Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Salamu Kutoka Kuzimu

Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Salamu Kutoka Kuzimu

Sehemu Ya Kwanza (1)

KIFO kaja duniani kwa kazi moja tu. Akikukuta umekwisha… Akikusalimia umekwisha… Hana mdhaha. Lakini sasa huyu anataka watu mashuhuri, watu wakubwa zaidi. Anataka kuifanya Afrika nzima iangue kilio na maombolezo ambayo hayajapata kutokea duniani. Na anataka hilo litokee siku moja, saa moja… “Bendera zote duniani zipepee nusu mlingoti”, anasema huku akichekelea. “Sijawahi kushindwa…” Jasho linawatoka watu mashuhuri. Damu inamwagika kama mchezo. Inspekta Kombora machozi yanamtoka. Joram Kiango anabaki kaduwaa.

SURA YA KWANZA

“Bado nasisitiza kuwa tusithubutu wala kujaribu kufanya lolote kabla ya kuhakikisha kuwa Joram Kiango yu marehemu”, ilidai sauti moja nzito.

“Naam, lazima afe”, sauti nyingine iliunga mkono. “Afe kabla hatujainua mikono kufanya lolote tulilokusudia. Hakuna asiyefahamu jinsi kijana huyu alivyo hatari anusaye shari na kuingilia kati kuharibu harakati zote. Hajasahaulika alivyowakorofisha wale mashujaa waliotaka kuuangusha utawala wa nchi ya Ngoko katika tukio lile lililoitwa Dimbwi la damu. Kadhalika bado hatujasahau alivyosababisha vifo na kuharibu mipango ya majasusi waliotaka kuiharibu nchi hii katika mkasa ambao mtu mmoja aliuandikia kitabu na kuuita Najisikia kuua tena. Kwa kila hali Joram Kiango ni mtu hatari zaidi ya hatari zote zinazoweza kutokea, Hana budi kufa”.

Kicheko kikavu kikasikika kidogo, kikafuatwa na sauti iliyokwaruza ikisema.

“Atakufa. Lazima afe. Na atakufa kifo cha kisayansi kabisa. Mpango huu tumeuandaa kwa uangalifu mkubwa, Na watekelezaji wake pia ni watu ambao wamehitimu vizuri katika nyanja zote zinazohusika na kazi hii, Tuondoe shaka kabisa. Mpango huu utafanikiwa kwa asilimia mia”.

“Kwa hiyo ndugu Mwemyekiti”, ilisema sauti ya mtu wa kwanza. “Niwie radhi kwa kukukata kauli. Ninachokuomba ni kuuahilisha mkutano huu na tusisubutu kukutana tena hadi hapo Joram Kiango atakapokuwa kaburini, Pengine mtaniona mwoga kupindukia, Lakni mimi sipedi kabisa kufanya jambo lolote wakati kijana yule akiwa hai. Mnajua jinsi alivyo na miujiza. Anaweza kuwa hapa akisikiliza mazungumzo yetu, kesho tukajikuta mahakamani bila kutegemea”.

Ilizuka minong’ono, sauti mbili tatu zilimuunga mkono msemaji aliyemaliza kusema. Jina la Joram liliamsha hofu katika mioyo yao. Wakatazamana…

Walipenda pia kumwona Mwenyekiti wao uso kwa uso. Kwa bahati mbaya, hawakuweza kuona uso wake isipokuwa kiwiliwili tu, ambacho kilifunikwa kwa mavazi ya thamani kama walivyokuwa wamevaa wao. Mwanga mkali uliotokana na taa ya umeme iliyowekwa kwa namna iliwachoma macho kila walipotamani kumtazama Mwenyekiti usoni. Ni yeye tu aliyekuwa na nafasi nzuri ya kuwatazama wote mmoja baada ya mwinginge kikamilifu na kuwasoma nyuso zao. Wakati wa kumtambua Mwenyekiti ulikuwa bado haujawadia hivyo hawakupaswa kumuona kabisa isipokuwa sauti yake tu.

Mkutano huo ulifanyika katika chumba cha siri, chini ya ardhi katika mojawapo ya majumba ya kifahari yaliyoko Jijini Dar es salaam.

Kila aina ya tahadhari iliwekwa kuhakikisha usalama wa mkutano huu wa awali. Mkutano ambao ulikuwa umeitishwa ghafla, kwa njia za kutatanisha, hata wajumbe hao walijikuta wamefika kwenye mkutano bila kufahamu kilichowaleta hapo.

Mwenyekiti akaufungua mkutano huo kwa maneno machache akisema: “Tunataka kuitetemesha Afrika na kuishangaza dunia. Tunataka kuachia pigo ambalo halitafutika katika historia ya Ulimwengu”. Wajumbe wakaelewa kinachoendelea. Ndipo mjume mmoja alipotoa rai ya kumaliza kikao hadi watakaposikia Joram Kiango amekuwa marehemu.

Tahadhari kubwa ilikuwa imechukuliwa wakati wa kuandaa mkutano huo. Wajumbe waliingia kwa siri kubwa wakipita milango tofauti, katika eneo hilo vilitegwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhakikisha kila mshiriki wa mkutano huo wa siri anahusika kwa njia moja ama nyingine. Walihakikisha pia hakuna kifaa au chombo chochote cha kunasa sauti ama kusikiliza maongezi hayo ya siri. Vinginevyo chumba hicho kingeweza kutoweka kisayansi kisionekane mlango wowote zaidi ya kuta za kawaida. Zaidi ya yote silaha za kisasa, hewa za sumu, buduki zisizotoa mlio, madawa ya kulevya na mbinu zingine zilikuwa tayari kutumika endapo lolote lingetokea. Kwa bahati mbaya, ni Mwenyekiti peke yake ndiye aliyejua mpango mzima kuhusu mkanda huo.

Kulikuwa na kila sababu ya kuweka tahadhari au uangalifu huo. Watu waliokutana katika mkutano huu hawakuwa watu wenye njaa ya pesa wala kiu ya utajiri. Ni watu mashuhuri walioshiba na kudhamiria kulinda shibe yao. Wote walikuwa na hadhi mitaani, nyadhifa serikalini, na heshima katika chama. Waliokutana hapa wote walikuwa na matarajio ya kuvuna matunda matamu. Matunda ambayo yangetokana na mkutano huo. Hakuna mjumbe aliyependa kukosa utamu wa matunda hayo. Hivyo wote walikuwa na dhamira moja.

“Inaonyesha kuwa Joram ni tishio kwa kila mtu hapa”, Sauti nzito ya Mwenyekiti ilisema. “Hilo linanifanya nizidi kuwa na imani juu ya dhamira yenu. Joram anaogopwa kuliko Polisi na jeshi zima la nchi hii, Kwanini? Wanajeshi mko hapa, polisi mko hapa, Chama tawala kiko hapa. Serikali iko hapa. Anayekosekana hapa ni mtu huyo anayejiita Joram Kiango. Mtu mtundu sana, ambaye utundu wake ni madhara kwa watu wenye dhamira maalumu. Hakuna atakayeshuku kuwa kauawa. Daktari atampima na kuona kafa kwa kansa ya moyo. Atauawa kitaalamu na kufa kistaarabu. Msiwe na shaka”.

Kimya kifupi kikafuata. Wajumbe wakatazamana usoni. Kimya kilimezwa na sauti ya Mwenyekiti alipoongeza maneno.

“Kwa hiyo, naahirisha kikao hiki kama alivyoshauri mjumbe. Tutakutana tena hapa baada ya wiki mbili, siku na saa kama za leo, kwa njia zetu zile zile, bila kusahau kuwa joram Kiango hatakuwa Joram tena ila hayati Joram Kiango. Na ifahamike kuwa kuitoa nje siri hii ni sawa na kujiwekea saini ya kifo chako mwenyewe”.

“Ni kweli Mwenyekiti”, sauti mbili tatu za wajumbe wenye hofu, ziliitikia.

Nyumba mbovu zilizojengwa bila utaratibu katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ambazo huishi kina mama kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao humudu kupanga katika nyumba hizi kwa ajili ya makazi na biashara isiyosemekana wala kuitamka. Biashara ambayo ni aibu kubwa kuitaja hadharani, japokuwa inafanyika hadharani bila kificho. Biashara ya kuuza miili kwa pesa chache za matumizi.

Tupo Mburahati, mbele ya moja ya majumba ya aina hii. Kaketi mwanamke ambaye umri wake haujaruhusu kumwita mwanamke. Yu msichana mwenye sura nzuri, mwendo mzuri na kila kitu kizuri, Hata mavazi yake si duni kama wenzake walioketi hatua chache karibu yake, mbele ya milango ya nyumba zao, Kwa jina msichana huyu anaitwa Waridi.

Ni juzi tu Waridi alipotokea hapa Mburahati na kujipatia chumba. Sifa na uzuri wake zilizagaa haraka haraka zikawafikia hata wale ambao si wateja wa biashara hii. Kwamba kaja msichana mzuri.Hakuna aliyetaka kujua katokea wapi, Hakuna aliyetaka kujua kwanini binti mzuri kama huyu aamue kutouthamini uzuri wake ambao ungemfanya aishi vizuri zaidi, akila na kunywa pesa za walionazo. Hakuna aliyejali.

Leo Waridi alikuwa katika hali yake ya kawaida. Hali ya ukimya na majonzi pamoja na kwamba alionekana akiwachekea mara kwa mara wateja wake. Hakuna aliyejua jeraha kubwa lililokuwa moyoni mwake. Jeraha ambalo lilikuwa siri yake na alipenda liendelee kuwa siri. Kutunza siri ni kazi kubwa kama kubeba mzigo mzito usiobanduka kichwani. Mzigo aliobeba kwa dhiki sana. lakini alistahamili kwanki maisha yake yenyewe yalitegemea utunzaji wa siri hii.

Mara akatokea mteja ambaye sura yake, mwendo wake na mavazi yake vilimtofautisha na wateja wa kawaida. Huyu alimtaka Waridi afunge biashara yake siku hiyo ili wafuatane wote nyumbani kwake.

“Haiwezekani. Ninaye bwana wangu ambaye huja kulala hapa”.

“Twende kwangu halafu nitakurejesha hapa haraka iwezekanavyo”.

“Haiwezekani vilevile”.

“Ziko pesa nyingi kwa ajili yako kama utakubali kwenda nyumbani kwangu”.

“Nimesema hapana”. Ghafla hasira zikampanda Waridi. AKashangaa kwanini kamchukia mtu huyu. “Toka kama hutaki”, alifoka na kumwacha mtu huyo kakalia kitanda chake.

Mteja huyu akatabasamu. Kwa waridi lilikuwa tabasamu la kebehi ambalo halikumshitua kuliko alivyotegemea. Swali fupi likaulizwa kwa sauti ndogo. “Huendi na mimi? Hata nikisema kuwa marehemu Bomba ni ndugu yangu pia nafahamu mpaka mahali alikozikwa?”.

Hilo lilimshitua kidogo Waridi. Mshituko ulipomtoweka yalifuata machozi mengi yaliyomtoka katika macho yake yaliyoduaa kwa hofu yakimtazama mteja huyo. Mwili wake ulikuwa umemlegea kiasi cha kumfanya ashindwe hata kusimama kikamilifu.

Waridi hakuwa na uwezo wa kufanya lolote. Ndipo mteja huyu alipomsukuma Waridi na kuanguka chali kitandani, akampambua mavazi yote na kumtenda kikatili yote aliyojisikia kumtendea.

Baada ya hapo mteja alimwamru Waridi kufuatana naye. “Tutatoka mara moja. Ukiendelea kukataa nami nitashindwa kutunza siri yako. Twende zetu. Nitakupa kazi ndogo tu, unisaidie. Kuna mtu anahitaji kufa. Utamsaidia wewe. Haitakuwa kazi kubwa kuua mtu wa pili mama. Au vipi? Tofauti pekee ni kwamba yule aliitwa Bomba na huyu anaitwa Joram”.

Waridi alimfuata kikondoo.

               **********************************

Huyu hakuwa mwingine zaidi ya Jodor Prosper kama alivyojiita katika ule mkutano wa siri uliofanyika usiku wa juzi. Yeye akiwa Mwenyekiti.

Jina hilo lilikuwa moja miongoni mwa majina yake kadha wa kadha ambayo huyatumia wakati tofauti na kwa dhamira tofauti. Kadhalika alikuwa mtu mwenye sura mbalimbali na miondoko aina aina. Kila jamii ilimfahamu Prosper yule yule katika jina na sura tofauti. Vivyo hivyo, tabia zake kubadilika mara kwa mara kama kinyonga anavyojibadili rangi. Katika kundi la wahuni Prosper yu mhuni mkubwa, katika jamii ya waungwana yu muungwana halisi, katika familia ya masikini Prosper alikuwa mmoja wao, na miongoni mwa matajiri yeye ni kama wao.

Huyo ndiye Prosper. Mswahili aliyezaliwa mahali fulani katika Pwani ya Bahari ya Hindi. Akiwa na miaka kumi na miwili, alitoweka numbani kwao kwa kudandia meli moja iliyotia nanga katika Bandari ya Tanga.

Meli hiyo iliyokuwa na mabaharia katili kupita kiasi. Walimpokea Prosper kwa ukatili usiosemekana. walimtendea mengi maovu, akitukanwa na kusimangwa. Aliishi kwa taabu mno, akiyastahamili yote hayo, mwishowe, akawa mnyama kama mabaharia wale.

Alisuguliwa akasugulika, akageuka kuwa Baharia binadamu mwenye moyo wa mnyama. Akamchukia kila mtu na hata kuichukia nafsi yake mwenyewe. Wakati wote Prosper alitawaliwa na fikra potofu. Alitamani kutenda jambo ambalo lingeiumiza jamii. Kwa bahati mbaya, hakuwa mwana sayansi mwenye vipaji vya ugunduzi, ugunduzi ambao ungemwezesha kuiteketeza jamii. Angekuwa na uwezo wa kujitengenezea bomu la nuklia angeifanya dunia itoweke katika uso wa ulimwengu.

Kwa kuwa, hayo yalikuwa mbali na uwezo wake, lakini alifanya ukatili mdogo tu. Hakuona shida kumtosa baharini mtu yeyote aliyebainika kudandia meli kama alivyofanya yeye alipokuwa mtoto. Wala, kwake haikuwa dhambi kufanya mapenzi na mwanamke na kisha kukata koo la mwanamke huyo asubuhi.

Pamoja na ukatili huu kuufanya kwa siri, lakini sifa zake ziliyafikia masikio mbalimbali. Mmoja kati ya watu waliovutiwa na unyama wa Prosper aliona fahari kukutana nae katika meli hiyo kwa siri. Wakaiacha meli hiyo. Safari yao ikaishia katika chuo kimoja kilichofichika kikiwa na watu wachache wenye moyo kwama wa Prosper. Kilikuwa chuo cha ujasusi kilichokuwa chini ya nchi kadhaa kubwa na tajiri. Kilifundisha mbinu kadha wa kadha kuhujumu siasa, uchumi na msimamo wa nchi kongwe na changa ambazo hazikuwa tayari kulegeza misimamo yao na zile zenye msimamo mkali.

Prosper alipohitimu tayari alikuwa hodari wa yote, kuandaa mauaji, kusababisha mapinduzi, kudhorotesha uchumi. Alikuwa mtu aliyeipenda sana kazi yake, na alifanya mengi yaliyowafurahisha na kuwatisha viongozi wake. Aliweza kusafiri hadi Afrika Kusini ambako alijitangaza kama mpigania uhuru na aliaminika na kushirikishwa katika harakati za ukombozi. Lakini aliweza kutoroka na siri zote huku akiwa tayari ameua na kuwaacha wapigania uhuru wakiuana wenyewe kwa wenyewe. Mtindo huo ameutumia sehemu mbalimbali duniani. Ingawa waliohujumiwa walimhisi baada ya kuondoka, lakini kwa jinsi alivyokuwa akiwaendea katika sura tofauti, na majina bandia, hakuna aliyeweza kumweka katika kumbukumbu.

Mfano ni leo alipokuwa akitoka na msichana huyu aliyechanganyikiwa; Waridi. Wajumbe wote wa mkutano ule ambao walibahatisha kuuona uso wake wasingeweza kumfikiria kuwa ndiye mtu yule yule waliyekuwa naye mkutanoni kwa jinsi alivyobadilika. Hata mwendo wake ulikuwa tofauti. Leo alitembea huku akichechemea kidogo.

Gari dogo aina ya Toyota lilikuwa likiwasubiri mara tu walipoifikia barabara.

“Ingia ndani ya gari”, Prosper aliamuru.

“Samahani…, samahani kaka, tu… tunaelekea wapi?”, Waridi alifanikiwa kuupata ulimi wake ambao alihisi ulikuwa mzito kutokana na hofu.

Prosper akaukunja uso wake huku akisema, “Sitaki maswali”, akapita upande wa dereva na kumfungulia mlango Waridi. Alipoingia ndani ya gari na kuketi, gari likatiwa moto na kuteleza juu ya barabara, likijitahidi kukwepa mashimo. Walipoifikia barabara ya Morogoro, gari hilo liliekezwa katikati ya jiji. Wakaiacha Magomeni, wakaingia Upanga, wakipita hapa na pele hata waridi asijue kama walikuwa wapi,

Gari lilisimama mbele ya jumba moja kubwa sehemu ambayo hisia zilimwambia Waridi kuwa ni katikati ya Jiji. Prosper alitelemka na kumwagiza Waridi amfuate. Walipokaribia mlango mmoja kati ya milango kadhaa ya jumba hilo, Prosper alimnong’oneza Waridi akisema; “Unasikia? sitiki vurugu la aina yoyote hapa ndani. Uwe binti mtulivu kama ulivyo sasa. Utafaidika na kutoka salama. Vinginevyo…” akaiacha sentesi hiyo ikielea na kuanza kushugulikia funguo.

Walipoanza kuingia, mlango wa pili ulifunguka na uso wa mzee wa Kihindi kujitokeza ukichungulia. “Aha… ni bwana Chain siyo? Karibu sana”.

“Shukrani”, Prosper alijibu.

“Naona leo uko na mama, au siyo?, Mhindi huyo aliendelea akitabasamu. “Shauri kazi ya vitabu iko chosa kidogo. Lazima starehe na dada kidogo”.

Prosper naye akajitia kucheka, “Eh, ndiyo. Lakini huyu ni sekretary wa kampuni yetu. Yeye amekuja kuchukua maandishi fulani kwa ajili ya kuchapishwa kwenye mashine wakati nitakapokuwa safarini”.

“Ah”, Mhindi alijibu huku akimtazama Waridi kwa tamaa ya wazi. Hili lilikuwa moja kati ya majumba ambayo Prosper alikuwa amepangisha vyumba ambavyo aliviyumia kwa shughuli zake. Hapa, mbali na kufahamika kwa jina la Chain Kimara, pia walimtambua kama msomi ambaye alikuwa akiutumia muda wake mwingi kufanya utafiti wa mambo kadha wa kadha ambayo alikuwa akiyaandikia kitabu. Hivyo, muda wote ambao Prosper alijificha chumbani akifanya shughuli zake za siri, wao waliamini kuwa alikuwa akiendelea na mipango ya kuhakikisha kitabu chake kinatoka. Akiwa hapa, hata sura yake ilionekana kama ya Profesa asiyependa kuuchezea muda wake kama ilivyokuwa tabia yake ya kisomi na kistaarabu.

Huko ndani picha ilikuwa hiyo hiyo, Waridi alilakiwa na chumba kikubwa kilichojaa vitabu vya kila aina , vilivyopangwa kistaarabu katika dawati maalumu. Katikati ya chumba hiki kulikuwa na meza kubwa yenye dalili zote za mashughuliko. Chumba cha pili kilikuwa na kitanda kipana, friji, radio na mahitaji yote ya chumba cha malazi. Ni katika chumba hicho alikokaribishwa Waridi.

Akajibwatika juu ya kochi lililomwelekea Prosper, aliyeketi juu ya kitanda.

“Nimekuita hapa ili nikutume kuua mtu”, Prosper alimweleza Waridi. Dakika ishirini zijazo nataka mtu huyo awe safarini akielekea kuzimu. Sasa hivi yuko katika baa moja hapa mjini akinywa pombe. Hiyo iwe pombe yake ya mwisho”, Prosper alisita akamtazama Waridi. “Utanisaidia kuifanya kazi hiyo bi mdogo”, akaongeza kwa sauti ya unyenyekevu.

“Siwezi kuua…” Waridi aligugumia.

Prosper alikunja uso akamwangalia Waridi kwa hasira huku akisema. “Sina haja ya kukukumbusha mara kwa mara kuwa najua yote yaliyompata marehemu Bomba. Naweza kutoa siri hiyo wakati wowote nawe ukajikuta ukining’inia juu ya kitanzi. Nitakufanyia hisani ya kuficha habari hiyo iwapo tu nawe utanisaidia kumtoa duniani mtu huyu. Tumeelewana?”,

Waridi hakujua ajibu nini. Kwa kila hali. alimwona mzee huyu kampatia na kamweka mahali panapomstahili. Hofu yake kubwa haikuwa kitanzu tu bali ilimuumiza kutajiwa mara kwa mara jina hilo la Bomba. Ilimuumiza sana kukumbuka kifo cha mtu huyo kilivyotokea na jinsi alivyotoa macho wajati anakata roho. Ilimuumiza zaidi Waridi kukumbuka kuwa dhambi hiyo ya kuua alikuwa ameifanya bure kabisa.

Ni miezi kadhaa tu iliyopita. Wakati huo Waridi alikuwa Waridi wa ukweli. Ua la uhakika ambalo kila nyuki alilitamani, kila kipepeo alilimezea mate. Lakini si wote waliolifikia. Na wachache waliofaulu kuligusa, hawakuwa vipepeo wala nyuki wa kawaida. Walikuwa zaidi.

Uzuri wa msichana huyu ulianza kujitokeza tangu alipokuwa kinda. Alipofikia umri wa miaka mwili tu, kila mtu alibaini kuwa mtoto huyu alikuwa hazina ya uzuri. Alipofika miaka sita watu walianza kunong’ona. Alipohitimu miaka kumi, wanaume wasiokuwa na staha, walianza kumnyatia. Miaka kumi na miwili Waridi alikuwa tayari akiwa kama malkia wa nyuki na kama nilivyosema awali; kwa vipepeo.

Pengine uzuri wake huo ulitokana na ule mchanganyiko maalumu katika umbo lake. Mchanganyiko wa damu za watu weusi, Wahindi, waarabu na Wazungu ambao walishiriki kumtengeneza. Kwani mama yake pia alikuwa mtu wa nipe nikupe. Alifanya biashara yake katika mji wa Mwanza, katika mojawapo ya vibana vibovu, akimkaribisha yeyote mwenye ‘chochote’. Mama huyu hakumfahamu kabisa mtu maalumu aliyeshirikiana naye kumpata Waridi binti yake wa pekee. Alichofahamu ni kuwa, kumpata binti mzuri ambaye watu walianza kumwita Waridi, hata jina lake la awali likasahaulika.

Kwa Waridi hakujua kama alikuwa mzuri kupidukia, lakini alishangaa kuwaona watu wazima kwa vijana wakimfuata na kumtaka kitu ambacho hakukifahamu maana ama umuhimu wake. Kitu kile ambacho alimwona mama yake akikifanya mara kwa mara kitandani.

Kisha akafahamu. Ilikuwa baada ya kukamatwa kwa nguvu na mzee mmoja aliyemtupa sakafuni, akamvua nguo na kumwingilia miguuni kwa namna ambayo ilimtia Waridi maumivu makali yaliyoambatana na faraja.

Waridi akayafahamu hayo, akaifahamu thamani ya uzuri wake, akaanza kuingiwa na kiburi. Akajidekeza na kutupilia mbali masomo. Huyo akamtoroka mama yake na kuingia mjini Tabora,ambapo aliishi kwa faraja kubwa. Daima wanaume walikuwa tayari kumhudumia kwa maneno matamu, malezi, mavazi huku akipewa fedha za kutosha.

Lakini Waridi hakutosheka. Daima alidai hiki na kile kwa wanaome ambao kila mmoja alijitahidi kutoa alichonacho. Lakini baada ya kupata walichohitaji wakamwepuka. Hivyo akauona mji wa Tabora haufai. Akasogea hadi Dodoma ambapo pia hakukaa sana, akapanda hadi Arusha. Mji huo ulipomchoka, akapaa na kushuka Jijini Dar es Salaam.

Ni hapo alipokutana na Bomba Kimara. Kijana huyu mwenye asili ya Kiarabu mtu ambaye Maua alimhitaji. Siku zote alionekana ‘kajaa’, Fedha kwa Bomba hazikuwa na tatizo. Wala hakuna uchungu kuzitumia. Kadhalika, fedha zake hazikuwa mfukoni kama wanaume wengine. Zake zilitoka katika soksi. Kitita cha elfu kumi kumi kikiwa kimefungwa kwa mpira kingewezaje kukaa mfukoni? Walizitumia fedha hizo na Waridi wakishirikiana kuhama baa moja kwenda nyingine, madansa, sinema, mahoteli na kila aina ya starehe.

Walikuwa wakiishi Magomeni Mikumi katika nyumba za msajili wa majumba ambayo Bomba alikuwa amekodi. Ni mara chache sana nyumba hii ilipowaona wapangaji wake, kwani mara nyingi walikuwa kama si Kunduchi Beach, basi wako Kilimanjaro Hoteli au Mbowe Hoteli na sehemu nyingine za starehe wakitumia.

Halafu ikafika ile siku ambayo Bomba alirudi nyumbani mapema kutoka kule alikokuwa akienda mara kwa mara na kurudi na pesa. Safari hii alirudi na mfuko wa ngozi ambao aliutua juu ya kitanda. Alionekana mtu mwenye wasiwasi mwingi kinyume na tabia yake. Hakujua kwa Waridi alikuwa chumbani humo akimtazama.

“Vipi mwenzangu?” Sauti ya Waridi ilimzindua. Akamgeukia akijaribu kutabasamu lakini tabasamu lilikataa.

“Waridi, kwenu ni wapi?” Bomba alihoji ghafla.

Swali hili lilimshangaza sana Waridi. Muda wote walioishi pamoja hawakuwahi kuulizana maswali ya aina hiyo.

‘Kwanini?” Bomba akaendelea. “Nataka urudi kwenu. Mimi naona maisha hayaniendei vizuri”, Bomba akaeleza. Baada ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akasema.

“Waridi, ni hadithi ndefu ninayo. Hadithi ambayo haifai kulifikia sikio lisilohusika. Ninachoomba ni wewe kwenda zako kesho. Kama hutaki kwenda nyumbani kwenu, rudi kwenye baa niliyokukuta. Naamini ukirudi pale baa haitapita dakika tano kabla hujaokotwa na mwanaume mwingine”.

“Kuokotwa?” Maua alijiuliza kwa hasira. Ghafla alijikuta kamchukulia Bomba kama mtu shetani. Hata sura yake sasa aliiona mbaya kama dhambi. Machozi yalimtoka na kuteleza juu ya mashavu yake. Akainuka na kutoka nje kimya.

Waridi alirudi ndani baada ya kumsikia Bomba akioga bafuni. Akafanya haraka kuuendelea ule mfuko ambao aliufunua. Macho yake yalikutana na furushi kubwa la noti ambalo hakuwahi kuliona katika maisha yake. Kwa kukadilia zilikuwa pesa nyingi. Kando ya pesa hizo, ililala bastola kubwa na tiketi moja ya ndege. Tiketi hiyo ilionyesha jina la Bomba kuelekea Nairobi.

Wazo likamjia Waridi. Bomba alikusudia kumtupa baada ya kupata pesa nyingi kama hizo ili aende zake Nairobi akatumie peke yake! Waridi akajishauri kuchota pesa kidogo afiche. Akasita. Alizihitaji zote. Akaamua kuzipata. Akazirudisha kama zilivyokuwa akatoka zake nje.

Usiku huo, Waridi alikuwa wa kwanza kulala. Alijitia kulia pole pole kwa namna iliyokusudiwa kumfanya Bomba aamini kuwa Waridi alimpenda kwa dhati. Ukweli ni kwamba katika maisha yake Waridi hakuwahi kumpenda mwanaume. Alipeda pesa. Mwanaume alimhitaji kwa ajili ya faraja ya mwili tu.

Bomba alikuwa amelala kando yake, alipoanza kukoroma, Waridi aliamka taratibu, akanyata hadi uani ambako alilibeba kwa taabu jiwe kubwa alilokuwa ameliandaa mchana. Akaingia nalo hadi chumbani ambako Bomba alikuwa akiendelea kukoroma. Akakilenga barabara kichwa chake na kuliachia jiwe lile.

Bamba alikurupuka kutoka usingizini na kupaa juu, alipotua kitandani. Alitoa mlio wa maumivu kwa sauti ndogo nyembamba ambayo ilimwingia Waridi rohoni na kumtia ganzi. Kichwa cha Bomba kilikuwa kimefumuka. Ubongo uliochanganyika na damu ulikuwa ukivuja kitandani na kuchafua mashuka. Lakini bado aliendelea kutapatapa huku na kule, akisema hili na lile, maneno ambayo Waridi hakuweza kuyaelewa. Ni macho yake ambayo yaliweza kumtisha Waridi zaidi… Macho ya Bomba yalikuwa yakimtazama kwa namna ya huruma na kutoamini alichokifanya.

Waridi hakuweza kustahamili. Akapiga kelele kwa hofu akakimbia nje ya chumba hiki ambako aliketi chini akitetemeka. Baada ya muda, alirudi ndani ambako alimkuta Bomba tayari amekuwa marehemu; domo wazi, ulimi ukiwa umesahaulikwa nje, upande mmoja ilikuwa kama picha ya kusikitisha inayotisha mno. Waridi akaona shida kuistahamili. Akajikaza kiume kwa kumfungafunga marehemu Bomba kwa blanketi kubwa kisha akajaribu kumuinua ili amtoe nje. Hakufaulu. Akamvuta hadi uwanni. Huko akajitahidi na kuifikisha mati chooni ambako kulikuwa na tundu kubwa lililofunikwa na bati. Akalifunua bati hilo, na kumtumbukiza marehemu Bomba. Kisha akalifunika kama lilivyokuwa awali.

Wazo lake sasa lilikuwa moja tu; kuzihesabu pesa zake kikamilifu, Lakini mwujiza ulikuwa ukimsubiri. Mfuko wa pesa ulikuwa umetoweka. Haukuwepo tena juu ya kabati, ambapo aliuona kwa mara ya mwisho kabla ya kuutoa mzoga wa aliyekuwa mpenzi wake Bomba ndani. “Uko wapi?”, Waridi alijiuliza huku akiutafuta mfuko huo kila kona ya nyumba bila mafanikio. Akabaki ameduwaa.

Mapambazuko yalimkuta bado kaduwaa katikati ya chumba, macho yakilitazama kabati kwa mshangao kana kwamba limeumeza mfuko huo wenye pesa. Waridi hakujua afuate lipi aache lipi.

Mara akajikuta akitoka nje ya nyumba hiyo. Alitembea kwa mkiguu hajui aendako. Baada ya kutwa nzima ya mzunguko usio na dhamira maalumu, Alielekea Mburahati ambako hakukawia kupata rafiki aliyemkarimu kwa kumsaidia kupata chumba cha muda. Baadae, Waridi alipata chumba chake. Siku zote moyo wake uliteswa na huzuni akikukmbuka kumwaga damu ya mtu asiyekuwa na hatia, hofu kwa kudhani kuwa wakati wowote polisi wangeweza kutokea kwa ajili ya kumchukua, na zaidi, maumivu makali moyoi kwa kuhisi ile sauti ya Bomba alipolia kwa uchungu na picha ya macho yake yalivyokuwa yakisihi.

Waridi hakuwa na la kufanya. Maisha yalimwendea vyema katika mazingira yake mapya, wateja wakimiminika kwa wingi hadi leo alipotokea mtu huyu wa ajabu ajabu ambaye anafahamu kila kitu kuhusu mkasa juu ya kifo cha Bomba.

“Siwezi… Siwezi kuua tena…?”Waridi alisema huku akibubujikwa na machozi.

“Huna ujanja, lazima utaua”.

“Utaua?”, Prosper alifoka kwa nguvu akiachia kofi kali ambalo lilimwingia Waridi kama aliyepigwa na kipande cha ubao. Akiwa msichana asiyezoea kupokea vipigo kutoka kwa wanaume, kofi hili lilimshangaza zaidi zaidi ya jinsi lilivyomwumiza. Lakini mshangao wake ulikoma pindi Prosper alipoongeza vipigo vingine vikali zaidi ambavyo vilimfanya Waridi ajikute akighalaghala chini damu zikimvuja hovyo kutoka usoni, puani na mdomoni.

Prosper akaangua kicheko, “Well”, akasema, nilikuwa sikupigi ila tu ilikuwa kukuandaa katika hali ambayo itakufanya umpate Joram Kiango kwa urahisi. Yeye ni mtu anayevutiwa sana na mambo ya damu. Hivyo atakapokuona atajileta mwenyewe kwako. Utakachofanya wewe ni kuhakikisha umempata dawa ambayo nitakupatia, Baada ya muda mfupi atakuwa marehemu. Itaonekana kafa kwa magonjwa ya kawaida tu. Hakuna atakayefikiria kama wewe na mimi tunahusika na kifo chake”,

Prosper alinyamaza kidogo akimwangalia waridi kuona kama maelezo yake yalikuwa yakimwingia, alipoona maneno yake yameanza kumwingia Waridi. Akaendelea. “Unaona iivyo kazi rahisi. Ni kazi ndogo tu. Inatofati sana na ile kubwa uliyofanya wakati ukimuua marehemu Bomba”.

Moyoni Prosper aliwaza; Waridi angejisikiaje kufahamu kuwa yeye Prosper muda wote ule alikuwa nje akisubiri fursa ya kumuua Bomba! Kwani, Bomba ambaye alikuwa mmoja wa magaidi wake, alikuwa ameshindwa kutimiza kazi fulani aliyopewa. Badala yake alipanga kutoroka na pesa ambazo alipewa kwa ajili ya shughuli maalumu. Ndipo ilipodi Bomba auawe usiku ule. Ni Prosper pia aliyepeya hadi ndani na kuzichukua pesa zile baada ya kuona kazi aliyokusudia kuifanya ilikuwa imefanywa na Waridi.

Prosper aliitazama tena saa yake. “Bado dakika tano Waridi”, Prosper alimwita Waridi, “Simama haraka ujiandae”.

Kiasi fulani Waridi alikuwa hoi, hivyo alishindwa hata kusimama, lakini Prosper akamsaidia na kumwongoza nje ambako walipanda gari. Humo garini, Prosper alitoa amri nyingine ambayo Waridi hakuitegemea.

“Vua nguo zako zote”.

Waridi aliduwaa na akasaidiwa kuzivua. Prosper hakusita kuzitatua.

“Nataka ufanye kazi nzuri tafadhali. Shika hii… Kamata na hii… Ni kazi ndogo sana… Kesho Joram Kiango atakuwa marehemu”?.

Baa hii ilikuwa imejaa watu wa kila aina; waliokuwa wakinywa na kustarehe kwa namna mbalimbali. Miongoni mwa watu hawa, alikuwemo Joram Kiango.

Yeye alitulia pale kaunta, juu ya stuli ndefu, pombe ikiwa wazi mbele yake, sigara ikiteketea mdomoni mwake. Kama ni furaha, yake ilikuwa tofauti na walevi ama wanywaji wengine. Hakusinzia hovyo wala kucheka pasipo sababu. Ukimya wake ulimfanya hata msichana wake Neema, ambaye alikuwa kando akinywa soda, amgeukie na kusema polepole.

“Tatizo lako ndio hilo, Joram. Uwapo huru unashindwa kuutumia uhuru wako. Tazama usivyo na raha. Mtu yeyote anayekufahamu akitokea hapa atadhani uko kizimbani ukisubiri hukumu ya kifo, badala ya kustarehe. Kwa nini?”.

Joram aligeuka kumtazama huku akimtengenezea tabasamu jepesi. Kama kawaida, macho yake yaliona kile ambacho yamezoea kuona katika umbo la msichana huyo. Umbo lenye urefu wa kadri, unene wa kadri na sura ambayo ilioana vizuri na umbo hilo. Sura ambayo ilisisimua moyo wa kila mwanaume aliyepata kumtupia macho Neema. Kadhalika, mavazi ya Neema yalikuwa ya kupendeza na yaliliafiki umbo lake. Lilikuwa gauni la kitambaa chepesi ambacho ni dhahiri kilitokea nje ya Afrika Mashariki. Si hayo tu yaliyomfanya Joram ampende Neema na kumthamini binti huyo. Macho ya mwanadada huyu yalikuwa na uzuri wa pekee, uzuri wa kubembelezabembeleza, uzuri wa kishujaa. Yalikuwa na nuru. Si nuru wa “mapenzi” bali nuru ya ujasiri.

Ujasiri huo ndio aliouhusudu Joram. Na ni kwa ajili ya kuuthamini ndipo mara kwa mara akawa akimshinda nguvu shetani wake ambaye alikuwa akitamani kumtia mweleka kwa kumnong’oneza akisema: “Sikia Joram Neema ni binti mzuri sana… na anakupenda sana… Kwa nini usisahau walao kwa siku moja awe mwenzi wako kikazi akastarehe naye kitandani?… Hujui… Utakuwa usiku mzuri kuliko usiku wowote mwingine…” Hayo Joram aliyapuuza na kuendelea kumwona Neema kama mpenzi wake wa dhati.

Mawazo hayo yalimjia tena Joram. Wakati huo, badala ya kumjibu Neema swali lake, alitabasamu tena, kisha akavuta sigara kwa utulivu. Tayari kusahau yote.

“Tazama!” Neema alilalamika. “Bado hata unashindwa hata kunijibu! Wamekuloga nini kaka yangu? Kwa kweli sijaiona siku yoyote ambayo uko kwenye starehe isipokuwa hapo tu unapokuwa vitani ukipambana na mikasa ya kutatanisha huku maisha yako yakiwa hatarini. Sijasahau niliposoma katika gazeti la Kiongozi jinsi ulivyokuwa ukicheka mbele ya bastola ya kumwuaji yule hatari katika tukio lililoitwa Lazima Ufe… kule Arusha”.

Tabasamu la Joram likageuka kicheko, “Mimi nilidhani kwamba wewe unanielewa vizuri zaidi mpenzi”, alisema. “Tatizo langu ni watu kutokunielewa. Hapa nilipo, kimya kama nilivyo, nina furaha na nimestarehe kabisa. Lakini watu watadhani sina raha. Niwapo mbele ya bastola huwa sicheki bali nimechukia sana. Tabasamu langu huwa ni moja ya silaha zangu kwa ajili ya kumlegeza adui. Kwa kweli silaha hiyo naipenda zaidi ya bastola. Kwani humfanya adui ashindwe kuitumia bastola yake.

“Huwa huna hofu?”.

“Sijui hofu ni kitu cha aina gani kwa kweli. Labda itabidi nimpate daktari mzuri anipime na kuona kama ninazo chembechembe za kitu hicho kinachoitwa hofu katika moyo wangu. Nadhani hili kwangu ni lazima…”

Neema akaangua kicheko. “U kiumbe wa ajabu sana Joram. Unaona sasa ulivyochangamka baada ya kuanza mazungumzo ya vifo na mauaji? Nadhani kifo chako kitakuwa cha kusikitisha sana”.

“Ni afadhali kuliko kufia juu ya kitanda Muhimbili, tena baada ya kuugua miezi kadha wa kadha”.

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, macho ya Joram yakauacha uso wa Neema na kumtazama mtu ambaye alikuwa ameingia ghafla katika baa hiyo. Pamoja na kuingia kama watu wengine, akiwa katika mavazi ya kawaida, suti nyeusi, macho yake yalimvutia Joram. Macho yake yakaonyesha dalili ya wasiwasi na tahayari. Joram hakuona kama wasiwasi huo ulikuwa wa kuwahi pombe. Hilo alilidhihilisha kutokana na macho hayo yalivyotembea huku na huko ndani ya baa. Yalipokutana na macho ya Joram, yalizidi kupatwa na hofu kubwa. Kisha mtu huyo akageuka ba kutoka nje. Mara kilio kikali kikasikika kutoka nje. Ilikuwa sauti ya msichana, akilia kwa uchungu.

“Mwanamke malaya, anapokula pesa za watu wahuni hupelekwa gizani ambako hufanyiwa unyama”, lilikuwa jibu la Joram.

“Umejuaje kuwa ni mwanamke malaya Joram?”, Neema alihoji. Wakati huo watu walikuwa wakitoka ndani ya baa kwenda nje kutazama. “Anaweza kuwa mke wa mtu aliyekamatwa na kuletwa huku kwa ajili ya kutendewa unyama, twende tukaone”.

“Hatuna muda huo…”

“Twende Joram”. Wakati huo Neema alikuwa wima akimvuta Joram. “Twende tafadhali…” Ikamlazimu Joram kukubali. Umati wa watu ulikuwa ukielekea nyuma ya baa, sehemu ambayo ilikuwa na kivuli chenye giza kilichotokana na msitu wa maua yaliyoizunguka baa hiyo.

Japo ndipo sauti ya msichana huyo ilisikika akilia.

Alikuwa kalala chali, nusu uchi, vazi lake pekee ilikuwa kipande kidogo cha kanga ambacho kilifunika sehemu ya kati na kuruhusu sehemu kubwa isiyostahili kuonekana hovyo, itazamwe na watazamaji.

“Nakufa jamani, nakufa…” binti huyo aliendelea kulia huku akitupa miguu huku na kule.

Mtu mmoja alikuwa na tochi. Akamulika. Mwanga wake ulinisa kitu cha kutisha zaidi. Damu. Damu nzito ilikuwa imetapakaa kando na juu ya mwili wa msichana huyo. Mara kitu cha kutisha zaidi kikaonekana. Kisu! Kisu kirefu chenye damu. Kilikuwa kando ya mwili wa msichana huyo.

“Kisu jamani”, mtu mmoja alilalamika.

“Nakufa… nisaidieni…” msichana huyu aliendelea kulalamika.

Kiasi Joram akaanza kuvutiwa. Hata hivyo Joram hakuvutiwa na kisu wala damu tu. Alikuwa akiutazama uso wa msichana huyo. Aliyaona macho yake. Alikuwa msichana mzuri sana isipokuwa macho yake tu. Yalikuwa macho yale yale aliyoyategemea kitambo. Macho ya msichana mlevi na malaya ambaye amekula vya watu na sasa vinamtokea puani. Hivyo aliushika mkono wa Neema na kumwambia. “Inatosha twende zetu”.

“Joram! Tumwache msichana huyu katika hali hii kweli?” Neema alilalamika.

“Ni kazi ya polisi. Haonyeshi kama atakufa”.

“Nakufa”, binti huyo aliendelea kulia. “Upo hapo Joram? Tafadhali nisaidie. Inama usnishike japo mkono. Naogopa wataniua. Tafadhali Joram”.

Kutajwa kwa jina la Joram kilisababisha watu waliokuwa hapo wamsahau msichana huyo mahututi, wakagauka kumtazama Joram, kijana mzuri wa sura, mrefu, nadhifu kwa mwili na mavazi, alionekana mpole tofauti na ilivyofikiriwa. “Kumbe huyu ndiye Joram Kiango!”, walinongona watazamaji. Mara kadha wamesoma habari zake magazetini na kutegemewa kuwa labda lilikuwa pandikizi la mwanaume linaloweza kuwatisha majambazi. Kumbe.

“Nisaidie Joram…” msichana akaendelea kulalamika.

Joram ni mtu anayechukia kutazamwatazamwa na kushangiliwa, basi aliondoka polepole huku akifuatwa na Neema. Alipofika ndani akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha 999. Sauti ilipomjibu alisema. “Hapa ni Forest of Flowers Bar… ndiyo Kinondoni. Njooni kuna mtu wenu anavuja damu…”

Polisi waliotummwa kuja kumchukuwa ‘majeruhi’ huyo walikuwa vijana wawili wenye imani moja dhidi ya wanawake malaya; kwamba malaya ni mwizi wa mchana. Hivyo, inapotokea akapigwa hata kuuawa ni haki yake kabisa.

Wakiwa na imani hiyo, polisi hao walimzoa Waridi bila huruma wala kujali malalamiko yake. Kama kuna jambo liliwasikitisha ni kule kuona kuwa kipigo alichopata hakikumsitahili kabisa. Majeraha machache yaliyokuwa usoni mwake na damu kidogo iliyokuwa ikivuja polisi hawa hawakuona kama ni adhabu iliyomtosha malaya kama huyu. Kama kuna jambo liliwashangaza polisi hawa, ni kuona kuwa kisu hicho kikali kilicholala kando yake hakikutimiza wajibu. Yawezekana washambuliaji wake walikuwa waoga, au hawakudhamilia lingine zaidi ya kumtisha tu.

Gari lilipoanza kuondoka, polisi hawakuchelewa kumtupia maswali kadha wa kadha, maswali ambayo hawakujali kusikiliza majibu yake. Na kwanini wapoteze muda kusikiliza uongo ulioandaliwa kitambo? Mmoja wa vijana hawa akajikuta kavutiwa na uzuri wa Waridi. Kwa kisingizio cha kumfuta damu, akanyoosha mkono wake na kumgusa titi lililokuwa wazi likiwatazama kama linawadhihaki. Mkono ukanogewa na kutelemshwa hadi kwenye paja lake jekundu lililonona. Mkono huo ukaanza ziara nyingine ya kupanda juu. Ulipoelekea kuvuka mipaka, Waridi akashindwa kustahamii zaidi. Akainua mkono wake na kuunasa mkono wa askari huyo na kuutoa juu ya paja lake. Baada ya kitendo hicho, Ndipo alipotanabahi kuwa kamgusa askari huyo kwa mkono ulioandaliwa maalumu

kwa ajili ya mtu mmoja tu, Joram Kiango. Waridi alijua kitakachomtokea askari huyo. Mara akaangua kilio kwa sauti kubwa. Kilio ambacho kiliwashagaza askari hao.

Walifanikiwa kumfikisha katika hospitali ya Mwananyamala ambapo alipokelewa na wauguzi wa zamu. Askari hao wakaaga na kuahidi kurudi hospitalini hapo kesho yake ili kuanza upelelezi wao.

Waridi aliwaomba wauguzi kumpeleka moja kwa moja bafuni. Huko alitupa dawa zote alizohifadhi mkononi, akanawa vizuri kwa dawa kama alivyoelekezwa na Proper. Ndipo aliporudi kwa wauguzi ambao hawakuonyesha nia ya kumhudumia kutokana na hali yake alikuwa hajambo. Walimuonyesha kitanda cha kulala katikati ya wagonjwa wawili, mmoja aliyelala fofofo kama maiti, wa pili alionekana akitapatapa kama mtu aliyekaribia kukata roho.

Waridi alilala kitandani hapo kwa dakika tano tu. Alikuwa akiwaza kwa makini. Hakuona anachofanya hapo hospitali. Wala hakuona sababu ya kuendelea kusubiri hadi atokee yule mtu ambaye aliamini angemwua na kushindwa kutimiza jukumu alilotumwa kulifanya. Wazo hilo likamfanya Waridi aamue kutoroka mara moja hospitalini hapo mara moja. Bila kufikiri mara ya pili aliinuka na kutoka kama anaelekea msalaani huku akipitia kanga moja ya yle mgonjwa aliyelala fofofo, akayafunika mavazi ya hospitali aliyovishwa na wauguzi ili ajisitiri. Alipotoka nje, akajitanda kanga hiyo na kufuata njia ya kutokea. Alijiingiza kwenye kundi la watu wengine waliokuwa wakitoka hospitalini hapo. Hakuna aliyemshuku kwa lolote. Dhamira yake ilikuwa kwenda Mburahati, akachukue chochote alichonacho, na senti kadhaa alizoficha chini ya godoro, kisha atoweke Dar na kwenda kokote mbali iwezekanavyo ambako mkono wa Prosper… usingemfikia kwa urahisi.

Lakini hakwenda zaidi ya hatua nne nje ya geti kabla ya kuisikia sauti ya mtu ikimwita kutoka nyuma. Akageuka kwa mshituko na kukutana ana kwa ana na Proper, ambaye alimjia akimchekea huku akisema kwa sauti ya dhihaka.

“Msichana mzuri… Umefanya vizuri… Nilitaka nije nikutoe mimi mwenyewe lakini kumbe umewahi kutoka. Pole kwa yote yaliyokukuta, ok usijali twende zetu, gari ile pale…”

Kesho yake ilikuwa asubuhi yenye mawingu kiasu cha kuvunja nguvu ya jua kali ambalo lilikuwa likitishia kutawala. Mmoja kati ya wale askari waliomchukua Waridi pale baa alikuwa tayari kawasili kazini kwake. Mkuu wake wa kazi alihitaji ripoti kamili ya “Kushambuliwa kwa yule msichana malaya” Akamtaka pia kujitahidi waliotenda tukio hilo watafutwe na kupatikaba haraka iwezekanavyo kwani mchezo wao wa kubaka wasichana si mzuri kimaadili hususan mchezo wa hatari.

Askari huyo akalazimika kumsubiri mwenzake kwa muda mrefu, hakutokea. Ikamshangaza. Kwa kuwa makazi yake hayakuwa mbali na kituo cha polisi cha Magomeni, askari huyo aliamua kumfuata nyumbani, Alimkuta! Lakini alimkuta katika hali ambayo haikuwa ya kawaida, Kwani haikuwa jambo la kawaida mtu aanze kuvaa suruali kabla haijafunika matako, aache kazi hiyo ba kuanza kuinamia sakafu hadi kichwa kigonge chini mfano wa mtu anayeswali. Na zaidi ya hayo mgeni aingie baada ya kupiga hodi mara kadhaa bila kuitikiwa, lakini akukute ukiendelea kuinama kimya kimya. Dakika mbili, tatu hadi tano.

“Bobi”, askari huyo alimwita mwenzake kwa mshangao, akijiuliza huu ni mzaha wa aina gani, na umeanza lini! “Bobi”, aliita tena askari huyo huku akimtazama tena kwa makini zaidi askari huyo. Ndipo alipoanza kuona povu lenye damu damu likimdondoka mwenzake mdomoni na puani. Akaruka nyuma, kisha akakusanya nguvu na kumsogelea ili amchunguze vizuri zaidi. Akayaona macho yake yalivyoduaa, akauona ulimi ulivyotoka na kutembea nje ya meno, akaona… Hofu ikamkumbuka ghafla. alikuwa akitazama maiti ya askari mwenzake. Hima akarudi kituo cha polisi kutoa taarifa.

Marehemu alipelekwa hosptali ambako daktari hakuchelewa kutoa taarifa kuhusu ugonjwa uliosababisha kifo hicho. “Ugonjwa wa moyo”, daktari alidai. Kwamba alikutwa na ugonjwa huo ghafla wakati akivaa nguo zake, ikabainishwa kuwa kifo cha askari huyo kilitokana na shinikizo la damu.

Hakuna aliyeshuku kuwa asakri huyo amekufa kwa sumu ile, ya aina yake, ambayo aliigusa kutoka kwa Waridi, na kuifikisha sehemu iliyokusudiwa kufika, mwilini mwake, bila askari huyo kujua.

Sumu hiyo iliandawaliwa kwa ajili ya Joram Kiango peke yake

Wakati huo huo Joram Kiango alikuwa akipokea simu iliyopigwa ofisini mwake.

“Sauti yako i tamu mno masikioni sister, yaelekea nawe u kiumbe mzuri sana. Siwezi kuukataa kamwe mwaliko wa mtu mwenye sauti nzuri kama hiyo, Baada ya saa moja nadhani nitafika… Haya… Ahsante… Umesema wapi vile… Heh… Light Lodge?… Hapo siyo?. Nitafika baada ya saa moja…”, akaweka simu chini na kuukunja uso wake akimtazama Neema Iddy, katibu wake ambaye pia alikuwa akumtazama.

“Nani?”, Neema alihoji kwa shauku.

“Anajiita waridi”.

“Waridi? Anataka nini?” Joram alipochelewa kujibu. Neema aliongeza. “Sikujua Joram kama nawe u mroho wa wanawake kiasi hicho. Sauti tu unaridhika na kuahidi kumfuata? Angalia Joram. Utaingia katika mtego. Una maadui wengi katika nchi hii”.

“Nalijua hilo”, Joram alisema. “Siendi kwa sababu ya sura wala sauti yake kama nilivyosema. Kilichonivutia ni maelezo yake. Anasema yeye ni yule msichana ambaye alipigwa pale baa ya Forest of Flowers. Anadai kuwa nia yake ni kunishukru pamoja na kunipa habari fulani ambayo inasisimua”.

“Malaya kama yule! Hana habari yoyote. Anachotaka ni kukupata wewe tu”.

“Hapana”, Joram alimkatisha. Sauti yake ndiyo iliyonifanya nivutiwe hata kumwahidi kuwa nitakwenda. Inavyoonyesha kuna kitu zaidi ya anachosema. Nahitaji kujua ni nini. Zaidi ya sauti, nadhani utakumbuka kuwa jana binti huyo alilia sana akilitaja jina langu. Sijui alivyonijua”.

“Ni mimi niliyekutaja kwanza”.

“Ni kweli, lakini hiyo siyo sababu ya kumfanya aniite jina langu mara nyigi tena kwa ufasaha kiasi kile. Ni kama mtu aliyekuwa akinifahamu kitambo”.

“Wewe si mtu unayefafamika Joram?”.

“Pamoja na hilo”, Joram aliongeza. “Ni wapi alikopata namba yangu ya simu? Tuseme kwenye vitabu vya simu. Kwa nini ahangaike kiasi hicho? Na kwa nini iwe mapema hivyo? Neema, huoni ni mwujiza huu? Jana tu alikuwa hoi. Leo anazungumza kwa uchangamfu kabisa na yuko logi badala ya hospitali! Huoni kama kuna jambo hapo? Yaonyesha kuwa ananitafuta. Yawezekana hata jana alikuwa akinihitaji mimi tu hakuwa majeruhi wala mgonjwa!” Akasita kidogo kabla hajaongeza kwa sauti ya chini akisema: Na atanipata. Kwa muda mrefu nimekuwa sina kazi ya kufanya”.

Wakati huo Joram alikuwa wima akivuta droo hii na ile, akiweka hiki mifukoni na hiki kiunoni. Mara akaanza hatua za haraka kuelekea mlangoni.

“Yaani unakwenda Joram, mara hii!”, Neema aliuliza kwa mshangao.

“Naam”.

“Mapema namna hiyo? Si umemwambia baada ya saa moja?”.

“Niliamua kumdanganya. Siamini kama yeye ananieleza ukweli mtupu, hivyo nami sioni ubaya wa kumweleza uongo kidogo. Nataka kufika mapema kidogo nione anachofanya”.

“Lakini ujihadhari”, Neema alimwambia wakati akivuka kizingiti cha mlango.

“Usijali Neema”, Joram akamjibu bila kugeuka nyuma.

“Anakuja! Na atakufa!” Proper alimwambia Waridi.

“Ondoa hiyo mikunjo ya hofu usoni uvae suruali yako nzuri kama ilivyo. Akifika mpe tabasamu, mpe mapenzi, kisha mkaribibishe pombe. Usisahau chupa hilo hapo ni kwa ajii yake, akionja tu yamekwisha, asipoinywa mpake hii kwa hila”.

Walikuwa katika chumba fulani, ghorofa fulani, katika jumba hili la light ambalo liko katika mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam. Proper alikodi chumba hiki kwa ajili ya kazi hii tangu jana alipomtoa Waridi kule hospitali. Usiku mzima aliutmia kumtisha Waridi kwa kila namna pale alipojaribu kuleta ubishi. Kisha alikuwa amemlazimisha kufanya naye mapenzi kwa njia zake za kinyama. Ilipofika alfajiri ndipo wakaanza kupanga mikakati ya mauaji.

Waridi alivishwa vazi jeupe la hariri, vazi hili lilifichua kila kitu kilichofaa kifichwa katika mwili wake. Kila jicho liliweza kuona mwili mzuri wa msichana huyo, ulikuwa ukimelelemeta kwa wekundu ndani ya mavazi hayo. Uso wake pia ulikuwa “kioo” kwa uzuri wake wa asili ulioshinikizwa kwa vipodozi murua vilivyotumiwa kistaarabu. Nywele zake zilitengenezwa kwa ile mitindo ya kisasa. Kwa kila hali, msichana huyu alionekana mtu tofauti kabisa na yule binti ambaye usiku wa jana tu alilala chini pale baa akiwa nusu uchi, akilia. Huyu alikuwa katika hali ambayo ilikusudiwa na ilitosha kuushinda ukaidi wa Joram Kiango dhidi ya wasichana warembo.

“Uwe msichana hodari. Ni kazi ndogo tu. Baada ya hapo utakuwa huru. Nitakulipa pesa za kutosha ukanisubiri Nairobi. Kutoka hapo tutakwenda zetu London au New York, tukatumie. Unasemaje?”.

Waridi hakujibu.

“Mbona husemi neno?” Proper alimwuliza Waridi. “Hofu ya nini? Hii ni kazi ndogo mno kuliko ile uliyoifanya kwa Bomba. Na bado itakulipa pesa nyingi zaidi ya ule uchafu uliochukua. Jitie furaha na ucheke kidogo”.

Kikcheko kilikuwa mbali na Waridi. Aliendelea kuduaa kama mzoga akisubiri lolote aliloelekezwa kulifanya. Hilo likamchukiza sana Proper.

Akasema. “Sikia wewe, endapo utavuruga tena mpango huu, sitasita kukuua papa hapa. Sasa hivi bado dakika ishirini Joram ataingia hapa. Nitakuwa chumba cha pili nikiangalia kila kitu. Ukishindwa au kuvuruga mpango huu nitakuua wewe na huyo Joram papa hapa. Nitakuua wewe kwanza na kisha Joram kwa hili hapa”, akatoa bastola ndogo kutoka kwenye mfuko wa koti lake.

“Sipendi kukuua”, Proper aliongeza. “Lakini ukinilazimisha nitaitumia kuwaua”. Akaitazama tena saa yake. “JOram anaweza kuwa anakuja sasa. Natoka. Kumbuka kuwa niko karibu na tayari kukuua endapo utavuruga mpango huu. Sawa? Proper alitoka na kumwacha Waridi ameduwaa kama alivyokuwa.

Baada ya dakika kadhaa mlango wa chumba hiki uligogwa, kisha ukafunguliwa. Joram Kiango alichungulia ndani na kisha kuingia polepole macho yake yakiwa yamepumbazwa na uzuri wa Waridi. Hakutegemea.

“Sisiter… mimi ni mgeni wako nadhani. Naitwa Joram Kiango”, alieleza Joram huku akiandaa tabasamu ambalo alijua linamfaa binti mzuri kama huyu.

Ndipo Waridi alipogeuka kumtazama.

Kama kuna wanawake ambao husimbua mioyo ya wanaume mara tu watokeapo mbele yao hata wanaume hao wakajisahau na kuzisahau shughuli zao, basi ni dhahiri pia wapo wanaume ambao huisumbua mioyo ya wanawake kwa kiwango kile kile. Na kama kweli wapo, miongoni mwao yumo Joram Kiango. Hayo yalijidhihirisha baada ya Waridi kumtia machoni Joram alipoingia chumbani.

Moyo wake ulipoteza mapigo kwa sekunde kadhaa. Roho yake ilihisi kupaa nje ya mwili wake. Kadhalika, damu ilimsisimka kiasi cha kumfanya ahisi ganzi mwili mzima. Hivyo, hakuweza kuyaondoa macho yake juu ya umbo la Joram ambaye alimsogelea polepole. Nusura wazimu umpande Waridi alipoona uso na tabasamu la Joram, lililotosha kuwa tiba kwa maradhi yake. Maradhi aliyoamini kuwa hayangeweza kutibika.

Kwa bahati mbaya, Waridi hakuwahi kupenda mwanaume katika maisha yake. Hivyo hakujua mapenzi ni nini. Hakuwahi kuyaonja. Kama angejua, angefahamu nini kitatokea. Badala yake alihisi maumivu moyoni na huzuni kubwa akilini mwake. Akanusurika kutokwa na machozi. Hakujua nini kinamtokea. Isipokuwa kitu kimoja tu alikifahamu, Joram hakuwa mtu wa kufa, Hakuona sababu ya kumwua, Asingeweza…

Tazama alivyosimama mbele yake kwa upendo na utulivu kama malaika asiye na hatia. Tazama anavyochekelea kwa furaha kama nuru, Mtazame. La, huyu kijana si mtu wa kufa. Waridi akawa ameamua hivyo.

“Nadhani mimi ni mgeni wako, mpenzi, Joram alisema tena, akinyoosha mkono wake kumgusa Waridi kwenye bega lake la kuume.

Joram alikuwa ameshangazwa na uzuri wa msicha huyu. Vipi wengine waumbwe kwa upendeleo kiasi hiki wakati wengine wasitofautiane sana na vinyago? alijiuliza. Mavazi mazuri ya msichana huyu pia yalimchanganya Joram; yalikuwa mavazi mapya ya thamani kubwa, kisha ya kihuni kama yalivyondaliwa mahususi kwa ajili ya kumtongoza! Hicho hakikumshangaza Joram, Lakini alishangazwa na uso mzuri wa msichana huyu ukiwa katika dimbwi la majonzi, mashaka, hofu na msiba. Hilo halikumshangaza hata kidogo.

“Ndio…ka… karibu kaka”, waridi alianza kusema huku akibabaika,

Joram alimvuta mkono na kumwongoza hadi kitandani, ambako alimketisha kisha naye akaketi kando yake huku akiendelea kuushika mkono wa Waridi.

“Nilikwambia kuwa sauti yako ni tamu kama ilivyo sura yako? Naamini sikukosea. Ama kweli umeumbika bibie. Ulimhonga nini muumba hata akakupendelea?”

Sauti ya Joram, tabasamu lake likasindikiza kila neno, hali hiyo ikamfanya Waridi aanze kuchangamka. Akasahau yote yaliyokuwa mbele yake na kujikuta kazama katika maongezi na Joram. Katika kipindi hicho kifupi bila kujifahamu Waridi alijikuta tayari akiwa ameufunua moyo wake wote kwa Joram, akimsimulia matatizo yake yote. Alipotanabahi alikuwa akisema: “Najisikia kutoweka nje ya nchi hii”.

“Kwanini?”.

Swahili hilo lilimzindia Waridi. Hakujua yapi alikuwa tayari kuyatamka ambayo hayakustahili kuiacha milki ya kinywa chake, Hofu ikamrejea. Akalikumbua jukumu lililokuwa mbele yake: kumfanya kijana huyu kuwa marehemu. Ama ni yeye atajayefanywa marehemu.

Hofu hiyo, ilizidi baada ya Joram kuinuka na kuiendea meza iliyokuwa na chupa mbili za pombe huku akisema: “Bia hii? Unaonaje nikianza kuimimina tumboni mwangu ili kupoza joto la Dar es Salaam kabla hujanieleza sababu za kuniita hapa? Siamini kwama kweli umeniita kwa ajili ya kunishukuru tu, yaani hilo likusukume kunitafuta…”

“Usinywe hiyo pombe”, Waridi alifoka.

“Kwanini mpenzi? Nilidhani umeiandaa kwa ajili yangu”, Joram alifuatwa na tabasamu la kukata na shoka.

Waridi alikuwa akitetemeka. Lakini asingeweza kusahau maneno ya yule mtu katili Proper alipomwambia: “Nitakuwa chumba cha pili… Ukishindwa tena nitakuua papa hapa…” Waridi hakupenda kufa, lakini pia hakuwa tayari kumuona kijana huyu asiye na hatia, afe. Afanye nini? Kwa kutojua la kufanya akaanza kulia. Mikono ya Joram ilitua tena mabegani kwa Waridi akimfariji na kumkumbatia huku akisema.

“Kama hutaki ninywe hii bia ni wazi kwamba kuna zawadi kubwa na tamu zaidi ya bia uliyoiandaa kwa ajili yangu. Kwa bahati mbaya nina mazoea ya kunywa pombe kabla ya yote. Kwa maana hiyo niruhusu ninywe bia moja tafadhali”.

“Usi…” Waridi alijaribu kufoka tena. Joram alimzuia kwa kuuziba mdomo wake kwa kiganja cha mkono wake huku akiweka kinywa chakr karibu na sikio la Waridi, akamnong’oneza.

ITAENDELEA

Salamu Kutoka Kuzimu Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment