MPANGO WA KANDO SEHEMU YA NNE
IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA
*********************************************************************************
Simulizi : Mpango Wa Kando
Sehemu Ya Nne (4)
MWANAJESHI ni mwanajeshi tu bila kujalisha kuwa yu mzee ama kijana. Licha ya umri wake kuwa umeenda lakini bado ule ukakamavu wa kijeshi bado ulikuwepo katika damu yake.
Ni kweli alikuwa amedhibitiwa vilivyo na mwanadada yule anayejitambulisha kwa jina la Tz 11 lakini mwanaye alipoingia pale ndani mzee Bosco alijikaza na kujaribu kusema neno lakini haikuwezekana, alikuwa amevunjwa taya yake tayari, alijaribu kusema akaishia kutema damu tu!!
Ama! Damu nzito kuliko maji, Sofia hakuwahi kudhani kuwa ipo siku ataingiwa na huruma itakayompeleka katika kutokwa machozi, aliwahi kuhudhuria misiba mingi lakini hakuwahi kudondosha chozi, sasa anamtazama baba yake mzazi akiwa katika hali ile mbaya anajikuta akitokwa na machozi hasahasa alipomuona mzee Bosco akijaribu kuzungumza lakini akishindwa kabisa.
Sofia alijiongeza, akamsogelea baba yake ili kuona kama kuna lolote anaweza kupata kutoka kwake, wakati huo bunduki yake ikiwa sawia katika kiganja cha mkono wake.
Akainama na hapo mzee Bosco akaukaza mkono wake akachovya damu iliyokuwa imemtoka na kutapakaa sakafuni.
Baada ya kuichovya akajikokota pembeni kidogo hadi katika sakafu isiyokuwa na damu, akaushusha mkono wake ule uliokuwa na damu. Akajikaza kiume akaandika kwa kutumia ile damu aliyoichovya awali.
“TZ 11”
SOFIA akasoma aliyoandikiwa bila kuelewa lolote, mzee wake akamsihi kwa vitendo kuwa atoke nje.
Kuna mambo mengi ya kupuuza katika huu ulimwengu lakini linapokuja suala la nduguyo wa damu tena ambaye ni baba mzazi hapa unaweza ukajikuta ukipuuzia mambo mengi ambayo uliwahi kufundishwa huku ukisisitizwa kuyazingatia bila kujalisha u pamoja na nani.
Sofia alitambua wazi kuwa baba yake amekuwa mwanajeshi kwa miaka mingi na hata alipomwamuru atoke nje basi kuna kitu alikuwa anamaanisha, lakini unaanzaje kutoka nje na kumwacha babako mzazi akiwa anavuja damu huku taya ikimuanguka?
Sofia naye alikuwa muathirika wa hali hii ya kibinadamu, alisita kutoka akamfuata baba yake pale alipokuwa huku akiwa hajui ni kipi cha kufanya, alipofika paler mzee Bosco akajitutumua na kutokwa na teke dogo kwenda kwa mwanaye likampata katika mguu wake.
Sasa akili ya Sofia ikafunguka akatambua kuwa yeye si tabibu hata akibaki pale ndani ni kazi bure tu, alichotakiwa ni kuwaachia matabibu kazi yao na yeye aende kuitafuta maana ya Tz 11.
Akatoka upesi, akamkuta katibu muhtasi akiwa ameuvuta mdomo wake na kuzidi kuifanya ile sura yake isiyokuwa na mvuto kuwa mbaya zaidi.
“Upesi wasiliana na viongozi wako… mzee Bosco anatakiwa kupata tiba ya upesi sana….. nimekuamuru si ombi!!” alizungumza kwa kumaanisha. Macho yake makali yakaulainisha ule mdomo wa yule dada na kuurejesha katika hali ya kawaida kisha ukaingia katika mshangao!!
Sofia hakungoja jibu lolote, upesi akaenda hadi katika mgahawa, alipofika pale mgahawani akashangaa kuona watu wanakurupuka, ni hapo ndipo alipojitazama na kugundua kuwa bastola yake ilikuwa mkononi mwake na jinsi alivyoingia kwa kasi kubwa pale ndani basi ilikuwa si jambo geni hata kidogo kwa hali ile kutokea.
Upesi akaihifadhi ilebastola na kisha akaelekea katika meza aliyomuacha Pocha…
Pocha hakuwepo!!
Alimngoja kwa dakika tano zaidi lakini hakuonekana.
Hofu mpya ikatanda!!
Lakini hofu ile haikudumu sana, Pocha akarejea asijue kuwa Sofia anakabiliwa na tatizo jipya.
“Ulienda wapi Pocha na tuliagana kuwa unabaki hapa mpaka narejea?” Sofia alihoji kwa ukali.
“Kuna rafiki yako mmoja hapa nilikuwa nimemsindikiza hapo nje kidogo…”
“Rafiki? Nilisema nina rafiki huku?”
“Aah! Hapana iola kuna kitu ameniagiza kwako nikaona si vibaya nikimsindikiza walau nimjue kidogo tu….” alijitetea Pocha na kisha akaendelea kuzungumza huku akiona hasira ya Sofia waziwazi.
“Amesema amependa ulivyomuangalia…. neno lake hilo likanivuta zaidi kwake kujua kulikoni… nafsi yangu imejikuta tu!!…. na mwisho akasema ukija nikusalimie…”
“Pochaa! Unaongea sana niambie ni nani?”
“Tz 11” alijibu Pocha kwa uoga kiasi.
Jibu lile likamweka Sofia katika bumbuwazi… akakumbuka maneno ambayo aliandikiwa na mzee wake kwa kutumia damu, ni jina hilohilo….
Sasa Sofia akagundua kluwa Pocha analo jambo la muhimu zaidi ya alivyokuwa anajenga ghadhabu juu yake. Akamuhoji Pocha kwa utulivu juu ya huyo Tz 11.
Pocha akaelezea kuwa ni binti fulani mrembo tu halafu mdogomdogo.
Majibu ya Pocha yakamvuruga Sofia, binti mdogo mdogo anawezaje kumvunja taya mzee jasiri na imara kama Bosco.
Mtihani ukaanza kuwa mgumu, sasa haikuwa tena kwa usalama wa Pocha pekee bali kwa ajili ya baba yake.
Na hakuna aliyehitajika zaidi ya Tz 11.
Ni huyu ambaye angeweza kutoa majibu yote.
_____
TOFAUTI na nyakati nyingine ambazo familia ya Caro huwa na furaha sana pindi Caro anaporejea kutoka London kuja kuwasalimia, safari hii furaha haikuwa kubwa sana.
Kuna jambo ambalo lilikuwa linawatatiza na mwenye majibu alikuwa ni Caro peke yake, walipanga kuwa muda utafika na watamuuliza ni kitu gani ambacho muheshimiwa Lucas huwa anaenda kufanya uingereza. Na wakati huo walikuwa wamejiandaa kumuuliza iwapo anaifahamu nambari ya simu ile ambayo ilitumika kuzungumza na mama Caro kisha kumweleza juu ya muheshimiwa.
Mpasuko uliokuwepo haukuwa mdogo, Edwin rafiki yake Lucas na mume halali wa mama Caro alikuwa anahisi kuwa huenda mkewe alikuwa na mahusiano na Lucas nd’o maana akapigiwa simu ile na kuelezwa kuwa amekaa tu mwenzake anaenda London kufaidi maisha na binti mwingine.
Mama Caro alizipinga vikali shutuma zile na yeye akataja hisia zake kuwa yawezekana kabisa Mheshimiwa Lucas ana mahusiano na mtoto wake wa kike Caro!!
Hivyo ni neno la Caro ambalo lingeweza kurejesha amani katika nyumba hiyo.
Baada ya kupokea zawadi kadha wa kadha kutoka kwa Caro hatimaye wadogo zake caro na ndugu wengine waliwapisha watatu hawa sebuleni kwa kile ambacho baba caro alidai ni mazungumzo muhimu.
Walipobaki watatu, wasijue kabisa kuwa mchezo wanaotaka kuucheza tayari umechezwa kimataifa na matokeo yalikuwa wazi, wakajaribu kuucheza tena.
Baba Caro akamuuliza Caro ju ya maisha yake jijini London na ukaribu alionao na muheshimiwa.
Caro hakushtushwa na tuhuma zile kwani ni siku mzili zilizopita alizungumza na Lucas na kuamua nini hatma ya mahusiano yao, wakaamua kuwa yaendelee kuwa ya siri la ili kuondoa utata huo basi wauzunguke mbuyu na kuwachota akili wazazi wake.
Caro akatumia fursa ile kuumaliza mchezo kisayansi.
“Naishi vizuri sana na ninafanya kazi zangu kwa mafanikio, Mheshimiwa huwa tunaonana naye mara moja moja kuna muda anakuja London na hatuonani kabisa, kuna mfanyakazi mwenzangu aliniambia kuwa mheshimiwa ana mchumba wa kizungu maeneo ya jiji la Liverpool, hivyo huwa anakuja na kuishi pale. Ujue ninapoishi mimi na kufanya kazi ni mbali sana kutoka Liverpool, hivyo sikutilia maanani na hadi sasa sitaki kujishughulisha na mambo yake… ujue wanaume wote naona tabia yao moja tu, labda wewe tu babab yang undo siwezi kukusemea lakini pale London hii ni tabia mtu anakuwa na mke pale London halafu jijini Manchester ana familia nyingine… ila tafadhali sana sina uhakika na hizi tuhuma sitaki kuitwa ushahidi, sitaki kuchanganywa kabisa kwa sasa nipo na maisha yangu…” alijibu kwa kirefu akiwa ametulia kabisa.
Jibu lake liliupooza moyo wa mzee wake pamoja na kuutuliza kabisa mtima wa mama yake.
Majibu ya kupangwa yaliyofanyiwa mazoezi ya kutosha!!
Jibu likairejesha amani!
Hawakujua kabisa kuwa mtoto wao alikuwa akiwachezea shere!
_____
Baada ya kutoka katika mgahawa wa magereza Tz 11 alitoa taarifa kwa bosi wake wa Nairobi akamueleza kila kitu alichoelezwa na Luteni mstaafu Bosco.
Akamueleza kuwa Bosco alikuwa akimfuatilia Manfredy Gregory kwa sababu alienda pale gerezani kumuulizia Pocha!
Akaelezea zaidi kuwa hata Bosco mwenyewe hajui ni kwa nini Pocha anafuatiliwa.
“Ulifuatilia na kumjua Pocha ni nani?” alihoji mwanadada wa Nairobi.
“Haikuwa katika makubaliano yetu mkuu… hiyo ni biashara tofauti kabisa!” alijibu kikaidi Tz 11.
Mwadada wa Nairobi akatokwa na tusi zito kwa lugha ya kiingereza, kisha akamuuliza anahitaji kiasi gani ili aweze kuifanya kazi kikamilifu.
Tz 11 akaitaja bei yake, dada wa Nairobi akamwambia aende kufuatilia huyo Pocha ni nani na kwa nini anatafutwa na Manfredy Gregory ‘Chopa’.
Tz 11 akaingia kazini tena….
_____
Umbile la mwanadada aliyezengea zengea katika mgahawa wa magereza ulivutia macho ya yeyote yule anayependa kutazama.
Dada yule alichukua nafasi huku marashi yake nayo yakisumbua pua za wanusaji wengi katika namna ya kuvutia na si kukera.
Muhudumu alifika na kumsikiliza haja yake, akaeleza kuwa anahitaji maji baridi makubwa. Muhudumu akaomba pesa yule dada mrembo akalipia.
Mazingira yale hayakuwa mageni kwa mteja huyu ni muda mchache sana uliopita alikuwa ametoka kuhudumiwa.
Kwa jinsi alivyojiweka alijuwa waziwazi kuwa wanaomtazama kimatamanio ni wengi sana na yupo ambaye atapenda kujitoa muhanga kati ya wengi wale wanaomtamani.
Hata kabla hajamaliza kufikiria ni nani ambaye atajipeleka katika himaya yake, tayari aliisikia sauti ya kiume ikimuuliza iwapo wanaweza kuketi wote.
Dada yule akatabasamu vizuri huku akiyaruhusu meno yake mawili ya mbele kuonekana.
Yule bwana akaketi kindakindaki akijiona ndiye aliyebarikiwa kupita wateja wote.
Binti yle alimtazama kwa chati, akagundua kuwa alikuwa ameketi na askari wa kawaida kabisa katika ile meza.
Alijua kitakachofuata baada ya hapo ni kusifiwa kuwa yeye ni mrembo sana na mambo mengine kemkem ambayo aliyazoea tangiapo.
Maaskari kwa tamaa!!! Naji asiyejua….
Kweli akaanza kutoa sifa kedekede, binti yule naye akazipoe kwa utulivu, wakazungumza mengi huku yule binti naye akimsifia kuwa anafurahisha sana kuzungumza naye.
Bwana yule alikuwa anakwepa sanakujitambulisha kazi yake lakini hakujua kuwa yule binti tayari alikuwa anjua kila kitu licha ya kwamba alivaa nguo za kiraia.
“Yaani hapa kuna kaka yangu alikuwa anaendesha pikipiki jana akagonga kibanda cha mama mmoja hivi basi pikipiki yake imekamatwa ndo najiuliza atakuwa kituo kipi. Hapa ninamtafuta askari mmoja hivi anisaidie….” binti alimueleza yule bwana.
“Unamjua kwa cheo chake au majina kama unajua jina lake nambie maana mimi hapa ni mzoefu sana nawajua watu….” alijibu akiendelea kuficha kazi yake katika namna ya kizembe.
“Dah! Kaka yaani hapa ni kama vile natwanga maji kwenye kinu, hata nikiomba kusaidiwa naona maelezo yangu hayajitoshelezi kabisa…” alijibu yule dada akionyesha kukata tamaa.
“We sema tu dada, huwezi kujua labda hata unanitafuta mimi hapa..” alisema yule bwana.
“Kwani na wewe ni askari?” mwanadada alimuuliza huku akionyesha kushangaa, yule bwana akafadhaika kuwa janja yake ilikuwa imefikia ukingoni ikabidi akiri tu nkuwa hiyo ndiyo kazi yake.
“Sawa basi mimi namtafuta mtoto wa luteni nani sijui.. Bosco eeh! Luteni Bosco nimeambiwa huku nd’o naweza kumpata yaani nikimpata huyo naamini kaka yangu atatoka maana nimesoma naye shule moja ya sekondari na kiukweli hapa mjini bila kujuana….. utaishia kulia kila siku.” Alijieleza kwa utulivu.
Yule askari akaguna kisha akafikiri kwa muda kiasi.
“We unamfahamu mtoto wake ukimuona?” askari akamuuliza.
“Hata ikiwa usiu wa manane nitamjua yule binti…” alijibu kisha akatabasamu.
“Dah! Hapa dada labda tu mimi niangalie uwezekanowa kukusaidia lakini kama ni ishu ya Luteni Bosco kuna tatizo alipatwa presha ikawa imepanda amepelekwa hospitali hapo Muhimbili na bila shaka watoto wake wote watakuwa hukohuko….” alijibu kwa sauti ya chini.
Yule dada akatoa maelezo ya uongo kabuisa juu ya huyo kaka yake aliyekamatiwa pikipiki, kisha akampatia ile namba ya simu yule askari ikiwa kuna lolote basi ampe taarifa.
Ilikuwa ni ndoto ya mchana askari yule kuipata namba ya dada yule mrembo.
Lakini ilikuwa ushindi mkubwa zaidi kwa yule mwanadada kwa kufahamu fika kuwa mzee Bosco amekimbizwa Muhimbili na mtoto wake atakuwa hukohuko.
“samahani jina nisevu nani” askari alimuuliza.
“NIchagulie lolote tu.. lakini ukikosa kabisa nisevu TZ 11” alimaliza kujibu huku akiwa amempa mgongo yule askari.
Akatoweka pale na sasa alikuwa nauhakika wa kumfahamu Pocha kupitia mtoto wa luteni Bosco.
Hakuwa akijua kabisa kama Sofia ndiye mtoto wa luteni. Hivyo alitarajia wepesi kabisa katika kuufanikisha mchezo wake.
______
KITENDO cha kuambiwa na Pocha kuwa kuna mwanadada ametuma ujumbe kuwa amependa macho yake jinsi alivyomuangalia, ujumbe huu ulikuwa na maana ya kawaida kabisa kwa Pocha ambaye hakuna kitu alichokuywa akikijua, na mwanadamu yeyote yule wa kawaida angeweza kuutafsiri ujumbe huu moja kwa moja vilevile, lakini kwa mwanadamu asiyekuwa wa kawaida huu ulikuwa ujumbe mzito sana.
Naam! Sofia naye hakuwa mwanadamu wa kawaida!
Aliielewa maana ya mtu wa kariba yake kusema ameyapenda macho yake, hii ilimaanisha kuwa mtu huyo amemtambua ujuzi alionao na anatamani wakabiliane.
Sasa baada ya kukabiliana na wahalifu nchini uingereza alipokuwa katika masomo kwa vitendo hili linakuwa jaribio la kwanza kabisa kwa mwanafunzi huyu aliyebobea katika mamabo ya upelelezi wa kimataifa na mapigano ya aina zote, aidha kutumia silaha ama la!!
Kuanzia alipopewa taarifa ile na Pocha aliongeza umakini huku akizifuata kanuni zote zlizofundishwa kambini na zile alizojifunza kulingana na matukio aliyokuwa ameyapitia.
Macho ya yule binti waliyetazamana naye ndicho kitu pekee alichokuwa anakikumbuka ili kumtambua adui yake, zaidi ya hapo hakuwa akikumbuka kitu kingine hivyo umakini wake mkubwa kabisa aliutilia katika kuyatazama macho ya raia anaopishana nao, zaidi ya yote alijitahidi wasitambue ikiwa alikuwa anawatazama.
ANMA KWA HAKIKA kila mjanja ana mjanja wake, na pale wanapojikuta ulingoni wajanja wawili basi mjanja mmoja anatakiwa kubuni ujanja wa ziada ili aweze kumshindwa mjanja mwenzake.
Wakati Sofia anawatazama machoni watu ili aweze kumbaini huyo binti wa kutisha anayejiita Tz 11, yeye Tz 11 alikuwa ameyafunika macho yake miwani kubwa ya jua yenye mahadhi ya kike.
Hakufanya hivi kutokana na kwenda na wakati japokuwa alikuwa amependeza, alifanya hivi ili kujiweka katika uhalisia usiokuwa wake kwa wale ambao labda waliwahi kuonana naye kabla ya tukio lolote lile.
Hadi anafika pale Muhimbili alikuwa ameyaziba macho yake, alipita jirani kabisa na Sofia aliyekuwa makini kutazama macho ya watu ili ajue nani hatari kwake.
Maskini Sofia alikuwa amezidiwa ujanja, Tz 11 akaingia moja kwa moja hadi mapokezi. Hapo alihitaji kujua ni wapi alipolazwa mzee Bosco.
Lengo kuu likiwa kumuona mtoto wake ambaye ndiye anayefahamu juu ya Pocha!!
_____
WAKATI Pocha akiwa anasakwa huku pia akiwa analindwa, kuna mtu mwingine naye alikuwa anamuwaza… huyu alikuiwa ni Chopa. Aliwaza mengi sana juu ya rafiki yake kipenzi wa gerezani ambaye alikuwa mkombozi aliyekuwa anahitajika sana wakati huu, alikuwa anatembea barabarani mwili tu lakini akili yote akiwa ameilaza kwa Pocha.
Kuna wazo lilimsihi kuwea asijihangaishe kwani Pocha aligeuzwa bibi gerezani na kuishia kuambulia magonjwa hatari ukiongezea na msongo wa mawazo basi swahiba wake yule aliaga dunia.
Wazo hili lilimfanya ajikute anayafumba macho yake na kisha kuingia katika hisia za uchungu sana, hatmaye likamtoka neno.
“Inalilah wahinalilah rajun!”
Alipomaliza kumwombea dua rafiki yake ikiwa aliaga dunia, akafikiria juu ya huyo mbunge ambaye alidai kuwa ili yeye awe huru basi labda mbunge huyo awe ameajiuzuru siasa ama amaetoka madarakani.
Alipowaza hivi akakumbuka ghafla gazeti alilolisoma jana yake katika vibanda vya kuuzia magazeti na vitabu.
“MHESHIMIWA LUCAS ATUA NA MAZITO KUTOKA UINGEREZA. awashukuru wanamwanza aamua kuachana na siasa za majukwaani, autema ubunge!”
Chopa akajiweka kando na barabara alipokiona kibanda kingine, akaenda tena ili kusoma yaliyojiri katika magazeti ya siku hiyo.
Alitamani sana kuiona tena ile habari ikiwa imeendelea kuandikwa ama zilikuwa fununu tu.
Alipofika alikuta watu wengi, kama ilivyo kawaida ya wat kujadili wanayoyasoma hasahasa kuelekea kipindi cha uchaguzi. Alijibanabana akapenya hadi akayafikia magazeti na kuanza kupitia kichwa kimoja kimoja hasahasa magazeti yaso’kuwa ya udaku.
“NI RASMI MBUNGE WA MWANZA AZUNGUMZA NA WAANDISHI.
HATIMAYE LUCAS AACHIA UBUNGE KABLA YA WAKATI
KUNANI MWANZA?
SIRI NZITO IMEFICHIKA KATIKA UAMUZI WA LUCAS”
Hivyo vilikuwa baadhi tu ya vichwa vikubwa vya magazeti.
Chopa akajifutia ile imani kuwa yawezekana Pocha rafiki yake alikuwa ameuwawa, badala yake akaipandikiza kauli ya kwamba huenda Pocha yupo huru uraiani.
Na ametolewa kimyakimya nd’o maana hata jina lake katika orodha ya wafungwa halikuwepo…..
Nini cha kufanya?
Hilo likawa swali gumu sana ambalo utekelezaji wake ulihitaji utulivu sana, Chopa alipoufikiria ukubwa wea Tanzania akajikuta anakata tamaa.
Alihisi kuwa kama kweli Pocha yupo huru basi atakuwa ametolewa kwa masharti kuwa asionekane mjini badala yake akaishi mbali kabisa.
Mambo haya aliyoyafikiria jambo jepesi lilikuwa moja tu, kuamini Pocha ni mfu ambapo angepiga goti kumuombea dua.
Hayo mengine yote aliyoyafikiria yalihitaji sana awe na pesa ya kutosha ili aweze kuwa anahonga hapa na pale, akaikumbuka kadi yake ya benki aliyoenda kuijaribu akajikuta alisahau namba za siri.
Akajiweka katika utulivu na kujaribu kukumbuka zaidfi, mara ikawa kama ndoto vile akaikumbuka siku moja aliyoenda kutoa pesa akiwa pamoja na caro ni siku hiyo alibadili namba ya siri na akaweka aidha mwaka wa kuzaliwa wa caro ama akaunganisha miaka yao wote wawili kwa ufupi… na hilo lilikuwa wazo la Caro.
Mambo yote angeweza kusahau lakini sio tarehe na mwaka wake wa kuzaliwa.
Akajiwekea ahadi kuwa siku inayofuata ataenda tena katika mashine nyingine za kutolea pesa ili aweze kujaribu, alihitaji kujua je? Ile kadi inafanya kazi ama haifanyi kazi tena….
Laiti kama angejua maana ya ule usemi wa kikulacho ki nguoni mwako, basi angekisaka upesi na kukitupilia mbali.
Chopa hakujua!!
Akafikiria kupata anuani za huyo mbunge aliyekuwa ameshika vichwa vya magazeti ili aweze kuanza harakati za kumsaka rafiki yake.
Ikiwa bado yupo hai!!
_____
HOFU!!
Wakati heka heka nyingine zikiendelea hapa na pale, hekaheka nyingine zilikuwa zimefunikwa katika chungu cha familia ya bwana Lucas zikisubiri siku ya kulipuka.
Na siku ya kulipuka huwa haijulikani, hili bomu ni ndoa ya mashaka.
Ndoa ikitawaliwa na mashaka, aidha mke kuwa na mashaka na mumewe ama kinyume chake, ndoa si ndoano bali ni bomu lenye hatari kubwa ambalo likilipuka madhara yake ni makubwa sana.
Ndoa ya Lucas ilikuwa katika dhahama hii.
Wakati mheshimiwa Lucas anazungumza na waandishi wa habari juu ya hatma yake ya ubunge na nini sababu alitarajia kuwa akifika nyumbani mkewe atazungumzia hizo siasa lakini mkewe alikuwa mtulivu kabisa hakusema neno lolote zaidi ya kumwambia kuwa anayaheshimu sana mawazo yake.
Ile hali ya utulivu ya mkewe ikamfanya ashangazwe sana haikuwa kawaida ya ubavu wake ule kuwa hivyo!
Alihisi kuwa labda mkewe hajapendezwa na maamuzi yale, akaamua kuwa mkimya pia ili asizue mengine.
Wakati anadhani ukimya huu utadumu sana, mara mkewe akaja na shambulizi la ghafla.
“Na mimi naachia ngazi ubunge naomba tufanye biashara wote huko London… nikusaidie kusimamia..” alizungumza Christina akiwa hana hata chembe ya utani.
Hoja hii ilikuwa sawa na ngumi nzito sana iliyotua juu ya paji la uso la Lucas na kumtupa chini akabaki anatapatapa.
Ilipita daklika moja ya mshangao, Christina hakuongeza neno wala Lucas hakujibu kitu.
“Uingereza? Aah! Sasa mke wangu wananchio wanakuhitaji sana ujue hautakuwa umewatendea haki….” alijiumauma Lucas
“Ila wewe ndiye umewatendea haki wananchi wa Nyamagana kwa kuwaacha ghafla hasahasa kipindi hiki wanachokuhitaji zaidi, tazama ulikuwa chama cha upinzania mwaka 1995 wakakuamini na kukupa ridhaa ya kulichukua jimbo lao, ukahamia chama tawala wasichokipenda lakini hawakujali chama wakakuchagua tena kwa kishindo tu…. leo hii unaenda London na unarejea unawaambia kirahisi tu mi sitaki kuwa mbunge tena… shame upon you Mheshiwa… si afadhali mimi ni mbunge wa viti maalumu sijafanya siasa za kuiba mioyo ya watu… mimi nitamuudhi muheshimiwa raisi tu aliyeniteua lakini sio maelfu kwa maelfu….” alijibu kwa ghadhabu kubwa sabna Christina, uso wa Lucas ukagwaya, kamwe hakuwahi kumuona mkewe akiwa katika hali ile kwa kipindi chote cha mahusiano yao.
“Lucas hii haina mjadala tutaenda wote London nasema, siutaki ubunge nakutaka wewe Lucas…..”ubunge haunimi ile amani niliyokuomba Lucas miaka iliyopita, ubunge haunipi mapenzi haya, ubunge ni mapito wewe ni wangu wa kudumu nakupenda Lucas…. nakupenda….!!” alisihi sana Christina na sasa machozi yalikuwa yanamtoka huku akizungumza.
Mambo haya yalimchanganya Lucas ambaye hakuwa na mapenzi ya dhati kwa mkewe na hata mpango wake wa kwenda uingereza ni ili kujiweka mbali na mkewe na kujikita karibu kabisa na mtoto wake aliyempata hukohuko uingereza.
Sasa wakati akiamini kuwa mambo yamefikia alipokuwa anapataka anakutana na mkewe akihitaji kuambatana naye kwenda kuishi uingereza.
Hofu ikatanda!!
Alijiuliza ni wapi mkewe amepata wazo la kufanya maamuzi yale…. hakupata msawazisho upesi.
Na laiti kama angeupata msawazisho usiku ule si bure angeweza kurukwa na akili.
Mkewe alikuwa amebeba kitu kizito sana……
Wakati Lucas akipata hofu sehemu nyingine katika jiji hilohilo palizuka hofu kubwa zaidi kwa mtu aliyejihesabia kuwa hawezi kuwa na hofu katika maisha yake.
_____
KITENDO cha kuyaficha macho yake kilimrahisishia kazi ya kupata alama tatu za mapema kabisa dhidi ya mpinzani wake ambaye walikuwa hawafahamiani vizuri, kilikuwa ni kitendo cha sekunde chache sana, wakati Sofia ameitwa ili kuweka sahihi juu ya baba yake kufanyiwa upasuaji ndipo Tz 11 alipokuwa akipasubiri ikli aweze kumchukua kijana aliyekuwa ameambatana na Sofia kwa muda mrefu.
Alifika na kumwekea bunduki na kisha kumsihi kwa utulivu kabisa kuwa amfuate.
Nani mjanja mbele ya silaha hii ya moto?
Hakuna!!
Akalazimika kumfuata, Tz 11 alipenya na mateka wake hadi akaifikia taksi, akamuingiza mateka wake nakumwamuru dereva aondoe.
Ile haikuwa teksi ya kawaida, ulikuwa ni mpango wa Tz 11.
Walipoketi akaiondoa miwani yake na kumtazama mateka wake.
“Tz 11…” mateka alimtambua kwa jina lake.
“Nambie Possian” ilijibu sauti ya Tz 11 huku akichanua tabasamu tamu kabisa.
Possian ‘Pocha’ alibaki akiwa amekodoa macho asijue ni kitu gani kilikuwa kinaendelea, lakini alijua kuwa ametekwa, kilichomduwaza ni kitendo cha kutekwa na yule binti mrembo.
Tz 11 hakujishughulisha na mshangao wa Pocha badala yake alichukua simu yake kisha akapiga kwenda Nairobi.
“Unaweza kuzungumza na huyu Pocha anayetafutwa na jamaa yako…” alizungumza kwa utulivu.
“Zungumza naye vizuri kisha naomba umchukue na Pocha mjuweke eneo salama kabisa, nakuja Tanzania baada ya siku nne au tano…..”
Tz 11 akakata simu baada ya kupewa agizo lile, ilikuwa ni kawaida yake hanyenyekei!!
Tz hakusubiri mazungumzo yamuda mrefu badala yake alianza kumuhoji Pocha.
“Nd’o ukanidanganya unaitwa Possian we mwanaume mbaya kweli mbona mi nilikwambia jibnalangu jamani….” Tz 11 alijaribu kuukumbushia usichana wake akazungumza kimadeko.
“Hapana sijakudanganya mkuu, naitwa Possian Clement Haule kifupi chake ni POCHA” alijibu kwa nidhamu ya hali ya juu Pocha.
Tz 11 akatokwa na tabasamu kutoka moyoni baada ya kusikia utambulisho ule. Akamuuliza maswali mawili matatu hadi pale walipoufikia mwisho wa safari yao katika nyumba asiyoijua.
Akaingizwa chumba cha kwanza na huko wakakuta mlango mwingine na penyewe akaingizwa.
Kilikuwa chumba kikubwa sana chenye kila kitu kasoro uhuru tu.
Akafungiwa pale ndani bila kuambiwa kitu chochote kile.
Baada ya masaa mengi kupita aliletewa chakula na yuleyule binti, safari hii binti akiwa amevaa kinguo cha kulalia ambacho kilikuwa kinaonyesha mapaja yake vizuri kabisa aliposimama kwenye mwanga.
Pocha akajikuta yu katika matamanio licha ya kuwa hakuwa akijua ni kwanini alitekwa na kupelekwa pale.
Wazo la kishetani likamkumba Pocha akajikuta akijisemea.
“Au ameniteka ili niwe mpenzi wake… ikiwa hivi nitafaidi kweli!!!” wazo lile likasindikizwa na funda la mate ya tamaa yaliyopita katika koo lake.
Yule binti alimuuliza maswali ya hapa na pale na kisha akamuuliza anauhusiano gani kati yake na mtu anayeitwa Chopa.
Hili lilikuwa swali lililomkurupua Pocha na kutambua kuwa hayupo pale kwa sababu ya mapenzi bali kuna jambo asilolijua limemfikisha pale alipo….
Swali hili ambalo alilijibu kiufasaha lilikuwa mwanzo wa yeye kufikiria mbali zaidi ambapo matekelezo yake yalizaa hofu isokifani kwa mwanadada TZ 11 ambaye anajiamini kuwa hakuna wa kumtia hofu!!
Matekelezo yake yakazua kipande kingine katika mkasa huu wa Ripoti kamili kiitwacho HEKAHEKA!!
HEKAHEKA!
ILIKUWA NI BAADA YA SIKU mbili kupita Pocha akiwa mtu wa kuletewa chakula kisha kufungiwa katika chumba kile ndipo akapandwa na hisia za ajabu kuwa Tz 11 hana nia nzuri kwake na pale alipo huenda amekaa akingoja kuuwawa tu baada ya kusingiziwa kesi isiyomuhusu.
Pocha akajiwekea matazamio ya kufanya juhudi zozote ilimradi tu aweze kutoroka ama kama ni kuuwawa basi auwawe akiwa anapambana.
Matazamio yake yalianza upesi kivitendo na ile anapiga hatua ya kwanza kabisa alijikuta anatabasamu tu peke yake ni kama mchezaji aliyerejeshwa katika uwanja wake wa nyumbani, mashabiki wakipiga kelele za juu kabisa wakimshangilia, mchezaji anajikuta akipatwa na nguvu sana na hatimaye kujikuta akiangukia upande wa ushindi.
Pocha alikutana na mlango uliofungwa kwa kutumia namba za siri, akaunyoosha mkono wake na kuzigusa zile namba, na bila kufikiria kwa muda mrefu akabofya kile kilichokuja katika kichwa chake kwa muda ule.
Alipofanya kwa mara ya kwanza akawa amekosea, akagusa mara ya pili, safari hii akausikia mlango ukiachia akauvuta na kuingia katika chumba kingine.
Kosa alilofanya ni kuingia kwa pupa baada ya kimuhemuhe cha kutoroka kumkumba, ile anaingia paole ndani alijikuta akikutana na ngumi kali ya usoni, kizunguzungu kikamshika akasaidiwa na ukuta hakuanguka chini akaangukia ukutani, akayafumbua macho yake akawa anaona watu wanne wanne kama sio watano, hata lile teke lililorushwa aliona ni mateke takribani matano yakimwendea akajikinga uso teke likaingia mbavuni, sasa akatokwa na mayowe huku akiomba kusamehewa.
“Nahitaji ufungue huu mlango ndani ya dakika moja….” sauti ilimuamrisha.
“Nafungua usinipige nafungua!!” Pocha alitetea huku akiwa ameuziba uso wake, alikuwa akitarajia shambulizi jingine kutoka kwa yule bwana mashuhuri wa kuadhibu.
“Upesi simama!!” sauti iliamrisha. Pocha akasimama huku akiuachia uso wake ili kumtazama mtu anayemuamrisha.
Alikuwa aneinama lakini ghafla alijikuta yupo wima, alikuwa ameukunja uso wake ukiugulia katika maumivu makali lakini sasa yalisahaulika kwa muda na kuwa mshangao mkubwa, alikuwa Pocha mwenye hofu lakini sasa alikuwa amebadilika na kuwa Pocha anayeduwaa!!
Hali hii ikamkumba na yule bwana aliyekuwa anamwadhibu!!
“Pochaaaaa!”
“Chopaaaa!!”
Wawili hawa walijikuta wakiitana majina yao, kila mmoja asiamini kile alichokuwa anakiona.
Haikuwa ndoto ile, maswahiba walikuwa wamekutana.
Mara ya mwisho walionana gerezani na sasa wamekutana katika himaya hii wasiyoielewa!!!
Chopa alipiga hatua kadhaa na Pocha naye akafanya hivyohivyo kisha wakakutana kwa nguvu na kukutana kisha wakakumbatiana.
Ni nani ambaye angeweza kulizuia chozi lake lisianguke???
Hakuna!!
Ilikuwa hivyo kwa wawili hawa wneye hadhi ya kuitwa marafiki wa dhati!!
Wakati Chopa anamueleza Pocha kuwa alifika hadi gerezani kumtafuta, Pocha naye akaelezea mkasa wake kutoka Dodoma akiwa amechezwa machale kuwa Chopa yu katika hatari na alikuwa akimuhitaji sana.
Maneno haya kutoka kwa kila upande yakawafanya wakumbatiane tena na kuangua kilio upya.
Lakini kilio hiki kilivunjwa na Chopa aliyemueleza Pocha kuwa wakati wa kuletewa chakulaulikuwa umekaribia.
Pocha akarejea chumbani kwake akifungua tena ule mlango, akaagana na Chopa wakikubaliana kukutana usiku mnene kwa ajili ya mpango madhubuti!!
Na huu ukawa muendelezo wa HEKAHEKA!!!
____
CHRISTINA mkewe Lucas hakushtuka asubuhi na kuanza kulalamika kuwa anataka kuacha ubunge na kisha kwenda na mumewe London, huu ulikuwa ni mchakato ambao ulianza siku kadhaa nyuma hata kabla Lucas hajazungumza na vyombo vya habari.
Hiyo siku alipokea ugeni ambao haukuwa ugeni katika ile maana halisi ya ugeni lakini alilazimika kuuita ugeni.
Huu ulikuwa ni ujio wa Carolina Edwin ambaye alizoea kumuita mama mdogo na yeye akamuita mwanaye. Ilikuwa ni kawaida kila anapotoka uingereza kituo cha kwanza ni nyumbani kwake na kisha safari kwenda Mwanza.
Hivyo hata sasa alikuwa akipita tu, alikaa kwa siku tatu kabla ya kupanda ndege kwenda Mwanza kwa wazazi wake, ilikuwa ni siku ya pili tangu Carolina awe pale nyumbani huku muheshimiwa Lucas akiwa bado nchini uingereza.
Siku hii Christina aliamua kutoka na Caro kwenda kuogelea katika mojawapo ya fukwe za kisasa zinazosifika zaidi jijini Dar es salaam kwa utulivu uliopo katika mazingira hayo.
Walifika fukweni majira ya saa kumi jioni, alianza Christina kuogelea akimuacha Caro aliyekuwa amejikita kuvuta ‘shisha’.
Baada ya takribani nusu saa ndipo caro alipovua nguo alizokuwa amevaa na kisha kuvalia nguo maalumu kwa ajili ya kuogelea kisha akajiunga na Christina katika maji.
Ni hapa ambapo Christina alikiona kitu ambacho kilimshtua sana, alijaribu kukipuuza lakini haikuwezekana kilikuwa ni kilekile alichokiona siku kadhaa nyuma kisha kikapotea machoni mwake akibaki bila ushahidi wa kutosha.
Christina alikuwa ameona kovu katika mgongo wa Christina, kovu hili lilikuwa limejichora na kuacha michirizi inayofanana na herufi ‘C’. Kovu hili aliliona siku ile ambayo alikuwa anazungumza na mumewe kupitia mtandao wa ‘Skype’.
Hisia za uchungu zilimtawala akajikuta akitokwa na machozi, bahati nzuri maji yalionyesha ushirikiano na kuyasomba machozi yakaondoka zake.
Hakuna aliyejua kama alikuwa analia.
Ile starehe ilikomea pale, Christina akajiuliza maswa li mengi sana.
Alijiuliza inawezekana vipi mumewe ambaye ni mtu mzima kabisa aende kushiriki mapenzi na yule mtoto ambaye ni sawa na mwanaye wa kumzaa kabisa, hili lilimfadhaisha sana alipojaribu kujenga picha kuwa yupo katika mzani wa mapenzi na yule mtoto sasa muheshimiwa anachagua yupi ni bora kati yao.
Christina alikumbwa na ghadhabu akajisemea kuwa ni heri aachane na Lucas kuliko hii fedheha iliyokuwa inamkabili, lakinmi hapohapo akakumbuka kuwa kuachana na Lucas ni kumpa nafasi ya kujimwayamwaya zaidi na yule binti.
Pia alipokumbuka kuwa alikuwa hajawahi kumzalia mtoto hata wa dawa mheshimiwa Lucas nguvu zilimwishia.
Hata kangeamua kuachana na Lucas, angeenda kwa nani?? Nani angekuwa radhi kumuoa mwanamke ambaye umri unazidi kwenda halafu hana mtoto.
Hili pekee halikutosha, lililomkosesha amani kabisa ni ule ukaribu aliokuwanao na wake wa wabunge na mawaziri wengine, kama angeachana na Lucas basi ule ungekuwa mwanzo wa kuwapoteza marafiki wa hadhi yake na angetakiwa kutafuta marafiki wengine.
Msumari wa mwisho ulikuwa ni vijembe ambavyo angevipata bungeni, ikiwa atazungumza lolote ambalo lina sintofahamu basi wapinzani watajenga hoja kuwa ikiwa ndoa yake pekee imemshinda kutunza itawezekana vipi kuwatunza wananchi na kuwatendea haki?
Jingine ambalo lilikuwa na uzito pia aliloliwaza ni iwapo huyo binti atamzalia mtoto muheshimiwa Lucas ni kitu gani kitajiri??
Mawazo haya yalimvuruga sana Christina, alimsihi Caro waondoke kwa sababu kichwa kinamsumbua, akamsihi Caro pia aendeshe gari wakati wa kurudi nyumbani.
Hilo lilitimizwa wakarejea nyumbani salama.
Christina alilala akiwa na mawazo tofauti tofauti, lakini asubuhi aliamka akiwa na wazo moja aliloliona kuwa ni la busara sana.
Christina aliamua kuipigania ndoa yake huku akiamini kuwa iwapo ataipoteza basi kamwe hawezi kuja kupata ndoa kama hiyo.
Ni hapa hekaheka zake ziliposhika kasi!
Sasa alikuwa hakamatiki wala hasikiki anahitaji kuishi uingereza akiwa na mume wake.
_____
PRISCA katibu muhtasi wa Lucas katika ofisi yake kubwa iliyopo Dodoma alikuwa mtu wa kwanza pale ofisini kugundua kuwa bosi wake hakuwa na raha kabisa tangu arejee kutoka katika safari yake kisha kufika nyumbani kwake jijini Dar es salaama na sasa uwepo wake ofisini.
Kwanza hakuwa nadhifu kama ilivyokuwa kawaida yake, nywele zake zilikuwa hazijachanwa.
Muonekano wa muheshimiwa Lucas haukuwa ukimuhusu Prisca na hata katika mkataba wake wa kazi kipengele cha kuingilia mambo binafsi ya bosi wake hakikuwepo.
Lakini wambea hawahitaji mkataba ili waweze kutumia vipaji vyao, inapobidi wanafanya.
Prisca hakutaka hili limpite hivihivi, akaingia ofisini kwa bosi wake ili kumpa taarifa kadhaa za pale ofisini tangu aliposafiri.
Alipofika bafuni akajifanya kushtuka kidogo, kisha akamuuliza bosi wake kulikoni. Alikuwa hajachana nywele zake na pia alikuwa ananuka pombe!!
Lucas alimtazama Prisca kwa muda kidogo bila kusema lolote. Prisca akajiwahi kuzungumza, alivyozungumza usingeweza kusema ni mmbea.
“Samahani muheshimiwa, najua si haki yangu kujua yanayokusibu… lakini kiubinadamu nimejikuta nakosa amani kukuona katika hali hii…. samahani kama nimefanya kosa kukuuliza…” alizungumza kinyonge, na hapo akageuka ili aweze kuondoka.
“Prisca!” Lucas akamuita, akaitika kwa nidhamu ya hali ya juu. Lucas akamuomba aketi… akafanya hivyo….
“Prisca, wewe ni binti mdogo sana lakini haimaanishi kuwa wewe ni mtoto…. najua nikisema mapenzi unanielewa…” akampa nafasi Prisca ya kutikisa kichwa ishara ya kukubali.
“Basi haya mapenzi ndiyo yananifanya nipo hivi, lakini usijali kabisa nitakuwa sawa tu hivi karibuni…..”
“Mh! Ni mama anakusumbua au?” aliuliza Prisca akimaanisha mke wa Lucas.
Lucas akasita kidogo kisha akatokwa na neno ambalo lilimsababisha Prisca aone muda wa kutoka kazini haufiki ili aweze kulitoa funda lililomkaba kooni.
Akaondoka pale ofisini akiwa amezungumza mambo mengi sana na bosi wake.
Lucas hakujua kabisa kuwa pombe sio chai, ukiifakamia hovyohovyo inageuka kuwa mwanaharamu.
Akili yake ya pombe akajikuta akimuona Prisca ni mshauri mzuri sana!!
Akamwaga matatizo yake ili ashauriwe!!
Pombe zilipomwishia alijilaumu kwa kumsirikisha Prisca mambo yale lakini alimpuuzia kwa kuhisi kuwa hawezi kuzua lolote la maana ambalo litamchafua yeye.
Ama! Usiku wa giza ni heri kuliko usilolijua, usiku wa giza unakufanya utembee kwa tahadhari ili usijikwae kwa sababu unajua huu ni usiku. Lakini USILOLIJUA………
_______
Usilolijua si sawa na usiku wa giza bali ni zaidi ya giza lenyewe.
Laiti kama usilolijua lingekuwa sawa na usiku wa giza basi Pocha na Chopa wasingeweza kufanya lolote katika usiku ule wa giza waliokubaliana kukutana.
Ilikuwa ni kawaida katika vyumba walivyokuwa wamehifadhiwa Chopa na Pocha kuna wakati ambao taa zinazimwa na kuunda giza nene sana, hata usiku huu ilikuwa vilevile.
Lakini mikono ya Pocha ina macho ya ziada haihitaji macho ya kawaida ya mwanadamu kuweza kutoa ‘loki’ za vitu tofauti tofauti. Alifanikiwa kuufungua mlango licha ya giza lile.
Akamshtua Chopa, wakaketi na kuzungumza kuhusu mustakabali wa maisha yao ndani ya vyumba vile ambavyo hawajui hata vinapatikana eneo gani ndani ya Tanzania. Na hawakujua kuwa ni baada ya vyumba vingapi wanaweza kuwa nje ya eneo lile, walitakiwa kwanza kuupata mwangaza kidogo ili wakiamua kutoka basi wasirudi nyuma.
Walizungumza mengi sana kwa sauti za kunong’ona. Kikubwa walitaka kujua nini chanzo cha yote haya, kama ilivyokuwa kule gerezani Pocha alijua ni kwa nini yupo gerezani na hata hapa anafahamu kuwa yupo kwa sababu alikuwa tu anatafutwa na Chopa.
Chopa amefanya kosa gani??
Hili lilikuwa swali zito sana lililohitaji ufumbuzi wa upesi.
Baada ya kuzungumza sana hisia zote za Chopa kuwa katika utata huu.
Hatimaye Pocha akasema hisia zake.
“Chopa kwa maelezo yako yote juu ya maisha yako ya utafutaji, mapenzi na tofauti zako na watu baadhi mimi kuna kitu nahisi hapa ambacho kipo nyuma ya haya mambo…..” akasita kidogo kisha akaendelea, “Kaka yaani hapa nisiseme eti machale yamenicheza ama vipi lakini katika majibu hata la uongo nalo jibu… mi nahisi huu ni MPANGO WA KANDO!!” Pocha alimalizia.
Kauli hii aliwahi kuisema awali kabisa wakiwa gerezani, akawa ameirudia tena kwa mara ya pili.
“Mh! Mpango wa kando? Kiaje unaufahamu huu mpango au? Maana gerezani ulinambia tena halafu haukuendelea kunieleza, Pocha tafadhali naomba unipe mwanga….”
“Ntakupaje mwanga ilihali na mimi nipo gizani, tusaidiane kulitafuta hilo jibu ambalo nd’o mwanga wenyewe kaka…” Pocha alijibu.
“lakini walau basi wewe unao huo mwanga, unahisi ni mpango wa kando.. nieleze ili na mimi niwe sawa na wewe kisha tuendelee mbele” Chopa akamsihi Pocha.
pocha akatulia kwa muda na kisha akapitia katika maelezo ya Chopa aliyotoa nayea akaelezea ambalo analihisi juu ya utata huu.
_____
Miaka kadhaa nyuma
MBEYA, TANZANIA
Wakati huu alijulikana zaidi kama Manfredy, haswaa na hili ndilo lilikuwa jina lake la kuzaliwa. Alikuwa mchapakazi, alikuwa ameajiriwa kama dereva lori lililokuwa linabeba mizigo ya viazi mbatata na mchele kutoka mjini Mbeya kupeleka sehemu mbalimbali za Tanzania ambazo zilikuwa zikihitaji sana huduma hiyo. Madereva wa barabarani wanayo tabia ya kujisifu kila mmoja akijitapa kuwa anaweza sana kuendesha gari kumpita mwenzake. Lakini kwa Manfred haikuwa hivi, alikuwa mtulivu sana aliacha kazi yake ijitangaze na kumpatia sifa.
Hakuwa na rekodi mbaya za kupinduka ama kugonga watu ama wanyama barabarani, hakuwa mlevi na lililosambaza sifa zake zaidi ni ile hali yake ya kuendesha gari kwa mwendo kasi lakini salama.
Hali hii ya kufika mapema zaidi Mbeya kisha kuingia mikoani na kisha kurudi Mbeya, wanyakyusa wakalifananisha lori alilokuwa anaendesha Manfredy kama helikopta ya mgombea uraisi mmoja wa chama cha upinzani, siku alipotua Mbeya mjini aliwaambia ile haiitwi Helikopta bali waiite Chopa inakwenda kasi kama yeye atakavyoingia kwa kasi ikulu.
Neno Helikopta likasahaulika na CHOPA likachukua nafasi, ilifikia hatua hata ndege za kawaida tu wakazi wa mbeya waliziita Chopa.
Hatimaye jina hili likahamia katika lori la Manfredy….. jina la Lori likahamia kwa Manredy wakamuita muendesha Chopa lakini hii haikufurahisha kutamka mdomoni. Wakalifupisha zaidi na kumuita Chopa.
Jina likamkaa, lile la kuzaliwa likasahaulika.
Manfredy akageuka kuwa Chopa.
Hakulichukia jina lile, alilipenda sana na kulifurahia katika nafsi yake lakini kwa nje hakusita kuwakumbusha watu kuwa Manfredy Gregory ndilo jina lake la kuzaliwa.
Maisha ni ujanja kabla hujapata!
Chopa alikuwa akibena abiria kadha wa kadha katika safari zake nyuma ya utambuzi wa bosi wake, alifanya hivi ilimradi kujipatia kipato cha ziada.
Katika pakia pakia hii kuna siku alipakia wanafunzi watatu wa kike, hawa walikuwa wana safari ya kwenda Dodoma lakini walikuwa hawana nauli ya kutosha.
Chopa alipewa taarifa hizi akazipokea katika lugha ya biashara akataja bei ya kawaida tu, baada ya muda akaambiwa kuwa asubuhi na mapema watakuwa wamefika eneo walilokubaliana.
Chopa alikuwa akiwaza kuwa watakuwa wanafunzi wa kiume, asubuhi inafika anapewa wanafunzi wa kike waliodai kuna chuo kikuu kimoja hapo Mbeya walikuwa wanasoma.
Walipozungumza ndipo Chopa akapata mustakabali, kuwa wanmgekuwa wanafunzi wa kitanzania wala wasingeweza kupanda lori lakini wale walikuwa kutoka nje ya Tanzania.
Wakiwa safarini walijitambulisha mmoja alikuwa anatoka Uganda japokuwa alikuwa mtanzania, mwingine Mnyarwanda na wa tatu alikuwa anatoka Somalia lakini wazazi wake walikuwa wakiishi Kenya.
Ni watanzania wanaojali zaidi nani atasema nini wakifanya hivi, lakini hawa hawakujali walitazama pesa walizokuwanazo katika mifuko yao.
Walizungumza mengi na kuifanya safari kuwa ya kuchangamka, Chopa akaelezea naye kwa upande wake.
Baadaye katika ongea ongea mara ikazaliwa mada kuwa madereva wa malori wanaongoza kwa umalaya, Chopa alijitetea sana lakini wale wasichana walikuwa na ushahidi mkubwa sana, Chopa alilazimika kukubaliana nao lakini akijitoa kati ya orodha ya madereva hao wahuni.
Walipokaribia Dodoma yalianza mazungumzo juu ya wapi watafikia, wawili walionekana kuwa na pa kufikia ambapo si pa uhakika lakini mmoja alikuwea njia panda hakuwa na uhakika sana kama anapotaka kufikia patakuwa sawa.
Chopa alikuwa kimya kabisa haya yalikuwa hayamuhusu.
Hadi wanafika Dodoma yule binti kutoka Rwanda hakuwa na uhakika wa ni wapi atafikia na ilikuwa ni usiku tayari.
Hapa sasa Chopa akalazimika kuzungumza, akamweleza yule dada kuwa anamrudishia pesa aliyolipia kama nauli ili aweze kutafuta nyumba ya kulipia aweze kulala.
Ule msaada wa Chopa pasipo na kuhitaji jambo klolote lile ulimstaajabisha yule dada ambaye baadaye alijitambulisha kwa jina la Nkozimakale ama kwa kifupi Nkozi.
Chopa akamwambia asijali, akaagana nao na kuwakaribisha tena pindi watakapohitaji huduma yake.
Nkozi na wenzake waliondoka wasiamini kile kilichokuwa kimetokea, dereva wa lori anakurudishia pesa uliyomlipa hakuombi namba wala kukushawishi ulale naye.
Ajabu!!
Ulipita mwezi mmoja, Chopa akiwa amesahau ile fadhila aliyofanya kwa yule dada, na si fadhila tu hata jina alikuwa amelisahau.
Ilikuwa rahisi sana kulisahau jina lile kwa sababu kila siku alikuwa na wateja wapya katika lori lake.
Siku hii akiwa jijini Mbeya maeneo ya Uyole simu yake iliita ilikuwa ni namba mpya, akapokea na kumsikiliza aliyekuwa anazungumza. Alikuwa ni mwanamke, alimjulia hali huku akimuuliza habari za siku nyingi.
Walizungumza kwa muda wa dakia moja, kisha Chopa akamsihi mpigaji ajitambulishe.
“Sijui kama utanikumbuka Chopa lakini naitwa Nkozi… Nkozimakale… yule dada…” kabla hajaendelea Chopa akadakia kiuchangamfu tayari alikuwa amemkumbuka.
Nkozi akatoa shukrani za dhati kwa usiku ule aliomsaidia bila kujalisha lolote. Chopa alimsihi asijali lolote, na kisha akamuuliza ni wapi alikuwa kwa wakati ule, Nkozi alikuwa Uyole pia.
Chopa akamsihi waonane kama inawezekana.
Nkozi akakubaliana na Chopa akamuelekeza alipokuwa hapakuwa mbali sana, Chopa akapiga hatua kadhaa hatimaye akakutana na Nkozi.
Moyo wa Chopa ulipiga kwa nguvu sana, tangu awe katika mahusiano na mpenzi wake wa muda mrefu Carolina hakuwahi kushtuliwa na mwanamke mwingine kama ilivyokuwa kwa huyu binti wa Kinyarwanda. Na hapa akakiri kuwa alikuwa anatazamana na kiumbe ambaye hawajawahi kuonana kabla.
Alikuwa amevaa sketi fupi kiasi iliyoruhusu mguu wake mweusi kuonekana vizuri na kuleta ile maana pendwa ya mguu wa bia. Alipopiga hatua kumsogelea Chopa ni kama mwili wake ulikuwa mzito kumuelemea, lakini hakuchukiza kwa jinsi alivyokuwa anatembea, badala yake alifurahisha macho ya wengi.
Pocha akiwa mmoja wapo!!
Ule mshtuko wa moyo ukazua mengine, Chopa akaona itaupendeza moyo wake akiwa karibu na Nkozi.
Kwa Nkozi naye ilikuwa hivyohivyo.
Wakapanga siku ya kukutana wazungumze zaidi.
Chopa alikuwa mwanaume kama wanaume wengine, msichana mrembo kama Nkozi unaanzaje kumueleza bayana kuwa eti unaye msichana mwingine aitwaye Carolina hivyo yeye awe katika nafasi ya pili.
Chopa akajikuta akiutapika uongo mdomoni na kuuacha ukweli moyoni. Licha ya Nkozi kumueleza kuwa hadi umri huo alikuwa amejihusisha na mapenzi mara moja tu na hakuyafurahia bado Chopa hakuwa na huruma na moyo wa Nkozi.
Nkozi kabla ya kumkubalia Chopa kuwa naye katika mahusiano alimweleza maneno ambayo Chopa aliyapuuzia lakini yalikuwa mazito sana.
“Chopa, mnamo mwaka 1994 nilizaliwa huko Rwanda, nikiutaja mwaka huo nadhani unaelewa ni kitu gani kilitokea nchini kwetu. Inasemekana mama yangu alinizaa baada ya kupigwa risasi pajani akashikwa uchungu na kunizaa kabla ya wakati na ni kwa neema zake Mungu hadi leo nipo hai. Kuna mwanajeshi mmoja wa kihutu alinisaidia kunifikisha hospitali ambapo ndio ilikuwa ponapona yangu lakini haya yote ni kwa mipango ya Mungu tu. Hivyo basi simjui baba wala mama yangu na simjui ndugu yangu hata mmoja, ninachofahamu ni kwamba watakuwa waliuwawa kwa kosa la kuzaliwa watutsi.
Nimelelewa na watu baki tu, na labda haya nd’o maisha yangu kulelewa na watu baki… hata wewe uliyenisaidia usiku ule ni mtu baki na niliyekuwa naenda kwake naye alikuwa mtu baki. Nikisema najikabidhi kwako leo Chopa elewa kwamba wewe unakuwa ndiye ndugu yangu….. sijiachii kwako kwa sababu tu nahitaji kuwa na mpenzi hapana… najikabidhi kwako kwa sababu nahitaji kuwa na ndugu walau mmoja tu. Uwe kaka yangu Chopa, uwe baba na mume kwangu…. nakusihi usiyapuuze maneno haya….mimi ni wako sasa.” Alimaliza Nkozi kisha akamkumbatia Chopa na kumpiga busu mwanana.
Na mapenzi yao yakaanzia hapo rasmi.
Kwa Nkozi likiwa ni penzi moja kwa mtu mmoja lakini kwa Chopa likiwa ni penzi moja kwa wanawake wawili. Caro anayejulikana kila kona na Nkozi anayejulikana kwa marafiki wa Mbeya pekee.
Penzi hili lilikuwa thabiti sana kwa sababu tu ubavu mmoja ulikuwa Dar es salaam na ubavu mwingine ukiwa Mbeya, akiwa Mbeya Chopa alikuwa anamjali zaidi Nkozi huku Caro akielezwa kuwa kazi zimemzidia na hawezi kuwasiliana naye mara kwa mara, na kinyume na hapo alipokuwa jijini Dar es salaam.
Mchezo huu uliendelea hadi pale Chopa alipoipoteza kazi yake baada ya mmiliki wa lori kufilisika na kuamua kuliuza lile lori.
Huu ukawa mwanzo wa penzi lile kuyumba na hatimaye kimya kikatanda baina ya pande hizi mbili…. Chopa akatabasamu akiamini kuwa Nkozi amejiongeza kivyake.
Nguvu zote zikahamishiwa kwa Carolina jijini Dar es salaam.
Lile jeraha aliloliacha katika moyo wa Nkozi bila kujua kuwa ni hatari sana kuumiza moyo wa aliyewahi kuumizwa hapo kabla.
Nkozi alikuwa mjeruhiwa mzoefu!!
______
ITAENDELEA
MPANGO WA KANDO SEHEMU YA TANO
Also, read other stories from SIMULIZI;