MPANGO WA KANDO SEHEMU YA KWANZA
NEW AUDIO

Ep 01: Mpango wa Kando

SIMULIZI YA MPANGO WA KANDO FULL EPISODE
MPANGO WA KANDO SEHEMU YA KWANZA

IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi : Mpango Wa Kando
Sehemu Ya Kwanza (1)
KADRI karandinga lilivyokuwa linazidi kushika kasi ndivyo akili yake nayo ikazidi kuamini kuwa hakuwa katika ndoto tena bali ni kweli alikuwa ameveshwa pingu katika mikono yake na alikuwa ametoka kuhukumiwa kwenda jela kwa miaka mitatu kwa kosa ambalo hata apewe utulivu mkubwa kiasi gani hawezi kulielezea, alishtakiwa kwa jina tofauti kabisa na kosa asilolijua hata kidogo. Alilalamika mahakami pale kuwa huenda amefananishwa na mtu mwingine lakini akaletewa ushahidi uliomuacha mdomo wazi na hapo masikio yakasikia sauti ya muhukumu ikisema kuwa ataenda jela kwa miaka mitatu na adhabu ya viboko kumi na viwili, sita wakati wa kuingia na sita wakati wa kutoka.
Alijaribu kujitikisa tena huenda alikuwa yu ndotoni lakini badala ya kushtuka kutoka ndotoni akashtushwa na maumiuvu baada ya kunaswa kibao na mtu aliyekuwa pembeni yake.
Ajabu yule mtu baada ya kumnasa kibao hakusema neno lolote bali akaendelea kuimba wimbo alioujua yeye mwenyewe katika namna ya kulazimisha kitu asichokiweza.
Baada ya kuimba imba kwa sekunde kadhaa akamgeukia.
“Nimekunasa kibao kwa sababu ulinitikisa nikiwa naimba wimbo wangu mzuri!!” alimweleza kisha kama ambaye hajamaliza ama anayesubiri kujibiwa alimtazama tena na kuzungumza.
“Hii ni mara yako ya kwanza kuja jela?”
“Ndio.. ni mara ya kwanza!!” yule bwana alijibu….
“Oooh! Karibu sana katika ulimwengu, samahani kwa kile kibao nilidhani wewe ni mwenyeji wa huku… naitwa Crispin sijui mwenzangu…” alizungumza huku akiwa anatabasamu.
“Naitwa Chopa!!” alijibu kwa kifupi.
“Doh! Kuna jamaa ana jina kama lako huko jela… sijui ni Chopa na yeye ama vipi. Ipo siku utakutana naye kama umenyeshewa mvua nyingi… aam! Kwani umenyeshewa mvua ngapi?” bwana aliyejitambulisha kama Crispin alimuuliza Chopa.
Chopa asiyejua nini maana ya mvua alibaki kushangaashangaa.
“Hujui mvua ulizonyeshewa jamaa!! Au dharau…”
“Sijaelewa maana ya mvua..” Chopa alijibu kiuoga. Yule bwana alicheka sana, kitendo kile cha kucheka kikasababisha harufu mbaya kutoka katika mdomo wake ianze kumbughudhi Chopa hata kabla hajaingia gerezani bado.
“Mvua ni miaka uliyohukumiwa….”
“Mitatu!” alijibu kwa ufupi.
“Ahaa! Kama ni miaka mitatu basi unaweza ukaonana naye, ujue tupo wengi sana kule hivyo ni ngumu sana kuwajua watu kwa majina….. halafu hata ukionana naye bado haina maana kwa sababu na yeye ni ndaro tu kama mandaro wengine…”
“Ndaro… ndaro ni nini!!”
“Alaa! Najisahau sana najiona kama nazungumza na mkongwe mwenzangu… ndaro ni fala ama mchovu asiyekluwa na sauti na ukiwa ndaro ni rahisi sana kugeuzwa malkia wa selo…” akasita akamsogelea Chopa sikioni na kumalizia, “Ukiwa malkia maana yake unawaniwa na wanaume na atakayefanikiwa anakuoa….”
Maneno haya ya maudhi yalimkera sana Chopa na wakati huo gari lilikuwa limefikia mlango wa gereza.
Bado Chopa alitaka kuamini kuwa ile ilikuwa ndoto lakini ukweli ulikuja pale alipocharazwa viboko sita vya nguvu, ikiwa ni mwanzo wa kuitumikia adhabu yake ya miaka mitatu gerezani.
Adhabu kwa kosa asilolitambua kabisa!!!
Baada ya viboko vile na kisha kupewa mavazi kama mfungwa rasmi, akamkumbuka mchumba wake Carolina, akakumbuka alivyomuona mara ya mwisho pale mahakamani akibubujikwa na machozi kumshuhudia mpenzi wake katika hali ile.
Akakumbuka mambo mengi kati yao, eti mpango wao wa kuoana ndani ya miezi sita mbele ilikuwa imemezwa na utata ule wa ajabu!!
Chozi la uchungu likamdondoka.
Mlango wa selo ukafunguliwa akaingia akiwa mgeni kabisa!!!

______

HALI ya Caro kiafya ilikuwa imedhoofu sana, mama yake alikuwa mtu wa kwanza katika familia kugundua kuwa mtoto wake hakuwa sawa katika upande wa afya ya mwili na mawazo pia. Macho yake alijaribu kuyaficha lakini bado yalionekana kuvimbiana.
Mama yake hakutaka kulilazia damu hili jambo, siku hiyo akamfuata Carolina chumbani kwake. Alimkuta akiwa analia sana na hapo ni punde tu baada ya kuingia akitokea alipotokea.
Mama alimfuata na kumkumbatia begani, akamfuta machozi na kisha akamuuliza nini kinamkabili.
Hii haikuwa mara ya kwanza kumuuliza swali hili tangu amuone akiwa katika hali ya sintofahamu, lakini siku hii alitaka majibu ya ukweli.
“Caro mimi ni mama yako, hakuna mwanamke yeyote hapa duniani aliyeupitia uchungu wa kukuzaa wewe Caro ni mimi tu! Zungumza na mimi binti yangu, sema mama anakusikiliza!!” mama aliongea kwa sauti iliyojaa hekima na upole sana kwa mwanaye.
Ni kama sauti ya mama ilizidisha uchungu kwa binti yake, Caro akaangua kilio kikubwa ikawa kazi ya mama kumbembeleza hadi akatulia.
“Mama! Mama…. Chopa wangu mama…. Chopa wanguu….” alizungumza huku akiugulia kwa sauti iliyotawaliwa na kilio.
“Chopa… Chopa amefanya nini tena….. ” alihoji mama yule mtu mzima.
“Chopa amefungwa mama, wamempeleka jela miaka mitatu leo mama.. leo hii Chopa amefungwa!” alishindwa kuzungumza kikawaida alikuwa anazungumza huku analia.
Mama alizidi kumtuliza na hapo Caro akaelezea juu ya mkasa uliomkumba Chopa, mkasa usioelezeka na kueleweka kwa sababu hata Caro mwenyewe hakuweza kuuelezea vizuri!!!
Mama alimpooza lakini ilikuwa sawa na bure!!
Siku hii ikawa mbaya sana kwa caro. Ikafuata siku ya pili na kuendelea, hali yake ikazidi kuwa mbaya. Hakuwa akienda kazini tena…. alikuwa ni mtu wa kulia tu ama kubaki ameduwaa kama mwenye utindio wa ubongo.
Japokuwa mama mtu hakuwahi kumuona Chopa hata siku moja, kila siku akiishia kupewa ahadi na mwanaye huyo lakinui alikiri kuwa huenda mwanaye alikuwa katika mikono salama sana. Kwa sababu alikuwa anapata afya na alikuwa mwenye furaha na amani mara zote.
Hivyo kitendo hiki cha Chopa kushtakiwa na kisha kupelekwa gerezani hakika kiliondoka na vyote alivyokuwanavyo!!
Hali ilipofika pabaya ikalazimika baba mtu apigiwe simu akiwa Mwanza kikazi, akasafiri upesi hadi jijini Dare s salaam ili aweze kushuhudia kwa macho hicho anachosimuliwa na mke wake, kwamba mtoto wake wa katikati na pekee wa kike alikuwa katika hali mbaya sana.

Kweli ilikuwa zaidi ya alivyokuwa anaelezwa, Caro hakuwa yule aliyemfahamu. Kwanza alikuwa amepungua sana uzito na kukondeana mwili. Alikuwa anayeelekea kupoteza uwezo wake wa kufikiri maana kuna maswali alikuwa akiulizwa anajibu anavyojua yeye na kisha kuja kujirekebisha baadaye.
Hii haikuiwa hali nzuri, baba akajaribu kuwasiliana na wanasaikolojia akawaleta pale nyumbani kwa ajili ya kumtazama Caro.
Baada ya juma moja wakaelezea kuwa mtoto wao anaathirika ubongo wake kwa sababu ubongo wake unafanya kazi kubwa ya kuusaka ukweli ambao haiwezi kuujua kamwe.
“Mtoto wako anautesa ubongo wake kwa sababu anataka kujua chanzo cha Chopa kutupwa gerezani na hakuna sehemu yoyote ya kuupata ukweli huo zaidi ya kumuona Chopa na amueleze, na kama mnavyosema kuwa imekuwa ngumu sana kuonanana Chopa kwa ambazo na nyinyi hamzitambui basi hii hali ikiendelea hivi kwa muda mrefu huyu mtoto mtampoteza kutoka katika ulimwengu wa wenye akili timamu!!” alizungumza yule mwanasaikolojia ambaye pia ni tabibu.
“Dokta unataka kumaanisha kuwa Caro anaweza kuchanganyikiwa?”
“Hapana simaanishi kuchanganyikiwa maana hapa alipo tayari amechanganyikiwa… namaanisha atakuwa mwehu wa kiwango cha juu!!” alijibu bwana yule kana kwamba lile ni tatizo dogo.
Baada ya jibu lile mama Carolina akasikika akianza kulia, mume wake akamtuliza na kumweleza kuwa kulia hakusaidiii kitu chochote kile jambo la msingi wamsikilize mtaalamu.
“Aaah! Kwa hiyo ndugu zangu, wazazi wenzangu…huyu mtoto anatakiwa afanyiwe maarifa upesi sana… sijui ni kipi kinaweza kufanyika kwa sasa lakini nipeni muda nitafakari ni kitu gani tufanye kumsaidia mtoto huyu…. poleni sana bwana na bibi Mtembei!!!” alimaliza na kuwaaga huku akiwashika mikono kwa zamu.
______
Majuma kadhaa yalikuwa yamekatika, siku hii baada ya kufanya kazi kuanzia asubuhi hatimaye muda wa chakula ulifika. Chopa alipanga foleni ndefu akifuata utaratibu, siku hii njaa ilikuwa imemsumbua sana na hakika japokuwa chakula cha gerezani kilikuwa kibovu bado alikitamani ili tu aweze kuitibu njaa yake.
Tatizo lilikuwa moja ambalo lilimkera na si yeye tu hata wenzake aliowasikia kwa ukaribu walikuwa wanannung’unika.
Yaani wao walipanga mstari kwa muda mrefu lakini kuna watu ambao walikuwa wanakuja moja kwa moja na kuchukua chakula bila kufuata foleni.
Chopa alipoona foleni haisogei kabisa alimwomba mfungwa mwezake, wa mbele na wa nyuma kumtunzia nafasi yake ili aweze kutoa malalamiko kwa askari magereza.
“Bro acha tu, tumeshalalamika kila mwaka lakini hakuna mabadiliko wanajuana nao hao…” bwana mmoja alimwambia Chopa huku akijilazimisha kutabasamu.
Chopa alisita kidogo kisha akaamua kwenda hivyohivyo kushtaki. Yule askari magereza badala ya kuisikiliza shida yake akamuuliza ana miaka mingapi gerezani. Chopa hakujibu yule askari magereza akakisoma kibandiko katika nguo yake.
“Yaani wewe hata miezio sita huna gerezani unalialia kisa chakula… una akili wewe… au nd’o wale walioingia humu kwa kesi ya kuiba kuku.” Alimjibu kwa kebehi.
“Nenda kwenye foleni bwana mdogo chakula kipo kingi utakula na hata usipokula leo bado hautakufa, au kama ukifa itakuwa vyema hautamalizia kifungo chako tena utakuwa huru!!”
Majibu yale yalimkera sana Chopa akajawa na hasira lakini akalazimika kurejea kwenye foleni.
Akiwa pale kwenye foleni alimuona yule askari magereza akiongea na wafungwa wawili na kisha wale wafungwa wakamtazama Chopa kwa pamoja.
Chopa akatambua kuwa yule askari kuna kitu alikuwa amewaambia juu yake.
Punde baada ya maongezi yale wale mabwana wawili wakatoweka machoni mwa Chopa.
Baada ya kama nusu saa wakatokea tena, safari hii walikuwa wamebaki watu wanne tu ili Chopa aweze kufikiwa zamu yake ya chakula.
Wale mabwana wakafika na kumuita kando Chopa. Chopa akawajibu kuwa ni heri achukue chakula kwanza halafu atawasikiliza.
“Oya nenda kawasikilize watemi hao…” jamaa aliyekuwa nyuma yake akamnong’oneza.
Chopa hakujibu!!
“Tumekuita!!” wakasema kwa pamoja wale mabwana. Chopa akawatazama , kisha akaenda upesi kuwasikiliza ili ikiwezekana aiwahi foleni.
“Tumekuona ulipojipenyeza katika foleni, umewapita wenzako waliopanga foleni muda wote wewe umefika na kujiingizaingizatu!! Kwa hiyo kuliko kukikosa chakula kabisa unaombwa kurudi nyuma kabisa ufuate foleni….” bwana mmoja mfupi aliyejazia kiasi fulani alizungumza kwa dharau tele.
Chopa alistuka sana , jinsi alivyokuwa ametulia katika mstari kwa zaidi ya masaa mawili halafu anaambiwa eti aliingilia.
“Bro utakuwa umenifananisha mkuu, mimi nipo hapa tangu saa ngapi sijui, nilitoka kidogo tu kumuuliza jamboyule askari…” akataka kuonyesha hakumuona huyo askari….
“Kuna askari alikuwa hapa… halafu nikarudi.” Alijitetea Chopa.
“Kwa hiyo kumbe basi mimi ni fala wa kutupwa, macho yangu hayaoni nimekufananisha si ndohivyo…” alihoji.
Chopa akageukia foleni na kugundua kuwa alibaki mtu mmoja ili aweze kuhudumiwa. Akaondoka na kuingia katika foleni ili aweze kupata chakula ambacho alikihitaji mno.
Kitendo alichofanya kikawaacha wafungwa wengine midomo wazi ni kama kuna kitu walikuwa wanajua kuhusiana na hao watu wawili.
“Mpishii! Usimpe huyo bwana chakula…” sauti ya yule mwingine mrefu iliamrisha. Chopa akageuka na kuwaona wale mabwana sasa wakianza kumsogelea, wakati huo ndo kwanza m,pishi alikuwa ameupakua ugali anahitaji kumuwekea Chopa katika sahani.
Akili ya Chopa ikafanya kazi upesi, jinsi walivyokuwa wanamsogelea ikamkumbusha baadhi ya matukio wakati huo akifanya kazi ya ubaunsa katika kumbi za starehe.
Hakuwa na mwili mpana lakini Chopa alikuwa anawakabili vyema wateja wasumbufu.
Na hii ilikuwa chanzo cha yeye kukutana na mchumba wake Caro!!
Kwa sababu alikuwa na njaa alitambua wazi kuwa akitumia viungo vyake wale mabwana watambana vibaya!!
Akabaki ametulia huku jicho lake likiwa limeona kitu tayari!
Wale mabwana wakamfikia na kwa sababu alishaitambua shari mbele yake akaona ni heri iwe alivyopanga!!
Ilikuwa ni kitendo cha sekunde moja, akaukwapua ugali wa moto uliokuwa umepakuliwa katika sahani ya mpishi!!
Akautuliza moja kwa moja katika uso wa yule bwana mrefu kisha akatokwa na teke moja kali sana likatua vyema katika kifua cha yule mfungwa mfupi.
Akawaacha wanaugulia kila mmoja akilia kivyake.
Wafungwa waliokuwa kwenye foleni na kandokando walikuwa kimya kabisa wasiamini kile walichokuwa wanakiona!!
“Nipakulie chakula!!” sasa akamgeukia mpishi!!!
Mpishi akatii!
Akampakulia!!
Wakatia anaondoka pale akamuona tena yule mtu mfupi akija mbiombio. Bila kuuweka ule ugali chini na mboga yake, Chopa akatokwa na teke jingine hili la sasa kali kuliko lile la kwanza, likamtupa mtu mfupi chini, sasa wafungwa wakatambua kuwa Chopa hakuwa anabahatisha wakaanza kushangilia!!
“Ukiendeleza huu ujinga wako hukumu yako itaisha hivi karibuni, nitakuua ukatumikie kifungo kaburini. Waambie na wenzako kuwa sipendi masihara!!” Chopa akainama pale chini na kumkoromea mtu mfupi. Kisha akaondoka zake!!!

_____

CHOPA mwenye ghadhabu moyoni lakini uso wake ukionekana kukifurahia kile chakula cha gerezani alikuwa akiyakata matonge makubwa makubwa na kuyachocya katika maharage ambayo yalikuwa hayachovyeki kutokana na kuwa yanashabihiana na maji kabisa… na hayakuwa yameiva vizuri na kama hyiyo haitoshi yalikuwa yamejaa wadudu.
Chopa alikuwa akiikunja sura yake kila alivyotaka kumeza tonge.
Akiwa anaendelea na safari ile ya kuyakata matonge na kumeza, alipokuwa ameketi alikuja mfungwa mwingine akiwa na sahani yake akaketi huku akiendelea kula kidogo kidogo, alikuwa anaangalia mbele pasi na kumtazama Chopa machoni lakini alikuwa nazungumza naye.
“Kamanda… wakikuuliza nini chanzo cha ugomvi sema walitaka kukugeuza bibi, hapo kidogo adhabu itapungua lakini ukisema ukweli tu utalimishwa heka tano peke yako au utapewa adhabu ya kukata mbuyu…..” Yule bwana alipomaliza kuzungumza yale alisimama na kuondoka zake bila kuaga bila kumtazama Chopa machoni!!
Maneno ya yule bwana hayakuonekana na maana hadi ilipofika wakati wa kuhesabiwa ili kila mmoja arejee katika selo yake.
Chopa alishangaa kuona anatengwa!!! Wenzake wote wakaingia yeye akabakizwa nje.
Milango ya selo zte ikafungwa, akabaki yeye pamoja na askari magereza wawili.
Akiwa wima bado hajui nini kinaendelea mara ghafla alipigwa ngwala akadondoka chini.
“Unajifanya kuwa tunalingana tumesimama na wewe umesimama….” alifoka bwana mmoja na kisha akaruka ghafla na kurusha mkono ili amnase kofi Chopa.
Chopa akapangua lile kofi!
Balaa likaanzia pale, akatajiwa kosa kuwa anajaribu kumpiga askari magereza.
Kwa kosa hilo atachapwa viboko vine.
Ikawa hivyo, Chopa akalambwa viboko vine vya nguvu!!
Hapo sasa akaulizwa ni kwa nini amepigana na wafungwa wenzake wakati wa chakula.
Upesi Chopa akalikumbuka jibu aliloandaliwa na yule mfungwa ambaye hakuwa akimjua kwa jina.
“Waliniambia maneno mabaya, waliniambia watanifanya mke wao!!” Chopa alijibu kwa kulalamika.
“Sasa ulipoambiwa hivyo ndio ukapigana!!” akatupiwa swali jingine. Akajitetea kuwa hajapigana bali alijaribuy kujitetea walipotaka kumlazimisha zaidi.
Naam! Jibu hili likawa ponapona yake!!
Mlango ukafunguliwa akaruhusiwa kuingia ndani huku akipewa onyo kali!!
Chopa aliingia ndani akaanza kugusagusa sehemu yenye upenyo aweze kupita.
“Kamanda!” ile sauti ya mchana ule ikamuita….. akajongea hadi alipoitwa!!
“Vipi umepona?” alimuuliza.
Chopa akaelezea kilichotokea, yule bwana akamwambia amshukuru Mungu kwani hapo ni sawasawa na amesamehewa tu!!
“Naitwa Pocha walizoea kuniita Mr. P nilipokuwa mtaani unaweza kuamua kuniita vyovyote….” hatimaye yule bwana akajitambulisha.
“Umesema unaitwa Pocha mimi naitwa Chopa almanusura tufanane majina….. ujue wakati naingia niliambiwa na bwana mmoja wa kuitwa Crispin kuwa kuna mtu nafananae majina.. nadhani ni wewe….”
Ikawa mkasa kwa mkasa wakatajiana makazi yao huko uraiani na kidogo wakagusia kesi zilizowaweka humo ndani.
huu ukawa mwanzo wa ukaribu kati ya Chopa na Pocha!!

_____

KITENDO cha kuzungumza na Pocha na kukumbushiana kwa kilaupande chanzo cha kutupwa gerezani kulimfanya Chopa aamke akiwa na mawazo mengi, kichwa kilimuuma sana kwa sababu hakuwa na jibu sahihi la chanzo cha yeye kutupwa gerezani akihukumiwa kukaa humo miaka mitatu.
Katika kumbukumbu zake hizi zilizomletea maumivu ya kichwa alishindwa kuelewa iwapo ni ugeni wake katika mambo ya mahakama na hizi kesi ama ni vipi lakini alijiona kama aliyeonewa kwa kutopewa nafasi walau ya kumtafuta mtu wa kumtetea.
Alipofikiria juu ya mtu wa kumtetea akawakumbuka marafiki pamoja na baadhi ya ndugu zake waliokuwa hapo mjini, ni kweli hawakuwa wengi na hawakuwa na uwezo lakini halahala jama damu ni nzito kuliko maji!!
Lakini sasa unakaribia mwezi mzima hao aliodhani wangeweza kumtetea hawajawahi hata kuja kumjulia hali akiwa gerezani.
Hawa hawakumuumiza sana kichwa aliyemuumiza kichwa alikuwa ni Caro. Inawezekana vipi mchumba wake waliyependana hadi wakati huo hajaenda kumwona gerezani, mara ya mwisho alimuona akiwa kwenye karandinga kupelekwa gerezani.
Kwa mchanganuo huo, Chopa akakiri kuwa katika huu ulimwengu ukiwa matatizoni unakuwa peke yako lakini ukiwa salama unakuwanalo jopo kubwa sana la marafiki!!
Chopa akaamua kusahau kuhusu kupata msaada, wazo lake likarejea juu ya usiku ule wa kukamatwa!!!
Akakumbuka kuwa siku nzima kuna mtu asiyemfahamu alikuwa akimtumia jumbe za ajabuajabu katika simu yake.
Akimpigia anakata, kisha anatuma tena ujumbe mwingine ambao Chopa aliamini wazi kuwa mtumaji alikuwa anakosea namba.
Lakini sasa akiwa gerezani anaona kuwa bwana yule hakuwa anakosea nambari bali alikuwa sahihi kabisa.
Chopa akajisikitikia kwa kuzipuuzia jumbe zile!!
“Lakini si ningekuwa mjinga yaani saa tano usiku mtu ananiambia niondoke nyumbani niende mbali kabisa na nisirudi kabisa nyumbani kwangu wakati huohuo Caro alikuwa njiani anakuja kulala nyumbani kwangu, hakika nisingeweza kufanya ule ujinga!! Ni kweli imenigharimu sana lakini kuna uonevu umetanda katika hili!!!” Chopa alizungumza kwa sauti kiasi huku akiwa anafyeka kipande alichopangiwa kufanya kazi siku hiyo.
“Chopa wa Chopa!!” ilikuwa sauti ya Pocha yule rafiki yake mpya wa gerezani.
Kwa mara ya kwanza akageuka na kumtazama kwa makini usoni mwake, alikuwa yu mjanja mjanja sana haikuhitaji akili nyingi kulifahamu hili.
“Usiache kufyeka hawakawii kutucharaza bakora hawa!!” Pocha akamuonya Chopa ambaye alitaka kujisahau.
Bila kusubiri Chopa akatii, wakaendelea kufyeka huku wakibadilishana soga hapa na pale.
“Jana uliniambia kuna mzito mpaka atoke madarakani labda na wewer ndo utatoka una maana gani??” Chopa alimuuliza swahiba wake yule.
“Aisee hausahau…. anyway mimi nilikuwa fundi simu hadi nilipokamatwa na kutupwa humu,eti nikabambikwa kesi ya wizi kwa njia za mtandao….. ila kiukweli ishu haikuwa wizi sema ujanja ujanja wangu uliniponza. Ujue kaka mimi hapa kuna kitu fulani hivi nahisi nimejaliwa, sijui ni machale sijui ni nini katika akili na mikono yangu ila kuna uhusiano fulani wa kipekee. Na ninakuhakikishia mimi nikitoka humu nahakikisha sikai hapa bongo tena, bongo majungu sana…..” Alizungumza Pocha huku akiendelea kufyeka kwa juhudi. Yaani ni kama walikuwa hawasemezani lolote.
“Yaani mimi katika kuunda simu, nikajikuta kuwa hizi simu hizi za kisasa hizi zinazofungwa kwa loki ya michoro ‘patterns’ basi we unaweka pateni zako mi ukinipa nikijaribu kama mara nne tu nishatibua kila kitu. Mwenyewe siwezi kuelezea hata inakuwaje…. basi bwana si unajua mjini kila kitu biashara bwana. Mtu akiniletea simu nitengeneza hasahasa wakinadada na akina mama, mi nafungua natazama picha nikikutana na picha za kibiashara nazitoa….”
Chopa akaingilia kati na kuuliza, “Picha za kibiashara nd’o zipi maana we nawe una maneno mageni kweli!!”
“…Picha za kibiashara ni zile mtu kajipiga akiwa mtupu ama amepiga na bwana yake wakiwa watupu mi naziuza kwenye magazeti ya udaku….. walikuwa hawanilipi pesa nyingi sana lakini ikafikia siku sasa ya mimi kuwa mjanja na kudai malipo makubwa na ninakuapia Chopa hilo dili lilikuwa dili langu la mwisho kabisa na nisingethubutu tena kufanya mchezo ule…..”

_____

___POCHA ANASIMULIA___

KIMVUAMVUA kilichonyesha katika jiji la Arusha kilipunguza mizunguko ya watu kuingia na kutoka mjini. Hali hii ilisababisha baadhi ya biashara kuzorota….
Kibanda cha kutengeneza simu na kuuza bidhaa ndogondogo kilichomilikiwa na Pocha ama maarufu kama Mista P. Kiliishiwa kukaliwa na marafiki waliokuwa wakijikinga wasinyeshewe mvua. Kwa mpita njia angeweza kudhani ni wateja wamemjalia Pocha hivyo wangeweza hata kumwonea tamaa. Lakini uhalisia aliujua Pocha mwenyewe. Tangu asubuhi alikuwa hajapata dili lolote la maana la kumwingizia pesa. Walau pesa ya kula tu!!
Na hapo mchana alikuwa amekopa chakula kwa mama muuza akiwa ameahidi kulipa jioni.
Majira ya saa kumi na dakika kadhaa jioni alikuja mteja, kama masihara vile Pocha alimuita kuanzia mbali. Mteja akaingia mtegoni, akamchangamkia na hatimaye akasema kuwa ana tatizo la simu yake anahitaji amesahau pateni zake anahitaji simu yake iflashiwe.
Pocha akaichukua ile simu na kuitazama vyema sana, ilikuwa simu ya maana sana na aliyeileta alioneka akuwa sio mmiliki halisi wa simu ilea ma la basi amenunuliwa na bwana yake mwenye pesa.
“Hii hapa elfu ishirini na tano mama!” Pocha aliinadi bei yake huku akiendelea kuitazama simu ile.
Bei ile ikamshtua yule mwanamama,ni kama hakuamini na hapo palikuwa na mawili aidha ilikuwa kubwa sana ama ilikuwa chini sana tofauti na matarajio.
“Na inatengemaa baada ya muda gani maana sitaki ilale!” alihoji kwa utulivu.
“Mara ya mwisho simu ya mtu kulala kwangu ilikuwa mnamo mwaka alfu tisa mia na tisini na mbili…. tofauti na hapo sijawahi kulaza simu ya mtu hapa dadangu!!” Pocha alipiga domo na kusababisha kila mtu kuangua kicheko.
Kasoro yeye tu ambaye hata tabasamu halikumtoka!!
Yule dada akalipia shilingi elfu kumi na kuahidi kuwa akikamilisha hilo zoezi anamlipa kiasi kilichosalia.
“Sasa kaka lakini si wanaflash kwa kutumia Kompyuta wewe hata kompyuta huna…” mwanamama alihoji huku akimpatia ile pesa.
“Mama, ubongo wa mwanadamu una akili mara bilioni moja kuliko kompyuta, Mista P ana ubongo uliotimia.” Sasa alijibu huku akitabasamu na kuikunja ile pesa.
“Kama kweli ubongo una akili kuliko kompyuta naomba basi uiflashi hiyo simu halafu namba zangu zisipotee kutoka humo…”
“Hilo tu, ukija andaa shilingi elfu kumi nyingine ya ziada… Mista P naitibu kama unavyotaka, yaani mimi hata simu ikivunjiika kioo naweza kuunganisha kwa kutumia ubongo wangu na sio gundi….joo baada ya saa zima mama” alijitapa Pocha na kuzidisha vicheko kwa watu.
Mwanamama akajiondokea huku akiwa hana imani ya kutosha na hili lilionekana usoni.
Punde baada ya kuondoka.
Akaitazama simu ile akatulia kwa muda akaitazama katika kioo chake na kisha akauruhusu mkono wake ufanye kama ufanyavyo kila siku.
Akapitisha michirizi ya kwanza ikakataa, akatulia akapitisha michirizi ya pili napo ikagoma. Wakati huo mvua ilikuwa imekatika na wale watu waliojazana pale kijiweni walikuwa wameondoka na kubaki watatu tu.
Hawa walikuwa wakimtazama Pocha huku wakimshangaa sana kwanini amepokea pesa ya watu wakati ni kweli hawezi kuiflashi ile simu!!
Pocha hakuwajibu, sasa alikuwa anajaribu michirizi ya tatu.
Akaipeleka mikono kama akili ilivyotaka.
Akafikisha mwisho, ikafunguka.
“Hureeeeeeeey!! Pesa mfukoni, na pesa hii imethibitishwa kwa matumizi halali kwa ajili ya Pocha… Mista P.” Pocha akatokwa na mayowe huku akiikunjua ile pesa na kweli ilikuwa imethibitishwa kwa matumizi halali kwa sababu tayari alikuwa ameifanya kazi.
Pocha akaondoka akiwa mwenye furaha moja kwa moja akaenda kulipa deni la chakula, akapita dukani akalipa deni la vocha aliyokopa.
Kisha akarejea ofisini mwake.
Tofauti na simu nyingine ambazo kitu cha kwanza akifanikiwa kutoa loki kifuatacho kinakuwa kutazama picha, kwenye hii alichelewa kufanya hivyo!
Na ilikuwa kama bahati mbaya sana akajikuta ameingia kwenye yasiyomuhusu.
Awali zilikuwa picha za kawaida tu, lakini mara akaanza kukutana na picha za ajabu ajabu, alikuwa ni yuleyule mwanamke akiwa na mheshimiwa mbunge wa jimbo mojawawapo la kaskazini, walikuwa watupu kitandani. Sijui kama ni mtu aliwapiga picha ama walikuwa wameiseti simu ili iwapige zile picha.
Pocha alipagawa, upesi akaondoka pale ofisini kwake na kuelekea kwa rafiki yake jirani ambaye yeye anamiliki kompyuta. Huku akazifyonza katika namna ya kunakiri zile picha zote. Kisha akarejea ofisini kwake na wakati huo yule mama alifika.
Pocha mwenye tabasamu akampatia simu yake huku akimweleza kuwa ndio kwanz amemaliza.
“Ukanitangaze mama waambie kuna jamaa anaitwa Mista P. Anatibu simu zote bila kupoteza namba…” wakati anatoa tambo hizi yule mama alikuwa anaduwaa asiamini kila alichokuwa anakiona mbele yake.
Kweli simu ilikuwa imetolewa loki na ilikuwa sawa kabisa.
Akalipia ile huduma na kuaga.
Alipoondoka POCHAnaye akafunga ofisi muda mfupi baadaye. Akaenda kwenye ile kompyuta na kuziweka zile picha katika santuri (CD).
Akaondoka zake kwenda kufanya biashara.
Safari hii akalitangaza dau lake mapema kabisa katika gazeti la udaki akawatumia moja ambayo haiwaonyeshi wakiwa watupu na kisha akasema kuwa anazo nyingine nyingi sana zinazouzika sana.
Lile gazeti likavutiwa na ile biashara!! Lakini halikuwa tayari kutoa ile pesa kwa awamu moja….
Wakamtumia nusu na yeye akatuma picha nusu!!

“Ujue Chopa kila sehemu kuna wakuda… yaani wakuda hawakosekani kila kona. Nahisi kuna mwandishi ambaye anamjua huyu mzito, basi akamvujishia zile picha.
Aisee nikajidanganya kuwa kuna siri baina ya watu wawili, tena sio wawili eti siri kati ya raia na gazeti la udaku. Kesho yake nikaingia kazini… ilwe nafika tu askari hawa hapa…. wakaninyaka.
Sijawahi kuruydi tena uraiani Chopa… na nilipigwa vibaya mno hadi niseme wapi pengine nilizihifadhi zile picha…. nikasema kila zilipokuwa lakini hawakuniamini wakaona jambo jema ni kuninyamazishia humu gerezani. Nd’o maana nakwambia mimi hadi kutoka humu ni mpaka muheshimiwa aamue ama afe na ninaombea afe kwa sababu maamuzi hawezi kutoa hivi karibuni maana anahofia kuwa huenda ninazo picha nyingine. Kwa hiyo huu ndo mkasa wangu kaka.”
Alimaliza kusimulia Pocha na kumwacha Chopa akiwa anayeduwaa, aliduwaa kwa sababu alikuwa akisikia tu kuwa wanaokwenda jela sio wote wenye hatia.
Sasa alikuwa amekutana na ukweli wenyewe.
Ila bora huyu alikuwa analijua lililomsababisha awe jela. Ila yeye Chopa hakuna alilokuwa akilijua hii ilimtesa sana…..

______

1995, Mwanza Tanzania.

Marafiki wawili waliokuwa wamesoma wote shule ya msingi na ile ya upili mjini Mwanza na hatimaye kuwa kati ya wanamwanza wachache kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam.
Lucas Kazioba na Edwin Mtembei!
Kama masihara vile alianza Mtembei kwa kumshawishi Luca wachukue fomu za kugombea ubunge. Luca aliduwaa sana kwa sababu hakuamini kama ingekuwa rahisi sana kama mwenzake alivyokuwa anawaza….
Kadri siku zilivyosogea mbele na jambo lile kuzungumzwa kisomi zaidi hatimaye wakakubaliana kuwa mmoja achukue fomu ya ubunge na mwingine fomu ya udiwani ilimradi tu isijekutokea siku moja wakajikuta majukwaani wakikandiana kwa sera tofauti.
Edwin yeye alikuwa amewahi kuwa kiongozi katika serikali ya chuo kikuu cha Dar es salaam lakini Luca ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza hivyo alikuwa akijifunza mengi sana kupitia kwa Luca.
Hata kuzungumza aliiga kwa Edwin!!
Siku zikaenda na kufikia siku ya kuchukua fomu, awali walikuwa wamekubaliana mmoja achukue fomu ya udiwani na mwingine fomu ya ubunge lakini lilipobaki juma moja kwa ajili ya kuchukua fomu Luca alitoa wazo jipya, kwa sababu yeye hakuwa vizuri sana katika kuzungumza mbele ya watu basi safari hii iwe ya Edwin halafu yeye atajaribu miaka ijayo. Lakini wazo lake halikuishia hapo akasema atachukua fomu kupitia chama cha upinzani ilimradi ajifunze siasa tu!!
“Aaah! Sasa wakikuchagua itakuwaje si nd’o yale ya kupondana jukwaani?” Edwin Mtembei alimuuliza Luca.
Luka alijibu kimasihara kabisa kwanza aliuponda sana upinzani kuwa kamwe hautakuja kuwa bna mbunge hata mmoja katika bunge la jamuhuri!! Hii ni kwa sababu huu ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na hakuna aliyetarajia maajabu yoyote kutoka kwa upinzani!!
Majibu haya yakamshawishi Edwin akakubaliana na uamuzi wa Lucas rafikiye.

Mambo yakaenda kama walivyopanga!!
Baadaye yakabadilika kama masihara, Edwin hakuchaguliwa na chama tawala lakini Luca akasimamishwa na upinzani ili awanie jimbo lile ambalo Edwin alipanga kuliwania.
Walikutana kujadili na Edwin akaapa kuwa atakuwa na Luca bega kwa bega katika kampeni zake.
Kiasi fulani Edwin alikuwa na pesa kumpita Luca hivyo alitumia pesa zake kusaidia usafiri na matangazo ya hapa na pale ili kuwavuta watu katika kampeni za Luca. Awali alifanya kwa siri ili chama alichotangazia nia kisijue hali ilivyoendelea mbele akajiweka wazi kuwa anamuunga mkono mgombea wa chama pinzani!!

Ikawa kama ndoto ya hayawani!!
Ndoto isokuwa na dalili ya kuwa kweli, lakini hatimaye Luca akampiku aliyekuwa mgombea wa chama tawala kwa kura za kumtosha kuwa mbunge wa jimbo lao.
Haya yote aliyaweza kwa sababu Edwin alikuwa anatumia muda wake mwingi kumkaririsha Luca maneno ya kuwashawishi wananchi.
Wananchi wakamuelewa na kumpigia kura zao.
Yule aliyedhani hawezi kuwa hata diwani wa kata,akabadilika na kuwa muheshimiwa Lucas Kazioba.
Miaka mitano baadaye akahamia chama tawala kwa sababu alizodai kuwa upinzani unababaisha!!!
Hiyo ilikuwa mnamo mwaka 2000.
Uamuzi huu ulipokelewa kwa shingo upande kabisa na rafiki yake Edwin am,baye hakuchukua tena fomu za kuwania ubunge kwa sababu hakutaka kukabiliana na rafiki yake wa muda mrefu!!!
Maisha yakaendelea.

_____

Dodoma, Tanzania
Septemba, 2011

Yalikuwa yamepita masaa manne tangu mgeni aliyekuwa amekuja kwa ajili ya kuonana na muheshimiwa mbunge alikuwa akingoja.
Awali alikuwa akitarajia kuwa punde tu baada ya taarifa kumfikia muheshimiwa basi walau atatoka na kumjulia hali na kumweleza ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.
Lakini haikuwa hivyo, hili jambo lilimkwaza sana kwa sababu alikuja pale si kama mwananchi wa kawaida bali alikuwa ni mtu wa karibu pia kwa muheshimiwa.
Hatimaye uvumilivu ukamshinda, akaenda tena pale mapokezi na kumuita yule katibu muhtasi na kumuuliza.
“Ulimwambia jina langu na akakusikia kabisa ama?”
Katibu muhtasi alibetua midomo yake mikubwa iliyojazwa rangi nyekundu, akageuza na macho yake juu na chini kisha akamjibu.
“Kila mtu ana jina babangu… na bosi hajasema anasikiliza mtu kulingana na jina lake hapa.” Alimaliza kujibu akaiweza sawa blauzi yake…..
“Aaah! Samahani dada, sina maana mbaya namaanisha kuwa ukimwambia jina langu walau ataujua na uzito wa shida yangu kwa sababu niliwasiliana naye hapo kabla…” yule mgeni alijiongoza asije kutawaliwa na hasira aliyokuwa ameihifadhi kifuani mwake akajibu kwa utulivu.
Kama ilivyokuwa awali dada yule alianza kwa kubetua midomo yake na kisha akageuza macho yake juu na chini kana kwamba ile ni njia mojawapo ya kujiandaa kujibu maswali.
Safari aliongezea jingine la kukwaza nafsi, alikuwa anatafuta ‘big g’ akaitafuta vyema kisha akaiweka katika ulimi wake na kuipuliza ikapasuka na kutoa kisauti cha kukera.
“Sasa kamamuliwasiliana naye hapo kabla mbobna usiwasiliane naye tena sasa hivi… we vipi babangu.” Alijibu kwa sauti iliyojaa maudhi.
Hili sasa yule mgeni likawa zito sana kwake.
“Mpumbavu wa adabu wewe shenzi kabisa, nina mtoto kama wewe umri sawa kabisa shenzi kabisa…. hiyo midomo yako kama ndo ilikupa kazi basi wewe na bosi wako hamna akili…jinga kabisa hili… mi ni mtu mzima vibinti kama wewe vijinga vijinga nilikuta navyo miaka mingi iliyopita na nitamsubiri hapa bosi wako aje akueleze mimi nilikuwa nani lilipokuja sualala wajinga wajinga kama wewe…. lione macho kama shetani!! Unaona kila mtu anayekuja katika hili dirisha anawaza ngono tu kama unavyowaza wewe…. wajinga nyie nd’o mnasababisha wabunge wetu walalamikiwe kuwa wanafata ngono Dodoma…. na laiti kama ungekuwa hapa nje ningekuchapa viboko na usingekuwa na popote pa kushtaki……” aling’aka yule mgeni ambaye kweli umri ulikuwa umeenda lakini alikuwa bado imara sana.
Ukali wake na matusi yote aliyomrushia yule binti yalikuwa dawa tosha kwa yule katibu muhtasi.
Dada akawa mnyonge kabisa, sasa hakubetua tena midomo wala kuzungusha macho badala yake alikazania kwenye neno moja tu.
“Nisamehe baba yangu….. basi yaishe baba yangu!!”
Baada ya takribani dakika tano ya songombingo lile akatoka aliyekuwa na mamlaka ya juu ya ofisi ile.
“Edwin!! Nini kinatokeatena hapo..” alihoji muheshimiwa mbunge!!
“Lucas intavyuu zako za kutafuta wafanyakazi anasimamia nani, huyu mjinga mjinga siku ukipata muda mueleze mimi ni nani na nilikuwa nani…..” alifoka Edwin! Muheshimiwa Lucas akamtuliza, akamshika bega na alipofika pale dirishani akatoa kauli ambayo ilimaanisha alichokuwa akizungumza Edwin dhidi ya yule dada.
“Vero, kesho sihitaji kukuona hapa….. afandee! Hakikisha huyu binti anakaguliwa vizurui kabla ya kuondoka hapa ndani. Si mfanyakazi tena katika ofisi hii!!” ilikuwa sauti kali ya Muheshimiwa!!
Kamamasihara dharau zikamtokea puani Vero!!
Akaipoteza kazi…..

Walipofika nje waliingia katika gari la muheshimiwa mbunge na Edwin hakusubiri wazungumze sana akamueleza kuwaamsikilize shida yake,
Lucas akawa msikivu kama alivyokuwa siku zote kwa Edwin!
Edwin akaelezea tatizo linalomkabili binti yake, akajieleza kwa kirefu sana kama lilivyokuwa na kisha akaelezea wazo lake.
“Nahitaji Lucas kama yawezekana na ninaamini inawezekana kabisa, nisaidie huyu mtoto walau akakae nje ya Tanzania hata kwa miezi miwili tu…. ujue Caro ndo binti yangu wa ujanani na sina binti yeyote… nisijieleze sana historia ya caro unajua mwenyewe nampenda sana yule mtoto. Eti sasa hivi daktari ananiambia eti Caro akiachwa kama alivyo anaweza kuwa mwehu au tahira wa kiwango cha juu kabisa aaargh!!” Edwin alishindwa kuzungumza akaanza kulia.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa Lucas kumuona swahiba wake akitoa machozi hadharani.
Nafsi ilimuuma sana!!
“Sasa Edwin unacholia nini eeh! Si umeshakuja huku kwangu na umesema unachohitaji niache basi na mimi niongee au? Tulia bwana Edwin!!” Lucas alimbembeleza rafiki yake wa muda mrefu.
Baada ya Edwinkutulia kidogo hatimaye Lucasa alizungumza nakutoa kauli yake.
“Edwin rafiki yangu unayenijua kupita marafiki zangu wengi, umenisimamia katika shida zangu mara nyingi sana na sihitaji kuzihesabu hizo mara nyingi ili nijue najihusisha katika hili kwa kiwango gani, tatizo lako ni langu nakumbuka hata caro alivyozaliwa tukiwa mwaka wa kwanza chuo tulihangaika wote kumbeba mama caro hadi hospitali, sasa hata hili siwezi kukuachia peke yako. Kajipange huko Mwanza ukiwa tayari niambie nimfuate caro lini…. nampeleka Caro London!! Sitaki ujinga kabisa linapokuja suala lako Edwin!! Nasema hivi nampeleka caro London… nini miezi miwili bwana nasema atakaa huko miezi sita kama tatizo bado halijaisha nampeleka Amsterdam Uholanzi huko…… Edwin wewe ni wangu. Haya sasa lipo la kukufanya ulie tena?? Kama lipo niambie!!” alimaliza kuongea vyema rafiki yule wa kweli.
Edwin akabaki mdomo wazi, wakati yeye akiwaza kuwa patakuwa na mlolongo mrefu katika kusaidiwa shida yake na akiwa anawaza walau Caro aende kuishi kampala ama Mombasa anashangaa huyu bwana anakusudia kumpeleka caro London!!
Alibaki akitokwa machozi ya furaha, akatoa shukrani za dhati na kwa mara chache kati ya nyingi wanazowasiliana akamuita kwa kutumia cheo chake.
Mheshimiwa Lucas Kazioba!!

_______

TANGU Pocha amuulize Chopa kuwa yawezekana ile kesi yake na hatimaye kuhukumiwa kwenda gerezani yaweza kuwa mpango wa kando, katu hakuwahi kumfafanulia nini maana ya mpango wa kando, zaidi alimweleza kuwa amegundua kuwa chanzo sio mpango wa kando huenda ni mambo mengine tu!!
Chopa akachoka kumsisitiza kwa sababu hata kama angejua sababu ya kufungwa hakuwa na namna ya kutoka gerezani.
Akaamua kupuuzia kujua maana ya lile neno.
Siku zikaenda hatimaye ukawa mwaka mmoja gerezani, Chopa sasa alikuwa yu mzoefu kabisa na hakujali kuhersabu siku kama alivyokuwa anafanya zamani hizo.
Alishazoea sasa kuwa hakuna wa kuja kumtembelea pale gerezani, hivyo ndugu zake ni wafungwa wengine wenzake alionao humo ndani.
Kama kawaida ukiwa mtetezi wa wanyonge unakuwa mtu wa watu, na hili lilikuwa kwa Chopa. Alipendwa sana.
Kama walivyonena wazee wetu wa zamani wenye maarifa walisema kuwa ni kawaida kabisa kuwa vizuri kamwe havidumu!!
Mwaka wa pili ulivyoanza pale gerezani, wakiwa wanapata chakula Pocha alimwomba Chopa wazungumze kidogo.
Chopa akatega sikio kumsikiliza……
“Chopa nina taarifa moja mbaya sana inayonisumbua kichwa changu…..” akasita kisha akapiga tonge moja la ugali.
“Mmoja kati yetu humu ndani anakaribia kuondoka, sasa sijui anaondoka kwa misingi ipi. Sijui ni kifo, sijui anahamishwa gereza, sijui ni msamaha wa raisi ama vipi?” alizungumza kwa majonzi Pocha.
“We nani amekwambia…..” Chopa aliuliza kwa makini.
“Mikono na akili yangu, nilikuwa nachora kitu fulani nikajikuta naingiwa na fikra hizo na mahusiano kati ya akili yangu na mikono nilikueleza pale mwanzo kuwa nayaheshimu sana…. sasa naomba na wewe uheshimu pia. Kama ikitokea kweli tunatenganishwa iwe kwa kifo, kuachiwa huru ama vinginevyo napenda nitumie fursa hii kukueleza kuwa umekuwa na umuhimu sana katika maisha yangu, na zaidi kama ni kuondoka kwa kifo naombea niwe mimi…” Pocha alisema akiwa anamaanisha.
“ Kwa nini wajiombea mambo mabaya Mista P”
“Chopa kabla haujaja hapa gerezani kuna wajinga wawili walikuwa wamekaribia kunifanya mke wao… najua kwa nguvu walizonazo halafuy eti wewe usiwepo watanioa wale. Hakuna kitu sipendi kama kufanywa hivyo, we mwenyewe si unawaona waliofanywa hivyo walivyo kwa sasa…..” alizungumza kwa majonzi sana.
“Tunalala nao selo moja ama…” Chopa aliuliza. Pocha akatikisa kichwa kukubali.
“Tukiingia kulala nionyeshe nitafanya kitu kizuri tu!”

____

ITAENDELEA

MPANGO WA KANDO SEHEMU YA PILI

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment