Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Tano
NEW AUDIO

Ep 05: Salamu Kutoka Kuzimu

Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Salamu Kutoka Kuzimu

Sehemu ya Tano (5)

“Mimi sijakwambia lolote ambalo nakusudia kukwambia huku huyo mwenzangu tayari amekuletea zawadi kubwa kama hii na kukuahidi kuzunguka nawe duniani”.

Nuru alimkatiza Duncan kwa kicheko ambacho kilichofuata sauti yake nzuri ikisema, “Huna haja ya kuwa na hofu na mzee yule. Sina wazo naye kabisa. Zaidi ya hayo, si nimekwambia walivyomfanya? Hana madhara kwa mwanamke yeyote”.

“Usiwe na kawaida ya kumwamini kila mzee kwa lolote analosema”, Duncan alimtahadharisha. “Sasa tafadhali rudia tena hatua kwa hatua jinsi ilivyotokea… hata mkafahamiana na mzee huyo, na yote mliyozungumza”.

Kwa mshangao kidogo Nuru alirudia hadithi hii nzima. Baada ya hadithi hiyo, Duncan aliuliza maswali mengi ambayo Nuru hakuona umuhimu wake. Ilimshangaza Nuru kuona kila jibu likimridhisha zaidi Duncan.

Hatimaye Duncan aliinuka kwenda bafuni. Aliporudi alikuwa na mkufu ule mkononi akamkabidhi Nuru huku akisema, “Naona saa yako ya kurudi kazini imewadia. Chukua zawadi yako, lakini tafadhali usiruhusu zawadi hizi zikununue. Jihadhari na wazee wa mjini”.

Nuru aliupokea mkufu wake na kuinuka kutoka kwenye kochi.

Alipofika nje ya chumba alisita kidogo. Ndiyo kwanza akakumbuka kuwa Duncan hakuwa amemweleza chochote ambacho angependa kuelezwa.

“Hapa Afrika, bandari ya Salama”.

“Nani mwenzangu”…

“Kigogo hapa… Napenda kujua kama lile ua bovu mmelichuma tayari au bado, na kama bado ni kwa sababu gani?”.

“Bado kidogo. Mtaalamu wetu amesema bado anafanya uchunguzi wa mwisho katika kubaini mizizi yake. Mara akikamilisha huo utafiti wake litang’olewa haraka iwezekanavyo”.

“Nataka ling’olewe haraka iwezekanavyo, mbegu zile ni hatari kusambaa. Unajua kesho ni siku ya mwisho? Hakikisha ua hilo linang’olewa.

“Bila shaka Kigogo. Mizizi tu ilikuwa haionekani vizuri katika darubini, hasa ilipofikiriwa kuwa mbegu zimesambaa hovyo. Sasa hali iko shwari. Mtaalamu wetu anaamini kuwa baada ya muda mfupi atakuwa tayari kalichuma”.

“Alichume haraka. Alichume kikamilifu. Sitaki lichumwe na mtu mwingine, anaweza kumeza maradhi yakaleta madhara. Over”.

“Off and over, Kigogo.

Chombo kilizimwa na kurejeshwa katika hifadhi yake. Msemaji alikuwa akifikiri kwa muda. Kigogo mikono yake ilikuwa ikitetemeka. Sio kazi rahisi, kupewa jukumu la kuua. Hasa kumuua mtu hatari ambaye yu macho zaidi ya Simba aliyejeruhiwa. Isitoshe, mtu huyo akiwa rafiki mkubwa, kama ndugu umpendae, mtu uliyeshirikiana pamoja katika maovu na unyama wa kila aina. Mtu kama huyo, kumwelekezea bastola na kumuua, kwa kuwa tu karopoka na kuamua jambo ambalo wakuu hawajaliamua! Aibu ilioje!.

Kwa hivyo, aliposikia habari ya kutorokea Mwanza kwa mwenzake, aliona kama bahati njema imemwangukia. Iwapo huyu aliyeamuriwa kumuua ametorokea huko na kuvuka mpaka, hatabeba jukumu la kumuua tena. Jukumu hili litawahusu wengine walioko huko aendako. Lakini mara wapelelezi wakaleta habari kwamba amerejea na yuko Arusha tayari kwa kusudio lake la kikatili. Ndipo alipowaarifu wakubwa. Nao wakamwamru kumuua. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kutekeleza amri. Akainua simu na kuzungusha namba fulani. Ilipopokelewa aliuliza, “Mmempata alipo?”.

“Bado, mzee…”

“Bado! Kwa nini?” alifoka.

“Ametoweka kidogo. Nadhani amejibadili tena. Unajua anavyoipenda tabia ya kinyonga. Mara ya mwisho tulimpata alipokuwa kajifanya chongo na mguu mbovu. Sasa haonekani. Bila shaka ame…”

“Hata kama atajigeuza kinyonga kabisa, lazima apatikane haraka, sawa?”.

“Sawa mzee”.

“Na mara mtakapomuona niiteni mara moja. Sawa?”.

“Sawa”.

“Au hamuifahamu adhabu ya kushindwa kutimiza wajibu?” Alikata simu na kuliendea kasha lake la silaha. Akachunguza silaha mbalimbali zilizokuwemo; bastola aina aina, viwambo vya kuzuia sauti na mabomu kadhaa. Akaviweka katika mifuko yake ya siri.

Kisha aliiunua simu na kulipigia shirika moja la ndege za kukodi.

“Tafadhali andaa ndege itakayonifikisha Arusha mara moja”, aliagiza.

“Umepata”, alijibiwa. “Ungependa kuanza safari ya kuondoka saa ngapi?”.


II

“Inspekta Kombora hapa naongea kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi…”

“Ndiyo, afande”.

“Nifahamishe, taarifa bado ni ile ile hakuna fununu yoyote ya yule mwenda wazimu Proper?”

“Bado afande. Tumefanya kila aina ya uchunguzi. Kila hoteli na kila nyumba za wanawake malaya zimechunguzwa kwa ustadi mkubwa, hajaonekana mtu yeyote wa aina yake. Arusha nzima imepekuliwa. Bila shaka atakuwa ametorokea nje ya nchi.

Labda. Lakini sipendi kuamini kuwa katoroka. Tumewasiliana na wenzetu wa Rwanda na Burundi. Hakuna dalili ya mtu mwenye tabia kama zake. Anaweza kuwa yumo humu nchini. Na kama yumo nchini, atakuwa hapo hapo Arusha. Mmebakiwa na masaa machache sana ya kukamilisha uchunguzi. Kesho kama mnavyojua viongozi wanaanza kuwasili, lazima mhakikishe kuwa jambo lolote la kipumbavu halitokei”.

“Hakuna jambo la kipumbavu litakalotokea mzee”, sauti ilieleza. “Hoteli nzima imepigwa ufagio. Wageni na wafanyakazi wote wamechunguzwa kwa makini. Kuna kijana mmoja tu ambaye alielekea kututia wasiwasi. Tabia yake ya kuzungumza na kila mtu, ilitutia hofu. Ilikuwa kama anayetafuta habari fulani. Lakini baada ya kumchunguza kwa makini tumebaini kuwa hana kasoro. Tunazo hata kanda za maongezi yake kwa wafanyakazi. Kama utapenda kusikia tunaweza kukutumia”.

“Msihangaike kuzituma huku. Leo nategemea kuwasili hapo Arusha wakati wowote. Anaitwa nani huyo kijana?”, alihoji Kombora.

“Duncan”.

“Vizuri”.

Proper alikuwa juu ya kitanda katika chumba cha mojawapo ya Hoteli nyingi za Mji wa Mwanza. Mkono wake wa kulia ulikuwa ukichezea matiti ya mischana mrembo aliyelala kando yake, mkono wa kushoto ulikuwa ukipepesa kiuno cha msicha huyu. Wote walikuwa uchi na miili yao ikitokwa jasho. Jasho liliendelea kuwatoka asubuhi hii yenye baridi kali. Jasho lililotokana na juhudi za miili yao katika kuthibitisha utaalamu na uwezo wao kimahaba.

Huyo alikuwa msichana wa tano tangu Proper aingie mjini Mwanza na kufikia katika hoteli hii… Wawili waliotangulia, alikuwa amewaona wa kawaida tu. Zaidi ya uzuri wao wa sura na maumbile ya kuvutia, kitandani hawakuwa na la ziada. Hivyo aliwapa ujira wao na kuwaaga. Lakini huyu wa tatu, hakuonekana kama alikuwa mtu wa kuagwa kwa urahisi. Sura haikuwa nzuri sana. Wala umbile lake halikuwa kama yale ambayo huwafanya madereva wa magari waroho wasababishe ajali barabarani kwa kuwatazama. Msichana huyu alikifahamu kile alichopaswa kuwatendea wanaume. Alielewa alichokusudia Muumba wake kwa kumwezesha kuwa na viungo tofauti. Kila kitendo chake kitandani alikitenda kwa ari na nia, bila uchoyo wa aina yoyote. Kila kiungo chake mwilini alikitumia kikamilifu bila hiana. Na hakuonekana mwanafunzi katika vitendo vyake vyote.

Ni hayo yaliyomfanya Proper ajisahau kwa kiasi fulani.

Ni kweli kuwa aliyoyaona Mwanza hayakuwa ya kawaida. Katika Jiji la Dar es Salaam ambako aliishi sana, kupata msichana au mwanamke wa kujiburudisha haikuwa tatizo. Ziko saa za jioni, au usiku, ambazo utajitokeza mitaani na kujipitisha. Hutavuka mtaa wa tatu kabla hujapata mtu ambaye ataivunja safari yake na kuandamana nawe hadi chumbani kitandani, ambako ataondoka alfajiri na siku ya pili. Lakini si hivyo kwa muda wa Mwanza. Hapa unachotakiwa kufanya ni kujipatia chumba chako kwanza katika moja ya hoteli nyingi zilizogaa. Kaa chumbani kwako kwa utulivu. Haitapita muda mrefu kabla hujapigiwa hodi na watoto wa kike ambao watajitia kuuliza hili na lile hadi maswali yao yatakapokufanya utoe jibu litakalowafanya waangukie kitendani.

Proper pia alitulia chumbani kwake kimya akingoja hodi yake. Haja yake haikuwa kujiburudisha tu, bali alitaka kujificha, ili aonekane kama wapangaji wengine. Kama vijana ambao waliamua kuonyesha ujana wao au wazee ambao waliifurahia fursa ya kuwaasi wake zao. Ndipo alipoanza kuwakaribisha wasichana mmoja baada ya mwingine hadi alipotokea huyu, ambaye hakuonekana kama alistahili kuondoka.

“Jina lako”, Proper alimwuliza huku akihamisha mkono mmoja kutoka kiunoni na kuupeleka kichwani kwa ajili ya kuchezea nywele ndefu zilizotimuliwa kutokana na zoezi lililokuwa likiendelea kitandani hapo.

“Sofia” msichana huyu alijibu kwa sauti ya mahaba. “Na wewe?” akaendelea kuuliza.

“Bakari, ingawa rafiki zangu hupenda kuniita Beka”, Proper alimlaghai.

“Kwa maana hiyo nikuite Beka siyo”.

“Hapana. Niite mpenzi”.

Sofia akacheka. Na kicheko chake kilikuwa cha kupendeza.

Baada ya muda, msichana huyu alipitiwa na usingizi. Kichwa akakiegemeza katika kifua cha Proper, mkono wake akauweka mahala fulani katika mwili wake, akawa amelala kwa utulivu mkubwa. Uso wa msichana huyu ulikuwa kama anacheka, kwa jinsi alivyokuwa amelala.

Proper alimtazama kwa muda. Kisha alijitoa kitandani hapo kwa uangalifu bila ya kumwamsha Sofia. Akaliendea begi lake ambalo alilifungua na kulichunguza. Sehemu za kawaida zilikuwa na mavazi yake, vitambulisho vyake bandia na vikorokocho vingine. Mifuko ya siri, ambayo kama alivyotegemea, wakaguzi wa uwanja hawakuweza kuifikia, ilikuwa na silaha zake, nyaraka zake muhimu, dawa zake maalumu, na pesa nyingi. Kila kitu kilikuwa kama kawaida. Proper akakirudia kitanda ambako alikiinua kichwa cha msichana huyo taratibu na kukirejesha kifuani kwake na mkono kuuweka kama ilivyokuwa awali. Kisha akayafumba macho yake kwa namna ya utulivu.

Lakini akilini hakuwa na utulivu wowote. Kichwa chake kilikuwa kazini kikitafakari matukio yote yaliyopita na ajali. Aliukumbuka kwa hasira mpangi wake madhubuti ambao aliuandaa kwa gharama kubwa na muda mrefu, na ulivyokaribia kumpotezea maisha. Ilimchukiza kuona kuwa waliokusudia kumwangamiza walikuwa watu wa upande wake. “Kwa ajili ya uoga”, aliwaz. Uwoga usio na msingi. Uoga ule ule ambao umewafanya kwa muda mrefu watumie pesa nyingi kukamilisha mabomu ya nyuklia, lakini hadi leo hawajadhubutu kufanya majaribio walao katika nchi moja. Wapi basi haja ya kusumbua vichwa? Yeye Proper angewaonyesha. Liwalo na liwe lakini mpango wake aliouanzisha lazima atautekeleza. Peke yake na kwa mkono wake Dunia ione Ulimwengu usikie.

Proper aliyarejesha mawazo yake kwa Inspekta Kombora na jeshi lake. Walikuwa wanafanya nini alijua kwamba, kifo cha yule Padri kiliwafungulia polisi mwanya fulani. Hata hivyo alielekeza fikra zake zote kwa kazi hii ya mwisho. Hakuna ambaye angeweza kulizuia pigo la mwisho, Pigo la kihistoria.

Proper alimtazama Sofia usoni. Akamuona alivyolala kwa utulivu. Angetokwa na kicheko kwa kumhurumia msichana huyu alivyolala kwa utulivu bila kufahamu amelala na mtu wa aina gani. Hajui kama amelala na kifo! Alinongona kimoyomoyo. Kisha alimwamsha na kumtaka wafanye tena mapenzi. Kama kawaida, msichana alikuwa tayari. Kama kawaida yalikuwa mapenzi ambayo yaliacha kumbukumbu akilini mwao.

“Wapi unaishi Sofia?” Proper aliuliza baada ya kukusanya pumzi kwa dakika kadhaa.

“Kirumba, nyuma kidogo ya Uwanja wa mpira”.

“Unaishi na nani Sofia?”.

“Peke yangu”, Kimya kifupi kikapita. “Kwa nini unapenda kujua?”.

Proper alipeleka ulimi wake kuchezea chuchu za Sofia kabla hajatoa jibu.

“Kwa sababu nyingi. Kubwa ni kwamba ni kwamba sijapata kukutana na aliyeniburudisha kama wewe. Nisingependa kutengana nawe tena, kwani nikikukosa huenda nisipate mtu wa aina yako. Hivyo, nimependa nihame hapa hotelini na kuishi kwako hadi shughuli zangu zitakapokwisha hapa Mwanza, halafu twende zetu pamoja Bujumbura. Unasemaje?”

Habari hii ilimfurahisha sana Sofia. Msichana huyu alikuwa ametoroka kwao Sengerema baada ya kupata mimba isiyokuwa na mwenyewe. Mimba hiyo iliishia chooni. Tangu siku hiyo, amekuwa mtu asiyekuwa na tumaini la kupata bwana wa kudumu. Sura yake pia, ilikuwa pingamizi kubwa. Daima mabwana aliowapata, walikuwa hawa wa ‘kuokota’ Mabwana waliosukumwa na uchu tu wa kuwa na mwanamke. Hali hii ilimfanya msichana huyu ajikabidhi kwa kila mwanaume bila kujali lolote, akiwatimizia kila haja bila aibu wala kinyongo. Lakini harakati zake za kuwaburudisha wanaume mara nyingi hazikumfikisha mbali. Mara kwa mara alikuwa akipewa ‘kwa heri ya kuonana’ na mabwana hao. Wengi waliwarudia wake zao. Wengine walikuwa wameishiwa. Na wengine walikusudia kuziponyesha pesa zao.

Ndiyo Sofia akayachukulia maombi ya ‘Mzee kijana’ huyu kama tunu aliyonunuliwa bila ya kutazamia. Aliyaona kama mwisho wa matatizo yake na mwanzo wa maisha mapya. Alimtazama tena Proper. Hakuona dalili yoyote ya mzaha katika sura yake. Kama kweli mtu huyu alikuwa na tatizo lolote, pesa hazikuwa mojawapo. Angekubali mara moja. Hata hivyo alikumbuka hali ya chumba chake, mazingira yaliyostahili jina la pango. Ndipo alipomweleza Proper kwa sauti iliyonasihi.

“Ningependa sana kukukaribisha kwangu. Lakini hali ya chumba kile… kwa kweli, hakifai kwa mtu kama wewe”.

Proper hakuwa mgeni kwa maisha ya wasichana wengi mjini. Alikwisha waona wengi ambao wawapo mitaani wanaonekana kama malaika kwa mavazi mazuri, lakini ukifika wanakoishi utadhani ni vijakazi. Alimsihi Sofia aondoe shaka. Alimweliezea kuhusu msingi wake wa kimaskani. Kwamba ameishi sana ‘gheto’ na maisha hayo anayapenda. “Nikiwa Dar hupendelea sana kutembelea sehemu za Manzese. Nikiwa Arusha makazi yangu ni Ngarenaro. Na nikiwa Moshi nastarehe zaidi nikiwa Majengo”, alimhakikishia. “Sababu hiyo ndiyo iliyonifanya niishi katika hoteli hii ndogo badala ya kubwa kama Mwanza Hoteli”.

Maneno hayo yalimaliza ubishi wa Sofia. Usiku uliofuata uliwakuta Kirumba katika chumba chake.

Chumba kilikuwa katika hali ambayo Proper aliitarajia. Raslimali za muhimu zilikuwa kitanda kikuukuu chenye godoro kukuukuu la sufi ambalo halikuwa na hadhi ya kuitwa godoro pia kulikuwa na sanduku, meza na sufuria mbili tatu zilizonuna kwa uchafu. Ambacho Proper hakutegemea ni ukarimu wa kunguni na mbu walikuwa huru katika chumba hicho. Walimlaki moja kwa moja bila kumpa fursa ya kujipumzisha.

Yote hayo Proper alilazimika kuyastahamili eti kwa sababu amependa, kumbe ni uhitaji tu. Alikusudia kujisetili akisubiri siku kuu ili atimize lengo lake. Hakuna askari wala mpelelezi yeyote ambaye angefikiria kumtafuta pale. Alitarajia kuwa wangeweza kumsaka katika mahoteli makubwa na kwenye vitongoji vikubwa vikubwa, siyo kwa malaya wa chini kama Sofia anayeishi maeneo yaliyosahaurika.

Siku mbili zikapita bila ya kitu chochote cha kawaida kutokea. Proper alishinda ndani akijisomea vitabu, nae Sofia alijishughulisha kutafuta vyakula na vinywaji. Sofia alikuwa akipewa pesa zilizozidi mahitaji yake ya kawaida. Proper alikuwa amemruhusu kununua mavazi mapya. Hali hii ngeni ilimuinua Sofia, akawa anapepea mfano wa kishata. Nafasi yoyote iliyojitokeza, ilitumiwa kufanya mapenzi. Sofia alijitia kila aina ya juhudu kumridhisha Proper. Lakini hakuweza kuutambua unafiki wa Proper. Akazidi kutekwa akili na vitendo vya mtu huyu. Hata hivyo sauti nyingine ilimnong’oneza atahadhari.

Jioni ya siku ya tatu, mambo yalianza kwenda mrama. Sofia alirejea kutoka mjini na gazeti mkononi. Alimfuata Proper aliyelala chali kitandani na kumfungulia ukurasa wa tatu ambao ulikuwa na picha sita chini ya kichwa cha habari kilichosema;

“TANGAZO LA POLISI.

JIHADHARI NA MTU HUYU- MARA UMWONAPO IARIFU POLISI. ANATAFUTWA KWA MAUAJI YA WATU WENGI NA ANAWEZA KUUA WAKATI WOWOTE, KUWAMAKINI”.

Proper alisoma haraka haraka. Kisha alizitazama picha hizo kwa makini. Moja ilikuwa yake halisi. Zilizosalia zilikuwa picha za kuchora. Zilikuwa zimechorwa kwa namna mbalimbali kuonyesha nywele zote; nyingine ilichorwa kuonyesha madevu mengi, nyingine kavaa miwani na kadhalika. Ni moja kati ya picha hizo ambayo ilikuwa imefanana kikamilifu na sura aliyokuwa akiitumia sasa. Alijitia utulivu na kumgeukia Sofia na kumwuliza kwa upole, “Ni hii tu uliyoiona habari ya maana katika gazeti lote”.

“Hapana. Nilitaka kukuonyesha huyo mtu. Naona mmefanana naye sana”.

“Tumefanana!” Proper alijitia kushangaa. “Mimi nafanana na huyo anayetafutwa kwa mauaji? Haiwezekani”.

“Mmefanana sana Beka. Nadhani ni wewe”.

“Usiwe mjinga Sofia, mimi siwezi kuwa muuaji”.

“Kweli kabisa. Hata yule rafiki yangu aliyekuja hapa jana amesema hivyo. Labda ungesoma hapa chini uone”.

Proper alianza kusoma kifungu hicho kilichoandikwa kwa herufi za mlazo.

Mtu huyu ni hatari sana, anatakiwa mapema mno. Zawadi nono ya shilingi laki nne itatolewa kwa mtu yeyote atakayewezesha kukamatwa kwake. Inasemekana kwa sasa yuko mjini Mwanza au mikoa ya jirani. Unaonywa tena kujihadhari naye…

“Ni wewe Beka?”, Sofia alisisitiza huku akimkazia macho.

“Siyo mimi”. Sauti ya Proper ilikuwa ya utulivu mkubwa.

“Kwani unanionaje mimi, naweza kuwa muuaji?”.

“Hapana, lakini hiyo picha inaonyesha ni wewe”.

“Achana na picha hii. Huoni kama huyu amechorwa tu? Usiwe msichana mjinga Sofia. Mimi ni mtu ninayejiheshimu sana huko kwangu. Wasichana kama wewe, wazuri zaidi yako, ninao kama ishirini hivi ambao wanalipwa mshahara mzuri kutoka katika mfuko wangu. Na wanaume wengi wasiopungua mia, wote wako chini yangu, wote wananiheshimu. Au kwa vile niko nawe katika chumba hiki hafifu ndipo umefikia hatua ya kuniita mwuaji?”.

“Sivyo mpenzi, ila…”

“Ila…”

“Nina mashaka yule rafiki yangu amekwenda kutoa taarifa polisi. Laki nne siyo pesa ndogo”.

“Polisi. Akiwaleta hapa, wakinikuta mimi watanitia ndani kufunza adabu. Ondoa hofu. Sofia njoo kitandani, tujipumzishe nikudokeze jambo. Lete ulimi tufurahi”.

Sofia alisogeza shingo. Hakutarajia radi iliyompiga ghafla. Lilikuwa pigo kali jepesi ambalo lilitua katika shingo na kulivunja kabisa. Sofia hakujua kapigwa na nini. Wala hakuona ugumu wa kufa. Alianguka chini na kupapatika kwa muda, kisha akakata roho.

Proper alifanya kazi haraka haraka. Aliuzoa mzoga wa aliyekuwa Sofia na kuulaza kitandani. Akaufunika vizuri kwa shuka. Kisha alikusanya vifaa vyake na kutoka nje. Giza lilikuwa limeanza kutanda. Hakuona haja ya kujificha kama alivyotegemea. Aliifuata polepole barabara iendayo mjini. Alipofika Mabatini, alisimamisha taksi na kuingia ndani.

Dereva taksi alikuwa kijana wa Kiarabu mwenye ndevu nyingi. Alimsalimu Proper kwa adabu, kisha akamuuliza wapi anataka kwend. Proper hakumjibu kwa maneno bali kwa kitendo fulani. Aliudidimiza mkono wake katika begi lake na kutoa bastola yake. Aliigandamiza ubavuni mwa kijana huyo.

“Ukifanya ujinga utapoteza maisha. Nataka wewe na gari hii mfuate matakwa yangu. Haya endesha mpaka nitakapokwambia wapi tuelekee”.

Huku akitetemeka, macho yakiwa yamemtoka, kijana huyo alilitia gari moto na kuliondoa taratibu huku mapigo ya moyo yakimwenda kasi kwa hofu.

Nuru alichelewa kufika nyumbani. yeye na wenzake Walikuwa wamechelewa kutoka kazini ili kukamilisha shughuli zote za maandalizi ya ugeni mkubwa. Ilikuwa saa mbili kasoro dakika chache alipojikuta mbele ya mlango wa nyumba yake, akiutia ufunguo katika tundu la kitasa cha mlango wa chumba chake.

Kabla ya kuanza kufungua kitasa cha mlango, alikuwa ameyatupa macho yake pande zote kwa matumaini labda ya kumwona tena yule mzee tajiri. Hakuwepo. Bila shaka alikuwa amesubiri kwa muda alipoona hatokei akaondoka zake, akadhani. Hata hivyo Nuru hakujua kama angependa kumwona tena mzee yule au la. Ingawaje Nuru alikuwa ametunukiwa zawadi ya mkufu wenye thamani kubwa, na ahadi ya kutembea duniani, lakini Nuru hakujua kama angependa kumwona tena au la.

Alichofahamu ni kwamba mashaka hayo yalikuwa yameanza pindi Duncan alipomwambia; “Unajua kidogo nina wivu… Tafadhali usiruhusu zawadi hizi zikununue …” Hakujua kwa nini, lakini maneno hayo yalikuwa yamemburudisha zaidi ya zawadi yenyewe. Hakuna kitu alichohitaji zaidi ya kuonewa wivu na Duncan. Alihisi kama wivu huo ulikuwa mwanzo wa safari mpya, ndefu, ambayo hakujua mwisho wake. Safari ambayo aliona itakuwa ya kusisimua zaidi ya ile ya Ulaya Magharibi aliyoahidiwa na yule mzee tajiri. Alasiri nzima Nuru alishinda kwa furaha kubwa kinyume cha alivyokuwa kabla ya kuzungumza na Duncan.

Alikuwa bado na furaha hiyo alipoingia ndani na kulipupa begi lake juu ya meza. Mkono wake wenye uzoefu ulipenya kiza na kuifikia swichi ya umeme. Akaibonyeza. Nyumba nzima ikamezwa na nuru ya rangi ya blue iliyokuwa ikitoka katika taa zake. Akavuta swichi ya kamba na kuifanya nuru hiyo ya blue itoweke na nyeupe kuchukua nafasi yake. Ni katika nuru hiyo alipoweza kumwona mgeni wake aliyekuwa ameketi kwa utulivu juu ya kochi akimtazama Nuru, uso wake ukaonekana kama wa mtu anayetabasamu.

Nuru alishtuka karibu akimbie. Hakujua ulikotokea uwezo ambao ulimfanya asite kukimbia na badala yake afoke kwa sauti ambayo ilitoka kama mnong’ono. “Nani wewe? Na umeingiaje humu?”.

Mgeni huyu alicheka kidogo. Kisha alimwuliza kwa upole, “Umenisahau mara hii? Hukumbuki jana tu tulikuwa wote humu humu ndani na tukapeana zawadi? Mkufu huo uliovaa…”

Nuru hakuyaamini macho yake. Aliyekuwa mbele yake hakuwa yule mzee wa jana. Alikuwa mtu mwingine kabisa mwenye sura nzuri, yenye dalili ya ujana. Zaidi, hakuwa na jicho moja wala mguu mbovu. Alikuwa na viungo vyake vyote, bila kovu wala dosari yoyote. Alivaa suti ya kijivu ambayo ilimkaa vyema mwilini. Haiwezekani Nuru aliwaza. Huyu hawezi kuwa yule mzee wa jana.

Mgeni huyo alikuwa akiyasoma mawazo ya Nuru. “Huniamini siyo”, aliuliza. “Lazima Lazima ufahamu kuwa katika dunia hii kuna watu wa kila aina. Wako wanaoishi maisha ya kawaida, na kuna wanaoishi maisha yasiyo ya kawaida. Wengine wanalazimika kutumia sura nyingi na majina mbalimbali, ili waweze kuishi. Mimi ni mmoja wao. Jana nilikuwa mzee mkongwe, mwenye chongo, leo ni kijana mzuri anayekufaa. Au sio?” alihoji akicheka.

Ni kicheko chake ambacho kilimfanya Nuru aafikiane naye moja kwa moja. Kilikuwa kile kile cha jana, kicheko ambacho kwa namna moja au nyingine hakikuwa cha kawaida. Kilikuwa kama kinachoficha uovu na ukatili fulani. Jambo ambalo lilimfanya Nuru apatwe na hofu.

“Sasa unataka nini?” Nuru alijitahidi kuhoji akifoka. “Sidhani kama nahitaji uhusiano na watu wenye tabioa kama zako. “Chukua mkufu wako uondoke”.

“Usijisumbue kuuvua”, mgeni huyo alisema. “Hiyo ni zawadi yako. Bado nakuopenda”, aliendelea. “Nina kazi ndogo sana yenye faida kubwa sana. Lakini kabla ya kazi hiyo nitapenda unieleze kikamilifu ni nani mliyekuwa mkizungumza naye leo hii chumbani kwake, pale hotelini?”.

Nuru hakutaka kuendelea kuzungumza na mtu huyu. Aliona kama kwa namna moja ama nyingine mtu huyo angemletea madhara au maafa. Kwa nini alazimike kutumia sura za bandia? Na aliingiaje humu ndani? “Sikia”, Nuru alifoka tena kwa nguvu. “Sitaki kuzungumza nawe. Toka haraka kabla sijakuitia polisi”.

“Naona hujanifahamu vizuri kuwa mimi ni nani”, mgeni huyo alisema huku akiinuka na kumsogelea Nuru. Ndiyo kwanza Nuru akaiona bastola ambayo ilikuwa wazi mkononi mwake ikimwelekea. “Endapo utawaita polisi, watakachofanya ni kuizoa maiti yako na kuipeleka hospitali ya Maunt Meru. Sasa utayajibu maswali yangu yote kwa adabu”.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Nuru kuelekezewa bastola. Ingawa amesoma matukio ya aina hiyo mara nyingi na kuona katika picha za sinema jinsi wasichana wenzake wanavyouawa kwa bastola, hakuona au kuamini kuwa siku ya leo ilikuwa ya mwisho katika maisha yake. Aliuona kama mchezo au mzaha wa kuchukiza. Hivyo aliruka kando na kuinua stuli ndogo ambayo aliirusha kwa nguvu kuelekea mgeni huyo. Ikamshangaza kuona mgeni huyo akiidaka kama mchezo na kuitua chini kwa utulivu. Wakati huo huo Nuru alipokea kofi zito ambalo lilimpeleka chini. Alipojaribu kusimama alirejeshwa chini kwa kofi jingine zito. Maumivu yalikuwa makali, lakini Nuru alishangaa kuona machozi yakigoma kumtoka.

“Sipendi kukuumiza bibie”, mgeni huyo alisema huku akimwinua Nuru na kumkarisha juu ya kiti. “U msichana mzuri sana. Sura yako haifai kuharibiwa kwa makofi. Keti tuzungumze kama watu wenye busara”. Alimazia akairudisha bastola yake kwenye mfuko wa koti na kukirudia kiti chake. “Napenda uniambie ni nani huyo kijana anayeitwa Duncan ambaye alikuchukua na kukupeleka chumbani kwake?”.

“Simfahamu vizuri”, Nuru alijibu.

“Anafanya kazi hapo hotelini?”

“Hapana. Ni mgeni”.

“Alifika lini?”

“Ana muda mrefu kidogo”.

“Alisema nini juu ya kidani hiki nilichokupa?”.

“Hakusema kitu isipokuwa alikisifia tu”.

“Kuna wakati mlikiondoa kidani na kukiweka kando. Mlifanya hivyo kwa ajili gani?”

Nurua akaanza kurejewa na hasira. “Kwani sina haki ya kukivua? Tulikiondoa ili tufanye mapenzi. Tuliona kinatusumbua”, Nuru alisema kwa dhamira ya kumuudhi. “Kama hupendi ondoka nacho sikihitaji”.

Mgeni alifikiri kidogo kabla ya kuuliza tena. “Una hakika huyo Duncan alipokitoa kidani hakuzungumza chochote akipeleleza juu yangu au juu ya kidani hiki?”.

Nuru hakukumbuka kitu hicho. Alichokumbuka ni kwamba katika maongezi ya jana sauti ya Duncan ilikuwa ya kawaida bila dalili yoyote ya kujua mengi juu ya mkufu huo.

Mgeni aliyasoma hayo katika uso wa Nuru. Akaridhika. “Wala hakukuonya usikivae tena?”, aliuliza.

“Aliniambia nikurudishie. Kwa hiyo chukua uondoke. Nataka kulala mapema”, Nuru alifoka.

“Kweli”, mgeni huyo aliunga mkono. Akacheka kidogo kabla ya kusema. Bi. Nuru tafadhali yasahau yote yaliyopita kati yetu. Ulikuwa mzaha tu. Nadhani utanisamehe nikikupa hii? Alitia mkono wake mfukoni na kuutoa. Ulikuwa umeshikilia kitita cha pesa. Hazikuwa chini la laki mbili. “Tafadhali pokea”.

Pesa ni pesa. Zina nguvu na starehe yake. Zinashawishi. Lakini hizi zilimtisha Nuru. Kuzipokea ilikuwa kama kupokea nauli ya kuelekea kuzimu. “Mara ngapi niseme kuwa sihitaji chochote kutoka kwako?, Nuru alifoka tena. “Ondoka na pesa zako. Zinanuka”.

“Zipokee. Kama hupendi ni juu yako. Lakini hizo sikupi bure. Ni malipo kwa kazi ndogo ambayo lazima utaifanya kesho mkutanoni”. Akaingiza tena mkono wake mfukoni na kutoa kopo la poda ambalo lilikuwa limefungwa katika mfuko wa nailoni. Hii ni zawadi yako nyingine. Poda ya aina yake. Wewe utakuwa mtu wa pili katika nchi hii kuitumia. Hata hivyo utalazimika kuitumia kwa uangalifu sana ukifuata maelekezo yangu. Unanisikia?”.

Nuru alitikisa kichwa kukubaliana na mgeni wake.

“Nisikilize kwa makini. Kesho utakwenda na poda hii kazini, ikiwa ndani ya pochi yako. Utakapowadiwa wakati wa kuwapatia wageni vinywaji ndipo utakapokwenda bafuni na kufungua poda hii. jipake ya kutosha usoni na mikononi. Kisha utarudi na kuanza kuwahudumia hao waheshimiwa. Hakikisha mikono yako inagusa karibu kila kikombe. Sawa?”.

Hofu na mshangao vilikuwa katika macho ya Nuru. Alimtazama mgeni wake kwa hofu ingawa hakuuliza chochote. Mgeni alimtoa hofu kwa kucheka kidogo.

“Naona una wasiwasi. Usiwe na haja ya kuogopa kitu. Matokeo ya kazi hiyo yatakuwa mzaha mwingine wa kusisimua sana. Viongozi kadhaa watasinzia kwa dakika mbili tatu bila sababu. Litakuwa jambo la kuchekesha kidogo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya dunia. Nitafurahi sana. Baada ya hapo utarudi zako kuchukua laki zako mbili uzifanye upendavyo. Halafu tutapanga mipango ya baadaye. Nitakuwa kijana sasa. Siyo mzee asiyeweza kitu. Unasemaje?”.

Nuru hakuwa na jibu. Hofu zilizidi kujengeka katika fikra zake. Hofu ambayo ilimfanya azidi kumchukia mtu huyu aliyekaa mbele yake. Alitamani amfukuze tena. Lakini hakuona kama ingesaidia. Hivyo alitulia kimya akimsikiliza, na kisha kuhamishia macho yake juu ya kopo la poda na laki mbili zilizolala juu ya meza.

“Nakukumbusha tena, Utajipaka uwapo mkutanoni tu. Dakika moja kabla ya kuanza kuhudumia”, alikumbusha.

“Nani aliyekwambia kuwa nitafanya kazi yako hiyo ya kishenzi?” Nuru alifoka, Ondoka na vitu vyako vyote. Nakuomba kwa mara ya mwisho. Au nitawaita polisi”.

Ndipo Nuru alipoiona hasira kali katika macho ya mtu huyo. Ilikuwa hasira baridi. Hasira ya kutisha. Ilijitokeza katika sauti na tabasamu lake aliposema kwa upole. “Utaifanya. La sivyo, nitakuua hadharani. Nitakuwa pale pale mkutanoni nikikutazama. Fanya chochote kinyume cha matakwa yangu na utaona nitakavyokufanya. Utajuta kuzaliwa na kujutia kifo

chako. Kitakuwa kifo cha kinyama kuliko unavyoweza kukadiria jaribu kukiuka uone”.

Shetani asingeweza kumtisha Nuru zaidi ya sauti hii: Ilikuwa sauti iliyoleta ukweli katika nafsi ya Nuru bila ya mzaha. Sauti iliyofanana na mauti yenyewe.

Ndio kwanza hofu ikautoka moyo wa Nuru. Akafumba macho na kuruhusu machozi mengi yamtoke. Alipoyafumbua mgeni wake hakuwepo. Alivyoondoka hajui. Pesa na poda vilikuwa mezani vikimsubiri. Akavuta pumzi na kuzishusha.

Sasa wakati ulikuwa umewadia. Umati mkubwa wa wananchi ulikuwa umekusanyika mbele ya hoteli ya Maunt Metru kiasi cha kulifanya eneo zima liwe kama msitu wa mitu yenye uhai wa rangi mbalimbali. Wake kwa waume, wazee kwa vijana walisimama juani kwa utulivu, kando ya barabara ya Moshi- Arusha kutoka mjini kati hapa hotelini. Kila mmoja alikuwa na shauku kubwa ya kuwaona viongozi hao ambao walitarajiwa kuwasili wakati wowote.

Kila mmoja alikuwa na sababu zake zilizomfanya asitahamili ukali wa jua na kuendelea kusubiri. Wengi walikuwa wameitikia wito wa Serikali iliyowataka kujitokeza kwa wingi kuwapokea viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika. Baadhi walifika eneo hilo kwa kufahamu kuwa ilikuwa fursa pakee ya kufika kuwaona ana kwa ana watu mashuhuri kama hawa ambao huwasoma kupitia magazeti na kuwasikia katika taarifa za habari za redio na televisheni. Pia walikuwepo wananchi ambao shauku yao ilikuwa kuwaona viongozi fulani tu baada ya kuzisikia sifa zake nyingi redioni. Kadhalika walikuwepo watu si haba ambao walikuwepo kwa jukumu la kuhakikisha usalama wa viongozi na wananchi hao.

Mtu mmoja tu alikuwepo kwa dhamira tofauti. Yeye alifika kwa ajili ya kushuhudia vifo vyao. Mtu huyo alipofikiria mshangao ambao utawapata wananchi baada ya kuwaona viongozi wao wakianguka mmoja baada ya mwingine, alichekelea kimoyomoyo. Kufa hadharani kama mzaha! Aliwaza kwa furaha. Kwa mara ya kwanza redio zote duniani zitangaze habari ya kusisimua. Magazeti yataripoti habari yenye moto. Televisheni zitatangaza kitu kinachostahili. Dunia itashangaa, ulimwengu utaduwaa. Litakuwa jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya dunia. Kwa mkono wake, atakuwa ameusimamisha mkondo wa historia ya Afrika. Atabadili historia! Furaha iliyoje aliwaza.

Na kwanini wasife? alijiambia. Kwanini ilihali kati yao kuna walioua wenzao na kusababisha madimbwi ya damu za watu wasio na hatia katika nchi zao kabla ya kupokonywa madaraka? Kwanini wasife hata wale ambao walipewa kura na wananchi lakini wamewasaliti kwa kusahau shida za watu hao na badala yeke ni wao pekee wanaonenepeana na kufura matumbo? Kwanini wasife hata wale ambao japokuwa hawatumii vyeo vyao kujaza matumbo bado wameng’ang’ania madaraka pasipo nia yoyote ya kuwaachia wengine madaraka nao watawale?. Wana haki ya kufa. Wote na kwa pamoja! Hadharani.

Wakati akiwaza hayo, Proper alikuwa katika umati wa watu waliozunguka hoteli ya Maunt Meru kama raia yeyote mwema. Macho yake yalikuwa wazi na makini kuutazama kila uso kwa makini. Nyuso nyingi alizoziona, uzoefu ulimuonyesha kuwa ni wapelelezi. Bila shaka walikuwa na silaha zao tayari, na walikuwa wakimtafuta yeye. Endapo wangemwona alijua kuwa wangemuua kwanza na kumsaili baadaye. Ndiyo alikuwa katika eneo la hatari. Hata hivyo hakuwa na hofu yoyote. Alikuwa na hakika kuwa wasingeweza kumpata. Wao walikuwa wakmtafuta Proper wanayemfahamu wakati yeye sasa alikuwa Proper mwingine ambaye hata mama yake mzazi aliyemzaa asingeweza kumfahamu. Zaidi, walikuwa wakimtafuta mtu mwenye bastola au bomu la kurushwa kwa mkono wakati yeye Proper alikuwa mikono mitupu kama raia wengine. Ama, kwa ulinzi wao wote madhubuti, watashangaa watakapoona viongozi wao wakianguka mmoja baada ya mwingine.

Hata hivyo hofu kidogo ilikuwa ikipenya katika moyo wake. Ikawa mara yake ya kwanza kuona hofu, na ikamshangaza zaidi ya ilivyomtisha. Anahofia nini? Nuru atamwangusha? Hilo halikumtia hofu. Alijuwa kuwa alikuwa amemweka Nuru katika kona ambayo asingeweza kuponyoka. Kidogo alimhukumu kwa kujuwa kuwa atakufa na viongozi hao mara baada ya kuwahudumia. Alimsikitikia zaidi Nuru kwa kujuwa kuwa kifo chake hakitapewa uzito wowote japo ni msichana mzuri mno. Itakuwa sawa na inzi aliyekufa pamoja na tembo.

Hofu iliendelea kuutekenya moyo wa Proper. Anaogopa nini? Alijiuliza tena. Kuna nini cha kuhofia ? Au amefanya makosa kuja hapa? Pengine angekaa mahala fulani akisubiri redio zimletee habari hiyo ya kusisimua? Upuuzi ulioje! Angepata wapi fursa nyingine ya kushuhudia kitendo kama hiki cha kihistoria? Pindi marais zaidi ya kumi, mawaziri zaidi ya ishirini na makatibu wasio na idadi wakifa kwa kulalia meza zao, mmoja baada ya mwingine, nani atakayehangaika kumtafuta mtu wa kawaida aliyeko katika umati wa watu wa kawaida?

Zaidi ya hayo, nani atakayefaulu kumpata? Wakati wao watakapokuwa wakiwafikisha marehemu katika hospitali ya Maunt Meru yeye atakuwa Namanga akitafuta njia za mkato. Wakati habari zitakapoanza kutangazwa yeye atakuwa angani akitokea Nairobi kuelekea New York ambako atanunua gazeti la TIMES na kujua nani na nani walikufa katika mkasa huo, nani mwenye bahati ya mtende aliyeponea chupuchupu. Suala la nani atachukua madaraka baada ya nani na atafanya nini zaidi ya nani hili hakuona kama linamhuru.

Mawazo ya Proper alikatishwa na gari la kwanza ambalo liliwasili. Lilikuwa na askari wengine kadhaa wenye vyeo vya juu. Kati yao Proper alimtambua Inspekta Kombora. Alionekana kama ambaye hakuwa amepata usingizi wa kutosha kwa siku mbili tatu hivi. Proper akamhurumia kwa kujua kuwa muda si mrefu atapata mshangao mkubwa katika maisha yake, mshangao utakaomfanya apelekwe hospitali na marehemu wengine, akiwa na ugonjwa wa moyo baada ya kuzimia kufuatia uzito wa tukio hilo.

Magari yakaendelea kufika. Viongozi mbalimbali walitelemka kutoka kwenye magari hayo huku wakishangiliwa na wananchi. Waliwasalimia wananchi kwa kuwapa baadhi mikono, kisha waliingia hotelini ambamo tafrija kubwa ilikuwa imeandaliwa ikiwasubiri.

Sasa! Proper alianza kuwaza moyo ukizidi kumdunda.

Nuru alikuwa mmoja wa watu waliondaliwa kwa ajili ya kuwapokea viongozi hao na kuwaongoza katika viti vyao. Aliifanya kazi hiyo kama kawaida huku akifanya kila aliloweza kuficha hofu na wasiwasi vilivyokuwa katika roho yake kiasi cha kumfanya atetemeke kidogo. Hata hivyo shamlashamla na vigelegele vilivyokuwepo vilisaidia kuifanya hali yake isishukiwe na mtu yeyote.

Hatimaye ukawadia wakati ambao Nuru alikuwa akiuogopa kuliko nyakati zote. Wakati wa kuanza tafrija. Sasa alitetemeka bila kipingamizi. Ilimshangaza kwamba hakuna mtu yeyote aliyeonekana kumshuku hadi sasa. Akayatupa macho yake nje, katika umati ya watu waliojazana mbele ya hoteli akisubiri viongozi watoke. Kama livyotegemea aliyaona macho ya yule mgeni wake wa jana akimtazama na kumkumbusha adhabu ya kifo inayomsubiri endapo hatafanya kama alivyoamriwa.

Hakuwa na la kufanya zaidi ya kwenda katika chumba chao cha maandalizi ambako pamoja na mkono wake kutetemke alitoa mfuko wake na kutoa ile poda, akaifungua karatasi ya nailoni na kuitazama kwa makini. Ilimshangaza kuona ilikuwa poda ya kawaida MALAIKA ambayo hutengenezwa na kimojawapo cha viwanda vyeti kilichomo katika mji wa Tanga. Hii kweli inaweza kufanya miujiza anayotaka ifanyike yule mwendawazumu? Nuru alijiuliza.

Ifanye, isifanye kwa hali yotote Nuru aliona kuwa alikuwa akifanya kosa kubwa sana katika maisha yake kwani kutii matakwa ya mtu yule wa ajabu. Maisha ya viongozi yana thamani kubwa. Kiongozi wa nchi ndiyo alama ya nchi yenyewe. Mamilioni ya watu yanamtegemea kiongozi. Vipi yeye Nuru, mtu asiye na lolote wala chochote ashiriki katika mzaha wa kuwafanya watu hawa wapumbazike kwa dakika kadhaa? Na vipi iwapo kuna madhara zaidi ya hayo aliyodai yule mgeni? Ni hayo yaliyomtia hofu.

Hata hivyo alijikuta hana njia zaidi ya kutii amri ile. Akaitoa poda hiyo na kujipaka kama alivyoelekezwa. Ikamshangaza kuona hata harufu ilikuwa ya kawaida, kama zilivyo poda za kawaida. Kisha akarejea ukumbini na kuanza kutoa huduma kwa viongozi. Muda si mrefu kazi ikawa imekwisha. Viongozi walitulia wakila na kunywa vinywaji vyao kama kawaida. Wawili watatu walizungumza na kutaniana. Kisha tafrija ikawa imekwisha. Wakaanza kuinuka kuyaendea magari yao, wananchi wakawashangilia.

Halikuwepo jambo lolote lisilo la kawaida lililotokea.

Ni hilo tu Nuru? alijiuliza kwa furaha. Akajidharau kwa kuhofia jambo lisilo na madhara. Bila shaka ulikuwa mzaha mwingine wa yule mtu. Kama ni mzaha, hata zile laki mbili zitakuwa mzaha pia? akajiuliza.

Haiwezekani! Proper alifoka kimoyomoyo huku akishindwa kuyaamini macho yake alipowaona viongozi hao, wote wakitoka na kuyaendea magari yao ambayo yaliwapeleka katika jumba la mikutano AICC. Haiwezekani kabisa. Sumu iliyokuwemo katika poda ile ilikuwa kamili na hali ambayo ingetosha kuua kwa harufu tu. Kwanini wasidhurike? Au ni kweli kuwa wengi wao wanalindwa na miti shamba yenye nguvu? Lakini kama kweli wana uchawi mbona mara nyingi wanakufa kwa kitu kidogo kama risasi ya bastola? Kama uchawi vipi hata yule msichana mdogo Nuru asidhurike? Haiwezekani! Lilifanyika jambo. Nuru atalijutia jambo hilo alilofanya! Proper aliwaza huku akiyasaga meno yake kwa hasira.

Mtu mmoja tu katika umati huo aikuwa akiyatazama yote hayo kwa furaha, tabasamu pana likiwa usoni mwake. Akiwatazama Nuru na Proper kwa zamu, Aliyaona mawazo yao. Tabasamu lake likageuka kuwa kicheko.

Mtu huyo aliitwa au alijiita Duncan.

“Utakufa kifo cha kinyama kuliko vifo vyote vya kinyama ambavyo vimewahi kutokea na wewe kuvisikia katika historia ya dunia. Na kabla ya kifo chako utanieleza ni kitu gani ulifanya hata poda ile ikashindwa kuwaua wale mnaowaita viongozi.

Kuwaua! Ndio kwanza Nuru akafahamu jukumu gani alikuwa nalo. Kwa muda akasahamu maafa ambayo yalikuwa mbele yake, badala yake alijisikia faraja kuwa mkono wake haukuwa umefaulu kuhusika katika kitendo cha kishenzi kama kile, kama kingetokea. Angewatazamaje binadamu wengine? Angeishije katika dunia hii na doa la damu nzito ya viongozi wa nchi za Afrika.

“Ulifanya nini wewe malaya?”.

Nuru akakumbuka kumtazama. Kila kitu kilikuwa wazi katika macho hayo. Yalitisha kama macho ya simba aliyejeruhiwa, yakitangaza mauaji. Hakuwa na chochote mkononi, bastola wala kisu. Lakini Nuru alijua mikono yake iliyokakamaa, ikitetemeka kwa hasira ilitosha kumuua kwa pigo moja tu. Tangu tafrija ilipokwisha Nuru alikuwa na wasiwasi. Alijua kuwa jambo moja au jingine lilikuwa limeenda kinyume cha matakwa. Alihofia sana kurejea nyumbani. Hivyo, waliporuhusiwa kuondoka yeye alipita kwa marafiki ambao alizungumza nao hadi saa tatu za usiku. Ndipo aliporudi nyumbani peke yake baada ya juhudi zake za kumshawishi mmoja wao kufuatana naye kutofanikiwa.

Hakushangaa kukuta zile laki mbili hazipo pale alipoziacha. Wala hakushangaa kuona ufunguo ukipenya kwenye tundu la kitasa na kufungua mlango taratibu. Kama alivyotegemea aliingia mtu yule yule akiwa katika sura na umbo la jana. Baada ya kuingia ndani aliufunga mlango kwa nyuma na kumtazama NUru kwa macho yake makali. Hakupoteza muda wake zaidi bali aliyasema yale aliyokusudia kuyasema.

Kwa mara ya kwanza Nuru akaupata ulimi wke na kujitetea kwa udhaifu, “Sikufanya chochote zaidi ya kutekeleza matakwa yako. Na kama nia yako ilikuwa kuwaua watu wale wasiokuwa na hatia basi Mungu hakutaka.

“Unajua hatia wewe?” Proper aliendelea kufoka. “Unasema ulifanya kila nilichokwambia? Ebu ilete poda hiyo niione”.

Nuru alitoa poda hiyo na kumkabidhi Proper. Nae aliipokea kwa uangalifu. Mara akatokwa na ukelele wenye mchanganyiko wa hasira.

“Uliupata wapi uchafu huu?” Proper alifoka.

“Ni wewe uliyenipa”, Nuru akasisitiza.

“Una wazimu”, aliunguruma Proper, “Mimi nikupe takataka kama hii? Poda! iliyotengenezwa hapa hapa!” Akamkazia Nuru macho baridi. “Nakuhurumia sana bibie… Yeyote aliyekupa wazo la kunidhihaki kiasi hiki amekupa wazo la kipumbavu kuliko yote. Utakufa. Na kitakuwa kifo cha kinyama. Naapa. Lakini kabla hujafa utaniambia nani aliyekupa poda hii?”

Nuru akabaki ameduwaa. Nafasi ya hofu kwa muda ikachukuliwa na mshangao. Mtu huyu ana wazimu? Nuru alijiuliza. Ni yeye mwenyewe aliyemletea poda hiyo jana. Wala hakuwa ameigusa jana usiku bali aliiacha pale pale mezani na kulala. Na alipoamka ilikuwa pale pale pamoja na pesa zake.

“Ni wewe uliyenipa. Mimi sikuigusa wala…”

“Vizuri” Proper aliingilia maongezi ya Nuru, “Yaelekea umeamua kunidhihaki. Sasa nitakuonyesha mimi ni nani. Nadhani hujui watu wangapi wamesafiri kwenda kaburini kwa mkono huu. Utawafuata. Utakwenda kuwauliza ili wakufahamishe mimi ni nani”, akasita kidogo akimtazama Nuru. “Umekuwa msichana mzuri sana. Hufai kufa kabla ya kuonjwa tuone kama uzuri huo ni wa nje tu, au hata ndani, hasa baada ya kukupa ule uongo wangu kuwa nilikatwa uume wangu. Nataka ujuwe mimi ni nani”.

Nuru akabaki ameduwaa. Alitamani kupiga kelele lakini sauti ilikuwa kama iliyouhama mwili wake.

“Vua nguo zako zote”.

Bado Nuru alikuwa ameduwaa.

“Nasema vua nguo zako. Au utapenda nizivue mimi? Usitegemee kuvuliwa nguo kistaarabu”, Proper alisema akimsogelea Nuru pole pole. Macho yake yalidhihirisha kila dalili ya unyama na yalimfanya Nuru ashikwe na hofu kubwa hivyo akabaki amekodoa macho.

“Utavua au nikuvue?” Proper alihoji tena mikono yake ikiliendea koo la Nuru na kuanza kuliminya.

“Hatazivua na wala hatavua nguo”, ilisema sauti nyepesi kutoka nyuma yao. Wote wakagauka kutazama. Msemaji alikuwa akitokea bafuni, akawasogelea taratibu sigala ikiwa mkono mmoja, bastola mkono wa pili. Aliwaangalia akitabasamu.

“Heko Bi. Nuru, U msichana shujaa kuliko nilivyotegemea. Umenifurahisha sana kwa kutobabaishwa kwako na huyu mwehu. Poa moyo. Hataweza kufanya lolote la kinyama tena kwako”.

Sauti haikuwa ngeni masikioni mwa Nuru. Ilikuwa sauti ambayo aliizowea sana. Sauti ambayo aliondokea kuihusudu hata akaipenda. Lakini sura na umbile lilikuwa la mtu mwingine asiyemfahamu kabisa. Umbo zuri lenye dalili zote za afya na sura ya kuvutia yenye kila dalili ya ushujaa. Sura ambayo ilioana sana na sauti yake. Kwa Nuru hii ilikuwa enzi yake ya miujiza. Hivyo, kwa kuzingatia alivyoifahamu sauti hiyo alisema pole pole, “Wewe ni Duncan”.

Mgeni huyo akacheka. U msichana shujaa na mwenye hekima sana. Umewezaje kunifahamu kwa urahisi kiasi hicho? Kisha akamgeukia Proper na kusema: “Hata hivyo rafiki yangu huyu ananifahamu kwa jina lingine kabisa. Nililazimika kujigeuza sura na umbile kuwa Duncan ili kumthibitishia jamaa huyu kuwa utaalamu wa binadamu kujibadili si jambo geni katika nchi hii. Kila mtu anaweza. Au sivyo Proper, ambaye wakati mwingine ulijiita Profesa Kimara”.

Proper alijikuta katika wakati mgumu mno katika maisha yake. Mshangao aliokuwa nao ulikuwa mkubwa kiasi cha kutawala hofu na hasira ambayo ilikuwa imeanza kujitokeza. Proper hakupenda kuyaamini macho yake, kuwa kijana huyo mwenye bastola mkononi, mwenye tabasamu la dhihaka usoni, alikuwa Joram Kiango mtu ambaye aliamini kuwa alikufa kitambo. Hivyo, aliondoa mikono yake kutoka shingoni mwa Nuru na kukirudia kiti chake alichokuwa amekalia.

“Haiwezekani. Huwezi kuwa Joram. Yeye alikufa kitambo kwa mkono wangu”.

“Alaa! Basi lazima ukubali kuwa amerudi kutoka kuzimu ili akupe salamu zako kutoka huko”.

Proper hakujibu. Wala hakuwa mtu wa kupoteza muda kuwaza kitu kimemfanya Joram kuwa hai hadi sasa. Bila shaka lilifanyika kosa fulani katika mauaji yale ya bomu. Na ni kosa hilo ambalo limempa Joram fursa ya kumshinda na kuharibu mipango yake yote kwa kufikiriwa kuwa hayuko tena duniani. Kwa kadri anavyomfahamu, ni yeye aliyekuwa ameingilia kati baini yake Nuru. Ni yeye aliyefanikiwa kuiba ile poda yake ya sumu na kuweka hii ya kawaida. Huo ndio mtindo wake. Kuharibu mipango madhubuti kwa namna ya dhihaka, kama mzaha. Hasira aliyokuwa nayo Proper kwa Nuru zikamgeukia Joram. Alitamani ainuke na kumrukia. Amuue kinyama kuliko historia ya mauaji ya kinyama duniani inavyoweza kukadiriwa. Amtafune mzima mzima! Alisita kwa kuiona bastola ya Joram ikimchungulia usoni.

Joram alikuwa akiyasoma mawazo ya Proper. Akacheka kidogo kabla hajasema.

“Ndiyo. Nililazimika kufuata mtindo wako wa uoga, kujificha katika sura za bandia ili niweze kupambana nawe vizuri. Dawa ya moto ni moto. Hata hivyo sina budi kukiri kuwa karibu nikate tamaa baada ya kuona siku zinakwisha kabla hujajitokeza kuanza harakati zako za kinyama. Kidogo nihadaike kama Inspekta Kombora na wasaidizi wake kuwa umekimbilia nje ya nchi. Hata hivyo sikukata tamaa. Niliijua njia ambayo ungeitumia kujaribu kuwaua viongozi kama wale ingekuwa kwa sumu ile ile ambayo ulithubutu kuitumia kwangu ukashindwa, lakini ukafaulu kumuua mpenzi Neema”, Joram alinyamaza kidogo kwa huzuni, akakumbuka jinsi Neema alivyokubali kuyapoteza maisha yake kwa ajili yake. “Ndiyo, ulimuua Neema pamoja na watu wengi wasio na hatia”, alieleza Joram.

Akaeleza jinsi alivyolazimika kukaa hotelini, akajifanya mtoto wa tajiri aliyeko Ulaya na kuzungumza na kila mtu, ingawa alizungumza mambo ya kawaida tu bila kutia dalili za upelelezi, lakini alikuwa kazini akimchunguza kila mfanyakazi. Akitazama kwa makini nani angekuwa na dalili yoyote ya kukutana na mtu mwenye tabia za Proper. Hasa nilitegemea kuwa ungewatumia wasichana wazuri”, alisita kidogo kisha akaendea. “Na kwa kuwa Maunt Meru hakukuwa na msichana mzuri zaidi ya dada yangu Nuru, ilinibidi nimtazame yeye kwa makini zaidi. Kidogo nikate tamaa hadi jana nilipomuoa Nuru akiwa katika hali isiyokuwa ya kawaida nikapata matumaini. Kisha nikakiona kidani ambacho ulimpa kama zawadi. Kidani ambacho kina mitambo ya kunasa sauti na kuisafirisha hadi ulipo. Nia yako ilikuwa kusikiliza anazungumza nini na akina nani. Hivyo nilipomshawishi akivue na kumhoji mengi bila ya yeye kujua uliamua kumtisha. Msaada ulionipa haukuwa mdogo. Uliniwezesha kuwa mmoja wenu katika mkutano wenu wa jana wakati ukimpa ile sumu na laki mbili baada ya kumtisha sana. Nilisubiri hadi ulipokuwa umeondoka na binti huyu amelala ndipo niliingia na kuichukua poda ile ya hatari na badala yake nikaweka hiyo ya kawaida ambayo nilinunua kutoka katika duka la jirani”.

Joram akamgeukia Nuru, “Laki mbili zako pia nilizichukua mimi. Ninavyomfahamu huyu nilijua alikuwa akisubiri usafiri pamoja na viongozi kisha arudi hapa na kuzichukua pesa zake. Hivyo, nimezihifadhi mahala ili baada ya shughuli hii iliyobaki uje uzichukue. Ni haki yako kabisa Nuru kwa usumbufu aliokufanyia”, Joram akamgeukia Proper.

“Wewe mshinzi pengine utafurahi kusikia kuwa sumu yako iko katika mikono ya vyombo vya usalama yaani polisi. Niliipeleka huko ili ichunguzwe. Baada ya uchunguzi ikijulikana nchi na kiwanda gani kinatengeneza sumu hatari kama hiyo, suala hili litapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Lazima anayehusika kutengenezwa kwa sumu hiyo aadhibiwe vikali. Wakati huu ambao viongozi wa Baraza la kutunga sheria la Umoja huo wanafanya kila juhudi kupunguza utengenezaji wa silaha za hatari lakini kiwanda hicho bado kinatengeneza sumu hatari kama uliyokuwa nayo wewe, kazi unayo ndugu”, alisema Joram.

Joram alisita kidogo akatoa sigara nyingine akaiwasha. Macho yake yalikuwa yakimtazama Proper kwa umakini wa hali ya juu. Tabasamu lilikuwa limetoweka na hasira kali kupokonya nafasi yake. Hata hivyo, Joram akaongea kwa utulivu, “Dunia haijapata kumwona mwendawazimu mshenzi kama wewe. mtu mwenye roho chafu zaidi ya mnyama. Ni ajabu kuwa huna mkia. Unyama wako umewazidi akina Adolf Hitler na Musoline. Umewazidi hata Nduli Iddy Amin wa Uganda na Bokasa. Hata Voster na Smith hawakufikii. kwa kweli ulistahili kufikishwa mahakamani ili dunia nzima ikuone. Inspekta Kombora na wasaidizi wake watafika hapa baada ya dakika chache. Watapenda kukuchukua mzima na kukufikisha mahakamani. Lakini nimelazimika kuwachelewesha kidogo ili wakifika hapa waikute maiti yako. Ni jukumu lao wao wenyewe kuamua kama watakutupa maiti yako vichochoroni iliwe na mbwa koko au kuifikisha mahakamani. Lakini lazima waikute maiti yako. Niliahidi nitakuua kwa mkono wangu mwenyewe ili kulipa kisasi kwa wote uliowaua kikatili, hasa mpenzi wangu Neema Iddy”.

Proper alianza kutetemeka kidogo, hofu ikamwingia. Ni rahisi sana kuua mtu. Lakini si rahisi kuuawa huku ukitazama. Akailaani bahati yake kwa kutochukua silaha yoyote siku hiyo. Kwa kweli alikuwa hazihitaji. Aliamini marais wangekufa kwa sumu. Na mwishowe binti huyo angekufa kwa mikono mitupu. kidole chake kimoja kingetosha kumwua.

Joram akamgeukia Nuru. “Bibie. Tafadhali toka nje ili nimalize kazi hii. Sipendi ushuhudie mwendawazimu huyu anavyokufa. Kesho jioni utapokea furushi lenye pesa zako zote. Mimi nitakuwa nimeondoka kurejea Dar es Salaam. Hivyo nadhani hii ni kwa heri ya kuonana”.

Nuru hakuinuka. Alikuwa akimtazama Joram kama mtu atazamaye mchezo wa kuigiza katika sinema. Yawezekana huu ukawa mwisho? Mwisho wa ndoto zake zote juu ya Duncan ambaye ametokea kuwa Joram Kiango? Joram ambaye alizisikia sifa zake mara nyingi na kumhusudu kupindukia? Asingependa uwe mwisho. Asingekubali. Mara akaangua kilio. Hakujua kinachomliza.

“Nuru”, Joram alitamka kwa mshangao.

Mtutu wa bunduki yenye nguvu ulikuwa ukiwachungulia kutoka nje kupitia dirishani. Bastola ilikuwa mikononi mwa mtu aliyeufunika uso wake kwa tambara jeusi. Bastola hiyo ilimwelekea Proper. Lakini ingeweza kumpata Joram vizuri zaidi. Aliyeshika bastola hiyo alisikitika kwa kuwa hakuwa amepewa amri ya kumwua Joram. La sivyo, ingekuwa kazi ndogo sana kwake. Hakujua lini ingetokea tena nafasi nyingine nzuri kama hii. Akailekeza vizuri katika paji la uso wa Proper.

                                 *************



                                           VII

“Nuru”… Joram alikuwa akisema tena wakati mlio wa kawaida ulipolipuka chumbani humo. Joram alijirusha chini akampitia Nuru na kuanguka nae sakafuni. Bastola yake ikaelekea mlangoni! Usingizi ambao hakuutegemea ulimpitia papo hapo.

Dakika chache baadaye alizinduka. Alishangaa kujiona akiwa kamkumbatia Nuru kama walivyoanguka. Alipotupa macho katika kiti alichokuwa amekalia Proper alishangaa kuona kitu kama uji ulichanganywa na damu nzito. Baada ya kutazama kwa makini ndipo alipofahamu ni kipi alichokuwa akikishuhudia. Ulikuwa ubongo wa binadamu uliotoka katika kichwa cha binadamu kilichofumuliwa kwa risasi. Yeyote aliyefyatua risasi hiyo alikuwa ameifanya kazi yake kikamilifu. Na hakusahau kuuchukua wa aliyekuwa Proper. Kwanini hakuuchukua ubongo wake pia? Joram alijiuliza. Au waliuacha ili uwe ushahidi kuwa adui yake amekufa? Hakuona kama ingemsaidia. Alikuwa ameapa angemuua kwa mkono wake. Yeyote angemuua alikuwa amemsaliti.

Hasira mpya zikampanda Joram. Akainua bastola yake na kuielekeza katika kifua chake. Akafumba macho. akajiuliza, kwanini apokonywe kazi kulipa kisasi kwa kumuua Proper, mtu aliyemuua mpenzi wake Neema.

“Joram”, sauti ndogo ya kike ikapenya masikioni mwake ikimwonya.

Akafumbua macho na kukutana na macho ya Nuru, yenya machozi na huzuni, ambayo yalikuwa yakimtazama kwa namna ya kusihi na kumbembeleza kama yanavyosema. “Huwezi kufanya hivyo”, Ingawa kwa mdomo hakusema lolote, Joram akajua kuwa asingeweza kujiua. Hakuwa mtu wa kujiua. Akaitupa bastola hiyo chini na kuinuka akitoka zake nje.

“Joram”, Nuru aliita akimfuata.

“Unataka nini zaidi?”.

Nuru alipomfikia alimshika mkono na kumwambia, “Huwezi kuondoka katika hali hiyo Joram. Nataka nikusaidie kukufariji umsahau Neema. Niko tayari kufanya chochote na kupoteza kila kitu mradi uusahau msiba wa ulionao moyoni. Tafadhali nipokee Joram”.

Ilikuwa sauti ile ile ya Nuru. Sauti isiyoweza kupingika. Na alimtazama kwa macho yale yale laini yanayosihi na kubembeleza. Macho ambayo hayangepuuzwa. Nuru alisema huku vidole vyake laini vikiuchezea mkono wa Joram katika hali inayoshawishi na kuchokoza kwa kiwango kisichostahimilika. Umbo lake lilikuwa lile lie lenye kila chemaambacho macho ya binadamu hustarehe kutazama na mikono ikiburudika kuligusa.

“Ndiyo, Joram ni shujaa. Lakini nani aliyesema kuwa ana moyo wa chuma?

TAMATI

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment