Saa la 25 Sehemu ya Tatu
NEW AUDIO

Ep 03: Saa La 25

Saa la 25 Sehemu ya Tano
Saa la 25 Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE (AMATA GA IMBA)


Simulizi: Saa La 25

Simulizi : Saa La 25

Sehemu Ya Tatu (3)

Ashura alijikuta hana la kufanya, alikaa kwenye chumba kizuri ambacho hakuwa kuingia maisha yake yote isipokuwa leo. Moyoni alijifariji akijua kuwa labda bosi kamuweka hapo kwa muda.

Mara mlango ulifunguliwa, Pedeshee Masharubu akingia na kufunga mlango nyuma yake. Ashura alibaki kumtazama tu, huku ameketi juu ya kiti kilichopo ndani ya chumba hicho.

“Mrembo, hujalala? Afadhali umenisubiri, mi nilijua nitakuta umelala” Masharubu aliweka pembeni mkoba wake, akavua kofia yake aina ya pama ambayo daima ilikuwa haiktoki kichwani. Akamsogelea Ashura na kuanza kumpapasa papasa matiti yake madogo. Ashura alimsukuma kwa nguvu Pedeshee.

“We mtoto jeuri ee!?” Masharubu aling’aka, akamsogelea tena, mara hii alipata kofi moja la uso kutoka kwa Ashura, kofi lile lilimuingia barabara Masharubu, hasira zikamshika, akavua mkanda wake wa ngozi na kumtandika Ashura. Ashura alipotaka kulia, Masharubu alimuonesha ishara ya kunyamaza, kisha akamchapa tena kwa kutumia ule mkanda, Ashura alipata maumivu makali sana, mkanda ule ulimchubua sana kutokana na vyuma vilivyokuwapo humo.

“Panda kitandani!” Masharubu alimuamuru Ashura, Ashura aliendelea kulia kwa uchungu bila kutoa sauti.

“Nasema panda kitandani, na leo utanikoma” Masharubu aling’aka kwa hasira huku akifungua vishikizo vya suruali yake, alipomaliza aliitupia pembeni na kumnyanyua Ashura ambaye wakati huo alikuwa amejikunyata kwenye kiti akilia, alimtupia kitandani na kuanza kumvua nguo zake kwa nguvu. Ashura alijaribu kujinasua lakini haikuwa rahisi, akiwa kama alivyozaliwa pale juu ya kitanda, hakuwa na la kufanya. Masharubu aliiende suruali yake kuchukua kitu Fulani. Ashura alinyanyuka na kutoka kitandani, Masharubu alimuona, akaacha kufanya analotaka na kumfuata Ashura

“Rudi kitandani Malaya we! Ukileta mchezo nakuua” Masharubu alimkaripia Ashura huku akiuchukua tena mkanda wake, alimchapa Ashura, Ashura hakuweza kuvumilia tena alinyanyua chupa ya kubwa ya dompo na kumpiga Pedeshee kichwani, Perdeshee aliyumba na kuanguka chini, kabla hajakaa sawa alikutana na chupa ya konyagi iliyopasukia usoni, Pedeshe Masharubu alichanika vibaya usoni na kichwani, damu zilitiririka na kuchafua shati lake alilovaa, alitulia kimya sakafuni. ‘Nimeua, mama yamgu mimi’, Ashura alijililia moyoni huku mkono wake mmoja kajishika kichwani na mwingine akiupigapiga. Kwa haraka alivaa gauni lake hakukumbuka nguo nyingine, akauendea mkoba wa Pedeshee alipoufungua alikuta maburungutu ya noti yamejifungafunga, akatetemeka sana afanyeje, achukue moja nyingine amuachie, au abebe begi zima, swali halikuwa na jibu, akabaki mdomo wazi.

Alitazama uku na huku kama kuna mtu mwingine anayemuona, alisahau kama yuko chumbani. Aliingiza mkono katika begi lile na kutoa bulungutu moja na kuyaacha mengine, akauendea mlango ili atoke nje. Alipofika mlangoni alisikia sauti za watu wakija upande huo huku wakiongeaongea aliogopa sana, akasubiri kidogo, akatazama tena begi lile ‘utajilaumu baadae’ sauti ya ndani ilimwambia. Akaona ujinga, alirudi na kuchukua begi zima kisha akatoka kana kwamba hakuna tatizo. Alitembea hatua za haraka haraka na kuziendea ngazi ambazo zilimpeleka mpaka chini, alipofika mapokezi hakuangalia mtu moja kwa moja alitoka nje na kuvuka barabara ya Morogoro, moja kwa moja aliiendea bajaji iliyokuw imeegeshwa hapo. Hakujua anaelekea wapi, mawazo yote yalikuwa kule alikomuacha Pedeshee, moyo wake ulimsuta, hakujua kama kaua au la.

“Anti mbona husemi tunaelekea wapi?”

“Niache Kimara mwisho” aliropoka wakati hata Kimara yenyewe haijui.

Muda kidogo walifika Kimara. Ashura akashuka na kumpa dereva wa bajaji noti ya elfu tano, hakudai chenji akapotelea mitaani na mkoba wake.

Akiwa ndani ya chumba kidogo, Ashura alijilaza katika kitanda kidogo chenye shuka kuukuu, usingizi haukuja kirahisi, alihisi kama anafuatwa mara kwa mara alishtuka kwa hofu. Alijilaumu kwa nini amechukua begi lile ambalo sasa lilikuwa likimtesa nafsi yake. Ashura hakujua la kufanya, moyoni alimlaumu sana Zai kwa kumdanganya, upande mwingine alimshukuru kwa kuwa sasa kapata pesa za kutosha kufanya lolote. Lakini alijiuliza itakuwaje watakapogundua kuwa yule Pedeshee amekufa mle chumbani, kama jina lake lilikuwa limeandikwa kwenye kitabu cha wageni. Upande mwingine aliona kuwa ni bora Pedeshee afe tu ili asifanye lolote maana kama atapona lazima atamtafuta kwa hali na mali.

Ashura aliuvuta ule mkoba na kumwaga yale maburungutu ya noti kitandani, lo! Hakuamini macho yake, noti nyekundunyekundu nyingi zilizofungwa katika mabunda kwa rubber band yalidondoka kitandani, kwa haraka haraka yalikuwa kama kumi na mbili, alipoingiza mkono ndani ya begi hilo kuona kama yameisha, alihisi anashika kitu cha baridi akakishika kwa kukipapasa akili yake haikugundua ni kitu gani, akakivuta nje, bastola! Ashura alitetemeka na kuitupa chini. Akili ilimzunguka hakujua afanye nini na bunduki hiyo, alibaki ameduwaa na kuishngaa bastola hiyo. Akiwa katikati ya mshangao uliochanganyika na mawazo, alisikia mlango ukigongwa, aliutazama kwa jicho baya na kuanza kusombelea yale maburungutu katika kile kibegi.

€ € € €

Zai alikosa raha, hasa baada ya kuona ukimya mkubwa si kwa Pedeshee wala Ashura, moyoni aliilaumu nafsi yake kuwa bahati kampa Ashura, labda wawili hao wanakula maisha kwenye mji Fulani na hoteli kubwa, kwani alimjua fika Pedeshee kuwa hakutaka shida kwa kitu alichokichagua hasa totos. Lakini haikuwa kawaida ya Pedeshee kuwa kimya, angeshamtumia meseji kusifia kitu alichopata. Hali hii ilimfanya Zai kukosa raha kabisa. Siku hii alichelewa kuamka, alikuta Kautipe ameshaandaa kila kitu mkekani, chain a karimati nne.

“Da Zai, Ashura mpaka saa hizi! Kwani kaenda wapi?” Kautipe alimchokoza Zai kwa swali lililochoma moja kwa moja fikra zake.

“Atarudi tu! Hebu we kunywa chai mi narudi sasa hivi” Zai alimwambia Kautipe, harakaharaka alivaa nguo yake na viatu, akachukua mkoba wake na kuondoka hata alisahau kama hajachana nywele, alikuwa anenda wapi hakujua, ilimradi tu safari. Kila alipompigia pedeshee kwa namba zake zote hakupatikana, jibu lilikuwa lilelile ‘labda jaribu baadae’.

“Mh! Utakuwa ushamuuza mdogo wako!” mmoja wa rafiki zake alimwambia Zai ambaye alionekana kuchanganyikiwa kwa kiasi kikubwa. Maswahiba zake walimpa maneno mengi sana ambayo kwa kiasi Fulani yalimtia kiwewe Zai, hakujua aamue lipi na apuuze lipi. ‘Bora nisingempeleka’ alijiambia moyoni, ‘au niripoti polisi?’ akajiuliza. Aliinua simu yake tena na kuipiga namba ya Pedeshee, jibu lilikuwa ni lilelile tu, hakuna mabadiliko, pepo wa mahangaiko alimkumba, Zai hakujua afanye nini, masaa kwa kwake yalienda mbio sana alitamani baada ya saa sita usiku basi lije saa lingine kabla ya saa saba, saa la ishirini na tano!

€ € € €

Nukushi iliyopo ndani ya ofisi ya Bw. Robinson ilitoa ukulele wa kuashiria kuwa kuna ujumbe wa kupokelewa, Bw. Robinson aliiruhusu na karatasi hiyo kuanza kujiandika polepole, ilipoishia aliivuta na kuitoa pale ilipo na kuanza kuisoma, alikunja sura, na kutabasamu kwa wakati mmoja.

Alipomaliza kazi moja kwa moja alimpitia mkewe kazini kwake na wawili hao wakaelekea nyumbani.

“Darling, nina supraiz nataka kukwambia!”

“Mmmh what beibi?” Bi. Robinson aliuliza kwa kudeka huku akijigeuzageuza kifuani kwa mumewe. Bw. Robinson akaivuta ile karatasi na kumpatia mkewe, mkewe akaisoma kwa makini nakuirudiarudia kana kwamba hakuielewa.

“What?!” aliuliza kwa mshangao mkubwa, akiweka katika kijidroo kilichopo pembeni mwa kitanda chao, akazikusanya nywele zake ndefu na kuzifunga pamoja, kisha akamwangalia usoni mumewe kabla ya kumpiga busu la kimahaba.

“Lini?” akamuuliza mumewe kwa sauti ya upole.

“Wiki ijayo, inabidi tuondoke” Bw. Robinson alimjibu mkewe.

Bw. Robinson alikuwa amepata barua ya kuombwa kubadilisha ofisi ya kazi kutoka Tanzania na kuhamia mahali pengine nje ya Afrika. Kwake halikuwa swala gumu kwani hakuwa na familia, ni yeye na mkewe tu. Walishapita nchi nyingi sana kuishi kwa vipindi tofautitofauti, walihamia Tanzania miezi minne tu iliyopita na sasa wanapata tena uhamisho kuelekea nchi nyingine katika bara jingine.

Mipango ya safari ilifanyika na kwa kuwa wao walikuwa wakifanya kazi katika ofisi za kibalozi haikuwa shida kukamilisha mambo yote kwa wakati mfupi.

Walikaa na kufikiri juu ya Tuntufye ‘Jane’, kama wao wanaondoka yeye wamuache vipi na wapi wakati mpaka muda huo hawakuwa hata wanajua wazazi au ndugu zake. Jane alishawaeleza tu kuwa hamjui baba, na hajui mama alipo. Hilo likawa swala gumu kwa wawili hawa, kweli hawakujua wafanye nini, walibaki kuhangaika juu ya hili.


“Tatizo lenu ubishi umewajaa!” alizungumza dada wa Mzee Njiku huku akiingia ndani ya gari ya kaka yake “nilishawaambia, huyu kalogwa hamkutaka kusikia, kiko wapi sasa!” alimaliza kusema huku akikaa vizuri kitini.

“Lakini maadamu tumejua hili, tumsake yule mwanamke mchawi kabisa” kaka mtu alisisitiza huku akiwasha gari na kuingia kwenye barabara hizo za vumbi kurudi mjini. Walimrudisha kwa nyumba ndogo yake na kumuacha hapo.

Mzee Njiku aliishi kwa shida sana siku hizo, manyanyaso ya kutoka kwa nyumba ndogo hiyo yalizidi, wakati mwingine alishinda bila kula ‘nani akupikie! Anayekaa nyumbani ndio aingie jikoni’, hayo ndiyo yalikuwa majibu.

Usiku mmoja alisikia kelele za watu wakiongea sebuleni, sauti za kilevi zilipenya masikio yake, kwa kuwa alikuwa katika lindi la usingizi alijua ni moja ya ndoto za siku hiyo. Mara alihisi mtu akimsukasuka kumsogeza pembeni.

“Toka! Kakae sebuleni mwanaume gani wewe, watu tuna mambo yetu” kwa sauti ya kilevi akiwa anapepesuka huku upande mwingine akikokotana na mwanaume wakiingia chumbani humo. Nyumba ndogo, alimfukuza chumbani mzee Njiku na kumfukuzia sebuleni. Mzee Njiku alipepesuka na kujigonga mlangoni baada ya kusukumwa na mwanaume mwenzake huyo ndani ya nyumba yake, aibu! Alihisi maumivu kichwani alipojishika alijikuta ana damu mkononi japo si nyingi lakini damu. Alijikongoja hadi sebuleni huku akiwa na taulo lake kiunoni.

Kutokana na afya yake kuwa dahaifu sana, Mzee Njiku aliombwa kustahafu kazi na kuahidiwa kinua mgongo baada ya muda mfupi. Siku hiyo ilikuwa ngumu kwake, alipompa tarifa hiyo nyumba ndogo wake, ugomvi mkubwa ulizuka ‘uhame nyumba hii!’ ndiyo kauli iliyosikika mara kwa mara ndani ya nyumba hiyo. Majirani walipita mbali, hakuna aliyesogea kutoa msaada. ‘Amezidi, kamuacha mkewe kwa kudanganywa na Kahaba’ mmoja wa wapiti njia alisema, ‘dawa hizo, kalishwa na kuogeshwa’ mwingine aliongezea. Mzee Njiku alisukumiziwa nje na kurushiwa kibegi chake ahame. Atafanya nini, alibeba kibegi chake na kushika suruali yake ili isidondoke, shati lake la Juliana lilikuwa likipepea kwa upepo, shati ambalo lilikuwa likimkaa vyema mwilini mwake, sasa lilipepea kana kwamba ndani yake hakukuwa na mwili wa binadamu.

Alisimama mbele ya nyumba yake aliyokuwa akiishi na na mkewe wa kwanza, mkewe wa ndoa, mwalimu wa shule ya msingi, aliyemuona hana maana hata, akishirikiana na dada zake hata kuhakikisha yuko jela miaka mitatu, ukiangalia kisa mapenzi, kapata kitu kipya, ama kweli kipya kinyemi ingawa kidonda na Mkataa pema pabaya panamwita.

Machozi yalimtoka, akiitazama nyumba hiyo kubwa ambayo aliijenga pamoja na mkewe wa ndoa kwa tabu sana. Sasa ilikuwa mali ya mtu mwingine, alishaiuza na pesa zote kutumbua na kimada huyo, lo! Mzee Njiku aliketi chini, mchana wa jua kali, waliomjua walimpita tu na kumwangalia, hakuna msaada amlilie nani.

Breki ya pili ilikuwa kwa kaka yake kumlilia hali, akakaribishwa japo kwa siku chache ili ajisitiri wakati akitafuta mahali pa kuishi. Ndugu zake walikutana kujadili yaliyomkuta mwenzao, hasira zikatawala vichwa vyao, chuki zikajaza nyoyo zao ‘atatutambua mwanamke huyu!,’ mwanamke aliyependwa na wifi na shemeji zake, leo hii wapendwa hawa wanatamka haya. Wakaahidi watahakikisha haki inatendeka mpaka nyumba ile ya nyumba ndogo kwa kuwa ni mali ya kaka yao. Kesi ikapelekwa polisi, jalada likafunguliwa, mahakama ikachukua mkondo wake, wakati huo Mzee Njiku bado anaegesha kwa kaka yake.

€ € € €

‘Mh! Polisi au nani?’ Ashura alijiwazia, akafunga vizuri kibegi kile na kuiweka sawia zipu ya begi lile, akatazama huku na huku hakujua la kufanya, chini pale aliiona bastola ile ikigaagaa, aliitazama kwa macho yake mawili, hapo akapata picha kumbe yule jamaa ni jambazi. ‘Zai alikuuza, Zai ni mbaya sana’ upande mmoja wa roho yake ulimwambia, alishikwa na hasira juu ya Zai, akapata taswira mbaya kabisa, ‘alitaka iweje?’ Ashura alijiuliza, akashtuliwa na hodi nyingine, sasa ilikuwa ya nguvu kidogo. Akatzama huku na huku, akaona wazi kuwa kama ni polisi watamkamata tu, hana la kufanya, akauende mlango taratibu akachungulia kwenye tundu la ufunguo ‘polisi!’, hakika Ashura alitamani ardhi ipasuke, alijua sasa mwisho wangu umefika, kujisalimisha utakuwa ujinga afanye nini, akili ikarudi, alitazama juu ya dali akaona kuna ceilingboard safi na kajimlango kadogo, kitendo cha haraka aliichukua ile bastola na kuitia katika kile kibegi, akachomoa noti kiburungutu kimoja na kukificha kwenye taiti yake aliyoinunua jana jioni baada ya kuacha nguo za ndani kule hotelini, akasogeza kiti na kukipandisha juu ya kimeza taratibu akweka kile kibegi chake ndani ya dari na kurudishia kajimlango kale

.

“Karibuni!” Ashura aliwakaribisha polisi wale wawili, mmoja wa kiume mwenye bunduki na mwingine wa kike. Yule wa kike akaingia ndani na kumuacha wa kiume mlangoni pamoja na mhudumu wa guest hiyo, alikiangalia chumba kile kwa macho ya kipolisi, aliinua godoro na kutazama uvunguni, kasha akaelekea chooni ambako hakukuwa na kitu zaidi ya sabuni ya kuogea na ndoo, alipekua hapa na pale kisha akaangalia juu dalini. Ashura ilibaki kidogo mkojo umtoke, alijua sasa siri kubwa itagundulika, alijikaza kiumwanamke lakini alihisi kama anaishiwa nguvu. Yule askari akatoka chumbani mle.

“Sio penyewe, hamna kitu” alimwambia yule wa kiume kasha wakaendelea chumba kinachofuata. Ashura bila kuchelewa, alitoka hadi kaunta na kukutana na mhudumu wa hapo.

“Dada, nina dharula naomba kurudisha chumba kama nitarudi nitakujulisha” alilipa chumba na kuondoka zake, alishuka ngazi haraka haraka, mpaka barabarani, lakini kabla hajaendelea zaidi kuelekea asikokujua akavutiwa na kundi la watu waliozunguka mbao ya magazeti. Nae akajipitisha kuona kilichowakusanya ni nini. ‘Jambazi sugu lanaswa limekufa hotelini’, gazeti moja la kila siku liliandika habari hiyo na kuweka picha ya mtu huyo, Ashura alipoiona picha ile ‘rudisha begi langu’ alihisi kama picha hiyo ikimsihi. Akavuta hatua chache na kupotelea mtaani. Breki ya kwanza ilikuwa ni dukani kwa msambaa kulikokuwa kukiuzwa kila aina ya nguo, aliijua aitakayo, baibui nzuri ya kufunika mwili mzima.

€ € € €

Mama Njiku alichanganyikiwa, hakumuona shoga yake mpaka siku ya pili, nini kimempata hakujua, kama kafa hakujua, kama anaumwa yuko hospitali hakujua.

Jua lilizama, kukakucha. Aliwatazama watoto wale wa mama Vituko ambao usiku wote walikuwa wakimlilia mama yao bila msaada. Mama Njiku hakuwa na la kufanya, aliichukua simu yake na kumpigia mama Minja wa Manyoni.

“Nimemsubiri sana jana hapa stendi lakini sijamuona” sauti ya mama Minja ilimkosesha raha mama Njiku ‘kanitoroka, kaniachia watoto’ , mama Njiku aliangusha machozi huku akiwatazama watoto wale na wa kwake waliokuwa wakinywa chai asubuhi hiyo, ‘mama atarudi sasa hivi’ aliwafariji, lakini ukweli ni kwamba hakujua nini kimempata shogaye.

“Hapa aliondoka jana asubuhi kuja huko lakini hata sasa hajarudi” alimueleza mama Minja ambaye nae kwa upande wake alipigwa na butwaa kwa tukio hilo.

Siku ilikuwa ni ngumu kwa Mama Njiku, kazi haikuweza kufanyika, kichwa chote kilisambaratika kwa mawazo pa si na majibu.

Mara nyingi alionekana akiegemea mlango kuangalia labdashigaye huyo atatokea hapa au pale lakini haikuwa hivyo, roho ilimuuma kwa uchungu masaa yalienda mbio kuliko siku zote, mara jioni ikaifukuza mchana na usiku ukatawala. Mama Njiku hakusikia hodi wala mlango kusukumwa.

€ € € €

“Umeuza mifugo, ukatoroka kijijini. Andika maelezo hapa kwenye karatasi hii” polisi mmoja alimwambia mama Vituko kwa ukali na kumwangalia kwa macho yaliyoonekana kuchakaa kwa kila namna na gongo.

“Mbona mi siwaelewi, nani aliyesema mi nimeuza mifugo huko nilikotoka?” Mama Vituko alijaribu kuwaelza askari wale huku akibubujikwa na machozi.

“Hayo mama utajibia mahakamani sisi hapa wajibu wetu tumemaliza sawa, haya andika.”

Kwa kauli za askri yule mama Vituko alielewa kuwa hapo kuna mchezo uliofanyika, alishangaa sana kuambiwa kuwa eti kosa lake ni kuuza mifugo kasha kutoroka kijijini. Mifugo ya kwake, mashamba ya kwake, baada ya mumewe kufa ndugu wanataka mali, leo tena etyi kauza mifugo na kutoroka kijijini, anatafutwa, amepatikana. Mama Vituko alibaki hana cha kufanya aliumia sana lakini alijuwa wazi kuwa kwa vyovyote ni njama tu za ndugu wa mumewe baada ya kuona kakataa kurithiwa na kaondoka nyumbani bila kuaga. ‘Wanataka nini kwangu, masikini mimi? Kila kitu nimewaachia bado tu’, Mama Vituko alijiwazia moyoni huku akiandika maelezo yote kadiri ya anavyojua.

“We mwanamke! Mbona umeandika tofauti na maelekezo?” yule askari alimkaripia mama Vituko kisha akaendelea “sie tumepata oda ya kukutafuta, hivyo kesho utarudishwa kijijini ulikotoroka ukasomewe kesi yako huko” yule askari alimaliza kuzungumza na kufunga faili lake kuukuu ambalo lilitimua vumbi kiasi Fulani katika ile meza yake.

Mama Vituko alirudishwa selo kusubiri hatima yake ambayo hakuijua ni nini mwishowe. Aliendelea kusota selo bila kujua lini atatoka. Alikaa ndani mle bila msaada, hakuna wa kuleta chakula, hakuna kuoga, siku hizo chache zilimfanya abadilike hata kuonekana kama msukule. Na hii ndiyo hali halisi iliyopo katika vituo vyetu vya polisi, watu walioonewa na kubambikiwa kesi wanajazwa, polisi wanawanyima haki zao badala yake unyanyasaji ndiyo unaoshika hatamu.

Baada ya kutoka katika nondo zile alipokuwa amesimama akiongea jambo na askari mmoja wa kike Jarina alirudi na kuketi karibu kabisa na mama Vituko.

“Vipi shoga!” mama Vituko alimuuliza Jarina, msichana waliyekutana naye umohumo selo.

“Mshua anataka kunitoa, nirudi uraiani” Jarina alimjibu Mama Vituko. Mama Vituko aliposikia habari hiyo kwake ilikuwa ni furaha sana maana aliona kuwa sasa atapata msaada kwa namna moja au nyingine. Aliongea naye kwa kirefu na kumpa maagizo Fulani ya kufanyia kazi akiwa huko uraiani ili kumsaidia, mojawapo lilikuwa ni kuoeleka taarifa kwa shoga yake Mama Njiku ambaye mpaka muda huo alikuwa hajui lolote.


Maisha mapya aliyoyaanza Tuntufye ‘Jane’ yalikuwa kama ndoto machoni mwake, hakuamini kilichopo mbele yake wala anachokiona. Kila akigeuka ni watoto wa kizungu tu, majumba makubwa na magari mazuri mazuri yalikuwa yakipita uko na huko. Watoto wa kizungu walikuwa wakimshangaa huyu mtoto mweusi, Tuntu alikuwa ameasiliwa na familia ya Robinson, na baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria waliondoka naye na kuhamia ughaibuni kikazi,sasa wakiwa na mtoto wao huyo waliyempa rasmi jina la Jane ‘Tuntu’ Elizabeth Robinson.

Jambo la kwanza walimpeleka shule ya elementary, ambako alijifunza mambo ya msingi kama lugha na vitu vidogo vidogo, na alionekana kuelewa kwa haraka sana, maisha yake ya ukarimu na upole yaliwavutia wengi wakiwemo waalimu na hata wazazi wa watoto wenzake. Jane Elizabeti ‘Tuntu’ , msichana aliyekulia mitaani huko Afrika Mashariki, aliendelea na maisha mapya huko Stokholm, Sweeden na kuanza kujenga msingi mpya wa maisha, polepole alianza kubadilika na kushahabiana na hali halisi na mazingira yaliyomzunguka. Katika yote Jane hakuweza kusahau jambo moja tu rafiki zake wa mitaani, mama na mdogo wake, Malogo.

€ € € €

Hodi iligongwa mara tatu hasa kwa sababu mlango huo haukufunguliwa. Ilikuwa imetimu kama saa mbili hivi usiku, Mama Njiku akiwa anawalaza watoto wake na wa mama Vituko baada ya kuwapa wali na maharage. Aliisikiliza hodi ile lakini alisita kwenda kufungua mlango, alijifikiria mara mbili mbili mwishoe aliinuka na kuuendea mlango.

“Nani?” hakujibiwa

“Nauliza, nani mwenzangu?” Mama Njiku aliuliza na kuganda pale mlangoni bila kufungua, sauti ya nje ikakohowa kikohozi kikali sana ambacho kwa mtu yeyote hata kama hakuwa na utaalamu wa utabibu angejua tu kuwa hiyo ilikiuwa ni TB na si kitu kingine. Mama Njiku alihisi huruma imemkaa moyoni, bila kujali kuwa mtu wa nje hajatamka kuwa yeye ni nani. Aliufungua mlango taratibu kwa hadhari kubwa sana.

“Haaaa!!” Mama Njiku alipata mshtuko wa moyo na ilibaki kidogo aanguke kama ukuta ule wa matope usingemkinga. Alijaribu kujikaza kiuanamke na kumtazama mtu yule japo kwa mwanga hafifu wa koroboi, mtu mwembamba, mrefu, aliyechoka kwa kupigwa na maisha katika nyanja zote, alisimama kwa shida akiyumba uku na kule, mkononi kashikilia mfuko mdogo wa Rambo uliionekana kuna kitu kama nguo. Mama Njiku alimtazama kwa makini mgeni huyu kuanzia juu mpaka chini, na kurudia tena na tena kufanya hivyo, akasonya na kuingia ndani ya nyumba yake, akageuka na kumtubia neon “Mimi si mchawi! mimi nimeiloga familia yenu! mimi nimekuroga, ukaanza vurugu ukafanya unachotaka ukishirikiana na dada zako, mkanifukuza na kifungo juu!” akashusha pumzi na kisha akaendelea kubwata kwa uchungu “Uliniona si mali mimi, ukanitupa kama tambala la deki, maisha yakakunyookea ukapata mke mwingine, liyependana …” Mama Njiku alianza kulia kwa uchungu, hata machozi yalipokatika Ligeuka mlangoni na kumkuta mgeni yule kasimama vilevile kama bismini la posta.

“Kimekuleta nini? Na nani aliyekuonesha nyumbani kwangu? Wewe! Afisa Elimu, ukae kwenye nyumba ya udongo kama hii!? Haiwezekani, Njiku ninayemjua mimi sio wewe”, Mama Njiku aliendelea kumshangaa mumewe wa zamani aliyekuja sasa akiwa mikono chini kuomba msaada.

“Sikiliza Mpe…”

“Nani mpenzi wako, usinishike staki. Kamshike uyo huyo” mama Njiku alikuwa mkali sana siku hiyo.

Mzee Njiku hakuwa na la kufanya, akiwa mkono mmoja kashikilia Rambo yake na wa pili kashikilia suruali yake ambayo inaweza kumdondoka muda wowote, alipiga magoti na kuomba msamaha kwa mkewe huyu, ama kweli fahari akivunjika mguu urejea zizini. Machozi yalimtoka, kilio cha toba iliyochanganyika na niwie radhi viliingia masikioni mwa Mama huyu aliyekua kasimama tu akimwangalia mzee huyu akilia kama mtoto.

“Nimekosa mimi mke wangu, marafiki na pombe vilinidanganya.” Mzee Njiku aliangusha kilio akiwa kapiga magoti katika sakafu ile ya vumbi ndani ya kanyumba kale ka udongo.

€ € € €

Kautipe alibaki hana la kufanya baada ya kukaa siku takribani mbili bila kumuona Ashura. Kila mara alimuuliza Zai, lakini jibu alilopewa ni lilelile ‘atarudi tu’, ingawa jibu lilikuwa jepesi namna hiyo lakini moyoni mwa Zai kitu hicho kilimpa mahangaiko makubwa sana.

Asubuhi ile alipokuwa kwenye pitapita zake aliona habari katika gazeti juu ya Pedeshee masharubu, hii ilimpa wasiwasi na homa isiyopimika ‘Ashura atakuwa wapi?’ alijiuliza pasi majibu.

Maisha yalikuwa magumu kwa Kautipe, ilikuwa haipiti siku mbili bila kukwaruzana na Zai, kwa kile Zai alichokiita ‘ugoigoi’, wakati mwingine hakuachiwa hela ya kula,. ilimuuma sana lakini hakuwa na la kufanya. Aliamua kujichanganya mtaani na wasichana wenzie kujaribu maisha kwa njia nyingine. Akiwa bado mshambamshamba katika jiji, vijana wengi walimtolea mate hasa kwa umbo lake alilojaliwa na Mwenyezi, ufupi na weupe wa wastani. Nani angeanza kumchokoza binti huyu? Hakuna, na haikuwa rahisi, daima alionekana kivyakevyake tu mtaani.

Siku moja akiwa dukani kununua sukari ndipo alipokutana na kijana mmoja mcheshi sana mwenye maneno mengi, kichwani alifuga rasta. Akaongea maneno mawili matatu na Kautipe, bila kuchelewa Kautipe akaingia kingi, wakiwa wanatembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea anakoishi Kautipe ndipo gari moja nyeupe aina ya landrover 110 ilisimama ghafla mbele yao, kama umeme vijana watatu walishuka na kuwakamta Rasta na Ashura na mojak kwa moja wakawapakia ndani.

Ashura alijaribu kujitetea huku na huku kwa vijana wale lakini haikusaidia kabisa kwani waliamuriwa kulala chini ndani ya gari ili wasione hata wanakopelekwa nao wakatii. Safari ikaishia Chang’ombe polisi.

“Kazi nzuri, leo mmempata ee!?” askari mmoja alionekana kuridhishwa na kazi ile, aliongea maneno hayo huku akijipigapiga kifimbo chake mkonopi.

“Chuchumaa chini!” amri ilitolewa, na wote wakatii, ashura na msichana mwingine wakatengwa na wale vijana wa kiume, wakakbidhiwa kwa WP mmoja aliekuwa jirani na hapo.

“Vizuri, huyu nae vipi?” yule askari mkubwa aliuliza.

“Huyu, tumemkuta na Rasta afande, lazima wanapiga kazi pamoja. Huyu msichana ni kama yule aliyetutoroka kule Mbagala” wale vijana wakamjibu afande huyo. Hapo ndipo Ashura akagundua kuwa kaingia katika kesi isiyo yake, alibaki kutoka machozi tu hakujua hata ni nini kinachoendelea, alijaribu kumsemesha yule WP lakini haikumsaidia, polisi ni polisi tu hata kama ni ndugu yako.

“Huyu nae analia nini hapa?” yule askari mkubwa alimuuliza yule WP

“Ana yake tu afande, anasema ahusiki wala hajui kinachoendele” yule WP alijibu huku akiwa kasimama kiukakamavu kuonesha nidhamu ya kijeshi.

“Binti, aliyekamatwa na ngozi ndiye mwizi wa nyama, usijali, utakuwa huru tu muda si mrefu, hatuwezi kukuweka hapa wakati huna kosa.” Yule askari mkubwa alimpoza Kautipe.

Mara wote wakaingizwa ndani ya jingo lile, wanaume upande wao na wanawake pia. Wakati wanaingia kwa mbali aliweza kushuhudia Rasta akipata kipigo kikali kutoka kwa polisi kabla ya kufungiwa kwenye nyuma ya zile nondo za chuma.

Joto halikuwa la kawaida katika kichumba hiko, Kautipe aliketi chini na wanawake wenzake waliooneakana katika pause tofauti, wengine wachafu, nywele timtim, wanaotoka maudenda umo humo, ilimradi tu walikusanyika watu wa nyanja zote za mtaani. Kautipe aliogopa sana hali hiyo kwani hakuweza kuishuhudia hapo kabla. Mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea mle ndani yalimvutia sana.

“Oya, we Choko,” mwanamke mmoja wa makamo alimwita mwenzie, huku akiwa katoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango “Eti pusha kaletwa mwana?” swali lile lilituwa masikioni mwa Kautipe hata kama halukumuhusu, alimwangalia mwanamke yule aliyechoka lakini hakuweza kujibu.

“Kaja, nimemuona muda si mrefu vijana wakimpa kibano cha mbwa mwizi, su, siijui imekuwaje safari hii, Kamanda kaingia tunduni mwana” sauti ilitoka upande wa pili wa chumba kile. Kautipe alipogeuka aligundua kuwa yule aliyejibu alimuona pale mlangoni kabla hajaingia katika selo hiyo.

“Nimepata habari njema” sauti ya askari mmoja ilisikika kwa nje, Kautipe aliisikia vizuri sana sauti ile na alihisi kama anaifahamu “ Mmemtia mkononi kubwa lao” alimalizia.

“Ndiyo afande!” alijibiwa.

“Safi sana, msumbufu sana huyu, sasa leo atatukoma” yule askari alimueleza mwenzake huku akionekana wazi kufurahia.

Rasta, kama alivyojulikana mjini, alikuwa kijana anayeishi ghetto huko Mbagala kwa mgeni nani, lakini daima alivinjari kona nyingi za jiji hasa wilaya ya Temeke. Hakuwa na kazi ya maana sana ukimuona, lakini daima hakuishiwa pesa ya kutumia. Alikuwa akimiliki gari ndogo ina ya Toyota Sprinter. Vijana wengi wa Temeke, Tandika mapaka Mbagala waliharibika akili kwa ajili yake, dawa za kulevya za kunusa, kujidunga sindano, bangi na hata kusafirisha unga hapa na pale ilikuwa ndiyo kazi yake maalum iliyomuweka mjini. Polisi walimtafuta sana, mara nyingi alikamatwa na kuwekwa kituo kidogo cha polisi Tandika na kesho yake tu watu wanamuona akitembea kwa mwendo wake wa kujidai mtaani akitamba kwa neon hili na lile, ‘Polisi kitu gani, pesa kidogo tu unatoka. Mtafungwa ninyi masikini, chezea pesa wewe’. Mara nyingi alitamka maneno hayo kwa nyodo. Wazazi ambao watoto wao wa kike kwa wakiume walikuwa wameshakuwa mataahira walipatwa hasira sana kwa sala hili, kila wakitoa taarifa polisi kuwa jamaa yuko sehemu Fulani, wanamkamata lakini kesho yake yuko uraiani. Wazazi wachoka ndipo walipoamua kupanda ngazi ya juu, kituo cha wilaya ya Temeke, wakasikilizwa na msakao ukaanza. Mara ya kwanza walimkuta huko Mbagala Kizuiani, kazi ya kumkamata haikuwa ndogo kwani vijana mateja japo walikuwa wamechoka sana walivurumisha mawe ya kutosha dhidi ya gari ya polisi, walikamatwa baadhi ya vijana akiwemo msichana mmoja aliyeonekana amekubuhu kwa kila kitu. Lakini kukurukakala, msichana yule aliwatoroka polisi na Rasta alikamatwa hata kufikishwa mahakamani lakini hakuna ushahidi, yuko huru. Kama kawaida, alitamba mtaa mzima kwa maneno yake ya kejeli huku akiimba nyimbo za Luck Dube na Bob Marley akijiita yeye ni freedom fighter.

Katika sakata lingine huko Mtoni alimuumiza polisi mmoja na kumchania sare yake, hapo sasa ndipo alipowatibua maswahiba zake hao, aliokuwa akiwapa hongo kila kukicha na kutamba mtaani. Alisakwa kwa udi na uvumba katika magheto yote huko Temeke, kila kijana aliyefanana na bangi au unga aliswekwa ndani na kichapo kikali ili aseme freedom fighter yuko wapi.

Kwa tukio lile Rasta alijificha maeneo ya Tuwangoma maana alijua alichokifanya siyo.

Siku ya tukio asubuhi, alikuja mara moja kwa Mangi kuchukua malipo yake baada ya Mangi kusukuma mzigo chini kwa chini, ndipo alipokutana na Kautipe, mtoto wa Kihehe kutoka Mawambala, mfupi, mnene, weupe wa sekunde. Rasta alipomuona Kautipe, mate yalimjaa akaanza swaga zake kwa Kautipe, ujanja hamna Kautipe akalowa kwa maneno na lafudhi ya ulimi wa kijana huyu, lo! Laiti angemjua basi angekaa mbali maana wasichana wengi walionasa mtego huo wameishia Keko na Ukonga, baada ya kuwatumia basi aliwabebesha mzigo na wengi kukamatwa.

Kautipe, alijikuta akizolewa na askari waliovalia kiraia ambao walimtaka hasa Rasta, lakini wote walikusanywa na kulundikwa selo huko Chang’ombe.

Kautipe anakutana na kizazi kingine, kizazi cha wabwia unga na wavuta bangi.

“kwa hiyo huyu ndiyo alikuwa Malkia wetu kwa sasa! Eh mzuri huyo.” Yule mwanamke aliyechoka kwa ulevi wa dawa alimueleza mwenzake huku udenda ukimtoka. Kautipe aliju wazi kuwa asemwaye ni yeye katika hilo lakini hakutaka kabisa kujibizana na wawili hao.

“Ah! Ras we, bora na wewe umeingia huku mwana, utakapoinuliwa utuvute na wenzio” yule mwanamke aliendelea na maneno yake. Ndani ya selo hiyo ndimo Kautipe aliposikia habari nyingi za Rasta, japokuwa maisha ya humo ndani hakuyafurahia lakini kiasi Fulani alijifunza mengi ya dunia kutokana na waliokuwemo humo.


Simu ya Mama Njiku iliita, na bila kusita aliipokea japokuwa ilikuwa namba ngeni.

“Halo, Eee nakusikia!” Mama Njiku alisikika akijibizana na sauti ya upande wa pili.

“Unasema?! Polisi… wapi… Mayoni? Halo halo halo…” simu ilikatika. Mama Njiku alibaki akiitazama simu ile kwa uchungu huku akitetemeka kwa hofu. Alikuwa amepata habari isiyo nzuri juu ya shogaye Mama Vituko.

Akivuta kigoda na kuketi kisha akapata wazo, akampigia simu Mama Minja, naye alistushwa na habari hiyo ambayo hakuitegemea. Yapata siku ya nne tangu Mama Vituko atoweke, Mama Njiku alimlaumu sana kwa kutoroka bila taarifa ukizingatia a;iacha watoto wake kwake na makubaliano ilikuwa aende tu kwa Mama Minja kuitika wito, kujua alichoitiwa na kurudi. Lakini kutoonekana kwake kulimfanya Mama Njiku ahisi kuwa kwa vyovyote atakuwa amepitiliza, wapi? Hata yeye hakupajua.

Mama Minja bila kuchelewa aliwasha gari yake na kuelekea kituoni ili kuona ni nini anaweza kufanya ili kumsaidia Mama Vituko. Escudo nyekundu ilipaki mbele ya kituo kidogo cha polisi Manyoni stendi.

“Huyu Mama anafata nini tena?” mmoja wa askari aliyekuwa zamu alimuuliza mwenziye.

“We tulia kama anafaulisha tunakamata hela fasta, njaa kaka” mwingine alijibu

“We! Humjui huyu mama, tuulize sisi. Hapo hakuna hela, ukimuona kaja hapa ni msala tu kaka”

“Karibu Mama, karibu sana” yule askari alimchangamkia Mama Minja na kumkaribisha.

“Asante mi si mkaaji sana hapa, nina shida” mama Minja alijieleza huku akiiweka vizuri simu yake ya bei mbaya mkobani.

“Sasa, mama, huyo mtu unayemtaka ameshahamishwa asubuhi hii, kapelekwa kijijini kwao ambako kesi yake itakuwako” yule polisi alimueleza mama Minja. Mama Minja hakujua afanye nini, alibaki kimya kwa muda, aliiangalia saa yake ya dhahabu mkononi na baadae kuushusha mkono.

“Alikamatwa kwa kosa gani?” Mama Minja alimuuliza yule polisi ambaye alionesha dalili zote za ulevi wa gongo na sigara zisizo kipimo.

“Mama, sisi kazi yetu ni kutekeleza wajibu tuliopewa na wakubwa. Hapa tuliletewa oda ya kumtafuta na kumkamata kisha kumrudisha huko kwao, na ndivyo tulivyofanya. Kujua ni kosa gani anatafutiwa kwa kweli sisi tutakudanganya.” Yule polisi alimaliza mazungumzo yake na kuvuta faili lingine kuendelea na kazi.

Mama Minja alishukuru na kuondoka kituoni hapo huku akiwa kabaki na mawazo mengi kichwani juu ya mama Vituko. ‘Nini kimemsibu, mbona kwa jinsi alivyo haonekani kama mwanamke mwenye matatizo hata kutafutwa na polisi?’ Mama Minja alijiuliza bila majibu, kila alipomkumbuka Mama Vituko na ukarimu aliyomtendea siku ile alipopatwa na matatizo, moyo ulimuuma sana na alijikuta anapata shauku ya kujua kulikoni, moyo mwingine ulimwambia ‘achana nae, umdhaniaye ndiye kumbe siye’, alitafakari kwa kina na kuamua kufanya analoona yeye kuwa ni jema, aliwasha gari na kutokomea mjini, aliendesha kwa kasi ambayo kila mtu aliyemfahamu alishangaa.

€ € € €

Swali lililomsumbua kichwa ni ‘nirudi mjini au nipotee mbele kwa mbele?’, Ashura alijiuliza huku akiwa tayari kituo cha basi, nafsi ilimsukuma atoroke mji kwa kuwa alijua endapo watafanya uchunguzi juu ya kifo cha pedeshee yeye atakuwa ni mmoja kati ya watuhumiwa, hili lilimuumiza kichwa sana.

‘Hata nikitoroka Zai atanitaja tu’, kwa kifupi alichanganyikiwa, akaamua kuketi chini katika kituo hicho cha basi ili kutafakari cha kufanya.

Uamuzi ulokuja ni kurudi Tandika japo kwa muda mfupi, lakini fikra yake ni kwenda kumchukua Kautipe na kuondoka nae pa si Zai kujua.

Haikumchukua muda kufika Tandika. Aliingia kwenye moja ya mgahawa uliopo jirani na nyumba anayoishi Zai kwa minajiri ya kuona kama Kautipe atatokezea kwa nje ili atimize azma yake hiyo. Soda aliyoagiza ikaisha, akaagiza nyingine hata jua likachwea akiwa pale, hakuna aliyemgundua kuwa ni nani. Alinyanyuka taratibu na kuelekea kwenye nyumba ile aliyopanga Zai, kwa mwendo wa taratibu alizipanda ngazi zile na kuipita korido ndefu mapaka katika mlango wa Zai, alisikiliza kidogo kama kuna mtu ndani lakini kimya kilitawala, alinyonga kitasa na kusukuma mlango lakini ulikuwa umefungwa. Akauacha na kurejea nje, akiwa anashuka ngazi zile akakutana na mama wa chumba jirani.

“Samahani dada, eti huyu mpangaji wa chumba hiki yupo?” Ashura aliuliza kwa sauti ya chini kidogo, mama yule alimkazia macho kabla ya kumjibu.

“Zai hayupo, tangu aondoke jana hajarudi tangu aende kwenye mishemishe zake. Hapa alikuwa anakaa na wadogo zake wawili, mmoja kaondoka sijui tangu majuzi na mwingine leo asubuhi amekamatwa na polisi na fikiri yupo kituoni.” Yule mama alimjibu Ashura huku akipita pembeni yake na kupotelea ndani.

Ashura alibaki kapigwa na bumbuwazi, jibu hilo lilimuweka njia panda hakujua lipi la kufanya, ‘hapa mpango ushafeli’ alijisemea moyoni huku akitoka nje ya nyumba ile, kuelekea nje. Alipoufikia mlango tu alikutana uso kwa uso na Zai akiingia mlango wa uani. Ashura alitaka kumsalimu kwa kumkumbatia lakini aliona kuna vijana wawili wanaomfuata nyuma yake, alipowaangalia tu aliona kuwa vijana wale walionekana wako serious hawapo kimzaha kabisa. Silka ya Ashura ilimtaka kupita tu, nae akatii aliwapita pale mlangoni bila kujulikana kisha akatoka kwa nje na kusimama kando ya dirisha japo asikie watazungumza nini.

“Haya funua pale… na kule… fungua hilo begi. Ulipojua tunakuja ukaamua kuondoa misokoto yote ee?” sauti ilitoka ndani ya chumba hicho na kupita masikioni mwa Ashura, “usipotoa ushirikiano, yule mdogo wako ataozea jela”, ile sauti iliendelea.

“Jamani mimi sifanyi biashara hiyo”, sauti ya Zai iliyokata tamaa ilisikika kutoka chumbani.

“Haya, zungumza sasa, fanya mpango tukamtoe mdogo wako”, mmoja wa wale vijana alisikika akisema. Hapo Ashura aligundua kuwa kwa vyovyote hao walikuwa polisi na kuna kitu wanachokitafuta kwa Zai, moyo ulimuenda mbio hasa aliposikia wakimtaja mdogo wake, alijua wazi kuwa alichokifanya kimejulikana na anatafutwa, lakini hakuelewa ni nani wanayezungumzia kumuachia, hapo aliunganisha na majibu ya yule mama ‘na mwingine leo asubuhi amekamatwa na polisi’, Ashura alijikuta machozi yakimtoka, moja kwa moja aligundua kuwa Kautipe yuko matatani.

“Hiyo siyo hela ya kutupatia sisi, we si unajua ile kesi ya mdogo wako ni kubwa halafu utupe elfu hasini! Tafuta laki tano kabla ya jioni tumalize kazi, kumbuka kesho asubuhi anapanda kizimbani, tumemaliza, haya twende” Ashura alisikia maneno yale na mara alijikuta kama anayetaka kuropoka kuwa atatoa hiyo hela, lakini aliwahi kuudhibiti mdomo wake. Laki tano angeipata wapi? Anajuaje kama ile hela yake kule darini ipo salama, hapo alihisi moyo ukimdunda kwa nguvu akaanza kuyalaumu maamuzi yake, ‘kwa nini lile begi aliliacha darini’, alihisi kitu kama kizunguzungu. Ashura akatoka eneo lile na kuelekea pembeni kidogo, kisha kuchukua muda kuwaangalia wale watu walio na Zai wakitoka na kuingia kwenye gari ndogo nyeupe wakatokomea.

Ashura akiwa kwenye bodaboda aliifuatilia gari ile nyuma na kuona ikiishia kituo cha polisi Chang’ombe. Alilipa na kumuomba namba ya simu yule dereva wa bodaboda, “pindi nikikuhitaji ntakupigia” alimwambia. Alitazama yale maandishi makubwa meusi pale kwenye lango kuu la jengo lile yaliyosomeka POLISI CHANG’OMBE, kisha akapotelea anapopajua huku akifikiria kesho yake kuwahi mahali hapo asubuhi ili ajue mahakama gani Kautipe atapelekwa ili apate hatima ya shoga yake huyo.

ITAENDELEA

Saa la 25 Sehemu ya Nne

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment