SIMULIZI

Ep 4: The Lost Boys

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 4
SIMULIZI The Lost Boys – Ep 4

IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI

******************

Simulizi : The Lost Boys

Sehemu Ya Nne (4)

“Halafu kuna videmu pembeni vikapiga,jamani huyu kaka vipi? Mbona kama kubwa jinga,ha ha haaaa?”.Junior alizidi kuongeza kumnyong’onyeza Hans na kuendelea kuleta vicheko vya haja mule ndani hata kwa Suarez ambaye alikuwa wala hayupo katika mkumbo huo.

“Halafu pale Eve alifyonza,ulimwona Junii.Hili jamaa si lilijitupa ndani maji halafu likazama,basi demu alijifuta maji na kufyonza. Ha ha haaaa”.Fred alizidisha utani.

“Halafu likaona limemfundisha mtoto kuogelea,kumbe mtoto anajua kuogelea toka zamani kinoma”.Junior alizidi kulembesha yale maongezi huku Hans akiwa haamini yale anayoyasikia.

“Umeona eeh. Mimi si wajua mzee wa mahotelini,siku moja wakati tupo pale Ken, akaniomba twende kuogolea. Mimi nikamwambia siwezi,akasema basi twende nikamuone yeye.

Acha bwana,mtoto anazamia yule,halafu kuna muda anaibuka na kujitupa kama yule Dolphin. Sasa jamaa leo likajidai limemfundisha,ha ha haaaa. Umebumba jamaa yangu”.Fred naye walishamfundisha maneno na ujanja wa mdomoni. Yale mambo ya upole hakuwa nayo kama mwanzo.

Wakati wote Suarez alikuwa anacheka bila kuchangia chochote,ni kama hakuwepo katika yale maongezi,lakini alishindwa asimame upande gani kwa sababu wale wote ni rafiki zake,na wale wote walimkaribisha mara ya kwanza,na yeye ndiye aliyewaleta kwa Eve. Akashindwa hata kutetea bali kubaki kucheka tu!.

“Embu ona hapa mwanangu.Lione hili jamaa”.Junior aliigeuza “laptop” ikaelekea kwa Suarez ambapo ndipo na Hans alikuwepo.

Akacheza ile picha ambayo alihitaji Suarez aione. Hapo alionekana Hans akikimbia kwa kasi ya hatari na kujitupa ndani ya maji.

Suarez alicheka sana kwa sababu ilikuwa ni tendo moja la kuchekesha mno kama ungepata kulishuhudia.

“Kwa hiyo wanangu mkanirekodi pia? Si ndio eeh. Poa bwana. Mmeshinda kwa leo,ila bado hamjashinda hata kidogo”.Hans aliongea kwa kusikitika huku akikaa kitandani kwake.

“Na ukileta uboya tu!.Tunaisambaza hii muvi chuo chote. Tunaandika LITAIRA likiwa na MREMBO,na facebook tunaiweka,na wale marafiki zetu wote wa watsapp,wataipata. Si wajua kilichotokea kwa WAGUMU? Basi kaa ukijua ile ni kazi yangu mimi”.Aliongea Junior kumchimba mkwara Hans ambaye alishapoa kitambo.

Maneno mengi yaliyowatoka wakina Junior yalikuwa hayana ukweli. Eve alikuwa hajui kuogelea kweli,na siku ile Hans ndiye alimfanya aweze kufanya zoezi lile japo si sana.

Ila waliongea yale kama kumtoa Hans mchezoni kwa makusudi kwani maneno yale yangemfanya Hans kuona kama alikuwa anakejeriwa na Eve.

Kimya kikatawala huku kila mmoja akiwa anafanya yake chumbani mule. Ni Fred ndiye aliyeanzisha maongezi tena na safari hii ni baada ya meseji kuingia kwenye simu yake.

“Daah! Kabadilisha siku,eti twende Jumatatu usiku. Hili jamaa litakuwa limemchosha sana. Ila poa,mi zangu za kijentromeni,si kama litaira kujitupa kwenye maji kama litembo”.Maneno hayo yalimfanya Hans amwangalie Fred kwa jicho la ubaya lakini alishindwa cha kufanya zaidi ya kumeza mate na kuongea maneno yaliyodhihirisha kuna kisasi mbele.

“We boya sasa hivi umekuwa mjanja eeh. Sasa ngoja,tutakutana pale katikati. Nitakuonesha mimi ndiye Hans The Crazy”.Aliongea Hans na kuweka earphone zake za simu na kuanza kusikiliza kilichomo mule.

Hakusikia majibu yaliyojibiwa na Fred bali aliona njia sahihi ni kutangaza vita rasmi kati yake na wale rafiki zake.

Uzuri wa Fred alikuwa ni mtu wa kumpeleka Eve maeneo tulivu hasa mida ya usiku. Mahotelini, migahawani,sehemu za maonesho,ndipo Fred alipendelea. Hali hiyo ilimfanya asijulikane wapi ataenda siku hiyo.

************

EVE NA ALFRED.

Ilikuwa ni Jumatatu ya saa mbili za usiku kama saa ya Fred ilivyoonesha pale alipoiangalia wakati yupo katika Hotel moja maarufu jijini Dar es Salaam. Alikuwa kakaa mahali fulani ambapo angeweza kumwona yeyote atakayeingia.

Hakukaa sehemu hiyo labda amwone Eve jinsi atakavyoingia bali alikaa hivyo ili aweze kuwaona na wabaya wake ambao ni Junior na Hans.

Alitangulia kufika kwa sababu alijua umuhimu wa mwanaume kutoka na mwanamke ambaye anamuhitaji. Siku zote aliamini mwanaume rijali ni lazima afike wa kwanza eneo pangwa kati yake na mwanamke anayetoka naye.

Elimu hiyo aliipata kutoka vitabu mbalimbali vinavyotoa sifa za mwanaume rijali au gentleman kama wenzetu wa ng’ambo wanavyolitamka kwa Kiingereza.

Baada ya kutulia kwa saa moja tangu afike pale,alimuona Eve akiingia na mpokezi wa wageni wa Hoteli ile kubwa,alionekana akiongea na Eve na hapo yule mpokezi akamuonesha mahala alipo Fred. Fred naye alipoona alikuwa anaangaliwa yeye,akanyoosha mkono kuonesha kuwa yeye yupo pale.

Kwa mwendo wa madaha uliopambwa na tabasamu la haja usoni pake,mwanadada yule mrembo ambaye alifanya hata wale waliokuwamo katika hoteli ile kugeuka na kumwangalia yeye,alimfata Fred pale alipokuwepo. Naye Fred kabla ya mtoto hajafika,tayari alikuwa kasimama na kwa ajili ya kumpokea.

“Oooh,Malaika wangu. Unaonekana mrembo usiku huu”.Fred aliongea huku akimshika mkono wa Eve na kuubusu.

Fred alicheza kama alivyoelezwa na katika vitabu vingi kuhusu mwanaume rijali. Jambo alilojifunza kutoka katika kusoma kwake huko,ni kutomkumbatia mwanamke ambaye si mwanamke wako bado,bali afanye zoezi dogo tu! La kumshika mkono na kuubusu. Na Fred alifanya hivyo.

“Inaonekana nimekuweka eeh”.Eve aliuliza huku bado katabasamu.

“Si sana na pia ni haki yangu kukaa nikikusubiri wewe Malaika uliyeletwa duniani kwa ajili ya kutangaza injili njema juu ya mioyo yetu”.Fred aliongea huku akijionya kuwa hata kama mwanamke kakuweka muda mrefu,kamwe usiseme umeniweka sana na wala usiseme ndio nafika sasa hivi,bali taja muda wa kati. Yaani ule kati ya umeniweka sana na nimekuja sasa hivi.

Eve akazidi kutabasamu baada ya maneno yale na kama kawaida Fred akazidi kuonesha urijali wake kwa kumvutia kiti kwa nyuma Eve,naye Eve akakaa huku tabasamu likizidi kutanuka kuliko lile la mwanzo alilokuja nalo.

Bila kuchoshana na kama mwanaume yeyote alivyotakiwa kufanya,mhudumu alikuja pale na kuweka vinywaji huku akigawa karatasi maalumu kwa ajili ya kujichagulia chakula. Si kama muhudumu alikosea kuleta vinywaji,bali taarifa hiyo Fred alikuwa tayari kampa mapema tu!.

Eve alishindwa kuvumilia hisia zake za furaha na kujikuta akiuliza swali na tabasamu kuu likiupamba uso wake.

“Ina maana unafanya haya yote kwa ajili yangu Fred?”.Aliuliza Eve baada ya kuona kile kinywaji ndicho anakipendelea na kilikuwa na gharama kubwa sana kwenye ile hoteli.

“Malaika wangu. Siku ya kwanza kukuona nilijiuliza sana kichwani kwangu”.Fred aliongea huku akishika kile kinywaji na kuanza kukifungua kwa vidole vyake.

Ni kimywaji ambacho kipo kwenye chupa ya shampeni,chenyewe kilikuwa hakina kilevi bali hupendwa sana na wanawake japo kilikuwa na gharama kubwa. Fred akawa anakifungua huku anaweka maneno yake.

“Nilijiuliza juu yako. Ni nani huyu atazamaye kama alfajiri,mzuri kama mwezi,safi kama jua wa kutisha kama wenye bendera. Huo ni uzuri wako Malaika wangu,unatisha kwa uzuri wako kama kile kikosi cha bendera viatani. Kile kikirudi nyuma,basi wanajeshi wote hurudi nyuma,kikienda mbele basi jeshi zima huenda mbele’”.Fred aliongea maneno ya kwenye biblia katika kitabu cha wimbo ulio bora.

Sidhani kama Eve alifahamu kwani alikuwa ni mwenye tabasamu juu ya sifa zile. Wakati yote hayo yanaendelea,tayari alikuwa akamaliza kufungua kinywaji kile na kukimimina katika gilasi ambayo ililetwa kwaajili ya Eve.Baada ya kumimina,akaendelea kutema neno.

“Embu jiangalie Malaika wangu. Hatua zako malidadi kama za twiga,mapaja yako a mviringo ni kama johari. Sifa ziende kwa kazi ya mikono ya MUNGU.

Nani atashindwa kuingia gharama juu yako Malaika wangu. Kama nilivyokwambia mwanzo,umeleta taarifa nzuri kuja kwangu,nami nilipozisikia moyo uliruka juu kwa furaha kama yule mama aliyemwona Bikira Maria wakati anamimba ya YESU.

Huu mzuri Malaika wangu,na hustahili kufanyiwa chini ya haya. Kunywa kinywaji ukipendacho na chagua chakula ukionacho wewe waweza kukila na kufurahia huu mtoko wetu”.Fred alimaliza kuongea na kumkaribisha Eve ambaye alishindwa hata kusema neno juu ya maneno yale matamu kwenda kwake.

Akachukua gilasi ile yenye kinywaji na kuitia midomoni mwake na kumimina kiasi kidogo ambacho aliona kitapita vizuri kooni mwake bila kuleta kashi. Wakati huo Fred alikuwa bize akichagua chakula atakachokula.

Hakupenda kumwangalia Eve wakati anakunywa kwa sababu ya imani yake ya kuwa mwanaume rijali,huwa amchunguzi mwanamke anayemtoa out bali humpa uhuru wa kufanya chochote.

“Fred. Wewe unasoma sana vitabu vya dini,si ndio eeh”.Aliuliza Eve swali lililofanya Fred na kisha akajibu kwa kukubali kwa kichwa.

“Sasa kama ni hivyo basi na mimi nataka kukuuliza huko huko”.Aliongea Eve.

“Uliza tu Malaika wangu”.Fred alimpa nafasi Eve.

“Unaamini kuwa kuna mwisho wa dunia? Au unaamini kuwa kuna siku wote tutakufa na kufufuka tena na baadaye kukawa hakuna kifo,kama vitabu vya dini vinavyosema?”.Eve aliuliza swali ambalo kama mfuatiliaji dini huwezi kusema haamini hilo,lakini lilikuwa ni swali la kupima ulijari wa Fred.

Wanaume wengi wangejibu labda kwa kuuliza,hilo nalo swali. Lakini Fred alikuwa mtulivu na kusoma mawazo ya mwadada yule na alipopata akili yake inawaza nini,alifungua kinywa chake na kujibu.

“Naamini hilo Malaika wangu. Naamini ipo siku tutafufuka na kuonana tena. Na nitamshukuru sana MUNGU kama ataniweka na wewe pale tutakapopata ufufuko.

U mwenye bashasha na busara ambazo ni MUNGU pekee ndiye anayejua kwa nini kakupatia. Zawadi yoyote utaipata kama ukimuomba mwanaume. Hata ukisema uletewe kichwa cha Yohane Mbatizaji,utaletewa kutokana na umuhimu wako katika macho ya kila akuonaye.

Sidhani kama una moyo mgumu wa kutoelewa haya uyasikiayo. Ila najua una moyo laini kama sufi ya kondoo wa bwana. Hakuna atakayekataa kufungwa na nila yako,kwani nila yako ni laini na kila mmoja hawezi kukataa kufungwa nayo.

U Malaika uwezaye kuwa mzabibu nasi tukawa matawi yako.Kwa jinsi navyokuangalia machoni kwako,sidhani kama nitakosea kusema kama nikisema unaweza kuingia ndani ya moyo ya mtu na kuvuta kiti cha moyo huo,nawe ukakaa daima ndani yake.

Namaanisha mwanaume yeyote anaweza kukukabidhi moyo wake,akakupenda, akakuthamini na akakupa kila kitu kinachoitwa mapenzi. Niamini Malaika wangu”.Fred aliongea kiasi kwamba hata yule aliyekuja kuchukua menu ya chakula walichoagiza alikuwa katanua mdomo huku aamini yale aliyokuwa anayasikia.

“Vipi kaka,mbona umeganda?”.Fred alimuuliza yule jamaa mhudumu.

“Nimekuja kuchukua menu ya chakula kaka”.Alijibu.

“Poa.Hizi hapa”.Fred alizikusanya menu zote mbili na kumpatia.

Wakati anaondoka baada ya kupewa orodha ile ya chakula ambacho Fred na Eve waliweka tiki kwenye chakula wanachotaka,yule mhudumu aligeuka nyuma na kwa bahati nzuri alikutana na macho ya Fred.

Mhudumu alimwonesha dole gumba ambalo lilipokelewa kwa tabasamu dogo kutoka kwa Fred,na kisha mhudumu alititia ndani kwa ajili ya kuandaa huduma aliyoombwa.

“Yaani wewe unaongea kuliko hata unavyoonekana. Una maneno ambayo yanaweza kumfanya mtu ajiulize mara mia ni wapi umeyapata. Mh! Eti naweza kuwa mzabibu nanyi mkawa matawi,kwani mimi Yesu?Ha ha haaa”.Eve aliongea na kucheka kitu ambacho Fred alikipenda sana hasa baada ya kumuona mwanamke aliyembele yake anacheka kwa sababu yake.

“Wanasema ukicheka unaongeza siku za kuishi. Lakini naamini yule anayekufanya ucheke,anaongeza siku za kuishi mara mia zaidi yako.

Malaika wangu,usiku huu umeniongezea siku za kuishi katika maisha haya. Huu wa muhimu kwangu kuliko unavyodhani. Nimekufanya uongeze siku,nawe umeniongezea siku zaidi kuliko zile nilizokupa wewe. Nani kama wewe Malaika wangu,endelea kucheka nione meno yako meupe na ya kung’aa kama vazi la Malaika aliyemtokea Bikira Maria.

Endelea kucheka Malaika wangu”.Fred aliongea na kumfanya Eve atikise kicha kushoto na kulia kama anasikitika lakini alikuwa amejawa na tabasamu lililoonesha dhahiri alikuwa haamini anachosikia,au kafurahishwa na yale maneno.

“Yaani wewe. Dah! Basi bwana”.Aliongea Eve na kushindwa kumalizia kauli yake. Wakati huo mhudumu alionekana akija na sinia kubwa lililosheheni chakula walichoagiza.

Mhudumu alifika mahala pale na kisha akaweka chakula mezani.Zoezi lililofata baada ya hapo ni kuwanawisha wageni wale wenye maneno mengi ya kuvutia. Alipomaliza,aliwakaribisha naye akapotea eneo lile akiwaacha wale wawili wakijihudumia vyakula walivyoagiza.

“Unapenda kuku eee”.Fred alimuuliza Eve baada ya kuona Eve anajiwekea kuku kwenye sahani yake.

“Sana. Ni nyama moja baridi isiyo na madhara makubwa kama zilivyonyama za wanyama wengine”Alijibu Eve huku akifunua sahani fulani ambayo ndani yake ilisheheni tambi.

“Na wewe unapenda ugali kwa samaki ee”.Naye Eve alimtupia swali kwa Fred.

“Hiyo ndio sababu ya mimi kuwa imara zaidi ya chuma. Ila wewe yakupasa kula vitu kama hivyo ili ujengeke mwili na kuwa laini. Huu ugali tuachie sisi wafanya kazi ngumu”.Alijibu Fred huku anamega tonge la kwanza la ugali.

“Kwani sisi hatutakiwi kuwa imara?”.Eve alitupa swali lingine lililofanya Fred asile kwanza bali kujibu swali lile.

“Kwa mwanamke kama wewe,hupaswi kuwa imara sana kimwili bali kiakili.Nasema hayo kwa kuwa yule utakayekuwa naye,tayari atakuwa imara kwa ajili yako. Atafanya chochote kwa ajili yako,na hatokuwa tayari kukupoteza. Ni lazima awe imara na ni lazima ale ugali kwa wingi,kama mimi”.Fred aliongea na kunyanyua mkono wake wenye tonge na kuanza kula.

Eve naye alifanya vivyo hivyo lakini yeye alitumia uma na kisu ambacho hakina makali kwa ajili ya kukatia nyama ile ya kuku.

****

Walipomaliza kula,walikaa kidogo na Fred alilipia gharama za vyote vilivyotumika pale. Kilichofuata ni wao kuanza kurudi yalipo makazi yao.

“F mi nataka tutembee kwa miguu hadi chuo”.Aliongea Eve huku akisogea pembeni ya Eve na kuingiza mkono wake katikati ya ubavu na mkono wa Fred,yaani chini ya kwapa la Fred na kisha akabana mkono wake katika mkono wa Fred huku akiongeza deko la maneno yake kwa kulalia bega la kijana yule aliyekuwa kavalia suti ya kijivu iliyomkaa vizuri kama mwanamichezo wa nchi za nje anaenda kuchukua tunzo.

“Usiku huu Malaika wangu.Huogopi?”.Fred alimuuliza Eve wakati huo walishatoka nje ya hoteli ile nzuri ya nyota kuanzia tatu.

“Hivyo hivyo. Nikichoka kutembea ndio nitapanda gari”.Aliongea Eve kwa deko zaidi lililomwacha Fred bila neno bali kumsisimua na kumjaza kichwa.

“Sawa Malaika wangu. Mimi sitaki kukuhudhi. Twende sasa”.Fred alijibu na safari ya kwenda kwao ilianza.

Baada ya mwendo mfupi kidogo huku wakiwa wanapiga soga taratibu. Fred alianzisha tena maongezi yake matamu.

“Malaika wangu. Hivi unaamini kuwa mtu akifa roho yake inabaki kukulinda wewe?Namaanisha kama unandugu au yeyote anayekujali,akifa anakuachia ulinzi hapa duniani,unaamini?”.Fred alimuuliza Eve.

“Mh! Hiyo hapana kwa kweli F”.Eve alijibu na kuendelea kujikunyata kwa Fred ambapo kulimfanya Fred atoe koti lake la suti na kumfunika Eve aliyeonekana anahitaji joto japo mavazi aliyoyavaa yalikuwa hayapitishi baridi sana. Ila kwa kuwa Fred alikuwa anaigiza urijali,ilibidi kuwa hivyo.

“Asante F.Lakini kwani wewe unaamini?”.Alishukuru kwa lile koti,kisha akarudi katika mada.

“Ndio naamini. Embu angalia angani”.Eve akatazama angani wakati huo bado wanatembea njia ambayo ilikuwa na watu kiasi.

“Unaona nini?”.Fred aliuliza.

“Naona nyota na mwezi”.Eve akajibu.

“Wazungu wanasema nyota ni macho ya wale wakupendao,waliokujali wakiwa duniani na wanaopenda kukuona unafanikiwa. Macho haya yanakuangalia vizuri sana. Yaweza kuwa ya mabibi na mababu wa zamani sana. Bado wanataka kukuona ukifanikiwa. Na ndio maana kukiwa hakuna nyota,ni rahisi sana mambo mabaya kukupata”.Fred alijibu lakini hakuishia hapo.

“Hata mimi nikifa,nitakuwa nyota. Nitakulinda kwa kila ovu,nitamsimamisha kila ambaye atataka kukudhuru. Hiyo ni kwa sababu nakujali sana Malaika wangu. Kama ukiniambia nife kwa ajili hiyo,nitakufa ili nikulinde”. Fred alizidi kutiririka maneno ambayo kwa mtu wa kawaida mwanzoni anaweza asiyaamini,ila kwa jinsi yanavyoenda,anakuwa hana budi kuyaamini kwani ni maneno matamu ya kuweza kumfanya yeyote ayasikiaye,kujiona yupo juu kuliko mwanamke mwingine dunia hii.

“Sina usemi hadi hapo”.Eve alikubaliana na maneno yale.

“Tupande basi gari,mi mwenzako nasikia baridi”.Fred alitoa ombi ambalo lilipita bila pingamizi.

Wakaita usafiri binafsi ambao ni tax. Safari ya kwenda yalipo makazi yao,ikachukua nafasi.

*****

Baada ya nusu saa,tayari Eve alifika yalipo makazi yake. Fred alimuomba dereva amsubiri kidogo ili amsindikize mwanadada yule hadi getini.

Kama kawaida ya Eve,ili asipoteze urafiki na wale watu,alimpatia Fred busu moja dogo katika midomo yake na kumfanya Fred atabasamu kwa furaha huku akijiona kama anaelekea kushinda ligi ile.

“Kesho kutwa nitataka nitoke na wewe tena. Naomba hilo F”.Eve aliongea huku akimwangalia Fred machoni.

Unadhani Fred angekataa?Alijibu haraka kwa kukubali,na hapo Eve alimpatia koti lake na kufungua geti la makazi yake,kisha akaingia humo na kufunga geti lile na kumuacha Fred akiwa anatabasamu mwanana. Alishangilia kidogo na kugeuka na kuanza kulielekea gari lililowaleta hadi pale.

******

Dakika nyingine kumi na tano,Fred alikuwa kishafika anapoishi na kama kawaida aliingia kwa fujo huku akitabasamu,lakini yeye hakuwa muongeaji sana kama wakina Junior.

“Vipi kaka?Mbona hautupi matokea huko?”.Suarez Emmanuel alimuuliza Fred baada ya kuona haongei chochote kama wale wenzake.

“Gentleman huwa haadithii mambo yake”.Fred alijibu kwa kifupi huku anavua viatu vyake karibu na kabati lenye nguo zake.

“Utakuja kuongea tu,boya wewe.Ngoja uone”.Hans aliongea kwa sauti ya chini na iliyojaa kithirani. Halafu akageuka upande mwingine wa kitanda na kuendelea kusoma kitabu alichokuwa anakisoma.

Ni kama Fred hakuisikia sauti ya Hans,lakini aliisikia sema akaipuuzia kwa kuwa alijua ni utani tu.

“Subiri muone boya litakachokifanya keshokutwa,ha haa”.Fred alijibu mnong’ono wa Hans huku akipanda juu ya kitanda chake wakati huo Junior yeye alikuwa kapitiwa na usingizi muda mrefu.

Asubuhi,marafiki wale walienda darasani lakini Hans alibaki chumbani huku akisingizia anaumwa kidogo,hivyo hawezi kwenda kuhudhuria masomo ya siku ile.

Walipoondoka,Hans alitoa makorokoro yake baadhi na kuanza kuyachanganya. Alitumia saa moja kuchanganya na kujaribu kazi yake aone kama inafanya kazi.

Baada ya kuona mafanikio,alitabasamu kwa mbwembwe na kuitengenisha michanganyo ile ambayo ilikuwa ni unga mweusi na maji fulani ya njano.

Unga aliuweka kwenye kifuko kidogo cha nailoni na yale maji kiasi alifanya hivyo hivyo. Maji na unga ule vikiwa vimetenganishwa,havina madhara ila vikichanganywa pamoja,ndipo vinaweza kusababisha madhara. Hans alivitenganisha na kuvificha katika kabati lake akisubiri siku ya kuvitumia.

*******

Baada ya masomo ya siku nzima. Hatimaye marafiki wale watatu walirudi chumbani kwao na walimkuta Hans akiwa amelala fo fo fo jambo lililofanya aonekane kweli jamaa ni mgonjwa.

Hakuna aliyemsumbua bali kila mmoja alianza kufanya yake huku kichwa cha Fred kikiwa kinawaza zaidi siku ya kesho yake ambapo alitakiwa kwenda kukutana na Eve.

Masaa yakaenda na kupotea,hatimaye ikafika usiku ambapo wote kwa pamoja walitoka kuelekea sehemu wanapouza chakula. Wote walionekana wana furaha,hata Hans aliyekuwa mgonjwa,alikuwa karudi katika hali yake kiasi.

Baada ya kula na kufurahi kwa pamoja,walirudi chumbani kwao huku bado furaha ikiwatawala. Hakuna aliyejua mipango ya mwenzie,ila kila mmoja alikuwa anacheka huku akipanga yake moyoni.

Usiku ukahitimishwa kwa marafiki wale kulala huku kila mmoja akiwa anaota mambo yatakayokwenda kutokea kesho yake,hasa Hans na Fred.

********

Asubuhi ya kesho yake kila mmoja aliamka mwenye tabasamu katika uso wake,matabasamu ambayo yalikuwa yanaonesha walikuwa hawana matata katika siku ile na walikuwa wazima wa afya.

Kila mmoja alianza shughuli zake ndogondogo kabla hawajaenda kujisomea na baadaye kwenda kujipatia kifungua kinywa kabla hawajaingia vipindi vya mchana ambavyo vingewapeleka hadi mida fulani ya chakula cha mchana. Hiyo ndio ilikuwa ni ratiba yao ya kila siku na waliifata vyema.

Baada ya masomo ya siku nzima,ndipo walirudi wanapoishi huku Fred akiwa anamzuka wa kufa mtu na kuona muda kama hauendi,alikuwa anabwabwaja maneno mengi kama simu la mtoto mdogo lile ambalo ukibofya namba moja linaanza kulia hivi,ukibofya namba mbili linalia vile na ukiofya namba tatu na nyingine nyingi,hulia linavyojua lenyewe.

Isikupite Hii: Pumbazo – Ep 4

Basi Fred alikuwa hivyo ,kila hadithi alitaka kuwemo hadi wenzake wakawa wanakereka.

“Baba Paroko niaje?Mbona umechangamka kama kachumbari iliyomwagiwa pilipili na ndimu halafu inaliwa na mlevi?.”Aliuliza Suarez.

“Aaah!Sitaki kujichafua kwa kununa kwani leo washika mapembe wanaisoma namba.”Fred aliongea kwa nyodo na kumaliza na cheko moja ya kejeri na majigambo kiasi chake.

“Hapo ndipo ulipokosea. Leo lazima cheko igeuke kilio.”Aliongea Hans kwa sauti ya chini lakini iliyomfikia vema Fred.

“Ha ha haaaa,anadhani na mimi nitakuwa likifaru kujitupa kwenye mimaji hadi iruke ruke pembeni. I am Gentleman”.Aliongea Fred na kuzunguka kidogo kama anacheza muziki.

Wakati hayo yote yanaendelea,walikuwa katika barabara wakorudi maskani waishipo.

“Ha ha haaa,eti likifaru. Jitu likajirusha pwaa. Duuh! Ile sehemu ikawa kama imetupwa bomu la nyukilia.Majitu mingine bwana.”Hapo Junior naye aliongea kumchokoza Hans.

“Leo mtaona historia nyingne tu!. Si watu wanajidai wamejanjaruka wakati tumewajanjarua sisi hadi leo wanavalia suruali chini ya mkanda na wakati walikuja hapa,suruali wanafungia mkanda shingoni. Kudadeki zao.”Aliongea Hans kumpiga dongo Fred.

“Ha ha haaa.Acheni kunichekesha bwana. Suruali inafungiwa shingoni,imekuwa tai hiyo?.”Suarez alisaili kinafki.

“It doesn’t matter. Nachojua nimewapiga gepu wewe na zee la kunuka domo.”Fred alijibu mapigo ya Hans na kuendelea kucheza barabarani kwa furaha.

Walindelea kurumbana hadi wakafika wanapoishi ambapo kila mmoja alijitupa kitandani kwanza ili atoe mchoko kabla ya kuikaribisha jioni.

****

Saa kumi na mbili jioni,Fred alikuwa anajiweka tayari kwa ajili ya kwenda kukutana na kimwana Eve. Mtoto ambaye kabarikiwa kila sifa ya urembo wa sura hadi tabia bila kusahau uzuri wa umbo na miondoko ya madaha. Nani ambaye angesipodata mbele ya kimwana yule matata.

Akiwa tayari kishajiwekea mavazi yake mahala pasafi na salama baada ya kuyanyoosha,Fred alitoka nje kwa ajili ya kwenda kuoga,na wakati huo aliwaacha Junior,Suarez na Hans wakiwa bize na vitabu vyao pale kitandani.

Baada ya dakika tatu za Fred kutoka nje,Hans alinyanyuka toka kitandani kwake na kwenda katika kabati lake. Hakuna aliyejua nini kinaendelea na hakuna aliyemfatilia kwa sababu walijua kaenda kwa nia binafsi.

Alifungua kabati lake na kuchukua vile vifuko viwili vya plastiki,halafu akageuka nyuma kuangalia kama Sua na Junior wanaenda na kipindi.Alipoona wapo bize na mambo yao,akaenda kwenye suruali ya Fred aliyopanga kuvaa siku ile.

Alichofanya ni kuweka vile vinailoni viwili kwenye mfuko wa nyuma wa suruali ile ya Fred.Vinailoni vile ambavyo kimoja kilikuwa na unga na kingine majimaji,ndivyo viliaribu kabisa mtoko wa Fred.

Baada ya kuhakikisha kafanikiwa kufanya zoezi lake bila kushtukiwa,Hans alirudi kitandani kwake na kuendelea kujisomea kitabu alichokuwa kakianza.

Nusu saa baadae,aliingia Fred kwa furaha huku tauro likiwa kiunoni, na shati alilotoka nalo likiwa begani na wakati huo huo mdomo wake ulikuwa unatoa mluzi wa wimbo wa Happy ulioimbwa na Pharrell Williums. Na uzuri alikuwa anaweza kucheza,hilo nalo likawa kivutio kwa rafiki zake.

Lakini ilikuwa kivutio zaidi pale alipokuwa anaendelea kucheza na mara akalitoa tauro kiunoni na kubaki na boxer moja ndogondogo iliyombana vizuri sana.

Basi kwa mbwembwe nyingi akaanza kucheza huku anaimba kiwimbo chake ambacho kilimkaa sana kichwani,tangu asubuhi.

Hata yule aliyekuwa anakisasi naye ilimbidi acheke tu! Maana jamaa alivyokuwa anayarudi na kile kiboxer,waweza sema LMFAO.

Huku anaendelea kutoa burudani ya kucheza,Fred alianza kujipaka manukato mbalimbali katika mwili wake kwa ajili ya siku ile ya faraja kwake.

Baada ya kumaliza hayo,alichukua singlend nyeupe na shati la kijani ya apple alilokuwa kalitundika kwenye kabati lake,akavaa. Alipomaliza,akatinduwa suruali yake ya kijivu,na bila kuichunguza akatinga mwilini mwake na kuichomekea vizuri mwilini.

Akachukua kioo kidogo na kuanza kutana nywele zake kabla hajachukua koti lake la kijivu ambalo alilivaa na kukamilisha suti iliyokuwa imemtoa chicha balaa. Kwa jinsi ilivyokuwa imemkaa,waweza sema huyu kocha tena Morinho au Gadiola.Au msanii mkubwa wa Marekani kama Justin Timberlake au labda Christian Ronaldo akienda kuchukua tunzo ya mchezaji bora wa dunia.Hakika jamaa alipendeza,uongo dhambi.

“Kaka leo umevunja kabati halafu ufunguo umeumeza.”Aliongea Suarez kumsifia Fred.

“Kawaida yangu,unadhani mimi wa makaptula kama tembo mtoto?.”Alijibu Fred huku akitupa dongo dogo kwenda kwa Hans.

“Na leo lazima mtu aje analia hapa.”Aliongea Hans na kugeukia upande mwingine wa kitanda chake.

“Halii mtu. Subirini kuletewa wifi yenu humu.”Fred aliendelea kuleta nyodo zake.

“Basi kaka we nenda kwa maana umeshaanza shombo zako hapa.”Aliongea Junior baada ya maneno kuntu kutoka kwa Fred.

“Naweza nisiondoke na usinifanye kitu.Ila kwa kuwa natakiwa kuondoka ngoja kwa sasa niwaache. But,siwaachi hivihivi.”Fred akatoa simu yake kwenye kipochi kilichokuwa kitandani kwake na kubofya namba kadhaa.

“Nambie Malaika wangu.Furaha ya macho yangu,utamu wa akili yangu na neno takatifu la ulimi wangu.”Fred alibwabwaja baada ya simu kupokelewa.

“Mi mzima Malaika wangu.Upo wapi sasa hivi.”Alisaili Fred baada ya salamu yake kuitikiwa.

“Okey,basi nakuja sasa hivi na teksi kuja kukuchukua,si tayari ushajiandaa ee.”Fred akaendelea.

“Aaah,Malaika wangu,wewe ndiye uwezaye kumfukuza hata shetani mbaya wa kichwa changu. Kwa nini hujali thamani nayokupa ya kutembelea taksi bali kutaka kutembea kwa miguu?.”Aliposema maneno hayo ni kama alimwamsha Hans usingizini kwani alijikuta akitabasamu kwa shangwe.

“Sawa Malaika wangu,najua unataka ufurahie uwepo wangu. Basi tutatembea.”Fred alijibu simu upande wa pili na kukaa kimya kidogo kabla hajamaliza maongezi yake.

“Sawa Malaika wangu.Nitakuja hapo baada ya nusu saa.”Fred akakata simu.

“Sasa nyie wazee wa mapembe,baadae tutaonana. Mi naanza kwenda taratibu,sitaki papara. Natembea kwa miguu hadi kwake na kisha nampeleka mtoto hotel za maana kama kawaida yangu.”Alijisifu Fred na kutoka nje huku Suarez na Junior wakimtakia safari yenye mafanikio.

“Hata usiponi-wish me lucky,lazima nitafanikiwa tu. Tembo mtoto wee.”Alirudisha kichwa chake kwa kuchungulia,ndipo aliongea maneno hayo akayaelekeza kwa Hans.

“Mi sina tatizo na wewe,utarudi tu hapa. Tutaona nani mshindi.”Alijibu Hans kwa sauti ya ujasiri na tulivu.

“Tcio bebee.Subiri wifi yako anakuja.”Aliongea Fred na kufunga mlango wa chumba kile,ikiwa tayari ni saa moja na dakika kadhaa.

*****

Fred mida ya saa moja na dakika zake arobaini na tano,alikuwa nje ya geti la makazi anayoishi Eve Johaness,mwanamke aliyekonga nyoyo za wanachuo karibu wote pale Dar es Salaam.

Ni kweli alitembea kwa miguu ili tu,asiwahi kufika na kumkuta Eve bado hajajiandaa kwani waliahidiana wakutane saa mbili za usiku ule.

Baada ya kufika,alimpa taarifa mrembo wake wa muda kwa kutumia simu yake kuwa tayari yupo nje anamsubiri. Nasema ni mrembo wa muda kwa kuwa Eve alikuwa kama kiti cha basi,leo kakaliwa na huyu,kesho kakaliwa na mwingine.Kwa hiyo huwezi kumuita huyo ni mpenzi wako wa kudumu na mbaya zaidi watu wenyewe walikuwa hata saundi hawajazitema.

“Nimekuweka sana wangu wa ukweli”.Aliongea Eve baada ya kutoka nje na kumkuta Fred akiwa kaegamia mti mmojawapo pale nje.

“Hata YESU alisema atarudi,lakini hadi sasa bado tunamsubiri.Sembuse wewe binadamu mwenzangu uliyeniahidi baada ya dakika kadhaa utakuwa nami? Siwezi kukata tamaa kusubiri kwani kufanya hivyo itabidi kwanza nikate tamaa kumsubiri YESU ndipo nikate tamaa kwako.

Swali lako nalijibu kuwa,hujaniweka hata kidogo. Ni halali yangu kukusubiri hata hadi asubuhi kwani wewe ndiye Malaika wangu. Ulindae moyo wangu na hata kichwa changu chenye wingi wa hamu ya kukuona na kukujulia hali.”Aliongea Fred kiufasaha na kumuacha Eve akiwa katika tabasamu mwanana lililokuwa linazidi kumbanjua Fred mabandu ya magome yaliyo-moyoni mwake na kuuacha moyo huo kuwa mweupe na wenye upendo ulikothiri furaha na amani.

Wakati huo alishamsubiri Eve kwa dakika kama kumi na tano. Na kweli aliwekwa sana tu! Ila kwa kuwa ni mrembo,atafanya nini sasa. Ila angekuwa dume mwenzake,sijui kama angekubali kuwekwa vile.

“Mmmh! Mimi nilidhani nimekuweka bwana maana umekuja mapema na halafu nilikuwa bado hata sijaoga wala kuchagua cha kuvaa,si waona mavazi yangu ya leo?.”Eve alijitetea huku anajiangalia.

“Hayo mavazi ni zaidi ya wewe unavyodhani. Umetoka sana Malaika wangu. Ungekuwa nchi za wenzetu,ungepita kwenye RED KAPETI,ila huku kibongo bongo,utamezewa mate na marijali kuonesha kuwa umependeza.”Fred alimpa sifa dada yule na kumuacha hana neno bali meno yaliyopangana kiustadi mdomoni mwake kutokeza na kumfanya Fred amsifu MAULANA kimoyomoyo kwa kumuumba kiumbe yule ghafi katika peo za macho yake.

Eve japo alikuwa kajikataa kuwa mavazi aliyovaa hayakuwa rasmi,ila kiukweli alikuwa katoka vibaya mun

Gauni lake la refu la silva na lenye ming’aro kadhaa kwenye mikanda iliyopita mabegani pamoja na mmoja mpana kiunoni pake,ulimfanya Eve ang’ae sana usiku ule wa haja kwa watu wale wawili.

Huku chini ali-match na viatu vya rangi ileile ya silva na juu nywele zake alizibana na banio la damu ya mzee,rangi ambayo ilikuwa inaendana na kikoti kidogo alichokiegesha mwilini mwake kabla hajakivaa kabisa pale alipofika kwa Fred.

“Mmmh!Haya bwana,sina cha kusema juu ya hilo.”Eve alikata kinywa cha Fred kwa kukubaliana na maneno yake.

“Sasa nadhani twaweza kwenda Malaika wangu.”Fred aliongea huku akiingiza mkono wa kulia kwenye mkono wa kushoto wa Eve kama wafanyavyo maharusi au waalikwa wawili wa jinsia tofauti wanapoingia kwenye tafrija mojawapo kubwa waliyoitwa.

Ilikuwa ni tayari saa mbili na dakika kadhaa za usiku na ilionesha wazi Eve alikuwa si wa kupanda gari hata pale Fred alipomba wafanye hivyo. Haikujulikana kwa nini,ila Eve alisema anajiona yupo vizuri kifuraha kama watatembea kwa miguu hadi huko wanapoenda.

Dakika thelathini za mwendo wao wa taratibu na wa madaha,tayari walikuwa wameshafika eneo moja la wazi lakini lenye mgahawa mkubwa ambao siku kama ile,kulikuwa kuna watu wengi sana hadi wengine wanakosa sehemu za kukaa.

Kwa kuwa wakina Eve walichelewa kiasi chake,walikuta nafasi nyingine zipo wazi kwa wale wa mwanzo kuondoka.

Walichagua nafasi moja nzuri na yenye mwanga ili waonekane hasa kwa mavazi waliyovaa usiku ule. Yalihitaji sana mwanga ili yavutie zaidi. Lakini kama Fred angelijua kitachomtokea,sidhani kama angechagua kwenda kwenye mgahawa mkubwa kama ule,na kuchagua sehemu yenye mwanga kama pale.

Lakini yote yalibaki kuwa kama ningeli……,basi ningeli….. Yalibaki kuwa majuto tu!

*********

“Unapaonaje hapa Malaika wangu.”Fred alianzisha maongezi baada ya kukaa mahala panapostahili na kumsubiri mhudumu kwa ajili ya kuagiza wanachohitaji.

“Oooh Fred,it is fantastic.”Alijibu Eve huku akiutazama mgahawa ule juu na pembeni kama unauthaminisha.

“Mmh Malaika wangu.Mi mwenyewe najua Kiingereza lakini sipendi sana kukitumia nikiwa na wewe. Napenda tutumie Kiswahili zaidi,kwani tunakuwa huru kuelewana kuliko kutumia vingereza ambavyo havina maana sana katika maongezi yetu.”Alisahihisha Fred baada ya Eve kutumia lugha ya Kiingereza katika maongezi yao.

Ni kweli Fred hakuwahi kutumia lugha nyingine akiwa na Eve,hiyo pia inakuweka vizuri katika mahusiano yako. Si njema sana kuchanganya lugha pale unapokuwa na msichana ambaye unahitaji uwe naye katika mahusiano.

Hali ya kuchanganya lugha uwapo na msichana au mwanamke,inatengeneza maono tofauti katika kichwa cha mtu uliyenaye kwa wakati huo. Na zaidi utaonekana kama unadharau sana hasa pale mtu uliyenaye kumbe shule ilimpiga ngumi katika maisha yake na hajawahi kusomea lugha unayoitumia.

Kingine utatengeneza ile kauli ya kujifanya unajua sana lugha fulani kuliko lugha ya ulimi wa mama yako. Hisia kama hizo si nzuri kama zikitengenezwa kwenye kichwa cha mwanamke uanayemtaka.

“Mh!Hapo kweli,umeniambia jambo la maana.Mimi kama mwanafunzi wa uandishi wa habari wa nchi hii,sipaswi kutumia lugha kwa kuchanganya changanya hasa pale napoulizwa swali kwa lugha fulani na mimi najibu kwa lugha tofauti niliyoulizwa nayo. Hapo sibishi Fred wangu.”Aliongea Eve huku akiwa anatabasamu lisiloishiwa unyevunyevu unaosababisha kutokauka kwa tabasamu lile.

“Nashukuru Malaika wangu kwa kuelewa hilo.”Alishukuru Fred na wakati huo muhudumu nadhifu wa mgahawa ule alikuwa kaja na kuwapa menu ya chakula wafanye yao.

Baada ya dakika kadhaa,tayari chakula walichokuwa wameagiza kilishakuja mezani kwao.Kitendo bila kupoteza muda,Fred alijivuta kwa mbele ya kiti alichokalia huku kitendo kile kikiwa kama ndio kinamalizia ule mpasuko wa vile vinailoni viwili alivyokuwa kawaviweka Hans mfukoni mwa suruali ya Fred.

Kile kinailoni cha kwanza chenye maji,tayari kilishapasuka muda mchache baada ya Fred kujivuta vuta kwenye kiti chake.Na ule ubaridi wa kimiminika kile Fred aliuhisi sema aliona aibu kuinuka kwa kuwa angeonekana kama kajisaidia haja ndogo.

Sasa wakati anajivuta kwa ajili ya chakula,ndipo kile kinailoni chenye unga nacho kilipopasuka na kusababisha sasa ule unga kuchaganyika na kile kimiminika ambacho kilikuwa bado hakijakauka kabisa kwenye suruali ya Fred. Hapo ndipo balaa lilianzia.

Wakati Fred anaendelea kujilia chakula alichoagiza,mara alianza kuhisi umoto moto kwenye makalio yake. Mara ya kwanza alidhani labda ni kiti au kuna moto karibu yake,lakini alipoangalia kulikuwa hamna hali hiyo na wala kiti alichokalia kilikuwa hakina uwezo wa kupitisha joto alilolihisi.

Alitaka kusimama ili ajikague lakini aliona aibu kutokana na ule umajimaji uliokuwa katika suruali yake.Ikabidi avumilie lakini uvumilivu ule ulikuwa kama unazidi kuchochea hali ya joto kuongezeka pale alipokalia.

Taratibu Fred alianza kuona chakula kichungu na kiti kikawa kama kina upupu kwa jinsi alivyokuwa anasota kwa kwenda mbele huku makalio yake yakiwa msaada mkubwa wa kufanya hayo yote. Lakini kama angejua,angesipoendelea kufanya vile,kwani joto lilizidi maradufu ya pale mwanzo.

Masikini Baba Paroko au Mzee wa Upako,uso ukambadilika ukawa kama kasikia habari mbaya eidha ya msiba au mlipuko wa mabomu kama yale ya Mbagala.

“Vipi Fred wangu,mbona amani hamna?.”Aliuliza Eve baada ya kuona uso wa Fred umekosa amani.

“Hamna Malaika wangu,sema najihisi vibaya kidogo.”Fred aliongea huku akilazimisha tabasamu lakini hali ya makalio yake,alikuwa anaijua yeye.

“Tumbo linauma?.”Eve aliendelea kuuliza maswali kutokana na muonekano aliokuwa nao Fred. Hakika alipaswa kuuliza swali la namna ile kwa maana uso ulikuwa unakunjwa na kukunjuka kama anajisaidia kweli uwani.

“Daah! Eve nakufa.”Fred aliongea kwa sauti ya chini lakini iliyojaa uchungu mkubwa wakati anaitoa.

Mwanamke wa shoka,Eve alijua mambo yameharibika kweli,hadi kaitwa jina lake halisi na mtu ambaye hajawahi kumuita hivyo.Kweli jamaa alizidiwa nusura ya kufa.

Lakini aibu yake ndio ilimponza kwani aliona aibu kunyanyuka licha ya maumivu yaliyikuwa yamamsurubu.

Eve alinyanyuka na kwenda hadi kwa Fred alipokuwa amekaa na kumshika bega huku akijaribu kumnyanyua kichwa alichokuwa kakilaza juu ya meza.

“Fred vipi?.”Eve aliuliza.

“Naungua.”Fred naye alijibu huku akionesha wazi anaemia kwa kuungua.

“Wapi sasa.”Eve naye akawa anasaili kwa makini akifata vitendo vya Fred.

Fred hakuwa na jinsi tena kwani hali ilikuwa mbaya sana kwake. Akamuonesha pale alipokuwa amekalia kuwa ndipo panamuunguza.

Eve kwa haraka alimuomba anyanyuke bila kujua hali ambayo ingetokea baada ya Fred kunyanyuka.

Fred kwa shida na uvumilivu uliomshinda,alianza kunyanyuka taratibu na wakati huo umati mkubwa ulikuwa unaangalia ile filamu japo walikuwa hawaelewi ni nini kinaendelea.

Fred akanyanyuka na kusimama wima. Dah! Kilichoonekana ni zaidi ya wengi walivyodhani.

Ile suruali aliyokuwa kaivaa ilikuwa kama karatasi lililoungua,na hatari zaidi ni pale Eve alipojaribu kuikung’uta kwa nyuma ile suruali.

Ni majivu pekee ndiyo yaliweza kumwagika pale suruali ilivyokung’utwa.Na kibaya zaidi ule mchanganyiko wa Hans uliweza kula nguo ya nje hadi boxer la Fred kwa sehemu kubwa sana na kufanya hata makalio ya Fred kuonekana.

Ilikuwa ni ahueni kwa Fred kwani maumivu ya kuungua yalipungua lakini shughuli ilibaki kwa wale waliokuwa wanashuhudia lile tukio. Wengi wao walicheka sana tena sana.

Fred aliona jambo la msingi ni kufunga koti lake kiunoni ili kuficha ile hali yake. Na baada ya hapo alitoka mahala pale haraka na kwenda mahala kumsubiria Eve ambaye naye chakula kilikuwa kichungu japo alikilipia kwa haraka.

Baada ya kukilipia chakula kile,Eve alitoka kwa kasi kumuwahi Fred ambaye alikuwa hajielewi elewi ni nini kimemtokea kwa muda mfupi ule aliokutana na Eve.

Huku nyuma baada Eve kuondoka,wahudumu wa pale walienda kwenye meza waliyokuwa wamekaa wakina Fred na kutaka kutoa vyombo lakini bila kutegemea Hans na Junior walifika kwenye meza ile na kukataza ule msosi kutolewa.

Hans na Junior walikuwa ni watu ambao hawana aibu kabisa.Hivyo wale wahudumu walipotaka kubisha,wakina Hans walianza maneno ya kejeri yaliyowafanya wale wahudumu wawili kuondoka kwa aibu.

“Yaone kwanza.Kumbe kazi yao kula vyakula wanavyoacha wateja,leo mmenoa.Tunakichukua na kusepa nacho.Hayooo,shutuuu!.”Maneno yalimtoka Hans baada ya wale wahudumu kukubali yaishe na kuanza kuondoka eneo lile.

Hans na Junior walifanya kazi ya haraka sana kwa kuchukua kile chakula na kukimwagia kwenye mifuko misafi na baada ya hapo,walikimbilia bodaboda walizokuja nazo na kupotea eneo lile wakiwaacha baadhi ya wateja hoi kwa vicheko na wengine kukarahika na vile vitendo visivyo na aibu kutoka kwa watu wazima kama wale wakina Hans.

*****

Kwa upande wa Eve na Fred,wenyewe walichukua usafiri binafsi wa taksi na kuwapeleka katika makazi yao.

Ndani ya taksi ile,Fred alikuwa kachanganyikiwa kwa hali iliyomtokea na aliona aibu sana kumuangalia Eve. Hata pale Eve alipofika makazi yake,Fred hakuthubutu kumwangalia usoni bali alimuaga kwa ishara ya mkono tu,bila kusema.

Safari ya kupelekwa makazi yake yalipo,ikaanza na hapo ndipo amani ya moyo ilipomrudia na kuanza kufikiria filamu nzima ya kilichomtokea.

“Hans.”Aliongea Fred baada ya kufikiria kidogo.

“Huyu ni Hans mjinga yule. Yaani Hans kanifanyia hivi kweli?.”Fred aliongea kwa sauti na kumfanya dereva wa taksi aliyopanda kumtazama kwa makini kwa kupitia kioo cha dereva kile cha juu.Maana alidhani mteja wake anaweza kuwa mwehu na kusababisha mambo mengine ndani ya gari.

“Kwa hiyo kanifanyia hivi kunikomoa au kisasi? Yaani huyu Hans kweli ananiabisha mimi? Mimi!!? Kabisa mbele ya umati wa watu, watu zaidi ya mia wameona makalio yangu. Kweli kabisa Hans unaniabisha mbele ya Eve? You will pay for this.”Fred aliongea kwa uchungu lakini yule dereva wala hakuingilia bali kuwa makini tu!Mtu wake asimkabe kama atapandisha ukichaa wake.

Baada ya dakika kadhaa,hatimaye taksi ilifika yalipomakazi yake. Fred akashuka na kumlipa yule dereva ujira wake kisha huku akiwa na koti lake kiunoni kama mtoto wa shule ya msingi,alianza kuelekea kilipochumba anachoishi na wenzake.

Alipofika,alifungua mlango na kuwasha taa. Aliwaona rafiki zake wote wakiwa wamelala na wengine kama Hans kukoroma kabisa

Alichofanya Fred ni kuanza kuwaamsha wenzake kwa kuwatingisha na kuwaita kwa kuwapigia kelele.

“Oya nini bwana?Tunakatishana stimu.”Hans aliongea huku akifikicha macho yake baada ya kuamshwa.

“Pumbavu wewe. Wewe wa kunifanyia vile Hans?.”Fred aliongea kwa hasira huku akimuangalia Hans kwa jicho la kummeza mtu.

“Nimefanyaje Baba Paroko?.”Hans aliongea kama kweli hajui kitu.

“Linajifanya halijui boya hili,umeliona linajifanya eti halijui lilichofanya.”Fred alizidi kuongea na safari hii alikuwa anaongea huku anawageukia kwa zamu wakina Junior na Suarez.

“Kwani kafanyaje Mzee wa Upako?Mbona hatukuelewi? Halafu mbona koti umelifunga kiunoni? Au ndio umemvalia kibwebwe mwanaume mwenzako toka huko ulipotoka.”Aliongea Suarez na kumfanya Hans uvumilivu wa kucheka kumshinda.

“Si unaona hili boya linacheka?Linajua lilichofanya.”Fred aliongea kwa jazba na kwa sauti ya juu.

“Kafanyaje kaka?Mbona hufunguki?.”King Junior Nickson naye aliuliza.

Mara Fred akafungua lile koti lake na kulitoa kisha akawageukiwa kwa kuwapa mgongo Hans na Suarez waliokuwa wamelala upande mmoja.

“Hapa umeridhika nini boya wewe?Nakuuliza umeridhika nini.”Ee bwana suruali yake ilikuwa imeungua tokea pale karibu na mkanda hadi huku chini karibu na magoti. Hakika ilikuwa ni kituko cha mwaka au cha siku ile maana hata makalio yake yalikuwa yanaonekana wazi bila kificho. Fred alikuwa kaaibika sana kwa kweli.

“Nakuuliza umefaidika nini hapa?.”Fred alizidi kuuliza huku bado kawapa mgongo Hans na Suarez.

Wakati anafanya hayo yote,Emmanuel Suarez,yeye alikuwa katika taharuki kubwa kutokana na kile alichokuwa anakitazama.

Kinyume na hapo,kwa upande Hassan Jenge,yeye alikuwa kaishiwa nguvu kwa sababu ya kucheka kicheko ambacho kilikuwa kimevutwa kwa muda mrefu na kikakauka kabisa. Ni kama mtoto mdogo pale anapoumia sana,kuna kilio fulani anakivuta hadi kinakauka,pale akiamua kukitoa nje sasa,ni kama filimbi.

Sasa na kwa Hans ilikuwa hivyo,alikivuta kile kicheko kwa ndani na pale alipokitoa nje,ama kweli kilikuwa kicheko cha nguvu.

“Umeona boya hili linacheka.”Fred aligeuka na kuanza kumfata Hans pale alipo kwa hasira. Wakati anafanya hivyo,ndipo pia alipompa fursa Junior na yeye kujionea majanga yaliyokea katika suruali ya rafiki yake.

Naye bila kusita akaangua kicheko cha nguvu.

Fred alimfata Hans pale kitandani na kuanza kumsukuma sukuma wakati huo Hans alikuwa anagalagala kitandani hana mbavu.

“Nakwambia wewe boya leo utaniambia nimekukosea nini.”Fred aliongea kwa hasira huku anamvuta Hans aliyekuwa hajiwezi kwa kicheko.

Wakati anafanya hayo ya kuhangaika kumvuta Hans pale kitandani,huku nyuma Junior alikuwa anazidi kuwa hoi kila alipoangalia kile kilichokuwa kinatokea nyuma ya suruali ya Hans. Hakuwa mvumilivu kwa kubana kicheko bali kukiachia kwa nguvu zake zote.

“We boya nakwambia hapa utashuka mwenyewe, boya wewe.”Fred aliendelea kumvuta Hans aliyekuwa kalegea kwa kicheko.

Hali hiyo ya Fred kumvuta Hans iliendelea kwa muda wa dakika zisizopungua mbili na zilikwama pale Fred alipochana fulana iliyokatwa mikono,mali ya Hans.

“Baba Paroko umenichania Tisheti langu kwa sababu ya ujinga wako,si ndio eeh.”Hans aliongea huku kakunja uso kuonesha kachukizwa na kile kitendo.

“Nakwambia we boya leo nakuchania hadi boxer lako. Utanieleza nimekufanya nini.”Fred aliendelea kumvuta Hans pale kitandani bila kujali kama kishaifanyia unyambirisi fulana ya Hans.

“Kwani Fred ilikuwaje kaka hadi ikatokea hayo yote? Mbona unamvuta tu jamaa kama alikuwa kwenye mambo yenu?.”Suarez alimuuliza Fred baada ya kuona zogo linazidi kuwa kubwa.

“Labda unisaidie kuuliza wewe kaka maana hadi nachaniwa shati hapa bila kosa.”Hans alijibu huku akijeweka mbali na Fred kwa kujisukumia ukutani kabisa mwa kitanda chake.

“Unajua nini Sua (Shua),huyu jamaa kaniwekea makemiko kwenye mifuko ya suruali yangu. Sasa nimefika pale tulipopanga kufika,tukakaa kwenye viti,mara nikaanza kuungua………”Fred hakumalizia Suarez anayehadithiwa akamkata ulimi.

“Ulifika mlipopanga,ilikuwa wapi? Mbona unaongea mafumbo? Kama ni kwenye moto ndipo mlipofikia,sasa kwa nini usiungue?.”Suarez aliongea na kumfanya Hans aanze kucheka tena.

“Wewe Sua vipi? Gentleman ahadithii mambo yake.Au umesahau?.”Junior aliongea huku akiwa naye anacheka balaa.

“Umeona ee Junior. Gentleman ahadithii ishu zake hata kidogo,ha ha haaaa. Unaleta mambo ya kwenye video hapa.”Hans aliongea huku akiwa anazidi kujisogeza mbali na Fred aliyekuwa kajaa gesi ya hasira nusura ya kupasuka.

“Ha ha haaaaa, Think Like A lady…..”Junior aliongea na kumuoneshea kidole Hans amalizie ile sentensi.

“Act Like A Man…. Ha ha ha haaa,jamaa alikuwa anajidai Dremer.”Hans naye alimalizia sentensi ile huku akimfananisha Fred na Dremer,jamaa mmojawapo aliyeigiza filamu ya Think like a lady,Act like a man. Filamu ambayo Fred alikuwa anaingalia sana na kuigiza vitendo vya mule kwa Eve.

“Embu acheni washikaji. Mwanangu Fred endelea ili tujue kama ni kweli au si kweli,ikibidi Eve aitwe na aambiwe hii ishu.”Suarez aliongea akimwambia Fred aliyekuwa kasimama katikati ya chumba kama anawanga.

“Mwanangu nilienda na mtoto hotelini……”Kabla hajamaliza Junior akadakia tena.

“Hotelini wapi? Pale mgahawani bwana.”Junior akaropoka.

“Kumbe na wewe boya unahusika,Junii na wewe unahusika kweli kwenye hili? Aisee kweli mlikamia”.Fred aliongea kwa uchungu hadi Suarez ilim-bidi ainuke na kushuka kule juu anapolala na kumkalisha kwenye kiti kimojawapo wanachosomea mule ndani.

“Sisi tulienda kununua msosi ndio tukaona picha zima,wala mimi sijui kilichokuwa kinaendelea. Eti Sua hatujakuaga kuwa tunaenda ule mgahawa kuchukua chakula?.”Junior alijitetea.

“Waliniaga mwanangu,na wala mi mwenyewe sijui kama ulikuwa umeenda kule.”Suarez alimpunguza munkari Fred ulioanza kujaa juu ya Junior.

“Aaag,kwanza mmeongea kuhusu chakula,mimi nimeshikwa na njaa ghafla.”Hans alinyanyuka na kufuata kabati lake ambapo alilifungua na kuibuka na sinia moja kubwa kiasi.Akaliweka juu ya meza ya kusomea iliyokaribu kabisa na alipokaa Fred.

Baada ya zoezi hilo dogo la kuweka sinia juu ya meza,akapekua tena kwenye kabati lake na kuchomoa mfuko mweusi uliokuwa umenona kwa nje kutokana na chakula cha ndani kuwa na mafuta sana.

Akafungua mfuko ule na kumwagia kilichomo kwenye sinia lilipomezani.

Ghafla hali ya chumba kile ilibadilika na kupambwa na harufu nzuri ya chakula kile kilichowekwa kwenye sinia.

Lakini hali pia ilim-badilika Fred na kuwa ya taharuki zaidi. Midomo ilim-baki wazi na macho yakiwa yamekodelea kile chakula hali ambayo baadaye ilizidi kubadilika kwa midomo kutaka kuongea lakini ilishindwa na kubaki vidole kuoneshea kile chakura kilicho-mezani,ungemuona ungesema huyu jamaa ni bubu.

Hali hiyo haikumfanya Hans kujichukulia paja na kuanza kulitafuna kwa uchu. Hapo hapo na Junior aliinuka toka kwenye kitanda chake cha chini na kwenda kujichukulia kilichopo kwenye sinia lile la Hans.

“Nimekitolea jasho hiki.Kupambana na wale wahudumu hadi kukipata wadhani jambo dogo lile.”Junior aliongea huku akishika mgongo wa kuku na kuanza ku-usosomola.

“Fred vipi kaka,mboa hivyo?.”Suarez alimuuliza Fred baada ya kumuona hana la kuongea bali kushikwa na kigugumizi.

“Chakula chetu,mimi na Eve.”Fred aliongea huku machozi kama yanataka kumtoka.

“Sasa nyie mliacha chakula chote hiki,nyie vipi?Na bahati yenu vinywaji hamkununua.”Hans hakuwa nyuma kuongea japo alikuwa anabugia tambi kwenye kinywa chake.

Fred hakuvumilia hali ile. Yaani kuaibika, ka-aibika, chakula kimelipiwa bila kuliwa. Halafu mbaya zaidi wanao-kila ndio hao waliomuaibisha. Haikuwezekana kukubalika kwenye kichwa cha Fred.

Hali hiyo ya kutovumilia,ilimfanya Fred akwapue lile sinia kwenye vidole vilivyokuwa vinaendela kufakamia ule msosi wa ghari,aliougharamia mpenzi wake kwaajili yake.

“Pumbavu zenu,sasa ole wake boya asogee.”Fred aliongea huku anaelekea pembeni na sinia lile la chakula kwa lengo la kukila peke yake.

“Mwanangu na sisi tumeweka chakula chetu humo,kwani chenu kilikuwa kingi hivyo.”Junior aliongea huku akimfata Fred kule ukutani alipoenda.

“Nitakumwagia hizi tambi,kuku na haya makachumbali usoni na hutonifanya kitu,nisogelee sasa.”Baba Paroko aligeuka gaidi kwelikweli.

Junior ilibidi harudi nyuma hasa alipofikiria muwasho wa ile kachumbali mdomoni,sasa anaambiwa atamwagiwa usoni.

Fred akawa m-babe mule ndani. Akachukua paja moja la kuku na kumrushia Suarez,naye Suarez akalidaka na kulitia mdomoni kwake.

Fred akageukia ukutani na wakati huohuo akawapa wakina Hans mgongo na kuwafanya waone ile suruali ilivyokuwa imeharibika.Kicheko kikaanza kwa kasi ya ajabu lakini Fred hakujali zaidi ya kuendelea kula huku akicheza taratibu na kukata kiuno kwa mbali. Hasira zikamuisha kihivyo maana angeendelea kuwa na hasira hizo,ingekuwa hasara kwake. Cha msingi aliona bora asahau,lakini si kwamba alisahau kabisa.

*****

Kesho yake waliamka wenye furaha kama jana yake usiku kulikuwa hakujatokea kitu. Walikuwa ni watu wenye amani kupitiliza huku ikionekana wazi hakuna kisasi baina yao.

Lakini ajuaye moyo wa mwanadamu una nini,ni yeye mwenyewe binadamu pamoja na MUNGU wake.

Moyo wa Fred ulikuwa haujafurahia kabisa kile kitendo alichofanyiwa na Hans. Pia alikuwa kampatia sana hasira Junior kwa kuwa mshirika wa Hans. Hayo yote aliyaweka moyoni na kuyapangia mkakati kabambe wa kuyalipa.

Bila wale jamaa zake kujua yaliyo-moyoni mwake.Fred alionesha mwenye amani na furaha kila wakati huku akiwa mstari wa mbele kukumbushia kilichomtokea jana.

****

Siku nne mbele toka siku ya tukio la Fred,ilikuwa ni zamu ya Junior kukutana na Eve. Fred alifahamu hilo,hivyo akaanza kutafuta njia za kulipa kisasi kwa alichofanyiwa na wale rafiki zake.

Aliangaika sana na mwisho wake aliona ni bora aende kwa wagumu kuomba msaada kwani Junior alionekana ni mtu makini sana kwenye mambo yake.

Haikuwa rahisi kwa Junior kuacha nguo zake hovyo,wala kabati lake. Kifupi alizidisha umakini hasa kila alipofikiria tukio lililomtokea Fred. Sasa Alfred aliamua kuomba msaada kwa Wagumu,walewale aliowahi kuwaabisha walipofika chuoni kwa mara ya kwanza. Ndio walewale wakina Moi Shabala,Kamanda wao Ban Diho na Sunday Magembe.

“Kwa hiyo mkuu unatakaje sasa.”Kamanda wa Wagumu,Ban Diho alimuuliza Fred baada ya Fred kutoa mkasa mzima ulimkuta.

“Nataka boya naye aibike mbele ya mtoto kama mimi nilivyoaibika.”Fred aliongea kwa hamasa juu ya nia yake

“Basi usijali. Cha msingi taarifa umetupa,sisi tutapiga kazi kama kawaida ila yapasa uache kitu hapa,hatupigi kazi bila mshiko,si wajua sisi makamanda.”Ban aliongea kwa makini huku akimwangalia usoni Fred aliyewafuata chumbani kwao.

“Hilo usijali,nyie niambieni kiasi mnachotaka.”Fred alizidi kujiingiza kwenye dhamira yake ya kisasi.

Kwa kuwa wale jamaa walikuwa na kisasi na lile kundi la akina Hans,waliamua kuutumia mwanya huo kulipa walichowahi kufanyiwa.

“Hapo utaacha elfu hamsini mwanangu.”Ban alimjibu Fred na kumuacha kinywa wazi.

“Kaka mbona kitu kidogo sana lakini umekaza hivyo. Au unaenda kuua? Sitaki mauaji,nataka aibike tu!.”Fred alishindwa kuzuia hisia zake juu ya ile bei aliyotajiwa na Ban.

“Hafi mtu hapa jembe langu. Tunataka kukufanyia kazi ya uhakika. We mwenyewe si wacheki makamanda tupo wangapi? Huyo dogo ataaibika mpaka mwenyewe utakuja na kutuongeza elfu hamsini nyingine. Ila kwa sasa,sisi tunataka hiyo fifte halafu kazi nzima tutaifanya wenyewe hadi iishe.”Ban alizidi kumvuta Fred ili amuingize kitanzini kwa ile hela aliyomtajia kama gharama.

“Fanyeni elfu thelathini basi,hiyo hamsini mimi sina.”Fred alibembeleza jambo kana kwamba anachotaka kufanya ni sheria iliyoruhusiwa na tume yakutunga sheria hapa nchini.

“Kama utataka kwa bei hiyo,itabidi na wewe uwemo kwenye mchakato huo. Sisi tutakutafutia kila kitendea kazi,halafu utakamilisha kazi hiyo we mwenyewe.Unasemaje.”Ban alikuwa mkavu na mwenye msisitizo wakati anaongea hayo.

“Mazee,mimi yamenishinda na ndio maana nimekuj kwenu. Nisaidieni bwana.”Fred alizidi kubembeleza huku shingo yake kaiweka upande kuwasilisha bembelezo lile.

“Sikiliza kamanda Fred,sisi tutakupigia kazi ya maana ambayo hutatambulika kama ni wewe bali yule Hans. Na kama Junior atamshuku yule,ni lazima atataka kulipa kisasi. Sasa wewe ndiye utatuletea mteja huyo. Na yeye tutampa bei kama yako,na kama yawezekana tutaipandisha juu iwe kama elfu sabini au laki moja. Wewe ndio utakuwa unamsukuma ili alipe kiasi hicho,tena ikibidi mkopeshe kiasi kilichozidi.

Akitulipa,sisi tunakata elfu hamsini yetu,kile kilichozidi tunakupa wewe kama shukrani ya kutuletea mteja. Hapo vipi kamanda.”Safari hii aliongea Moi Shabala kibiashara zaidi.

“Hapo haina noma. Basi nipeni nusu saa kwanza nikafanye mambo benki.”Fred aliomba ruhusa na kutoka chumbani kwa akina Ban akiwa ameridhika na maamuzi yake juu ya kulipa kisasi kwa Junior.

*****

Alienda benki na kufanya muhamala wa fedha kwa kiasi cha shilingi elfu sabini. Elfu ishirini aliweka pembeni na elfu hamsini akaiweka mahala kwingine. Hapo tayari akawa amekamilisha kazi iliyompeleka benki na akawa tayari kwa ajili ya kuingia vitani,vita ya kijinga kabisa kuwahi kutokea katika maisha ya mwanadamu wa leo.

Baada ya dakika zisizopungua arobaini,Fred alikuwa chumbai kwa akina Ban akifanya makabidhiano ya fedha zile alizoenda kuzichomoa benki.

“Mzigo ndio huo hapa wazee. Nataka kazi ifanyike bila mimi kujulikana, na pia nataka siku ya tukio na mimi mnitaarifu ili niwepo eneo hilo nione kitakachotokea.”Fred alikuwa anatoa kiasi cha fedha huku anaongea hayo.

“Hamna shaka hata kidogo. Deal done.”Ban alikamilisha maongezi huku akikabidhi noti tano nyekundu,fedha halali kwa malipo nchini Tanzania kwa Sunday Magembe aliyekuwa katoa tabasamu la pongezi kwa kamanda wao,Ban.

“Basi fresh. Mambo yote ni kesho. Dogo ndio anaenda kukutana manzi. Fanyeni yenu kama kawa.”Fred aliweka hitimisho juu ya maongezi yale na kutoka nje chumba kile akiwa na uhakika wa kazi yake kufanyika bila zengwe wala kokoro.

Ama hakika alipania kufanya kisasi,kitendo cha kutoa kiasi kile cha fedha kwa ajili ya kumuaibisha mwenzako,ni kitendo cha kijasiri sana kupata kutokea kwenye dunia ya sasa,dunia iliyojaa vituko kila kona ya pembe zake. Yote yanabaki kuwa siri yake,hakuna aliyepaswa kujua kama analipa kisasi zaidi ya wale aliyowapa kazi ile.

*****

Huku nyuma baada ya Fred kuondoka,Ban alipanga jeshi lake kwa ajili yakutimiza kazi waliyokuwa wamekabidhiwa na Fred,kazi ya kuhakikisha Junior anaaibika mbele ya umati wa watu.

“Umeona maboya hayo? Sasa ni muda wa wao kuaibika,walidhani tumesahau ya siku zile? Sasa hapa ni kuwafanya waaibike bila sisi kugundulika. Yaani tunacheza chezo huku tunawapakazia wao. Tunakula hela,na bado tunawaabisha. Huo ndio mpango.”Aliongea kamanda mkuu wa chumba kile,Ban Diho.

“Hapo kamanda umecheza kama Pele. Naikumbuka sana ile siku tuliyotembea uchi. Mi kidogo nihame na chuo,ila nikajikaza kiume tu.”Moi Shabala naye aliongezea chachandu juu ya maongezi yale.

“Na hapo lazima ziwamwagike haswaa,si walijidai manunda. Sasa wamekutana na manunda square.”Ban aliongea kwa chuki iliyokuwa wazi kabisa.

“Ndio maana yake. Watajua wenyewe wakipigana,wakikatana mapanga,wakitishiana bastola na hata wakichinjana. Cha msingi sisi tupange jinsi ya kumwaibisha huyo dogo ili akome.”Mdomo wa Sunday nao haukuwa nyuma kudhibitisha kuwa yupo ndani ya wenzake na hawezi kuwatosa.

“Hapa watasanda tu!.Sisi ndio maji,ukishindwa kwa kutunawa,utatugida tu.”Ban alimaliza tambo zilizokuwa zinaendelea chumbani mule na sasa alikuwa kajiweka wima kwa jili ya kuanza kazi ya kuupanga mkakati uliokuwa umewatinga mbele yao.

BAADA ya dakika kadhaa za kukaa mule chumbani kwao.Ban na kundi lake walikuwa wameshamaliza makakati watakaoutumia kwa ajilli ya Junior,na hakika ulikuwa ni mpango wa uhakika kwa ajili ya kijana machachari pale chuo kikuu kwa kupiga gitaa la solo,kijana aliyekwenda kwa jina la Junior King Nickson.

“Kwa hiyo kila mtu acheze nafasi yake maze. Wewe Moi na Mose,anzeni leo kufatilia maeneo ambayo dogo atakuwepo,mzee nani hapo Sunday, nenda katafute dawa hiyo na mimi naanza kualika watu na ishu nyingine.”Ban alitoa majukumu ambayo tayari walikuwa wameyajadiri.

“Haina kwere Kamanda mwenyewe. Hapo wenyewe watasema yuwiii.”Sunday aliyatoa hayo huku ananyanyuka pale alipokuwa kakaa na kwenda kwenye kabati lake. Nadhani alienda kuvaa mavazi mapywa kwa ajili ya kazi hiyo ambayo waliamua kujitolea kuifanya kwa moyo mmoja.

ITAENDELEA

SIMULIZI The Lost Boys – 5

Leave a Comment