Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
Simulizi : Tutarudi Na Roho Zetu?
Sehemu Ya Tatu (3)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Baada ya kuongea nao kwa marefu na mapana ndipo waandishi wa gazeti hilo wakatoa habari hizo zikiwa zimepambwa kwa picha nyingi za kuchora, picha ambazo ziliwachora Joram na Nuru katika sura na mavazi tofauti; wakijaribu kuonyesha jinsi gani wanavyoweza kujibadili. Chini ya michoro hiyo kulikuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa herufi nzito yakisema; “Unashauriwa kujihadhari nao. Ukimwona ua kwanza, uliza maswali baadaye.”
SASA ENDELEA
Gazeti hilo lilisomwa kote duniani. Maelezo yake yalidakwa na TV na redio zote duniani. Watu wengi, ambao walimchukia Joram walizidi kushangilia, hali wale waliompenda walizidi kushangaa.
“Sijui amepatwa na nini mtoto huyu,”Inspekta Kombora alifoka huku akilitupa gazeti hilo mezani. “Yuko London na anafanya anavyojua. Anazidi kulipaka matope jina lake ambalo tayari amelichafua.”
Ilikuwa dhahiri kwa yeyote amtazamaye Kombora machoni kwamba alikuwa hajapata usingizi wa kutosha kwa muda mrefu. Mambo mengi yalimkabili kichwani kiasi cha kumpokonya hata hamu ya kula. Angewezaje kustarehe wakati siku zilikuwa zikisogea huku halijapatikana lolote la haja katika kukomesha tishio kutoka nchi adui ambalo lilitaka serikali iache msimamo wa kimapinduzi, la sivyo ajali zingeendelea kutokea. Tanzania kuacha kuzisaidia nchi zinazopigania haki na uhuru wake ilikuwa ndoto ya kupendeza. Kamwe isingetokea. Lakini kuendelea kusaidia nchi hizo huku ukisubiri maafa ya hatari sana, kwa nchi yake na rafiki zako hali huna uwezo wa kufanya lolote ilikuwa ndoto ya kusikitisha sana, ndoto ambayo ingeweza kutokea.
Walikuwa wamefanya yote ambayo wangeweza kufanya katika juhudi za kuhakikisha usalama. Yote; mema kwa maovu. Magereza ya Keko na Ukonga yalikuwa yamejaa wageni wengi ambao ama waliingia nchini kinyume cha utaratibu, au hati zao zilitia mashaka. Wote hawa walihojiwa kwa maneno na vitendo. Waliokuwa watakatifu waliachiwa, wenye madhambi ya magendo na uzururaji wakifunguliwa mashitaka. Ni mtu mmoja tu ambaye alielekea kuwa na mengi au machache ambayo yangehusiana na usalama wa nchi.
Huyu alikamatwa katika hoteli ya New Africa baada ya kulala hapo kwa siku moja. Wapelelezi walimshuku baada ya kumsikia akiulizauliza maswali juu ya watu walikufa katika hoteli hiyo; ni wa aina gani na walikufa vipi. Alipokamatwa na kutakiwa kutoa vitambulisho, hati zake zilionyesha kuwa ni mwanachama wa ANC ambaye ametoroka kutoka Namibia. CID waliwasiliana na ofisi hizo. Jina la Kweza halikuwemo katika orodha ya wanachama wa ANC. Ndipo lilipofunguliwa bomba la maswali dhidi yake. Na ni hapo ilipodhihirika kuwa hakuwa mtu wa kawaida jinsi alivyoweza kuyajibu maswali yote kwa ukamilifu kama ambaye alijiandaa kuyajibu.
Begi lake ambalo lilikaguliwa harakaharaka bila ya kuonekana chochote, lilipekuliwa tena. Baada ya jitihada kubwa iligundulika mifuko ya siri ambayo ilificha silaha, vyombo vya mawasiliano na vitu mbalimbali vya kijasusi. Alipoulizwa alikovipata alikanusha kuwa havifahamu, wala hakupata kuviona vitu hivyo. Ni majibu hayo ambayo yalimuudhi Kombora hata akaamua apelekwe katika chumba cha mateso ili, kama hasemi, autapike ukweli. Taarifa zilizomjibu Ispekta Kombora zilisema kuwa alikuwa hajasema lolote.
Ndipo alipolitupa gazeti alilokuwa akisoma habari za Joram, na kumtoa akilini kwa muda. Akaondoka na kuingia katika lifti ambayo ilimteremsha chini ya ardhi kiliko chumba cha mateso. Kombora hufika katika chumba hiki kwa nadra sana. Harufu ya mchanganyiko wa damu, kinyesi, jasho na machozi ni jambo moja ambalo humfanya aape kuwa asingerudi tena kila anapofika humu. Jambo jingine ni sura za watesaji. Sura hizi humtisha zaidi ya mateso yenyewe, zikimfanya aamini kuwa watu hao kama kweli wana roho, basi wana roho za chuma. Nayo macho ya wanaoteswa si jambo ambalo macho ya mtu mstaarabu yatapendezwa kuangalia.
Leo hii alimkuta Kweza, au kilichosalia katika umbo la aliyekuwa Kweza; akiwa amelala sakafuni, sura yake ikiwa haitambuliki kwa kuvimba na kuchubuka. Vidole vyake vyote tayari vilikuwa vimevunjika, jicho moja limetumbuka na meno manne yamepotea. Watesaji walikuwa wamemwinamia wakimdunga sindano ambayo ilikuwa na waya, iliyotokea katika soketi ya umeme.
“Mwachieni kidogo,” Kombora aliamuru akikiendea kiti na kuketi. “Mleteni hapa.”
Kweza alisimamishwa mbele ya Kombora, akitetemeka kwa uchungu na maumivu makali. Nusura Kombora amhurumie, huruma hiyo ilimtoka mara moja mara alipomfikia mtu huyo; mtu mweusi; kibaraka, msaliti wa juhudi za weusi wenzake katika kujikomboa kutoka kwenye udhalimu ambao umewaandama miaka nenda rudi. Mtu kama huyu ahitaji kuhurumiwa hata chembe.
“Wewe!” Akafoka. “Kwa nini hutaki kusema ukweli? Kama ukisema ukweli tutakuacha uende zako.”
Pamoja na maumivu aliyokuwanayo mtu huyo, alicheka, “Nimekwisha sema kila kitu. Tatizo lenu ni kwamba hamtaki kuelewa ninachosema. Na juu ya kuniacha niende zangu nimewaambieni mara nyingi kuwa sihitaji kwenda popote. Naomba mkichoka kunitesa, mniue.”
“Umesema ukweli? Ukweli gani?”
“Nimesema kuwa mimi sifahamu chochote juu ya maswali mnayoniuliza. Nilichofuata ni kumtafuta rafiki yangu Chonde ambaye inasemekana amefariki. Nilitaka kufahamu amefariki vipi ili niitulize roho yangu.
“Chonde rafiki yako vipi?”
“Alikuwa rafiki wa kalamu. Sikuwahi kuonana naye ana kwa ana.”
Kombora alimtazama kwa makini. Macho yake makali yalimfanya Kweza aangue tena kicheko dhaifu huku akisema, “Mnaupoteza bure muda wangu na wenu. Mimi sifahamu chochote. Nanyi hamna lolote ambalo mnaweza kufanya zaidi ya kusubiri maafa kama nilivyoambiwa. Mwenye akili ningemshauri aikimbie nchi hii mapema badala ya kusubiri kifo cha kutisha cha moto mkali utakaokuja na ufukara wa kutisha baada ya moto huo.” Akaangua kicheko kingine dhaifu. Safari hii alicheka kwa muda hata akateleza kutoka mikononi mwa askari waliomshika na kuanguka chini. Hapo chini alitulia kwa muda kisha akapapatika na kukata roho.
Kombora na wenzake walisogea na kuimana wakimtazama. Hakuna aliyefahamu kama alikuwa na sumu kinywani au aliitapika roho yake. “Miujiza, iliyoje!”
SURA YA SABA
WALIKUWA wameitembelea miji mingi maarufu ya dunia. Walionja anasa na starehe za kila mji. Baada ya kutoroka kutoka London kwa hima walikwenda Ufaransa ambako walipitia miji mbalimbali na kuingia Paris. Toka Paris walikwenda New York ambako hawakukaa sana kabla ya kuruka tena hadi Washington, HongKong, Moscow na kwingineko.
Ingawa ziara yao ilikuwa ya starehe, lakini ilikuwa ziara ngumu kiasi cha kumtatanisha Nuru na kumsisimua Joram. Safari zao nyingi zilikuwa za kujifichaficha usiku na mchana kuwaepuka polisi na wapelelezi ambao ama walimhitaji Joram kwa makosa ama kuzishuku hati zao za usafiri, ambazo mara kwa mara zilikuwa za bandia. Hila za hali ya juu, pamoja na ruswa nzito, ni njia pekee iliyowafanya wafanikiwe kuiepuka mitego yote ya CID, KGB, INTERPOL na wapelelezi wa nchi mbalimbali.
Katika tukio moja kwenye mji mmoja, ilimlazimu Joram kujifanya mwanamke malaya ili kuwaepuka polisi ambao waliizingira hoteli aliyokuwemo. Polisi hao walipoingia katika chumba ambamo walitegemea kumnasa Joram walijikuta wakirudi nje kwa aibu baada ya kukuta wasichana wawili, waliofanana kwa uzuri, wakiwa nusu uchi juu ya kitanda chao kwa namna ya kufanya mapenzi ya wao kwa wao. Wakati askari hao wakisubiri nje ili kuwahoji vizuri, Joram na Nuru walitumia dirisha kuondoka zao na kila kilichokuwa chao.
Katika tukio jingine Joram alilazimika kuiteka nyara ndege ndogo ya abiria na kuilazimisha kutua katika uwanja ambao haukukusudiwa jijini New York. Kutoka uwanjani hapo walipata kinga kwa risasi za askari walioizingira ndege hiyo kwa kuwachukua rubani na msaidizi wake huku wakizielekeza bastola katika vichwa vyao. Polisi walikuwa wakiwafuata kwa mbali, televisheni ikiwaona na kuwaonyesha kwa kila mtu. Lakini ilifika mahali ambapo si polisi wala rubani waliojua kilichotokea. Polisi waliikuta ndege hiyo ikiwa imesimama kando ya nyumba, marubani wakiwa usingizini kwa kunusa dawa fulani bila kutaraji. Watu walioshuhudia tukio hilo, wakiwa hawajui kinachotokea, walidai kuwa waliwaona “vijana wazuri” msichana na mvulana wakishuka kutoka ndege hiyo na mizigo yao na kuingia katika jumba la jirani ambamo hawakuonekana wakitoka tena.
Harakati na machachari yao katika miji mbalimbali ziliondokea kuwa habari ambazo ziliwavutia sana waandishi wa habari. Mara kwa mara televisheni, redio na magazeti zilitoa habari zinazowahusu; Leo kaonekana hapa; hapa kafanya hivi; pale alifanya vile, na kadhalika.
Habari hizo zilipambwa kwa picha zao zinazovutia, kurudiwarudiwa kwa historia ya maisha ya Joram kiango pamoja na kutiwa chumvi nyingi ili kugusa masikio ya watu wote na kumsisimua kila mmoja. Hivyo, jina lilipanuka na athari kuneemeka. Ilikuwa kama dunia imesita kushughulikia masuala yaliyo muhimu na kuandamana na Joram katika ziara yake hii ndefu, jambo ambalo lilimfanya kila mpelelezi kuwa na hamu kubwa ya kubahatika kumtia mikononi Joram ili amfikishe kunakohusika.
Jambo ambalo lilimshangaza Neema katika mkasa huo mzima ni jinsi ambavyo alielekea kufurahishwa na jinsi habari hizo za aibu juu yake zilivyopata nafasi kubwa katika vyombo vya habari. Iliendelea kumfurahisha Joram badala ya kumchukiza. Nuru ambaye alimfahamu Joram asivyopenda sifa alijikuta akijawa na msgangao kwa mabadiliko hayo ya Joram.
Hata hivyo mshangao wake ulianza kupungua pale Joram alipoanza au alipolazimika kumshirikisha katika baadhi ya mambo aliyokuwa akiyafanya. Jambo la kwanza lilikuwa mazoezi ya viungo. walifanya kila starehe, lakini baada ya starehe, wakiwa chumbani kwao, walifanya mazoezi makali ya viungo. Mazoezi ambayo awali yalimtoa Nuru jasho, machozi na damu. Lakini baada ya muda machozi na damu vilikoma na jasho kupungua. Akawa hodari, akiwa bega kwa bega na Joram katika kila jambo. Zoezi la pili lilikuwa la matumizi ya silaha mbalimbali ambazo Joram alikuwa akizinunua kwa siri sana.
Alimwelekeza Nuru namna ya kuzificha mwilini, namna ya kuzitumia na kumfundisha jinsi ya kulenga shabaha kwa ukamilifu. Nuru alikuwa mwepesi wa kuelimika.
Hayo yaliufanya moyo wa Nuru uwe na tumaini kubwa. Sasa aliamini kuwa Joram alikuwa na jambo fulani zito la muhimu ambalo alikuwa akishughulikia. Pengine katika safari hiZo za mji hadi mji alikuwa akimhitaji mtu kwa madhambi fulani. Mtu gani huyo? Na ni madhambi gani aliyoyafanya?
Maswali ambayo yaliimarika hasa kutokana na simu nyingi ambazo Joram alikuwa akipiga kwa rafiki zake sehemu mbalimbali ulimwenguni, ambazo mara kwa mara zilikuwa katika mafumbo ya aina aina. Japo alimsikiliza kwa makini Nuru hakuambua chochote cha haja, zaidi ya kuishia kuhisi tu. Wakati wote huo Joram hakukoma kujifungia.
Halafu ikaja jioni ya leo, ambapo Joram alionekana mtulivu kuliko ilivyokuwa siku zote. Sigara ziliteketea mdomoni mwake moja baada ya nyingine, macho yake yakimtazama Nuru ambaye alikuwa ameketi juu ya meza ya kuvalia akishughulikia nywele zake. Joram alimtazama kwa makini kwa dakika kadhaa, kisha alimsogelea na kumshika bega.
“Nilichoshika hapa ni kipande murua cha kazi ya sanaa ambayo ni mfano halisi wa kazi ya Muumba. Nadhani hana budi kujivunia mafanikio yake”, alisema akitabasamu.
Nuru aliinua uso kumtazama.
“Kwa bahati mbaya kazi hii ya sanaa iki katika hatari ya kuharibika endapo itandelea kuandamana na binadamu wenye akili mbaya kama Joram Kiango”.
Hilo lilimfanya Nuru atabasamu. Alijua Joram anaelekea wapi. Siku hizi mbili alikuwa akimchunguza kwa makini na kuona mabadiliko katika fikira zake. Alikuwa akiona na kushuhudia kutoweka kwa ile starehe ya kujisingizia katika nafsi ya Joram na badala yake starehe kamili kuchukua nafasi yake. Mfano wa mtu ambaye yuko katika jahazi hafifu katikati ya bahari iliyochafuka anapobahatika kufika pwani salama. Hivyo alijua kuwa Joram ana neno. Akamhimiza kulisema kwa kumwambia, “Unachotaka kufanya Joram ni kunitisha… Lazima uelewe kuwa sitishiki ng’oo. Tumekuwa nawe katika heri na shari. Tutakuwa pamoja jehanamu na peponi. Usijisumbue kuniambia lolote lenye dhamira ya kututenga”.
Joram akacheka. “Una akili nyepesi sana Nuru”, akamwambia. “Nilichokuwa nikielekea kukuomba ni kukushauri urudi nyumbani, uniachie kazi iliyoko mbele yangu. Ni kazi chafu, ya hatari, yenye nuksi, ambayo sidhani kama itanifanya nirudi nyumbani na roho yangu”.
“Nimekwisha sema usijisumbue kunitenga. Nina hamu na kazi nzito, chafu yenye damu. Sijasahaun nilivyoshirikishwa kuwaangamiza wakuu wa nchi wasio na hatia. Nahitaji kujitakasa. Ni damu pekee itakayonitakasa. damu ya adui wa Afrika.
Joram aliduwaa huku akimtazama msichana huyo. Hakuwa na shaka kuwa msichana huyo ni shujaa. Lakini hakujua kuwa ni shujaa kiasi hicho. Ndiyo, alimtegemea sana katika msafara wake. Lakini hakukusudia kumwingiza katika mkasa ambao ilikuwa dhahiri kuwa pamoja na ugumu wa maandalizi yake ya muda mrefu hadi sasa matekeo yake yalikuwa gizani. Yeye alikuwa tayari kwenda, tayari kufanya kazi inayompeleka; uwezekano wa kurudi haukumsumbua. Kufa kusingemtisha sana mradi atakuwa ameifanya kazi yake. Kifo chake ni jambo moja, kusababisha kifo cha mtoto wa watu, mzuri kama Nuru, ni jambo jingine.
“Sikia Nuru. Labda huelewi… Nakusudia kwenda toka hapa sio nchi ya kawaida. Ni nchi ambayo kuna watu wenye kiu kubwa ya damu ya mtu mweusi na njaa kubwa ya roho zetu. Na ninahitaji kujipeleka moja kwa moja mikononi mwao. Kwa ufupi nategemea kwenda Afrika Kusini…”.
“Tutakwenda pamoja”.
…Na ninachokwenda kufanya ni hujuma. Wakinigundua watanitafuna mbichi”.
“Watatutafuna pamoja”.
Joram akaduwaa. “Labda nikufunulie kila kitu kilivyo Nuru”, Joram akamwambia. “”Nisubiri”, alisema akiliendea begi lake lililokuwa limefurika kwa vitabu aina aina pamoja na encyclopedia ambazo Joram alikuwa akizitumia kwa muda mrefu kujaribu kuyasoma yake maandishi ya kijasusi ambayo aliyapata katika mfuko wa hayati Chonde. Humo alitoa karatasi ndefu, iliyoandikwa kwa mashine, ikiwa tafsiri ya maandishi hayo. Alimkabidhi Nuru na kumwabia asome haraka haraka.
MPANGO KABAMBE WA KUIFANYA AFRIKA ITUPIGIE MAGOTI
Taarifa hii ni siri kubwa miongoni mwa watu wachache sana, wa ngazi za juu katika serikali yetu. Ni taarifa ya mafanikio ya jaribio lililofanyika muda mrefu, kwa gharama kubwa, baina ya wana sayansi wetu na waliotoka katika nchi marafiki duniani; juu ya uwezekano wa kufanya nguvu za nukria zitusaidie katika kuwaweka Waafrika, na ikiwezekana dunia nzima katika kwato zetu.
Itakumbukwa kuwa kifungu kikubwa cha pesa kilitengwa ili kufanyia majaribio haya. Kwa siri kubwa sana mtambo madhubuti ulijengwa na setilaiti kutupwa angani. Mbili kati ya setilaiti hizo zilidondoka katika nbahari ya Hindi kabla ya kuonyesha matokeao. Lakini setilaiti ya tatu imetimiza majibu. Majaribio yamefanywa na kuleta matokeo ya kuridhisha kabisa. Mtu wetu alitumwa Lagos na kutega gololi maalumu ambazo baada ya kufyatuliwa zimeifanya setilaiti hiyo iliyoundwa kwa madini yanayoifanya isionekane kwa macho iweze kuingia katika anga la nchi hiyo na kuachia bomba la moto mkali ambao uliteketeza uwanja na watu kadhaa. Jaribio la pili lilifanywa huko Harare ambako maghala yaliteketea. Jaribio la tatu na la mwisho linakusudiwa kufanywa Tanzania, katika jengo la Benki Kuu inayojengwa. Hatuna shaka kuwa jaribio hilo litafanikiwa.
Baada ya jaribio hilo ndipo tutaanzisha mpango wa kuzifanya nchi zote zinazojiita za mstari wa mbele, kutupigia magoti. Mtu wetu anayekwenda Tanzania ni mtu wa kutegemewa, aliyeishi huko miaka mingi. Atapewa pesa nyingi zitakazomwezesha kwenda mahala popote duniani, na kumnunua mtu yeyote. Huyu atakuwa na jukumu la kusubiri amri yetu ili aachie vipigo vingine ambavyo vitaifanya Afrika itokwe na machozi huku dunia ikilalamika…
Nuru aliinua kichwa ghafla kumtazama Joram. Tayari uso wake ulikuwa umelowa jasho la hofu na mshangao. “Joram” Nuru alifoka, “Mungu wangu. Huoni kama hii ni habari ya kutisha kuliko zote? Tunawezaje kustarehe hivi huku nchi yetu ikiwa mashakani?”.
“Imenichukua siku nyingi kuigundua. Waliyaficha maandishi hayo kwa hila ambazo zingemtoa jasho mtu yeyote mwenye akili timamu. Hata hivyo ugunduzi huu hautatusaidia chochote. Kama ulivyosoma setilaiti hiyo iko angani na haionekani kwa macho. Inaendeshwa na mtambo ambao uko katika himaya yao, bila shaka ukilindwa kwa hali na mali. Hakuna njia nyingine zaidi ya kuubomoa mtambo huo”.
“Je. Tukitoa siri hii kwa dunia?”, Nuru alimuuliza Joram.
“Haisaidii. Umoja wa Mataifa utalalamika na kuilaani Afrika Kusini. Pengine watawekewa vikwazo vya kiuchumi. Unadhani hayo yatawafanya watuhurumie?”. Mara ngapi wamelaaniwa? Mara ngapi wamewekewa vikwazo? Hapana Nuru. Lazima nifike Afrika Kusini. Dawa ya moto ni moto”.
Nuru alitulia kwa muda akiitafakari taarifa hii kwa makini. Mara aliinuka na kumwendea Joram. Akamkumbatia na kumnong’oneza masikioni. “Samahani sana mpenzi. Nilikuelewa vibaya sana ulipoiba pesa benki. Vilevile nilishangaa unavyozitumia pesa hizo vibaya kwenda huku na kule ukuwa hujali matusi ya waandishi wa habari. Sasa nimekuelewa. Nimeelewa kwanini ulifanya vile. Ulikuwa ukijiandaa kwenda Afrika Kusini. Ulichofanya ilikuwa kuilaghai dunia ili uonekane mhalifu na mkimbizi asiyeweza kuishi popote isipokuwa Afrika Kusini. “Sivyo mpenzi?”. Joram alipochelewa kujibu Nuru aliongeza, “Mpenzi. Wewe ni shujaa kuliko mashujaa wengine niliopata kuwasikia. Tutakwenda pamoja Afrika Kusini…”.
“Tatizo siyo kwenda Nuru. Tatizo ni kurudi. Unaoneje, tutarudi na zoho zetu?”.
Wakati Joram na Nuru walipokuwa wakizungumza hayo, Kombora alikuwa Ikulu mbele ya Rais akitokwa na jasho jembamba. Alifika ofisini, akiwa hoi kwa ukosefu wa usingizi wa siku kadhaa. Mara alipopata simu ambayo ilimtaka kwenda Ikulu mara moja, alilitia gari lake moto na kufunga safari hiyo ya dharura hadi Ikulu ambako alielekezwa katika chumba cha faragha. Humo aliwakuta Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Katibu Mkuu katika Wizara ya Ulinzi. Aliwasalimu kishujaa, ingawa tayari moyo ulikuwa ukimdunda kwa kujua kuwa hakuwa tayari kuyajibu maswali yao.
“Nini hiki? Rais alimwuliza akimsogezea kijibarua ambacho kiliandikwa kwa mkono.
Kombora alikipokea na kukitazama. Hakuwa na haja ya kukisoma kwani ilikuwa moja kati ya zile barua ambazo zilikuwa zikiwafikia wakubwa wa nchi za mstari wa mbele mara kuwatisha ili waache msimamo wao dhidi ya Afrika Kusini.
“Isome,” Rais alihimiza.
Kombora akakisoma. Mara alielewa sababu ya kusisitiziwa aisome. Ilisema: “ONYO LA MWISHO.” Ikarudia kutaja sehemu muhimu ambazo aliyeandika barua hiyo alikusudia kuzichoma, sehemu ambazo ni pamoja na Ikulu. Baada ya kuikodolea macho, Kombora aliyarudisha katika uso wa Rais. “Nimeisoma mzee.”
“Barua hiyo imekutwa katika ofisi yangu,” Rais alieleza. “Ni dhahiri kuwa aliyeileta anao uwezo na nafasi ya kufanya lolote katika nchi na ofisi hii. Kwanini mmempa haki hiyo?”
Kombora hakujibu. Hakujua ajibu nini. Yeye na vijana wake wote walikuwa taabani katika mapambano haya. Majasusi wengi ya Afrika Kusini yalishikwa, lakini halikutokea lolote ambalo lingeweza kusaidia kukomesha vitisho vya ainaaina. Mengi yalikuwa majasusi wa kawaida, ambayo ama hawakuwa na lolote la haja au yalitumwa kwa ajili ya masuala yasiyo na uzito mkubwa. Wapelelezi wake ambao walikuwa nje pia walivitesa vichwa vyao bila ya kupata matunda ya kuridhisha. Nusura Kombora apate hasira kwa lawama hizo ambazo hakuona kama zinamstahili. Alitamani ainuke, atangaze kujiuzulu. Lakini hayo hakuyafanya kwa kukumbuka kuwa hasira si dawa. Na licha ya hayo aliona wazi kuwa lawama zilimstahili. Kufanya kazi ni kupata matokeo ya kazi hiyo. Kazi isiyo na matokeo haiwezi kuitwa kazi.
“Sina haja ya kukulaumu,” Rais aliendelea. “Nauona ugumu wa jukumu mlilonalo. Nilichokuitia ili kukukumbusha kwa mara nyingine ni kuwa hata kwa bei ya roho zetu hatuwezi kukubali kufuata masharti ya utawala huu dhalimu. Lazima tupambane nao. Na huu ni wakati pekee wa kuonyesha moyo wetu. Uoga hauwezi kutufanya tukubali kuwa mateka wa utawala haramu kama huu. Lazima tushinde,” akasita kidogo akimtazama Kombora kwa makini. “Inspekta,” aliongeza kwa sauti ya amri kidogo. “Huu ni wakati wako. Kuna wakati wa njaa; wakulima hutakiwa kuiokoa nchi; wakati wa uhaba wa fedha za kigeni wafanyakazi viwandani huombwa kujitoa mhanga; wakati wa vita jeshi hulazimika kulinda nchi. Huu ni wakati wako, Inspekta. Nchi inakuhitaji na kukutegemea. Gavana wa Benki amepewa amri ya kukupa kifungu chochote cha pesa unazohitaji, Mkuu wa jeshi ameambiwa akuruhusu kutumia kikosi chochote na Bunge limependekeza uruhusiwe kufanya lolote. Kazi kwako,” Rais alimaliza akainuka na kutoka.
Kombora alipumbazuka kidogo juu ya kiti hicho. Jasho jembamba lilikuwa likimtoka. Mara akajilaani kwa kusita kuleta barua ya kujiuzulu kwake. Hakujua angefanya nini zaidi. Aliwatazama viongozi ambao walikuwa wametulia, wakimtazama. Kiongozi mmoja alitamka neno ambalo halikumfikia Kombora. Mwingine alitikisa kichwa. Kombora akainuka na kuwaaga. Alipoifikia gari yake ndipo alipokumbuka kuwa ile barua ya vitisho bado alikuwa nayo mkononi. Akaitia mfukoni na kuamuru gari limrudishe ofisini.
Kidole kimoja kamwe hakivunji chawa; Kombora aliwaza akiwa kaketi ofisini mwake akifikiria afanye lipi zaidi kufanikisha vita hivi ambavyo havikuwa na uelekeo maalumu. Akamwagiza opereta wake kumpatia viongozi wa ofisi zote za usalama katika nchi za mstari wa mbele, pamoja na Naijeria. Alipowapata alipanga nao kufanya mkutano wa dharura ambao ulikusudiwa kujadili hali inayozikabili nchi zao. Ilikuwa kama wote walikuwa wakiusubiri kwa hamu wito huu. Wakaafikiana kukutana Jijini Dar es Salaam siku mbili baadae.
Kombora, akiwa mwenyeji, alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huu uliofanywa kwa siri kubwa. Mkutano huu ulijumuisha watu wenye sura mbalimbali, umri tofauti, viwango tofauti vya elimu; wote wakiwa na dhamira moja. Kila mmoja alieleza tishio lililokuwa likiikabiri nchi yake na kila mmoja alieleza hatua ambazo tayari zilikuwa zimechukuliwa. Lakini wote waliafikiana kuwa matunda ya juhudi zao hayakuwa ya kuridhisha. Wote walifahamu kuwa matunda ya maafa yaliyokuwa mbele yao siku za usoni, endapo yasingekomeshwa, yangesababisha maafa na vilio ambavyo historia haikupata kuvishuhudia.
“Jambo linalotisha zaidi ni maoni au hisia za wanasayansi wetu,” mjumbe mmoja alieleza. “Wanaamini kuwa moto huu unatokea angani katika chombo ambacho hakionekani kwa macho. Hivyo, jukumu letu ni kukilipua chombo hicho. Tutawezaje wakati hatukioni?”
“Labda tuilazimishe Afrika ya Kusini ikiteremshe.”
“Hilo ndilo tatizo. Tutawezaje kuilazimisha? Tumejaribu kutazama uwezekano wa kuishambulia kijeshi kwa pamoja na kuona si rahisi. Wao wamejiimarisha sana kiulinzi angani, majini na nchi kavu. Nasi Waafrika umoja wetu unalegalega kiasi kwamba hatuwezi kuafikiana mara moja. Vilevile, wakati tutakapokuwa tukijiandaa kwenda huko madhara waliyotishia yatakuwa yakiendelea kutukia.”
“Lakini haiwezekani tukubali kuwa hatuwezi kufanya kitu,” Kombora alieleza kwa sauti. “Lazima tufanye jambo. Jema au baya, lazima tulifanye mapema.”
Aliungwa mkono.
Mara simu ikaroma katika meza ya Kombora. Akaitazama saa yake na kuona kuwa zilikuwa zimesalia dakika nane kutimia saa kumi za alfajiri. Akainua simu hiyo na kusikiliza. Ilipigwa na msaidizi wake ambaye alimwomba atoke nje mara moja. Kombora akawataka radhi wageni wake na kutoka.
Dakika chache baadaye alirudi ndani akiwa kaandamana na mgeni mmoja ambaye alikuwa katika hali ya kusikitisha. Mgeni huyo alikuwa mtu mweupe, aliyevaa mavazi yaliyochakaa. Mwili wake ulikuwa umejaa majeraha na mikwaruzo mingi kiasi cha kumfanya aonekane mahututi. Hata hivyo, macho yake yalikuwa na uhai.
“Huyu ni mgeni ambaye amekamatwa huko mpakani mwa Malawi na Tanzania leo,” Kombora alieleza. “Amesema ametoroka kutoka Afrika ya Kusini kuja baada ya kuponea chupuchupu. Maelezo yake nadhani yatatufaa katika kikao hiki,” alimaliza akimwashiria mtu huyo kujieleza.
“Kwanza ningependa ieleweke kuwa mimi sio mzungu, “mtu huyo alisema. “Mimi ni mtu mweusi, mzaliwa wa Soweto,” alisema akifungua vifungo vya shati lake. Kila mmoja alitokwa na macho ya mshangao kwa kuona kuanzia tumboni alikuwa na ngozi nyeusi. “Ngozi hii nyeupe iliyokaa usoni na mikononi ni matokeo ya plastic surgery ambayo nilifanya miaka kumi iliyopita ili niweze kuingia miongoni mwa makaburu na kuiba siri zao ili zitusaidie katika vita vyetu vya kujikomboa,” alisita kidogo. Kisha akaendelea. “Nimefanya kazi mbalimbali katika jeshi hilo, daima nikiwa macho kupeleleza hiki na kile. Majuzi ndipo nilipogundua jambo la kutisha zaidi. Niligundua kuwa umejengwa mtambo ambao unaendesha Setilaiti ambayo haionekani kwa macho inayotumiwa kuteketeza majumba na sehemu muhimu za kiuchumi katika nchi za kiafrika. Nikaanza upelelezi wa makini kutafuta uwezekano wa kuangamiza tishia hilo. Kwa bahati mbaya, walinishuku katika upelelezi wangu. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kuikimbiza roho yangu. Hata hivyo, nimeona mengi, nadhani naweza kutoa mchango madhubuti ambao utatuwezesha kushinda.”
Wakuu hao wa upelelezi walimtazama mtu huyo kwa makini kisha wakatazamana. Mmoja alicheka, mwingine akatabasamu.
“Hatimaye….” mmojawao alinong’ona.
SURA YA NANE
KATIKA jumba fulani, mtaa fulani, jijini Johannesburg, makaburu wanne waliketi katika ofisi moja wakisikiliza taarifa za kijasusi kutoka Tanzania. Jasusi moja lilikuwa likiwaarifu kwa kutumia chombo maalumu juu ya msafara wake na mafanikio ya shughuli zake.
“Nimefika salama na kuwakabili nikiwa katika hali ya kusikitisha iliyonifanya niaminike kama mmoja wao. Wameumeza kabisa uongo wangu. Sasa hivi wananiamini sana. Wameniuliza mwaswali mengi na nimewajibu kiume nikiwapa taarifa za uongo. Nadhani wamekusudia kuwatuma wapelelezi wao huko, ingawa hawakupenda kunishirikisha moja kwa moja. Hata hivyo, msijali, nitakuwa macho nikiarifu kila kitendo chao hatua kwa hatua.”
Makaburu wakatazamana tena na kutabasamu kwa namna ya kupongezana. Mmoja wao hakuona kama tabasamu linamtosha. Yeye aliangua kicheko. Kisha aliona kicheko hakitoshi. Akainuka na kuliendea kabati lililokuwa nyuma yake ambamo alitoa chupa kubwa ya pombe kali, aina ya JohnWalker na glasi nne. Akazileta mezani na kuziweka mbele ya kila mmoja. Akaifungua na kumimina. “Lazima tusherehekee ushindi.” Baadae akaongeza, “Sitoi ruhusa ya kunywa ofisini isipokuwa inapobidi kufurahi. Mwanadamu hana budi… Cheers…”
Kaburu huyu kwa jina aliitwa Von Iron, kwa sura hakutofautiana sana na mtoto mchanga ingawa kiumbo alikaribiana na kiboko aliyeshiba vizuri. Yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa kamati hii maalumu ya BOSS ambayo iliundwa kuzishughulikia kikamilifu nchi za kiafrika ‘zinazojitia kichwa ngumu.’ Amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hili la kijasusi tangu lilipoundwa miaka mingi iliyopita. Mara kwa mara kazi yake imekuwa nzuri kwa wakubwa zake. Haikupata kutokea mpango aliouandaa ukashindwa kutoa mafanikio, jambo ambalo lilimpa heshima na hadhi machoni mwa weupe na kumfanya jazanda ya mauti katika fikra za weusi. Ni yeye aliyebuni uwezekano wa kuitumia nguvu ya nyuklia kuwaangamiza Waafrika. Hakuwa Mwanasayansi, lakini alipewa jukumu la kushirikiana nao, akiwa na uhuru wa kutumia kiasi chochote cha pesa hadi majaribio yalipofanyika na kutoa matunda ya kupendeza. Kadhalika, ni yeye aliyebuni mpango wa kuwapa ngozi nyeusi baadhi ya wapelelezi wao, kwa kupoteza pesa nyingi katika hospitali zinazofanya Plastic Surgery. Watu hao waliingizwa kwa hila katika vikundi vya wapigania uhuru na kujifanya wenzao huku wakitoa siri zote na hata kuua inapobidi. Mmoja wa watu hao ni huyu ambaye alikuwa akiwafurahisha sana kwa taarifa zake kutoka Tanzania.
Yeye alifanyiwa mabadiliko ya ngozi yake miaka mitano iliyopita, akawa mweusi na kutibua mambo mengi katika chama cha SWAPO na ANC. Majuzi alirudishwa Ulaya ambako alirudishiwa ngozi ya mtu mweupe usoni na mikononi, kisha akatumwa Tanzania ambako waliona ni chimbuko la misukosuko yote dhidi ya utawala wao, na hasa ili wajue nini kinafanyika katika kutapatapa kwa Serikali na wananchi wa Tanzania juu ya mtambo wao wa aina yake ulioko angani baada ya kutoeleweka kilichomtukia mtu wao, Chonde, hata akafa katika hoteli moja. Zaidi, huyu alikuwa amepewa akiba ya kutosha ya zile gololi zinazouongoza mtambo huo kulipua miradi teule ili wakati utakapowadia waachie pigo hili walilokusudia kulifanya, “Pigo la mwisho.”
Umaarufu wa Von Iron dhidi ya ngozi nyeusi ulichipuka katika roho yake tangu utotoni baada ya kukua katika familia ya kitajiri ambayo iliwatenda waafrika kama wanyama. Hayati baba yake alikuwa na mgodi wa dhahabu. Watumishi wengi walifanya kazi humo huku wakilipwa ujira hafifu mno kiasi cha kuwafanya washindwe kuyamudu maisha. Jambo hilo hakuna aliyeonekana kulijali, hata katika fikra za Von ikajengeka kwamba mtu mweusi ni chombo cha mtu mweupe, ambacho hakina haki wala thamani.
Halafu ikatukia maafa katika mgodi. Baba yake alikuwa katika moja ya ziara zake adimu wakati ilipotokea hitilafu hii ambayo hadi leo chanzo chake hakifahamiki. Hitilafu hiyo ilisababisha maafa makubwa kwa wafanyakazi wengi, weusi kwa weupe. Hayati Iron mwenyewe aliponea chupuchupu. Kama asingejitokeza mtumishi wa Kiafrika, mzee mkongwe, ambaye alitumia nguvu zake zote kumtoa katika chumba kilichokuwa kimefunikwa kwa mawe, siku hiyo angeyapoteza maisha yake. Hata hivyo, jukumu hilo lilimgharimu mzee huyo maisha yake kutokana na majeraha mabaya aliyopata. Kifo hicho kilimsikitisha sana mzee Iron hata akajitolea kuishi na mtoto pekee wa mzee huyo ambaye alikuwa msichana mzuri, ingawa uzuri huo ulipotoshwa na unyonge aliokuwa nao rohoni. Uamuzi wa kuishi na Mwafrika katika nyumba moja, ukiwa jambo geni sana wakati huo, uliisababishia familia yake mgogoro mkubwa, hasa mkewe. Lakini Iron hakulikubali hilo asilani. Badala yake akazidisha mapenzi kwa msichana huyo huku akiahidi kumpeleka masomoni, nje ya nchi.
Halafu ikatokea. Mzee Iron akafumaniwa na msichana huyo. Ilikuwa habari iliyojaa aibu kubwa masikioni mwa kila mtu mweupe. Lakini Iron hakuona aibu. Alikitetea kitendo chake na kukataa matakwa ya mkewe kwamba msichana huyo yatima afukuzwe. Hata mkewe alipotishia kujiua Iron hakukubali kumtupia msichana huyo lawama ambazo hazikumstahili. Ikatokea tena. Wakafumaniwa kwa mara ya tatu. Hapo mama Iron hakustahamili zaidi. Alirudi chumbani ambako alichukua bastola na kumwua msichana yule mweusi.
Mzee Iron alizirai kwa hasira. Fahamu zilipomrudia aliipokonya bastola hiyo kutoka mikononi mwa mkewe na kumpiga risasi mbili kifuani. Kisha alijilenga kichwa na kufyatua risasi zote zilizosalia. Vifo vyao vilikuwa simulizi kubwa mitaani kwa muda mrefu. Vilimwacha Von katika msiba wa uyatima, msiba ambao ulizaa hasira dhidi ya mtu mweusi; akijua kuwa ni mtu mweusi aliyemnyima haki ya kuwa na wazazi. Jambo hilo lilimfanya siku zote awe mstari wa mbele katika kutukuza na kutekeleza taratibu zote za ubaguzi. Daima alikuwa mkatili kuliko wakatili, mnyama kuliko wanyama dhidi ya mtu mweusi. Matokeo yake yakawa kupata vyeo vilivyomwezesha kuwa na mamlaka juu ya uhai na kifo kwa kila mtu mweusi katika shirika hili la kijasusi. Wengi waliuawa kwa ajili yake, mengi yaliendelea kufanyika ili kumkomoa mtu mweusi kutokana na mapendekezo yake. Lakini hakukoma kuendelea kubuni. Mtambo uliokuwa angani ukisubiri kuiharibu Afrika huru ulikuwa moja tu kati ya ubunifu wake.
Pamoja na kutenda mengi ya kikatili, pamoja na kuhakikisha watu weusi wengi wasio na hatia wakipoteza maisha yao, bado Von hakuona kama viumbe hawa walielekea kumpigia mtu mweupe magoti. Badala yake waliendelea kusimama kiume wakitetea haki yao. Alipokufa huyu, alizaliwa huyu, wimbo uleule ukiwa mdomoni. Hata Mandela, ambaye alikuwa kifungoni, alipoteswa bado aliendelea kuwa na msimamo uleule. Hilo, kiasi lilimtisha sana kaburu Von. Hakuwaelewa kabisa watu hawa. Wana nini katika damu yao?
Swali hilo lilikuwa likimletea maswali mengine ambayo yalijenga hisia fulani, maswali yaligongana kichwani mwake. Alikuwa akijiuliza: baba yake aliona nini katika nywele kavu, ngozi nyeusi na sura ya kusikitisha ya yule msichana wa Kiafrika hata akadiriki kumwua mkewe na kujiua mwenyewe! Aliwahi kusikia hadithi ya mtu mwingine ambaye alimwacha mkewe na kukimbia na msichana mweusi hadi Marekani ambako walifunga ndoa. Wana nini watu hawa? Iko siri gani ndani ya ngozi zao zinazotisha? Labda ingebidi alifumbue fumbo hili kwa kumpata mmoja ili aonje? Lakini…mweusi… Hapana. Mara kwa mara aliyafukuzia mbali maswali hayo ambayo yalimjia bila taarifa, hasa alipoukumbuka uyatima wake.
“Cheers,” Von aliropoka tena.
Wenzake wakageuka na kumtazama kwa mshangao. Kisha wakatabasamu kimyakimya, wakiendelea kunywa taratibu. Baada ya vinywaji hivyo, Von aliamua waendelee na kikao chao.
Walivuta mafaili ya suala la Chonde na kuangalia wamefikia wapi juu ya kisa cha kifo chake na mali zake zilielekea wapi. Bado haikueleweka nani alimuua na maiti ya pili chumbani mle ilikuwa ya nani. Zaidi haikufahamika vitu alivyokuwa navyo, ambavyo ni vya hatari na siri kubwa, vilikwenda wapi. Kitu kimoja walikuwa na hakika nacho. Vitu hivyo havikufika mikononi mwa polisi, jambo ambalo liliwafanya waafikiane kuwa watu waliomwua Chonde na kumwibia pesa nyingi na vitu alivyokuwanavyo ni majambazi wa kawaida, ambayo yangevitupa vifaa vile muhimu kama takataka na nyaraka za siri kama uchafu. Kitu ambacho wangejua kukitumia ni pesa za Tanzania na za kigeni ambazo zingewachukua miezi mingi kabla ya kuzimaliza.
Pesa hazikuwa tatizo kwa akina Von. Walilitupa suala hilo kando bila kinyongo, hasa wakijua kuwa tayari mtu wao mwingine, Clay, alikuwa nchini Tanzania akiwa na kila kitu kilichohitajika na tayari kwa yote waliyohitaji kufanya. Alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya Chonde kwani uongo aliokwenda nao ungemfanya aonekane kama almasi machoni mwa maafisa wa usalama wa nchi zote za mstari wa mbele za Kiafrika.
“Nadhani iliyobaki ni kuongeza ulinzi katika mtambo wetu,” Von aliendelea. “Ingawa Clay yuko kwao na atatuarifu kila wanachokusudia kufanya, lakini kuna mengine watakayoshindwa kumwambia. Ni wazi kuwa watatumwa wapelelezi waje, lakini sitaki warudi. Nadhani tunaelewana.”
Akaungwa mkono.
Mara simu ya dharura ikaanza kulia. Ikiwa simu ambayo hulia kwa nadra sana, Von aliinua mkono na kuidaka mara moja. “Von hapa,” akanguruma katika chombo cha kusemea.
“Bosi, hapa ni kikosi cha ulinzi wa anga. Ndege zetu za ulinzi zimeizunguka ndege moja ambayo ina watu wanne tu, rubani na msaidizi wake na abiria wawili ambao ni mwanamke na mwanamume. Rubani wa ndege hiyo anaomba kutua, akidai kuwa ametekwa nyara na abiria hao ambao wamejitambulisha kama Joram Kiango na mpenzi wake Nuru. Tunauliza kama tuwaruhusu kutua au tuwalipue”.
“Nani, Joram?” Von aliuliza.
“Ndiyo. Joram Kiango. Yule…”
Mara Von akalikumbuka jina hilo vizuri. Halikuwa jina la kupendeza hata chembe masikioni mwake, ingawa siku mbili tatu zilizopita limesikika kwa namna ya kupendeza kiasi. Joram kuja Afrika Kusini! Baada ya kuharibu mipango yao mingi ya kuikomoa Tanzania! Bila shaka ni kujaribu kujificha baada ya kuiibia nchi yake akiba yote ya pesa za kigeni. Vizuri. Tutampa hifadhi ya kudumu. Anaweza kujificha milele katika makaburi yetu. Hatuna roho mbaya.
“Umesema Joram siyo? Sikia. Huna haja ya kutumia silaha kubwa. Anaweza kufa polepole. Mwambie atue.”
Kwa Afrika Kusini ilikuwa kama nafasi ya dhahabu. Vyombo vyote vya habari vilishangilia kwa nguvu kuwasili kwa Joram na Nuru katika nchi yao. Waliipamba habari hiyo kwa kutia chumvi nyingi juu ya wizi wake. Walieleza jinsi alivyopokonya pesa hizo, alivyozitumia kwa starehe sehemu mbalimbali duniani, alivyofaulu kuwalaghai polisi wote wa dunia, na mwisho alivyoona hana hila zaidi ya kukimbilia Afrika Kusini, ili ajifiche maisha.
“Huu ni mfano hai kwa watu weusi kote ulimwenguni,” mtangazaji mmoja wa televisheni alieleza. “Hakuna asiyemfahamu huyu Joram. Alijifanya mpigania haki, usawa na usalama wa watu wake. Amesababisha vifo vya watu wengi ambao walikuwa na nia njema ya kuikomboa nchi yake. Ndivyo walivyo watu weusi wote. Wanawalaghai wenzi wao na kuwafanya waote mikia misituni eti wakidai haki na uhuru. Matokeo yake ni kuwafanya, hao wenzi wao, vijakazi, wakati wao wakituna matumbo mara tu baada ya kupata madaraka. Natumaini watu weusi wote mnaodanganywa mtaitumia nafasi hii kuuona ukweli wa mambo. Ngozi nyeusi ni dalili ya laana. Nywele fupi ni dalili ya akili ndogo. Bila hekima na uongozi wa mtu mweupe Afrika ingekuwa bado gizani, na endapo ataondoka mtu mweupe giza litarudi…”
Hayo yalisemwa baada ya watu kuwatazama Joram na Nuru wakitoka katika ndege iliyowaleta, huku wakiwa wametanguliwa na rubani ambaye walikuwa wamemshikia bastola. Nje ya ndege Joram aliitupa chini bastola yake na kuweka mikono yake juu. Ndipo Polisi wa makaburu ambao walikuwa wameuzingira uwanja wakiwasubiri, wakajitokeza na kuwakimbilia. Wakawavamia na kuwakagua harakaharaka. Walipoona kuwa hawana silaha nyingine wakawaongoza kuliendea gari lililokuwa likisubiri. Muda wote huo kamera za televisheni na zile za wapiga picha wa magazeti ziliwaelekea Joram na Nuru kwa ukamilifu. Kama kuna chochote kilichowashangaza watazamaji ni jinsi sura za vijana hawa zilivyoonekana tulivu, nzuri, zisizo na dalili zozote za ugangwe kama walivyotegemea.
Msafara wa gari uliishia katika jumba moja kubwa lenye ghorofa kadhaa. Humo, badala ya lifti waliyoingia kuwapandisha juu iliwateremsha chini ambako walijikuta katika chumba kilichoelekea kuwa maalumu kwa kuhoji mateka. Askari waliokuwa nao waliamuru kusubiri, kisha wakatoka na kuufunga mlango nyuma yao. Baada ya muda waliletewa chakula na vinywaji. Wakala na kunywa.
Baada ya muda, kama walivyotegemea, walianza kutembelewa na maafisa wa upelelezi, ambao waliuliza maswali kemkem. Maswali yote waliyajibu kwa ukamilifu kama walivyojiandaa; kwamba walikuwa wameishiwa na hila za kuwaepuka INTERPOL wakaona hawana njia nyingine zaidi ya kukimbilia huku ambako wangehitaji hifadhi.
Baada ya maswali yalifuata mawaidha na badala ya mawaidha ikawa kashfa. “Wewe kama Joram Kiango ambaye nchi yako na Afrika nzima ilikutegemea huoni aibu kufanya ulivyofanya na kuja huku?” aliulizwa
“…Utajisikiaje utakapolazimika kufuata matakwa yote ya ubaguzi na kulazimika kushuhudia Waafrika wanavyonyanyaswa?”
“…Unaweza kukiri hadharani kuwa viongozi wote wa Afrika ni wadanganyifu na hawajui watendalo?”
“…Ukipewa bastola ili umuue mpigania uhuru yeyote atakayematwa, utafanyaje?”
“…Huyu msichana na uzuri wake wote ni malaya? Mbona anakubali kuandamana na mwizi?”
Yalisemwa mengi zaidi ya hayo. Yako ambayo Joram alijibu kwa namna ambavyo alijua walimtegemea kujibu. Mengine hakuyajibu, akijua kuwa walimtegemea kutojibu. Mengine ilimlazimu kuinama kwa haya akiwa na hakika kwamba walitarajia aone aibu. Baadhi ya maswali aliyakwepa kijanja akijua ni mitego iliyokusudiwa kumnasa.
Kutoka hapo walipelekwa katika chumba kilichokuwa na mitambo mingi ambayo eti ingeonyesha kama walikuwa wakisema ukweli au la. Waliwekwa katika mitambo hiyo na kuanza kuulizwa tena maswali. Yote hayo Joram alikwishamfafanulia Nuru kabla hawajaondoka Paris kuja Kinshasa, Zaire, ambako waliiteka nyara ndege ile ya kukodi. Alimweleza kuwa ambacho mtambo kama huo unaweza kuonyesha ni dalili za moyo kudunda na damu kuchemka mara unapoulizwa swali ambalo litakushtua au unapobuni uongo. Hivyo, endapo utazungumza kwa kujiamini haitaonekana dalili yoyote.
Ndivyo ilivyotukia. Saa chache baadaye walichukukuliwa na gari kutoka katika chumba hicho na kupelekwa katikati ya mji ambako waliingizwa katika nyumba moja kubwa na kuelekezwa katika chumba kilichokuwa na vitanda viwili. Humo walikuta mizigo yao yote. Ingawa mizigo yao ilikuwa kama ilivyokuwa, lakini Joram hakusita kugundua kuwa tayari ilikuwa imekaguliwa kwa ukamilifu. Hilo alilithibitisha baada ya kufungua na kukuta kila kitu kimo isipokuwa furushi la pesa zilizokuwa zimesalia. Hilo pia alilitegemea. Hivyo, hakubabaika. Akamwendea Nuru na kumvuta mkono akimwelekeza kitandani ambako alimketisha ili ampumzike kidogo.
“Pole,” alimwambia.
“Kwa?”
“Usumbufu.”
“Mbona bado sijasumbuka. Naamini huu ni mwanzo tu, kuna mengi yanayokuja na nitakuwa tayari kuyakabili yote…”
“Shii,” Joram alimnyamazisha. “Usijisikie huru kiasi hicho,” alinong’ona. “Bado tuko chini ya ulinzi mkali. Yawezekana wanatutazama na kutusikiliza. Kiswahili si lugha ngumu kiasi hicho. Endelea kujihadhari.”
Moyoni Joram alikuwa na sherehe kubwa. Alikuwa akishangilia mafanikio ya msafara huo ambao ulienda kama alivyokusudia kuelekea kuzaa matunda. Kufika Afrika Kusini na kupata mapokezi yenye hadhi kwa kiwango hiki ilikuwa jambo pekee la pili ambalo alilihitaji sana. Jambo la awali ambalo alihakikisha limefanikiwa kabla hajabandua mguu wakekuiacha dunia huru na kujitosa jehanamu kiasi hiki ilikuwa kulisafirisha sanduku lake ambalo lilikuwa na kila kitu alichohitaji katika jukumu lililokuwa mbele yake. Kati ya vitu vilivyokuwemo ni pamoja na pesa za matumizi muhimu, silaha aina aina, madawa ya kila aina, ramani mbalimbali, ngozi na sura za bandia ambazo zingemfanya aonekane mtu mweupe, na zaidi ya yote ni vile vijigololi maalumu ambavyo alivipata kutoka kwa hayati Chonde.
Ilikuwa imemgharimu uongo mkubwa na pesa kuweza kulifikisha sanduku lile katika nchi hii. Alikuwa ametumia hila za kumwendea mfanyabiashara wa Kimarekani ambaye alikuwa akisafirisha mizigo yake moja kwa moja kutoka Ufaransa. Baada ya kujijenga kwake kwa urafiki bandia alimhadaa kuwa amepata oda ya kuuza madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini. Mmarekani huyo alikataa kabisa kujihusisha kwa hali yoyote katika biashara ya aina hiyo. Joram alikazimika kumpigia magoti kwa maneno huku akimpa pesa nyingi na kumwahidi sehemu kubwa ya faida. Ndipo sanduku hilo liliposafiri pamoja na mizigo mingine muhimu ya Joram. Na aliarifiwa kuwa sanduku hilo limefika salama. Ilimpendeza sana Joram kuona kati ya watu wengi waliokuja kiwanjani kushuhudia wateka nyara hao wakitelemka kutoka ndani ya ndege, mmoja wao alikuwa Mmarekani huyo aliyeitwa Moore. Ilimpendeza zaidi kuwa Moore hakuweza kufahamu kuwa mteka nyara huyo ndiye yule aliyekuwa rafiki yake siku tatu zilizopita nchini Ufaransa. Joram akiwa amekariri ramani ya nyumba ya Moore kama anavyovifahamu viganja vyake vya mkono, alikuwa akiisubiri kwa kiu kibwa fursa ya kuweka mikononi mwake mizigo yake.
Kabla ya kuoga kama alivyohitaji kufanya, Joram alijitia shughuli na kufanya kama anayepanga vitu chumbani kwake vizuri. Alichokuwa akifanya hasa ni kitu au vitu fulani na haukupita muda kabla ya kukiona alichokuwa akitafuta. Kipande kidogo sana cha kioo kilichokuwa kimejitokeza sakafuni katika pembe moja ya chumba kama kilichosahauriwa na waashi kwa bahati mbaya. Joram alijua kuwa nyuma yake kipande hicho kulikuwa na nyaya ambazo zilisafiri hadi kwenye mtambo ambao ulikuwa na jukumu la kupeperusha kila wanachoongea au hata kuwaona. Baada ya kuona hayo Joram alilidhika, akijua kuwa alikuwa hana haraka ya kuwa msiri. Alihitaji faragha kwa usiku mmoja tu, na katika usiku huo alijua ambacho angefanya kuufanya mtambo huo ushindwe kuwajibika kwa dakika kadhaa.
Wakaoga.
Wakalala.
Jasho jembamba lilikuwa likiwatoka maofisa wanne wa Boss ambao walikuwa katika chumba fulani wakiwashuhudia Joram na Nuru walipokuwa wakifanya mapenzi katika chumba chao. Maofisa hao walikuwa wamekaa katika chumba hicho kwa muda mrefu, dhamira yao kuu ikiwa kupata hakika kama kweli Joram alikuwa hana hila nyingine iliyomleta Afrika Kusini zaidi ya ukimbizi. Taarifa za maofisa wote waliotumwa kuwahoji na ambao walikagua mizigo yao haikuonyesha hila wala ila yoyote. Hata hivyo upinzani uliokuwepo uliishia kuamuliwa kuwa wapewe chumba hiki na kuachiwa uhuru kiasi fulani ili waendelee kuchunguzwa. Chumba hiki kilikuwa maalumu na siri kubwa isipokuwa kwa maofisa wachache wa ngazi za juu. Ndipo jukumu la kuwatazama Joram na Nuru likawaangukia kaburu Von Iron na wenzake.
Ndipo walipolazimika kutokwa na jasho. Kwani walikuwa wakitazama kwa namna moja ilikuwa kama picha ya kupendeza sana, kwa maaana nyingine picha ya kuchukiza, inayotesa na kuadhibu.
Ilikuwa picha ya kupendeza wakati walipokuwa wakiwatazama Joram na mpenzi wake Nuru walipokuwa wakitazamana kwa mapenzi pindi wakati wakijiandaa kulala. Ikaanza kuchukiza walipoanza kuvua mavazi yao na kuketi kama walivyozaliwa huku wakibusiana. Na ilianza kutesa walipojibwaga kitandani na kufanya mapenzi kiroho mbaya bila kujali au kujua kama wanatazamwa, kana kwamba walikuwa wakiwaonyesha watazamani kwa makusudi.
Von Iron aliuzima mtambo huo na kulifuta jasho lililokuwa katika paji lake la uso. Hakujiamini kuwatazama wenzake machoni, akihofu wasije wakasoma kitu alichokuwa akikisoma akilini. “Tukutane kesho…” Von aliamuru akianza kutoka nje. Bila kuinua macho aliweza kuhisi kuwa wenzake walikuwa wakimhurumia zaidi ya walivyokuwa wakijihurumia wao. Alijua vilevile kuwa wenzake hao walijua kama alivyojua yeye kuwa baada ya kuagana nao angerudi katika chumba hicho.
Alirudi.
Akiwa peke yake aliwatazama kwa makini na uhuru zaidi, akisherehekea kila hatua iliyofuata katika mapenzi yaliyokuwa yakiendelea mtindo mmoja juu ya kitanda. Tangu alipokuwa amewaona Nuru na Joram katika televisheni hajua kuwa wangeweza kuwa wazuri kiasi hiki. Kadhalika hakutegemea kuwa Mwafrika aliyevua nguo angeweza kuwa kiumbe mzuri kama hawa, aliwategemea kuwa viumbe wa kutisha sana kama mizimu. Kumbe sivyo.
Aliendelea kuwatazama. Alijipinda na kujinyoosha kwa maumivu na tamaa kubwa huku mkono wake mmoja akiubembeleza uume wake, mkono wake wa pili ukiwa umelea kichwa kwa wivu wa masikitiko. Starehe au mateso yake yalikoma Joram alipozima taa.
Von alijifariji kwa kuizima mitambo hiyo na kubonyeza ile ambayo ilimfanya akague ulinzi na usalama wa ule mtambo wa nyuklia unaoendesha Satilaiti maalumu iliyoko angani ikisubiri kufanya kazi ambayo haitafutika katika kurasa za historia ya dunia. Aliuona ulinzi ulivyokuwa makini. Askari wanne wenye machine guns walikuwa wakipita kwa zamu kulikagua jengo hilo. Ndani mafunzi wenye silaha walikuwa machio wakikagua mwenendo wa mtambo huo kwa umakini na uangalifu mkubwa. Von aliweza kuona katika screen kubwa iliyokuwa mbele ya wanasayansi hao jinsi setileiti hiyo ilivyokuwa ikielea huku na huko katika bahari ya Hindi kando ya pwani ya Afrika Mashariki. Alitabasamu kidogo alipojikumbusha utaalamu wa hali ya juu uliotumika katika kuunda chombo hicho hata kisiweze kuonekana kwa macho ya kawaida.
Kisha alibonyeza mahali fulani kuondoa mtambo huo machoni kwake. Badala yake alibonyeza mahali ambapo palimwezesha kuona gereza la ardhini ambamo kulikuwa na mateka au wafungwa ambao walitakiwa kuteswa hadi kufa. Humo kulikuwa na kila aina ya mateso. Haikuwepo njia yoyote ya kuweza kutoka isipokuwa kwa funguo maalumu ambazo alidhihifadhi yeye mwenyewe.Von aliwatazama wafungwa au mateka hao waliokuwa wakikaribia kufa. Baadhi yao walikuwa weupe, Mmarekani mmoja ambaye alikuwa mpumbavu kiasi cha kuamua kuwasaidia wapigania haki wa Afrika Kusini, pia walikuwepo Warusi wawili ambao pia tabia zao hazikuwa tofauti na mzungu huyo pamoja na watu weusi watatu. Ni hawa watu weusi ambao walimfanya Von aangue kicheko kwa sauti. Alijiuliza walikuwa wamepatwa na nini weusi hawa hata wakathubutu kujileta wenyewe huku kama wapumbavu. Mtu atajipeleka jehanamu na kutegemea atatoka salama?
Zimesikika habari nyingi za watu ambao waliwahi kufa na baada ya siku kadhaa kufufuka. Watu hao hudai kuwa walipokuwa wafu wamefika peponi na kuwaona malaika. Haijawa kutokea hata mtu mmoja ambaye aliwahi kwenda jehanamu na akarudi duniani. Hawa weusi aliwaona kama watu walipenda sana kufa vifo vya kikatili. Jambo la kusikitisha kwao ni kwamba BOSS iliarifiwa tangu walipoondoka Naijeria na Tanzania na kuja Botswana. Iliarifiwa pia walipoanza mbibu za kuvuka mpaka. Hivyo hila zao za mmoja kujifanya wendawazimu asiyejua analofanya na mwingine kujitia mkimbizi anayeishi kambi ya wapigania uhuru hazikuwa na mafanikio yoyote. Von hakupenda kuwaona ana kwa ana. Aliamua wafungiwe katika chumba cha mauti wasubiri kifo. Hawa walikuwa wawili tu kati ya wanane ambao walikuwa wamekamatwa siku mbili zilizopita. Wawili walikuwa wameuawa kwa mateso wakati wakihojiwa. Mmoja alikuwa amejiua mwenyewe kwa sumu baada ya kumvamia askari aliyekuwa akimhoji na kumjeruhi vibaya kwa kisu kabla hajameza vidonge ambavyo vilimuua mwenyewe.
Wapelelezi hawa walikuwa ni matokeo ya juhudi za kuthibitisha uwezekano wa kuwepo kwa mtambo maalumu unaoziadhibu nchi za Kiafrika. Von alifahamu kuwa bado wangekuja wengi zaidi, weupe kwa weusi, lakini kamwe wasingefika popote pa haja. Na kamwe wasingefika popote kwani zilikuwa zimesalia siku mbili tu kabla ya Afrika huru kuipigia magoti Afrika Kusini na kusubiri vilio na maombolezo yasiyo na mfano. Von alicheka tena, safari hii kwa kujipongeza akijua kuwa sifa ndogo kuwa na wadhifa kama aliokuwa nao sasa. Roho za watu wengi kuwa mikononi mwako zikisubiri tamko lako kabla ya kuteketezwa!
Kisha Von aliufunga mtambo huo na kurudi nyumbani kwake. Akiwa kapera ambaye hakujua lini angeoa alijikuta akikosa usingizi alijikuta akimfikiria Nuru na kumwonea Joram wivu. Bila kufahamu anachokifanya Von alijikuta akiapa kwa jina la Mungu kuwa asingekufa kabla hajamuonja. “Mara moja tu…” alijiambia. “Nione wana nini wanawake weusi…”
Kesho yake aliamuru Joram na Nuru waletwe katika ofisi yake. Akiwa amezungukwa na wasaidizi wake Von alijitahidi kuwatazama Joram na Nuru kwa namna tofauti kabisa na ile iliyokuwa ikipita katika akili yake.
“Sina haja ya kuwahoji chochote”, Von aliwaambia kwa sauti nzito. “Kwa kiasi mlichohojiwa naamini mmeonyesha kuwa mmechoshwa na upuuzi wa hawa viongozi wanaojiita wanamapinduzi katika nchi zenu. Sivyo?”
“Kwa maana hiyo mngependa kuishi huku daima. Msimamo wenu ni wa kishujaa. Nawapenda watu shujaa. Ni hilo ambalo limenisukuma kuwaacha hai pamoja na kuwapa heshima ya kuwaita hapa ili niwape habari njema”.
Joram akiwa amesimama mbele yake, akiwa kamshika Nuru mkono, hakuwa na haja ya kuambiwa huyu ni nani katika nchi hii. Alimfahamu mara moja kuwa alikuwa mkuu wa shirika la kijasusi la utawala huu. Kwa maana nyingine alikuwa adui yake namba moja. Mtu ambaye asingeondoka bila kumpa adhabu ya risasi ya kichwa kwa hatia ya kusababisha maafa kwa Waafrika wengi wasio na hatia. Hata hivyo Joram hakuonyesha dalili yoyote katika macho yake alipouliza kwa upole, “Habari njema ipi? Tumeruhusiwa kupewa uhuru zaidi ya huu tulionao? Tunajiona kama ndio tuko kifungoni”.
“Mko huru kuliko mnavyostahili”, Von alimjibu Joram. “Habari njema niliyotaka kuwapeni ni juu ya uhalibifu ambao utazitokea nchi za Kiafrika kesho saa nne mchana endapo hawatawatuma viongozi wao hapa leo kuweka saini mikataba ya kuwa watiifu kwa utawala huu na kutothubutu kuwasaidia wendawazimu wanaodai uhuru wa Namibia na haki hapa Afrika Kusini. Kama hawatafanya hivyo hadi saa tatu na nusu za mchana. Nyie mtapewa heshima ya kushuhudia moja kwa moja Ikulu zinavyoungua, majengo yanavyoteketea na watu kupoteza maisha. Mtabahatika kushuhudia jambo la kupendeza. Jambo la kihistoria”.
Macho yake yaliwatazama Joram na Nuru kwa umakini. Nao wakifahamu kuwa kuna kitu kilitakiwa kuonekana katika macho yao, Joram aliruhusu tabasamu kidogo huku Nuru akifuta machozi.
“Ni habari njema”, Joram alisema polepole baadaye akauliza. “Habari njema…, tunaweza kuruhusiwa kurudi chumbani kwetu?”.
Binadamu hajapata kuwa na adui mwingine, mkubwa na mkatili katika maisha yake zaidi ya kifo. Ni kifo pekee ambacho kimeishinda akili ya binadamu. Hakukosea yule mwanamuziki aliyeimba “kifo hakina huruma, kifo ni kiboko yao”. Hutokea binadamu akawa na shughuli zote, siku nenda rudi bila kukipa kifo wazo lolote hadi kinapotokea bila kutegemewa. Ni hiyo sababu pekee inalomfanya mwanadamu asitokwe na jasho la hofu siku zote za maisha yake kwa kuogopa kifo. Kwa vile hutokea bila ya kutegemewa.
Hivyo hakuna kifo kibaya kama kifo cha kusubiri siku na saa. Hasa kifo cha kinyama na cha kikatili kama hiki ambacho kilikuwa kikitegemewa na watu kadha wa kadha katika nchi kadha wa kadha za Kiafrika. Leo ilikuwa imewadia siku ile. Siku ambayo Afrika ya Kusini ilikuwa imetoa kuwa ingekuwa ya mwisho kabla ya kuachia pigo la mwisho ambalo lingeiteketeza miji yote ya nchi zilizoko mstari wa mbele.
Pamoja na ukweli kwamba tukio hili lilikuwa limeamriwa kuwa siri kubwa sana miongoni mwa wahusika, kama yale mengine ambayo huishia katika masikio ya wachache na hutoweka bila ya raia wa kawaida kuyapata, lakini hili kwa njia moja ama nyingine lilikuwa limevuja na kusambaa mitaani. Jambo ambalo lilisababisha mashaka na hofu kubwa mitaani. Wananchi waumini wa dini walitoroka makazini na kukimbilia kwenye makanisa na misikiti ili kutubu dhambi zao zote na kumbembeleza Muumba awanasuwe awanasuwe katika janga hili. Wale ambao hawakumwamini Mungu walitulia katika vikundi vikundi wakizungumza kwa utulivu. Wachache sana waliamua kuyamalizia maisha yao huku wakinywa pombe katika baa ambazo hazikufunguliwa milango.
Viongozi wa Chama na Serikali walikuwa katika vikao vya dharura wakijaribu kujadiliana hili na lile. Lolote la haja halikupatikana, japokuwa yalitokea mapendekezo mengi. Jambo ambalo kila mmoja alitamani kutamka ingawa ulimi ulishindwa kutamka hadharani kwa aibu, ni ambalo lingewahakikishia wananchi uhai na usalama wao. Lakini maadamu ungekuwa uhai usio na uhuru, na usalama usio na uhakika na hakuna aliyethubutu kupendekeza hivyo. Iliyonaki ilikuwa kupeana moyo tu kuwa haiweze kutokea, na endapo itatokea cha kufanya ni kujaribu kuepuka majengo ambayo yanaweza kuelekea kuyavuta macho ya muuaji. Ilielezwa pia kuwa kote nchini wananchi walikuwa wakichimba mahandaki kwa ajili ya kujificha.
Ikulu, Rais na baraza lake la mawaziri walikuwa katika kikao cha muda mrefu. Kikao ambacho kilichukua siku nzima, hata usiku ukaanza kukaribia. Inangawa kilikuwa kikao cha siri sana, lakini ilikuwa dhahiri kuwa chochote ambacho kilikuwa kikijadiliwa ndani hakikupata ufumbuzi ya tatizo. Mmoja alikuwa amependekeza kwa mara nyingine kuwa nafasi hiyo itumike kuivamia Afrika Kusini kijeshi, “Ili tukomeshe kabisa suala hili la kutishiwa na kuonewa mara kwa mara. Tutumie majeshi yetu yote ya nchi za mstari wa mbele kuingia nchini humo na kuanzisha mapambano ili kuunda utawala halali. Najua, adui ana jeshi imara na silaha kali sana. Lakini wingi witu wetu utasaidia tutashinda…”
Mapendekezo hayo yalijadiliwa lakini hayakuonekana kama yangekuwa jibu la kuziokoa nchi za Afrika na kumaliza tatizo ambalo lilikuwa mbele likisubiri saa chache ili litokee. mwingine akatoa wazo. “Si rahisi kutumia masaa manane yaliyobaki kukusanya majeshi na kuyaongoza katika nchi nyingine na kuanzisha vita. Zaidi yote, hatari au mkasa ambao uliokuwa ukisubiriwa ulikuwa ukitokea angani, hivyo uvamizi huo usingesaidia au kuzuia maafa hayo…”. Baraza la mawaziri liliendelea kujadiliana kwa utulivu katika ukumbi huo wa Ikulu. Jengo hilo likiwa miongoni katika majengo kadhaa yaliyokuwa katika orodha ya kulipuliwa ilikuwa kana kwamba Rais na mawaziri wake walikuwa wameamua kikisubiri kifo hicho kwa pamoja; kufa kiofisa…
Binadamu aliyekuwa na hali mbaya kuliko wote nyumbani nchini Tanzania aliitwa Inspekta Mkwaju Kombora. Yeye alikuwa akitaabika kimwili na kiakili. Juhudi zake zote, pamoja na wenzake wa kutoka nchi mbalimbali, zilikuwa kama upuuzi. Upelelezi ulikuwa haukuzaa matunda yoyote yale. Na hasa upelelezi huo ulikuwa kama umewafanya wazidi kujipalia mkaa wa moto; kwani ilikuwa dhahiri kuwa kila jambo linaloafikiwa hapa wakati huo huo utawala wa makaburu unakuwa na taarifa nalo. Hayo yalithibitika alipoarifiwa kuwa wapelelezi wote waliotumwa kuingia Afrika Kusini walikuwa mikononi mwa makaburu. Ilikuwa kama waliopelekwa kufa makusudi kabisa. Jambo ambalo lilimfanya ashuku mara moja kwamba miongoni mwao alikuwemo chui aliyejivika ngozi ya kondoo.
Hivyo Insipekta Kombora aliugeuza upelelezi wake kutoka mstari wa mbele na kuanza kuchunguza mstari wa nyuma. Na haukupita muda kabla dalili hazijajitokeza kuwa huyu mgeni aliyedhaniwa kuwa msamaria mwema, ambaye alileta fununu nyingi kutoka Afrika Kusini angehitaji kuchunguzwa zaidi. Uchunguzi ukaanza katika vikosi vyote vya wapigania uhuru duniani, katika vyuo na hospitali ambazo alidai amepitia na hata Afrika Kusini. Taarifa zilizidi kuongeza haja ya kutazamwa kwa makini. Na haukupita muda kabla kabla ya watu waliokabidhiwa jukumu la kumwangalia hawajatoa taarifa kuwa alikuwa mtu wa BOSS. Habari hiyo ilimuumiza sana Kombora. Alitoa amri kuwa mtu huyo aliyejiita Clay achunguzwe kwa makini sana, kwani kwa vyovyote leo ilikuwa siku ya mwisho iliyotolewa na utawala huo haramu na lazima angekuwa na jambo la kuarifu kwa mabwana zake.
Baada ya hayo Insipekta Kombora aliendelea na shughuli katika ofisi yake. Alipokea na kujibu simu na walkie talkie nyingi ambazo hakuona kama zilikuwa zikimsaidia chochote. Aliwasiliana na maofisa wenzake katika nchi za Zambia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Naijeria na kwingineko kujaribu kuona wamefikia wapi. Hakuna alichopata zaidi zaidi ya yale aliyotegemea. Kwamba wananchi walikuwa wakitaabika na kulalamika mitaani katika hali ya hofu kubwa. Kwamba hata makazini hawakuwa wamekwenda.
ITAENDELEA
Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;