SIMULIZI

Ep 3: The Lost Boys

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 4
SIMULIZI The Lost Boys – Ep 3

IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI

*********************************************************************************

Simulizi : The Lost Boys

Sehemu Ya Tatu (3)

Hakuwa mtu wa kuvaa rangi ya kijani kwa nyeusi kama baadhi ya wanawake wengine wa pale chuo.Ukivaa hivyo utakuwa kama jalala,yaani utaonekana mchafu.Rangi zilizofifia zinaenda na rangi za kung’aa bwana.Na ndivyo Eve alivyokuwa akijipanga katika mavazi yake.Acheni wakina Junior wadate aisee.Mtoto alikuwa anaweza haswaa.

Uzuri huo wa Eve ndio ulimfanya hata Ban adate na kuingia mwenyewe laini.Na uzuri huohuo ndio unawaingiza mtegoni wale jamaa walikuwa wanajiita Ant-Girls.Ni hatari na balaa juu yake hasa pale ilipogundulika wale wote walikuwa wanamtaka msichana mmoja,ambaye ndiye waziri mkuu wa chuo kile kwa wakati ule

HUYO NDIYE EVE JOHANESS.

**********

Ilipita wiki tangu wakina Hans wakutane na Eve.Kila mmoja alikuwa anakutana na Eve kwa muda wake na kuna muda walikuwa wanakutana naye kwa pamoja na kuongea naye mambo mbalimbali yanayotokea pale chuoni na duniani.

Eve alitokea kuwaelewa sana wale jamaa kutokana na ucheshi na mambo yao.Kila mmoja alikuwa akitumia kipaji chake kufikisha hisia zake kwa mwanadada yule mlimbwende.

Aliyejua kutunga tenzi,alifanya hivyo na aliyejua kuitumia biblia kwa kugeuza mistari ya kitabu kile na kuwa mistari ya kufikisha hisia zake,naye alifanya hivyo.

Huku mwanasayansi naye akichanganya maneno na falsafa za wanasayansi na kuwa mistari ya mapenzi inayovuta hisia za kila mwanamke atakayesikia yale maneno.

Hiyo ndiyo sababu kubwa ya Eve kupenda kukaa na wale jamaa kwani kila muda alikuwa anapata maneno matamu kupitiliza.

Licha ya hayo yote kutokea,hakuna aliyewahi kumtamkia moja kwa moja kuwa wanampenda mwanamke yule.Wote walikuwa wazee wa mistari tu!.Lakini hakuna aliyewahi sema au kumwambia Eve kuwa anahitaji kuwa mpenzi wake.

Hilo ndilo lilikuwa tatizo la hawa jamaa japo wenyewe wakikutana peke yao,wanaambizana kuwa wameshampiga saundi mtoto yule na wanasubiri majibu tu!.

Mambo yalizidi kunoga pale wale wagumu waliporudi chuoni.Walikuwa wamebadilika sana kitabia,na kila mtu aliwapenda kwa nidhamu waliyoionesha baada ya kurudi.Sasa wakawa mstari wa mbele kushirikiana na wenzao huku rafiki zao wakubwa wakiwa ni walewale wakina Hans.

Hali ile ya wakina Junior kutambiana kila wanapokutana,ikazua kiriba cha roho.Kwa nini huyu hivi na mimi hivi?.

Kiriba hicho cha roho kikaanza kutengeneza wivu taratibu na matokeo ya wivu huwa ni chuki baina ya watu.Na ndicho kilichofuata baada ya wivu ule.

Kila mmoja akatafuta njia maalumu ya kumpindua mwenzake.Huyo Mtakatifu Fred naye aliamua kwenda na wale wahuni nyama kwa nyama.Kama wao waliamua kumfanyia uhuni,basi na yeye aliamua kuwa kama wao.Si mwajua kuwa ukitaka kumuua Shetani ni lazima na wewe ujivike ushetani.Basi ndivyo ilivyotokea kwa Fred.

Msaada mkubwa walioona utawasaidia ulikuwa ni kwenda kwa wagumu na kusema matatizo yao huku wakitoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kazi hiyo kufanyika.

Hakuna aliyejua kuwa mwenzake anawatumia wagumu kumwaribia na nafasi kama hiyo ndiyo wagumu waliona kama nafasi ya kulipa kisasi chao japo kisasi hicho walikuwa hawataki kilete majanga kama kile cha mara ya kwanza.Hichi kilikuwa kisasi cha akili ambacho kilikuwa kina lengo la kuwakusanyia hela zao tu.

Naam,wagumu walipewa shavu la kufa mtu kwa ajili ya kuharibu mikakati ya mmoja wa kundi la akina Hans. Ban na wenzake walikuwa ni watu wa kuagiza tu! Tuletee ichi ili kazi ikamilike haraka,au fanya hivi na toa ichi halafu usubiri matokeo.Hiyo ndiyo ikawa kazi ya wagumu.

Kwa upande wa Suarez yeye aliamua kukaa pembeni na kuwashangaa jamaa zake kwa nini wamechanganyikiwa kiasi kile kwa muda mfupi tu!.Alikaa pembeni kwani hata alipowashauri walikuwa wagumu kuelewa na wagumu kufikiri kwa mtendo yao

Wote kwa muda tofauti ,walimpa Suarez mikakati yao. Pale alipojaribu kuwarekebisha,walimwijia juu na kumuona kama anawazingua tu!Hivyo wakaacha kabisa kumpa taarifa jamaa huyu na taarifa zikawa zinapelekwa kwa wagumu.

Suarez akawa mtu wa kutabasamu na kuwaona hawa jamaa kama marimbukeni tu!.Ipo siku watadamka na watajijua kuwa walikuwa wanabugi sana.Hivyo aliwaacha na kubaki muangalia filamu ile ya bure kabisa,yenye wingi wa vituko na vichekesho visivyokwama.

Eve yeye alikuwa hana taarifa zozote kutokana na ule mkanganyiko baina ya wale rafiki zake wapya.Yeye alichojua ni kwamba ana marafiki wenye maneno matamu yanayoweza kusababisha chakula kikajila.Hakujua kama wenzake tayari wanacheza ligi kuu na kombe likiwa ni yeye.

Na kizuri zaidi kundi lile lilikuwa pamoja kama zamani.Yaani ni kama walikuwa hawajawekeana bifu,wote walionekana wana furaha sana pale wanapokutana. Hakuna aliyejua roho ya mwenzake zaidi roho yake na MUNGU pekee.

Hawa watu watatu,namaanisha Hans,Junior na Fred.Walijipanga sana kimaneno kwa ajili ya Eve.Na mengi waliyaongea yalikuwa ni maneno matamu ambayo kiukweli hata wasichana wengine wangeyasikia au wao ndio wangekuwa wanaambiwa,sidhani kama wangekataa kuwa japo na mmoja wa wavulana hao watatu.

Ngoja nikupe maongezi ya kila mmoja wao akikutana na Eve.

JUNIOR NA EVE.

Mara nyingi Junii au alipenda sana kumpeleka Eve chuo cha kule mlimani.Na walipenda sana kukalia mawe yale ya mlimani.

Huku wakipata upepo na vinywaji mbalimbali walivyotoa supa-maketi ya Mlimani City.Junior alikuwa anam-mbeleza kwa gitaa Eve huku akitoa maneno yake ya kisanii kumwelekea mrembo yule ambaye siku zote alimuona Junii kama mtu mchangamfu na mwenye wingi wa maneno.

“Wajua nini My Beautiful”.Junior alianza kumuongelesha Eve baada kumpigia gitaa kwa muda.

“Nambie tu My Junior”.Eve naye alimwambia huku akisogea karibu kabisa kwa Junior kwani tayari alishajua maneno matamu yanaanza kumwagika kutoka kinywani kwa kachaa yule mjanja mjanja lakini bonge la boya kwa kimwana Eve.

“Nataka ufahamu kuwa fahari ya moyo wa binadamu ni kuona furaha kwa mwenzake ikikamilika bila bugudha.Kama mimi hapa sasa hivi,najisikia sana fahari kuwa na wewe na ninadhani nawe wajisikia the same way”.Junior alimuanza taratibu Eve kama hataki vile.

Eve aliyekuwa kapambwa na tabasamu huku asielewe siku ile ni nini Junii ataongea,alizidi kujipenyeza kwa Junii na kumgusa kwa makusudi na kifua chake kwenye eneo la ubavu wa kijana yule msanii.

“Endelea sasa msanii wangu.Mi najisikia fahari sana niwapo na wewe Junii.Unanifanya nisahau mengi.Embu endelea kunipa fahari hiyo My Junior”.Junior kusikia hivyo na kile kifua kilivyokuwa karibu yake,wacha kabisa.Jamaa likawa bwege kama si fala kabisa.

“Daah!Beautiful unanifanya nione dunia kama imeegemea upande wangu na vitu vyote vizuri katika maisha haya vimeterezea upande huohuo ambao mimi nipo mimi.Muda wote wanifanya nijisikie raha na amani niwapo na wewe.

Sauti yako nyembamba kama nota namba moja katika gitaa,ndiyo hasa inayonifanya nijisikie nipo hewani pale napoisikia sauti yako mwanana ya kumtoa samaki magamba bila kisu.

Nashindwa kukwambia huu kiasi gani mwenye mvuto.Ila kama MUNGU akiniuliza huu mzuri kiasi gani,naweza nikamjibu kwa kumwambia kuwa kakuumba kwa udongo wa kipekee ambao hakuna binadamu mwingine aliyewahi kuumbiwa udongo huo”.Junior alikuwa anafunguka maneno ambayo hadi leo hatujui aliyatoa wapi.

“Mmmh!My Junior,ya kweli hayo jamani?”.Eve ilibidi aulize.Lakini uliza yake ilikuwa ina jambo ndani yake.Kauliza ili Junii aendelee au kauliza ili kujua kama maneno ya Junii ni ya kweli,au kauliza ili aonekane kama kachangia kitu.Mimi na wewe hatujui,ila moja ni jibu lake.

“Sasa nikudanganye nini My Beautiful One.Embu angalia machoni pangu”.Junior alimuomba Eve atazame macho yake.Na Eve naye akatazama huku katoa lile tabasamu lake la kumtoa samaki magamba.

“Najua bado hujajua ni kwa nini umeangalia macho haya.Ila naomba kukuuliza.

Ndani ya macho haya umeona nini?”.Junii alimuuliza Eve swali ambalo laweza kukufanya ujue kama mwanamke huyo anaelewa maana ya mapenzi uliyonayo kwake au haelewi.

Inawezekana Eve alijua ni nini ajibu,lakini kwa kuwa alikuwa hataki kuonekana kama anaelewa,akajibu kinyume na mimi nayeandika nilivyodhani.

“Naona mboni My Junior”.Eve alimjibu huku bado tabasamu likitamba kwa mbwembwe usoni pake.

“My Beautiful One.Sidhani kama ndani ya macho yangu waweza kuona kitu kama hicho.Sawa kuna mboni,ila pia ukiangalia vizuri utajiona na wewe.

Nataka uelewe kuwa macho ni zaidi ya kioo.Macho ni zaidi ya kujieleza uonacho.Macho yangu ukiyaangalia,nadhani wajua wazi kuwa yanaeleza ni kiasi gani Junior mimi nashindwa kufumba macho pale napoona sura yako au napoikumbuka.Niamini My Beauty,wewe ni zaidi ya mboni uionayo wakati unaangalia macho yangu.

Siwezi kusema ya moyoni yaliyojificha lakini kama unataka kujua ya moyoni,ni lazima ujue haya ya machoni uyaonayo.

Moyo ni zaidi ya jinsi uujuavyo katika sanaa hii ya Maulana”.Hapo Junior aliposema sanaa ya Maulana,alionesha tendo kwa mikono yake kwa kutengeneza duara angani.Akimaanisha sanaa ya Maulana ni Dunia.Akaendelea.

“Moyo waweza kubeba kila kitu ambacho binadamu hawezi kukibeba kwa mikono yake.Na hata mikono hiyo ikibeba,itaambulia kudondosha au kukipoteza.Lakini moyo ukiamua kubeba,umebeba tu! Ni wewe mwenyewe kuamua kupoteza au kukitupa kitu ulichokibeba.

Isikupite Hii: Geza Anasakwa Auwawe Ep 01

Kwa mfano siri za watu.Ni moyo pekee waweza kubeba hiyo kitu.Hakuna awezaye kuifanya siri hiyo ipate kopi yake kana kwamba umeihifadhi labda kwenye karatasi au CD.

Ndivyo ilivyo katika mapenzi.Kwanza ni moyo ndo una-disaidi kuwa huyu ndiye na huyu siye.Huyu aingie na huyu aisiingie.

Baada ya hapo ndio unapeleka kwenye ubongo na kumwambia ubongo aweke kumbukumbu juu ya moyo ulichoamua.Vinginevyo bila moyo kungekuwa hakuna mapenzi au upendo wowote kwa mwanadamu”.Junior alikuwa anabwabwaja maneno ambayo kiasi fulani yalikuwa kama yanamfungua Eve.Na kwa mwonekano yalikuwa yanamuingia vilivyo Eve.

“Mmmh!My Junior.Lakini upendo si wajengwa kwa hisia kwanza ndio unapelekwa moyoni?”.Eve ilibidi afanye kama swali lakini kiukweli alikuwa anataka kujua zaidi kupitia kwa Junior.

“Hapana My Beautiful. Hisia ni hali ya nje tu! Lakini moyo ndio kila kitu katika kuthibitisha upendo au mapenzi.

Hisia zaweza kuwa ndio au siyo.Yaani,waweza sema kuwa nampenda pale ulipomwona tu! Hizo ni hisia ndizo zimekutuma useme hivyo.Lakini siku zote moyo ndio unasema kweli kuwa umempenda.

Umewahi kusikia kuwa watu wameachana kwa sababu hawaendani au mke anakuwa nakiburi kwa mme wake na yupo tayari hata kupewa taraka ili aondoke.Umewahi sikia hiyo kitu?”.Junior alimuuliza Eve.

“Hiyo nimesikia sana.Na hata rafiki zangu wamewahi kunihadithia mambo kama hayo kuwatokea”.Eve alijibu huku bado yupo karibu kabisa na Junii ambaye alikuwa anamsikiliza huku anashusha juisi ya embe kwenye koo lake.

“Sasa hao walifuata hisia.Hao hisia ziliwatuma kuwa tunapendana ,na hisia hizo hizo ndizo ziliwaambia kuwa tufunge ndoa.Lakini walipotulia,waligundua kuwa mioyoni mwao hakukuwa na kitu kinachoitwa upendo bali ni hisia ndizo ziliwafanya wadhani wanapendana.

Huwa siamini kuhusu hisia hata mara moja.Hisia zaweza kusema kimbia na moyo waweza kukukataza usikimbie hasa katika hatari.Mara nyingi hisia hana ujasiri,ila moyo bwana,naupa hongera mno.Unaweza kuvumilia.”.Junii alizidi kutema madini na kumwacha Eve hana neno bali tabasamu lisiloisha hamu.

Licha ya tabasamu hilo,Eve hakuthubutu kumuuliza Junii maneno yake yana maana gani.Na si Junii pekee ni hadi Hans na Fred,wote walikuwa wana maneno kama yanaendana,lakini Eve hakuweza kuuliza nia na madhumuni ya maneno hayo.

Alifanya hivyo akijua kwamba wale wavulana wamempenda na wanamuhitaji,lakini walishindwa kumwambia moja kwa moja bali kubaki wakiongea mafumbo kama wamemeza kamusi ya Wahenga.

Pia Eve alishindwa kuuliza kwa sababu alifahamu endapo atauliza tu!.Basi maneno yale yatageuka na kuwa sumu ya kumtongoza,yaani endapo atauliza basi atakuwa kawapa upenyo watu wale wanene wanachoki-feel mioyoni mwao.

Udhaifu wa kutongoza kwa vijana wale watanashati,ukawaponza na kubaki wakiumia na maumivu yao huku kila siku wakibuni misemo mipya ya kuongea.

“My Beautiful.Angalia jua”.Junior aliongea baada ya kumwacha Eve kwa muda akitafakari maneno aliyoyatoa.

“Yaah,My Junior.I see and I think it is gone”.Eve alimjibu Kiingereza Junii.Wakati huo jua ndilo lilikuwa likiwahi machweo yake,yaani ilikuwa ni muda wa saa kumi na mbili na nusu au na dakika zaidi ya thelathini.

“Noo.My Beautiful.Sijamaanisha uangalie ili unipe jibu ya kuwa linaenda kuzama.Nataka nikwambie siri moja ya jua hili ulionalo sasa hivi”.Junii alimrekebisha mawazo Eve.

“Tell me My Junior”.Eve kwa wahka naye akaitika.

“Jua ni kitu cha ajabu sana katika maisha yetu. Kwanza si choyo na halina ubinafsi kwa vitu vinavyofanana nae.Hapa na maana mwezi na nyota.

Jua katika muda wake wa kuwaka,unaweza kuuona mwezi na hata nyota.Lakini mwezi na nyota,zina ubinafsi sana.

Vitu hivi katika kuwaka kwake,huwezi kuliona jua hata kidogo.Namaanisha,jua linapozama linaachia kazi ya kuleta nuru mwezi na nyota.Na saa nyingine kukiwa kuna dalili ya mvua hasa mida ya usiku,mwezi na nyota,hujificha ndani ya mawingu na kutuacha sisi binadamu gizani.

Lakini jua,kamwe halifanyi hivyo.Litapambana na dalili ile ya mvua na saa nyingine linajificha ndani ya mawingu lakini baada ya kutufikiria sisi kuwa tupo gizani,hujitokeza na kuendelea kupambana ili tupate mwanga wake.Hiyo ni siri ya jua ambayo mimi nimeigundua”.Junii alimaliza na kumwacha Eve makusudi ili amuulize.

Kama alivyotegemea Eve akaingia line na kuuliza maana ya maneno yale.

“Haha ha haaa.My Beautiful.Kwanza tuanze kushuka huku ili turudi kwetu”.Junii alimwambia Eve,naye Eve hakuwa na kipingamizi zaidi ya kushuka katika mlima ule waliokaa karibu saa moja na nusu wakiongea na kunywa.

Huku wanatembea kurudi mjengoni wanapoishi,Junior aliendelea kutema madini yake.

“Napenda sana binadamu mwenye tabia ya jua kuliko hivi vitu vingine kama mwezi au nyota.Natamani kukwambia kuwa wewe ni kama jua kwa watu”.Eve aliposikia hivyo,alitabasamu na kumsogelea Junii tena na kupitisha mkono wake kwenye mkono wa Junii kisha akamlalia Junii kidogo kwenye bega.

“Kwa nini unasema hivyo my Junior”.Eve alimuuliza Junior huku akijiweka sawa kuzipokea sifa kedekede kutoka kwa msanii yule.

“Popote waliporafiki zako na wewe upo. Kamwe huwaachi wakiwa peke yao. Umekuwa ukiwahakisi mwanga wako kama jua lifanyavyo kwa nyota. Hutaki wakae gizani kama kuna hali hiyo. Nathibitisha haya baada ya kukuona mara nyingi sana upo karibu yetu. Hata iwe saa ngapi,tukikuita waja. Hakuna mwanadamu kama wewe,naweza kusema hivyo.

Umebarikiwa moyo wa jua,moyo ambao hutaki kumwona mwenzako akipata shida wala kuteketea. Kama nikisema wewe ni zaidi yao,sidhani kama nitakuwa nakosea. Hu mzuri kuanzia nje mpaka ndani. Hu mwema kiakili hata matendo. Upo tayari kutoa faraja kwenye mwenye simanzi na upo tayari kufariji kwa kila neno zuri kwa mwenye kuhitaji maneno ya faraja”.Junior alikuwa akibwabwaja maneno mazuri na masafi kwenda kwa kimwana yule,lakini kila alipotaka kutamka hisia zake kutoka moyoni kuwa anampenda Eve,alishindwa na kubaki akiangalia mbele.

Udhaifu huo Eve aliujua hivyo ilikuwa ahueni kwake kwani kama Junior angetamka kuwa anahiotaji kuanzisha mahusiano ya kimapenzi naye,basi mambo aliyoyapaga yasingetimia.

“Mmmh!My Juu,ya kweli hayo”.Eve aliuliza huku bado katoa tabasamu lake mwanana lililopamba hata njia wanayoikanyaga.

“Kwa nini nikudanganye My Beautiful. Umeumbwa kwa ajili ya watu kama sisi wenye kuhitaji faraja. Wewe ungekuwa kiungo katika mwili wa mnyama basi ungekuwa moyo au kichwa. Na kama nikiulizwa una umuhimu gani katika maisha yangu,ningesema wewe ni damu mwilini mwangu. Ukiondoka nakuwa sina uhai,ukisimama nakuwa katika koma na ukimwagika,unaniachia maumivu”.Maneno yalizidi kukandamizwa na Junior.

“Mmmh!Haya bwana.Naona karibu tunafika madarasani. Natamani niendelee kukusikiliza,lakini daah!Yanibidi niende My Junii. Nitakuja kukuona tena kesho,palepale mnapopataga chakula nawenzako”.Eve alikuwa anamwambia Junior baada ya kufika maeneo yalipo madarasa yao.

“Okey, My Beautiful. Uende salama na ukawaangazie wote wenye giza huko uendapo. Wewe ni jua kama nilivyokwambia,usiubane mwanga wako kwa wanaouhitaji”.Junior alimwambia Eve naye Eve kuonesha kama shukrani au ili asimuumize Junior atakapoondoka,au labda kumpa moyo ili Junior ajione mwenye bahati,akambusu shavuni Junior halafu kwa sauti nyembamba na ya kubembeleza,akamnong’eneza sikioni kwa kumwambia kwa heri my Junii.

Safari yao ikaishia hapo huku Junior akibaki kaduwaa asiamini kama ni yeye aliyepewa busu zuri kama lile na mtoto mzuri kama yule.

Alimwangalia Eve jinsi anavyoenda anapoenda naye Eve kama alijua anaangaliwa na Junior,aligeuka na kisha akabusu mkono wake wa kulia na kumfanyia ishara ya kulipuliza busu lile kwenda kwa Junior.

**********

Junior alifika kwa wakina Fred na aliwakuta wote watatu wapo. Wote hawa walikuwa hawana siri juu ya mambo yanayotokea wakikutana na Eve. Japo walikuwa hawafichani,lakini walikuwa wanadanganyana sana. Na ndicho kilitochotokea kwa Junior baada ya kufika mle ndani.

“Tehe! Tehe! Teheeeee. Mtabakia kushika mapembe tu!Maziwa anakamua mtu mwinginee.Tehe! Tehe! Teheee”.Junior alianza mbwembwe zake kwa kucheka kama katuni.

“Naona umeshaanza kujungua mwenyewe. Haya bwana,ila hayo maneno tu! Hata vyombo vya habari siku hizi vinatemeana”.Hans aliongea baada ya Junior kusema maneno yake.

“Sasa kama nyie ni washika mapembe,nisiseme?. Mnakukuruka kushikilia mapembe ng’ombe,na ling’ombe linawarusha-rusha na kuwadoboa tumboni na mapembe yake lakini hata hamkomi. Jingine limeshikilia miguu yake huku chini,linapigwa na kwato za kidevu lakini bado bishi. Utakufa Baba Paroko,hii ligi ya watu wazima.

Wewe Hans kamata mapembe na saidiwa na huyu Suarez.Wewe Baba Paroko,kamata kwato mzee. Mimi nakamua taratibuuu,kama nanawa vile. Najinywea vyangu. Nyie endeleeni kudobolewa na mapembe”.Junior alikuwa anaongea hayo huku anavua viatu vyake na kwenda anapolala.

“Dah!Kwa hiyo na mimi nipo Junior”.Aliuliza Suarez baada ya maneno ya Junior.

“Sasa utakosa wewe. We upo kila usehemu. Ukichoka kupigwa pembe,njoo kwa Baba Paroko umsaidie kupigwa kwato za chembe.Ha ha haaaa”.Junior aliongea kwasharau na kupandisha miguu yake kitandani,kisha akalala kifudifudi.

“Daah! Haya bwana. Ila kama kweli sisi washika mapembe na kwato,sidhani kama kesho kutwa nitaenda kushindwa kukamua maziwa”.Aliongea Hans na kuficha uso wake kwa kitabu.

Maneno hayo yalimshtua Junior na kumfanya akae na kumuuliza Hans.

“Unaenda kukutana naye?”.Junior aliuliza.

“Unauliza jibu tena”.Hans akajibu kwa kifupi wakati huo Fred yeye alikuwa kimya akiwatazama wale jamaa wanachoongea. Siku zote Fred alikuwa mtulivu sana,hakuwa na papala kaika maongezi yake,ila akiongea huwa yanawachoma sana na ndio maana hata Junior aliwachoma kwa maneno yake kwani ndio tabia zao.

“Ha ha haaa,linaenda kula makombo yangu”.Junior alimwambia Hans.

“Yawezekana leo ndo mara yako ya kwanza kukutana Eve wewe. Mwenzako kesho mara ya ………. Eti mara ya ngapi Jogoo wa Jiji”.Hans alijidai kasahau idadi alizokutana nazo na Eve,hivyo akamuuliza Suarez ambaye alikuwa shabiki wa timu ya Liverpool ambao wanajiita majogoo wa jiji.

“Sijui mara ya arobaini hiyo. Daah!Ujue sina uhakika kwa sababu siku nyingine huniambiagi.Ila nahisi itakuwa mara ya arobaini au arobaini na tano hivi”.Alijibu Suarez ili kumuumiza Junior.

“Yaah! Wewe sikukwambiaga mara kumi tu! Kwani sikutaka ujue nimempeleka gesti gani. Kwa hiyo nimekutana na Eve kitu kama mara hamsini hivi mdogo wangu. Unavyosema naenda kula makombo yako,nakushangaa sana. Mi najua hata mate hujawahi kuambulia zaidi ya kuumiza miodole yako kwa kupiga gitaa.

Mgitaa wenyewe unalia kama mgobole wa kuulia tembo au ukipiga sauti nyembamba linalia kama unanoa kisu,hadi unamuumiza meno mtoto mzuri kama yule”.Hans alikuwa anamiga madongo Junior hadi chumba kizima kikawa kimetawala vicheko.

“Eti sijala mate, Thubutuu,wewe unacheza na mimi nini?Leo mtoto nimempa maneno matamu hadi kalegea na kunipa ulimi wake mwenyewe. Mi napiga saundi hata mti wa mbuyu ukizisikia uweza kukatika au kulala hapo hapo. Napiga saundi hadi simba dume linabadilika sauti na kuwa kama ya mtoto wake”.Junior alizidi kujiifia kwa uongo na kuwaacha watu wakitafakari maneno yake kwa kuwa walikuwa hawana uhakika kama ni uongo au kweli.

Uzuri wao walikuwa hawajali kuchangiwa kwa maneno. Leo unaweza kukuta Hans anasemwa na chumba kizima,halafu kesho Junior na siku nyingine ni Fred. Sasa siku ile ilikuwa ni zamu ya Junior na aliyataka mwenyewe

“Kwenda zako huko.Nilikuwa nakusikiliza kitambo.Tangu umeingia hapa”.Alikuja Fred na kumrukia kwa maneno Junior.

“Tena wewe Baba Paroko kula ngumu,kwa sababu huna sumu.Siku ile kum-kiss manzi ukajiona ndo kidumee. Mwenzako leo nimepewa lile orijino kabisa”.Junior naye akajibu mapigo kwa Fred.

“Acha kutudanganya. Domo lenyewe linanuka hadi huku halafu unasema umekula mate mtoto yule. Sijui umekunywa manini. Usituzuge hapa,huwezi kula mate na maarufu yako ya karanga mdomoni. Eti nilionea maneno matamu,unamaneno gani matamu wewe kama si kulia lia tu!. We si bongo fleva,kazi yako kulia tu!.Nenda huko kaimbe kulia lia magerezani kama ule wimbo wa Tunda. Lakini huna maneno matamu zaidi ya kujisumbua”.Aliongea Fred maneno kumwendea Junior.

“Ha ha haaa.Mzee wa Upako mpe huyo. Kazi kulia kama PNC,wagumu kama Chid Benz tunazidi kunguruma kwa mtoto hadi anasalula viwalo vyake mwenyewe”.Aliongeza Hans lakini Fred naye alimkata.

“Na wewe sepa zako hapa.Huna lolote,yule demu hujala wala nini. Kama umekula niambie umekula lini ili nikuulize swali”.Fred alimwambia Hans.

“Yule wiki iliyopita nilikuwa naye kwenye lodge moja kule Sinza. Hadi nikaoga naye”.Hans alijibu kwa kujiamini wakati huo Junior alishapewa vyake na kutulia,na Suarez yeye alikuwa mtu wa kusikiliza na kucheka kutokana na yale maongezi.

“Eheee,hapo hapo. Sasa mimi nilipiga pale wiki mbili zilizopita na kuna alama nilimwachia kiunoni.Niliandika kwa wino ambao hata ukae mwezi haufutiki. Na nilimwandika wakati kalala,hivyo hajui kama kaandikwa. Niambie,umeona alama hiyo wakati unaoga naye?Na kama umeiona,imeandikwaje. Sema ukweli usidanganye”.Fred alimuuliza Hans ambaye kidogo aligwaya baada ya maneno yale.

Hamna hata mmoja aliyekuwa anamwambia mwenzake ukweli,ilikuwa basi tu! Kutambishiana.

“Jibu.Lione kwanza kichwa lake kama kibuyu cha kuchotea maji kijijini”.Junior alimpa kavu la uso Hans baada ya kumwona kagwaya kujibu.

“Mzee waUpako umetisha. Jamaa kanywea kama mchicha japo mara ya kwanza alikuwa kajaa sufuria”.Suarez alimpa sifa Fred.

“Msijifanye mnajua hapa,kumbe tunaojua tumetulia tuli. Keshokutwa ukienda kukutana naye,mwangalie kiunoni,utakuta nimeandika kwa herufi kubwa jina langu. Hapo ndo utajua kuwa washika mapembe na kwato ni nyie,sisi wazee wa nyonyo tunakamua taratibu maziwa yetu. Mtaniambia nini nyie,mimi fundi. Udambwidambwi mwingi kama Mbwiga Wa Mbwiguke,si fundii.

Mafundi hatuchafuki,sisi wazee wa biliji tu! Sasa wewe kibarua endelea kupigwa kwato na domo lako linalonuka kama kwapa la mwehu”.Akamaliza Fred na hapo kimya kikafuata huku kila mmoja akiwa haamini alichoongea Fred.

Wote walijua ni kweli Fred anaweza kuwa ametembea na Eve hasa kwa sababu alikuwa anajiamini sana katika matendo yake. Lakini haikuwa hivyo,Fred alikuwa ni mtu wa maneno tu kama wao.

“Daah! Mzee wa Upako au Mzee wa Biliji,naona umewanyamazisha wananchi wote. Sasa nadhani watasoma,maana tambo zilikuwa nyingi sana hapa”.Suarez aliongea huku akitabasam baada ya kimya kidogo kupita.

“Hawa wote ni makuku tu! Mchana majanja,usiku yapo hoi kwa kuchoka kwa sababu ya mchana kuchakua chakua majalalani. Kila mbuzi ale kutokana na urefu wa kamba yake.

Kama leo wewe Junior uemtoka naye,hatujakufatilia. Keshokutwa Hans,hamna kumfatilia. Mimi kaniambia Jumapili. Natoka naye usiku kwenda kupata naye msosi hotelini,sitaki usumbufu. Mimi zangu hotelini,wewe Jun wajua wapi unapokutana naye na wewe Hans wajua yako. Hamna kuharibiana,sawa?”. Wote wakajibu sawa na mjadala ukafungwa hapo.

***********

HANS NA EVE.

Kama walivyoahidiana siku tatu zilizopita,ndivyo ilivyokuwa mida fulani ya mchana katika siku ile ya Ijumaa.Eve akiwa na Hans katika fukwe za Coco,walikuwa wametulia kwenye kivuli kimoja cha mwamvuli wa ufukweni na kila mmoja alikuwa katikamavazi ya ufukweni.

Hans akiwa kavaa kaptula moja nyepesi ambayo ilikuwa maalumu kwa maeneo yale,alionekana mwenye tabasamu pana mbele ya mrembo Eve ambaye naye alikuwa kavaa kiblazia kidogo kilichoficha kifua chake lakini kikiacha kitovu nje,na kwa huku chini kajifunga kama mtandio wa ulioanzia maeneo ya tumboni hadi miguuni.

Muda wote Hans alikuwa anatamani ule mtandio wa Eve japo udondoke ili aone kama kweli kuna mwandiko wa Fred kwenye kiuno cha Eve.

Hans akiwa amelala pale kwenye kivuli,alimuona Eve anakuja na vikombe vya plastiki viwili ambavyo ndani yake kulikuwa na koni aina ya Vanilla. Ule mtandio aliokuwa ameuvaa ulikuwa unaangaza na kuonesha nguo yake aliyovaa ndani ambayo ilikuwa ni ya ufukweni zaidi.

Mwangaza ule wa mtandio ambao ulichagizwa zaidi na jua kali ambalo lilikuwa linawaka muda ule,ulimfanya Hans amkodelee Eve macho tangu alipokuwa anatoka kule aliponunulia koni hadi pale alipokuwa Hans.

Eve aliyaona macho yale ya Hans na alijua kachizika kwa yale mapigo.Japo aliona aibu kiasi fulani lakini ilibidi avumilie ili apate anachokitaka kwa Hans,ambacho ni maneno matamu.

Alipofika pale mbele ya Hans,alitabasamu na kumuuliza mbona anamwangalia vile.

“Bado najiuliza MUNGU alichanganya kemikali gani hadi akakutoa kiumbe kama wewe. Sidhani kama MUNGU kakuumba kwa udongo bali kemikali maalumu ambazo ukizichanganya huwezi kupata madhara bali faida ya zao kama wewe,zao lililonifanya nikuite sweet. We ni mtamu Eve”.Hans aliongea huku bado Eve akiwa amesimama mbele yake kwa tabasamu la haja toka usoni pake.

“Mmh! Hans,yanaukweli hayo usemayo?Mbona mi wa kawaida tu! Embu niangalie”.Eve aliongea hayo kama kutaka uhakika kwa Hans na hapo akageuka na kumpa mgongo kidogo Hans na kisha akamgeukia tena.

“Daah! Unajua Eve unaweza kuitoa dunia kwenye mhimili wake na kuifanya ijizungushe kwenye mhimili wako?”.Hans alifanya kama kumtupia swali Eve na kumfanya Eve atabasamu zaidi ya pale na kisha akaenda hadi pale karibu na Hans ambapo palikuwa na kiti kingine cha kulala maalumu kwa ajili ya ufukweni.

“Bwana mimi sielewi hayo Hans,hayo mambo ya dunia kujizungusha si mambo ya Jegrafia?Mimi nilisoma HKL bwana,hata sijui”.Eve aliongea kwa kudeka baada ya kukaa kwenye kile kiti mlalo cha ufukweni.

Hans kusikia hivyo ndio akajiona kama mtu mwenye bahati kuliko hata bahati yenyewe. Akainuka pale alipokuwa kalala na kisha akakaa kumwelekea Eve ambaye naye alikuwa amekaa na vikombe vyake akiwa kavishikilia.

“Leta kwanza nikusaidie hivyo vitu maana naona kama mkono yako itachoka”.Alichukua zile koni na kuziweka pembeni kisha akarudi usoni kwa Eve.

“Sweet Eve,si wajua kuwa dunia inajizunguka kwenye mhimili wake,huku inafuata njia zinazoitwa Obiti na wakati huo huo inakuwa inazunguka jua?Kwani hata hilo la form two hukijui?”.Hans alimuuliza Eve.

“Aaah!Zamani sana hiyo Hans.Ila nakumbuka kidogo”.Alimjibu Eve.

“Basi nisikutese Sweet wangu. Naposema dunia itaacha kujizungusha kwenye muhimili wake na kukuzunguka wewe,namaanisha hata dunia itakufuata wewe unachotaka. Hata ukiiambia zunguka kutoka kati kwenda kulia,itatii au ukiiambia izunguke pembeni kwenda kati napo itatii,hii ni kwa jinsi ulivyokuwa mzuri.

Kama tupo vitani,sina haja ya kubeba mabomu kama Rambo au Shoziniga,wewe ni silaha tosha ya kuwaua maadui. Una madhara matamu na si machungu kama bomu la nyukilia. Naapa mbele ya MUNGU,wewe hujaumbwa na udongo bali kemikali zenye harufu nzuri na utamu uliopitiliza. Hujawekewa asidi kwenye kemikali hizo ulizoumbiwa bali umewekewa asali ambayo siku zote nahisi MUNGU alikuwa ameihifadhi ili aje akuumbie wewe”.Hans akazidi kutema maneno matamu mbele ya mtoto mzuri Eve.

“Wewe HANS wewe. Hivi hujui MUNGU anakuona na kukusikia maneno yote unayoongea?”.Eve alimuuliza Hans huku akimwangalia kwa macho ya yaliyojaa furaha.

“Sidhani kama MUNGU anakataza mimi kukusifa wewe kwa jinsi navyokuhisi moyoni mwangu. MUNGU hakatai hilo,ila cha msingi nisivuke mipaka na kumkufuru”.Hans alimjibu Eve na kumwacha mtoto yule mwenye uzuri wa kuita bila swali.

“Mh!Haya bwana.Basi naomba koni,isije ikayayuka bure maana ikiyayuka inakuwa mbaya”.Eve alikata shauri na Hans akampatia koni na kisha wakaanza kuburudika kwa kiburudisho kile.

Wakati wanaendelea kuburudika,mara kwa mbali ikasikika sauti ya meli ikipiga honi.Hapo Eve akapata swali la kumuuliza Hans.

“Eti Hans,ni kwa nini meli na ukubwa wake haizami kwenye maji lakini shilingi mia na udogo wake inazama?”.Eve alimuuliza swali la Fizikia Hans.

Hans akatabasamu kidogo na kujiweka sawa kwa ajili ya kujibu swali hilo. Japo lilikuwa ni swali la kifizikia,lakini pia Hans alilipeleka mbali zaidi na kuwa la kimapenzi.

“Hilo swali wengi sana wanapenda kuliuliza hasa wale wasiopitia Physics. Ila kwa kuwa umeniuliza,nitakujibu na kukupa mfano hai.

Hapo tunarudi kwenye Law of Floatation,yaani hapo utalezea kuhusu vitu kuelea hasa meli.Law ina state hivi………….(Akaelezea hiyo sheria ya vitu kuelea).

Sasa najibu swali lako kama ifuatavyo”.Eve alikuwa kimya na makini wakati hayo yote Hans anayaelezea.Alionekana wazi mwenye uhitaji wa kufahamu alichouliza.Hans akaendelea.

“Meli kwa huku chini kabisa,ina nafasi kubwa sana ambayo nafasi ile haina tundu hata moja litakalopitisha maji. Yaani ni kama pulizo ile sehemu au dumu ambalo halina kitu na lililofungwa na kifuniko chake. Basi na kule chini ndipo papo hivyo.

Dumu likiwa halina kitu ndani yake,waweza kuelea nalo hata kilomita mia bila kuzama,lakini endapo litaingiza maji basi ujue utazama tu.

Na meli kwa pale chini,imeundwa kwa mtindo huo. Kule chini kuna hewa na ahairuhusiwi maji kuingia. Na nafasi ile ya hewa imepimwa ili kubeba uzito fulani wa mizigo. Kama ukizidisha,ndio unakuta meli inazama.

Shilingi mia au shilingi kumi,hazijatengenezwa na nafasi chini yake bali zenyewe ni mzigo ndo maana zinazama.Umenipata?”Hans alimaliza na kumtupia Eve swali.

“Sina swali aisee,upo juu Hans nimekubali”.Eve alimjibu Hans.

“Nashukuru Sweet. Sasa ngoja nikwambie kitu kuhusu wewe”.Hans aliendeleza tena maongezi.

“Ehee”.Eve akakaa mkao wa kula kwa ajili ya kusikiliza maneno toka kwa Hans.

“MUNGU kakuumba kwa mtindo wa meli,Sweet. Hata ubebe mangapi sidhani kama waweza kuyazamisha. Sweet,najua umebeba mengi sana moyoni mwako,naomba usiyazamishe hata kama yamekuzidi. Elea nayo hadi mwisho wake,naamini MUNGU atakupa zawadi ya kipekee katika maisha yako. Kamwe usijaribu kuyazamisha haya uyaonayo na kuyasikia.

Acha nikusifie Sweet Eve. Uwezo wako wa kubeba haya niongeayo waweza shinda meli zote za jinsia yako. Sikufananishi na ile meli kubwa kama Titanic ila naweza kukufananisha na lile Safina alilotengeneza Nuhu kabla ya MUNGU kuleta Gharika”.Alipofika hapo Eve akarudi nyuma kidogo na akawa kama anamshangaa Hans kwa yale maneno.

“Wewe Hans. Hayo maneno ya Biblia umeyatoa wapi. Na Sayansi na dini ni wapi na wapi?”.Eve akauliza huku bado akimshangaa Hans.

“Ha ha haaa. Sweetie,hujui kuwa nakaa na Mzee Wa Upako? Anatupaka maujuzi mara moja moja. Japo tunajidai hatusikilizi,lakini ndio hivyo,huwa tunachukua maujanja.

Halafu asikudanganye mtu,hakuna mtu ambaye anamuamini MUNGU kama mwana Sayansi.

Ngoja nikupe kidogo kuhusu hawa Wanasayansi hasa wale wa hali ya hewa na wanaopaa na vyombo kwenda nje ya sayari hii ya dunia”.Eve kusikia hivyo alisogea tena karibu na Hans na kumsikiliza.

Eve alikuwa anapenda sana kujifunza mambo mengi kupitia watu tofauti tofauti,hivyo uwepo wa Hans,Fred na Junior,ulimfanya ajifunze mengi sana asiyoyajua. Hans akaendelea.

“Kuna mwanasayansi mmoja,jina nimemsahau,ila yeye alikuwa kajiweka sana kwenye mambo ya Meteolojia,haya mambo yanayohusu hali ya hewa.

Yeye alisema kuwa, kama jua litapungua au kuongezeka uwezo wake wa kuwaka basi dunia inaweza kudondoka. Yaani zile nguvu za ukinzani ambazo ni kama sumaku,na ndizo hizo zinaiweka dunia iendelee kuzunguka katika muhimili wake bila kudondoka,eidha zinaweza kuongezeka nguvu na kuifanya dunia ipoteze mwelekeo au zinaweza kupungua nguvu na kuifanya dunia idondoke. Hiyo yote itatokana na jua kuongezeka na kupungua uwezo wake wa kuwaka.

Kwa maana hiyo,yeye alimaanisha kuwa dunia inategemea sana nguvu za jua katika kujiendesha kwake.Na huyu Mwanasayansi ana Law yake. Ngoja nitakuletea siku moja umjue.

Baada ya kusema hayo,akakaa muda mrefu na hiyo Law yake ikawa inatumika sana.Lakini baadaye lile bara la barafu linaitwa Antakatika,barafu ikaanza kuyeyuka. Vina vya vyanzo vya maji kama bahari na maziwa,vikaanza kupungua. Wachunguzi wakachunguza,wakagundua kuwa miale ya jua imekuwa mikali sana,yaani jua limeongezeka ukali wake.

Walipoenda kuitazama dunia waone kama itakuwa inapoteza mwelekeo,waliikuta ipo vilevile. Mwendo na sehemu ilipo,vilikuwa palepale. Yule mwanasayansi alitikisa kichwa na kusema mwacheni MUNGU awe vilevile MUNGU,hakuna ajuaye uwezo wa MUNGU”.Hans akawa anampa soga Eve ambayo kweli ilimvuta na kumfanya awe kimya.

“Mh! Hans wewe ni kiboko”.Alisifu Eve.

“Na si huyo tu! Wanasayansi wote wanamwamini MUNGU kuliko mtu yeyote. Kuna wale waliotengeneza maroboti. Wameweza vyote,lakini kumpa pumzi wameshindwa,wakasema hiyo ni kazi ya MUNGU. Hivyo japo wanajidai wajanja,lakini bado wanaenda nyumba za ibada na kumuomba MUNGU ili awasaidie”.Hans alizidi kutema madini kwa mtoto mzuri.

Kimya kikapita na kila mmoja akawa anaburudika na kiburudisho chake.Ni Hans ndiye alianzisha tena maongezi mengine.

“Sweetie,wajua kuogelea?”.Hans alimuuliza Eve.

“Mmmh! Mwenzako hata sijui”.Alimjibu Eve.

“Twende nikakufundishe”.Hans aliongea na bila kusubiri jibu alikuwa tayari kanyanyuka na kumnyooshea mkono Eve ili aushike naye anyanyuke.

Eve akabaki bila tendo.Kukataa anashindwa na kukubali anashindwa.Ila kwa kuwa alikuwa katoka na mtu,ilimbidi akubali.

Ni kama Hans alikuwa anasubiri sana kipengele kile ili aone alama ambayo Fred alisema kamchora Eve. Muda huo ukafika aisee.

Eve akatoa ule mtandio baada ya kunyanyuka na akabaki na nguo fulani kwa ajili ya ufukweni ambayo iliacha kiuno chake wazi.

Hapo Hans alicheka sana hadi Eve akauliza una nini.

“Daah!Nimemkumbuka sana Mzee Wa Upako. Jana nilimwambia natoka na wewe tunaenda beach akasema niangalie sana mavazi yangu. Sasa ndio nimekuangalia wewe mavazi yako na mimi,daah! Nimeamua nicheke tu! Hata hatuendani aisee”.Alidanganya Hans ila ukweli alicheka kwa sababu hakuona huo mwandiko ambao Fred alisema kamuandika Eve kiunoni.

“Ha ha haaa,utajiju. Wewe unakuja beach kama unaenda kucheza mpira”.Eve naye alishadadia na hapo akaanza kuelekea palipo na sehemu maalum ya kuogelea huku Hans akiwa pembeni yake.

Eve akatoa ule mtandio baada ya kunyanyuka na akabaki na nguo fulani kwa ajili ya ufukweni ambayo iliacha kiuno chake wazi.

Hapo Hans alicheka sana hadi Eve akauliza una nini.

“Daah!Nimemkumbuka sana Mzee Wa Upako. Jana nilimwambia natoka na wewe tunaenda beach akasema niangalie sana mavazi yangu. Sasa ndio nimekuangalia wewe mavazi yako na mimi,daah! Nimeamua nicheke tu! Hata hatuendani aisee”.Alidanganya Hans ila ukweli alicheka kwa sababu hakuona huo mwandiko ambao Fred alisema kamuandika Eve kiunoni.

“Ha ha haaa,utajiju. Wewe unakuja beach kama unaenda kucheza mpira”.Eve naye alishadadia na hapo akaanza kuelekea palipo na sehemu maalum ya kuogelea huku Hans akiwa pembeni yake.

Walipofika Hans ndiye alikuwa wa kwanza kujitupa majini na kuanza kuogelea huku Eve akiwa nje anaogopa kujitupa majini. Ilibidi Hans atoke na kumfata pale nje maji ya kumuuliza kwa nini ajumuiki naye.

“Mi naogopa bwana Hans”.Eve akamjibu Hans kwa sauti ya puani.

Hans akacheka kidogo na kisha akaanza tena maneno yake aliyobarikiwa na muumba.

“Ujue Eve usiwe kama mtoto mdogo bwana. Haya ni maji tulivu ambayo hayana kakala kama yale ya baharini. Haya ni maalumu hayawezi kupwa wala kujaa. Yale ya baharini kuna muda yanaenda mbali zaidi,na hapo watu ndipo wanapopata nafasi ya kuchezea fukwe za bahari. Lakini baadaye maji yale hurudi na kujaa fukwe yote hii.

Hii kama hujui inatokana na mzunguko wa dunia. Ngoja nikupe mfano hai”.Hans alitoka pale alipo Eve na aliporudi alirudi na chupa ambayo aliweka maji kiasi bila ile chupa kujaa,kisha akaanza kumwonesha anachomaanisha.

“KWA mfano,fanya hapa ndipo sisi tupo”.Akaonesha kule chini ya chupa ambapo chupa ilikuwa imesimamia.

“Si waona kuna maji eeh. Basi dunia inazunguka namna hii”.Akazungusha ile chupa hadi kule chini ambapo alisema ndipo wapo wao kukawa juu.

“Si waona maji yamehama eeh,na ukirudisha tena,maji yanajaa. Basi mfano huu ndio dunia ikifanyacho na ndio maana tunapata kupwa na kujaa kwa bahari.

Na ndivyo binadamu wengi walivyo,wapo wa kupwa na wapo wa kujaa. Kamwe usiyaogope maji bali ogopa walimwengu ambao ndio hawa watu.

Kuna muda huwa hawana madhara na mambo mengi,yaani wanakuwa wana roho nzuri na ya upole wenye wingi wa mambo. Hali hiyo hufanya watu wanajiita wanafunzi au wenye uhitaji wa kujua, waende kujiokotea chochote kupitia watu hawa.

Lakini kuna hawa wasiopenda kuchezewa sharubu,hawa ndio wazee wa kurudi na kujaa mahasira.Hawa si rahisi kuokota chochote kwao,kwani hawakupi nafasi hiyo hata kidogo. Muda wote wanakuwa wanamiliki eneo lao.

Sidhani kama wewe Swetie upo hivyo. Najua wewe ni kama mimi,siku zote ni watu wa kupwa tu! Tunaruhusu watu waokote chochote pale tunapokupwa. Kamwe usiruhusu kujaa bali jifunze kupitia wao pale wanapokuja kuokota chochote kwako”.

“Mmmh! Wewe Hans hayo yote unayoongea umeyatoa wapi? Mbona kama mwanafalsafa vile. Yaani haya makubwa,na madogo yana nafuu. Haya bwana,ngoja mi niendelee kuokota”.Eve alimwambia Hans baada ya Hans kuweka kikomo katika maongezi yake.

“Mi nilitaka ufahamu kuhusu kupwa na kujaa kwa bahari na ni vipi hali hii inaendana na maisha yetu. Kaa ukifahamu kuwa kila kitu hapa duniani kimeumbwa ili tukitawale sisi. Na kaa ukijua kuwa kila kitu kimeumbwa ili kitufundishe sisi jinsi ya kuishi na jinsi ya kufanya mambo yetu.

Kwa mfano,mchwa. Wale wameumbwa ili watufundishe jinsi ya kufanya kazi. Mti umeumbwa ili sisi tujue kutoa kama ujuavyo wenyewe kutoa kivuli na hewa safi”. Hans aliendelea kumpa maneno mazuri Eve.

“Mmmh! Hans unanidanganya bwana. Na je bata,kuku na mbwa. Hao nao wameumbwa kwa ajili ya sisi kujifunza kupitia wao?.Embu angalia tabia zao. Wanalelewa vizuri na mama yao lakini baadaye wanakuja kuzaa naye tena. Au kama ni mbwa dume,basi kila mbwajike linamtaka,huyo tena wasema kaumbwa ili tujifunze kupitia yeye?”.Eve alimuuliza swali ambalo lilimfanya Hans atabasamu kidogo na kusahau kuwa wameenda pale kuogelea na si kupiga stori.

“Kwani Sweetie,haya maisha umeumbwa kujifunza mazuri pekee?au mazuri na mabaya. Na hivi wajua kuwa mbwa anawakilisha dhambi katika vitabu vya dini? Mbwa alishalaaniwa kwa kupewa dhambi ya urafi. Huyo kuku na bata ndipo watu wanajifunzia tabia za ubakaji na mambo machafu ya kutembea hata na watu saizi ya wazazi wao.

Kila kitu duniani kimeumbwa kitufunze,niamini mimi Swetie. Lakini ndio hivyo,wapo wanaojifunza maovu na wapo tunaojifunza mazuri”.Hans alimwelezea Eve na Eve alibaki bila swali bali kumwangalia Hans bila kummaliza,na mwisho alitikisa kichwa kama kusikitika lakini alikuwa haamini yale aliyoyasikia.

“Vipi Swetie,mbona wasikitika?”.Hans alimuuliza.

“Wewe ni jiniazi Hans”.Alisema ya moyoni.

“Ha ha haaa,twende basi kuogelea kidogo halafu tuondoke si wajua jua linaenda hilo na usafiri wa huku ni majanga tupu”.Hans alitupa kete yake nyingine kumvuta Eve waende kuogelea.

“Lakini nikizama hii kesi ni yako”.Eve alitoa onyo mapema huku akisogea na kukaa kisha akaweka miguu yake kwenye maji yaliyo kwenye “swimming pool” ya pale.

Hans yeye alirudi nyuma kama hatua kumi kisha akaanza kukimbia kwa kasi sana kuelekea ilipo swimming pool ile. Alipofika karibu aliruka juu huku katanguliza mguu mmoja mbele kama anampiga mtu teke la uso. Hakuruka hivyo peke yake bali aliambatanisha na sauti ya kama ya kujikakamua.

“Iyaaaaa”. Baada ya sauti hiyo ilisikika sauti ya kutumbukia kwenye maji na eneo lile lilitapakaa maji kutokana na mtupo wake ule. Ni kama bomu lilitupwa kwenye swimming pool ile.

Eve kama walivyo wanawake wengine walikuwa hoi kwa kucheka na wanaume wengine waliokuwa eneo lile walikuwa wanashndwa kumtafsiri jamaa. Mbele ya mrembo kama Eve,anafanya kituko kama kile.

Hayo yote Hans hakuyafikiria bali alipoibuka toka kule alipokuwa amezama alimfata Eve pale alipo na kuanza kuongea naye huku ameweka mikono yake kwenye mapaja mazuri ya mwanadada yule.

“Njoo basi ndani na wewe”.Hans aliongea kistaarabu kama si yule aliyetoka kufanya kituko muda wa dakika moja uliopita.

“Yaani wewe bwana. Unavyoongea na mambo yako kama si wewe.Embu mwone kwanza”.Eve aliongea huku katabasamu na kumshika kidevu Hans.

“Kwani nimefanya nini Swetie. Embu acha hizo bwana,njoo tuogelee”.Hans aliongea huku akishika kiuno laini cha Eve na kuanza kumvutia ndani ya maji Eve.

Eve naye alikuwa hana kipingamizi bali kuingia ndani maji ila akiwa na uwoga kiasi fulani.

“Ukiogopa ndo unazama”.Hans alitania na kumfanya Eve atake kukimbia lakini Hans alishamkamata vizuri hivyo hakuweza kuondoka.

“Usijali Sweet.Unapokuwa na mimi,usalama unakuwa mkubwa kuliko hata ukiwa na usalama wenyewe. Mimi ndiye Hans The Man,usiogope”.Hans aliongea maneno hayo kwa sauti ya kunong’ona huku kamnyanyua Eve ndani ya maji. Mikono yake mmoja ukipita chini ya mapaja na mwingine nyuma ya mgongo na wakati huo Eve alikuwa kabana mikono yake kwenye shingo ya Hans.

“Ukinizamisha Hans”.Eve aliongea huku akiwa na uoga pale Hans alipokuwa anamshusha majini taratibu.

Alifanikiwa kumshusha na alikuwa kaweka mikono yake nyuma ya mgongo wa Eve na kumwambia aiachie miguu yake isiwe inagusa chini. Eve alifanya hivyo na alionekana kama anaelea. Tabasamu likaupamba uso wa Eve hasa alipojua ladha ya maji yale kwa kuyaoga bila kuzama. Uoga ukamtoka ghafla.

Na Hans naye ni kama alikuwa anamfundisha mtoto baiskeli,taratibu akaanza kumwachia Eve. Naye Eve alikuwa makini akiichezesha miguu yake. Hadi Hans anamaliza kuiachia mikono yake kutoka katika mwili wa Eve,Eve tayari alikuwa kishaweza kuogelea kifudifudi bila kuzama.

Watu walioona tendo lile hawakusita kupiga makofi kwa furaha. Makofi yale yalikuwa kama yanaenda kwa Hans kwa sababu wengi walioyapiga walikuwa wanawake.

Sasa wale matozi waliokuja na wasichana wao,mioyo yao sijui ilikuwaje. Lakini kwa Hans ilkuwa kama hatua moja kwenda mbele. Tatizo likabaki palepale,hawezi kumwambia kama anampenda Eve.

Hilo ni tatizo ambalo limesababishwa na wao wenyewe huko walipotoka. Hawakutaka kuwa na wanawake katika maisha yao,hivyo walikuwa ni waoga na wasiojua ni wapi pa kuanzia kusema nakuhitaji uwe nami katika dunia hii ya mapenzi.

Hans kama ilivyo kwa Junior na Fred,akabaki anaumia kwa maumivu hasa pale sifa za kuwa yeye ni mume mzuri wa Eve zilipokuwa zinatoka kwa watu waliokuwepo pale kwenye swimming pool.

“Hans umeniona?”.Eve alimtoa mawazoni Hans kwa swali hilo na kumfanya Hans apambe uso wake kwa tabasamu la kuchonga.

“Yeah.You did it Swetie”.Hans aliitikia huku akimfata Eve pale alipo na kumshika vizuri kiunoni na kumwomba waondoke kwa kisingizio muda umeenda.

Walitoka ndani ya maji na kuelekea zilipo nguo zao za mtaani. Walizivaa na kuchukua usafiri wa binafsi kuelekea yalipo makazi yao.

“Yuhuuuuu”.Hans alifungua mlango wa chumba anachokaa na kuingia huku akitereza kwa mguu mmoja na kutoa sauti hiyo.

Hakuta salamu bali aliingia kwa maneno ya kujigamba kama kawaida yao,.

“Basi mtoto nikamkamata namna hii kwenye kiuno chake laini kama manyoya ya kifaranga cha kuku. Nikamvutia kwangu taratibu,mtoto akavutika na hapo mdomo wangu ukawa unaelekea kwenye kinywa chake na kisha ndimi zetu zikatoka na kuingia kinywani kwa mwenzake. Wajua nini kilitokea?”. Hans aliongea huku akibakiza swali ambalo kila mtu alijua ni wapi alikuwa anaelekea kusema.

“Kwenda zako huko,unamdanganya nani kihivyo?”.Junior ndiye alianza kuongea huku Fred yeye akiwa bize na Biblia yake.

“Hujajibu swali mdogo wangu na tuachie kelele na domo lako linalonuka kama mavunja genge. Hata Swetie aliniambia kuwa unanuka mdomo,kwa hiyo chuna tu!”.Hans alimjibu na kumnyong’onyeza Junior.

“Sasa kama uongo asiseme bwana!! Acha uongo wako”.Fred naye aliingilia. Ni kama Hans alikuwa anamsubiri Fred aongee.

“Kwenda na acha kutuzingua wewe na Biblia yako. Kwanza unamtukana MUNGU kwa kujidai mtu wake wakati liongo balaa”..Hans alimwambia Fred.

“Mimi sijui kusema uongo,sema naendana na mazingira yenyewe. Kama mnajisifu na mimi nisijisifu?”.Fred alijitetea kabla ya Hans hajaendelea na lawama.

“Kwani nini aisee,mbona mnatuweka kwenye mafumbo?”.Suarez aliwauliza Hans na Fred.

“Si huyu anayejidai Baba Paroko sijui Mzee wa Upako. Alisema kamwandika mtoto kiunoni”.Hans aliongea na kukaa kimya na kusikiliza kama Suarez atakuwa anakumbuka maneno yale.

“Eee ndiyo.Jamaa alisema”.Suarez alionesha kumbukumbu zake.

“Basi mtoto hana alama yoyote kiunoni na huyu boya alisema ile alama yaweza kukaa mwezi bila kufutika. Jiongo kichizi,hiloooo”.Hans aliongea huku akimzomea Fred.

“Ha ha haaa. Embu usinikumbushe mwenzako. Hili jamaa mnadhani ni litoto humu? Hata kwa demu linaleta huu utoto.

Leo lilijidai li-Van Damme likajitupa ndani ya mimaji kama linguruwe. Ha ha haaaa”.Fred alijibu mapigo na kumwacha Hans akiwa kama amepata hasira.

“Kwa hiyo mwanangu tunafatana eeh. Si tuliagana hakuna kuingiliana katika ishu hizi? Mmeamua kunifatilia si ndio Wa Upako”.Hans alionesha wazi kaumia kwa kitendo kile.

“Hapa tumezidi kudanganyana ndio maana tumeamua kushuhudia kama hayo msemayo ni kweli. Ha ha haaaa,jamaa likajidai li-Chuck Norris. Eti iyaaaaaa,halafu pwaaaaah. Mimaji eneo lote kama gunia la mahindi limedondoshwa toka juu ya ndege na kutua kwenye bwawa,kumbe li-mtu,halafu jitu zima tu! Ha ha haaaa”.Junior naye aliongezea maneno na kumfanya Hans limshuke kama kapigwa na maji ya baridi.

“Sisi hatujakuingilia Hans. Ila na sisi tuliamua tuje kufurahi coco ndio tukakukuta na wewe. Tungekuingilia tungekuja hadi pale,lakini hatukuja bali kukuangalia jinsi ulivyojitupa ndani ya maji kama dubuwasha.Ha ha haaaa”.Fred aliongea na kuzidi kucheka.

ITAENDELEA

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 4

Leave a Comment