Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
Simulizi : Tutarudi Na Roho Zetu?
Sehemu Ya Nne (4)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Baada ya hayo Kombora aliendelea na shughuli katika ofisi yake. Alipokea na kujibu simu na walkie talkie nyingi ambazo hakuona kama zilimsaidia chochote. Aliwasiliana na wenzake wa Zambia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Naijeria na kwingineko kujaribu kuona wamefikia wapi. Hakuna alichokipata Zaidi ya yale aliyotegemea, kwamba wananchi walikuwa wakitaabika na kulalamika mitaani katika hali ya hofu kubwa, kwamba hawakwenda hata kazini. Ilikuwa kama waliokuwa wakisubiri kifo na maafa hayo. Watu wengi walizifungulia redio na televisheni zao kusubiri habari mbaya kokote Afrika. Na kwamba ingawa vyombo vya habari vya dunia nzima viliendelea na ratiba zao kama kawaida, lakini ilikuwa dhahiri kuwa kuna jambo, zito na la kutisha, ambalo lilikuwa likisubiriwa na kila mtangazaji. Kombora aliachana na taarifa hizo na kuulizia maendeleo ya maofisa ambao aliwakabadhi jukumu la kumtazama Clay na yote anayoyafanya. Haikumpendeza aliposikia kuwa alikuwa katika hali ya kawaida, kama ambaye hakuwa na lolote la kufanya.
“Endeleeni kumwangalia kwa makini,” aliwaamuru
SASA ENDELEA
Ofisi ilikuwa haikaliki. Kila Kombora alipojaribu kutulia juu ya kiti, kiti hakikuelekea kuafikiana naye. Kila alipoinuka ili atoke, hakujua angeelekea wapi. Unawezaje kutulia na huku unahesabu saa kusubiri kifo au maafa ya kusikitisha ambayo ni aibu kwako, kwa taifa lako na bara lako zima? Aliendelea kutaabika kimwili na kimawazo, akipokea na kusikiliza habari kutoka sehemu mbalimbali. Mara zilimfikia habari za Joram na Nuru kuwa walikuwa wameingia Afrika Kusini na kuomba hifadhi ya kisiasa. Kwa kombora zilikuwa habari za kushangaza sana. Habari za kusikitisha. Habari zinazotia aibu. Joram Afrika kusini! Hata hivyo, alikwishachoka kushangazwa na habari za kijana huyu anayeitwa Joram. Mambo yote aliyokuwa akiyafanya, ambayo yaliwafikia watu wa habari, Kombora aliyasikia au kuyaona katika vyombo vya habari. Angeweza kumsifu Joram kwa mbwembwe zake ambazo ziliwafanya polisi wote wa miji mbalimbali na nchi zilizoendelea washindwe kumtia mikononi. Lakini kila alipokumbuka kuwa mbio hizo za Joram zilikuwa za kukimbiza akiba pekee za pesa ya kigeni alizoibia nchi yake alijisikia vibaya. Hayo yakifuatwa na tishio lililokuwa likizidi kusogea, vilimfanya ajilazimishe kuliondoa jina hilo akilini mwake.
“… Inspekta Kombora anaongea. Namba ngapi hiyo?…” alijibu sauti katika walkie talkie iliyokuwa mkononi mwake. Alipotajiwa namba alijikuta akisikiliza kwa makini zaidi. Ilitoka kwa kiongozi wa makachero ambao walikuwa wakifuatilia nyendo za Clay.
“… Inaelekea kama tutamkamata red handed, mzee. Sasa hivi anaunganisha mitambo yake ya mawasiliano…”
“Nisubiri. Nakuja mara moja.”
Dakika mbili tatu baadaye, Kombora alikuwa miongoni mwa polisi wanne waliokuwa katika chumba fulani katika hoteli ya Kilimanjaro. Chumba hiki kilikuwa cha nne kutoka chumba cha Clay. Hata hivyo, kutokana na mitambo waliyoitega kitaalamu, japo hawakuwa wakimwona, waliweza kumsikia anavyoongea katika chombo fulani cha kijasusi.
“Sikiliza mzee… sikia…” askari mmoja alimwambia Kombora huku akitweta.
“…Ndiyo. Ndiyo… nimefanikiwa kupanda katika majumba ya kutosha. Moja Ikulu.. hapa Kilimanjaro moja… jengo la IPS moja… Kitegauchumi… Muhimbili… Benki Kuu ya muda… Tipper… kiwanda cha Urafiki na sehemu mbalimbali muhimu. Tunachosubiri ni saa moja tu. Ikifika, kwa jinsi nilivyotega inaelekea jiji zima litalipuka. Mimi nitaondoka hapa wakati wowote…”
“Unasikia mzee?… Unasikia?…”
Kombora hakusubiri kumsikiliza afisa huyo. Aliwaamuru kumfuata kukiendea chumba cha Clay. Kinyume cha mategemeo yao waliukuta mlango ukiwa wazi. Naye alikuwa kaketi kwa utulivu juu ya kochi, gazeti mkononi. Yeyote ambaye angeingia bila ya kufahamu kinachotokea angemdhania kuwa alikuwa akisoma gazeti.
Aliwalaki Kombora na wenzake kwa utulivu wa kushangaza. “Karibuni. Vipi, mbona ghafla hivyo? Kuna habari mpya?” aliuliza.
“Inuka na uweke mikono yako juu,” Kombora alifoka, tayari akiwa na bastola yake mkononi akiifanya idadi ya bastola zilizomwelekea kuwa nne.
“Vipi Inspekta! Mbona sielewi?…”
“Mikono yako juu!” Kombora alinguruma.
Clay akainuka na kuiweka mikono yake angani.
“Acha gazeti.”
Aliliachia. Ndipo kilipoonekana kikasha kidogo chenye ukubwa wa kiberiti ambacho alikuwa nacho mkononi. Kombora alimsogelea na kuiweka bastola kifuani mwake huku akimwuliza kwa ukali, “Nini hicho?”
“Kwa nini Inspekta?… Hiki sikifahamu. Nimekiokota sasa hivi tu.”
Jibu hilo lilimchukiza Kombora kupita kiasi. Alijibu kwa pigo zito la ngumi ambalo lilitua barabara katika uso wake. Clay alipepesuka lakini hakuanguka, jambo ambalo lilimshangaza na kuzidi kumchukiza Kombora. Pamoja na umri wake mkubwa hakumbuki lini alipata kumpiga mtu ngumi nzuri kama hiyo na mtu huyo akaendelea kusimama. Akarudi nyuma hatua mbili na kumwamuru askari mmoja amkague. Ni hapo lilipotukia jambo ambalo halikutegemewa. Kwa wepesi usio kadirika Clay alichomoa kisu na kumchoma askari huyo. Kisu cha pili kilimkwaruza Kombora mkononi. Papo hapo alichupa mlangoni akienda zake. Lakini hakuwa mwepesi zaidi ya risasi tatu za polisi ambazo zilimfanya aanguke mlangoni kifudifudi. Wakamvuta chumbani na kumlaza kitandani bila kujali damu zilizoendelea kumtiririka kutokana na majeraha makubwa ya risasi hizo. Wakamkagua na kumpokonya bastola nyingi na visu sita zaidi.
“Sema haraka, ulikuwa ukiwaarifu nini mabwana zako?” Kombora alimwuliza.
“Itakusaidia nini Inspekta?” alihoji kwa udhaifu na maumivu makali. “Huna unaloweza kufanya. Bado saa chache sana. Kama utapenda kufahamu nilikuwa nikiwaarifu mafanikio ya kazi yangu. Nimefaulu kutega katika majengo mbalimbali. Wakati utakapowadia mlipuko utakaotokea utakuwa wa kupendeza sana. Laiti ningekuwa hai nione na kusikia vilio vyenu!”
Kombora hakujua aseme nini. Hakujua kama ilimpasa kumtisha au kumbembeleza mtu huyu ambaye kila dalili ilionyesha kuwa angekufa haraka. “Mpelekeni hospitali,” aliamuru.
“Ya nini Inspekta? Sipendi kufa kwa moto… naweza kufa kwa njia nzuri zaid…”
Kombora hakumsikiliza. Akamgeukia askari wake aliyekuwa mahututi. Yeye pia hakuwa na dalili ya kuishi sana. Kisu kilimwingia kifuani upande wa moyo. Jambo hilo lilipandisha hasira za Kombora dhidi ya Clay. Akamgeukia na kumtazama usoni.
Alimwona akitafuna kitu. Akakumbuka majasusi mengi ya utawala huo yalivyokuwa yakiishi na sumu kali mdomoni. Matumaini ya kupata habari zozote za haja yalikuwa mbali. Akamgeukia na kumwuliza taratibu, “Sema tafadhali… tunawezaje kuzuia mkasa huu ulioko mbele yetu?”
Clay alicheka kwa maumivu huku akijikongoja kusema, “Labda uchukue furushi moja katika mfuko wangu ukaangalie unachoweza kufanya.”
Moyoni alifahamu kuwa mfuko huo ulikuwa na akiba nyingine ya vile vigololi, ambavyo alikuwa hajamaliza kuvitega. Hivyo, aliamini kuwa Kombora angevifikisha Central Police na kulifanya jengo lao liwe moja ya majengo mengi yatakayopigwa na radi hii iliyoundwa na binadamu. Hilo likamfanya ajitahidi kucheka, tena kifedhuli huku akisema kwa tabu, “Usijali Inspekta… muda si mrefu tutakutana huko kuzimu… Tutakuwa wengi sana… mimi natangulia…”
Kombora hakuona kama mtu mwenye roho ya kinyama kama huyo alistahili kufa kiungwana kiasi hicho. Hivyo, akaichomoa bastola yake na kumsindikiza akhera kwa risasi ya kichwa ambayo ilimfumua kabisa fuvu lake.
Walitazamana kwa macho yaliyojaa hisia. Mmoja akitabasamu, mwingine akiinama kwa haya. Mmoja akainua mkono wake na kuutua juu ya paja la mwenziwe. Mwingine akaufunika mkono huo kwa kiganja chake na kuanza kuutomasatomasa kimahaba. Mkono wa pili ukainuliwa na kutua juu ya kifua cha mwenziwe, ukitafuta uwezekano wa kupenya, ndani ya mavazi yake. Vijilima viwili, laini, vilivyosimama kwa namna ya kupendeza macho katika kifua hicho havikuruhusu mkono huo kupenya kwa urahisi. Mkono ukaviacha vilima hivyo na kuanza kufungua vifungo vya vazi hilo. Mara kimojawapo cha vilima hivyo kikajitokeza, kikimeremeta kwa wekundu na uhai wake. Wakatazamana tena. Kisha akakisogeza kinywa chake na kukifanya kimeze chuchu za kijilima hicho. Mdomo ulipohama kifuani ulikwenda katika kinywa cha mwingine ambako ulianza kunyonya ulimi uliokuwa ukisubiri. Mara wakaachana na kuanza kuvua mavazi yao moja baada ya jingine. Tahamaki wakawa wamesimama kama walivyozaliwa, kila mmoja akishangazwa au kuridhishwa na uzuri wa mwingine. Kisha wakakumbatiana kwa nguvu. Mmoja aliguna, mwingine akanong’ona.
“Nuru…”
“Joram…”
Kitanda kikawalaki na kuwafariji. Hawakuhitaji shuka. Walikuwa kama walivyohitaji kuwa, wakifanya mapenzi kwa namna ambayo walihitaji, kwa kiwango ambacho hakikadiriki. Vitendo vyao vilifuatiwa na maneno ya mapenzi ambayo yalisikika kwa sauti ya kike, mara chache sana yakijibiwa kwa sauti nzito ya kiume.
Kisha ghafla, vitendo na sauti zao vilitoweka machoni na masikioni mwa mtu ambaye alikuwa akishuhudia kila kitendo chao, “Shit,” mtu huyo, kwa jina Von Iron, alifoka. Alikuwa akikifuatilia kila kitendo kwa tamaa kubwa, huku akiburudika. Lakini haikuwa burudani rahisi kwani kuona huko kulimfanya atetemeke mwili mzima na roho kwa uchu na tamaa, huku jasho likimtoka na damu kuchemka. Alijaribu kujifariji kwa kuubembeleza uume wake kwa mkono wake huku macho yake yakiwa yamekazwa kutazama katika mtambo wake. Mkono haukuwa na faraja yoyote. Mara mbili aliutoa na kuufuta kwa leso yake kwa jinsi ulivyochafuka kwa manii yaliyomtoka kwa wingi. Alitamani aondoke hapo na kuacha kutazama vitendo hivyo, lakini macho hayakumruhusu. Akaendelea kutazama, akiendelea kujifariji kwa mkono wake. Moyo wake ulikuwa unadunda na alishindwa kustahimili zaidi ya mkono kujifariji. Alihitaji mwananmke. Na si mwanamke yeyote isipokuwa yule mwanamke aliyekuwa akimtesa sana, mwanamke wa Kiafrika; Nuru.
Mwanamke mweusi! Von alishangaa kimoyomoyo. Ana wazimu? Hata hivyo, alijua kimoyomoyo kuwa asingestahimili hadi atakapompata. Alijifariji kwa kujiambia kuwa angemwua baaada ya kutenda naye mara moja tu, ili yasije yakampata yaliyompata hayati baba yake.
Ni tamaa hiyo ambayo ilimfanya akatae katakata madai ya wenzake waliomtaka amruhusu Joram na msichana wake wauawe mara moja.
“Ni jambo la hatari lisilo na busara kumwacha hai mtu hatari kama huyo hasa katika kipindi hiki,” mwenzake mmoja alimwambia. “Japo amekimbia kwa na hawezi kurudi, lakini ni mtu ambaye hafai kuaminika. Kumwacha hai ni sawa na kuishi na nyoka chumba kimoja.”
“Atafanya nini?” Von alikuwa amekanusha. “Hana awezalo kufanya. Bado saa chache sana tutamleta katika televisheni atazame nchi yake inavyoteketea. Baada ya hayo tutamchinja kwa urahisi kama kondoo. Usijali. Waache waishi usiku mmoja zaidi.”
Usiku ni kitu alichokuwa akikisubiri kwa hamu, akikumbuka yale aliyoyaona usiku wa jana. Na ulipowasili hakuwaalika wenzake kwenda kutazama. Kwa kisingizio cha “Kumchunguza kwa makini.”
Alikwenda peke yake. Akaburudika kwa faraja inayotesa. Hivyo, vitendo hivyo vilipotoweka machoni mwake, lilikuwa kama pigo kwake. Aliamini kuwa kulikuwa na hitilafu ya mitambo iliyowaunganisha na chumba hicho. Lakini kwa kuwa mitambo hiyo ilikuwa automatic, na ilitegeshwa kwa namna ya kuweza kujirekebisha yenyewe, alisubiri kwa utulivu.
Katika kipindi hicho cha kusubiri ndipo ilipomjia wazo la kuyafikiria mambo ambayo yangetokea mara tu baada ya usiku huu. Kesho, wakati kama huu bila shaka nchi kadhaa za Kiafrika zitakuwa katika maombolezo makubwa huku majeneza yakiwa yamejaa maiti zilizoungua na hospitali zikishindwa kuhimili idadi ya majeruhi watakaoponea chupuchupu. Mpango huo uliotokana na ubunifu wake ulipita kwa tabu sana baada ya wakubwa kulalamika kwamba ulikuwa wa kikatili mno lakini yeye Von na wenzake wachache walifaulu kuwashawishi na wakaafiki baada ya kuwakumbusha tena na tena kuwa ANC ilikuwa haifanyi mchezo bali ilikusudia kupokonya utawala, jambo ambalo lingewatia watu weupe wote mashakani, chama hicho kinapewa onyo kali, onyo ambalo kamwe lisingeweza kusahauliwa. Dawa ya moto ni moto… na sasa wakati huo wa kutumia dawa hiyo, iliyokuwa ikichemshwa kwa muda mrefu na gharama kubwa ulikuwa unawadia. Lipi lingeweza kumpendeza Von zaidi ya hilo? Nani angeweza kufurahi zaidi yake?
Mara akajisikia kucheka kwa furaha. Alijisikia kusheherekea kila chozi litakalotoka katika uso mweusi kwani machozi hayo kwake yangekuwa faraja ambayo isingemsahaulisha ukatili wa mtu mweusi ambaye alimfanya awe yatima. Maelfu ya weusi yatateketea kwaajili ya malaya mmoja mweusi, aliwaza. Watakilipia kifo cha mama yake mpendwa, pamoja nao Joram Kiango na msichana wake… aliendelea kuwaza. Lakini kabla ya kifo chao lazima ampate huyu msichana anayeitwa Nuru. Aliyoyaona kwa macho yake yalikuwa hayastahimiliki. Alihitaji kuyaona kwa vitendo. Alihitaji kuijua siri iliyomo katika ngozi hii nyeusi, siri ambayo ilimfanya amkose mama na baba milele, baada ya hapo ndipo Nuru angemfata Joram akhera.
Mawazo hayo yalimpandisha mori hata akakumbuka kuyarejesha macho yake katika screen iliyokuwa ikimwonyesha chumba cha Nuru na Joram. Hakuona chochote. Mitambo bado ilikuwa haifanyi kazi. Akaitazama saa yake. Ilikuwa ikikaribia saa kumi za alfajiri. Saa mbili zilikuwa zimepita tangu mitambo hii ilipokorofisha. Von hakuamini. Isingewezekana kuwa mitambo hiyo iwe haifanyi kazi kwa muda wote huo ilikuwa imepangwa kuwa ingeweza kujiwasha yenyewe dakika tano tu baada ya kila hitilafu. Vipi leo ikatae? Na hasa akiwemo Joram Kiango ambaye, pamoja na matatizo yote aliyokuwa nayo, iliamriwa asiachwe huru zaidi ya dakika tano?
Hima Von aliinua simu na kuzungusha namba za mmoja wa makachero waliopewa jukumu la kulala macho katika jumba hilo alimokuwemo Joram. “Sikia,” Von alimwambia kwa sauti ya amri. “Tumia kisingizio chochote uingie katika chumba chake humo ndani fanya kila hila uone kwanini mashine hii imegoma kufanya kazi.”
Akiwa anaijua vizuri kazi yake, mtu huyo alivaa ovaroli lake jeupe na kuchukua vifaa vya umeme hadi chumbani kwa Joram. Aligonga mlango kama kawaida. Kisha akagundua kuwa ulikuwa wazi. Akaufungua polepole na kuingia. Macho yake yalidakwa na umbo la Nuru akiwa kavaa vazi la kulalia, jepesi kiasi cha kufichua umbo lake zuri la ndani kwa kiwango cha kutosha. Kando ya Nuru alisimama kijana wa Kizungu aliyevaa nguo zake zote, suti, kama ambaye alikuwa hajalala kabisa. Fundi huyo bandia alidhani kuwa kabla ya kubisha hodi mara ya kwanza aliwasikia wakicheka. Lakini hayo yalimtoka akilini mara alipomwona msichana huyo akiangua kilio huku akisema kwa kwikwi.
“Afadhali umefika fundi, nadhani utanisaidia.”
“Kuna nini?” kachero huyo aliuliza.
“Huyu hapa,” Nuru alisema akiuelekeza mkono kwa mzungu aliyesimama kando kwa utulivu. “Huyo ameingia humu chumbani kwa nguvu na kutaka kuninajisi. Mtoe nje, tafadhali.”
“Yuko wapi bwana wako?”
“Yuko bafuni.”
“Anafanya nini muda wote huo?” fundi bandia aliuliza huku akizidi kumkodolea Nuru kwa macho yenye tamaa. Mara macho yake yaliuona mfuko uliokuwa wazi kando ya kabati. Akaona vitu vilivyokuwemo. Aligutuka kidogo na kurudi nyuma huku akiupeleka mkono wake mgongoni kuchukua bastola yake. Alikuwa amechelewa sana. Wakati huohuo kisu kilipenya katika kifua chake. Pigo la pili lilimfanya ateremke sakafuni bila ya ubishi. “Mzungu” aliyekitumia kisu hicho alikitupa uvunguni na kuifuta mikono yake kwa shuka.
“Fanya haraka Nuru,” alihimiza akiirudia maiti na kuilaza vizuri kando ya kitanda.
Dakiaka chache baadaye mlinzi aliyekuwa akililinda jengo hilo kwa mlango wa nyuma aliwaona vijana wawili wazungu, mvulana na msichana wakimjia. Mikononi walikuwa na mizigo yao ambayo haikuwa chochote zaidi ya mifuko midogomidogo.
“Tunawahi uwanja wa ndege,” kijana wa kiume alieleza.
Ingawa walizungumza kiingereza kamili lakini mlinzi huyo alishuku jambo katika sauti hiyo hasa akiwa analifahamu jengo hilo lilivyo, hakuamini kuwa walikuwa wasafiri wa kawaida.
“Naweza kuona vitambulisho vyenu?”
“Bila shaka,” mwanaume alijibu akiutia mkono wake mfukoni. Ulitoka na kisu ambacho kilididimia katika kifua cha mlinzi huyo. Maumivu makali yaliyochanganyika na mshangao vilimfanya afyatue bunduki yake bila shabaha yoyote. Mara akaanguka chini na kukata roho.
Mlio wa bunduki alfajiri tulivu kama hiyo, uliwashitua watu wengi. Zaidi yao wote alikuwa Von Iron, aliyekuwa bado kaketi katika chumba kilekile, akisubiri matokeo ya mtu aliyetumwa chumbani kwa Joram. Alisubiri kwa muda ambao aliuona mrefu kupindukia. Alipojaribu kuwasiliana naye kwa walkie talkie ndogo iliyokuwa imevaliwa kama saa ya mkono hakupata majibu yoyote. Akaendelea kusubiri. Na katika subira hiyo ndipo aliposikia mlio wa bunduki ambao hakuutegemea. Akafanya hima kumtuma kachero mwingine katika chumba hicho. Mara moja akapata majibu ambayo yalimfanya atokwe na jasho jembamba.
Dakika chache baadaye alikuwa miongoni mwa maafisa sita wa ngazi za juu katika BOSS waliosimama chumbani humo mbele ya maiti ya mwenzao, ambayo yalilala sakafuni juu ya dimbwi la damu nzito. Joram hakuwemo, wala msichana wake. Vitu vyao vichache vilikuwa vipo, ingawa baada ya kupekuliwa havikuonekana na chochote cha haja zaidi ya mavazi na vitabu. Katika vitabu hivyo kilipatikana kitabu kimoja cha Physics ambacho kilionekana kuwa kilisomwa sana kwa jinsi kilivyokuwa kimepigiwa mistari chini ya maneno fulanifulani. Baada ya uchunguzi mdogo ilidhiirika kuwa msomaji alizingatia mambo ya setilaiti na nyuklia. Hilo liliwafanya waunge mbili na mbili na kupata nne.
“Ana wazimu,” Von alifoka. “Kama amekuja hapa akiwa na ndoto ya kufahamu chochote juu ya setilaiti yetu hii maalumu wazimu unamsumbua. Amekuja kuinadi roho yake.” Akawageukia wenzake na kuwatazama kwa lile jicho lake kali la kutisha, jicho ambalo lilikuwa msingi uliowafanya waendelee kumwogopa na kutomkosoa. “Mnasikia? Mtafuteni haraka, aletwe hai, atakufa taratibu kama mbwa wenzake.”
Kabla hawajatawanyika kutoka chumbani humo, ziliwafikia habari nyingine mbaya zaidi. Maiti ya mmoja wa walinzi wa jengo hilo imeokotwa ikiwa na kisu kifuani. “Aliuawa kwa aina ya kisu ambacho kimemwua huyu.” Kachero huyo alieleza.
“Mnaona?” Von alinguruma. “Sasa namtaka akiwa hai au maiti. Haraka iwezekananvyo, tafadhali…”
Kulitangazwa msako mkali katika jiji la johanesburg mitaa yote ilifurika makachero ambao walichunguza kila uchochoro. Ilikuwa siku ngumu mno kwa watumishi weusi ambao walilazimika kuwahi kazini asubuhi hiyo. Wengi wao waliambulia kuishia katika vituo vya polisi ambako waliteswa na kusumbuliwa kwa kosa ambalo hawakulifahamu. Mtu au watu waliokuwa wakitafutwa hawakupatikana. Badala yake hadi mapambazuko kulikuwa na taarifa ya vifo vya watu wanane zaidi, watano wakiwa wameuwa kwa kisu, watatu kwa risasi za bastola. Wengi kati ya marehemu hao walikuwa watu wakubwa katika ofisi zao au walinzi wa majumba fulanifulani yenye umuhimu mkubwa. Ilikuwa dhahiri kuwa hiyo ilikuwa kazi ya Joram Kiango.
Von alizidi kupandwa na hasira. Hakuelewa kabisa dhamira na manufaa ya mauaji hayo. “Wazimu unamsumbua,” aliwaza. Kisha alihisi kuwa ameelewa. Joram alikuwa akilipiza kisasi dhidi ya maafa yatakayoipata nchi za afrika saa chache baadaye bila shaka alikuwa akijifariji kwa kumwaga damu zisizo na hatia. “Anajisumbua,” Von alisema. “Atalazimishwa kutazama katika televisheni, moto utakavyoiteketeza Dar es Salaam. baada ya hapo ndipo atakapokufa kifo cha kusikitisha…
Von akaamuru ufanyike msako mkubwa zaidi. Polisi wote na jeshi la ulinzi wakaingizwa katika msako huo. Kila mmoja aliambiwa anamtafuta nani na afanye nini baada ya kumpata. “Akileta ubishi muue, vinginevyo mlete hai.”
Ingawa Von alitegemea habari hiyo iwe siri, lakini hakufahamu iliyafikia vipi masikio ya watu wa habari. Ilimshangaza televisheni ilipokatiza matangazo yake ya kawaida na kueleza kutoweka kwa Joram Kiango na mauaji aliyokuwa akiyafanya. Ikatolewa picha ya Joram na msichana wake walipokuwa wakishuka kutoka ndege iliyowaleta nchini humu ikiwa imetekwa nyara. Pia zilionyeshwa baadhi ya maiti alizoziua.
“…jihadhari nae, ukimwona muue kwanza, muulize maswali badaye…”
Mtangazaji wa kipindi hicho alieleza.
Tangazo hilo liliamsha hofu ambayo haikupata kuonekana katika jiji hilo. Watu walizidi kubababika wakiogopa hata kuifungua milango yao ilipogongwa na yeyote. Wako ambao kazini hawakutaka kwenda.
Dakika chache baadaye ilibidi Von ajitokeze katika televisheni na kuwataka wananchi wasiwe na hofu yoyote, kwamba kutoroka kwa Joram lilikuwa tatizo dogo sana ambalo lingerekebishwa kwa muda mfupi. Akawafahamisha kuwa badala ya hofu leo ingekuwa siku yao ya kufanya sherehe kwani Afrika na dunia nzima itaziona nguvu za Afrika Kusini. “Wote ambao wamekuwa wakionea kijicho na kuitesa nchi yetu leo watatupigia magoti,” aliendelea. “Tulieni, msiwe na wasiwasi wowote. Ikifika saa nne fungueni redio na taelevisheni zenu muone…”
Watu hao ambao walikuwa wakitafutwa kwa udi na uvumba, alfajiri iliwakuta wakiwa wamesimama mbele ya hoteli moja ndogo katika mtaa uliojaa watu waliokuwa wakijadiliana. Macho yao yaliwatazama raia hao wa makaburu waliojaa wasiwasi kwa dhihaka. Kadhalika, waliwakebehi askari na poli ambao walikuwa wakipita huku na huko katika mtaa na vichochoro huku wakiwapita bila ya kuwatupia macho. Isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuwashuku kwa urahisi. Pamoja na kukesha, pamoja na kuchoka kwa kazi ya kwenda hapa na pale huku wakilazimika kuua na kuua tena, bado walijitahidi kuwa katika hali ya kawaida kama raia yeyote wa kawaida katia nchi hiyo. Hali ambao ilitokana na mavazi waliyovaa pamoja na rangi yao.
Yeyote aliyewaona aliamini kuwa alikuwa akiwaona vijana wengine wa kikaburu. Hayo yalikuwa matokeo ya moja ya shughuli nyingi ambazo Joram alifanya kwa gharama kubwa sana aliposafiri hapa na pale katika miji mbalimbali. Alimpata mtaalamu ambaye aliwatengenezea ngozi za bandia zilizovaliwa usoni, mikononi na kufunika vichwa vyao kwa nywele za kizungu. Vitu hivyo ni miongoni mwa mali zake ambazo alizisafirisha kwa hila kwa kumtumia yule Mmarekani Moole.
Kwa ujumla Joram aliona kuwa mambo yote yalikuwa yakienda kama yalivyopangwa, ingawa kiasi yalianza ghafla kuliko alivyotegemea. Alishtuka sana jana alipoambiwa na yule kiongozi wa BOSS kwamba leo saa nne wangeilipua Dar es Salaam na miji mbalimbali ya nchi za Kiafrika kwa ile silaha yao iliyoko angani. Hivyo, hakuwa na simile tena moyoni. Ndipo alipolazimika kufanya mapenzi ya hali ya juu na Nuru akiwa na hakika kuwa anatazamwa na ule mtambo wao ambao alikwisha uona. Alifanya hivyo ili kuwapumbaza watazamaji hao. Baada ya hapo ndipo alipofanya hila kukorofisha mtambo huo. Katika kipindi hicho cha kutoonekana aliondoka na kupenyapenya kwa hila katika viochochoro hadi nyumbani kwa Moole ambako alibisha mlango na kufunguliwa na Moole mwenyewe. Alipoomba mzigo wake Moole alikanusha kabisa kwamba hakuwa amechukua mzigo wa mtu kama huyo. Lakini ngumi mbili tatu zilimfanya amwongoze ghalani ambako Joram alimvamia na kumfunga mikono na miguu, kisha akaufungua na kuchukua vile vitu muhimu tu. Akarudi haraka hadi chumbani kwake ambako, akisaidiwa na Nuru alipekuapekua na kupata ramani walizoziandaa, pesa na vitu vingine. Ni wakati Joram alipomaliza kujivisha ngozi hizo zilizomfanya aonekane kama alivyo sasa, alipoingia yule kachero wa kwanza. Hila aliyoitumia Nuru ya kujifanya kuwa alikuwa akipambana na mzungu aliyetaka kumnajisi ilimsaidia sana. Ndipo kachero huyo alipopata kile alichostahili kupata. Nao akafanya haraka kumsaidia Nuru kuvaa “Uzungu” wake na alipokamilika walivichukua vilivyokuwa muhimu na kuingia mitaani.
Wakiwa wameikariri ramani hiyo kikamilifu, kazi waliyoifanya mitaani humo ilikuwa kufuata yale majengo waliyokusudia na kutega vile vigololi vilivyopatikana kwa Chonde na kuvitegesha katika kipindi cha saa tatu kamili. Walifanya kazi hiyo kwa ukamilifu kuliko walivyotegemea. Watu wachache ambao walilazimika kupoteza maisha ni wale walioshuku jambo au kujaribu kuwazuia kufanya kazi yao. Wakiwa hawajui kuwa wanapambana na nani watu hao walikufa kwa utulivu kabisa, isipokuwa yule ambaye kifo kilimtetemesha hata akaamua kuruka dirishani kutoka ghorofa ya nne akiwa na kisu kifuani.
Sasa kazi ya kutega vigololi ikiwa imekwisha, Joram alimtazama Nuru na kumnong’oneza, “Awamu iliyobaki ni yangu peke yangu. Ni lazima niingie katika mtambo wao na kuulipua. Nikiweza kuulipua kabla ya madhara tuliyoandaa katika jiji hili kutokea litakuwa jambo jema sana. Nikishindwa, mioto itakapoanza nenda pale ambapo nimekuonyesha katika ramani ukanisubiri.”
“Hatuwezi kwenda wote?”
“Haiwezekani. Tumelijadili hilo mara nyingi sana.”
Wakakubaliana.
ITAENDELEA
Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;