MPANGO WA KANDO SEHEMU YA TATU
NEW AUDIO

Ep 03: Mpango wa Kando

SIMULIZI YA MPANGO WA KANDO FULL EPISODE
MPANGO WA KANDO SEHEMU YA TATU

IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi : Mpango Wa Kando
Sehemu Ya Tatu (3)

SEHEMU YA 7

MAHALI FULANI JIJINI NAIROBI.

Simu ya dada mmoja iling’ara kumaanisha kuwa ilikuwa inaita aliitazama namba ile na kuitambua kuwa ilikuwa ni mpya katika simu yake.
Aliipuuzia kwa mara ya kwanza, ikapigwa tena kwa mara ya pili na ya tatu bado hakuipokea alikuwa ametingwa na shughuli nyingi sana za kimasomo akiwa chuoni.
Simu ile safari hii ilipokea ujumbe, akabofya ukafunguka.
“POKEA SIMU NI MUHIMU. TZ 11”
Ujumbe ule ulimshtua sana na aliufahamu umuhimu wa huyo bwana mwenye kitambulisho TZ 11 (TZ eleven) katika simu yake.
Upesi akaacha kila alichokuwa anakifanya, akatoka njea na kuingia msalani. Alipoufunga mlango tu, simu ile ikaita akaipokea upesi.
“Yupo huru ameingia benki maeneo ya Ukonga, Dar Es salaam jioni hii ya leo. Nakusikiliza wewe sasa!” sauti ile ya kike ilimuuliza kwa utulivu sana. Binti yule aliduwaa sana na badala ya kujibu akatupa swali.
“Imekuwaje mapema hivi si ilitakiwa kuwa next year ama?”
“Kuna haja gani ya kujadili juu ya goli ulilofungwa…. tafadhali jadili unasawazisha vipi ama hutaki kusawazisha jiandae kutoa sababu za kujitetea kwa nini umefungwa…” sauti ya mwanamke kutoka upande wa pili ilijibu kwa ukali kidogo.
“Hakikisha unamfuatilia kwa ukaribu….utanipa taarifa zake kwa juma moja.”
“Akaunti yangu ni ileile sijaibadilisha, tanguliza nusu ya malipo ya kazi hii.” Akamaliza upande wa pili na kukata simu, akimuacha yule binti aliyekuwa pale msalani kwa lengo la kuongea na simu pekee akijikuta ameshikwa kweli na tumbo la kuhara!!!

MTAFUTANO!

Giza lilikuwa limetanda tayari, Possian Clement alikuwa chumbani kwake akiwa mbele ya kioo akijitazama. Alilitazama tumbo lake jinsi lilivyokuwa limenona kwa sababu ya kitambi.
Alitikisa kichwa huku akitokwa na tabasamu la karaha, alisikitika kwa sababu kile kitambi kilikuwa kimekuja bila idhini yake na alikuwa amechelewa kupambana nacho na hakuweza tena kupambana nacho kutokana na mazingira aliyokuwa akiishi.
Alitambua wazi kuwa hata afanye mazoezi kutwa mara tatu bado lile tumbo linalomning’inia haliwezi kuondoka kwa sababu alikuwa akiishi katika mazingira ya kuridhika sana mjini Dodoma.
Mbaya zaidi alikuwa akiishi kama mwanamke anayemtegemea mwanaume kwa kila kitu maishani mwake, watu hawa hujulikana zaidi kwa jina la ‘golikipa’.
Possian hakuyazoea haya maisha kabisa lakini hakuwa na budi kutii bila shurti hadi pale muda utakapofika wa kusimama yeye kama yeye tena.
Si kwamba alikuwa yu mtoto mdogo la! Alikuwa ni mtu mzima apataye miaka thelathini na mbili.
Lakini wakati wake wa kusimama yeye kama yeye ulikuwa haujafika bado.
Alipomaliza kujitazama kwenye kioo, alitoa shati lake kisha akajinyoosha kitandani huku akikwepesha macho yake ili asilione tumbo lake.
Ni kweli kutolitazama haimaanishi lingeondoka katika mwili wake lakini ingesaidia kuliondoa katika fikra zake.
Akiwa amejilaza pale kitandani usingizi ukampitia bila kutarajia, lakini usingizi ule haukudumu kwa muda mrefu kabla hajakurupuka na kujikuta amesimama wima jasho likimtoka huku akizungumza peke yake. Maneno yake yakiambatana na kile kilichokuwa katika fikra zake.
Kilikuwa kitu cha kutisha kwa kiasi kikubwa japokuwa hakuwa na ushahidi nacho lakini ni mambo mengi ameyafanya pasi na kuwa na ushahidi na yalikuwa yanaleta uhakika baadaye.
Hakuweza kulala, akauitazama saa yake ilikuwa ni saa mbili na nusu usiku, akavaa shati lake na kutoka pale chumbani.
Akaenda sebuleni ambapo alimkuta Sofia, binti mkubwa katika familia ile ambaye mara kwa mara huwa haonekani nyumbani, lakini hizo mara chache ambazo huonekana basi huwa karibu naye walau kimazungumzo ya hapa na pale.
Possian alifika na kuketi akitazamana ana kwa ana na binti yule mrembo wa haja aliyejengeka mwili wake vizuri katika mvuto wa kike.
Sofia alikuwa amejikita katika kutazama filamu iliyokuwa inaendelea.
“Possian vipi mbona jasho!”
“Nina matatizo makubwa Sofia na ni wewe unayeweza kunisaidia, ni wewe pekee Sofia na si wakati mwingine bali ni wakati huu…”
Sofia akaachana na filamu akaweka umakini kumsikiliza Possian.
Kuona vile Possian akaendelea kuzungumza.
“Sofia kuna rafiki yangu kipenzi yupo katika matatizo makubwa sana!!”
“Rafiki? Wewe unaye rafiki gani tena wakati hauwasiliani na mtu yeyote nje ya nyumba hii!!”
“Dada Sofia nakuomba sana unielewe kadri uwezavyo kwa sababu manenio nitakayokueleza hayana uzito sana kiushahidi na yanaweza kuwa kama vituko tu. Nakusihi sana usiyachukulie kama kituko.” Alisihi Possian na kisha akaanza kujieleza kinagauubaga akijitahidi kutilia mkazo anayoyasema.
Alitumia dakika saba kujieleza kwanza juu ya yeye ni nani.
“Mh! Umesema jina lako maarufu ni nani na kwanini sasa unaitwa Possian hapa….”
“Sio kwamba Possian sio jina langu, nilizaliwa nikiitwa Possian Clement Haule…. lakini nikiwa darasa la saba mwalimu wa kiingereza kubna simulizi alitusimulia na ndani ya simulizi hiyo kuna jina alilitaja la kiingereza nasi tukatokea kulipenda mno. Niliporudi nyumbani jina lile likagoma kunitoka kabisa, nikajikuta nalitazama jina langu bila kujua kwa nini nalitazama sana na hapo nikaliona lile jina alilotutajia mwalimu. Kesho yake nikaenda ubaoni wakati mwalimu hajaingia nikachukua chaki nikaandika Possian Clement haule… kisha nikanyofoa herufi katika kila jina.. na hapo nikaandika ubaoni POCHA!!
Tangu wakati huo jina langu la kuzaliwa likasahaulika hadi ukubwani kila anayenifahamu ananifahamu kwa jina la Pocha!!” alijibu kwa utulivu wa hali ya juu. Sophia akajikuta akitokwa na tabasamu lililovutia.
“Nimelipenda sana jina lako jipya Mr. Pocha!! Haya umesema kuwa una uwezo wa kutoa loki kila aina ya simu….. nihakikishie na hilo kisha nitakusikiliza sasa juu ya hilo lililokuleta… hii hapa simu yangu, nakupa dakika kumi na tano unitolee loki…. ukimaliza tutaongea….”
“Fanya dakika tatu Sofia ili tuzungumze juu ya hii shida yangu! Tafadhali” Pocha aliomba.
Jibu la Pocha lilimshtua Sofia, yaani mtu kapewa mtihani badala aombe kupewa muda mrefu anaomba muda upunguzwe….. mtu wa aina gani hii.
“Haya sawa” akamkubalia huku akipandisha mabega juu kana kwamba anaupuuzia uwezo wa Pocha.
Pocha akaichukua simu ya Sofia, akaitazama kwa sekunde kadhaa kisdha akauweka sawa mkono wake……
Hazikuwa dakika tano ile awamu ya kwanza tu simu ya Sofia ikaachia!
Yule dada aliruka mbali kana kwamba Pocha alikuwa amemtekenya pasi na hiari yake.
“Possian we Possian..nani amekupa password zangu..eeh! nani?” alihoji Sofia lakini kwa Pocha hata hakuwa ameshtushwa na jambo hili.
“Sofia naomba basi tuzungumzia hili jambo langu kama una uwezo wa kunisaidia tafadhali nifae….” alimsihi. Sophia akiwa katika mshangao bado aliketi asiamini kile kilichotokea, aliichukua simu yake kutoka mikononi mwa Pocha.
“Bado Pocha bado…. ujue nina simu mbili…..haya hii hapa nyingine… ifungue. Hii hautaweza hata kwa dawa najua….. nikupe muda gani?” alimuuliza, badala ya kujibu Pocha ambaye damu ilikuwa ikimchemka vyema alikwapua ile simu, akaishika akatulia kwa sekunde kadhaa akapiga mchapuo wa kwanza akakosea, Sofia akaanza kumcheka.
Akaenda ya pili hola… Sofia akaonekana kufedheheshwa akiwaza ni wapi aliitoa namba yake ya siri ya simu yake kubwa.
Wakati anawaza haya akiwa ameacha kumtazama Pocha kwa kuamini kuwa hataweza kuipatia namba ya simu ile nyingine alishangaa Pocha akimuuliza.
“Huyu mtoto hapa juu ni wako.. maana mnafanana kweli”
Sophia alipogeuka alikuwa simu imefunguliwa tayari.
Mdomo ukamfunguka!!
Sasa alikiri kuwa mbele yake palikuwa kiumbe moja wa ajabu sana… huenda ni wa ajabu kupita yeye mwenyewe anavyojidhania!!
Sasa alimsikiliza shida yake vizuri.
“Umesema Chopa… Chopa ni nani?” Sofia akamuuliza Pocha.
Pocha akajieleza kuiwa amekumbwa na hisia kuwa Pocha yupo huru lakini yupo matatani tena, tena matatizo makubwa sana ambayo yanamnyemelea ili kumuharibia tena maisha yake.
Pocha akamsimulia Sofia juu ya utata wa kesiya Chopa hadi kuishia kutupwa gerezani bila kuijua kesi yake huku akinyimwa hata uhuru wa kutembelewa na ndugu na marafiki.
Maelezo ya Pocha yakamuingia vyema Sofia.
Akamwambia Pocha kuwa alfajiri wataondoka kuelekea huko Ukonga anapodai kuwa hisia zimemtuma kuwa Chopa anapatikana.
Sofia alikuwa ameamua kuucheza mchezo huu akiwa na matumaini ya kujifunza kitu zaidi katika masomo yake.
Masomo ambayo yalikuwa yanamfanya asionekane nyumbani mara kwa mara.
Wakati Sophia na Pocha wakiagana na kwenda vyumbani kulala.
Kiumbe mwingine alikuwa kitandani akiukosa usingizi kwa sababu ya mambo yaisyomuhusu anayojilazimisha yamuhusu!!
_____

YALIKUWA ni majira ya saa nne usiku, kwake hakuona kama usiku ulikuwa umeenda sana. Alikuwa amejikita katika simu yake.. mara kuwapigia marafiki zake mara kuwapigia ndugu zake.
Alikuwa akizungumza nao kwa muda mrefu huku akiwakatia walipojaribu kumpigia simu.
Na ilifikia hatua hata asipoulizwa shida anajifanya kuulizia shida ilimradi tu aweze kujiweka katika nafasi ya kutoa msaada.
Huyu hakuwa mwingine bali ni Priska yule katibu muhtasi wa mheshimiwa Lucas. Alikuwa akiwashwa na zile pesa alizopewa kama bakhshishi na bosi wake baada ya kumfokea pasi na sababu ya msingi.
Alimaliza kuwapigia watu simu aliokuwa anawakumbuka kichwani, na hapo alikuwa amejilaza tu7 akiwasubiri rafiki zake waje kumpitia waende mahali kuzitumia pesa zile, wakati anaendelea kutafuta majina mengine ya kuwapigia simu akakutana na jkina alilolihifadhi na kisha kulisahau.
Hili jina alilihifadhi “KWANINI”
Akatabasamu baada ya kulitazama jina lile akabofya kitufe cha kijani. Simu ikaita hadi ikakatika, akapiga tena safari hii ikapokelewa na mwanamke.
Alipogundua ni mwanamke akakata!!
Akang’ata kidole chake na kufikiria kuwa kama kweli anataka kuujua umbe basi ni heri atumie nambari ya tofauti ili aweze kuupata ama kuusambaza bila kujulikana.
Akajipekua na kutoa kadi yake nyingine ya simu!
Akaiweka katika simu ile na kumpigia yule mwanamama.
Simu ikapokelewa, mama yule aliongea akionekana dhahiri kuzidiwa na usingizi.
“Mama unalala sana nd’o maana wenzio kila kukicha wanaruka London, wanakula raha za ukweli huko akija kwako ni kulala tu… unapiga simu hazipokelewi shosti upo hapo! Na mwaka huu utapiga simu sana hadi madole yaote sugu hayo mwenzako humwambii lolote kuhusu London.
Nimeufikisha kama ulivyo ubuyu wangu utajua mwenyewe uumeze ama uuteme!! Na ujue hata ukiutema huu ubuyu wa Zenji una kapilipili kwa mbali bado utakuwasha tu bibie……endelea kulala!! Tena bibiwee usije ukaniletea uchuro eti nimekosea namba.. hahahahah! Ukidhani ninmekosea namba basi na mimi nitakuuliza mheshimiwa Lucas unamjua humjui.. kama unamjua bibiwee labda ukaroge maana siku hizi ni mara kumi kwa mwezi anaenda kula vitamu London…. hahahahah unaloooo” akamaliza kuzungumza akakata simu na kuizima.
Kisha akajigalagaza kitandani akicheka kwa sauti ya juu sana. Ilikuwa usiku lakini hakujali alikuwa akiishi na wadogo zake wawili wangeanzaje kumwambia eti dada unapiga kelele tumelala.
Nafsi ya Prisca ikapata ahueni baada ya kuzungumza na yule mama huku akimrushia vijembe bila kumpa nafasi ya kujibu chochote.
Amakweli umbea ni kama tabia, utajisahaulisha halafu baadaye inarejea tena!
Prisca alikuwa merejea tabia yake.
Ni heri angeufanya usiku huu uwe wa mwisho kuusambaza umbe huo asiojua madhara yake bila kujua anaowapigia simu ni akina nani!!!
Wakati yeye anaikata simu…..
Mke wa Edwin rafiki kipenzi wa Mheshimiwa Lucas alikuwa anamuamsha mume wake kwa fujo.
Alipoamka akamuelezea kila kitu kama kilivyotokea.
“Wewe Lucas alikuaga kuwa anaenda London?” Mama Caro alimuuliza mumewe.
“Hapana na ni kawaida yake kuniaga akiwa anenda safari za mbali, taarifa niliyonayo ni kwamba wiki ijayo Caro anakuja nyumbani sina taarifa kuhusu safari yake.” Edwin alijibu akiwa amekaa kitako.
“Kwani mama Caro wewe unahisi nini hapo…. maana we nawe kwa presha za ajabu ajabu haujambo…”
“Sio hivyo mume wangu, maneno aliyozungumza huyo binti ni ya kawaida hata hayatishi lakini moyowangu umepiga kwa nguvu sana punde tu baada ya kumtaja muheshimiwa Lucas. Nikikumbuka juzi hakupokea simu yetu na wala hakujihangaisha kutupigia…”
“Hebu ngoja..naomba hiyo simu…” Edwin alichukua simu kwa mkewe, akapiga namba za Lucas zikawa hazipatikani.
Akapiga namba za mkewe simu ikaita kwa muda mrefu kabla ya kupokelewa.
“Samahani shem, nimekuharibia usingizi wako.” Alianza kuzungumza kwa utulivu na anayelazimisha furaha.
“Najaribu kumpigia Luca lakini simu yake haipatikani, kama upon aye hapo naomba niseme naye jambo ni la muhimu sana…” akazungumza na kisha kuusikiliza upande wa pili ukatoa majibu.
“Aah sawa basis hem ulale salama na samahani kwa usumbufu” akaaga na kukata simu.
“Nini amekujibu eeh! Luca yupo London? Eeh!” mama Caro akauliza huku akijawa na hamu ya kujua yalojiri.
“Yah! Ameenda London ghafla….” alijibu kinyonge Edwin!!
Mama caro akabaki kimya, Edwin naye hakuwa na la kusema.

_______

KITENDO cha kupigiwa simu usiku ule na bwana Edwin kiliukatisha usingizi wa Christina mke wa Lucas, hakuna baya lolote alilowaza lakini badala yake alikarahika alipogundua mtu msomi kabisa kama bwana Edini anaweza kushindwa kutambua kuwa ule ni usiku na mtu amelala tena sio mtu tu bali ni mke wa mtu, licha ya hayo bado anapiga simu!!
Usingizi ulipogoma kabisa Christina aliwasha kompyuta yake akaingia katika mtandao maarufu wa ‘skype’ ili aweze kuzungumza na mumewe huku akimuona kupitia kamera ya kompyuta. Mara nyingi alipokuwa nje ya nchi walikuwa wakitumia njia hii.
Lakini hii ilikuwa mara ya kwanza kufanya hivi usiku!!
Aliingia mtandaoni na kupiga simu ile ya bure kabisa, bahati nzuri alikuta mawasiliano ya mumewe pia yapo hewani.
Simu ile ilipokelewa akamuona mumewe lakini hata kabla hawajaongea vizuri ikakatwa.
Christina akahisi kuwa ni tatizo la mtandao, akazima kompyuta yake na kujaribu kuutafuta usingizi tena.
Ile anajigeuza geuza kuusaka usingizi mara akahisi kama kuna kitu amekiona na hakipo sawa kabisa, alikaa kitako pale kitandani huku mapigo yake ya moyo yakienda mbio kabisa.
Akatulia kwa muda na hapo akahisi kuna kitu kisichokuwa sawa amekiona kwa mumewe kabla simu yake aliyopiga kwa kutumia ‘skype’ haijakatwa na kisha mumewe kupotea katika mtandao.
Christina alijaribu kupuuzia hisia zake lakini zilizidi kumsumbua kuwa kuna kitu cha ziada alikiona pale kitandani, mumewe hakuwa peke yake.
Donda la wivu likainyakua nafsi yake ya uvumilivu, vyeo kadhaa alivyokuwanavyo bungeni havikuwa na maana tena. Sasa akawa kama mtoto mdogo, akachukua simu yake ya mkononi na kubofya namba ambazo mumewe anazitumia kila anavyokuwa London.
Simu iliita bila kupokelewa, alipopiga mara ya pili simu ikakatwa tu, na mara ya tatu haikupatikana kabisa.
Christina hakuweza kulala kabisa, alilia kama mtoto mdogo, japokuwa hakuwa na uhakika kama ni kweli alichokiona ni sahihi kuwa mumewe hakuwa peke yake pale kitandani lakini suala la pili la simu kukatwa na kisha kuzimwa lilimsogeza hatua moja zaidi katika hofu ya kutapeliwa penzi lake.
Christina alijikuta akikesha bila kutarajia huku kichwa kikimuuma sana.
Yaache mapenzi yaiendeshe dunia, kama wewe hayajawahi kukuendesha basi wewe ni mfu hauishi katika dunia hii anayoishi Christina na mumewe Lucas!
Wakati Christina akiwa katika mkesha wa kuyalilia mapenzi kuna viumbe wengine wao walijikuta katika mojawapo ya mikesha mibaya kupita yote mkesha ambao hawatakuja kuupitia tena katika maisha yao!!

______

MAJIRA ya saa mbili nne usiku vijana wawili nadhifu walikuwa katika ukumbi mmoja wa starehe, walikuwa wakipata vinywaji baridi kwa chati huku wakibadilishana mawazo ya hapa na pale.
Macho yao yalikuwa yakitazama upande ambao walitakiwa kutazama wakati wote, hawakuwa pale ukumbini kwa sababu ya starehe za kawaida bali walikuwa wakitii amri kutoka kitengo cha juu yao.
Waliamua kunywa vinywaji baridi ikiwa ni geresha tu ilimradi uwepo wao pale usimtishe wala kumtia mashaka mtu yeyote yule.
Watu wote pale ndani hawakuwajali kabisa vijana walew wawili kwa kuwachukulia kuwa ni wateja kama wateja wengine waliofurika katika ukumbi huo ambao baadaye majira ya saa sita palitarajiwa kuwa na onyesho la msanii fulani wa muziki ambaye jina lake limefifia na anafanya maonyesho hovyo tena katika mazingira yoyote yale ilimradi tu kuganga njaa.
Kasoro mwadada mmoja tu ambaye yeye alikuwa anakunywa pombe kali, huyu nd’o aliwatazama kwa jicho la tofauti alihisi wale wapo pale kwa sababu zao nyingine tu na sio kupata burudani ambayo wengi waliifuata pale.
Aliamua kufikiria hivyo kuanzia awali alipofunga safari kuelekea hapo ukumbini bila kutarajia. Na sasa aliona ulikuwa muda muafaka wa kuwahoji hao vijana wawili ni kwanini wapo hapo ukumbini kinyume na mioyo yao ilivyokusudia.
Mwanadada yule aliyevalia sketi fupi maarufu kwa jina la kimini’ ikiwa na mpasuo uliolionyesha paja lake nono alipiga funda za pombe ile mfululizo hadi akaimaliza katika ile chupa.
Alifanya hivyo katika mtindo wa tarumbeta!!
Naam! Alipohakikisha kuwa anaweza kusimama wima vizuri bila kuziona nyotanyota alipiga hatua hadi maliwatoni.
Alitumia takribani dakika mbili huko, kabla hajarejea pale ukumbini akiwa peku mguu mmoja.
Alihangaika huku na kule kisha akakivua kile kiatu chenza na kukimbilia katika meza ya wale vijana.
Alikuwa mwenye hofu sana na alionyesha kupagawa.
“Kaka zangu nisaidieni…nisaidieni huyo mlevi kanichukulia simu yangu halafu anataka kunipiga….. nisaidieni kaka zangu uuuuuwi simu yangu mimi uuuuwi!” alilalamika huku akirusha mikono huku na kule.
“Tulia tulia dada!! Nani na yupo wapi?” mmoja kati ya wale vijana akamkaripia akimtuliza huku akiwa amesimama wima tayari.
Yule dada akacheza na akili yake, upesi akamshika mkonio na kumvuta huku akiwa bado anaugulia kwa uoga. Alitambua kuwa mikono yake ni laini sana, na alijua wapi pa kumshika mwanaume vizuri ili atambue kuwa ameshikwa na mwanamke laini.
Yule kijana mbiombio akafuata nyuma, akafika hadi kule msalani.
“Alikuwa hapa uuuwi simu yangu!” alilia yule dada huku akimpa nafasi kijana atangulie mbele kuangaza vizuri.
Ewala! Apewe nini kingine katika mipango yake zaidi ya kupewa kisogo namna hii katika namna aipendayo.
Yule dada akaipandisha ile sketi yake fupi kiasi kwamba nje ilibaki chupi tu iliyoonekana, sketi yote ikamezwa na kiuno, teke moja maridhawa likamtoka na kutua katika mgongo wa yule kijana kiasi kwamba likamsukuma na kumbamiza ukutani vibaya mno, mdomo ukachanika huku ukiacha damu kiasi katika ukuta, dada yule akiwa bado chupi nje akaifikia ile damu na kuifuta upesi kisha akamnyanyua kijana asiyekuwa na nguvu tena akamsukuma na kumwingiza katika choo cha wanawake!
Alijua kwa pigo lile yule bwana atabaki kugumia tu asiweze kusema walau neno moja.
Akakifunga kile choo vyema kwa kutumia kufuli jingine kabisa alilokuwa ameliandaa tayari.
Kisha akatoka na kutimua mbio kiuoga vilevile safari hii akiwa na damu katika blauzi yake, damu aliyoifuta pale ukutani baada ya kijana wa kwanza kupasuka mdomo vibaya mno.
Akatoka mbio hadi kwa kija naliyebakia pale, alifika na kumwonyesha ile damu.
“Kaka amempiga na chupa huyo mlevi Mungu weeee!! Anamuua… atamuua…. uuuuuwi!” alizungumza huku akirukaruka kama kuku aliyechichwa vibaya sasa amemtoroka mchinjaji kabla hajamaliza kumchinja!!
Alijua kwa tego lile mwanadamu wa kawaida hawezi kuponyoka, na vijana wale kwake walikuwa ni wanadamu wa kawaida tu.
Kijana wa pili hakutumia muda kufikiri, akajisahau kabisa kuwa alikuwa haitaji kujulikana yeye ni nani.
Hapohapo akatoa bastola yake kiunoni na kumwamuru yule dada amtangulize eneo la tukio.
Dada akatii huku akionyesha hofu kubwa machoni juu ya ile bunduki.
Lakini moyoni alikuwa katika kicheko akifurahia kuumaliza mchezo katika njia inayofurahisha.
Safari hii hakunyoosha niia kuelekea tena kule uani badala yake alienda katika chumbacha kuvutia sigara kilichokuwa jirani na kile choo.
Akaonyesha kwa kidole huku akionyesha uoga wake wa kike kuhusu kutangulia.
Yule bwana akatangulia akiwa makini na bunduki yake. Alipoufungua mlango, yule dada akatokwa na ngumi moja kali sana ikatua katika kisogo cha yule kijana, bunduki ikamtoka huku akitua mle ndani, nukta iliyofuata yule dada alikuwa ametanda pale ndani ameidaka ile bunduki alikuta wapo watu wawili wanavuta sigara. Akawaamuru wapige magoti kisha waangalie ukutani.
Wakatii huku sigara zikiwatoka midomoni.
“Nyie ni askari najua na sihitaji vitambulisho vyenu….. bnani amewatuma huku?” alihoji yule dada.
Askari yule akagoma kujibu!
Dada yule naye hakuuliza mara ya pili.
Akafanya kama anaondoka na kisha ghafla akaizungusha ile bastola upande wa kitako na kwa nguvu sana akambamiza nacho kisogoni yule askari aliyegoma kujibu akidhani atabembelezwa.
Huo ukawa mwisho wake.
Wale vijana ukutani aliwarukia teke la ajabu akiisambaza miguu yake yote miwili kisha kwa pamoja kila mmoja akaupokea mguu mmoja mgongoni hivyo akajibamiza ukutani na kupoteza fahamu!!
Akatoka akiiacha ile bunduki pale ndani.
Akaenda kule chooni, akaufungua mlango na kujihakikishia kuwa yule bwana hakuwa anakoroma tena bali alikuwa amenyamaza kimya tayari na damu ilikuwa imetapakaa sana pale ndani.
“Ndugu yako nimemuuliza ni nani amewaagiza kuja hapa kumfuatilia yule kijana hajanijibu nimemuacha ameenda zake kulala. Je na wewe hautanijibu!!” alimuuliza.
“Luteni Bosco!!” alijibu kwa shida sana.
“Asante wewe unazo akili nyingi sana, sasa ukienda mpe taarifa kuwa umekutana na TZ 11 na yeye anafuatilia dili hilohilo ambalo yeye luteni anafuatilia… kwa hiyo mwambie anisamehe bure!! Natetea ugali wangu!” alizungumza yule dada na kisha akatokwa na ngumi kali ikatua katika shingo ya askari yule huo ukawa mwisho wake.
Akakichukua kiatu chake, akauchukua mkoba wake mdogo na kisha akatoa blauzi nyingine na kubadilisha upesi.
Wakati anatoka akamuona mtu aliyekuwa akimfuatilia na yeye akiwa katika hatua za mwisho kutoka pale ukumbini.
Hakuwa mwingine bali alikuwa ni Manfredy Gregory ‘CHOPA’.
Tz 11 akatokwa na tabasamu hafifu kisha akaivaa miwani yake na kisha akenda mahali alipokuwa Chopa na kuanza kumbughudhi mara amalazimishe wakacheze mziki, mara amwambie kuwa anamtaka kimapenzi.
Aliyafanya yote haya ilimradi tu kumkera Chopa ili afanye maamuzi ambayo hajayapanga!
Kweli Chopa akakereka na kufikia hatua ya kuondoka hapo ukumbini ili aende katika ile nyumba ya kulala wageni aliyofikia!!!
Nini kingine tena utahitaji TZ 11 zaidi ya mambo kujipanga yenyewe namna hii??
Chopa alipotoka na yeye akatoka akipishana na watu waliokuwa wakisukumana kwenda kushangaa tukio lililotokea katika chumba cha kuvutia sigara.
_____

ILIKUWA yapata majira ya saa nne asubuhi wakati luteni mstaafu Bosco mkuu wa gereza la Ukonga alipopigiwa simu mbili zilizoachana kwa dakika chache sana.
Simu ya kwanza ilikuwa ni taarifa juu ya uwepo wa mtoto wake pale ofisini na alieleza kuwa ana shida kubwa sana ya kuonana na luteni.
Akiwa katika gari yake anapigiwa tena simu, safari hii ilikuwa ni simu ya upepo iliyofungwa katika gari lake.
Simu hii ikatoa taarifa juu ya vifo vya askari wawili katika ukumbi wa starehe.
Taarifa hii ilionekana kuwa ya kawaida sana kwake kabola hajatajiwa nambari za askari wale waliouwawa.
Moyo wake ulidunda mara mbili ya kawaida. Aliuliza mazingira ya vifo hivyo akaelezwa kuwa hawakupigwa risasi na bunduki zao wote zimekutwa salama kabisa bila kutumika walau risasi moja.
Taarifa hii ilimpagawisha sana, akamuamuru dereva aongeze mwendo kasi.
Baada ya dakika arobaini alikuwa kituoni tayari, alifikia moja kwa moja kwa mtu wa mapokezi ambaye ndiye alimpa taarifa kuwa kuna bwana mmoja alikuja kumuulizia Pocha pale gerezani. Na baada ya taarifa hiyo luteni akawaagiza vijana kumfuatilia mtu huyo wamtambue ni nani na ikiwezekana wajue ni kwa nini anamtafuta Pocha.
Luteni alimuuliza maswali lukuki yule mtu wa mapokezi ikiwa alimuuliza yule bwana jina lake, mtu wa mapokezi akakiri kuwa alimuuliza na alilinukuu pembeni kabisa.
Luteni akaliomba lile jina, akapewa jina Manfred Gregory!
Baada ya hapo akiwa anataka kuondoka mtu yule wa mapokezi akamkumbusha kuwa mwanaye alikuwa anamngoja!!
Akaenda moja kwa moja alipoelekezwa mwanaye yupo, ni katika mgahawa uliopo jirani na gereza maarufu kama hoteli ya Magereza.
Akaingia pale na kuangaza huku na kule, laiti kama isingekuwa ujasiri wa kijeshi basi angeweza kuanguka, hii ni baada ya kumuona Pocha akiwa katika mgahawa ule.
Akajipapasa kiunoni kutambua uwepo wa bunduki yake, lakini kabla hajaitoa akatambua kuwa yule binti aliyeketi na Pocha ni Sofia binti yake….
Alipiga hatua mpaka akaifikia meza ile na kuketi!
Sofia akamsalimia babake, Pocha naye akafanya hivyohivyo, Sofia alijua wazi kuwa baba yake yupo katika sintofahamu. Akamueleza kwa kifupi kilichowaleta Dar es salaam ghafla.
Akaelezea zile hisia za Pocha ambazo hata yeye Luteni alikuwa akizifahamu na ndo chanzo kikubwa cha kufanya maarifa hadi Pocha kuishi Dodoma huku waliomfunga wakiamini yupo gerezani.
“Mzee, usihoji sana maneno mengi najua unaniamini kuwa siwezikufanya jambo la kishenzi wala la kipuuzi… nahitaji kujua kitu kimoja tu je? Kuna uwezekano wa kujua kama kuna mtu aitwaye Chopa alifika hapa kumuulizia Pocha?” alihoji Sofia kwa utulivu.
Baba mtu alimjua vyema mwanaye na hapa hakuwa akiongea na mwanaye wa kawaida bali alikuwa akizungumza na mmoja kati ya wapelelezi chipukizi wanaoipenda kazi yao.
Hivyo hii ilimuondolera ile hofu alijua Pocha hawezi kuwa na ujanja wowote wa kumlaghai Sofia.
Mzee Bosco aliondoka hadi mapokezi kule na kumuhoji yule mtu wa mapokezi kama kuna mtu mwingine aliyekuja kumuulizia Pocha zaidi ya huyo Manfredy, mtu wa mapokezi akakataa kuwa hakuna mtu yeyote na huyo Manfred ndiye mtu wa kwanza kufanya hivyo tangu Pocha atolewe gerezani katika njia za kinyemela.
“Au umewahi kupata mgeni yeyote anayeitwa Chopa labda….” aliuliza mzee Bosco.
Mtu wa mapokezi akafikiria kwa kina kisha akasema hajawahi pia kukutana na jina hilo.
Mzee Bosco akarejea mgahawani na kuwaeleza alichojibiwa.
“Manfred Gregory ndiye kiumbe pekee ambaye alikuja kumuulizia Pocha na nikawaagiza vijana wangu kumfuatilia… mjinga ameua vijana wangu kama kuku…Sofia mwanangu hajatumia silaha amewaua kwa mikono na miguu yake yule mshenzi.. halafu aaaargh! Sijui nimefanya ujinga gani wale askari aaargh walikuwa vijana wadogo… huyu Manfredy ni nani Pocha?” Luteni msaatafu Bosco akamgeukia Pocha.
“Sijawahi kusikia jina kama hilo mkuu!” alijibu kwa nidhamu ya hali ya juu Pocha.
“Huyo Chopa naye umesema umehisi sijui naye ni nani?”
“Rafiki yangu wa karibu sana…. alinisaidia sana nilipokuwa gerezani, aliniepusha na mengi lakini badaye akahamishwa gereza sijui aliachiwa huru ama vipi lakini aliondolewa!!” alijibu Pocha!!
“Pocha huu si muda wa kuwatafuta marafiki zako, ujue ni kiasi gani unaweza kuhatarisha kazi yangu…..” alitaka kuendelea kuzungumza. Sofia akamkanyaga mguu.
Kisha akamnyanyua Pocha na kumweleza mzee wake kuwa atampigia simu ikiwa kuna msaada wowote watahitaji.
“Sofia!!” mzee Bosco alimuita mtoto wake wakati anataka kuondoka. Sofia akarudi upesi na kutega sikio.
“Ukifanikiwa katika pitapita zako huko kumpata huyo Manfredy sijui nani nani…namtaka akiwa hai… hai kabisa…mshenzi ameua vijana wangu wawili Sofia yaani wawili tena kwa dhihaka kubwa kabisa eti hajatumia silaha…..” Mzee Bosco alilalamika…..
Sofia akampiga begani kisha akaondoka!!
Baba yake akamsindikiza kwa macho.

___

Nairobi Kenya.
4:00 Asubuhi

Muda wote alikuwa akiitazama simu yake kusubiri kama kuna taarifa yoyote ile kutoka Tanzania, hakuna aliyejishughulisha naye kwani kila mmoja alikuwa katika harakati za kuingia katika chumba cha mtihani pale chuoni.
Wakati wenzake wakiwaza mtihani mmoja tu yeye alikuwa yu katika dimbwi la mitihani miwili.
Mtihani wa chuo ambao haukumtoa jasho sana kwa sababu hata kama angesema asiufanye bado alikuwa na namna ya kutumia pesa na kuonekana kuwa ameufanya na kufaulu na hata kama ingeshindikana na asiwe mwanafunzi kuanzia siku hiyo bado asingebabaika katika maisha yake.
Mtihani wa pili uliokuwa ukikiumiza kichwa chake ni kitendo cha kijana mmoja raia wa Tanzania aitwaye Chopa kuwa huru tena uraiani kabla ya muda uliokusudiwa.
Sasa alikuwa akihitaji kujua hatua zote ambazo Chopa alikuwa akipitia, na taaruifa ya mwisho aliyopewa usiku uliopita ni kwamba Chopa aliingia ukumbi wa starehe lakini kuna askari waliovaa kiraia walikuwa wakimfuatilia.
Hili jambo lilimuumiza sana kichwa, na simu ya pili aliyopigiwa usiku huohuo ilimueleza kuwa aliyetoa agizo la Chopa kufuatiliwa sio taasisi bali ni mtu mmoja aitwaye Luteni Bosco, kuhusu sababu ya kwanini ameagiza hivyo huu sasa ulikuwa ni mtihani wenyewe ambao jibu lilikuwa halijapatikana.
Binti huyu mwanafunzi wa chuo alijiuliza sana kuna kitu gani kinaendelea!!
Hatimaye ujumbe aliokuiwa akiusubiri uliingia.
Ujumbe kutoka kwa Tz 11.
“ANAKABIDHI CHUMBA! NIFUATANE NAYE AU NIMFUATILIE BOSCO?” Ujumbe ulihoji.
Binti akautazama kwa muda kisha akajibu.
“FANYA YOTE!”
Halafu akaizima simu yake na kuingia katika chumba cha mtihani.
“Odongo why are you late?” sauti ya kike ya mkufunzi ilimuuliza binti huyu wakati anaingia pale darasani.
“I’m sorry!” alijibu kwa kifupi kisha akachukua nafasi yake.
Wakati anaufanya mtihani na Tz eleven naye alikuwa yupo kazini.

______

SOFIA BINTI BOSCO, licha ya umachachari wake hakuna kitu kigumu kilichokuwa kikimsumbua siku zote kama mwanzo. Alikuwa akiumiza sana kichwa na kujichukia yeye mwenyewe anapokuwa katika kuusaka mwanzo wa kitu chochote kile.
Safari hii tena alikuwa katika kuutafuta mwanzo wa mkasa huu, alisikia kuwa askari wawili waliuwawa, alisikia pia kuna bwana anaitwa Manfredy alikuja kumuulizia Pocha lakini hakulisikia jina Chopa katika mlolongo wote huu.
Na Chopa ndiye alikuwa mwanga katika mkasa huu.
“Pocha una uhakika kuwa Chopa yupo huku Ukonga?” Sofia alimuuliza Pocha baada ya akili yake kukwama kabisa katika kuupata mwanzo.
“Da’ Sofi ujue mimi sio kwamba ni Mungu najua kila kitu, zile ni hisia na hadi sasa sielewi huwa zinakuja vipi… hivyo naogopa kusema nina uhakika maana utaniuliza tena yupo wapi” alijibu Pocha kwa utulivu kabisa. Lilikuwa jibu tosha kabisa kwa Sofia na ulikuwa ukweli.
Sofia alituliza kichwa kisha akamuuliza tena.
“Umewahi kumuwaza mtu tena na mwisho ikawa kweli?”
“Ndio ni Chopa tena nilimuwazia kuhusu kuhamishwa gereza ama kuuwawa ilimradi tu niliwaza kuwa kuna mmoja kati yetu atamwacha mwenzake…” alijibu Pocha tena kwa umakini mkubwa.
“Ujue Ukonga kubwa sana hii,… tunataka kumtafuta mtu ambaye hatuna namba yake… dah!” Sofia alizungumza huku akionyesha dhahiri kuanza kukata tamaa. Ile hali hata Pocha aliigundua.
Simu ya Sofia iliuvunja ukimya ulioanza kutanda! Akaipokea na kusikiliza kwa muda kisha akaikata bila kujibu chochote.
“Baba anasema aliyewaua vijana wake anadaiwa kuwa ni mwanamke….” Sofia alisema kisha akaendelea, “Ujue babangu yule anawadharau sana wanawake sijui kwa nini, yaani hapo atakuwa amechukia sana… haamini kama mwanamke anaweza kumuua mwanaume.” Alimalizia Sofia, kisha mpango ukabadilika akamweleza Pocha kuwa babake amemuagiza eneo la tukio akatazame kwa kina nini kilichojiri.
Upesi wakarukia pikipiki katika mtindo wa ‘mshkaki’ na kutokomea.
Wakati wawili hawa wakiwa katika pikipiki kuelekea ule ukumbi wa starehe.
Tz 11 yeye alikuwa katika pikipiki pia kuelekea alipopajua yeye!!

____

SOFIA alifika eneo lile na kujitambulisha kwa baadhi ya askari, walibaki kumtazama kwa macho ya mshangao. Alikuwa ni binti mrembo wa wastani ambaye alionekana kana kwamba ni myonge na hawezi kuwa na uytaalamu wowote katika mambo magumu kama yale.
Sofia aliingia moja kwa moja katika kile chumba cha kuvutia sigara ambacho kulikuwa na maiti moja, akaitazama vizuri kisha akaenda chooni. Akamgusa gusa yule bwana baadhi ya maeneo kisha akatikisa kichwa na kuwageukia maaskari.
“Huyu bwege anajua maana ya kuua….” alisema vile kisha akaomba njia akatoka na kuanza kumpigia simu baba yake ili aweze kumueleza kiundani.
Alipiga simu ikaita bila kupokelewa, akapiga mara ya pili simu haikupokelewa pia.
Akapuuzia kuendelea kupiga kwa sababu kilichotakiwa kufikishwa ni taarifa tu na katu taarifa isingeweza kubadili ule umauti kuwa uhai tena.
Sofia alipiga hatua kadhaa hadi akafika nje alipomuacha Pocha!
Alimkuta Pocha katika hali isiyokuwa ya kawaida, Pocha alikuwa kama mwenye mawenge fulani hivi yanamsumbua kichwani.
“Sofia una uhakika kila kitu kipo salama hapa…” Pocha alimuuliza.
“Yah! Kwani kunani?”
“Aaah! Sijui nina nini mimi yaani mapigo ya moyo yako mbio sana…. sijui hata ninafumbwa kitu gani mimi… ila kuna jambo.. ila kama hapa pako salama basi sawa tuendelee huenda huko mbele kuna shida” alijibu kwa unyonge Pocha.
“Haya ngoja nimpigie mzee mara ya mwisho asipopokea mi tutakutana jioni nimpe majibu ya alichoniagiza.”
Akaingiza namba na kupiga, simu ikaita pasi na kupokelewa.
“Pocha eeh! Twende zetu….” Sofia alisema huku akianza kutangulia.
Pocha akamfuata nyuma, mwili unakubali lakini akili ikiwa imekataa kabisa kuwa sawa.

_____

Damu nzito ilikuwa ikimtoka puani na midomoni, taya zilikuwa zimelegea kiasi kwamba hakuweza kuufunga mdomo wake. Hii ikasababisha avuje udenda ulioambatana na damudamu.
Alikuwa amepiga magoti, si kwa kukusudia ama kuamrishwa na mtu la! Bali asingeweza kusimama kutoka pale alipokuwa.
Kitako cha bunduki kilikuwa kimelainisha magoti yake ambayo yalikuwa yameupoteza ule ukakamavu wake wa siku za nyuma. Alikuwa amejibu maswali yote kama alivyoulizwa lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kujikuta katika pona pona.
Macho yake yalikuwa yakimuangalia mwadada aliyekuwa mbele yake katikanamna ya mshangao na nyingine ikiwa ni namna ya kuomba msamaha katika namna nyingine.
Lakini tatizo lilikuwa ni msamaha kwa kosa gani?
Mwanadada yule akiwa bado na yule mzee ofisini kwake alinyanyua simu yake na kubofya nambari kadhaa, alipojaribu kupiga akagundua kuwa simu yake haina salio la kutosha.
“We babu, simu yako ina dakika za kupiga nje ya bnchi… nahitaji kama dakika moja tu!” yule binti alimuuliza yule mzee ambaye hakuwa na uwezo wa kusema lolote. Akatikisa kichwa kukataa.
“Mzee Bosco mi nakuuliza kwa sauti we unanijibu kwa kichwa aisee wazee wa siku hizi mna dharau kweli. Haya endelea na dharau zako ipo siku zitakuponza…” alizungumza yule binti kwa masikitiko makubwa.
“Halafu siku ukitengemaa vizuri afya yako waambie wakuu wako wa kazi mchezo wa kuweka kamera ambazo hazifanyi kazi waache, yaani nimetumia muda mwingi kujivalisha haya mawigi kumbe kamera hamna….wakikuuliza nani ametoa huo ushauri waambie ni TZ 11” alimalizia binti yule kisha akampungia mkono luteni Bosco na kutoweka.
Alitoka huku akiwaaga wafanyakazi wengine pale kana kwamba hakuna lolote baya lililotokea.

____

SIMU ya Sofia iliita wakati akiwa katika pikipiki, akatokwa na tusi la kawaida alilolizoea pindi anapokereka.
“Yaani mshua anazingua nimempigia muda wote hapokei halafu sasa hivi anapiga nisipopokea analalamika, oya punguza mwendo!” akamwamuru dereva wa pikipiki. Kisha akaipokea simu.
“Mzee nipo kwenye pikipiki!” alizungumza na kisha akataka kukata simu, lakini kuna kitu cha tofauti alikisikia. Alisikia kama muungurumo wa kiumbe , akasikiliza kwa makini akasikia tena muungurumo.
Akaita jina la baba yake akitanguliza cheo chake lakini hapakuwa na jibu zaidi ya muungurumo.
Sofia akaikata ile simu na kisha akamuamuru dereva abadili uelekeo na kufuata njia ya kuelekea gereza la ukonga.
Dereva akatii!!
Walipokaribia gerezani Ukonga, Sofia akamzuia dereva, akamlipa ujira wake kisha akasubiri alipoondoka ndipo akaongozana na Pocha hatua kwa hatua hadi katika ule mgahawa waliokutana awali. Akamuacha pale, kisha akiwa makini kabisa alisimama ili aweze kutoka nje.
Wakati anatoka aligonganisha macho na binti aliyekuwa anakunywa soda , japokuwa ilikuwa kwa sekunde moja tu ya kutazamana Sofia alisisimka sana kwa sababu alitambua kuwa alikuwa anatazamana na kiumbe ambaye si wa kawaida kabisa. Lakini hakupoteza muda kumfikiria kiumbe yule badala yake aliendelea na hamsini zake….
Akatoweka na kufika kule gerezani, akazifiokia ofisi za baba yake na kumkuta katibu muhtasi akiwa amejikita katika kusikiliza muziki huku akijaribu kuimba baadhi ya beti.
Sofia akamuulizia mzee Bosco.
“Yupo lakini hadi itakapotimu saa sita na nusu ndipo ataanza kuonana na watu sasa hivi ametingwa sana.. samahani eeh!” alizungumza dada yule huku tabasamu likiwa limemtawala.
Sofia alisihi kuwa ni lazima aingie ndani, akajitambulisha kuwa yeye ni mtoto wa mzee Bosco lakini katibu muhtasi yule ambaye kwa namna moja alipitia kupiga kwata katika ngazi ya kuruta alitoka upesi na kusimama mbele ya Sofia.
“Binti nitakuwasha makofi halafu hutakuwa na cha kunifanya nitakutupa selo sasa hivi. Nimesema hiyo ni amri!” alifoka yule dada.
“Na nikiivunja hiyo amri kwa sababu za usalama wa mzee wangu je?”
“Ni sisi tunaoujua usalama wa mzee wako, wewe kama ni baba yako usalama wake unaujua hukoo nyumbani not hiya” alizungumza kwa kusisitiza huku akichombeza kiingereza mwishoni.
Sofia alipiga hatua moja mbele zaidi, yule dada akajaribu kumsukuma, lakini alijikurta akiwa amesukuma gogo zito lisilotikisika, Sofia akapenya na kuufikia mlango wa mkuu wa gereza.
Akausukuma huku bunduki yake ikitoka katika kiuno na kuhamia kiganjani.
Sofia aliruka katika namna ya kubiringita sambasoti na kutua katikati ya ofisi ile, akageuka huku na kule akimaanisha kuwa yeyote atakayejileta mbele yake ni halali yake.
Alikuwa amemuona baba yake akiwa katikati ya dimbwi la damu pale ofisini kwake lakini hilo hakulizingatia kwanza, aliulinda usalama wa eneo linalomzunguka.

_____

Wakati Sofia akiwa amejikita katika kujiweka vyema dhidi ya adui yeyote anayeweza kujitokeza.
Upande wa Pocha hakuwa amekaa peke yake, bali alikuwa yu na msichana mrembo sana asiyeishiwa tabasamu usoni kwake.
Alikuwa amejitambulisha tayari majina yake bandia. Pocha naye akajitambulisha lile jina lake la Possian.
Binti yule aliingia pale kwa gia ya kumsalimia Pocha na kumsifia kuwa mchumba wake ni mrembo sana. Dada yule aliendelea kumdadisi Pocha kwa uchache ikiwa mchumba wake yule anafanya kazi hapo Ukonga ama la.
Pocha akajitahidi kukwepa kumzungumzia Sofia!!
Baada ya mazungumzo ya kama dakika tatu, binti yule aliaga katika namna ya aina yake.
“Akirejea mwambie nimempenda sana alivyonitazama wakati anaondoka… akikuuliza jina langu usiseme Getruda mwambie TZ 11” Akakishika kiganja cha Pocha na kukiminyaminya kisha akaondoka zake akimwacha Pocha akiibiaibia kuyasindikiza maungo ya nyuma ya binti huyo.

ITAENDELEA

MPANGO WA KANDO SEHEMU YA NNE

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment