Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Tatu
NEW AUDIO

Ep 03: Salamu Kutoka Kuzimu

Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Salamu Kutoka Kuzimu

Sehemu ya Tatu (3)

Alirejea haraka nyumbani kumsubiri yule mwanamke aliyeleta picha hiyo. Alipoitazama saa yake aliona ni mapema mno, ingempasa kusubiri kwa masaa mengi zaidi kabla hajatokea. Neema asingeweza kusubiri kwa muda mrefu kiasi kile. Alikuwa na kiu kali ya kumpata mwuaji wa Joram. Huyu Profesa anahusikaje? Pengine anaweza kuwa na fununu fulani ya haja? Hamu ya kuyapata majibu ya maswali hayo ikaushinda nguvu wajibu wake wa kumsubiri Unono kama alivyoelezwa. Badala yake aliisoma tena anuani ile akaiweka picha mezani na kisha akatoka nje kuendea kituo cha mabasi.

Mara akahisi kitu fulani kikimnong’oneza achukue bastola yake. Akarejea ndani katika chumba chake na kuichukua bastola. Baada ya kuhakikisha kuwa bastola hii ilikuwa na risasi zake zote kwenye magazinei, akaiweka kwenye mkoba wake wa kawaida na kuanza safari upya kuelekea mtaa wa India, anakoishi Profesa Kimara.

Proper alikuwa ameketi katika chumba chake cha kusomea aliposikia kengere ya mlango ikilia akashituka. Akainua kichwa kwa mshangao. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kugongewa mlango akiwa chumbani. Majirani zake walifanya ujirani wao wote nje. Rafiki zake ‘bandia’ aliwakaribisha nje kabisa ya nyumba hii.

Muda mfupi kabla ya mlango kugongwa, alikuwa akimalizia kuandika mpango wake kabambe ili baadaye auhariri, na kisha kuuingiza katika mtandao maalumu ambao ungeyrsafirisha maandishi hayo hadi mahali fulani katika nchi fulani huko Ulaya, kwa wakubwa zake. Mpango huo alikuwa ameubuni yeye binafsi, akauhakiki na kuona kuwa lazima utafanikiwa. Yangekuwa mafanikio makubwa ambayo yangeitetemisha Afrika na kuitikisa dunia nzima.

Kwa kuwa hili litakuwa pigo la aina yake, ambalo halijapata kuitokea dunia kwa muda mrefu. Pigo zito kama lile lililotokea wakati wa gharika lililoua watu wote na kumwacha Mungu na familia yake tu. Au kama lile bomu la Atomic lililopigwa na Mwamerika ambalo liliua maelfu ya Wajapani kule Hiloshima. Hili lake pia ingawa alikusudia kuziteketeza baadhi ya nchi, lakini litafanya machozi mengi yamwagike kiasi cha kufanya lisifutike katika kurasa za matukio ya kihistoria duniani.

Mafanikio lazima. Hakukiona kipingamizi chochote. Polisi walikuwa gizani wakitetemeka na kusubiri kwa hofu bila kufahamu wanachosubiri. Watakapotanabai, kazi itakuwa imekamilika. joram Kiango, ambaye alihofiwa kama tishio, ingawa yeye proper hakuona vipi angeweza kumletea vipingamizi, sasa yuko kuzimu. Wafu wenzake watamsimulia ilivyotokea.

Pengine tatizo lingetokana na viongozi wake huko Ugaibuni. Labda ni wao wangeweza kumpinga kutokana na woga wao. Lakini mpango huo ulikuwa wake binafisi, ameubuni, ameuandaa na lazima autekeleze. Imekwisha mgharimu muda na pesa nyingi, zake binafsi wakati akiuhakiki. Yeyote asingeweza kumshawishi abadili mpango wake, zaidi ya hayo, hakumbuki lini waliwahi kupewa changamoto nzito kama hiyo. Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Zaire (Congo), Patrice Lumbumba? Kuuawa kwa Rais Nguabi? Unyama aliofanyiwa Edward Mondolane wa Msumbiji? Hapana. Yeye Proper atafanya zaidi ya hayo. Ataifanya dunia ielekeze macho na masikio hapa.

Kengere ya mlango iliita tena. Ni nani huyo? Proper alijiuliza akificha vifaa vyake vyote. Haraka na kwa utaalamu aliuvua uso wa Proper na kujivika ule wa Profesa Chain Kimara wenye dalili zote za hekima na mshughuriko, uso uliomlaki Neema Iddy aliyekuwa amesimama mlangoni akijiandaa kubonyeza kengere kwa mara ya tatu.

“Karibu mama”, Proper alisema huku akisimama kando kumpisha mgeni wake apite. Kichwani alikuwa kajawa na mshangao mkubwa. Sura nzuri ya msichana huyu haikuwa ngeni machoni mwake ingawa hakuwahi kuiona sura hii ana kwa ana kwa leo. Ilikuwemo katika majarada yake. Ilikuwa sura ya Neema, Katibu Mahsusi wa Joram Kiango. Amewezaje kunishuku mapema kiasi hiki? Proper alikuwa akijiuliza. Si kitu, alijiambia. Nilikosea sana kumsahau. Alistahili kufa kitambo. Alistahili kwenda na Joram. Madaamu kajileta mwenyewe.

“Dada, karibu ndani”, Proper alimhimiza Neema.

“Asante, lakini sikai. Nilitaka… Ni…” Neema alikwama kidogo. Uso uliokuwa mbele yake hakuona kama ulifaa kusumbuliwa kwa maswali yaliyoeleweka. Aliuona kama uso wa msomi mwenye hekima na mengi, ingawa macho yake yalikuwa na kitu zaidi ya uso, alijiona mpumbavu kuja hapa bila subura. Huyu haelekei kuhusika katika kifo cha joram.

“Haraka ya nini?” Proper alimkatiza huku akimtengenezea tabasamu ambalo lilimtoa hofu Neema. “Utaingia ndani, utakaa, unywe walau chupa moja ya bia kisha tutaongea”.

“Hapana, hapana”, Neema alimkanusha, “Sitaki kuupoteza bure muda wako. Nilitaka ku…”

Alikatizwa tena, akashikwa mkono na kuvutwa ndani kistaarabu. Akaonyeshwa kiti ambacho aliketishwa polepole.

“Sikai sana. Samahani kwa kukupotezea muda wako, Nilitaka kujua kama unajua chochote kuhusu Joram Kiango?”, alifaulu kuuliza.

“Joram! Namjua sana. Sidhani kama yupo mtu asiyemjua, Kifo chake kimenishtua sana. Alikuwa kijana wa ajabu sana”. Kisha Proper alijitia kushituka kidogo alipouliza, “Unadhani ni kweli Joram Kiango kafa hivi hivi tu? Mimi siamini. Nadhani wamempa sumu. Wewe waonaje?” Neema alipochelewa kujibu, Proper alijitia kushituka tena, “Lakini wewe ni nani? Na ulitaka mimi niseme nini kuhusu Joram au unataka mawazo gani kutoka kwangu?”.

Neema alijiona mjinga zaidi. Huyu msomi wa watu alionekana hajui lolote. Yawezekana yule mwanamke wa ajabu, Unono, alikuwa punguani pia. Picha ya mzee huyu pengine aliiokota au kuiiba mahala na kuileta kwake. Mzee huyu hakuonekana kujua chochote cha muhimu juu ya kifo cha Joram.

Haraka Neema akainuka na kuaga.

|Haraka hii? Proper alihoji kwa mshangao. Safari hii alionyesha mshagao halisi. Alikuwa akitafuta nafasi nzuri ya kumtia Neema mikononi mwake. Japokuwa kiti alichokalia Neema kingeweza kutimiza wajibu wake lakini Proper hakukusudia kutumia njia hii. Na njia hii ilikuwa rahisi zaidi. Proper angeweza kukanyaga mahala fulani chini ya meza kisha voti kadhaa za umeme zingepita katika kiti hicho na kumwua Neema papo hapo. Hakufanya hivyo kwa sababu mbili. Mosi, alikuwa bado hajafahamu msichana huyu anajua nini na anataka nini kwake, na pia hakutaka Neema afie nyumbani kwake.

“Huwezi kuondoka bila kunywa chochote? Siwezi kuruhusu binti mzuri kama wewe atoke nyumbani kwangu pasi ya kuonja chochote, Vilevile hatujazungumza”.

“Samahani. Sijisikii kunywa chochote”.

“Na uichotaka kuuliza juu ya Joram?”.

“Nimebadili mawazo”.

“Kwanini?”.

Huku akianza kutoka ndani ya nyumba hii Neema alisema, “Nilikosea…”.

Hakujua kilichompiga. Hakusikia maumivu yoyote. Alijikuta akianguka polepole huku Profesa Chain akimtazama kwa kicheko cha kebehi. Hakuwa na uwezo wsa kupiga kelele japo alijaribu, akahisi fahamu zikimtoka taratibu.

Neema aliposhutuka kutoka katika usingizi mzito, alijikuta amelala kitandani akiwa uchi, kando Proper alikuwa amemkumbatia kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukizichezea chuchu zake. Lakini pia ulimi wa Proper ulikuwa katika kinywa cha Neema. Neema alishituka na kujivuta kando kwa nguvu huku akitamka maneno ambayo hayakusikika kikamilifu. Hata hivyo hakufaulu kujitoa katika mikono yenye nguvu ya Proper ambayo ilizidi kumbana.

“Bado kidogo mpenzi”, Proper alisema, “Tutafanya mara moja zaidi kisha nitakuruhusu utakwenda zako”, Sauti ilifuatiwa na kicheko ambacho katika masikio ya Neema kilijaa jeuri na kebehi.

“Nini kinatokea hapa?” Neema alifanikiwa kuuliza swali, huku mshangao ukimtoka na aibu ikianza kumwingia.

“Tunafanya mapenzi, ndio maana nikasema bado kidogo halafu nikuruhusu uondoke zako”, Proper alimjibu Neema.

“Mapenzi!” Neema alihoji huku akifoka. “Nitakushitaki”, Neema alifanikiwa kumwambia Proper.

“Kwa nani?”.

“Umeninajisi. Umenitenda pasi hiari yangu. Siwezi kuvumilia upuuzi huu, nitahakikisha unafika kwenye vyombo vya sheria”, Neema alisisitiza.

Kicheko kingine kikamtoka Proper. “Usiwe kama mtoto mdogo”, alisema Proper akiendelea kucheka, “Nani atakuelewa? Zaidi, nani atakuamini? Ulivyo mrembo kila mmoja ataamini kuwa unatosha kabisa kumfanya Profesa yeyote mwenye hisia asahau majukumu yake kwa muda ili afanye mapenzi na wewe. Nani atakanusha nikisema kuwa jana tulikutana mitaani tukaahidiana uje leo na umekuja? Au kuna yeyote aliyeniona nikikuvuta huko nje na kukuleta hapa ndani?”

Maneno hayo yalimwingia Neema. Hakuona uwezekano wowote wa kuifanya hatia ya mtu huyu idhihirike . Lakini alikuwa na hofu moyoni. Si hofu ya kufanya mapenzi bila kukusudia. Hofu yake ilitokana na kutofahamu kitu gani kilimfanya apoteze fahamu na kuvuliwa mavazi na … Pia hofu ilimzidi kwa kutokuwa na hakika na yote yaliyofanyika baada ya kupoteza fahamu. Ilikuwa kama ndoto ya kitambo anayokumbuka kwa shida. Ilikuwa kana kwamba ananusa harufu iliyomfanya apoteze fahamu. Pia, alikumbuka kuwa alimsikia mtu huyo alipokuwa akimhoji kuhusu kifo cha Joram Kiango, naye akiropoka kila kitu alichofahamu. Alimweleza juu ya yule mwanamke mwenye sura mbaya ambaye aliileta picha yake. Kisha alikumbuka kuwa alinyweshwa kitu fulani na kuambiwa, “Hiyo itakufanya usafiri leo hadi aliko mpenzi wako Joram. Usisahau kumsalimu. Baada ya hapo ndipo nguo zilipovuliwa. Akaletwa kitandani ambako…

“Pamoja na kufanya mapenzi”, Profesa Kimara, au Proper alikuwa akiendelea, “Nitakulipa vema, Sina mkono wa birika , hususan kwa mabinti awzuri kama wewe. Umenifanya nimsahau mke wangu aliyefariki miaka kumi iliyopita”. Alisema huku akiushughulisha mkono wake kutambaa kutoka katika matiti ya Neema hadi tumboni mwake, mkono huo ukateleza hadi katikati ya miguu ya Neema.

Neema akausukuma mkono huo kando na kujiinua kwa nguvu. “Sijapata kumwona mtu mshenzi kama wewe”, alifoka kwa hasira akiyaendea mavazi yake yaliyokuwa juu ya kochi.

“Kwanini mpenzi? Nipe nafasi nyingine uone jinsi nilivyo mstaarabu katika suala zima la mapenzi. Tafadhali. Mara moja tu halafu utakwenda zako…”.

Sauti ilikuwa ya mapenzi. Ni tabasamu lake ambalo lilibeba kitu kingine kabisa. Kitu kisicho karibu na mapenzi hata kidogo. Kitu ambacho kilikuwa kinyume kabisa na mapenzi na mahaba. Jambo ambalo lilimuongezea hasira Neema. Alizivaa nguo zake haraka haraka, Akautwaa mfuko wake na kuanza kutoka.

“Siku yoyote ukijisikia tena kufanya mapenzi unakaribishwa”. Proper alisema huku akifungua pochi lake na kutoa kiasi cha pesa.

“Sihitaji chochote kutoka kwako”, Neema alifoka huku akitoka.

Alipofika kituo cha basi alifungua mkoba wake kuangalia. Kila kitu kilikuwa sawa isipokuwa bastola yake! Hakujua cha kufanya.

Alipofika nyumbani, Neema aliketi juu ya sofa akajaribu kufikiri, mara akahisi hana nguvu za kufikiri lolote. Alichokitaraji ni pumziko tu. Mara akausikia usingizi mzito ukimnyemelea. Kitanda alikiona mbali. Akajinyoosha juu ya kochi usingizi mzito ukamchukua.

Ulikuwa usingizi wa aina yake. Ulimchukua moja kwa moja na kumtoa katika dunia hii na kumpeleka katika dunia nyingine. Dunia yenye kiza kizito. Dunia isiyo na hisia.

Unono alipoingia alimkuta Neema katika usingizi huo. Awali hakufahamu kinachotokea. Akapoteza dakika kadhaa akilihusudu kwa wivu umbo zuri la Neema ambalo lililala kifudifudi juu ya kochi. Kisha akapoteza dakika zingine kadhaa akijaribu kumwamusha kwa kumsukuma. Mara akaiona damu nzito iliyokuwa ikimtoka Neema midomoni na puani, Ulimi ulivyoponyoka kutoka kinywani na kuduwaa nje, upande mmoja. Akayaona macho yalivyotoka nje. Kila kitu kilitangaza mauti ya Neema.

“Amekufa”, Unono alifoka huku akiruka kurudi nyuma.

Kifo. Unono alikifahamu sana. Alikifahamu sana toka wazazi wake wote wawili walipokufa kwa ajali ya gari wakati huo akiwa na umri wa miaka mitano tu. Alikifahamu kifo miaka minne baadaye wakati shangazi yake aliyekuwa mlezi wake wa pekee, alipofariki kwa kipindupindu. Naam, alikifahamu kifo na madhara yake. Lakini hakupata kuwa karibu na kifo kiasi hiki. Hakuwahi kumugusa mtu aliyekata roho na kumsukasuka. Hivyo, alipouondoa mkono wake juu ya mwili wa Neema, aligeuka na kuanza kutoka nje mbio, huku akipiga kelele.

Hakwenda mbali kabla ya kutokea gari yenye dereva mwenye haraka zake, ambayo ilimgonga Unono na kumwua pale pale.

Watu walioshuhudia ajali hiyo, hasa baada ya kumuona alivyokuwa akikimbia hovyo barabarani, na kumuona alivyokuwa, waliamini mara moja kuwa alikuwa ‘Mwendawazimu mmoja’ amegongwa na gari na kufa.

                    ******************************

Miongoni mwa watu walioshuhudia ajali hii ni Proper. Kama watu wengine yeye pia ajali hii ilimsikitisha. Tofauti ni kwamba yeye hakusikitika kwa kuona maisha ya binadamu yakiteketea ghafla katika hali ya kutisha kama hiyo, la. Kwanza hakuna jambo lolote lililomsisimua katika maisha yake zaidi ya kumuona mtu akikata roho. Hakuna mchezo alioupenda au kuujua zaidi ya kuua ama kushuhudia kifo.

Proper alisikitika kukosa fursa na kuzungumza na Unono ili kujua yote anayofahamu juu yake na wapi alikopata picha ambayo Neema aliizungumzia wakati alipomhoji baada ya kumlewesha kwa dawa zake. Aliamua kummalizia Neema, baada ya kuona kuwa hakujua lolote lingine la haja. Ndiyo akamnywesha sumu ile maalumu ambayo ilikusudiwa kumuua Neema kwa utulivu, baada ya muda fulani. Kisha alimfuata kwa hila hadi hapa ambapo alijificha katika uchochoro akimsubiri Unono. Alifanikiwa kumwona wakati anaingia ndani na alivyotoka mbio. Kabla hajaanza kumfuata, ilitokea gari na kumgonga kwa bahati mbaya.

Proper alifanikiwa kujisokomeza katikati ya umati wa watu waliojaa hapo barabarani. Akiwa kajibadili kimavazi na kitabia, hakuwa yule profesa Kimara tena, bali mmoja wa watu kadhaa wa mkitaani na hakuna yeyote ambaye angeweza kumshuku. Hivyo hakuna aliyemwona akiinama na kuokota mkoba wa marehemu na kwenda kando ambako aliufungua na kupekuwa ndani. Ndani ya mkoba huo hakukuwa na chochote alichohitaji. Aliutupa mkoba huo chini na kupishana na watu waliokuwa wakielekea kwenye tukio hilo la ajali, akaelekea nyumbani kwa Neema.

Hakuna aliyemwona akiingia. Alisimama kando ya kitanda akitabasamu kwa ‘uzuri’ wa kazi yake. Neema alikuwa amekufa kwa namna aliyotaka. Yeyote ambaye angeingia na kumtazama haraka haraka angedhani yuko usingizini. Hata hivyo Proper hakuridhika kikamilifu. Akambeba na kumlaza juu ya kitanda na kumfunika kwa shuka hadi usoni. Kisha akafanya msako wa haraka haraka. Alikuwa akiitafuta ile picha aliyosema Neema. Hakuiona. Akalazimika kuondoka

Mlangoni alikutana na jirani mmoja wa Neema ambaye alimtazama kwa macho ya kuuliza japo hakuuliza chochote.

“Nilikuwa mgeni wa huyu dada lakini naona amelala”, Proper alieleza.

“Amelala?” jirani huyo alihoji akijaribu kuchungulia ndani. alipoona mwili wa Neema umetulia kitandani aliamini. “Naona tumwache alale. Shoga yetu lapatwa na msiba mkubwa”.

Akiufahamu umbeya wa wanawake wa Dar es Salaam, Proper hakusubiri kumsikiliza. Alifanya haraka kurejea nyumbani kwake ambako aliendelea kuandaa mpango wake. Kisha akaipitia tena taarifa yake ambayo alikwisha iandaa kwa ajili ya kuipeperusha nje. Aliirekebisha taarifa hiyo hapa na pale, kisha akavuta mtambo wake wa kupeperusha habari na kuufungua. Kisha aliufunga na kusubiri muda wa majibu. Aliyahofia majibu hayo lakini hakujali. Maadamu alikuwa kadhamiria. Lolote lisingemfanya ashindwe kuutekeleza.

Kidogo hofu ilikuwa ikimwingia kwa kufikiri wapi yule marehemu aliyegongwa na gari aliipata picha yake na vipi picha hiyo isipatikane ingawa alikuwa ameitafuta kwa umakini. Kuna jambo la kutisha linamnyemelea? Wapi? alijiuliza.

Hakuna vipi angeweza kuacha mwanya wa kupatikana kwa urahisi. Mambo mengi ama yote aliyotaka yafanyike kikamilifu alikuwa akiyafanya mwenyewe, japo alikuwa na watu wengi chini yake ambao wanalipwa vyema na wamekamilika kimauaji. Wote hao yeye anawafahamu lakini hakuna yeyote anayemfahamu. Yeyote anayedhani kuwa anamfahamu basi alikuwa akijidanganya kwani Proper unayeongea naye leo si Proper wa kesho. Kadhalika vifo vyote vilivyotokea alivitekeleza mwenyewe kiufundi zaidi ya alivyofundishwa. Alimuua Waridi kikatili, ili polisi waamini kuwa ni mwendawazimu mwingine ambaye anaipenda sana kazi ya kuua watu wasiokuwa na hatia. Joram amekufa kwa bomu, Neema alikuwa msiri wa Joram! Yeyote aliyemuua Joram asingesita kumuua Neema. Zaidi, Neema kafa kwa sumu ile ile iliyokusudiwa kumuua Joram. Katika hali kama hiyo, nani angefanya nini kumtia hatiani kwa urahisi? Polisi? Wao wasingeenda mbali na ukweli. Joram aliyekuwa na uwezo wa kunusa chochote sasa yuko kuzimu.

Hata hivyo Proper alihisi kama uovu fulani uliojificha kando ukimnyemelea. Kama angeipata ile picha… Kama yule mwanamke asingepatwa na ajali… angeweza kujisikia salama zaidi. Aliifukuza hofu kwa kujiliza kwa moja ya sigara zake kali, ambazo huzivuta kwa nadra sana. Kisha akaitazama saa yake. Alipoona imepungua dakika moja ili kupata majibu yataarifa yake, aliubonyeza mtambo wake. Karatasi yenye maandishi ikajitokeza. Akaichukua na kuanza kuisoma.

…Utapewa majibu rasmi kesho muda kama huu… taarifa hiyo ilieleza, akaisoma tena kisha akaichana, mabaki akayatia katika mtambo mwingine wa kusaga karatasi hata ikawa kama majivu.

Hakujua jibu rasmi litakuwa lipi na lilimhusu vipi. Alichotuma yeye halikuwa swali wala ombi. Ilikuwa taarifa ambayo watake wasitake ingefanyika. “Wapuuzi”, aliwaza. Akawatoa akilini na kuanza kuandaa mkutano mwingine baina yake na washirika wake. Washirika ambao kiasi fulani hawakuwa zaidi ya mateka wake.

Mkutano huo wa siri ulifanyika chini ya Uenyekiti wa Proper. Bado alifanya mpango wake kuwa siri, alijificha nyuma ya taa kali za umeme kwa namna ambayo iliwafanya washirika wake wasimuone vizuri japokuwa walikuwa na matarajio ya kazi.

Mkutano huu kama ulivyokuwa wa awali, ulikuwa umeitishwa kwa namna ya hadhari na siri, jambo ambalo liliwaongezea mashaka baadhi ya wajumbe. Kila mmoja alijikuta akiwa mkutanoni bila kutarajia wala hiari.

Huyo alikuwa akipita zake mitaani, kaiacha pale gari na dereva wake. Mara kashikwa mkono na mtu aliyekuwa akipita ghafla. Alipoutazama mkono wake aliona kadi ndogo yenye maandishi yasemayo ‘BAADA YA NUSU SAA… NJOO PALE KWA SIRI… ONYESHA KADI HII MLANGONI’. Akijua maana ya kadi hiyo, mtu huyo alimruhusu dereva wake kuondoka. Kisha akatembea kuelekea nyumba hiyo ambayo nje ilionekana kuwa nyumba ya kawaida lakini kwa ndani ilikuwa nyumba ya aina yake. Mlangoni kila aliyetoa kadi aliruhusiwa kuingia katika chumba ambacho kilikuwa na lifti iliyowasafirisha kwenda chini ambako walipitishwa vyumba kadhaa hadi kwenye chumba cha mkutano.

Mwingine alikuwa kastarehe na mkewe nyumbani kwake. Alipoinuka kwenda maliwatoni aliuona mkono wa mtu ukiingia kupitia dirishani ukiwa umeshika kadi iliyosomeka. ‘BAADA YA NUSU SAA… Aliipokea na kumuaga mkewe haraka kuwa anarudi kazini. Lakini nje aligeuza safari na kuelekea kwenye kikao cha Proper. Mwingine alikuwa kazini. Simu ilipigwa ghafla ikimwarifu kuwa ana mgeni alimsubiri kwenye mghahawa mtaa wa pili. ‘Mgeni’ huyo alimkabidhi kadi yake iliyomtaka kufika haraka kwenye kikao, ambapo sasa wajumbe wote walikuwa wamefika wakimsubiri Mwenyekiti afungue mkutano.

“Tungeanza kwa kukumbushana kuwa Joram ambaye tulimuona kama tishio kwetu sasa ni marehemu. Yuko kuzimu. Hiyo ni habari njema. Au?”, alihoji.

“Nadhani ni habari njema”, mmoja wa wajumbe alijibu, “Igawa kifo chake hakikuwa kizuri sana . Watu wanashuku kuwa pengine alipewa sumu. Nadhani bado wanaendelea na uchunguzi wa kifo chake”.

“Wanajisumbua, hakuna watakalogundua kuhusu kifo cha Joram”, Mwenyekiti aliwajibu. Kisha alicheka kidogo na kusema, “Pia napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha kuwa Joram hakufa kwa sumu. Walipanga hila ili watulaghai tu baada ya kunusurika kwake. Nililazimika kumteketeza kwa bomu”.

Hii ilikuwa taarifa ngeni kwa wajumbe. “Si lazima watazidisha mashaka? Nazungumzia polisi. Walipoona amepona kufa kwa sumu na hatimaye kuuawa kwa bomu nadhani watakuwa macho sana, wakipeleleza kwa makini zaidi hadi…” akasita kidogo baada ya kuona ameongea muda mrefu zaidi ya anavyotakiwa kuongea.

“Hadi nini?”, Mwenyekiti alihoji. “Hakuna lolote watakalogundua. Watakuwa wakibabaika tu kama mfamaji asiye na msaada wowote. Hawatafahamu iwapo ubaya utatoka mashariki au magharibi. Hawatajua ni kitu gani kinatokea. Watakapofahamu, mambo yatakuwa yamekamilika. Watakachofanya ni kuteremsha bendera zote nusu mlingoti na kuanza maomboleza ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya dunia.

Wajumbe waliduwaa. Mioyo yao ikadunda kwa hofu. Ingawaje walikuwepo mkutanoni kama washiriki kamili katika njama hii, lakini hawakuelewa barabara kilichokusudiwa. Tamaa ya pesa nyingi zaidi, madaraka makubwa zaidi, ndio sababu zilizowafanya wakubali kushiriki katika mkutano huo wa siri. Lakini hayo hayakuwafanya watokwe na mashaka. Hawakujua kama mambo yalikuwa heri kama alivyodai Mwenyekiti wao au shari kama miayo yao ilivyokuwa ikinong’ona. Hasa mashaka hayo yalitokana na kuteuliwa kwao. Hakuna mjumbe aliyefahamu wajibu wake. Hakuna aliyekuwa na fununu sababu ya kuteuliwa kuhusika katika mkutano huo. Ni kweli kwamba wajumbe hao walikuwa watu wenye nafasi nyeti katika chama na serikali. Ni kweli pia wote walikuwa pamoja kwa nafsi zao: wote wangependa cheo zaidi na pesa. Lakini umoja huo haukuwafanya washindwe kujiuliza vipi mtu huyu anayejificha nyuma ya mwanga, mbele yao aliwezaje kuisoma mioyo yao, hata akawateua katika jumuia hii. Vipi aliweza, japo katika nchi na ulimwengu mzima? Watu wenye njaa kama zao ni wengi mno, endapo si wengi. Sheria na katiba zisingekuwepo, kulinda haki na usawa, ingethihirika ni jinsi gani wengi walivyo na tamaa ya madaraka na kiu ya kupata pesa.

Ingawa kuna sheria zinazotisha, pamoja na katiba zinazoadili, wengi huzikiuka kwa siri na kulinda nafasi ya kufanya mengi kinyume cha mwelekeo. Wako wachache walio ‘jaaliwa’ wakafaulu kufanya mengi kwa siri wakati wao ndio wanaongoza kulinda katiba na sheria za nchi. Baadhi ya watu hao ni hawa ambao sasa hivi walikuwa mbele ya Proper wakimsikiliza kwa hofu. Walikuwa na mengi ambayo waliamini ni siri zao binafsi, ambayo hawakupenda jamii ifahamu. Hata hivyo tamaa yao haikuwa kubwa kiasi cha kuwafanya wafurahie jambo la kutisha wasilolifahamu eti kwa ahadi ya pesa na vyeo zaidi.

“Unakusudia kufanya nini?”, mmoja wa wajumbe alifoka ghafla.

“Ndiyo… Tufahamishe ni jambo gani unataka kufanya?”, mwingine alidakia na kuuliza.

Proper kama mtu aliyekuwa akiyasoma mawazo yao kitambo, alicheka kidogo, kisha akawaambia. “Sikilizeni. Kazi iliyo mbele yenu ni ndogo kuliko kazi zote mlizowahi kufanya… Hamna haja ya kuwa na hofu yoyote”.

Alipoona wametulia kumsikiliza aliendelea, “Nimepata fununu kuwa hivi karibuni utafanyika mkutano wa viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaojiita wenye msimamo wa kimapinduzi wamealikwa pia. Nitakachohitaji kwenu ni ratiba kamili ya mkutano huo, wapi kiongozi fulani analala, wapi anakula, jumba lipi wanakutana na kadhalika. Nataka taarifa kamili, ya siri, si ile ambayo hutangazwa katika magazeti yanayouzwa mitaani. Kulingana na nafasi zenu najua kazi hiyo ni ndogo mno. Kitakachofauata niachieni mimi.

“Nini kitafuata?”, mjumbe mmoja aliropoka kwa shauku.

“Mara ngapi nimewaambia kuwa bendera kadhaa zitapepea nusu mlingoti kwa siku kadhaa katika nchi kadhaa wa kadha?. Nataka kufanya jambo fulani ambalo halijawahi kutokea sasa kifanyike. Kitu ambacho bado hakijafikirika. Kitu ambacho historia haitakisahau. Kwa muda mrefu amekufa kiogozi mmoja. Safari hii nataka kuona viogozi wengi wamekufa wote kwa wakati mmoja. Tena nitafarijika kama watakufa pamoja katika viti na meza zao. Huenda wataanguka mmoja baada ya mwingine, wakati wakiagana. Ama kweli litakuwa jambo la kusisimua sana…”

“Kusisimua!” Mmoja wa wajumbe aliropoka na kufoka baada ya kupatwa na mshangao. “”Kusisimua!”, alirudia tena, “Sikuwa na hakika. Sasa nimeamini kuwa una wazimu. Hata hivyo, wazimu wako unakudanyanya sana kukutuma udhani kuwa mimi naweza kushiriki kuinua mikono yangu katika kuwaangamiza watu ambao licha ya kwamba, hawana hatia, wanajitesa kutwa kucha kuwasaidia wanyonge wanaonyimwa haki zao?”.

Mjumbe huyo ambaye sasa alikuwa amesimama wima, akitetemeka kwa hasira huku akitokwa na jasho aliwatazama wajumbe wenzake. Alipoona wote wana dalili ya kumuunga mkono aliongeza. “Huna budi kulionea aibu wazo lako la kipumbavu…”

“Keti”, Proper alimwamru. “Hujui unalosema. Maneno yako yamejaa ndoto au nyimbo ambazo hao unaowaita viongozi, sijui watetezi wa wanyonge gani, wamekuwa wakizijaza katika vichwa vyenu. Nani anayemtetea nani katika dunia hii? Mnyonge hujitetea mwenyewe. wale wanachofanya ni kutetea matumbo yao. maisha na vyeo vyao tu kwa visingizio vingi. Wamehitimu katika taaluma ya kusema maneno mazuri na kutoa ahadi tamu katika masikio ya wanyonge kiasi cha kuwafanya waonekane kama miungu ambayo wanadamu wanaitegemea!”,

“Hata hivyo”, mjumbe huyo alidakia, “Siwezi kushiriki upumbavu kuangamiza damu za watu wasiokuwa na hatia”.

“Bado hujajua usemalo”, Proper alimjibu kwa mara nyingine. “Naweza kuwa mwema kukukaribisha katika mpango huu ambao utasaidia kuyabadili maisha yenu kuwa ya heti na utajiri mkubwa. Lakini siwezi kuwa mpole kiasi hicho kiasi cha kuacha mpango huu ambao nimeuandaa kwa miaka mingi uharibike kwa ajili ya woga na ujinga wa yeyote kati yenu. Nadhani sasa nimeeleweka?”.

Proper akanyamaza kidogo ili kutoa nafasi kwa wajumbe waweze kuyatafakari maneno yake.

Ulikuwa ujumbe wa kutisha kwa wajumbe walioshiriki mkutano huo, Kilichofuata yalikuwa maafa na ukatili mkubwa kwao au yeyote ambaye angethubutu kukanusha au kutoa siri hii. Ukweli huo uliwatia hofu wajumbe hata wakatazamana kwa dalili ya kukata tamaa ya maisha.

Kama anayesoma mawazo yao. Proper akarudia kuongea kwa sauti ile ile ambayo japokuwa haikuwa kali, wala yenye hasira, lakini sauti hiyo iliubeba ujumbe kamili, alieleza jinsi alivyodhamilia kutenda yote aliyosema. “Najua kwamba majalada yenu kazini hayaonyeshi doa lolote, Na raia wengi nchini wanayo picha nzuri juu yenu. Picha iliyowawezesha mkachaguliwa kushika nyadhifa katika sehemu mbali mvali muhimu za uongozi. Lakini kuna upande wa pili wa picha hizo. Upande wenye kila aina ya uovu, ukatili, na kukiuka taratibu za nchi. Nyie mnadhani upande huo wa pili ni siri zenu binafsi ambazo hakuna anayefahamu. Kwa bahati mbaya au nzuri, mimi nafahamu kila jambo. Namfahamu kila mmoja wenu vilivyo. Pia ninao ushahidi mzuri ambao ukiwekwa hadharani utayafanya majina yenu yanuke kama takataka”.

Wajumbe walianza kuchanganyikiwa. Ndio kwanza wakaifahamu ‘bahati’ iliyowafanya wateuliwe kushiriki katika kundi hili. Proper alikuwa amewateua baada ya kuwapeleleza kwa muda mrefu na kuwaweka katika kona moja ambayo ilikuwa vigumu kujitoa. Wakaanza kutapatapa, kila akijiuliza ni vitendo vingapi alivyofanya kwa siri na vimefahamika.

Kuna yule ambaye kabla hajateuliwa kuwa mbunge alikuwa mfanya biashara mkubwa wa magendo ya madini na bangi alivyosafirisha kwenda nje ya nchi. Hadi sasa biashara hiyo hajaiacha kwani uchumi wake unategemea biashara hii. Biashara hii imemfanya ajenge jumba la kifahari huko Ughaibuni na kufungua kiwanda hapa nchini akitumia majina ya mtu mwingine. Haya kumbe yanafahamika.

Mwingine ni yule ambaye huuza siri za nchi kwa mashirika ya kijasusi huko nje ya nchi. Wao humlipa pesa nyingi sana pia wamemwahidi hifadhi ya kisiasa endapo lolote lingemtokea. Mambo haya yakifanyika kwa siri sana, hakujua kabisa kama yangeweza kufahamika. Kumbe…

Na kuna huyu ambaye aliyeshiriki katika kuandaa kifo cha mgombea mwenza katika uchaguzi wao. Kadhalika alikuwa, kiungo muhimu katika kufanikisha kifo cha kiongozi shupavu ambaye alionekana kuwa kauawa na majahili wa nje. Kitendo ambacho kilimpatia pesa za kutosha. Kama yote hayo yanajulikana!… Kama kuna ushahidi!…

Kila mjumbe alijikuta katika nafasi ngumu mno kwa maisha yake ya baadaye. Baada ya kutazamana tena, na kila mmoja kuona hofu katika macho ya mwenzake, waliyarejesha macho yao kwa Proper kwa namna iliyosihi. Kukiwa hakuna jambo ambalo alihitaji zaidi ya hilo, Proper aliongeza.

“Labda yupo ambaye haogopi aibu. Ambaye yuko tayari nitoe ushahidi huo, Au kama kuna mwingine anabuni mbinu ya kutoroka akajifiche mbali. Ndoto za aina hiyo ningeshauri, mziondoe akilini. Ingawa sioni fahari kusema haya lakini sina budi kukufahamisheni kuwa hatua tuliyofikia katika suala hili ni ndefu mno. Hivyo yeyote atakayekiuka kwa njia yoyote afahamu kuwa hatafika mbali. Kifo kitakuwa kando kikimsubiri. Wala hatajua kapigwa na kitu gani?. Atakayenusurika ni yule mwenye uwezo wa kutoroka bila roho yake tu”.

Hofu ilizidi kutawala mioyo ya wajumbe hao. Tamaa na matumaini yao yote ya utajiri zaidi na vyeo ikaanza kudidimia. Walio waoga walijiona kama ambao tayari wako safarini kuelekea kuzimu. Mashujaa kiasi waliduaa tu. Wale ambao wana mioyo migumu zaidi walimtazama. “Kwame”, kwa namna ya kupima uwezo wa kifo chake yeye kabla na baada yao.

Kama anaesoma mawazo yao Proper alisema. “Naona wapo wanaodhani kuwa nastahili kufa”, akacheka kidogo, “Hilo ni wazo la kipuuzi kuliko yote. Mimi ni mtu ambaye hafi kwa urahisi. Na kabla hujaniua utakuwa umefufa wewe, bila kujua kitu gani kimekupiga”. Akacheka tena kabla ya kuongeza, “Pamoja na hayo ndugu zangu mawazo yote ya nini? Maelezo yangu niliyokupeni hayakuwa ya kuwatisha isipokuwa kuwaonyesha hali halisi ilivyo. Nina hakika hakuna baya lolote litakalotokea kusababisha hali hiyo. Bado nawaomba tusiogopane. Tuwe marafiki na tutimize wajibu wetu vyema. Tusisahau kuwa mpango huu una utajiri ambao wengi wenu hamjawahi kuugusa na vyeo ambavyo msingeweza kuvikalia”.

“Wala msihofu kuwa utawala wenu utakuwa wa kidikteta hata muwe kama maadui wa wananchi wenyewe. Mbinu zitafanyika mara tu baada ya vifo vya wakubwa wachache, ili majina yenu yazibe mapengo hayo. Sifa zenu zitaimbwa redioni na kutangazwa magazetini, vikao vyote vya chama havitauona ubovu wenu, hata raia watawapenda na kuwategemea. Mmoja wenu atakuwa Rais. Ni kazi ndogo sana, mradi kila mmoja atimize jukumu lake dogo lililoko mbele yake”.

Ingawa sauti ya Proper ilikuwa inasema ukweli, wajumbe waliona kama anawadhihaki.

Kutoka hapo Proper aliharakisha kukiendea chumba ambacho kilikuwa na mtambo wake wa kupeperushia habari. Alipofika, alitazama saa yake na kusubiri dakika kadhaa, kisha alibonyeza hapa na pale. Mara ikatoka karatasi iliokuwa na maandishi yaliyosema:

Ua limechanua bustanini lafaa kuchumwa.

Proper alielewa maana ya ujumbe huo. Ilikuwa lugha ya siri ambayo ilikuwa ikimfahamisha kuwa kulikuwa na mzigo wake mahali pao pa siri.

Mahali hapo ni katika chumba chake cha pili katika nyumba yake nyingine, mtaa fulani. Katika kona moja ya chumba hicho, lipo kasha la takataka ambalo haliwezi kuvutia macho. Humo huwekwa ujumbe wa hatari zaidi ama silaha, madawa ya kulevya na kadhalika. Yote yake ambayo viongozi wake wa nje huofia kupeperushwa katika mtambo wao kwa hofu ya kunaswa katika mitambo ya adui, huletwa hapa, nae kuarifiwa.

Lililomtoa jasho Proper ni kutokumjua mtu huyo ambaye makao makuu walikuwa wakimtumia kuleta habari hizo. Kwa mjibu wa madaraka yake, ni yeye aliyekuwa mkuu wa mambo yote ya kijasusi katika kanda hii. Watu wote walikuwa chini yake. Wala hakufahamu wakati gani anafanya shughuli zake. Proper alikuwa na shauku kubwa ya kufahamu. Aliwahi kukiuka utaratibu na kuanza kuendesha upelelezi ili amfahamu. Lakini alishangaa alipopewa onyo kali kutoka makao makuu kwa kitendo hicho ikamlazimu kutii, ingawa kwa shingo upande.

Kwa hivyo, alipokuwa akiendea ujumbe huo, alikuwa mtu mwenye mashaka hasa alipozigatia kuwa ujumbe alituma haukuhitaji jibu refu zaidi ya ‘Ndiyo’ alipofika chumbani humo katika sura ya jina tofauti alijifungia na kuliendea kasha hilo. Alipekuwa taka chache za karatasi kabla hajaifikia bahasha pana ambayo iliandikwa herufi moja tu juu ‘P’ akaitatua kwa uangalifu akashangazwa na harufu tamu ya poda au manukato ambayo iltoka katika bahasha hiyo. Kwa jinsi alivyokuwa na haraka ya kufahamu jibu la pendekezo lake, hakusita kujiuliza maana na dhamila ya harufu hiyo tamu, Alichofanya ni kuanza kuisoma.

Agenti 034/X/P

Tumepokea taarifa yako na kuipitia kwa makini. Tumeshangazwa sana na wazo lako la kinyama. Inaonyesha hujui kwanini uko hapo. Tumekuweka hapo si kwa ajili ya kutenda ukatili wa kujifurahisha bali katika kulinda maslahi yetu kiuchumi na kisiasa.

Wazo lako ni hatari sana kwani linakusudia kumwaga damu nyingi kuliko inavyostahili, jambo ambalo litafanya, kati ya unaokusudia kuwateketeza hujui kama tunao watu wetu tunaowategemea ingawa hadharani tunawaruhusu wajifanye kama wanatulaumu, kutulaani. Kuondoka kwao madarakani kuna hatari ya kuja watu ambao pengine tutashindwa kuwamiliki. Kwa muda mrefu tumevumilia vitendo vyako ambavyo haviambatani na wajibu wako. Umekuwa ukiutumia wadhifa tuliokupa kuufariji moyo wako wenye kiu ya kumwaga damu. Safari hii umevuka kiwango. Ofisi hii imeshindwa kustahamili zaidi. Pamoja na kukuonya uondoe ndoto za kipuuzi kama hizo, tunakutaka uichukulie barua hii kama taarifa ya kukupokonya madaraka yote uliyokuwa nayo. Kuanzaia sasa. Uko huru…”

Proper alipofikia hapo, aliruka kando ghafla akageuka nyuma yake akitazama kila upande, bastola yake ikiwa mkononi tayari kwa lolote. Hakuona chochote alikuwa peke yake chumbani hakuamini. Akaanza msako wa kuchunguza hapa na pale, bastola ikimtangulia. Ingawa hakuona mtu wala kitu lakini hofu ilimpanda. Ajuavyo yeye, barua hiyo ya kumnyanganya wadhifa ilikuwa pia ikiashiria hukumu ya kifo. Akiwa mtu ajuaye mengi ya hatari asingeweza kuruhusiwa kuwa ‘huru’ kwa urahisi kiasi hicho. Alichoamini yeye ni kuwa yeyote aliyeleta barua hiyo pia alikuwa na jukumu la kumuua. Wala asingemruhusu kuishi kwa muda wa dakika nyingi baada ya kupokea taarifa hiyo. Lakini mboba yuko peke yake? Nani ambaye angemuua na lini? alijiliulza huku akiendelea na uchunguzi wake kwa hadhari kubwa!

Haikuwepo dalili yoyote ya uovu.

Hakuona dalili yoyote ya hatari.

Mara alijiona akiwa mzito zaidi kuliko kawaida. Kichwa chake pia kilimuelemea ghafla na macho yake yakashindwa kuendelea kutimiza wajibu. Aliyaskikia maungo yake yote yakianza kulainika. Aliona kana kwamba angeanguka sakafuni. Ndipo alipoelewa mwisho wake ulivyopangwa. Ile harufu tamu aliyoinusa katika bahasha aliyokuwa nayo mkononi haikukusudiwa kumburudisha. Ilikuwa sumu kali yenye jukumu la kumuua. Sumu ambayo ilikuwa ikitimiza wajibu wake. Akasonya kwa kutowaza hilo toka awali. Proper angekubali kufa kwa mkono wa mwanaume mwenzake. Hilo, hakulitazamia na asingeruhusu litendeke Proper Mbezi na mwenye kiburi kikubwa. Alijikongoja kuitafuta bastola yake. Akakielekeza kifuani tayari kuifyatua. Kisha alikumbuka kuwa sumu iliyokuwa ikikaribia kumuua haikuwa ngeni kwake. Alikuwa ameisoma katika vitabu vya kemia vya kijasusi na kuifahamu kuwa ilikuwa imegunduliwa siku chache zilizopita. Sumu hii iliitwa Crycine, na ingeweza kumua mwanadamu kwa dakika chache sana. Hata hivyo, alikumbua pia kuwa, Dawa pekee ya sumu hiyo ni maji. Aliirejesha bastola yake kibindoni akajikongoja haraka kuelekea bafuni. Ambako alijaza maji kwenye beseni na kujitumbukiza ndani yake. Akahakikisha pia maji mengi yanaingia tumboni mwake. Baada ya muda, alijisikia akirudiwa na uwezo wake kimmwili na kifikra. Akajipoa kutoka majini na kuvaa mavazi yake.

Hasira kali zilikuwa zimemjaa kichwani mwake. Hasira dhidhi ya yule aliyepitisha uamzi wa kumuangamiza. Na hasa dhidi ya huyu aliyepokea amri ya kumuua bila kukumbuka ni nani kakusudiwa kuangamizwa. Alikumbuka mchango wake kwa shirika hili la ujasusi ambalo lilimtuma hapa nchini. Mchango ambao kila mara huhatarisha maisha yake. Akaona kuwa alistahili kupata medali na si kifo.

Proper si mtu wa kustahamili uovu kama huo. Aliamua kulipa kisasi. Na hakuiona njia nyingine ya kulipiza zaidi ya kuendeleza mpango wake kama alivyopanga, Ili wajue kuwa hakuwa na mzaha. Na huyu aliyethubutu kumtegea sumu? Lazima afe, alijiambia. Maadamu wamekwisha mhukumu kifo sasa walikuwa ni maadui zake. Haikuwepo haja ya kuwasamehe. Kuhusu usalama wake binafsi alijua angefanya nini. Mara baada ya kufanikisha mpango wake huo angetoweka na kwenda mbali ambako angeanza maisha mapya. Kweli, mkono wa majasusi ni mrefu na umetambaa kila upande wa dunia, lakini usingemgusa yeye. Alijua vipi angeweza kujificha na kujigeuza kuwa mtu mwingine kabisa. Hii dunia ya pesa, nae alikuwa nazo za kutosha asingeshindwa kuzitumia zimgeuze kuwa mtu mwingine. Ikibidi atajigeuza kuwa mwanamke kabisa. Wazo hilo lilimfanya Proper atabasamu.

Alikuwa na uhakika kuwa huyu mtu aliyetega sumu hii lazima atarudi kutazama matokeo ya kazi yake, pamoja na kuchukua maiti ili aifiche kokote alikopanga. Akaamua kumsubiri mtu huyo kwa namna aliyotaka yeye. Alijifanya maiti aliyefia juu ya kochi, mkono mmoja na kichwa vikining’inia. Mkono wake wa pili ulikuwa umeshika bastola kwa uficho kiasi kwamba yeyote ambaye angeingia asingeweza kuiona wala kushuku.

Mtu huyo aliyekuwa akisubiriwa aliingia kimya kimya kama kivuli. Ilikuwa baada ya dakika kadha wa kadha kupita bila ya lolote kutokea. Ndipo Proper aliposhtukia mkono ukitua juu ya kifua chake kupima kama moyo ulikuwa ukifanya kazi. Hakujua mtu huyo alikuwa ametokea wapi. Wala hakuwa na haja ya kumtazama alikuwa nani. Taratibu aliinua mkono wake wenye bastola na kufyatua risasi tatu mfululizo. Mwili wa mtu huyo ulimwangukia pale kwenye kochi huku akitapatapa. Proper alipoinuka na kumtazama hakuweza kumtambua. Uso mzima ulikuwa umefumuliwa na risasi kiasi cha kuacha nyama nyama zenye damu ambazo hata mama yake aliyemzaa asingeweza kumtambua. Kiwiliwili kilikuwa salama. Kilikuwa kiwiliwili cha mzungu kilichofunikwa na mavazi ambayo kidogo yalimshitua Proper. Yalikuwa mavazi ya kipadri. Proper aliutia mkono wake katika moja ya mifuko mingi ya vazi hilo na kutoa kijimsalaba ambacho kilikuwa na maandishi yasemayo “Father Peter Jamaa” amemuua Padri! Proper alishangaa. Kumbe ni Padri huyu ambaye siku zote alikuwa siri yake na makao makuu! na asafiri salama huko peponi.

Masaa matatu baadaye Proper alikuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam akisoma ratiba ya safari za ndege. Mkononi alishika begi lake dogo jeusi ambalo hata hivyo lilikuwa na vifaa vyake muhimu tu. Begi hili lilikuwa na mifuko kadha ya siri ambayo wakaguzi wasingeweza kuifikia. Mifuko hii ya siri ilihifadhi baadhi ya silaha zake na pesa za kutosha.

Hakujua alikotaka kwenda. Alichojua ni kwamba ilimlazimu kuondoka hapa nchi kwa muda ili kuwahadaa waajiri wake ambao bila ya shaka wangeanza kumuwinda kwa hasira kali zaidi. Vilevile kuondoka kwake kungempa ahuweni na fursa ya kusubiri siku aliyohitaji ili aachie lile pigo lake la mwisho. Kama kawaida, Ndege za Shirika la Ndege Tanzania ATC zilikuwa zimejaa, lakini baada ya dakika ishirini hivi alipata taarifa kuwa, ingewasili ndege ya AEROFLOT itokayo Nairobi, Kenya ikielekea Bujumbura, Burudi kupitia Mwanza, ambayo ingekuwa na nafasi. Proper alikata tiketi ya Mwanza na kuisubiri. Ilipowasili, alikuwa abiria wa kwanza kuingia ndani ya ndege.

kwa Inspekta Kombora alikuwa amevurugikwa kichwa kiasi cha kuchanganyikiwa kama alivyokuwa, simu hii ilikusudiwa kumtia kichaa zaidi.

Alikuwa katika ofisi yake, juu ya kiti ambacho hakikukalika, mara kwa mara akipiga hatua kuelekea dirishani ambako alisimama akichungulia kana kwamba alitegemea wakati wowote kuona uovu aliokuwa akiutarajia kutokea. Uovu ambao hakuujua, ingawa hakuwa na shaka kuwa ungekuwa wa kutisha kuliko mengi yaliyokwisha tokea.

Lolote lingeweza kutokea, aliamini Inspekta Kombora. Dunia hii iliyojaa waovu, nchini humu wakiwemo wa kutisha. Wako watu wenye mioyo ambayo husherekea kitendo chochote cha unyama. Watu ambao hutabasamu waonapo maafa na kushangilia waonapo mauaji. Watu kama hao si wachache. Si kuna yule aliyejaribu kuitia moto Benki kuu? Bila ya kujali wala kujiuliza kuwa nchi na wananchi wangetukiwa na nini baada ya pesa zote za hapa na za kigeni kuteketea! Si wako wale ambao wamepanga kuwaua viongozi ambao wamechaguliwa na wananchi? Naam, waovu wapo na si haba.

Lakini hawa wanataka nini?

Ni swali hilo ambalo lilikuwa limezidi kuneemeka katika kichwa cha Inspekta Kombora na hasa lilimtesa zaidi ya hofu yenyewe. Swali hilo ambalo lilianza kumsumbua tangu watu hawa wasiojulikana walipoanza kumfanyia njama Joram na hata kufanikiwa kumuua! Isitoshe, hawa waovu wamemuua Neema, Katibu wa Joram! Swali hili liliongezeka nguvu na kutisha zaidi mara alipopokea habari za kifo cha Neema katibu wa Joram! Ingawa kilionekana kama kifo cha kawaida machoni mwa watu wa kawaida, lakini Inspekta Kombora aliamini kuwa yalikuwa mauaji. Na hospitali ilithibitisha hivyo baada ya kugunduliwa kwa sumu kali mwilini mwake. Sumu ile ile aliyokuwa ametegewa Joram.

Watu hawa wasiojulikana, walikuwa wamekwepa mbinu zote za upelelezi. Kufikia sasa, hakukuwepo na fununu yoyote. Wala haikuwepo hakika kama alikuwa mtu mmoja au kikundi kimoja kilichokuwa kikifanya haya. Kifo cha yule malaya mzuri, Waridi, kifo cha Joram,kifo cha Neema… kifo, kifo kipi kingefuata? Na ni vifo tu au pamoja na… pamoja na nini?… Aliendelea kutaabika kimawazo. Ni mawazo hayo yaliyomzidishia hofu na mashaka mengi kichwani.

Haya, na sasa simu hii isiyoeleweka inachohitaji! Kombora alikitazama chombo cha kusikilizia kwa hasira. Kisha alinguruma tena kwa nguvu zaidi.

“Unasemaje wewe?”

“Mbona mkali hivyo Inspekta. Hutaki kupata salamu zako?”

Kombora alikumbuka sauti hiyo. Haikuwa ngeni masikioni mwake. Hata hivyo, alishindwa kukumbuka mwenye sauti hiyo moja kwa moja. Sauti hiyo ilionyesha dalili na dhamira maalumu. Kombora alishindwa kuikata simu hiyo kama alivyokusudia awali. Badala yake aliuliza.

“Salamu salamu kutoka wapi?”

“Kuzimu”

“Nini?”

Kicheko kikasikika kutoka upande wa pili: “Mbona unashtuka Inspekta? Si kuna rafiki yako aliyekwenda huko hivi karibuni? Anaitwa Joram Kiango. Au umemsahau mara hii?”

Sekunde chache zilizofuata Kombora alikuwa akisikiliza kwa makini zaidi. Dakika chache baadae tayari alikuwa ndani ya gari yake, bastola kibindoni, akimweleza dereva wapi apelekwe, kama alivyokuwa akielezwa katika simu.

Mara alitokea mmoja ya wasaidizi wake ambaye baada ya kupiga saluti alisema, “Mzee, kuna tatizo jipya limetokea.” Kombora alimjibu kwa kumkazia macho askari huyo. Hivyo akaongeza haraka haraka, “Father mmoja ametoweka tangu jana.”

“Ametoweka!” Kombora alifoka. “Mmekwisha mtafuta katika makanisa yote?”

“Kila mahali…”

“Katazameni hata makaburini. nasikia huwa anaenda juko kuombea watu.”

“Tumetazama huko pia lakini…”

Kombora akataka kwa ukali: “Aongeze nenda kata katika nyumba ya wanawake malaya. Nasikia wengine wana mahawara zao.” Lakini hilo hakulitamka kwa kuchelea kuonekana mhuni mbele ya “vijana” wake. Badala yake alisema, “Sikia ninaharaka sana, nitarejea baadaye. Kwani kitu gani hasa kinawatia wasiwasi kwa mtu kutoweka usiku mmoja tu? Watu si hupotea hata kwa wiki na wakarudi salama?”

“Damu.”

“Damu?” Kombora alihoji kwa mshangao.

“Nguo alizokuwa kavaa zimeokotwa mtaani. na zilikuwa na damu .”

“My God!” Kombora alinong’ona akiingia katika gari na kumwashilia dereva atie gari moto.

#
#
#

Wajumbe wote walikuwa wamehudhuria mkutano huu, ingawa baadhi hawakuuona kama ulikuwa mkutano wa kawaida. Kwanza, hawakutegemea kama ungeweza kufanyika mapema kiasi hicho na kisha njia zilizotumika kuitisha mkutano huu hazikuzingatia usalama wa hali ya juu kama walivyozoea. Safari hii kila mmoja alikuwa amepata kadi kwa njia ya posta ‘Express’ ikiwa wa ujumbe mfupi sana ambao kila mmoja aliuelewa ukisema “LEO SAA MBILI PALE PALE.”

Kila mmoja alikuja kwa shingo upande. Hofu ikiwa tele moyoni pamoja na hasira dhidi ya “Mwenyekiti”. ‘Mwenyekiti alikwisha wafanya kuwa kama mateka au watumwa wake. Ahadi zake za utajiri na vyeo vilikuwa na ladha ya uchachu mdomoni. Hawakuwa na hila ya kumwepuka. Haikuwepo njia nyepesi, hasa walipokumbuka mauaji ya kinyama ambayo mtu huyu alikuwa akiyaendesha bila ya serikali kumshuku. Zaidi, wasingeweza kusahau maneno yake aliyowaambia katika mkutano wa mwisho akisema “Kifo kitakuwa kando kikikusubiri…” na “Hautajua kitu gani kimekupiga.” Hivyo walimtii na kufika mkutanoni. Na waliketi kwa utulivu kumsubiri afungue mkutano baada ya kumkuta katulia nyuma ya meza yake, juu ya kiti na, kama ilivyo kawaida, nuru ya taa ikiwamulika macho hata wasiweze kumuona kikamilifu, na kumfanya yeye awaone vyema zaidi.

“Nadhani hatukutegemea mkutano huu ndugu Mwenyekiti,” Mjumbe mmoja aliinuka na kuropoka ghafla. “Umeuitisha kinyume cha kanuni iliyowekwa na haukuwa na usalama. Bila shaka lipo jipya lililokulazimisha kuuitisha. Pengine ingefaa uanze kutueleza mapema ili tuweze kuondoka mahala hapa.”

“Ni kweli” Sauti mbili tatu zilimuunga mkono.

“Kweli kabisa,”Mwenyekiti alisikika akiunga mkono pia. “Lakini ningeomba tufanye subira kidogo. Yuko mgeni mmoja ambaye amealikwa kama msikilizaji tu wa kikao hiki.”

Sauti yake ilikuwa ngeni masikioni mwao. Haikuwa ile ambayo waliizoea. Ikawafanya washangae. Mmoja wao hakuwa amevutiwa na sauti hiyo. Yeye kilichomshangaza zaidi ni madai ya Mwenyekiti.

“Mgeni?” aliuliza kwa sauti ya juu kidogo. “Nadhani tulikubaliana kitambo kuwa suala hili ni siri kubwa baina yetu tuliopo hapa tu. Vipi tena mambo ya kuleta wageni wengine?”

Mwenyekiti alikohoa kidogo kabla hajamjibu mjumbe huyo kwa kusema, “Nchi hii ni kubwa sana ndugu zangu. Tulioko hapa hatuwezi kuifaidi peke yetu. Lazima tuwakaribishe baadhi yao vilevile. Mmoja wao ni huyo ambaye atafika hapa karibuni,” alimaliza kwa kuitazama saa yake.

Sasa ilikuwa dhahiri kuwa sauti hii ilikuwa ngeni kabisa masikioni mwao. Baada ya juhudi zao za kumtazama kutozaa matunda kwa sababu ya nuru iliyotengwa, waligeuka na kutazama kwa mshangao. Mwenyekiti akiusoma mshangao wao, alisikika akiangua kicheko, kicheko ambacho kilitofautiana kabisa na kile cha kikatili walichokizoea.

Kabla hawajajua la kufanya, mlango ulisikika ukugongwa na kisha ukafunguka. Mgeni aliyeingia alikuwa wa mwisho kati ya watu wote ambao wajumbe wangependa kumuona wakati huo. Inspekta Kombora, Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Polisi Nchini ambacho hujishughulisha na masuala ya hujuma za kiuchumi na kisiasa! Mtu ambaye sifa zake za ushindi dhidi ya watu wa aina hiyo si haba. Alikuwa kavaa mavazi yake kamili ya kikazi. Nyota zikipepea mabegani.

Kombora pia aliduwaa mbele ya umati huu. Haikuwepo sura yoyote ngeni machoni mwake. Wote walikuwa watu ambao madaraka yao yalifanya picha zao kutokea magazetini mara kwa mara, majina yao kutajwa redioni, na katika mikutano ya hadhara walikalia vile viti vya mbele vinavyowaelekea watu. Sasa wanafanya nini katika chumba hiki ambacho kilikuwa siri mno hata akawa amekifikia baada ya mzunguko mrefu kutoka chumba hadi chumba? Alipoyatupa macho kumtazama yule huyo aliyejiweka kitini mbele yao kwa maana ya uenyekiti, aliyarejesha chini mara moja baada ya kulakiwa na ile nuru kali ya taa za umeme.

“Sijaelewa…” alianza kusema. Kisha alinyamaza ghafla ili kufikiri kabla ya kutia neno lolote katika kikao hiki. Simu iliyopigwa ilimwambia aje hapa, ili apewe salamu zake kutoka kwa Joram, kuzumu. Alikubali kuja hapa hasa simu ilipomwelekeza katika jumba hili. Jumba ambalo machoni mwa wapita njia lilikuwa la kawaida lakini kwake halikuwa la kawaida. Kwa muda mrefu, alikuwa akilitupia macho yenye maswala ambayo yalitaka kujua kipi hasa kinachofanywa kwenye nyumba hii. Alikuwa hajapata nafasi hadi leo hii.

“Karibu sana Inspekta,” sauti ya mwenyekiti ilimhimiza. Nimefurahia sana kufika kwako. Haja yangu ni kutaka ufahamu kuwa tulioko mbele yako ni raia na wazalendo wa nchi hii wenye njaa kubwa ya utajiri na kiu kali ya vyeo kiasi cha kushiriki kikamilifu katika njama za hatari ambazo hazijawahi kutokea katika historia ya ulimwengu.” Wote walimsikiliza kwa mshangao. Kombora aliduwaa. Wajumbe walitetemeka.

“Labda nirudi nyuma kidogo kimaelezo. Mpango huu umeandaliwa kwa muda mrefu. Majaribio ya aina aina yamekwishafanyika. Sumu maalumu zimeandaliwa. Moja ya sumu hizo ni ile ambayo ilikusudia kumuua Joram Kiango. Iliposhindwa, msichana aliyeteuliwa kuutekeleza mpango huo, aliuawa kikatili kuliko kifo chochote cha kikatili kilichowahi kutokea. Utakumbuka Inspekta kuwa, Viungo vya msichana huyo viliokotwa chumbani kwake mfano wa nyama inayouzwa. Baada yake ndipo Joram aliuawa kwa bomu. Viungo vyake vilitapanywa ovyo hata asijulikane kabisa. Sivyo Inspekta? Na baada ya Joram, akauawa Neema Iddi yule msaidizi wake. Ni sisi hawa ambao tuko mbele yako…”

Wajumbe ambao walikuwa wakitetemeka walianza kuinuka. mmoja alipiga hatua mbili tatu kuelekea mlangoni. Lakini alirejeshwa na bastola ya Kombora ambayo ilikuwa ikimwelekea. “Yeyote atakatyeinuka atakuwa maiti. Kuanzia sasa, wote mko chini ya ulinzi.”

“Usiwe na haraka Inspekta,” Mwenyekiti aliendelea kwa utulivu kama awali. “Bado kuna mengi yatakayokusisimua. Kumbuka umealikwa kama msikilizaji tu. Tulioko mbele yako si tishio kubwa kwako. Yuko kiongozi wetu ambaye si mroho sana wa vyeo na utajiri, lakini anayo maradhi ya hatari zaidi. Yeye ni mtu anayependa sana mauaji. Mengi kati ya mauaji yaliyokwisha fanyika ameyafanya kwa mkono wake. Na anafurahia sana kuua. Twaweza kusema kuwa ana wazimu. Yeye ndiye kiongozi wa mpango huu na ameapa kuwa ataufanikisha. Kwa bahati mbaya hayupo hapa tena. Ametoweka…”

“Wewe ni nani?” Kombora alifoka.

“Mjumbe tu mwenye jukumu la kukupa salamu kutoka kuzimu aliko…”

“Sikia,” Kombora alikatiza tena. “Huu sio wakati wa mzaha ata chembe. Kuna mtu mmoja tu mwenye sauti na tabia kama yako. Mtu ambaye alifariki kitambo na nilimzika mwenyewe. Joram Kiango. Sasa wawa ni nani? Huonekani kama mmoja wa kikundi hiki cha hatari sana. Pengine hii ni ndoto tu kesho mambo yatakuwa shwari?”

“Sio ndoto Inspekta” Mwenyekiti huyo alijibu. Labda nindoe nuru hii inayowanyimeni nafasi ya kuniona vyema.” Aliupeleka mkono wake chini ya meza na kubonyeza mahala. Nuru ikatoweka. Aliyekuwa nyuma ya nuru hiyo alikuwa Joram Kiango!

Na alikuwa akitabasamu.

“Joram Kila mmoja aliropoka kwa mshangao. Akuna aliyeyaamini macho yake.

“It can’ be true,” Kombora alifoka kwa lugha ya kigeni. Akijisahihisha mara moja akisema, “haiwezekani. Lazima iwe ndoto ulifariki kitambo Joram. Dunia nzima inafahamu hivyo.”

“Ndiyo,” Joram alijibu baada ya kucheka kidogo. “Nilifariki. Na ni rafiki zangu hawa ambao walinihukumu kifo na kuhakikisha nimekufa. Lakini kuna mengi yalitokea. Nadhani Muumba alikuwa alikuwa hajaweka saini katika mkataba wa kifo changu, au ameikubali rufaa yangu. Hivyo nimerudi ili nitoe salamu zangu kwa kikao hiki. Salamu nilizozipata uko akhera,” alimaliza akiachia tena tabasamu.

Lakini tabasamu la dhihaka.

Tabasamu ambalo liliwatesa sana wajumbe zaidi ya kufichulika kwa ukweli. Wote walikuwa wameamini kuwa Joram alifariki kama walivyoafikiana. Na walikuwa wamesikia hivyo katika vyombo vya habari. Na walikuwa wamehakikishiwa na “Mwenyekiti” wao ambaye hawakuwa na shaka kuwa angetimiza jukumu hilo. Vipi tena Joram awe hai! Tena mbele yao! Akiwadhihaki na kuwakebehi! Kitu gani kinatokea! La kutisha zaidi ni kufahamu kuwa Joram bado yu hai. Waliona matumaini yao yakifa mbele yao. Tazama anacheka! Tazama macho yake yanavyotoa nuru ambayo inadhihirisha kuwa siri kamili alikwisha fahamu. Siri ya kutisha ambayo inatosha kuwafanya wahukumiwe kitanzi! Yu wapi? “Mwenyekuti” huyu aliyewatumbukiza katika mkasa huu? Au tayari ametiwa mikononi?

Kombora hangeweza kustahimili, akasema “Sikia Joram. Pengine nimeanza kuzeeka mno. Lakini nadhani mtu yeyote aweza kutiwa kicha na suala huli kama nilivyochanganyikiwa sasa. Kabla sijaanza jukumu lolote la muhimu nadhani unao wajibu wa kufafanua vipi uko hai baada ya lile bomu ambalo lilitapanya maungo yako. Sipendi kuamini kuwa umekufa ukafufuka…”

“Sikufa Inspekta,” Joram alifafanua. “Lile bomu halikunidhuru,” akaendelea kueleza

Bomu lilipuka muda mfupi baada ya Joram kumwona mtu yule aliyekuwa akinyatia mlangoni. Joram hakujuwa mtu yule katokea wapi. Anachojua ni kwamba, aliona kila kitu ndani ya nyumba kikipaa angani na kutua sakafuni. Alijikuta chini ya vitu vingi ambavyo vilimkandamiza sakafuni. Kichwa kilisikia maumivu makali. Maumivu ambayo yalimfanya asikie kelele za watu bila ya uwezo wa kuomba msaada. Mwishowe, kukawa kimya. Joram akafahamu kuwa watu wameondoka katika eneo hilo bila ya kumwona. Tumaini la kunusurika likamtoka. Akatulia asubiri kifo. muda si mrefu, alizirai.

Fahamu zilipo mrudia, alijikuta yumo katika chumba cha nyumba mbovu mbovu kalazwa kitandani akihudumiwa, ndio macho yake yalipopambana na kitu chenye sura ya kutisha na kuchekesha. Kitu ambacho kilikuwa mithili ya binaadamu. Dalili pekee iliyomfanya ajuwe kuwa mtu huyo ni mwanamke, ni furushi la matiti lililokuwa kifuani bila mpangilio wowote uwezao kuvutia macho ya mwanaumwe.

ITAENDELEA

Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Nne

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment