Saa la 25 Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE (AMATA GA IMBA)
Simulizi : Saa La 25
Sehemu Ya Pili (2)
€ € € €
Mama Njiku na Mama Vituko walitokea kuwa marafiki sana japokuwa walitofautiana katika mtiririko wa maisha, Mama Njiku mwalimu aliyeomba kustahafu kwa ajili ya mapenzi kwa mumewe leo hii amekuwa mfanya usafi katika stendi ya mabasi ya kuelekea mikoani eneo la Misuna, vumbi na jua vikimuakia lakini alifanya yote ili watoto wake wapate japo chakula na mwingine aliyeko shuleni aendelee kusoma. Alikwishaizoe a hali hiyo na kuona kila kitu ni kawaida kabisa, ucheshi wake ulimfanya kufahamiana na watu wengi sana, moyoni mwake hakuwa na kinyongo na mtu yoyote, si mumewe wala aliyemuibia mumewe.
Furaha yake iliongezeka alipokutana na Mama Vituko na kumchukua nyumbani kwake, mwanamke mjane mwenye watoto wawili aliyetoroka nyumbani baada ya kutakiwa kurithiwa na shemeji yake na kunyang’anywa mali yote aliyochuma na marehemu mumewe kwa jasho na miba, leo hii anajikuta akipoteza kila kitu na kubaki na watoto wake hawa wawili. Kwa kuwa hakukuwa na nafasi tena katika kampuni anayofanyia kazi mama Njiku hivyo ilimlazimu Mama Vituko kuchekecha akili nini cha kufanya ili kujimudu kimaisha kuliko kuwa mzigo kwa mama Njiku. Katika kanga yake ya Mombasa aliyovaa alikuwa amefungia hela aliyotoka nayo kijijini, hela hii shilingi laki moja aliiwekeza karibu miaka mitano iliyopita hakujua lini itamsaidia lakini sasa aliona kuwa wakati umefika, alipoongea na shoga yake huyo walikubaliana kuanzisha mgahawa, Mama Njiku alikuwa pia na akiba kidogo wakachanganya na kutafuta eneo karibu kabisa na soko la mitumba katikati ya mji wa Singida, maisha mapya yakaanza. Japo haikuwa rahisi, mwanzoni chakula kiliwadodea san asana na walikimwaga kila kukicha lakini mama Vituko alimpa moyo shoga yake kwamba ipo siku mambo ya tanyooka ‘mvumilivu hula mbivu’ hivo hivo waliendelea kujikongoja katika biashara yao ya chakula.
Siku moja aliingia mama mmoja katika mgahawa huo, alionekana wazi jinsi alivyochoka na kuchanganyikiwa tangu usoni mwake, aliketi kwenye kibenchi kidogo ndani ya mgahawa huo na kujiinamia kama mtu anayetafakari kitu.
“Karibu dada, tukusaidie nini?” Mama Vituko alimuuliza.
Yule mama aliinua uso na kukutana macho na mama huyu anayeonekana kuzeeka kwa matatizo na si umri, alitikisa kichwa kuonesha ishara ya kuwa hakuwa anahitaji chochote,
“Mbona una huzuni sana?” Mama Vituko alimuuliza tena na kumpa kikombe cha maji ya kunywa
“Basi japo maji” Mama Vituko alimpatia maji ya kunywa, na yule mama akayapokea na kunywa kidogo kisha akaweka kikombe kile juu ya benchi lingine lililo mbele yake. Alimtazama mama Vituko jinsi anavyohudumia wateja wake na kuwasikiliza vizuri, hakuwa na lugha chafu kama walivyo mama lishe wengine, akajikuta anavutiwa na utoaji huduma wa mama huyu.
“Nimeibiwa kila kitu” yule mama alimueleza mama Vituko huku machozi yakimtoka
“Pole dada, basi usijali Mungu atakutazama kwa jicho la pekee” Mama Vituko alimueleza maneno hayo yule mama ambayo yalimchoma sana moyoni.
“Sina chochote!” yule mama alimwambia mama Vituko. Mama Vituko alijawa na huruma sana, akampatia chakula, kinywaji na baada ya mazungumzo mafupi kati ya wamama hawa, Mama Vituko alimpatia yule mama shilingi mia saba imuwezeshe kufika Manyoni japokuwa kwa jinsi alivyo mama yule haikuwa mtu wa kupewa mia saba.
“Nikifika nitakutafuta, nipe namba ya simu” yule mama alimuomba mama Vituko, lakini mama Vituko hakuwahi hata kumiliki simu maishani mwake hivyo alimpa namba ya mama Njiku na wakaagana.
€ € € €
Tuntu hakupenda tena kutembea mchana kutokana na tukio lile lakmchoma Ravi kwa kipande cha chupa, alijua atakapoonekana ni mawili aidha akamatwe na polisi au apigwe na vijana wa Kihindi maana kwa vyovyote alijua kuwa wanafahamu lililotokea. Daima mchana alikuwa akishinda feli kupaa samaki na kupata ujira kidogo wa kumuwezesha kula na lipomaliza alitafuta sehemu yenye maficho na kulala.
Usiku huu Tuntufye alikuwa na njaa sana kwa maana mchana wote hakuweza kufanya mpango wa kupata pesa, alishinda akilala tu alikuwa hajisikii vizuri hata kidogo, njaa ile ilimnyima raha na kumfanya atoke katika maficho yake usiku mnene, alitembea taratibu kwa mwendo wakuogopa, njia nzima alikuwa peke yake aliowaona ni walinzi tu magari machache yakipita, hakujua anaelekea wapi wala anatafuta nini maana kwa muda huo kila mtu alikuwa amelala, kila ofisi ilifungwa. Aliendelea na safari yake mpaka maeneo ya Kilimanjaro Hotel, akafikiri labda akiingia hapo atapata chakula kwa kuwa alijua siku zote kuwa katika hotel huwa kuna chakula, alipofika getini walinzi walimfukuza kwa fimbo asiingie atasumbua wageni usiku huo. Tuntu hakubisha aliondoka na kuzunguka mtaa wa nyuma yake, alifikiri aende Kisutu kwa ombaomba wengine ili akapate japo kama kuna mwenye kipande cha mkate, katika pitapita ile akakutana na kundi la wasichana waliotawanyika barabarani, kila mmoja alionekana kana kwamba hamfahamu mwingine, mavazi waliyovaa yalimstua Tuntu walikuwa kama wako uchi, Tuntu aliogopa na kujificha ili wasimuone akijua hawa wanaweza kuwa si binadamu.
“We njoo hapa!” Tuntu alisiki sauti ikimwita nyuma yake, bila kuangalia alitimua mbio huku akipiga kelele za kuomba msaada, akiwa katika barabara ya Ohio Tuntu alitimua mbio huku akiangalia nyuma kama wanamfuata.
Kelele za msuguano wa tairi za gari na lami vilisikika usiku ule na kufuatiwa na kishido kikali, Tuntu alipaishwa juu kidogo na kudondokea kwenye boneti ya gari ile, Ajali!
Mama wa kizungu aliteremka kutoka ndani ya gari ile akifuatiwa na mwanaume wa kizungu pia, wote kwa pamoja waliwahi kumchukua Tuntu ambaye alikuwa hajitambui kwa muda huo, alikuwa amelala kimya.
“Is she dieng?” yule mama wa kizungu alimuuliza mumewe kwa lugha ya kiingereza kama amekufa au la
“For sure, I don’t know” alijibiwa na yule mwanaume akimaanisha kuwa hajui, huku akiwa amembeba Tuntu mikononi mwake alimpakia katika kiti cha nyuma cha gari hiyo, aligeuza gari kwa kasi na kurudi alikotoka kupitia barabara ya Ally Hassan Mwinyi walipofika Las Vegas Casino walikunja kulia na kueleke hospitali ya Aga Khan.
€ € € €
“Da’ Zai, ina maana hiyo kazi yako mnaingia usiku tu?” alihoji Ashura kama kawaida yake alipomuona Zai anajiandaa mida ya saa mbili usiku kutoka.
“Ee mimi nipo usiku siku zote lakini wapo wanaoingia mchana” Zai alijibu huku akitupia kiboksi Fulani kidogo mkobani
“Da Zai, hiyo nini?” aliuliza Ashura akioneshea kile kiboksi
“Ee na wewe yatakushinda, mjini hapa” Zai alijibu huku sasa akiwa anamalizia kuvaa kiatu cha mwisho “ Kesho nitaenda kuwatembeza mjini mmesikia?” alimalizia bila kusubiri jibu aliondoka.
Zai aliondoka na kuwaacha Ashura na Kautipe katika kile kijichumba kidogo wakiwa hawana la kufanya, waliogopa kutoka nje wakijua watapotea maana jiji hili lilikuwa na mishemishe nyingi kuliko Iringa walikotoka.
Malogo, alitokea kuwa mwanafunzi mwenzye bidii na akili sana shuleni hata waalimu walimstaajabia anagali bado darasa la kwanza, bruda Fransisko alikuwa akimpenda sana motto huyu, alikuwa akimfundisha mambo mengi sana na Malogo alikuwa msikivu sana, akiwa anacheza na watoto wenzake daima alikuwa makini kuwaelekeza kucheza vizuri na wenzako walipokorofishana alikuwa wa kwanza kusuluhisha, alikuwa Mpatanishi. Kitu kimoja tu ambacho Malogo alikikosa ni ndugu, labda kwa mabali alimuona mama yake mpaka dakika ya mwisho, kumbukumbu ya dada yake haikurudi kabisa kichwani kutokana na umri aliokuwa nao wakati ule, hakumjua baba wa ndugu mwingine, kwake bruda Francis alikuwa ndiyo kila kitu.
Walipokuja kutembelea kituo hicho watu kutoka mataifa ya nje walivutiwa sana na Malogo, na waliangusha machozi pale waliposikia kuwa Malogo aliokotwa tu mitaani huko katikati ya mji, hii iliwafanya wamkumbatie daima kwa upendo wenye mguso, hata msichana mmoja wa Kijerumani alijitolea kumsomesha, hiyo ikawa ni fursa kubwa kwa mtoto huyu masikini kumpata msaada huu kwa maana wengine wote walikuwa wakifadhiliwa lakini yeye tu alikuwa amekosa mfadhili, lakini daima Mungu hamtupi mja wake.
Sasa we sikiliza! Mi nataka unitafutie kabinti kadogodogo ambako bado hakajajua sana, umenielewa?” Pedeshee Masharubu aliongea kwa sauti ya kilevi akiwa ndani ya gari yake ndogo aina ya Peugeot 406, hakupenda kushuka kuangalia wasichana hao waliojipanga hapo, yeye moja kwa moja aliongea na mmoja wao kwa mtindo wa kumrushia maneno. Zai alikuwa upande wapili wa barabara hiyo lakini aliisikia kwa makini sauti hiyo ya kilevi ya Pedeshee Masharubu,
“Hakuna! Ukinitafutia utapata donge nono, nyie si mnanijua mimi Pedeshee Masharubu” aliendelea kuongea na hakika sauti yake tu ilikuwa inatosha kukujuza hata wewe usiowajua walevi. Zai alizunguka haraka upande ule baada ya kusikia ‘donge nono’,
“Pedeshee…” Zai aliita huku akitokea kwa nyuma ya gari ile.
“Ee… Beibiii” Pedeshee alijibu kimahaba na kumpa mkono Zai
“Niambie mtoto mzuri, ila we umezeeka” Pedeshee alimkejeli Zai huku akimpigapiga makalioni.
“Sasa! Mi nna dili, kuna kitoto mi naweza kukuletea” Zai alimueleza Pedeshee
“Enheeee! We umenikuna kabisa” Pedeshee alijibu kwa furaha aliposikia dili ya Zai “panda gari tuongee biashara” alimalizia. Zai akafungua mlango wa nyuma na kujitoma ndani huku akisindikizwa na misonyo mikali kutoka kwa wenzake.
“Mh, niambie un mtoto mdogomdogo” Pedeshee aliuliza
“Yupo, we sema utanipa ngapi zangu na ngapi za mtoto” Zai alichangamkia biashara huku kichwani akipanga kumuuza mmoja wale aliowaacha nyumbani.
“Pesa kitu gani!” Pedeshee alimwambia Zai huku akimuonesha wallet iliyonona noti nyekundu nyekundu tu mpaka inashindwa kufunga vizuri.
“Ok! Nipe dili” Pedeshee alimwambia Zai
“Nipe hela” Zai nae alijifanya jeuri kidogo. Walipoelewana Pedeshee aliondoa gari na kutokomea, waliiacha barabara ya Ohio na kuichukua Bibi Titi mpaka Nkurumah na kukunja kushoto kuelekea Chang’ombe, moja kwa moja gari iliegeshwa mbele ya klabu ya usiku ya Tandika By Night, na wawili hawa waliteremka na kuingia ndani, bar ailikuwa imeshona watu wa kila mtindo waliovaa kila mtindo wa nguo. Ndani ya klabu hiyo kulikuwa na nyumba yenye vyumba sita vya kupumzikia, vyumba vyenye kila huduma, sauti inayotoka huko nje haikuwa na ruhusa kupenya humo ndani, kiyoyozi masaa yote na maji ya moto yalipatikana japokuwa Dar es salaam ni joto.
“Kamlete nimthaminishe” Pedeshee alimuagiza Zai. Bila ajizi Zai hakulaza damu kwenye hela aliondoka na kuelekea ghetto kwake na kuwakuta wawili hawa wamelala fofofo, ‘nimchukue nani’ alianza kuwatazama vizuri, na hapo akapata jibu amuamshe Ashura, kwa kuwa Ashura alikuwa na mwili mdogo, japokuwa amefanya kazi za bar huko Mabanda ya CCM, Iringa; lakini mwili wake bado ulikuwa mdogo hata watu wengi hawakupenda kumsumbuasumbua. Ashura alikurupuka kutoka usingizini baada ya kumwagikiwa na maji ya baridi ambayo Zai aliyachota kwenye mtungi kwa lengo hilo
“Da’ Zai nini, bwana ah” Ashura alilalamika
“Amka wewe unalalalala kwani hapa kwa baba yako” Zai alimwambia Ashura ambaye alibaki katumbua macho
“Twende” alimuamuru
“Wapi? Da’ Zai, usiku saa hii” Ashura alilalamika
“Twende ukauone mji, mi si niliwaambia leo ntawapeleka mjini” Zai alisisitiza
“Ngoja nimuamshe Kau” Ashura alitaka kumuamsha Kaundime, kumbe hakujua hila za dada yao huyo.
“Vaa hii, fanya fasta tunasubiriwa, muache Kau alale, ye zamu yake kesho” Zai alimpa nguo nzuri Ashura na kumpodoa kidogo kisha wakatoka nje na safari ikaanza.
€ € € €
“Hali yake sio mbaya ila amepata mstuko tu” Dr Ramesh Shivj aliwaeleza Bwana na Bibi Robinson, ambao walimleta Tuntufye hospitali hapo. Kisha Dr Ramesh akachukua faili lake na kalamu, akaandika vitu fulanifulani ndani yake na kisha akawaita wale wazungu ofisini, wakaketi na kuwahoji maswali kadhaa
“Ok, jina anaitwa nani?” Daktari aliuliza, lakini akaona hakuna jibu sipokuwa wawili hawa walibaki kutazamana tu
“Aaah! Mmm! kwa kweli hatumfahamu, tumemuokota tu” alijibu Bi Robinson kwa Kiswahili chake cha kubabaisha.
Kati yao hakuna aliyejua jina la huyu mtoto, na wangejuaje wakati hakukuwa na mtu wa kumuuliza, walitazamana tena, sasa kwa dakika kama mbili hivi wote wakaanza kutokwa na machozi, kisha wakamgeukia yule daktari ambaye bado alikuwa akiwatazama akiwa na akalamu yake mkoni
“JaneElisabeth!” walitamka kwa pamoja bila kutegemea. Daktari akaandika jina lile katika faili lake na baada ya hapo akaliweka jirani kabisa na alipolala Jane mpya ‘Tuntufye’.
Jane Elisabeth Robinson, alikuwa ni mtoto pekee katika familia yao, Bi Robinson alishindwa kuishi na mumewe baada ya kuonekana hashiki mimba tangu walipofunga ndoa yao huko Kansas, Marekani. Kutokana na utaalam wa kitechnolijia katika dunia ya kwanza waliweza kupata tiba ambayo ilirejesha uzazi wa mama huyu na baada ya miaka kumi ya ndoa yao walipata mtoto wa kike, furaha iliyotawala nyumba yao haikuwa ndogo, walimtunza kama mboni ya jicho lao, na kwa kuwa daktari aliyewatibia katika kliniki maalumu ya afya ya uzazi huko Vienna, Austria, aliwaambia ‘hamtazaa mtoto zaidi ya mmoja’. Alipokuwa na umri wa miaka mine alianza shule ya awali ‘elementari school’ katika mji wa Alkansas uko huko Marekani. Alikuwa kila siku akichukuliwa na basi la shule kwenda na kurudi, akifika nyumbani wazazi hawa walifurahi kumuona motto wao huyu waliyempenda sana ‘lakini wewe ukimpenda na Mungu atampenda zaidi’. Siku isiyofahamika na yoyote katika uso wan chi ilifika. Siku hiyo iliyokuwa na baridi kali, ukungu ulijaa kila mahali, asubuhi hiyo Jane alikuwa akienda shuleni, alichokuwa akisikia ni honi tu za basi la shule lakini basi lenyewe hakuliona ‘Jane Jane come quickly’ watoto wenzake walimuita, na wito huo ndiyo ulimfanya Jane kuingia barabarani ili kuwahi basi lile upande wa pili, ‘kifo hakina breki’. Hata kelele za breki hazikusikika, Jane aligongwa na gari iliyokuwa inapita eneo hilo na kupoteza uhai palepale. Habari zilipofika kwa wazazi wake, ilikuwa kazi kubwa kuwatuliza, laiti ingekuwa kwetu, tungesema ‘kuna mkono wa mtu’. Kila aliyemjua Jane alihuzunishwa sana na msiba ule, lakini basi, Wazaramo hujifariji kwa kusema ‘abwelile kabwela’.
Bw na Bi Robinson walibaki hawana mtoto kwa miaka yote, na baadaye wakapata safari ya kikazi kuja Tanzania.
Siku ya tukio walikuwa wakitokea Bagamoyo mapumzikoni, kurudi nyumbani kwao maeneo ya Garden katikati ya jiji, ndipo walipomgonga mtoto huyu, hawakuwa na jinsi zaidi ya kumsaidia, na sasa hapo hospitali walijikuta wakimkumbuka binti yao Jane aliyefariki kwa ajali kama hiyo, walilia sana na kufarijiana, nafsi zao ziliwasuta kwa kuwa dreva aliyemgonga Jane alifungwa kwani Bw na Bi Robinson hawakukubali hata kidogo, sasa limekuja kwao, nao limewatokea lilelile.
€ € € €
Simu ya mama Njiku iliita, alipoitazama hakuijua namba ile, kwa maana ilikuja tupu bila ya jina, aliitazama vizuri namba ilie lakini ilikuwa ngeni kabisa. Moyo wake ulikwenda mbio kutokana na simu hiyo ambayo iliita mara kadhaa na kukatika kisha kuanza tena. Kwa woga Mama Njiku aliinua simu ile, akitetemeka mikono alibonyeza kitufe cha rangi ya kijani na kuilekeza simu hiyo moja kwa moja sikioni
“Halo!” aliitikia mama Njiku kisha akatulia simu sikioni kusikiliza upande wa pili unasema nini.
“Aaa, ndiyo (…) ametoka kidogo mimi ndiyo nipo” Mama Njiku aliongea na mtu wa upande wa pili, na baada ya muda kidogo wa maongezi hayo alikata simu na kuendelea na kazi yake ya kuhudumia wateja.
Muda si mrefu mama Vituko alirudi kutoka sokoni na kuungana na shoga yake huyu katika kazi yao ya kila siku, baada ya kupungua kwa wateja mama Njiku alimueleza mama Vituko juu ya simu iled iliyopigwa kipindi ambacho yeye, mama Vituko hakuwepo lakini ilikuwa kwa ajili yake.
“Shoga, kuna simu ilipigwa hapa” Mama Njiku alianza kumueleza mama Vituko huku akirekebisha kanga yake ili imkae vizuri kiunoni kisa akaendelea “amesema anaitwa mama Minja”.
“Aaa si ni yule mama nilikusimulia” mama Vituko alijibu kwa kuvuta sauti kidogo kama kawaida ya akina mama.
“Sasa ngoja nimbip uongee naye, ana shida na wewe” Mama Njiku akabip ile namba na mara tu simu ile ikapigwa, mama Vituko aliipokea na kuongea na mama yule kwa dakika kadhaa kisha akarudisha simu kwa mama Njiku akiwa na uso wa furaha.
“Vipi mwenzangu, mbona una furaha hivyo?” mama Njiku alimtupia swali shogaye
“Mungu hamtupi mja wake shoga” mama Vituko alojibu huku mikono yake akiishikamanisha kana kwamba yupo katika sala Fulani.
“Mh, hebu tuketi kwanza unipe umbea” Mama Njiku akatamka hayo huku akimshika mkono shogaye, wakaketi katika benchi na kuanza kupiga soga juu ya kilichojiri kupitia simu hiyo.
Mama Minja ni mwanamke mjasilia mali, mwenye makazi yake huko Manyoni, anamiliki maduka mbalimbali na ana majumba ya kupangisha, hakuna mwanamke asiyemjua mama Minja huko Manyoni kwa jinsi alivyowainua wanawake wengi kiuchumi. Kila mtu alimshangaa sana kwa moyo wake huo, daima aliwakusanya akina mama wenzake na kuwafundisha juu ya ujasiliamali mdogo. Wengi wao waliibuka kimaisha kutokea hapo na siku zote hawatoacha kumshukuru mama Minja.
Siku hiyo alifika mjini Singida kwa ajili ya kufanya mambo yake ya kibenki kwa kuwa yeye ni mfanya biashara mkubwa. Kwa kuwa hapendi makuu siku hiyo alikuja kwa usafiri wa kawaida tu, alipofika kituo kikuu cha sokoni alishuka katika daladala ile ili taratibu aelekee katika benki ya CRDB, kabla hajafika mbali, vijana wa kijiweni walimuona na kumuweka kwenye target, alipokaa vibaya tu pochi yake ya mkononi iliyokuwa na pesa taslimu, vitambulisho na akadi za benki ikwenda, simu kubwa ya kisasa walitambaa nayo. Mama Minja alipiga ngolo ya msaada na kujishika mikono kichwani, hakuna alichokiona isipokuwa wapiti njia ambao walibaki wameduwaa jinsi tukio lile lilivyofanyika kwa uharaka na wepesi wa hali ya juu.
Kuchanganyikiwa ndiyo tukio lililofuata baada ya hayo, alijikuta hana la kufanya, akitembea anayumba na kutaka kudondoka, moja kwa moja lijikuta kaingia ndani ya mgahawa huu wa mama Njiku na shoga yake, bahati siku hiyo alikutana na mama Vituko. Ukarimu aliouonesha mama Vituko, ulimgusa mama Minja toka ndani ya moyo wake, na hapo ndipo alipoanza kufikiri juu ya mama huyu na mwenzake ambao wanaendesha mgahawa huo kwa shida ilimradi maisha yaende. Kutokana na uzoefu wa mama Minja, alielewa kabisa kuwa kwa hali ilivyokuwa ya mgahawa huo daima wateja watakaopata ni walewale wa hali ya chini kama wapiga debe, waendesha daladala, wabeba mizigo kidogo na wauza nguo.
€ € € €
Zai alizihesabu pesa alizopewa katika bahasha na Pedeshee, si haba shilingi za Kitanzania elfu themanini. Siku aliiona imemnyookea sana kwake, alizishika na kufanya kama anajipepea na pesa hizo. Alizihesabu tena na tena kisha akachomoa noti mbili nyekundu na kuziweka katika sidiria yake na zile sita akazitia mkobani ‘hakai mtu bure, mi nikulishe tu, we kazi yako kula kulala, nyooo”sonyo fupi lilisindikiza wazo hilo. Alitazama mezani akakuta bado kinywaji chake hakijaisha kinamhitaji, akanyanyua chupa ile ya kijani na kujimiminia chote aliposhusha chupa ile ilibaki tupu, akaweka mkoba wake vizuri na kutoka nje ya club hiyo, gari ya Pedeshee haikuwa pale alipoiacha, Pedeshee alikua kaondoka na Ashura baada ya kurubuniwa na Zai kuwa mzee huyo alikuwa anahitaji msichana wa kazi na Ashura akaona maisha si ndiyo haya, kazi inakuja yenyewe, akaondoka na Pedeshee huyo, Ashura asijue kinachomkabili.
Ashura alitulia tuli kwenye kiti cha mbele mkono wa kushoto wa Pedeshee Masharubu, muziki laini wa Lionel Richie ulikuwa ukisikika kutoka katika redio iliyokuwa ndani ya gari hiyo ya Kifaransa, ulaini wa kiti hicho ulimfanya Ashura kuanza kusinzia kwa mbali, hakuna aliyeongea mpaka muda huo, wote walikuwa kimya, Pedeshee alikuwa na simu yake muda mwingi huku akiendesha kwa mwendo wa wastani. Baada ya kuongea maneno kadhaa katika simu hiyo aliiweka kwenye kikasha maalumu kilichoshikamanishwa na kioo kikubwa cha mbele, akautoa mkono wake kwenye gia na kumshika Ashura pajani huku akiutambaza mkono ule kuelekea juu karibu kabisa na kiuno cha Ashura. Mwili wa Asura ulisisimka na akautoa mkono wa Pedeshee huyo huku amekunja sura.
“Aaaa mrembo nini tena?” Pedeshee alimtupia swali kwa lafudhi ya kubembeleza, kisha akaurudisha mkono wake tena pajani kwa Ashura. Ashura aliogopa sana, ijapokuwa aliwahi kufanya kazi za kuuza pombe huko kwao Iringa lakini hakuwahi kushikwashikwa na mwanaume kiasi hiki mpaka akapewa jina ‘sista’. Leo hii mwanaume huyu, umri wa baba yake, anaanza kumpapasa katika mapaja yake.
“Niache!” aling’aka Ashura huku akiutoa mkono wa Pedeshee pajani kwake kwa nguvu, mkono ule ukagonga kwenye kirungu cha gia, Pedeshee akaugulia maumivu kidogo.
“Hivi we binti, zimo kweli?” aliuliza kwa ukali
“We unanishikaje huku!? Huoni hata aibu” Ashura alimkaripia Pedeshee
“Eh! We mkali ee? Usijali huo ukali utaisha tu”Pedeshee aliendelea kumsemesha Ashura. Gari ilipaki maeneo ya Ubungo, mbele kulikuwa na jingo refu lililokuwa likiwaka taa za aina aina, mji ulikuwa mtulivu kwa upande huo hakuna vurugu isipokuwa watu wachache waliopita huku na huku.
“Nifuate” Pedeshee alimuamuru Ashura huku akizipanda ngazi za jengo hilo.
“Ndio, Mzee wa kazi” msichana mrembo alimkaribisha Pedeshee kwa lugha ya utani
“Kama kawaida, palepale” Pedeshee alitoa pochi yake mfukoni na kumpatia pesa msichana yule.
“Hamna shida naona leo una Chick” msichana yule alimtania Pedeshee huku akitoka upande wakaunta na kuzungukia upande wa pili na kumuita Ashura “Kadada nifuate huku”. Ashura hakuju kinachoendelea, alimfuata dada yule huku akipiga fikra kuwa labda kesho na ye atakuwa mmoja wa madada anaowaona hapo wamependeza ndani ya suti zao. Moyoni alimshukuru sana Zai kwa moyo wake huo wa kumtafutia kazi kwa mtu huyu ‘nenda na huyu baba kuna kazi atakupa’ maneno ya Zai yalimrudia Ashura mara kwa mara.
€ € € €
Baada ya wiki moja, Tuntufye aliruhusiwa kutoka hospitali, Bw na Bi Robinson hawakuwa na jinsi ilibidi wamchukue kwenda kuishi nae nyumbani kwao mpaka atakapopona kabisa.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake Tuntu aliingia ndani ya jumba la kifahari lenye kila kitu hata vile ambavyo hakupata kuviona vilikuwamo ndani hapo, alishindwa hata ni wapi pa kukanyaga mguu wake katika sebule hiyo, maana usafi wa marumaru zilizobandikwa chini hapo hazikustahili kukanyagwa naye. Alisita, mlangoni hakujua ni nini anatakiwa kufanyam, alibaki kaduwaa kwa sekunde kadhaa. Tuntu alihisi kama anaingia peponi, akifikiria tu kuwa pale kaletwa kwa gari zuri, gari ambalo mara nyingi aliyaona yakipita tu barabarani, na hakuwahi kufikiri hata siku moja kuwa ipo siku angeweza kuketi ndani ya moja ya mgari haya. Fikra ziliendelea kumzunguka kichwani, tangu alipotoka na mama yake pale kwa mjomba wake, hakuwahi tena kuingia ndani ya nyumba ya aina yoyote ile hata iwe kibanda cha nyasi. Siku hii kwake ilikuwa ni siku ya ajabu sana hakuwahi kuifikiria kama ingeweza kutokea, ama kweli, mshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Jane !!” sauti iliita kutoka ndani ya jumba hilo lakini muitaji hakuonekana. Tuntu alibaki kasimama pale mlangoni hajui nini cha kufanya, huku akiwa na fimbo moja ya kutembelea katika mguu wake wa kushoto, alimuona mama mmoja mnene, mweupe, akitokea katika moja ya milango ya nyumba hiyo.
“Jane, mbona nakuita muda wote upo kimya? Au hukunisikia?” Mama yule aliuliza kwa sauti kavu kidogo. Tuntu alibaki akimtumbulia macho tu, maana yote kwake yalikuwa kama mkanda wa filamu. Alibaki kujiuliza ‘ni nani Jane?’ lakini hakupata jibu.
“Nifuate mdogo wangu” yule mama alimwambia Tuntu huku akielekea alikotoka. Tuntu alijivuta taratibu hasa ukizingatia mguu wake wa kushoto bado ulikuwa ukimuuma.
“Fanya haraka! Mi nna kazi nyingi” yule mama aling’aka huku akimtazama Tuntu. Tumtufye alijitahidi hivo hivo mpaka ndani ya chumba kile. Chumba cha wastani kilichokuwa na kitanda kipana cha chuma, meza ndogo ya kusomea na midoli ya kuchezea watoto.
“Hiki ndiyo chumba utakachokuwa unalala mpaka utakaporudi ulipotoka, ole wako uchafue hizo shuka, si unaona zilivyo safi” yule mama alitoa maelekezo hayo kwa ukali. Tuntufye ‘Jane mpya’ alikielekea kiti kidogo kilichokuwa katika meza hiyo ya kusomea na kuketi kwa taabu hasa kutokana na maumivu ya mguu na mbavu. Ijapokuwa alikuwa mahali pazuri na pa usalama, sasa aliona kama yupo kifungoni hasa kwa ukali wa muda mfupi aliyouona kwa yule mama aliyemkaribisha. Tuntu hakuzoea kukaripiwa, hakuzoea kupangiwa hiki husifanye au hiki fanya, maisha yake yalikuwa daima ni kuamua mwenyewe, leo ntalala wapi, leo ntakula nini. Kutokana na makaribisho hayo, Tuntufye alihisi kuwa kumbe wanaoishi kwenye majumba makubwa wote wanaishi kama huyu mama, alijikuta akimuogopa sana, hata aliposikia sauti ya viatu vikitembea verandani alijua wazi kuwa labda mama huyo anakuja kwake, atamwambia nini sasa, alibaki kutulia. Usingizi wa dharula ulimpitia katika kijikiti kile na kusombwa na ndoto mbalimbali za kufurahisha na za kuhuzunisha.
Mlango ulisukumwa na kuwa wazi, Bi Robinson aliingia ndani yachumba kile na kumkuta Jane, amelala kwenye kiti kile kidogo.
“Salome!” Bi Robinson aliita.
“Yes Mom” yule dada mnene alikuja kwa hatua za haraka mpaka pale mlangoni alipo bosi wake.
“Kwa nini mtoto amelala kwenye kiti?” alimuuliza kwa lugha ya kiingereza, Salome alitaka kwenda kumchukua Tuntu lakini alikatishwa na bosi wake.
“No! muache, utamuumiza” Bi Robinson, alishikwa na huruma sana kumuona Tuntu pale alipolala. Alimtaka Sakome aondoke maana alielewa wazi kuwa Salome lazima ameshamuuzi Jane wake, kwa kuwa alimjua sana tabia zake hata wajapo wageni wake, huwa ni mchoyo na mbaguzi.
Bi. Robinson, alimnyanyua Jane taratibu na kumlaza kitandani. Bi. Robinson alitokea kumpenda sana Tuntufye ‘Jane’, hata alipomtuma dereva aende kumchukua hospitali, alitamani sana kama angekwenda mwenyewe lakini alikuwa na kazi nyingi ofisini, aliona siku haiendi kabisa, masaa yamesimama. Kitu kikubwa alichokitamani ni kuongea na Tuntu japo ajue ni wapi anapotoka na wazazi wake wako wapi. Alisubiri kwa hamu aamke ili japo asikie sauti ya mtoto huyu inafananaje, aliona wazi kuwa Mungu kamrudishia Jane wake katika mtindo mwingine.
Siku chache baadae…
Bi. Robinson alifuta machozi yaliyoshindwa kujificha ndani ya macho yake, mumewe alikuwa ameketi, kichwa kakiinamisha na mikono yake kuigemeza magotini pake akitafakari hili na lile. Bi. Robinson alimpigapiga Jane mgongoni kama kumtuliza kwa machungu aliyonayo. Moyo wake ulijawa na huzuni sana baada ya kusikiliza kwa makini juu ya maisha ya msichana Tuntufye.
Tuntufye ‘Jane’akishindwa kuedelea kusimulia hasa alipogusia juu ya mama yake “sijui yuko wapi na mdogo wangu Malogo” aliangusha chozi lililofuatiwa na kilio cha uchungu kati ya wote watatu, hata aliyekuwa mkalimani alishindwa kujizuia.
“Kwa nini unaniita Jane? Mimi jina langu ni Tuntufye” alimtupia swali Bi.Robinson, kabla ya kulijibu kwa nza alitulia kimya kwa sekunde kadhaa.
“Hatukujua jina lako halisi” Bi. Robinson, alinyanyuka na kuingia ndani, baada ya dakika chache alitoka na picha mkononi, akampa Tuntu, picha ya motto wa kike wa kizungu aliyevalia sare nadhifu za shule, tabasamu pana lililomfanya Tuntu naye kutabasamu.
“Huyu ndiye Jane Elizabeth Robinson, aliyekuwa motto wangu pekee” Bi. Robinson alimueleza Tuntu habari yote ya Jane, mara kwa mara alikuwa akitoa machozi.
Tuntufye, alijinyanyua kutoka kwenye kiti alichokalia, polepole alijitembeza huku akisaidiwa na gongo moja, kila mtu alimwangalia ni wapi alikuwa akielekea, alisimama mbele ya mti wa ua waridi, akachuma vikonyo vitatu vya ua waridi la rangi nyekundu. Jirani na mahali walipokaa katika uwanja mkubwa wa nyumba hiyo, kulikuwa na kila aina ya maua ya kupendeza, na pembeni kabisa kulikuwa na dimbwi la maji lililojengwa vizuri, hata ndege wa angani hawakuisha kutua hapo kupoza kiu baada ya nizunguko yao ya muda huku na huko. Tuntufye, alisimama mbele ya dimbwi hilo akachukua ua moja na kulirusha majini’
“Jane, upumzike kwa amani…” maneno hayo yalimtoka Tuntufye bila kutarajia na yaliwafikia wazazi wa jane bila shida, mara hii Bw. Robinson alitoa chozi. Tuntu akageuka na kurudi alikokuwa ameketi, lakini kwanza akaenda moja kwa moja kwa Bw. Robinson na kumpa ua mojawapo kisha akafnya vivyo hivyo kwa Bi.Robinson
“Jane yupo pamoja nanyi…” Tuntu alisema maneno hayo na kuanza kulia. Bw na Bi Robinson kwa pamoja walimkumbatia na kumbembeleza lakini hata wao walishindwa kuivumilia dakika hiyo. Walikumbuka tukio la mwisho alilolifanya binti yao wakati wakiwa huko Alkansas, USA.
kumbukumbu
Jane alitoka shule akiwa na furaha sana mpaka nyumbani ambako baba na mama yake walikuwa wakimsubiri kwa hamu, wakiwa katika bustani kubwa nje ya nyumba yao hiyo. Aina nyingi za maua zilikuwa hapo, moja kwa moja Jane aliliendea ua rose ‘waridi’ lililokuwa limechanua vizuri, alichuma vikonyo vitatu vya waridi jekundu na kumpatia moja mama yake, lingine baba yake na la tatu alipamba chumbani kwake.
Kitendo cha Tuntu kufanya vile, kiliwagusa sana na waliona huu ni muujiza kabisa kwao, ndiyo maana iliwaliza sana. Kiasili Bw na Bi.Robinson hawawapendi sana watu weusi lakini mara hii walijikuta wanashindwa wafanye nini. Kila mmoja kwa wakati wake alijiuliza ‘au Mungu anatujaribu?’. Sasa ndiyo waliamini kabisa kuwa Tuntu ni zawadi kwao kuwaondolea upweke katika maisha yao, kitendo cha mwisho kilichofanya na Jane Elizabeth siku moja kabla ya kufa kwake kwa ajali ya gari, leo kinakuwa cha kwanza kufanywa na Tuntu baada ya kutoka hospitali alikokuwa anatibiwa baada ya kugongwa kwa gari la wawili hawa.
“Siwezi kuishi na mwanaume kama wewe! Kila siku we unaumwa tu, tutakula nini ee?” sauti kali ya nyumba ndogo ya Mzee njiku ilipasua anga kupitia madirisha ya mbao za mninga yaliyopachikwa vizuri kabisa katika nyumba hiyo. Mzee Njiku, Afisa Elimu, alikuwa ameketi juu ya kigoda kidogo huku mikononi akiwa ameshika ungi akichambua maharage jioni hiyo, hakusema chochote isipokuwa kumwangalia tu mama huyo wa Kirangi kutoka Kondoa, akipayuka maneno makali.
“na ukiendelea kuumwa umwa utahama humu ndani, hapa sio Zahanati wala kituo cha afya” aliendelea kupayuka bila staha.
Hali ya Mzee Njiku ilidhohofu siku hadi siku, hakuwa na uwezo tena wa kufanya kazi, muda mwingi alikuwa akiutumia kulala tu, kama alitegemea faraja kutoka kwa mama huyu ambaye mwamnzo wa mapenzi yao hata bafuni alipelekwa akiwa kabebwa mgongoni, sasa alikumbana na vurugu. Amani iliondoka katika nyumba hiyo nzuri kuliko zote mtaani hapo aliyojenga kwa ajili ya nyumba ndogo iliyomfanya kusahau hata ndoa yake na kuhamisha maisha yote huku, ‘mwanamke si ndiyo huyu’, alijipa moyo na kujiachia hata kutekwa mwili na roho. Masikini Mzee Njiku, aliyejifanya ndege mjanja ambaye sasa kanasa kwenye tundu bovu. Alipokuwa ameshautwika ugimbi wake enzi hizo, alimuona mwanamke huyu kama Malkia wa Sheba kwa uzuri alonao, mapambo yake mwilini kama Yezebeli. Hakika mwanaume yeyote lijali; angenasa tu. Mzee Njiku alipoanza tabia za kunywa pombe hasa na rafiki zake hawa wapya ndipo alipoanza kumsogelea mwanamke huyu ‘mpe moja, bili kwangu’, ndivyo alivyoanza, kesho aliongeza, baada ya hapo alijikuta amezama kabisa kwa mwanamama huyu, aliyekuwa anaishi kwenye nyumba ya kupanga.
Ushauri wa rafiki zake ulikuwa mzuri sana kwake wakati huo ‘huwezi kuwa na nyumba moja’, naye alilewa na ushauri huo, ukizingatia, wakati ulipokuwa ukipenya sikioni na muda uo huo pombe ilipita kwenye koromeo.
Siku chache baadaye, Afisa Elimu akaonja asali, lo! Kwa nini asichonge mzinga?, kumbe hakujua kuwa nyuma ya urembo kuna rangi halisi na penye urembo pana ulimbo.
“Hatuna budi kumpeleka Hospitali!” Kaka wa Mzee Njiku aliwaambia ndugu zake baaada ya kuona hali mbaya ya mzee Njiku.
“Kaka, hospitali tutahangaika tu na kupoteza pesa zetu, tumezipata kwa jasho!” kaka mdogo aliongea kwa msisitizo huku akitoka sebuleni na kuelekea nje.
“Hospitali hamtaki twende, nikiwaambia tufanyeje mpo kimya, sasa mi nieleweje?” aliuliza kaka wa Mzee Njiku.
“Huyu amelogwa!” dada yake alilipua
“Ati! Amelogwa na nani?” kaka wa mzee Njiku aliuliza kwa kung’aka
“Hilo la kuuliza? Mkewe wa zamani kamloga huyu mzee” dada wa Mzee Njiku alishindilia msumari wa moto. Kila mtu alitahayari ndani ya nyumba ile, hakuna aliyesikilizwa. Kaka yao kila alichotaka kusema hakuna aliyeunga mkono hoja yake, kila mtu ‘jamaa kalogwa, jamaa kalogwa’. Dhana ya ushirikina ikachukua nafasi kati ya wanandugu wale, kikao kikavurugika, uamuzi ukapitishwa apelekwe kwa mganga kupiga ramli.
Alfajiri ya saa kumi na moja, kaka mdogo wa Mzee Njiku alitoka na gari yake aina ya Escudo Helly Hansen, pamoja nae ndani ya gari kulikuwa na dada wawili wa Mzee Njiku, mwenyewe Mzee Njiku pamoja na nyumba ndogo wa Mzee Njiku. Safari ilikuwa ni kuelekea kwa mganga maarufu, mganga Matomola kutoka Sumbawanga. Majira kama ya saa nne asubuhi walifika katika kijiji cha …………. Barabara ya kuelekea Tabora.
“Nimewaona tangu mbali saaaana, karibuni kilingeni, hapa ndo kwa mganga Matomola, kila mwenye shida huituwa hapa” Matomola alianza porojo zake za kiganga. Akachukua manyanga yake na kuanza kutikisa tikisa na kuongea lugha isiyoeleweka, pembeni yake alizungukwa na tunguli nyingi sana na pembe za wanyama mbalimbali.
“Mmmm! Kuna kazi kidogo, si mchezo” Matomola aliwaeleza wateja wake, mara baada ya kuchungulia ndani ya kibuyu kimojawapo.
“Tawile” wateja waliitikia.
“Ndugu yenu amelogwa” Matomola aliendelea kusema huku akipiga chafya kali sana
“Tawile”
“Nia yenu ni nini? Kumjua mlogaji, au kumuadhibu?” Matomola aliuliza, huku akiwaangalia kwa sura yake chafu iliyojaa masizi ambayo alijipaka uso mzima.
“Tawile”
Mzee Njiku alikuwa amekalishwa kwenye kigoda cha miguu mitatu huku akitetemeka kwa baridi. Kaka yake mdogo alibaki nje, ndani kulikuwa na dada zake pamoja na wifi yao.
Sokomoko alitikisa vibuyu vyake na yule msaidizi aliendelea kupigapiga manyaga kwa bidii zote, maneno ya ajabu yalimtoka Matomola kwa kasi kama cherehani ya Mchina.
“Mmmmm! Mmmmm! Mdugu yeni kalogwa” Matomola aliongea kwa sauti tofauti na ya mwanzo, akapiga chafya na kuendelea “aliyemloga ni mtu wa karibu sana”
“Tawile”
“Kuna mtu hampendi mzee huyu kwa sababu ya utajiri wake na kazi alonayo”
“Tawile”
“ Mke mkubwa ndiye aliyemloga ndugu yenu, baada ya kuachana na mali kumpa bi mdogo, yeye kaamua kumloga” Matomola aliongea kwa saut ileile.
Wateja wakashtuka kwa neon hilo la Mganga, wakatazamana wao kwa wao, kila mtu akimwambia mwenzake moyoni ‘si nilisema’.
€ € € €
Jua lilikuwa ni kali sana eneo la Manyoni stendi, Mama Vituko alikuwa akimtafuta mwenyeji wake lakini hasimuone. Akasogea kidogo kwenye kivuli karibu na duka dogo akanunua kinywaji kupoza koo. Tatizo hapo hakuwa na simu ambayo ingeweza kumsaidia kumpata mwenyeji wake, hakuwa na jinsi, ilibidi atulie kungoja mwenyeji wake muda atakaotokea.
Punde si punde, gari moja ndogo nyekundu iliingia stendi hapo, kwa kuwa hakukuwa na gari ingine haikuwa vigumu kuiona, ilitembea kwa mwendo wa taratibu sana na kusimama mahali Fulani, mwanamama nadhifu alishuka na kuelekea madukani. Mama Vituko alimwangalia kwa makini sana mama yule, hakuamini kama anayemuona ni Mama Minja au ndugu yake, mavzi aliyovaa ni ya gharama sana utafikili ‘first lady’, Mama Vituko alijikuta anaogopa hata kumsogele mwanamama huyu kwa jinsi walivyo tofauti. Kitenge alichovaa mama Vituko ni hiko alichonunuliwa na marehemu mumewe miaka minne nyuma, kilishaanza kuchoka kwa kupambana na sabuni kali za mara kwa mara kwani ndiyo kilikuwa kauka nikuvae. Akiwa anajishauri afanyeje kumkabili mwenyeji wake, alijikuta akishikwa bega na alipogeuka alikutana uso kwa uso na polisi mmoja wa kike. Mama Vituko alibaki kapigwa na butwaa akitazamana na binti yule aliyevalia sare za kipolisi zilizonyooshwa kwa pasi, na kunyooka kwelikweli.
“Samahani we ndiyo Mama Vituko?” aliuliza askari polisi.
“Ndiyo mimi mwanangu, unasemaje?” Mama Vituko alijibu kwa unyenyekevu
“Unatakiwa kituo cha polisi, maelezo mengine utayakuta uko huko” yule polisi wa kike aliondoka na Mama Vituko na kuelekea kituo kidogo cha polisi kilichopo hapo stendi.
“Huyu kweli mama Vituko!” aliongea polisi mwingine wa kiume aliyesimama katika sehemu ya mapokezi.
“Wanangu, mbona sijui kosa langu nimefanya nini?” Mama Vituko aliuliza huku machozi yakilowesha blauzi yake nyeupe aliyoinunua jana yake tu katika soko la mitumba.
“Mama hayo utauliza Mahakamani, sisi hapa ni kutekeleza wajibu wetu tu” polisi yule alijibu kwa mkato huku akiendelea kuandika andika kati kitabu chake kikubwa, hakujali hata ni nani anayeongea naye, ama kweli Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Mama Vituko alijikuta hana la kufanya, kutokana na kutokujua haki zake mbele ya polisi kama inavyowakuta Watanzania wengi, wanalundikwa selo, wanakamatwa na kupigwa bila kuambiwa makosa yao, na mwisho wanaozea jela wakati wanaostahili bado wanakula maisha mtaani. Haki za raia, nani wa kusimamia haki za raia? Kama ndiyo hao wanaokamata na kupiga watu ovyo, kuwabambikizia vipisi vya bangi, ili mradi tu utoe kitu kidogo. Kama huna kitu kidogo, basi we ndiye Mtuhumiwa namba moja, kweli haki inauzwa na sheria inanunuliwa.
Mama Vituko aliwekwa selo akiambiwa asubiri maelekezo mengine, maelekezo gani, kutoka kwa nani, lilikuwa ni swali lisilo na jibu, Mama Vituko alibaki kimya ndani ya kijichumba kile kidogo, akiwa hajui la kufanya kabisa, alitafakari hili na lile, nafsi yake ilimlaumu huyu na yule lakini wote aliwaonea tu, mwisho alijilaumu mwenyewe lakini bado hata yeye alijionea vilevile, alibaki kwenye giza kuu, giza lisilo na nyota wala mbalamwezi. Hakuonana na Mama Minja, isipokuwa ameishia selo, ambapo hajui nini hatima yake.
ITAENDELEA
Saa la 25 Sehemu ya Tatu
Also, read other stories from SIMULIZI;