SIMULIZI The Escrow Mission Episode 05
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
*********************************************************************************
OBOBO ALIINGIA taratibu ndani ya chumba chake, akasimama mlangoni na kukiangalia kwa makini, moyo wake ulipiga chogo chemba baada ya kuiona ile bastola yake a,iyoipoteza kimakosa pale Kenya Lodge. Hakuamini anachokiona, alitazama huku na huku akachomoa bastola yake na kuiweka sawia kiganjani mwake, akapita kona hii na ile akiangalia hapa na pale akidhani labda adui yake yupo ndani. Alipohakikisha hayupo kila kona akaiendea ile bastola, hakuigusa kwanza. Mshenzi huyu alikuja hapa, na kama alikuja keshanijua nilipo, sasa ni kubadilisha mbinu, akajisemea kisha akachukua simu yake na kupiga namba namba Fulani.
“Yes, zile faili bila shaka umezipata…” akaongea na mtu wa pili kwa lugha ya kiingereza.
“Ndio, umefanya kazi nzuri, lakini bado mmoja anazo naye tunazihitaji pia,” ile sauti ikaeleza.
“Sawa, hiyo utaipata usiku huu kwa maana nikikamilisha tu sina budi kuondoka haraka kwani hapa si mahala pazuri kwa sasa,” Obobo akazungumza.
“Ndiyo, ukizipata hizo, nitahakikisha usafiri wako wa kuelekea Dar upo tayari ili kukuondosha hapa na malipo yako utayapata usiku huu huu…”
“Ok! Call you later,” Obobo akakata simu na kukusanya kiilicho chake akatia kwenye begi lake dogo la mgongoni tayari kwa kuondoka. Akafikiria mara mbili tatu akajua akienda kurudisha chumba itakuwa rahisi kwake kujulikana kuwa kaondoka, alichofanya ni kuhesabu pesa za malipo, akaziweka mezani na kuzikandamiza na jagi la maua kisha taratibu akatoka na kupitia mlango wa nyuma na kupotelea mitaani mpaka barabara kubwa na kukodi tax.
“Wapi mzee?” Dreva akauliza
“Uwanja wa ndege!” akajibu, “Ninawahi ndege lakini nikiikosa utanirudisha huku,” akaongeza kusema.
“Sawa hakuna tabu ni elfu kumi tu,” yule dereva alimweleza Obobo naye akampatia noti hiyo, safari ikaendelea mpaka eneo hilo la Uwanja wa ndege/ lengo kubwa la Obobo halikuwa ni kusafiri kama alivyomwambia huyo kijana ila alitaka kufika kukamilisha kazi yake kwa Mheshimiwa Segeratumbo. Akatoa waleti yake kubwa na kuchomoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpatia kisha akachikua pakiti la sigara na kuiweka kinywani.
“Una kiberiti?” akamwuliza yule dereva. Naye badala ya kujibu akampatia, Obobo akawasha ile sigara, akavuta pafu moja kubwa na moshi wake kumpulizia usoni yule dereva.
Kizunguzungu cha ghafla kikamvaa yule dereva, akajikuta akiona watu watatuwatatu, mara akahisi kichwa kizito, “umenifanya nini we-we?” akajitahidi kumuuliza Obobo lakini alihisi mtu huyo anazidi kuwa mbali naye, akainua mikono na kujaribu kushika hapa na pale, akajiegemeza kitini na kukufunikwa na kiza kinene. Obobo akateremka na kuzunguka upande wa dereva, akafungua mlango huo na kufyatua kile kiti kikalala kisha akaufunga na kuufungua wa nyuma upande uleule na kumvuta yule dereva mpaka nyuma akamkalisha kitini na kumfunga mkanda kisha akampachika kofia kichwani. Ilikuwa rahisi kwa yeyote anayemwona kujua kuwa mtu huyo yupo kwenye usingizi. Obobo akakamata usukani na kutoka eneo hilo taratibu, akauacha uwanja wa ndege na kuifuata ile hoteli aliyofikia Segeratumbo.
Kabla hajafika maegeshoni, alimwona mheshimiwa huyo akitoka ndani huku wasaidizi wa hoteli hiyo wakiweka mabegi yake mheshimiwa garini. Anaondoka! Akawaza Obobo huku moyoni mwake akiona kuwa mara hii kazi itakuwa ndogo kwani ni kufanya tu kama alivyofanya kwa Msesema. Akasimamisha gari yake na kuendele kumtazama dereva wa Segeratumbo akipanga mabegi ya bosi wake garini na baada ya dakika kumi ile Toyota Prado iliondoka taratibu na kuiacha hoteli hiyo. Obobo aliifuata nyuma kwa umbali kama wa mita mia moja hivi huku kichwani mwake akipiga hesabu za jinsi ya kuupata mkoba wenye nyaraka au kujua nyaraka hizo zilizobaki ziko wapi.
§§§§
Saa kumi na mbili za jioni, Kamanda Amata aliwasili Isanga Inn, kwa kutumia mlango wa nyuma aliingia bila kugundulika na kukifikia chumba cha Obobo, akachomoa bastola yake ndogo na kuiweka sawia kiganjani, akatikisa mlango, uko wazi. Akausukuma taratibu huku kichwani mwake akiwaza kufanyiwa kama kile alichomfanyia adui yake pale Kenya Lodge. Akausukuma mlango kwa nguvu kisha akaruka na kutua mwisho wa chumba, peupe! Hakuna mtu. Kamanda Amata akatahayari, kaondoka? Akajiuliza. Alipotupa jicho mezani, hakuiona ile bastola.
“Shiiit!” Akang’aka na moja kwa moja akaliendea kabati, hakuna kitu, bafuni, hakuna kitu. Akaiendea ile meza na kupapasa mkono wake kwa chini akatoa kile kidubwasha alichokibandika kwa ajili ya kunasa mazungumzo yoyote yatakayoendelea mle ndani. Akakitoa na kukizima kisha akaminya kinobu cha ‘scan’ wakati huo akiwa kapachika vifaa vya kusikilizia.
Kwanza akasikia mlango kuguliwa na kufungwa, ukapita ukimya kisha akasikia mlio wa simu na kusikiliza mazungumzo yale. Kamanda Amata alisikia sauti ya Obobo tu na ile ya pili hakuweza kuisikia. Akakiweka mfukoni kile kidubwasha na kutoka mle chumbani, akatoka kwa mlango ule alioingilia na kuzunguka mbele ya hoteli hiyo akaingia na kufika kaunta, pale akaulizia kama mwenyeji wake yupo, akaambiwa yupo ndani tangu afike hajatoka. Amata akajua kuwa kwa vyovyote Obobo katoroka bila kuaga, kwa maana hata zile pesa amezikuta pale mezani kama zilivyo.
“Mpigieni simu mwambieni kuna mgeni wake hapa kaunta,” akawaambia na mmoja wale wahudumu akachukua simu na kupiga ile namba ya chumba, simu ikaita na kuita haikupokelewa.
“Mh! Haipokelewi labda katoka,”
“Basi nitakuja baadae!” akaaga na kuondoka huku kichwani akijua wazi kuwa Obobo amewacheza shere pale hotelini. Moja kwa moja alifikia katika ofisi yao ya siri na kukutana na Madam S, akampa kile kidubwasha naye akakipachika kwenye ile mashine yake ambayo iliweza kusafirisha sauti hiyo mpaka kwenye mtambo wao kule shamba Dar es salaam ambako Chiba alikuwa huko akifuatili mambo mbalimbali ya kazi zao.
Madam S alikuwa akirudia kusikiliza hiyo kauli ya Obobo
“Yes, zile faili bila shaka umezipata…”
“Kuna mtu tayari anazo hizo faili,” Madam akamwambia Amata.
“Ndiyo!”
“Sawa, hiyo utaipata usiku huu kwa maana nikikamilisha tu sina budi kuondoka haraka kwani hapa si mahala pazuri kwa sasa,”
“Hapa atakuwa anazungumzia nini? Nini hiyo ambayo ataipata?” Madam alihoji.
“Mh!”
“Sawa, hiyo utaipata usiku huu…”
“Sawa, hiyo utaipata usiku huu…”
“Ina maana atampatia usiku huu?” madam akauliza.
“Nini?” Amata akauliza.
“ Labda faili lingine…” Madam akaotea.
“Enheee uko sawa madam, kwani mpaka sasa nani na nani wameripoti kuibiwa faili hizo?” Amata akauliza kwa shauku.
“Katibu wa Bunge na Mheshimiwa Kibanio…” Madam akajibu huku akitikisa kichwa juu chini, “na Segeratumbo naye analo faili linguine japo hajaripoti kama limeibwa au lipo…”
“Sasa hilo ndo litakuwa la tatu ambalo huyu hayawani anataka kulikabidhi usiku huu kwa mteja wake…” Amata akaeleza.
“You are so intelligence Amata!”
“Segeratumbo yuko hatarini, anaishi hoteli gani? Kama una dodoso yoyote,” Amata akamwambia Madam S huku akiiangalia bastola yake kama ipo sawa.
“Niliuliza, wanasema amefikia Air port Resort,”
“Sawa, niko njiani…”
“Ok! Call you later,”
Madam S alisikiliza sentensi hiyo ya mwisho ya Obobo kwa mteja wake.
“Atampigia tena baadae, nafikiri sasa muda huo ni wa kukabidhiana faili hilo,” akamalizia kusema.
“Sasa tunafanyeje, tusubiri tuwakamate hapo wote wawili au mi niende hukohuko Airport Resort?” Amata akahoji.
“Huwezi kujua ujanja wa adui yetu, nenda mi nitakujulisha lolote lile. Gina na Scoba wako patrol, wewe nenda huko na Chiba kule Dar yupo kwenye Cyber Patrol, nina uhakika usiku huu kila siri itadhihirika lakini kumbuka siri sirini,” Madam S akamwambia Amata.
“Yes Mom!” akajibu na kuondoka.
Ngrrrrrrrrrrrrrrr! Ngrrrrrrrrrrrrr! Simu ya mkononi ya Madam S ikaunguruma pale mezani sekunde chache tu baada ya Amata kuondoka, alipotazama kwenye kioo ilisoma ‘TSA 2’ Chiba! Akawaza na kubofya kile kidubwasha cha kijani.
“Mheshimiwa Matata!” Chiba alitamka hilo jina tu na Madam S akaonekana kupigwa bumbuwazi.
“Mheshimiwa Matata? Acha masikhara Chiba, umejuaje?” akauliza.
“Mimi ndio Chiba wa Chiba, nimesikiliza sana hiyo sauti mliyoituma na kabla yake kulikuwa na mlio wa batani za simu iliyokuwa inabonyezwa kuoiga namba hiyo. Kumbuka mpigaji hakuzima button click, na kila button ina mlio tofauti na nyingine, nimeisoma hiyo milio nikaitafsiri kwenye tarakimu ni 0986 777123, nimeipekuwa kwenye mtambo wangu hapa imenipa jina hilo,” Chiba alieleza kitaalam kidogo.
“Ok, Chiba sasa fanya hivi, hakikisha unakamata mawasiliano yake kutoka sasa tunavyoongea na nyuma kidogo ili tuwanase wote usiku huu ikiwezekana,” Madam alieleza.
“Copy and clear!” Chiba akajibu na kukata ile simu.
Shiit! Yaani Mheshimiwa Matata yumo kwenye sakata hili, siamini. Anadiriki kufanya haya, basi hakuna wa kumwamini duniani, Madam akawaza na kujitupa kitini.
§§§§
Kamanda Amata aliegesha gari yake katika maegesho ya hoteli hiyo, na moja kwa moja akaiendea kaunta na kumkuta mhudumu akiwa ametingwa na kuhudumia wateja jioni hiyo.
“Samahani, Mheshimiwa Segeratumbo, mwambie kuna mgeni wake hapa!” Amata akamweleza yule mhudumu lakini akakutana na macho ya mshangao kwa mbali.
“Una miadi naye?”
“Hapana, ila nina shida naye kiofisi,”
“Mheshimiwa amekwishaondoka kama saa moja nyuma hivi,” yule mhudumu akamweleza Amata.
“Aaah! Ameondoka yaani yupo hapa Dodoma au…”
“Kasafiri karudi Dar na chumba keisharudisha,”
“Ok!”
Amata akarudi garini huku kichwa kikimzunguka, akainua simu na kumpigia Madam S.
“Mheshimiwa ameondoka kwenda dar leo!” akamwambia.
“Sawa, njoo hapa haraka kuna habari nyeti sana juu ya hili,” Madam akamwambia Amata kisha simu ikakatika.
Dakika tano zilizofuata Amata alikuwa tayari akipanda ngazi za nyumba hiyo.
OBOBO ALIENDELEA kuifuata ile gari ya Segeratumbo, wakapita Area C na kutokea barabara ya kuelekea Dar es salaam. Ile gari ikapinda kushoto na kuanza kutimua mbio kwa safari hiyo ndefu, Obobo naye akapinda hukohuko na kuongeza kasi kuhakikisha haiachi mbali sana ile gari. Walipopita eneo la Nane Nane na kuanza kuiacha Dodoma mjini, Obobo alichomoa bastola yake na kuiweka tayari, akapandisha vioo vyote na aliichagua gari hiyo kwa sababu ilikuwa na vioo vya giza, akiwa kwenye kasi ile akaipachika sox yake usoni na kuiweka vizuri usoni.
Akawasha indiketa ya kuipita ile gari ya Segeratumbo, na dereva wa ile gari akapunguza mwendo kidogo na kuiruhusu ile GX 100 ipite. Mbele ya gari ya Mheshimiwa kulikuwa na lori kubwa lenye kontena juu yake, Obobo akapiga honi na kulipita lile lori akiwa kwenye kasi ileile, lile lori nalo lilikuwa kasi. Ijapokuwa ilikuwa ni taabu lakini alifanikiwa kulipita, alipolimaliza tu, alitazama kioo chake cha kuendeshea kilicho ndani juu ya kioo cha mbele akaiona gari ya Segeratumbo nayo inalipita lile lori. Akawasha indiketa ya kusoto na kuingia kushoto ghafla, yule mwenye lori akapiga honi na kukanyaga pedeli za breki, ile lori ikayumba kwenda kushotolakini yule dereva akairudisha kulia ikazidi na lile tela la nyuma likaipiga gari ya Segeratumbo. Dereva wa Segeratumbo alikosa uelekeo akashindwa kuifuta barabara, kutokana na kasi aliyokuwa nayo, ile Land Cruiser ilitoka nje ya barabara ikanyanyuka juu na kugonga mbuyu uliokuwa pembeni kama mita kumi na tano hivi.
Obobo aliegesha gari yake mbele kabisa na kuivua ile sox, akaipachika bastola yake kiunoni na kuifunika na koti alilovaa. Kwa mwendo wa kukimbia akapita lile lori huku akimwacha dereva wake kaduwaa bado akiwa ndani ya gari. Akaifikia gari ya Segeratumbo akakuta inafuka moshi mzito kwenye eneo la boneti kabla hajakaribia, kishindo kikubwa kikasikika, mlipuko ukatokea, ile gari ikarushwa kutoka pale ilipo ikadondokea kando na kuanza kuwaka moto. Obobo alisogelea eneo la tukio, moto ulikuwa unaongezeka kiasi kwamba ilikuwa ngumu kufanya uokozi wowote.
Bahati nzuri yule dereva wa lori akashuka na mitungi ya kuzimia moto miwili mikubwa, kwa kushirikiana na Obobo wakaweza angalau kupunguza moto, wakajitahidi huku na huku na kumtoa Mheshimiwa Segeratumbo akiwa na hali mbaya sana, wakajitahidi tena na kumtoa dereva wake ambaye alikuwa ameungua vibaya. Wakasimamisha gari na kupakia watu hao ili kuwahishwa hospitali. Obobo akachunguza hapa na pale na kuona briefcase ya Mheshimiwa ikiwa imetulia kwenye kochi la nyuma, akaufungua mlango kwa nguvu ukafunguka lakini moto ulikuwa kipingamizi kikubwa sana.
“Sasa unafanya nini wewe?” yule dereva wa lori akamuuliza Obobo.
“Naitoa briefcase yake si unajua hawa waheshimiwa wana miswada mingi ya kiserikali, sasa ikiungua hapa taifa linapata hasara kwani kumbukumbu zinapotea,” alijibu huku akiwa amevua koti lake.
“Ngoja ngoja!” yule dereva wa lori akamwambia na kuja na mti mkubwa, wakaisukuma ile briefcase mpaka upande wa pili,
“zunguka kule ukaitoe, hakuna moto sana!” akamwambia na Obobo akafanya hivyo na kuweza kuipata ile briefcase, alipojaribu kuifungua ilifunguka kirahisi tu. Akaitazama ndani kulikuwa na mafaili kadhaa na kompyuta ndogo, akachambua harakaharaka na kuliona lile faili analolihitaji, ok! Akatikisa kichwa na kuifunga. Dakika hiyohiyo walisikia ving’ora vya gari ya polisi vikija upande huo, na kabla ya wao kufika iliwasili gari nyingine Land Cruiser VX iliyokuwa ikipepea bendera ya Tanzania upande wa kushoto wa boneti lake. Mheshimiwa Matata aliwasili eneo la tukio akakutana na Obobo wakapeana mikono, Obobo akamkabidhi ile briefcase. Wakaongea kidogo na kisha Obobo akaondoka kama anakwenda kuingia kwenye ile GX 100, lakini akatokomea vichakani na kurudi upande aliotoka. Mbele akaibukia barabarani na kuingia kwenye tax moja iliyokuja sambamba na ile gari ya Mheshimiwa Matata.
§§§§
Akiwa mlangoni mara tu baada ya kumaliza zile ngazi alikutana na Madam S aliyekuwa akitoka ofisini na kuubamiza mlango wake kwa nguvu.
“Vipi Madam kuna nini?” akauliza kwa hamaki.
“Twende Amata twende!” Madam akampigia kelele huku akiwa tayari kamaliza zile ngazi na kumwacha Amata pale juu, alichoshuhudia ni kile kifaa alichovaa Madam S sikioni akajua kwa vyovyote yuko kwenye mawasiliano na Chiba, hakuna kujiuliza. Kamanda Amata aligeuka na kumfuata Madam wakaingia garini na ile gari ikaondoka kwa kasi.
“Gari ya Segeratumbo imepata ajali kwa taarifa nilizopewa na Gina na Scoba, vilevile Chiba ananiambia kuwa Obobo yuko eneo la Ihumwa na anaendelea kuwasiliana na mteja wake, inawezekana wanakabidhiana mzigo wao huko,” akaeleza Madam.
“Ongeza mwendo Madam!” Amata akamwambia huku akiweka kifaa chake cha mawasiliano sikioni na kufyatua ile mashine ndogo pale kiunoni mwake.
“Gina! Umefika eneo la tukio?” akauliza.
“Ndiyo tupo hapa eneo la tukio, gari imeshazimwa moto lakini mashahidi wanasema majeruhi wameondolewa mapema sana kuwahishwa hospitali,” Gina akajibu.
“Chiba anasema kuwa adui yetu yuko hapohapo maana amemjaribu kumfuatilia kwa GPS iliyofungwa katika simu yake na mpaka sasa inasoma kuwa yuko hapo…”
“Inawezekana, hapa watu ni wengi kwa sasa, lakini sijamuona kwa muonekano ule ambao ninaujua, ngoja tuangalie,” Gina akajibu na kujichanganya katika kundi hilo la watu huku akijaribu kupepesa macho yake kutazama sura za watu.
Kwa mbali kijana mmoja alikuwa akihojiwa na polisi akionesha kutoka barabarani jinsi ajali hiyo ilivyotokea, alikuwa ni yule dereva wa lori. Ile GX 100 bado ilikuwa palepale imeegeshwa nje ya barabara upande wa kushoto.
Dakika saba hivi Madam S aliwasili eneo lile, akaegesha gari mbele kabisa, mita nyingi tu mbele ya eneo la tukio. Kamanda Amata akashuka na kukifyatua kile kifaa chake cha mawasiliano kwani hakutaka kujulikana na wanausalama. Akachukua simu yake na kuingia code Fulani ambayo moja kwa moja ikaunganisha simu na kile kifaa ambapo sasa alikuwa kama mtu anayeongea na simu.
“TSA 2!” akaita.
“TSA 1 nakusoma,”
“Nipe uelekeo wa adui alipo,” akamwambia.
“Ok, simama hapo ulipo kwa sekunde kama ishirini hivi,” akamwambia na Amata akasimama kusubiri.
Chiba huko aliko aliingia kwenye mtambo huo ‘GPS locator’ na kuingiza code namba za wote na kuanza kuwaona mmoja baada ya mwingine kwenye kile kioo kikubwa, kila mmoja alimuona akiwakawaka kwa kidoti chekundu lakini adui akampa kidoti cha njano.
“TSA1”
“Unasomeka TSA2”
“Hapo ulipo, upande wa kushoto wako tu,” akamwelekeza, “mita zisizozidi ishirini adui yako yupo,” akamaliza. Sauti hiyo ilisikika na wote hivyo kila mmoja akaazna kumwangalia Kamanda Amata kasimama wapi, wakamuona kila mmoja kwa uelekeo wake.
“Lolote linaweza kutokea” Amata akasema, ujumbe huo ukafika kwa wote.
“TSA5 kazini”
“Copy!”
“TSA 3 kazini”
“Copy!”
Hiyo ilimaanisha wote wako tayari kwa lolote litakalotokea wakati huo. Kamanda Amata akaiona ile GX 100 mahala pale.
“TSA 2 hapa ni GX 100 maegeshoni,”
“Check in!” Chiba akajibu kutoka katika mtambo mama.
Kamanda Amata akawaendea maafisa wa polisi waliokuwa wamesimama eneo hilo, akawaonesha kitambulisho cha upolisi kama ACP kutoka makao makuu, wakakuka kwa salamu kisha akawaambia waikague hiyo gari ambayo muda wote ilikuwa hapo. Wakatii, wakaenda kwa tahadhari kadiri ya maelekezo ya kazi yao. Amata akachomoa bastola na kuiweka tayari kwa lolote na wengine wakafanya hivyo. Yule afisa wa polisi akaizunguka ile gari, hakuona kitu kupitia kioo cha mbele, akasogelea na kuuvuta mlango wa dereva hamna kitu alipogeuka nyuma akakuta binadamua aliyelala usingizi mzito akiwa kafungwa mkanda.
Akatoa ishara kuwaita wenzake, Amata akasogelea na kutazama hali ile, gari ilikuwa tupu, mtu mmoja anayekoroma kwa usingizi mzito, juu ya kiti kulikuwa na simu iliyofunguliwa, betri kwake, mfuniko kwake na na mashine kwake.
“Mpekue huyo!” akamwambia yule polisi kijana, akampekua na kutoa leseni ya kuendeshea gari.
“Masoud Matonya!” akasoma lile jina kwa sauti, akaendele kupekua na kumkuta na shilingi 40,000 mfukoni na simu tu, zaidi hakuna kingine.
“Huyu kapewa dawa ya usingizi, apelekwe hospitali haraka nah ii gari muifikishe kituoni,” RTO aliyekuwa hapo akatoa amri wakati Amata akiwa keshachukua ile simu.
“TSA 1, umempata adui, mko pamoja hapohapo,” sauti ya Chiba aliunguruma katika simu ya Amata.
“TSA 2 adui kama adui hayupo labda kama kaiba sura na mavazi ya polisi, hapa kuna gari iliyotelekezwa na mtu mmoja aliyelala usingizi zaidi ya hapo kuna simu tu iliyofunguliwa funguliwa nimeikuta juu ya kiti, nahisi ni simu ya adui,” Amata akaeleza.
“Oooh shiit katucheza shere, ondoka eneo hilo haraka fuata maelekezo mengine, nimeshajua alichokifanya,” Chiba akaamuru.
“TSA abandon area quickly!” Madam aliwaeleza kwa njia ileile ya simu kuwataka kuondoka eneo hilo haraka nao wakafanya hivyo. Scoba na Gina wakaingia katika gari yao na Amata akarudi kwa Madam S wakaondoka zao.
“TSA 1 simu uliyoiokota ni ya mtindo gani?”
“Android, Samsung Note 8,”
“TSA 1, tumempoteza adui kwa sababu GPS location yake ilikuwa haitoki kwenye sim card bali kwenye betri, simu za kisasa hasa za Android zimefungwa chip ndogo sana katika betri ambayo inakuonesha uelekeo ulipo nah ii kwa sababu za kiusalama kama hivi,” Chiba alieleza.
“Copy!” akajibu Amata.
“Adui namba mbili, Mheshimiwa Matata yupo eneo la hoteli ya Mtakatifu Gasper hapo Dodoma, wahini, mkimbana huyo mtampata namba 1, mara ya mwisho wamewasiliana wakiwa hapo eneo la ajali,” akamwelekeza.
Madam S aliongeza kasi na kuliacha eneo hilo. Giza lilikuwa tayari limeifunika dunia upande huu wa Afrika na kufanya usiku kutawala. Madam S akakunja kushoto na kuingia katika lango la hoteli hiyo, akaegesha gari na kuteremka huku akimrushia ufunguo mhudumu wa kupokea wageni kuwa aiweke gari vizuri. Hatua za haraka zilimfikisha katika kaunta ya hoteli hiyo.
“Tuna shida na Mheshimiwa Matata!” Madam S akamwambia.
“Ana kikao hahitaji kusumbuliwa,” akajibiwa.
“Narudia tuna shida na Mheshimiwa Matata,”
“Mheshimiwa ametoa maagizo asisumbuliwe na mtu yeyote hata kama ni mama yake mzazi,” yule mhudumu akajibu tena kijeuri. Wakati huohuo Gina aliwasili waple kaunta na akasikia ujeuri wa huyo mwanadada, hakuuliza, alichomo apingu yake ambayo huificha kwenye jieans lake kila aendapo, akamzungukia na kumkamata mikono akaizungusha kwa nyuma.
“Aah! Samahani jamani nimekosa!” akalalamika yule mwanadada. Gina hakujali hilo akamfunga pingu na kumtoa kaunta.
“We unajibu jeuri mtu usiyemjua?” Gina akauliza.
“Hapana dada bahati mbaya tu, haya mjibu haraka,”
“ Mama, namba 403!” akajibu huku akitetemeka.
“Gina! Mwache mpumbavu huyo,” Madam S akamwambia na Gina akamfungua ile pingu na kumwa.
Madam S akamgeukia Amata na kumtazama.
“Kamasalimie kwa sauti tu, kisha uje!” akamwambia na Amata akatoka na kupanda lifti mpaka ghorofa ya 4 chumba namba tatu hii ndio huandikwa namba 403 yaani ghorofa ya 4 chumba namba tatu. Akaufikia mlango na kuutazama kwa makini ulikuwa umefungwa, akachomoa kile kifaa chake na ule waya akaupenyeza uvunguni, kile kitu kama kijifungo akahakikisha kinafika upande wa pili bila kuonekana, na ile mashine akaitumbukiza kwenye birika la maua lililokuwa jirani na mlango huo kwa maana kifaa hicho hakiwezi kufanya kazi kama vitakua umbali wa zaidi ya mita mbili yaani ile transmitter na kile kifaa cha sikioni, alipokikisha kinafanya kazi akaondoka taratibu na kuelekea nje. Wote wane kila mmoja wawili kwenye gari yao wakeingia garini na kuweza kunasa sauti zile za mazungumzo lakini Chiba TSA2 akiwa Dar alikuwa akizipata na kujaribu kuzifanya kusikika kwa uzuri zaidi.
CHUMBA NAMBA 403
“Tumemaliza kazi kwa wakati! Tumewakomesha wapumbavu wale wanaojifanya kuwaharibia watu mambo yao!”
“Wataweza wapi! Mmoja kafa na huyo aombe Mungu wake apone”.
“Lakini Matata huyu jamaa ulimtoa wapi maana anafanya kazi kwa wakati kabisa?”
“Aaaa mjini hapa mi nilipoona mambo yanatuzidia maana mzee Nnandi hapa alikuwa nusu kufa kwa BP, nikaongea na rafiki yetu Pancho Panchilio si unajua yule jamaa ni mtata sana katika ishu kama hizi. Ndiyo akaniletea huyu jamaa tukakubaliana malipo na kila kitu.”
“Nimeshammalizia pesa yake. Hivi usiku huu anaondoka na Auric Air mpaka Dar kisha kwao sijui wapi, mwenyewe hataki kujulikane,”
Yale mazungumzo yalikuwa yakisikika vyema kabisa katika zile gari na wote walikuwa wakifuatilia kwa makini.
“Sasa hili ndo limekwisha?” mazungumzo yakaendelea.
“Tayari, na mzee nimeshampa taarifa, kasema sawa”.
“Na gawio la wale jamaa kule ughibuni vipi maana wao walishiriki parefu kuandaa huu mpango pesa?”
“Wote wamepata, mtaalamu wetu keshaingiza kwenye akauti zao za Swizz Bank,”
“Wacha tujipongeze asee, tumeweza”.
“Sasa twendeni hapo bar kuna hafla fupi na wazee wengine wanakuja muda si mrefu!” sauti ya aliyeonekan mwenyekiti wa kikao ilisikika na mara ukasikika mlio wa maji chooni kisha mlango ukifunguliwa na kufungwa.
“Aaaa! Waheshimiwa, tazameni hii, hii siyo earpiece?” Nnandi akauliza.
“Maweeeee! Nani katuwekea, ina maana kasikiliza mazungumzo yote”.
“Msichanganyikiwe na vidubwasha kama hivi, wenye vitu hivi na watu wa Usalama wa Taifa na nitamwita boss wao atueleze hebu kiokote twende nacho,” sauti ya Matata ikasikika.
§§§§
“Ha ha ha ha!” Madam S aliangua kicheko. Na Amata naye akafuatia kucheka.
Katika gari ya pili Gina aliinua simu yake na kupiga namba ya kampuni ya ndege ya Auric, akawauliza kama wana ndege inayokuja Dodoma kesho yake. Wakamwambia kuwa ndege yao imekodiwa usiku huo kuja Dodoma na kurudi Dar. Lakini hata siku ya pili ndege itakuwepo kwenye ruti zake za kawaida za Dodoma, Iringa, Mbeya.
“Ok, asante sana nitakupigia tena. Gina akakta simu. Kisha akabonya namba nyingine na kuongea na amata.
“Kamanda Amata, ndege ya Auric ipo njini kuja Dodoma, imekodiwa, nafikiri adui yetu anaondoka na hiyo kama mabosi wao walivyozungumza,” Gina akamwambia Amata.
“Uko sahihi, Gina na Scoba mtabaki hapa nahitaji uthibitisho wa picha za wote waliohudhuria tafrija hiyo, mimi namshughulikia huyu jamaa kabla hajaiacha ardhi ya Dodoma.
Mpango ukasukwa na kusukika.
“Madam S ngoja nikatembelee chumba namba 403 kwa mara ya pili na kwa haraka,” Kamanda Amata akaaga na kuondoka mpaka katika hoteli ile na kukifuata kile chumba, alipofika kwanza alitaka kuhakikisha kama hakuna mtu hivyo akachomoa kamera yake ndogo sana iliyounganishwa na waya mrefu tu, akaiingiza chini ya mlango na kuiinua kidogo huku kwa nje aliweza kuona kila kitu kupitia kijisikirini kidogo alichokishika mkononi, hawapo, akajisemea na kuinuka, akatia mfukoni kamera yake akaiichukua ile mashine yake ya mawasiliano isipokuwa ile earpiece haikuwapo. Akacheza na funguo yake na kuingia ndani ya chumba hicho kikubwa kilichobeba kitanda kimoja cha 5×6 na seti moja ya sofa ya viti vidogo. Katikati ya sofa hizo kulikuwa na meza ndogo juu yake kuliwekwa mafaili kadhaa na briefcase iliyoonekana kuchakaa kwa kuungua na moto hapa na pale ilikuwa pamoja nazo. Akaijongelea na kuyapekua yale mafaili. Dah! Watu washenzi kabisa, mafaili yote haya hapa, zama zenu zimekwisha, akawaza na kuyakusanya yote, kisha mezani akaacha ujumbe kwenye karatasi ulioandikwa kwa kalamu ya chuma akachukua ile briefcase bila kuichika mkono wake akaweka ndani yake na kuifunga kisha taratibu akakiacha kile chumba na kupotelea nje.
Katika mlango mkubwa wa hoteli hiyo alipishana na vigogo kadhaa wakiingia ndani akajua tu bila shaka ndio waalikwa wenyewe. Moja kwa moja akajitoma ndani ya gari ya Madam S na kuketi vizuri.
“Umepata chochote?” madam akauliza.
“Nimepata vyote, faili zote tatu za ule muswada hizi hapa na hii ni briefcase ya Segeratumbo na kabrasha zake za ofisi zimo humo,” Amata akaeleza.
“Hongera kwa kazi!” madam alimwambia huku akiondoa gari kuelekea uwanja wa ndege.
“Na sasa ni kumtia nguvuni yule hayawani, umejipanga?” madam akamwambia Amata
“Bila shaka, nitamtia nguvuni kwa nguvu ndogo tu ila akileta jeuri, safari hii nitamuumiza”.
§§§§
Madam S aliegesha gari ndani ya uwanja wa ndege baada ya kupata kibali maalum kutokana na kazi yake. Kamanda Amata akateremka na moja kwa moja akaiendea ndege ndogo iliyokuwa imeegeshwa muda huohuo hapo, akaingia ndani mpaka chumba cha rubani.
“Samahani, huruhusiwa kuwa huku!” yule rubani wa kike akakmwambia Amata.
“Husijali mrembo, usalama upo, keti kwenye kiti chako,” Amata akamwambia yule rubani mwanadada. Bila ubishi akaketi katika kiti chake huku Amata akiketi katika kiti kingine cha upande wa pili.
“Mteja unayemfuata anaitwa nani?”
“Obadia Obasanjo,” akajibu yule rubani.
“Ok, usiwe na wasiwasi, shida yangu utaijua sasa hivi,” akamwambia na kumwonesha kitambulisho cha upolisi, kitambulisho bandia. Yule mwanadada akatulia kitini kusubiri kinachofuata.
Obadia Obasanjo au Obobo kama anavyojiita aliingia ndani ya ndege hiyo akiongozwa na rubani mwingine wa kiume. Msafiri alikuwa peke yake, akaketi kwenye kiti cha starehe kabisa na kufgunga mkanda yule. Yule rubani wa kiume akaelekea kwenye chumba cha kazi na huko akamkuta Amata.
“Kaa hapo, funga mlango wako, ondoa ndege,” Amata alipenda kupambana na Obobo ndege ikiwa hewani kwa maana alijua ikiwa chini hapo vita inaweza kuwa kubwa. Ile ndege ikachukua barabara ya kuruka na ilipokuwa tayari aiakaiacha ardhi ya Dodoma taratibu na kupasua anga.
“Hii ndege usiipeleke popote, izungushe hapahapa ili nimalizane na mtu wangu,” Amata aliwaambia na ndege ilipokuwa tayari hewani imetulia, alifungua mlango na kujitokeza katika kile kijisebule kidogo ambacho Obobo alikuwa ameketi kwa starehe kabisa huku akijimiminia whisky baridi.
“Endelea kufurahia maisha lakini bado haujanikimbia!”
Sauti hiyo ya kamanda Amat ilimshtua Obobo mpaka ile chupa ikaanguka chini, alipotaka kuinyanyua Amata alichomoa bastola yake kiunoni.
“Iache hapo hapo! Kaa vizuri kitini hayawani mkubwa wewe,” Amata akamwambia. Obobo akarudisha mgongo wake kitini na kushusha pumzi ndefu. Kamanda Amata akafyatua pingu yake kiunoni na kumwonesha kwa kuining’iniza.
“Hii hapa ndiyo saizi yako, sasa ni mguu kwa mguu mpaka panapokustahili na ukatueleze kwa nini ulikuj nchini,” Kamanda Amata akamrushia ile pingu ajifunge mwenyewe kumbe hakujua kama Obobo alikuwa akisubiri kitendo hicho. Obobo akaidaka na kuirudisha kwa Amata kwa kuirush na wakati huo akainuka kitini na kuichukua ile chupa ya whisky. Kamanda Amata akaidaka ile ile pingu na sekunde hizo hizo akaiona ile chupa ikija kwake kwa guu lake la kulia alijizungusha na kuipiga teke ikatawanyika vipande vipande. Obobo alimuwahi Amata kwa minajiri ya kumkaba lakini akili ya Kamanda ilikuwa mbele zaidi, alipoushusha mguu wake akapiga msamba Obobo akapita hewani. Kamanda Amata akafyatua pigo moja la karate lililotua kwenye korodani.
“Aaaaaiiiiiggghhhhh!” Obobo alipiga kelele huku mikono yake yote akiikusanya kwenye dhakari yake. Amata alinyanyuka na kumfumua teke moja kali lililotua usoni, likamweka wima na kisha akajibwaga upande wa pili. Obobo alijisahaulisha maumivu yake, akainuka kwa kasi na kupeleka shambulizi la makonde mazito lakini yote Amata aliyaepa ila moja wpo akazunguka nalo na kuudaka mkono kwa mbele akaupinda.
“Aaaaiiigh!” Obobo akaguna tena, “Umenivunja mkonoooo!” alipiga kelele huku viungo vya mkono wake vikiachana. Amata akamnyanyua na kumbwaga chini kwa mbele, Obobo alitua kama mzigo kutokana na ukubwa wa mwili wake, pande la chupa ile ya whisky likamchoma pajani na kuzama huku nje likiacha kitako tu.
“Kwisha jeuri yako pumbavu mkubwa wewe!” Amata alsema huku akisindikiza sentensi hiyo na sonyo refu. Akaichukua ile pingu pale chini na kuifunga mikono ya Obobo, akiwa pale chini hoi.
“Naitwa Kamanda Amata, TSA 1, hapa uponyoki paka wewe!” akajigamba Amata kisha akawaambia wale marubani wateremshe ile ndege chini.
MADAM S ALIITAZAMA SAA YAKE ilitimu saa nne na nusu za usiku wakati ile ndege ikiegeshwa mahala pake. Gari mbili za polisi zilikuwa zimewasili na moja ni ile pikapu yenye boksi kubwa la kuhifadhia wahalifu. Vimulimuli vyake vilikuwa vikipendezesha uwanja huo. Vijana wawili wenye bunduki aina ya SMG wakaongozana na Madam S pamoja nao RPC wa mkoa wa Dodoma alikuwapo. Mlango wa ndege ukafunguliwa na Amata akajitokeza kwanza.
“Wawili wengine tafadhali,” akaita na askari wawili wasio na silaha wakingia ndani ya ndege hiyo na kutoka na Obobo wakiwa wamemshika huku na huku na mikono yake ikiwa imefungwa kwa pingu. Suruali yake ilikuwa imeloa damu nzito, maumivu makali ya jeraha la mguu na mkono vilimfanya ashindwe kujimudu peke yake. Akiwa chini ya ulinzi mkali aliingizwa ndani ya lile pikapu lenye box na kufungwa minyororo kwenye vyuma vilivyotengenezwa ndani yake. RPC na Madam S wakatikisa ile minyororo kwa zamu kuhakikisha kama imefungwa sawasawa walipojiridhisha wakatoka na kufunga mlango wa kwanza kisha wale askari wenye bunduki wakaingia na kufunga mlango wao kwa ndani.
“Asante kamanda,” Madam akashukuru.
“Asante na wewe”.
Wakaingia garini na kuondoka, mbele ilitangulia gari ya polisi ikifuatiwa na ile ya RPC kisha ikaja iliyombeba Obobo, ikafuata ya Madam S na Amata na mwisho ikamalizia nyingine ya polisi, vingora vikali viliufanya msafara huo kuachiwa barabara.
DAR ES SALAAM
Baada ya siku 2
“Nashukuru sana, kwa maana hapa hali ya hewa ilishaharibika, mmefanya kazi kubwa ijapokuwa ni ninyi wenyewe mliamua,” Mkuu wan chi alimwambia Madam S walipokutana kwenye kikao ndani ya jengo la Ikulu.
“Ilibidi kutokana na ghasia za wananchi kudai haki yao, hatupendi kuona Watanzania wanateseka kwa kupigwa virungu na mabomu ya machozi wakati tatizo ni viongozi wenyewe. Inabidi uwaambie watu wako, uliowapa dhamana ya nchi hii waache kutumia maisha ya Watanzania kwa manufaa yao. Watanzania wamechoka na siku wakichoka zaidi nchi hii itabadilika rangi,” Madam S akamwambia Mheshimiwa Rais huku akimkabidhi yale mafaili. Akayapokea na kuyapekua ndani yake akapitia kidogo hapa na pale akatikisa kichwa.
“Watu hawana huruma na nchi yao! Hata huyu naye, na huyu lo!” akatamka.
Unasema hayo kutoka moyoni au ndio kujikosha tu, kama walio chini yako wanayafanya haya ina maana nawe mkubwa unafanya yaya haya, si ajabu una interest kwa hili, Mungu na wanadamu, Shetani na wahuni,” Madam S akapitisha ukimya uliotawaliwa na mawazo, chozi likamdondoka.
“Madam S vipi?” Mheshimiwa Rais akauliza.
“Aaah hapana Mheshimiwa, kawaida tu,” Madam alijibu huku akifuta machozi.
“Ok, haya yatafanyiwa kazi, na kila aliyehusika atashughulikiwa lakini nikitoka Washington kwani nitaacha tume maalumu ya kuchunguza watu hawa mmoja kwa mwingine,” Rais wa Jamhuri akamwambia Madam S.
Uchunguzi gani wakati kila kitu kiko wazi? Madam akajiuliza.
“Sawa Mheshimiwa, hilo ni wazo zuri,” akajibu na kupeana mikono kisha wakaagana. Madam S taratibu akatoka na kuteremka ngazi za jengo hilo tayari Scoba alikuwa keishafika kwa kumchukua.
“Vipi Madam?” Scoba akauliza.
“Tutafika tu, hata kama ni kesho!” Madam S akajibu, huku mlango ukifungwa nyuma yake
††† MWISHO †††
Also, read other stories from SIMULIZI;