Saa la 25 Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Saa La 25

Saa la 25 Sehemu ya Tano
Saa la 25 Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE (AMATA GA IMBA)


Simulizi : Saa La 25

Sehemu Ya Kwanza (1)

Dar es salaam

Giza liliendelea kupambana na mwanga wa taa zilizoko kwenye majumba ya wahindi katikati ya jiji la Dar es salaam, barabara hii ilikuwa nyeupe kabisa ni magari machache tu ambayo yalikuwa yakipita kwa wakati huo, hakukuwa na mbalamwezi wala nyota hazikuonekana kabisa, ulikuwa usiku wa mawingu mazito na hali ya kaupepo iliendelea kupunguza joto la jiji hili ambalo husifiwa kwa hali hiyo na kila mtu aliyewahi kufika hapa. Wengine walikuwa bado kwenye starehe zao muda huo, wakila maisha kwa kucheza muziki au kula na kunywa vinywaji aina aina, pesa ziliteketezwa tu kwa kugawa kwa wauza miili katika majumba hayo, hata hawakujua kuwa kuna kufa baada ya maisha hayo, hiyo kwao ilikuwa ni hadithi ya kufikirika tu, wengine walikuwa wako katika majumba ya filamu wakiburudisha macho yao kwa kuangalia maigizo haya ya kizungu yaliyooneshwa ka njia ya picha kwa kutumia chombo kilichofanana na baiskeli iwapo kwa fundi, wengine wakiwa wamelala wakifurahia raha ya magodoro na upepo wa mapangaboi yaliyofungwa katika mapaa yao yakining’inia na kuwapa upepo mtamu ili tu kupunguza joto la ndani, wengine wakiwa mahospitalini wakiteseka kwa magonjwa, wakiomba kila siku ee Mungu utuchukue, wengine walikuwa katika kutimiza wajibu zao za kazi katika kulijenga taifa. Maisha yaliendelea kila kona kwa jinsi zake, kwa kila mtu kwa namna yake.

Usiku huo hali haikuwa hivyo kwa msichana Tuntufye, ulikuwa usiku wa mateso na mawazo mengi, usiku uliojaa majonzi na machozi, ‘kwa nini mimi?’ Swali lililojirudia mara kwa mara moyoni mwa msichana huyu mdogo, mbichi lakini asiye na kwao, asiye na pakuishi, asiyejua lolote juu ya maisha, Ombaomba aliyekuwa akiomba kila siku katika barabara ya Bibi Titi jijini Dar es salaam. Tuntu kama wenzake walivyozoea kumwita hakujua hata mama yake yuko wapi maana miaka michache nyuma walirudishwa kwao kutokana na amri ya mkuu wa mkoa ili kukomesha aibu hii ya Ombaomba katika jiji hili, jiji la kimataifa linalofikwa na wageni aina aina ambao macho yao labda yanapofuka yakiona ombaomba wakati huko walikotoka wamejaa kuliko hapa. Akiwa amekaa kwa kujikunyata huku akilia kwa vikwifukwifu katika kiambaza cha ukuta wa uzio wa makaburi ya Kisutu, Tuntu alikuwa na maumivu makali sana katika sehemu zake za siri, hakuwa na msaada, hakujua amlilie nani, kila alipoyaangalia makaburi yale alitamani labda mojawapo lingekuwa limemfunika yeye mateso haya yasingempata, uchungu, hasira, chuki, gadhabu, kisasi nivitu ambavyo vilichanganyika moyoni mwake na kuleta wazo moja tu ‘kifo’ , lakini kila alipotaka kuamua hilo alimuwaza mama yake kipofu ambaye sasa hakujua hata yuko wapi, kafa au mzima, alimkumbuka na mdogo wake wa kiume Malogo ambaye mara ya mwisho alimuacha na mama yake akimnyonyesha karibu na njia panda ya barabara ya Ohio na Bibi Titi yeye akiwa anaombomba katika magari yapitayo eneo hilo ndipo aliporudi na hakuwaona tena mama na mdogo wake huyu aliyewapenda sana, tangu hapo Tuntu aliishi maisha ya tabu ya kulala vibarazani, hakuwa hata na nguo ya kubadilisha alikuwa ‘Chokoraa’ faraja yake ilikuwa tu ni watoto wenzake ambao wote walikuwa na hali kama yake, pesa kidogo anazopata ndiyo hizo apate chakula na wakati mwingine wenzake wa kiume umnyang’anya na kumuacha akilia bila msaada, wapita njia walimpita siku zote hakuna hata ambaye aliguswa juu ya msichana huyu. Tuntu, msichana wa mdogo wa miaka tisa alizoea maisha haya ya kuombaomba tangu anapata akili mpaka wakati huo ambapo alishaanza kila dalili ya kubalehe, hakuwahi kulala kitandani wala kula chakula kizuri kama binadamu wengine, alipojiangalia yeye na watoto wengine waliopita eneo hilo na wazazi wao au wadada wa kazi wakipelekwa shule au hata kutembea aliona kuwa kati yake na wao kuna nafasi kubwa sana ambayo yeye hawezi kuwafikia wao na wala wao hawawezi kumfikia yeye, aliwaangalia kila siku na kukata tamaa.

Tuntu alijaribu kunyanyuka kutoka pale alipokuwa amekaa lakini ilikuwa ni vigumu sana kwani alihisi hata kiuno kama kimeteguka, alijivuta kwa kutambaa taratibu kama kiwete mpaka upande wa pili wa barabara kwenye kibaraza ambako ombaomba wengine walikuwa wamejilaza hapo. Akajiangalia vizuri sehemu zake za siri ndipo alipogundua kuwa ameumizwa vibaya sana kwani damu nyingi zilikuwa zikimtoka, Tuntu alikuwa amebakwa, alianza kulia upya hata kilio kile kilimuamsha mama mmoja aliyelala jirani na hapo, mama huyo alipomuuliza kulikoni Tuntu alimueleza mkasa mzima, mama yule alisikitika sana lakini atamsaidiaje, alimwangalia Tuntu jinsi alivyoumizwa hakuwa na la kufanya alimsafisha kwa maji machafu aliyokuwa nayo katika chupa ya plastiki na kumuweka matambala angalau yazuie damu kuendelea kutoka, zaidi ya hapo alisikitika tu kwa maana hakujua la kufanya. Tuntu alilala usingizi mzito jirani na mama yule akiwa amejisitiri tu na maboksi kujizuia japo na mbu wenye hasira wanaotafuta damu kwa nguvu kila kuchwapo. Usiku ulioandamana na ndoto za majinamizi ukapita kwa tabu sana katika maisha ya Tuntu.

€ € € €

Kajua katamu ka mashariki kalichomoza pande za baharini, hatimaye mji nao ukaanza kujazwa na watu na magari ya aina aina, lakini hivi vyote havikumpa tumaini kabisa Tuntu, alijikalia hapo kajikunyata na kulaza kichwa chake kwenye magoti yake akijaribu kufikiri tu kuwa mama yake na mdogo wake wako wapi lakini hakupata jibu aliambiwa tu na wenzake kuwa ‘wamechukuliwa kwenye lori na wengine wengi wakapelekwa kusikojulikana,’ kila alipokumbuka hayo machozi yalimtoka upya kabisa.

“Tuntu! Leo huwendi kuomba?” mtoto mwenzake alimuuliza lakini Tuntu alijibu tu kwa kunyanyua mabega yake juu kuashiria ‘siendi’ . Mawazo ya Tuntu yalisafiri kwenda mbali sana asipopajua, akiwaza na kufikiri hili na lile lakini zote zilikuwa ni ndoto za Alinacha tu, ndoto zisizokuja kuwa kweli hata siku moja, mimi na wewe tusingeweza kujua ndoto ile ilikuwa ni juu ya nani au ya nini. Watoto wa Kihindi walipita eneo hilo wakienda shuleni wengine kwenye baiskeli wakifurahia maisha na wengine kwenye magari mazuri mazuri ya baba zao wakiwa wamening’inia madirishani wakiangalia nje jinsi maghorofa na watu wakirudi nyuma badala ya kwenda mbele. Wao ndani ya magari na hawa masikini wakiwa kwenye viambaza vya nyuma kuwakumbatia na kuwanyonyesha watoto wao huku wale wakubwa kidogo wakienda kuomba kwa mabwanyenye hao ili kupata angalau cha kuweka tumboni ‘sina!’ ilikuwa ni jibu lililotolewa na walio wengi wkati kwenye vidroo vya gari zao kulionekana manoti ya mejaa, ama kweli ‘tajiri na mali yake masikini na watoto.’

Maisha yalikuwa yakibadilika kama taa za kuongozea magari zilivyobadilika, nyekundu ‘simama’, kijani ‘nenda’, njano ‘kaa tayari ama kusimama au kuendelea’ lakini kwa ombaomba hawa daima ilikuwa ni nyekundu tu haikuweza wala haikuwa na dalili za kubadilika, maisha yasiyo na kesho ili mradi kilipatikana cha kula hata kama hakikustahili au hakikufaa kwa afya ya binadamu kama wataalamu wa afya wanavyosema, lakini ‘Mungu aliwalinda’.

Safisha safisha jiji ilifanyika kwa amri ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Mheshimiwa Yusuph Makamba, kurudisha ombaomba wote kwao, serikali ilitoa behewa kadhaa za treni ya reli ya kati kuonesha kuwa inawajali lakini kwa wenye akili ilikuwa ‘je wanaenda kwao kufanya nini!’ ilishangaza kwa kuwa walikuja mjini kutafuta ridhiki yao kwa mtindo huo,leo wanaonekana takataka, wanarudishwa kwao na hakuna njia mbadala ya kuwatoa katika umasikini huo wa kutupwa, serikali ikasahau kuwa kule inakowapeleka ‘kwao’ ndio makao makuu ya nchi japokuwa wao wamekaa na matumbo yao huko Dar es salaam na hawataki kuhamia makao makuu ya nchi, Dodoma. ‘Nani akakae Dodoma?’wengine walijiuliza ‘yeye mbona yuko Msasani’ mwingine alimalizia.

Dar es salaam ndiyo kila kitu, nani kakudanganya, kila mtu aliyezaliwa Tanzania, nje ya Dar lazima alale akiota juu ya jiji hili, jiji la raha lenye kila kitu. Vijana kutoka pande mbalimbali za nchi walipigania kufika Dar, ukitoka Dar kwenda kijijini kwako wewe ndio ‘Digala’ mjanja wewe, kila kitu unajua wewe, hata miondoko na mavazi utabadilisha, utaheshimiwa na kila mtu hata balozi wako wa nyumba kumi kisa nimetoka Dar, kila mtu kila kona, Dar.

Jiji la Dar lilibeba kila aina ya watu, baada ya vijana na mabinti kukimbilia katika jiji hili la maraha wakiamini kuwa huko hakuna shida ya maisha, pesa bwerere walifanya kila mbinu kulifikia jiji hilo ‘na mi ntakuwa wa mjini’ ndilo wazo lililotawala vichwa na mioyo yao, masikini wa Mungu kumbe hawakujua kuwa ‘Mjini shule’.

Mambo hayakuwa kama walivyofikiria walipofika Dar, kilichobadilika kwao ni aina ya majengo na wingi wa magari kwa kuwa kule kijijini kila gari lipitalo ni la mission ukimuona mzungu ni Padre na si zaidi ya hapo. Maisha yaliwawia magumu katika kila nyanja, walipoenda viwandani na kwenye makambpuni kuomba kazi waliambiwa ‘hakuna kazi’, jua liliwawakia vijana wa kike kwa wa kiume hawakujuwa nini wafanye, pesa zikawaishia hata nauli ya kurudi kijijini hawakuwa nayo, lakini hata wangekuwa nayo ‘nitachekwa’ walijiwazia kwa hilo.

Mwisho wake vijana walikuwa vibaka na wasichana walijiuza na kufanya kazi katika mabaa ili mradi posho kidogo kutoka kwa wanaume wenye uchu wa ngono na kupapaswapapaswa kwa angalau shilingi mia tano wapate chai asubuhi. Waliokosa mbinu waliishia vijiweni kujidunga sindano za madawa ya kulevya na kuwa teja wakidondoka mate kama wagonjwa.


Mahali Fulani huko

Singida Vijijini

“Wewe Mwanamke huwezi kupata urithi, nani aliyekwambia wanawake wanarithi? Hapa kwetu wanawake wanarithiwa baada ya waume zao kufariki” Mzee Malombe alimueleza mke wa marehemu katika kikao cha ukoo kilichoitishwa katika kugawana mali za Mrehemu. Mke wa marehemu, mama Vituko alibaki amejikunyata na watoto wake kwenye kona ya nyumba ya mumewe ambayo sasa waliambiwa si mali yao tena, akiwa kajawa na machozi machoni pake hakuwa na sauti ya kupinga uamuzi wa wazee hao.

“Sasa lile shamba la ng’ambo kule atarithi kaka mkubwa, mifugo hii yote watarithi wajomba, hii nyumba itakuwa mali ya ukoo, na wewe mama Vituko kuanzia leo utarithiwa na shemeji yako mdogo huyo hapo pembeni yako, ndiye atakuwa mumeo” Mzee Malombe aliendelea kugawisha mali za marehemu.

Akiwa ndani ya nyumba ile alilia sana alimkumbuka sana marehemu mumewe hakujua afanye nini katika hili

“Kwa nini hukunichukua mimi kwanza?” Mama Vituko alilia sana, usiku huo hakupata hata usingizi alikuwa akilia tu huku kaikumbatia picha ya mumewe aliyopiga enzi za uhai wake. Alihisi kama Jinamizi la mateso na majonzi likimuandama, mali alizochuma na mumewe wakiteseka shambani kwa mvua na jua, leo hii zinagawiwa kwa ndugu ambao hata uchungu wa kuzitafuta hawakuujua.

Kurithiwa na shemeji yake, hilo halikumuingia akilini hata kidogo, moyoni mwake alijisemea ‘haiwezekani’, alifikiria afanye nini mawazo kichwani mwake yalipita kwa kasi kama maji yanayotelemka bondeni, kila uamuzi alioufikiria ama aliuona wa kishetani au aliwawazia watoto wake wataishi vipi, mwisho alijikuta hana la kufanya alikuwa mpole akaamua kubaki kuona nini kitachofuata, moyoni mwake hakukubali hata kidogo mali zake na watoto ziende bure ‘nitalipigania jasho langu’ huo ndiyo uamuzi alioufikia na kuuona kuwa ni wa busara kuliko wote.

“Sikubaliani na chochote mnachotaka” alijikuta akilopoka mbele ya wazee wale

“Unasemeje we mwanamke, mbona huna adabu kiasi hicho, unafikiri huu ni mchezo!” Mzee wa Ukoo. Mzee Malombe aling’aka kwa hasira huku akimuoneshea fimbo yake kwa mama Vituko.

“Mali hizi nimechuma na mume wangu, ni haki kurithiwa na familia yake, yaani mimi na watoto hawa wawili” Mama Vituko alijikuta kapata ujasiri wa ajabu kuwajibu wazee wale.

“Kelele!” fimbo ya mzee Malombe ilikwishatua mgongoni mwa mama Vituko, kisha akaendelea kuongea huku akiuma meno yake

“Kama hutaki kurithiwa itakubidi uondoke kijijini hapa na vitoto vyako, unapinga mila!!”

“Hata kama ni mila siwezi, mila gani za kizamani hizi, mnatukandamiza, wanaume” alizungumza huku akilia na kutoka nje, akina mama waliokuwa hapo nje walimshika na kumfariji kwa maneno matamu ‘yote yataisha’ tu walimueleza maneno hayo.

Kwa miaka mingi sana kumekuwa na ukandamizaji wa wanawake hasa katika haki ya kurithi, hii imepelekea migogoro mingi sana katika koo na familia nyingi sehemu mbalimbali, mila ya kurithi mke iliyopitwa na wakati imesababisha maambukizi mengi ya magonjwa ya zinaa miongoni mwa jamii katika koo nyingi za kiafrika.

Kikao cha wazee wale hakikufikia muafaka kwani baada ya mama Vituko kutoka nje kwa hasira wazee wale walishindwa kuelewana wakaamua kuitana siku ya pili yake.

Usiku wa siku hiyo mama Vituko alishapanga kutoroka na watoto wake wawili, hakuona haja ya kuwaacha kwani alijua watateseka kwa kumkosa, kwake ilikuwa ni bora kuondoka nao kama ni kuishi watajua uko huko mbele ya safari. Alishtuka usingizini na kutoka pale kitandani alipokuwa amelala na watoto wake, taratibu alishuka chini na kusimama wima, akasogea dirishani na kuchungulia nje, kulikuwa ni giza mahali pote, akarudi mpaka karibu na mtungi wa maji akausogeza pembeni na kuingiza mkono kwenye kashimo kadogo alipoutoa ulikuwa na noti za shilingi elfu mojamoja nyingi sana zilizokunjwa pamoja, bila kuchelewa akazichukua na kuzitia katika sidiria yake iliyopoteza rangi yake halisi kutokana na maji machafu yaliyotumika kufulia huku ikiwa muda wote mwilini kwa kuwa ilikosa msaidizi. Aliwaamsha watoto wake ambao hawakujua chochote kinachoendelea usiku huo

“Shhhhh!!!” aliwapa ishara ya kuwa watulivu, alichukua kifurushi kidogo na kumbeba motto wake mdogo mgongoni na huyu mwingine akamshika mkono kutembea mwenyewe, kwa mwendo wa tahadhari wakatoka nje na kuvuka nyumba kadhaa kisha kutokomea kwenye msitu wa jirani. Safari ya kwenda kusikojulikana ikawa imeanza katika mtindo huo, mwendo ulikuwa mrefu usiku huo mpaka motto wa kiume aliyekuwa akitembea mwenyewe alichoka sana, mama Vituko hakuwa na jinsi alimnyanyua na yeye na kuendelea na safari yake. Nuru hafifu ilianza kulifukuza giza, Mama Vituko alikuwa amechoka kwa mwendo mrefu na watoto wale, aliketi chini ya mti mkubwa uliokuwa kandokando ya barabara akisubiri usafiri ‘naenda wapi?’ yeye mwenyewe hakujua.

Punde si punde basi aina ya Leyland lilifika eneo hilo likiwa linaelekea mjini, hakuwa na la kuuliza alipanda na watoto wake, basi lilikuwa limejaa lakini wasamalia wema walimpa kiti ake yeye na watoto, mbele ya safari alinunua maji na biskuti kwa ajili ya watoto wake ili angalau kupoza njaa watakapohitaji.

Safari iliishia mjini Singida, Mama Vituko na watoto wake walishuka ilikuwa tayari ni mchana, jambo la kwanza alitafuta mgahawa ili kupata chochote yeye na watoto wake, baada ya hapo alifikiria je safari iendelee au iidhie hapo, aliketi chini akiwaangalia watoto wake wakichezea vikopo vya maji kama magari wakiwa na furaha tele, Malaika wale hawakujua kabisa ni nini kinaendelea duniani, Mama Vituko aliingiwa na uchungu mkali na kuanza kudondosha machozi kumkumbuka mumewe.

€ € € €

Tuntufye alikuwa pamoja na watoto wenzake katika shughuli ya kuomba jirani katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi karibu na pacha ya kuingia Agha Khan. Magari mengi yalikuwa katika foleni ya kuingia mjini siku hiyo ya jumatatu, aliyetoa shilingi mia, hamsini au hata mia mbili ilikuwa ni tosha kabisa kwa watoto hawa. Kila hela aliyoipokea alikuwa akiihifadhi vizuri katika kifuko alichokishona kwa vitambaa na kukivaa ndani ya gauni lake chafu lisilojua maji, kila aliyepita hapo na gari lake alimtazama sana motto huyu mwenye uso wa mviringo, mfupi kwa umbo na sura upole, alionekana ni mtu aliye na mashaka na woga uliochanganyika na shida nyingi ukimtazama tu kutoka usoni kwake.

Watoto wenzake walimuonea donge sana Tuntu siku hiyo maana alipata pesa nyingi sana asubuhi hiyo, lakini daima yeye hakupenda kuona wenzake hawana raha kwa kukosa hela, alitoka barabarani na kuketi chini ya kamti kadogo akiwaacha na wenzake wapate angalau za kuwapa mama zao wanaowasubiri.

Jua lilikuwa kali sana, Tuntu na wenzake walipokuwa wakirejea taratibu huku wakiendelea kuomba hapa na pale, mchana huu magari yalikuwa machache sana hivyo watoto hawa walikuwa wakicheza huku na kule kukimbizana na kurushiana vijiwe na michezo mingine mingi, Tuntu aliamua kupita katikati ya majumba ya wahindi maeneo ya Upanga ili apate urahisi kutokea maeneo ya Kisutu ambayo daima ndipo ilikuwa maskani yao. Alikatisha mtaa wa kwanza na wa pili kulikuwa na jalala kubwa sana, tuntu alisimama mbele ya jalala lile na kuliangalia kwa muda, … alimuona motto mmoja wa kiume akiwa katikati ya jalala hilo akipekuapekua kutafuta chochote chakula, Tuntu japo alikuwa ombaomba lakini alijua wazi kuwa kula vitu vya jalalani ni hatari kwa afya, alimuangalia kwa huruma sana mototo yule, Tuntu aliumia sana machozi yakaanza kumtoka akamuita yule motto, naye bila kusita akaja kwa Tuntu

“Usile vyakula vya jalalani, kesho uje barabarani tuombeombe tupate hela” Tuntu akatoa shilingi mia nne akampatia motto yule ambaye shukrani yake haikuweza kuificha katika macho yake.

“Mi naitwa Tuntufye” Tuntu alijitambulisha

“Mimi naitwa Hassani” naye alijitambulisha kwa Tuntu. Wakaagana wakikubaliana kesho waende kuombaomba pamoja. Tuntu alitudi katika kijibaraza ambacho daima walikuwa wanalala akakutana na wenzake wameshafika muda mrefu wakiwa wanacheza mdako mchezo unaopendwa na watoto wengi hasa wa kike. Kwao siku ilikuwa imepita na sasa ilisubiriwa kesho.


Ashura na Kautipe ni wasichana marafiki sana tangu wakiwa wanasoma shule ya msingi huko katika kijiji cha Mawambala mkoani Iringa. Walikuwa wote tangu utoto wao mpaka umri wao wa balehe, daima hawakuachana, siri ya huyu aliijua huyu nay a mwingine vivyo hivyo.

Baada ya miaka mingi kupita walijikuta hawana maendeleo yoyote kiuchumi, hii ilikuwa ni hali iliyowapa uchungu sana katika maisha yao ukizingatia wasichana wenzao wengi waliokwenda huku na kule kufanya vibarua waliporudi kijijini walileta japo doti ya kitenge cha Sungura kwa mama zao au kitambaa cha suruali kwa baba zao. Ilifika kipindi nao walikaa chini kuamua jinsi ya kupambana na maisha

“Kautipe, nimechoka maisha ya kijijini” Ashura alimueleza kautipe

“Kila siku nataka nikwambie hilo, mi natamani kubadilisha mazingira sasa” Kautipe aliongezea.

“Kweli shoga, tuzaliwe Mawambala, tukulie hapahapa hata kutoka kidogo aaah we” Ashura alikazia

“Tutafute hela twende zetu town” Kautipe alimalizia. Baada ya mazungumzo marefu kati ya wasichana hawa wawili waliamua kufanya biashara ndogondogo ili kupata hela itakayowaondoa pale kijijini na kuelekea mjini.

Mungu si Athumani walijipati hela ambazo ziliwawezesha kufika japo Iringa mjini, wakiwa pale wakafanya kazi ya kuuza bar katika maeneo ya Vibanda vya CCM kwa miezi kadhaa na kufanikiwa kupata pesa ya kutosha kuweza kujikimu maisha yao.

Tama ya kufika katika jiji kubwa linalosifika na kila mtu iliwaingia, kila waliposikia sifa ya jiji hilo mioyo yao iliwaenda mbio kuliko kawaida kila mmoja wao aliazimia lazima afike japo kusafisha macho na kutoa ushamba kidogo. Mwenye bahati habahatishi, siku moja katika kuhudumia wateja wao, mmoja kati ya wateje hao alikuwa akitokea Dar es salaam, alikuja kikazi tu mjini Iringa, katika mazungumzo yao ndipo walipogundua kuwa ni mtu wa mjini, Kaundime akaazisha urafiki wa karibu sana na kijana huyo akimkirimia kwa kila atakalo ilimradi tu aende Dar es salaam kuosha macho. Alipomsimulia shoga yake Ashura waliamua kufanya kila hila wapate nafasi katika gari ya kijana huyo kama lifti kuelekea Dar es salaam. Walijaribu kumpigia simu rafiki yao Zai ili wafikapo huko awe mwenyeji lakini hawakumpata isipokuwa walikumbuka tu alivyowaelekeza mara ya mwisho sehemu anayoishi. Waliamini kuwa lazima wangempata na kwa msaada wake basi maisha yao yangekuwa rahisi sana kwa kuwa huko kuna kazi nyingi na za kila aina.

Usiku huo hawakupata usingizi kabisa kila walipofikiria juu ya safari yao ya Dar es salaam.

Ukarimu kwa Watanzania haukuwa kitu cha ajabu sana tangu kuhasisiwa kwa taifa hili na Mwl Nyerere. Mama Vituko na watoto wake waliketi katika kibaraza cha duka mojawapo lililopo hapo stendi ya mabasi ya Misuna, mjini Singida wakiwa hawajui pakwenda jioni hiyo, jua lilikuwa limekwishachwea na kagiza kalikwishaanza kuingia. Mama mmoja mfagizi wa eneo hilo alimuona mama huyu wa watoto wawili tangua mchana aliposhuka kwenye basi, lakini alishangazwa alipomkuta tena stendi hapo, alimsabahi na kumhoji maswali machache, huruma ilimjaa aliposikia mkasa uliomkuta mwanamke mwenzake, alimkaribisha nyumbani kwake ili waishi japo kwa siku chache.

Ilikuwa nyumba ndogo iliyojengwa kwa matope na kuezekwa kwa nyasi, vyumba viwili vya kulala na sebule ndivyo vilivyoijaza nyumba ile, hakukuwa na kiti isipokuwa mkeka na vigoda viwili. Mama huyu mwenye watoto watatu alikuwa ameachika kwa mumewe, ni maisha haya tu ndiyo yaliyomfanya aishi katika hali hiyo ili kujipatia ridhiki yake na watoto wake.

Wakiwa katika maongezi ndipo mama huyu alipomsimulia kisa na mkasa mpaka akajikuta katika hali hiyo

Miaka 10 iliyopita

Maeneo ya Kiomboi.

Mzee Francis Njiku aliondoka nyumbani kwake Kiomboi miezi mingi nyuma na kuhamia nyumba ndogo huku akimuacha mke wake wa ndoa na watoto.

Walipofunga ndoa Mama Njiku alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi huko Mtinko na Mzee Njiku alikuwa mkulima mwenye elimu ya darasa la kumi na mbili, wakiwa ndani ya ndoa Mama Njiku alimpenda sana mumewe akatumia kila alichonacho kukuendeleza kielimu baada ya miaka mitano mbele Mzee Njiku alipata stashahada ya kwanza ya ualimu na kuajiriwa serekalini, miaka ya kwanza alichapa kazi kwa nguvu sana pamoja na mkewe walijijenga sana, walijenga nyumba moja kubwa na kuendeleza shamba lao kwa kuweka mifugo mingi ya aina mbalimbali. Baada ya miaka kadhaa Mzee Njiku alipandishwa cheo na kuwa afisa elimu wa wilaya ya Singida,

“Sasa mke wangu, nina wazo nataka nikushirikishe” Mzee Njiku alikuwa akiongea na mkewe walipokuwa chumbani kwao wao wawili kama walivyokutana.

“Ndiyo mme wangu, nakusikiliza” Mama Njiku alimsikiliza kwa makini mume wake

“Kwa kuwa sasa mimi mumeo nina nafasi nzuri kazini, unaonaje wewe ukiomba kustahafu kazi yako halafu utunze mifugo, mashamba na mali tulizonazo” Mzee Njiku alimueleza mkewe kwa upole na upendo mkubwa. Mama Njiku hakuwa na kipingamizi kwa wazo la mumewe, baada ya wiki moja alianza kulifanyia kazi wazo hilo na baada ya miezi mitatu alikuwa tayari amepata barua yake ya kustahafu.

Maisha yaliendelea kama kawaida nyumbani hapo kwa miaka kadhaa. Baada ya muda Fulani Mzee Njiku alibadilika sana kitabia alianza kurudi nyumbani kwa kuchelewa, alikuwa daima akirudi saa kumi jioni lakini sasa alianza kurudi saa moja usiku mara saa tatu, mke wake alipomuuliza alipigwa sana, Mzee Njiku akaingia katika ulevi wa pombe wakati mwingine hakujulikana hata ni wapi analala ni asubuhi utamuona akirudi. Hali ilizidi kuwa mbaya hela ya chakula nyumbani haikuwa ikiachwa tena ‘chinja ng’ombe ule’ ndiyo jibu alilolitoa kwa mkewe kila alipokumbusha kuhusu hela ya chakula cha watoto.

Mzee Njiku alikuwa amepata nyumba ndogo, kwa kuwa alikuwa akichekwa na rafiki zake wanapokuwa wakinywa pombe, Mzee Njiku alishawishika na kutumbukia katika janga hilo, akamtwaa mwanamke mmoja ambaye walikutana sehemu Fulani katika moja ya kazi zake, mwanamama huyo hakuwa na ajizi alimpokea Mzee Njiku kwa huba na penzi la bandia ilimradi afaidi kila alichonacho, alijihakikishia kuwa hapo hawezi kuchomoka na alikuwa tayari kufanya lolote, Mzee Njiku alipikwa akapikika, alisahau nyumbani na huduma zote alihamishia nyumba ndogo.

Mama njiku alibaki na watoto wake nyumbani hana la kufanya aliendeleza shamba lao na mifugo lakini aliona tu Mzee Njiku akija na kuchinja mbuzi bila taarifa wala kujua nyama inakwenda wapi. Watoto walianza kufukuzwa shule kwa kuwa hawakuwa na karo, Mama Njiku alipokwenda kwa mawifi na mashemeji kuwaeleza juu ya tabia ya kaka yao jibu alilolipata hakulitegemea tena lilimti uchungu ‘ulifikiri kaka yetu mjinga, uliyokuwa unamfanyia ndiyo yamekurudia’. Mama Njiku hakuwa na la kufanya, maisha yalikuwa magumu kila upande hakuwa na msaada tena kwani hata wachache waliomsaidia walichoka.

Mzee Njiku alishawishiwa na nyumba ndogo kumnyng’anya mke mkubwa nyumba ili wapangishe, na yeye bila kupinga alikubaliana naye na kazi ya kumfukuza mke wake katika nyumba ikaanza, siku hiyo mama Njiku hakukubali hata kidogo ugomvi ulikuwa mkubwa sana ulizuka kati ya Mzee Njiku na Mkewe wa ndoa katika ugomvi huo Mzee Njikui alianguka na kuvunjika mkono, dada wa mzee Njiku waliripoti Polisi na mama Njiku akawekwa ndani.

Mama Njiku alijikuta akihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kudhuru mwili lakini nyuma yake nyumba ndogo alikuwa amehonga hela kwa Hakimu kuhakikisha kuwa Mama Njiku anawekwa anatumikia kifungo ili yeye apate kufaidi kila kilichopo, ama kweli sheria inauzwa na haki inanunuliwa. Mbele ya Mwanamke huyu Mshumami, Afisa elimu Mzee Njiku hakuwa na thamani tena, alikuwa kama zezeta aliyekubali kila anachoambiwa.

€ € € €

Akiwa na mwanae Malogo, mama huyu mwenye upofu uliosababishwa na ugonjwa wa trakoma alikuwa akipita madukani kuombaomba ili mradi apate chochote cha kula yeye na mtoto wake mdogo, ilikuwa ni ngumu kwake lakini hakuwa na jinsi ilibidi afanye hivyo ili kunusuru maisha yake. Kila siku aliomba tu Mungu amchukue akapumzike lakini alipomkumbuka mwanaye huyu alibaki kutokwa na machozi. Mumewe alishakufa, yeye akabaki na watoto hawa wawili, afanyeje! Ndipo alipoamua kuwa aende Dar kwa kaka yake, na kaka yake alikubali kumtunza dadaye wa pekee. Lakini hali haikuwa hivyo, ugomvi uliozuka kati ya kakae na mkewe haukuwa mdogo ‘usiniletee vipofu wako nyumbani kwangu’ maneno aliyomueleza mumewe mara kadhaa, hakumpenda wifi yake wala watoto wake, mumewe alipoondoka hakuwapa chakula na mara nyingine aliwalazimisha kulala kwenye banda lililokuwa likifugiwa kuku.

Ndoa haikunoga hata kidogo, afanye nini? Amfukuze dada yake kipofu au amfukuze mkewe? Lilikuwa ni swali gumu lililousumbua moyo wa bwana huyu, alimpenda dada yake na akampenda mkewe.

Siku moja alirudi nyumbani baada ya safari ya siku tatu nje ya mkoa na kukuta dada yake na watoto hawapo, alichanganyikiwa hakujua afanyeje, alipomuuliza mkewe alikuwa mkali ‘kawatafute, we si ndiyo ndugu zako!’ jibu lilikuwa ni hilo.

Mama kipofu na wanawe waliamua kuondoka katika nyumba hiyo yenye kero na manyanyaso na kwenda kuanza maisha mapya huko mjini, maisha ya kuombaomba kwa wapita njia, alipochoka alimtuma binti yake Tuntufye akaendelee na kazi hiyo.

Sasa akiwa Dodoma baada ya kurudishwa ombaomba ndipo alipopotezana na bintiye huyu, kila kukicha alimlilia sana Tuntu, alitamani kama atokee hapo kimiujiza lakini haikuwa hivyo.

Siku hiyo ya tukio Tuntu na wenzake wachache walikwenda kuomba kama kawaida yao isipokuwa tu walibadilisha mtaa, siku hiyo walienda mtaa wa Azikiwe kuelekea picha ya Askari huku nyuma wazee wao ambao wengi walikuwa tayari ni vipofu na wengine walioathirika kwa ugonjwa wa ukoma walijikuta wakivamiwa na mgambo wa jiji na kuzolewa kupelekwa stesheni ili warudi kwao, mkuu wa mkoa wakati huo Mzee Yusuph Makamba alihakikishia umma wa Watanzania kuwa atafanikisha kazi hiyo ijapokuwa aligonga mwamba kwa Mzee Matonya aliyekuwa maarufu kwa staili yake ya kuomba akiwa kalala chali bila kujali mvua wala jua.

Tuntu alitungua kilio kikali sana alipokuta vibaraza vile vimekuwa vyeupe kabisa hakuna mtu, alianza kukimbia kuelekea mnazi mmoja huku akilia na kumuita mama yake kipenzi, alipofika mnazi mmoja kwenye mnara wa uhuru hakujua aende wapi alibaki akiushangaa mnara huo ambao uliendelea kumpa matumaini, aliamua kurudi alikotoka na hapo maisha ya pekee yalianza. Alikuwa anaombaomba barabarani akipata pesa zingine ananunua chakula na zingine anaficha anapopajua yeye ili mradi maisha yakawa yanaenda.

Baada ya kurudishwa kijijini kwao Mpamantwa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, alijikuta hana cha kufanya na jamii yote ilimtenga, ndipo aliposogea Dodoma mjini ili apate ridhiki wakati huo motto wake Malogo alikua akiendelea kukua kwa kimo na akili, kila siku alimuona mama yake akifanya kazi hiyo na yeye alikuwa akimsaidia kushika fimbo kumuongoza.

Watu walikuwa wakipita asubuhi kuelekea makazini ndipo walipomkuta Malogo akilia kando ya mama yake aliyelala chini katika korido ya maduka ya wahindi, mtoto huyu alilia huku akimtikisa mama yake aliyelala kimya katia sakafu hiyo baridi. Wapiti njia waliihofu hali ile wakasimama na walipokuja kumuangalia mama yule, tayari alikuwa amefariki, Malogo alibaki peke yake, alibaki katika ulimwengu wa kiza, hakuna baba, hakuna mama, hakuna dada, wote hawa aliwaona katika kumbukumbu finyu ya utoto isiyohifadhi chochote kwa muda mrefu.


Maisha hayakuwa mepesi kama walivyofikiri, Zai aliwakaribisha shoga zake hawa katika ghetto lake lililopo huko Tandika Mwembeyanga, hakuwa na kingine zaidi ya ghetto hilo lenye godoro moja lililowekwa chini na box moja lililohifadhi viwalo vyake.

“Karibuni wageni, hapa ndiyo nyumbani jisikieni huru tu!” Zai aliwakaribisha rafiki zake Ashura na Kautipe. Mbele yao waliona nyumba kuukuu ambayo hata matofali yake yalishaanza kuchoka kwa kuliwa na maji ya mvua inyeshayo kila wakati katika jiji hili la Dar es salaam, haikuwa ile nyumba kubwa aliyowaambia ina kilakitu ndani. Ashura na Kautipe walitazamana lakini hawakuwa na lakufanya walimfuata mwenyeji wao huyo na kuingia ndani ya kijichumba hicho kidogo chenye joto. Waliketi juu ya godoro lililopo haponadani, Zai akawaacha na kwenda kuwatafutia japo tuviazi wale wapoze njaa.

“Zai !” Kautipe alivunja ukimya

“Bee! Unasemaje Kau?” Zai aliuliza

“Hapa ndipo unapoishi?” alimtupia swali

“Eee unapaonaje? Pabaya au?” Zai alijibu na kurudisha swali

“Hamna, pa kawaida tu, bado unafanya kazi katika kampuni ile ulotuambia?” Kautipe alizidi kudadisi

“Mh! Kau, mbona una maswali hivo mtoto? Kule nilifukuzwa kazi halafu vibaka wakaniibia kila kitu, yaani hapa ndo naanza upya” Zai alimjibu Kautipe huku akibinua mdomo na kusonya kisha akaendelea

“Karibu Bongo, hapa ndo mambo yote, kwa Waswahili tunasema mgeni siku ya kwanza…” Zai alijinyanyua na kutoka nje

“Na we Kau kwa maswali eh!” Ashura alimsema Kautipe

“Jamani si nauliza tu, si alituambia anafanya kazi katika kampuni ya madawa ya nywele, na anakaa nyumba kubwa. Sasa nashangaa” kautipe alimjibu Ashura na mara mlango ukasukumwa Zai, akaingia ndani na kamfuko ka Rambo kadogo

“Kuleni wageni, hapa maisha kama karata” Zai aliwaambia Kautipe na Ashura huku akiwawekea chips zile katika sahani kuukuu ya bati iliyokuwa juu ya ndoo.

Ashura alibaki kutazama tu wakati Kau alipigwa na bumbuwazi, hakuna kati yao aliyetegemea hali hiyo lakini wafanye nini, walishambulia chipsi zile kwa kasi kubwa maana walikuwa na njaa kali, aliyewapa lifti akuwa na tabia ya kusimama simama vituoni. Baada ya kula walijilaza katika kigodoro hiko wote wawili na kila mtu aliota ndoto zake, hakuna aliyejua kama Zai alitoka au alilala pamoja nao, maana usingizi wa uchovu uliwamaliza wote.

Mtaa wa Ohio, Zai alichelewa kidogo kufika siku hiyo wenzake walimshambulia kwa maneno

“Umeridhika siku hizi ee?” mmpja wao waliemwita kwa jina la ‘sista’ alimtupia swali hilo Zai huku akimwangalia kwa jicho la dharau

“Si hivyo Sista, ila nimepata wageni wa ghafla nyumbani.nikashindwa kutoka kwa wakati.” Zai alijibu huku akijiweka sawa kuanza night shift yake

“Mi nilijua unapiga juu kwa juu siku hizi, maana nimeshapata habari zako” Sista alizidi kumsema Zai ambaye wakati huo alikuwa akiendelea kuvua baibui lake na kubaki na sketi fupi sana iliyo si juu tu ya magoti bali sentimeta chache chini ya kiuno chake chembamba, iliyoruhusu hata nguo ya ndani kuonekana japo kwa macho ya wizi, juu alibaki na kiblauzi kilicho funika juu ya kitovu na kuishia chini ya mazowa wakati kikishikiliwa na kamba nyembamba zilizopita juu ya mabega yake, hakuvaa sidiria ilimradi tu awatege wapiti njia kwa chuchu zake zilizochongoka na kusimama kama mishale ya saa tisa kamili. Alipohakikisha yuko vizuri alimalizia kwa kujipulizia marashi safi kutoka bara la uarabu. Zai alikuwa akihusudiwa na kila mpita njia hata wasichana wenzake walikiri kuwa Zai ni mzuri na mrembo mno, lakini kila mtu alishangaa kwa nini mrembo huyu hakupata japo mpenzi wa kumficha ndani, hiyo ilikuwa siri yake ambayo ni yeye na Muumba wake tu waliijua. Baada ya kuwa hapo kwa muda mrefu, siku hiyo haikuwa nzuri kabisa kwa wadada hawa, hakupatikana wa bei mbaya wala wala wa mia tano kwa ujumla hali haikuwa yenyewe, hali hii ilibidi Sista aamue kuwa kila mtu arudi akapumzike mpaka siku ya pili akiwaacha kwa kuwaambia kuwa kama likitokea zali basi yeyote aweza kuitwa.

€ € € €

Mtawa, bruda Fransisco Kobelo wa Shirika la Roho Mtakatifu alikuwa katika harakati zake za kila siku kupita kufundisha dini mashuleni, hakuna hasiyemfahamu mtawa huyu wa kanisa Katoliki maana kila alipopita alipenda kuwapa peremende watoto waliokuwa wakicheza mitaani.

Daima alikemea sana wazazi ambao hawakupenda watoto wao wasome na kuwaacha wakizurula, mtawa huyu alikuwa akisomesha vijana wengi katika mashule mbalimbali na wengine walikuwa katika vyuo vya ng’ambo na wengine tayari walikuwa maofisini wakifanya kazi na kupata mishahara minono, wapo waliomkumbuka na wapo waliomsahahu lakini yeye hakujali yote hayo kwani alikumbuka msemo wa wahenga ‘tenda wema uende zako usingoje shukrani’.

Asubuhi hiyo alikuwa akipita katika viunga vya mji wa Dodoma kutafuta mahitaji ya watawa wenzake ambao siku hiyo walibaki na majukumu mengine, akiwa anapita karibu kabisa na viwanja vya Nyerere katikati ya jiji la Dodoma, moyo wake wenye neema ya pekee ulimueleza kitu, daima alisikiliza kile ambacho alikisikia moyoni mwake, alisimama na kuangalia huku na huku ili kujua ni nini kinampasa kufanya, pembeni kidogo alimuona mtoto wa kiume akiwa amelala karibu na kopo kubwa la maua, Bruda Fransisco alimsogelea malaika huyu na kumtazama kwa huruma, alipiga magoti na kufanya ishara ya msalaba kama wafanyavyo watu wa dhehebu hilo kisha akamnyanyua mtoto yule aliyeonekana kulegea sana kwa kukosa chakula au maji ya kutosha. Kila mtu alimwangalia mtawa yule, hakujua ni nini kinamsukuma kutenda haya yote

“Ataweza kuwalea wote hawa?” baadhi ya wapita njia walikebehi lakini yeye hakujali maneno yao alifanya lile lililompasa kutenda. Alimnyanyua mtoto yule na kumuweka begani kwake kisha kuondoka.

Malogo alilelewa katika kituo maalumu cha kulelea watoto cha shirika la Roho Mtakatifu maeneo ya Ihumwa mjini Dodoma. Akiwa chini ya malezi bora ya bruda Fransisco Kobelo, alijifunza mambo mengi yakiwemo maadili mema. Bruda Fransisco alimuangalia Malogo kwa jicho la pekee sana kwa kuwa yeye alikuwa ndiye mdogo kuliko wote katika kitua hicho alihakikisha anapata mahitaji yote yanayotakiwa, japokuwa hakujua historia yake kwa maana katika kitabu chake aliandika historia za watoto wote ili kumsaidia kupata ufadhili toka ng’ambo kwa ajili ya malezi yao, lakini kwa Malogo ilikuwa ngumu historia yake haikuandikika kwa maana alikuwa na umri mdogo wala hakujua kinachoendelea duniani.

Tuntufye alikuwa amechoka sana siku hiyo, hela zake kidogo alizozipata aliweza kununua chakula na maji kisha akatafuta kivuli cha muenbe pembezoni mwa mahakama ya Kisutu na kuuchapa usingizi. Alishtuliwa na mtu aliyemkanyaga mguu, akaamka na kuinua uso wake, aliyemuona hapo hakumtegemea kabisa, Ravi Mavalanka, kijana wa Kihindi mwenye roho ya mbaya daima alipowakuta watoto hawa aliwapiga na kuwanyang’anya hela zao, hivo kila walipomuona walimkimbia. Tuntu alimtazama kijana huyu mwenye macho mabaya kutokana na ulevi wa kubeli, ndiyo huyu kijana aliyembaka Tuntu miezi miwili iliyopita. Tuntu alishikwa na jinamizi la hasira, roho ya mauti ikauteka moyo wake, alijikuta anashindwa kuvumilia kumtazama kijana huyu, alinyanyuka pale alipo na kusimama wima akimtazama kwa macho hasira, mara machozi membamba yakaanza kumtoka msichana huyu mwenye sura nzuri ya mviringo iliyokosa matunzo, mwenye gauni chafu lililokosa maji na sabuni kwa kipindi kirefu

“Mpenzi jambo, leo umepata ngapi?” Ravi alimuuliza Tuntu huku akiweka vizuri begi lake la shule mgongoni mwake na kumsogelea.

“Unikome! Mpenzi wako nani?” Tuntu aliongea kwa hasira huku akirudi nyuma

“Lete hela halafu ukatafute zingine, kama huna nakufanya kama siku zile, unakumbuka ee?” Ravi alimueleza Tuntu kwa kebehi huku rafiki zake wakimshangilia, Ravi alimfikia Tuntu ambaye sasa muembe ule ulimnyima nafasi ya kurudi nyuma zaidi, akiwa anavuta makamasi mara kwa mara moyo wake ulikuwa ukienda mbio kwa hasira na uchungu, hakumpenda kijana ahuyu hata kidogo,

“Usinisogelee mimi” Tuntu aling’aka, Ravi alimshika Tuntu mikono na kuwaita wenzake wamnyang’anye hela, Tuntu alijaribu kujinasua alipoona anashindwa na wale wengine wanaanza kumshika maungoni mwake alimmng’ata Ravi mkononi na kumuumiza vibaya, Ravi alimuachia Tuntu na Tuntu akaanguka chini, Ravi aliendelea kumfuata Tuntu sasa akiwa na hasira damu zikimvuja katika mkono wake

“Nakuua we Chokoraa! Nakuua leo” Ravi alikuwa akilia huku akivua begi lake na kulitupa chini akamkimbilia Tuntu kumuwahi kabla hajanyanyuka, Tuntu alipoona hilo alijihami akajua hakika leo anauawa. Wenzake na Ravi walisimama pembeni kuangalia mbabe wao huyo anavyomshambulia yule Chokoraa, lakini alipomfikia Tuntu walimuona Ravi akijishika tumbo na kuanguka chini huku damu nyingi zikimtoka maeneo ya mbavu. Tuntu alichomoka na kukimbia kutoka pale. Ravi alilala chini huku akihema taratibu, wenzake walipanda basikeli zao na kuondoka wakamuacha Ravi palepale.

Tuntu alijawa na woga sana, mbio zake ziliishia maeneo ya Kivukoni, alijichanganya na wauza samaki katika soko la samaki la kimataifa la Feli na kuanzisha makazi yake huko. Daima nafsi yake ilimtesa sana alijua wazi kuwa amemuua, aliogopa akijua lazima akamatwe, nafsi yake ilihangaika na hakupenda kuwa karibu na mtu yoyote, kila mtu alimuogopa, maisha yake yakawa ya upweke, akilala viti vya kupumzikia vilivyo mbele ya Ikulu ya Tanzania, daima aililiangalia jingo hilo jeupe linalopepea bendera juu yake lakini kamwe hakuona dalili ya mtu kuishi ndani ya jengo hilo.


“Yaani hakikisha hakumbuki hata kwao, ulifanikiwa kumuondoa kwa mkewe lakini ndugu zake bado wanamfatafata sana, mi sifaidi mali zake.” Hawara wa Mzee Njiku alimueleza mganga Matomola, alipokwenda kuongeza nguvu ya dawa ili sasa awapumbaze na ndugu zake.

“Aaaa ha ha ha ha usijali mama, hapa ndiyo kwa mganga Matomola, hakuna kinachoshindikana ha ha ha ha!!” Mganga kama kawaida yake alichukua vitu kama unga mweusi na kuutia kati tunguli moja iliyoonekana kutoa moshi, katikisa kichwa chake na kupiga chafya kali.

“Mmmm; unajua, kazi hii ni ndogo tu!” Mganga alimpa moyo yule mama na kumpa kitu Fulani kilichoviringishwa katika jani kavu la mgomba.

“Sasa nenda kaandae chakula uwaalike ndugu zake kisha changanya hii dawa chakulani kama kiungo, ha ha ha ha kazi imekwisha mama” Mganga yule alimaliza na kumruhusu aende.

Baada ya miezi sita

Afya ya Mzee Njiku ilianza kudhoofu taratibu, mara mafua, mara vikohozi, mara malaria zisizoisha, alitibiwa kila hospitali lakini hali yake ilibaki kuwa tete, ndugu na wanaukoo walikaa vikao kujadili mustakabali wa afya ya ndugu yao huyu, maana kama kutibia walitibia mpaka wakakosa la kufanya.

Mzee Njiku hakuwa na lingine bali kulala na kuamka, siku akipata nafasi alikuwa akienda kazini na wakati mwingine alipumzika nyumbani. Kipindi Fulani alilazwa hospitali kwa muda mrefu, walipoona imeshindikana kwa dawa za hospitali sasa wakaamua kumfanyia maombi, maombi ya kila dini na dhehebu lakini bado mambo yalikuwa yaleyale, waliona labda mchungaji huyu hafai, wakabadilisha na kwenda kwa mwingine lakini bado hali haikuwa nzuri pamoja na jitihada zote hizo, akinyanyuka atafanya kazi labda wiki mbili na baadae atarudi tena kitandani.

ITAENDELEA

Saa la 25 Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment