Saa la 25 Sehemu ya Tano
NEW AUDIO

Ep 05: Saa La 25

Saa la 25 Sehemu ya Tano
Saa la 25 Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE (AMATA GA IMBA)


Simulizi: Saa La 25

Sehemu Ya Tano (5)

Storangsvagen – Finland

“Binti yako ni genius kabisa” Mr Jarvinen alimueleza mama Robinson

“Yeah, hata mimi namuona akiwa nyumbani, mara nyingi anafnya vitu kwa akili sana” Bi Robinson alijibu.

“Pia ana upendo sana na ushirikiano na wenzake, hakika ni binti wa ajabu sana” Mr Jarvinen aliendelea kumueleza mama Robinson juu ya Tuntufye anavyofanya vizuri shuleni, mpaka shule inavyomhusudu kwa unahiri wake hata kuamua kumsaidia kwa hali na mali ili afike mbali kieleimu.

“Jane, katika maisha yako ungependa kuwa nani?” Mr Jarvinen alimuuliza Tuntu.

“Ninapenda kuwa mwanasheria, ili nikatetee haki za wanyonge na wanaodhulumiwa” Tuntu alijibu kwa ufasaha swali lile.

Jane Elizabeth Robinson au Tuntufye, sasa alikuwa ni msichana mzuri wa sura na umbo, shepu ya kike hasa ilianza kuchukua nafasi yake katika mwili huo, hata yeye aliona mabadiliko hayo na daima alijiangalia sana katika kioo chake cha chumbani huku akijigeuzageuza wakati mwingine akiwa kama alivyozaliwa. Lakini jambo moja halikumtoka moyoni mwake, aliwakumbuka sana wenzake aliyowaacha huko mtaani wakiendelea kuombaomba, aliapa moyoni siku akimaliza masomo yake angependa kuishi Tanzania na kufanya kazi katika nchi yake, furaha yake daima ilipotea kila alipomkumbuka mama yake na mdogo wake Malogo, hakujua wako wapi wala wanafanya nini. Mara nyingi alipojiwa na picha au kumbukumbu ya Ravi, mvulana aliyembaka pale katika makaburi ya Kisutu, hasira na kisirani vilimkaba koo ijapokuwa hakuwa akijua kama Ravi alikufa siku ile alipomchoma na chupa au alipona, ilikuwa ni siri ambayo kamwe asingeweza kuijua jibu lake.

Masomo ya Tuntu yalienda vizuri sana hata waalimu wake walikuwa wakimkubali msichana huyu kwa bidii na juhudi alizonazo. Daima alizifikiri ndoto zake jinsi atakavyozitimiza.

€ € € €

Mheshimiwa Hakimu Bw Kilipa, aliketi juu ya kiti chake, na mbele yake kulikuwa na wasaidizi wake, karani wa mahakama pamoja na muendesha mashitaka bila kukosa wazee wa baraza.

Mama Vituko alisimama kando ya wote, kwa utulivu akimsikiliza muendesha mashitaka akisoma shitaka lake, shitaka geni masikioni mwa Mama huyu mpole. Alikuwa akishitakiwa kwa kosa la kuuza shamba na mali mbalimbali za marehemu mumewe kisha kutoroka, kwa namna moja au nyingine aliwadhulumu watoto wake mwenyewe. Shitaka hilo lilisomwa takribani dakika ishirini.

Baada ya maswali kadhaa aliyohojiwa na Hakimu, Mama Vituko alikana shitaka hilo na cha kushangaza zaidi hakimu hakutoa nafasi ya kuwekewa dhamana, hivyo mama Vituko alirudishwa lumande mpaka kesi itakaposomwa tena pale upelelezi utakapokamilika.

Kila mtu mahakamani pale alisikitishwa na uendeshaji wa kesi hiyo, alilaumu kwa namna asiyoijua.

Mama Minja na Mama Njiku walikuwa wameketi chini ya mti wakiwa kimya kila mtu akiwa na wazo lake, kila mmoja akitafakari cha kufanya.

“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni” Mama Njiku alivunja ukimya

“Kabisa, mi sielewi kabisa juu ya uendeshaji wa kesi hii” mama Minja alijibu

“Haki haitendeki, kwa nini?” mama Njiku alilalamika

“Siku hizi haki inauzwa na sheria inanunuliwa” mama Minja alimjibu

“Kweli kabisa, hata mi naona. Rushwa imekuwa tatizo, rushwa inawakandamiza masikini, watu wanakosa haki zao kwa sababu ya rushwa, mh! Rushwa adui wa haki.” Mama Njiku aliongea kwa masikitiko.

Nje ya mahakama hiyo watu walisimama makundi makundi wakijadiliana hili na lile juu ya kesi ya mama Vituko, hakuna hata mmoja aliyeridhishwa na uendeshaji wa kesi hiyo, jina la hakimu Kilipa lilitajwa katika midomo ya walio wengi nje hapo.

“Huu ni ujinga…” alisikika mlevi mmoja aliyekuwa akipita jirani kabisa na mahakama hiyo “kwa nini watu mnapenda kuonea binadamu wenzenu? Halafu kwenye pombe mnajisifu eti tumemkomoa atakoma, nie! Mungu yupo, naapa haki ya Mungu mtauona moto wa Jehanam apa hapa duniani” alimaliza kauli yake na kuyumba kwa nguvu, almanusura aangukie watu waliopo hapo.

“A aaa, mzee, acha hayo maneno hapa, sio mahali pake” Mtu mmoja alimwambia yule mlevi huku akimvutia pembeni.

“Lazima niseme, na nnasemea hapa hapa, si wameandika hicho kibao kuwa huu ni ‘Uwanja wa Haki’ , huu ni uongo huu ni uwanja wa rushwa na chuki. Lazima niseme kwani hatuyajui hayo bwana,” aliendelea kubwabwaja, yule mzee bado alikuwa akimsihi kupunguza kelele zake kwani mahakama bado inaendelea.

“Mzee si nimeshakwambia acha maneno yako, utajiletea matatizo bure, kasemee kilabuni kule sio hapa,”

“Siachi kusema, na ntasema sana, mi inaniuma anavyoonewa huyu mama,” akageuka upande wa lile kundi lililokuwa likimkataza kuongea hayo, akavuta hatua mbili tatu za tabu kidogo sasa akiwa kaweka mikono yake nyuma, kwa sauti ya chini kidogo akawauliza “hivi nyie hapa, kuna asiyemjua huyu mama?” wote wakanyamaza kwa Sali lile “kuna asiyejua kinachoendelea? Niambieni nyie mnaojifanya mnajua sana, eh? Baba Vituko mpendwa wetu Mungu amuweke pema” akayumba kidogo na kusimama tena “alipokufa alimuachia mkewe mali nyingi, mashamba waliyoyatafuta kwa jasho lao. Leo hii ndugu wa mumewe wanasemaje? Eti kauza mashamba na kutoroka na watoto, eti ndiyo kamuwekea sumu mumewe ili afe nay eye afanye hivyo! Mh, kwa mwenye akili haiingii akilini hata kidogo” akaanza kuvuta hatua zake zisizo na muelekeo huku akipiga mruzi kana kwamba si yeye aliyekuwa akiyazungumza hayo. Kila mtu aliyemsikia akiyazungumza hayo alitulia kutafakari akiwemo Mama Minja na Mama Njiku ambao walifika kijijini hapo kujua nini kitajiri kwa shoga yao.

“Hata sisi tuna uwezo mkubwa wa kutoa pesa ili kesi iende tutakavyo, lakini si haki na si jambo jema hata kidogo” Mama Minja Lisimama kutoka pale alipokaa, na taratibu alivuta hatua kuielekea gari yake, kila mtu alimtazama hasa kwa mwendo wake wa maringo na kujiachia, zaidi walivutiwa na mitikisiko ya tako lake lililotulia vizuri mwilini mwake. Aliingia kwenye gari yake na kuondoka taratibu na shoga yake Mama Njiku. Akiwa bado hajaliacha eneo la Mahakama, alimuona hakimu akitoka mahakamani na kuelekea upande uleule waliokuwapo wao.

“Hebu tumsubiri kidogo” Mama Njiku alitoa wazo, na mama Minja alisubiri, punde tu hakimu Kilipa alilifikia gari hilo.

“Mheshimiwa habari!” mama Njiku alimchokoza

“Salama tu akina mama, nyie wazima?” aliwajibu

“Sisi wazima sana tu”

“Nikiangalia haraka haraka ninyi si wa hapa, eti? Maana sisi wa huku kijijini twajuana sote” aliongea hayo huku akichekacheka.

“Hapana tulikuja tu hapo mahakamani kufuatilia kesi ya ndugu yetu” Mama Njiku alimjibu.

“Aaa ipi hiyo?”

“Ni ya yule mama anayeshitakiwa kwa kumpa sumu mumewe na kisha kuuza mali za familia”

“Oook, naijua hiyo. Kumbe yule mama ni ndugu yenu ee? Aisee” yule hakimu alijifanya kushangaa sana, Mama Minja alikuwa haongei kitu alibaki kumwangalia tu juu mpaka chini.

“Ndiyo hivyo Mheshimiwa, tunasikiliza tujue nini kitajiri kama atashinda au atashindwa, yote ya Mungu” mama Njiku alimalizia

“Aaaa ha ha ha teh teh the, mnajua akina mama kila jambo linawezekena, mtu kushinda au kushindwa inawezekana ili mradi tu wanandugu mmejipanga vipi,” alijichekesha huku akijifanya anataka kuondoka, Mama Minja alidakia mazungumzo

“Yaani hapo unamaanisha nini maana mi sijaelewa…”

“Unajua, hata sisi mahakimu hatupendi watu walundikane kule mahabusu au magerezani. Lakini hatuna jinsi kabisa. Kwa hiyo kama wanandugu hawataki ndugu yao aende huko wanajipanga tu”

“Sawa mheshimiwa, hebu tupe namba yako ya simu tutakutafuta kabla ya tarehe tajwa ya kesi hiyo” Mama Minja aliomba. Bila kuchelewa Kilipa alitoa business card yake na kumpatia Mama Njiku. Kisha wakaagana na Mama Minja akaondoa gari.

“Ndugu tujipange” mama Minja alimueleza Mama Njiku kisha wote wakacheka

“Ee ngoja tukajipange, tutakupigia” mama Njiku alimalizia.

Hakuna asiyemjua Mama Minja katika eneo la Manyoni, mwanamke aliyeinua maisha ya akina mama wengi na vikundi vya vijana katika eneo hilo, alikuwa akitoa mikopo ya riba nafuu na muda mrefu, mwenye upole na kumsikiliza kila mtu mwenye shida na kumsaidia inapowezekeana. Aliguswa sana na maisha ya Mama Njiku na Mama Vituko, moyoni mwake alikuwa akifikiri jinsi ya kuwasaidia ili awatoe katika hali ile lakini ndiyo likatokea hili la Mama Vituko, Mama minja hakukata tama kwa kuwa alijua kuwa mama Njiku ni mwalimu kitaaluma nay eye anamiliki shule ya msingi na chekekechea huko Manyoni aliona ni vema amuajiri katika moja ya shule zake. Mama Njiku alifurahi sana kurudi katika kazi yake aliyokuwa akiipenda, siku chache baadae alihamia Manyoni na kupata nyumba ya vyumba viwili ambayo ilikuwa ni mali ya Mama Minja, watoto wake na wale wa Mama vituko waliingia shuleni hapo na kuanza kusoma, kwa ujumla maisha yalibadilika, kutokana na kazi hiyo mpya mgahawa wake kule mjini aliukodisha kwa mama lishe mwingine na yeye kukusanya kodi ambazo zilisaidia kuwalea watoto wake na wale wa shoga yake.

€ € € €

Damdam alikuwa ameketi juu ya kochi kubwa akiangalia mpira katika runinga yake kubwa iliyo hapo sebuleni.

“Kautipe!” aliita

“Bee” kautipe aliitika kutoka chumbani alipo, na kutoka kwenye korido ndefu kuelekea sebuleni

“Mbona umekaa chumbani peke yako, hutaki kungalia tamthiliya, njoo uketi hapa” Damdam alimueleza Kau huku akimtazama msichana huyo mbichi kabisa.

Kau kwa uoga aliliendea kochi lile na kuketi pamoja na Damdam.

“Niite anko, umesikia Kau?”. Kautipe alijibu kwa kutikisa kichwa. Damdam aliliendea jokofu kubwa lililopo sebuleni hapo na kutoa chupa Fulani ya wine nyekundu na kutia kwenye bilauri kisha kumletea Kautipe na nyingine kubaki nayo mwenyewe, kama alijuwa kuwa Kautipe atalewa kwa wine hiyo basi alikuwa amecheza pata potea kwani Kautipe alishazoea kutumia vinywaji hivyo hasa alipokuwa akiuza grossary huko kwao Iringa.

Damdam alimwangalia Kautipe alivyokuwa akinywa wine ile kwa utulivu mkubwa sana huku macho yake yakiwa runingani, alimtazama kwa uchu wa mapenzi, kila mara alibadilisha aina ya mikao na uwekaji miguu kwa maana uzalendo ulionekana kumshinda, jicho halikuwa runingani tena bali lilishia kwa Kautipe. Alitamani amrukie lakini aliona si ustaarabu. Kautipe alibadili aina ya mkao na kujiegemeza upande mmoja wa kochi hilo huku makalio yake akiyaacha upande alipo Damdam. La haula, Damdam Lijikuta akianza kupapasa eneo hilo la nyuma la Kautipe

“Anko mi sitaki bwana” Kautipe aliiondoa mikono ya Damdam mwilini mwake.

“Aaa usiogope anko, nashika tu kidogo” Damdam alibembeleza, kisha akasogea zaidi alipo kautipe na kuanza kumpapasa taratibu.

“Anko sitaki ah!” kautipe aling’aka na kusimama kuondoka lakini Damdam alimshika na kuvuta katika kochi Kautipe alijikuta akirudi kochini lakini alijikuta amepakatwa na Damdam, mikono ya Damdam ilikuwa tayari ikipapasa kifua cha Kautipe, Kautipe alibaki kukataa kataa lakini hakuchomoka alianza kujinyooshanyoosha ….


Damdam aliona kazi iliyo mbele yake ni nyepesi hasa kwa jinsi ambavyo kautipe alikubali kila ambacho Damdam alikifanya, kautipe alijikuta kaishiwa nguvu katika mikono ya Damdam, mikao yote aliyowekwa kwake ilikuwa sawa, alitii kila mchezo na alitoa ushirikiano wa kutosha kwa Bwana Damdam.

Baada ya kumaliza mambo yao hayo, Kautipe alijifanya kulia na kukimbilia ndani. ‘Wasichana bwana!’ Damdam alijisemea moyoni alipomuona Kautipe katika hali ile. Akiwa katika furaha ya kutimiza azma ya mwili wake kwa Kautipe mara kengele ya mlangoni iligonga, Damdam alishtuka hasa ukizingatia hakuwa na mihadi na mtu yeyote siku hiyo ‘nani huyo?’ alijiuliza huku taratibu akitoka nje kuliendea geti, akalifungua kwa tahadhari, alipomuona mtu aliyegonga alifungua mlango na yule mtu akaingia ndani harakaharaka.

Damdam alimkuta yule mtu amekaa juu ya kochi akihema, akaliendea jokofu na kumtolea toti moja ya Pushkin na kumpatia.

“Uhhh Thank God!” yule mtu alionekana kuokoka katika jambo la hatari sana “Master, samahani kwanza nimerudi kabla ya wakati” alimueleza Damdam.

“Hata mimi nashangaa, maana nilitegemea nikuone hapa wiki mbili zijazo!” Damdam aliongea kwa mshangao.

“Master, huko kwa Madiba kimenuka, ndege tunduni” Jese alimueleza Damdam ‘Master’.

Damdam alinyanyuka kitini na kuanza kuonekana kuchanganyikiwa ghafla.

“Martha yuko ndani!?” aliuliza kwa sauti ya mshangao

“Habari ndo hiyo, mi unavyoniona nimechomoka kwenye midomo ya mamba, wananisaka mzigo upo court kaka” Jesse alizidi kueleza.

Damdam aliinua bilauri yake iliyosheeni kinywaji na kuimiminia yote tumboni kisha akaitupa chini bilauri ile kwa kishindo na kugawanyika vipandevipande.

‘Tumekwisha’ alijisemea Damdam huku akijitupa kochini, akili na ubongo wake vilikufa ganzi ghafla hakujua nini cha kufanya.

“Ok nimekuelewa, nenda kajifiche tutatafutana kesho jioni” Damdam alimwambia Jesse.

“Lakini Master wewe vipi? Wakikuotea hapa itakuwaje?” Jesse aliuliza

“Usijali, nitawapa namba ya mzee waongee nae” Damdam alijibu kwa majivuno.

€ € € €

“Hii tabia lazima ikomeshwe!” Mama Minja alimueleza mama Njiku ambaye walikuwa wameketi pamoja wakibadilishana mawazo, “Kwa sababu watu wanapoteza haki zao kwa hela za wengine. Rushwa, nachukia sana rushwa” Mama Minja aliendelea kuongea kwa jazba.

“Si wewe tu, nchi yetu inanuka rushwa na wengi hatuipendi lakini tutafanyaje?” Mama Njiku alijibu kwa swali huku akiendelea kunywa soda yake taratibu.

“Ukienda mahakamani rushwa, mahospitalini rushwa, kila sehemu rushwa, lazima tuitokomeze” Mama Minja aliendelea kuongea. Mazungumzo yote haya yalizaliwa baada ya kesi ya mama Vituko ambayo Mama Minja na Mama Njiku waligundua kuna uonevu mkubwa sana hasa baada ya mazungumzo na Mancatcher, kijana aliyemwaga siri yote iliyojificha nyuma ya pazia.

Rushwa, ilikuwa ikizungumzwa na kupingwa vinywani mwa viongozi wengi wa chama na serikali lakini bado ilikuwa janga la taifa, watu wengi wanakosa na kupoteza haki zao kwa sababu ya rushwa, watu wanakosa huduma mahospitalini kwa kuwa hawana pesa za kuhonga.

Mama Minja alifikiri kwa kina juu ya hilo, akatikisa kichwa kuonesha kuwa amepata ufumbuzi.

“Mama Njiku, nimeshapata ufumbuzi, nitalifanyia kazi na iwe fundisho kwa wote wenye tabia kama hiyo”, alimaliza na kunyanyuka kitini, akaaga na kuondoka.

Simu ya Mama Minja iliita, alipoiangalia alikutana na namba ngeni asiyoijua, aliitazama mara kadhaa kwa kuwa daima hakupenda kupokea simu asizozijua. Moyo wake ulimshawishi kuipokea simu hiyo nae akafanya hivyo.

“Hallo… ee nakusikia” aliongea na sauti ya upande wa pili

“(…) ndiyo nakuelewa (…) Ok, kwa hiyo hizo tu zinatosha na mambo yatakuwa sawa? (…)sawa nimekuelewa basi nipe muda kidogo maana pesa kwangu sio shida” Mama Minja alishusha pumzi na kuirudisha simu yake pochini. Aligeuza gari na kurudi tena kwa mama Njiku kumpa habari hiyo.

“Ee shoga vipi?” Mama Njiku aliuliza

“Mh! Mheshimiwa kanipigia simu, anasema tukimpa laki tatu tu mama Vituko atakuwa huru” mama Minja alimueleza mama Njiku.

“Lakini mi ninavyojua, kesi kama yake ambayo wamesema ameua mumewe mbona huyu hakimu hawezi kuiamua, anataka hela tu” Mama Njiku aliongea kwa hisia

“Aaaa Kweli, sasa huyu dawa yake kajichemshia mwenyewe. Subiri najua cha kufanya, hela nitampa lakini za serikali sio zangu” mama Minja alimaliza na kuaga kwa mara ya pili.

“Rafiki yako, inaonekana alishambuliwa na mwanamke kwa sababu katika uchunguzi wetu tafutishi zilizopatikana ni nguo za ndani za kike, shanga moja” afisa polisi alimwambia Damdam huku katikati yao chupa za pombe zilikuwa zikiteketea.

“Mh! Kwa jinsi ninavyomjua swahiba sio rahisi kushambuliwa kijinga vile, lazima kuna kitu, au walimzunguka wapiganaji wenzake! Haingii akilini kabisa bwana Thomson” Damdam alitoa dukuduku lake ka afande huyo wa kitengo cha upelelezi Magomeni.

“Inawezekana bwana Damdam, uchunguzi wa daktari umebaini kuwa kabla ya shambulio hilo swahiba alikuwa amelewa sana na pigo lililomuua ni la kichwani maana alikuwa amechanika vibaya na kupoteza damu nyingi. Hata hivyo atu wa mapokezi walitueleza wazi kuwa mtu wa mwisho kuingia nae ni kabinti kadogo ambako hakajulikani hata kameenda wapi, hivyo tuko mbioni kukatafuta tukatie nguvuni” Thomson alimaliza mazungumzo yake.

“Ok Bro, nimekupata. Siku ile ilikuwa anikabidhi pesa yangu ambayo nilikuwa namdai kama wiki mbili ilikuwa milioni tisa na nusu. Ina maana nyie hamkukuta pesa yoyote?” Damdam aliuliza kwa shaka zito.

“Oh no! hatukukuta hata shilingi moja, zaidi ya zile za mifukoni tu.”

Damdam alishusha pumzi, akavuta kumbukumbu ya wiki kadhaa nyuma…..

“Oya Damdam, ile ishu yetu imekamilika swahiba, tuonane mida ya saa nne usiku kijiwe nikupe mzigo” Pedeshee Masharubu alimpigia simu Damdam jioni ya siku hiyo.

“Ok! Kwa nini isiwe hata jioni jioni hivi?”

“Hapana, leo nimefanya kazi kubwa huko Zenji nimetoka na Milioni za kutosha, sina budi kujipongeza na kuifurahisha nafsi yangu, leo nataka katoto kabichi kabisa ambako hakajaanzwa bado, nikimaliza yote nitakushtua swahiba” Pedeshee alinguruma kwenye simu.

Pedeshee Masharubu na Damdam walikuwa marafiki wa muda mrefu sana kutokana na kazi zao haramu. Pedeshee alikuwa ni jambazi la kuogopwa lililotoroka mikono na pingu za polisi mara nyingi, alikuwa akifanya kazi zake katika ngazi za kimataifa, alijulikana kama Masharubu kutokana na ndevu ndefu alizozifuga pembezoni mwa midomo yake, kutokana nakuhonga manoti kila kukicha kwa wasichana warembo, hawakusita kumwita Pedeshee.

Walikutana na Damdam jijini Nairobi katika harakati tofauti, Damdam alikuwa kadhulumiwa mzigo wa dawa za kulevya za thamani ya milioni sabini, ndipo alipokutana na Masharubu katika mtaa maarufu wa Koinange hapo Nairobi. Masharubu alimuahidi kumuokolea mzigo hu ndani ya masaa matatu endapo atakua tayari kumpatia shilingi milioni kumi tu. Damdam alikubali, na Masharubu akamwambia asubiri palepale mpaka ampigie simu. Akiwa na vijana wake makini watatu, waliuvamia mtaa wa maduka mengi wa Uthiru Kenoo, kama walivyoelekezwa na Damdam hawakukosea, tajiri maarufu wa eneo hilo alikuwa kataitiwa kiasi kwamba alitoa mzigo wote na pesa nyingine juu, kwa kupoteza ushahidi wakamuondolea uhai kwa risasi takribani tatu za kifua.

Damdam hakuamini alichopewa mkononi mwake, wakiwa katikati ya mitaa ya Korogocho. Masharubu na Damdam waliafikiana kulipana Dar es salaam na siyo katika nchi ya kigeni. Hapo ndipo uswahiba huu ulipoanza wakati mwingine hata kubadilisha wanawake ilikuwa ni jambo la kawaida kwao…….

“Haina shaka swahiba nakuaminia, we pita Ohio omba msaada wanafuga wale watakupatia kamoja” Damdam alikata simu na kusubiri usiku huo kuonana na Pedeshee bila kujua kuwa swahiba wake mauti yalimkuta kabla ya miadi yao.

“Thomson, nina hamu na mtu aliyemuua Pedeshee, nikimjua…”

“A a a aaaa usianze mambo yako, we waachie polisi wanafanya kazi yao, usije ukajiingiza matatizoni bure” Thomson alijibu huku akiinua bilauri yake iliyojaa bia na kujimiminia kinywani. Afisa upelelezi Thompson alikuwa alikuwa ni mtu wa karibu sana wa Damdam hasa katika kumsaidia kuvusha mizigo yake na kumaliza vijikesi vidogodogo, alikuwa akipatiwa pesa mara nyingi na Damdam ili awezeshe mambo.

“Unajua mpaka sasa upelelezi umefikia pazuri sana, na mtuhumiwa atatiwa mbaroni haraka iwezekanavyo” alizungumza huku akiitua bilauri yake mezani kwa kishindo, bia zilianza kukolea na siri za ofisi zikaanza kumwagika hadharani.

“Enhe, hebu nambie hiyo habari…” Damdam alidakia

“Tulikusanya baadhi ya changudoa na makahaba wa mtaa wa Ohio na Garden kwa nyakati tofauti kwa kuwa tulijua soko la Pedeshee lilipo, hasa kwa kutumia simu yake tulinasa mazungumzo mbalimbali katika laini yake ya mwisho, wakatuambia kuna mwenzao aliyeondoka na Pedeshee siku hiyo na kumuahidi kumtafutia katoto bikira” Thomson alibwabwaja

“Ah, jina lake, maana wale wengi nawafahamu” Damdam aliuliza kwa shauku

“Jina sikumbuki mpaka nikaangalie kwenye faili, kama siyo Ziada, no sina uhakika”

“Pale mmmm no hakuna ninayemfahamu kwa jina hilo ila kuna mmoja anaitwa Zainabu” Damdam alirahisisha kazi.

“Ewaaaaaa Zaina, yeah ni huyo na sasa ndiye tunayemtafua, yeye tukimpata hii kazi itakuwa imekwisha”

Moyo ulimpasuka Damdam alibaki hajiwezi, aliegemea kiti alichokaa na mara jasho jingi likaanza kumtiririka, hakuamini alichokisikia. Thomson alishangaa kumuona katika hali ile.

“Vipi kaka?” alimuuliza

“Hapana, nilijisikia vibaya ghafla, lakini niko poa” akainua chupa yake ya vodka na kujimiminia bila kuzimua.

“Ah no, nikupeleke nyumbani, tutaongea kesho”

Thompson alimkokota Damdam mpaka kwenye gari yake na kumrudisha nyumbani.


Upepo ulivuma taratibu na vumbi la hapa na pale liliendelea kusumbua watu waliopo eneo hilo. Mama Minja aliketi meza tofauti na Mama Njiku katika grossary hiyo iliyopo jirani kabisa na barabara kuu eiendayo Tabora, katika eneo la Puma. Mama Minja alikuwa akiendelea kunywa taratibu kinywaji akipendacho cha Redds, huku akiangaza macho huku na huku kumatazama mgeni wake ambaye wameahidiana kukutana hapo, mara kwa mara alikuwa akiitazama saa yake ya dhahabu kujua wakati.

Punde si punde mgeni wake aliwasili eneo lile na kujikaribisha kiti, kisha akaagiza bia baridi na kupiga funda moja la nguvu.

“Samahani kwa kuchelewa dada angu, si unajua tulikuwa na kikao cha mahakimu wa mahakama za mwanzo hapo mahakama kuu” hakimu Kilipa alimuomba radhi Mama Minja.

“Ah, usijali hata hivyo haujachelewa sana kama ambavyo Waswahili wafanyavyo.” Mama Minja alimjibu huku akicheka na wote wakacheka na kugonga viganja vya mikono yao.

“Ok tusipoteze muda, keshokutwa ndiyo ile kesi ya ndugu yenu, sasa umejiandaaje ili tuwasuke watu tumalize utata?”

“Kama tulivyoongea mheshimiwa ila nimekuwekea na cha juu”

“Ha ha ha ha umefanya vizuri sana, ndiyo marupurupu haya, mishahara yenyewe serikalini ni midogo tunafanya tu ilimradi tusilale njaa” hakimu Kilipa aliongea huku akichekacheka.

Mama Minja aliivuta pochi yake na kuchomoa kiburungutu cha noti nyekundu, mpya kabisa zilizojipanga sawia kama zimetoka kiwandani muda huo.

“Hivi hapa hawatuoni kweli hapa?” hakimu Kilipa aliuliza

“Aaa usiogope sisi tpo kwenye biashara we unaiuza sheria na sisi tunanunua haki, basi. Ndiyo maana mpaka leo wanaofia jela masikini na wanaotesa mtaani matajiri ila wa nje ndiyo wahalifu na wa ndani ni wasio hatia, tutafika tu”

Maneno ya mama Minja hayakugonga sawasawa ngoma za sikio la hakimu Kilipa, tayari akili yake ilishalewa na manoti hayo, alishaanza kufikiria hili na lile la kufanya pindi tu afikapo kijijini, ‘watanitambua, kazi si ndiyo hii’ alijisemea kimoyomoyo huku akiendelea kuhesabu harakaharaka zile pesa.

Mara ghafla vijana wawili walisimama pembeni ya meza hiyo mmoja kila mmoja upande wake, wote wanne walibaki wakitazamana.

“Sisi ni maofisa TAKUKURU , tumewakamata mkitoa na kupokea rushwa” hakimu Kilipa alipigwa na butwaa akabaki midomo wazi ikimtetemeka hakujua ajitetee kwa lipi

“Ah Jamani, mi sijapokea rushwa, hapa tupo kwenye mpango tu wa kibiashara” alijaribu kujitetea lakini haikusaidia, alimeza mate mengi maana aliona kuwa kiu iliyomshika haikuwa ya kawaida “Hivi vijana mnajua mnanidhalilisha, mimi ni mheshimiwa hakimu”

“Rushwa haina mwenyewe” mmoja wa vijana wale alijibu na kisha wakawachukua wote wawili lakini hasa aliyelengwa ni Hakimu Kilipa, mpenda rushwa na mnyonya haki za wanyonge.

Mama Njiku alijinyanyua kutoka pale alipoketi baada ya gari iliyowachukua Mama Minja na hakimu Kilipa kupotelea mjini, aliingia katika gari ya mama Minja na taratibu dereva aliondosha mahali hapo, ‘akashike adabu’ alijisemea mama Njiku.

€ € € €

“Sisi tulikuja wawili, mimi na mwenzangu anaitwa Ashura” Kautipe alikuwa akimueleza Damdam walipokuwa mezani wakinywa chai. Ni siku ya nne tangu kautipe aingie ndani ya ksri hili, alikuwa haruhusiwi hata siku moja kutoka nje, Damdam alimgeuza kama mkewe hata siku mbili za mwisho alimuhamishia chumbani kwake kwa nguvu.

“Sasa mwenzio yuko wapi?” Damdam aliuliza

“Aaa mi sijui ni muda sasa hatujaonana, kuna siku alitoka na da Zai alienda kumtafutia kazi tangu hapo sijamuona, kila nikimuuliza da Zai ananikaripia tu.”

Damdam alimsikiliza Kautipe kwa makini sana, huku akili yake ikijaribu kuunganisha matukio ‘au Zai ndiyo alimuunganishia Pedeshee huyo mwenzake’, mawazo yaligongana kichwani mwa Damdam, akaamua kukata shauri, akainua simu yake ili ampigie Zai lakini kabla hata hajafanya hivyo aliona simu yake ikiita, alipoiangalia kiooni iliandika Zai, alibonyeza kitufe cha kupokelea huku akijiwazia moyoni ‘lazima nimnase leo niujue ukweli, na afande Thompson amkute hapa hapa’ hasira zikamshika ghafla akaanza kusugua meno yake, gadhabu ikakitawala kichwa chake.

“Hello beibi, jamani hivi siku tatu bado tu huyo mwali wangu arudi nyumbani” sauti ya Zai ilisikika upande wa pili. Kimya kilitawala Damdam alisahau hata anatakiwa kujibu nini, kama aliyekurupushwa usingizini alianza kuongea

“Zai hakikisha unafika hapa haraka sana”

“Kuna nini beibi mbona unaonekana kugadhibika hivyo?”

“Nimekwambia uje nina mazungumzo na wewe, fanya haraka sana chukua TAX nitalipa”

Zai alikata simu na kujifikiria mara mbili, ‘mh ana nini huyu mwananume? Au Kau nae keshaharibu, watoto majanga hawa’ alijisemea huku akirudisha simu yake katika pochi. Akavuta hatua chache kutoka katika ghetto lake na kukifikia kituo cha Tax cha Mwembeyanga, moyo wa Zai ulikuwa ukianza kuongeza kasi, alihisi kuna jambo, lakini alijipa moyo ‘wacha niende’.

Damdam alitoka nje na simu yake mkononi, mara hii hakutaka mtu asikie anachokiongea, alizunguka na kuliacha geti upande wa pili.

“Kaka nimekurahishia kazi” aliongea na Thompson kwenye simu

“Nini Damdam?”

“Zai anakuja nyumbani muda si mrefu, uje umkusanye hapa, naumia sana na kifo cha swahiba wangu”

“Aaa ok! Ila umetuwaisha kidogo, tunakuja kikazi zaidi, dakika kumi tutakuwa maeneo hayo” Afande Thompson alikata simu.

Moyo wa Damdam sasa ulikuwa adui mbaya kwa Zai, alimsubiri kwa hamu ili ahakikishe anajua nini kiliendelea. ‘Hivi akiwa si yeye, itakuwaje? Ah potelea mbali kwani mi ndugu yangu!’. Damdam alirudi ndani na kumkuta Kautipe akimalizia kuondoa vyombo mezani, alimtazama kwa jicho lile amtazamalo mara nyingi. Aliitazama saa yake ilimuashiria kuwa ilishatimu saa nne asubuhi, mara alisikia geti likigongwa, liligongwa taratibu na mwisho wake likagongwa kwa nguvu, Damdam alitaka kwenda kufungua lakini roho yake ilimrudisha kitini.

“Kautipe mama, hebu nenda ukaangalie ni nani anayegonga, mwambie mwenye nyumba hayupo aje kesho” Damdam aliagiza. Kautipe alivaa malapa yake na kuliendea geti, akalifungua kwa shida kidogo na mara likamtii, mbele yake alisimama msichana mwenye mwili mdogo aliyevaa baibui na kuruhusu macho yake tu yaonekane.

“Kautipe!” msichana yule aliita. Kautipe alishtuka kusikia jina lake, akakodoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.

“We nani?” akauliza

“Mimi Ashura, tuondoke haraka panda kwenye gari” Ashura aliongea kwa sauti ya polepole kidogo huku akijifunua lile baibui upande wa usoni. Kautipe hakuamini macho yake alipomuona shogaye huyo. Kitendo bila kuchelewa, Ashura alimshika mkono Kautipe na kuingia nae katika tax aliyokuja nayo.

Damdam aliendelea kungoja pale kochini lakini akaona sekunde na dakika zinakatika bila kautipe kurudi, ‘nini kimetokea?’ alijiuliza huku akijiinua kulielekea lile geti, bahati nzuri alilikuta bado li wazi akajitokeza robo tatu ya mwili wake kuchungulia nje, hakumuona Kautipe wala kivuli chake. Damdam alihisi damu ikimwenda mbio, kijasho chembamba kilimtiririka hakujua afanye nini, alitokeza mwili mzima kuangalia vizuri nje, aliangaza huku na huko lakini hakumuona Kautipe, akaweka mikono yake kiunoni, akatikisa kichwa.

“Bro vipi, mbona hivyo?” sauti ya muuza maji aliyekuwa akipita hapo ilimkatisha mawazo yake.

“Ah, hamna kitu dogo, nilikuwa namcheki mdada wangu wa kazi alikuwa ametoka nje” alijibu huku akiliendea geti kurudi ndani

“Kama ni yule binti mbona kaondoka na tax hapa kaelekea hivi” alimjibu huku akimuonesha upande ambao gari ile imeelekea.

“Aah Ok, asante, nilishasahau kama nimemtuma” alijibu Damdam kwa kumzuga, kumbe alikuwa keshazidiwa kete na Ashura.

€ € € €

“Ongeza mwendo kaka, maana nahisi mpenzi hali yake mbaya” Zai alimuhimiza dereva kuwahi na dereva kijana anavyopenda sifa, aliongeza mwendo na gari ile ilikuwa aikipepea kama kishada, waliiacha barabara ya Chang’ombe na kuchukua ile ya Mandela kuitafuta Buguruni, simu ya Zai iliita

“Ee dear, nipo njiani nakuja”

“Hivi Zai unanifanyia nini mimi, umekuja hapa umemuiba Kautipe halafu unanizuga, eti ‘niko njiani nakuja’” aliongea na kumalizi kwa kubana pua.

Masikini Zai hakuelewa chochote kilichotokea huko kwa Damdam, ‘Kautipe kaibwa au katekwa’ alijiwazia.

“Damdam, hivi mbona leo unanifanya bwege hivi, unajua mi sikuelewi” Zai aliongea kwa wahka huku pua yake ikiwa imepambwa kwa matone madogomadogo ya jasho.

“Hebu simamisha gari kwanza!” alimuamuru dereva ambaye sasa alikuwa mwendo kasi kama wa kilomita mia na ishirini kwa saa akiyakaribia mataa ya Tazara. Lahaula! Alipokanyaga breki tu kumbe nyuma yake lori kubwa la mafuta lilikuwa linakuja karibu kabisa, kishindo kikubwa kikasikika puuuuu! Lori lile liliigonga ile gari kwa nyuma na kuikanyaga vibaya sana, watu walikimbilia eneo lile kwa minajiri ya kutoa msaada lakini wengi walikuja ili kuona nini cha kuiba muda huo. Michirizi ya damu ilionekana ikisambaa barabarani na watu walikwishajaa katika eneo tukio.

€ € € €

“Ashura, sasa huku wapi?” Kautipe alimuuliza Ashura huku wakitembea harakaharaka kuielekea barabara ya Malamba Mawili.

“Huku ndo geto, Kautipe, hata hivyo nilikuwa nataka nikupate ili tupange mkakati” Ashura alimueleza Kautipe.

Baada ya mwendo kidogo waliingia kwenye nyumba Fulani ya wageni, Ashura alichukua funguo na wakaingia ndani.

“Uhhhhhhh!” zilikuwa ni pumzi za uchovu za Ashura baada ya kujitupa katika kitanda kikuukuu.

“Mh shoga, yule da Zai hafai kwa chai wala kwa ugali” Kautipe alishindwa kuvumilia alipasua la moyoni.

“Kwa nini?” Ashura aliuliza

“Kwenda kuniweka mi kwa lile baba, kila siku linataka na sijui kama halijaniambukiza Ukimwi maan lilikuwa linanilazimisha hata kinga halikumbuki”

“Mambo ya Zai muachie Zai mwenyewe” Ashura alimwambia Kautipe ambaye alionekana kusikitika sana kwa hali ile.

“Yaani Ashura, umasikini wetu unakuwa fimbo ya kutuchapia. Ina maana ukinisaidie lazima nikulipe fadhila?” Kautipe aliongea kwa kuumia sana.

“Nani aliomba msaada, wewe au Zai?”

“Atakuwa Zai mwenyewe, maana mi nilikuwa polisi sielewi kinachoendelea huko duniani, kesi ya bangi linikabili wakati hata mmea wenyewe siujui” Kautipe alianza kutoa machozi, “Ningejua nisingekuja mjini.”

“Pole, ila Zai lazima tumuoneshe kazi hawezi kutufanya sisi majinuni, ila kwa sasa shoga hapa ni kupanga safari tuuondoke mji wa watu.” Ashura alizungumza huku akiwa anavua baibui lake, “Heri yaw ewe mambo aliyonifanyia Zai mimi, sintomsahau, usione navaa hivi, najua siku na muda wowote lazima niwe mikononi mwa polisi”

“Kwa nini Ashura?”

“Nimeua, nimeua mtu…”


Mahakama ilifurika watu, kila mmoja akitaka kujua hatima ya Mama Vituko. Mama Vituko alonekana kuchoka kwa kusota rumande zaidi ya mwezi mmoja huku kesi yake ikipigwa danadana, ikidaiwa ushahidi haujakamilika. Siku hii kila mtu alitaka kujua hasa nini kitajiri mahakamani hapo, walalamikaji, ndugu wa marehemu walikuwa wamekwishafika wakijua kazi imekwisha ukizingatia na donge nono walilompa Mheshimiwa Kilipa, wakina mama wenye uchungu na mwenzao nao walikuako kujua hatima ya shoga yao, kila mtu aliongea lake.

“Mizee ile haina hata huruma!” Mama mmoja alikuwa akimnong’oneza mwenzie

“Tena lile linalotembelea fimbo, lina roho mbaya ka Shetani” mwingine alidakia

“Haya tusikilize tu, Mungu atamsaidia shoga”

“Coooouuurrttttt” muito wa kuhashiria kuwa mahakama inaanza ulitangulia kama kawaida na watu wote walisimama na baadae kuketi. Kila mtu alishangazwa kumuona hakimu mwingine na si yule waliyemzoea, maswali vichwani yalizunguka ‘Yuko wapi Kilipa leo?’ mmoja alijiuliza, ‘eee afadhali tumsikie na huyu, yule mpenda hela sijui yuko wapi leo’,mzee mwingine alijiwazia mwenyewe

Kama ilivyo ada kwa mpangilio wa mahakama jalada la Mama Vituko lilisomwa mbele na muendesha mashitaka mbele ya hakimu.

Hakimu Bwana Filbert Mtendamema aliyepewa kibali maalumu kutoka kwa jaji mkuu ili aweze kusikiliza na kuamua juu ya kesi inayohusisha mauaji, alikuwa ametulia kimya akifuatilia neno kwa neno katika kusikiliza kwa jalada lile na baada ya muendesha mashitaka kumaliza.

Hakimu alimuuliza mama Vituko kama anakubaliana na yaliyosomwa, lakini mama Vituko alikana, hakukubaliana nayo. Hivyo ikawa ni wakati wa kusikiliza ushahidi kutoka upande wa mashitaka (Prosecution side), shahidi wa kwanza alitoa ushahidi wake juu ya kifo cha ndugu yao na uuzwaji wa mashamba na mali za marehemu, alieleza kuwa siku ya tukio marehemu alikuwa akila chakula na mkewe mara akazidiwa ghafla na kutokwa jasho jingi, walikodi pikipiki na kumuwahisha kituo cha afya lakini haikuchukua muda marehemu alishindwa kupumua vizuri na kufa, kadiri ya daktari ilithibitika kuwa marehemu amekula sumu mbaya aina ya Cyanide ambayo humfanya mtu kushindwa kutumia hewa kwa haraka na kupoteza ufanisi wa uendeshaji mwili wake, ndiyo maana haraka sana alifariki. Shahidi huyo aliongezea kwamba kabla ya kifo hicho mama Vituko alikuwa amepata mtu ambaye alitaka kununua mashamba makubwa ya marehemu hivyo aliona njia nzuri ni kumuua mumewe ili yeye atekeleze hilo, ndiyo maana alipojua kuwa atagundulika akatoroka nyumbani yeye pamoja na watoto na kwenda kusikojulikana.

Mahakama yote ilibaki kimya kabisa ikisikiliza ushahidi ule ukitolewa dhidi ya mama Vituko.

Mama Minja na Mama Vituko walikuwa miongoni mwa wasikilizaji wa kesi hiyo. Muda wote macho ya mama Vituko yalijaa machozi aliona wazi jinsi shemeji zake walivyojipanga kummaliza.

Shahidi wa pili nae alieleza kwa kukazia yaleyale na aliwasilisha taarifa ya kidaktari iliyoandikwa mara baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, taarifa ile ilichukuliwa na kuambatanishwa na viambatanisho vingine ili kusaidia upelelezi.

Baada ya ushahidi huo kukamilika, ilikuwa ni nafasi ya hakimu kutoa mahamuzi ya kimahakama, kwanza kabisa ilionekana wazi kuwa mama Vituko ana kesi ya kujibu kadiri ya ushahidi uliotolewa. Hakimu Filbert Mtendamema aliiahirisha kesi na kumpa uhuru mama Vituko kuandaa utetezi wake kama ni kutumia mashahidi au kujitetea yeye mwenyewe.

“(…) Kesi itatajwa tena baada ya siku kumi na nne.”

Nje ya mahakama kila mtu alikuwa akiongea juu ya utofauti wa uendeshaji wa kesi hiyo, kila mtu aliridhika na jinsi utaratibu ulivyokuwa siku hiyo, lakini bado waliumiza vichwa kuwa sasa mama Vituko kakutikana na kesi ya kujibu.

“Mh hivi ina maana ni kweli mama Vituko kamuu mumewe!?” akina mama walikuwa wakiulizana wenyewe kwa wenyewe pa si na majibu.

“Bibi we, hakimu wa kweli Mungu, tusubiri hiyo baada ya siku kumi na nne tuone mbivu na mbichi” mama mwingine aliwajibu wenzake.

€ € € €

“Hebu mpigie simu hakimu Kilipa, kwa nini leo hakuwepo?!” alilalamika Mzee Malombe.

“Aaaa lakini huyu mama lazima tummalize, atajitetea nini, we si umeona ushahidi wetu ulivyoenda shule, aaaa hata awe jaji hapa ni kifungo tu tena cha maisha” aliongea kaka mkubwa wa marehemu.

“Lakini kweli atatetewa na nani? Hao shoga zake wa mjini wanaokuja na gari hapa, hawana lolote hawa, hawajui a wala be” Mzee malombe aliongezea.


“Sasa mama Minja” Mama Njiku alimgutusha mama Minja kutoka katika lindi la mawazo.

“Mm niambie”

“Tunafanyaje katika hili la mama Vituko?”

“Usiumize kichwa tutaenda kuongea na mama Vituko ukohuko mahabusu ili tujue kama atajitete mwenyewe au la, lakini sasa kesi imefika mahali pazuri sana” mama Minja alimueleza mama Njiku

“Lakini mi ule ushahidi wa washtaki umeniogopesha, au kweli mama Vituko kalitenda hili!” mama Njiku aliongea kwa woga kidogo.

“Mama Njiku, usiumize kichwa tutaenda kuongea nae na yeye ndiye atatueleza ukweli”

Mama Minja na mama Njiku waliagana na kila mmoja kushika njia yake kuendelea na majukumu mengine.

€ € € €

“Nitafurahi sana kama likizo yangu hii ningekwenda kusalimia Tanzania” Janeth Tuntu Elizabeth kama alivyokuwa anajiita alikuwa akimueleza baba yake Mr Robinson walipokuwa katika mgahawa mmoja huko Helsinki, katika mapumziko yao ya mwisho wa mwezi.

“Ni sahihi kabisa, lakini utafikia wapi na kule hauna ndugu unayemjua?” Mrs Robinson alimuuliza.

“Mmmm hapo ndio kazi ipo, ntafikia hotelini” alijibu.

“Hapana. Utafikia ubalozini na huduma zote watakupatia wao nitwaambia, je ungependa kwenda lini?” Mr Robinson alimuuliza Tuntu.

“Mwezi huu nipo likizo daddy, lakini pia ninapenda kwenda kutembea sehemu mbalimbali za Tanzania” Tuntu alijieleza.

“Usijali kila kitu nitapanga tukirudi” Mr Robinson alijibu huku akijinyanyua kutoka katika kitanda alicholalia wakati akipunga hewa katika pwani ya Hietaranta, pwani ambayo watu wengi walipenda kwenda hasa kipindi cha joto kwani maji yake huwa ya vuguvugu na mazuri kuuogelea.

Jane Tuntu Elizabeth, baada ya masomo yake ya awali na kufanya vizuri, sasa alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wanaochukua masomo ya sheria katika chuo kikuu cha Helsinki, Finland, bado akiwa katika chuo hiko alionekana jinsi alivyo hodari katika masomo yake. Hakuna mkufunzi asiyemjua Tuntu kutokana na kuwapo uhaba wa weusi kati nchi hizo za Scandnavia. Tuntu alikumbuka sana nyumbani na sasa aliomba kutumia likizo yake kwao Tanzania. Bila kinyongo alikubaliwa wazazi wake wa kufikia na kuja Tanzania kama mgeni kwa maana hakujua hata ndugu mmoja wa kufikia kwake. Lakini nyumbani ni nyumbani na mwenda kwao si mtoro.

HATIMA

Maisha yana mambo mengi, mazuri kwa mabaya. Kila mtu anaona kwa jicho lake, uonavyo wewe si nionavyo mimi.

Tunatakiwa kuwasaidia wenye shida bila kuwabagua, kuwatendea haki pa si kujali maana kuna leo kuna kesho hujui huyo unaemtendea hayo utamkuta wapi kwani ramani ya maisha ya mwanadamu ni Mwenyezi Mungu pekee aijuaye.

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment