MPANGO WA KANDO SEHEMU YA TANO
NEW AUDIO

Ep 05: Mpango wa Kando

SIMULIZI YA MPANGO WA KANDO FULL EPISODE
MPANGO WA KANDO SEHEMU YA TANO

IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi : Mpango Wa Kando
Sehemu Ya Tano (5)

WAKATI ULIOPO

POCHA alitabasamu baada ya kuwa ameusikia mkasa wa Chopa kwa urefu kabisa.
“Yaani nilihisi tu huu ni MPANGO WA KANDO….” Alkazia, sasa Chopa alikereka kwa kauli hii yenye utata.
“Pocha eeh! Ujue hatupo gerezani hapa acha masihara yako, hapa hatuijui hata kesho yetu tupotupo tu, nini maana ya huo mpango?” aliuliza kwa kukoroma.
“Chopa rafiki yangu, ni mwanamke wa nje….. chanzo cha haya yote ni mwanamke wa nje…. Tanzania mnamuita mchepuko ama vyovyote vile lakini nchini Kenya anajulikana kama MPANGO WA KANDO…… na huu utata utake usitake mpango wa kando anahusika. Iwe huyo uliyemtaja kutoka Rwanda ama yeyote ambaye haujanitajia unamjua mwenyewe… kama asingekuwa mpango wa kando nakuhakikishia usingekuwa hapa hadi dakika hii….” Pocha hatimaye alimweleza Chopa kiuwazi kabisa juu ya hisia zake.
“Unamaanisha Nkozi anaweza kuwa nyuma ya haya yote Pocha??
“Siijui hata sura yake Nkozi japokuwa naelewa kuwa atakuwa na pua ndefu ya kitutsi, nisimsingiziea nisiyemjua ila huu ni MPANGO WA KANDO!!” Alimaliza Pocha kisha akamuaga Chopa wakakubaliana kuwa watulie kila mmoja atafakari na kisha usiku mwingine warejee wakiwa na jibu la nini wafanye.

_____

SOFIA BOSCO alikuwa katika pembe moja ya chumba alichokuwa amelazwa baba yake mzazi. Alitambua wazi kuwa ikiwa baba yake atapona basi kuna kitu atakuja kukisema ambacho ni hatari sana kwa watu waliomfanyia vile, hivyo kwa taarifa yoyote ile kuwa mzee Bosco yu hai watafanya kila namna ili waweze kumuangamiza kabla hajasema neno lolote.
Hali hii ilimfanya Sophia awe mlinzi wa ziada pasi na kushtukiwa na mtu yeyote yule kuwa anamlinda mzee wake.-
Walikuwepo walinzi kutoka serikalini lakini hawa wote Sofia hakuwaamini ipasavyo hasahasa linapokuja suala la rushwa. Ikiwa mtu anaweza kumuuza ndugu yake kwa thamani ya pesa kivipi hawa washindwe kumuuza baba yake mzazi?
Hili lilimfanya amsahau Pocha kwa muda na hata alipokuja kumkumbuka alikuwa amechelewa Pocha hakuwa jirani na eneo lile la hospitali.
Upesi akawaweka watu wawili katika mzani, baba yake mzazi na Pocha. Baba akawa mzito zaidi… akaamua kumweka kiporo Pocha!!
Akabaki analinda mtu asiyewindwa na mtu yeyote yule!!
Akiwa katika ile pembe Sofia aliwaona watu wakiingia na kutoka katika wodi mbalimbali, mara akawaona mwanamke na mwanaume ambao haikuhitajika ushahidi wa mahakamani ili wakiri kuwa wapo katika mahusiano, walikuwa wanasukumi kitoroli kidogo ambacho ndani yake alikuwa amebebwa mtoto mdogo. Aliwatazama furaha walizokuwanazo. Katika nafsi yake akakiri kuwa wawili wakiwa katika mahusiano thabiti kisha wakapata mtoto mahusiano yao yanakuwa na amani sana.
Sofia akajiuliza maswali mawili matatu.. kisha akajipekua akaitoa simu yake na kuibofya ikatoa mwanga akaitazama katika kioo, akaitazama kwa muda picha ya yule mtoto aliyekuwa katika kile kioo. Akatokwa na kite cha ghahabu kabla hajaamua kuifunga. Kisha akairejesha simu yake mfukoni.
Akajizuia kufikiria mengi kuhusu maisha yake, badala yake akaendelea kuwa makini kabisa na kila mtu anayeingia na kutoka katika wodi aliyolazwa baba yake!!
_____

SIMU YA MUHIMU

POCHA na CHOPA walikutana takribani mara tatu katika kuweka mipango sawa, hadi wakati huo Pocha alikuwa amefanikiwa kufungua milango mitatu kasoro mlango mmoja tu wan ne ambao haukufungwa kwa nambari za siri. Huu ulikuwa umefungwa kwa kutumia kitasa.
Siku zote hizo walikuwa anaifungua milango ili kupata mustakabali wa eneo ambamo walikuwa wamehifadhiwa bila kujua nini hatma yao.
Hatimaye ikafika siku waliyokusudia kujitoa muhanga kupiga hatua mbele bila kurudi nyuma, kabla ya kufikia hatua hii walizungumza kwa muda mrefu Chopa akamuelezea Pocha mazingira ya kutekwa kwake, alielezea jinsi huyo binti anayejiita Tz 11 alivyokivamia chumba chake, na Chopa alivyojaribu kumkabili alikutana na kitu cha tofauti kabisa. Kila ngumi aliyokuwa anaitupa ilikuwa inaishia hewani, yule binti ni imara zaidi ya imara yenyewe.
Jinsi alivyodhibitiwa hadi kutolewwa nje ya kile chumba katika namna za kimafia alikiri kuwa hata zoezi lao la kutoroka ikitokea wanakutana na yule binti basi mpango utakuwa umeishia hapo.
Asubuhi baada ya kuwa wamehudumiwa kifungua kinywa kila mmoja kwa wakati wake walingoja ikapita dakika zipatazo arobaini na tano, Pocha akatoka kule chumbani kwake na kuingia kwa Chopa. Walikuwa wameamua kama ni kufa wafe kishujaa.
Walipeana maneno ya kijasiri yenye kuhamasisha sana, kisha wakakubaliana kuwa ikitokea mmoja amefanikiwa kupenya na akiona wazi kuwa mwenzake hawezi kupenya basi hakuna kurudi nyuma ni kusonga mbele tu!
Kuliko wote kukamatwa tena ni heri mmoja akawe shuhuda.
Wakakumbatiana na kuuendea mlango, Pocha akaitoa loki.
Wakaingia chumba kingine na huko hivyohivyo, palikuwa kimya kabisa. Hatimaye wakakifikia kile chumba kilichokuwa kinahitaji kung’olewa kitasa ili waweze kupita.
Ili wapiti walilazimika aidha kuuvunja mlango ama kuutafuta funguo ili waweze kuufungua.
Kuhusu kuuvunja hili lilikuwa jambo la hatari sana kwa sababu lazima wangepiga kelele, na hawakuwa wakijiamini kama wapo peke yao eneo lile, na kama hawapo peke yao basi mtu wa nje akisikia purukushani hizi lazima atatoa taarifa. Na hizo taarifa zikimfikia Tz 11 basi kila mmoja ataambulia kipigo cha mbwa mwizi.
Pocha akaanza kuhaha huku na kule katika mabegi kadhaa pale ndani akiutafuta funguo bila mafanikio. Alijaribu kutafuta kitu ambacho wanaweza kukitumia labda kuuvunja mlango, lakini hakikupatikana.
Akiwa anaelekea kukata tamaa mara alikutana na kitu ambacho kilirejesha matumaini, alikuta kuna simu imehifadhiwa mahali ikiwa imefunikwa na nguonguo kadhaa, bila shaka ilikuwa pale kwa ajili ya kuingiza moto wa umeme.
Simu hii haikuwa imefungwa kwa nambari za siri, Pocha akaichukua na kubofya nambari kadhaa, simu ikaanza kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
“Unampigia nani?” Chopa aliuliza kwa kunong’ona.
Chopa akamfanyia ishara kuwa awe na subira.
Chopa akatulia!!
Simu ikapigwa mara ya pili, ikaita tena kwa muda mrefu lakini safari hii ilipokelewa.
“Sofia… Sofia… ni mimi Pocha..” alizungumza kwa sauti ya chini ikiwa inaambatana na kitetemeshi cha uoga.

______

SIMU aliyopigiwa majira ya saa nane usiku huku Pocha akimsisitiza kuwa mahali walipo ni mchana kweupe kabisa ilimchanganya, kama yeye aliyepo maeneo ya Muhimbili jijini Dar es salaam ni saa sita kasorobo usiku inakuwaje anapigiwa simu yenye nambari za Tanzania na kisha mpigaji anadai kuwa mahali alipo ni mchana kweupe.
Sofia akaumiza kichwa kwa muda mrefu kabla hajajipuuza na kujicheka, alijicheka kwa sababu alijisahau kabisa na kuishi ulimwengu wa kawaida ambapo ni rahisi sana kuchezewa akili yake.
Akatikisa kichwa chake na kuhamia katika ulimwengu ule wa kipelelezi na kijasusi.
Upesi akaichukua simu yake ile yenye picha ya mtoto mbele yake, akabofya mara kadhaa kisha akaingiza ile namba. Akajaribu kuisoma kwa kutumia teknolojia ni mahali gani ilikuwa inatokea.
Akashusha pumzi zake kwa nguvu sana ilipomjibu kuwa eneo ilipo simu ile halitambuliwi na teknolojia hiyo.
Akacheka kidogo na kisha akakiri kuwa mchezaji wa mchezo huo amepitia njia zilezile ambazo yeye mwenyewe ni aidha anapitia ama bado anapitia.
Swali lake likawa moja, je huyu mpinzani wake tayari amefuzu mafunzo yote ama bado yupo darasani?
Kama amefuzu basi huu mtihani utakuwa mkubwa sana kwake na anaweza kufa kama kuku ama kudhalilishwa kama mtu aliyekamatwa ugoni kisha kuachwa aende zake na mgoni wake baada ya kuumbuliwa.
Sofia akakiri kichwani mwake kuwa hapo lazima aicheze hiyo karata ambayo anapaswa kuicheza.
Akaichukua simu yake na kupiga tena zile nambari ambazo Pocha alitumia kumpigia, Pocha akapokea upesi.
Sophia hakumwachia upenyo wa kusema lolote lile badala yake akampa maelekezo.
“Nisikilize kwa makini sana Pocha, usikate simu lakini naomba muda huu.. bonyeza reli.. kisha usiiachie alama ya reli bonyeza nyota kisha bonyeza namba sifuri….. tafadhali zingatia na ufanye hivyo sasa hivi, anza na reli kisha nyota halafu namba sifuri…. fanya sasa hivi!! Lolote litakalotokea tafadhali usifanye jambo lolote la kipuuzi.. baki hapo ulipo.” alisihi Sofia.
Pocha akatii na kufanya alivyoelekezwa…… alipofanya vile kwa usahihi kabisa simu ile ikazima palepale na hata alipojaribu kuiwasha haikuwaka tena!!!

Kwa upande wa Sophia upesi alichukua pikipiki ya mojawapo wa askari aliyekuwa akiimarisha ulinzi pale alimweleza kuwa anaenda mahali kununua kitu anarejea punde!
Alifanya vile ili kama kuna mpango wowote unataka kufanywa basi ufe mara moja!!
Hakuwa akienda jirani, alipita kituo cha mafuta akajaza tangi kwa unusu!!
Kisha akaipandia pikipiki na kuondoka kwa mwendo mkali sana, ulikuwa ni usiku na hapakuwa na msukosuko wowote barabarani.
Aliendesha huku akiwa anaitazama simu yake mara kwa mara, alitambua kuwa akichelewa kwa saa zima zaidi basi hatakuwa na namna nyingine ya kumtambua walau huyu adui yake walau kwa sura na ubora wake katika Nyanja hizo.
Alikuwa amebakiwa na dakika tano tu za kuweza kufika eneo analotakiwa kufika akiongozwa na simu yake.
Hapo alishuka katika pikipiki yake na kuiegesha eneo lililokuwa linauza pombe, aliingia pale ndani kama mteja, akaikabidhi pikipiki kwa mlinzi na kumpatia noti kadhaa ili aimarishe ulinzi zaidi katika chombo chake. Kisha akaingia na kutokea mlango wa nyuma.
Akapiga hatua akiwa anaisoma simu yake ikiwa inamuonyesha uelekeo.
Hatimaye akaiona nyumba fulani iliyojitenga ikiwa inawaka taa ambazo mng’aro wake wa nje ulimaanisha kuwa hapo ndani ni angavu zaidi.
Upesi akaihifadhi simu yake na kutulia kwa muda akiwa amejiaminisha kuwa alipokuwa ni sehemu sahihi kabisa.
Alikuwa amevaa mavazi anayoyapenda hasahasa akiwa katika hekaheka.
Suruali iliyombana na fulani pamoja na viatu vyepesi vya mazoezi.
Sofia alitulia pale kwa dakika moja nzima bila kutikisika mwili lakini macho yake yakifanya kazi kwa kasi mno. Alitazama kama kuna dalili yoyote ya uwepo wa kiumbe hai eneo lile.
Kwa ile dakika nzima hakusikia chembe ya uhai eneo la nje, akapiga hatua kwa tahadhari kubwa sana akafika nyuma ya ile nyumba, akatazama sehemu yoyote ambayo angeweza kuitumia kuingia ndani, hakufanikiwa kuona sehemu yoyote, alijua wazi kuwa kupita mlango ni kujihatarishia usalama.
Akiwa bado katika kufikiria nini cha kufanya, aliona kivuli kikijongea katika nyumba ile huku kikiyumbayumba, Sofia akatulia tuli bila kujitikisa hadi alipohakikisha kuwa uelekeo wa kiumbe kile ulikuwa ni katika lango kuu la kuingilia katika ile nyumba.
Akahesabu hatua hadi ziliposimama mlangoni, naye akanyata kwa kutumia vidole vya mbele huku akiwa makini kabisa macho yake yakiwa yamelizoea lile giza.
Alipofika katika kona, akainama na kuokota jiwe. Akalitupa pembeni yake likatoa kishindo mithili ya mtu kutua pale.
Alifanya vile makusudi, yule mtu akasita kufungua mlango, akawasha tochi yake na kumulika eneo lile, na hapo akanza kusogea ili aweze kuona ni kitu gani kilichoanguka.
Kwa Sofia huu ulikuwa ni ushindi mdogo sana wala hakutaka kupoteza muda, akajirusha upesi akaipiga teke ile tochi, na kabla hajapiga kelele akamdhibiti kikamilifu yule bwana akatulia tuli.
Sofia akamsukuma wakauendea mlango, yule bwana alikuwa ameweka funguo tayari hivyo alichofanya Sofia ni kumalizia kufungua kisha bila kutarajia akamfyatua teke kali mgongoni akaingia na ule mlango vizuri, sekunde iliyofuata Sofia akiwa na bunduki yake mkononi alikuwa akizunguka huku na kule ili kumkabili yeyote atakayejiweka katika anga zake.
Damu yake ilikuwa inachemka vilivyo!!!
Alikuwa ni msichana mrembo kwa kumtazama lakini alikuwa na roho saba. Roho ngumu kama ya paka…
Yule bwana ambaye alikuwa amelewa sasa pombe zilibaki kutoa harufu tu mdomoni lakini kichwani zilikuwa zimekatika.
“Pocha yupo wapi? Jibu moja tu sihitaji maelezo..” aliunguruma Sofia sasa sauti yake ilikuwa sio ile ya kuremba.
“Simjui mimi ni mgeni…. haki ya Mungu…” ile anamalizia kuapa tu… Sofia aliruka hewani, yule bwana akajiziba uso akauacha mgongo wazi, Sofia aliutaka huohuo.. akambamiza na kitako cha bunduki katika uti wa mgongo, yule bwana alianguka chini kama mzigo huku akilia kama mtoto mdogo.
Kilio chake kiliambatana na maneno ya kujitetea kuwa hajui lolote.
“Aliyekufundisha kuwa sugu hata mimi alinifundisha hivyo hivyo kwamba nisiseme ukweli mpaka nikione kifo sekunde moja kutoka katika uhai wangu…. sasa ngoja…” Sofia akairejesha bunduki mahali pake.
Akamkumba yule bwana pale chini akauchukua mkono wake na kuunyonga.
“Aaaargh!! Aaaargh hili Geto la Rama sio kwangu nisamehee aaaargh! Unaniuaaaa….” al;ilalama yule bwana huku akitokwa na hewa za aina zote safi na chafu!!
“Rama ni nani?” Sofia akahoji….. yule bwana akonyesha ishara ya ukutani, Sofia akatazama akakutana na picha ya mwanaume aliyejazia kimazoezi akiwa na mwanamke pembeni yake.
Ile anataka kuuliza zaidi juu ya Rama mara akasikia sauti ikimuamuru.
“Tulia hivyohivyo wewe kumbe ukitikisika tu nafyatua ubongo wako…” ilikuwa sauti ya kiume ikiunguruma.
Sofia alitulia kimwili lakini sio kiakili, alijua kuwa ameelekezewa bunduki, na siku zote muuaji anayemaanisha huwa haelekezei bunduki miguuni, bali kichwani ama maeneo ya moyo.
Kuna amri ambayo Sofia alikuwa akiingoja, na kama yule bwana angeitoa hi indo ilikuwa ponapona yake.
Kweli kama alivyowaza, ikawa!!
“Nyanyua mikono yako na uiweke kisogoni!!”
Kwa mwanadamu wa kawaida hii amri ni nzito na huwezi kuwa na ujanja tena lakini sio kwa Sofia na watu wa kariba yake.
Ile anainyanyua mikono yake akachomoka na kisu cha kufyatua, na sekunde iliyofuata akainama akageuka kwa kasi…. yule bwana akafyatua kwa papara….
Risasi ikatoka sambamba na kisu…… ile Risasi ikausambaratisha mlango wa chumba kilichokuwa mbele yao.
Kisu kikasambaratisha paja la yule bwana na kumwachia maumivu makali sana bunduki ikamtoka mkononi.
Ule mlango uliosambaratishwa ukaambatana na mayowe ya watu waliokuwa ndani ya kile chumba. Sofia akapita kama kipanga akaitwaa ile bunduki, akafyatua risasi nyingine, akawa amemalizia paja la upande wa pili kisha akaruka katika kile chumba kingine.
Akatua akiwa amepiga goti moja, mkono wa kushoto akiwa na bunduki moja na kulia nyingine, mdomoni akiwa amekiweka vyema kisu chake cha kufyatua.
Alikuwa tayari kwa lolote na aliifurahia hali ile kupita kawaida.
Midomo miwili ya bunduki ya Sofia ikajikuta ikitazama na wanaume wawili waliokuwa wamekumbatia.
Kimya kilipudumu wakati wao walijiandaa kupokea kifo, waligeuka na kutazamana na Sofia.
Wanaume hawa wawili walikuwa ni mapacha wasiozaliwa tumbo moja, Pocha na Chopa!!!
Sofia akaishusha silaha yak echini,badala ya kumshangaa Pocha ambaye wanafahamiana kwa muda mrefu akajikuta akikaziana macho na Chopa!!
“Ni wewe ama nakufananisha?” Sofia akauliza…..
Lakini haukuwepo muda wa Chopa kujibu lolote.
Ikazuka tafrani nyingine kubwa zaidi!!!

______

LONDON
HEKAHEKA INAENDELEA

Mheshimiwa Lucas alitua katika uwanja wa ndege akiwa na tabasamu usoni. Alikuwa na kila dalili ya furaha.
Ndio, lazima afurahi kwa sababu alikuwa upande wa ushindi!
Lucas alikuwa amefanikiwa kumlaghai mkewe hadi akakubaliana naye kuwa hatakwenda uingereza na hataachia ngazi ya ubunge.
Lucas alikuwa ametumia siasa nyingi sana hadi akafanikiwa kumweka sawa mke wake huyo ambaye hawakubahatika kupata mtoto.
Baada ya kufanikiwa katika hili alimtumia tena prisca kumfanikishia kupata tiketi ya kwenda uingereza.
Sasa alikuwa uwanjani akimngoja mtu aliyetakiwa kuja kumpokea, hakuwa mwingine bali alikuwa ni Carolina Edwin, walikumbatiana wapenzi hawa ambao kiumri waliachana mbali kabisa. Caro alikuwa ameambatana na Bryan mtoto wake.
Baada ya kukumbatiana pia na yuole mtoto hatimaye waliingia katika gari, Caro akiwa ni dereva wa kaondoka zao.
Safari hii haikuwa hotelini bali nyumbani kwa Caro. Nyumba ambayo kodi yake analipa Lucas.
Walifika salama salmini nyumbani bila kuwa na mashaka yoyote, ile wanafika tu kitu cha kwanza Caro akamuhoji Lucas kuwa ameweza kumshawishi mkewe hadi akamkubalia.
Lucas alimnanga mkewe kwa kiasi kikubwa sana, alionyesha kumchukia waziwazi huku macvho yake yakitangaza ni kwa kiasi gani ametekwa na penzi la Carolina.

Kitu ambacho hakujua Lucas na Carolina ni kwamba ule usemi wa mnyongew mnyongeni lakini haki yake mpeni huwa unafanya kazi hata kama unadharauliwa.
Siku saba za awali Lucas mtu huru kabisa walizitumia kujirusha katika kumbi mbalimbali za starehe na Carolina, wote walionekana kuifurahia hali ile hasahasa Caro ambaye starehe za London zilikuwa zimemkosha sana na hakuwaza kuziacha hivihivi zimpite.
Walienda viwanja vya mpira kutazama mechi ilhali hakuna hata mmoja kati yao aliyekuwa mpenzi wa mpira wa miguu.
Juma lililofuata walianza kuweka mikakati juu ya maisha yao ya baadaye na hapo Lucas akamtamkia Carolina rasmini kuwa liwalo na liwe anahitaji waoane ili wamtunze mtoto wao.
Wazo hilo lilikuwa la ghafla sana kwa Caro na alimuomba Lucas wasitumie muda mrefu kulijadili hilo badala yake walipuuzie kwanza, akataja sababu moja kuwa ni ukaribu baina yake Lucas na Edwin babake Caro.
Kichwani mwake Caro hiyo haikuwa sababu kubwa sana juu ya ukaribu wa baba yake na Lucas, kuna mambo mawili yalikuwa yanamtatiza, la kwanza likiwa ni ule umri wa Lucas alikuwa ni mkubwa sana kwake kwa miaka mingi mno. Lakini lilikuwepo la pili ambalo alikuwa akijiuliza sana kuwa siku likimzidia kichwani mwake itakuwaje na Lucas atalipokeaje?
Wakati akiyawaza haya na kujiona yu katika utata wa hali ya juu. Maisha hayakusimama bali yaliendelea kwenda mbele.
Akajisahau kuwa mzahamzaha……..
Ikawa juma la tatu likikaribia kuwa juma la nne.
Siku hii ilianza vizuri sana, waliamka wote asubuhi wakafanya mazoezi kisha wakamuamsha Bryan na kumwandaa kwa ajili ya shule.. baada ya hapo wakapata kifungua kinywa wakamsindikiza Bryan shuleni. Wao wakarejea nyumbani kufanya shughuli nyingine.
Majira ya jioni kama saa kumi na moja balaa likaanza.
Lucas akapigiwa simu kutoka Tanzania akielezwa kuwa kuna ndugu yake amepatwa na tatizo kubwa hivyo anatakiwa upesi sana kurejea nyumbani.
Alijaribu kuhoji ili apewe walau muhtasari kwa ufupi lakini mpiga simu alimsihi sana kuwa haina maana kuzungumzika kwenye simu afanye upesi aende nyumbani.
Wakati Lucas akijiuliza ni kitu gani hasa kimetokea akiwa ameanza utaratibu wa kutafuta tiketi mara anapewa taarifa na Caro ambaye alikuwa mkewe wa London kwamba kuna simu imepigwa kutoka shuleni kwao Bryan kuwa mtoto hajaonekana kuanzia majira ya saa sita walipotoka kupumzika.
Wakauliza kama kuna namna yoyote ya mtoto kuwa amefika hapo nyumbani jibu likawa ni hapana.
Sasa Lucas alitaka kupasuka kichwa, taarifa zikatolewa vituo kadhaa vya polisi. Shule nayo ilikuwa katika hekaheka za kumtafuta Bryan.
Hadi zinapita siku mbili bado Bryan alikuwa hajapatikana, huku kamera zilizotengwa maeneo kadhaa ya pale shuleni zikishindwa kung’amua kabisa ilikuwaje yule mtoto hakuonekana.
Wangeweza kusema lada amenguka kwenye mashimo ya vyoo lakini yalikuwa yapo mbali kabisa na ni mpaka kutumia nguvu kuyafunua ili uweze kufikia hatua ya kutumbukia mle, sasa huyu mtoto mdogo ilikuwaje?
Simu kutoka Tanzania nazo zikazidi kumbughudhi Lucas akajikuta hana namna zaidi ya kumuacha Caro akibubujikwa na machozi na yeye akikwea ndege kurejea nchini Tanzania ili kukabiliana na tatizo jingine.
Tatizo asilolijua!!

____
Christina alikuwa mnyonge na aliachwa Tanzania huku moyo wake ukimuuma sana. Angefanya nini wakati hakuwa na ushahidi wa kutosha kuwa mumewe anajihusisha kimapenzi na Caro?
Ni kweli kuna alama aliiona mgongoni mwa Caro lakini je huu ni ushahidi tosha?
Jibu ni hapana…
Lakini hata kama ni hapana bado kitendo cha Lucas kuwa na mwanamke wa nje ni kosa kubwa, lakini angefanya nini??
Dawa ilikuwa kuupata ushahidi wa kutosha na kisha kujiandaa kukabiliana na ukweli uliopo mbele yake.
Christina alipomkubalia Lucas kuwa aende uingereza peke yake, huku nyuma hakubweteka bali akili kumkichwa akatafuta namna ya kuujua ukweli ambao aliamini kuwa utamuumiza sana.
Akawasiliana na balozi wa Tanzania nchini uingereza ambaye ndiye aliyemfanyia mpango hadi kufanikiwa kuingia bunhgeni. Akamueleza ukweli juu ya mumewe, balozi yule mtu mzima akamwomba awe mtulivu atamsaidia kuujua ukweli.
Baada ya hapo akamuunganisha na kijana mmoja wa kitanzania aishiye Londoni, akahakikishiwa kuwa kijana yule ni muaminifu kabisa.
Akamweleza kila kitu kisha kijana akaiomba picha ya Lucas.
Christina akaituma na kisha akayangoja majibu.
Yule kijana aliyepewa lile jukumu alikuwa kimya na alimsihi sana Christina awe na subira na wala asimkumbushe kwa sababu anaijua kazi yake.
Kweli ile subira ikaivuta kwa ukaribu kabisa heri lakini hii heri haikuwa tupu ilibeba mengi ndani yake.
Siku hiyo alipokea simu kutoka London kijana akamwomba aingie katika mtandao kuna vitu amemtumia katika barua pepe yake.
Lakini kwa ufupi akamueleza jambo.
“Mume wako ako na mpango wa kando huku London..” alizungumza kwa lafudhi ya kikenya yule bwana.
“Mpango wa kando ni nini?” Christina alihoji….
“Utamuona katika hizo document” alijibu na kukata simu.
Christina upesi akaingia katika kompyuta yake, kabla ya kufanya jambo lolote lile akamuomba Mungu ampe uvumilivu wa lolote atakaloliona, lakini kubwa zaidi aliombea kuwa na awe mwanamke yoyote yule lakini sio Carolina ambaye ni kama mtoto wake.
Alifungua vitu alivyotumiwa huku akitetemeka sana…
Macho yake yalimshuhudia mume wake akitanua na yule mtoto… picha zao wakiogelea huku wamekumbatia ziliiumiza sana nafsi ya Christina.
Alijikuta analia sana mbele ya ile kompyuta yake.
Kilio chake hakikusaidia lolote lile.
“Looh! Lucas.. yaani na huyu mtoto kabisa…..” akajisemea huku akiyafuta machozi yake.
Wakati akilia kwa uchungu mkubwa, kuna mwanadada mwingine yeye alikuwa katika biashara yake isiyokuwa na malipo.

Huyu alikuwa ni Prisca, baada ya kuwa amezungumza kinaga ubaga na bosi wake akiwa amesimama kama mshauri. Aliyapata mengi sana ambayo hakuwa akiyajua kabisa.
Kuyajua mambo haya kukamfanya ajiulize ikiwa yale maneno aliyoongea na yule mama ambaye aliamini ni mpenzi wa Lucas wa Tanzania kweli yalimtosha ama hayakutosha.
Mbea hana huruma, akaangukia kwenye upande kuwa yale maneno hayakumtosha kabisa yule mama aliyepiga simu kisha haikupokelewa.

Jioni ya siku hiyo akaichukua tena ile namba maalumu, akabofya zile namba na kumpigia.
Simu ikapokelewa na mwanaume.
“Edwin naongea mwenye simu anaoga…” ilijibu sauti ya kiume.
Prisca naye akaiigiza huku amebana pua.
“Edwin naongeaa nyokonyoko…. wanaume sijui mkoje nyie… mwenzako ameona huyo hafai we unaona dhahabu eti mmepeana hadi simu kwa uaminifu gani mliokuwanao labda?? Eeh! Uaminifu gani mtu kaachwa hata wuiki haijapita ushajiona we ndo bonge la bwana unajua kutuliza nafsi sivyo?” alizungumza kwa shari Prisca asijue hata anaongea na nani.
“Sasa sikia nikwambie na umfikishie huyo hawara wako, mwambie chanzo cha Lucas kuruka London tumekijuaaaa kumbe halizaiiiii hahahahahahahaha unalooo unayejifanya bwaaaana tuone kama utamzalisha sasa… au mna mpango gani wenzangu labda….” alihoji Prisca lakini cha ajabu sasa hakumwachia nafasi ya kuongea yule mwanaume.
“Tena mwambie apigie mstari kabisa… huko London ana katoto kana kama mwaka na miezi kanasoma na ndo amehamia huko sasa ili akalee vizuri.. we jikalishe hapo mwanaume suruali wenzako wanamkimbia we umejikaliza tu hapo.. hovyoooooooo!” alimaliza na kukata simu hapohapo.
Akatoa ile kadi yake, kisha akaanza kucheka huku akikiri kuwa umbea wa siku hiyo ameutoa kwa kutumia utaalamu wote na popote ulipofika umempiga za usoni muhusika wake.

Wakati Edwin anapokea simu mkewe ndo kwanza alikuwa anamalizia kuoga….. hivyo asilimia kubwa na maongezi aliyasikia, na simu ilipokatwa mama Caro akazungumza.
“Mume wangu, huyu ni Caro anatembea na Lucas rafiki yako.” Aliweka kituo.
Lucas akaruka na kusimama wima katikati ya ile sebule.
“Una uhakika? Umejuaje?” alihoji kwa ghadhabu sana.
“Mama carom bona huo urafiki ndo utaisha nakwambia…” alizidi kung’aka.
“Hata urafiki ukiisha lakini Caro ndiye aliyezaa na Lucas tayari….utafanyaje?
“We mama Caro umekuwaje wewe umemuona mwanangu Malaya sana kwenda kuzaa hovyo tu. Sikia haya maneno ya huyu Malaya wa wapi sijui yasikufanye ukanitukania mtoto….sitaki tugombane mama caro..” alikuja juu Edwin. Lakini mama Caro alimtazama tu, alipomaliza kufoka akamshika bega na kumkaliza chini.
Lucas akatii!!
“Baba Caro usilifanye jambo hili kuleta ugomvi kati yangu na wewe. Tulipotoka na Caro wote tunajua sasa usiniuzie kesi nisizostahili lakini hili jambo niligundua mapema tu lakini sikuwa na uhakika… wewe ni mwanaume huwezi kujua lakini Caro amezaa tena kwa upasuaji, niliona alama za mshonio katika tumbo lake lakini sikutaka kumuhoji, kwa sababu niliamini yeye ni mtu mzima kama lipo analotaka kutushirikisha atatushirikisha. Na maziwa yake nayo yamemuanguka niliona anavyopigana kuyalazimisha yawe wima….. Edwin mume wangu tuna mjukuu…” alimaliza Mama Caro. Akamwacha Edwin swahiba wake Lucas akiwa anatetemeka kwa hasira kali.
Alikuwa anamjua mumewe hakuhitaji kumbembeleza badala yake alienda katika jokofu akamchukulia maji ya baridi kabisa akamwekea mbele yake.
Kisha akatoweka!!

_____

MWISHO WA UBAYA.

ULE muda ambao Sofia alikuwa ameutumia kumshangaa Chopa akiamini kuwa ile sio mara ya kwanza kumuona, alifanya kosa kubwa sana kuupoteza umakini wake, katika sekunde kadhaa alijikuta akipokea mapigo mawili makali mgongoni, kisha akamshuhudia Pocha naye akipokea ngumi kali usoni na kuweweseka akatua chini, Chopa alijihami kurusha teke lakini liliishia kudakwa, akamuona aliyemdaka ule mguu alikuwa anaenda kuuvunja mguu wa Chopa.
Upesi Sofia akajitanua na kuchana msamba kisha akajizungusha na kumchota miguu yule dada, akamsomba hadi chini. Dada yule akatokwa na kilio cha maumivu, lakini upesi akasimama na hatimaye wakawa wanatazamana ana kwa ana.
Haikuwa mara ya kwanza kutazamana, siku ya kwanza walitazama pale katika mgahawa wa magereza huku kila mmoja akiikiri kuwa mwenzake hana macho ya kawaida.
Tz 11 alikuwa ana kwa ana na Sofia.
Hapakuwa na muda wa maongezi bali shughuli kwa kwenda mbele, Sofia akiwa na jukumu la kuwakomboa Pocha na Chopa huku Tz 11 akifanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanabaki pale nsdani ili aweze kulinda kibarua chake.
Pocha na Chopa walibaki chini kuutazama mpambano huu wa wakali wanaojua ni kitu gani wanafanya.
Wakati Tz 11 akiwa ni muuaji wa kulipwa ‘Proffessional killer’, Sofia yeye alikuwa ni mpelelezi mashuhuri aliyepitia mafunzo haya nchini Cuba na kufanyia kazi zake kivitendo nchini uingereza.
Ama! Waliofunzwa wamefunzwa, mapigo waliyokuwa wakitoa yalikuwa yanafanana kuanzia mtindo hadi uzito.
Hii ilisababisha mchuano kuwa wa kukata na shoka, hakuna aliyeruhusu ngumi imuingie wala teke.
Sofia alikiri kimoyomoyo kuwa alikuwa amekutana na kiboko yake.
Lakini hii haikumuogopesha badala yake ilimfanya kuwa mashuhuri zaidi na makini, baada ya kugundua kuwa mitindo yao karibia yote inafanana na hii kuufanya mchuano kuwa mgumu, Sofia aliamua kuingiza mafunzo kadhaa ya kijeshi aliyokuwa akipewa na baba yake.
Na alimvizia Tz 11 alipoduwaa tu akambadilishia mtindo na kisha akamuingia na ngumi tatu kali za uso kabla hajajirusha juu juu na kumtandika kichwa kikali sana mwanadada yule na kufanikiwa kumtupa chini.
Tz 11 alipogundua kuwa anaelekea kuzidiwa baada ya kulainishwa na pigo lile maridhawa, aliruka upesi na kuikamata shingo ya Pocha!!
Akamweleza Sofia kuwa akifanya upuuzi wowote ule anaivunja shingo ya Pocha.
Sofia alijua kuwa yule dada hana masihara hata kidogo na kuua sio jambo jipya kwake, alimtazama kwa makini jinsi alivyokuwa anavuja damu. Akajipongeza moyoni kwa kumwadabisha kiumbe yule mgumu kabisa anayejua mapambano ya ana kwa ana.
“Ni kitu gani unahitaji kutoka kwa hawa…” Sofia alihoji huku akiwa mtulivu kabisa.
“Nipo kazini nadhani unajua siwezi kukujibu.” Alijibu kwa jeuri huku akihema juu juu.
“Sawa muue halafu uje tuendelee kupambana, ili na mimi nikuonyeshe ni ladha gani mtu anaipata akiwa katika kuvuta pumzi zake za mwisho… muue upesi ama la nitamuua mimi mwenyewe…” Sofia alizungumza kiujasiri sana, macho yakamtoka Pocha aliposikia kuwa Sofia anatia saini katika fomu yake ya kifo.
Sofia alizungumza yale lakini akiwa hajajipanga ni jambo gani afanye ili kumuepusha Pocha na dhahama ile.
Akiwa katika utulivu ule mara mlango ulisukumwa mtu akaingia, Sofia bila kuuliza anayeingia ni nani aligeuka na kutokwa na teke kali kisha sekunde iliyofuata alikuwa ameikamata shingo ya yule dada kama Tz 11 alivyoikamata shingo ya Pocha.
“Ngoja nikufundishe kuua maana naona we unatania” Sofia alizungumza huku akijiweka vyema tayari kwa kuua.
Bila kutarajia akiwa ameikamata shingo ya yule dada Sophia alishangaa Chopa anasimama wima akitamani kusema neno lakini neno lenyerwe halikutoka, akazidi kutembea upesiupesi kwenda alipokuwa Sofia.
Alipomfikia akamsihi amwachie yule binti, Sofia alipoendelea na msimamo wake Chopa akatokwa na ngumi kali ikatua katiika uso wa Sofia. Akalainika na kumwachia yule binti.
Ngumi ile ilikuwa na uzito haswa!!
Hata alipokuja kusimama wima alishangaa sana.
Akamtazama Chopa na kisha akamtazama yule dada aliyekuwa amepigwa kabali ile ya nguvu.
“Sofia….” yuledada aliita huku akishindwa kuamini alichokuwa anakiona.
Sofia alibaki katika mshangao mkubwa zaidi, Tz 11 naye akabaki kukodoa macho kugundua wawili hawa wanafahamiana, Pocha yeye alikuwa mtazamaji tu!!!

_____

Kuna mambo mengi ya kukera katika huu ulimwengu, huyu linamkera hili na mwenzake lile. Ilimradi tu dunia haina usawa siku zote.
Mapenzi yameishikilia dunia kwa asilimia kubwa, kati ya maumivu kumi utakayosimuliwa ama kusimulia basi mawili kati ya hayo chanzo chake ni mapenzi.
Inasumbua sana akili kwa muda mrefu unapoyaamini maneno ya mtu na kufikia hatua ya kumkabidhi maisha yako ukamuelezea kila kitu kuhusu wewe kumbe mwenzako anayasikia na kuyapuuzia huku akijifanya kuyaremba maneno yako na neno lake moja tu, ‘nakupenda’.
Mwisho wa siku anakuacha na kwenda zake baada ya kupata kile alichokuwa anakihitaji.
Hali hii huzua hofu ya mapenzi na chuki hata kwa wasiotakiwa kubeba lawama.
Maumivu ya mapenzi yanaweza kukubadilisha na kuwa mwanadamu nje lakini mnyama hatarishi sana katika moyo wako.

KITENDO cha Chopa kumsaliti Nkozi miaka kadhaa iliyopita kilimuathiri sana binti yule wa Kinyarwanda, alikuwa mtu wa kulia kila mara masomo yalimuwia magumu sana.
Marafiki zake wawili yule binti wa kisomali na binti wa kitanzania ambaye ni Sofia hawa ndio waliokuwa wakimtuliza.
Alipokuja kuwaeleza kuwa kilio chake sio tu kwa sababu ya kuachwa katika mataa na Chopa bali kiumbe ambacho Chopa amekiacha katika tumbo lake.
Chopa alimuacha Nkozi akiwa yu mjamzito!!
Marafiki wale wakamshauri sana Nkozi kuwa aitoe mimba ile kwa sababu kuzaa mtoto asiyekuwa na baba kwa hali ile ya kimaisha lilikuwa tatizo kubwa sana.
Nkozi ambaye ile ilikuwa mimba yake ya kwanza kabisa aliufikiria uamuzi wa rafiki zake na kuamua kufanya walichomshauri.
Mimba ikatolewa na hapo akakata mawasiliano kabisa na Chopa alifanya vile ili aweze kumsahau.
Akiwa palepale chuoni ukiwa ni mwaka wa pili alikuja kugundua kuwa kuna tatizo analo, akajaribu kutafuta ushauri kwa madaktari bingwa.
Mwisho wa siku akaambiwa kuwa kizazi chake ni kibovu, na kiliharibiwa ile siku aliyokuwa anatoa mimba.
Taarifa hizi zikakianzisha kilio upya, akamkumbuka Chopa na ahadi zake hewa.
Akajenga chuki ya hali ya juu.
Ni katika kipindi hiki ambacho Sofia aliondoka kwenda kusomea mambo ya upelelezi na mapigano nchini Cuba.
Nyuma akawaacha Nkozi na rafiki wa kisomalia.
Msomali huyu ndiye ambaye baadaye aliijenga dhana ya kisasi katika kichwa cha Nkozi akamsimulia mikasa kadhaa juu ya kisasi.
Nkozi akajikuta anahitaji kumyoosha chopa kwa mambo yote aliyomfanyia lakini alijiwekea ahadi kuwa ikiwa atamkuta Chopa hayupo katika mahusiano yoyote yale atamsamehe kwa maneno lakini akimkuta yupo katika furaha ya penzi na yeye akiwa anaemia tu kwa kusalitiwa na kisha kupoteza kizazi basi ataipata ya motomoto.
Shughuli ikaanza yule binti wa kisomali akamuunganisha Nkozi na mtandao alioufahamu unaohusika na kesi ambazo haziwezi kusikilizwa mahakamani.
Kesi kama ya Nkozi.
Ilikuwa upesi sana akapewa majibu kuwa Chopa na mchumba wa mtu na muda wowote ule wamepanga kuoana.
Nkozi hakufikiria mara mbilimbili akatoa tamko kuwa Chopa avurugwe vibaya mno bila kuumizwa mwili bali akili yake.
Mipango ikaenda sawa, wakati huo Nkozi hana mahaba na mwanaume yeyote yule zaidi ya kuyafanya mapenzi kuwa biashara.
Biashara iliyokuwa inalipa haswa kutokana na umbile lake la kuvutia sana.
Ikawa kama alivyotamka, Chopa akajikuta akitupwa gerezani akipewa hukumu isiyokuwa na kichwa wala miguu lakini miaka mitatu ilihusika.

Ikiwa haijakatika miaka mitatu, Nkozi aliyekuwa masomoni Nairobi nchini Kenya anaelezwa kuwa Chopa yu uraiani, anaamua kumfuatilia tena. Lakini safari hii zile hisia zilizojizika za muda mrefu zinaibuka tena, hisia za chuki iliyokithiri juu ya wanaume.
Anatoa agizo Chopa ahifadhiwe sehemu maalumu ili aje kumuadabisha mwenyewe.
Anafunga safari kutoka Nairobi anapewa maelekezo ya jinsi ya kufika eneo la tukio.
Anapofika anakumbana na hili balaa.
Sasa anatazamana ana kwa ana na Chopa lakini pia anakutana na Sofia rafiki yake kipenzi.
Sasa wanamtazama Chopa anayetia huruma, ule ukarimu wake wa kuwapakia katika lori lake miaka ya nyuma na kisha kumpatia Nkozi pesa kwa ajili ya malazi, wakamtazama kisha Nkozi akayasahau aliyopanga kufanya juu ya Chopa badala yake akahoji kulikoni.
Pocha akaelezea tena jinsi Chopa alivyowasaidia watu wengi gerezani wasionewe, Nkozi akakumbuka ukle moyo wa Chopa wa enzi zile, Sofia naye akakumbuka uchangamfu na maneno ya Pocha siku anawasafirisha kwenda Dodoma bila kuwabughudhi!!
Nani atamfunga paka kengele?
Hili likawa ni swali kwa yeyote ambaye anaweza kuanza kumuhukumu Chopa.
Tz 11 aliyekuwa kimya wakati wote alizungumza maneno machache tu.
“Kwanza wewe dada sijui ndio Sofia, nakupigia saluti… upo vizuri umenihenyesha… pili wanasema ukitaka kumuua nyani ni kosa la jinai kumtazama usoni,. Nyinyi mmetazama tayari, kama ni heri basi haya mambo yaishie hapahapa…. pia wewe Chopa katika haya uliyopitia jifunze mambo mengi ya kuzingatia…. kubwa ni kuwa makini na usiwe mtu wa kupuuzia mambo….. nilikutumia ujumbe kukupa tahadhari hata kabla haujakamatwa usiku ule lakini ulikuwa unapuuzia….” alimaliza Tz 11 kisha akatoka nje akiwaacha wajuanao kuendelea na mazungumzo yao.

_____

LUCAS alifika nyumbani kwake akiwa hayupo sawa kabisa, alipotoka alikuwa ameacha tatizo na huku anapoingia anaenda kuambiwa tatizo. Alikuwa anatembea lakini akili ilikuwa ipo nukta chache kabla ya kumruka.
Alifika nyumbani kwake majira ya saa kumi jioni, alipokelewa na mkewe alimuuliza kuna tatizo gani limetokea hadi akapewa taarifa ile ya dharula arejee nchini Tanzania.
“Mama na baba ni wazima eh!” alihoji huku akionyesha kupagawa waziwazi.
“Wazima tu… nadhani tatizo ni mpango wa kando…” mkewe alimjibu huku akimpokea begi lake.
“Mpango wa… ndo nani huyo aaah! Ndo kitu gani hicho…” aliuliza hovyohovyo.
“Karibu ndani mume wangu….” Christina alimsihi mumewe.
Naam! Akaingia na kukaribishwa sebuleni na Edwin pamoja na mkewe. Walikuwa watulivu sana, wakamsalimia…
Lucas alibabaika wakati anawajibu ile salamu yao. Alijiuliza kichwani mwake kuwa je wale wamekuja kuna tatizo wanataka kutatuliwa ama wamekuja kuzua tatizo jipya.
Hakupata majibu, akachukua nafasi katika kochi!!
Kimya kikatanda kama dakika mbili nzima nadhani kila mmoja alikuwa akisubiri mwenzake aanze kuzungumza, mama caro ambaye walau ndo alikuwa na hali njema katika moyo wake alianzisha mauzungumzo ambayo wao watatu walikuwa wameyaongea vizuri kabisa hapo awali.
Mama Caro alizungumza kwa utaratibu kabisa hadi alipofikia suala la Lucas kuwa na mahusiano na mtoto wake, kwa hilo Lucas alikuwa mkali akalikataa waziwazi, ni hapo ambapo urafiki uliingia ndoa, Edwin alipandwa hasira akatoka alipokuwa ameketi akamvamia Lucas na kumtandika ngumi chini ya jicho lake, ukageuka ugomvi mkubwa na wa kuachanisha walikuwa wanawake, hii ilileta ugumu sana Lucas alitwangana na Edwin. Watu wazima hawa waliangushana chini huyu akimpiga mwenzake hapa na yeye anajibu kwa pigo jingine.
Mkewe Lucas alipoona huu ugomvi hautenganishwi kwa hali ya kawaida, upesi akakimbia ndani akaufungua mlango kisha akarejea na kile kilichofanya ugomvi ukafikia mwisho.
Alirejea akiwa na mtoto….
Lucas alikodoa macho yake na hakuamini kabisa kile alichokuwa anakishuhudia mbele yake alikuwa anamuona mtoto ambaye siku kadhaa nyuma alipotea jijini London na sasa anakutana naye ndani ya nyumba yake, mtoto ambaye alizaa na Caro mtoto wa rafiki yake.
Kufikia hapo sasa Lucas alipiga magoti na kuomba msamaha kwa kila aliyekuwa pale ndani, Edwin hakutaka kumsikiliza, akiwa amechanika mdomo wake aliondoka na kumsisitiza Lucas kuwa asahau kabisa kama waliwahi kuwa marafiki.
Mume ameondoka mke abaki kufanya nini?
Mama Caro naye akafuata nyuma akimwendea mume wake…..
Ndani wakabaki wanafamilia na yule mtotro mgeni aliyefikishwa nchini Tanzania kwa njia za kimafia baada ya Christina kuamua iwe hivyo ilimradi tu kumuonyesha mume wake kuwa hakuna siri ya kudumu katika dunia hii.
Lucas alilia sanma huku akijutia kila alichokifanya lakini aliomba tu adhabu kubwa ya kupewa ni kusamehewa na hakuna kingine. Maana alikuwa amejiadhibu tayari kwa yote aliyopitia.
“Mpigie simu mke mwenzangu mwambie asihangaike mtoto yupo Tanzania kwa mama yake mkubwa…” Christina alizungumza huku machozi yakimlenga lenga.
Kauli ile ilimuumiza sana Lucas….
“Lucas, ni nini hiki umenifanyia na utu uzima huu lakini eeh! Ni nini?” alihoji Christina huku akishindwa kabisa kujizuia kuangua kilio.
Lucas alitamani sana kumbembeleza lakini akili yake ilikuwa imeganda hajui la kufanya.

____

MAMBO HADHARANI.

Simu kutoka Tanzania ilimueleza Caro kuwa hana haja ya kuendelea kubaki London ni heri arejee Tanzania kukabiliana na ukweli.
Simu hiyo alipigiwa na mama yake mzazi ambaye alimueleza kuwa hata mtoto anayehangaika kumtafuta huko London basi yupo Tanzania.
Caro akaona kweli hakuna haja ya kuendelea kubaki nchi za ugenini wakati mtoto wake yupo Tanzania.
Alifanya safari ya haraka sana lakini hakusafiri peke yake aliambatana na mtu mwingine kutoka nchini uingereza.
Alipokelewa uwanja wa ndege na mama yake ambaye bado alikuwa yu jijini Dar es salaam pamoja na mume wake.
Lucas hakutaka kuzungumza na mtoto wake kwa sababu alijua jazba aliyokuwanayo na alihofia huenda anaweza kufanya jambo baya, kitendo cha Caro kufanya mahusiano ya kimapenzi na Lucas rafiki yake kilikuwa kimemtonesha moyo wake vibaya mno.
Caro alizungumza na mama yake kwa kirefu sana akimuelezamazingira yote jinsi yalivyokuwa.
Maelezo ya caro yalikuwa na kitu kipya alichokuwa amekificha kwa siku nyingi sana huku akimini kuwa itafika siku ya kukiweka wazi.
Mama Caro akaenda kumueleza mumewe juu ya hilo jambo.
Jambo hilo likawafanya kwa mara nyingine tena wafunge safari kwenda nyumbani kwa Lucas.

____

Wakati wawili hawa wakikusudia kwenda nyumbani kwa Lucas. Upande mwingine wa shilingi Pocha alikuwa amekinai kuishi maisha ya mashaka, tangu atolewe gerezani na mzee Bosco alijiona hana amani kabisa kwa sababu mtu aliyemsababisha aende gerezani bado hakujua ni nini hatma yake, alizungumza na Chopa kwa kirefu akaelezea kusudio lake la kwenda nyumbani kwa muheshimiwa ambaye alihusika katika kumpeleka gerezani ili aonane naye wazungumze kama ni msamaha na amuombe ilimradi tu aanze maisha mapya akiwa na amani tele.
Ili kulifanya jambo lile liende vyema alimsihi Sofia waambatane naye ili lolote litakalokwenda kinyume aweze kuwasaidia.
Sofia akakubaliana nao na wakaipanga siku ya kwenda nyumbani kwa huyo mbunge ambapo Pocha alikuwa akipatambua vyema.
Siku ikafika ya kuchambua pumba na mchele ili kila mtu aweze kubaki huru.
Walitumia usafiri wa daladala hadi wakafika mahali walipotakiwa kupanda bajaji.
Wakaenda hadi nyumbani kwa yule muheshimiwa, walipofika getini wakajieleza kwa kina kuwa wanahitaji kuonana na muheshimiwa, mlinzi akadai kuwa ana wageni wengine wa muhimu sana na hawezi kuonana na mtu yeyote.
“Chopa na Pocha hakuna harufu mnaisikia…. kuna harufu naisikia halafu naifananisha…” Sofia aliwauliza wenzake, wakatikisa vichwa kukataa.
Lakini harufu ile ilikuwa imembadilisha Sofia kabisa, ni kama kwa dakika kadhaa alikuwa ameondoka katika eneo lile kifikra na kwenda mbali sana. Alikuja kushtuliwa na Chopa aliyemwambia kuwa mlinzi amewataka waketi mahali kusubiri ruhusa zaidi.
Wakaenda jirani na nyumba ile na kuketi katika viti!!
Pocha alikuwa akiwaza juu ya usalama wake na Sofia akiwaza juu ya harufu aliyoinusa… ni Chopa pekee aliyekuwa hana mawazo sana.
Zaidi alikuwa akimuwaza Nkozi!! Hakumuwaza kwa mabaya wala hofu.
Baada ya kimya cha muda mrefu mara vilisikika vishindo ndani ya nyumba, na mara kelele za wanawake wakilia kuomba msaada zilisikika…..
Sofia alitamani kuingia ndani lakini hakuwa na ruhusa ile.
Akiwa bado vilevile mara zile kelele zilizidi kuja nje… ni kama kulikuwa na ugomvi mkubwa.
Hatimaye ule ugomvi ukahamia nje ukisindikizwa na sauti za akina mama.
Wale watu waliokuwa wanapigana walipofika tu nje watu wawili Pocha na Sofia walimtambua mmoja mmoja.
Pocha alimtambua mheshimiwa mbunge Lucas Kazioba huku Sofia akimtambua William Mackzube.
Wakabaki kutazamana Sofia asiamini alichokuwa anakiona mbele yake, William mackzube amefata nini nchini Tanzania tena bila kumwambia wakati wanawasiliana mara kwa mara.
“Carooo!!” mara Chopa naye akasimama wima alikuwa amempata wa kumtambua…. baada ya kwenda gerezani na hatimaye kutoka anakutana na Caro katika mazingira asiyoyatarajia.
Ule ugomvi ukaishia pale, William Mackzube akamuuliza Sofia imekuwaje yupo pale, Sofia naye akamuuliza amekuja lini Tanzania.
Mara caro naye akadakia.
“Wililiam huyu ni nani?”
William akashikwa na kigugumizi.
Wakiwa bado katika kushangaana mara akatoka yule mtoto wa Caro.
Upesi Sofia akaichukua simu yake akaitazama ile picha ya mtoto akamtazama na yule mtoto mbele yake.
“Nilikwambia William huyu ni mtoto wako ukapinga vikali… haya yapo wapi? Sofia alizungumza huku akimtuhumu William.
Sasa siri zote zilikuwa nje, ukweli ulikuwa mchungu sana kuumeza lakini ilibidi tu kuupokea, William alikuwa ndiye baba halali wa mtoto Bryan, wakati Caro anajihusisha na Lucas alifanya vile ili kupata pesa ya kumwongoza katika maisha yake pamoja na kumsaidia mpenzi wake William Mackizube aliyekuwa na hali mbaya kiuchumi, kwa pamoja walikubaliana kumbambika ile mimba Lucas ilhali haikuwa kweli.
Lucas alikuwa na tatizo la kizazi!!
Uhakika huu ukamfanya muheshimiwa Lucas apoteze fahamu palepale.
“Kumbe William ulinifanya mimi MPANGO WA KANDO!!” Caro hatimaye alizungumza baada ya kugundua kuwa kumbe William Mackzube ni mchumba wa Sofia ambaye alikuwa pale pamoja na akina Chopa.

“Caro yaani miaka michache hivyo ukashindwa kunivumilia….. nimemuumiza msichana wa watu Nkozi aliyenipenda kwa sababu yako, tazama sina hata cha kumpooza hawezi tena kuzaa… Caro nd’o upo hivyo kweli….. kumbe yawezekana hata kipindi nipo nawe ulinifanya MPANGO WA KANDO bila mimi kujua…” sasa ilikuwa zamu ya Chopa kulalamika akimtazama Caro machoni.
Caro alikumbwa na aibu…..
“Na muheshimiwa akiamka kutoka katika kuzimia mkumbusheni kuwa mimi naitwa Pocha ni yule kijana ambaye alinipeleka gerezani kisa tu MPANGO WA KANDO wake aliyekuja kutengeneza simu nikazifumania picha zao. Nilidhani kuwa wakati ule nilifanya makosa kumbe kufuga mpango wa kando ni tabia yake” Pocha naye alizungumza lake

Mzee Edwin alimshika mkono wake mkono akamchukua na Bryan kisha akazungumza.
“Naondoka na mtoto wangu pamoja na mjukuu wangu, hakuna hata mtu mmoja aliyekuja kumtolea mahari, ambaye ana maanisha kumuona mwanangu apatafute nyumbani aje tuzungumze…..” alimaliza kuzungumza akaondokana mkewe.
Huku nyuma wakabaki Sofia, Pocha, Chopa, Wiliam, Christina na muheshimiwa Lucas akiwa amepoteza fahamu.
Sofia akawaomba Pocha na Chopa waondoke, hakutaka kumsikia kabisa William Mackzube msaliti.

____

KIHITIMISHO

Ilianza kama utani, Pocha akajinadi kuwa yeye hana mpango wa kando wowote ule, Sofia akachukulia utani. Lakini sura ya Pocha ikamaanisha alichokuwa akikisema hatimaye Sofia akautua ujasiri wake kando akaangukia katika mikono hatari katika kufungua namba za siri zozote zile duniani.
Sofia akaangukia kwa pocha.

Chopa hakuwa na cha kumlipa Nkozi zaidi ya kulifufua penzi lao. Hawakuwa na uwezo wa kupata mtoto lakini waliamua kuianza ile safari tena…..

Caro hakutaka kuolewa na hakutaka kumsikia William, wazazi wake wakasikiliza alichotaka mtoto wao. William alipomtafuta walimpuuzia, akalazimika kurejea uingereza katika shughuli zake.

Fahamu zilimrejea Lucas na kujikuta yupo hospitali alipopata tiba vyema na kurejea nyumbani. Alikutana na mlinzi tu getini.
Mlinzi akampatia ujumbe aliouacha mkewe.
“Siwezi kuwa na mwanaume niliyemvumilia kwa miaka mingi huku nikijua kuwa ni yeye mwenye matatizo halafu ananisaliti akijiona yeye ni bora zaidi, nimeondoka naenda kutafuta mtoto na watu wanaojua kuzaa sio wewe hayawani”
Ulikuwa ujumbe kutoka kwa mkewe, ujumbe ambao haukuwa umedhibitiwa ili usisomwe na mtu mwingine hivyo kwa namna yoyote ile yule mlinzi lazima tu aliusoma.
Jambo hili lilimfadhaisha sana Lucas akatamani kama siku zingerwejea nyuma ili asifanye upuuzi alioufanya kujihusisha kimapenzi na Caro ambaye alimbambikia mimba isiyokuwa yake akaihudumia kwa mapenzi mazito, akamsomesha mtoto wa mwanaume mwenzake akajiona yeye ndiyo baba kumbe hakuna kitu.
Ule usemi wa mwisho wa ubaya ni aibu ukamwangukia mbele yake hakuweza kuukwepa ule mwisho aliouona.
Aliwaza na kuwazua huku akipiga hatua kuelekea ndani. Hakuna lililokuwa sahihi kufanya kwa wakati ule.
Akaingia moja kwa moja hadi chumbani kitandani akameza dawa za kutuliza maumivu ya kichwa.
Akasinzia hadi aliposhtuka siku iliyofuata na kukuta simu yake ikiita.
Alikuwa ni Prisca katibu muhtasi wake, akaitazama kwa muda kabla ya kuipokea.
“Haujambo Prisca!”
“Sijambo bosi shkamoo, ulikuwa umelala?”
“Nimelala hadi sasa Prisca si unanisikia au?” alijibu kwa jazba kidogo.
“Kwa hiyo hata magazeti hujayasoma?” Prisca aliuliza.
“Magazeti? Kuna nini kwenye magazeti…..” alihoji, sasa alikuwa anazungumza vizuri na hofu yake ikasikika waziwazi.
“Hebu ngoja nikusomee hili nililonunua…. “ akasikika Prisca akizifungua kurasa.
“Kumbe tatizo ni mtoto chanzo cha mheshimiwa Lucas kuukacha ubunge… mkewe atibua kila kitu aamua kuachana naye akazae pengine…. aelezea machafu yote ya muheshimiwa….”
Lucas hakutaka kusikiliza zaidi akaikata simu, alipokata simu kwa prisca ilikuwa furaha. Kama kawaida yake umbea haudumu katika kifua chake, alikuwa ameutua tayari.

Baada ya kukata simu ya Prisca, Lucas hakuwa na haja tena ya kupokea simu ya mtu mwingine.
Alimfikiria Edwin walipotoka na urafiki wao… akajiona aliyelaaniwa kwa kitendo alichofanya cha kutembea na mtoto wake.
Nafsi ikamsuta akaona hana njia nyingine ya kujisafisha bali njia moja tu.. kukimbia!!
Kweli alitii wazo hili na akafanya maamuzi….

Baada ya siku tatu, mwili wake ulikutwa chumbani kwake ukiwa unaoza na kutoa harufu.
Alikuwa amekufa baada ya kunywa sumu!!!
Hizi ndizo zilikuwa mbio zake alizoziita sahihi baada ya kukumbwa na mambo mabaya mfululizo.
Edwin rafiki yake kipenzi alisimamia taratibu zote za msiba, akamzika rafiki yake huku akiwa amemsamehe kabisa.
Caro hakuhudhuria mazishi yale na Christina vilevile…….
Kifo cha Lucas kikahitimisha ule msemo usemao kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha.
Nami mwandishi wako George Iron Mosenya nimeifikia ncha…..

Ikiwa kuna sehemu yoyote ambayo nimeenda kinyume usisite kunishauri

TAMATI!!!!

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment