Born to Die Sehemu ya Nne
NEW AUDIO

Ep 04: Born to Die

Born to Die Sehemu ya Kwanza
Born to Die Sehemu ya Nne

Simulizi : Born To Die

Sehemu Ya Nne (4)

Mvua ilinyesha kwa kipindi kirefu na yote iliishia katika miili ya wale vijana. Baada ya masaa manne, ndipo viongozi wa mafunzo yale walipokuja na kuanza kutoa maneno yao ya kuwapa moyo na kuwafunza mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kuvumilika wakati yanaendelea pale kambini.

“Hakuna neno mateso wala mateso yenyewe pale unapokuwa unajifunza kitu kitakachokutoa katika utumwa. Juhudi na maarifa yako, ndio chanzo cha wewe kuwa hapa na ndio chanzo cha wewe kutoka hapa ukiwa umewiva na tayari kwa lolote. Kama hutoweza kuvumilia haya machache ya hapa, kamwe huwezi kuvumilia kumkingia risasi mwenzako ili asife. Hapa tunajifunza ujasiri na siyo ushujaa. Kumbuka hilo.” Aliongea Luteni Japhet. Si Peter wala Vanessa ambao walikuwa wanagonganisha meno yao kinywani kwa sababu ya baridi iliyokuwa inaendelea kuwanyambua katika miili yao bali ni wanajeshi wote walikipata cha mtema kuni.

“Kwa sasa nendeni nyumba ile pale, kuna jambo kwa ajili yenu.” Akaongeza Luteni na wanajeshi wale walinyanyuka na kuanza kwenda kwenye jengo moja ambalo lilikuwa pana na lenye nafasi kubwa kuanzia juu mpaka kwenye upana. Lilikuwa linawaka taa ambazo zilileta joto la kuifanya baridi ile itokomee kwa muda.

Huko walikuta watu wa huduma ya kwanza pamoja na matabibu wakubwa kabisa toka nchi za maghalibi.

Alipita mwanajeshi nmoja mmoja, na kisha akachunguzwa macho yake kwa tochi ndogo yenye mwanga mkali. Baada ya kuchunguzwa, matabibu wale walitaka mwanajeshi akifuate kidole chake cha shahada jinsi anavyokipeleka. Matabibu pia waliwauliza namba za vidole ambavyo wananyooshewa. Hiyo yote ni kuona kama wameathirika macho yao. Na baada ya kufanikiwa kujibu, walipita na kwenda kwa watu wanaofuata ambao hao kazi yao ilikuwa ni kutoa majaketi mazito pamoja na magwanda mapya ya kijeshi bila kusahau viatu vya jeshi.

Wanajeshi wale wapya walifurahi na kuna wengine walivua nguo zilizokuwa miilini mwao na kuvaa mapigo mapya. Wakajisikia ahueni kutokana na joto jema la mavazi mapya.

Baada ya hapo wakapewa chai na kahawa ya moto kwa ajili ya kuchoma moto misuli. Ilikuwa ni ahueni kwao na kwa furaha, walijikuta wanakaa bila kulala hadi siku iliyofuata ambapo kama mazoezi, basi yalikuwa ni kiboko.

BAADA YA MWEZI MMOJA.

Vijana wale walikuwa si wale tena ambao walikuwa wanyonge na wajinga kabla hawajaingia kambini. Sasa waliweza karibu mazoezi yote waliyopewa. Walijituma na kujiamini kiasi kwamba hakuna akiyekuwa anadharau akifanyacho mwenzake. Uzuri hakuna aliyepoteza maisha ama kukimbia kambi kutokana na kazi na mazoezi mazito waliyokuwa wanaendelea kuyapata.

Katika mwezi mzima, walishajaa misuli yao na kuwa tayari kwa mapambano ya ana kwa ana. Ndani ya wiki mbili walikuwa wanajifunza kutumia mapanga ya jadi pamoja na visu.

Waliwekewa migomba na miti migumu kwa ajili ya kuikata kata kama vile binadamu. Baada ya zoezi la kukata migomba na miti kumalizika, wao kwa wao walipewa mipambano katika sekta ile.

Vanessa na Peter bado walikuwa ni moto wa kuotea mbali katika mafunzo yale. Vanessa alikuwa kinara wa kila kundi ambalo aliwekwa na vivyo hivyo kwa Peter.

Siku hiyo ya mapanga, kila mwanajeshi alipambana na wapinzani kadhaa na baadae walitaka kujua nani mshindi katika mipambano ile waliyoiandaa.

Si kama walikuwa wanakatana kweli bali pale walipopata upenyo wa kutaka kukata, walionesha kwa ishara kuwa angekata mahala fulani au saa nyingine wanapiga kwa ubapa.

Siku hiyo wakataka kumpata mshindi wa jeshi zima lenye watu mia na hamsini (150).

Ulikuwa ni mpambano mrefu lakini mwisho wa yote, fainali alikuwepo Peter na Vanessa. Wakali wa kambi nzima, wapenzi wa kweli katika kambi ile. Lakini sasa roho zao zilikuwa zimejazwa ujasiri zaidi ya mwanzo.

“Hakuna huruma katika mapambano. Yule umuoneaye huruma, ndiye anayekuua mwisho wa siku.” Siku fulani za nyuma, Kamanda Bonito aliwaambia wanajeshi wake katika zoezi la kuwajenga ujasiri kufanya wa lolote.

“Wanaume wengi mnadharau sana wanawake. Mnawaonea huruma kijinga sana na mwisho wake huwa nyie kuuawa. Nakupa mfano mdogo tu.”

Kamanda Bonito akatulia kidogo na kuwatazama wanajeshi wake, kisha akaendelea. “Makamanda wengi majasiri, wanawake ndio huwaua kwa wanawake hao kutumwa kufanya hivyo. Fatilia vema historia ya vifo vya makamanda wengi duniani. Mi nakupa mfano wa Kamanda mmoja akiyetokea huko Yugoslavia. Mnamo miaka ya 1960 alibuni ndege ya jeshi ambayo sasa inaitwa Harrier Jet. Yenyewe hupaa bila kukimbia mwendo mrefu. Yaani yenyewe, hupaa ikiwa imesimama hapohapo. Katika karne ya juzijuzi, kuna wamarekani wawili ambao waliandika kitabu kinaitwa ‘True Lies’, James Cameron na Randall Flakes. Hawa walielezea kilekile ambacho kamanda yule wa Yugoslavia alikibuni. Kitabu kile kilichukuliwa na kisha kikapelekwa katika kiwanda cha kutengenezea filamu. Wakamchagua Arnold Schwarzenegger kuigiza filamu ile ya ‘True Lies’. Ukiangalia vizuri utaona ndege kama ile ambayo inapaa ikiwa imesimama hapohapo.

Lakini Kamanda yule aliyebuni kwa ajili ya NATO unajua alikufaje? Aliuawa na mwanamke ambaye alitokea kumpenda kupindukia. Hivyo ndivyo makamanda wengi hupoteza maisha yao. Sasa wewe kama utamuonea huruma mwanamke na kumpa mgongo, amini hufiki mbali. Sitaki wewe uwe Kamanda utakayekufa kwa sababu ya mapenzi ya kijinga.” Maneno hayo yalijirudia katika kichwa cha Peter na kujikuta akitabasamu huku kakamata vema panga lake tayari kupambana na Vanessa.

Kundi zima lilikuwa limewazunguka vijana wale ambao katika uwanja wa mapambano, hakuna hata mmoja aliyewahi kuwapiga. Na si mapambano tu, bali hata mazoezi ya kijeshi. Kifupi walikuwa tishio kubwa na la kuogopeka katika uwanja ule waliokuwepo.

Luteni Gon, kama kawaida yake alikuwa katikakati kuwatenganisha wale vijana kabla hajawaruhusu waanze mpambano ambao ungeamua ni nani mbabe wa kutumia mapanga katika kikosi kile.

“Baada ya hapa, kesho tutaanza kujifunza kutumia silaha. Leo, mimi nitamaliza kazi yangu niliyopangiwa kuifanya. Kuanzia kesho, mtakuwa na watu wa kuwafunza silaha. Jiandaeni.” Luteni Japhet Saigon aliongea na baada ya hapo aliwaruhusu Peter na Vanessa waanze mpambano mkali na kwa hamasa ya kutaka kumuonesha Luten Saigon kuwa mazoezi yalizama vyema miilini mwao.

Vanessa ndiye alianza mpambano kwa kasi ya ajabu kwa kumvamia Peter na panga lake kali ambalo alilenga kumkata shingoni. Peter akiwa katika wepesi wa hali ya juu kuliko kipindi wakati kafika katika kambi ile, alikwepa pigo la Vanessa kwa kurudisha shingo yake nyuma na kufanya upanga ule mkali kupita bila kugusa sehemu yake yoyote ya mwili.

Vanessa hakuishia hapo. Baada ya kumkosa kumkata Peter, alijipindua kwa makini na kurusha teke zuri lililomkuta Peter kifuani na kumsogeza nyuma mwili wote badala ya shingo na kichwa pekee. Wanajeshi wenzao wakapiga makofi ya pongezi kwa pigo lile toka kwa Vanessa.

Peter akatabasamu na kumuangalia Vanessa ambaye alikuwa kakunja sura na kaiweka kikazi haswa kuliko utani. Tabasamu lile, likawa kama dharau kwa Vanessa, akachomoka kwa mara ya pili akiwa na panga lake mkononi, akalirusha kwa lengo lile lile la mwanzo, lakini safari hii Peter aliinama na kubaki akitizama tumbo la Vanessa wakati pale alipoinama. Peter akapiga ubapa tumbo la Vanessa na kumfanya msichana yule ashtuke kwa sauti ya hamaniko. Peter akasimamisha kichwa chake na kumuangalia Vanessa ambaye alikuwa kashika tumbo huku anamtazama yeye.

“Umakini ni njia nzuri kuliko kutumia hasira. Kuweni makini.” Sauti ya Saigon ilitoa onyo ambalo lilimfanya Vanessa awe makini badala ya kufuatilia tabasamu la kejeli alilokuwa analichanua Peter mara kwa mara.

Ikawa zamu ya Peter kuanzisha mpambano kwa kwenda kwa Vanessa na kumrushia teke la kwenda mbele lakini Vanessa alijirudisha nyuma haraka na kwa kasi kabla ya Peter hajashusha teke lake chini, mtoto yule wa kike alichepuka kwa wepesi na kumrukia Peter kwa miguu yote miwili ambayo ilitua kifuani. Vanessa akadondokea mgongo na wakati huo Peter aliyumba kwenda nyuma lakini alipomuona Vanessa yupo pale chini, akajitupa kwa kasi huku akiwa kanyoosha panga lake tayari kwa kulitua mwilini kwa Vanessa ambaye baada ya kuona hali hiyo, alibingirikia pembeni na panga lile la Peter likakita chini. Kwa haraka, Vanessa akiwa pale chini, vivyo hivyo kwa Peter, akampiga teke la shavu mwanaume yule na kumsogeza pembeni kidogo na yeye.

“Points. Mnatakiwa mcheze na points. Kosa lako dogo, mwenzako anachukua alama muhimu ambazo zinaweza kukutoa duniani. Ongezeni umakini.” Saigon aliwahasa tena. Wote wakanyanyuka na kutazamana kwa umakini wakati huo Peter alishapoteza tabasamu ambalo alikuwa analichanua hovyo hapo mwanzo.

Vanessa sasa akiwa na akili yenye ujuzi mwingi ndani yake, alitambua safari hii ni kufa ama kupona katika mpambano ule wenye wingi wa mapigo ya kumendea.

Peter alizama katikati ya mpambano na kuanza kurusha ngumi zilizochanganyikana na mikato mbalimbali ya panga lake kali. Safari hii ni wazi alikuwa na nia ya kumaliza mpambano.

Akiwa katika urushaji wa mikato yake, Vanessa yeye alikuwa katika harakati za kupangua na kukwepa kila njia zile ngumi zilizokuja kwa kila mitindo.

Peter akiwa katika dhamira ya kufanya kweli, aliruka juu huku panga lake akiwa kalenga utosi wa Vanessa. Vanessa aliona akicheza anaweza kupotea ama kupotezwa na Peter. Akakinga panga lake kichwani na kisha akachana msamba ambao ulikuwa kama kupunguza kasi ya Peter na panga lake.

Lile panga la Peter lilitua juu ya panga la Vanessa na kutoa cheche lakini bado binti yule hakujali na badala yake, akajibetua na kumkata mtama Peter uliompeleka chini na hapohapo Vanessa akajibetua kwenda mbele na kusimama wima. Haraka akajitupa pale alipo Peter na kupiga teke mkono uliokuwa na panga ambalo nalo lilikubali na kwenda pembeni.

Peter akatazama panga lake na alipojaribu kujibiringa ili alifuate, alikutana na teke zito la kifuani lakini halikumfanya aache kusimama na kukabiliana na Vanessa uso kwa uso.

Mpambano ulikuwa mkali na ulimsisimua kila mmoja pale katika kambi. Mwisho wake ulikuwa ni mpambano huu kukosa mbabe kwani Peter alifanikiwa kulipata panga lake na wakati analiokota, Vanessa alikuwa nyuma yake kisha akamteka kwa kuuweka upanga wake nyuma ya shingo. Lakini wakati kafanya hivyo pale Peter alipokuwa kapiga goti, naye alikuwa kauweka upanga alioukota katika tumbo la Vanessa.

Watu wakiwa wanadhani kuwa Vanessa kashinda, walimuona Peter akinyanyuka huku mkono wake umenyoosha panga katika tumbo la Vanessa. Gon alikuwa wa kwanza kupiga makofi ya pongezi baada ya kuona hali na wengine wakafuata na kukubali kuwa mpambano ulikuwa si wa kitoto.

“Mmeonesha uwezo mkubwa sana vijana. Mmenifurahisha mno. Naondoka na kurudi nyumbani kifua mbele kwa kuwafundisha wanafunzi mafundi kama nyie. Hongereni.” Aliongea Luteni Japhet Saigon kwa furaha huku akienda na kuwakumbatia Vanessa na Peter.

Vijana wale walishukuru kwa kila kitu huku wakiwa wametabasamu kwa matukio yale waliyopongezwa. Huo ndio ukawa mwisho wa Luteni Saigon, mwanajeshi wa ardhi wa jeshi la Hispania. Alijua mazoezi yote na aliweza kuwatengeneza vijana kutoka katika uraia hadi uwanajeshi. Aliwaaga vijana wale huku aliahidi kuja kuwatembelea kila atakapokuwa na muda.

Wakiwa katika mstari wao huku wanamtazama Luteni Saigon akiondoka na gari pana la kijeshi, wanajeshi wale wapya walishuhudia gari lingine pana likija huku nyuma likiwa limejaza wanajeshi wengine na nyuma zaidi ya gari hilo, kulikuwa na roli lililofungwa turubai la rangi ya kijani iliyoiva hadi kukaribia weusi.

Baada ya gari lile kusimama mbele ya mistari waliyoipiga wale wanajeshi wapya, alishuka mwanajeshi mmoja na kwenda upande wa pili ambapo alifungua mlango wa upande huo na kisha kusimama pembeni akisubiri mtu aliyomo atoke.

Mwanajeshi mrefu na mwenye misuli kiasi, aliibuka tuko ndani na kuangalia anga la nchi ile akiwa kavalia mawani nyeusi na kombati ghali za jeshi la nchi za huko alipotoka.

Yule bwana aliyefungua mlango alipomuona yule mwanajeshi aliyetapakaa vyeo katoka, yeye alipiga saluti ya heshima huku usoni akiwa hana hata chembe ya kucheka.

“The Taker.” Sauti ya yule kijana mwembamba aliyekuwa akitaka kuwa mdunguaji, ilisikika ikinong’ona huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu pana mno.

Hilo ndilo jibu. The Taker ama Dolph Moris, aliyewapokea mwanzoni kule porini walipofikia, ndio alikuwa kashuka toka garini.

Alikuwa ni mtu wa Urusi na maisha yake yote alijikabidhisha katika jeshi la Urusi ambalo siku zote hupambania sera za Ujamaa.

“Ni furaha iliyoje kuwepo hapa tena,” aliongea The Taker baada ya kuwaangalia wanajeshi wote na kukubali kazi nzima iliyofanywa na Luteni Saigon. “Kama mmeweza kuishi hapo mwanzoni, basi kwangu mtaishi zaidi na zaidi. Nani ananikumbuka?” The Taker aliwauliza wale vijana na yule bwana mwembamba aliyemtambua pale mwanzo ndiye aliyejibu haraka lile swali.

“Safi kijana. Unaitwa nani na wewe?” Aliulizwa yule kijana.

“Naitwa Al Bashir Salum,” Alijibu kwa furaha yule kijana.

“Safi Al Bashir. Utakuwa unavyotaka kama utanisikiliza,” Alimpa moyo kijana wa watu.

“Tutaanza rasmi kutumia silaha za moto. Mtapata mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kujua kutumia bunduki na silaha nyingine kama hizo. Cha msingi ni wewe kuweka kichwa chako katika kila nukta ya tukifanyacho,” The Taker aliongea huku akienda huku na huko na wakati huo wanajeshi kadhaa walikuwa wanapakuwa maboksi ya mizigo mbalimbali iliyokuja na roli kubwa lililofuatana na gari aliyopanda The Taker.

The Taker aliendelea kuongea hili na lile katika zoezi ambalo alitegemea kulifundisha. Alipomaliza, aliwataka vijana wale wakapumzike kwa ajili ya kujandaa na safari nzito ya kesho yake.


“Pity,” Vanessa alimuita mpenzi wake. “Ni safari nyingine tunaingia. Ni safari ambayo ni ya mwisho kwetu sote katika mafunzo haya. Tukitoka hapa, sisi si wale tena bali ni wengine kabisa. Nategemea utakuwa na mimi katika kila jambo.” Akatabainisha ya moyoni mwake Vanessa.

“Njia tulizopita Vanee, ni njia ambazo binadamu mwingine ukimwambia apite, anaweza kukataa.” Peter alitiririka akiwa kakipakata kichwa cha Vanessa katika mapaja yake. “Baba yangu alikwishawahi kuniambia kuwa, safari ya wapendanao, ni safari ambayo anaifananisha na vipepeo viwili vinavyopendana. Huwa haviachani na mambo yao huwa ya kuvutia sana na mfano wa kuigwa vilevile. Sisi ni kama hao vipepeo Vanessa, sijui kama nitakuja kukuacha katika lolote lile. Wewe ni zaidi ya yule kipepeo aliyekufa katika kumuokoa kipepeo mwenzake lakini bado akafa. Siwezi nikakuacha kwani umenisaidia mengi Vanee.” Alimaliza Peter na kumfanya Vanessa anyanyuke na kumkumbatia yule kijana kwa upendo wa hali ya juu.


“Leo ni siku nyingine ya gharama sana katika maisha yako na yangu na yetu sote,” Aliongea The Taker au Dolph, wakati huo meza ya mbele yake kulikuwa kumejaa silaha za moto za kila aina. “Hizi ndizo silaha ambazo mtajifunza kuzitumia kwa sasa. Lakini baadae kila mmoja atachukua silaha ambayo anaona inampendeza na anaweza kuitumia ipasavyo.” Alizidi kuongea Dolph hadi pale alipoamaliza kuongea ndipo akawaita vijana wale waje mbele kwa makundi yenye watu kumi na wakati huo walikwisharudi ile kambi ya porini badala ya ile ya ifukweni.

Kundi la kwanza kila mmoja alichukua silaha na kuelekezwa cha kufanya kabla ya yote. Wanajeshi walioongozana na Dolph walikuwa wanawaelekeza wale vijana jinsi ya kuipanga bunduki mwanzo hadi mwisho.

Baada ya masaa matano ya kuwafunza kupanga bunduki, ilikuja zamu ya kuona kama zoezi lile limeingia vichwani mwao. Bunduki zilizokuwa zimepunguliwa, zimewekwa tena mikononi mwa wale vijana na kuanza kuzipanga kama zilivyo.

Katika zoezi lile, hakuna aliyeweza kufanikiwa kirahisi kupanga. Lilikuwa ni zoezi gumu na zito hasa kutokana na silaha ambazo wamepewa wazipange. Hadi saa moja inaingia, hakuna aliyekuwa kafanikiwa kuipanga bunduki yake kama inavyotakiwa.

Si kama ukishindwa waweza rukia zoezi lingine, la hasha! Pale waliposhindwa, walipewa siku nyingine zaidi na zaidi. Hadi baada ya wiki mbili, ndipo vijana wale walikuwa wameliweza zoezi lile ambalo The Taker alisema si gumu kama bichwa vyao vinaubongo mwepesi.

Siku ya mwisho alitafutwa mtu ambaye anaweza kupanga bunduki haraka kuliko wenzake. Katika kushindana huko, Al Bashir aliweza kushinda huku Vanessa na Peter wakiwa wameachwa mbali sana.

“Safi sana kijana. Unaonesha ni kiasi gani unahitaji kuwa mtu fulani,” The Taker alimpa hongera Al Bashir kwa kuonesha nyota njema tangu asubuhi.

“Si kwamba wengine mmefanya vibaya, lakini kwa uwezo wa Mungu, nashukuru mmefanya vema sana katika zoezi hili. Kesho ni siku ya kuanza kucheza na risasi za bandia.” Alimaliza The Taker na kuwaacha wale wanajeshi wakiwa na sura za furaha huku wakianza kujaribu tena kupanga bunduki ambazo zilikuwa zimepanguka.


Katikati ya nchi ya Senegal, hususani katika mji mkuu wa nchi ile, nauzungumzia Dakar. Mambo yalizidi kuwa mabaya sana. Machafuko ya kisiasa yalizidi kuchukua nafasi yake na ni wazi ilikuwa ngumu machafuko hayo kutia nanga.

Serikali iliyokuwa madarakani, iliendeleza wimbi la ubabe kwa serikali iliyotoka madarakani.

Viongozi wa nyuma waliendelea kuuawa kwa ukatili mkubwa ambao kwa macho ya kawaida usingestahimili kuangalia.

Watoto wasiyo na hatia waliendelea kuachwa mtaani bila msaada wowote wa kiutu. Vilio vya wakina mama viliongezeka kwenda kwa Muumba na wenye uwezo wa kuzuia vita vile viliyokuwa havina mjadala wa kukaa meza moja na kuelewana.

Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika, waliingilia kati mara kadhaa mgogoro ule wa serikali dhidi ya serikali iliyong’ooka madarakani, lakini ilishindwa au kama si kushindwa, basi ilichochea vita vile kwani mataifa makubwa yalikuwa yameweka mikono yao katika nchi ile katika kusambaza dhana za kivita. Hali ilikuwa tete katika taifa lile la watu weusi, hali ilikuwa mbaya kwa wakina mama na watoto wao wadogo.

Ubakaji, wizi wa mali, vifo vya kumwaga damu, magonjwa ya mlipuko na ya kuambukizwa, dondoko la uchumi, njaa, upotevu wa mali asili, watoto wa mitaani, upungufu wa watu na wafanyakazi, dondoko la Elimu, na mambo kadha wa kadha, yaliendelea kuikumba nchi ile ndogo kwa Jiografia.

Omba kuendelea kuona vita kwenye runinga na kuisikia katika maredio au mitandaoni, lakini kamwe usiombe uone ukweli vita katika nchi yako, hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Siasa ilitengeneza makundi katika nchi, makundi hayo yalizidi kumaliza nguvu kazi ya watu katika nchi ile.

Chama kilichokamata madaraka, kilikuwa na watu wake na chama kilichoondoka kilikuwa na watu wake. Wao kwa wao wakawa hawapendani. Si jambo la ajabu kwa kijana kumuua kijana mwenzake kisa wapo vyama tofauti. Hali ilikuwa mbaya na nchi ilihitaji msaada mkubwa wa ukombozi.

Lakini ni nani ambaye ataleta ukombozi huo? Hapo ndipo wananchi wanakumbuka maneno ya mwanamziki mkongwe wa reggae, muasisi wa muziki ule, Bob Marley katika wimbo wake wa Redemption Song. Alisema hivi, nanukuu. “Emancipate yourself from mental slavery, None but ourselves can free our mind. Have no fear for atomic energy, ‘Cause none of them can stop the time. How long shall they kill our prophets, While we stand aside and look?” Yaani, kuupata mwenyewe uhuru wa kifikra.

Hakuna atakayetupa bali sisi wenyewe. Tusiogope nguvu za atomiki kwani kati ya hivyo hakuna kinakachosimamisha muda. Ni lini wataacha kuwaua manabii wetu wakati tumesimama na kuangalia?.

Maneno hayo ya Bob Marley ndio yalifanya baadhi ya watu kuasi serikali iliyomadarakani na kwenda kuanzisha jeshi ambalo litaipindua serikali hiyo.

Wakati jeshi imara la waasi linaandaliwa huko maporini, huku katika kambi waliyoiacha, baadhi ya wanajeshi walizidi kupambana kufa na kupona ili kujitoa katika utumwa wa ambao wameingizwa na watu wenye uchu na madaraka na roho mbaya pia.

Kambi ya Born To Die ilizidi kuongeza vijana wanawake kwa wanaume na kuwapatia silaha za mapambano kwa ajili ya kutokomeza vuguvugu ambalo lilikuwa limeshika kila kona muhimu ya nchi ile.

Wakati hayo yanaendelea katika nchi ile, huko mataifa ya mbali walikuwa wanakenua kila kukicha kwa sababu waliyoyapanga yalikuwa yanazidi kufanya vizuri.

Silaha ambazo zilikuwa hazina majina, zilitengenezwa kwa wingi na kumwagwa Afrika hasa katika nchi zenye vita. Mambo yalizidi kuwa mabaya sana katika bara la Afrika.

Wakati hawa wanawauzia silaha waasi, wengine wanauza kwa serikali iliyopo madarakani. Mwisho wake ilikuwa ni vifo hata kwa wale ambao hawana hatia.

Bado nasisitiza kuwa Afrika haitopata ukombozi kama sisi waafrika wenyewe bado tutakuwa na akili tegemezi, akili ya kuwatukuza na kuwaamini watu weupe kuliko weusi wenzako.

Amini kuwa, kama upo chini ya jua hili, basi vyote vilivyochini kama wewe, haviwezi kuwa juu yako. Unahaki ya kuishi na kufanya kama wao. Unahaki ya kuchagua ukipendacho na kukifanyia kazi. Unahaki ya kutembea kifua mbele hata kikiwa wazi ili mradi upo huru na nchi au dunia uliyopo.

HAKUNA, nasisitiza tena HAKUNA ambaye anaweza kukaa juu yako kama naye yupo chini ya jua hilihili linalokuchoma wewe. Ni MUNGU pamoja na taifa lake la huko mbinguni ndilo lenye mamlaka ya kukaa juu yako. Kama yupo anayejaribu kukaa juu yako, basi unahaki ya kumpinga ama hata kumdhuru pale atakapoonesha nia mbaya juu yako. Si kwa sababu ya kutafuta heshima, bali ni katika kuipa uhuru nafsi na akili yako.

Hakuna kitu kibaya kama kuwa mtumwa wa fikra, nafsi na moyo. Heri uwe mtumwa wa mwili, yaani usurubike mwili wako, utaabike mwili wako, uumie, uchafuke, upoteze hisia, upoteze viungo vyako vya mwili kuliko kuwa mtumwa wa hisia, fikra na moyo. Kama utapigana katika kuondoa utumwa wa vitu hivyo, basi tambua kuwa hata utumwa wa mwili utakuwa huru.

Kama fikra na hisia zako za roho utaziendesha mwenyewe, basi mwili wako utakuwa huru kwa kuendeshwa na fikra au hisia huru ulizonazo.

Tusiwe watu wa kuwaabudu sana watu fulani eti kwa kuwa wanaupeo mkubwa katika maamuzi au vichwa vyao. Kama wao wanaupeo huo, wewe ukose kwa sababu gani? Ukitoa rangi yako ghali nyeusi, ni nini ambacho mzungu au mtu mweupe kakuzidi?

Rangi nyeupe si rangi ya kuisifu kwani ni rahisi kuijua kuliko rangi nyeusi. Mtu mweupe awapo na furaha, basi hubadilika hadi kuwa wa njano. Lakini apatapo hasira, basi huwa mwekundu. Lakini mtu mweusi, huwezi kumjua kama anafuraha ama kakasirika hadi umsogelee na kumuhoji.

Unatakiwa kuwa mjivuni kwa rangi yako, unatakiwa kusema mimi ni mweusi na mimi ni Muafrika, na sasa nasimama katika kujikomboa katika utumwa wa fikra ambazo zimepandikizwa na ngozi mbovu za weupe. Jivune kwa vile ulivyo.

Usichekelee Waafrika wenzako wanapopigana vita kwani mwisho wa siku bara hili litabaki mashimo ya machimbo na matuta ya makaburi ya watoto zako, ndugu zako na rafiki zako. Unatakiwa kujua kuwa leo wanaanza huko palipo dhaifu, lakini kesho wanakuja kwako. Afrika tusimame katika umoja na kupinga silaha chafu zinazoingizwa katika bara hili, tupinge kuingiliwa katika siasa zetu na zaidi, tusiwe na umimi katika madaraka tunayopatiwa na wananchi.

Naamini kuwa mwisho wa haya ni wote sisi kufa kwani hakuna atakayeishi milele. Lakini vema ufe wakati unapambana kuliko kufa katika utumwa wa nafsi, fikra, roho na mwili. Hakuna aliyezaliwa na kitu, lakini unatakiwa kufa kwa sababu ya kitu. (Born For Nothing, But Die For Something) Na hakuna asiyekuwa fulani, wote tumezaliwa ili tuwe fulani. (No body is nobody, we all born to be somebody)

Pigania unapotakiwa kuwa. Hivyo ndivyo wanamapinduzi tunaamini.


Nchi ya Senegal ikawa ndani ya sakata zito la kupigana vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini vita hivyo vilichochewa na mataifa makubwa kwa kuwauzia silaha. Wakati Serikali inapewa silaha na nchi za Amerika na washirika wake Wa Kibepali, Waasi wakawa wanapewa silaha na nchi za Asia, nchi zinazoamini sera ya Ujamaa katika maamuzi na uongozi wao.

Licha ya haya yote ambayo baadhi ya Waafrika, tena wengi tu! Kuona ni msaada, lakini katika vichwa vinavyojua kufikiri kwa kina, pale ilikuwa si msaada bali utumwa katika nchi yako. Utumwa ambao unaangamiza hata rangi unayofanana nayo. Wapo walioliona hili na waliamua kupigana nalo.


Mafunzo ya silaha yaliyoongozwa na Dolph Moris au The Taker, yalizidi kukata mbuga huku vijana wote wakionesha hali ya kuelewa haraka somo lile. Walilenga vema pale walipopewa zoezi hilo na walifanikisha mambo mengi katika kutafuta silaha hizo.

Al Bashir, kijana mwembamba na mrefu, ukimuona unaweza kusema ni.mtu wa Somalia, sehemu ile ni kama alikuwa anaisubiri kwa hamu sana. Alionesha uwezo mkubwa wa kutumia silaha kwa kulenga na kucheza nazo. Alikuwa mwepesi sana kubadilisha silaha pale nyingine zilipomuishia. Hali hiyo ilimfanya The Taker ampende sana. Lakini hakumpa kichwa, wala hakutaka kumgeuza kijana yule mgema kwani mgema ukimsifia sana, unajua nini kitatokea.

“Siku ya leo, utakuwa siku ya mwisho katika mafunzo ya matumizi ya silaha,” Aliongea The Taker. “Nitawagawanya katika makundi kadhaa na kila kundi litatumia njia mbalimbali za kijeshi ili kulipiga kundi lingine.” Alizidi kuelezea The Taker.

“Watu mia na hamsini, kila kundi watu kumi. Hivyo makundi yanatakiwa kumi na tano. Yataondoka makundi mawili kwenda kuchukua bendera mahali fulani ambapo mtapewa ramani ya kufika huko kwenye bendera.

Bunduki zenu zinatoa risasi zenye rangi, hivyo ukijiona unarangi, basi wewe umepigwa risasi. Kila kundi litavaa nguo rangi zake.” Alitoa maelezo mengi sana ambayo yalikita vema katika vichwa vya vijana wale na baada ya hapo, makundi yakapangwa huku akifanya makusudi kwa kuwaweka kundi moja Peter, mtaalamu wa kusoma ramani, Vanessa mtaalamu wa mapigano na kukwepa vizuizi pamoja na Al Bashir, mtaalamu wa silaha na kulenga.

“Kumbuka, kundi litakalofanikiwa kuipata bendera mapema kwa nyie wa kwanza, litapambana na kundi linatakaloshinda katika safari ya pili. Na la safari ya tatu litapambana na la safari ya nne na kuendelea. Baadae atatafutwa mshindi mmoja.” Jiwekeni katika utayari. Zoezi hili litaenda hadi usiku.” Alisisitiza The Taker.

Zoezi lile lilianza moja kwa moja kwa kasi kubwa na kila kundi lilionesha wazi lilikuwa na nia ya kushinda zoezi lile dogo sana lakini lenye umuhimu ambao kwa nchi za Afrika zingefaidika kama wangefanikiwa kumaliza mafunzo yale ya kijeshi.

Kundi la wakina Peter, au Green Rebels kama walivyoitwa na kiongozi wao kutokana na mavazi waliyopewa wayavae, lilikuwa ni kundi tishio kuliko makundi yote.

Uwezo wa Al Bashir katika kuchukua shabaha kwa kujificha hata juu ya mti na kisha kufanya kilichosahihi, ndicho kilichowapa ushindi Vanessa na wenzake wote. Ilikuwa ni furaha kubwa sana usiku ule ambao walimaliza mafunzo ya kulenga shabaha na kutafuta bendera katika msitu mmoja uliopo barani Afrika, hasa pembezoni mwa bara hilo.

Baada ya kufurahi na kuruka ruka huku wakiletewa vilevi na vyakula mbalimbali vya kuwapa furaha, waliambiwa wakalale porini kwenye giza zito, macho yakawatoka huku uoga ukiwavaa bila kikomo.

“Ndio hivyo. Nendeni mkalale porini huko. Huku hatutaki mtu. Mnaruhusiwa kulala kwa makundi.” Alisisitiza The Taker na bila kufikiria, wanajeshi wakakurupushwa toka kwenye hema kubwa walilokuwemo na haraka wakakimbilia katika pori walilokuwa wanafanyia mazoezi mara kwa mara.

Vanessa akiwa kakamatwa mkono na Peter, walifika kwenye mti mmoja na kukaa hapo bila kuona chochote kwa sababu giza totoro lililokuwepo usiku ule wa manane.

“Sijui kwa nini wamefanya hivi,” Peter aliuliza kwa sauti kubwa.

“Hata mimi sifahamu.” Sauti nene ilijibu swali la Peter na kumfanya Peter ashtuke na sasa akajua kuwa pale hakuwepo yeye na Vanessa pekee bali na wengine.

Kila kitu katika jeshi huwa na sababu yake. Kila jambo hutendwa katika makusudi maalumu ya kuliendeleza jeshi liandaliwalo mahususi kwa mapigano fulani.

Baada ya kufika porini na wanajeshi wale kulala bila kutambua wamelala wakiwa wangapi, kesho yake asubuhi na mapema, wakuu wa mafunzo yale walifika sehemu ile na kukuta makundi kadha wa kadha yakiwa katika usingizi.

“Amkeni wote,” Aliamrisha Dolph na wanajeshi wote waliamka na kusimama wima tayari kwa kupokea neno lolote toka kwa wakuu wao.

“Safi sana,” Sauti ya Kamanda Bonito iliongea na kusogea mbele zaidi ya makundi yale. “Jinsi mlivyolala, ndivyo mtakuwa mnafanya kazi tutakazo waagiza. Kila kundi nitatoa jina mimi na kiongozi. Cha msingi mjue majukumu yenu tu!” Aliongea Bonito na baada ya maongezi mengi, alitoa majina kwa kila kikundi. Makundi yalikuwepo kumi na saba lakini kundi la Peter ndilo lilisheheni wanajeshi nguli akiwepo Vanessa na Al Bashir pamoja na wengine wanne.

Baada ya majina hayo, kauli yao ikawa moja tu. “Chochote mtakachofanya, ni kwa sababu mmezaliwa kufa. We all Born To Die (Wote tumezaliwa kufa)” Bonito aliongea kwa sauti na wanajeshi wote walishangilia na kusema kwa nguvu,

“We all born to die,” Baada ya sauti hiyo, Kamanda Bonito alijiweka mstari wa mbele na kuanza kukimbia kwenda kwenye kambi waliyokuwepo jana usiku. Wanajeshi wake wapya na wa zamani, wakamfuata kwa nyuma hadi huko.

Ghala kubwa likafunguliwa. Ndani ya ghala kulikuwepo na silaha za kila aina. Silaha ambazo walizishusha kipindi cha nyuma. Silaha ghali na hatari sana katika maisha ya binadamu.

Kila mwanajeshi akakamata silaha yake na kutoka nje ambapo walipanga mistari huku wote wakiwa wanatweta na jasho la ukombozi likiwatoka kila mahala kwa hamasa.

“Tunaenda kuikomboa Afrika toka mikononi mwa madikteta. Tunaenda kuitoa Afrika toka kwa wanyonyaji. Wote tuseme Afrikaaa,” Bonito aliongea na wanajeshi wote wakanena jina hilo kisha risasi nyingi zikaanza kumwagwa hewani.

“Twendeni nyumbani sasa.” Bonito alizidi kuhamasisha na wanajeshi wote wakiwa ndani ya vifaru na magari ya kijeshi yaliyobeba silaha nyingi, wakaanza kurudi katika kambi yao ya mwanzo iliyokwenda kwa jina la Born To Die.


BAADA YA MIEZI MIWILI.

Nchi ya Senegal ilikuwa katika moto wa hali ya juu katika vita. Waasi walivamia na kuwateka viongozi waliyomadarakani na kupeleka onyo kwa utawala wote uliokuwa unakandamiza wananchi wa nchi ile.

Hali ilikuwa ngumu na tete kwa serikali. Kila siku ni kheri ya jana katika uongozi ule ambao ulihatarisha maisha ya waasi wengi waliokuwa kitu kimoja kwa muda ule.

Waasi waliokuwa wanatumwa kufanya machafuko maeneo wanayopatika viongozi wa nchi ile, walifanya vurumai ambalo lilikuwa ni hatari kwa kila jicho la atakayeona.

Peter na wenzake ambao mara nyingi waliiweka serikali katika hali mbaya ya kifikra na mioyo, walikuwa wanavuruga vya kutosha pale wanapopewa kazi hiyo.

Wakiwa na bendera nyeupe iliyoandikwa maandishi makubwa mekundu ya “BORN TO DIE”, walileta tumbo joto kila gari lao lilipofunga breki katikati ya miji ya Senegal. Waliogopeka na ni wazi serikali ilishindwa kuwazuia kabisa vijana wale pamoja na waasi wengine ambao hawakuchoka kudai haki zao.

“Huu ni mwanzo tu. Vita kamili ya kuondoa uongozi nyonyaji unakuja rasmi,” Sauti ya Kamanda Bonito Muchakila, ilisikika kwenye kanda ya video moja ambayo ilitumwa katika vituo vikubwa vya habari duniani.

Viongozi kadhaa wa nchi ile walionekana kwenye kanda hiyo wakiwa mahututi kutokana na kipigo na Bonito alikuwa anaongea maneno mengi huku akiwatolea mfano wale mabwana.

“Mkuu. Tunatakiwa kukaa na hawa jamaa.” Ulikuwa ni ushauri toka kwa mshauri wa Rais wa nchi ya Senegal baada ya kutazama kanda ile kwa kuirudia mara kwa mara.

“Tutaanzia wapi? Mambo yamekuwa magumu. Tusipoangalia tunapinduliwa na tutaishia kuchinjwa kama kuku,” Rais alionesha wasiwasi wake.

“Ndio maana nakwambia tuombe maongezi ya amani na hawa watu,” alishauri tena kwa msisitizo yule mshauri.

“Tunaanzia wapi sasa?” Rais akauliza huku akigonga meza ngumi nzito.

“Hamna shaka kuhusu hilo, kama upo tayari, niruhusu tukawatafute,” Aliongea yule bwana na kusubiri jibu la Rais.

“Fanya hivyo haraka kabla hawajaanza kuleta fujo hata Ikulu. Wakileta ubishi, tunaita washirika wetu waje watusaidie kuwasaka maana sisi tumeshindwa.” Rais alitoa ruksa na saa hiyohiyo, yule mshauri alitoka nje na kwenda anapopajua.

Baada ya wiki mbili, Rais aliletewa ujumbe wa kuhitajika na kiongozi wa Waasi katika misitu mikubwa inayopatikana Kongo. Kamanda Bonito alichagua huko kwa sababu ana washirika wenzake wengi ambao wanaweza kumsaidia kama Rais ataleta uhuni.

Rais akapokea ujumbe ule na kisha akaandaa walinzi wake kumi kwa ajili ya ulinzi wake akiwa huko na wengine wengi aliwaacha katika Ikulu yake ili kuzuia mapinduzi kama yatataka kutokea.

Baada ya siku tatu aliitikia wito wa Kamanda Bonito wa kwenda katika msitu huo mpana bila kuogopa kwani walichoenda kukijadili ni amani tu na si kutekana. Akiwa na walinzi wake kumi, alifika alipohitajika na alimkuta Kamanda Bonito akiwa kakaa kwenye kiti huku kakunja nne na mdomoni akiwa anavuta sigara moja kubwa ya Kirusi.

“Karibu mheshimiwa,” Alimkaribisha kiti kilichokuwa mbele yake ambacho kilitenganishwa na meza moja kuu kuu.

Nyuma ya Kamanda Bonito alikuwepo Peter na Vanessa waliokuwa kama walinzi watiifu wa Kamanda Bonito. Bonito aliwategemea sana wale watu katika ulinzi wake na kila mara aliwasihi sana wasije wakamgeuka kwa sababu walisikia siri nyingi alizokuwa anaongea na wageni wake.

Rais alisogea kwenye kile kiti cha mbao na kukivuta, kisha akabweteka mwili wake mzito na mnene kwenye kile kiti.

“Huna haja ya kuja na watu wote hawa katika sehemu ambayo wajua wazi tukiamua kukumaliza hata sekunde huchukui,” Bonito aliongea huku akisigina sigara yake kwenye meza iliyokuwepo pale.

“Nimekuja kuongea na wewe. Hawa hawakuhusu. Twende kwenye maongezi,” Rais alionesha msimamo wake na Bonito alitabasamu kidogo kisha maongezi marefu yalianza kuchukua nafasi yake katika pori lile.

“Nachotaka ni mimi kuwa waziri mkuu, na wewe kuwa Rais kama ulivyo. Sina nia mbaya bali ni katika kuweka usawa wa kimadaraka na wa nchi. Nikiwa waziri mkuu, basi wananchi wapatao shida, nao watakuwa salama pamoja na watu wangu. Huo ndio usawa niutakao kwa sasa,” Ni baadhi ya maongezi ambayo Bonito aliyasisitiza yatimizwe. Rais akainamisha kichwa katika mjadala ule na alipoinua, alipata jibu au tuseme alipata cha kufanya.

“Nina washauri pamoja na wenzangu, naomba nirudi nikaongee nao kabla sijaamua peke yangu.” Rais aliweka bayana mawazo yake na Bonito hakuwa na kinyongo kuhusu hilo.

“Siku mbili zinatosha sana kufanya maamuzi.” Bonito alimpa siku mbili za Rais kufanya alichoahidi.

“Nadhani zinatosha,”

“Safari njema mheshimiwa.” Bonito alimuaga Rais na mheshimiwa yule alisimama na kugeuka tayari kwa kuondoka.

“Mheshimiwa,” Bonito alimuita na Rais akageuka. “Siku nyingine usije na hao mabwana. Nita……” Bonito aliweka ishara ya bastola kwenye vidole vyake na kufanya kama anamfyatulia mmoja wa walinzi aliokuja nao Rais yule. Alipofyatua, mlinzi alipigwa risasi ya bega na kumsababishia maumivu makali mno.

Haikujulikana risasi ile imetoka wapi lakini ilileta uoga kwa wale walinzi kupita maelezo. Rais alitabasamu bila uoga na kisha akageuka zaidi na kwenda hadi pale kwa Bonito.

“Tatizo lako ni dogo sana. Ubabe utakuponza. Sikujui, hunijui. Kuwa makini.” Aliongea Rais. ” Papasa chini ya kiti chako.” Akamaliza Rais na kuanza kuondoka na bila kupoteza muda, Bonito alipapasa chini ya kiti alichokalia na gapo alikutana na vitu kama vipande vya sabuni.

Akaving’oa toka pale vilipopandwa. Alikutana na mabomu matatu ya masaa, wakati huo Rais alionesha ishara ya kuwaita watu wake akiwemo yule aliyepigwa risasi ya bega na wote wakamfuata kwa nyuma kuondoka eneo lile.

“Haya mabomu kayaweka saa ngapi?” Aliuliza kwa mshangao Kamanda Bonito baada ya Rais kutitia toka eneo lile.

“Yupo vizuri. Hayo mabomu yaliwekwa kwa kigari kidogo kilichotumwa chini kwa chini na kuibukia chini ya kiti chako. Ni teknolojia ya Marekani hiyo. Kuwa makini siku nyingine.” Aliongea mtaalamu mmoja baada ya kuchunguza sana chanzo cha yale mabomu kuwepo kwenye kiti cha Bonito.

Bonito akacheka na hapohapo akageuka na kuwatazama Vanessa, Peter na Al Bashir ambaye alijificha mahala na bunduki ya kudungulia (Sniper Rifle) na ndiye aliyempiga risasi ya bega mlinzi wa Rais wa Senegal.

“Mmefanya vema vijana. Baada ya hapa, nitawapa ruhusa ya kulishughulikia suala la Vanessa. Jiandaeni.” Alitoa pongezi Bonito na kuwaacha wale watu wakiwa wamesimama na mioyo yao kuwadunda hasa baada ya kusikia kushughulikiwa suala la Vanessa.

Siku mbili zilizofuata, Rais alirudi tena palepale na kukubali kufanya kile ambacho Bonito alikitaka. Maongezi yalichukua muda mwingi sana hadi kufikia muafaka halisi.

Hadi Rais wa Senegal anaondoka eneo lile akiwa na wanajeshi wake kadhaa kama kawaida, tayari walishasaini baadhi ya makaratasi ambayo yalikuwa na mikataba ya amani. Hilo ndilo lililosaidia nchi ya Senegal kupungua machafuko ya kila siku.

Baada ya makubaliano hayo, Bonito na walinzi wake watakatifu, walirudi nchini Senegal katika kambi yao ya Waasi.

“Vanessa. Sasa ni wewe na wenzako.kwenda kumaliza haja zako. Upo tayari?” Bonito alimuuliza Vanessa ambaye alijibu haraka kuwa yupo tayari kwa hilo. Bonito akatoa bahasha moja kubwa kiasi na kuitupia mbele ya meza yake.

Vanessa akachukua bahasha ile na kuifungua. Humo akakutana na picha za mama mmoja aliyeanza kuzeeka pamoja na za vijana wengine kama yeye, wakiwa wawili lakini wanajinsia za kiume. Pia kulikuwa na picha nyingine ya binti kama wa miaka kumi.

Alipopekua zaidi, akakuta picha ya mwanaume mwingine aliyeenda hewani na mweusi sana. Naye alikuwa katika hali ya uzee lakini alionekana bado mkakamavu.

Chini ya picha hizo kulikuwa na ramani na sehemu fulani ya ramani hiyo kulikuwa na alama iliyochorwa kwa wino mweusi na kuwekewa jina ambalo lilitumika katika sehemu ile. Vanessa akatabasamu na kumuangalia Bonito kwa macho ya faraja.

“The ball is in your path. Is up to you now. (Mpira upo katika njia yako. Ni kazi kwako sasa)” Bonito alimwambia Vanessa na binti yule alitoka ndani ya ofisi ile akiwa katika tumaini jipya kwenye kutimiza azma yake.

KONGO, SAA TATU USIKU.

Nyumba moja kubwa ilikuwa imetawala vicheko vya hali ya juu kati ya mama na watoto waliokuwa wanaendelea kupata chakula cha usiku.

Mama yule ambaye umri ulikwishakwenda kiasi chake, alikuwa anawatania watoto watatu ambao mara kwa mara walimuita mama kila walipozidishiwa vicheko.

Hakuna aliyehisi unyonge ama maumivu wakati wakiwa na mama yao kipenzi na mzazi wa pekee.

Mavazi ghali waliyokuwa wameyatinga miilini mwao, ilionesha wazi walikuwa si watu wa shida ndogo ndogo hasa za kifedha.

Nje ya nyuma kubwa waliyokuwepo wale wanafamilia, kulikuwa kuna walinzi waliokuwa wanalanda huku na huko kila mara. Walizunguka jumba lile la thamani, lililojitenga na nyumba nyingine za wananchi wa mtaa ule.

Licha ya walinzi lundo waliyokuwa wanasilaha za moto na zimwagazo risasi kwa wingi bila kuchoka, pia kulikuwa na mbwa kadhaa waliokuwa wamezagaa huku kila mmoja kashikwa na mlinzi. Mbwa hao walinusa kila mara walipopita mahali.

Uzio wa ukuta uliozungushwa katika nyumba ile, ulitandazwa nyaya ambazo kila sekunde zililia sauti ya umeme, ikimaanisha nyaya zile zilikuwa zinaumeme mkali.

Katika kila kona za uzio ule, kuliwekwa kamera ghali kabisa za CCTV na kila mara zilichukua matukio ambayo yalikuwa yanaendelea katika eneo zima la jumba lile la kifahari kama hekalu.

Mita kadhaa kutoka nje ya uzio wa jumba lile lilipo, kulitengwa pia kamera na kiashiria fulani ambacho ukikigusa hutoa mlio mkali na kuamsha uimarikaji wa ulinzi kwenye jumba lile.

Vanessa, Peter na Al Bashir, walikuwa mbali kabisa na eneo lile huku darubini zao zikiwekwa mara kadhaa katika macho yao kuona kama watapata chochote cha kuwaingiza eneo lile. Walipewa taarifa za kila kitu ambacho kinazunguka jumba lile hivyo walikuwa si wenye papara katika kazi ambayo imewasogeza eneo lile.

“Huyu Malaya kajidhatiti sana, utasema nyumba ya Papa wa Vatican.” Aliongea Vanessa wakati anashusha darubini yake kifuani.

“Kuna kazi moja nzito mno hadi kuingia ndani ya hekalu lile. Hasa zile kamera na ‘alarm’. Zitatupa shida sana,” Peter aliongea kwa utaratibu.

“Kweli kabisa Pitty. Cha msingi tujigawe. Badala ya kwenda sote ndani, basi ni kheri Vanessa aende. Hata akionekana, atajifanya anashida ya kuingia,” Alishauri Al Bashir ambaye mgongoni alikuwa kavaa begi refu mfano wa yale mabegi wanayowekea magitaa. Sema lenyewe lilikuwa refu na jembamba.

“Umesema neno Bashir. Acha nijipange, au unasemaje Pitty?” Vanessa alimtazama Peter usoni kabla hajafanya chochote katika maamuzi yale waliyoyapanga.

“Sasa si itabidi uache silaha zako. Unadhani pale utapita hivihivi?” Peter akamuuliza huku naye akiwa anamtazama Vanessa.

“Ndiyo nataka kuacha hivyo. Baada ya mimi kuingia ndani, yapaswa Bashir ufanye kazi yake ya kusafisha njia ya Pitty.” Aliongea Vanessa huku akivua mkoba wa kiunoni ambao ulikuwa na visu. Na kisha akavua koti na nyuma yake akatoa mapanga mawili marefu na makubwa (Machette). Akaviweka pembeni na baada ya hapo, akambusu Peter kabla hajaanza kwenda alipopanga.

Vannesa baada ya kujiona yupo safi, akashika njia moja kwa moja kwenda katika jumba lile ambalo ni wazi alipanga kwenda kufanya matendo ambayo yatanyong’onyeza kabisa familia ile.

Wakati Vanessa anasonga huko, Al Bashir alishusha begi lake na kulifungua kisha akatoa mtutu wa bunduki mrefu sawa na begi lile. Akachukua risasi kadhaa zinazotumika kwenye bunduki ile ya kudungulia, na kuziweka sehemu yake kwenye bunduki. Akaikoki na kujaribu kulenga kabla hajaondoka sehemu ile na kumuacha Peter akisubiri kuitwa ama kuruhusiwa aende alipo Vanessa.

Kabla hajalifikia geti lile, mlio mkali ulinza kulia na wakati huo mbwa nao walianza kubweka kwa nguvu na kuwafanya walinzi wa jengo lile wakae kitako tayari kwa lolote ambalo linataka kujiri. Wakatoka walinzi watatu wenye bunduki pamoja na mbwa na kumsogelea Vanessa ambaye alikuwa kanyoosha mikono juu na uso wake ukiwa ndani ya uoga mkubwa.

“Unataka nini we’ binti.” Aliuliza yule mlinzi mmoja huku akimmulika Vanessa kwa mwanga mkali wa kurunzi.

“Nina shida na Madam Diana Winto. Tafadhali nisaidieni.” Vanessa aliongea huku sauti yake akiiweka katika hali ya kilio.

“Unamtaka wa nini? Una mihadi naye?” Aliulizwa tena Vanessa.

“Hapana jamani. Nina matatizo, nimefukuzwa huko na wazazi wangu wameuawa wakati tumekuja kutalii. Naombeni msaada jamani, nimetoka mbali,” Alilia Vanessa na kuwafanya wale walinzi waamini kiasi chake hasa kwa rangi ya uchotara aliyokuwa kaichukua kwa wazazi wake wote wawili.

“Nenda kamsachi,” Aliongea mlinzi mmoja na kwa umakini mlinzi yule alisogea huku bunduki yake kamlenga Vanessa. Akaanza kumkagua Vanessa kwa makini kuona kama anakitu chochote kitachokuwa cha hatari kwa familia ya nyumba ile.

“Hana kitu,” Aliongea mlinzi baada ya upekuzi kuisha. Walinzi wale wakapumua na kushusha mitutu yao ya bunduki, kisha mmoja wao ambaye alionekana ndiye kiongozi, akashika kitu kama kishikizo ambacho alikivaa sikioni.

“Kuna binti anataka kumuona mama,” Aliongea yule mlinzi. Upande wa pili ukamjibu na yule mlinzi akamtazama vema Vanessa kabla hajaendelea kuongea na mtu aliyekuwa hewani.

“Ni mweupe mwenye nywele ndefu. Sijui ni wa nchi gani ila anasema ni mtalii.” Akajibu yule mlinzi kabla ya kumuuliza tena Vanessa. “Umetoka nchi gani binti,” Ni swali alilotupiwa Vanessa.

“Nimetoka Uingereza.” Alijibu Vanessa huku akivuta kamasi. Yule mlinzi akaongea tena kwenye simu yake lile jibu alilopewa na Vanessa.

“Una uhakika hana chochote chenye madhara?” Upande wa pili wa mawasiliano uliuliza na yule mlinzi aliafiki bila kumkagua tena Vanessa. “Basi nawasiliana kwanza na Mama.” Alijibu tena yule bwana kabla hajatulia kwa dakika zipatazo tatu. “Okay. Mlete ndani,” Ruhusa ilitolewa na moyo wa Vanessa ulijawa na furaha baada ya kushinikizwa awafuate wale walinzi.

“Mambo yanaenda poa,” Peter aliongea kwenye simu ya upepo maneno yaliyomwendea Al Bashir.

“Ndio kaka. Naona kila kitu.” Ali Bashir naye alijibu na kurudisha jicho lake kwenye kioo cha lensi kilichokuwepo kwenye bunduki ile maalumu kwa udunguaji.

Vanessa akapelekwa hadi kwenye geti maalumu la kukagulia, na baada ya kugundulika hana chochote chenye madhara, akaongozwa na walinzi wengine hadi ndani.

“Kazi yako imebaki Bashir.” Aliongea Peter baada ya kumuona Vanessa kaingia ndani ya jumba lile. Bashir akatabasamu na kwa uchangamfu mkubwa, akaikoki kwa mara ya pili vema bunduki yake. Akaweka jicho lake na mtu wa kwanza kumchukua alikuwa ni mlinzi mmoja aliyekuwa peke yake eneo la pembeni, huyu alikuwa anavuta sigara.

Bunduki yenye uwezo wa kuipeleka risasi hadi zaidi ya mita mia tano, ikiwa imefungwa kiwambo cha kuzuia sauti, ilibanja kidogo na mlinzi yule mvuta sigara, akadondoka wakati huo kwa haraka Bashir alikuwa anaikoki bunduki yake na kumdungua mbwa aliyekuwa kafungwa pembeni kidogo na mlinzi mvuta sigara.

Kazi ilikuwa inafanyika kwa haraka na kwa umakini mkubwa ili waliopo ndani wasisikie yanayotukia nje.

Ndani ya dakika tano, walinzi wapatao kumi walikuwa chini na mbwa zao zikiwa zinahema kwa shida.

“Upo vema Bashir.” Alimsifia Peter.

“Asante kaka.” Bashir alijibu akiwa na tabasamu la bashasha.

Ndani ya jengo lile la gharama, Vanessa alikaa kimya kwenye sebule kubwa na lililowazi kwa kiasi kikubwa na kiasi kidogo kilichobaki, kilienea samani za mbalimbali za mbao na madini kadha wa kadha yaliyotapakaa ukutani na mezani.

“Karibu binti,” Aliongea Mama yule wa makamo ambaye alikuwa anapata chakula na wanawe watatu huku huko nje pakiwa tulivu kabisa.

Vanessa akamtazama yule mama na hapohapo akakumbuka maisha yake ya nyuma kabla hajafikia kuitwa binti. Alikumbuka jinsi mama yule alivyokuwa anamlilia mama yake shida, akakumbuka jinsi alivyokuwa anapiga magoti kwa mama yake ili asaidiwe japo sukari kijiko kimoja, akakumbuka jinsi mama yule alivyokuwa anapendwa na mama yake. Tabasamu hafifu likamtoka Vanessa baada ya kumuona yule mama ambaye alipambwa na vito kadhaa vyenye madini ya nchi ya Kongo.

Mama yule akajibweteka kwenye kochi moja lililopo ndani mle. Akazirudisha rasta zake kwa nyuma na hapo uso wake uliopambwa kwa vipodozi mbalimbali, ukaonekana vema lakini haukuficha uzee wake uliosababisha ngozi kuchuja na kusinyaa. “Sijui unaitwa nani binti,” Aliuliza tena yule mama.

“Naitwa Vanessa.” Akajibu Vanessa.

“Oooh! Vanessa.” Mama yule akafurahi kulisikia jina lile na hapo akakunja mguu wake mmoja kwa kuupandisha juu ya mwingine, akakunja nne. “Jina zuri sana.” Akaongeza na kumfanya Vanessa atabasamu tena.

“Asante.” Shukrani ikamtoka Vanessa. Na hapo watoto watatu wa mama yule wakatoka vyumbani walimokuwepo na kujiunga na mama yao kusikia kilichomleta Vanessa usiku ule.

Baada ya muda kidogo, alitoka mwanaume mwingine mrefu na mweusi naye akaungana na familia ile. Vanessa akamtazama yule bwana na sura yake ndio ikamfanya mapigo yake ya moyo kumdunda kwa kasi kuliko hapo mwanzo. Kichwa chake kikarudisha mawazo yake tena nyuma.

Licha ya mama yake kufanya wema wote ule kwa yule mama ambaye sasa anatazamana naye, lakini malipo yake yalikuwa ni kifo. Tena kifo cha kikatili sana. Kifo cha kuchinjwa kama kuku wa sikukuu. Na mtu aliyepewa dhamana ya kumchinja mama yake, alikuwa kakaa kwenye kochi akitikisa kichwa na kula raha za maisha ndani ya mali za wananchi wa Kongo.

“Vanessa,” Sauti ikamtoa mawazoni Vanessa na kumuangalia yule mama ambaye alikuwa anamtazama. “Mbona nakuita lakini husikii? Au ndio maumivu ya kupoteza wazazi?” Aliuliza yule mama na Vanessa alijikuta akilipukwa na moyo wake kwa swali lile.

“Utajisikiaje ukipoteza wazazi wako?” Aliuliza Vanessa kwa sauti ya kikakamavu.

“Nimekwishawapoteza. Roho iliniuma sana.” Akajibu Mama yule na kumtazama Vanessa.

“Na hawa watoto zako unadhani watajisikiaje wakikupoteza wewe?” Akauliza tena Vanessa.

“Nadhani watakubali matokeo kwani kazi ya MUNGU haina makosa.” Akajibu.

“Vipi kama utapotea machoni mwao huku wao wakitazama jinsi unavyochinjwa kwa jambia?”

“Nani wa kufanya hayo yote?” Aliuliza yule mama huku akicheka kuonesha dharau juu ya kauli za Vanessa.

“Unadhani hawa watoto watavumilia kumuona mama yao kachinjwa halafu muuaji anaendelea kuvuta hewa bila ushuru?”

“Binti kwani unashida gani?” Akiuliza yule mama kwa wahka.

“Nina shida na shingo ya Diana Winto na ya Silvano Buje.” Macho ya Vanessa yakamtazama yule mwanaume mrefu baada ya kutaja jina la Silvano Buje.

Macho ya Bwana yule yakamtoka pima. Hakujua Vanessa katoa jina lake wapi kwa sababu hakuwahi kulitoa jina hilo nje. Hata wale watoto hawakujua jina la mtu anayeishi na mama yao.

“Una matatizo ya akili wewe?” Aliuliza Diana.

“Unakumbuka siku ile porini ulimfanya mama yangu. Unakumbuka? Unamkumbuka Vivian Cilas?” Vanessa aliuliza na macho ya Diana yakatumbuka na saa hiyo akaanza kupiga kelele kuwaita walinzi.

Badala ya kuitikiwa, ukimya ndio ukatawala katika jengo lile. Walinzi waliomleta Vanessa, walidunguliwa kwa risasi za Al Bashir.

Na pia kuna walinzi kadhaa walikuwa kwenye kijumba kidogo chenye kuendesha mitambo ya kung’amua wezi, nao walikuwa wamekwishajipatia risasi za vichwani. Kimya kikachukua nafasi katika mji ule na wakati huo Peter alikuwa anasogelea geti la jumba lile, mali ya waziri mstaafu wa wanawake na watoto.

“Nadhani umekwishamkumbuka. Nimekuja kumlipia kisasi.” Akaongeza maneno yake Vanessa.

“Ohoo. Kwa hiyo wewe ni Vanee. Kibinti cha yule mbwa.” Aliongea yule mama kwa sauti ya kukera.

“Ukimuita tena mama yangu jina hilo, nakuua sasa hivi.”

“Unasemaje we malaya?” Mtoto mmoja ambaye alionekana ni mkubwa kuliko wengine, alimuuliza Vanessa swali huku akielekea pale alipokaa Vanessa.

“Kaa mbali we mshenzi. Usiingilie huu ugomvi,” Aling’aka Vanessa kwa hasira na yule kijana hakuacha kwenda alipoakaa Vanessa. Kabla hajafika alipikusudia, risasi moja ya kichwa ilitua kichwani kwake kumfumua ubongo.

Familia ile ikashtuka kwa lile tukio na baada ya kutuliza akili zao, wakaona ni Vanessa ndiye mleta shida. Bila kufikiri, watoto waliyobaki wakachomoka walipokuwa wamekaa na moja walikweanza kwenda alipo Vanessa lakini hawakumaliza safari yao, kila mmoja alipokea risasi yake kwenye kichwa. Watoto wa familia ile wakateketea kwa njia hiyo na kilio kikubwa kikapazwa na yule mama na wakati huo Slivano alikuwa kimya akitikisa kichwa chake kushoto kulia akionesha kusikitika.

“Unataka nini binti. Nitakulipa.” Alilia mama yule kwa uchungu huku anampigia magoti Vanessa.

“Naitaka roho ya mama yangu. Kama hauna, naitoa yako” Vanessa akajibu.

“Nilikwambia Diana. Tungemaliza wote siku ile. Ukabisha, ona sasa.”Silvano akiongea huku mguu wake mmoja akikanyaga chini kama muimba kwaya.

“Ilipaswa tuteketeze familia nzima ya Mzee Gomez ili leo hii tule matunda ya kazi yetu. Lakini tulifanya kosa kuwaacha, hasa huyu mdogo. Sasa naona wazi badala ya kula matunda ya kazi nzuri, tunaelekea kula matunda ya unyama wetu,” alizidi kuongea Silvano. Diana, mama aliyetoa amri kwa Silvano ili mama wa Vanessa achinjwe kama kuku, aliuacha mwili wa mwanaye ambaye alikuwa kampakata kwenye mapaja yake, kisha akanyanyuka na kukaa kochini macho yakiwa mekundu sababu ya kulia.

“Hatuna cha kupinga kwa sababu ukiua kwa upanga, basi utakufa kwa upanga pekee. Niliua kwa upanga, adhabu yangu ni upanga.” Aliongea Mama yule huku kichwa chake kakiinamisha chini. “Niliweka ulinzi wote huu kwa sababu nilijua ipo siku mtoto huyu atakuja kunitafuta. Hatimaye yametimia.” Diana Winto aliongea kwa kukata tamaa.

“Na kweli yametimia.” Vanessa aliongea na kutoa kipaza sauti kidogo alichokuwa kakibana kwenye sidiria. “Niletee dhana zangu Pitty.” Aliongea Vanessa kwenye kinasa sauti kile na baada ya dakika tatu, Peter alikuwa ndani ya jengo lile akimkabidhi Vanessa mapanga mawili yenye makali pande zote.

Peter alimtazama Vanessa kisha akakumbuka mbali sana. Akakumbuka tangu akiwa mtoto alipoambiwa na baba yake kuhusu kisasi na roho ya kisasi.

“Mtu mwenye roho ya kisasi, ni hatari kuliko katili lile chinja chinja. Ni heri mara mia moja ukutane na duma mwenye njaa porini, utakimbia kadiri ya uwezavyo na unaweza kupona kuliko kukutana na mtu mwenye kisasi na wewe. Kama kuna mtu anakisasi na wewe, ni ngumu kumkimbia athirani. Huwezi kumkimbia mwenye roho iliyojaa kisasi na wewe. Hadi atimize kusudio lake, ndio utakuwa katika amani. Sasa yategemeana, amani unaweza kuipatia kaburini au akakuonea huruma mwenyewe.” Maneno hayo yalipita kichwani kwa Peter kama mshale wa kimakonde. Akiwa anamtazama Vanessa aliyekuwa kazama kwenye chuki mbele ya wale watu wawili, maneno ya baba yake yakazidi kutambaa kichwani.

“Njia ya kumshinda adui si kisasi bali hekima na maarifa. Kisasi ni njia nyingine ya kuongeza maadui hasa pale utakapogundulika kuwa umefanya kosa au kulipa kisasi. Hakuna jambo baya kama kisasi, na kamwe usiwe mbele kushabikia kisasi kwani hupoteza malengo na sifa za mlipaji. Lakini kwa upande mwingine, kisasi uiweka roho katika amani hasa kwa wenye roho hiyo. Nakushauri mwanangu Peter, hata litokee jambo gani kati yetu, kisasi weka kando. Kuwa adui wa kisasi kama ulivyo adui wa kifo na magonjwa. Kuwa wewe kama wewe, usiruhusu moyo wako utawaliwe kwa visasi. Usiruhusu kuapa kila mara kuwa lazima utimize kitu fulani kulipiza jambo fulani. Yaache ya nyuma yapite, ishi dunia inayokutazama. KAMWE KISASI KISIWE LENGO LAKO KATIKA MAISHA. ISHI MAZINGIRA AMBAYO HAYANA VISASI, UTAFIKA PAZURI.” Peter alimtazama Vanessa na kutambua kuwa binti yule alikuwa amedhamiria kutimiza azma yake ya kulipa kisasi.

Hakuwa na jinsi licha ya kumsisitiza sana mpenzi wake aachane na roho ile. Peter akageuka na kuanza kuelekea kwenye lango la kutokea pale sebuleni. Wakati anatoka, alisikia sauti ya Vanessa ikiongea na wale aliodhamiria kuwatenda.

“Siku zote naamini kifo ni kosa letu kama tunavyoweza kupika chakula kibichi. Kifo ni kosa dogo sana ambalo unalitenda. Ni sawa na wakati unaruka sarakasi halafu ukafanya kosa kwa kujipindua kiajabu ajabu, ukadondokea kichwa. Na kifo kipo vivyo hivyo.” Vanessa aliongea huku akiwa anaanda moja ya panga lake. “Mama yangu alifanya kosa dogo sana lililosababisha kifo chake. Kosa lenyewe ni kukupenda wewe.

Mama alikupenda kuliko alivyotupenda sisi na alikuona kama MUNGU mtoto licha ya kuwa yeye ndiye alikuwa anakusaidia. Hilo ndio kosa alilolifanya mama. Kosa hilo, likapelekea kifo chake.

Kosa hilohilo, ndilo linakufanya wewe ufe pamoja na uzao wako. Ulifanya kosa kuniacha hai na ulifanya kosa kumuua mama. Ulifanya kosa kubwa kuniacha niendelee kupumua na wakati ulikwishamuua mama. Na kosa lako hilo, mimi siwezi kulirudia. Nitakuua na kulipua kabisa nyumba yako. Nadhani nitapumzika kwa amani baada ya hapa.” Maneno hayo ya Vanessa yalipenya masikioni kwa Peter na kijana yule aliminya kitasa ghali cha mlango wa jumba lile. Ulipofunguka, akatoka nje na kuwaacha wale wazee wakiwa na Vanessa. Alijua kuwa hawawezi kumdhuru Vanessa kwa lolote kwani Vanessa alikuwa ni hatari kuliko wale walivyodhani.

“Kama ningekufa bila kukuona wewe mtoto, ningetangaza hadharani kuwa unisamehe kwa yote. Nimeua wengi kwa vifo vya kutisha, lakini nakubali kuwa mama yako nilifanya kosa kumuondoa duniani. Hakustahili yule mwanamke. Hakustahili hata kuguswa na manyoya ya mbwa bali alistahili ulinzi wangu kwani wema alionipa Vivian, hata rais wa nchi hii hajawahi kunipa. Nisamehe Vanessa.” Aliongea mama yule kwa uchungu wakati huo Silvano alikuwa akitikisa kichwa kwa masikitiko.

“Nitakusamehe nitakapoona damu yako ikimwagika na ukilia kwa uchungu. Hapo nitakusamehe.” Maneno hayo yalimshusha Diana kwenye kochi na kupiga magoti kisha akachana blazia aliyoivaa na kifua chake kikawa wazi na wakati huo alinyanyua uso wake juu akionesha shingo yake.

“Kama kifo ndio msamaha wangu, nipo tayari kukipokea,” Mama yule aliongea kwa sauti ya kumaanisha na Vanessa alisogea hadi nyuma yake na kukamata nywele ndefu za yule mama. Akaweka upanga wake kwenye shingo ya kizee aliyopewa Diana, akaanza kuikata kama anakata shingo ya kuku.

“Hii ni kwa mama yangu.” Damu ziliruka huku na huko na kuchafua sebuke lote la mama yule. Kazi ilifanyika kimya kimya, mama yule hakutoa sauti ya kilio wakati wa tendo lile. Vanessa alikuwa mwenye nguvu kupita maelezo.

Akaubwaga mwili wa Diana na yeye akabaki na kichwa cha yule mama kikitiririka damu kama nguo inayoanikwa kambani bila kukamuliwa.

Akamtazama Silvano, mlinzi wa Diana aliyekuwa kainama tangu alipomaliza kuongea maneno yale ya kumkumbusha Diana kuwa walifanya kosa la kumuacha Vanessa tangu utotoni.

Vanessa akakiinua kichwa cha mama yule na kumuonesha Silvano.

“Zamu yako we mbwa,” Aliongea kwa sauti ya ukatili ambayo ilimfanya Silvano anyanyue kichwa chake na kumwangalia yule mtoto wa kike akiwa akakamata kichwa cha hawara wake. Silvano akatabasamu tabasamu la kukereka kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko.

“MUNGU hakumuumba binadamu kuwa tishio au Shetani. Shetani anatengenezwa. Wewe ni Shetani uliyetengenezwa, sawa na mimi nilivyotengenezwa. Sijilaumu mimi wala kukulaumu wewe, nawalaumu waliotutengeneza. Kama si uroho wa madaraka ya sisi waafrika, leo hii mimi ningekuwa mtu mwingine tofauti na kuwa muuaji.” Mzee Silvano aliongea kwa uchungu maneno hayo. Akaendelea, “Afrika bara langu, Kongo nchi yangu.

Kwa sababu ya uroho wa watu weupe kutaka kila kitu kiwe chao, leo hii mimi nikawa muuaji ili kujipendekeza kwao. Nikawa kibaraka kwa wenye uroho wa mali na wanyonyaji wa dunia hii. Tulitaka kila kitu tukimiliki sisi, zikiwemo roho za zisizo na hatia. Tukasahau malipo ni hapa hapa duniani. Sisemi kukuomba msamaha, nakufungua ubongo wewe usiyejua unamtumikia nani, kama umeamua kuishi maisha ya risasi, basi risasi ndio itakayokumaliza. Nilishi kwa upanga, nakufa kwa upanga.” Alimaliza Silvano na kuinamisha kichwa kama mwanzo. Vanessa alikuwa kafura kwa hasira pale alipomtazama mzee yule, akakumbuka jinsi alivyochomoa panga na kukata shingo ya mama yake kipenzi, mama yake mzazi, mama yake wa pekee, kisha kichwa kile wakatupiwa mbwa wakitafune. Akafikiria maneno makavu aliyoambiwa dakika chache zilizopita. Hasira zikamzidi, akajikuta anafanya maamuuzi ya ukweli na bila uoga.

“Unadhani mimi ni wewe?” Vanessa aling’aka kwa sauti ya juu na kusogea pale alipoinama mzee yule, akanyanyua panga lake juu na kulishusha nyuma ya shingo ya Silvano, akakata shingo ile kwa nyuma na kichwa kikadondoka chini huku mwili wa Silvano ukiruka juu na baadae kutua kwenye kochi huku damu zikichuruzika kwenda hewani toka katika shingo ya Silvano. Ni sawa na bomba lililopasuka halafu maji yakawa yanapaa angani. Ilitisha, hakika nakwambia.

Mwili wa Silvano ulikuwa ukijaribu kupigania uhai wake lakini ulikuwa kama unacheza mchezo wa makida makida, mwisho wake ulikakamaa na kutulia pale kwenye kochi. Silvano akawa kafa kwa upanga.

Vanessa akameza mate na kushusha pumzi ndefu, akatupa panga lake chini na kuanza kuelekea katika mlango wa kutokea.


“Mmefanya ile kazi,” Vanessa alimuuliza Peter baada ya kutoka nje.

“Ndio. Tumeimaliza zamani sana. Tullikuwa tunakusubiri wewe,” Peter alijibu kwa upole.

“Okay. Tuondokeni,” Vanessa alishauri huku akiwa kiongozi wa Peter katika msafara ule kuelekea alipokuwepo Al Bashir.

“Wapo wapi wale walinzi na mbwa wao?” Aliuliza Vanessa wakati anapita geti la jumba lile.

“Nimewakusanya na kuwaweka huko kwenye chumba cha mitambo,” alijibu Peter na wakati huo alikuwa anamtazama Vanessa kwa makini hasa kwa alivyokuwa kachafuka kwa damu za binadamu. Moyo ukamlipuka Peter licha ya yeye pia kuwa mfanya wa yale matendo kila alipotumwa lakini alichokifanya Vanessa, kama ni tunzo basi yapaswa apewe mgodi wa almasi.

“Safi. Nadhani historia imewekwa leo. Sasa naweza kufa.” Aliongea Vanessa huku akiwa katika mwendo wa kasi kutoka eneo lile.

Walifika kwa Al Bashir na wote wakatoka eneo lile usiku uleule. Wakaingia porini kwa kutumia Jeep waliyokuwa wameiacha mbali kabisa na eneo lile.

Huku nyuma baada ya masaa mawili ya wao kuondoka, mlipuko mkubwa ulifumuka katika jengo la Bi. Diana Winto. Mabomu matatu aina ya C4 yaliyopandwa katika jumba lile, yalitosha kabisa kuiharibu kasri lile na kuchoma vyote vilivyomo. Hata askari walipokuja kuzima moto, waliambulia mafuvu na uchunguzi ulipofanyika, waligundua kuwa wale maiti walipigwa risasi na wengine kuchinjwa. Swali likabaki ni nani aliyefanya yale?

Wakiwa kwenye Jeep ya jeshi ambayo haijazibwa, Vanessa akiyekuwa safi baada ya kuoga na Peter kwenye mto mmoja uliopo kwenye misitu mizito ya Kongo, misitu ambayo waasi wengi wa Kongo hujificha humo walikuwa wakicheka kwa furaha na wakati huo Al Bashir akiwa katika usukani naye akiwa katika hali sawa na ya wale wapenzi wawili.

“Kama Kamanda Bonito atamaliza tofauti zetu, nitakuoa Vanessa na Bashir atakuwa bestman wangu.” Peter aliongea kwa furaha na Vanessa alimlalia Peter begani kwa deko. Safari ilikuwa hivyo kwa dakika nyingi sana. Cheko, furaha na faraja vilitawala wakati wanapita katika msitu huo wa Kongo.

“Hey Bashir.” Vanessa alimuita Al Bashir ambaye alikuwa makini katika kuendesha ile Jeep. Akaitika kwa kutikisa kichwa.

“Sisi wazijua historia zetu, lakini yako hatuijui. Ni maisha gani uliyapitia wewe?” Vanessa alimtwanga swali Al Bashir ambaye alitabasamu kidogo kabla hajaanza kusimulia kilichotokea katika maisha yake.

“Baba yangu alikuwa mwanajeshi wa jeshi la Somalia. Mama yangu alikuwa na kazi ya kutulea sisi tuliokuwepo watano. Mimi nikiwa wa tatu na miaka yangu nane na wadogo zangu mapacha wa mwaka mmoja kila mmoja. Tulikuwa tunaishi Mogadishu. Hali ya maisha ilikuwa mbaya kwetu, mbaya sana tu licha ya baba yetu kuwa mwanaheshi mtiifu wa jeshi la nchi ile. Utiifu huo ukawa ndio sababu ya baba yangu kuonewa. Mshahara akawa hapewi na akipewa si ule anaotakiwa kuupata. Alidhurumiwa mara kwa mara na wenye madaraka lakini bado aliipenda kazi yake na mara kwa mara aliwachukua kaka na dada yangu na kwenda nao mahala kwa ajili ya kuwapa mbinu za kijeshi. Nilitamani sana na mimi niwe miongoni mwa wakubwa zangu lakini baba alinikataza akinisisitiza kuwa ipo siku atanichukua.” Wakati Al Bashir akiongea Vanessa na Peter walikuwa kimya wakimtazama kijana yule wa Kisomali akisimulia maisha yake.

“Nakumbuka siku moja baada ya kurudi na wale wakubwa wangu baba alifoka sana huku akilalamika kuwa anachowafundisha wale watoto wanakipuuzia……..”

MIAKA KADHAA NYUMA.

“Lakini mume wangu, hawa watoto wamesema wanataka kuwa wanajeshi hapo baadae ama unataka kuwalazimisha tu.” Sauti ya mama aliyekulia katika dini hasa kutokana na mavazi yake, ilikuwa ikisikika vema kwenye masikio ya mumewe.

“Fatuma, hawa wanatakiwa kujua njia za kujilinda. Nchi yetu ipo pabaya sana kwa sasa. Muda wowote tutakuwa katika vita nzito, nani wa kuwalinda hawa wadogo? Eeh! Embu fikiria Fatuma.” Mumewe alimjibu kwa swali mkewe aitwaye Fatuma.

“Hapana Hamad, japo sijui kitakachotokea, lakini waache watoto wawe na uhuru wa maisha yao. Allah hawezi kutuacha katika mateso haya tuliyonayo na kututumbukiza kwenye mateso mengine. Wapeleke watoto wapate elimu.” Aliongea Fatuma kwa sauti ya upole huku akimbembeleza mmoja wa pacha aliowapata mwaka mmoja uliyopita.

“Ohoo, unataka waende shule. Unataka waende shule, si ndio eeh. Wakajifunze elimu ya ukoloni. Basi hamna tabu. Nitamchukua Bashir kwa ajili ya mafunzo.” Maamuzi hayo yalifanyika baada ya wiki. Mzee Hamad, mwanajeshi wa Somalia, aliwapeleka shule kaka na dada wa Al Bashir na kumchukua Bashir kwa ajili ya mafunzo madogo ya jeshi. Hakumpa magumu sana bali yale ya kujihami na kutumia silaha za kila aina.

Al Bashir alipenda sana kile ambacho baba yake alikuwa anamfunza na kila siku alionesha nyota ya mafanikio kwa kile ambacho anafundishwa.

“Bashir.” Siku moja alimuita kwa utaratibu mwanaye, alikuwa Hamad. Bashir akaitika kwa kumtazama baba yake usoni. “Umeona hii?” Alimuuliza huku akitoa bunduki ndefu maarufu kama sniper rifle au bunduki ya mdunguaji. Bashir akaafiki kuwa kaiona.

“Huyu ndiye mke wangu wa ukweli. Lakini usimwambie mama yako, sawa?” Aliongea huku katabasamu Mzes Hamad, na Bashir alikubali kuwa hatotoa siri. “Huyu ndiye nayempakata kwa muda mrefu sana. Nampenda sana.” Aliibusu ile bunduki. “Nataka nikupe wewe mwanangu. Huyu atakuwa mtoto wako japo mimi ni mke wangu. Sawa?” Akaaafiki tena Al Bashir.

Mzee Hamad akaaibongonyoa yote kisha akaanza kumfundisha Al Bashir jinsi ya kuipanga.

“Jeshi la nchi hii haliniachi kwa sababu mimi ndiye mtaalamu wa hii bunduki kuliko yeyote. Na ukijua kuipanga hii, hata upewe bunduki ya aina gani, huwezi kushindwa kuipanga.” Aliongea huku akimalizia kitu cha mwisho kukiweka kwenye bunduki ile.

Akaanza kuipangua tena kisha akaanza kumuelekeza Al Bashir kwa makini kabisa jinsi ya kupanga bunduki ile.

“Hiyo ndio sababu ya mimi kuwa hivi leo hii. Baba yangu linifunza mengi sana kuhusu silaha hasa sniping. Baada ya kuniona nimekuwa poa aliacha kazi hiyo ya kunifundisha na kunipeleka shule kwani mama alitaka sana tusome kuliko kukalia silaha tu.” Alikuwa akiwahadithia wakina Vanessa. Al Bashir.

” Sikujua kama baba alikuwa anauwezo wa kinabii ama nini kwani vita kubwa ilitokea na tukawa tunapigwa na kuuawa kama kuku. Ndugu zangu wote waliuawa na jeshi la serikali licha ya wao kulazimishwa kukamata silaha kwa ajili ya mapambano. Walikufa kikatili kaka na dada zangu. Wale wadogo zangu mapacha, pamoja na mama, ikawa kazi yetu mimi na baba kuwalinda. Tuliwalinda lakini mwisho wake baba aliuawa na pia mama. Wale wadogo zangu sijui walipelekwa wapi na lile jeshi haramu lililoibuka nchini kwetu.” Alilalama Al Bashir. ” Baadae ikabidi nikimbie na kuingia Uganda na baadae Tanzania, kisha Kongo ambapo nilipata nafasi ya kulelewa na baadae nikaletwa hapa Senegal nikiwa mdogo tu. Lakini baba yangu na mama yangu waliuawa kwa kunyofolewa utumbo wao kwa mundu kali kabisa.” Alimaliza hadithi yake Al Bashir na wote wakashusha pumzi ya nguvu.

“Sipati picha ulikuwaje wakati wazazi wako wanapoteza maisha. Mimi mwenyewe sikuona wakati wazazi wangu wanauawa, lakini najua ilikuwa ni picha ya kusikitisha sana. Sasa sipati picha kwako ambaye uliashuhudia. Si kusikitisha pekee bali ilitisha,” Aliongea Peter huku macho yake anatazama mbele gari linapoelekea. “Lakini kwa kuwa upo nasi leo, sidhani kama picha ile bado imetawala kichwani mwako japo najua ipo kweli. Jaribu kusahau Bashir,” Alishauri Peter.

“Ndicho nachojaribu kukifanya kwa sasa. Naangalia mbele katika kulikomboa bara langu toka kwenye hivi vita vikavu vya wenyewe kwa wenyewe, naamini ipo siku tutaishi kama tupo ahera.” Aliongea Al Bashir huku akiendelea kuendesha gari.

“Naamini tutafanikiwa.” Peter aliongezea.

“Ndio tutafanikiwa. Lakini Vanee, nakuomba kilichotokea jana, uachane nacho kabisa katika maisha haya. Pigana na kinachokutazama na si kilichokukwaza hapo kale. Maisha si maisha kama roho yako itajaa kutu ya visasi. Hutofanikiwa kulipa visasi vyote katika maisha yako. La msingi ni kutazama ya ndwele pekee.” Alimshauri Vanessa, Al Bashir.

“Ilikuwa ni lazima nifanye vile Bashir. Kuna muda ili mzigo wa fikra uutue, ni lazima ufanye kile ambacho unahamu ya kukifanya. Bila kufanya haya ya jana, ya kesho kwangu yangeweza kuwa magumu sana. Kama wanaishi bila kumfikiria MUNGU atawafanya nini, basi yabidi nasi tuishi katika njia hiyohiyo. Kwangu sijaona kosa ambalo nimelifanya, nimepeleka roho zao panapohusika kama wao walivyozipeleka roho ambazo hazina hatia huko zilipo. Na nadhani, Mama na Baba wanajisifu kuwa na mtoto kama mimi.” Aliongea Vanessa kwa sauti ya msisitizo.

“Upo sahihi. Nadhani sasa tutafanya kazi kama inavyotakiwa.” Al Bashir aliongea na wakati huo gari lao lilikuwa linachanja mbuga nzito iliyotapakaa wanyama wa kutisha, wadudu wa kustaajabisha na miti iliyofungamana kiasi kwamba giza kubwa lilikumba sehemu ile.


“Kazi nadhani imekamilika,” Kamanda Bonito Muchakila, alikuwa akiongea huku meza iliyopo mbele yake ikiwa imewekwa makaratasi na mafaili mbalimbali, lakini kubwa zaidi alikuwa kapandisha miguu yake juu ya meza hiyo na sigara akiwa anaipuliza hewani kwa mbwembwe.

“Ndio Kamanda. Sasa tunaweza kufanya mengi mengine,” Alijibu Vanessa ambaye alikuwa mkabala na Peter kushoto, kulia akiwepo Al Bashir. Walikuwa wamekwishafika katika kambi ya Born To Die na jambo la kwanza kabisa walifika katika ofisi ya Kamanda wao, kiongozi wa kambi ile.

“Okay. Safi sana. Sasa kuna mengi yanatakiwa kutokea ndani ya wiki hii. Mkataba wa amani umeshasainiwa, na siku tatu zijazo tutakuwa na mkutano wa adhara pamoja na Rais wa nchi. Waandishi wa habari na watu wengi watakuwa wanatazama na kusikiliza tunachokiongelea.” Bonito aliongea kwa makini kabisa. “Sasa ulinzi wenu ni muhimu, ninyi ndio kila kitu katika mkutano huo. Naomba mpange kamati ya ulinzi na baada ya siku tatu, tutaenda kwenye huo mkutano. Vifaa maalumu vilivyoendelea, vimekwishakuja. Vitasaidia katika ulinzi na kujihami kama mambo yatakwenda hovyo.” Alimaliza maelezo mafupi Bonito.

“Sawa Kamanda. Ni vifaa toka wapi?” Aliuliza Peter.

“Kutoka Urusi. Kwa wale waliokuja kutupa mazoezi.” Alijibu Bonito.

“Sawa mkuu. Lakini ni muda wa kutangaza amani na si kushiriki tena kuingiza silaha na vifaa vyao vya maangamizi. Naomba ulifikirie hili,” Alishauri Peter wakati huo Bonito alikuwa anamtazama kwa makini.

“Baada ya kuingia madarakani, ndicho kitu cha kwanza nitakachokifanya. Hamna silaha, hamna wazungu kutuingilia. Sasa hivi wacha tujikombe,” Bonito alijibu.

“Lakini wakati unapanga hayo, kubali pia kugeukwa na hao utakaowasaliti,” Vanessa naye alishauri jambo ambalo lilizama vema katika kichwa cha Bonito.

“Nendeni mkaandae kikosi cha Ulinzi. Peter simamia yote hayo.” Baada ya kuwazua, Bonito alishauri jambo hilo na wote kwa pamoja wakaafiki na kutoka huku wakimuacha Bonito katika njia panda.


ITAENDELEA

Born to Die Sehemu ya Tano

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment