SIMULIZI The Lost Boys – Ep 2
NEW AUDIO

Ep 2: The Lost Boys

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 2

IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI

*********************************************************************************

Simulizi : The Lost Boys

Sehemu Ya Pili (2)

“Usiwe na shaka Kamanda. Huwa sikosei mimi”.Moi alijigamba.

“Basi fresh. Sasa sikilizieni matokeo yakitoka,ha ha haaaa. Wameingia choo cha kike wajinga wale”.Aliongea Ban na wote walitabasamu kwa kujipongeza kwa shughuli waliyoifanya.

VIPINDI vya chuoni viliisha mida ya saa saba mchana, na sasa wanachuo wengi walikuwa wametoka madarasani kwao na kuelekea vyumbani mwao. Wengi kati ya hao,walikuwamo pia wakina Junior ambao walikuwa madarasa tofauti lakini walisubiriana ndio warudi wote chumbani kwao.

Walikuwa wakitembea huku wakicheka kutokana na kushibana kwao kwa muda mfupi. Ucheshi wa Junior na ukichaa wa Hans ulichonganyika na uchangamfu wa Suarez,ulimbadilisha sana Fred. Naye taratibu akaanza kuzoea baadhi ya misemo ya kihuni na aliitumia kuna muda. Alianza kuendana na mazingira yaliyokuwa yanamzunguka.

Baada ya mwendo wa dakika ishirini,hatimaye walifika mlangoni mwa chumba chao na kuingiza ufunguo ambao hakuwa na hiyana. Ulipita,na ulipotekenywa kwenda kulia,nao ulitii na kuufungua mlango wa chumba kile.

“Mama yangu”.Ni Junior alitoa ukelele mkubwa ambao uliwafanya wenzake nao kuingia haraka.

“Haaaa!!!”. Hans alitoa mshangao huku macho yamemtoka pima kama kaona mtu anachinjwa hadharani au kaona mtu anatembea uchi.

“Haiwezekani jamani”.Maneno yalimtoka Suarez huku akiikana ile hali aliyoiona chumbani kwao.

“Mimi naenda kusema kwa Mwalimu”.Fred aliongea hayo huku akianza kutoka nje ya chumba kile kwa lengo la kwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa juu.

“Njoo hapa. Unaenda wapi sasa dogo. Tulia hapa tujadiliane,muafaka ukipatikana ndo waweza kufanya utakacho”.Hans alimvuta mkono Fred na kumrudisha ndani kabla hajatokomea.

“Hapa kuna kujadiliana kaka?Embu ona walichofanya”.Fred aliongea kwa hasira huku akijitoa mikononi mwa Hans.

“Nakwambia tujadiliane ili kwanza tujue nani kafanya hivi na tuna uhakika kuwa kafanya? Sio tunamuita Mwalim halafu tunaanza kumbwela hapa”.Hans aliongea,na ushauri huo wote waliona wa maana.

Wakaingia ndani zaidi ya chumba kile na kutafuta sehemu iliyosafi na kukaa.

“Hapa ni nani mnadhani anahusika?”.Hans alianza kuongoza mjadala ule huku kila mmoja akiwa kimya na uso kumshuka kwa hali waliyokuwa wamezungukwa nayo.

“Ni lazima watakuwa WAGUMU tu!.Si unakumbuka niliwaambia kuhusu wao kufanya kisasi?Yawezekana ndio wameanza hivi”.Aliongea Suarez kwa upole huku akiwa anajitahidi kuficha mahamaniko yake ambayo yangeweza kuzaa machozi.

“Ndio haohao. Hakuna wengine. Kwa kuwa wameanza ku****** zao lazima watalipa”.Aliongea Junior kwa hasira huku akiweka tusi ndani ya maneno yake.

“Hapa twendeni kwa mwalim ili tutoe taarifa. Lazima watakuwa wale tu!”.Aliongea Fred huku msimamo wa kutoa taarifa ukiwa mbele zaidi.

“Hapa hamna kutoa taarifa wala nini.Wakijua kuwa tumechukia,ndiyo itakuwa raha yao. Cha msingi na kusafisha geto na kutoa haya manguo na kuyafua vizuri,au tukanunue nyingine ili tuwakomoe tu!. Haya magodoro nayo twaweza kuyatupa. Kuanza na mwanzo si kitu,ila lazima walipe,haki ya MUNGU watalipa”.Aliongea Junior kwa jazba zaidi.

“Eheee,huo ndio mpango. Hakuna kufaidisha wengine.Hapa ni kimyakimya,tunatoa nguo zetu,halafu hamna kuongea na mtu. Tunafua zinazoweza kutakata,hizi nyingine zilizoharibika,tunazitupa tu!. Haya magodoro,ni ya kutupa. Hayana kazi”.Hans aliungana na Junior.

“Sasa hela tutapata wapi sasa hivi katikati ya mwezi. Boom lenyewe limeisha”.Fred aliongea kwa masikitiko huku akimuangalia Hans.

“Usijali mzee nani. Tutasaidiana katika hilo”.Aliongea Suarez kumpa Fred moyo.

“Ngoja kwanza”.Hans alitoa simu yake ya mkononi na kubofya namba fulani na kisha akaiweka sikioni.

“Haloo Baba shikamoo”.Hans alianza kwa salamu baada ya simu kupokelewa.

“Huku wazima,vipi huko”.Aliendelea kuongea na mzazi wake.

“Na shida na fedha kidogo,kuna vifaa yapasa niwe navyo”.

“Haya nitashukuru sana Baba. Mwambie na mama”.

“Haya Asante”.Alimaliza maongozi yake na kuwageukia wenzake.

“Muda si mrefu kiasi cha kutosha kitaingia M-Pesa”.Hans aliongea kwa tabasamu mwanana.

“Hivi mwanangu,baba yako ndo yule Daktari mkuu wa Muhimbili?”.Junior ilibidi aulize.

“Siyo huko tu!Baba ni daktari bingwa wa magonjwa yote sugu na ni mtaalam wa kufanya oparesheni zilizoshindikana”.Alijibu Hans kwa majigambo.

“Na mama yako yupo?”.Fred aliuliza.

“Mama ni mbunge wa viti maalum”.Alijibiwa.

“Mhh! Haya kaka. Ngoja tuone”.Aliongea Junior na kuacha maongezi. Hapo kilichofuata ni kusafisha chumba chao na kutoa nguo zao zote. Uzuri hawakuvunja vitu vya mle ndani,wao waliharibu nguo na sehemu ya kulala.

***********

Ni muda wa saa kumi na mbili jioni.Tayari walisharudi chuoni kutoka kufanya manunuzi ya vitu vyao muhimu. Kiasi cha laki saba alichotumiwa Hans,kilitosha kununua magodoro mawili mazuri,na baadhi ya nguo zake na za Fred.

Junior yeye alikuwa hana shida sana ya mambo ya kifedha japo Hans pia alimsaidia pale alipokwama. Kwa upande wa Suarez,alikuwa kama Hans tu!. Kazi yake aliyoiacha kwa muda,ilikuwa inamuingizia pesa kila mwisho wa mwezi,kwa hiyo akawa hana shida.

“Sasa tumerudi. Tupange jinsi ya kulipa kisasi”.Aliongea Hans na wote wakawa kimya kumsikiliza.

“Cha msingi tujifanye kama hatujapatwa na majanga. Ila kwao lazima ijulikane kuwa wamepatwa na majanga. Sawa jamani”.Hans alizidi kuendesha kikao kile.

“Hapo kwenyewe. Na ngoja sasa,watajuta kutufahamu”.Aliongea Junior.

“Hapo hata mimi nimo,lazima walipe”.Fred akakomelea neno.

“Kama kawa,si wanajidai maninja. Wataona”.Suarez naye alionesha uwepo wake katika kundi.

Wakaanza kupanga cha kufanya ili kulipa kisasi,na baada ya kama nusu saa,muafaka ukapatikana wa kulipa kisasi. Kila mtu akakubali kisasi icho.Baada ya hapo shughuli nyingine zikaendelea.

Zikapita siku kama tatu bila wakina Hans kufanya chochote.Lakini muda wote huo walikuwa wanafuatilia mienendo ya akina Ban na watu wake.

Waligundua mengi sana katika fatilia yao,lakini kubwa zaidi ilikuwa ni muda wao wa kutoka na kuingia vyumbani mwao.Hiyo walifanya kimyakimya sana hadi Ban na washirika wake wakagundua kuwa wanapangiwa kitu.

Alichofanya Ban na rafiki zake ni kuwa makini na chumba chao zaidi ya kitu chochote pale chuo. Hawakujua ni nini walichopangiwa na wakina Hans na ndIo maana walihaha.

Mara wiki ya kwanza ikakata bila usumbufu wowote. Wakina Ban walitabasamu na kuona wao ni washindi katika mapambano,lakini kumbe kitu kinachoitwa subira,ni bora kuliko kukukuruka.Na hicho ndicho kilifanyika kwa Junior,Hans,Fred na Suarez.Walikuwa wanasubiri wakati muafaka wa kufanya yao.

Hatimaye wiki ya pili ikaingia huku amani ikiwatawala vilivyo Ban,Sunday,Moi na Mose au Wagumu kama walivyozoeleka kuitwa pale chuoni.

Amani iliwatawala kwa kuwa kundi pinzani lilikuwa kama halina mpango na wao bali kuheshimiana kila walipokutana. Amani ikawa amani kwa wagumu wale.

Lakini kuna siku moja ambayo sidhani kama Ban na wenzake wanaweza kuisahau siku ile kwa kilichowakuta.

Ikiwa ni usiku mmoja wenye kila hali ya kuitwa usiku tulivu,Ban alipigiwa simu na msichana ambaye aliomba akutane naye usiku uluule ambao ulikuwa ni usiku wa kama saa nne kuelekea saa tano hivi. Jamaa kwa furaha na kihelehele cha kujifanya anajua sana huku ikichagizwa na misifa aliyokuwa nayo,akaona kama ana zali kwenda kukutana na Waziri Mkuu wa Chuo kile.

Waziri Mkuu wa Chuo kile alikuwa anafahamiana sana na Suarez kwa sababu walisoma wote shule ya Sekondari na pia walikuwa wanachukua masomo yanayofanana pale chuoni.

Dada huyo,Suarez ndiye alimpanga kwa sababu wale wakina Junior walikuwa hawana kabisa marafiki wa kike,hiyo ni itikadi waliyotoka nayo huko chini. Walikuwa hawajui kabisa kama kuna kitu kinaitwa wanawake,na zaidi walikuwa hawana hata mpango wa kuongea nao.

Huyu Suarez kila siku alikuwa anawashauri sana kuongea nao,japo na yeye alikuwa hana mpenzi kutokana na hapo mwanzo kuumizwa.

Hawa wakina Junior wenyewe walipanga mpango wa kuwakomoa wakina Ban huku wakihitaji wanawake wa kuwachanganya.Hivyo kwa ujuzi kabisa wa kukakaa wiki zile mbili,waliweza kupata wasichana watatu,huku wadada hao wakipatikana kwa msaada mkubwa wa Suarez.

Wale wadada wawili,walipangwa kuwazingua Moi na Sunday na huyu Waziri mkuu,yeye alipangwa kumzingua kubwa la maadui lenyewe,Ban Diho.

Uzuri sasa upo hapa. Japo wadada hawa walipangwa kwa wiki karibu moja na nusu,lakini waliwahi kukutana na Junior,Fred na Hans mara mbili tu!.Huku yule Waziri Mkuu akiwa hajawahi kabisa kukutana na hawa watu zaidi ya Suarez.

Wasichana wale waliunda urafiki na Wagumu kwa siku kama tano. Walikuwa wana uwezo wa kuwashawishi wagumu mpaka wakafanya wanachohitaji. Muda mwingi walikuwa wanawasema sana vibaya wakina Junior kitu kilichofanya wale wagumu kupenda sana kukaa na wale mabinti wawili.

HUYU dada mwingine ambaye alikuwa na jukumu kubwa kwa Ban,yeye alikuwa haonekani na wale wadada wengine bali yeye alikuwa kaanzisha urafiki wa karibu na Ban. Huyo ndiye yule Waziri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hakuna aliyejua nia ya wakina Junior zaidi ya yule Waziri Mkuu ambaye alipewa mkanda mzima uliotokea.Hadithi yote alipewa na Suarez.Hivyo kwa kuwa yeye alikuwa kiongozi,aliona ni heri jambo lile liishe kiuanachuo ila na yeye akiwa shahidi kama kiongozi,na ndio maana alikubali kisasi kilipwe,na kisha wote atawaita na kuwaonya kwa kuwekeana mabifu yasiyo na mpango.

Wale wadada wengine,wao walipewa hela kiasi na wala hawakuhitaji kuuliza kwa nini wamepewa majukumu yale.

**************

Baada ya Ban kupigiwa simu,alitoa tabasamu kubwa kwa kitendo cha dada yule Waziri Mkuu kumuita usiku ule.

Licha ya kuwa Waziri Mkuu,pia dada yule hata angeshiriki u-miss vyuo,angepata tu!. Alikuwa ni mzuri hasa,yaani kwa pale chuo,msichana yeyote alipenda kujifananisha na yule Waziri Mkuu asiye na majigambo wala mapozi kwa mwanachuo au hata mtu baki.

Saa nne za usiku,mrembo yule anampigia simu Ban ili wakaonane. Na yeye Ban bila kufikiria, aliwaaga kwa kuwadanganya rafiki zake kuwa anaenda kukutana na mzazi wake.

Chumba chao kikabaki na Sunday,Moi na Mose. Ambao wawili kati yao,nao pia walipigiwa simu na kila mmoja kwa wakati wake akaondoka kwenda kwa hao wasichana wanachuo ambao kwa muda mfupi walishakaa vichwani mwa Wagumu.

Chumba kikabakiwa na Mose peke yake. Huyu yeye hakupangiwa mwanamke ila kuachwa kwake, ilikuwa ni makusudi.

************

Baada ya Ban kwenda huko alipoitwa,akaanza kubabaishwa na Waziri yule Mkuu kwa lengo la kupoteza muda.

Kwa kuwa mwanaume ni dhaifu sana kwa mwanamke,yaani ni sawa na mfupa kwa fisi,basi Ban naye alilegea akawa bwege kabisa.

Hakujua hayo yote ilikuwa ni fitina za wakina Junior,ndio maana hata pale aliposhikwa mkono na kuvutiwa gizani zaidi,yeye alivutika kama bwege vile. Na hatimaye kazi ya yule dada ikawa inaelekea ukingoni.

Isikupite Hii: Geza Anasakwa Auwawe Ep 01

Sasa Ban alikuwa uso kwa uso na vijana watatu waliovalia kininja.Kwanza kabisa wale maninja walizuga kama ni vibaka na wanataka kuwapora.Mmoja wapo alimvuta dada mkuu pembeni na Ban alivoona hivyo,alianza kuomba msamaha ili dada yule asifanywe chochote.

Lakini kumbe ilikuwa ni ujanja tu!Mpango ulipangwa, ukapangika. Hatimaye kwa kuwa alijidai nunda basi dada wa watu aliachwa na mzigo wake akabebeshwa yeye.

************

Baada ya kama robo saa ya tukio lile kwa Ban,likatokea tukio kama lilelile kwa Sunday na Moi. Hali iliyofanyika kwa Ban,ndiyo iliyofanyika kwa Moi na Sunday. Nao walitekwa kama kawaida.

Baada ya kutekwa na maninja wale,walivuliwa nguo zote na kubaki kama walivyozaliwa. Wakati huo Ban alikuwa kaachwa mbali kidogo huku naye kavuliwa nguo na kufungwa kamba.

Sunday na Moi,walipovuliwa nguo,wakapelekwa hadi kwa Ban ambaye alikuwa anapigwa na baridi pale alipokuwepo.

Wakawarundika na kuwafunga kamba,kisha wao wakapotea eneo lile na kuelekea vilipo vyumba vya mateka wale.

Huko walikuta mlango umefungwa na kwa kuwa walishajua kuna mtu mmoja kabaki, basi ni lazima wangegonga na kufunguliwa kwa sababu yule wa ndani angejua kuwa wale ni wakina Ban.

Mawazo yalikuwa sawa kabisa. Wakiwa vilevile kininja,waligonga mlango kistaarabu na bila hata kuulizwa ni nani,mlango ukafunguliwa. Hapo wakaingia kama kawaida maninja watatu na kumsukumia Mose ndani kwa nguvu. Naye akayumba yumba hadi akadondokea kitandani.

“Ni nani nyie”.Mose aliuliza kwa sauti ya uoga yenye utetemeshi huku macho yake makubwa na mekundu yakimtoka kama jusi lililobanwa na lango la kanisa.

“Shiiiiiiiiiii. Ukipiga kelele tu! Tunaondoa shingo yako na maini yako tunaenda kulia wali kantini huku mdudu wako tunaupeleka Super Market ya Mlimani City ukauzwe kama sonseji”.Ninja mmoja alimtisha Mose. Huyo alikuwa ni Junior,lakini Mose hakutambua ni nani.

“Poa,lakini nimefanyaje?”Mose aliendelea kuuliza kwa uoga.

“Ngoja utaelewa sasa hivi”.Alijibu ninja mwingine huku akimsogezea uso kwa karibu zaidi. Huyo alikuwa Suarez,wakati huo ninja Hans yeye alishaanza kupekua makabati ya mle ndani.

Kwa msaada mkubwa walioufanya wale maninja watatu,waliweza kuvuruga nguo zao zote za mle kabatini na kuziweka sehemu moja.

“Zetu zilichafuka kichizi. Sasa zenu hazichafuki,zitafanyiwa sayansi hadi zikome”.Ninja mwingine aliyekuwa hajaongea hata mara moja,sasa alifungua mdomo wake, na baada ya hapo akatoa chupa moja kubwa ya maji.

Chupa ile ilikuwa imejaa kimiminika chenye rangi ya njano.Na alipofanikiwa kutoa chupa ile mfukoni,alitoa kichupa kingine kidogo chenye unga mwekundu.

Akachovya kidogo ule unga kwa kutumia kitu kama eye droper. Eye Droper ni kile kichupa kinachotumika kuweka dawa ya macho au ya sikio,ambacho ukitaka kuweka dawa ile,unakiminya,nacho kinatoa tone la dawa.

Baada kuuvuta ule unga kwenye eye droper,akatoa eye droper nyingine yenye maji meupe na kutonesha kwenye ile chupa kubwa ya maji. Hapo maji ya njano yakawa ya blue.

Akachukua ule unga,nao akauweka kwenye maji yale ya blue. Ghafla ulifuka moshi mkubwa sana kutoka kwenye chupa ile.

Ninja yule mwanasayansi,akatabasamu tabasamu la ushindi. Na hapo hapo alichukucha kwa nguvu hadi maji yale yakawa meusi kabisa.

Kitendo bila kuchelewa akaanza kumwagia nguo zilizokuwa mbele yake na zile walizokuwa wamevaa wakina Ban.

Baada ya hapo,alimsukuma pembeni Mose na kuanza kumwaga maji yale kidogo kidogo kwenye magodoro ya mule ndani. Aliporidhika,akamgeukia Mose na kuongea naye.

“Sisi tulikaa kimyaaa,sasa zamu yenu. Sikiliza kwa makini huko nje kitakachokuja kutokea kwa wenzako”.Huyo ni Hans alikuwa anamwambia Mose ambaye tayari alikuwa ameelewa ni wakina nani.

Alikaa kimya huku akiangalia chini kwa hasira zilizojaa uoga.

“Hiyo dawa niliyomwaga hapo,subiri kwa dakika kumi,utaona matokeo yake”.Hans alimaliza,akawakusanya washirika wake na kupotea mle ndani.

***************

Kule kwa wakina Ban,walikuwa wanajitahidi kufungua zile kamba hadi wakafanikiwa.

Kwa kuwa ilikuwa ni usiku sana,waliona ni afadhari hasa pale walipoona kulikuwa hamna watu waliokuwa wanakatiza katiza.

Walijifariji na kushika njia ya kurudi chumbani kwao huku wakiwa vilevile uchi,na pale mbele walikuwa wamepaficha kwa mikono tu!.Umbali wa kutoka pale walipo hadi chumbani kwao,ilikuwa ni kama dakika tano kwa miguu.

Walipofika walikuta kumetulia sana,kitu kilichowapa moyo kuwa hakuna watu muda ule.

Wakachungulia getini kuhakikisha kama ni kweli mawazo yao yalikuwa sawa. Baada ya kuona ni kweli,wakaingia getini wakiwa wanakimbia huku wameinama eti wasionekane.

Lakini wakati wanafanya hivyo,mara mbele yao wakatokea wanachuo wenzao kama mia hivi au mia mbili,tena wanawake wakiwa kwa asilimia kubwa sana.

“Sapraiziiiiii”.Zilisikika sauti za wanawake zikisema na kuwaacha wakina Ban wakiwa wameganda na kutopata cha kufanya kwa wakati ule.

Walibaki wamekodoa macho bila kujua wafanye nini pale walipokuwa wamesimama. Kukimbia hawawezi,kutembea hawawezi wala kunyata kwao ni shida.

Baadhi ya wanachuo walitoa hadi simu zao na kuanza kuwafyatua picha kuonesha kuwa wamefurahia sana ile hali.

****************

Pale wale wadada walipomaliza kazi yao ya kuwapelekea Moi na Sunday kwa wakina Junior,moja kwa moja walirudi vyumbani mwao na kuanza kuwapa taarifa wenzao wa karibu na kuwaomba wajikusanye ili wawakaribishe watu hao kwa kuwafanyia sapraizi.Na kweli walifanikiwa sana kuwakusanya wanawake wenzao.

Kwa upande wa wanaume,ilikuwa ni kazi ya Fred kuwakusanya na kuwapa taarifa za ugeni wa usiku ule,na kila aliyepata habari zile,alimtaarifu mwenzake. Hivyo kundi sasa la kuwasubiri wageni wale waliokuwa uchi,likawa kubwa na lote lilijificha nyuma ya majengo yale wanayokaa wanachuo wengine.

Pale walipowaona wakina Ban wanakuja,ndipo waliamua kuibuka huku mstari wa mbele kabisa wakiwamo wale wasichana wawili. Yule Waziri Mkuu hakuthubutu kuonesha uso wake eneo lile wala kuwapa taarifa wasichana wengine kwa sababu yeye ni kiongozi na hawezi kufanya utoto kama ule. Na isitoshe Suarez na washirika wake,walipanga mpango huo wa kuwakusanya watu bila kumwambia waziri yule,kwani wangempa taarifa hiyo,basi wangepingwa vikali.

Sasa wakina Ban uso kwa uso na umati wa watu uliokuwa unaongezeka kila dakika ili kushuhudia wagumu walivyokuwa wanaaibika. Hakuna aliyewajali kwani hawa jamaa walikuwa hawapendwi hata na wakufunzi wa chuo kile kutokana na tabia zao za kibabe,hivyo ile ikawa kama komesha kwao.

Wakati wapo katika mshangao huo,mbele yao wakatokea wakina Junior na kuanza kucheka huku wakioneshea vidole kwenye miili ile iliyokuwa tupu.

“Daaah!Mwanangu una manywele kifuani,kama chipanzee. Ha haaaaa”.Junior alitoa kejeri huku wengine wakifuata kwa cheko.

“Mwanangu na wewe uwe unanyoa bwana,khaaa!.Yaani japo umeziba kwa mkono lakini hayo manywele yametokeza hadi juu ya vidole. Nyoaga bwana”.Hapo Hans naye aliongeza udambwi wake huku akioneshea sehemu za hatari za mmoja wa wale wahanga.

“Daaah!Mwanangu huyu jamaa ana dude,hadi mkono unakataa kuziba. Ha ha haaaa,si utoe tu kaka tuone”.Junior alizidi kupaka na kusababisha vicheko vitawale eneo lile.

Wote walikuwepo mahali pale,namaanisha Junior,Fred,Suarez na Hassan. Na hapo hapo wakina Ban walishawaelewa wabaya wao. Kwa ujasiri mkubwa,waliwapangua watu na kupita katikati yao na kuwaacha wakishangilia.

Hadi wanafika vyumbani mwao,walikuwa hawaamini kama ni wao ndio wamefanyiwa yale tena na watu wadogo kama wakina Junior. Waliumia sana mioyoni mwao,lakini ndio hivyo ilikuwa imetokea.

“Na haya manguo nani kayarundika hapa?”.Ban aliuliza baada ya kuona nguo zao zimerundikwa sehemu moja.

“Walikuja hao jamaa,maninja na kufanya hivyo”.Mose alijibu kiunyonge na kusababisha Ban atake hata kumpiga ngumi,lakini alizuiliwa na wakina Sunday.

“Sasa mwanangu kafanyaje hadi umpige badala ya kuzichukua na kujistiri?”.Moi alimuijia juu Ban.

“Huyu boya,kwa nini aliwaacha wafanye hivi?”.Ban alisahau yeye alichofanyiwa na kumwona Mose ni boya.

“Kwani waliokuvua nguo wewe ni wakina nani?.Mbona hatusemi kuwa wewe ni boya. Hao hao waliokuvua ndio walimvamia na huyu. Na hii yote tunakulaumu wewe. Wewe ndiye chanzo cha sisi kuaibika pale nje sababu ya babe wako na kuanzisha mabifu na watu bila sababu. Kumbuka wewe ndiye uliwachokozaga wale,ukatuingiza na sisi na sasa leo tunaaibika. Nakwambia leo ukimgusa mtu humu,tunakuchana chana na viwembe,boya wewe”.Sunday alimwijia juu Ban hadi kila mtu aliogopa mle ndani.

Ilishazoeleka kuwa Ban ndiyo kiongozi wao na ni mbabe kuliko wale wote,hivyo walipomuona Sunday anamkoromea boss wake,wote wakaanza kuogopa kwa kitakachokuja kumtokea Sunday.

“Unasemaje wewe mbwa,rudia tena kauli yako.Sijakusikia vizuri”.Ban alimuijia juu Sunday huku anamfuata na alipomkaribia,alimdaka shingo kwa vidole vyake na kuanza kumsukumia ukutani. Hapo Sunday naye hakukubali,akamvaa Ban kwa kumkumbatia na kisha akamgeuza na kumbwagia kwenye kitanda kimoja wapo kilichokuwa karibu yake.

Kinyume na matarajio yao,wakidhani labda kitanda kitawapokea kikakamavu,haikuwa hivyo. Kitanda kile kilitoboka ghafla na kubaki chaga tu. Ni godoro zima lilikuwa kama limeoza kwani lilipukutika na kuwa kama vumbi.

Wote walikumbwa na mshangao kwa kile walichokuwa wanakiona,na kitendo bila kuchelewa.Mose aliwapa habari kuwa magodoro yao yalimwagiwa maji ambayo yanasemekana ni ya kisayansi.

Hapo kila mmoja akawa anashika godoro lake,lakini kitendo cha kuweka mkono tu!Godoro likapukutika na kubaki chaga peke yake.

Wote wakabaki midomo wazi huku kulia wakishindwa,kuongea ni kazi na kucheka ndo kabisa mtihani.

“Hata hizi nguo wamezifanya hivyo hivyo”.Mose alikomelea komeo la mwisho kwa alichokitambua.

Hapo Ban akawa kama kachanganyikiwa kabisa,na vile alikuwa uchi basi unaweza kumkimbiza Mirembe au Muhimbili wodi ya waliowehuka.

Alienda kwenye lile rundo la nguo zao na kisha akajaribu kugusa. Kweli kitu kikaitika. Nguo zote zika wa majivu.

“Daah!Hawa wasen**@@ leo wametuweza haswaa. Sina cha kusema wala kuongea hadi hapa. Sijui tutalala kwenye chaga na kujifunika ngumi au vipi. Kuaibika tumeaibika,kisa ujinga tu!”.Ban alijikuta utu uzima ukimuingia ghafla na kujilaumu kwa wichokifanya kwa wakina Junior.

“Sasa tutafanyaje hapa?”.Ilibidi Moi aulize na wakati wote wapo sawa kasoro Mose aliyekuwa kavaa bukta na singland ya kulalia.

“Sijui tutafanye aisee”.Ban ajibu huku kama machozi yanataka kumtoka.

“Hatuna hata cha kuvaa. Huku hostel vyumba vyote tumegombana nao,ni vipi tutaanza kuomba msaada wa japo mataulo ili tujifunge hadi kesho”.Ban alizidi kutia huruma.

“Naona sasa umekubali nachokisema.Huu ni ujinga wetu na uchokozi usio na maana ndio umesababisha haya yote.Ilikuwa haina haja ya kwenda kuwachafulia chumba chao wala nguo zao”.Sunday aliongea kwa jazba hadi akawa anatema tema vimate vilivyomrukia sawa kabisa Moi usoni.

“Oya mvua bwana. We badala ya kufikiria cha kufanya sasa hivi,unaanza kulaumu tu!Hayo yamepita,sasa tugange yanayokuja”.Moi aliongea huku akijifuta tule tumvua usoni.

“Muache aendelee tu!.Anajidai ndio anaona sasa hivi. Kwa nini angesipokataa siku ileile?Eti sasa hivi anajidai ndio anaona”.Ban aliongea huku bado akiwa na mawazo ya juu kilichotokea.

Wakati wapo katika mawazo hayo,ghafla mlango wao ukafunguliwa na Junior pamoja na Hans waliingia na kuwarushia baadhi ya nguo.

“Vaeni hizo. Sisi tumewafanya na kuwalinda,lakini nyie mlituacha mayatima”.Aliongea Hans na kuondoka mle ndani kwao,yeye na Junior.

Waliwapa nguo zilezile ambazo walizichafuaga wao wenyewe wakina Ban.

“Daah! Kweli nimeamini,kile unachokidharau, ndicho kitakachokuja kukustiri baadae.Tulidharau nguo hizi siku ile na kuzikinda kinda,lakini leo ndo zimekuwa za kujistiri miili yetu”.Aliongea Ban kwa hisia kali huku akimalizia kuvaa shati moja ambalo lilikuwa na baka moja kubwa mgongoni la tope waliloliweka siku za nyuma.

“Yaap.Inauma sana.Zile nguo tulipozifanya vile nadhani hata MUNGU kaona upumbavu wetu. Watu wanalia kuwa hawana nguo,lakini sisi tunaenda na kuzichakaza nguo hizo hizo bila huruma.Hii ni laana na MUNGU kalipa.Wala siwalaumu hawa jamaa,wana haki.Bila kufanya hivi,yawezekana MUNGU angelipa kivingine tu!”.Sunday naye aliongea kuungana na mwenzake.

“Ooups.MUNGU atusamehe tu!Huu ubabe usio na maana,leo umetutokea puani.Ni saa saba sasa,nani awezaye kutusikiliza na wakati hakuna hata mmoja anayetupenda hapa hostel?”.Ban alizidi kuonesha masikitiko yake.

“Daah!Sasa kama tunafikiria kulipa na kisasi,ni hapahapa tuambiane mimi nijitoe maana siwezi kufanyiwa hivi tena. Hizi ni Sayansi,ipo siku tutamwagiwa yale maji na sisi kuwa kama haya magodoro”.Mose naye alitoa mchango wake.

“Hapana. Sasa hivi ni muda wa kujirudi na kuelewana na kila mtu hapa chuo. Kaa ukiamini kuwa hawa jamaa wamejipanga sana,na wapo radhi kutumia fedha ili walipe tutachowafanyia. Sisi na vijisent vyetu vya ualimu,unadhani tunaweza kukodi wanawake na kuwavuta hawa jamaa?.Kwanza sijawahi kuwaona na wanawake.Tuache haya mabifu yasiyo na msingi wowote.Ni muda kufuta haya yaliyotokea usiku huu”.Ban aliongea kwa mara ya kwanza kauli ya kukubali kushindwa na iliungwa na mokono na washirika wake wote.

Na hapo tena mlango ulifunguliwa na kundi lote la Hans liliingia huku likipiga makofi.

“Tunashukuru sana kwa kuwa sasa mmejielewa,na imewauma pia kama ilivotuuma sisi.Ila samahani sana kwa tulichokifanya. Na nimesikia mkimtaja MUNGU kuwa kawalipa.Nasi imetuuma sana kwani tumezifanyia nguo zenu kitu mbaya na wakati kuna wengine tangu wamezaliwa hawajawahi kuvaa nguo mpya,lakini sisi tumezifanyia maafa nguo ambazo tungezipeleka kwenye kituo cha watoto yatima,wangeshukuru sana.Lakini si kitu,nadhani yote haya ni kumwachia MUNGU afanye yake. Ila namuomba sana msamaha kwa tulichokifanya”.Hans ndiye aliyeongea huku wakina Ban wakiwa vichwa chini wakisikiliza ujumbe ule.

“Sasa tumemjua MUNGU,nimependa sana haya maongezi. Tusali sana jamani,haya yote ni malipo ya dhambi zetu,iliniuma sana kwa mlichotufanyia,na ndio maana nilikuwa mstari wa mbele kulipa kisasi. Lakini sasa hivi najuta kwa kushindwa kukontroo hasira zangu na kulipa kisasi wakati MUNGU hapendi hiyo hali”.Aliongea Fred na kuungwa mkono na wengi mle ndani.

“SASA tumemjua MUNGU,nimependa sana haya maongezi. Tusali sana jamani,haya yote ni malipo ya dhambi zetu,iliniuma sana kwa mlichotufanyia,na ndio maana nilikuwa mstari wa mbele kulipa kisasi. Lakini sasa hivi najuta kwa kushindwa kukontroo hasira zangu na kulipa kisasi wakati MUNGU hapendi hiyo hali”.Aliongea Fred na kuungwa mkono na wengi mle ndani.

Kila mmoja aliongea yake na uzuri yale maneno ya waliyokuwa wanaongea wakina Ban yalikuwa yanasikilizwa kwa uzuri kabisa na wakina Hans.

Baada ya maongezi hayo,walikubaliana kumaliza tofauti zao,na bila kinyongo waliwachukua wakina Ban na kwenda kulala nao chumbani kwao.

HUO NDIO UKAWA MWISHO WA VURUGU ZILE,HUKU THE LOST BOYS WAKIWA WAKINA BAN KWA SASA.

*****

SEASONI II

Kesho yake asubuhi taarifa zikazagaa sana kwa kilichotokea na wale waliopiga picha wakaamua kuzisambaza pale chuoni kama njugu. Kila mtu akawa na picha zile kwenye simu yake.

Hakuna aliyejua ni nani anahusika na matendo yale zaidi ya wale wasichana wawili pamoja na wagumu na kundi la akina Hans.

Yule Waziri Mkuu alizipata zile picha na alisikitika sana lakini alikuwa hana cha kufanya zaidi ya kumuita Suarez na kumuuliza kwa nini waliamua kufanya vile. Suarez alieleza kila kitu na kuwa wamekubaliana na wagumu kumaliza lile bifu.

Dada yule Waziri aliposikia wamemalizana,alifurahi sana kwani alijua kwa picha zile,lile bifu ndo ligechachamaa.Lakini baada ya kusikia bifu limeisha,alifurahi sana.

“Nimefurahi sana kusikia maneno hayo Emma. Ila kuweni makini wasije kuwageuka tena”.Alionya dada aziri.

“Aaah hamna hiyo kitu”.Suarez Emmanuel alimtoa shaka dada yule.

“Okey,nashukuru kusikia hivyo.Sasa nataka kuona washirika wako na kuwahasa kuhusu hili jambo na pia kuwasalimia kwa sababu sijawahi onana nao.Jana niliwaona lakini sikuwaona vizuri sababu ilikuwa giza sana”.Aliongea dada yule mrembo,ombi ambalo lilipita na Suarez alimpeleka moja kwa moja kwa rafiki zake.

“Oya,yule dada aliyemzingua Ban anataka kuonana na nyie”.Suarez aliwaambia wakina Hans waliokuwa chumbani kwao wakifanya kila mtu kazi yake.

“Aaag,huyo tushamalizana naye.Hatuitaji mwanamke huku sisi”.Aliongea Hans na kuungwa mkono na Junior.

“Oya yupo hapo nje.Ngoja nimuite ili mumwambie wenyewe”.Suarez aliwaambia hivyo na kutoka na aliporudi,alikuwa na yule dada.

Wakina Hans walipomuona yule dada,wote walishikwa na butwaa,si Junior,Hans mwenyewe na Baba Paroko Fred.

“Habari zenu jamani”.Dada yule aliwasalimia lakini hakuna aliyejibu,wote walikuwa wamegandisha macho yao wakiwa hawaamini wanachokiona.

“Oya mnasalimiwa”.Ilibidi Suarez awatoe kwenye ule mkanganyiko.

“Eeeeh,unasemaje Sure”.Hans aliuliza kama anatoka usingizini.

“Dada anawasalimia huyu”.Suarez alijibu huku anataka kucheka.

“Aaah.Poa dada mambo”.Wote walijikuta wanashuka vitandani mwao na kumpa mkono dada yule kwa pamoja.

“Safi”.Dada yule alijibu huku anawashika mikono yao mmoja mmoja.

Bado kila mmoja alikuwa haamini anachokiona kwa wakati ule.Hata pale walipoachiwa mokono yao,walibaki wamegandisha bila kuishusha.

“Okey.Naona kama mna kitu.Mimi naitwa Eve Johaness,sijui wenzangu mnaitwa wakina nani”.Ilibidi yule dada ajitambulishe jina lake,lakini bado wakina Hans walikuwa wameganda tu!

“Oya mazee dada yetu anawasalimu,hamsikii au ndio mwajidai wagumu hapa”.Ilibididi Suarez afanye kazi ya ziada kuwaamsha wale majamaa walioganda kama mazombi.

Alikuwa anawaamsha huku anawapiga visogoni.

“Hamna mzee nani.Dah! Akili sijui ilienda wapi.Unasemaje dada!!??”.Hans alikuwa kama jinga fulani lilitoka kujanjarushwa na wajanja,kwa jinsi alivyoshtuka na kuuliza lile swali.

“Ee kweli.Dada umesemaje”.Naye Junior alikurupuka toka kwenye ule mshangao,wakati huo Fred alikuwa naye anajiweka sawa ili kusikia Eve atasema nini.

“Nimesema naitwa Eve Johaness.Wenzangu sijui mnaitwa wakina nani”.Eve alijitambulisha tena kwa vijana wale na kubaki akiwaangalia usoni akisubiri jibu la maombi yake.

“Okey Eve.Nataka kukuita Eve The Beautiful One,upo tayari?”.Junior alianza hivyo huku akinyoosha tena mkono wake kumpa Eve kama salaam.

“Whetever you like”.Eve naye alijibu kizungu zaidi.

“My name is Junior.Au ukipenda niite Nickson King Junior.Mi nipo Arts hapa chuoni.Masomo yangu ni muziki zaidi na lugha”.Alimaliza Junior na kumpa heshima Eve ya kuinamisha kidogo kichwa chini kama wale watumishi wa malkia wakimuona malkia anapita.

“Okey.Napenda kukuita Junior.Mimi nipo nasomea uandishi wa habari na huyu rafiki yenu”.Eve aliendelea kujitambulisha na wakati huo Hans alishasogea mbele kwa ajili ya kutoa utambulisho wake.

“Mimi napenda kukuita Sweet Eve.Your so sweet Eve.Just like an candy or honey.Nimekuwa kama mtambo baada ya kukuona”.Hans ni kama alishaanza kutupa kete zake kitu ambacho sidhani kama wenzake walikifurahia hasa Junior na Fred.

“Babu si ujitambulishe tu! Maneno mengi kama umejiunga na baba lao”.Junior alishindwa kuvumilia kwa jinsi Hans alivyokuwa anaendelea kuongea.

Uzuri wa Hans japo alikuwa hana mpango na mapenzi,lakini alikuwa anazijua kete za kuwazidi wenzake.Hadi pale walipofikia,Junior alishapoteza kete kwa kuropoka bila mpango.Na Hans alishalijua hilo,hivyo akazidisha mbwembwe za kujiongezea pointi.

“Wajua nini Eve.Napenda kujitambulisha kwako kama kijana mtulivu kabisa ila ukinichokoza ndio nakuwa kama kichaa.Sishangai huyu jamaa anavyonipigia kelele mbele ya Sweet Baby kama wewe.

But anyway.Naitwa Hassan Jenge,au Hans J.Nipo hapa UDSM katika masomo ya Sayansi.Ukisikia Hans The Scientist,ndio mimi.Karibu sana katika Ikulu yetu Sweet Eve”.Hans alijitambulisha huku akimpisha na kumwoneshea kitanda chake akakae pale”.Eve alitabasamu jambo lililofanya Hans ajione mshindi.

“Sikai sana Hans.Nitakuja siku nyingine.Usijali”.Eve alijibu huku bado kachanua tabasamu lilelile la mwanzo.

“I respect that Sweet Eve.Ila sijajua kama umelipenda jina la Sweet Eve”.Hans aliongea tena wakati huo naye Fred alishasogea mbele kwa ajili ya kujitambulisha.

“Jina lolote kwangu sawa tu!Wala usijali.Hata ukiniita tusi,hamna tatizo”.Eve alijibu huku bado katoa tabasamu lake ambalo linaweza kuhamisha ghorofa kutoka Posta na kulipeleka Banana au Kivule.

“Okey Sweet Eve”.Hans alikubali na kurudi nyuma kumwachia Fred ajitambulishe.

Kinyume na walivyotarajia labda Fred atabugiza au ataanza kuleta za Kiparoko,Fred akawa nyoka mwenye sumu kali hatari.Sumu iliyowaua wao wote.

“Habari yako mrembo.Napenda sana kutumia Kiswahili kuliko Kiingereza na ndo maana nakupa jina la Malaika badala ya Angel.

Wewe ni Malaika Eve,kwani nilipokuona nilijua kuwa umenileta taarifa nzuri kwangu kama yule Malaika alivyomtokea Bikira la Maria na kumwambia atazaa mtoto, naye atamuita Yesu.

Nawe umenitokea kama vile,na kuuacha moyo wangu ujawe na furaha kwa taarifa nzuri ya uzuri wako uliyoniletea mimi hapa leo. Wewe ni Malaika,niamini nachokwambia Eve.Wewe ni Malaika”.Fred alikuwa anaongea hayo na baada ya kumaliza alishika mkono wa Eve na kuubusu kwa huku nyuma.

“Mmmh!.Mi sina usemi hapa Suarez”.Eve alishindwa kuvumilia na kujikuta akitabasamu na kumwangalia Suarez ambaye muda wote alijiona mshindi sana kwa kuwafanya hawa watu ambao kwao wasichana walikuwa sumu.Alifurahi kuwaona wakianza kuamini kuwa msichana ni sumu isiyoua bali sumu inayonenepesha na kutoa furaha.

Ujue bado siamini”.Suarez naye aliongea baada ya kushuhudia busu la kwanza kutoka kwa Fred.

“Achana na hawa Malaika wangu. Mimi naitwa Alfred Musita,au Fred…………”.Wakati anaendelea kujiambulisha yanayoendelea,Junior alidakia bila kujua anazidi kupoteza pointi.

“Fred au Baba Paroko,au ukishindwa kabisa muite Mzee wa Upako”.Watu walikaa kimya wakimshangaa Junior kwa yale maneno.Eve naye hata tabasamu lilimuisha na kubaki katika alama za mshangao.

Fred alikuwa ni mtalaam,nahisi alimzidi sana Hans.Kwani kitendo kile cha Junior kuropoka,kilikuwa kama kumtupia kobe kwenye maji ili umuue au kumwagia petrol moto ili uzime.

“Yap.Malaika wangu.Nampenda sana Junior kwa kuwa anamalizia maneno niliyoyaanza,hivyo usishangae wala kupoteza tabasamu lako mwanana mithili ya Miss anayegombania U-miss mbinguni”.Fred alimsafisha Junior wakati huo akichukua pointi nyingine kwa kurudisha tabasamu la Eve kwa maneno yake matamu.

“Kama alivyosema mkubwa wangu Junior.Humu wamezoea kuniita Mzee wa Upako kwa sababu ya kupenda kusoma Biblia.Lakini mimi nipo Biashara,nasomea Uhasibu katika chuo hichi”.Fred aliendelea kujitambulisha kwa kujiamini mbele ya mrembo yule wa chuo.

“Nimefurahi kukujua Fred.Napenda kukuita Fred.Na nimependa sana uchangamfu wako”.Aliongea Eve kumwelekezea maneno hayo Fred.

“Karibu sana Malaika wangu.Naomba kitu kimoja kama hutojali”.Fred alizidi kuonesha mbwembwe zake za kitakatifu lakini zenye bashasha za kutosha.

“SEMA tu! Fred”.Eve alimpa ruhusa Fred.

“Naweza kubusu shavu lako?”.Fred alifunguka huku kamkazia macho yaliyo makavu na yasiyo na utani Eve.

“A a a a.Hiyo hamna aisee.Mimi huyu kama mgeni wangu nakataa hiyo kitu”.Suarez aliingilia kati jambo lile huku akiwa hana mbavu kwa kinachotokea mbele ake.

Hans na Junior walitoka macho huku wakiwa hawaamini kinachotaka kujiri mbele ya mtu ambaye wao walimchukulia kama bonge la mtakatifu.

“Mhh!Sure umeombwa wewe au mimi?Embu mwache bwana apate anachohitaji”.Eve alimpiga stop Suarez ambaye alikuwa anamsukuma Fred kwa pembeni huku akiendelea kucheka.

“Dah! Haya bwana,kwa kuwa umetoa ruhusa.Sina jinsi”.Suarez ilibidi akubaliane na maneno ya Eve na kumwachia Fred ambaye alimfata Eve pale alipokuwa kasimama na kumshika kiuno,wakati huo Eve aligeuza shavu la kulia na Fred alidondosha midomo yake juu ya shavu lile linalong’aa mithili ya almasi.

“Nimefurahi kupata kiss lako Fred.Your so sweet”.Eve alimwambia Fred baada ya busu lile.

“Hapana Malaika wangu.Sweet ni jina lako kwa Hans.Na mimi nimefuahi sana kupata shavu lako.Umeumbwa ukaumbika, Eve”.Fred alimaliza na kurudi nyuma kwa ajili ya kusikiliza kitu kinachofuata.

“Haya jamani.Naona wa mwisho siku zote ndio kapata kinachostahili.Siku zote jiwekeni nyuma bwana,si mmeona mwenzenu”.Suarez alianzisha mazungumzo baada ya kimya kidogo,wengi wao wakifikiria kilichojiri muda mfupi uliopita hasa kitendo cha Fred kuvua ngozi ya utakatifu na kujivika ngozi ya ukidunia.

Eve alikuwa mtu watabasamu muda wote kana kwamba hana tatizo kwa chochote kilichotokea muda ule.

Siku zote ili utengeneze urafiki na watu wengi ni lazima uwape wanachohitaji lakini usivuke mipaka.Busu kavu ni kitu cha kawaida sana hasa ukiwa umeelimika na kutoa ule udigitali kwa kuweka uanalojia.Namaanisha yapasa kuingia dunia wanayoishi wenzetu walioendelea lakini usisahau mila na desturi za unapotokea.

“Mimi sina neno.Nadhani wote tumeona.Sasa tumpe muda dada yetu aseme kilichomleta”.Suarez aliongea huku akimpisha Eve aweke maneno machache yaliyomleta pale.

Alichosisitiza Eve ni kumaliza bifu lililokuwa kati yao na wakina Ban ambao kwa muda huo walirudi majumbani kwao kwa sababu ya aibu iliyowakumba na kwenda kujipanga tena hasa kimavazi.

Baada ya maneno hayo,wote walikubaliana na ushauri huo na wote kwa pamoja walitoka na kumsindikiza kimwana yule ambaye kwa mara ya kwanza aliwafanya wahisi dunia ilikuwa imewapita sana katika wanawake.

**************

Baada ya kumsindikiza msichana yule,wao walirudi na kuendelea na kazi zao chumbani kwao lakini maongezi makubwa yalikuwa ujio wa Eve katika maisha yao.Kila mmoja aliapa kivyake baada ya kugunduana kuwa wote wanamtaka msichana yule.

“Mimi nitamwimbia na kumpigia gitaa hadi anilalie kifuani.Huku akitamani nisiache kufanya hivyo”.Junior alijigamba mbele ya wenzake.

“Tatizo lako Junior wewe ni ropo-ropo sana.Unatakiwa kucheza na pointi kaka.Kulikuwa hakuna haja ya kuropoka saa zile,mara Mzee wa Upako,sijui unamkataza Hans asiendelee. Hizo achana nazo kijana.Fanya yako halafu uone”.Suarez alitoa ushauri wake juu ya alichokiona kwa Junior.

“Huyo tushamtoa kwenye ligi.Mimi nitampa sayansi za mapenzi hadi kila akikaa anataka kupewa sayansi hizo”.Hans naye alichombeza mikakati yake.

“Wewe Hans tatizo lako ni kujisifia kaka.Hans J mara Hans the Scientist,ooh sijui mimi ni kijana mtulivu.Hivi unadhani hakujui tabia yako?.Ulitakiwa kujitambulisha matendo yako kama yalivyo na si kuzuga zuga”.Suarez aliendelea kutoa mapungufu ya kila mmoja.

“Mimi nitampa vipande vya Biblia na kuvigeuza kuwa mistari ya mapenzi juu ya mtoto yule aliyeacha poda kwenye lips zangu.Duuuh! Wananionea tamaa”.Fred hakuwa nyuma kujisifia mbele ya wenzake.

“Wewe ulianza vizuri sana.Lakini ulipoharibu ni pale ulipotaka kiss.Kwanza manzi fikra zake zitajengeka kuwa ulitaka kuwaonesha wenzako kuwa wewe ni bora, na zaidi atakuona kama limbukeni kwa ulichokifanya.Hivyo usidhani kama umewashinda wenzako.Bado mna kazi sana ya kurekebisha hayo mambo.

Na uzuri manzi mwenyewe tangu nianze juana naye,sijawahi kumsikia ana skendo au hata boy.Kwa hiyo wazee,kazi ni kwenu”.Suarez alimaliza na kwa kuwa alikuwa anauzoefu kiasi chake,wote walitulia na kuyachanganua yale maneno yenye ushauri.

EVE JOHANESS.

Kama alivyojitambulisha kwa akina Junior.Yeye alikuwa anasomea uandishi wa habari katika chuo kile kikuu cha Dar es Salaam.Alikuwa sanjari na Suarez katika kusoma huko.

Inavyosemekana alimaliza Mbeya Day kidato cha nne na kidato cha sita alisoma na Emmanuel Suarez shule ambayo haijafahamika hadi leo.

Matokeo yake yalikuja mazuri sana na kumfanya aje pale UDSM kwa ajili ya kusomea uandishi wa habari.

Katika mapenzi alikuwa haijulikani kama alikuwa anaye au hana.Ila watu wake wa karibu wanasema kwa pale chuoni hana,na kuongeza kuwa hawajui kuhusu huko nje kwa sababu hakuwahi kuongelea masuala hayo na wenzake.

Alikuwa ni mzuri wa sura, na umbo lake jembamba kiasi lililobebwa na kiuno kilichozama ndani na kuibuka na kitambi kidogo kwa nyuma.Kitambi ambacho wahuni wanaweza kukiita ushuzi ila sisi wastaarabu tunayaita makalio.

Alikuwa ana makalio ambayo yalikuwa hayafanyi watu kusema ni ya kichina bali kusema kabarikiwa kuwa na makalio yanayowatoa wanaume wakware mimate ya uchu.

Upande wa sura,ni kweli alifaa kuitwa majina yote kasoro tusi tu!Na majina mengine mabaya-mabaya.Ila yale majina ya Malaika,Sweet na Beautiful yalifaa kabisa kuitwa binti yule mwenye kila sifa ya kuyapokea majina kwa mikono miwili.

Alikuwa si mweupe sana wala mweusi kiviile.Bali alikuwa ana-rangi ya asili ambayo kwa sisi wataalamu wa watoto hawa wa kike tungeita rangi ile ni ya chotara.

Na ndivyo ilivyo.Eve Johaness alikuwa ana asili ya baba Mtanzania tena wa Mbeya na mama alikuwa ni raia wa Uswis. Sasa Eve alichukua rangi mbili za wazazi wake,yaani ya kizungu na ile ya Kinyakyusa.

Uso wake ule ulibeba macho fulani madogo lakini si kama ya watu wa Asia,yaani Wachina au Wajapani.Yeye alikuwa ana-macho madogo lakini yenye mwangaza kutokana na kuwa ya uviringo na huku shavuni kukichagizwa na mashavu mazuri ambayo kwa mwanaume anayejua maana ya uzuri anaweza kusema yale mashavu yametengenezwa kwa unga wa ngano na si udongo.

Hiyo ni kutokana na ulaini wa mashavu yale na utamu ule wa mashavu uliongezewa bashasha za kutosha na dimpoz ambazo zilikuwa pande zote mbili,yaani shavu la kushoto na kulia.

Nikiwa bado hapo hapo kichwani,naenda hadi kwenye nywele zake ambazo kama ulizoea kumuona Rihanna mara kwa mara,basi akitokea Eve machoni kwako,hutosita kumuita Rihanna sababu ya nywele zake ambazo yeye alikuwa akizibadilisha rangi kila wiki.

Tuache haya ya kichwani.Nakupeleka kifuani.

Haya yote nakuelezea ili upate picha halisi na kujijibu mwenyewe kwa nini hawa jamaa watatu ambao wasichana kwao ni sumu,wagande na kudata huku kila mmoja akiapa kwa wakati wake kuwa watafanya kila njia ili wampate.

Alikuwa na kifua saa sita.Kama hujui kifua saa sita ni nini.Basi kaa ukijua kuanzia leo kuwa alikuwa anachuchu kiduchu ambazo zinawaacha watu wenye hela zao wakibakiwa na uchu wa kutaka hata kuziona zikiwa wazi.

Zilikuwa hazina kero wala kupigwa jeki kama zile za Nicki Minaj.Hizi hata zisipovishwa sidiria zilionekana wazi zimesimama dede.Lakini alipenda kuzipa sidiria ili asiwaumize maboya boya wa chuo kile.

Nashindwa kumwelezea uzuri wa miguu yake.Ila naweza kusema ni miguu ambayo ilifamfanya aonekane mrefu kiasi na asiyekuwa na tatizo au kusababisha watu wamcheke mtu aliyesimama naye kwa kuonekana mfupi kuliko yeye. Eve alikuwa hana maurefu hayo ya Hashim Thabit wala maurefu ya Twiga.Na zaidi hakuwa mfupi kama kifaru wala ufupi wa kuigizia vichekesho.

Mimi namjua Eve,kwani hata akitembea alikuwa si wa kujiaibisha kwa kutembea kama kundi la nyumbu au pundamilia linapita.Alikuwa hana vishindo vya wanyama hao wala kutimua mavumbi hata kama anatembea kwenye vumbi hilo.

Nje ya hayo maumbile yake.Eve alikuwa anaweza kujipanga kimavazi aisee.Hakuwa wa kuvaa makachumbali,yaani hakuwa wakuvaa nguo zenye rangi nyingi.

Si mwajua kachumbali navyokuwa na rangi nyingi? Utakuta kitunguu kina rangi yake,nyanya rangi yake,pilipili rangi yake,karoti kama zipo zitakuwa na rangi zake,pilipili hoho ukiamua kuweka inakuwa na ukijani wa kukolea kuliko pilipili ile ya kuwasha.Wengine wanaweka kageji kwenye kachumbali hiyo ambayo nayo ina-rangi yake.

Sasa kuna watu wanavaa kachumbali bwana.Lakini kwa Eve,ilikuwa tofauti sana.Kama akiamua kuvaa rangi tofauti,basi alizipangilia.Kama nyeusi alijua inaendana na rangi za kung’aa kama njano,pinki na nyeupe ambayo hiyo nyeupe inaendana na rangi yoyote.

ITAENDELEA

SIMULIZI The Lost Boys – Ep 3

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment