MPANGO WA KANDO SEHEMU YA PILI
NEW AUDIO

Ep 02: Mpango wa Kando

SIMULIZI YA MPANGO WA KANDO FULL EPISODE
MPANGO WA KANDO SEHEMU YA PILI

IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi : Mpango Wa Kando
Sehemu Ya Pili (2)

Walipoingia katika selo zao Pocha akafanya kama alivyoagizwa…
Chopa akawabana watu wale huku akiwaeleza kuwa yeye ni mtu wa usalama wa taifa hivyo ikitokea ameondoka pale ndani wakijifanya kumsumbua Pocha watakiona cha mtema kuni……
Aliwabana katika maana halisi ya kuwatia adabu!!

Ikawa giza na kulipopambazuka alikuwa ni Chopa aliyetolewa gerezani, na hakuna aliyejua wapi amepelekwa!!
Kitendo kile kikamfanya Pocha ajiulize mara mbilimbili juu ya uhusiano wa akili yake na mikono yake.
Na ni vipi atumie uhusiano huu katika kujiweka katika hali nyingine ya kimaisha!!
Akaamua kulishughulikia hilo jambo.

Majuma mawili baadaye akapambana aweze kuonana na mkuu wa gereza!!!
Akafanikiwa kuonana naye akamuelezea alichopanga kumweleza akiamini kuwa kitakuwa na manufaa kwa upande wake…………

______

KWANZA ilianza simu ya mkononi, iliita kwa muda mrefu kiasi. Mwenye simu akaitazama katika kijicho cha kuchungulia kana kwamba anaepusha kumtambua ni nani aliyepiga ile simu. Ilikuwa kama alivyodhani mpiga simu alikuwa yuleyule asiyetaka kuipokea simu yake. Haikuwa kwa sababu ya madeni ama ubaya wowote lakini nafsi ilikuwa ina mashaka labda kuna lolote baya limefichuka tayari.
Baada ya simu ya mkononi kuacha kupokelewa simu ya mezani ilianza kuita. Ilikuwa nambari ileile inampigia.
“Prisca!! aliita kwa sauti ya wastani na baada ya sekunde kadhaa mbele yake alikuwa amesimama msichana aliyevalia nadhifu!
“Bee muheshimiwa!! Yule binti aliitikia wito.
“Pokea hii simu mwambie kuwa nipo katika kikao tangu asubuhi sijarejea ofisini….” alitoa maelekezo yale kivivu kabisa.
Yule binti alitii, lakini alipoufikia mkonga ana kutaka kuunyanyua simu ilikuwa imekatika tayari.
“Naona amekata!” alijieleza Prisca.
“Ok! Namba ya dada wa Airport si unayo, mwambie anifanyie utaratibu wa tiketi ya kwenda London baada ya masaa arobaini na nane mwambie azingatie sana na isishindikane!! Nenda ukawasiliane naye sasa hivi, mimi natoka… nitakachochukua kwako ni tiketi na sio maneno” alizungumza kwa ukali kiasi wakati huo anasimama.
“Mh! Bosi wangu huyo safari zaidi ya raisi wake!!” Prisca alisema kiutani huku akitabasamu, hii haikuwa mara yake ya kwanza kumtania bosi wake huyo.
“Whaat! Mpumbavu nini, tangu lini umeanza kazi ya kunipangia safari, nakuuliza we binti nilikuajiri hapa kuanza kunihesabuia mara ngapi au kutimiza yale ninayokuagiza… shwain kabisa….kwa hiyo mi nikisafiri kuliko raisi wangu inakuumiza nini, ul;itaka usafiri wewe au.. haya basi kuwa mbunge mimi niwe sekretari wako… hovyo kabisa… nipishe hebu nipite.. pishaa!! Mambo ya Lucas naomba umuachie Lucas mwenyewe bastard!!” alibwatuka muheshimiwa mbunge akimuacha katibu muhtasi wake akiwa haamini anachokiona mbele yake na kukisikia, hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa bosi wake huyo kumfokea na kumtukana namna hii. Bosi huyu alikuwa mtani wake sana.

Muheshimiwa Lucas Kazioba alipiga hatua kubwa kubwa akatoka nje akiwa amebeba koti lake la suti. Alipofikia gari lake akaanza kujipekua huku na kule huku akizungumza peke yake.
Alipekua kila kona, na mara akapata wazo kuwa huenda anachokisaka kwa fujo zote hizo amekisahau ofisinii ile anageuka ili arudi anamuona Prisca akijongea kwa hekima zote na adabu kumuendea akiwa amezishikilia funguo za gari za bosi wake.
Fadhaiko likamuandama muheshimiwa akajisikia vibaya sana kwa maneno aliyomuambia binti yule lakini bado binti hakuweka kinyongo akatambua kuwa amezisahau funguo akampelekea.
“Prisca… nisamehe mama yangu, nimevurugwa kupita maelezo nadhani unanijua si mtu wa kutukana na kufoka kama nilivyofanya nakuomba sana unisamehe….” Lucas aliyasema yale huku aibu zikiyatawala macho yake, lakini pia sauti yake ilikuwa imechoka sana. Bila shaka kuna jambo zito lilikuwa linamkabiri.
“Usijali muheshimiwa Lucas, sisi ni wanadamu na kamwe siku huwa hazilingani…nimelielewa hilo na nimeyasahau yote palepale. As long as hujanipunguza mshahara basi yote yaliyobaki huenda nilistahili…” Prisca alijibu huku akijilazimisha kutabasamu.
Maneno ya Prisca yakamchoma Mh. Lucas, na sasa hakutaka kuomba tena msamaha kwa maneno, akamsihi Prisca asubiri kidogo. Akafungua gari lake na kunyofoa bahasha moja ya rangi ya dhahabu!!
“Pokea hii…. haina maana yoyote mbaya nimejisikia tu. Hii itakusaidia kuwa maikini wakati unazungumza na dada wa airport kuhusu tiketi yangu, si unajua wanavyokera watu wa airport… sasa hii ni kinga ya kutokwazika. Basi baadaye!!” akapanda kwenye gari bila kusubiri asante ya prisca!!
Lucas alipoondoka upesi Prisca akaifungua ile bahasha, akahesabu zile pesa kana kwamba anahakikisha wakati hakutajiwa kiasi sahihi ni ngapi…..
Ilikuwa mshahara wake wa miezi miwili, shilingi laki tisa!!
Prisca alisahau kabisa kama alitukanwa na bosi wake.
Amakweli pesa sabuni ya roho!!
Lakini Prisca alikuwa wa tofauti kidogo, licha ya pesa zile kumsahaulisha matusi ya bosi, lakini kile kitendo cha bosi kuitaka safari ile ya haraka huku akiwa amepagawa hakukipuuzia hata kidogo alihisi kuna jambo zito linamkabili bosi wake.
Umbea ni kama rangi ya ngozi jama unaweza kujifanya umeuacha lakini likitokea tukio la kuhusu umbe utajikurta umeshiriki tu!!!
Prisca hakuiacha asili yake!!
Akairejea fani yake!!!
Laiti kama angeikumbuka ile kauli ya umbea hauna posho abadani asingejihusisha tena na umbea…. lakini hakuukumbuka usemi ule.
Ni kawaida ya vijana wa kisasa kuwapuuzia wahenga!!!
Prisca naye alikuwa kijana.

_______

Desemba, 2013
Mara, Mugumu Serengeti

__MTU HURU__

Lango la gereza lilifunguliwa, takribani mwaka mzima uliopita lango lile lilipofunguliwa yeye na wenzake walikuwa wameveshwa bangili zisizopendeza machoni kuzitazama na usiombee kuzivaa.
Walikuwa wameunganishwa kwa pingu, na kama si pingu basi walikuwa wamewekwa katika karandinga huku ulinzi ukiwa mkubwa sana.
Lakini siku hii alikuwa huru kabisa, alisindikizwa hadi getini, hapo alikuwa amekabidhiwa pesa kiasi sawa na ujira wake kwa kulitumikia gereza. Akapewa na ziada ya usafiri kwa sababu hapo awali alihamishwa kutoka gereza la Ukonga Dar es salaama kabla ya kupelekwa Kiomboi Singida na hatimaye gereza la mahabusu la Mugumu Serengeti!!
Gereza pekee katika wilaya ile.

Alipiga hatua kama sita kisha akapiga goti chini akainama akainyanyua mikono yake juu akaanza kumshukuru Mungu huku akilia kilio kikuu kwa sauti ya chini kiasi lakini machozi yakibubujika kwa kasi.
“Mungu! Mimi si mtiifu sana kwako, sikumbuki kama nimekutumikia kwa muda mrefu lakini kwa uweza wako wewe nipo hai na huru leo… ninayo mengi ya kukushukuru lakini naomba nikukabidhi kwako wenzako waliobaki katika gereza hili moja kati ya magereza mabovu niliyowahi kuyashuhudia katika mapito yangu, Baba iamshe serikali ifike huku na kuuimarisha ukuta wa gereza hili kabla haujawaangukia waja wako, waamshe wabunge waje kutazama huu mrundikano katika gereza, waamshe wanasheria waje kuwatetea waliofungwa kimakosa ama kwa kuonewa…. na kuu la msingi baba nipunguzie hii hasira ama la kam,a hii hasira haitafutika katika moyo wangu, naomba unisamehe baba kwa sababu sitatulia kabla ya kumtafuta yeyote yule aliyehusika katika mpango huu…. mpango wa kunipotezea dira ya maisha yangu…..”
Alikaa kimya akiwa ametulia pale chini kwa muda akiamini kuna wapiti njia kadhaa wanamshangaa lakini hilo halikumuumiza kichwa.
Akasimama hatimaye hakujihangaisha kujifuta vumbi!!
Akageuka kulitazama lango la gereza ambalo lilikuwa limefungwa tayari. Akatikisa kichwa na kulazimisha tabasamu, alipopiga hatua nyingine mbele akajisemea.
“Asante raisi kwa msamaha huu kabla ya kukimaliza kifungo changu, najua sikustahili wapo waliostahili kusamehewa….. ila asante”
Akamaliza na kujifuta machozi kisha akapiga hatua kuelekea popote anapoweza kuelekea.
“Babaa… baba!” alisikia sauti ya mwanamke ikimuita.
“Tacho hano mona wane.. tacho ulaghere! Weii mona wane….” mwanamke yule alizungumza kikabila…. yule mtu huru hakuelewa anachomaanisha lakini ishara ya mkono ni kama alikuiwa akimuita.
“Wewe ni wa huku kwetu…” yule mama alimuuliza huku akionyesgha huruma ya hali ya juu.
“Hapana mama..shkamoo, mimi si wa huku..”
“Aaah! Nilidhani ni mkurya, nilikuita uje ule chakula mtoto wangu, aaah! Ona walivyokuchubua chubua….aaah! gereza hili gerezaaa lilimmeza mtoto wangu wakampiga akafia huko eti kisa alimtukana balozi… aaargh!” mama akashindwa kuzungumza akaanza kutokwa machozi.
Na wakati huohuo akaifungua chupa ya maziwa ambayo alikuwa anauza kama biashara akammiminia mtu huru. Yule bwana akapokea na kunywa, maziwa yale yalimchangamsha na kumtia nguvu.
“Unaitwa nani?” alimuuliza wakati anamalizia kunywa yale maziwa.
“Naitwa Manfred Gregory!!”
“Mnifureti!!” alijari8bu kutaja jina lile yule mama… lafudhi ya kikurya ilikuwa ikimsumbua.
“Niite CHOPA!!” mtu huru akabadilisha jina ili kumrahisishia yule mama.
“Chopa.. eeh! Pore mwanangu, sasa usiangarie nyuma usitazame sijui nani alikuweka ndani sijui nani alikudhurumu haki yako we kapambane na maisha tu. Yariyotokea uyasahau sawa mwanangu!!” mama alimsihi Chopa.
Chopa akakubaliana na yule mama ambaye ‘R’ na ‘L’ zilikuwa tatizo kwake.
Akamshukuru kwa maziwa kisha akaondoka, akatembea hadi alipoipata nyumba ya kulala wageni!!
Akaipata ya bei ya kawaida akaingia humo. Akaoga tena kwa mara nyingine, hapo awali alioga gerezani kabla ya kutoka rasmi!!
Wakati anaoga akawa anakumbuka juu ya siku yake ya mwisho uraiani!
Siku aliyokamatwa na kisha kutupwa gerezani akisomewa shtaka la kughushi vyeti feki na kujipatia kazi asiyostahili hivyo alikuwa anashtakiwa na jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
Kesi hii ilimfanya asite kidogo kuoga, akaanza kuzungumza peke yake.
“Yaani mimi nimeishia kidato cha nne, nikapata daraja la pili, halafu anatokea mtu anasema nimeghushi vyeti?? Kazi yenyewe bora ingekuwa inaingiza milioni nyingi, yaani kazi ya mshahara laki na nusu chakula na usafiri juu yangu, anakuja mtu ananipeleka gerezani… hivi hii ni haki?? Eeh! Ni haki hii?” alijiuliza mwenyewe.
Alipomaliza kuoga akakiendea kioo kikubwa kilichokuwa kimebandikwa ukutani.
Hapa ndipo Chopa alilia kama mtoto tena..
Mwili wake ulikuwa na mabakamabaka, ngozi yake ilikuwa hovyo kabisa, akageuka na kujitazama mgongoni.
Ilitisha sana hali aliyokuwanayo, mfanowe ngozi yqa punda aliyebebeshwa mzigo kwa muda mrefu akachubuka na kuacha jeraha na mwenye punda asijali hayo akaendelea kumbebesha mizigo.
Chopa alilia sana na hii hali aliyoitazama kwa macho yake mwenyewe ikamfanya azidi kuifikiria kesi yake.
Na hapo akazikumbuka tena zile jumbe alizotumiwa kabla ya kuingia gerezani.
Akaukumbuka ujumbe wa kwanza.
“SIKU ZAKO ZINAHESABIKA SI UNAJIFANYA MJUAJI! TUTAONA MJUAJI NANI KATI YA MTU HURU NA ANAYEENDA KUUPOTEZA UHURU.”
Huu ulikuwa ujumbe wa kwanza siku ile asubuhi, ujumbe alioupuuzia kwa kuamini kuwa umekosea njia.
Chopa alihangaisha sana kichwa chake, akawafikiria ndugu zake. Eti hakuna hata mmoja aliyefika gerezani kumjulia hali…..
Akamfikiria Caro mchumba wake, eti na yeye kwa miaka hiyo miwili hakuwahi kwenda japo kumsalimia!!
Kichwa kilimuuma sana alipoyafikiria haya, kujiepusha na haya akajirusha kitandani. Godoro laini lisilokuwa na hiyana likampokea, akalivuta shuka na kujifunika.
Nadhani haitakiwi kuendelea kusimulia kilichotokea!
Miaika miwili hujalalia godoro lililo katika mazingira mazuri halafu unajikuta eneo kama hilo……
Zilihitajika kelele za milio ya risasi kumwamsha mtu huru huyu, Chopa!
Wakati Chopa analala usingizi wa samaki aitwaye Pono….
Mahali pengine nchini Tanzania kulikuwa na majadiliano mazito!
Kuna mtu huru mwingine alikuwa anaongezeka!

______

Dar es salaam!!

AWALI bibie Christina au maarufu kama mama Lucas alikuwa anadhani ni utani mumewe alipomtumia ujumbe kwa njia ya simu na kumueleza kuwa ana mpango wa kuachana na siasa haraka iwezekanavyo.
Christina aliamini kuwa huu ni utani kwa sababu mumewe ambaye raisi alikuwa na kila dalili ya kumpa uwaziri eti leo hii aseme anataka kuacha siasa.
Aliujibu ujumbe ule kwa kicheko tu! Kisha akapuuzia.
Majira ya saa nane mchana mumewe alirejea nyumbani akionekana kuwa hakika ana jambo zito kichwani mwake.
Alifika na kuingia chumbani moja kwa moja, Christina ambaye alikuwa mbunge viti maalumu alifuata nyuma na kuingia chumbani alipoingia mume wake.
“Una nini muheshimiwa!!” alimuuliza, ikiwa ni kawaida yao kuitana cheo hicho wanapokuwa nyumbani.
“Kama nilivyokuandikia ujumbe ule ninamaanisha nilichokwambia, nahitaji kuwa mtu huru!!”
“Mtu huru??” aliduwaa Christina mkewe Lucas Kazioba!!
“Ndio nahitaji kuwa mtu huru nifanye mambo yangu, miaka yote hii kuanzia mwaka 1995 nadhani sasa niwaachie nyie, na jimbo langu la Nyamagana achukue mtu mwingine, ujue siasa ni kama mbio za vijiti tunapokezana unapochoka na kumpatia mwenye nguvu!!” alijibu Lucas kwa sauti iliyopooza.
“Mume wangu, hebu acha masihara basi…. uache siasa wakati raisi amekuahidi uwaziri na ndiyo ilikuwa ndoto yako mpenzi wangu!!” mke wa Lucas alihoji huku sasa aklimshika mumewe begani.
“Siutaki tena huo uwaziri acha awape watu wengine, yaani hata nikiambiwa kuwa 2015 ni mimi nitagombea uraisi kwa tiketi ya chama sitakuwa tayari, sio tu najivua madara hapa naacha siasa kabisa. Nitabaki kuwa mshauri tu kwa vijana wanaotaka kujiunga na siasa!!” alisisitiza Lucas….
Sasa Christina ambaye alikutana na mume wake huyu bungeni mnamo mwaka 2007 na kuanzisha mahusiano na hatimaye kuoana mwaka 2009, alianza kuamini kuwa Mh. Lucas hakuwa na masihara hata kidogo.
Akabaki kimya asijue la kusema. Akiwa kimya bado, mumewe alizungumza tena kama kumaliza ule mjadala.
“Panapo majaliwa kesho kutwa alfajiri nitakuwa aidha ndani ya KLM ama EMIRATES nakimbia London mara moja….. sasa mi napumzika naomba uniamshe saa kumi.” Akamaliza mazungumzo yale huku akiaga kwenda London kama anayeenda soko la jirani hapo kununua bilinganya na matembele.
Mh. Christina Lucas alichoka!!!
Mumewe alikuwa amebadilika ghafla mno.

_____

FAHAMU zilimrejea tena Chopa majira ya saa kumi na moja jioni, maziwa aliyopewa na yule mama mkarimu wa kikurya yalimfanya alale vyema bila tumbo kumpigiza kelele za kuomba chakula.
Lakini majira hayo ya saa kumi na moja tumbo lilianza kulalamika kuwa yale maziwa yalikuwa yamemalizika.
Chopa akaamka na kuingia bafuni kujimwagia maji tena, kisha akatoka kwenda nje kutafuta chakula na kukata tiketi ya basi kwa ajili ya kwenda Arusha siku inayofuata.
Hii ni baada ya kuambiwa kuwa hakuna mabasi yaendayo Dar es salaam moja kwa moja, hivyo ilikuwa ni lazima aunganishe!!

SIKU ambayo Chopa anafanya safari yake ya kwenda Arusha ndani ya jiji la Dar es salaam mheshimiwa Lucas naye alikuwa katika maandalizi ya mwishomwisho kwa ajili ya kuruka kwenda nje ya nchi.

______

LONDON, Miaka miwili nyuma (2011).

Ilikuwa safari yake ya kwanza kabisa kwa usafiri wa ndege.
Ikiwa ingekuwa safari ya kutoka Mwanza kwenda Dar es salaam pekee ilikuwa ya kihistoria kwake, vipi kuhusu safari ya kutoka Dar es salaam kuelekea katika mojawapo ya majiji yanayozungumzwa zaidi duniani.
Jiji la London!!
Hakika kuna baadhi ya matatizo hayatatuliwi na wanasaikolojia, badala yake yanatatuliwa na mazingira.
Caro alikuwa hajawahi kuota kuingia katika ulimwengu huu.
Mheshimiwa Lucas alimfikisha Caro nyumbani kwake na kumtambulisha kwa mkewe ambaye tayari walikuwa wamejadiliana naye kuhusiana na matatizo yanayomkumba binti huyo. Hivyo makubaliano ya kumsaidia waliyapanga wote wawili.
Baada ya siku mbili za mapumziko Lucas akaongozana na Vero kuelekea jijini London.
Walitumia ndege ya shirika la Emirates.
Ilikuwa safari ndefu sana lakini kwa Caro ilikuwa safari ya kushangaza mno, uso wake ulionyesha mshangao ule na hamu zote za kutua jijini London.
Wakati Caro akiuliza maswali ya hapa na pale na Lucas akimjibu kiufasaha, hatimaye Vero alipitiwa na usingizi.
Ni hapa ambapo Lucas alijikuta akipatwa na kumbukumbu za kipuuzi sana ambazo alijaribu kuzipuuzia lakini ziliendelea kumuandama.
Kwanza aalijisemea, “hawa watoto wa kike hawa wanawahi kweli kukua, kaone haka katoto”
Alisema hayo huku akiweka picha mbili katika kichwa chake, picha ya kale katoto kadogo Caro kalikozaliwa mnamo mwaka 1992 wakati huo wakiwa chuoni mwaka wa kwanza na rafiki yake kipenzi Edwin.
Baadaye Caro akafikisha miezi miwili hatimaye mwaka…….
Akaukumbuka utani waliokuwa wakirushiana na Edwin, Lucas alimwambia Edwin kuwa amezaa mtoto mrembo sana hivyo apambane sana kusoma ili aje apate kazi nzuri amlinde mtoto wake, Edwin naye akamwambia Lucas afanye upesi azae mtoto wa kiume ili siku moja amuoe Caro na urafiki wao ili amlipishe mahari kubwa sana ya kumkomoa.
“Yaani Luca ukileta mtoto wako anataka kuona huyu malikia wangu nakuhakikishia kuwa nitakufilisi, yaani nakutajia mahali hata milioni mbili”
Luca akaukumbuka usemi huu akajikuta akitabasamu, aliifikiria milioni mbili ya wakati ule wakiwa wanasoma ilivyokuwa pesa kubwa yenye thamani akaifananisha na ya wakati uliopo akasikitika sana.
Maisha yakaendelea hatimaye Caro akafikisha miaka kumi, Luca akazidi kumsifia Edwin kuwa hakika kwa caro amelamba dume!!
Si tu alikuwa mrembo bali hata darasani alikuwa vizuri!!
Alipomaliza kumfikiria caro wa enzi zile akamtazama Caro aliyeketi pembeni yake, caro mwenye umri wa miaka kumi na tisa mwaka huo 2011.
Macho ya Lucas yakaanguka katika kifua cha yule binti, akazikumbuka enzi zile kakiwa katoto kalikuwa kanatembea kifua wazi na hakuna aliyejali, sasa aliuona mzigo mdodo wa embe dodo changa zilizoota katika upande wa kifua chake katika namna ya kupendeza.
Kisha akafumba macho yake na kukumbuka maumbile ya nyuma ya binti yule.
Akapandisha macho yake hadi katika midomo ya Caro, hapa sasa akajikuta akimeza mate ya matamanio bila ya kutarajia.
Akauchukua mkono wake na bila kutarajia akamgusa Caro shavuni!!
Caro akashtuka kutoka usingizini. Mheshimiwa Lucas akajikuta akitokwa na swali la kipuuzi.
“We Caro hivi ulikuwa umelala au?” alimuuliza kizembe!
Caro akajibu hapana!!
Lucas alijaribu kuzikabili hisia zilizomwandama lakini zilikuwa zimekuja kwa nguvu kubwa sana iliyousukuma moyo wake katika namna ya kushindwa kujizuia.
Alijilazimisha kuukumbuka urafiki kati yake na Edwin ili aweze kumchukulia Caro kama mtoto wake lakini hata hii haikusaidia.
Mara akamtazama tena Caro aliyesinzia, na hapo akakumbuka kuwa kuna bwana aitwaye Chopa ambaye yupo gerezani akitumikia kifungo cha miaka mitatu, eti huyo bwana ndiye ambaye ana mamlaka ya kuzitoa nguo za caro na kumfanya vyovyote atakavyo.
Hili jambo likamkera sana mheshimiwa mbunge na kuhisi huyo bwana ambaye hamjui hata sura yake, hana hadhi ya kummiliki Caro.
Akavihesabu vidole vyake.
“2011, 2012, 2013, 2014 mh! Bado sana kutoka kwake!!” akajisemea baada ya kuihesabu hukumu ya Chopa.

SANDERSON HOTEL, LONDON

Jiji la London ni mojawapo ya majiji yenye uwingi wa Hoteli za kisasa nyingi zakiwa ni za hadhi ya nyota nne na tano.
Jiji hili lina jumla ya hoteli elfu moja na mia sita, na katika orodha hiyo hoteli ya Sanderson ni ya arobaini kwa ubora.
Wakati akiwa Tanzania mheshimiwa mbunge tayari alikuwa amefanya mawasiliano kwa ajili ya kuandaliwa chumba kwa ajili ya usiku huo atakaofika London.
Ilikuwa kama a,livyoagiza, alipotua uwanja wa ndege akapokelewa na gari kutoka hoteli hii.
Kuanzia pale uwanja wa ndege ungeweza kugundua ni kiasi gani hii hoteli ilikuwa na huduma za kisasa. Kujali mteja na kwenda na muda!!
Kufikia chumbani huku hapasimuliki, kuanzia sehemu ya kulala hadi bafu la kuoga.
Vyote hivi vilikuwa vigeni sana kwa Caro.
Ilianza kama masihara, wakala pamoja wakazunguka hapa na pale na kisha ukafika usiku wa muheshimiwa mbunge aidha kukabilianana tamaa iliyomuandama ama kutii kiu yake na liwalo na liwe.
Muheshimiwa mbunge alitumia faida ya goli la ugenini, Caro yu mgeni jijini London akiwa anashangaa kila kitu anachokiona.
Siku hiyo walilala chumba kimoja, kila mtu akiwa katika kitanda chake.
Usiku huo ukapita salama kabisa, ukaja usiku wa pili na wa tatu katika hoteli hiyo ambayo kila panapoitwa asubuhi basi shilingi lakini nne za kitanzania zinakuwa zimeteketea.
Hivyo kwa siku tatu zilikuwa ni milioni moja na laki mbili, sahau kuhusu kufuru nyingine wanazofanya wakienda kutembea kati kati ya jiji la London.
Hatimaye ikawa siku ya tano, muheshimiwa mbunge akaamua iwe itakavyokuwa.
Akatumia ule usemi wa mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio.
Caro akiwa kuku mgeni na kamba yake mguuni muheshimiwa akarusha mpunga kuku akaufuata.
Ikawa usiku wa namna yake, muheshimiwa alijua itakuwa kuwa jambo la aibu sana mbele ya rafiki yake iwapo atagundua kilichotokea.
Hivyo akaamua kutumia umafia. Akamwekea Caro kilevi katika kinywaji, Caro akabwia bila kujua. Usingizi ukamkumba.
Mheshimiwa Lucas akamwingilia Caro kimwili pasi na hiari ya yule binti!!
Palipopambazuka Caro alijikuta chumbani peke yake kama alivyolala usiku uliopita.
Muheshimiwa alifika pale baadaye sana na kujifanya asiyejua lolote, lile hata na alikuwa wa kwanza kumweleza Caro kuwa huenda hali ya hewa imemfanya awe mnyonge kama alivyokuwa siku hiyo.
Siku hiyo alipelekwa chuo cha mambo ya ushonaji, fani ambayo alikuwa anipenda. Muheshimiwa akalipia gharama zote na kisha akamuaga Caro kuwa anarejea Tanzania.
Kabla hajaondoka alimsihi sana akizungumza na baba yake asimueleze hali ya kualala chumba kimoja, akatumia lugha ya kiutu uzima.
“Caro nisingeweza kulipia laki nane kwa usiku mmoja kwa vyumba viwili, najua haipendezi kulala chumba kimoja lakini naamini unaelewa!! Wewe ni binti mkubwa unaweza kuchanganua…. nimejitahidi nilipoweza.” Akamsihi na ikawa hivyo.
Baada ya hapo ikawa ni tabia kila akisafiri kuja London anatumia ujanja uleule kumuingilia Caro kimwili.
Hatimaye baada ya mwaka mmoja Caro akainasa mimba!!
Hii ilibadili kila kitu!!
Muheshimiwa akamtamkia Caro waziwazi kuwa anahitaji awe naye kimapenzi……
Tofauti na alivyodhani kuwa caro atamkatalia alishangaa anakubaliwa upesi tu!

______

WAKATI ULIOPO.(2014)

LUCAS alifika nchini uingereza akiwa mtu asiyekuwa na raha kabisa, alifikia hoteli ileile ambayo miaka kadhaa nyuma alikuwa akilala na Caro.
Usiku huu hawakutumia tena vitanda viwili, bali kitanda kimoja wakiwa kama mtu na mpenzi wake, kitanda kingine alilala kiumbe mwingine kabisa asiyejua hata nini maana ya afrika na Tanzania kwa ujumla.
Huyu alikuwa ni Bryan, mtoto wa Caro na Lucas.
Mtoto ambaye hata wazazi wa Caro walikuwa hawamjui, kwa sababu alimfanya kuwa siri kubwa sana, siri kati yake na muheshimiwa mbunge!!
Lakini pia kulikuwa na siri nyingine, siri iliyofananana bomu la nyuklia ambalo likilipuka halina simile linaua maefu kwa makumi elfu!!
Usiku huu walijadili mambo mengi sana na hatimaye muheshimiwa akamueleza Caro kuwa ameamua kuachana na siasa ili apate muda mrefu wa kumlea mtoto wao hukohuko London.
Uamuzi huu Caro aliupinga kwa kumueleza muheshimiwa Lucas kuwa kitendo cha yeye kuacha kazi na kisha kuwa na safari za mara kwa mara jijini London zinaweza kusababisha mkewe akashtuka na hata wazazi wake wakashtuka kuwa kuna jambo linaendelea.
“Pia Lucas tambua nilikueleza na tukakubaliana kuwa Chopa akitoka gerezani utakuwa mwisho wa mahusiano yetu, sasa huoni kama utaniharibia?” Caro alihoji.
Lucas akatulia akimtazama kwa muda kisha akamueleza jambo ambalo awali hakuwahi kumueleza.
“Caro ujue ni kwamba wewe ni msichana wangu wa kwanza kabisa kushiriki naye mapernzi nje ya ndoa yangu, na nilijua kuwa ni bahati mbaya tu. Lakini kupitia usaliti huu nimegundua jambo moja kubwa sana ambalo limeiathiri akili yangu kwa kiwango kikubwa mno.
Hivi haushangai Christina nimemuoa wakati wewe ukiwa sijui form two vile, ulikuwa mdogo sana eti hadi leo hajawahi kushika mimba zaidi ya kuniambia aliwahi kubeba mimba yangu kisha ikaharibika….. umri unaenda eti sina hata mtoto wa kujisifia mtaani akiona baba yake natema pointi bungeni, au mtoto wa kutaniwa kuwa babako ameongea pumba leo bungeni…… sasa sio hisia tena mke wangu ana matatizo ya kizazi na kama hiyo ndivyo, nimempata mtoto niliyekuwa namtamani siku zote kwanini nisitumie muda mwingi kuwa naye……” aliweka kituo.
“Lucas, usinambie eti unataka kumuacha mkeo…”
“Nilimuacha tangu niliposhuhudia tumbo lako likizidi kukua na ulipokubali kwa hiari yako kuwa mpenzi wangu…” Mheshimiwa alijibu.
Caro akachoka na kujilaza kwenye kitanda.
Mazungumzo yalichukua muda mrefu na kamwe msimamo haukubadilika Lucas alikuwa ameamua iwe atakavyo.
Walilala huku Caro akimweleza Lucas kuwa anataraji kusafiri kwenda Tanzania kuwasalimia wazazi wake kwani ilikuwa imepita miezi miwili hajaenda.
Lucas akamkubalia kwa sababu haikuwa mara ya kwanza kufanya hivyo!!
Alikubali bila wasiwasi wowote kwa sababu alijua kuwa bado mwaka mmoja Chopa atoke gerezani hivyo hakuna namna yoyote ya wawili hawa kukutana.
Ni usemi usiobadilika kila siku kuwa, laiti kama tungelijua lijalo na tungezificha nyuso zetu ili lisituumbue usoni!!
_____

ASUBUHI majira ya saa nne, tayari Chopa alikuwa amekabidhi chumba katika nyumba ya kulala wageni alipokuwa ameuweka ubavu wake kwa usiku ule alioingia jijini Dar es salaam.
Sasa alikuwa hana tofauti na vijana wengi wa mjini, alikuwa amevalia suruali yake ngumu aina ya ‘jeans’ iliyoukamata vyema mwili wake na juu alikuwa amejivisha fulani nyekundu isiyokuwa na maandishi ya aina yoyote ile, chini alivaa makubadhi!! Hii ni baada ya bei ya kiatu kumshinda!!
Alipanda daladala akiwa mkimya kabisa, alienda hadi maeneo ya Makumbusho, akachepuka mitaa kadha wa kadha hadi akaifikia ile nyumba ambayo kabla hajaenda jela palikuwa nyumbani kwao Caro mchumba wake.
Alikuwa akiombea sana amkute Caro. Nia ikiwa moja tu amuulize ni kwanini amemtenga kwa miaka miwili mfululizo pasi bna kukanyaga gerezani alipokuwa amefungwa!
Alipofika pale alikutana na sura ngeni machoni pake, akalazimika kuulizia na hapo akaelezwa kuwa anaowaulizia walihama mwaka mmoja na nusu uliopita na walihamia jijini Mwanza lakini hakuna hata mtu mmoja aliyefahamu eneo rasmini walipohamia.
Chopa akashusha pumzi zake kwa nguvu sana huku akiwa amejishika kiuno. Waliomjibu wakaendelea na shughuli zao.
Naye alipokosa lolote la kuuliza akageuka kurejea alipotoka, alipita mitaa miwili zaidi akaiona nyumba ambayo ilikuwa haina mabadiliko sana, nyumba ile zamani aliwahi kuishi rafiki yake Caro. Na mara nyingi alikuwa akikutana na Caro eneo lile kwa ujanja ujanja kuwa ameenda kumsalimia rafiki yake.
Chopa akajaribu kuvuta kumbukumbu ya jina la yule rafiki yake Caro lakini jela ilikuwa imemvuruga vibaya mno hakuna alichokuwa anakumbuka.
Alijiuliza iwapo aende ama asiende, moyo mmoja ukamsukuma mwingine ukamvuta.
Akachukua maamuzi ya kwenda, akalifikia geti na kugonga mara tatu, hatimaye mlango ukafunguliwa na mwanamke mtu mzima kiasi akiwa amebeba mtoto mgongoni.
Chopa akampa salamu zake na kisha akajaribu kuulizia kwa kadri alivyodhani anaweza kueleweka.
“Sasa kaka unamuulizia mtu ambaye hata jina lake humjui unamaanisha niwaambie nyumba nzima watoke nje ili uwakague au? Maana sikuelewi mara ananifanana mimi mara sijui nini….” yule mama akamuuliza huku akionekana wazi kukwazika na uwepo wa kijana yule.
Chopa hakuridhika akaendelea kusihi, yule mama akamwambia aendelee kukaa pale nje na kuwakagua wanaoingia na kutoka mle ndani huenda akamuona anayemfananisha.
Alimpa jibu lile kisha akaondoka.
“Mama samahani nimemkumbuka anaitwa Victoria, ni Victoria.” Chopa akamsihi yule mama.
Mama yule akageuka upesi.
“Umesema…”
“Anaitwa Victoria yeah ni Victoria sidhani kama nimekosea.. anafanana na wewe sana tu..” Chopa aliendelea kuzungumza akiwa amechangamka.
Yule mama akapiga hatua mbili zaidi kumkaribia Chopa.
“Unamtakia nini huyo Victoria…”
“Aaam! Si kwa ubaya mama yangu….”
“Sijakuuliza iwapo ni kwa wema au ubaya na hata ingekuwa kwa ubaya bado usingesema ungedanganya tu!!” alijibu kwa kujiamini.
“Aaah! Ni siku..ni miaka mingi sijaonana naye walah! Nahitaji kumsalimia tu…ni miaka mingi” Chopa akamjibu.
“Haya nimwambie nani anamuita…”
“Sijui atanmikumbuka… lakini mwambie Manfredy asipoelewa mwambie Chopa wa caro!!” alijibu huku uso wa tumaini ukijengeka katika muonekano wake.
Asalaale!! Yule mwanamke akakodoa macho yake, akapiga hatua zaidi kumsogelea Chopa. Hali hii ikamshtua Chopa… yule mama alikuwa anataka kusema neno lakini hakuweza kusema.
Alipomfikia Chopa alimkumbatia kwa nguvu sana kisha akamuachia.
Chopa alimtazama yule mwanamke, alimshuhudia akiwa katika mvua ya machozi….
“Chopa shemeji yangu pole Chopa…ona ulivyokonda Chopa… ona ulivyobabuka ngozi Chopa aaah! Walikuonea Chopa shemeji yangu…….”
Sasa Chopa aliweza kumtazama vizuri zaidi yule mwanamke aliyekuwaakimfananisha na Victoria….
Hakuwa amefananisha bali aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Victoria mwenyewe.
Wakakumbatiana kwa mara nyingine, huku Chopa akimsihi Victoria asiendelee kulia sana kwa sababu sasa yupo huru na kinachotakiwa ni kuyatazama maisha katika jicho jingine na si kwa kutazama yaliyopita.
Victoria alimkaribisha ndani Chopa walizungumza kwa muda mrefu sana juu ya maisha yalivyoenda kasi katika ulimwengu wa uhuru aliouacha.
Chopa alilalamika sana kuwa Caro alimtupa moja kwa moja na kamwe hakwenda kumsalimia gerezani.
“Chopa shemeji yangu yaani Caro usimlaumu kabisa, amepambana yule akatafuta wakili akatafuta sijui vitu gani, mwisho anakuja kuambiwa mara umehamishwa gereza mara hauruhusiwi kuonana na mtu…. wamemtesa sana kimawazo hadi akaugua hakuwa akijitambua tena…. mara ya mwisho nadhani ni mwaka juzi mwanzoni hivi niliwasiliana naye akasema kuwa yupo Mwanza lakini muda wowote ule anaweza kwenda nje ya nchi…. akaniambia atakuja dar tutazungumza kirefu… lakini ikawa bahati mbaya alipokuja dar mimi nilikuwa nipo chumba cha kujifungulia. Hivyo alipiga sana simu na kutuma sanja jumbe lakini mimi sikuwa na fahamu maana nilijifungua kwa upasuaji. Nilikuta tu ujumbe wake akinisihi vile vitu vyako nikutunzie ipo siku utatoka yeye anaondoka….” alimaliza kusimulia kwa uchungu Victoria.
“Vitu gani tena…. na pole sana kwa uchungu wa uzazi uliopitia” Chopa alizungumza huku dhahiri akionekana kuwa na kiherehere cha kujua ni nini kiliendelea zaidi.
“Yaani huwezi amini mama alikuwa ananishangaa kweli nilivyokuwa mkali mtu akitaka kugusa huo mzigo.” Alizungumza huku akisimama kuelekea ndani, Chopa akabaki kusubiri.
Baada ya kama dakika mbili Victoria alirejea.
“Vipi unalikumbuka hili?” alimuonnyesha begi dogo. Chopa akafikiri na kusema kuwa halikumbuki.
Victoria akatikisa kichwa kusikitika.
“Ujue shem jela kuna mambo mengi sana yanaudhi, yanatibua akili na kukufanya ujione wewe si mwanadamu. Kushuhudia wafungwa wanakufa, kushuhudia wanaume wakigeuzwa wanawake, na mambo mengine mengi yasiyosimulika. Nisamehe bure lakini ukweli ni kwamba asilimia 70 ya mambo niliyoyaacha huku duniani hata siyakumbuki kabisa…..” Chopa alizungumza kwa sauti tulivu sana huku akionekana kuzidiwa na hisia za alichokuwa anasimulia.
Victoria akampatia lile begi na kumwambia kuwa humo kwenye begi kuna baadhi ya vitu ambavyo Caro alimsihi sana avitunze na kumpatia akitoka gerezani.
Chopa akalifungua begi.
“Mh! Hivi hii ndio ile simu yangu au?” aliuliza Chopa huku akicheka.
“Ona na hii ni ile saa, aah! Masikini hii saa alininunulia Caro wangu hii naikumbuka halafu wewe ndo uliniletea siku ile….” Chopa aliitazama ile saa kwa muda chozi likamdondoka.
Victoria naye ikawa hivyohivyo!!
“Hii simu ni nzima kweli?” alizungumza kama anayejiuliza.
“Juzi tu nimetoka kuichaji, Caro aliniambia niwe naichaji isije ikfa…”
Chopa akaiwasha, kweli ikawaka na ikaandika maneno ambayo yalimkumbuisha mbali sana.
“LIWAKE JUA, INYESHE MVUA SITAKUBADILIKIA C WA C”
Maneno yale aliyaandika Caro katika simu yake na simu ya Chopa pia. Wawili hawa walizoea kuitana C wa C yaani akiita Caro anamaanisha Chopa wa caro na akiita Chopa anamaanisha Caro wa Chopa.
Baada ya maneno yale simu ikaomba michirizi ya siri ya kuifungua.
Chopa akajaribu kwa mara ya kwanza ikagoma, akajaribu ya pili hakufanikiwa kitu.
“Shem! Ombea sana jela ibakie kuwa hadithi tu katika maisha yako na familia yako…. yaani huwezi amini nimesahau password!!” alizungumza kwa masikitiko huku akijilaza katika kochi katika namna ya kuegemeza kisogo chake hivyo akawa anatazama darini.
“Halafu shem nimeiona hii simu nd’o nimekumbuka vizuri sasas kuwa ni mojawapo kati ya kitu ninachokihitaji sana kwa sasa…”
“Basi hapo huna ujanja itabidi uiflashi” Victoria akatoa ushauri.
“Hapana Shem hii nikiiflashi kila kitu kitapotea kutoka humu kuna namba ya mtu na meseji zake, naamini huyu mtu anajua kwanini mimi nilipelekwa jela…. huwezi amini hadi sasa sijui kwanini nilifungwa gerezani…”
“Shem hayo yamepita tena umesema wewe mwenyewe basi hapo la msingi ni kutazama mbele….”
“Hapana Viki, naweza kusema yameisha je nikianza kutazma mbele halafu huyu mtu anichukue tena na kunipeleka gerezani patakuwa na maana gani, natakiwa kuwa mtu huru katika maana halisi ya kuwa huru…… siwezi kuishi maisha haya ya mashaka shem acha nimjue tu, nikishamjua wala sitazua mengine.” Alisimamia msimamo wake Chopa.
“Mh! Sasa hapo ndo mtihani, hakuna fundi wa kukutolea hizo loki bila kupoteza hizo namba na meseji.”
Aliposema vile mara Chopa akasimama wima, akarusha ngumi hewani kama mtu anayeshangilia akarukaruka juu kana kwamba amefunga goli.
“POCHAAAAAAA!!!” Akapiga kelele za wastani. Akiwa mwingi wa furaha.
“Una nini wewe Pocha nd’o nani?”
“Mtaalamu wa kutoa loki ya simu yoyote ile bila kupoteza namba wala kupoteza meseji yoyote ile…..” Chopa alizungumza na kisha kumwagia sifa kemkem Pocha.
Na hapo akaaga kuwa anaeneda kuona uwezekano wa kuonana naye. Akachukua namba za simu za Caro na kumsihi kuwa atawasiliana naye kwa lolote lile.

Chopa akaondoka na kuelekea gereza la Ukonga.
Huko akafanya mazungumzo pale ofisini na kujieleza shida yake, akadai anamuulizia ndugu yake ambaye hajui amefungwa gereza gani. Lakini ameelekezwa kuwa ni hapo Ukonga ndipo amefungwa.
Akaulizwa jina lake akataja jina moja tu la Pocha.
Ilikuwa ngumu sana kupata msaada kwa kutaja jina moja tu. Lakini bado walipekua jina lile kwa utulivu lakini hakuna jina lililofanania lile katika orodha ya wafungwa wote pale Ukonga!!
Alipewa daftari akajihakikishia hadi katika orodha ya wale wanaotumikia vifungo vya maisha hapakuwa na jina Pocha!!

Chopa akaaga na kuondoka akiwa mnyonge kabisa, ile furaha yake yote ikayeyuka!!!
Alitembea kwa mwendo mrefu kiasi, akajihisi kichwa kinamuuma sana. Akauona mti wenye kivuli akakusudia kujipumzisha kwa muda pale, akalifungua tena begi lake na kupekua hapa na pale vitu vya ziada ambavyo Caro alimuhifadhia.
Alijikuta akitabasamu alipokutana na kadi zake za benki. Alimfikiria sana Caro na kukiri kuwa yule alikuwa ni binti wa kuigwa, alikuwa ni yule asiyesahau fadhila na anayeona mbali.
“Sijui zimefungiwa?” alijiuliza…..
Baada ya kupumzika kwa muda akataka kupanda daladala, lakini akajikuta akicheka mwenyewe kwa sababu yeye alikuwa ni mzururaji hakuwa na sehemu rasmi ya kwenda sasa kulikoni kupanda daladala, akanuia kulala hukohuko Ukonga siku hiyo.
Kwa sababu muda ulikuwa bado unaruhusui akaamua azurure kidogo.
_____
ITAENDELEA

MPANGO WA KANDO SEHEMU YA TATU

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment