Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Pili
NEW AUDIO

Ep 02: Tutarudi na Roho Zetu

SIMULIZI Tutarudi na Roho Zetu
Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Tutarudi Na Roho Zetu?

Sehemu Ya Pili (2)

Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Tatu

ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA

Nzuri sana, shemeji,” msichana huyo alizungumza kwa furaha huku akimtazama Joram kwa mshangao. “Pole sana shemeji,” aliongeza.

“Kwa?”

“Ule mchezo wa jana. Unajua mimi mpaka sasa siamini kama mlikuwa mnacheza tu. Nilidhani mlikuwa mnapigana. Yule bwana kashikilia kuwa ni mchezo tu”.

“Ulikuwa mchezo. Mazoezi ya viungo. Wazungu huita practice.”

“Mpaka mtoane damu?”

SASA ENDELEA

Hakujua Joram alivyoisherehekea habari hiyo. Alitupa maneno mengine mawili matatu, kisha akairudia meza yake. Akaendelea kunywa na kuvuta. Japo alionekana katika hali ya utulivu, lakini macho yake yalikuwa makini, yakimtazama kila anayeingia na kutoka. Aliwaona wengi. Na kati yao alikuwemo yule ambaye alihitaji kumwona.

Alikuwa rafiki au adui yake, Chonde. Aliingia na kuifuata meza ambayo haikuwa na mtu, akaketi. Mara tu Joram alipomwona akainuka na kwenda kupiga simu ambayo alizungumza maneno machache sana. Kisha alikirudia kiti chake na kumwita mhudumu ambaye aliombwa kuleta bia nne. Mhudumu huyo alipozifikisha chupa hizo Joram alimwelekeza azipeleke kwa Chonde. Kisha alitulia akimtazama Chonde alivyokuwa akibishana na mtumishi huyo kwa zawadi hiyo ambayo hakujua ilikotoka hadi alipoelekezwa na kumwona Joram. Akazipokea na kuanza kunywa.

Lakini baada ya dakika kumi meza ya Joram ilifurika kwa chupa kumi zilizoletwa na mtumishi yuleyule kwa niaba ya Chonde. Walitazamana kwa muda. Baada ya muda Chonde alihamia meza ya Joram.

“Za tangu jana?”

“Siyo mbaya.”

Wakaendelea kunywa kwa muda. Kila mmoja akimsoma mwenzake. Kisha Chonde alitokwa na kicheko chembamba. Joram aliungana naye kwa tabasamu dogo.

“Pole sana.”

“Kwa?”

“Yale ya jana.”

“Lilikuwa zoezi tu. Usijali.”

Kikafuata kimya kingine, kimya ambacho Joram alikivunja kwa kuanzisha maongezi ambayo Chonde alizungumza kwa uangalifu akiepuka lolote ambalo Joram alihitaji kufahamu juu yake. Pamoja na Joram kuzungumza kwa ujanja na hila za kila aina, bado Chonde alimfanya ajione mtoto sana katika dunia ya upelelezi na mzembe katika elimu ya saikolojia. Ni hapo alipozidi kuamini kuwa Chonde hakuwa mtu wa kawaida. Na kama alikuwa jasusi bado hakuwa jasusi la kawaida. Alikuwa zaidi. Jambo hilo liliongeza hasira za Joram dhidi ya mtu huyo. Amshinde vipi katika mapambano ya mwili na amshinde tena katika mapambano ya kiakili? Hata hivyo Joram hakujali sana, akijua kuwa dakika hii ambayo anaipoteza na Chonde, mahala fulani, yuko mtu ambaye anaifanya kazi ile ambayo yeye alishindwa kuifanya jana, kazi ya kufungua kile kijaluba cha Chonde na kuona kimehifadhi nini hata kilindwe kwa kiwango kama kile. Hivyo, akaamua kumruhusu Chonde aendelee kumlaghai na kumdhihaki.

“Mwanamapinduzi aliyekata tamaa,” Chonde alisema. “Aibu ilioje kukata tamaa hali nchi yako iko mashakani? Si ungejaribu kutoa mchango wako?”

Joram hakumjibu.

Kisha kama aliyekumbuka jambo Chonde alisema ghafla, “Nasikia msichana wako ametekwa nyara!”

“Umesikia wapi?”

“Kwani ulidhani siri?”

Hilo lilimshitua Joram. Alishangaa kuona mtu huyo alivyo mwepesi wa kupata habari. Baada ya kuisoma barua ile Joram hakuipeleka polisi wala kuchukua hatua zozote zaidi ya kutabasamu tu. Lililomfanya asifanye lolote hasa ni kule kuwa kwake na uhakika kuwa barua ile aliielewa zaidi ya mwandishi wake alivyotaka aielewe. Bila shaka mtu huyo alikuwa amezidokoa habari hizo kwa polisi. Jambo hilo lilimfanya azidi kumfanya Joram kuamini kuwa hakuwa mtu mwenye mkono mrefu tu bali alikuwa na masikio mapana.

Yeyote aliyeketi kando akiwatazama watu hawa wawili wakiongea angeamini kuwa ni kikao cha marafiki wa siku nyingi. Asingeamini kuwa yalikuwa kama maongezi baina ya Chatu na Mbwa, au baina ya Malaika Gabriel na Ibilisi.

Yule msichana wa mapokezi alikuwa mmoja kati ya watu walioamini hivyo. Alikuwa amewatazama kwa muda mrefu na kushuhudia wanavyocheka na kutabasamu, akayasahau mashaka yote aliyokuwa nayo juu ya urafiki wao na kuamini kuwa pambano la jana lilikuwa zoezi la viungo. Hivyo, alizama katika shughuli zake na kuwatupia jicho mara moja moja.

Chonde alikuwa akifunua mdomo kuongea kitu wakati saa yake ilipotoa mlio ambao haukuwa wa kawaida. Ulikuwa mlio wa sauti nyembamba sana, ulimfikia Joram kwa mbali sana. Chonde aliitazama saa hiyo kwa utulivu, kisha alimtazama Joram kwa makini zaidi. Dakika mbili baadae aliendelea kunywa kwa utulivu. Dakika ya tatu aliinuka na kuaga kuwa anaelekea msalani. Joram alisubiri dakika tano, kisha akamfuata. Hakumkuta. Akafahamu kuwa mlio katika saa ya chonde ulikuwa ishara ambayo ilimkumbusha kitu fulani, jambo lililomfanya Joram kuhofia mtu wake ambaye wakati huu alikuwa katika chumba cha Chonde. Hivyo, akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha namba za simu za chumba hicho. Haikupokelewa. Toka kwenye simu, Joram alitoka nje ya hoteli na kukodi gari ambalo lilimpeleka New Afrika. Akajipenyeza kwa hila hadi ghorofani, mbele ya chumba hicho. Akatega sikio na kusikiliza kwa makini. Chumba kilikuwa kimya kabisa. Ukimya huo ulimtisha sana. Aliyaamini sana masikio yake. Na kwa vyovyote alitegemea kuwa na mtu chumbani humo. Akasikiliza kwa makini zaidi. Bado hakusikia chochote. Akaufungua mlango taratibu na kuchungulia.

Macho yake yalivutiwa na mtu aliyelala chali juu ya sakafu utumbo wake ukiwa nje, macho yake yakidhihirisha kuwa roho ya mtu huyu pia ilikuwa nje. Kabla Joram hajajua kuwa ilimpasa kuingia chumbani humo au la, sauti nzito aliyoifahamu sana ilimhimiza ikisema, “Usiogope. Karibu ndani.”

Msemaji alikuwa kajificha nyuma ya mlango, bastola kubwa ikiwa mkononi mwake ikimtazama Joram kwa uchu.

“Ingia na ufunge mlango. Nadhani hutapenda kufia hapo mlangoni kama paka. Njoo ndani ufe kistaarabu kidogo.”

Joram akaingia. Hakujishughulisha kumtazama Chonde aliyesimama nyuma ya mlango na bastola yake. Badala yake alimtazama marehemu na kushuhudia alivyouawa kinyama. Tumbo lake lilikuwa limebomoka kwa kitu ambacho hakikuwa risasi wala kisu. Bila shaka ulikuwa mlipuko wa bomu. Kifo hicho kilimsikitisha sana Joram. Huzuni ikamshika. Kwa huzuni hiyo alimgeukia Chonde na kufoka kwa hasira akisema, “Shetani mkubwa. Kwa nini umemwua mtu huyu asiye na hatia?”

“Ni wewe uliyemwua,” Chonde alimjibu Joram.

“Mimi! Nimemwua vipi?”

“Usijifanye hufahamu. Bila shaka ni wewe uliyemtuma kuifanya kazi ile ambayo mwenyewe ilikushinda. Kazi ya kujua katika kisanduku hicho mna nini. Nami nikifahamu kuwa pamoja na kukuadhibu, kama nilivyokuadhibu usiku wa jana usingekata tamaa ndipo niliamua kutega bomu dogo kando ya kisanduku hicho. Wakati huohuo mtu yeyote anayekigusa saa yangu inaniashiria. Hivyo tulivyokuwa tukinywa hapo hotelini nilishangaa kuona dalili za mtu.

“Nikafahamu kuwa mtu asiye na hatia anakufa. Nimemkuta kisha kata roho.” Akageuka kumtazama marehemu kwa muda. Kisha aliyarejesha macho katika uso wa Joram na kusema, “Ni wewe uliyestahili kuwa chali, utumbo nje, badala ya mtu huyu, Joram.”

Joram asingeweza kukanusha. Kifo cha kijana huyo kilimsikitisha sana. Alikuwa mmoja kati ya vijana wake smart ambao huwatumia kwa hili na lile, kijana ambaye alikuwa amemsaidia sana katika harakati zake zilizopita. Hakupata kushidwa hata mara moja isipokuwa leo ambapo ameyapoteza maisha yake. Joram akajilaumu kumtuma katika kadhia hiyo. Hamu yake ilikuwa ni kumshinda na kuutawanya ubongo wake sakafuni…

Kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yake, vilevile Chonde aliongeza kwa sauti nzito, “Hata mimi sikufahamu kama wewe ni mtu hatari sana Joram. Unastahili kufa mara moja.”

Maisha yakiwa ukingoni, Joram alijua kuwa alihitaji kuikusanya akili yake yote ili ajiokoe. Hakujua afanye nini. Walikuwa na bastola moja tu, na ilikuwa katika mikono ya Chonde. Kuipata bastola hilo ilikuwa ndoto ya mchana. Chonde alikuwa macho kama kipepeo. Na bado Joram asingemudu kuitumia mikono yake. Hata hivyo, alitegemea kitu kimoja tu kimsaidie kutafuta muda wa kuokoa maisha yake. Muda. Muda waweza kufanya maajabu. Hata asipookoka, si inapendeza endapo ataufaidi uhai wa dakika chache zaidi.

“Najua ninakufa,” alisema. “Nadhani unafahamu vizuri kuwa nakufa kwa ajili ya tamaa ya kutaka kujua siri uliyoificha katika kijisanduki hicho. Nifanyie basi wema wa mwisho. Nifungulie kisanduku hicho nife nikijua mna nini.”

Chonde alicheka, “Tatizo lako Joram ni kule kufikiria kuwa unacheza na mtoto mdogo. Unachojaribu kufanya ni kuvuta muda. Wakati huohuo unathubutu kuendelea na upelelezi wako ili endapo lolote litatokea – kitu ambacho siamini – utoroke na kutoa siri hiyo nje. Kwa taarifa yako siri iliyoko katika kisanduku hicho ni nzito kuliko bara zima la Afrika. Kwa maneno mengine, ni siri ambayo dunia nzima inapigania kujua. Kwa bahati mbaya watu tunaoifahamu siri hiyo ni wachache sana. Na tumeshona midomo. Hata maiti siwezi kuisimulia siri hiyo. Nadhani hilo linakutosha. Sasa jiandae kufa. Ungependelea risasi ya kichwa au kifua?”

Joram alimtazama usoni na kuliona tabasamu la kifedhuli katika macho yake, tabasamu ambalo halikuwa na mzaha. Akajaribu kuicheza tena karata yake ya mwisho. “Jana ulinishinda kwa judo. Vipi ukiniua kwa mikono? Nadhani ni aibu na dalili za uoga kutumia risasi pasipo na umuhimu.”

Chonde alicheka tena. “Ningependa kukuua kwa mikono mitupu. Hata hivyo, sina muda wa kutosha. Umebakiwa na nusu dakika ya kuishi. Utapenda kufa ukiwa umefumba macho au nikuue ukinitazama?”

Sasa mzaha ulikuwa mbali na sauti ya Chonde. Mauaji yalikuwa wazi katika macho yake. Joram akajua kuwa maisha yake yamefika ukingoni. Akiwa ameshuhudia vifo vingi vya risasi alitabasamu kimoyomoyo na kuamini kuwa hatimaye zamu yake imefika. Hata hivyo, bado aliyapenda maisha. Bado aliipenda dunia. Na alikuwa akiiacha moja kwa moja. Hivyo, badala ya kuyafumba macho yake aliyafumbua kwa nguvu na kuyakaza usoni. Hiyo pia aliifanya kuwa karata yake ya mwisho kwani kuua si mchezo, hasa kumwua kiumbe asiye na uwezo wa kujitetea.

Ilimsaidia. Nusu ya dakika ilipita Chonde kaielekeza bastola katika kifua cha Joram, kidole chake kikigusa kiwambo cha kufyatulia risasi, lakini alisita kuifyatua. Mara mlipuko wa bastola ukasikika. Joram alijirusha kando na kutua chini ambapo aliruka tena hadi upande wa pili wa kitanda. Risasi mbili tatu zaidi zikasikika, kama zinazopigwa bila shabaha yoyote. Kisha kimya kikafuata. Kimya hicho kilitoweka kwa mkoromo wa mtu aliyekuwa akikata roho. Ndipo Joram alipojiinua na kuchungulia. Ikamshangaza kumuoa Chonde kalala chini, kifudifudi, damu zikimvuja katika tundu kubwa la risasi katika uso wake. Joram alichupa na kuirukia bastola iliyokuwa mikononi mwa Chonde. Akajicheka kwa kuona akipokonya bastola kutoka katika mikono ya marehemu aliyekata roho kitambo. Akaikimbilia suit case ya chonde pamoja na kile kisanduku. Akavichukua na kuanza kutoka.

Mara mlango ulifunguka ukifuatwa na bastola ambayo ilichungulia kwa uangalifu. Bastola ikaingia ikifuatiwa na binadamu ambaye aliufunika uso wake kwa kofia kubwa na miwani. Alikuwa kavaa suruali na koti la kiume katika hali ambayo ingemfanya mtu yeyote amfikirie kuwa pande la mwanamume. Lakini Joram alimfahamu mara moja. Akaitelemsha bastola yake ambayo aliishika na kumkimbilia huku akisema kwa furaha, “Nuru nawezaje kukushukuru Nuru?”

Walikumbatiana na kubusiana kwa furaha.

Kisha walitengana mara moja na kutazamana. “Umewezaje kunifahamu mara moja kwa urahisi kiasi hiki? Tangu nimetoweka watu wanashindwa kunifahamu”.

“Nadhani nakufahamu zaidi ya wanawake wote. Zaidi ya hayo nani mwingine ambaye anaweza kuhatarisha maisha yake kuipenyeza risasi katika tundu la ufunguo ili kumwua mtu ambaye alikuwa tayari kuniangamiza? Kwa kweli sijui namna ya kukushukuru Nuru!”

Wakakumbatiana tena.

“Nuru! Niliwahi kukwambia kuwa u mzuri? Niliwahi kukuambia kuwa hawakukosea waliposema kuwa wewe ni binadamu aliyekuja duniani kwa makosa badala ya kuwa malaika kama ulivyokusudiwa? Nadhani walikosea Nuru. Wewe ni malaika. Tazama ulivyo mzuri! Tazama ulivyotokea na kuipokonya roho yangu kutoka katika kinywa cha mauti. Nuru, nawezaje kukushukuru Nuru?”

Hayo yalipita katika kichwa cha Joram wakiwa wamekumbatiana. Joram alitamani kuyatamka kwa sauti, lakini hakufanya hivyo. Badala yake alisema, “Nakupenda.”

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Nuru kumsikia Joram akilitamka neno hilo. Mara kwa mara alimtesa kwa kutojua kama kweli alimpenda au la. Ingawa walifanya mapenzi, mara nyingi, lakini bado Joram hakuwahi kulitamka neno hilo kwa sauti ambayo ililipa uzito kama huo. Kadhalika, macho yake hayakufichua mapenzi yake kwa hali yoyote. Hivyo, kwake ilikuwa zaidi ya habari njema. Hata hivyo, bado alikuwa na la kusema. “Sikuamini Joram,” alimnong’oneza. “Pamoja na kutoweka kwangu nikiwa nimetekwa nyara hukujishughulisha kunitafuta. Walao kutoa taarifa polisi.”

Joram akaangua kicheko. “Usinichekeshe Nuru. Waweza kuwa ulifanikiwa kuwalaghai watu wote pamoja na polisi, lakini mimi hukunidanganya. Nilijua kuwa ilikuwa hila uliyoiandaa tu ili unishawishi kuingia katika vita. Mwandiko wa barua ile pamoja na kuuvurugavuruga, kwa mtu aliyesomea miandiko kama mimi, nilifahamu kuwa ni wako. Vilevile ile damu iliyodondoka pale haikuwa na uzito wowote. Nilijua umejikata kidole makusudi. Na ile vurugu iliyofanyika chumbani haikuwa na umuhimu. Kwa vyovyote, majasusi khatari kama hawa wasingefanya mchezo usio na umuhimu kama ule. Hivyo, nilikuwa nikikusubiri nikitegemea utokee na tuendelee na starehe zetu.”

“Starehe?” Nuru aliuliza kwa mshangao. Alishangaa kuona Joram alivyoigundua hila yake kwa urahisi. Ilimshangaza zaidi alipodai starehe wakati wamesimama kando ya maiti mbili ambazo zilikuwa hata hazijapoa kwa ajili yao. “Starehe Joram? Nilidhani tumeingia kazini.”

Joram akatabasamu. “Sikia Nuru, siyo tabia nzuri kuzungumza kando ya maiti za binadamu. Pamoja na kwamba bastola zilizotumika zilikuwa na viwambo vya kupoteza sauti bado mtu yeyote anaweza kutokea na kutukuta katika hali hii. Nasi hatuna muda wa kuyajibu maswali ya polisi. Twende zetu mara moja,” alimaliza akiichukua mizigo yake na kuanza kutoka. “Nifuate. Twende kwa utulivu kama tutokao chumbani kwetu.”

“Kumbuka tu wanaume wawili,” Nuru alisema akitabasamu.

Waliteremka na kuiacha hoteli bila ya tatizo lolote. Watu wawili watatu waliokutana nao waliwatazama kikawaida.

Baada ya kuingia mitaani Nuru aliifichua bastola na kumpatia Joram akisema. “Chukua bastola yako. Samahani kwa kuichukua bila idhini yako. Nadhani uliihitaji sana. Ningeweza kukupotezea maisha.”

Tabasamu likamtoka Joram. “Hata hivyo umeniokoa. Kama ningeingia nayo pengine Chonde angeniua kwanza na kunisimanga baadaye,” Joram alijibu. “Nimepata nyingine. Hii umeipataje?”

“Nilienda kwako kuichukua”.

“Na umewezaje kunusa kuwa niko katika chumba kile nikisubiri kufa hata ukaja kuniokoa?”

“Ni rafiki yako aliyekuokoa. Hayati Edward ambaye, kwa bahati mbaya, mshenzi yule amemwua. Unajua nilipotoka hotelini kwa kisingizio cha kutekwa nyara, nilienda kujificha kwake? Tulijadiliana nae namna ya kurudisha moyo wako katika msimamo unaotakiwa. Mara ukampigia simu na kumpa maelekezo ya kwenda kufungua kisanduku hicho. Aliponieleza maelezo yako na jinsi ulivyoponea chupuchupu mara ya kwanza ndipo nilijua kuwa umerudi kazini. Nilitaka nije kwako mara moja. Lakini yeye aliniomba nisifanye pupa. Akaniomba nifuatane nae katika hoteli na kujificha kando nikimlinda. Nilifanya hivyo. Mara nikaona mtu mwenye dalili za kikafiri akiingia chumbani humo, bastola mkononi; ingawa ilifichwa sana. Kabla sijafahamu la kufanya nilikuona wewe pia ukinyatia na kuingia. Ndipo nilipojivuta mlangoni na kuchungulia katika tundu la ufunguo. Nikamwona Chonde akiwa tayari kukuua. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kumlenga na… na …”

Mara Nuru aliangua kilio. Akamgeukia Joram na kumkumbatia kwa nguvu akisema, “Nimeua mtu… Nimeua mtu, Joram…”

“Watu huuawa,” Joram alimnong’oneza. “Hebu jitahidi kuwa msichana shujaa kama ulivyo, Nuru. Usingemwua angeniua. Watu watakusikia. Twende zetu chumbani.”

“Lakini nimeua, Joram… nimeua…”


Ulikuwa usiku mfupi sana kwa Joram. Alikuwa na mengi ya kufanya ambayo hakuweza kuyatekeleza. Ilimchukua muda mrefu kumshawishi Nuru kwa vinywaji na mahaba ili asahau hofu yake ya kuua mtu. Baada ya usiku wa manane ndipo Nuru alipoacha kuweweseka na kupitiwa na usingizi mzito. Lakini alimkumbatia Joram kwa nguvu. Ilimlazimu Joram kutumia hila fulani na kujitoa mikononi mwake na kumfanya akumbatie mto.

Akinyata kwa utulivu, Joram alikiendea kisanduku cha marehemu Chonde na kutazama uwezekano wa kukifungua. Isingekuwa kazi rahisi. Ilihitaji utaalamu wa hali ya juu au risasi ya bastola. Joram hakuwa tayari kuitumia risasi kwa hofu ya kumwamsha Nuru. Na utaalamu siyo jambo ambalo lingepatikana kwa dakika moja. Hivyo, alikiweka kando kisanduku hicho na kuuchukua mfuko wa Chonde ambao haukumchukua muda kuufunua mifuko yake ya siri ambamo alitoa nyaraka mbalimbali na kuzisoma kwa makini. Yale maandishi wa kijasusi ni jambo jingine ambalo lilihitaji muda na utulivu mkubwa ili kueleweka. Hivyo, hakupoteza muda kujaribu kuyasoma. Badala yake alichukua hati ya kusafiria ya Chonde, kile kijisanduku na nyaraka zote alizoona muhimu. Vitu vingine alivifungafunga katika mfuko na kuvificha mahala ambapo aliamini kuwa visingepatikana kwa urahisi.

Baada ya hapo alichukua begi lake na kutoa vitu vyote vilivyokuwemo. Alichukua kinyago fulani cha hoteli na kukifunga katika mfuko wa nailoni na kuutumbukiza katika begi lake. Akalinyanyua kupima uzito wake. Kisha akaliweka mezani, na kuacha balbu ambayo ilikuwa ikitoa nuru nyekundu iendelee kuwaka. Akalitupa taulo lililokuwa kiunoni mwake na kujilaza kitandani kwa utulivu akiutoa mto aliokuwa ameukumbatia Nuru na kuichukua nafasi hiyo. Akainua mikono ya Nuru na kuifanya ituwe kiunoni mwake. Akayafumba macho yake na kujifanya kulala. Lakini asingeweza kulala alikuwa akiyasubiri mapambano kwa hamu.

Joram hakujua kuwa alikuwa amepitiwa na usingizi mzito. Alipoamka alikutana na macho mazuri ya Nuru yakimtazama kwa utulivu. “Za asubuhi, mpenzi,” Nuru alimsalimu Joram.

“Nadhani siyo mbaya.”

Nuru alitulia kidogo kabla ya kuongeza, “Nilikuwa nikisubiri uamke ili tuzungumze mpenzi. Nadhani haya yatakuwa maongezi yetu ya mwisho”.

“Kwa vipi?”

“Unajua jana nimeua mtu? Wakati wowote polisi watafika hapa na kunitia pingu. Endapo nitanusurika kitanzi siwezi kunusurika kifungo cha maisha.” Akasita tena na kuongeza, “Leo nimeota mpenzi. Nimeota nikining’inia juu ya kitanzi. Wewe na watu wengine mkiwa kando mkinicheka. Nilijaribu kukuita unisaidie lakini sauti haikuweza kutoka.”

Joram akacheka. “Nani aliyekwambia kuwa utafungwa? Polisi wangemfahamu mtu aliyemwua bila shaka ungepata medali ya dhahabu badala ya kukuvika pingu. Licha ya hayo, hawawezi kabisa kufahamu nani alimwua. Unajua, uliingia hotelini mle ukiwa mwanamume? Ni mimi tu niliyeweza kukufahamu,” Joram akacheka tena. “Lakini yote hayo ya nini? Leo tunaenda zetu Nairobi.”

“Kufanya nini?”

“Kutumia.”

Nuru akashikwa na mshangao. “Nilidhani umeingia kazini Joram.”

Joram alitabasamu kabla ya kumjibu akisema. “Kuna mpelelezi mwenzangu maarufu anayeitwa Willy Gamba, aliwahi kusema kazi na dawa. Mpelelezi ni binadamu vilevile. Lazima astarehe na kuburudika. Yawezekana tutaenda Nairobi tukiwa kazini. Sasa, sikia Nuru. Nitafunga mizigo yetu yote na kukutaka ukanisubiri Uwanja wa ndege. Hapana usiende Terminal II nenda kanisubiri Terminal I uwanja wa zamani. Nataka twende kwa ndege ya kukodi.”

“Ndege ya kukodi!” Nuru hakustahamili kuficha mshangao wake. “Kwa kweli, suala zima linanitatanisha. Kwanza, nadhani hatuna pesa za kutosha kutuweka hotelini kwa siku tatu zaidi.”

“Nani aliyesema kuwa hatuna pesa?”

Saa mbili baadaye Joram alikuwa mtaa wa Sokoine akielekea benki ya City Drive. Mkononi alikuwa na mfuko wake mkubwa ambao ulionekana mzito. Alipoingia benki alimfuata meneja aliyeongea nae jana ambaye alimpokea katika hali ya kujuana. Baada ya salamu za kawaida Joram alipewa fomu alizotakiwa kujaza. Akajaza kwa makini na kuzirejesha kwa meneja ambaye alizipitia. Kisha alitakiwa kuonyesha mali yake aliyohitaji kuhifadhi kwa utaratibu wa Self-Custody. Akafungua begi lake na kutoa kinyago.

“Ni hicho tu?” meneja aliuliza. “Nilidhani una kidani cha almasi,” akamjibu kwa sauti ya mzaha.

Moyoni meneja huyu aliamini kabisa kuwa ndani ya kinyago hicho mlikuwa na kipande cha almasi au Tanzanite. Kwani hakuona sababu nyingine ambayo ingemfanya Joram ajiingize katika gharama kubwa kwa ajili ya kinyago cha Mmakonde mmoja.

“Hiki kina thamani kama roho yangu,” Joram alimjibu meneja.

“Ni kumbukumbu ambayo iliachwa na babu mzaa babu ambayo inalinda ukoo wetu. Niliwahi kudhani kwamba ni utamaduni wa kipuuzi nikakidharau, lakini yalinipata makubwa. Nusura nipoteze roho. Tangu nimekithamini na kuwa nacho, mambo yameniendea kama ninavyotaka.”

Meneja huyo alielekea kumwamini. Wakainuka na kuelekea shimoni. Waliwapita wafanyakazi wanaotunza akaunti za watu, ambao hawakujishughulisha kuwatazama zaidi ya ule mtazamo wa kawaida. Wakateremka ngazi na kuingia vyumba vya chini. Ni hapo Joram alipomgusa meneja huyo bega na kumwambia, “Sikia bwana meneja. Sihitaji kuhifadhi kinyago hiki wala kitu kingine. Nahitaji pesa. Za kigeni.”

Sauti yake ikiwa ileile, makini, iliyotulia, ikamfanya meneja huyo kudhani kuwa huo ulikuwa utani mwingine wa Joram. Hivyo, aligeuka akitabasamu. Lakini tabasamu lake liliyeyuka ghafla na nafasi yake kumezwa na hofu iliyochanganyika na mshangao mara alipokutana na bastola kubwa ikimchungulia kifuani.

“My God,” aliropoka kwa hofu.

“Usiogope,” Joram alimnongoneza. “Endapo hutakuwa mbishi hutaumia. Kwanza pesa hizo sio zako. Nifunguliea nichukue kidogo na kuondoka zangu.”

“Sina ufunguo,” meneja alijibu. “Zaidi ya hayo, vitasa hivi hufunguliwa na watu wawili kwa pamoja. Sioni unavyoweza kuzichukua.” Akavuta pumzi kwa nguvu kabla ya kuongeza, “Licha ya hayo ndugu Joram, nashindwa kuamini kama kweli unadiriki kukifanya kitendo hicho. Unajua wewe ni mtu mwenye hadhi kubwa hapa nchini na duniani kote. Kwa nini uichafue hadhi hiyo? Kama unataka pesa hata ungeiomba serikali ungepewa. Hakuna asiyejua mchango wako katika kuilinda nchi hii.”

“Yaelekea huufahamu ubahili wa serikali hii wewe,” Joram alimcheka. “Sasa tusipoteze muda. Mimi ninazo funguo ambazo zinafungua kila kufuli. Sidhani kama kufuli zenu zitashindikana. Nitakupa funguo hizo ujaribu mmoja baada ya mwingine. Nitakuwa nyuma yako nikikutazama. Ukifanya ujinga utapoteza maisha yako.”

Juhudi hizo hazikufua dafu. Ndipo alipoamua kufumua kitasa kwa risasi. Bastola ilikuwa na kiwambo cha kupoteza sauti, na, kwa hivyo, ulitokea mlio wa kawaida tu.

Dakika iliyofuata walikuwa ndani ya chumba cha fedha za kigeni, Joram akiwa kamsimamia meneja ambaye aliamriwa kutoa kinyago na kupakia mabunda ya noti za Dollars, Pounds na nyinginezo. Mfuko uliposhiba, Joram alimwamru meneja huyo kuondoka. Aliuchukua mfuko na kumtaka atangulie.

“Tutatokea mlango wa uani na kwenda nje kupitia geti. Bastola itakuwa mfukoni lakini tayari kuvunja mgongo endapo utafanya ujanja au ujinga wowote. Tembea kama kawaida bila kugeuka nyuma.”

Walitoka na kuelekea uwani badala ya ofisini. Wafanyakazi wawili watatu waliwatazama kwa mshangao lakini tabasamu la Joram liliufanya mshangao wao utoweke. Tabasamu hilohilo liliwafanya askari wa geti wasishuku lolote kumwona meneja wao katangulia akitokea mlango ambao huutumika kwa nadra sana.

Barabarani Joram alimtaka meneja huyo kuendelea na safari akiifuata barabara ya Samora bila kugeuka nyuma. Meneja huyo alitembea kwa dakika kadhaa. Aliipita Benki ya Nyumba na kuifikia barabara ya Samora. Hapo alisimama kungoja amri nyingine. Hakusikia. Akatulia kwa muda akiogopa kugeuka nyuma. Alipoona macho ya wapita njia yakianza kumtazama kwa maswali ndipo alipojitahidi kugeuka nyuma. Akajikuta akiwa peke yake. Hakujua Joram yuko wapi. Kwanza aliduwaa kwa muda. Kisha alirudiwa na fahamu, akainuka na kuondoka mbio kurudi ofisini. “Tumeibiwa,” alimwambia mfanyakazi wa kwanza aliyekutana nae. Akaingia ofisini kwake na kuvuta king’ora cha ishara. Dakika chache baadaye polisi waliwasili na kuanza kuuliza maswali yao.

Wakati huo Joram alikwisha badili mavazi yake na kuvaa yale ya kizee pamoja na ndevu za bandia zilizojumuishwa na miwani kumfanya aonekane mtu mwingine kabisa. Kadhalika alikwisha badili teksi mbili ambazo zilimteremsha sehemu mbalimbali. Hii ya tatu alimwambia dereva, “Airport, tafadhali. Fanya mwendo wa kuruka.”

Dereva hakumwangusha.

Wakati polisi walipoanza kuweka vizuizi vya njiani, yeye alikuwa akimaliza kumlipa bwana fedha nauli ya ndege.

SURA YA TANO*

JIJI la Nairobi lilimraki Joram Kiango na Nuru kwa hewa yake yenye ubaridi ambao ulikuwa kinyume kabisa cha joto waliloliacha Dar es Salaam. Waliuacha Uwanja wa Kimataifa wa Kenyatta kwa teksi ambayo iliwafikisha Hilton Hotel.

“Mr. and Mrs. Charles Moris,” Joram alijitambulisha katika kitabu cha wageni.

Mhudumu wa mapokezi aliwatazama kwa muda akivutiwa na sura na maumbile yao. Kisha aliwapatia chumba kimoja Self-Contained, kama walivyotaka. Akawakabidhi kijana mmoja ambaye aliwaongoza hadi katika chumba chao ghorofa ya nane. Baada ya kuwafikisha aliwapa ratiba ya chakula, vinywaji na maelekezo mengine ambayo masikioni mwa wasikilizaji wake yalikuwa kama wimbo baada ya kuyasikia mara kwa mara. Walimkubalia yote na kumtupia maswali huku mara kwa mara wakimuonyesha meno kulijibu tabasamu lake ambalo halikuwa na mpaka. Kisha Joram alimfukuza kwa kumpa noti ya shilingi mia moja ambayo ilidakwa kwa heshima zote na kupotelea mfukoni.

“Wakati wowote, ukihitaji chochote usisite kuniita, mzee. Naitwa James,” alieleza akitoka.

“Bila shaka, James”.

Mara tu walipobaki peke yao, Nuru alimtupia Joram jicho lililojaa maswali. Alipoona Joram hatamki lolote aliamua kuzungumza. “Nadhani una mengi ya kunieleza Joram. Kila nilipojaribu kukuuliza kisa cha safari yetu tulipokuwa angani hukupenda kunijibu.”

“Sidhani kama kweli. Ulikuwa hupendi kuzungumza mbele ya yule rubani.”

“Kwa nini? Kwani kuna siri yoyote?”

“Bila shaka. Ulipokuwa uwanja wa ndege Dar es Salaam ulikuwa umejivika mavazi ya kizee tofauti na ulivyokuwa asubuhi. Ulipofika hapa jambo la kwanza ulilofanya ilikuwa kujibadili mavazi na kuwa kama ulivyo. Tulipofika hapa umelipa kwa fedha za kigeni bila shaka yoyote. Umezipata wapi? Na…”

“Alaa! Hivi sijakwambia? Kati ya pesa nyingi tulizopata katika mfuko wa marehemu Chonde nyingi zilikuwa za kigeni,” Joram alidakia. “Nadhani nilikuonyesha Nuru.”

“Ulinionyesha. Na kwa nini umeamua kupanga kwa jina la bandia?” Nuru aliendelea kusaili. “Na hapo watakapoomba kuiona hati ya usafiri utawaonyesha nini?”

“Hilo lisikusumbue. Uongo sikuanza jana. Lakini sababu kubwa iliyonishawishi kuandika jina la bandia ni hofu ya kusumbuliwa na waandishi wa habari. Unawajua walivyo, Nuru. Mara nyingi hawana kitu cha kuandika. Hivyo, wanapopata kijambo watakikuza ili kijae ukurasa. Umaarufu wangu nchini Tanzania ni jambo ambalo waandishi wa Nairobi wanaweza kuliondolea uvivu kwa haki kabisa.” Akasita na kucheka kidogo. Halafu akaendelea, “Hapana Nuru. “Tumekuja kustarehe. Tunahitaji kustarehe. Nairobi ni mwanzo tu wa starehe zetu. Toka hapa, tutakwenda zetu London, Paris, Hong Kong, New York na kokote ambako roho itatuita. Lazima tufurahi.Binadamu huishi mara moja tu. Hana budi kuitumia nafasi hiyo ili akifa awe amefaidi maisha.”

Joram aliongea kwa sauti imara, ingawa Nuru alihisi na kuamini kuwa hakuwa mkweli. Hata hivyo, kwa kadri alivyomfahamu alihisi kuwa Joram alikuwa na jambo, jambo ambalo lilikuwa halijakamilika kichwani mwake na hakuona haja la kuliongelea. La sivyo, ingewezekanaje Joram ashambuliwe na mtu, Nuru amuokoe kwa kumwua mtu huyo, waache maiti chumbani na kukodi ndege hadi huku, wapange kwenda zao bila sababu yoyote maalumu? Hiyo si itakuwa hadithi? Bila shaka kuna jambo.

Nuru alilingoja jambo hilo kwa hamu. Baada ya kuwa na Joram kwa muda mrefu, baada ya kukinaishwa na starehe, na baada ya risasi aliyoifyatua kuondoa roho ya mtu, roho ya Nuru ilikuwa juujuu ikitegemea jambo, jambo jipya. Jambo ambalo litampa haki na wadhifa halisi wa kuwa na Joram Kiango kama alivyokuwa hayati Neema Idd. Alikuwa ameamua kuichukua nafasi ya Neema, katika mwili na akili ya Joram si kuichukua kwa kunywa pombe na kucheza muziki. Ni kuichukua kikazi. Na ni kazi hiyo ambayo aliisubiri kwa hamu.

Nuru alipomtazama tena Joram alimwona kazama katika mawazo mengi. Akamwacha na kuingia bafuni ambako alioga kwa utulivu. Alipotoka bafuni hakumuona Joram. Badala yake alipata kipande cha karatasi Joram akimtaka radhi kuwa amelazimika kwenda maktaba mara moja.

Upweke ulimfanya aamue kwenda chumba cha maongezi ambako alijipatia bia mbili huku akiitazama televisheni. Aliangalia vipindi kadhaa vya burudani na taarifa za habari. Hakukuwa na mapya zaidi ya yale ambayo yameondokea kuwa ya kawaida masikioni na machoni mwa binadamu. Macho yalipokinai televisheni, aligeukia chupa ambayo ilikuwa mbele yake.

Mara akatanabahi ameketi na mtu ambaye alikuwa akizungumza. “Nasema, samahani naweza kuketi nawe?”

“Bila samahani?”

Mtu huyo aliketi na kuanza kumwaga vinywaji na maongezi. Maongezi yake yaligeuka kumtaka Nuru. Alisema mengi, akidai kwa viapo kuwa hakupata kumuona msichana aliyeumbika kama Nuru, kwamba alikuwa tayari kufa ili ampate. Mara mikono yake ikakosa utii. Ikaanza kutambaa juu ya mapaja ya Nuru. Ni hilo lililomwondoa hapo na kumrudisha chumbani kwao.


Joram alikuwa hajarudi. Saa kadhaa tayari zilikuwa zimepita. Alipotahamaki, usiku ulikuwa umeingia. Alikula peke yake chumbani humo akiogopa kwenda chumba cha maakuli ambako kulikuwa na wanaume ambao hawakuzoea kukubali kuwa mwanamke angeweza kuwa pale peke yake. Uchovu ulimfanya ajilaze kitandani. Hakujua usingizi ulivyomchukua. Alipoamka alijikuta yuko mikononi mwa Joram.

“Samahani mpenzi,” Joram alimnong’oneza.

Hakujishughulisha kumjibu kwa maneno. Badala yake alilijibu busu la Joram kwa vitendo. Kisha usingizi ulimchukua tena. Alipoamka aliupeleka mkono kumkumbatia Joram. Akajikuta akigusa godoro tupu. Joram hakuwa kitandani. Alipofumbua macho alimwona kainama mezani akisoma kwa makini. Akanyoosha mkono na kuichukua saa yake ndogo ya mkono kuitazama. Ilikuwa saa kumi na nusu za alfajiri. Hakuona sababu ya kumsumbua Joram. Akajifunika na kujaribu kulala. Usingizi haukuafikiana nae. Baada ya kuoga na kufungua kinywa asubuhi hiyo Joram alimwomba Nuru kuwa angerudi tena maktaba. “Leo nitamaliza shughuli zangu. Baada ya hapo tutakuwa pamoja katika kila la heri na shari,” alimweleza. Kisha akampatia kitita cha noti akimwambia.”Unajua tutakuwa na msafara mrefu? Nataka uende huko ukiwa katika hali halisi ya kuvutia kila macho ya mwanamume. Kwa hiyo, tafadhali leo pitapita madukani ununue kila vazi ambalo litakustahili. Usijali bei. Kumbuka pesa tunayo.”

Nuru alizipokea na kumuuliza, “Na wewe huhitaji nguo mpya?”

“Nahitaji. Hata hivyo, sina haraka. Wanaume huwa hawatazamwitazamwi kama wanawake.”

“Najua unahitaji muda wa kuwa peke yako,” Nuru alimwambia. “Endelea baba, siwezi kukuzuia.”

Mara tu Nuru alipoondokaJoram aliingia kazini. Alifungua begi lake na kutoa nyaraka za Chonde ambazo alitumia kila njia, kuzielewa. Akatoa kitabu ambacho alikipata kwa taabu sana kinachoeleza mbinu mbalimbali za kusoma maandishi ya mafumbo.

Akaketi na kuanza kutumia kitabu hicho kuyasoma tena maandishi ya Chonde. Haikuwa kazi ndogo. Ilihitaji muda mrefu na utulivu mkubwa. Alichofanikiwa ni kupata mwongozo ambao ulieleza namna ya kukifungua kile kisanduku. Akakifungua bila tabu yoyote.

Ndani mlikuwa na vijigololi kumi na viwili. Joram alikiinua kimoja na kukitazama kwa makini. Katikati ya kigololi aliona vidude vilivyokuwa vikichezacheza mfano wa saa za electronic. Alikitazama kigololi kwa makini akijaribu kutafuta umuhimu wake, hakuupata. Chini ya vigololi hivyo Joram alipata ramani ambayo alipoikunjua alikuta kuwa ni ya Jiji la Dar es Salaam. Ramani hiyo ilionyesha majengo maarufu kama Ikulu, vituo vya kijeshi, mabenki, na kadhalika. Vitu vyote hivyo vilikuwa vimewekewa namba za kirumi kuanzia moja na kuendelea. Namba ya jengo la benki kuu iliyoungua ilikuwa imewekewa alama ya x kwa wino mwekundu.

Mara baada ya kuona hayo Joram alipatwa na wasiwasi. Alihisi kuwa, kwa namna moja ama nyingine, Chonde alihusika na moto ulioteketeza Benki Kuu. Hofu yake kubwa ilikuwa zile hisia kuwa alama zilizofuata ambazo zilikuwa hazijawekwa x kwa wino mwekundu zilikuwa katika orodha zikisubiri, jambo ambalo lingeleta maafa na madhara makubwa kwa nchi na wananchi. Zaidi, ingekuwa ushindi mkubwa kwa maadui wa taifa. Hivyo, kwa mara nyingine, alifanya sherehe moyoni kushangilia kifo cha Chonde.

Kisha alifunga sanduku hilo kikamilifu na kuirudia meza ambayo aliinamia na kuanza kujifunza tena mbinu za kuyasoma maandishi hayo kwa makini zaidi.

Alikuwa hajatulia vizuri mlango ulipofunguka ghafla na Nuru kuingia huku macho yake yakiwa mekundu kwa mchanganyiko wa hasira na mshangao. Alisimama akitweta na kumtazama Joram kwa namna ya mtu ambaye hakujua la kusema.

“Usiniambie kuwa kuna mtu aliyekuvamia kwa nia ya kukunajisi mchana wote huu,” Joram alimwambia kwa dhamira ya kumfariji.

“Acha mzaha Joram. Sikutegemea kama ungekuwa mtu wa kufanya kitendo kama kile.”

Joram aliinua uso wake kumtazama.

“Kufanya nini?”

“Kuiba”.

“Kuiba?”

Nuru akamkazia jicho la hasira. “Usijifanye hufahamu. Dunia nzima sasa inafahamu. Kwa kweli, sikutegemea kabisa. Imenishangaza kukuona katika televisheni ukitangazwa kama mtu hatari ambaye ameweza kuiba fedha za kigeni ambazo nchi yake inazitegemea kama dawa.” Akasita akamtazama kwa chuki ambayo ilichanganyika na mshangao, “Kwanini ulifanya hivyo, Joram?”


“Bado siamini kama amefanya hivyo,” mtu mmoja alikuwa akifoka pia, akiwa kaketi katika kundi la watu wenye hasira na mshangao kama yeye. Mabega yao yalikuwa yakimeremeta kwa nyota ambazo zilipamba magwanda yao kudhihirisha madaraka yao.

“Amefanya, lakini siamini kama Joram ni mtu wa kutenda kitendo cha aibu kama hiki. Jambo la kusikitisha zaidi ni jinsi habari hiii ilivyovuja kiasi cha kuyafikia masikio ya adui zetu. Leo nimesikia habari hizo na Afrika Kusini,” Kombora aliendelea kulalamika.

“Ujerumani pia imetangaza afande,” mtu mmoja aliongeza.

“BBC vilevile,” mwingine aliongeza.

“Unaona, basi? Unaona habari mbaya zinavyosafiri upesiupesi? Pamoja na kwamba Joram ametuasi kimsimamo tulikuwa na haki ya kumsetiri kwasababu ya vitendo vyake vya nyuma. Sasa nadhani hatuna tunachoweza kufanya. Maji yamekwishakumwagika, hayazoleki. Lililopo ni kutafuta uwezekano wa kumpata na kurudisha pesa zote, hasa za kigeni.”

“Hilo ndio tatizo mzee,” msaidizi wake mmoja alijibu. “Taarifa za mwisho zinathibitisha kuwa hayupo kabisa hapa nchini. Kuna dalili kuwa ametorokea nchi jirani kwa ndege ya kukodi.”

“Lazima, lazima apatikane,” Kombora alisisitiza. “Pesa alizochukua ni nyingi sana na zinahitajika sana. Hana haki ya kuzifuja kwa starehe zake binafsi. Wasiliana na nchi jirani zote. Wasiliana na Interpol. Waarifu kuwa tunamhitaji Joram kwa hali na mali. Maadamu siri imekwishafichuka, hakuna haja ya siri tena.”

Baada ya majadiliano marefu jalada hilo lilifunikwa na kuletwa jingine ambalo lilikuwa “zito” Zaidi. Lilihusu mkasa au maafa yaliyotukia taifa pamoja na lile tishio la maisha na majumba muhimu. Walipima juhudi zao zote wakilinganisha habari mbalimbali. Haikuwepo dalili yoyote ya kujenga matumaini.

Kisha wakavirudia vifo vya watu wawili katika chumba kimoja cha hoteli hapa Jijini. Dalili zilionyesha kuwa marehemu walikuwa watu wasiofahamiana kabisa. Pekuapekua yao katika chumba hicho haikuwapatia kitu chochote zaidi ya mavazi ambayo yalionyesha kuwa yameshonwa nchi za nje. Nyaraka walizohitaji, ambazo zingeweza kuwasaidia, hawakuzipata. Ilielekea vifo hivi vingeingia katika yale majalada ambayo kesi zake hazikuwahi kutatuliwa. Hivyo, baada ya kuzitazama tena picha za marehemu wote, zilirudishwa katika majalada na kufungiwa.

Kikao kikaendelea.


“Kwanini umefanya hivyo, Joram?” Nuru aliendelea kufoka.

Joram, ambaye alionekana kimawazo yuko maili kadha wa kadha nje ya chumba hicho, alimtazama Nuru kwa muda. Kisha ikawa kama amemkumbuka. Tabasamu dogo likamtoka, likifuatwa na sauti nzito, “Ilikuwa lazima nifanye vile, iko siku utaelewa Nuru.”

“Nitaelewa!” Nuru alifoka, “Nitaelewa nini, mwanamume mwenye heshima zake na hadhi yake duniani anapothubutu kuingia benki na kuiba pesa ambazo nchi na watu wake wote wanazitegemea? Siwezi kuelewa kabisa, Joram. Ambacho naweza kuelewa ni wewe kuondoka sasa hivi na kwenda zako ofisi ya Ubalozi wetu ukaombe radhi na kurudisha kila senti. Tafadhali fanya hivyo, Joram.”

Hilo lilisababisha kicheko kwa Joram. “Nina haki ya kula pesa za Tanzania kama wengi wao wanavyozila, Nuru. Huoni watu wenye mishahara ya shilingi elfu mbili wanavyojenga majumba ya mamilioni? Unadhani wanazipata wapi bila ya wizi? Tofauti yangu na wao ni kwamba mimi nimeiba kimachomacho, wao wanaiba kisirisiri. Mwizi ni mwizi tu.” Akasita kidogo kabla ya kuendelea, “Acha tuzitumie Nuru. Acha tuzifaidi. Hii ni nafasi pekee katika maisha yetu ambayo hatujaisahau. Jisikie starehe…”

“Siamini kama maneno hayo yanatamkwa na Joram Kiango. Kwanini umebadilika kiasi hicho Joram?”

Kabla Nuru hajapata jibu mlango uligongwa na kufunguka taratibu. James aliingia. Uso wake ulionyesha kuwa alikuwa na habari ambayo si nzuri sana. Baada ya kubadilishana salamu za kawaida aliwataka radhi na kumchukua Joram chemba.

“Kaka, samahani. Unajua pamoja na kujiita kwako Charles Morris, ni watu wachache sana ambao waliamini? Sura yako si ngeni kabisa hapa Kenya. Umetokea mara nyingi katika magazeti na televishani. Wewe ni yule mpelelezi mashuhuri Joram Kiango. Sivyo, kaka?”

Joram alipochelewa kumjibu, James aliendelea, “Ziko habari mbaya zilizotokea katika vyombo vya habari. Inasemekana umetoroka kwenu ukiwa umechukua fedha nyingi za kigeni. Kwa jinsi ninavyokufahamu nashindwa kuamini kama ni kweli. Lakini hilo si muhimu sana kwa sasa. Nilichofuata ni kukufahamisha kwamba sasa hivi wapelelezi wa hoteli hii wamekaa kikao wakilijadili suala lako. Waweza kutiwa msukosuko mkubwa. Kwa hiyo, nakushauri utafute mbinu yoyote ambayo itakufanya uokoe maisha yako. Nina ndugu yangu anayeishi Nyeri. Anaweza kukuficha kwa muda.”

Joram alicheka na kumshukuru James. “Usijali rafiki yangu. Nitajua la kufanya. Kwa sasa niache nijipumzishe kidogo na kufikiria la kufanya.” Baada ya hayo aliutia mkono wake mfukoni na kuutoa ukiwa umeshikilia noti kumi za mia mia ambazo zilidakwa na James kabla hazijamfikia. “Kajipatie bia mbili,” alimwambia akigeuka na kurudi chumbani.

“Unaona Joram? Twende zetu ofisi ya Ubalozi,” Nuru alimdaka juujuu kwa maneno hayo.

“Kufanya nini?” Joram alizungumza kwa upole kama kawaida yake. “Tutakwenda zetu tunakotaka. Sasa hivi uwe binti mtulivu na ufanye kama nitakavyokuambia, tafadhali. Baada ya dakika chache tutakuwa zetu angani tukielekea katika mji mwingine wenye starehe kuliko huu.”

“Haiwezekani, Joram. Lazima ukaombe radhi na kurudisha pesa za watu,” Nuru aliendelea kukanusha.

“Alikuwa ameishi na Joram kwa muda mrefu. Lakini alikuwa hajapata kumuona Joram anavyokasirika. Leo hii aliziona hasira zake. Aliiona nuru kali na tena baridi, ikijitokeza katika sauti yake ndogo, nzito, aliposema taratibu, “Haya. Nenda zako ofisi za Ubalozi. Chukua na pesa zetu uwapelekee.”


Dakika mbili tatu baadae mzee mmoja wa kiume, mwenye mvi nyingi na ndevu za kutosha alionekana akitoka katika hoteli hiyo. Alikuwa kafatana na kijana wa kiume mwenye sura nzuri ambaye alikifunika kichwa chake kwa kofia pana na macho kwa miwani ya jua. Mikononi mwao walikuwa na mifuko yao. Wafanyakazi waliowatazama wakiondoka hawakuweza kukumbuka wageni hawa waliingia lini na iwapo walikuwa katika vyumba vipi. Waliwasindikiza kwa macho hadi walipotoka nje na kukodi teksi.

Kati ya wafanyakazi walioshuhudia wakiondoka ni James Kamau. Hata ndoto haikumjia kuwa alikuwa akiwatazama Joram Kiango na Nuru wakiondoka.

SURA YA SITA

SAA chache walikuwa angani tena, katika Ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza, wakielekea London kupitia Cairo, Misri.

Sasa habari za “Wizi wa Joram” zikiwa zimetapakaa duniani kote, zikienezwa na kila chombo cha habari, haikuwa kazi ndogo kwao kuipata fursa hii ya kuiacha nchi ya Kenya. Polisi mitaani na katika vituo vyote vya usafiri walikuwa macho wakimtazama kila mtu ambaye alielekea kufanana na Joram. Passport na vitambulisho vyao vilitazamwa kwa makini zaidi, huku maswali mengi yakiulizwa. Hata hivyo, Joram na Nuru walifaulu kupenya vizingiti vyote huku wakicheka kimoyomoyo, kwani askari hao hawakuwatazama kabisa kwa jinsi walivyojibadili kimavazi na kitabia, kinyume kabisa cha matarajio ya askari.

Nuru aliuficha uzuri wake kwa kuiondoa ile hali ya uvulana aliotoka nayo hotelini na kujivika nywele zilionekana nusu zingemezwa na mvi. Mavazi yake pia yalikuwa yale ambayo vijana wasingependa kuyatupia macho zaidi ya mara mbili. Jambo ambalo lilifanya wawe sawa na huyu mzee mkongwe aliyekuwa akitembea kidhaifu, mfuko mgongoni na mkwaju mkononi. Hali zao pia zilikuwa za wakazi halisi wa Nairobi. Hati zao za halali pamoja na picha zao zilifichwa vilivyo katika mifuko ya siri iliyokuwemo katika mfuko waliorithi toka kwa hayati Chonde.

Ndani ya ndege Joram alitulia akinywa bia aliyoletewa kwa utulivu, huku mara chache akimtupia Nuru maongezi mafupi mafupi. Baada ya muda ambao haukuwa mrefu alipitiwa na usingizi. Aliamka ndege ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Cairo. Misukosuko ya abiria wanaoshuka na kuingia ilipopungua walizungumza na Nuru maongezi machache ambayo dhamira yake kubwa ilikuwa kuwafanya watazamike kama watu wa kawaida wasio na dosari yoyote machoni mwa wasafiri wengine.

Safari ilipoanza tena Joram alikiweka kiti chake katika hali ya kulala akimwacha Nuru akipekua kitabu chake kutafuta alipokuwa ameishia. Ikiwa safari ndefu, ya kuvuka bahari kubwa kama hii ya Atlantic, Joram alikusudia kutumia vyema kufidia usingizi ambao hakuupata kiukamilifu alipokuwa Nairobi. Na ndivyo ilivyomtukia. Hakupata nafasi ya kuyafumbua macho yake kuyatazama maji mengi yaliyotapakaa kote. Alipoamshwa na Nuru na kutazama dirishani, alishangaa kuona wakizunguka juu ya Jiji la London wakisubiri kutua.

“Imekuwa safari fupi kuliko nilivyotegemea,” alisema.

“Hata! Ilikuwa safari ndefu sana kama ilivyo,” lilikuwa jibu la Nuru.

Taratibu, ndege ikashuka na kutua bila msukosuko wowote katika uwanja mashuhuri wa Heathrow. Pilikapilika za abiria kuchukua mizigo na kutaka kutoka mapema zikaanza. Joram na Nuru, wakiwa miongoni mwa abiria walioshuka mwisho, walichukua mizigo yao na kupita katika ofisi za forodha na abiria wengine waliokuwa wakisubiri usafiri.

Dereva mmoja, msichana, wa shirika la usafiri la Avis and Hertz, aliwafuata na kuwashawishi kuingia katika gari lake. Akawapeleka mjini katika Hoteli maarufu duniani ya Wilson Place ambapo walijipatia chumba maridadi. Mapokezi yakiwa ya kistaarabu, huduma za kistaarabu, na wahudumu waliosomea ustaarabu, yote yaliwafanya waone kama wako nyumbani badala ya ugenini, jambo ambalo liliwafanya wasijali chochote juu ya malipo makubwa yanayodaiwa na hoteli hiyo.

Kuna mzungu mmoja, mshairi, au mpenzi tu wa taifa lake ambaye aliwahi kusema: “When a man is tired of London, he is tired of life for there is all that life can afford,” kwamba binaadamu anayekinaishwa na Jiji la London basi amekinaishwa na maisha kwa ujumla kwani London inacho kila kitu ambacho maisha ya binaadamu yanahitaji. Joram na Nuru wasingemwona mtu huyo kuwa mwongo sana. Pamoja na kwamba wote hawakuwa wageni sana wa jiji hili, macho yao yaliendelea kuvutwa na vitu mbalimbali siku yao ya pili walipoamua kuzunguka jijini.Walikodi gari lililowatembeza kila mahali kufuata matakwa yao. Kwanza, walipenda kuona mto ule maarufu unaougawa mji wa London, Thames. Waliyatazama maji yake yanayopita kwa utulivu pamoja na madaraja yake murua. Kisha walizunguka katika miji ya Kingstone, Bromley, Croyon na kwingineko, wakiona mambo tofautitofauti katika mitaa mashuhuri kama Oxford, Kingsway, Dean na Sheftebury. Usiku ulipoingia walikwenda katika jumba la Her Majesty kutazama michezo ya kuigiza.

“Kesho tutakwenda kutembea Epping Forest,” Joram alimnong’oneza Nuru walipokuwa wakirudi hotelini kwao.

“Ningependa kuingia Richmond Park,” Nuru alimjibu.

“Nilipokuja kozi hapa miaka minne iliyopita nilidhamiria kuingia lakini sijui ilikuwaje nikashindwa, safari hii nisingependa kushindwa tena.”

“Huwezi kushindwa. Tuna muda na pesa. Tutafanya kila kitu ambacho roho itatutuma kufanya. Nafasi kama hii hutokea mara chache sana katika miaka ya maisha yote ya binaadamu.”

Chumbani kwao walivua uzee na kuurudia ujana wao. Wakatazamana na kucheka kidogo. Kisha walikumbatiana na kuongozana kitandani. Muda mfupi baadaye Nuru alikuwa akikoroma taratibu, huku Joram akinyata kukiacha kitanda. Aliiendea mizigo yao na kuikagua kwa makini. Kila kitu kilikuwemo kama kilivyokuwa kimehifadhiwa. Akatoa kile kisanduku chenye vigololi na kuvitazama kwa makini. Kisha alivirudisha na kuchukua vitabu vyake ambavyo alikuwa akivisoma au kufanya majaribio ya maandishi na mahesabu kwa umakini na utulivu. Mara kwa mara alichana karatasi hii na kujaribu ile, mara akiacha kuandika na kuanza kusoma kwa umakini, kisha akianza tena kuandika.

“Siwezi kukusaidia mpenzi?”

Sauti ilimzindua Joram kutoka katika lindi hilo la shughuli iliyokuwa mbele yake. Aligeuka na kumtazama Nuru ambaye alitulia nyuma yake, uchi kama alivyozaliwa, macho yake yakitazama mahesabu katika karatasi za Joram.

“Samahani kwa kukuvuruga. Nimekuwa nyuma yako kwa zaidi ya saa nzima sasa. Nadhani hata hujui kuwa kumepambazuka.”

Ndipo Joram alipotupa macho nje. Hakuamini. Nuru ya jua lililochomoza kitambo ilikuwa ikipenya dirishani kwa uangalifu. “Samahani Nuru. Usingizi ulinipaa ndipo nikaja mezani kupoteza muda,” alisema akianza kufunika karatasi zake.

“Kupoteza muda?” Nuru alimwuliza. “Nimekutazama kwa muda mrefu sana. Hata kuna nyakati ambazo ulikuwa ukisema peke yako. Najua una jambo ambalo linakusumbua, jambo ambalo umeamua kuliweka siri rohoni mwako. Hutaki kunishirikisha. Huniamini hata kidogo! Sijui nifanye nini ili uniamini Joram!”

“Ndiyo. Afanye nini ili amwamini?” Joram alijiuliza. Msichana huyo ambaye ameacha kila kitu hata kazi na nchi yake ili awe pamoja naye! Msichana ambaye kuwa nae kumemsaidia sana katika kujifariji na msiba wa Neema na aibu aliyoipata kwa kushindwa kumuua Proper! Msichana ambaye majuzi tu aliyaokoa maisha yake kwa kumwua mtu ambaye angemwangamiza bila huruma! Zaidi ni msichana mzuri wa sura na tabia, msichana ambaye ni ndoto ya kila mwanaume!

“Sikia Joram, huwezi kukadiria kiasi gani nakuamini na kukutegemea. Sifai kuambiwa lolote. Kwako mimi ni mwanamke tu ninayefaa kwa mapenzi ya kimwili. Siwezi kuwa Neema ambaye alikuwa mwenzi wako kikazi ambaye kimwili hukuwahi kumgusa.”

“Sivyo Nuru.”

“Wala sifahi lolote hata kukusaidia katika hesabu za fizikia unazopiga au kusoma maandishi hayo na kuyalinganisha na hayo ya kijasusi kama unavyofanya. Sifai hata kwenda maktaba kukusaidia kupekua walao kitabu unachokihitaji.”

“Nuru!” Joram alifoka kwa sauti ambayo masikioni mwa mtu asiyemfahamu ingekuwa ya kawaida tu. “Nilidhani wewe ni mtu pekee unayeweza kunielewa. Nilidhani unaifahamu tabia na msimamo wangu. Sina tabia ya kuyachukua matatizo yangu na kuyabwaga mikononi mwa binadamu mwingine. Sijazowea kuchukua fumbo ambalo limenishinda kufumbua na kumwomba mtu mwingine anisaidie. Wala tabia hiyo siwezi kuianza leo. Hivyo, ninapokuambia sina la kukuambia maana yake sina la kukuambia. Nadhani umenielewa.”

“Nadhani nimekuelewa. Hata zile pesa ulizozipokonya City Drive, ambazo tunachezea sasa naamini ni fumbo jingine ambalo hukupenda kulifumbua. Sivyo mpenzi?”

Joram akatabasam, “Yaelekea mimi na wewe tutakuwa na safari ndefu kimaisha.”

Wakashikana mikono na kurudi kitandani.


Baada ya kuzitawala na kuzinyonya sana nchi zetu nyingi za Kiafrika, na baada ya ‘kutoa’ uhuru shingo upande, Uingereza iliendelea kujifanya baba na mama wa makoloni yake ya awali. Falsafa hii ndiyo chanzo cha vijimsaada kadha wa kadha. Eti pia Uingereza ndiyo mtaalamu wa habari zinazohusu nchi zilizokuwa chini ya himaya yake. Na habari ambazo hupata nafasi katika vyombo vya habari mara nyingi huwa ni zile ambazo si nzuri sana kwa masikio ya wasikilizaji, yaani habari za aibu, kushindwa, rushwa udikteta, uzembe na kadhalika. Uteuzi huu wa habari hizo mbovu na kuacha zile njema ni ushahidi mwingine ambao huonyesha kuwa Uingereza ingependa kuendelea kuitawala Afrika hadi siku ya mwisho ya dunia.

Habari za wizi wa fedha za kigeni katika Tanzania zilikuwa tamu mno katika magazeti, redio na televisheni zote za Uingereza. Zilipambwa kwa wino na rangi mbalimbali na uongo ainaaina hata zikawa kubwa kuliko zilivyostahili kuwa. Hiyo ilitokana hasa na mwizi wa pesa hizo alivyokuwa mtu maarufu duniani. “Ndivyo walivyo waafrika…” liliandika gazeti moja.”Kati yao hakuna mwaminifu…” Gazeti jingine lilipendekeza kuwa Tanzania isipate msaada wowote wa kimataifa bila ya pesa hizo kurudishwa. “Tunaamini kilichofanyika ni njama tu baina ya Joram na viongozi wa serikali yake,” Televishen moja ilitangaza.

Habari hizo zilianza kuwa za kawaida machoni na masikioni mwa Joram na Nuru. Hawakuzijali wala kuzishughulikia. Hata hivyo, kuna gazeti hili ambalo liliwashtua zaidi. Mwandishi wake alikuwa amesafiri hadi Dar es Salaam ambako alifanya utafiti wake binafsi, akihonga hapa na kuiba habari pale hata akawa ameunganisha taarifa ambayo ilidai kuwa Joram alikuwa ametorokea Nairobi kwa ndege ya kukodi. Mwandishi huyo alisafiri hadi Nairobi ambako utafiti wake ulimfikisha katika chumba alichokuwa Joram na Nuru kwa majina bandia. “Kwa kila hali sasa hivi Joram yuko London,” lilieleza gazeti hilo. “Dunia haiwezi kupumbazwa na hila zake za kujibadili sura na umbile. Kwa hali ilivyo, atakuwa akiishi katika hoteli kubwa kwa jina la bandia.”

“Imekuwa tabia ya kawaida,” gazeti hilo liliendelea kueleza. “Kila wanapofanya madhambi yao huko kwao hukimbilia huku. London imejaa watu weusi ambao wanaishi wanavyotaka baada ya kufanya maovu – au mema ambayo yalionekana maovu – huko makwao. Wako wachoyo, wahujumu, wazembe, wanafiki na kadhalika. Wengi wameziacha nchi zao zikiwa masikini zaidi huku roho za watu zikiteketea katika vita na mauaji yasiyo na mwisho. Uingereza tunawakaribisha na kuishi nao kama binadamu wenzetu. Miongoni mwa watu hawa sasa yumo Joram Kiango, mtu aliyejifanya na akaaminika kuwa ana roho ya kipekee yenye upendo na ushujaa kama ngao kwa jamii yake. Kumbe alikuwa fisi katika ngozi ya kondoo. Huyu, Uingereza haiwezi kumstahamili. Lazima apatikane, ahukumiwe na kupokonywa kila senti aliyobaki nayo.”

Nuru alimaliza kuisoma habari hii huku akitetemeka kidogo. Lakini ilimshangaza alipoinua uso na kukutana na ule wa Joram ambao ulikuwa ukichekelea. Hilo lilimshangaza. Akiwa mtu ambaye ameishi na Joram kwa kipindi cha kutosha, alikuwa na hakika kuwa amemfahamu Joram vya kutosha. Asingelaghaika kama watu wengine kung’amua wakati gani anacheka kwa hasira na wakati upi anajifanya kuchukia hali amefurahi. Tabasamu hili, ambalo lilikuwa likiendelea kuchanua katika uso wa Joram, halikuwa tabasamu batili, bali tabasamu halisi, tabasamu ambalo huutembelea uso huu kwa nadra sana. Hivyo, ilimshangaza sana Nuru. Alimtegemea Joram kujisingizia kucheka huku rohoni akibabaika na kukata tamaa. Si kushangilia kama aliyepata tuzo au ushindi mkubwa baada ya shindano gumu.

“Sijakuelewa Joram, sidhani kama hii ni habari njema,” alimwambia.

“Wala sidhani kama una haki ya kutegemea habari njema tangu ulipokubali kuandamana na mwizi mkubwa kama huyu,” Joram alimjibu taratibu. Alipoona uso wa Nuru bado una maswali na dalili za kutoridhika, aliongeza, “Kinachonichekesha ni huyu Mwingereza anavyojifanya ana uchungu na nchi yetu kuliko sisi wenyewe. Utafiti aliofanya hautokani na moyo wake wa kuwajibika bali ni nguvu alizonazo kiuchumi, uwezo ambao ameuiba toka katika makoloni miaka nenda rudi.” Alikohoa kidogo kabla ya kuongeza, “Hawawezi kunitisha kabisa. Nitaishi hapa nikistarehe katika jiji hili kubwa ambalo linapendeza kwa madini yaliyoibwa toka makwetu, yaliyochimbwa kwa jasho la babu zetu. Nitaondoka hapa tu tutakapokuwa tayari kuondoka. Sivyo, dada Nuru?”

“Nilichosema ni jinsi unavyoifurahia habari hii badala ya kuionea aibu. Sikutegemea. Au nakosea. Pengine hili ni fumbo jingine?”

Joram hakumjibu.

***

Jioni hiyo maisha yaliendelea kama kawaida. Joram alijipitisha hapa na pale akifanya hili na lile. Sasa ilikuwa dhahiri kwa Nuru kuwa alikuwa katika shughuli kubwa na ngumu kinyume cha alivyoiruhusu sura na sauti yake kuonyesha. Nuru hakujisumbua kumuuliza lolote akichelea kupoteza muda wake kwani ingekuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa ukimtegemea kucheza rumba. Hata hivyo, Nuru alipopata wasaa alimkabili Joram na kumwambia taratibu,”Unadhani mwandishi yule anatania anaposema watafanya juu chini kututafuta? Huoni kama tunaweza kupatikana? Hila hizi za kujibadili si zimekuwa teknolojia ya kawaida siku hizi? Sidhani kama zinaweza kutusaidia.”

“Najua, mpenzi. Ninachojivunia ni wingi wa watu na ukubwa wa jiji hili. Itachukua muda hadi wafike hapa na kutukamata. Wakati huo hatutakuwa hapa tena, bali tutakuwa angani tukimalizia kuitembelea nchi ya mwisho ya dunia. Usijali Nuru. Starehe bila hofu yoyote…”

Joram hakuumalizia usemi wake kabla ya kuusikia mlango ukigongwa. Wakatazamana huku wakisikiliza. Mlango uligongwa tena kwa nguvu kuliko mwanzo. Joram hakuwa mgeni na ugongaji wa polisi. Kwa mara ya kwanza akajikuta kuwa alikuwa amekosea sana kuwadharau polisi wa Uingereza kiasi hicho. Akamtupia Nuru jicho ambalo lilibeba ujumbe ambao masikioni mwa Nuru ulieleza waziwazi “Cheza nao.” Papo hapo akatoka na kuingia bafuni huku akiufunga mlango nyuma yake.

Mlango ulipogongwa tena Nuru aliinuka na kuufungua. Kama alivyotegemea mlango ulipofunguka aliingia askari mmoja mwenye cheo cha Sajenti akifuatana na mmoja kati ya maofisa wa hoteli hiyo.

“Samahani sana dada,” afisa huyo alieleza. “Tumelazimika kukusumbua kidogo. Nadhani utatuwia radhi. Huyu hapa ni Sajini Brown kutoka Scotland Yard, yuko katika ziara ya kuwatembelea wageni wote wa hoteli hii ili kutazama hati zao za usafiri na maswali madogo madogo ambayo nadhani utamjibu. Ni mzunguko wa kawaida tu kwa ajili ya tukio dogo ambalo wangependa kulikamilisha ili wasirudi tena katika hoteli hii.”

“Bila samahani,”Nuru alijibu akimgeukia polisi huyo ambaye alikuwa akitoa kitambulisho chake.

“Kwa kawaida hapa kwetu hatusumbui wageni,” askari huyo alieleza. Tunatimiza ombi la INTERPOL tu,” alisita akimtazama Nuru kwa makini zaidi. Sijui dada unaitwa nani?”

“Mrs Prosy Godwin”.

“Kutoka?”

“Naijeria”.

“Yuko wapi bwana Godwin?”

“Ametoka, nadhani atarudi baada ya dakika chache.”

“Naweza kuona hati zenu za usafiri pamoja na nyaraka nyingine kama zipo?”

“Bila shaka,” Nuru alimjibu akiendea mfuko ambao aliufungua na kutoa hati. Akazikabidhi kwa askari huyo ambaye alianza kuzipekuapekua.

Dakika hiyohiyo mlango wa bafu ulifunguka. Askari alipogeuka kutazama alikutana na pigo ambalo lilitua katika shingo yake kikamilifu. Pigo lililokusudiwa kummaliza, lakini halikutimiza wajibu. Lilimfanya apepesuke na kuegemea ukuta. Mkono wake ukapaa kukinga pigo la pili huku mkono wake wa pili ukisafiri kuitafuta bastola. Joram hakuruhusu mkono huo utoke na bastola. Aliachia judo ambayo ilitua ubavuni mwa askari huyo na kumlegeza. Pigo lililofuata lilimlazimisha kuanguka sakafuni. Baada ya kazi hiyo ndipo Joram alipomgeukia afisa wa hoteli ambaye alikuwa kaduwaa, mdomo wazi, kama asiyeamini macho yake.

“Mwinue ndugu yako na umpeleke bafuni,” Joram alimwamuru.

“Vipi bwana Godwin? Nadhani hukumwelewa huyu bwana. Alikuwa hana nia mbaya zaidi ya… ya…”

Joram hakuwa na muda wa kuchezea. Alijua afisa huyu alihitaji nini kumtoa mshangao. Pigo moja tu, ambalo halikutegemewa lilimfanya afisa huyo aanguke chini kama gunia. Hima, Joram alianza kuwavutia bafuni mmoja baada ya mwingine. Kisha aliufunga mlango wa bafu kwa funguo na kumfuata Nuru ambaye pia alikuwa ameshangaa.

“Kwa nini umefanya hivyo Joram? Haikuwepo kabisa haja ya kuwashambulia. Askari huyo asingegundua lolote. Sasa watajua kuwa uko hapa na wataanza kututafuta kwa udi na uvumba.”

Si kitu. Kwa nini tujikombekombe kwao? London si mji mzuri pekee yake katika dunia hii. Bado tuna haja ya kuiona miji mingine.”


“…Ni mtu wa hatari duniani. Ameidhihirishia dunia kuwa hana tofauti na yule mwuaji mwingine anayetafutwa duniani kote, Carlos. Sasa kinachotakiwa kufanyika si kumtafuta yeye bali roho yake. Vinginevyo, dunia itakuwa imestarehe ikisubiri kuimarika kwa kiumbe mwingine wa hatari zaidi ya faru mwenye wazimu.”

Hayo yalikuwa mapendekezo ya mwisho katika gazeti lile lililohisi kuwepo kwa Joram Jijini London, na hatimaye kuandika juu ya tukio la kutisha lililowapata askari wa Scotland Yard na Afisa wa hoteli. Watu hao ambao walifunguliwa kutoka katika bafu saa kadha wa kadha baada ya Joram kuondoka zake, walieleza jinsi walivyowakabili watu ambao mtu yeyote asingefahamu kuwa wangeweza kuwa Joram Kiango na Nuru. Askari huyo alieleza hayo akiwa katika chumba cha X-ray, kuangalia uwezekano wa kuungika kwa mbavu zake tatu zilizovunjwa na Joram.

Baada ya kuongea nao kwa marefu na mapana ndipo waandishi wa gazeti hilo wakatoa habari hizo zikiwa zimepambwa kwa picha nyingi za kuchora, picha ambazo ziliwachora Joram na Nuru katika sura na mavazi tofauti; wakijaribu kuonyesha jinsi gani wanavyoweza kujibadili. Chini ya michoro hiyo kulikuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa herufi nzito yakisema; “Unashauriwa kujihadhari nao. Ukimwona ua kwanza, uliza maswali baadaye.”

ITAENDELEA

Tutarudi na Roho Zetu Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment