chumba hicho lakini alikuwa peke yake. Akayaacha yale makabrasha na kuanza kupekua kwenye makabati, hakuna kitu. Mheshimiwa Kibanio alijitupa kitandani na kupiga ngolo.

Hakuamini kama kabrasha hizo za muswada muhimu ambao alitakiwa kuuwasilisha mchana huo hazikuwepo, zimekwenda wapi? Lilikuwa ni swali gumu kutegua, akiwa juu ya kile kitanda alijikuta akilia kama mtoto. Akakurupuka na kukusanya yale makaratasi pale chini akayaweka mkobani na kutoka chumbani mle kama mtu aliyechanganyikiwa. Alipoushika mlango akakuta upo wazi, haujafungwa, akasimama na kutazama ndani. Nani kaufungua huu mlango? Nimeibiwa! Akawaza na kujikuta akiishiwa nguvu. Alipokuwa akiuvuta mlango kuufungua akaona karatasi ndogo ikipeperushwa kwa upepo na kuingia sentimeta chache ndani ya chumba hicho. Akaiokota mara moja na kuitazama, ilikuwa na maandishi machache tu.

…Ukitaja hata jina moja tu, yatakukuta yaliyomkuta Msesema…
Kisha mwisho wa maneno hayo kulikuwa na kipicha kidogo cha fuvu la binadamu.

“Shiiit! Ina maana Msesema kauawa? Au ujumbe huu umekosewa?” akajiuliza kwa sauti ndogo. Akiwa anatetemeka, akatoka ndani ya chumba kile na kuteremka ngazi za hoteli hiyo ya Dodoma na kufika chini kabisa kwenye maegesho.

“Mheshimiwa vipi leo? Mbona umekawia sana?” dereva wake akamwuliza.

“Hata sijui kwa kweli nimelala sana, nahisi naumwa maana kichwa chote kizito,” akajibu huku ile gari ikiwa inatoka polepole katika maegesho yale.

§§§§
“Ukimya wetu wa siku tatu umemfanya adui yetu ajitokeze na kufanya mambo yanayoaminika kuwa ni shetani pekee anayeweza,” Madam S alimwambia Amata.

“Ndiyo, ni mbinu nzuri sana uliyotushauri kuitumia, na sasa kama unavyosikia, kabrasha zimeibwa palepale bungeni, inashangaza!” Amata akajibu.

“Yeah, ujue hapa kuna mtu mwenye taaluma kama si ya ujambazi basi sijui tuite ya nini, we kuingia mle ndani ilhali ulinzi mkali na kamera kila kona vyote hivyo vizikubaini. Sasa pale kesi yote inamwangukia Mwambene, katibu wa bunge, lakini hapana, kutokana na wapi tumefikia huyu mtu ni profesheno, lazima tuingie kazini kwa akili zote na nataka apatikane akiwa hai ili tujue nini kipo nyuma ya pazia,” Madam S alimwambia Amata,

“Koh! Koh! Koh!” akakohoa kidogo, “Sasa nataka uendelee na kazi, pambana na huyo mtu na umlete mikononi mwangui akiwa na pumzi yake, licha ya hili tu najua atakuwa na mengi sana,” Madam alimalizia kusema, akatoa miwani yake na kuiweka mezani.

“Umesomeka Madam!” Kamanda Amata akajibu huku akinyanyuka, “Nani yuko nyuma yangu?” akauliza.

“Gina, nimeshamuweka tayari”.

“Asante!” Amata akajibu huku akiwa tayari kasimama kwa kuondoka.

“Ofisi yetu imehamia hapa kwa siku chache lakini namnata huyo mtu akiwa hai ili kutoka kwake tujue nani amemtuma,” Madam akasisitiza.

Amata akaondoka na kuiacha ofisi hiyo ndogo na kutokomea mjini mpaja hotelini kwake, alipoingia tu jicho lake lilizunguka chumba chote na kugundua kuwa kuna upekuzi wa siri uliofanyika. Wameshajua nilipo, akawaza, kisha kwa hatua za taratibu alikipita kitanda mpaka usawa wa dirisha, alipokaribia kijimeza kidogo kilicho pembeni mwa kitanda ambacho juu yake kuna taa ndogo kwa ajili ya kusomea, saa yake ikapiga ikamfinya na kutoa mlio Fulani mkali. Amata akasimama na kuiinua ile taa akaichunguza na kugundua kuwa kuna kidubwasha kidogo sana kimebandikwa pembeni, alipokiangalia alikijua kidubwasha hicho chenye kazi ya kunasa sauti na kutuma mahala Fulani.

Zaidi ya hilo alikitambua kifaa hicho kuwa kina uwezo mdogo wa kurusha mawimbi hayo na si zaidi ya mita 200 za mraba. Adui yangu hayuko mbali kama si yeye basi kibaraka wake, akawaza huku akifungua kabati kubwa la nguo, akachukua kijiredio chake kidogo ambacho hutumia kurekodi sauti mbalimbali, akakibonya na kutafuta sauti aliyoona itamfaa adui yake, akataka kuweka ile ya mtu anakoroma, akaona hiyo sio sawa kwa muda husika, akatafuta nyingine ya kufaa akakiweka katika ile meza kisha akakiwasha, wakati kikiendelea kutoa sauti hizo za mahaba zilizorekodi watu wawili wakifanya mapenzi huku wakiongea maneno ya mahaba, akasogea pembeni na kuvuta meza nyingine akaiweka nyuma ya mlango, akafunga mapazia yote na kuzima taa.

Giza hafifu lilitawala chumba hicho, ile mashine iliendelea kutumbuiza pale mezani. Amata akaketi, bastola yake akaiweka mezani na kisha kujimiminia pombe kali aina ya GIN na kuinywa taratibu akimsubiri mgeni wake kwani alijuwa kwa vyovyote atakuja.
Kutokana na uchovu aliokuwa nao Amata, kijiusingizi kilikuwa kikimnyemelea kwa mbali, lakini mara kwa mara alikuwa akipambana na hali hiyo. Kama alivyodhani ndivyo ikawa, alihisi kitasa cha mlango kikinyongwa taratibu, akageuza shingo na kuangalia kule mlangoni huku bastola yake iliyofungwa kiwambo ikiwa tayari imekaa kinganjani.
Kabla Amata hajamwona mtu huyo aliona kwanza mlango ukisukumwa taratibu na domo la bastola lililofungwa kifaa cha kuzuia sauti likitangulia na kutema risasi nne mfululizo kuelekea kitandani. Alitamani kucheka lakini akajizuia kwa kuwa haikuwa mahala pake.

“Shiit!” sauti kutoka nje ya mlango ikasikika na mara yule mtu akaingia mzima mzima. Alikuwa ni pande la mtu, mwanaume aliyevalia jeans na fulana nzito, usoni mwake alivaa soksi iliyoficha uso wake na kuacha macho tu.

“Karibu katika mikono ya shetani!” Amata aliongea kwa sauti nzito iliyomfanya yule bwana kushtuka na kusimama ghafla, “nilitaka uje na umekuja mwenyewe, ondoa magazine kwenye silaha yako bila kuigeuka,” akamwamuru.
Yule bwana akataka kuuvuta mkono wake wa kushoto kufanya hilo.

“No! tumia mkono huohuo ulioshika bastola,” akamwambia, naye akafyatua ile magazine ikaanguka chini na risasi zake zikatoka ndani yake na kutawanyika,

“weka na bastola yako chini,” akamwambia, naye akafanya hivyo.

“Geuka huku mikono yako ikiwa kichwani, ukiniletea ujinga nakumaliza, sina urafiki na viumbe vibaya kama ninyi, mnaotoa roho za watu bila sababu,” akamwambia na Obobo akafanya hivyo, sasa wakatazamana uso kwa uso.
Akainua glass yake na kupiga funda moja la kinywaji, kabla hajamaliza kinywaji kile. Alijikuta bastola yake ikimtoka mkononi mwake ka teke kali alilopigwa na Obobo. Obobo skstus kando kwa miguu yake miwili na kusimama tayari kwa mapigano. Amata akachukua ile chupa na kumimina kinywaji kwenye glass yake bila wasiwasi wowote, huku Obobo akimtumbulia macho kwa kitendo hicho. Akiwa katika kuzubaa huko chupa ile ya pombe ilitua kichwani kwa Obobo na kuvunjika, Amata aliruka kutoka katika kiti alichokaa na kutu mbele ya huyo jamaa kisha konde moja zito likatua shavuni mwa Obobo na kumpeleka chini bila kipingamizi. Obobo akajibetua na kusimama wima kisha akaruka samasoti na mguu wake wa kwanza ukamkosa Amata ule wa pili ukatua begani mwake. Maumivu nakali yakalipenya bega la Amata, hakujali, konde zito la Obobo likaufuata uso wa Amata naye akaepa, la pili akaepa, la tatu akaepa na kuruka ‘beki’, kwa mtindo huo wa sarakasi akampiga mateke mawili mazito chni ya kidevu, Obobo akajibamiza ukutani.

Amata akatua kitandani na bila kuchelewa, akateremka na kupeleka mapigo matatu ya karate yaliyompata Obobo sawasawa na kumsababishia kizunguzungu, Obobo akajitupa chini na kuiwahi bastola ya Amata lakini Amata alilitambua hilo, akavuta teke moja kali lililotua shavuni mpaka karibu na sikio na kumtupa Obobo upande wa pili, Amata akaiokota ile bastola na sekunde hiyo hiyo, Obobo akona hatari iko upande wake, alijikunja na kujikunjua kama samaki akaruka na kujipiga kwenye kioo cha dirisha, akadondokea nje na kupotelea mtaani.

“Shenzi kabisa, hiyo nimekuonjesha, kazi bado inakuja!” Amata alijisemea mwenyewe huku akiwa ameshalifikia lile dirisha na kumwona mtu huyo akipotelea mitaani.
Akaiendea ile bastola ya Obobo pale chini na kuiokota kisha akazipachika zile risasi katika magazine na kuiweka mahala pake, kwa mikono yake miwili, kwa kutumia ule wa kushoto akai-slide kwa upande wa juu na kuruhusu risasi ya kwanza kutumbukia chemba. Bastola la kizamani kweli kweli lo! Akawaza huku akiiangalia angalia, ilikuwa ni Smith and Wesson.

§§§§

Hali ya sintofahamu iliwakumba Wabunge baada ya kukosa kusomwa ile ripoti iliyodaiwa kuwa ina majina ya watu waliokwapua pesa za ESCROW. Spika alipotangaza kuwa swala hilo litajadiliwa kikao kijacho wengine wakazomea na wengine wakakosa ustaarabu hata kuamua kutoka nje.

“Kwa nini isisomwe? Haijaibwa wala nini, wameikalia tu kuficha maovu ya wakubwa, hii nchi hii mpaka tutoke hapa tulipo labda aje kuongoza Yesu au Mtume Muhamad” alilalama mmoja wa waheshimiwa huku akiingia kwenye Shangingi lake tayari kwa kuondoka. Ilikuwa ni vikundi vikundi vya watu watatu au wane; hapa na wengine kule, kila mmoja akilaumu kutosomwa kwa taarifa hiyo toka kwa Mheshimiwa Kibanio.
Watu alijawa na shahuku ya kusikia majina hayo yakitajwa hadharani lakini haikuwa hivyo wakati wengi wao wakiamini kuwa faili hilo halikuibwa bali ni mbinu za wakubwa ni wachache tu walioumiza kichwa kuwa kimtokea nini hata faili hizo zipotee katika mazingira ya kutatanisha.

Katika moja ya vyumba vya mikutano nyeti ndani ya jengo hilo la Bunge kulikuwa na kikao kinachoendelea, kikao cha kamati ya usalama ya Bunge. Agenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kuona juu ya upotevu wa faili hizo.
Mvutano mkubwa ulikighubika kikao hicho baada ya kusikiliza taarifa ya Katibu wa Bunge.

“Wewe si ndio mwenye funguo itakuwaje hilo faili lipotee?” aliuliza mmoja wa wajumbe. Wakati wakiendelea kubishana mara akaingia Spika ambaye muda wote alikuwa akifunga kikao cha Bunge, akakaribishwa na kupewa taarifa ya wapi kikao kimefikia, alipojiridhisha na taarifa hiyo akawasilisha pia taarifa ya upotevu wa nakala kama hizo ambazo zilikuwa mikononi mwa Mheshimiwa Kibanio na wakati huo taarifa za kuvamiwa kwa Mheshimiwa Segeratumbo nazo zikawasilishwa.

“Yote haya tulikuwa hatujayasema kwa sababu za kiusalama, lakini kumbe tumekosea,” akasema Spika.

“Kwa hiyo kuna mtu au watu ambao wanazisaka kwa udi na uvumba? Basi haina haja ya kuumiza kichwa kwa maana watu hao tunao humuhumu,” mjumbe mmoja akatia neno katika kikao hicho.

“Isiwe tunazugana hapa!”

“Tunazugana vipi? Msesema amekufa kwenye ajali ya ajabu tu, na hizi nyingine ndio zinaleta utata mara mia, tumekwisha.”
Kikao kilichukua muda mrefu, majadiliano yalifikia muafaka kuwa uchunguzi ufanyike na ikiwezekana wanaohusika wachukuliwe hatua.

“Mheshimiwa Msesema alipopata ajali alikuwa na mwanamke mle ndani ya gari hivi haiwezi kuwa ni mmoja wapo?” mjumbe mmoja aliogeza.
Kila mtu alishangaa kwa taarifa hiyo hakuna aliyeijua kwanza ijapokuwa wachache wao waliichukulia ni hali ya kawaida. Jopo hilo likaamua kuwa yule mwanamke akamatwe kwa mahojiano kisha baada ya hapo ndio wajue nini chakufanya. Maamuzi yakaandikwa na kuwekwa katika faili.

“Lakini nitaomba msubiri kwanza kabla sijatoa go ahead ya hili,” Spika aliwaambia.

“Aaaah kikao cha kamati kimeamua!” mwenyekiti wa kamati akaunguruma kwa jazba.

“Nina maana yangu kuwaambia hilo…”

Wakakubaliana na kile kikao kikaisha. Kila mtu akatawanyika.

***
“Kwisha habari yao! Bado kumkomesha mmoja, yule anajifanya mjanja,” Mheshimiwa Nnandi aliwaambia wenzake Kagosho na Matata.

“Tumekodi jabali, mtu anyejua kazi yake,” Matata akaongeza kwa sauti ya kilevi.

“Eti leo walikuwa na kikao cha kamati ya usalama kwa lipi? Hawajui kuwa kati yao kuna mwanetu mle! Hii nchi yetu bwana tutakula tunavyotaka, nani wa kutubabaisha?” Kagosho naye alibwabwaja.
Watatu hawa waliendelea kujipongeza kwa kula na kunywa, kila mmoja kichwani mwake akifikiri tu jinsi gani ya kutumbua pesa hizo ambazo si muda zimetolewa kwenye akaunti hiyo na kuwafikia walengwa kwa mbinu tofauti.

MIAKA MIWILI ILIYOPITA
BENKI KUU YA SERIKALI

GAVANA WA BENKI HIYO alikuwa katika kikao kizito katika moja ya ofisi nyeti za serikali, katika kikao hicho agenda kuu ilikuwa ni jinsi gani ya kifunga hiyo akaunti yenye mabilioni ya pesa yaliyoingia kutokana na mradi hewa wa nishati ya umeme.

“Watu tumefanya kazi kubwa kuhakikisha hili linawezekana, sasa ni wakati wetu kula njasho letu,” mmoja wa wajumbe alikiambia kikao.

“Ni sawa usemalo, lakini unajua kuwa hizi fedha ni za umma?” Gavana aliuliza.

“Za umma! Kivipi? Hivi we unajua tumestrago kiasi gani kufanikisha hii akaunti kunona? Watu tumetengeneza mikataba tumekwenda Thailand tukafanya yetu. Tumerisk kazi zetu ujue, si kwamba hatukuwa na plan bali pesa hizi kuja katika akaunti hii ni kosa moja dogo tulilifanya, na hili lilisababishwa na watu kama wewe,” mjumbe mwingine mwenye ushawishi kwa maneno yake alimwambia yule Gavana.

“Sawa, sasa ninachouliza ni kwa nini hizi pesa zikae hapa?” gavana aliendelea kurusha maswali.

“Swala sio kwa nini, swala ni jinsi gani tutagawa hisa za wenye nazo?” mjumbe mwingine akadakia.

“Hisa! Hisa kivipi?” Gavana akashtuka mpaka akasimama.

“Ndiyo, hisa, watu wamewekeza mapesa kibao katika mradi huu, kwa kuwa tulisema itafika wakati wenye hisa zao wapate gawio lao, na wakati huo ndio sasa,” yule mjumbe wa kwanza akasema.

“Sikilizeni, mambo ya mahesabu hasa ya pesa kama hizi hauendi hivi, wala mgawanyo haufanyiki kama mnavyofikiria ninyi. Kwa kuwa pesa hizi nilizipokea kama gavana kwa maandishi kutoka kwa kiongozi mkubwa basi na zitagawiwa mnavyotaka ninyi kwa utaratibu uleule wa kimaandishi…”

“Unamaanisha nini hapo?” mjumbe yule wa kwanza akadakia.

“…Namaanisha wale waliosaini ili ziletwe hapa na kufunguliwa hii akaunti ya Tegeta Escrow ndio hao hao wasaini kuziondoa,” yule Gavana alifafanua kwa lugha rahisi,

“Isitoshe Mkaguzi mkuu wa serikali CAG lazima atakuja kufanya ukaguzi wake kwani Bunge la bajeti limekaribia,” akaongeza.
“Kwa hiyo!”

“Kwa hiyo mniache nifanye mawasiliano na hao watu kisha nitawajulisha nini kimeamriwa,” Gavana akamaliza.

MIEZI MITATU ILIYOFUATA
TAARIFA ya maandishi iliyosainiwa na watu kadhaa wenye vye vikubwa vywenye maamuzi ya juu ilifika katika ofisi ya Gavana wa fedha. Ijapokuwa alitumbua macho lakini hakuwa na la kusema au kuamua. Pamoja na taarifa hiyi iliambatanishwa orodha ya majina ya watu na akaunti zao za benki ili pesa hizo zielekezwe kwenye akaunti hizo kwa viwango vilivyopangwa.

“Come on!” alijiseme hukua kijiegemeza kwa nguvu katika kiti chake cha kunesanesa. Alipoona akili yake haifanyi kazi akainuka na kutaka kutoka ofisini aliposhika kitasa cha mlango simu yake ya mezani ikaita, akasimama kwa hofu na kuiangalia. Kwa masikitiko akairudia na kunyakuwa kutoka pale kwenye kikalio chake.

“Hello…”

“Umepata barua elekezi juu ya zile fedha ulizoziita za umma?” ile sauti ikamwuliza.

“..Ndi-ndi-yo nime-pa-pata!”

“Ok, sasa fanya kama ilivyokuagiza,” ile sauti kaendelea kusema.

“…La-la-ki-n…”

“DO IT NOW, THERE IS NO LAKINI HAPA!” ile sauti ikafoka. Yule Gavana akakaa juu ya kiti chake huku mwili ukitiririkwa na jasho la kutosha, ingawaje kiyoyozi kilikuwa kikijitahidi kuifanya hewa ya humo ndani kuwa tulivu lakini sasa ilikuwa ni mithiri ya tanuru la kuokea mikate. Kila alichokishika kilikuwa cha moto kwake. Akaikamata ile barua kwa mara nyingine, akairudia kuisoma kwa makini na baadae akitafsiri kwa kiingereza ili aone kama maana zinafanana. Mwili wake ulikuwa ukikumbwa na hali mbili mara baridi na mara joto, kipindi Fulani alijipepea kwa gazeti na wakati mwingine akafunga vizuri tai yake, ilikuwa ni sintofahamu ndani ya kichwa chake. Muhuri wa moto uliogongwa na mtu aliyeonekana kuwa na nguvu ulionekana bila shida mwisho wa ile barua na nembo yake tukufu ilikuwa pale.

‘Sina cha kufanya lakini huu ni msala huu!’ akawaza na kuwazua kisha akainua simu yake na kupiga kwenda kwa mtu mwingine. Dakika moja tu alikuja kijana mmoja nadhifu na kupewa maagizo yale, naye bila ajizi maadam ‘mkubwa kasema’ akaenda zake na kufanya uhamisho wa fedha hizo.
Gavana alihisi kichwa kikimuuma, alihisi joto kali kwa mbali aliona kama mwili wake unapoteza nguvu, aliamua kutoka ofisini na kumwomba dereva wake kumfikisha hospitalini haraka kwa uchunguzi.

***
Baada ya zoezi hilo kukamilika watu wengi wakaingiziwa pesa mamilioni kwa mabilioni wakiwamo wafanyabiashara wakubwa, viongozi wa dini, wananchi wa kawaida, viongozi wa serikali na hata watoto wa vigogo waliyakwaa mapesa hayo. Taarifa hiyo iliastua wananchi na wabunge wanaopenda haki na hatima ya Taifa lao.

“Huu ni ufisadi mkubwa, haiwezekani,” mmoja alijisemea hilo.

“Yaani wamegawana!” mwingine alijikuta akitamka.

“Hii nchi inatisha, inabidi tufike wakati tumwogope Mungu!” huyu naye alijikuta akitamka baada ya kusoma habari hiyo gazetini.

“Mamaaaaa we! Hata huyu yumo, mijitu haina aibu,” mwingine alijikuta anapiga kelele.

SEHEMU FULANI FULANI – Siku nyingi tu zilizopita

“Sikiliza! We usiogope, nitatumia akaunti yako ile ya P.O.T Bank, nitaingiza kama Bilioni 19.99 hivi, wewe pale kuna kamisheni yako umesikia kijana!” Mzee Fulani alimwambia kijana mmoja katika ofisi yake mchana huo. Siku hiyo aliwaita watu kama saba hivi ambao alikuwa akiwaamini kuliko anavyojiamini mwenyewe.

“Lakini mzee…”

“Sikiliza wewe: Unataka pesa?”

“Pe-pe-pe-sssa? Ndi-yo, the, kwani kuna asiyependa pesa?” yyle kijana alijibu kwa kuweweseka.

“Sasa katika hizo pesa nitakupa shilingi Milioni mbili na nusu,”

“Hapo sawa! Hamna shida, akaunti yangu ndiyo hiyo hiyo mzee,”

Kila mmoja alijua ni jinsi gani atasafirisha pesa zake kutoka kwenye akaunti hiyo na kufikia akaunti yake binafsi. Hali hiyo wapenda uzalendo hawakuweza kuvumilia, walipigia kelele, wakatangaza maredioni, wakaandika magazetini, wananchi wakakasirika, wakapaza sauti zao dhidi ya dhukuma hiyo ya haki.
Kati ya watu walioibuka katika sakata hilo kama wapenda uzalendo alikuwa Mheshimiwa Msesema, Segeratumbo na Kibanio.

USIKU FULANI

“Pesa tumepata tena nyingi mno ambazo tutakula milele amina, lakini kuna vijitu viko vitatu vinataka kuleta tabu, hivi wanajua tumetoa jasho kiasi gani kutengeneza hii hela?” Mheshimiwa Matata akawauliza wenzake.

“Wajue wapi? Wanataka wapate sifa tu wale,”

“Dawa yao iko jikoni, tena haina haja ya kuwafanyia mbaya ila tuwashawishi tu nao wenyewe wataingia mtegoni,”

“Kwa ngapi?”

“Milioni mia mbili tu kila mmoja akamalize shida zake,” Matata akamaliza huku Nnandi na swahiba wao wakikata kilaji.

***

“Ngriiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii! Ngriiiiiiiiiiiiiiiiiiii!…” Msesema alishtuliwa na simu iliyo katika kijimeza chake pembeni tu mwa kitanda, akamruka mkewe na kushuka upande wa pilia akinua simu hiyo.

“Unaongea na Mheshimiwa mkubwa sana, Bwana Matata!”

“Ndiyo Comrade!”

“Najua una njaa kama walivyo wanaojiita Wazalendo wenzio, yeyo anayejiita mzalendo huyo ana njaa tu. Najua mbinu zako na wenzio Kibanio pamoja na Segeratumbo. Sasa kuna Milioni mia tisa; tatu kwa kila mmoja, kesho asubuhi kijana wangu atakuletea hundi…”

“Hapana! Siwezi kabisa, hiyo ni rushwa, na rushwa ni adui wa haki, mimi ni Mzalendo hata kama wazalendo ni wenye njaa basi ninyi mabwanyenye mistake wazalendo tufe njaa, tunazitaka pesa za umma zirudi zinufaishe wananchi. Tazama watoto wetu hawana vitabu vya ziada wala kiada, madawati ni shida, madawa hospitalini ni kitendawili, huduma za afya ni dhoofu, vifo vya akinja mama na watoto vinaongezeka ilhali ninyi mnahubiri kupungua kwa asilimia zake. Kuweni na huruma jamani, hizo ni pesa za umma na tutapigana mpaka mwisho. Kumbuka kwamba Mzalendo akichoka damu itaongea…” akakata simu.

“Pumbav sana, limekata simu, linajifanya linajua kumbe linaungua na jua, wacha wafe masikini,” Mheshimiwa Matata akawaambia wenzake.
Ushawishi kwa watu hao watatu ili wakubali kutoufuatilia mpango huo viligonga mwamba. Ndiyo kwanza wakawachochea na wao wakauwasha moto bungeni, mpaka ikapelekea Katibu wa Bunge na Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini kumuomba Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa akaunti hiyo. Ukaguzi huo ulilenga kufanya uchunguzi wa kina ambao ungetoa taarifa kamili yenye kuonesha hali halisi kuhusu miamala (transactions) kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa kuhusiana na ukaguzi huo.

MIEZI SITA BAADAE

Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ikauomba umma uvumilivu kwa kuwa ukaguzi huo ulichukua muda mrefu kutokana na hadidu zilizotolewa kuridhiwa na ofisi ya Bunge pamoja na ile ya Wizara ya Nishati na Madini.
Taarifa hiyo kwa umma ilielezea na kufafanua kuwa…
‘ Kwa kuwa Hadidu za Rejea pekee haziwezi kuonesha ukubwa wa kazi bali utekelezaji wa kazi yenyewe ndio unaoweza kutoa taswira halisi, ni vyema umma wa watanzania ukatambua kuwa Ukaguzi huu haujaweza kukamilika kwa kipindi kilichokadiriwa awali hivyo ukaguzi unaendelea kwa kuzingatia Hadidu za Rejea na kifungu cha 29 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008.’

Kwa kuwa wahenga walisema mvumilivu siku zote hula mbivu ndipo ilipofika wakati ambapo ukaguzi huo ulikamilika na hekaheka za huku na huko zikaanza. Watu matumbo yakawa moto, miguu haifanyi kazi wengine mahospitalini. Taarifa hiyo ya ukaguzi ilianisha majina ya watu waliojichotea mifedha hiyo na akaunti zote ziliainishwa wazi wazi.
Waheshimiwa; Msesema, Segeratumbo na Kibanio walizipata taarifa hizo kutokana na vyanzo vyao na kuahidi kutaja majina ambayo hayajaorodheshwa katika orodha hiyo.
“He! Kumbe kuna wengine hapa hawajorodheshwa, tobaaaah!”

7
OBOBO alijifungia ndani ya chumba chake akiwa anajiganga hapa na pale baada ya kupata kichapo kutoka kwa Amata. Mwanaharamu yule kaniumiza, alijisemea kwa sauti ya kusikia mwenyewe. Taya lake lilikuwa na maumivu makali ndipo alipogundu kuwa kapoteza jino moja. Lo! Nilikuwa simjui vizuri yule jamaa, inaonekana yuko vizuri sa kwenye martial arts, nitamtia mkononi, safari hii nitampa mapigo ya kifo, Obobo akajisemea huku akimaliza kujifunga ile clip bandeji katika mkono wake. Akiwa katika kazi hiyo simu yake ikaita, akaiangalia ilikuwa namba tupu isiyo na jina. Akainyakua mara moja na kuipokea baada ya kuona namba ile ni ya Tanzania.

“Hey! Hapa kuna mpango kutoka jeshi la polisi kumpata yule mwanamke aliyekuwa na Msesema ili afanyiwe mahojiano, nafikiri anaweza kutuharibia mpango wetu,” ile sauti kwenye simu ikamwambia Obobo ambaye aliitambua mara moja kuwa ni ya mteja wake.

“Nimekupata, nitalishughulikia mara moja,” akajibu na kukata simu. Akainuka kutoka pale alipoketi na kuuendea mkoba wake, akaufungua na kutoa bastola nyingine baada ya ile ya kwanza kupotelea kule kwa Amata. Hii ilikuwa kidogo sio ya zamani sana. Magnum 22, akaichukua na kuibusu kisha akachukua na kifaa chake cha kuzuia sauti, akaviweka mahala pake katika lile jaketi alilovaa, akachukua moustache wa bandia na kujibandika chini ya pua yake, miwani ya duara kwenye vioo vyake akaipachika machoni kisha akajitupia kofia kubwa yeusi ‘pama’ na kuingia zake mjini, busy day, akawaza.

Jua lilikwishafika Maghalibi, wamachinga walikuwa wakifungafunga bidhaa zao katika mitaa mbalimbali ya Dodoma tayari kurudi kwa wapenzi wao. Obobo alkatisha mitaa miwili mitatu kuelekea hospitali ya mkoa wa Dodoma, nikimmaliza huyu, namsaka Segeratumbo kazi imeisha, akajiwazia wakati akilikaribia lango la hospitali.

***

“Da yule jamaa ana mwili wa chuma asee,” Kamanda akamwambia Gina pindi tu alipoingi ndani ya kile chumba na kukuta kipo vululu vululu.

“Mmepambana muda mrefu sana ee?” Gina akauliza wakati akimganga Amata jeraha lake la mguuni.

“Hapan kidogo tu, ila lo!”

“Nini?”

“Madam kasema nimhakikishe nampata akiwa hai, mtihani mkubwa sana huo!” akamwambia Gina na wakati huo simu yake mfukoni ikaita. Alipoitazama ilijiandika OK, akaiinua na kuiweka sikioni mara moja.

“Nimepata taarifa kuwa Kamati ya Usalama ya Bunge inanza uchunguzi dhidi ya upotevu wa zile nyaraka,” Madam S alizungumza kwa upole.

“Nakusoma bibi…”

“Na uchunguzi wao unataka kuanzi kwa yule msichana Cheupe, polisi wanataka kumkamata kwa mahojiano ya awali, lakini hawajui pa kumpata,” Madam akaendelea.

“Nakusoma bibi…”

“Nimepata taarifa hiyo name kuonesha kuwa sisi hatupo katika sakata hilo nimeruhusu waendelee, sasa tumia akili yako kabla hawajatuaharibia kazi yetu,”

“Message received, work in progress…” kamanda akajibu.

“Waitin for process,” Madam akamalizia na kukata simu. Amata akakurupuka kutoka pale alipo na kusimama wima, akamtazama Gina kisha akaliendea kabati na kutungua fulana moja maridadi, jeans na raba zake zisizofanya kelele kwenye sakafu, akavuta mkoba wake na kuufungua akachukua bastola moja ndogo ‘Beretta’ akaipachika kwenye kijikoti chake, kamba, visu vidogo vidogo vine na silaha nyingine alizoamini kuwa zitamsaidia katika hili au lile.

“Vipi Kamanda!” Gina akashangaa

“Kuna hatari kubwa inataka kutokea, lazima nikamwondoshe Cheupe pale hospitalini. Jeshi la polisi limeanza uchunguzi wa hili sakata la upotevu wa nyaraka, na wanataka kumsaka Cheupe kwa mohjiano sasa wakimpata watatuharibia kazi na ni vipi kama adui yangu naye kapata hiyo taarifa?”

“Ili kupoteza ushahidi lazima atamuua Cheupe,” Gina akajibu.

“Basi kama ni hivo, twende tulkauwahi uhai wake,” kamanda alimwambia Gina na wakati huo alikuwa keishaukaribia mlango, Gina akawahi kutoka nay eye akaufunga nyuma yake. Walipofika kaunta akalielekea dirisha mpaka alipokaa mhudumu wa mapokezi.

“Samahani dada, kuna uharibifu umetokea kule chumbani, naomba utume timu yako ikathaminishe ili nilipe kabla sijaondoka,” alipomaliza tu kusema akaondoka zake lakini hatua tano mbele akasimama kama sekunde tatu hivi akarudi tena pale dirishani. Yule mwanadada mhudumu wa mapokezi akasimama kumsubiri kujua nini tena. Amata alifika dirishani na kutazama dhabibu zilizokuwa kwenye bakuli kubwa, akacukua moja na kutia kinywani kisha akaondoka zake.

Iliwachukua dakika kama tano hivi kufika katika hospitali hiyo, Gina alijifanya kuzubaa nje na Amata akaingia moja kwa moja mpaka kwa yule muuguzi aliyemwachia kazi.
Kashinde alikuwa ameketi katika kijiofisi kidogo akisoma gazeti la siku hiyo, akashtuka aliposikia hodi na kisha mlango ukasukumwa.

“Oh, umenishtua kaka!” akasema huku akinyanyuka.

“Vipi mgonjwa wetu?” akauliza Amata.

“Anaendelea poa, unataka kumwona?”

“Sio kumwona tu, nahitaji kumwondoa hapa haraka,” Kamanda akamjibu Kashinde huku tayari akiongoza njia kuelekea kwenye kile chumba walichomhifadhi.

“Hakuna aliyekuja kukusumbua?” akauliza.

“Wapo. Sema niliwakatalia ka ulivyonieleza,”

“Good!”

Amata alipoukaribia mlango wa kile chumba, akasita kidogo, akasimama.

“Vipi?” Kashinde akauliza.

Amata hakujibu badala yake, taratibu, akamsukuma nyuma Kashinde na kumpa ishara ya kurudi alikotoka huku mkono mmoja ukiwa tayari na bastola nje na ule wa pili ukarudi kuchukua kile kifaa cha kuzuia sauti na kukizungusha pale kwenye domo la bastola. Taratibu akauendea mlango wa kile chumba na kushika kitasa chake, alipojaribu kukikunja ili afungue, hakikukunjika.

“Mh!” akaguna na kujaribu tena, hakikutikisika kabisa, akarudi nyuma hatua tatu na kupiga kwa mguu wake mmoja ule mlango ukavunjika eneo la kitasa na kufunguka huku ukisukuma kiti kilichowekwa kukinga mlango huo usifunguliwe. Cheupe hakuwepo kitandani, kitanda kilikuwa tupu na mashuka yalikuwa yamesukwasukwa kando. Akanyata kwa mwendo wa paka awindaye panya. Matone manne ya damu katika shuka nyeupe za MSD yaliusisimua mwili wa Amata, alipotupa jicho mita mbili hivi ng’ambo alimuona Cheupe kalala kimya, huku linga ikiwa imemwangukia juu yake.

“Cheupe!” akaita na kumuwahi pale chini alipomgeuza, Cheupe alikuwa akiangalia tu bila kufumba macho huku kifuni mwake kukiwa na matundu mawili ya risasi. Amata aliinua shingo na kuangalia dirisha ndipo alipogundua kuwa limevunjwa kioo chake.

“Kashindeeeee!” akaita na sekunde hiyohiyo Kashinde alifika na wauguzi wengine, Amata alimwacha chini Cheupe na kuwahi dirishani, alilichungulia kushoto na kulia na kuona mtu akiishia kwenye kona.

“Shiiiiiit!” akang’aka na kuchumpa kwenye lile dirisha akatua chini na kuruka sarakasi iliyomsidia kukoswa na risasi tatu kutoka kwa Obobo, aliyejibana kwenye kona ya ukuta. Akakamata saa yake na kuizungusha mara mbili kisha akaiminya kitufe cha kati upande wa pembeni.

***
“Piiiiiip! Piiiip!” saa ya Gina ilitoa huo mlio huku ikimfinya mkono wake akajua kuna hatari, akajitoa pale getini alipokuwa akiongea na mlinzi na kuingia upande wa jengo la huduma ya dharura, akapitiliza na kutokea upande wa pili, ndipo alipomwona Amata akijiinua kwenye mchanga, alipogeuka upande wa pili alimwona yule mwanababa aliyevaa kofia kubwa jeusi.

“Freeeze!” alimpigia kelele huku tayari akiitoa bastola yake na kumfyatulia lakini hakuweza kumpata. Amata aliinuka na kuanza kumtimua kwa mbio za mchangani bila kelele ila bastola yake ilining’inia mkononi.
Obobo aliruka wigo wa michongoma kama anayeruka msingi wa nyumba na kutua upande wa pili, na wakati huohuo kamanda Amata aliruka sarakasi maridadi na kuupita wigo ule akatua upande wa pili na hapo alimshuhudia adui yake akiinua bastola kumlenga, akachumpa upande mwingine na zile risasi zikachimba kwenye mnazi. Obobo akaondoka eneo hilo kwa mbio, na Amata akainuka na kuanza kumtimua upya kabisa. Hatua kama mia moja hivi Obobo akasimama baada ya kukutana na ukuta mkubwa unaotenganisha nyumba za shirika la nyumba la taifa na zile za shirika la leri.

Amata hakujiuliza mara mbili, aliruka hewani na kutanguliza miguu yote miwili iliyoenda kutua kifuani kwa Obobo na kumpepesua mpaka chini. Obobo hakuchelewa akajiinua pamoja na kuwa na mwili mkubwa, akasimama wima na kutupa konde zito lililompata Amata sawia, naye akapoteza stamina na alipotaka kujiweka sawa aliuona mguu wa adui yake ukidhamiri kumchota kwa ngwara, akauwahi na kuruka juu ule mguu ukapita peke yake, alipotua chini akajiruvyema na goti lake kulikuja likatua katika kidefu cha Obobo. Akajaribu kujitutumua yule mjinga akakuta network inakata, akasimama kimapigano na kuweka mikono yake kwa mtindo wa mauaji. Amata naye akajiweka sawa, mapigo ya karate yasiyopungua ishirini na nne yalivurumishwa na Obobo, lakini mpaka pigo la mwisho lilimkuta Amata alkiwa kayakinga yote, na mgongo wake ulikuwa umetuna na mikono ikiwa imeweka alama ya x mbele ya kifua chake.

Obobo alipojaribu tena, alijikuta akichezea karate tatu za kifua na mbili zikatua usoni, kisha ngwala maridadi ikaichota miguu yake usawa wa magoti akajikuta anashuka na kupiga magoti udongoni. Amata alirusha teke akidhamiria kukiuka maagizo ya boss wake. Adui yake akawa makini kwa kuudaka ule mguu na kuuzungusha kwa nguvu, maumivu makali yalipita kwenye mifupa ya Amata, akawahi kujigeuza na kumfumua teke la upande wa pili shavuni na kuufanya mguu wake kuwa huru lakini alianguka vibaya.\
Obobo alivuta hatua mbila na kukanyaga ukuta wa nyumba kisha akajibenjua na kutua nje ya ule wigo, hakuchelewa mojamojakavuka majumba ya shirika la reli na kuliwahi treni lililokuwa likitoka stesheni kuelekea Singida kwa kuwa pale lilikuwa halina kasi akalidandia na kutokomea nalo.
Gina aliwasili eneo la mapambano wakati Obobo akipotelea, Lijaribu kufyatua risasi lakini ziliuchimba ukuta na kumkosa mshenzi yule padogo sana.

-“Mtoto wa Malaya wewe!” akatukana huku akiukamata ule ukuta na kujivuta juu, akamshuhudia Obobo akidandia treni na kutokomea.
Kamanda Amata alishuhudia ufunguo ukitoka katika mfuko wa suruali ya Obobo na kudondoka chini, hivyo alipoanguka alitambaa na kuuchukua akautia mfukoni.

“Pole Kamanda,”

“Usihofu!”

“Tax, mzee Tax!” kijana mmoja alimwambia Amata. Alipoinua sura yake akatabasamu kwa kumwona Scoba keishafika eneo lile, akaingia kwenye hiyo tax na wote wakaondoka eneo lile.

“Pole sana comrade,” Scoba alimwambia Kamanda Amata huku akichukua barabara ya kwenda Dar es salaam.

“Masikini Cheupe!” Amata alisikitika huku akiukunjakunja mguu wake.

‘Isanga Inn 17’ ule ufunguo ulikuwa umeandikwa hivyo kwa maandishi ya kuchoma kwenye kijiplastiki kidogo.

“Scoba, geuza gari,” Amata akatoa amri.

“Uelekeo wapi kamanda?” akauliza Scoba huku tayari akiwa amekwishawasha indiketa ya kushoto na kuiacha hiyo barabara ya Dar es salaam na kupita ofisi za CDA kama anakuja, Nyerere Square.

“Isanga, twende Isanga,” akamwambia Scoba naye bila ajaizi alitekeleza.

ISANGA INN
“Simama hapa!” akamwambia Scoba naye akaegesha gari kama mita mia moja kutoka katika hiyo hoteli, “Nipe dakika kumi na tano hivi, Gina linda mkia wangu,” akatoka na kuondoka. Sekunde ishirini zilimfikia Kamanda Amata kwenye sebule kubwa sana iliyo na viti vichache tu na watu wachache walikuwa wameketi wakijisomea magazeti. Hakuongea na mtu alipita kwenye ujia mrefu huku akisoma namba za vyumba hivyo.

“Kumi na saba!” akauona mlango na kuusoma kwa sauti ndogo. Akapachika ufunguo na kuuzungusha ukafungua, akasukuma mlango taratibu na kujikaribisha ndani kama kwake. Kitanda kikubwa kilionekana kama kimelaliwa muda si mrefu, vitu vilikuwa vimewekwa ovyo ovyo tu. Katika meza moja kulikuwa na mafaili kadhaa yamewekwa hapo, akaiendea na kuyapekua pekua hakuna lile analolitaka.

“Kayaweka wapi mshenzi huyu?” akajiuliza kwa sauti ndogo tu huku akiinua hapa na pale, “Sio kesi!” akasema na kuingiza mkono katika mfuko wa siri wa jaketi lake, akachomoa kitu kama kiberiti hivi, akakipachika chini ya meza kisha taratibu akajivuta kwenye kabati na kuangalia, hakuna jipya.
Akachomoa ile bastola ya kizamani ya Obobo aliyoiacha kule chumbani mwake, akaiweka mezani na risasi zake akazipanga pamoja nayo.

“Hii ni salamu yako, ukiiona ujue mwisho wako u karibu,” akajisemea kwa sauti kama anayeongea na mtu kaisha akaufungua mlango na kuondoka zake akiuacha ufunguo kwa ndani.

§§§§
Kamanda Amata alijiinamia, uso wake ulionesha huzuni hisiyojificha kwa kifo cha Cheupe, bado nilikuwa namhitaji kwa upelelezi, yule hayawani kamkatisha maisha, nitamtia mkononi, safari hii hatoweza kuniponyoka. Nimefanya makosa mara mbili lakini sio mara ya tatu, akawaza huku bado akiwa kajiinamia. Mkono laini ukamgusa begani.

“Kamanda!” Gina akaita kwa sauti ya upole.
Kamanda akageuka taratibu na kumtazama mrembo huyo.

“Basi ameshakufa,” Gina akamweleza huku akimvuta mkono na kumwingiza kwenye gari ambapo Scoba aliiondosha moja kwa moja mpaka katika ofisi yao ya siri ambayo Madam S alikuwa akiwasubiri.

“Karibuni!” akawakaribisha, nao wakaketi vitini lakini Amata bado alikuwa akisikitika sana, “Pole Amata najua lililotokea kule hospitali lakini ndiyo hivyo katuwahi, vipi umepata lolote?”

“Hapana, Madam, yule mshenzi sijui hata kaficha wapi zile faili, nimefika mpaka chumbani kwake sijaziona, lakini nipe saa moja au mbili nitajua kila kitu,” Amata akaeleza.

“Chiba alikuwa anajaribu kuyanasa mazungumzo yake lakini imekuwa ngumu sana, inaonekana jamaa anajua nini anatakiwa kufanya,” Madam alieleza.

“Usiwe na hofu, atakamatika tu, hawezi kuponyoka nchi hii. Lakini huyu bwana hawezi kuja kufanya kazi hii bila kuletwa na mtu, ina maana nyuma yake kuna watu waliomtuma, akina nani?” Amata akaonesha wazi dukuduku lake.

“Ndiyo na sasa nataka uchunguzi ufanyike ndani ya waheshimiwa wenyewe ili tujue kama kuna aliyemkodi huyu jamaa…”

“Siyo ‘kama kuna alaiyemkodi’, nani aliyemkodi, huyo ndiyo ni wa kushughulikia,” Amata almkatiza Madam S na kubadilisha kile alichokuwa akiongea. Mipango na mazungumzo ilifanyika na mitego yote ya kumnasa Obobo ilifanyika. Baada ya kikao hicho cha siri Amata aliondoka akiapa kwa Madam S kuwa siku hiyo hatolala mpaka aujue mwisho.

ITAENDELEA

SIMULIZI The Escrow Mission Episode 05

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment